Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lucy Thomas Mayenga (5 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia leo kusimama hapa na kwa kweli nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa sababu hiki ni kipindi changu cha tatu ndani ya Bunge, namshukuru sana Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri na nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya na Baraza la Mawaziri. Watu wamekuwa wanafanya kazi vya kutosha, wanapiga kazi ambayo inasifika sana na kila mtu kwa kweli anaona utendaji wao, ingawa kuna wengine wamezidi zaidi, wengine viwango vyao ni vya juu sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumzia kuhusu suala la makato ya kwenye kiinua mgongo. Hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha amegusa pabaya kwa Waheshimiwa Wabunge. Hata hivyo, nafahamu kwamba una busara sana, kwa hiyo utafikiria tena upya ili angalau mambo yakae vizuri sina haja ya kueleza zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza bajeti hii ni bajeti ambayo ina kila sababu ya kutuonesha na kutupa imani kwamba huko mbele tunakokwenda pako vizuri sana. Naisifu kwa sababu angalau imetuonesha na inatupa picha kwamba huko mbele yale ambayo tunayafikiria yameanza kidogo kuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala zima la uchumi wa viwanda. Tunapozungumzia suala zima la uchumi wa viwanda, najiuliza, kwamba tunazungumza kuhusu suala la uchumi wa viwanda je, tuko tayari? Kwa sababu tunaweza tukakaa tukazungumza mambo mazuri sana na tukawa na mipango mizuri sana, tukapiga makofi hapa tukawa na sifa nyingi sana lakini tusipofunga mikanda na kusema kwamba hapa sasa tumeamua kufanya kazi vya kutosha, haya masuala yataishia kwenye makaratasi na utekelezaji wake utakuwa ni mgumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu lipo jambo moja ambalo sijapata picha sawasawa, suala hilo ni la Inter-Ministerial Coordination. Wizara hii na Serikali hii kwa ujumla kwenye suala hili la uchumi wa viwanda, Wizara ya Kilimo inashirikiana vipi na Wizara ya Elimu, Wizara ya Nishati, Wizara ya Maji na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu tunapozungumzia uchumi wa viwanda, huu ni uchumi na ni biashara ambayo ni mkakati wa muda wa kati na muda mrefu. Sisi wengine siyo wafanyabiashara wakubwa, lakini angalau tunajaribu jaribu kidogo. Kwa hiyo, ninapozungumzia hivi ni kwa sababu tukisema kwamba tunazungumzia viwanda lazima tujiulize, Wizara ya Elimu imejiandaa kwa kiwango gani? Wizara ya Maji licha ya kwamba Tanzania ni Taifa ambalo ni la tatu duniani kwa wingi wa maji, imejiandaa kwa kiwango gani ili kuweza ku-facilitate? Kwa sababu kiwanda bila maji ni kitu ambacho hakiwezi kwenda. Wizara ya Kilimo imejiandaaje? Wizara ya Nishati imejiandaaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipokuwa makini tutajikuta kwamba watu wanakuja, wanasema sisi ni wawekezaji tunataka kuwekeza, mimi nataka kuja kuwekeza labda pengine kwa wananchi wangu wa Shinyanga kule, nataka nifungue kiwanda cha kitu fulani, lakini akikaa anaanza kwanza kujiuliza wakati anafanya due-diligence, hivi maji hapa nitayapataje? Anajiuliza hivi umeme bei yake na upo kwa kiwango gani? anajiuliza hivi kwa mfano, kama nikifanikiwa kama endapo nitawekeza kwenye kilimo, masoko yako wapi? Anajiuliza hivi, hapa nikifungua kiwanda human resource nitaitoa wapi? Kwa hiyo, haya ni maswali ambayo inatakiwa kama Serikali kwa ujumla wetu tujiulize kwa pamoja ili tuweze kuwa wote na kauli moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu sisi kama Watanzania, wapo Watanzania ambao tunafanya kazi vizuri sana, lakini wapo watu ambao wamezoea business as usual. Wao kazi yao mtu anaingia ofisini, tunaona hata kwenye ofisi na taasisi za Serikali, mtu anaingia asubuhi saa mbili anatoka saa tisa, uvivu na ile kukaa tu kwa kujiona kwamba mimi sina tatizo lolote yaani mtu anakaa tu ile laissez-faire imekuwa ni tatizo letu. Kwa hiyo, hatuna budi sisi kama Viongozi na Wanasiasa tuseme kwamba tumejiandaa vipi kwenye hili suala.