Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel (135 total)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa bila malipo huduma za uzazi wa mpango na za afya kwa Wajawazito na Watoto chini ya umri wa miaka mitano kama Sera ya Afya inavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara ya kwanza kusimama hapa mbele, nitumie fursa hii kumshukuru Mungu, kushukuru Chama changu, kumshukuru Rais wetu kwa kutupa nafasi hii. Pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Siha kwa kuendelea kuniamini lakini nimshukuru mke wangu kwa kuendelea kunipa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Sera ya Afya ya mwaka 2007, ukurasa wa 19, kifungu 5.3.4 ambacho kinahusu Afya ya mama na mtoto na Tamko la Sera Kipengele (c) Sehemu ya (i), inaelekeza huduma bila malipo kwa Huduma za Afya ya Uzazi na Watoto chini ya miaka mitano. Baadhi ya maeneo wamekuwa wakifanya kinyume na tamko la kisera na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa pale wananchi wanapotoa taarifa. Katika kipindi cha mwaka 2015-2020, Serikali ilitoa huduma kwa wenye uhitaji bila malipo likiwemo kundi hili zenye thamani ya bilioni 880.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Wizara inawaagiza Waganga Wakuu na Mikoa na Wilaya ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa utekelezaji wa sera na miongozo ya afya katika ngazi ya mkoa na halmashauri kutimiza kikamilifu majukumu yao kwa kushughulikia haraka kero na malalamiko ya wananchi pia utekelezaji wa suala hili ambalo siyo tu ni tamko la kisera lakini pia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho chama kilichounda Serikali. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-

Je, ni kwa nini dawa za shinikizo la damu hazitolewi katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma,Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dawa za kutibu shinikizo la damu zimegawanyika katika makundi kulingana na namna zinavyofanya kazi na athari zake,hivyo basi utoaji wake unazingatia utaalam na uwezo wa kitaaluma, ndiyo maana kuna dawa hutolewa katika ngazi za Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa na Hospitali ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha ushauri mzuri wa Mheshimiwa Mbunge unatekelezeka, Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli imepeleka wataalam wengi wenye shahada ya udaktari mpaka ngazi ya kituo cha afya kwa lengo la kuhakikisha huduma nyingi na bora kama ulivyoshauriwa na Mheshimiwa Mbunge zinapatikana kuanzia ngazi ya chini na pia dawa hizi zimehusishwa katika mwongozo mpya wa matibabu nchini ili ziweze kutumika mpaka ngazi ya kituo cha afya na zahanati.
MHE. LUCY T. MAYENGA (K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI) Aliuliza: -

Nchi yetu imekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa Afya ya Akili: -

(a) Je, nini chanzo cha ugonjwa huo?

(b) Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wagonjwa hao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, afya ya akili ni ile hali ya mtu kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kimaisha ikiwemo utambuzi, uzalishaji wa mali, kutunza familia na kumudu shughuli za kijamii. Magonjwa ya akili ni pale mtu anaposhindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha ikiwa ni pamoja na kushindwa kumudu shughuli za kijamii, kujitunza, hisia na utambuzi ambapo sababu za magonjwa haya ni mchanganyiko wa sababu za kibaiolojia, kisaikolojia na kimazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa haya, Serikali imefanya yafuatayo: -

(1) Kuandaa Sheria ya Afya ya Akili ya Mwaka 2008 ambapo sheria hii inatoa mwongozo na utaratibu wa namna ya kuwapokea na kuwahudumia watu wenye ugonjwa wa akili.

(2) Kuandaa Sera na miongozo ambapo wagonjwa wa afya ya akili ni miongoni mwa makundi maalum ambayo huduma zake zinaweza kutolewa kwa msamaha kwa watu ambao hawana uwezo.

(3) Serikali inahakikisha kuwa huduma hizi zinatolewa katika ngazi zote za huduma za afya kuanzia kwenye jamii, ngazi ya afya ya msingi, mkoa, kanda, mpaka hospitali maalum ya Taifa ya afya ya akili.

(4) Kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu za afya ya akili kwenye vituo vyote vya huduma za afya.

(5) Kuongeza udahili wa wanafunzi wa uzamivu (Masters) katika masomo ya wagonjwa wa akili.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali ya Mkoa wa Iringa mashine ya CT-Scan?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa huduma za kibingwa za vipimo vya mionzi kwa kutumia CT-Scan. Katika kuzingatia umuhimu huu tayari ilishakamilisha kufunga mashine hizi kwenye Hospitali za Kibingwa Taifa, kanda na Hospitali mbili za Rufaa za Mikoa zilipata mashine hizi mnamo Desemba, 2020 ambazo ni Mwananyamala na Sekou Toure.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zoezi hili ni endelevu, Serikali inaendelea kuziwezesha hospitali zingine zote za Rufaa za Mikoa ikiwemo Iringa kufunga mashine hizi kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha za utekelezaji wa mpango huu.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa wodi ya wazazi utaanza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa Hospitali za Rufaa za Mikoa zinazoboreshwa. Napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba Mshauri Elekezi wa Ujenzi wa Wodi ya Wazazi ameshapatikana, ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, hatua inayoendelea hivi sasa, ni mchakato wa zabuni ya kupata mkandarasi atakayefanya kazi ya ujenzi, ambapo ujenzi huo unategemewa kuanza mwezi Machi, 2021. Mradi huu utatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo la hospitali ambazo zinaendelea kutoza fedha akinamama wanaojifungua kwa njia ya kawaida?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Sera ya Afya ya mwaka 2007, Ukurasa wa 19, kifungu 5.3.4 ambacho kinahusu afya ya mama na mtoto na Tamko la Sera Kipengele (c) Sehemu ya (i), inaelekeza kuhusu huduma bila malipo kwa Huduma za Afya ya Uzazi na Watoto chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2015 - 2020 Serikali ilitoa huduma kwa wenye uhitaji bila malipo likiwemo kundi hili, zenye thamani ya shilingi takriban bilioni 880. Hivyo, Wizara inasisitiza watoa huduma wote kuzingatia utekelezaji wa tamko hili la kisera.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa tayari Wizara imewaelekeza na kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri ambao ndio wasimamizi wakuu wa utekelezaji wa Sera na Miongozo ya Afya katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri kutimiza kikamilifu majukumu yao kwa kushughulikia haraka kero na malalamiko ya wananchi ikiwemo vituo vya kutolea huduma za afya kuacha kuwatoza fedha wajawazito na watoto wanapofika kituoni kupata huduma.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH Aliuliza: -

Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kupambana na ugonjwa wa Malaria, bado ugonjwa huo unaendelea kuwaathiri wananchi wakiwemo watoto: -

Je, Serikali inaweza kutuambia hatua zilizofikiwa za kutokomeza ugonjwa huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitekeleza afua na kazi mbalimbali za kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini na kufanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria kutoka zaidi ya asilimia 40 mwanzoni mwa miaka ya 2000 mpaka asilimia 7.5 mwaka 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara inatekeleza Mpango Mkakati wa Malaria (National Malaria Strategic Plan 2021 – 2025) ambao umeweka malengo ya kupunguza kiwango cha Malaria kutoka asilimia 7.5 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025. Lengo mahususi ni kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria ifikapo 2030.
MHE. MWANTUMU M. ZODO Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na upungufu wa Watumishi wapatao 16,000 kwenye Sekta ya Afya nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta ya afya ambayo kwa kiasi kikubwa hivi sasa imetokana na mahitaji mapya yanayotokana na ujenzi na upanuzi wa hospitali za rufaa za kanda, mikoa, ujenzi wa hospitali za Halmashauri, ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto ya uhaba wa watumishi ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita 2015 hadi 2020 Serikali iliajiri watumishi wapatao 14,479 na zaidi ya watumishi 565 walipatiwa ajira za mkataba kwa kugharamiwa na makusanyo ya vituo vya kutolea huduma za afya. Pia katika mwaka wa fedha 2020/2021 sekta ya afya inatarajia kuajiri jumla ya watumishi wapya 12,476.
MHE. MARIAM M. NYOKA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia ukarabati mkubwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa ni ya muda mrefu na majengo yake yamechakaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariamu Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ukarabati wa majengo chakavu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kubomoa majengo chakavu manne; jengo la Masjala ya zamani, choo cha nje cha wagonjwa, jengo la viungo bandia na jengo la zamani la huduma za kifua kikuu, kwa ajili ya kujenga jengo la kisasa la wagonjwa wa dharura ambalo limefikia asilimia 95. Mradi huu unagharimu jumla ya shilingi 630,340,507.00, ambapo hadi sasa fedha hiyo imetolewa yote. Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2021. Ahsante.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wajasiriamali wadogo kupata Bima ya afya kupitia utaratibu wa vikundi ambao ulikuwa msaada mkubwa sana kwenye jamii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya inatoa kitita mahususi cha mafao kwa makundi maalum ya wajasiriamali ambao wamejirasimisha shughuli zao kupitia mwamvuli wa jumuiya au vyama vyao vilivyorasimishwa.

Mheshimiwa Spika, makundi ya wajasirimali yanayonufaika na utaratibu wa bima ya afya ni pamoja na makundi ya wakulima kupitia Vyama vya Ushirika 225 vyenye idadi ya wanachama 6,196; vikundi 17 vya umoja wa wamachinga; wajasiriamali wadogo; wachimbaji wa madini; wavuvi; na mamalishe ambavyo vina idadi ya wanachama 2,315; na vikundi vya umoja wa madereva bodaboda, malori na daladala ambavyo vina idadi ya wanachama 303.

Mheshimiwa Spika, kwa makundi ya wananchi ambao ni wajasiriamali lakini hawamo katika mwamvuli wa jumuiya za wajasiriamali zilizorasimishwa, Mfuko umeanzisha vifurushi vya bima ya afya vya hiari ambavyo vinazingatia umri, ukubwa wa familia, aina ya huduma na gharama halisi za matibabu nchini ambapo hadi tarehe 31 Machi, 2021 wanachama 32,343 wameshajiunga na mpango huu.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwa jamii na kwa kutambua matatizo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha na Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyaainisha, Serikali inakamilisha Rasimu ya Muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo itawasilishwa Bungeni mwezi Juni, 2021.
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza:-

Je, ni kiasi gani cha Zebaki kinaingizwa nchini kila Mwaka?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Nehemia Gwau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019 kiasi cha Zebaki kilichoingizwa nchini kilikuwa ni tani 24.42, ambapo mwaka 2020 kilikuwa ni tani 22.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba zebaki ni kemikali inayotakiwa kudhibitiwa kwasababu ina madhara ya afya ya binadamu kama vile kusababisha upofu, kutetemeka viungo, kupoteza kumbukumbu, kuharibika ngozi, tatizo la ini na figo.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi Serikali, kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti uingizaji wa Zebaki kwa kuwasajili wale wanaoingiza Zebaki nchini na kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka sheria.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, lini Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Mawenzi litakamilika na kuanza kutoa huduma stahiki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbuge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na ujenzi wa jengo la kuwahudumia mama na mtoto ambalo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 70. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetolewa na kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha dhilingi bilioni 57 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ambayo imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya vifaa na vifaatiba. Aidha, huduma zitaanza kutolewa baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukamilishaji usimikaji wa vifaa ifikapo Januari, 2022.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha utaratibu maalum wa kuvuna viungo vya binadamu kama vile figo na moyo kwa ajili ya Watanzania wenye uhitaji wa viungo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa zimeanza kutoa huduma ya uvunaji na upandikizwaji wa figo nchini tangu mwezi Novemba, 2017 kutoka kwa wachangiaji walioridhia. Hadi sasa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepandikiza figo 62 na Hospitali ya Benjamin Mkapa imepandikiza figo 18. Aidha, kwa upande wa upandikizaji wa moyo, Serikali inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya upandikizaji wa viungo nchini kama ambavyo Mbunge ameainisha, Serikali imeandaa Muswada wa Kutunga Sheria itakayoongoza taratibu za uvunaji, utunzaji na upandikizaji wa viungo ambayo ipo kwenye hatua ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau. Hata hivyo, kwa kuwa huduma zimeanza kutolewa, kwa sasa nchi inatumia miongozo ya kimataifa inayosimamia uvunaji na upandikizaji wa viungo.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Mwaka 2018 KFW Germany walisitisha udhamini kwa huduma za Afya kwa Mama na Mtoto Mkoani Tanga: -

(a) Je, ni juhudi gani zimefanyika kuhakikisha Mdhamini huyo anaendelea na udhamini wake Mkoani Tanga?

