Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Hata hivyo, naomba kwa ruhusa yako kabla sijasema ninayotaka kusema, nitoe shukrani za dhati kabisa kwako wewe mwenyewe, Katibu wa Bunge na timu yenu ya wafanyakazi wa Bunge kwa jinsi mlivyokuja kutufariji huko Kakonko. Wewe mwenyewe umesafiri kilometa 816 hadi Kakonko, tunakushukuru sana. Umeonesha mapenzi makubwa sana na kwa kweli familia inashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee pia naomba niwashukuru Wabunge wote, lakini hasa wale Wabunge 27 waliokuja Kakonko pale, tunawashukuru sana kwa kuja Kakonko, kwa kuja kutuhani.

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako nimeagizwa pia na familia ya marehemu kwako wewe mwenyewe, mengine nitakwambia tukiwa faragha, lakini mama yake mzazi, kaka zake na mke wake wanashukuru sana, sana kwa kazi iliyofanywa na Bunge, kwa jitihada iliyofanywa na Bunge hadi kufikisha mwili wa marehemu Mheshimiwa Bilago nyumbani kwao. Tunasema ahsante sana na Mungu awape nguvu na afya tele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niende kwa Wizara, kwanza, naunga mkono hoja hii, hoja muhimu sana. Pia niwape hongera ya kazi Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Kijaji; Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu na timu yote ya Wizara bila kumsahau Mkurugenzi Mtendaji wa TRA wanafanya kazi nzuri, hongereni sana, mazingira haya ni mapya, wachape mwendo, tuko vizuri na wao wako vizuri. Sisi Wabunge wengi tunawapa hongera ya kazi, tunawatakia kazi njema katika mazingira haya mapya, hakuna kukata tamaa, ni kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina machache, nina mambo matatu hivi, nitakuwa na hili la Wazabuni, nitazungumzia TRA Kasulu, nitazungumzia miradi ya PPP na mwisho kama muda utaniruhusu nitazungumzia soko la bidhaa, commodity exchange market katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na hili la malipo ya Wazabuni, nashauri sincerely hili jambo nimesoma kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 24 mpaka 26 amezungumzia malipo ya wazabuni. Hata hivyo, lipo tatizo kubwa kati ya madai ya Wazabuni, muda wanaotoa huduma zao, uhakiki wa madeni haya na hadi hawa watu kulipwa jamani.

Mheshimiwa Spika, hivi inawezekanaje Mzabuni analisha shule zetu za sekondari na zingine za msingi hizi za shule maalum, anawezaje kukaa anadai Serikali miezi 11? Huu uhakiki maana yake nini? Nafikiri wenzetu wa Wizara ya Fedha hii waichukue k ama changamoto, hawa suppliers wetu waki-supply, nitoe mfano tu mdogo, kwa sababu kuna wapiga kura wangu walitoka Kasulu, Buhigwe na Kibondo kuja hapa na nikakutana nao; wanadai TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, Katibu Mkuu wa TAMISEMI amewaandikia Hazina madai mbalimbali ambayo yameshahakikiwa. Madai hasa hasa ya Wazabuni wa elimu na wiki jana hiyo barua mwenyewe nimebahatika kuiona kwa sababu ilikuwa ni pressure kubwa sana. Inawezekanaje Mzabuni adai Serikali miezi 11. Naomba sana kupitia Wizara hii na wenzake Serikalini, warekebishe utaratibu, kweli wafanye uhakiki, tujiridhishe kwamba madeni haya ni halali, lakini Wazabuni wenye madeni halali walipwe kwa wakati jamani. Inachukua muda mrefu sana, sana.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano katika Jimbo langu la Kasulu peke yake Wazabuni wanayodai elimu, wanadai elimu zaidi ya shilingi milioni 500 na wamesubiri zaidi ya miezi kumi na kwa bahati nzuri kile kitabu cha madai mwenyewe nimekiona. Naomba sana wenzetu wa elimu mjaribu ku-fast track, wafanye uhakiki kweli, tujiridhishe na madeni, lakini hatimaye madeni haya yalipwe.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika madeni ya Mawakala wa mbolea. Hilo limekuwa sasa ni kizungumkuti. Mawakala hawa tangu niko Kamati ya Kilimo miaka miwli iliyopita tuliletewa orodha na orodha ilikuwa inahakikiwa basi tuombe Mheshimiwa Waziri wale ambao wameridhika kwamba wana madai halali ya pembejeo walipwe basi fedha zao.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumzia juu ya hawa wazabuni ambao wame-supply mbolea. Nakumbuka tangu kwenye Kamati ya Kilimo limejadiliwa jambo hili na Waziri wa alituletea orodha ya wanaodai, lakini kukawa kwamba linafanyiwa uhakiki. Ni jambo jema, lazima tujue nani hasa tunamlipa, lakini wale waliohakikiwa tafadhali sana, wale ambao wamejiridhisha kwamba hawa ni wadai halali walipwe fedha zao, muda umekuwa mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii sintofahamu ya Mabenki kuwatisha, kuuza mali zao, nadhani haijengi heshima ya Serikali, nina uhakika wala hata haijengi heshima ya Chama cha Mapinduzi. Naomba sana, wazabuni halali walio-supply huduma ya pembejeo na kadhalika walipwe baada ya kuwa wamefanya uhakiki na kuwe na timeframe kwamba wazabuni hao wanalipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni jambo kidogo ambalo liko local, sisi Mkoa wa Kigoma, Wilaya ya Kibondo na Kakonko, Wilaya ya Kasulu na Buhigwe hatuna ofisi za TRA. Naomba kupitia kwa Mheshimiwa Waziri sina uhakika kama anaijua Buhigwe, Kasulu na Kibondo iliko sina uhakika. Haiwezekani TRA waendelee kukaa kwenye vijumba vya kupanga panga…

