Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa ajili ya muda, nianze kwa kuunga mkono hoja. Naomba nianze na kipengele cha kwanza kinachogusia rasilimali fedha. Najua kwa kupitia Taarifa ya Kamati, ukurasa wa tatu na wa nne kwa ujumla wake naomba kipengele hiki muhimu tukione kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa tatu ule, kipengele hiki kinagusa hilo suala la rasilimali fedha, anasema: “Baadhi ya mafungu ya Wizara yamepata fedha za kutosha na hivyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Vile vile kuna mafungu ambayo hayakupewa fedha za kutosha, hivyo kuathiri utendaji kazi wake.” Hilo ni eneo la fedha.
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, tunaambiwa, kama Wizara ya Fedha na Mipango imeshindwa kuwezesha kwa baadhi ya vifungu vyake kupata fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake ya msingi, itawezaje kuhakikisha mafungu ya Wizara nyingine kupata fedha za kutosha?
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa rasilimali fedha, najua Wizara hii ni muhimu. Kama yenyewe tu inapata shida eneo la fedha, vipi kuhusu Wizara nyingine? Naomba hilo liangaliwe sana. Nalisema hilo kwa maana ya suala hilo hilo la rasilimali fedha, kuna huu mradi wa LGDG ambapo kwa nia njema kabisa, Serikali ilikuwa imekusudia kwa wakati mmoja kutoa fedha ili kumaliza miradi viporo, lilikuwa ni jambo jema sana. Kwa mfano, kule kwangu kwa kupitia ruzuku y a Serikali, kwa kupitia TAMISEMI of course, lakini Wizara ya Fedha iki-facilitate hilo jambo, kuna zaidi ya Sh.923,475,000. Fedha hizi zilikuwa zimelenga maeneo ya elimu na afya.
Mheshimiwa Spika, leo mashaka yangu ni kwamba tunakwenda karibu robo ya mwisho na bahati mbaya fedha hizi ambazo Serikali ilikuwa imekusudia kupeleka huko katika wilaya na maeneo mbalimbali, kwa bajeti hii inayokuja, hakuna sehemu fedha hii inasomeka. Kwa hiyo, nilichokuwa naomba kwa namna yoyote ile, tuhakikishe fedha hizi zimekwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, kuhusu suala la rasilimali fedha, napongeza kwamba kwa kupitia Taarifa ya Kamati kuna maeneo mbalimbali yanazungumzia suala la Wizara kuendelea kufanya mazungumzo ili ama kupunguziwa au kusamehewa madeni. Najua hilo likifanyika, litaendelea kutoa nafasi ya fedha za ndani zinazopakana kugharamia bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, najua na nakubaliana na wale wote na Wizara tunaomba Mheshimiwa Waziri alielewe vizuri, nakubaliana na maelezo yaliyotoka kwenye Kamati kwamba ukitaka kukusanya mapato zaidi, ni lazima uwekeze zaidi, siyo kutegemea mapato bila kuwekeza. Kwa hiyo, naendelea kuomba namna yoyote ile ambayo itatusaidia kwenda kuongeza mapato.
Mheshimiwa Spika, katika hili niendelee kushauri, najua ndugu zetu wa TRA lengo ni kuhakikisha nchi inapata fedha kwa kupitia kodi. Bado nashauri namna rafiki, najua suala la kudai kodi siyo jambo jepesi, linataka kusukumana, lakini kwa kupitia namna rafiki, bado inaweza ikamfanya mtoaji wa kodi akaona umuhimu wa kutoa kodi ikienda sambamba na elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, eneo la mafao ya wastaafu na mirathi, naona hili katika Taarifa ya Wizara, ukienda ule ukurasa wa 39 na 40, najua kimetengwa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kulipia michango ya mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hadi kufikia Aprili, 2018 kiasi cha shilingi bilioni 716.1 sawa na asilimia 71 kilikuwa kimetengwa.