(b) Je, Serikali ina mpango gani kupata Mdhamini mwingine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya KFW ilianzisha mpango wa Bima ya Afya kwa akinamama wajawazito na watoto. Mpango huo ulitekelezwa kwa makubaliano ya kipindi maalum toka 2012 hadi 2018. Mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa dhana na umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inakamilisha Rasimu ya Muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao utawasilishwa Bungeni mwezi Juni 2021, swali la Mheshimiwa Mbunge lenye kipengele (a) na (b) litaenda kupata suluhisho. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuwahamasisha wadau mbalimbali katika kuchangia miradi ya Sekta ya Afya, ikiwemo Bima ya Afya kwa Wote.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Katavi kwani ujenzi huo unakwenda kwa kusuasua?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi ambapo kwa sasa ujenzi umekamilika kwa wastani wa asilimia 70. Ujenzi kwa upande wa maabara umefikia asilimia 98 na jengo kuu la hospitali umefikia asilimia 42. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 9.82 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 3.97 kimetolewa na kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 57 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.85 zitatumika kukamilisha ujenzi huu ifikapo Januari 2022.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Katavi umekamilika kwa wastani wa asilimia 70, ambapo ujenzi kwa upande wa maabara umefikia asilimia 98 na jengo kuu la hospitali umefikia asilimia 42. Mradi huu unagharimu jumla ya shilingi bilioni 9.82 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 3.97 zimetumika na bilioni 5.85 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 na zitatumika kukamilisha ujenzi huu ifikapo Januari, 2022. Ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, ni nini mpango wa Serikali wa kukamilisha Mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambao umeanza tangu mwaka 2008/2009 bila kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo la kuwahudumia mama na mtoto katika Hospitali ya Mawenzi umekamilika kwa asilimia 70. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetolewa na kutumika.

Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kimetengwa kwa mwaka 2021/2022 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.6 zitatumika kukamilisha ujenzi na kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kitatumika kununulia vifaa tiba na ujenzi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Januari, 2022.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaandaa utaratibu mzuri wa matibabu kwa watu wenye ulemavu wakati ikisubiri Bima ya Afya kwa wote?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL). alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka utaratibu wa kuwatambua watu wenye ulemavu kupitia Kamati za Watu Wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya kijiji na kuwaunganisha kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya kulingana na mahitaji yao. Aidha, kupitia mipango kabambe ya afya ya halmashauri Serikali imeendelea kuwatengea rasilimali kulingana na mahitaji yao. Mfano kwa walemavu wa ngozi wanawezeshwa mafuta ya kuzuia jua (Sun Cream) ambayo kwa sasa hutengenezwa katika Hospitali ya Kanda ya KCMC, na bidhaa hii imeingizwa kwenye orodha ya bidhaa za afya zinazosambazwa na Bohari ya Dawa (MSD).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetoa miongozo ya miundombinu ya kutolea huduma kwa kuzingatia haki za watu wenye ulemavu. Pia, Wizara imeendelea kutengeneza miongozo na mafunzo kwa watoa huduma ili kuwezesha na kuboresha utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mswada wa Bima ya Afya kwa Wote unakuja, hii ni fursa muhimu sana kwa sisi Wabunge kutengeneza sheria nzuri zitakazolinda haki za watu wenye ulemavu. Ahsante.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawapatia wazee hasa wa vijijini bima ya afya ikiwemo ya CHF inayotolewa na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, huduma za tiba ni haki ya msingi ya wazee wote. Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa matibabu hususan kwa wazee wasiojiweza nchini kwa kuanzisha madirisha kwa ajili ya matibabu kwa wazee. Serikali imeendelea na zoezi la utambuzi wa wazee na kuwapatia vitambulisho vya matibabu. Hadi kufikia Machi, 2021 jumla ya wazee 2,344,747 wametambuliwa sawa na asilimia 87 ya makadirio ya wazee wote nchini. Kati yao wanaume ni 1,092,310 na wanawake ni 1,252,437. Aidha, wazee wasio na uwezo 1,087,008 na wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure na wazee 856,052 wamepatiwa kadi za matibabu za Afya ya Jamii yaani CHF.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na kukamilisha rasimu ya Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha wananchi wote wakiwemo wazee kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha kwa mfumo rasmi na ulio mzuri zaidi. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -

Majengo mengi katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara yamechakaa; je, ni lini Serikali itaanza ukarabati wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara - Ligula ni moja kati ya Hospitali za muda mrefu hapa nchini ambazo miundombinu yake imechakaa sana. Katika jitihada za kuboresha miundombinu ya Hospitali hiyo, kwenye bajeti ya 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 201 kimetolewa kwa ajili ya ukamilishwaji wa jengo la kuhifadhia maiti ambalo ujenzi wake umekamilika na vifaa vimenunuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi bilioni moja kimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa Majengo ya Wagonjwa wa Nje (OPD), wodi za wanaume na wanawake, upasuaji, wodi ya uangalizi maalum na kichomea taka. Ukarabati huo unatarajiwa kukamilika Machi, 2022. Ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Hospitali ya Wagonjwa wa Afya ya Akili ya Mirembe ambayo Miundombinu yake imeharibika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kumtumia Wakala wa Majengo (TBA) imeanza upembuzi yakinifu wa majengo yatakayofanyiwa ukarabati pamoja na yale yatakayobomolewa na kujengwa upya. Aidha, kupitia upembuzi huo Serikali itabaini gharama halisi za ujenzi na
ukarabati wa Hospitali hiyo. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2021.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: -

Je, ni lini Hospitali ya Kanda ya Kusini itaanza kutoa Huduma kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Spika ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Mlapo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara imewekewa jiwe la msingi tarehe 26/07/2021 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango na huduma zimeanza tarehe 1 Oktoba, 2021. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta teknolojia mbadala ili kunusuru afya za wananchi wanaotumia zebaki kwa matumizi mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na taasisi zake, ipo kwenye mpango wa kutafuta teknolojia mbadala na tayari vikao vya pamoja na taasisi zinazohusika na uchimbaji wa dhahabu vinafanyika ili kupata teknolojia isiyohitaji zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu na hivyo kuondoa athari za kiafya kwa jamii na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa elimu juu ya matumizi sahihi, kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa katika siku za usoni matumizi ya zebaki ni dhamira ya Serikali katika kulinda afya ya jamii na mazingira. Ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -

(a) Je, tangu janga la Corona lianze ni Watanzania wangapi wamepata maambukizi; wangapi wamekufa; na wangapi wamepona?

(b) Je, ni fedha kiasi gani zimetengwa na Serikali na zimefanya nini na wapi katika kukabiliana na janga hili?

(c) Je, nini kinapelekea gharama za kupima Covid- 19 kuwa kubwa na ni dawa gani zilizofanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuwa zina uwezo wa kuzuia au kutibu Covid-19?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika na mlipuko wa Ugonjwa wa Covid-19. Hadi kufikia tarehe 25 Oktoba 2021, idadi ya Watanzania 26,164 ndio waliothibitika kuwa na maambukizi. Kati ya hao, 725 walifariki na 25,330 walipona.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani kiasi cha shilingi bilioni 158 zimetumika kununua vifaa mbambali ikiwemo mitambo 19 ya kuzalisha hewa ya oxygen yenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 hadi 300 ambapo mitambo saba tayari imeshasimikwa na 12 ipo katika hatua ya usimikaji. Fedha nyingine zilinunua PPE, dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na magari 105 ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Sekta ya Afya imepokea kiasi cha shilingi bilioni 466.78 ambazo zitatumika katika kupambana na Uviko-19 ikiwemo kujenga na kusimika vifaa katika majengo ya matibabu ya dharura (EMD) 115, ujenzi wa wodi za uangalizi maalum (ICU) 67, ununuzi wa magari 253 ya kubebea wagonjwa, magari nane ya damu salama, usimikaji wa mitambo 10 ya kuzalisha hewa ya oxygen, vitanda 2,700 kwenye vituo 225 vya kutolea huduma za afya, kununua na kusimika mashine 95 za X-Ray, CT-Scan 29, mashine 4 za MRI pamoja na kufanya tafiti sita kuhusu tabia za virusi vya korona.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama halisi ya kumpima mgonjwa mmoja ni Dola 135 na Serikali sasa inatoza Dola 50. Hivyo Serikali inachangia Dola 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti mbalimbali zimefanyika duniani kuhusu dawa, ila hadi sasa dawa zilizopo zinatumika kutibu tu madhara yatokanayo na virusi. Hata hivyo kilichothibitika kwa sasa kusaidia kuondoa vifo ni chanjo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kusimamia kikamilifu Sera ya Afya ili akinamama wajawazito na watoto wasitozwe gharama katika vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, licha ya kuwepo kwa sera na miongozo inayotaka huduma itolewe bure, kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya wananchi walio katika makundi hayo katika maeneo mbalimbali kudaiwa fedha katika vituo vya umma vya kutolea huduma. Ili kuepukana na malalamiko hayo, Serikali inawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya, Bodi za Afya na watoa huduma za afya kutekeleza Sera na miongozo inayohusu matibabu bure kwa mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali inawakumbusha Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi kuwa ni jukumu lao pia kusimamia miongozo inayotolewa na Serikali. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Wodi za Wagonjwa wenye matatizo ya Ubongo na Akili katika Hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini vilevile kumshukuru Rais wetu kwa kuendelea kutuamini mimi na Mheshimiwa Ummy Ali Mwalimu kusimamia Wizara ya Afya kwa niaba yake Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Temeke ipo katika mchakato wa kukarabati jengo lililokuwa likitumika kwa wagonjwa wa kisukari ili liweze kutumika kwa ajili ya kulaza wagonjwa wa akili. Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala imetenga kiasi cha shilingi milioni mia mbili kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wagonjwa wa akili. Pia, Hospitali ya Rufaa ya Amana kwa kuwa ujenzi huo upo kwenye mpango mkakati wa miaka mitano wameelekezwa kutenga bajeti ya ujenzi wa jengo la afya ya akili katika bajeti ya mwaka 2022/2023. Ahsante.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya upungufu wa Madaktari Bingwa na vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete Mkoani Tabora?
NAIBU WAZIRI WA AFYA Alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa Kitete ina Madaktari Bingwa watatu wanaotoa huduma ya wanawake na watoto. Pia, Serikali imetoa ufadhili wa masomo kwa Madaktari sita wa hospitali hii ambao wanasomea fani mbalimbali za kibingwa; fani hizo ni Wanawake na Afya ya Uzazi mmoja, Masikio, Pua na Koo mmoja, Magonjwa ya Ndani wawili, Huduma za Dharura mmoja na Mionzi (Radiolojia) mmoja. Madaktari hao wanatarajiwa kuhitimu mwaka wa masomo 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) pamoja na vifaa vyake, jengo la huduma ya mama na mtoto, jengo la dharura (EMD) pamoja na vifaa vyake na ununuzi wa CT-Scan Pamoja na jengo lake ambapo shughuli hizo zote zimeanza.
MHE. LUHAGA J. MPINA K.n.y. MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -

Mwaka 2018 Mkoa wa Simiyu ulitenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha Kuzalisha Vifaa Tiba vitokanavyo na malighafi ya pamba na utaratibu wa kuanza ujenzi umeshakamilika, lakini kibali cha ujenzi toka Serikali kuu kimechukua muda mrefu.