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano tu mdogo nitolee, National Housing ni Shirika letu la Umma, lakini siyo wawekezaji, National Housing, wanajenga nyumba za Serikali wanaziuza, Wabunge tumekuwa mara nyingi sana tunapiga kelele kwamba nyumba hizi bei yake ni kubwa sana, lakini ukikaa na National Housing wanakwambia kwamba tunapokaa wakati tunaanza hii project ya kuanza kujenga nyumba sehemu, tunajikuta kwamba maji mimi mwenyewe National Housing ndiyo nivute, umeme mimi mwenyewe ndiyo nikae nifanye hizo jitihada, kwa hiyo unajikuta ile pesa ambayo unaiweka pale ni kubwa sana kiasi ambacho baadaye inabidi irudi kwa mlaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu suala zima la mifumo yetu pia. Mifumo yetu na system yetu ya nchi ya kuchukulia mambo, lazima tubadilishe pia sheria zetu za kazi kabla ya kuanza kukaribisha hawa wawekezaji. Sheria ya Kazi iliyopo sasa hivi inatakiwa iwe fair kwa mwajiri pamoja na mwajiriwa. Hivi sasa unakuta Sheria ya Kazi ime-base zaidi kwa yule mwajiriwa kiasi kwamba anajiona kama Mungu mtu, sasa nini kinachotokea?
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea sasa ni kwamba, watu wanafanya kazi, mtu anajua kwamba kwa mfano, mimi kama labda nafanya kazi kwenye shirika lolote labda pengine tigo, airtel na kadhalika, anaweza mwingine aka-misbehave, mwingine anafikia kiwango hata cha kuiba lakini haya mashirika na haya makampuni, hiki naomba Serikali kwa kweli tujitahidi sana, tuwe makini sana, tukae tujiulize na ikiwezekana tuunde timu ya kuangalia hawa wawekezaji tu tulionao hapa, sasa hivi kabla ya kuwakaribisha hawa wengine kwenye uchumi wa viwanda, wana matatizo gani? Maana kinachotokea sasa hivi, mtu anaiba airtel au anaiba tigo kwa mfano au anaiba sehemu nyingine yoyote lakini kinachotokea ni kwamba lile shirika au hiyo ofisi wanamchukua yule mtu wanamwambia tu naomba u-resign.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu. Nianze kwa kutoa shukrani zangu nyingi sana kwa Waheshimiwa Wabunge wote walioko katika Bunge hili kwa support kubwa waliyonipa na hatimaye sasa
nimekuwa Mrs. Jamal, ahsanteni sana. Haya makofi naomba yaendelee mpaka mwisho najua kuna sehemu yatagoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe pongezi za dhati sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu wake Mheshimiwa Mavunde, wanafanya kazi nzuri sana na kazi kubwa sana. Leo nimesimama hapa, kwanza kwa kweli nina hasira kwa sababu kuna baadhi ya vitu ambavyo havijanifurahisha hata kidogo na kuna baadhi ya vitu ambavyo nikiviangalia unamwangalia mtu halafu unasema; hivi huyu anategemea nini? Unakosa majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa nafasi ya kipekee nimpe pongezi zangu za dhati sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa sana ambayo anaifanya yeye pamoja na Baraza lake la Mawaziri, wanafanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi ambayo asilimia 32 ya mapato ya ndani yanakwenda kulipa madeni, katika nchi ambayo malimbikizo ya madeni yapo asilimia sita, katika nchi ambayo Mheshimiwa Rais anapozunguka au Waziri Mkuu au Mawaziri wanapozunguka Rais anaanza kuombwa kuanzia vidonge kwenye