Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene niweze kuchangia kwenye taarifa hii muhimu sana inayohusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na Mwongozo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nichukue fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi kubwa anayofanya. Takwimu rasmi ziko wazi kwamba uchumi wa Tanzania ndiyo uchumi unaokua kwa kasi kuliko chumi zote za nchi za Afrika Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeupitia Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa na kwa mujibu wa mpango huu, Serikali imepanga kukusanya na kutumia takribani shilingi trilioni 33 na kati ya hizi takribani shilingi trilioni 23 ambayo ni sawa na asilimia 69 ni fedha ambazo zinatokana na mapato yetu ya ndani. Naipongeza Serikali na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuja na mpango ambao hatimaye tutatengeneza bajeti ambapo asilimia 69 karibu asilimia 70 ya fedha zote zitagharamiwa kutokana na fedha zetu wenyewe za ndani. Natoa pongezi sana kwa hatua hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia vipaumbele vilivyoorodheshwa kwenye mpango huu lakini nina ushauri kwamba kipaumbele namba moja ambacho tunatakiwa kupambana na kuhangaika nacho ni kukuza uwezo wa kukusanya mapato. Katika bajeti siku zote tunazungumza namna tunavyotumia fedha lakini bajeti na mpango siku zote vina pande mbili; kwanza inabidi uwe nazo ndiyo unaweza kuzitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kipaumbele changu cha kwanza nadhani Serikali itumie nguvu, itumie mikakati na ubunifu na wataalam wote ilionao ili kuhakikisha kwamba tunapata mapato kwanza kabla ya kuona kwamba tutayatumiaje. Hii itawezekana tu pale ambako tutaweza kuwa wabunifu na kuja na vyanzo vipya vya mapato. Tupanue wigo na tuondokane na zile njia za kiasili (traditional ways) za kupata fedha ambazo kila mwaka ndiyo tunazo hizo hizo. Kwa hiyo, lazima tuumize vichwa tuje na vyanzo vipya. Mazingira yetu ya kiuchumi na kijamii yanawezesha jambo hiki kuwezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni lazima tuwe na namna ambayo tutaweza kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato. Kwa sababu kuwa na vyanzo vya mapato ni jambo moja lakini kuweza kukusanya na kudhibiti mianya ya upotevu wa hayo makusanyo ni jambo lingine. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba ni lazima Serikali kwa kupitia Wizara ya Fedha iimarishe namna ambavyo mapato yatakusanywa lakini yatadhibitiwa ili yasiweze kuponyoka na kwenda kwenye vyanzo vingine ambavyo havitarajiwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa kuwa na mapato unajionyesha kutokana na mwenendo wa namna ambavyo tumekuwa tukipanga bajeti lakini namna ambavyo tumekuwa tukitoa fedha kwenda kutekeleza bajeti hizo. Taarifa ya Kamati ya Bajeti ukurasa wa 16 umebaini kwamba kumekuwa na mwenendo usioridhisha wa utoaji wa fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2016/ 2017 bajeti ya fedha za maendeleo ilikuwa ni shilingi trilioni 11 lakini zilizopelekwa zilikuwa ni shilingi trilioni 6.4 tu ambayo ni asilimia 55 tu ya fedha zilizopaswa kupelekwa. Mwaka 2017/2018 bajeti iliyotengwa ili kwenda kugharamia miradi ya maendeleo ilikuwa shilingi trilioni 11.4, lakini fedha zilizoweza kupatikana na kwenda zilikuwa shilingi trilioni 6.5, hii ni sawa na asilimia 57 tu. Ndipo hapo umuhimu wa kuwa na fedha unakuja kabla ya kufikiria kutumia. Kwa sababu kupanga bajeti ni jambo lingine lakini kuzipata fedha ili ziende zikagharamie ni jambo lingine. Ndiyo maana unakuta bajeti ni kubwa lakini fedha zinazokwenda ni ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nadhani ni kipaumbele, nikubaliane na maoni ya Kamati ya Bajeti ukurasa wa 24 ambapo imependekeza Serikali ione kwamba ni jambo la kipaumbele kutenga na kupeleka fedha kwa ajili ya kuezeka na kukamilisha maboma ya zahanati na shule yaliyopo nchi nzima. Ukipita kwenye Majimbo ya Wabunge wengi utakuta kuna maboma mengi ya zahanati, madarasa ya shule ambayo wananchi walitumia nguvu zao lakini Serikali iliahidi ingekamilisha lakini haikukamilisha. Jambo hili linavunja moyo wananchi. Nakubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti yaliyoko ukurasa wa 24 kwamba Serikali itafute fedha, itenge na ipeleke fedha ili maboma ya zahanati na shule yakakamilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye maji. Kuna matatizo kwenye sekta ya maji. Wakandarasi wengi wamefanya kazi lakini hawajalipwa mpaka leo. Katika Halmashauri yangu ya Nzega kuna wakandarasi wanadai zaidi ya shilingi milioni 560 tangu mwezi Juni. Wamekamilisha miradi ya maji, wametengeneza performance certificate lakini hawajalipwa. Kwa hiyo, jambo hili linadhoofisha ukamilishaji wa miradi ya maji na baadaye linaleta malalamiko kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu ni kwamba miradi hii kama ya maji ambayo ina vyanzo vya fedha mahsusi, Serikali ihakikishe kwamba miradi hii inakamilika. Kwa hiyo, hawa wakandarasi wa maji ambao naamini wako nchi nzima, fedha zao zitengwe, zipelekwe na wakalipwe ili miradi ya maji iweze kukamilishwa na wananchi wetu waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni miradi ya umeme, REA III kasi ni ndogo. Natambua dhamira ya dhati ya Serikali lakini kuna haja ya kuongeza kasi na hii maana yake ni kuongeza fedha ili wakandarasi hawa waweze kutandaza na kusambaza umeme kwa kasi ambayo inatarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.