Je, ni lini Serikali itatoa kibali kuruhusu ujenzi kuanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia mifuko ya WCF na NHIF ilipanga kujenga kiwanda cha kuzalisha vifaa tiba vinavyotumia malighafi ya pamba chenye thamani ya shilingi bilioni 59.4. Wakati wa upembuzi yakinifu wa awali ilionekana kutumia miundombinu tuliyonayo, kiwanda hicho kinaweza kujengwa kwa shilingi bilioni 8.4 na kuokoa shilingi bilioni 51.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya mwisho inamalizika mwishoni mwa mwezi wa pili ili kukutanisha mifuko husika na Serikali ya Mkoa wa Simiyu kupeana mwelekeo.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje katika kupunguza ama kumaliza kabisa changamoto ya ukosefu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imepeleka Bohari ya Dawa (MSD) shilingi bilioni 333.8 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba ambapo sasa Bohari ya Dawa ipo katika hatua mbalimbali za manunuzi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kupeleka fedha kwa ajili ya manunuzi, Serikali imetoa shilingi bilioni 18 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha dawa eneo la Idofi, Mkoani Njombe ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge ndani ya siku mbili vya kutosha nchi nzima kwa miezi mitatu na ujenzi umefikia 70%. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiwanda cha kuzalisha gloves kilichopo Njombe kimekamilika kwa asilimia 100 na sasa kipo kwenye majaribio; na kikikamilika kitaweza kukidhi mahitaji ya nchi kwa 85%. Aidha, kiwanda cha Keko kimefufuliwa na kinazalisha kwa sasa aina 12 za dawa. Ahsante. (Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELA aliuliza: -

Je, Serikali imefikia wapi kuhusu kufanya uchunguzi ili kujua chanzo cha ugonjwa wa saratani katika Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa na ina mpango gani wa kudhibiti ongezeko la ugonjwa huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabula Enock Shitobela, Mbunge wa Viti Maalum lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imeshafanya utafiti wa kina nchi nzima uliosaidia kutambua kuwa Kanda ya Ziwa ni saratani zipi zinaongoza ambazo ni saratani ya kibofu cha mkojo, saratani ya mji wa uzazi wa kinamama, saratani ya damu, macho na figo. Aidha, wataalamu wamekusanya sampuli za damu za watu 7,000 ambao hawana saratani ili kulinganisha na sampuli za damu za wenye saratani. Utafiti huu utasaidia kubaini chanzo cha hizo saratani. Hivyo, kwa sasa bado utafiti unaendelea na visababishi vinavyosemwa bado ni nadharia tu kutokana na shughuli za kijamii katika maeneo husika.

(b) Mheshimiwa Spika, hadi sasa mpango wa kudhibiti ongezeko umejikita katika kutoa elimu ya afya kwa viashiria vinavyodhaniwa pamoja na kuzingatia mkakati wa kitaifa kwenye maeneo saba yaliyoainishwa ili kudhibiti viashiria vya saratani. Ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -

(a) Je, ni kwa nini Serikali iliifuta iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)?

(b) Je, Serikali haioni kwa kuifuta TFDA itashindwa kudhibiti ubora wa vyakula ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilifutwa kwa kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Fedha Na. 8 ya mwaka, 2019 iliyohamishia majukumu ya udhibiti wa chakula na vipodozi kutoka TFDA kwenda Mamlaka ya Udhibiti wa Viwango (TBS). Lengo la kuhamisha majukumu haya ilikuwa ni kuondoa mwingiliano wa majukumu, kati ya TFDA na TBS na kuweka mazingira wezeshi ya uendeshaji wa biashara nchini.

(b) Serikali imeendelea kudhibiti ubora wa chakula kupitia Taasisi ya Viwango Nchini (TBS). Aidha, wataalam wa chakula waliokuwa TFDA pamoja na vifaa vya maabara vya uchunguzi wa ubora wa chakula vilivyokuwa vinatumika TFDA vilihamishiwa TBS ikiwa ni pamoja na shughuli zote zinazohusiana na udhibiti wa ubora wa chakula. Hivyo, kufutwa kwa TFDA hakuwezi kuathiri usimamizi wa ubora wa chakula nchini. Ahsnate. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kuharakisha utoaji wa matokeo ya tafiti za ndani za tiba asilia za kutibu maradhi mbalimbali kama inavyofanya kwenye tafiti za nje ya nchi kwa kuziundia Tume ya Jopo la Wachunguzi mapema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa taarifa za utafiti mbalimbali zinazohusiana na dawa za asili zilizofanywa kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zinazolenga kuonyesha ufanisi na usalama wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili mpaka Septemba 2021, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi ya NIMR, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC, zilitekeleza utafiti wa ufuatiliaji wa ufanisi wa dawa saba za asili zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa lengo la kupambana na maambukizi ya UVIKO-19. Matokeo ya utafiti huu yalitolewa na kutangazwa kwa umma kupitia vyombo vya habari mbalimbali. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Kanda ya Magharibi kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Kainja Andrea, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga fedha za ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Magharibi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na tayari kazi ya kuandaa michoro ya hospitali hiyo imeshaanza na upembuzi yakinifu wa eneo ambalo itajengwa kwa kuzingatia ukaribu wa wananchi wote katika mikoa inayounda Kanda ya Magharibi. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je ni lini Serikali itakabidhi majengo yaliyokuwa ya Hospitali ya Muhimbili kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ili kupunguza uhaba wa majengo katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shaban Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba majengo hayo yanayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Muhimbili (MUHAS) na chuo kimekuwa kikiyatumia majengo hayo kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wake.

Mheshimiwa Spika, aidha, Chuo kikuu MUHAS bado kina mipango ya uendelezaji na upanuzi wa eneo hilo ili kutimiza majukumu yake, katika kuzalisha wataalam wa afya nchini.

Mheshimiwa Spika: Serikali tayari imepeleka fedha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za dharura kwenye Hospitali ya Bagamoyo na hivyo naomba majengo ya Chuo Kikuu MUHAS yaendelee kutumika kwa shughuli za ufundishaji na utafiti kwa wanafunzi wa Chuo cha MUHAS. Hata hivyo uwepo wa Chuo cha MUHAS ni fursa kwa ukuaji wa Hospitali ya Bagamoyo na ni fursa kwa watu wa bagamoyo kitiba na kiuchumi. Ahsante sana.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuongeza maduka ya kutolea dawa kwa kutumia Bima ya Afya ili kuondoa usumbufu wanaopata wananchi wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa Mwanakwerekwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba idadi ya maduka na vituo vinavyotoa huduma za Bima ya Afya Zanzibar ni vichache ambapo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Juni, 2021 hadi Desemba 2021 idadi ya vituo vimeongezeka kutoka 19 hadi 65.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhamasisha wamiliki wa vituo vya kutolea huduma za afya na maduka ya dawa kujiunga na huduma ya bima ili kuwafikia wananchi wote. Ahsante.(Makofi)
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, ni kwa nini ugonjwa wa TB hauwezi kuonekana kwa mara moja unapompata mwathirika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ugonjwa wa TB huchelewa kuonekana kutokana na tabia na mwenendo na vimelea vya TB kuzaliana taratibu mwilini na mara nyingi hudhibitiwa na kinga ya mwili wa aliyeambukizwa. Hivyo kila mgonjwa ataanza kuonesha dalili za ugonjwa kutegemea hali ya kinga ya mwili wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa wito kwa wananchi kuwahi mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya kupimwa mara tu wanapojisikia dalili zifuatazo; homa za mara kwa mara, kikohozi cha wiki mbili au zaidi, kutoa makohozi yaliyochanganyika na damu, kupungua uzito kwa haraka bila sababu ya msingi na kutokwa jasho jingi hasa usiku. Aidha, ninashauri jamii iwe na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kutambua magonjwa mapema na hatimaye kuanza matibabu mapema. Ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kufanya utafiti wa chanzo cha watoto wachanga kugeuka njano baada ya kuzaliwa na Mama kuishiwa nguvu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti nyingi zimefanyika Kitaifa na Kimataifa kujua chanzo cha watoto wachanga kugeuka njano mara baada ya kuzaliwa. Tafiti hizo zimeonyesha kuwa hali ya umanjano inayotokea ndani ya masaa 24 baada ya kuzaliwa inaonyesha tatizo la kiafya (Pathological) na linahitaji kutambua sababu na kutoa tiba stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo likitokea baada ya masaa 24, mara nyingi linatokana na sababu za kawaida za mwili wa mtoto kupunguza chembechembe nyekundu nyingi alizokuwa nazo tumboni kwa Mama, hata hivyo hili pia uchunguzi wa kina ni muhimu ili kujihakikishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utafiti ni muhimu na ni suala endelevu katika afya. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziriwa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa hadi sasa ina jumla ya Madaktari Bingwa watano wa fani za afya kama ifuatavyo; mama na uzazi wawili, magonjwa ya watoto wawili pamoja na madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani (physician) mmoja. Katika kuongeza idadi ya madaktari bingwa, Wizara imepeleka kusoma jumla ya madaktari watano kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, ambao ni madaktari wawili wanasomea upasuaji, daktari mmoja anaesomea upasuaji wa mifupa, daktari mmoja anasomea magonjwa ya dharula na daktari mmoja anaesomea kinywa, sikio na koo, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, nini chanzo cha vifo kwa akinamama wanaojifungua kwa njia ya upasuaji siku chache baada ya upasuaji?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ufuatiliaji wa vifo vitokanavyo na uzazi uliofanywa na Wizara ya Afya kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 umeonesha kuwa vifo ambavyo vilisababishwa na matatizo ya dawa za ganzi (nusu kaputi) na upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni ni 58 yaani 3.3% mwaka 2018; vifo 80 yaani 4.8% mwaka 2019; vifo 65 yaani 4.0% mwaka 2020; na vifo 65 yaani 4.1% mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, sababu kuu za vifo hivi ni nne ambazo ni ajali ya dawa za ganzi/nusu kaputi, kupoteza damu wakati au baada ya upasuaji, tatizo la damu kuganda na maambukizi ya bakteria baada ya upasuaji.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma inatekeleza mkakati wa kuwajengea uwezo watumishi wa vituo vya huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za Taifa katika eneo la utoaji ganzi (nusu kaputi) na upasuaji kwa usalama kwa kuzingatia miongozo ya Wizara ya Afya. Ahsante.
MHE. IDRISSA JUMA ABDUL-HAFAR aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupambana na visababishi vya maradhi yasiyoambukiza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Idrissa Juma Abdul-Hafar, Mbunge wa Jimbo la Mtoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi milioni 725 kwa ajili ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza (2021 – 2026) ambao umeainisha mikakati mahsusi ya udhibiti wa visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo:-

(1) Kuimarisha uratibu na ushirikishwaji wa sekta mtambuka;

(2) Kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma;

(3) Kuwajengea uwezo watumishi katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza;

