Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jambo la kwanza kabisa, napenda niseme tu kwamba naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Taifa haliwezi kujengwa na kundi moja, Taifa hili litajengwa na Watanzania wote. Hotuba ambayo leo tumeisoma hapo, naomba sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango ajaribu kuitumia, italisaidia Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tumekuwa tuna- table hotuba zetu lakini kila mwaka tunashauri ni namna gani Serikali yetu ihakikishe kwamba inachukua ushauri na baadaye inatekeleza ushauri huo lakini kila wakati ushauri huu hamuufanyii kazi. Nasi hatuchoki kwa sababu tuko kwenye nchi hii na hatuna nyingine ya kuishi, mngekuwa peke yenu kwenye nchi hii tungewaachia mwendelee na matatizo yenu lakini kwa sababu Taifa hili ni letu wote, tutaendelea kushauri mpaka kipindi ambacho mtakuja kuelewa na mkaamini kwamba tunahitaji kujenga Taifa hili tukiwa wamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia sana kuhusiana na mpango ambao umeletwa siku ya leo. Ukweli tu ni kwamba shughuli ambazo zinafanyika katika nchi hii, tumeona kabisa badala ya kuhakikisha kwamba tunapeleka maendeleo kwa wananchi lakini tunaona maendeleo haya yanakuwa kwenye vitu badala ya wananchi. Hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kuhusiana na hali halisi ya uchumi wa nchi hii. Hebu tuangalie, katika Taifa hili tunasema Serikali inataka kuondoa umasikini. Unaondoaje umaskini wa Watanzania kama hakuna namna yoyote ya kupeleka fedha katika maeneo ambayo wananchi wengi wanapatikana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nichukulie kwenye suala la kilimo, uvuvi na mifugo karibu 65% ya Watanzania wako kule lakini huwezi kuamini fedha za maendeleo hazipelekwi kule. Mpango unaletwa hapa lakini inaonesha siyo kipaumbele cha nchi. Sasa tunataka kujua ni namna gani Serikali hii ambayo mnasema ni ya Awamu ya Tano, maana mimi najua ni Serikali ya CCM ile ile, lakini nyie mnajipambanua kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, huu ni uwongo mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016/2017 tulitenga bajeti kwenye kilimo shilingi bilioni 101 lakini fedha ambayo ilikwenda kutekeleza shughuli za kilimo kule ilipelekwa shilingi bilioni 3 peke yake. Hapa tunasema kwamba tunakwenda kupunguza umaskini wa Watanzania, unapunguzaje umasikini wa Watanzania wakati kinachoonekana ni kwamba mnatekeleza uchumi wa vitu na siyo uchumi wa watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili limekuwa ni sugu. Ukienda kwenye upande wa mifugo, tulitenga shilingi bilioni 4 lakini mpaka sasa hivi fedha ambayo ilipelekwa kwenye mifugo ilikuwa karibu shilingi bilioni 3 peke yake. Tunaona kabisa ni jinsi gani ambavyo Serikali haijajipanga kumaliza umasikini wa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika nchi hii tatizo kubwa lililopo ni mazingira mabaya ya biashara. Kwa kweli katika nchi yetu kumekuwa na tatizo kubwa sana la mazingira magumu ya kufanyia biashara. Tusipoliangalia jambo hili, tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu. Sasa hivi tunasema kwamba wawekezaji waje katika nchi hii itakuwa ni jambo gumu, kwa sababu hata wawekezaji waliopo Tanzania ambao ni wazawa wameshindwa kufanya biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona biashara inafungwa...
K U H U S U U T A R A T I B U . . .
