Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka mitatu. Ni ukweli usiopingika kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Wasaidizi wake imefanya kazi kubwa sana kwa kipindi hiki tulichonacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli ule ule usiopingika Mheshimiwa Waziri wa Fedha amefanya jitihada kubwa sana, kila ambayo tulidhani tunaweza kuyafanya toka tulipoanza, tumeyafanya kwa sehemu yake kwa kiasi kikubwa sana. Haitakaa itokee na haitawezekana kila linalofanyika na Serikali watu wakalisema vizuri, hasa wanapoitwa Wapinzani. Nianze kwa kuishukuru Serikali, moja kati ya mipango ambayo inatazamia kuifanya ni kuhakikisha nchi yetu na miji yetu yote mikubwa inapimwa, inapangwa, inarasimishwa na kuhakikisha Watanzania hawa wanaondokana na wimbi la umasikini ikiwa ni moja ya kipaumbele, lakini ikiwa ni sehemu ya kuongeza thamani ya ardhi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Wizara ya Ardhi imefanya kazi kubwa sana, hasa kuhakikisha ardhi kubwa inapimwa lakini kuendelea kukagua mipaka na kuweka mipaka ili kuonyesha maeneo yanayostahili kutumika na yasiyostahili. Maeneo yote ya miji ambayo yametengenezewa mpango kabambe yanazo changamoto kubwa. Ukichukua kwenye miji mikubwa, kwa mfano, Mwanza ni moja kati ya mji ambao umetengenezwa kwa ajili ya mpango kabambe lakini huu mpango kabambe unaenda sambamba na urasimishaji wa makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaofanya zoezi la urasimishaji wa makazi ni Halmashauri. Nami naiomba sana Serikali, Halmashauri zetu peke yake haziwezi kufikia kiwango tunachokitegemea kama Wizara. Ni vyema sasa Serikali ikaangalia uwezekano wa kuwekeza fedha. Nami niwapongeze, Serikali imenunua vifaa kupitia Wizara kwa ajili ya upimaji, hii ni hatua kubwa sana. Vifaa hivi vikitumika vizuri, Wizara ikiwezeshwa, Halmashauri zikawa zinapewa kazi ya kupima maeneo na tukatengeneza mipaka zitaondoa migogoro ya ardhi ambayo bado ni mikubwa sana kwenye nchi hii. Kwa namna tunayoendanayo, hatuwezi kumaliza kwa wakati na migogoro itaendelea kuwa mikubwa kila leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukizungumza kwenye mpango mkakati wa upangaji miji, chukulia mfano wa Mwanza, ni mji ambao umeinuka, una milima mingi, yako maeneo bado hayatakiwi kupimwa. Unapozungumza kuweka mkakati wa kuboresha maeneo, wanapokuja wadau kushiriki kwenye ule mpango, wanapomkuta mwananchi hajamilikishwa hili eneo, bado hana haki ya lile eneo na kipande ambacho amekiishi zaidi ya miaka 40. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali, moja ya mkakati ni kuhakikisha maeneo yote yanayotakiwa kurasimishwa kwenye miji yapimwe, yarasimishwe na wananchi hao wakabidhiwe hati. Kwanza, tunaongeza thamani ya eneo lakini pili tunamtambua mmiliki ambaye ametusaidia kutunza eneo hilo zaidi ya miaka 40. Haya yamejitokeza Nyamagana kwenye Kata zaidi ya tatu, Igogo, Nyachana, Mbugani, Isamilo, Mabatini na nyingine nyingi pamoja na miji mingine yote mikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine napenda nishauri, tumezungumza habari ya viwanja vya ndege. Ni kweli kabisa tunatamani kila sehemu kuwe na kiwanja cha ndege ikiwezekana. Nami nashukuru sana, nataka niishauri Serikali, viwanja ambavyo viko kimkakati tuvipe kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, unapozungumzia uwanja wa ndege wa Mwanza, uwanja ule uko kimkakati. Haiwezekani leo tuna miaka sita tunauangalia tu hatutaki kuujenga uwanja ule kwa kiwango kinachostahili. Leo tuko 70% upande gani? Ni