(4) Kuimarisha na kusimamia shughuli za utafiti; na

(5) Kuhamasisha wananchi kuhusu njia za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Njia hizi ni pamoja na kufanya mazoezi, pamoja na kuzingatia kanuni bora za lishe.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kupeleka Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mifupa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hadi sasa Hospitali ya Rufaa ya Lindi ina jumla ya Madaktari Bingwa watano ambao ni Daktari Bingwa wa Upasuaji mmoja, Madaktari Bingwa wa Afya ya Uzazi na Mtoto wawili, Daktari Bingwa wa Mionzi mmoja na Daktari Bingwa wa Dawa za Usingizi mmoja.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza idadi ya Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Wizara imepeleka kusoma jumla ya Madaktari saba, ambao Madaktari wawili wanasomea Udaktari Bingwa wa Watoto, Madaktari wawili Ubingwa wa Upasuaji, Daktari mmoja Ubingwa wa Mionzi, Daktari mmoja Ubingwa wa Mifupa na Daktari Bingwa wa Afya ya Uzazi na Watoto mmoja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Serikali inakamilisha taratibu za uhamisho ili kumpeleka Hospitali ya Lindi. Ahsante.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya uhaba wa madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa hadi sasa ina jumla ya madaktari bingwa kumi na moja. Madaktari bingwa wa afya ya akina mama na uzazi wanne, madaktari bingwa wa upasuaji wawili, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani mmoja, madaktari bingwa wa watoto wawili, daktari bingwa wa macho mmoja na daktari bingwa wa mionzi mmoja.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza idadi ya madaktari bingwa, Wizara imepeleka kusoma jumla ya madaktari kumi na mbili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Iringa, ambapo madaktari wawili wanasomea


kinywa, sikio na koo, madaktari bingwa wa mifupa wawili, daktari wa magonjwa ya dharura mmoja, madaktari bingwa wa watoto wawili, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani wawili, daktari bingwa wa meno mmoja, daktari bingwa wa usingizi mmoja na daktari bingwa mbobezi wa masuala ya watoto mmoja. Ahsante.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha huduma za afya zikiwemo dawa muhimu katika hospitali zetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa kuboresha miundombinu ikiwemo kuweka vifaa tiba vya kisasa, kuajiri wataalam wa afya pamoja na kuwapandisha madaraja ili kuongeza morali ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na hadi kufikia tarehe 30 Oktoba, 2022, Serikali imekwisha toa jumla ya shilingi bilioni 74.3 kwa ajili ya manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuimarisha upatikanaji wake katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya nchini. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, kuna Wataalam wangapi wa huduma za utengamano na mazoezi ya viungo physiotherapist katika Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro una jumla ya wataalam 15 kati ya 30 wanaohitajika wa huduma za utengamao na mazoezi ya viungo ambapo Kilosa kuna mtaalam mmoja, Hospitali ya Rufaa Morogoro kuna wataalam wanne, Mvomero mtalaam mmoja, Ifakara Hospitali wanne na Mzinga Hospitali wataalam watano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha watalaam tisa wa huduma za utengamao wameombewa kibali cha ajira katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje katika kupambana na changamoto ya upungufu wa Wataalam wa Mazoezi Tiba na huduma ya Utengamao nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeajiri jumla ya wataalam 84 wa mazoezitiba na huduma mtengamao katika ajira za mwezi Julai, 2022. Hata hivyo, kufanya idadi ya wataalam wa mazoezitiba na huduma mtengamao kuongezeka kutoka 653 hadi 737.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa kuna jumla ya vyuo vikuu vinne ambavyo ni Muhimbili, KCMC, Bugando na Zanzibar vinavyotoa taaluma, hivyo kupunguza changamoto ya uwepo wa wataalam katika soko la ajira.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA aliuliza: -

Je, kuna utafiti wowote ambao umefanyika ili kubaini dawa za ganzi/nusu kaputi zinazosababisha vifo kwa wanaojifungua kwa upasuaji?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher Mnzava, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonesha kuwa sababu zimegawanyika katika makundi matatu:-

(a) Sababu za vinasaba (DNA);
(b) Sababu zinazohusiana na ganzi ila siyo za moja kwa moja; na
(c) Sababu zenye mahusiano ya moja kwa moja na ganzi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, vifo vya namna hii hutokea mara chache sana na ndiyo maana wakati wote tunawashauri akinamama wajawazito kuhudhuria kliniki ili kutoa muda wa kutosha kufuatiliwa na pale inapohitajika kufanyiwa upasuaji usiwe wa dharura. Aidha, jamii inahamasishwa kutoa lishe bora kwa wajawazito.
MHE. NANCY H. NYALUSI atauliza: -

Je, ni lini Serikali itafunga Mtambo wa Mashine ya Oxygen katika Hospitali ya Rufaa ya Iringa ili kuhudumia wagonjwa wa dharura?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 599.3 kwa ajili ya manunuzi ya mtambo wa kuzalisha Hewa Tiba ya Oksijen na ujenzi wa chumba cha kuhifadhia mtambo huo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na tayari hatua za manunuzi zimeanza na mradi huu utakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2022.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea wahudumu wa kada mbalimbali za afya nyumba bora ili kuboresha makazi yao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imejenga nyumba 176 na katika mwaka wa fedha 2022/2023 itajenga nyumba 300 za kukaa familia tatu kwa kila nyumba. Ahsante.
MHE. AGNES M. MARWA K.n.y. MHE. STELLA A. IKUPA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa kuna vyumba maalum kwa ajili ya kujifungulia wanawake wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Alex Ikupa, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshalitambua tatizo hilo na kwa muda mrefu sasa marekebisho yamekuwa yakifanyika kwenye miundombinu isiyo rafiki kwa wanawake wenye ulemavu na tayari kwenye ramani mpya za ujenzi wa vituo vya afya, hospitali, ununuzi wa vifaa tiba, mahitaji kwa watu wenye mahitaji maalum yamezingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaboresha kadi ya kliniki ya Watoto chini ya miaka mitano ili kusaidia ufuatiliaji wa wingi wa damu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’azi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kadi za kiliniki ya watoto ziliboreshwa tangu mwaka 2011 kwa kuzingatia miongozo ya Shirika la Afya Duniani, ambapo maboresho hayo yamezingatia maeneo yasioacha maeneo hatarishi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo unaelekeza kutumia mbinu za kitabibu kutambua wingi wa damu kwa mtoto bila kumtoboa na wale wenye dalili za upungufu hupelekwa kwenye vipimo zaidi, ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itabadilisha Sera ya Chanjo kitaifa ili kuwakinga watu wengi zaidi badala ya kutibu mtu aliye na ugonjwa tayari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa, gharama za kutibu ugonjwa wowote ni kubwa zaidi kuliko gharama za Kinga kupitia chanjo, kwa magonjwa yanayozulika kwa chanjo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imelifanyia kazi suala hilo kwa kupitia Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 2009 kifungu 19 ambapo inawataka wazazi na walezi kuhakikisha Watoto chini ya mwaka mmoja na wajawazito wanapatiwa chanjo ili kuwakinga na magonjwa yanayozuilika na chanjo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutoa wito kwa wazazi, walezi na wajawazito kuhakikisha wanafika vituo vya kutolea huduma za afya ili kupatiwa chanjo.
MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza gharama za malipo kwa Akinamama wanaojifungua kawaida na wale wa operesheni?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dorothy George Kilave, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya inaendelea kutekeleza Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayoelekeza kutoa huduma za matibabu bure kwa makundi maalum, ikiwemo akinamama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano. (Kipengere 5.3.4 chenye Tamko linalosema “Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inayotoa huduma bila faida na mashirika ya Kimataifa itaendelea kutoa huduma bila malipo kwa wanawake wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano”).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vituo vya binafsi visivyo na ubia na Serikali ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utakapopitishwa utakuwa suluhisho la tatizo hili.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, kwa nini huduma za afya kwa Watoto Njiti zinatozwa fedha ilihali Sera ya Afya inaelekeza huduma bure kwa Watoto chini ya miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utoaji wa huduma za afya kwa watoto chini ya miaka Mitano wakiwepo Watoto Njiti kwa vituo vya Serikali na vile vya binafsi vilivyo na ubia na Serikali ni bure na ni takwa la kisera.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utamaliza utata huu kwa wananchi wanaotibiwa katika vituo binafsi vya huduma za afya.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kutoa elimu juu ya ugonjwa wa fistula?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupambana na ugonjwa wa fistula Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa njia zifuatazo: -

a. Kuzuia mimba za utotoni kupitia elimu ya uzazi kwa vijana.

b. Kuwaelemisha akinamama kuhudhuria kliniki mapema ili wapate huduma muhimu na kupata ushauri wa mpango wa kujifungua.

c. Kutoa elimu kwa wajawazito kujifungulia katika vituo vya afya ili kuwahi kupatiwa msaada kama kutatokea tatizo la uchungu pingamizi au jingine.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya upanuzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu ya majengo ya huduma za dharura, huduma za wagonjwa mahututi, huduma za mionzi ambapo majengo haya yamekamilika na yanatumika. Pia ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.8, umefanyika. Pamoja na maboresho hayo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 350 kwa ajili ya umaliziaji wa jengo la upasuaji wa mifupa ambapo jengo hili litakamilika mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya usanifu wa majengo yanayokusudiwa kujengwa ikiwa ni sehemu ya mpango wa upanuzi wa hospitali hii.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, ni lini Hospitali ya Kanda ya Kusini iliyopo Mtwara itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Kanda ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa hospitali hii inatoa huduma ya wagonjwa wa nje (OPD) na wagonjwa wa kulazwa (IPD). Aidha, Serikali itaendelea kuipa hospitali hii kipaumbele katika mpango wa bajeti ili kuhakikisha kuwa inakamilika ifikapo mwaka 2025.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali isitoe matibabu bure kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge Sikonge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Matibabu ya watoto chini ya miaka mitano wenye matatizo ya kiafya ikiwemo Selimundu ni bure kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007. Hivyo utambuzi na matibabu ya watoto wenye tatizo la selimundu hutolewa bila malipo.

