Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Niabu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na fadhila kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako Tukufu ikiwa ni mara yangu ya kwanza kabisa kusimama ili kujibu hoja za Wabunge wa Kamati yetu ya Nishati na Madini katika hotuba yetu ya kwanza kabisa ya kuomba Bunge lako Tukufu kuidhinisha kupitisha bajeti ya Wizara hii mpya ya Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kwa kuniamini na kuniteua kuwa msaidizi wake kwa kunipa majukumu ya kuwa Naibu wa Waziri wa Madini ambapo Wizara hii ni mpya na yenye majukumu mazito ya kulinda rasilimali hii muhimu kwa nchi yetu. Napenda kumhakikishia Rais wangu na Watanzania wote kuwa nitakuwa mwaminifu na mchapa kazi mkubwa, nitatumia uwezo wangu, nguvu zangu, uaminifu wangu, uadilifu wangu kusimamia na kuongoza sekta hii muhimu na bila kumuangusha Rais wangu na Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kumshukuru Waziri wangu, Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki kwa ushirikiano na maelekezo anayonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara hii mpya. Kipekee, namshukuru sana Mheshimiwa Kairuki maana yeye amekuwa ni mtu muhimu sana kwangu kwa jinsi anavyonipatia mbinu na maarifa ya kuongoza na kujiamini katika kutekeleza majukumu ya Wizara hii muhimu na yenye changamoto nyingi. Mheshimiwa Kairuki siyo mtu wa kujivuna kama mnavyomuona hapa ni mchapakazi na asiye mchoyo wa kukupa ujuzi na uelewa wa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kunisaidia maarifa ya kutatua changamoto zinazotukabili katika Wizara yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Doto Mashaka Biteko pacha wangu, kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu mwenzangu wa Wizara ya Madini. Kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuongezea nguvu katika Wizara yetu kwa kutambua uwezo usiokuwa na mashaka wa Mheshimiwa Doto Biteko. Basi ni uhakika kuwa changamoto na majukumu ya Wizara hii yenye changamoto nyingi sasa kwa umoja wetu, kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Wizara hii wakiongozwa na Katibu Mkuu Prof. Simon Samwel Msanjila ni hakika kuwa tutaendelea kusimamia vizuri sekta hii na bila shaka yoyote tutaendelea kuhakikisha tunatekeleza Ilani ya chama chetu Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa niwashukuru sana familia yangu kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia katika kutimiza majukumu yangu. Kwa kweli wananivumilia sana kipindi napokuwa sipo nao katika kutimiza majukumu yangu ya kulitumikia jimbo langu na Taifa langu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu wa kipekee kabisa napenda kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo Maswa Mashariki, kwanza kwa kunichagua kuwa Mbunge wao. Nina imani kuwa hawakukosea kunichagua na ninawaahidi kuwa nitaendelea kuwatumikia kwa nguvu zangu zote na kwa kila hali na mali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niendelee kuwashukuru sana kwa kunivumilia kuwa mbali nao pindi napokuwa katika kutekeleza majukumu yangu ya Unaibu Waziri wa Madini. Napenda kuwaahidi kuwa nitaendelea kuwa nao katika kuhakikisha Maswa yetu inaendelea kupata maendeleo kadri tunavyotarajia na mambo mazuri zaidi wategemee yanakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea na hotuba hii, napenda kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri wangu aliyoileta katika Bunge lako Tukufu. Baada ya kusema hayo, naomba sasa niendelee kwa kujibu baadhi ya hoja zilizojitokeza pindi Waheshimiwa Wabunge walipokuwa wakichangia bajeti hii ya Wizara hii ya Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamechangia na wamechangia vizuri sana. Kamati ya Nishati na Madini nayo imetoa mapendekezo yake, Wabunge waliochangia, wamechangia wengi kwa mdomo na wengine wamechangia kwa maandishi, napenda kuwaambia kwamba tumesoma maandishi yote na tumeona mawazo yao mazuri. Tunapenda kusema kwamba tutaendelea kuchukua ushauri wao na kuweza kuutendea kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile namshukuru AG kwa maneno mazuri aliyoyatoa leo, kwa lecture