hospitali mpaka kwenye ndege watu wanalalamika, Rais huyu kwa kazi hizi anazozifanya kwa kipindi hiki kifupi alichofanya kazi, anastahili pongezi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukakaa hapa kukaanza kuongea kirahisi rahisi kwamba Rais huyu amefanya hivi, Rais huyu hafai, Rais huyu sijui amefanya hivi ni rahisi sana kuongea namna hiyo, lakini Wabunge baadhi wamezungumza; hivi sisi Waheshimiwa Wabunge maana nianze hata na mimi mwenyewe kwa sababu nipo humu ndani; katika kipindi hiki cha 2016 mpaka sasa hivi mmefanya nini kwenye Majimbo yenu? Hivi kila mtu akisema akae hapa aanze kuulizwa orodhesha ulichokifanya atasema amefanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema makofi yaendelee najua yatagoma; mimi nimekaa hapa Bungeni kwa kipindi cha miaka 12 kuanzia mwaka 2005 mpaka leo hii niliingia hapa Bungeni nikiwa mdogo sana. Naomba kutoa tahadhari kubwa sana kwa Wabunge ambao ni wapya na hasa Waheshimiwa Wabunge ambao ni vijana. Wako watu ambao ni Genuine kabisa kutoka pande zote mbili; kutoka upinzani na pia na huku. Kuna watu ambao wakiongea unajua kabisa huyu anaongea ni kwa kutoka kwenye dhamira yake lakini kwa experience yangu kuna watu nimeshuhudia tangu nimeingia hapa Bungeni miaka 12 hii kuna watu wananunuliwa na ni Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wana interest zao nyuma, mambo yao yameharibika, wanakuja hapa wanataka kutuvuruga. Kuna mtu anakuja hapa anasimama kwa sababu mume wake alikuwa fisadi ameondolewa kwenye madaraka anasimama hapa anataka kutuvuruga.
Kuna mtu anakuja anasimama hapa kwa sababu alikuwa anapewa pesa na mafisadi, mambo yamekuwa magumu anakuja hapa anataka kutuvuruga, kila saa Serikali mbaya, Rais mbaya, sijui vitu gani vibaya; tunaomba samahanini sana hayo maneno yenu mnyamaze mkaongee huko barabarani. Hapa tunataka tukae tuongee masuala ya maana, masuala ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeishi Rwanda kwa kipindi cha miaka kadhaa siwezi kusema ni miaka mingapi na kule walikuwa wanajua mimi ni Mnyarwanda. Nimeishi uswahilini ya Rwanda na nimeishi Masaki ya Rwanda; watu ambao ni viongozi wanakuwa wazalendo, kuna mambo ambayo ni ya msingi, mtu anakaa nazungumza kwa ajili ya nchi yao. Watu wanakaa wana-discuss issues ambazo ni za maana leo hii tumekuwa viongozi ni mambo ya Twitter, sijui Whatsapp, meseji za kipumbavu pumbavu ni aibu kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatakiwa tutumie muda ambao huu tunao kukaa, kufanya mambo ambayo ni ya maana. Kwa nini hatukai tukashauriana kwamba jamani hebu tufundishane ujasiriamali tunafanyaje, hebu jamani twende tukamfuate Mheshimiwa Waziri wa Fedha, jamani Mheshimiwa hebu tusaidie, tunataka tujiunge Wabunge 20 tufungue kiwanda, Mheshimiwa Waziri wa viwanda hebu tusaidie Wabunge 50 tunataka tukae tuweke mitaji yetu, tunataka tufanye biashara ya maana, matokeo yake watu mnakaa mnaanza kuchanganyikiwa, mnakuwa hamna hela mkitoka hapa maisha magumu, mmekaa wengine hapa mnapiga makelele, mnapata hizo nguvu kwa sababu mpo
ndani ya vyama vyenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatakiwa watu muweze kukaa kila mtu amekuja hapa kwa nguvu yake na kila mtu amekuja hapa kwa moyo wake na anajua yeye mwenyewe nini kilichomleta. Sasa msikae hapa mnaanza ku-insight other Members of Parliament to turn against the Government hii ni adabu mbaya, mbaya, mbaya kupita kiasi. Kama mna mambo yenu huko pembeni nendeni mkayamalize, kama mna jambo lenu huko pembeni nendeni mkakae mkaongee huko, lakini siyo mnakuja hapa eti Bunge zima likae liongee mambo ya ajabu ajabu…
Taarifa....