Mheshimiwa Spika, suluhisho la tatizo hili ni Bima ya Afya kwa Wote.
MHE. BAHATI K. NDINGO K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha Bima za Afya za Wazee ili ziweze kutumika wakiwa nje ya Mikoa ambayo wamepewa Bima hizo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kukamilisha Muswada wa Bima ya Afya kwa wote, Serikali inaelekeza vituo vyote vya huduma kuwapatia huduma wazee wasio na uwezo waliotimiza vigezo hata wakiwa nje ya maeneo yao. Ahsante. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha Bima za Afya za Wazee ili ziweze kutumika wakiwa nje ya Mikoa ambayo wamepewa Bima hizo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na mchakato wa kukamilisha Muswada wa Bima ya Afya kwa wote, Serikali inaelekeza vituo vyote vya huduma kuwapatia huduma wazee wasio na uwezo waliotimiza vigezo hata wakiwa nje ya maeneo yao. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma za Afya kwa Wazee hasa wa Mkoa wa Arusha kwa kuwapatia dawa kupitia mfumo wa bima tofauti na iliyopo sasa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishatoa maelekezo kwa wasimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuwa wazee wasio na uwezo na waliotimiza vigezo wapewe huduma za Afya wakiwa nje na ndani ya mikoa yao. Aidha, Serikali ipo kwenye hatua ya ukamilishaji wa Muswada wa Bima ya Afya kwa wote utakaowezesha makundi yote kupata huduma za afya.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ni kutoa elimu kinga, kusomesha Madaktari Bobezi kwenye eneo hili pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba vya teknolojia ya juu katika utambuzi na tiba ya magonjwa yasiyoambukiza.
MHE. KABULA E. SHITOBELO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza kabisa tatizo la vifo vya akinamama katika Mkoa wa Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali ya Mheshimiwa kabula Enock Shitobelo Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeimarisha huduma za akina mama kujifungulia katika vituo vya huduma katika Mkoa wa Mwanza kwa kujenga vituo vya afya 22 vinavyotoa huduma za upasuaji, na inaendelea na ujenzi wa vituo vya afya 15 vitakavyotoa huduma za upasuaji mara vitakapokamilika. Aidha, serikali imeimarisha utoaji wa elimu ya Afya ya uzazi kuhusu viashiria vya hatari kwa akina mama wajawazito na kupitia ajira mpya zilizotangazwa itapeleka wataalamu zaidi ili kuhakikisha akina mama wajawazito wanapata huduma sahihi kutoka kwa wataalamu, ahsante. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya vifaa vya kufundishia na uhaba wa Wakufunzi katika Chuo cha Afya kilichopo Hospitali ya Kitete?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya vifaa vya kufundishia katika Chuo cha Afya Tabora na tayari imepeleka vifaa vyenye thamani ya Shilingi Milioni 115.7 kwa ajili ya kuboresha mafunzo kwenye chuo hicho. Pamoja na ununuzi wa vifaa hivyo, Serikali imepeleka Shilingi Milioni 267.8 kwa ajili ya ukarabati wa maabara Nne za kufundishia. Aidha, mpaka sasa Serikali imepeleka watumishi 11 wanaofundisha chuoni hapo ili kupunguza upungufu wa wakufunzi. Ahsante.
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, Serikali kwa kushirikiana na Wahisani ina mpango gani mahsusi wa kutoa Bima za Afya bure kwa watu wenye Ulemavu wa kudumu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Afya imetoa utaratibu wa kusaidia watu wenye mahitaji maalum wasio na uwezo. Hata hivyo Serikali inakamilisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ambapo utawezesha watu wote wakiwemo watu wenye ulemavu kupata huduma katika vituo mbalimbali vinavyotoa huduma za afya, ahsante.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kununua gari la utawala na gari la Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mhehsimiwa Spika, Serikali imenunua magari 727 kwa ajili ya kubebea wagonjwa na magari 146 kwa shughuli za kiutawala. Hadi sasa magari 20 yamepokelewa na magari 117 yapo njiani kutoka kwa mtengenezaji.

Mheshimiwa Spika, magari yote yanatarajiwa kuwasili nchini na kukabidhiwa katika vituo vya kutolea huduma kabla ya mwezi Juni 2023. Aidha, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Hospitali zitakazopata mgao wa magari hayo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawaajiri Wataalam wanaojitolea kwa muda mrefu kufanya kazi katika Hospitali mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwenye hospitali zetu kumekuwa na watumishi wanaojitolea. Wizara imetoa Mwongozo wa kuwalipa nusu mshahara kwa mapato ya ndani. Hata hivyo hospitali zetu za Mikoa, Kanda na Taifa zimeweza kuwalipa hadi asilimia 40 ya watumishi wote wanaojitolea mshahara kamili kwa kutumia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Spika, Wizara itashirikiana na Wizara ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuona namna bora ya kuwapa kipaumbele kwenye ajira watumishi ambao wamekuwa wakijitolea kwenye vituo vya huduma za Afya kuliko walioko nje wakisubiri ajira.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi wa Afya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu mwaka 2018 ilikuwa na watumishi 130. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wizara iliwapanga watumishi 70 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu na kuhamisha wengine 18 hivyo kufanya jumla ya watumishi kuwa 218.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuwapanga watumishi katika mikoa hii ya pembezoni mwa nchi ili kufikia malengo kwa kadri tutakapokuwa tunapata vibali vya kuajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -

Je, lini Serikali itapitia upya masharti ya fomu za bima ya afya ili kuondoa upotevu wa fedha za Vituo vya Afya kwa kushindwa kujaza fomu hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini na Balozi wa Afya ya Akili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, makato ya madai ya bima ya afya kwa watoa huduma za afya hayasababishwi na vipengele vilivyoainishwa katika fomu za bima ya afya (Fomu 2A na B). Sababu za Makato ya madai husababishwa na: -

(i) Kutozingatiwa kwa miongozo ya Tiba nchini inayotolewa na Wizara ya Afya;

(ii) Baadhi ya watoa huduma kuwasilisha madai yenye udanganyifu katika utoaji wa huduma;

(iii) Kutozingatiwa kwa bei zinazoainishwa katika Mkataba wa Huduma baina ya Mfuko na Watoa Huduma; na

(iv) Kutozingatiwa kwa taratibu za uwasilishaji wa madai ulioainishwa na Mfuko kwa mujibu wa Mkataba.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -

Je, ni lini changamoto ya ukosefu wa Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete itatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kitete hadi sasa ina jumla ya Madaktari Bingwa watano, ambapo Daktari Bingwa wa Afya ya akina mama na Uzazi mmoja, Madaktari Bingwa wa Watoto watatu na Daktari Bingwa wa Upasuaji ni mmoja.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza idadi ya Madaktari Bingwa, Wizara imepeleka kusoma jumla ya Madaktari - sita kutoka hospitali ya Rufaa ya Kitete ambao Madaktari - wawili wanasomea ubingwa wa magonjwa ya ndani, Daktari wa Magonjwa ya Kinywa, Sikio na Koo - mmoja, Ubingwa katika Mionzi ni mmoja, Ubingwa katika magonjwa ya dharura mmoja na Daktari Bingwa wa Afya ya akina Mama na Uzazi ni mmoja.

Mheshimiwa spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti matumizi holela ya Dawa za Binadamu nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti matumizi holela ya dawa za binadamu nchini Serikali inatekeleza mambo yafuatayo: -

(i) Kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ikiwemo vipindi vya elimu kwa umma kwa kutumia wataalamu wa dawa.

(ii) Kusimamia muongozo wa matibabu nchini unaobainisha matibabu kwa kila ugonjwa ikiwemo dawa zinazohitajika kutibu magonjwa hayo.

(iii) Kusimamia weledi wa watoa dawa katika maeneo yote yanayohusika na utoaji wa dawa kama vile maduka ya dawa na vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutoa bima za afya kwa wafungwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdulkarim Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hakuna mpango mahususi wa bima ya afya kwa kundi la wafungwa. Katika kuhakikisha kuwa wafungwa wanapata haki yao ya msingi ya kupata huduma ya afya, Serikali imeweka utaratibu maalum wa kutoa huduma za matibabu kwa wafungwa katika magereza mbalimbali nchini kupitia vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakamilisha Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo utakapokamilika utakuwa suluhisho la upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi yote ya kijamii wakiwemo wafungwa. Naomba kuwasilisha.
MHE. YAHAYA O. MASSARE K.n.y MHE. TOUFIQ S. TURKY aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa Saratani nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taufiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitumia njia mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na ugonjwa wa saratani kupitia vipindi vya redio na televisheni, machapisho na magazeti, mitandao ya jamii kama Facebook, Instagram na pia televisheni sehemu za kusubiria wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kutoa elimu ya ugonjwa wa saratani kama ifuatavyo: -

(i) Kuandaa kampeni mbalimbali za uelimishaji wa jamii na uchunguzi wa awali wa saratani nchini ikiwemo huduma Mkoba.

(ii) Kuandaa mtaala wa mafunzo wa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani kwa watoa huduma wa ngazi za msingi ili kuwajengea uwezo wa kutoa elimu kwa jamii.

(iii) Kuandaa vipindi mbalimbali na machapisho ya utoaji wa elimu ya afya dhidi ya magonjwa yasisyo ya kuambukiza ikiwemo saratani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imejenga nyumba 50 za watumishi zenye thamani ya shilingi bilioni 3.4 katika Hospitali za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwemo nyumba moja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashauriano yanaendelea ndani ya Serikali ili kukamilisha mchakato wa kuhamisha gereza la mkoa ili kutoa nafasi ambayo itawezesha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kuendelea na upanuzi wa huduma mbalimbali ikiwemo ni pamoja na ujenzi wa nyumba za Madaktari.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuupitia tena Muundo wa Utumishi wa Madaktari Bingwa wa mwaka 2022?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Na.1 wa mwaka 2009 kwa kada zilizo chini Wizara ya Afya ambao umeainisha miundo na sifa za wataalam mbalimbali wanaopaswa kuajiriwa na kufanya kazi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inakamilisha Mapitio ya Miundo ya kada za afya ambayo inatarajiwa kukamilika Mwezi Mei, 2023 na kuwasilishwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata idhini. Miundombinu hii itakapokamilika itaweza kukidhi mahitaji ya kiutumishi kwa wataalam mbalimbali wa afya wakiwemo Madaktari Bingwa.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na ongezeko la Wagonjwa wa Kansa ya Kizazi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali katika kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa kansa ya kizazi, kwa kufanya yafuatayo: -

Moja, kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na ugonjwa wa saratani kupitia vipindi vya redio, televisheni, machapisho na magazeti, mitandao ya jamii kama facebook, Instagram na pia televisheni za sehemu za kusubiria wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Pili, Serikali inatoa chanjo kwa wasichana ili kuwakinga na kirusi kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi.

Tatu, kuanzisha huduma za awali za uchunguzi na matibabu ya saratani ya mlango wa kizazi kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za Taifa.

Nne, Serikali imeimarisha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu kwa kuhakikisha uwepo wa wataalamu na vifaa tiba kwa ajili ya kukabiliana na Saratani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha huduma za dialysis kwa Wagonjwa wenye kipato cha chini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa huduma za matibabu ikiwemo huduma ya kusafisha figo (dialysis) kwa wagonjwa wote bila kujali kipato cha mgonjwa husika. Huduma hizi kwa sasa zinatolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na Hospitali Maalum, ikiwemo Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa wananchi wenye kipato kidogo kufuata taratibu zinazopelekea wao kupata misamaha ya huduma ikiwemo huduma hii ya usafishaji wa figo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. FURAHA N. MATONDO K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELO aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza wauguzi katika Hospitali ya Bugando kwani kwa sasa ina upungufu wa wauguzi 1,200?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Bugando ina watumishi jumla 1,930, wauguzi wakiwa 667. Katika watumishi hawa wote, Serikali inawalipa mishahara watumishi 1,120. Hopsitali ya Bugando kwa mapato yake ya ndani inawalipa watumishi 2,205 mishahara kamili pia inawalipa watumishi 605 nusu mshahara.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga hospitali kubwa katika Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera una Hospitali kubwa ya Mkoa ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imekamilisha jengo la huduma za dharura (EMD) ambalo limegharimu shilingi 560,000,000, jengo la uangalizi (ICU) lililogharimu shilingi 650,000,000, jengo la huduma za mionzi (Radiology) lililogharimu shilingi 237,000,000, nyumba ya mtumishi iliyogharimu shilingi 90,000,000 pamoja na ununuzi na ufungaji wa mashine ya CT-Scan ambayo imegharimu kiasi cha shilingi 1,810,000,000 na huduma zimeanza kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kupeleka fedha zaidi kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera ikizingatia pia kuboresha eneo la majanga na magonjwa ya mlipuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, upi mkakati wa kutokomeza wizi wa dawa na vifa vya afya, hatua zilizochukuliwa kwa wahusika na fedha zinazopotea kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Suala la kupambana na wizi na ubadhirifu wa bidhaa za afya si la Serikali pekee bali ni suala letu sisi wote, hasa wawakilishi wa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali katika kutatua tatizo la wizi wa dawa na vifaa tiba kama ifuatavyo: -

a) Kufanya agenda ya ulinzi wa bidhaa za afya kuwa agenda ya kudumu katika vikao vya kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya.

