Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Augustine Vuma Holle (6 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ambayo nimeipata kuingia kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Niwashukuru sana wapigakura wangu wa Jimbo la Kasulu Vijijini kwa kura nyingi sana ambazo wamenipa na kunipa Halmashauri yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nimpongeze sana Mheshimiwa Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana kuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, lakini na Baraza lake lote ambalo leo hii linachapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu mimi pamoja na Watanzania wengi tunayo imani kubwa sana pamoja na kasi ambayo mmeanza nayo. Chapeni kazi, longolongo, umbea, majungu, achaneni nayo, fungeni masikio angalieni mbele, pigeni kazi. Mwanafalsafa mmoja aliwahi kusema kwamba; “you cannot carry fundamental changes without certain amount of madness.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo niseme tu, nimepata nafasi ya kusikiliza michango mingi sana pande zote mbili katika kuboresha kitu hiki. Nimewasikiliza Wapinzani, lakini nimeguswa sana sana aliposimama kuchangia Mheshimiwa Lema. Mheshimiwa Lema ameongea vitu vingi sana hapa ambavyo kimsingi vimenigusa, lakini kwa sauti yake ya upole ya kutafuta huruma ya wananchi, imedhihirisha kwamba, yale Maandiko Matakatifu yanayosema kwamba angalieni watakuja mbwa mwitu wakiwa wamevaa ngozi ya kondoo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, Mheshimiwa Lema amesema sana kuhusu demokrasia. Anadai kwamba Chama cha Mapinduzi kinakandamiza sana demokrasia katika nchi hii, lakini tukumbuke chama chake, mgombea wao Urais mazingira ambayo walimpata, kahamia kwenye chama chake, kesho yake akapewa kugombea Urais, hiyo ndio demokrasia! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Chama chao ni yule yule na wakati wa uchaguzi wale wote waliotangaza ndiyo wagombea Uenyekiti walifukuzwa kwanza na uchaguzi ukafanyika je, hiyo ndio demokrasia?
Pia kuhusu Viti Maalum, hakuna chama ambacho kimelalamikiwa katika nchi hii kama Chama cha CHADEMA katika mchakato wa kupata Wabunge wa Viti Maalum hiyo ndiyo demokrasia? Mnataka demokrasia tufuate maslahi ya CHADEMA, hiyo ndiyo demokrasia ambayo mnataka tuje kwenu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niendelee kusema tu, wakati Lema anasema alimwambia Mwenyekiti atulie na ninyi nawaambia tulieni mnyolewe.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lema amezungumza kuhusu ugaidi hapa. Naomba nisema ugaidi ni inborn issue ni issue ambayo mtu anazaliwa nayo na sifa zake ni uhalifu na kila mtu anafahamu historia ya Lema hapa. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Anasema kwamba, anasema, tulia unyolewe tulia, tulia unyolewe vizuri, tulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa....
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wamesema watu hawa kama nchi hii itakuwa na vurugu basi mapato au uchumi wa nchi hii utashuka, lakini kila mtu anafahamu kwamba Arusha ni Mji ambao ulisifika kwa kuwa na amani sana, Arusha ni Mji ambao ulisifika kwa kuwa na uchumi wa hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hapa Mjumbe yule aliyesimama amesema uchumi wa Arusha umeshuka. Leo hii kila Mtanzania anajua kwamba Mheshimiwa Mbunge aliyeko sasa hivi wa Arusha Mjini amekuwa ni chanzo cha kuchafua amani ya Mji wa Arusha na amesababisha uchumi wa Arusha kuporoka kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanataka twende kwao tukajifunze nini hawa! Tulieni mnyolewe vizuri. Lakini naomba niseme, ndugu zangu lazima tuwe makini sana na niwasihi, Wapinzani ni marafiki zangu sana wengi. Lazima tuwe wakweli na tulitangulize Taifa letu mbele.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Tunapoomba kuchangia, tuchangie katika namna ya kujenga, siyo katika namna ya kubomoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu Mpango huu, mpango huu.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa baada ya kuzungumza hayo, niende kuzungumza yale ya wananchi wangu wa Jimbo la Kasulu Vijijini, dose imeshaingia hiyo.