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokisema nilisema kwamba, katika kipindi ambacho nimekaa hapa Bungeni nimeshuhudia Wabunge wa aina hiyo wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu afikishe salamu zetu kwa Mheshimiwa Rais aende akamwambie kwamba tuko nyuma yake, tunajua kazi kubwa ambazo anazifanya, tunajua Serikali hii kazi kubwa ambayo inaifanya na tuko nyuma yake kwa njia yoyote ile. Hatuwezi kunyamazishwa lakini ninachoweza kuwaambia, hawa ambao wanaweza kupambana naye, yupo mpaka 2025 ambao wanadhani kwamba 2020 ni mwisho, they are very wrong na wanajidanganya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwaambia hata baadhi ya Wabunge ambao tuko huku kwenye Chama chetu, kila siku nasema na kuna mtu mmoja nimeshawahi kumwambia; You cannot win the fight with your Boss, you are messing up with the very wrong person katika Awamu hii
ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo hapa Bungeni, kipindi cha uchaguzi uliopita, wote tulikuwepo hapa labda hawa wengine wageni ambao hawakuwepo lakini walikuwa wanafuatilia. Baadhi ya Wabunge tulikuwa tunaona tabia za ajabu ajabu walizozifanya ukiwa humu ndani, watu na heshima zao. Mimi nimeingia hapa kwa mara ya kwanza ulikuwa unamwona Mheshimiwa Mbunge unadhani kwa sababu ya umri wake ni mtu mzima, ‘shikamoo Mheshimiwa’ baadaye unakuja kukaa baada ya mwaka mmoja, baada ya miaka miwili, unasema kumbe hata ‘mambo’ hastahili kwa sababu ya jinsi vitu anavyovifanya vya aibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua na wala siyo siri, tulikuwa tumekaa hapa, watu wakati wa uchaguzi, makundi yaliyokuwepo, sasa mimi nasema hivi; kama yale makundi yalikuwepo, kama ni masuala ya interest nyingine ambazo tunazo tuachane na hizo biashara sasa hivi tukae tujenge nchi yetu. Tukae tufanye kazi, tukae tuanze kuangalia maendeleo ya nchi yetu yanakwendaje, wengine hapa kwanza hata muda wenyewe wa kuuliza maswali hatuna kwa sababu unawaza biashara tu sasa unamshangaa mtu mwingine kila saa amekaa ‘Serikali hii sijui imefanya hizi’ mimi nasemaga hivi hawa watu wanatoa wapi muda? Mwisho mtakosa Ubunge mrudi nyumbani kule maisha yaanze kuwa magumu, shauri zenu. Ndiyo ukweli wenyewe si nyie mnajijua? Niliwaambieni haya makofi yatafika mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata siku moja Simba Wazungu wana msemo kwamba; “The lion does not turn around when a small Dog barks” Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu wala msihangaike na hawa watu ambao wanapiga makelele ya ajabu ajabu, maneno ya ajabu ajabu, wanasema vitu vya ajabu ajabu, ninyi kaeni, fanyeni kazi mwendelee kuwepo kwenye mstari na tuko pamoja, tunaowaunga mkono ndani ya hili Bunge ni wengi zaidi kuliko hawa wachache ambao wanapiga makelele. Tuwaache waendelee kupiga makelele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niseme; watakuja siku moja kula matapishi yao, wapo watu ambao tumewashuhudia leo mtu anasema hivi kesho anakuja unamshangaa huyo huyo anasimama Serikali hii nzuri sana. Unashangaa haya maneno ametolea wapi, watakuja kurudi
kula matapishi yao lakini wakati huo tutakuwa tayari tumeshawajua.
Mheshimimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nina hasira sana. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kunipatia nafasi hii, ninakushukuru sana. Nianze kwa kum-quote Profesa mmoja wa Kenya ambaye anaitwa Patrice Lumumba, yeye alisema kwamba; “Magufuli is the real deal.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wangu kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya kiasi ambacho amewafanya mpaka baadhi ya watu wameanza kuchanganyikiwa, wanahisi kama Mheshimiwa Magufuli amekaa miaka saba, wakati ndio kwanza ana mwaka mmoja na nusu. Na ninapenda kuwaambia kwamba hii ni mpaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa ambayo leo hii nimeamua kusimama hapa, kwanza ni utendaji wake, lakini vilevile ni jinsi ambavyo ameshughulikia suala hili la makinikia. Suala hili la makinikia wananchi wangu, kwa mimi ambaye natokea Mkoa wa Shinyanga, wamenituma wanasema kwamba, katika vitu ambavyo utazungumza usiache kuelezea furaha kubwa tuliyokuwanayo sisi kwa jinsi ambavyo Rais ameweza kutusaidia, walau kuonyesha njia ambayo tunajua sasa tutafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimesoma magazeti, kuna gazeti moja nikasoma limeandika kwamba, kuna utafiti wa TWAWEZA, wanasema kwamba sijui umaarufu wa Mheshimiwa Rais Magufuli umeporomoka kwa sababu anapendwa na watu wa kada ya chini! Mimi nilikuwa nataka niseme jambo moja, wala hajakosea kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania ni maskini wale ambao ndio wanachukua asilimia kubwa asilimia 70. Kwa hiyo, kwa Rais kukubalika kwa watu asilimia 70 na kupingwa au kutokukubalika kwa ile asilimia 30 mimi naona ni jambo zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa mtu yeyote, kiongozi yeyote ambaye unajua unachokifanya hiki ndicho ambacho kinatakiwa kufanyika. Wewe hutakiwi upendwe na watu wachache ambao tena wengi mara nyingi wanakuwa ni mafisadi au wanakuwa ni watu ambao umewagusa kwa namna moja au nyingine, inatakiwa wewe upendwe na wale watu ambao ndio wengi.

Kwa hiyo, kwa Rais kukubaliwa na watu wa kada hii ya chini ndio hasa kitu ambacho tunakiunga mkono na kwa kweli, ndio kinaonyesha kwambam Rais wetu yuko imara sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho wakati nachangia…

TAARIFA ...

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote mwenye akili timamu lazima apokee hiyo taarifa. Ni ukweli kabisa utafiti umefanyika between mwezi wa tatu na mwezi tano na ndiyo kipindi masuala ya vyeti fake yamesemwa masuala ya mafisadi yamesemwa kwahiyo hawa wenzetu hii asilimia 30 tunawajua ni wakina nani na hawa wa Makinikia na wao pia tunawajua na wenyewe pia wanajijua na wengine wako humu humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye kuzungumzia suala hili la makinikia mimi nina ushauri mdogo. Mtanisamehe sauti yangu kidogo inakwaruza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hili la Makinikia mimi nilikuwa na ushauri kidogo biashara hii ni biashara kubwa sana, ninampongeza sana sana Profesa Mruma na pamoja na Profesa Osoro. Profesa Mruma nimekuwa naye kwenye board ya Williamson Diamond kwa kipindi cha miaka kama nane, kwa hiyo biashara hii ya diamond ninaifahamu kwa kiwango cha chake. Biashara hii inaitwa holding business. Biashara hii hata ikija kutokea duniani leo hii dhahabu zote zikaisha almasi zote zitakaisha kwenye mashino yetu aidha Afrika au sehemu nyingine yoyote. Of course sana sana ni Afrika. Biashara hii bado itaendelea kufanyika kutokana na nature ya hii biashara jinsi ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu nilikuwa naomba kushauri kwamba amekuja huyu CEO wa Barrick, lakini inatakiwa sisi kama Tanzania tukae naye. Mimi ambacho naomba kushauri naomba kwamba timu yetu ya Tanzania tufanye upembuzi mzuri sana wa watu wa kukaa na huyu mtu. Hawa wenzetu ni wazoefu sana wa hizi biashara ni tycoon wa hizi biashara, ni biashara ambazo zina pesa nyingi sana lakini wenzetu wame-deal na hivi vitu maeneo mbalimbali kupita kiasi zaidi yetu sisi. Kwahiyo, lazima kwenye kuchagua