b) Kujenga uwazi wakati wa kupeleka bidhaa za afya na kuwapa wakuu wa wilaya na Wabunge nyaraka za makabidhiano ya dawa na vifaa tiba kwa ajili ya rejea.

c) Kuimarisha mifumo ya usimamizi wa bidhaa za afya ikiwemo kufunga mifumo ya kielektroniki pamoja na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara.

d) Kuimarisha kamati za usimamizi za vituo kwa kuzijengea uwezo kuhusu majukumu yao katika usimamizi wa bidhaa za dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilifanya uchunguzi wa ubadhilifu wa bidhaa za afya na taarifa kuwasilishwa kwenye semina ya wabunge, na kupelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kufanya thamani halisi ya bidhaa zilizopotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -

Je, hadi sasa hali ya ugonjwa wa figo ipoje nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarim Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika hapa nchini Tanzania katika jamii ulionyesha kuwa asilimia saba ya Watanzania wanaishi na ugonjwa wa figo, ambao kwa kiasi kikubwa unahusishwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa sukari na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe rai kwa wananchi kupima afya mara kwa mara kwani kwa kuchelewa kutambua tatizo la afya madhara yake ni makubwa na gharama ya matitabu inakuwa kubwa.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kumaliza upungufu wa madawa na vifaa tiba katika hospitali zetu nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali zetu nchini kwa kutekeleza yafuatayo: -

(1) Kuipatia mtaji Bohari ya Dawa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuwa na bidhaa za afya muda wote;

(2) Serikali kutoa fedha za ununuzi wa bidhaa za afya kila mwezi kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali;

(3) Kuhakikisha suala la usimamizi wa bidhaa za afya linakuwa sehemu ya ajenda ya kudumu ya Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa;

(4) Kuwasimamia watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuweza kukadiria makadirio sahihi (forecasting); na

(5) Vituo vya kutolea huduma za afya kutumia fedha zinazotokana na malipo ya huduma na dawa kununua bidhaa za afya kuliko kutegemea fedha zinazotolewa na Serikali pekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. HAWA M. CHAKOMA K.n.y. MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isiwekeze fedha Kiwanda cha Viuadudu Kibaha ili kutokomeza malaria nchini?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali na Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mhemishimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2023, Serikali imenunua viuadudu vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.9 na kutumika katika ngazi ya halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa viuadudu kutoka Kiwanda cha Kibaha, kwa kipindi cha mwaka 2024 - 2026, Wizara ya Afya imeomba kupatiwa jumla ya shilingi bilioni 129.1 kwa ajili ya utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji wa viuadudu ili kuangamiza viluilui vya mbu kwenye mazalia ili kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya inashirikiana na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Viwanda kuhakikisha kiwanda kinapata ithibati kutoka Shirika la Afya Duniani ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza afua hii kutoka kwa wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanzisha Mamlaka ya Kuratibu na Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imekwishaunda programu maalum ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ndani ya Idara ya Tiba ambayo ina jukumu la kuandaa miongozo na mikakati ya kisekta kwenye mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu imekwishatekeleza jukumu hili kwa kukiongezea jukumu Kitengo cha Afya Moja (One Health) kusimamia magonjwa yasiyoambukiza chini ya Kurugenzi ya Menejimenti ya Maafa, naomba kuwasilisha.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-

Je, Tanzania ina Madaktari Bingwa Wazalendo wa magonjwa ya binadamu wangapi na katika magonjwa gani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adamu Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Tanzania ina jumla ya Madaktari Bingwa Wazalendo 2,469 ambao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika kwa fani mbalimbali za Udaktari Bingwa. Kati yao Madaktari Bingwa 2,098 wapo katika Sekta ya Umma na Madaktari Bingwa 371 wapo Sekta Binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Madaktari hawa wamegawanyika katika maeneo 28 ya Ubingwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JACQUILINE N. MSONGOZI aliuliza: -

Je, lini Serikali itatoa fidia kwa Madaktari na Manesi wanaopoteza maisha wakihudumia Wagonjwa wa Magonjwa ya Mlipuko?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Msongozi Ngonyani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kujali mchango mkubwa wa Watumishi wanaohudumia wagonjwa wa magonjwa ya milipuko wakiwemo Madaktari na Wauguzi. Aidha, napenda kufahamisha Bunge lako tukufu kwamba Serikali hutoa fidia kwa watumishi waliofariki kwa sababu za kuwahudumia wagonjwa, wa magonjwa ya mlipuko kwa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura ya 263, marejeo ya Mwaka 2015 kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Tanzania. Fidia zinazotolewa ni pamoja na gharama za mazishi na pensheni kwa wategemezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kusaidia upatikanaji wa Bima ya Afya kwa watoto wasio na wazazi ambao walikuwa wakilipiwa bima na wahisani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrissa Juma, Mbunge wa Mtoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa mfumo wa kulipia watoto kupitia Toto Afya Kadi umebadilika na kwa sasa unafanyika kupitia utaratibu wa shule na vifurushi vya bima ya afya vya najali, wekeza na Timiza.

Mheshimiwa Spika, suluhisho la kudumu la tatizo hili, ni kukamilika kwa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao tunaamini utawezesha watoto wengi zaidi wasio na changamoto ya kiafya na wenye changamoto za kiafya kulipiwa Toto Afya Kadi. Hatua hii itasababisha kuwepo kwa uhai na uendelevu wa Mfuko wa Bima ya Afya, naomba kuwasilisha.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo la ukosefu wa dawa kwa wazee wanaopata huduma ya matibabu bure katika hospitali nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ukosefu wa dawa kwa wazee, Serikali imeamua dawa ambazo zinatumika sana na wazee zilizokuwa hazitolewi kwenye vituo vya afya na zahanati zianze kutolewa katika ngazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imewajengea uwezo watumishi wa vituo vya huduma za afya ili kuweza kufanya maoteo halisi kulingana na mahitaji ya dawa ya vituo husika.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza gharama za matibabu kwa akina mama wanapokwenda Kliniki Sumbawanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Afya ya mwaka 2007 kifungu Na. 5(3) na (4)(c) kinaelekeza kuwa huduma za afya ya uzazi ikiwemo kuhudhuria kliniki, wakati wa uchungu, wakati wa kujifungua, na baada ya kujifungua pamoja na uzazi wa mpango zitakuwa zikitolewa bila malipo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kutowatoza gharama za uzazi wanawake wote wanaofika vituoni kupata huduma ya afya ya uzazi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. SALMA R. KIKWETE K.n.y. MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza:-

Je, Serikali inafanya nini kuhakikisha uviaji mimba usio salama unakwisha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha uavyaji mimba usio salama unakwisha kama ifuatavyo: -

(i) Kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike ambao wapo chini ya umri wa kuzaa, klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe ili kuepuka kupata mimba zisizotarajiwa.

(ii) Kusimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo ili kuwawezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwaasa vijana, akina mama na wanaume wote kwa pamoja wachukue hatua za kuhakikisha kuwa mimba zinazopatikana zinakuwa zimepangwa na wawe wanahudhuria katika kliniki zetu za uzazi wa mpango ili waweze kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa ili kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama, ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza huduma za afya na dawa zinazotolewa na Bima katika zahanati na vituo vya afya?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuongeza huduma za afya na dawa zinazotolewa na bima katika Zahanati na Vituo vya Afya imefanya yafuatayo:-

(i) Kuongeza idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya zahanati kutoka aina 254 mwaka 2015 hadi kufikia aina 451 mwaka 2023.

(ii) Kuongeza idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya kituo cha afya kutoka aina 414 mwaka 2015 hadi kufikia aina 828 mwaka 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa zilizoongezeka zipo katika miongozo ya Serikali na hivyo zinalipiwa na Bima ya Afya kwa wanufaika wa mfuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuongeza dawa Serikali imeboresha miundombinu, uwepo wa vifaatiba, huduma za maabara pamoja na rasilimali watu. Hata hivyo, Serikali inatambua kwamba kuna maeneo ya nchi ambayo uboreshaji huu haujafikia, hivyo ipo katika mikakati wa kuyafikia maeneo hayo.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, ni kwa nini Wananchi wanaotumia Bima ya Afya wanalalamika kuhusu huduma wanazopatiwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekuwa ni nguzo muhimu katika uboreshaji wa huduma za Afya Nchini ambapo Taasisi Binafsi za Afya pamoja na Vituo vya Huduma za Afya vya Serikali vimeonekana kutoweza kujiendesha bila uwepo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kutokana na Watanzania wenye uwezo wa kulipa fedha taslimu kuwa wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 ya mapato ya vituo vya huduma za Afya vya Serikali pamoja na binafsi vinategemea Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri hayo kumekuwepo na changamoto za kimiongozo ambapo dawa chache zilikuwa zinatolewa katika zahanati na vituo vya Afya. Serikali imefanya maboresho kwa kuongeza idadi ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambapo kwa ngazi ya zahanati imeongeza kutoka aina 254 hadi 451 na kwa ngazi ya vituo vya Afya toka aina 414 hadi 828.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi milioni 725 kwa ajili ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza (2021 – 2026) ambapo umeainisha mikakati mahususi ya udhibiti wa visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni kuimarisha uratibu na ushirikishwaji wa sekta mtambuka; Kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma; Kuwajengea uwezo watumishi katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza; Kuimarisha na kusimamia shughuli za utafiti; pamoja na kuhamasisha wananchi kuhusu njia za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Njia hizi ni kufanya mazoezi, pamoja na kuzingatia kanuni bora za lishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA K.n.y. MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka vifaa kwenye Jengo Jipya la Mama na Mtoto katika Hospitali ya META Mkoani Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaatiba kwa ajili ya jengo la huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Meta, Mkoa wa Mbeya. Aidha, vifaatiba hivyo vimeshaanza kupelekwa na kufungwa katika jengo la Mama na Mtoto kupitia Bohari Dawa (MSD).

Mheshimiwa Naibu Spika, jengo hili limeanza kutumika na ufungaji wa vifaatiba katika vitengo mbalimbali unaendelea na utakamilika mapema mwezi Julai, 2023. Naomba kuwasilisha.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza:-

Je, Serikali ina mchango gani katika kuboresha huduma za Hospitali ya KCMC ambayo inatoa huduma za afya kwa Kanda ya Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeboresha huduma za Hospitali ya KCMC kwa kupeleka fedha za miradi mbalimbali, kulipia mishahara pamoja na ufadhili wa masomo kwa wataalam kama ifuatavyo:-

(i) Serikali inalipa stahiki na mishahara ya watumishi 905 waliopo KCMC ambapo jumla ya shilingi 983,612,500 hutumika kila mwezi.

(ii) Katika Mwaka wa Fedha 2023 Serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya dawa, vitendanishi na vifaatiba.

(iii) Katika mwaka wa fedha 2023 Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya hospitali na shilingi milioni 263.6 kwa ajili ya uendeshaji.

(iv) Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa ufadhili wa masomo ya ubingwa bobezi kwa watumishi 15 kada ya afya wa KCMC wanaosoma ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuwasajili wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati kwenye utaratibu wa Bima ya NHIF?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeanzisha mpango wa bima ya afya kwa wanafunzi wa ngazi zote kwa kuchangia shilingi 50,400 kwa mwaka ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu wakiwa masomoni, likizo na wakati wa mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2023 mfuko umeshasajili jumla ya wanafunzi 342,933 ikiwemo wa Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu. Zoezi hili la kusajili wanafunzi ni endelevu kupitia shule na vyuo.
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza:-

Je, nini chanzo cha ugonjwa wa manjano kwa watoto wachanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tafiti nyingi zimefanyika Kitaifa na Kimataifa kujua chanzo cha watoto wachanga kugeuka njano mara baada ya kuzaliwa. Tafiti hizo zimeonesha kuwa hali ya umanjano hutokea ndani ya masaa 24 baada ya kuzaliwa inaonyesha tatizo la kiafya na linahitaji kutambua sababu na kutoa tiba stahiki.