nzuri aliyotupatia, katueleza historia nzuri ya sheria za madini. Kwa kweli kila mmoja aliyesikia ameweza kuona tunatoka wapi na sasa tunakwenda wapi katika kusimamia hii sekta yetu muhimu kabisa ya madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria ambaye naye ameelezea vizuri kuhusu mikataba na leseni ambazo kwa kweli toka siku za nyuma jinsi zilivyokuwa zikitukandamiza na mikataba mbalimbali ambayo ilikuwa inakandamiza maslahi ya nchi yetu. Ameeleza vizuri, ametusaidia kutupa somo zuri ambalo kwa kweli kila mmoja aliyesikia ameweza kuelewa na kuona ni jinsi gani tunavyoenda sasa kusimamia rasilimali yetu hii ya madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamechangia, tumepata pongezi nyingi sana, mimi Naibu mwenzangu pamoja na Waziri wetu. Napenda kusema kwamba kwa pongezi mlizotupa mmezidi kutupa chaji/betri ya kuweza kufanya kazi kwa moyo kwa sababu tunaona ni jinsi gani mmeridhika na kazi tunazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi nyingine iliyokuja ni jinsi gani Wizara yetu imeongeza kukusanya maduhuli. Tumeweza kukusanya maduhuli kupita kiasi ambacho kilikuwa kimepangwa, mpaka sasa hivi tuna zaidi ya 130% ya makusanyo ya maduhuli tuliyoyakusanya. Tumeweza kufanikisha kwa sababu kwanza kabisa tumeweza kurekebisha Sheria yetu ya Madini ya mwaka 2017 ambapo tumeongeza kiasi cha mrabaha kwenye madini ya metali pamoja na madini ya vito ambapo sasa tunakusanya 6%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, makusanyo yameongeza na kwa kweli hii inatia moyo tutaendelea kufanya kazi hii ya kukusanya maduhuli kwa sababu Wizara yetu typically kazi yake ni kukusanya maduhuli. Tukishakusanya maduhuli haya tunapeleka katika Mfuko Mkuu na wenyewe utapeleka fedha kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo na kuweza kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wameongea mambo mengi naweza nikachambua moja baada ya lingine na siwezi kumtaja kila mmoja. Wengi wameongelea kuhusu tafiti mbalimbali ambazo kwa kweli ziko chini ya Taasisi yetu ambayo tunaiongoza katika Wizara yetu ya Madini yaani GST - Geological Survey of Tanzania, wameongea kwa kirefu. Kwa ujumla inaonekana kabisa GST wanahitajika kufanya kazi kubwa ya kufanya tafiti mbalimbali ili tuweze kuwasaidia wachimbaji wetu kuwapa taarifa mbalimbali za kijiolojia waweze kuchimba maeneo ambayo yana tija, yenye deposit nyingi ya madini, waweze kutumia fedha au mitaji yao kwa kuchimba maeneo ambayo wanaweza wakachimba kwa kupata faida ili waweze kupata fedha ambazo kwa kweli zitawasaidia katika kuinua uchumi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika GST mambo mengi yameongelewa kwamba tafiti wanazofanya ni zile za awali. Wabunge wengi wamependekeza kwamba tuende mbele, GST iwezeshwe fedha waweze kufanya tafiti ambazo zinaweza kuona kiasi gani cha madini tuliyonayo ili iwe rahisi sasa tunapokwenda kumpatia mtu leseni, aidha, tuuze leseni kwa njia ya mnada hapo baadaye kwa kuona kabisa kwamba tuna deposit ya uhakika, mwekezaji anapokuja ikiwezekana tumuuzie leseni ambazo tuna uhakika kuna madini kiasi gani. Hiyo itatuwezesha kupata wawekezaji ambao kwanza watanunua pengine kwa mnada na watakapoweza kununua itakuwa na tija na sisi tutakuwa tuna uhakika kwamba anaponunua kwenda kuchimba tuna uhakika atachimba kwa kiasi gani na sisi Serikali tutapata kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengi yameongelewa kuhusu STAMICO. Mheshimiwa Waziri wangu atakuja na ataeleza msimamo uliopo kuhusiana na STAMICO.