watu wa kukaa nao meza moja lazima tuchague watu ambao vichwa vyao viko sawa sawa kikweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye suala hili la makinikia mimi nilikuwa naomba kuuliza Wizara ya Fedha, miaka ya nyuma BOT walitoa wayver kwa makampuni yote ya madini ambayo wanachimba hapa Tanzania ambayo yanatoka nje kwamba mnaruhusiwa kuweka pesa zenu nje. Ile wayver ilitolewa wakati ule Gavana akiwa Dkt. Balali mpaka sasa hivi wayver ile haijarudishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ya haya makampuni walisema kwamba sisi tunataka tuweke pesa zetu huku nje kwa sababu hapa Tanzania hakuna mabenki ambayo ni international, lakini vile vile na sisi ambao ni wafanyabiashara ya hizi biashara. Sisi mikopo yetu tunaitoa huko nje. Sasa hawa watu sasa hivi international bank zipo nyingi hapa Tanzania. Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kweli mimi nitaomba jibu hapo baadaye utakapokuja kuhitimisha uje utuambie ni sababu zipi zilizofanya mpaka leo hiki kitu kimekuwa kimya hakisemwi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama tunavyoelewa kwamba pesa hizi zilikuwa zinawekwa hapa Tanzania, sisi Tanzania hapa tumekuwa tunalalamika bei ya dola imekuwa kubwa wafanyakabiashara wanalalamika. Pesa hizi zikiwa zinawekwa hapa tutafaidika hata mzunguko wetu wa pesa, urari wa biashara utaweza kuonekana na mzunguko wetu wa pesa itakuwa ni rahisi zaidi kwa sababu hata dola itachuka at least ita-stabilize vizuri kuliko ilivyo sasa hivi. Nilikuwa naomba jambo hili liweze kuliangalia kwa macho makali zaidi na kwa kweli ulifanyie kazi kwa haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo nilikuwa nataka nizungumzie. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake dada yangu Dkt. Ashantu wanafanya kazi nzuri sana ni watu ambao siyo waongeaji sana lakini kwa kazi wanapiga vizuri sana. Mmefanyaka kazi nzuri sana bajeti ni nzuri sana kusema za ukweli. Huwezi kuwa mtu mwenye akili timamu ukasema bajeti hii ina matatizo ina dosari za hapa na pale kwa sababu ni ile tu kwamba hatuwezi kumaliza matatizo yote kwa mara moja. Lakini hatuwezi kusema kwamba bajeti hii mbaya, bajeti hii ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kwenye suala zima la kuwasaidia wajasiriamali wadogo tusiishie tu kwenye masuala ya administrative pamoja na facilitation, mimi nilikuwa naomba tu tujikite zaidi kwenye jinsi ya kuwasaidia hawa wajasiriamali wadogo.

Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kukuambia ujaribu kumulika pale Airport - TRA ya kwako. Kuna matatizo makubwa sana wakati tumekaa tunazungumzia habari za kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, Mheshimiwa Waziri wafanya biashara hawa wadogo wako akina mama, wako vijana wanaangaika wanakwenda nchi mbalimbali kuja kuleta bidhaa. Wanafanyabiashara ambazo mitaji yao ni dola 20000/30000 siyo pesa nyingi, lakini mtu analeta mzigo akifika pale airport anapata usumbufu wa hatari. Inakuwa inamkatisha mtu tamaa mpaka anaona kwa nini nimeanza kwenda. Anapata visa anamaliza anatoka anakenda huko nje kwenda kufanya hiyo biashara lakini akiingia hapa Tanzania anapata usumbufu kupita kiasi na rushwa pale imezidi. Mimi nakuambia kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo nilikuwa nataka nilizungumzie, Wizara ya Afya, uchumi ni afya, Wizara ya Afya nilikuwa naomba nitoe wazo Bunge hili liunde Kamati ya kushughulikia suala zima la Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeoza, haifai na kama ikiwezekana Mheshimiwa Rais na angekuwepo hapa leo Mheshimiwa Waziri Mkuu, nadhani ningempa message kwa sababu yeye alijua jinsi ya kuzungumzia angeifuta kabisa. Ofisi ya Mkemia Mkuu inatakiwa ifanye control ya chemicals ambazo zinaingia Tanzania jambo ambalo hawafanyi hata kidogo. Kuna kampuni inaitwa TECHNO imeiingiza chemical kampuni moja tu. Imeingiza chemical ambazo ni nyingi wanaulizwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali hawajui hata idadi ya Chemicals ambazo zimeingizwa hapa Tanzania. Kemikali hizi zinatumika hospitalini, kwenye