Mheshimiwa Spika, tatizo hili likitokea baada ya masaa 24, mara nyingi linatokana na sababu za kawaida za mwili wa mtoto kupunguza chembechembe nyekundu nyingi alizokuwa nazo tumboni kwa mama, hata hivyo hili pia uchunguzi wa kina ni muhimu ili kujihakikishia.

Mheshimiwa Spika, suala la utafiti ni muhimu na ni suala endelevu katika tiba.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana wakati wote katika hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, Serikali inatekeleza na kusimamia yafuatayo:-

i. Kuiwezesha MSD mtaji ili iweze kufanya kazi kama bohari ya dawa badala ya kufanya kazi kama idara ya manunuzi,

ii. Utoaji wa fedha za kununua, kutunza na kusambaza dawa kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 16,

iii. Kuboresha utendaji wa MSD na kuiwezesha kuwa na mikataba ya muda mrefu ya ununuzi wa dawa,

iv. Kuboresha maoteo ya bidhaa za afya na kuchukua hatua kwa upungufu unaobainika,

v. Kufunga mifumo ya kielektroniki ili kuimarisha usimamizi wa dawa na kuwezesha dawa kutolewa kulingana na wagonjwa husika,

vi. Kusimamia Muongozo wa matibabu katika kuhakikisha dawa zinazonunuliwa, kutunzwa na kuandikwa na Madaktari zinazingatia muongozo wa matibabu,

vii. Kudhibiti mianya ya upotevu na wizi kwa kuwa na kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha dawa zinakuwepo vituoni,

viii. Kuanzisha maduka ya dawa ya hospitali za umma yatakayokuwa na dawa muda wote kwa ajili ya wagonjwa wa ndani na nje ya hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuzielekeza Halmashauri na viongozi wote wa vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanatumia zaidi ya asilimia 50 ya mapato yao kununua dawa na bidhaa nyinginezo za afya.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza:-

Je, ni kwa namna gani Serikali inalinda afya ya mama mjamzito na mtoto mchanga?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kulinda afya ya mama mjamzito na mtoto mchanga, Wizara inafanya yafuatayo:-

(1) Kila mama mjamzito anayehudhuria kliniki anapata vipimo muhimu ikiwemo vipimo vya wingi wa damu, shinikizo la damu na kipimo cha protini kwenye mkojo ili kubaini mapema matatizo ya ujauzito;

(2) Matibabu na huduma ya mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano yanatolewa bila malipo katika vituo vyote vya Serikali;

(3) Serikali imeimarisha upatikanaji wa vifaa tiba kwa ajili ya kutibu matatizo yatokanayo na uzazi kwa kufikia asilimia 50 kwa vituo vyote vya kutolea huduma; na

(4) Watoa huduma za afya ya uzazi wamejengewa uwezo ili waweze kutoa huduma stahiki kwa akina mama wanaopata changamoto za uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa wananchi wote hasa akina mama wajawazito kuhakikisha wanahudhuria kliniki na pia kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza vifo vya watoto wenye umri kati ya sifuri hadi mwaka mmoja?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka mipango ya kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa sifuri hadi mwaka mmoja kama ifuatavyo: -

Moja, kuongeza vituo vyenye vyumba maalumu kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye hali mahututi (Neonatal Care Unit) kutoka 18 mwaka 2017 kufikia 175 mwaka 2023.

Pili, kutoa mafunzo kwa watoa huduma juu ya namna ya kutoa huduma jumuishi kwa watoto wachanga na watoto wakubwa (Integrated Management of Childhood Illness-IMCI).

Tatu, kuimarisha huduma za kukinga na kuzuia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kama vile surua, nimonia, kuharisha, donda koo, kifaduro, pepo punda na polio kwa kuongeza utoaji wa chanjo za watoto chini ya mwaka mmoja kufikia kiwango cha zaidi ya asilimia 98 ya utoaji wa chanjo ya Penta 3.

Nne, Serikali imeongeza vituo vinavyotoa huduma kwa watoto waliozaliwa wakiwa na uzito pungufu (Kangaroo Mother Care) ambapo kwa sasa vituo 72 na Hospitali 175 zinatoa huduma hizi. Aidha, kwa mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kuongeza vituo 100 ili kufikia vituo 275 ifikapo mwezi Juni, 2024.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadeta Kasabago, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza afua kuu zifuatazo katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria: -

(i) Udhibiti wa mbu waenezao Malaria kupitia njia kuu zifuatazo:-

(a) Kusambaza vyandarua vyenye dawa kwa jamii kupitia kampeni za kugawa vyandarua kwa kila kaya; kliniki za mama wajawazito, watoto na vituo vya kutolea huduma kwa makundi maalum kama wazee.

(b) Upuliziaji wa dawa ukoko kwenye kuta ndani ya nyumba katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria.

(c) Unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ili kuuwa viluilui wa mbu.

(ii) Kuhakikisha vipimo na dawa za malaria zinapatikana wakati wote katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Vipimo na dawa za Malaria zinapatikana bila malipo kwenye vituo vyote vya kutolea huduma vya Serikali.

(iii) Kuhamasisha jamii kutumia njia mbalimbali za kujikinga na ugonjwa wa malaria.

Mheshimiwa Spika, ili kuharakisha kufikiwa kwa azma ya kutokomeza ugonjwa wa malaria hapa nchini, Serikali imeanzisha Baraza la Kutokomeza Malaria (End Malaria Council) lililozinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 25 Aprili, 2023. Ahsante.
MHE. STELLA I. ALEX K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurahisisha huduma ya upatikanaji wa bima ya afya kwa wananchi wake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua ya ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ambao utawezesha kurahisisha huduma ya upatikanaji wa bima za afya kwa wananchi wote. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:-

Je kuna Sheria ya Huduma ya Afya inayosimamia utoaji na upatikanaji wa huduma za afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya inasimamia Sheria zifuatazo thelathini zinazolenga kusimamia ubora, utoaji wa huduma, maadili ya kitaaluma, kiutumishi na upatikanaji wa huduma za afya nchini, ahsante.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha Kitengo cha Watoto Njiti katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa sasa ina sehemu maalum yenye uwezo wa kulaza Watoto Njiti 18 kwa wakati mmoja. Hata hivyo, ujenzi unaendelea wa Bilioni 1.2 utakaowezesha hospitali kuwa na vitanda 42. Kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 zimetengwa Shilingi Bilioni Sita kwa ajili ya ujenzi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa Vyumba vya kuhifadhi maiti nchini vinakuwa na majokofu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zakharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hospitali zote 28 za Rufaa za Mikoa zina majokofu ya kuhifadhia maiti. Pia hospitali 16 za Mikoa zimepewa majokofu mapya kati ya hospitali 28 za Rufaa za Mikoa. Aidha, Serikali inatambua kuwa tatizo kubwa la upungufu lipo kwenye hospitali za Wilaya na vituo vya Afya vipya. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imepanga kununua majokofu 103 kwa ajili ya kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa bei elekezi ya vifaa vya tiba hasa vya macho, pua na koo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeandaa kanuni za kudhibiti bei za dawa na tayari zimekwishawasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Bei elekezi za vifa tiba zitaandaliwa mara baada ya kukamilika kwa kanuni za bei za dawa elekezi. Ahsante.
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutoa matibabu bure kwa maradhi yasiyoambukiza kama kisukari, pressure na shinikizo la damu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Jimbo la Chaani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza yana gharama kubwa na yanahitaji tiba wakati wote. Serikali imekuwa ikitoa msamaha wa matibabu kwa wagonjwa ambao wamethibitika hawana uwezo wa kugharamikia matibabu hayo kwa mujibu wa Sheria ya Afya. Hata hivyo, Serikali ipo katika hatua ya mwisho za ukamilishaji wa Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ambao utawezesha wananchi wote kupata huduma za afya katika Vituo vya Afya nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaboresha Kitengo cha Watoto Njiti katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa sasa ina sehemu maalum yenye uwezo wa kulaza Watoto Njiti 18 kwa wakati mmoja. Hata hivyo, ujenzi unaendelea wa Bilioni 1.2 utakaowezesha hospitali kuwa na vitanda 42. Kwenye bajeti ya mwaka 2022/2023 zimetengwa Shilingi Bilioni Sita kwa ajili ya ujenzi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE K.n.y. MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza: -

Je, Serikali haioni kuna haja ya watoto wachanga kutumia Bima za Afya za Mama zao?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Nehemia Gwau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa kukitokea changamoto kwa wazazi wenye bima wanaojifungua watoto wao kushindwa kupata huduma hasa kwenye vituo vya huduma za afya vya sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Afya alishatoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha watoto wachanga wenye uhitaji wa huduma wanapata huduma za afya bila kikwazo chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuelekeza Watendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya na vituo vyote vya huduma za afya nchini kuhakikisha watoto wanapata huduma kwani Mama yupo na kadi yake inayoonesha ushahidi wote kuhusu mtoto husika na ni mtoto wa ngapi kwenye familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaasa wazazi na viongozi wa hospitali husika kukomesha kabisa matukio ya kughushi nyaraka ambayo pia ndiyo yanapelekea kuwepo na usumbufu wakati mwingine. Naomba kuwasilisha.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: -

Je, lini Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuanza Ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Magharibi ambapo ujenzi utaanza na jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD).

Mheshimiwa Spika, ujenzi huu utaanza mwezi Januari 2024, ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, kwa nini NHIF inazuia matibabu ya baadhi ya wagonjwa wenye Bima za Afya wakiwa hospitali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwa na zoezi la uhakiki wa uhalali wa wanufaika wa Mfuko wa Bima ya Afya. Zoezi hilo lilileta usumbufu ambao ungeweza kuzuilika kama wahakiki hao wangetumika wataalamu wenye miiko ya taaluma ya tiba. Wizara ilipopata malalamiko hayo ilifuatilia mara moja na kufanya maboresho ambayo yaliyoondoa usumbufu kwa wateja.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuielekeza Menejimenti ya Mfuko wa Bima ya Afya katika kipindi cha miezi mitatu, ihakikishe inaboresha mifumo ya TEHAMA itakayoweza kuondoa usumbufu na pia kudhibiti udanganyifu pasipo kuwa kero kwa wanufaika wa Mfuko, naomba kuwasilisha.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusamehe gharama za matibabu kwa marehemu ili kupunguza maumivu kwa wafiwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilishatoa maelekezo kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kupitia Waraka Na. 1 wa 2021, wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya pamoja na Waganga Wafawidhi wa hospitali kwa ngazi zote nchini, kuzingatia maelekezo ya mwongozo huu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma pasipo kuwepo kwa vikwazo vya kuchelewesha marehemu kuzikwa.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi wa kutosha katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyopo Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mtwara ilizinduliwa mwezi Oktoba, 2021 ikiwa na watumishi 45. Kwenye kibali cha sasa cha ajira imepangiwa watumishi wapya 112 itakayofanya idadi ya watumishi kufikia 157 mwezi Julai, 2022, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-

Je, ni lini ombi la kubadilishana Hospitali ya Mkoa na ya Wilaya litafanyiwa kazi kuruhusu upanuzi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, hivyo mwezi Julai 2022 timu ya wataalamu itakwenda Mkoani Iringa ili kuja na ushauri wa kitaalamu wa namna ya kutekeleza suala hili bila kuathiri mfumo wa utoaji wa huduma za afya katika Mkoa, ahsante.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga uzio katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huu utaanza mwezi Januari, 2024 na kukamilika mwezi Septemba, 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. FURAHA N. MATONDO aliuliza: -