Suala la kwanza, kwanza niungane na mchangiaji Mheshimiwa Zitto Kabwe kwa alichozungumza hapa, alizungumza kwamba, Kigoma ni miongoni mwa mikoa ambayo imeachwa nyuma sana. Pamoja na Mpango mzuri ule, naomba niseme kwamba kwanza kwa suala la miundombinu, iko barabara ya kutoka Nyakanazi mpaka Kidahwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wote wa Mkoa wa Kigoma wote wanafahamu kwamba hapo ndipo uchumi wa Kigoma umefungwa. Naomba sana Serikali ya Awamu ya Tano, niseme tu kwamba bajeti ijayo kama haitakuwa na barabara hii nitatoa shilingi kwenye bajeti hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni kuhusu reli ya kati kwa standard gauge. Reli ya kati ni mhimili wa uchumi wa nchi nzima ya Tanzania, lakini waathirika wakubwa sana ni sisi watu wa kanda ya magharibi. Naomba niseme tu, niungane na wachangiaji wote, tuhakikishe reli hii ya kati inajengwa kwa standard gauge. Narudia maneno yale yale, kama kwenye bajeti tutakapokutana hapa kuja kujadili maendeleo haya, reli hii kama hamjatuletea kwa kinagaubaga tutaijengaje kwa kweli nitatoa shilingi. (Makofi)
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine...
MWENYEKTI: Ahsante sana.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nishukuru kwa kunipa nafasi hii angalau niweze kuchangia kidogo kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, niungane na wenzangu kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, lakini pia na Waziri Mkuu pamoja na Baraza lake la Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo na kasi ya hapa kazi tu ambayo sifa zake zimetamalaki Tanzania nzima lakini pia na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nilishukuru sana kuona kwamba barabara ya Kidahwe - Nyakanazi imewekwa kwenye kipaumbele, Malagalasi hydropower ipo na Kiwanda cha Sukari - Kigoma Sugar nacho pia kimepewa kipaumbele. Najua haya yatakuwa ni chachu ya maendeleo katika Mkoa wetu wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la umeme wa REA. Naomba Waziri mwenye dhamana husika, Mzee wangu Mheshimiwa Profesa Muhongo, lakini pia Naibu Waziri wake, suala la umeme wa REA katika Jimbo langu la Kasulu Vijijini bado utekelezaji wake siyo mzuri, ni wa kusuasua. Nashukuru sana Naibu Waziri alifika Jimboni kwangu pale tukaweka mikakati mizuri lakini napenda kumkumbusha tu kwamba, bado utekelezaji siyo mzuri na aweze kusukuma kuhakikisha kwamba umeme wa REA unafika kwenye Jimbo langu la Kasulu Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa mapato, nipende kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo imeendelea kuongeza kukusanya mapato kila mwezi. Napenda kuwakumbusha kwamba mpakani kule bado zipo fedha zinapotea. Jimbo langu limepakana na nchi ya Burundi, kule wako watu ambao bado wanaingia pasipo kutozwa ushuru formally. Pia fedha zingine zinaishia kwa wajanja wachache ambao ni Maafisa. Kwa hiyo, ni bora sasa, Wizara husika ikaenda kuweka pale utaratibu wa namna ya kukusanya fedha zile ambazo zitakuja kusaidia Halmashauri yetu lakini pia na nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimdokeze Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mzee wangu Mheshimiwa Simbachawene kwamba pale Kasulu bado kuna majipu, nakuomba sana utue mahali pale. Ripoti ya CAG mwaka jana ilionyesha upotevu wa shilingi bilioni 5.9, lakini mpaka leo hakuna kitu ambacho kimefanyika kushughulikia