majengo ya abiria, running way, jengo la mizigo au ni controlling tower? Kwa hiyo, ni lazima tuhakikishe tunaweka kipaumbele kwenye mambo ambayo tunatazamia yatazalisha matokeo makubwa ili Serikali iweze kupata kipato kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho napenda kuchangia ni juu ya sekta binafsi katika utekelezaji wa viwanda vya ndani. Ni kweli naunga mkono, ni vyema kila mkoa ukawa na hivyo viwanda 100, nami napongeza sana na Wakuu wa Mikoa wamefanya kazi kubwa lakini hivi viwanda 100 vina uwezo wa kuajiri mtu 1 mpaka 5. Dhamira yetu sisi tulioko kwenye miji mikubwa tunavyo viwanda vya kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mwanza tuna viwanda vya samaki. Namshukuru Mheshimiwa Dkt. Mpango amesisitiza kuhakikisha tuna viwanda vinavyotumia malighafi ya ndani. Viwanda vya samaki vya Mwanza malighafi ya ndani ni samaki, operesheni imepita sasa hivi mazao ya samaki ni makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ni lazima tukubaliane kwamba bila kuvipa uwezo viwanda hivi, ambavyo mnyororo wake ni mkubwa, vitaajiri watu wengi lakini vitaongeza ukuaji wa kipato kwa kila mtu mmoja mmoja kuanzia mvuvi, mchuuzi mpaka uuzaji mkubwa. Ndiyo maana tunazungumza habari ya kiwanja cha ndege, tunazungumza habari ya ujenzi wa meli na kuboresha meli nyingine zote zilizopo. Tukifanya hivyo itatusaidia sana. Lengo ni lazima tuwe na kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nawashukuru sana Wizara ya Afya, wamefanya jambo moja zuri sana kupitia TAMISEMI. Kila Kituo cha Afya kinachotakiwa kujengwa kinapelekewa fedha zake, kama ni shilingi milioni 500 au ni shilingi milioni 400 na wanaamua tunataka kujenga vituo 200, vinajengwa 200 kwa wakati na vinakamilika. Sasa haya ni lazima tuenende nayo katika kuhakikisha tunausaidia umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno kwamba vitu tunavyovifanya haviwasaidii watu siyo kweli. Hivi leo unataka kuniambia zahanati zinazojengwa haziwasaidii wananchi wa kawaida? Zinawasaidia akina nani? Kwa hiyo, ni lazima tukubali, kupanga ni kuchagua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Mwakajoka pale amesema, nchi hii tumepewa wote, lakini aliyepewa nchi hii sasa hivi kuhakikisha anaishughulikia, anaijenga sawasawa ni aliyepewa dhamana, ni Chama cha Mapinduzi. Hiki ndicho kina dhamana ya kuangalia wapi kuna tatizo na wapi hakuna tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumechagua kupeleka maji, kujenga hospitali, kupeleka dawa, kutengeneza barabara, meli na standard gauge na haya ndiyo mahitaji ya wananchi. Leo Waheshimiwa Wabunge mniambie nani kwenye mikutano alishawahi kuulizwa suala la Katiba? Binafsi sijawahi kuulizwa swali la Katiba na nimekuwa na mikutano zaidi ya 1,000, wananchi wanauliza maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunapozungumza Katiba, niulize humu ndani leo mnisaidie, nani anaitaka Katiba? Ni mwananchi, mwanasiasa au nani mwingine? Sote tunajua, sisi wanasiasa ndiyo tunataka Katiba kwa sababu tunataka dola, tunataka madaraka. Utafika wakati tutajua ni wakati gani tubadilishe Katiba kwa manufaa ya Watanzania na wakati gani tuendelee mbele? (Makofi)
(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliongea bila mpangilio)
Kwa hiyo, hizi nyingine ni porojo na kelele nyingi haziwezi kutusaidia. Nachoamini, Watanzania wengi leo kila unayemgusa anataka yatokanayo na maendeleo, mambo yanayotatua changamoto zake za kila kunapokucha. Huo ndiyo msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.