SPIKA: Mheshimiwa Nsanzugwanko huna uhakika kama Mheshimiwa Waziri anapajua Buhigwe?

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, eehhh! Maana yake angekuwa anapajua pengine angekuwa ameshajenga Ofisi ya TRA, ndivyo ninavyofikiri hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana watujengee Ofisi za TRA angalau wenzetu wa Wilaya ya Kakonko na Kibondo wanaweza kuwa na TRA moja pale Kibondo wakai-share na sisi Kasulu na Buhigwe tukawa pia na Ofisi ya TRA.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anajua sisi Halmashauri ya Mji wa Kasulu tumeshatoa Kiwanja bure kwa ajili ya kujenga Ofisi za TRA. Sasa kile kiwanja kinakuwa chaka, kinakuwa pori, ningeshauri sana kupitia yeye na Mkurugenzi Mtendaji wa TRA nadhani ananisikia hapa watujengee Ofisi ya kisasa ya TRA. Mji wa Kasulu na Mji wa Kibondo ni miji inayokua kwa haraka sana, inahitaji huduma za kibiashara.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, ambalo napenda nilisemee ni hii miradi ya PPP; nimesoma kwenye kitabu cha bajeti, umezungumzia PPP karibu kurasa tatu, lakini katika maelezo ya Waziri haoneshi exactly ni mradi gani wa PPP ambao Serikali ume-finalize sasa unatekelezwa hakuna hata mmoja, ni maelezo tu.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya PPP tangu tumeitunga ndani ya Bunge hili ni zaidi ya miaka 10 sasa. Sasa ningependa pengine Waziri atakapokuja atueleze ni miradi ipi hasa wamei-finalize ya PPP ambayo inakwenda kutekelezwa na pengine ikibidi pia waitofautishe kati ya miradi ya huduma na miradi ya uzalishaji. Nawiwa sana hii PPP tungejielekeza kwenye miradi ya kilimo na ufugaji maeneo ambayo tuna uhakika yatazalisha fedha ili tuweze kupata fedha zingine.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo ningependa nilisemee, ni hii commodity exchange market. Waziri ameileza sana ukurasa wa 63 mpaka ukurasa wa 65, hili ni jambo geni. Kwanza ningeomba kupitia kwako pengine Wabunge wote tungepitishwa kwenye somo hili, hii stock exchange ni kitu gani? Kuna maelezo mengi sana pale na baadhi ya Makampuni ambayo yamekuwa registered kwa ajili ya kuhudumia hii commodity exchange.

Mheshimiwa Spika, ni vyema Wabunge wenyewe tungepata semina kubwa tukaelewa maana ya jambo hili. Ni jambo kubwa sana na nchi zingine zinatumia jambo hili kwa ufanisi mkubwa sana, lakini hapa bado ni kitu kipya, sisi wenyewe Wabunge hatukielewi vizuri, ningeshauri kupitia kwako tuwe na semina ya Bunge zima kuhusu hiki kitu kinachoitwa commodity exchange market. Ni kitu muhimu sana, lakini sina uhakika kama kinafahamika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kwa sababu Wizara hii ya fedha ndiyo wanagawa rasilimali fedha, naomba niendelee kuwakumbusha na hili nitalisema sana hata kwenye bajeti kuu, miradi ile ambayo tumeshaanza nayo itekelezwe, ikamilike.

Mheshimiwa Spika, barabara ya Nyakanazi ile uliyopita kutoka Airport mpaka Kakonko ndiyo inaitwa barabara ya Nyakanazi, umeiona, hipitiki. Sasa kwa sababu nakumbuka tangu mwaka jana ni moja ya miradi ya vielelezo.

Miradi ya vielelezo naomba itekelezwe.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja hii.