watu ambao walihusika na upotevu ule. Watumishi walikuwepo lakini pia na viongozi wa halmashauri walikuwepo. Kwa hiyo, ni vyema Mheshimiwa ukatua pale kwa ajili ya kushughulikia watu hawa ili fedha zile ziweze kuja kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Kasulu Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo. Mheshimiwa Mwigulu, wananchi wanakusubiri sana Jimbo la Kasulu Vijijini uende ukamalize tatizo au mgogoro wa pori la Kagerankanda. Wananchi kwa muda mrefu sana hawana maeneo ya kutosha kwa ajili ya kilimo kwa sababu tu ya uwepo wa hifadhi ya pori la Kagerankanda ambalo kimsingi ukiangalia uhitaji wake sio mkubwa. Nadhani mipaka ile ilichorwa zamani wakati ambapo uhitaji wa ardhi haukuwa mkubwa. Kwa sasa kimsingi hatuwezi kuendelea kufuga miti ile ilhali watu wanakufa na njaa. Kwa hiyo, nikusihi sana Mheshimiwa Waziri uweze kufika pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Bunge lililopita Mheshimiwa Waziri ulisema kwamba, Wabunge tuje hapa tuseme ni lini tunahitaji mbolea za ruzuku ziweze kufika Jimboni kwetu. Naomba niseme kwamba Jimbo la Kasulu Vijijini tunahitaji tupokee mbolea ya ruzuku mwezi wa nane kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nipende kusisitiza tu kwamba, Watanzania wa Jimbo la Kasulu Vijijini wanayo imani kubwa sana na Serikali ya Awamu ya Tano na wana imani kubwa sana na kasi ambayo inakwenda nayo. Niwatie nguvu sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, hizi mbwembwe ambazo unaziona hapa, watu kugomea kuchangia na kususia vikao vya Bunge, hizi sarakasi tu wanajaribu kupanda kichuguu wakati mvua imenyesha, ni suala la kisikitisha sana. Nadhani hata Watanzania wanashuhudia nini kinatokea. Watu ambao waliwachagua kwa ajili ya kuja kimsingi kuwasilisha matatizo yao na kuyashughulikia wakisusia vikao mahsusi ambavyo vingeenda kutatua matatizo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwashauri ndugu zangu Wapinzani lakini pia na uongozi wa Bunge hebu tumshauri Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akae chini atafakari aone kama nafasi ya kuwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado inamfaa, ajipime vizuri. Kwa sababu ukiangalia namna ambavyo anaendesha kambi hii ni kinyume kabisa na matarajio ya Watanzania ambao wanahitaji maendeleo kwa nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Upinzani napenda kuwashauri kitu kimoja, nimesikia wakiitwa majina mengi sana ambayo mengine siyo mazuri kuyataja, lakini suala la kuja kujipanga kugomea mipango madhubuti ya kwenda kutatua matatizo ya wananchi, kujipanga kuchafua Serikali ambayo inakwenda kwa kasi ya ajabu, kujipanga kukwamisha maendeleo kwa namna yoyote siyo tabia ya kibinadamu ni tabia ya kinyama kabisa ambayo inafaa kulaaniwa na watu wote wanaopenda maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wako watu ambao wakati mwingine wanalazimishwa kufikiria kinyume na vile ambavyo wanaamini kwa sababu tu labda kiongozi amesema, wanalazimika kufuata vile ambavyo wameelekezwa. Tabia hii wako wanyama ambao kiongozi akitangulia bila kujua anaelekea wapi, anaelekea shimoni, anaelekea mtoni au kiongozi wa wanyama wale anaelekea kwenye miiba, anaelekea kuliwa na mamba, wao huunga mkono na kumfuata nyuma, wanyama hawa wanaitwa nyumbu. (Makofi)
KUHUSU UTARATIBU
MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu.....