Mheshimiwa Spika, nasema suala hilo ni jema Mheshimiwa kwa maana ya kujali mafao ya wastaafu na mirathi. Niendelee kusisitiza Mheshimiwa Waziri, wafanyakazi hawa, wastaafu hawa ni uti wa mgongo wa Taifa hili, ni watu ambao waliitumikia nchi hii kwa uzalendo mkubwa. Inapofika sehemu mtu kastaafu, ni wajibu wa Serikali kuendelea kumwangalia mtu huyu. Nashauri sana hilo liendelee kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo Mheshimiwa, kuna suala la uhakiki wa madeni ya watumishi na Wakandarasi na Wazabuni pia. Eneo hili la madeni najua mara ya mwisho Serikali ilitoa kiasi cha fedha kwenye kuonesha jitihada za kuanza kupunguza madeni ya wafanyakazi. Nafahamu kwa ujumla wake, katika eneo hili kule Mkoani kwangu Katavi, eneo tu la madeni ya watumishi kuna takribani Sh.501,918,296/= ambapo humo ndani pia tuna madeni yanayowagusa Wazabuni, kuna Watumishi wasiokuwa Walimu na kuna Walimu.
Mheshimiwa Spika, ninachoomba, ili kuondelea kutoa tija kwa watu wetu, eneo hili la madeni ya Watumishi na Wazabuni kama ambavyo imesomeka katika maeneo mbalimbali, nilikuwa naomba liendelee kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, najua kuna suala linazungumziwa kuhusu kupuangua kwa mfumuko wa bei. Kati ya vipengele vilivyoongelewa kuhusu suala la kupungua kwa mfumuko wa bei, limeongelewa suala la kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula kama baadhi ya vitu vilivyosaidia kupunguza mfumuko wa bei. Narudi kwenye point ile ile ya msingi, tunapofarijika na kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula, mtu wa kawaida ambaye hana elimu ya uchumi, anatamani kuona kumbe kama hili linachangia kwenye kufanya mfumuko wa bei usiwepo lakini yeye aliyeshiriki kuzalisha chakula kwa namna gani anapata moja kwa moja mafao ya yeye kukizalisha chakula. Nikilisema hilo, tafsiri yangu tuendelee kuangalia namna ambapo huyu mzalishaji wa chakula na yeye anapata manufaa ya moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, najua lugha zote hizi zinazoongelewa hapo, tunaambiwa kwamba kutoka mwaka 2017 kwa maana ya mfumuko wa bei ilikuwa 5.3, napongeza hilo, lakini kwa maana ya 2018 umeshuka mpaka 3.8. Huu mfumuko wa bei na kushuka kwake ni jambo jema, lakini naendelea kuishauri Serikali yangu, namna pekee ya mtu wa kawaida kuliona hilo, usomeke kwenye mifuko yake. Ikisomeka kwenye mifuko, tunakuwa tunaimba wimbo mmoja, wananchi na Serikali yao.
Mheshimiwa Spika, najua kwa maana ya malengo ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2018/2019, umeandaliwa kwa kuangalia dira ya 2025, lakini kuna malengo endelevu ya 2030. Ukija katika ukurasa wa 85 kwa maana ya Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa maana hii ya malengo ya mpango wa bajeti, inasema hivi:
“Baadhi ya vitu ambavyo wamezingatia ni pamoja na masuala mtambuka kama vile jinsia, watu wenye ulemavu, mazingira, UKIMWI, makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi na masuala ya lishe kwa jamii pamoja na maelekezo na ahadi zilizotolewa Kitaifa.”
Mheshimiwa Spika, niendelee kushauri. Kama kumbe bajeti hii malengo na mipango yake inazingatia suala hilo; masuala ya walemavu, masuala yanayogusa UKIMWI, nilikuwa naomba suala hili liendelee kusomeka. Walengwa kwa maana ya walemavu wafike sehemu wakutane na kile ambacho mipango inaelekeza kwamba watu hawa wameguswa moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, eneo la UKIMWI naomba niendelee kushauri, mara nyingi na watu wengine wamekuwa wakiliongelea hili. Wakati tukitenga fedha kwa ajili ya kusaidia masuala ya watu wenye maambukizo na vinginevyo, nashauri eneo la watu wazima kutumia sehemu kubwa ya fedha na walengwa wakawekwa pembeni, jambo hili naliona halina tija. Kwa hiyo, naomba niendelee kusisitiza, wakati tunazungumzia suala hilo tujaribu kuendelea kuangalia kwamba walengwa, fedha sehemu kubwa iende ikawaguse walengwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, nami niendelee kupongeza kama nilivyosema mwanzo. Naunga mkono hoja. Nakushukuru.