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ni kwamba kuna madeni mengi katika Migodi ya Buhemba na Kiwira. Madeni hayo mengine yalikuwa makubwa, Mheshimniwa Naibu Waziri mwenzangu ameeleza kuhusu madeni ya STAMIGOLD. Kuna madeni ambayo yalikuwa ni makubwa mno ambayo kwa kweli tulikuwa tunaona yana forgery lakini sasa tutatuma timu kwenda kuhakiki madeni hayo na tukishakupata uhakika wa madeni hayo basi Serikali itakapopata fedha itahakikisha kwamba inawalipa wale ambao wanadai wakiwemo wafanyakazi na wale watu ambao walikuwa wamechukuliwa maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Waheshimiwa Wabunge wameongea kuhusu vifaa duni kwa wachimbaji. Napenda kusema kwamba bado Wizara yetu ina kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba tunawasaidia wachimbaji wetu kwa kuwapa elimu lakini kuangalia namna ya kuwawezesha kupata mitaji na kuweza kupata vifaa vya kisasa ili wachimbe kwa gharama ndogo waweze kupata return kubwa na wao itakuwa imewasaidia katika kujiendeleza katika miradi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wameongelea kuhusu mikopo, ni kweli kabisa wachimbaji wengi hawana sifa ya kukopeshwa na mabenki yetu. Wanapokwenda kukopa benki, benki haziko tayari kuwapa fedha kwa ajili ya ku-rise mitaji yao ni kwa sababu hakuna taarifa za uhakika, hakuna taarifa zinazoonyesha kuna deposit kiasi gani. Hivyo basi, sisi kama Wizara kwa kushirikiana na GST tunaangalia namna bora ya kufanya tafiti vizuri kuweza kuona deposit zenye uhakika. Deposit hizi pamoja na ripoti za GST ziweze basi kutumika kupeleka benki na kuweza kuwa-identify kwamba huyu mtu anaweza akakopeshwa kiasi fulani na atakachokopeshwa basi benki inakuwa na uhakika kwamba huyu mtu atarudisha na huyu mtu atabaki na fedha kwa maana ya kupata faida zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, masoko ya madini pia yameongelewa. Kwa kweli tunakwenda kujiandaa kutafuta masoko ya madini mbalimbali yakiwemo madini ya vito, dhahabu na madini mengineyo. Tunaangalia namna bora ya kuweka masoko, ikiwezekana katika madini ya dhahabu basi tuanze walau na masoko ya kila mkoa watu waweze kuchenjua madini yao, wapeleke sehemu, wanunuzi wafike pale, waweze kununua madini na Serikali tutakuwa pale na tutawapa support ya kutosha. Pia Serikali tutakuwa imara kusimamia kuweza kupata kodi yetu na sisi kuwapa export permit, kuwapa urahisi na kupunguza ile bureaucracy ya kupata export permit. Kwa hiyo, tuko tayari, tumejipanga na tutahakikisha kwamba kila mkoa tutaweza kuwawekea mazingira ya kuanzisha soko la madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengi yameongelewa na Waheshimiwa Wabunge ikiwemo kodi. Ni kweli kabisa kuna kodi zingine ni nyingi, kwa mfano, kwenye dhahabu kuna kodi nyingi ambazo pengine baadhi ya wachimbaji wanashindwa ku-comply na kodi hizo. Tutaendelea kutoa elimu ya kodi, tutaendelea kutoa elimu ya kulipa mrabaha (royalty) ili wachimbaji waweze kuzifahamu kodi hizo, waweze kutunza nyaraka mbalimbali zinazohusiana na kodi ili kuweza kuwapa unafuu na kuweza kujikinga na kutozwa kodi mara mbili mbili yaani double taxation. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano withholding tax mtu anapolipa anashindwa kuweka risiti, anapokwenda kutoa madini yake ku-export TRA wanamchaji tena, wanapomchaji tena analalamika kwamba anachajiwa mara mbili. Hii ni kwa sababu watu hawa wengine wanakosa ile elimu ya kutunza nyaraka. Tunaangalia namna bora ya kuondoa kodi kero lakini wakati huohuo tutaendelea kutoa elimu ya mlipa kodi kwa wachimbaji ili kodi hizo zisiwe mzigo kwao, waweze kufanya biashara vizuri na waweze kupata faida katika biashara hiyo ya uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine yameongelea kuhusu mikataba, Mheshimiwa Waziri wa Katiba hapa ameelezea kuhusu mikataba mibovu. Suala hili limeelezewa kwa namna mbalimbali na Waheshimiwa Wabunge wameongea vizuri sana. Kwa somo la leo, nina hakika kabisa kwamba wameweza kupata somo la uhakika kwa maana ya kwamba uwelewa utakuwa umeongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema sisi pamoja na Wizara yetu tutaendelea kujipanga kama walivyopendekeza Waheshimiwa Wabunge tuwe na semina za mara kwa mara ili kuweza kuwaelimisha Waheshimiwa Wabunge kuhusu kodi mbalimbali, mikataba mbalimbali pamoja na shughuli za uchenjuaji wa madini kama vile tulivyofanya katika maonyesho ya madini tuliyoyaleta. Kwa maonyesho haya, watu wamejifunza, wengine walikuwa hawajawahi kuona tanzanite, kwa mara ya kwanza Waheshimiwa Wabunge wameona tanzanite na dhahabu na jinsi ya ku-process madini hayo. Mungu akitujalia tutaendelea kutoa elimu zaidi kwa Wabunge waweze kupata ufahamu na tunapoingia katika Bunge lako watu wawe wanachangia kitu wanachokifahamu