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tu sana na nisingependa muongeaji anifanye nikaenda mbali zaidi kwa sababu kama ni kuminya demokrasia wao ni vinara na hayo yamejidhihirisha wazi, hata kupitia kwenye Kamati za LAAC na PAC ambapo wajumbe wako wa Upinzani na wa CCM lakini…
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nina imani muda wangu umeulinda vizuri maana wanajaribu kunitoa kwenye mstari ili nisiseme kile ambacho nataka kukisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba hapa ni Bungeni na kila mtu kaja kwa kura ambazo amepewa na wananchi na kila mtu anao uhuru wa kusema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe tu jambo moja kwamba wako watu ambao wakati mwingine wanajaribu kukuondoa kwenye kile ambacho unahitaji kuzungumza, labda niachane nayo hayo. Tuko hapa mbali na kuzungumza namna ya kuleta maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu lakini pia lazima tuweke sawa ili kuhakikisha kwamba tunalinda misingi ya demokrasia na kuikuza vizuri na hatimaye nchi yetu iwe katika nafasi nzuri sana katika nyanja ya demokrasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi nimeyazungumza hapa lakini itoshe kusema kwamba naunga mkono hoja vizuri kwa asilimia 100 na Serikali ya Awamu ya Tano iendelee kuchapa kazi vizuri na wana CHADEMA wakubali wajumbe wa PAC na LAAC watoke CUF bila kinyongo chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adimu ya mimi kuweza kuchangia kwenye hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria, lakini pia na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kueleza masikitiko yangu kwa hali ambayo imejitokeza jioni ya leo. Ama kweli hii imedhihirisha kwamba mkuki kwa nguruwe lakini kwa binadamu ni mchungu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hoja, kwanza napenda kumshukuru Mzee wangu Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe kwa kutuonyesha umahiri wake leo tena kwa kupitia hotuba yake ambayo ameitoa hapa. Napenda kulikumbusha Bunge hili kwamba umahiri wa Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe haujaanza leo, huyu ndiye aliyeongoza Kamati ambayo ilimuondoa madarakani fisadi papa namba moja Ndugu Edward Ngoyai Lowassa. Mzee Mwakyembe tunakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe yako mambo machache ya kukushauri tu mzee wangu. Suala la kwanza ni Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2006…
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Kifungu 32(1), nanukuu, kinasema; ―Mfanyakazi atakuwa na haki ya likizo ya ugonjwa angalau siku 126 kwa kila mzunguko wa likizo.‖
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili limeleta utata wakati mwingine kwa sababu wako wagonjwa ambao wameugua zaidi ya muda huu. Naomba sana kipengele hiki kiweze kurekebishwa ili watu wapate nafasi ya kuweza kutibiwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la wafanyakazi wa migodini. Watu hawa wamekuwa wakifanya kazi ngumu na wakati mwingine kulingana na mazingira duni ya migodini wamekuwa wakipata shida au matatizo ya kiafya na mara baada ya kupata matatizo ya kiafya huwa wanaachwa na waajiri wao na hatimaye wanakuwa maskini wakubwa sana. Kwa hiyo, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho hili nalo alizungumzie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejikita tena kwenye hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni…
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia ukurasa wa 11, Mheshimiwa Tundu Lissu anasema kunyamazisha upinzani na kukaribisha udikteta. Labda niwakumbushe watu hawa kwamba upinzani umejiua wenyewe yaani wamejikaanga kwa mafuta yao wenyewe. Moja, wamejikaanga kwa unafiki wao uliopitiliza, nitasema hapa ambao hasa umeongozwa na huyu huyu ambaye ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria.
KUHUSU UTARATIBU...
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme tu kwamba kwa taarifa zilizozagaa na ambazo kila Mtanzania anazifahamu...
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba wagonjwa wa namna hii kwao wako wengi, mbona Mheshimiwa Mnyika yuko Muhimbili naye anatibiwa hivyo hivyo tu.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa mujibu wa Kanuni nifute kauli hiyo ya Mirembe na naomba kuendelea na unilindie muda wangu. (Makofi)
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilisema hayo kwamba nimejiridhisha na kauli hizo za mtaani kwa sababu moja ya unafiki…
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mtu huyu amekuwa ni mnafiki namba moja katika nchi hii. Nitathibitisha unafiki na uongo wake.
Kwanza wakati anachangia hapa amesema eti anashangaa kwa nini Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania hajastaafu wakati aliosoma nao wamestaafu, anashindwa kujua kwamba siyo kila unayesoma naye umri wake ni sawa.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Amesema aliosoma nao. Wakati mimi nasoma nimesoma na watu ambao wana umri wa baba yangu lakini mtu huyu ni msomi na anajua mambo yote haya anaamua kupotosha Taifa kupitia chombo kitakatifu cha Bunge kwa makusudi kabisa. Ndiyo maana nasema unafiki huu unanirejesha kwenye hizi rumors ambazo nimesikia mtaani.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hilo nimeshafuta na mimi naendelea na mchango wangu. Sasa kama unaniambia kwamba niache kuchangia kwa kumzungumzia mtu huyu…
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Hapa nafanya hivyo ili kuweka record clear, kwa namna ambavyo amepotosha Bunge, kwa namna ambavyo …
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unilindie muda wangu. Wewe unataka nini?