Je, lini Bima ya Afya kwa watu wote itaanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Furaha Ntengo Matondo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ilipitishwa na Bunge tarehe 1 Novemba, 2023 na Mheshimiwa Rais ameidhinisha sheria hiyo tarehe 19 Novemba, 2023 na imechapishwa katika gazeti la Serikali la tarehe 1 Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambapo kwa mujibu wa Kifungu cha kwanza cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Waziri anaweza kuteua baadhi ya vifungu vya kuanza kutumika. Baadhi ya vifungu ambavyo vinaweka mifumo imara ya kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote vimeainishwa na kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sheria itatangazwa kuanza kutumika kabla ya mwisho wa mwezi wa Aprili, 2024 kwa tarehe itakayotajwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. TARIMBA G. ABBAS aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali juu ya Bima za Afya kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimba Gulam Abbas, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali kuhusu Bima ya Afya kwa Watoto ni kuwaomba Watanzania wote, viongozi wote, kisiasa, kidini na kimila kuwa suluhu pekee ni sisi wote kuungana na Serikali katika kuhamasisha umma kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote pale utekelezaji utakapoanza, naomba kuwasilisha.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza: -

Je, ni lini jengo la huduma ya usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo litajengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Jimbo la Mpanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ambapo kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi 224,750,000 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma ya usafishaji damu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, suala la vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama lina ukubwa na madhara gani nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa, matatizo yatokanayo na utoaji mimba ni moja ya sababu inayochangia vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara yanayotokana na utoaji wa mimba usio salama ni pamoja na maambukizo makali kwa mfumo wa uzazi ambao unaweza kupelekea mgonjwa kutolewa mfuko wa uzazi na wakati mwingine kupoteza maisha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga uzio katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa wa ndani pamoja na ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. FURAHA N. MATONDO aliuliza:-

Je, lini Bima ya Afya kwa watu wote itaanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Furaha Ntengo Matondo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ilipitishwa na Bunge tarehe 1 Novemba, 2023 na Mheshimiwa Rais ameidhinisha sheria hiyo tarehe 19 Novemba, 2023 na imechapishwa katika gazeti la Serikali la tarehe 1 Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambapo kwa mujibu wa Kifungu cha kwanza cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Waziri anaweza kuteua baadhi ya vifungu vya kuanza kutumika. Baadhi ya vifungu ambavyo vinaweka mifumo imara ya kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote vimeainishwa na kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sheria itatangazwa kuanza kutumika kabla ya mwisho wa mwezi wa Aprili, 2024 kwa tarehe itakayotajwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: -

Je, lini Serikali itatumia drones kusambaza dawa katika Zahanati zetu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilishakamilisha mfumo ambao unahifadhi taarifa zote za vituo kuanzia ngazi ya zahanati hadi Taifa. Mfumo huu utasaidia kupata taarifa za kijiografia (Geo coordinates) za vituo vyote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tupo kwenye hatua ya kuingiza vituo vyote kwenye mfumo huu ili kuufanyia majaribio na pia kutazama gharama za usafirishaji dawa kupitia mfumo huo wa ndege maalum (drone) ukilinganisha na usafirishaji kwa njia ya magari ili maamuzi sahihi yafanyike katika kutekeleza wazo hili zuri la Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR aliuliza:-

Je, tafiti zipi ambazo Taasisi za Tiba Asili zimekamilisha na kuweza kuwa suluhisho la maradhi mbalimbali kama Tiba Mbadala?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdallah Ameir, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021 – 2024 zaidi ya tafiti 50 zimefanyika ndani ya nchi juu ya ubora na usalama wa dawa zinazotumika kwa tiba asilia kwa kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Mheshimiwa Spika, baadhi ya tafiti hizo ni pamoja na utafiti wa dawa ya Saratani ya NIMREGENIN, Dawa ya TANGHESHA inayotibu Selimundu, Dawa ya PERVIVIN inayotibu tezi dume, Dawa ya WARBUGISTAT inayotibu magonjwa nyemelezi na Dawa ya NIMRICAF inayosaidia mfumo wa upumuaji.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka Watumishi pamoja na Vifaa Tiba katika Hospitali ya Mkoa wa Geita?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mkoa wa Geita ina jumla ya watumishi 349. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imepeleka watumishi 22 wa kada mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita. Pia Serikali imepeleka vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga jengo la kuhifadhia Maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024 Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 12.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi utaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 na kukamilishwa mwaka wa fedha 2024/2025. Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wagonjwa wa figo kupata matibabu ya kusafishwa figo kwa gharama nafuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassor Kisangi, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali katika kupunguza gharama za kusafisha figo ni kununua vifaatiba na vitendanishi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji. Pia Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utakapokamilika utakuwa suluhisho la kudumu. Hata hivyo, sera ya afya ya nchi inaelekeza hakuna Mtanzania anayetakiwa kufa kwa sababu ya kukosa fedha, hivyo Serikali imekuwa ikitoa msamaha kwa wasio na uwezo na waliotimiza vigezo.
MHE. AMINA ALI MZEE K.n.y. MHE. TAUHIDA C. GALLOS aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha Sera ya Wazee kupata matibabu bure inatekelezwa katika kila Kituo cha Afya nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wazee wasio na uwezo wa kugharamia huduma za afya wameendelea kupatiwa huduma hizo kwa utaratibu wa msamaha. Hata hivyo, ni kweli kuna changamoto kwenye baadhi ya maeneo. Kuanza kwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote itakuwa suluhu ya kudumu katika kutatua tatizo hilo.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, upi mpango wa kurejesha TFDA kwani imeacha masuala ya chakula na inakinzana na utaratibu wa usimamizi wa chakula na madawa duniani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kuimarisha mazingira ya biashara nchini ilifanya maamuzi kupitia Bunge lako Tukufu ya kuhamisha majukumu ya usimamizi na udhibiti wa ubora wa chakula na vipodozi kutoka iliyokuwa TFDA na kuyapeleka TBS ambako ndiko afua zote za usimamizi zinatekelezwa huko kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kurejesha usimamizi huo kwa TMDA bado linaendelea kujadiliwa ndani ya Serikali na mara litakapokamilika mapendekezo ya utekelezaji yatawasilishwa Bungeni. Naomba kuwasilisha.
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:-

Je, ni kweli kauli ya Serikali kwa hospitali kutozuia maiti kwa sababu ya deni la matibabu ni ya kisiasa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilishatoa maelekezo kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kupitia Waraka Na. 1 wa mwaka 2021 wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya pamoja na Waganga Wafawidhi wa Hospitali kwa ngazi zote nchini kuzingatia maelekezo ya mwongozo huu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma pasipo kuwepo kwa vikwazo vinavyochelewesha marehemu kuzikwa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Je, ni madhara gani humpata mtoto anapozaliwa na kuchelewa kulia au kutolia kabisa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, madhara yanayoweza kumpata mtoto anapozaliwa na kuchelewa kulia ni kuathirika kwa ubongo ambapo hupelekea:-

(i) Kupata utindio wa ubongo;

(ii) Kuchelewa kwa hatua za makuzi na maendeleo ya mtoto kama vile kuchelewa kukaa, kutembea na kuongea; na

(iii) Kutochangamana na wenzake au kutokucheza na wenzake na kadhalika, madhara ni mengi.

Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa kila mjamzito kuanza kliniki mapema mara tu anapogundulika kuwa na ujauzito sambamba na kuhakikisha wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma ili ikiwa kuna tatizo la uzazi pingamizi watoa huduma waweze kuwasaidia mapema kabla mtoto hajaathirika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza gharama za kusafisha figo kupitia Bima ya Afya kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) inafanya jitihada za kununua vitendanishi na vifaa vinavyotumika kusafisha figo moja kwa moja kutoka viwandani ili kupunguza gharama za huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa wananchi mara utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utakapoanza waweze kujiunga kwani ni njia pekee ya kuweza kuwasaidia kuepuka gharama za matibabu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya Ugonjwa Sugu wa Kisukari nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mkakati wa tano wa Sekta ya Afya, imetoa kipaumbele kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari kama ifuatavyo:-

(1) Kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma juu ya kujikinga na ugonjwa wa kisukari kama vile kuzingatia ulaji unaofaa, kushughulisha mwili, mazoezi ya viungo pamoja na kuepuka matumizi ya pombe na tumbaku;

(2) Kuimarisha upatikanaji wa dawa, vitendanishi na mashine za kupimia sukari katika maeneo yote ya kutolea huduma za afya; na

(3) Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya kibingwa kwa wataalamu wa afya juu ya matibabu ya ugonjwa wa kisukari.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:-

Je, hospitali ngapi zimetenga vyumba vya kujifungulia wanawake wenye ulemavu nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali zote za rufaa za mikoa, hospitali 28 na hospitali sita za kanda (CCBRT, Mtwara, Chato Bugando, KCMC na META Mbeya) na Hospitali 184 za Halmashauri zina vyumba vya kujifungulia wanawake wakiwemo wanawake wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 21.1 kwa ajili ya kununua vifaatiba vitakavyowezesha kuboresha huduma za uzazi kwa akina mama wakiwemo wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja kuhuisha Taasisi ya Lishe badala ya kuifuta kabisa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya ilipokea maelekezo ya kufutwa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kupitia tamko la Serikali lililotolewa na Msajili wa Hazina tarehe 15 Desemba, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Afya inatarajia kuanzisha Programu ya Taifa ya Lishe pamoja na kuanzisha Kitengo cha utafiti wa lishe katika Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR). Hivyo, yale majukumu yaliyokuwa yanatekelezwa na TFNC yatafanyika kwa upana wake na Programu ya Taifa ya Lishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Wizara imeshaanza mchakato wa kuanzisha programu ya lishe.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. SYLVIA F. SIGULA aluliza: -

Je, nini chanzo cha ongezeko la wagonjwa wa figo nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la magonjwa ya figo hapa nchini kwa sasa yanachangiwa zaidi na sababu zifuatazo: -

(i) Ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza hususani shinikizo la damu pamoja na kisukari;

(ii) Matumizi holela ya dawa hasa zile za maumivu;

(iii) WAVIU wasiokuwa na ufuasi mzuri wa dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI;

(iv) Kutozingatia mtindo wa maisha unaofaa hususani matumizi makubwa ya chumvi, tabia bwete na matumizi ya vilevi hasa pombe na tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuielimisha na kuiasa jamii kuhusu kujikinga kwa kubadili mtindo wa maisha ambao unajumuisha ulaji usiofaa hususani matumizi makubwa ya chumvi, vyakula vyenye sukari nyingi au nafaka zilizokobolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imeimarisha huduma za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza pamoja na matibabu ya UKIMWI ili kuzuia madhara haya yasijitokeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo la kuwatenga walioathirika na magonjwa ya mlipuko Kagera?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la kuwahifadhi wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza lililopo katika mpaka wa Mutukula, Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera ambalo limegharimu kiasi cha shilingi milioni 140. Kwa sasa jengo hilo limekamilika na limewekewa huduma za maji, umeme, kuwekewa vitanda na tayari limeanza kutumika kuwahifadhi wanaohisiwa kuwa na magonjwa ya kuambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 kiasi cha shilingi milioni 80 kimetengwa kwa ajili ya maboresho ya sehemu ya nje ya jengo hilo ikiwamo kuweka sehemu yenye kivuli (lounge) kwa ajili ya wasafiri, pamoja na uwekaji wa viyoyozi na samani nyingine kwa ajili ya utoaji wa huduma.