Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia huu mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuipongeza Serikali, kumpongeza Mheshimiwa Rais mwenyewe kwa namna anavyofanya, kwa namna alivyoanza kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Wamesema hapa kwamba tayari Rais ameweza kuhakikisha kwamba mipango ya ununuzi wa ndege imekamilika na inaendelea vizuri, barabara za lami zinaendelea kutengenezwa lakini pia reli inaendelea kujengwa, reli ya kisasa kabisa ambayo ni standard gauge, lakini pia ujenzi wa meli katika maziwa makubwa nao unaendelea na mipango mingine mingi mizuri inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa namna anavyoisimamia vizuri hii Wizara ya Fedha na Mipango, kweli anaitendea haki anaisimamia vizuri sana. Nimpongeze pia Naibu Waziri wake, anafanya kazi nzuri, tuombe Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki waendelee kufanya kazi na hatimaye sisi Watanzania tuweze kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nichangie kidogo kwenye kilimo; Sekta ya Kilimo kwa sehemu kubwa Tanzania ndiyo inayotegemewa zaidi. Zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo cha mazao mbalimbali, lakini pia kuna zao hili la mahindi ambalo sehemu kubwa, karibu nchi nzima tunalima, lakini pia mikoa sita ya Nyanda za Juu Kusini; Mbeya, Rukwa, Katavi, Ruvuma, Songwe na Njombe ndiyo wanaolima sana haya mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukienda kwenye mikoa hii mahindi ya mwaka jana yamejaa kwenye nyumba na mwaka huu yamejaa, wakulima hawajui wafanye nini na wakati huo huo msimu wa kilimo umeshaanza lakini hawajauza mazao yale na mbolea inauzwa bei juu, kwa hiyo sasa hatujui namna gani Serikali itatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe Serikali, ili tusiweze kuwa na hali kama hii huko mbeleni tujitahidi kuwa na kitengo maalum ambacho kitahusika sanasana na utafiti wa masoko ya mazao yote ya kilimo kwa maana ya mazao ya biashara na yale ya chakula, kuwe na kitengo hicho ambacho kitazunguka nchi nzima na kufanya utafiti ni wapi zao lipi litauzwa ili tuondoe hii adha kubwa ambayo wakulima wanalima halafu mwisho wa siku haya mazao yanabaki bila kupata soko na mwisho wa siku inakuwa ni hasara kubwa kwa wakulima na pato la Taifa linapungua kwa sababu tunakuwa tumezalisha kitu ambacho hakiwezi kuuzwa kinabaki tu kwa ajili ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana hiki kitengo kitatusaidia kuhakikisha kwamba mazao yote yanapata masoko huko duniani kwa sababu sasa hivi tuna masoko pale DRC, wanahitaji mahindi, Kenya wanahitaji mahindi, sasa sijajua kuna tatizo gani kwa nini mahindi hayaendi huko DRC au hapo Kenya ambapo wana shida ya chakula. Kwa hiyo, tufanye hivyo, tuanzishe kitengo maalum ambacho kitafanya utafiti wa masoko hasa masoko haya ya mazao ambayo tunazalisha hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo lingine juu ya Mradi wa Mchuchuma na Liganga, ule wa makaa ya mawe na chuma. Huu mradi ni wa muda mrefu na umesemwa muda mrefu sana kwenye vitabu toka mwaka 2016 tulivyoingia Bungeni lakini mpaka sasa bado haujaanza, taarifa zinaonesha kwamba bado mazungumzo yanaendelea. Sasa tunaomba kujua ni lini mazungumzo haya yataisha? Kwa sababu huu mradi ni muhimu; kwanza unakwenda kuzalisha chuma ambacho kitasaidia kutoa raw material kwenye viwanda vyetu. Lakini pili utazalisha umeme ambao utasaidia sasa, utawezesha hata viwanda vidogo vidogo viweze kufunguliwa kwa sababu kutakuwa kunawaka umeme na utakuwa wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali mchakato