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilindwe kwa mujibu wa Kanuni. Nimekuja hapa kwa mujibu wa Kanuni.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri. Afya ni msingi wa maisha ya binadamu awaye yote kwa vile kuwa na afya mgogoro ni chanzo cha kufilisika kwa shughuli zote za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya kabisa Wilaya yetu ya Mbogwe mwaka huu wa fedha Halmashauri yetu iliweka katika bajeti yake jumla ya shilingi bilioni 1.5, hata hivyo kutokana na ukomo wa bajeti fedha hizo zikaondolewa kwenye bajeti. Naishauri Serikali yetu ione umuhimu wa kusaidia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe. Tuna taabu Mbogwe, sikieni kilio chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutujengea theatre mbili katika vituo vya afya vya Masumbwe na Mbogwe ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la UNFPA kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na kuvipatia vituo hivi vya afya ambulance mbili, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kituo cha afya cha Mbogwe bado hakijafunguliwa rasmi kwa vile vifaa havijakamilika katika theater licha ya kwamba kweli gari la wagonjwa la UNFPA lipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbogwe tuna uhaba mkubwa wa watumishi katika Idara ya Afya kwenye vituo vya afya na zahanati, naiomba Serikali ilione jambo hili na itupatie watumishi wa kutosha Wilayani kwetu.

Mhesimiwa Mwenyekiti, aidha naiomba Serikali itusaidie kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya vya Ilolangula Ikunguigazi, Ikobe, Nhomolwa, pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe ili kuboresha huduma za afya Wilayani Mbogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Geita ni mpya tunahitaji hospitali ya rufaa yenye uwezo wa kuhudumia wananchi wilayani wanapopata rufaa. Ujenzi wa hospitali ya rufaa utakuwa ukombozi kwa wananchi wa Mkoa mpya wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru, ahsante kwanza awali ya yote nipende kupongeza na niseme naunga mkono hoja ya hotuba ya Waziri Mkuu.

Pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kutupa uhai huu, Waziri Mkuu hotuba yako ni nzuri sana. Imeeleza ni namna gani ambavyo Serikali imejipanga na kujipambanua lakini namna gani ambavyo imekuwa ikitekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwanza na yale mambo ambayo yapo kwenye Jimbo langu. Nipende kushukuru Serikali, nipende kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa hela ambazo ametupa jimbo la Kasulu Vijijini shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha afya pale Nyakitonto lakini pia shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha afya pale Hospitali ya Muyowozi lakini nipende kushukuru Serikali pia kupitia Waziri wa Afya kwa namna ambavyo ananipa ushirikiano pamoja na TAMISEMI kwenda kuanzia Hospitali ya Wilaya pale Muzye, pale mkandarasi atamaliza kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la viwanda nipende kumwomba Mheshimiwa Mwijage na Serikali kwa ujumla kwamba kuna mwekezaji alikuja kwetu pale Kigoma Sugar kwenye Jimbo langu. Mwekezaji yule alipewa ardhi ili aweze kufanya kilimo cha miwa na kuanzisha kiwanda, lakini ameshindwa kufanya hivyo na ameenda kinyume na mkataba. Sasa tunaomba Serikali iweze kumnyang’a mtu huyu eneo lile na hatimaye waweze kuwavutia uwekezaji kwa watu wengine ili kwamba watu wengine waweze kujitokeza na kufanya kilimo cha miwa na hatimaye kiwanda cha sukari tuweze kuwanufaisha watu wa Kasulu Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Maliasili na Utalii, tarehe 20 Julai kama sikosei Mheshimiwa Rais alikuja Wilaya ya Kasulu, pomaja na mambo mengine ambayo alisema aliruhusu wananchi waendelee kulima sehemu ya kipande cha msitu wa Makere kusini yaani Kagerankanda na alifanya hivyo kutokana na mateso makubwa ambayo wananchi walikuwa wakiyapata kwa kupigwa na watu wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu wako watu ambao sijajua kiburi wanakitoa wapi, wanaendelea