mashule yetu, wanafunzi wanakwenda kufundishwa kwa ma-chemicals ambazo zime expire, wanafunzi wanakwenda kufundishwa kwa chemicals ambazo nyingine siyo zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu kama hivi tukiendelea kukaa tukivinyamazia, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali akakutana na hili jambo linatia aibu nasikitika tu kwamba sikupata nafasi ya kulizungumza kwa urefu wakati wa Wizara Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanazozifanya licha ya changamoto kubwa na nyingi zilizopo kwenye Wizara yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa heshima na taadhima Mheshimiwa Waziri apokee ushauri wangu kuhusu suala la kuwapa offer madaktari na timu yote ya madaktari hao kutoka Marekani ambao walifanya kazi kubwa kuwasaidia watoto wetu wa Kitanzania katika ajali iliyohusisha wanafunzi, walimu na dereva wa shule ya Lucky Vincent. Mheshimiwa Waziri, madaktari hawa walikuwa wamekuja Tanzania kwenye programu tofauti lakini wakiwa nchini waliona nia ya kwenda kutembelea vivutio vyetu ambapo walikutana na ajali hiyo eneo la Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu hii ilifanya kazi kubwa ya kuwasitiri watoto wetu ambao walifariki lakini waliendelea pia kuwasaidia waliojeruhiwa kwa kuwapeleka nchini Marekani kwa ajili ya matibabu. Huu ni moyo wa kipekee, kwani ilibidi wakatishe safari yao kutokana na tukio hilo. Naiomba Wizara licha ya ukweli kwamba madaktari hawa wana uwezo, lakini sisi kama Watanzania tuna njia nyingi za kuwashukuru kutokana na kitendo hicho, na kwa kuwa walionesha nia ya kutaka kwenda kwenye vivutio vyetu naona itakuwa ni jambo jema kama tukitambua mchango wao kwa kuwapa offer hiyo ya kuja bure kwenye vivutio vyetu popote watakapotaka kutembelea. Kama ikikupendeza basi tuwape offer ya muda mrefu ili waweze kujipanga na kuamua siku watakazotaka wao wenyewe.

Mheshimiwa Waziri, hiyo itasaidia kuonesha shukrani yetu lakini pia itasaidia kuendelea kutangaza utalii wetu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia hii nafasi. Vilevile ninaomba kwa nafasi ya pekee nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ambaye kwa kweli kwa kiwango kikubwa yeye ndiye aliyesababisha mpaka leo hii Tanzania kwenye vita hii tumeweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa msimamo mkubwa alionao dhidi ya vita hii. Vile vile kwa nafasi na upendeleo wa kipekee nimpongeze Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Kamishana Siang’a, ninampongeza sana. Ninampongeza sana kwa sababu anafanya kazi na amefanya kazi kubwa sana, ndani ya muda mfupi na katika mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamishna huyu ndiye yule ambaye alikataa rushwa ya shilingi milioni 800. Kwa kweli ni kitu ambacho kwanza ni nadra maana hata katika hali ya kawaida unaona kabisa kwamba kama ni mtu ambaye si mzalendo na hauna uzalendo wa dhati kutoka moyoni mwako, ni kitu ambacho ni kigumu sana, kwa hiyo ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ninampongeza kwa sababu alifanya kazi hii katika mazingira magumu sana ya sheria; alifanya kazi hii katika mazingira ambayo sheria hii ilikuwa haitumiki Zanzibar, katika mazingira ya sheria ambayo yalikuwa hayaruhusu mamlaka hii kumiliki silaha, mazingira ambayo hata yeye mwenyewe kuweza kutaifisha na kufanya mambo mengine yote ili kuweza kukabiliana na hawa wauzaji wa dawa za kulevya ilikuwa haiwezekan lakini aliweza kupambana na hatimaye sasa hivi kwa kweli watu wanasema kwamba misuli imekaza lakini kwa hawa wauzaji wa dawa za kulevya imekaza zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie kwenye suala hili la dawa za kulevya kwa upande wa Zanzibar. Mimi nilikuwa ninategemea kwamba leo Wazanzibari wote wangekuwa na kauli moja kwamba sheria hii wanaiunga mkono kwa asilimia 100 bila kusita. Nasema hivyo kwa sababu matatizo haya ya madawa ya kulevya athari zake ukiachilia mbali athari za kijamii kwa maana ya kwamba maradhi na nyingine lakini ina athari kubwa sana kwenye masuala ya uchumi…

T A A R I F A . . .