huu wa mazungumzo ni vizuri uwahi basi ili angalau huu Mradi mkubwa wa Mchuchuma wa makaa ya mawe na chuma uweze kuanza ili mwisho wa siku tuweze kupata faida hizo na pia tufungue fursa za vijana kupata ajira kwenye maeneo hayo ambako chuma kitazalishwa, lakini pia kutakuwa na makaa ya mawe, lakini kwa maeneo hayo pia na viwanda vingi vitaongezeka kwa sababu tuna raw material sisi wenyewe lakini pia tuna umeme wa kutosha nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme juu ya uvuvi, niipongeze Serikali, imeendelea vizuri lakini pia nipongeze Wizara inaendelea kudhibiti uvuvi haramu, nawapongeza sana mnafanya kazi kubwa maana tukiacha samaki wakapotea itakuwa ni mbaya, lazima tuwe na samaki waendelee kuzaliana na tuendelee kuuza na nipongeze kwamba tayari Serikali imeanza mpango wa kujenga bandari ya uvuvi, nipongeze sana, tunataka twende kwenye uvuvi, siyo tu ule wa mwaloni, siyo tu ule uvuvi wa territorial, twende sasa kwenye uvuvi wa ndani, twende kwenye EEZ, kwenye Exclusive Economic Zone, ndivyo nchi zilizoendelea zinavyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake Nchi kwa mfano Korea Kusini, Mauritius lakini pia nchi kama Seychelles, wale wanafanya uvuvi wa ndani na kupitia uvuvi huo wanaingiza pato kubwa sana. Kwa hiyo mimi naamini kwamba tukianza sasa tukajenga hiyo bandari lakini pia tukanunua meli ya uvuvi tukaweza kuvua mpaka ndani ya bahari tutaweza kuinua uchumi wa nchi yetu kwa kasi kubwa sana. Kwa hiyo niombe sana jambo hili tulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nakumbuka Mheshimiwa Zungu, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, amekuwa akilisemea sana hili jambo. Kwa hiyo niombe Serikali yangu muweze kufanyia kazi hili mapema ili angalau tuingie kwenye uvuvi ambao unaweza ukawa una manufaa kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme juu ya soko, hasa soko la zao la chai; kwa kweli sielewi kwa nini hatuleti ule mnada ambao unafanyika kule Kenya. Miaka mingi tumesema na wenzetu Wakenya wanafaidika sana kufanyia mnada kule kwa hiyo sisi tunazalisha chai nyingi na ni wazalishaji wazuri na tunazalisha chai bora, kwa nini tunapeleka kuuza Kenya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inavyoonekana duniani inaonekana katika East Africa inayoongoza kuzalisha chai ni Kenya na chai ya Kenya ni bora, kumbe kwa sababu chai hiyo inauzwa Kenya. Kwa hiyo, niombe Serikali yangu, na Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo mpo hapa, mfanye utaratibu wa kuhakikisha kwamba mnada wa chai ufanyike hapa hapa nchini. Ukifanyika hapa nina uhakika tutapata bei nzuri kuliko ilivyo sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kilo inauzwa shilingi 314, ni hela ndogo sana, lakini ikiuzwa hapa, mnada ukawa hapahapa nchini naamini hata zile kodi nyingine, kodi pengine za soko zile, zitabakia hapa hapa nchini. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali yangu tujitahidi tuhakikishe kwamba soko au mnada wa chai unahamia Tanzania haraka iwezekanavyo ili faida zinazotokana na kuwepo na huo mnada tuweze sisi Watanzania kuzipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyokwenda kuuza Kenya wanaofaidika ni Wakenya na sasa hivi karibia viwanda vyote wanachukua Wakenya. Sasa lazima tujiulize kwa nini wanachukua Wakenya hivi viwanda? Inawezekana pengine agenda ni hiyo kwamba tuendelee kuuza hiyo chai ule mnada uendelee kufanyika kule Kenya. Kwa hiyo niombe sana Serikali yangu, mimi naamini ni Serikali sikivu mtayafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya niunge mkono hoja, ahsante sana.