kuwanyanyasa watu ambao wanaenda kulima Kagerankanda, hii haikubaliki ni kinyume cha maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, niombe chonde chonde Mheshimiwa Kigwangalla umenipa ushirikiano katika hili, tulimalize hili wananchi waendelee kulima vizuri na hatimaye waweza kufaidi kauli ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Waziri Mkuu chapa kazi, yasema nguvu ya mamba iko kwenye maji; na maji yako wewe ni sisi tupo, tuko nyuma yako tunaona kazi kubwa ambayo wewe pamoja na Mheshimiwa Rais mnaifanya kwa ajili ya Watanzania leo haya mambo mengine makelele hayo tuachane nayo nawaambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwepo Bungeni hapa kwa muda wa miaka kama miwili na kidogo. Moja ya kitu ambacho nimegundua humu Bungeni ni kwamba tunayo macho mawili ya kibinadamu. Liko jicho ambalo ni zima lenye afya lakini liko jicho ambalo lina chongo humu ndani. Nasema hivyo kwa sababu gani, haiwezekani watu tunawambia Serikali inajenga na imeanza ujenzi wa Standard Gauge Railway kutoka Dar es Salaam na Mkandarasi amepatikana na ujenzi umeanza lakini watu wanabeza wanaona kama ni reli ya udongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,haiwezekani tuwaambie watu kwamba tunanunua ndege na ndege zimekwishafika tatu zimeonekana, lakini watu wanazibeza wanaona kama ni parachute sio ndege. Tunawaambia watu kwamba hawa watu huyu kwamba hao viongozi wenu wana matatizo, wanafanya makosa wanaenda kinyume na utaratibu na wanapaswa washughulikiwe kama wahalifu wengine wao wanaona hapana wanaonewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nipende kusema kitu kimoja, ifike pahala tujitahidi sana kutenganisha kati ya kazi ya vyombo na Mheshimiwa Rais maana mtu anafanya makosa, anaenda kinyume na utaratibu, anavunja sheria halafu akianza kushughulikiwa, unakuta watu wanasema kwamba anashughulikiwa na Mheshimiwa Rais nani kasema? Nani kasema, hii ni nchi ambayo inaongozwa kwa mujibu wa sheria mtu yeyote anapokuwa amefanya makosa inapaswa ashughulikiwe kama mhalifu mwingine. Haya maneno ya watu kukimbia kwenda wapi kwenda kwa mabwana zao kutafuta sijui…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kukushukuru sana kwa nafasi hii nzuri ili na mimi niweze kuchangia Muswada huu wa upatikanaji wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona ndugu yangu Heche alivyosikia jina langu limetajwa, baada yake alianza kutokwa na povu kama nimeandaliwa kwa ajili ya kumjibu. Niseme tu, mimi ni Mkristo safi, nitaendelea kusema ukweli, maana yake najua ukweli kwa mujibu wa dini yangu humweka mtu huru siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais, alivyokuja kwenye kampeni Jimboni kwangu pale Kasulu aliahidi kwamba atafuta vumbi Wilayani Kasulu na juzi nimeenda kule kwenye ziara yangu ya kuwashukuru wananchi, nimekuta ujenzi wa barabara upo kwa kasi ya ajabu. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Rais. Nasema hayo kwa sababu wananchi waliniambia niseme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, napenda kuishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa Muswada huu. Muswada huu nimeupitia vizuri kuanzia kifungu cha kwanza mpaka kifungu cha mwisho cha 24. Nimeusoma vizuri lakini pia nimepata nafasi ya kupitia hii schedule of amendment to be moved na Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba mwandishi mmoja anaitwa Malisa, mwaka 2004 aliwahi kusema katika chapisho lake liitwalo Freedom of Information and Access to the Government Record Rose Around the World, alisema; “Access to information is the notion that public can obtain information and the possession of the state and in some countries private entities are information for the purpose of being informed about the activities of the state.”
Kwa tafsiri isiyo rasmi kwamba upatikanaji wa taarifa ni dhana ya kuwa Umma unaweza kupata taarifa zilizo chini ya himaya ya Serikali na katika baadhi ya nchi taasisi ya mtu binafsi kwa madhumuni…
Kwa madhumuni maalum, hiyo nimesema siyo rasmi.