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, yeye alikuwa ni sehemu ya Wazanzibari, lakini hasa nilikuwa nimem-target Mheshimiwa Ally Saleh kwa sababu naye pia ni Mzanzibari. Kwa hiyo, kwa wale ambao wanaunga mkono sheria hii tupo pamoja, lakini kwa wale ambao hawaungi mkono kwa sababu pia wewe unaweza ukawa ni mmojawapo, lakini kuna wenzenu pia hawauingi mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kusema mengi lakini ninachotaka kusemea ni kwamba hata kama tunaunga mkono sisi viongozi na sisi ambao ni Wabunge Wazanzibari tuliopo humu ndani, ninaomba sasa maana yake nilikuwa sitaki kusema lakini ninaomba kwenda mbele zaidi. Ninaomba tufanye kazi ya ziada kwa tume ya kudhibiti na kupamba na madawa ya kulevya Zanzibar. Imeunda zaidi ya miaka kumi, lakini mpaka sasa hivi haijakamata hata kilo tano, naishia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala haya ya madawa ya kulevya yana athari nyingi sana. Zipo nchi ambazo zimekuwa zikifadhiliwa kutokana na athari hizi za dawa za kulevya zimeingia kwenye matatizo makubwa sana kisiasa, kiuchumi na nyingine pia zimepinduliwa. Nchi kama Nicaragua, Panama, Mexico na kadhalika na wengi pia mnajua historia hizo, wapo katika hali ngumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo vita hii ninaomba wote tuwe na kauli moja kwa sababu vita hii inahusu kuanzia wale wadogo ambao ni watumiaji lakini hata na sisi pia wakubwa. Kwa sababu ambao wamekuwa wakikamatwa mara nyingi huko wanasemwa sana, lakini bado miongoni mwetu kuna watu ambao baadhi yao wapo katika nafasi mbalimbali, si lazima wawe Wabunge ni watu ambao wapo katika nafasi kubwa lakini wamejiingiza kwenye biashara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba kupongeza sana sheria hii na kwa kweli ninaomba serikali kwenye utekelezaji wa sheria hii isimuangalie mtu usoni, awe mtoto wa mkubwa, awe mwenyewe ni mkubwa awe sijui ni nani, tuangalie na tuweze kuchukua hatua zinazostahili. Haiwezekani watu walikuwa wamefikia kiwango cha kuingiza katika nchi yetu mpaka tons as if ni unga wa mahindi, haiwezekani. Kwa hiyo, sheria hii ikate kotekote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza kuhusu taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu suala la kifungu cha dhamana kwamba ile kupunguza gramu. Ili mtu alewe kutokana na unga anatakiwa atumie 0.01 gramu ya unga ndipo analewa. Sheria iliyopita ilikuwa ni kwamba mtu akikamatwa na madawa ya kulevya haya ya viwandani, heroin au cocaine ikiwa ni chini ya gramu 200 anapata dhamana, sasa nini kilichokuwa kinafanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichokuwa kinafanyika ni kwamba wafanyabiashara walikuwa gramu 200 anazigawa kwa watu tofauti tofauti, kwa sababu anajua kwamba akikamatwa na gramu 200 au zaidi mtu mmoja itakuwa ni matatizo. Gramu 200 anaweza kutengeneza, gramu moja ya dawa za kulevya inatengeneza kete 100 kwa maana hiyo gramu 200 ni zaidi ya kete 20,000…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)