Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijaalia kuweza kuwa hapa na kuweza kuchangia katika hoja iliyopo hapo mezani. Vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu aliteremsha vitabu vinne na aliwateremshia Manabii mbalimbali ikiwemo Injili alimteremshia Nabii Issa (Alayh- Salaam); Taurati kwa Nabii Mussa; Zaburi kwa Nabii Daud na Quran kwa Nabii Muhammad (Swalla-Allah Alayh Wasalaam).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia na madhumuni ya kuteremsha vitabu hivi ni kuwaweka binadamu katika mfumo wa kujua kuna Mwenyezi Mungu na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika matendo yaliyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitabu hivyo vyote hakuna mahali palipozungumzia suala la ushoga. Ushoga ni dhambi ambayo haitakiwi na inatakiwa ikemewe, sio mfumo wa kiafrika ni mifumo ya watu wa nje, wao waendelee na mifumo wao na watuachie na utamaduni wetu wa kiafrika wa kumuabudu Mungu aliye sahihi katika vitabu vyake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo ninakwenda katika hoja iliyopo mezani. Mipango iendane na maeneo ambayo sasa hivi yalikuwa nyuma kwa muda mrefu. Mkoa wa Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Singida hii ni mikoa ilikuwa nyuma na Serikali inahitajika isimame kutoa kipaumbele na kuwahurumia wananchi wa maeneo hayo ni na wao waendane na wenzao. Nitazungumzia Mtwara Corridor na baadhi ya maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usinione pengine napenda sana kuangalia Mikoa ya Lindi na Mtwara, ndiyo mikoa ambayo iko nyuma, hakuna cha kubishana katika hilo. Tuliletewa Mradi wa LNG (Liquefied Natural Gas), ule mradi umenyamaza, upo kimya, hatujui kinachoendelea ni kizunguzungu. Wananchi wa eneo la Likong’o wamechukuliwa maeneo yao huu ni mwaka karibu wa nne au wa tano hawaruhusiwi kulima wala kufanya maendeleo ya namna yoyote, hawajalipwa fidia zao na hali ngumu ya uchumi kama hivi tunategemea watu kama wale wanafanya nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri mwenye dhamana atuambie mradi mkubwa kama ule umefikia wapi hata kwa kutoa semina kwa Wabunge, Wabunge wawe na uelewa, lakini wale wananchi ambao wananyanyasika na ardhi zao, hawajui wanalima nini, wanakula nini, Serikali imetumia kitu gani cha kuwasaidia wale watu. Wamejipanga vipi kuwainua watu wale ambao ni maskini wanategemea mikorosho na kilimo chao wapate chakula, sasa hivi hawana chakula. Naomba Serikali yenye dhamana ikawahurumie wale watu na iwatengenezee mazingira bora kwa kila Mtanzania inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuja katika suala la mazao mchanganyiko kuna korosho, pamba, alizeti, katani, dengu, maharage na kadhalika. Wananchi wamekwama na mazao yao, hawajui wafanye nini. Mbaazi za mwaka jana hazikuuzwa zimekaa majumbani na nyingine zimeachwa shambani mpaka zimeharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe angalau ushauri; Rwanda wenzetu wamejiingiza katika mfumo wa kibiashara unaitwa African Improvement Food. Hiyo maana yake wamejiunga na taasisi mbalimbali za nje wanatengeneza mifumo ya mazao yao kupeleka direct nje bila kupitia kwa wababaishaji wa katikati ambao wametunzungusha kwa muda mrefu. Leo karanga za Dodoma, Singida na Shinyanga zinapelekwa Rwanda na kahawa ya Bukoba inapelekwa Uganda. Sasa tujiulize kwa nini wenzetu wameweza sisi tumeshindwa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na taasisi moja Board of External Trade sielewi imefia wapi, ina maana wale wange-link na mashirika mbalimbali ya nje ya kibiashara kama soko la European Union tungekuwa sasa hivi tusingekaa tunababaishana na watu ambao wameshakuwa