Nataka niseme kwamba ni wakati sahihi kabisa Muswada huu umekuja, wazungu wanasema, information is power. Taarifa ni zao la habari, kama ikitolewa visivyo sahihi huzaa habari isiyo sahihi. Kama Taifa hatuna utaratibu, hatuna sheria ya upatikanji wa taarifa, maana yake inaweza ikatupelekea katika mazingira ambayo kila mtu hawezi kuamini. Maana yake taarifa hizi ambazo siyo sahihi zimesababisha baadhi ya Mataifa kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe; vinapelekea baadhi ya usalama wa nchi mbalimbali duniani kupotea na kujikuta wakiwa katika mapigano na umwagaji wa damu. Kwahiyo, kuwa na sheria ya upatikanaji wa taarifa ni kitu sahihi kabisa na mimi naunga mkono Mheshimiwa Waziri mswada huu umekuja katika wakati sahihi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekaa nikafuatilia vizuri sana michango ya sehemu zote mbili; wapinzani na wengine lakini nimeona wengi tu hapa hasa ndugu zangu wa Upinzani wanarukia tu, hawajapata nafasi ya kuupitia vizuri muswada huu na wala hawajapata nafasi ya kupitia hii schedule of amendment. Kwa sababu naona ndugu yangu Mheshimiwa Heche pale na wengine waliosimama wakasema kwamba adhabu ni kali sana; lakini nikisoma kwenye schedule of amendment kipengele (c), ukija pale (a), (b), (c); kipengele cha (c) tena imeandikwa “by deleting sub clause and substituting for it the following; namba 6 (a):-
“Any person discloses exempted information other than information related to the national security commit an offence and shall on conviction be liable to imprisonment for the term not less than three years and not exceeding five years.” (Kicheko/Makofi)
Sasa nyie mnavyosema kwamba miaka 10 mpaka 15, maana yake mmerukia tu, mnataka kulidanganya Taifa; mmerukia bila kuangalia hii schedule of amendment.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, wamesema hata hapa kwamba sheria hii ipo Bara peke yake. Labda niseme kwamba sheria hii Uingereza ilitungwa mwaka 2002. Uingereza kule ilivyotungwa Scotland wao walikuwa hawakuitumia, kama sisi tunavyofanya hivi, wamekuja kuiingiza mwaka 2002. Kwa hiyo, tupo sahihi, tupitishe sheria hii bila mizengwe yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wamekuja hapa wakasema kwamba hii sheria iondoke, yaani hawataki kufanya chochote. Sasa mimi nadhani tumekuja hapa tunalipwa na Watanzania. Tunalipwa mamilioni ya Watanzania kwa siku ili tupate nafasi ya kutunga sheria kama kazi yetu ya Kikatiba kama Wabunge. Sasa muswada umekuja hapa, badala tutoe michango ya kuuboresha na hatimaye iwe sheria nzuri na kurekebisha Tanzania, wewe unakuja unasema kwamba iondoke, yaani maana yake upokee hela tu pasipo kufanya kazi yoyote; hii ni akili kweli jamani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba ifike mahali tuwe wazalendo wa kutosha, tusizungumze tu hapa kwa sababu ya kutaka umaarufu, tusizungumze hapa tukaacha maslahi mapana ya nchi pembeni. Amekuja hapa ndugu yangu, mtani wangu, Mheshimiwa Lema jana kasema mshahara wa dhambi siku zote ni mauti, na mimi nasema, hayo ni maneno ya Kanisani, sisi hapa Bungeni tunasema kwamba mshahara wa kutoheshimu mamlaka ni kibano. Kwa mfano, umeambiwa ulipe kodi, halafu unakaa haulipi kodi, vyombo vyako tutatoa nje hata kama ni kiongozi mkubwa katika nchi hii. Umeambiwa Kanuni zinasema kwamba tutii Kiti hapa Bungeni, wewe hauachi kutii Kiti hapa Bungeni, wewe utatolewa hata kama ukifunga bandage mdomoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu, naomba unilindie muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nasema hapa kwa sababu uzalendo wa watu, hasa ndugu zetu hawa umeondoka. Wamekuwa wakijaribu kutanguliza maslahi yao mbele pasi kutanguliza maslahi mapana ya Taifa. Wamekuja hapa Bunge lililopita, wamefungwa midomo na kiongozi wao wakaondoka, walivyoondoka kule wameshindwa kuona udikteta wa kiongozi wao…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu, tafadhali! Wameshindwa kuona udikteta wa kiongozi wao…
…wanakuja kutuambia kwamba Mheshimiwa Rais…
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu, tafadhali.
MHE. AUGUSTINE V. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuweka vizuri hali ya Bungeni. Niseme tu kwamba Muswada huu umekuja wakati sahihi na wote tuungane kwenye kuupitisha. Ahsante sana.