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hajui kanuni, ngoja niendelee tu, nitamsamehe hivyo hivyo, kwa sababu ameamua kusimama tu na yeye auze sura kidogo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli tu ni kwamba mazingira ya kufanya biashara ambayo yapo katika nchi hii ni tata sana. Lazima tukubaliane, tusipoweza kuondoa kero ambazo zinawahusu wafanyabiashara katika Taifa hili, tujue kabisa tunakoelekea Taifa hili linakwenda kuzama na tutaendelea kusema tu kwamba Taifa linaenda vizuri lakini ukweli ni kwamba mazingira ni magumu, hata wafanyabiashara wa ndani wanashindwa kufanya biashara, biashara zinafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka uliopita tulimwambia Mheshimiwa Dkt. Mpango atupe sababu ni kwa nini biashara katika nchi hii zinafungwa? Alichokisema Mheshimiwa Dkt. Mpango ni kwamba wafanyabiashara wengi wanakwepa kodi. Hiyo siyo kweli. Wafanyabiashara wanalipa kodi lakini mazingira yamekuwa magumu, hata taarifa za Kimataifa zinaonesha kabisa kwamba tuko kwenye nafasi mbaya sana. Nchi hii katika mazingira bora ya biashara tunashika nafasi ya 167 kwamba mazingira ni magumu. Kwa hiyo, tunaomba tunaposhauri jambo hili tuwe tunaeleweka tunashauri kwa sababu ya maslahi ya nchi hii. Hatushauri kwa sababu tu tunataka kuzungumza ndani ya Bunge hili. Naomba hilo jambo lieleweke vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na sekta binafsi hazishirikishwi ipasavyo katika Taifa hili. Kumekuwa na tatizo kubwa sana. Serikali hii inaonekana inafanya kazi kama vile ni Serikali ya ujamaa na ukisoma mpango hapa unasema sekta binafsi inashirikishwa lakini ukweli ni kwamba sekta binafsi haishirikishwi kabisa katika kupanga maendeleo ya nchi hii na kuhakikisha kwamba Taifa hili linasonga mbele. Kwa hiyo, naomba sana haya mambo yote yajaribu kutazamwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, leo tumepata taarifa kwamba wale wadau wa korosho ambao walikuwa wananunua korosho wameamua kuachana na korosho zetu na sasa hivi hawatanunua tena korosho. Kwa sababu Mheshimiwa Rais alisema kwamba Serikali itanunua, tunaomba kesho ikiwezekana tupate taarifa kwamba Serikali sasa inapeleka fedha na kuanza kupima hizo korosho za wakulima ili wakulima hawa waendelee kuuza korosho zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikia tena yule mtu ambaye alinunua tani 500, anasema alikosea tu sifuri ile, lakini ukweli tu alikuwa ameamua kununua tani 50 ambazo alikuwa ameshalipia kipindi kile. Kwa hiyo, tunaomba Serikali pia ijiandae kununua hizi korosho kama ambavyo imewaahidi wananchi wa Mtwara na Lindi kuhakikisha kwamba korosho zao zinanunuliwa na wanapata hizo fedha kwa ajili ya kujiandaa na kilimo katika msimu unaokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza ni kuhusiana na sekta binafsi ambavyo inashirikishwa katika Taifa hili. Ukiangalia kwenye mikopo ya Serikali, mkopo wa ndani mpaka sasa hivi umefikia karibu shilingi trilioni 5. Hizi fedha ambazo zinaoneshwa kwenye mkopo wa soko la ndani ni kwamba kama Serikali inaendelea kukopa kwenye sekta za fedha za ndani, tafsiri yake ni kwamba inaendelea kuhakikisha kwamba mabenki yanashindwa kukopesha wafanyabiashara wadogo wadogo ambao ni wajasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo hii ambayo Serikali inakopa kwenye soko la ndani badala yake tena imeshindwa kuziwezesha sekta binafsi ili ziweze kuhakikisha kwamba inatekeleza miradi yote ambayo Serikali inakuwa inakopea hizi fedha. Kinachoendelea ni kwamba tumeona makampuni makubwa ambayo yanatekeleza miradi mbalimbali katika nchi hii ni ya nje siyo makampuni ya ndani. Tunaomba Serikali hii ihakikishe kwamba inayawezesha makampuni ya ndani ili fedha ambazo zinazokopwa katika masoko ya ndani zihakikishe kwamba pia makampuni ya ndani yanatekeleza miradi mbalimbali ambayo inafanyika katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haiwezekani, tunaomba pia Serikali iweke sheria ikiwezekana makampuni ya ndani yashirikiane na makampuni ya nje ili percent kidogo ambayo inaweza ikapatikana kwa ajili ya kutekeleza miradi hii kwa wakandarasi wa nje, basi na wakandarasi wa ndani waweze kupata fedha hizo. Kwa hiyo, tunaomba jambo hilo lifanyike kama ambavyo tunashauri.