Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kuweza kupata nafasi ya tatu ili kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa na Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti wa Mwaka 2019/2020. Kwanza kabisa niipongeze Wizara na wataalam kwa kazi kubwa wanayoifanya na kwa kutuletea hizi nyaraka. Nyaraka hizi zimekuja zioko vizuri tu, zisingekuja hizi nafikiri watu wasingekuwa na maneno mengi ya kusema, lakini nyaraka hizi zimeandikwa kwa umahiri mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipenda nianze kwanza kuhusu mwenendo na viashiria vya uchumi. Napenda niseme jambo kidogo hapo, ndugu zangu nafikiri wapo Waheshimiwa Wabunge huwa hawarejei tulipotoka, lakini Mheshimiwa Waziri katika Bunge lililopita alikwishaweka vigezo, unaposema uchumi unakua na projection ni 7.2 maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimshauri tena Waziri hilo darasa atakapokuwa anahitimisha aweze kulifungua tena kwa sababu wapo watu wana ubishani ambao hauna takwimu. Hata hivyo, pia wanachanganya sana kukua kwa uchumi na suala la umaskini, upimaji wa umaskini una vigezo vyake na kukua kwa uchumi kuna vigezo vyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ukurasa wa nane kwenye hotuba ya Waziri napenda nizungumzie suala la uhimilivu wa deni la Taifa. Jambo hilo pia katika kikao kilichopita lilishafunguliwa darasa humu tunapimaje uhimilivu wa deni la Taifa. Niipongeze Serikali kwa kuwa wazi kwa sababu Serikali imesema deni la Taifa limekua kutoka dola za Marekani milioni 25 mpaka 27, kwa hiyo, Serikali haina jambo la kuficha hapa imeeleza wazi na vigezo vya upimaji viko wazi. Kwa hiyo, hao wanaotaka kubishana na takwimu inabidi wajipange ili waweze kueleza hili jambo kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze tena Wizara, Wizara imetuletea documents tatu, nafikiri wengine hawana au hawajazisoma. Moja ya document inasema taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 mpaka 2018/2019, ukifuatilia hapo utaona mambo makubwa ambayo yameshafanyika ndani ya miaka mitatu. Sasa watu wanaposema mpango unafeli sasa inakuwa ni changamoto kubwa sana. Nawashauri waende wakasome tena na hiyo Waziri hana sababu ya kuwajibu kwa sababu wanazo hizo nyaraka za rejea ambazo wanaweza wakasoma wakiwa mahotelini kwao au kwenye nyumba walizopanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la makusanyo ya mapato. Napenda nijikite kwenye suala la ukusanyaji wa mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Tumeona wamekusanya asilimia 89, kwanza niwapongeze asilimia 89 kwa watu ambao wanajua ukusanyaji wa mapato hiyo ni A na wamefanya kazi kubwa sana ukizingatia wapo watu wengine wanataka kukwepa mapato kwa hiyo kunakuwa na ushindani. Kwa hiyo, TRA wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona changamoto za ukusanyaji wa mapato, lakini moja ya eneo ambalo lilizungumzwa na ambalo tumekuwa tukizungumza ni suala la sekta isiyo rasmi. Ni muhimu TRA wakaa chini wakaangalia namna ya ku-formalize hiyo sekta isiyo rasmi. Jambo kubwa ambalo limekuwa linaleta changamoto ni viwango vikubwa vya kodi au viwango visivyo rafiki. Kwa hiyo, hawa watu tunaotaka kuwa-formalize lazima tufanye utafiti tuone tunawaingizaje kwenye wigo wa kodi, kwa hiyo wanaweza wakaanza kidogo tukawatambua; tukiwatambua, tukawalea watakuwa wanakua kidogo kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nalisema kwa dhati kabisa kwa sababu natoka vijijini; kumekuwa na malalamiko makubwa sana na mengi kuhusu viwango vya kodi na utaratibu mzima wa ukadiriaji. Kwa hiyo, niwashauri wenzetu wa Mamlaka ya