wababaishaji tumewatajirisha sasa hivi wamekuwa wanatudhalilisha katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ubabaishaji wamezoea kutuona wananchi wa Tanzania tukiendelea kuwa maskini wao waendelee kuwa matajiri na hawapo tayari kushirikiana na sisi angalau kututoa katika umaskini. Tanzania ya kuweza kusaidia viwanda na maendeleo ya kilimo inawezekana, tujipange tunaweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni champion na hoja mara nyingi itakuwa haieleweki lakini kutakuwa na siku watu wataielewa. Nina hoja kubwa ya Selous, nina hoja kubwa ya mjusi tunakimbizana na mama ntilie. Pato la mjusi nani analisimamia? Nataka nitoe onyo au niisaidie Serikali kwanza Lindi Vijijini iitwe Tendeguru District, maana yake ukisoma suala la Tendeguru wanasema it’s a loss science, it’s not a loss science, it’s a life science. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wanavyosema Tendeguru haijulikani duniani wakati mimi Riziki nilikuwa Tendeguru juzi na watakapokuja wao wakienda kuvumbua pale wataonekana sisi tumeiacha Tendeguru haionekani. Naomba kila Mtanzania ajifunze kukimbia na maendeleo ya Tanzania. Mapato yale kuyaachia vijiji vile wakiwa hawana shule, maji na barabara; revenue ambayo inapatikana kule tuje na sisi tupate mrabaha, tatizo lipo wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku nalizungumza tatizo lipo wapi? Mjusi yule toka mwaka 1903 yuko Tristan Ujerumani wanafanya exhibition, wanapata mapato, hivi jamani Serikali hii mnashindwa hata kujua Lindi inapata nini au tozo yake ni nini? Mimi nakuwa hapa kila siku nayumba napiga kelele hamnielewi ninalolizungumza, lakini nina imani kutatokea watu wachache watakaoniunga mkono na kulielewa hili suala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Selous; Selous ni ya pili katika dunia kwa ukubwa wake. Selous ni eneo ambalo ni shamba la bibi linachezewa, watu wanachimba madini, wanamaliza wanyama na matokeo yake pato la utalii wa Tanzania litapatikana wapi. Kuna corridor ya Tembo kutoka Selous kwenda Niyasa na Niyasa – Selous. Kuna corridor ya Tembo kutoka Rukwa Rukwati kwenda mpaka Katavi – Zambia, hizi corridor zote hazijakuwa promoted. Tunahitaji kufanya promotion ya kutosha na tutoe hela ya kutosha utalii wa Tanzania badala ya kutegemea asilimia 17.2 naomba sasa hivi kwa pamoja tujipange.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu ambao tupo katika Kamati moja ya Kupambana na Ujangili na Kuendeleza Conservation twende kwa pamoja tupambane kwa hili mpaka tujue Selous inapata pato la aina gani na matumizi yake yanakwendaje ili nchi nayo ipate uchumi bora badala ya kukimbizana na mama ntilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja upande wa barabara. Ili tuendelee tunahitaji uchumi bora ambao utapatikana katika mawasiliano na ikiwemo barabara. Nahuzunika sana, juzi wamekwenda kupiga kelele Liwale wamepata kiti Liwale lakini Liwale iko kisiwani. Ina maana wanawapenda watu wa Liwale wawapigie kura lakini Liwale iendelee kuwa kisiwa, zikianza mvua za mwezi wa 11 hakuna hata Mbunge wa Liwale kwenda Liwale, mimi sielewi. Kwa nini wanawafanya watu wa Liwale wawe kisiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Dar es Salaam ukifika Nangurukuru kwenda Liwale unazunguka mpaka Nachingwea, ni miezi mitatu tu ndipo unakwenda Liwale. Wanalima korosho, ufuta na mbaazi hali yao ni duni kwa vile hawana barabara. Naomba Mwenyezi Mungu alijaalie Bunge hili na wanaonisikia hao wenye kuweka hizo hela na mafungu waisaidie Liwale, Nachingwea na maeneo mengine ili uchumi wa Tanzania uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sina mengine, nawashukuru sana.