na iwe rahisi kuweka michango mizuri na kupata ushauri mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya mwaka 2017 imezuia ku-export raw minerals yaani madini ghafi. Watu wa Mundarara, Mheshimiwa hapa Kalanga amezungumzia, tulikwenda kule Mundarara tukaenda kutoa ahadi kemkem. Ahadi mojawapo ilikuwa ni kwenda kuwaeleza kwamba sheria hii na mabadiliko yake siyo mzigo kwa wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli raw minerals zimezuiliwa kutoka lakini tunaangalia namna ya kuja na mwongozo bora na wa kitaalam ambao utaweza kuonyesha tutaweza ku-process madini yetu katika kiwango gani na kile kiwango ambacho kinakubalika ku-export. Tutakapoleta mwongozo huo basi kila mchimbaji ataweza ku-comply na sheria hiyo na itakuwa siyo mzigo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi watu wa Mundarara niwaeleze kwamba wasiwe na wasiwasi, ahadi tulizowapatia ziko pale pale, tutawaletea mwongozo wataendelea kuchimba kwa faida kubwa. Kama alivyosema Naibu mwenzangu pale Mundarara wamejenga nyumba nzuri na majengo mazuri, kwa kweli hali ya pale ukifika unaona kabisa fedha inayotokana na machimbo inakuwa na tija katika jamii inayowazunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumziwa suala la CATA Mining. CATA Mining ni mgodi wa mchimbaji wa kati ulio katika Mkoa wa Mara. Huyu mchimbaji alikuwa na leseni sita yaani Primary Mining Licences ndani ya eneo la jeshi. Watu wamesema kwamba kuna mgogoro, Waheshimiwa Wabunge niwahakikishie hakuna mgogoro katika mgodi ule. Sasa hivi tumewashauri kwamba wakae na Jeshi la Wananchi Tanzania waelewane, Jeshi la Wananchi Tanzania lina ile surface right yaani anamiliki ardhi ya juu, yule mchimbaji amepewa leseni ya kuchimba pale kwa maana kwamba yeye ana mining right, kwa maana ana haki ya kuchimba pale, sasa wao wakae kwa pamoja na wamekwisha
kuelewana, sasa hivi ule upande wa pili ni kwamba zile Primary Mining Lisences zao sita zitakwenda kuunganishwa na kupata kitu kimoja ambacho tunaita Mining Lisences. Hiyo Mining Lisences itakuwa chini ya kampuni inaitwa CATA Mining yaani kampuni ya Mtanzania mmoja anayemiliki 50% na Mkanada anayemiliki 50%. Kwa umoja wao wataingia mkataba na Jeshi la Wananchi ili waweze kuchimba haraka na iwezekanavyo. Kwa kweli tunaona mgodi huu una potential kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo, wananchi zaidi ya 400 ajira zao ziko pembeni, wameshindwa kufanya kazi kwa sababu mgodi huo umesimama wakisubiri mikataba hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawahakikishia kwamba mgodi huo baada ya kupata Mining Lisence wataanza operesheni, wananchi wa maeneo hayo wataweza kupata ajira. Vilevile sisi kama Serikali tutaendelea kupata kodi kutoka katika mgodi huo ili nayo iweze kupeleka kwa wananchi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mengine Waheshimiwa Wabunge wameyaongea, wameongea maneno mazuri, Mheshimiwa Kanyasu ameongea, kuna Wabunge wengi hapa wameongea na mzee wangu hapa Mheshimiwa Mwambalaswa katupa hongera nyingi. Kwa kifupi, kuna malalamiko ya kuchanganya leseni, unakuta kuna leseni ya utafiti na watu wengine wameomba leseni za kuchimba madini ujenzi. Wizara yetu tutaendelea kuhahakisha kwamba tunawapa leseni hizo watu waweze kuchimba madini ujenzi na tuna hakika kwamba yatawasaidia wananchi kupata material ya kuweza kufanya ujenzi katika maeneo yao, vilevile sisi Serikali tutapata marahaba kutoka kwenye madini ujenzi na kuongeza maduhuli katika Wizara yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niendelee kukushukuru wewe na Bunge lako Tukufu, niwashukuru Wabunge kwa mawazo na maneno ambayo wametupa toka jana yametupa afya njema kwa sababu tumeona kwamba kweli Bunge letu lina upendo. Bila kujali upande wowote, wametoa mawazo mazuri na wametupa hongera nzuri. Mawazo yao waliyoyatoa tunayachukua, tutaendelea kufanya kazi kwa uhakika na tutaendelea kuhakikisha kwamba tunafuata ushauri wanaotupatia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda tena kusema kwamba naunga mkono hoja hotuba ya Waziri wangu wa Madini, Mheshimiwa Angellah Jasmine Kairuki. Ahsante sana kwa kunisikiliza.