Mapato wakae watoe mapendekezo ambayo mapendekezo hayo yataweza kuwashawishi watu kuweza kulipa kodi badala ya kukwepa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ugharamiaji wa miradi ya kielelezo. Kabla sijafika kwenye ugharamiaji wa miradi ya kielelezo niseme kwenye ukusanyaji wa Mamlaka ya Mapato lazima tuangalie zile nguzo kuu za uchumi, tukiimarisha nguzo kuu za uchumi, tukiimarisha nguzo kuu za uchumi tutegemee makusanyo mengi kutoka kwenye kodi za ndani. Hii biashara ya bidhaa kutoka nje kuingia huku ndani ikikata tunakuwa hatupati mapato ya kutosha. Kwa hiyo, lazima tuhakikishe kwamba uchumi wetu unaweza kuongeza ukusanyaji wa mapato katika ile idara ya kodi za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugharamiaji wa miradi ya kielelezo. Ugharamiaji wa miradi ya kielelezo ni jambo muhimu sana, miradi imeanishwa na ilianishwa tangu tulivyowasilisha mpango wa miaka mitano na mara nyingine wenzetu hawa wanakuja kusema hiki kimetoka wapi, lakini wakichukua kile kitabu cha mwanzo kabisa wataweza kuona miradi hii yote imetoka sehemu gani. Kwa hiyo, ni muhimu fedha zikatolewa na fedha hizo zitolewe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la mikopo na misaada kutoka nje. Takwimu zinaonesha kwamba hatukuweza kufanikiwa sana na sisi tulitegemea sana huko, sasa lazima tuweke mpango mkakati imara wa kuona kwamba hilo jambo haliwezi kuturudisha nyuma, tuhakikishe kwanza vyanzo vyetu vya mapato tunavifanyia utafiti wa kutoka na tunaangalia associated risk kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sekta ya kilimo; sekta ya kilimo na yenyewe ipo kwenye suala zima kuna miradi ya kielelezo kule kuna mashamba ya sukari na vitu vya namna hiyo. Nipendekeze kabisa kwamba mpango huu lazima uangalie namna ya kumsaidia mkulima wa kawaida (mkulima mdogo). Wakulima wadogo hawana access na mikopo, kwa hiyo wakulima wadogo wakiweza kupata mikopo wataweza kuchangia kwenye kilimo ambayo ni malighafi, malighafi hiyo itakwenda kwenye viwanda. Hilo ni jambo muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia kwenye vyombo vya habari juzi tu mbegu ya alizeti kilo moja Sh.35,000; sasa nani anayeweza kumudu Sh.35,000 na akalima na huo uzalishaji wake umepimwa wapi. Ni muhimu jambo hilo likaangaliwa na yale mazao ya kimkakati yakafuatiliwa kwa karibu kama ambavyo Waziri Mkuu amekuwa akifuatilia suala zima la zao la pamba na korosho. Sasa na zao la alizeti lifuatiliwe. Kama tuliongeza kodi kwa mafuta yanayotoka nje ni muhimu mazao kama alizeti yakapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo ukipita ukitoka Shelui ukaja Singida, Dodoma mpaka Gairo yapo mafuta mengi sana barabarani wananchi wanashika yapo mkononi. Je, kuna mkakati gani wa kuweza kuyaingiza hayo mafuta kwenye mzunguko wa kawaida (ulio rasmi) na wale wananchi wakaweza kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala zima katika sekta ya afya, tulizungumza mwanzo, suala la ugharamiaji wa maboma ambayo nguvu za wananchi zilitumika. Jambo hilo bado halijapata jawabu lake. Tumejikita kuweza kutoa fedha kujenga vitu vya afya na Hospitali za Wilaya tunashukuru, lakini yapo maboma mengi sana ambayo wananchi waliyajenga na walitarajia Serikali iwasaidie kufunika. Tunaomba jambo hili na lenyewe liangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo hayo marefu, nishukuru Serikali kwenye mipango mikakati yake kwa kuweza kuboresha miundombinu kwa sababu miundombinu ni mhimili mkubwa wa uchumi ikiwemo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa mzungumzaji)

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.