Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Lucy Thomas Mayenga (19 total)

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika na mikakati ambayo imeendelea ambayo imekuwa ikifanywa hivi sasa inaonyesha kwamba nchi yetu itakuwa ni Taifa bora. Lakini vilevile kwa kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka na kwa miaka mingi ya nyuma Serikali yetu imekuwa ikisomesha Watanzania wengi katika nchi mbalimbali lakini baadhi ya Watanzania ambao ni Madaktari waliamua kuondoka hapa Tanzania na kwenda nje kwa ajili ya sababu kuwa zikiwa ni maslahi.
Je, Serikali ina mkakati gani maalum wa kuweza kuwarejesha Madaktari hawa ambao sasa wamepata uzoefu mkubwa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba Serikali yetu imekuwa ikiongeza udahili kwa ajili ya kufundisha Watanzania wenzetu kwenye fani za tiba kwa kiasi kikubwa sana katika miaka ya hivi karibuni. Hivi tunavyozungumza hapa kwa mwaka mmoja tuna uwezo sasa hivi wa kuzalisha takribani Madaktari wa tiba 1,000. Hiki ni kiasi kikubwa sana na ni uwekezaji mkubwa sana ambao umefanywa na Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutambua uwekezaji huu mkubwa uliofanyika ni kweli nakiri kwamba tumekuwa na uwezo mdogo wa kuwa- absorb kwenye system wale wote wanaohitimu kwenye fani za tiba na utabibu kwa ujumla wake. Serikali ya Awamu ya Tano tayari ina mkakati mahsusi wa kuhakikisha tunaongeza kiasi cha Madaktari ambao wanakuwa absorb kwenye system ya kutolea huduma za afya ili tuwe na Madaktari wengi zaidi ambao wanafanya kazi kwenye Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maslahi mpaka hivi ninavyoongea hapa Madaktari ni mojawapo ya fani za kitaalamu hapa nchini ambao wanalipwa vizuri sana kuliko wengine. Hivi ninavyoongea Daktari anayemaliza masomo yake ya Degree analipwa vizuri sana kuliko ukilinganisha na fani zote zile kwenye Serikali na tunavyoongea kwenye sekta binafsi sasa wanaanza kupata shida kuajiri Madaktari ambao wamehitimu kwa kuwa ndani ya Serikali maslahi ni mazuri zaidi kuliko hata yale ya kwenye sekta binafsi na ni jambo la kujivunia. Kwenda nje pia siyo jambo la kusema ni baya, kwa sababu wa navyoenda wengi wao wanakaa miaka mitatu, miaka sita wanarudi nchini kuja kutoa tiba hapa na tayari wanakuwa wameshapata uzoefu wa kufanya kazi nje ya nchi. Kwa hivyo, ni fursa na hatuwezi kuwabana kwa njia nyingine yoyote ile zaidi ya kusema tuboreshe maslahi ndani ya Serikali ili Madaktari waweze kutoa huduma kwa Watanzania wengi hapa nchini.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri. Kama majibu yalivyo yanadhihirisha kabisa kwamba kuwataka au watu wa Kahama kuendelea na umeme wa jenereta wakati Watanzania wote na yeye mwenyewe anafahamu kwamba Wilaya ya Kahama ni kati ya Wilaya ambazo ni kitovu cha uzalishaji wa chakula especially mchele na kwa jinsi hiyo kuwazuia kwa namna moja au nyingine wasifanye uzalishaji wenye tija. Nimeshukuru amesema kwamba utaratibu umeanza wa kuwapatia umeme wa uhakika. Ningetamani sana kuona kuwa hili linapatiwa ufumbuzi haraka na ningetaka sasa aseme ni lini ambapo umeme huo utapatikana kwa uhakika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tatizo la kukatika kwa umeme siyo la Kahama peke yake, ni la maeneo mengi sana Tanzania, likiwepo eneo la Kigamboni, Dar es Salaam, ambapo kule mnaamka mnaulizana kwenu upo? Leo umeme upo? Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI anaweza kutusaidia kujua kwamba eneo la Kigamboni sasa litaacha kukatiwa umeme kila siku, kila mara especially siku za Jumapili kuanzia lini? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, Kahama imeunganishwa kwenye lane ya Shinyanga ambayo msongo wake ni wa KV 33 na sisi tunajua kwamba umeme huo ni mdogo, ulitosha kwa wakati huo lakini siyo kwa sasa. Kwa hiyo kinachofanyika, nadhani hata kabla ya bajeti yangu kwisha, Ijumaa atawaona watu wa TANESCO wako pale, wameondoka leo, wamekubaliana na Mgodi wa Buzwagi, Buzwagi ndiyo iko karibu sana na Kahama. Kwa hiyo, umeme utavutwa kutoka Buzwagi 33 KV kwenda Kahama. Kwa hiyo, huku watakuwa na wa Shinyanga, huku watakuwa na wa Buzwagi, tatizo hilo litakwisha.
Mheshimiwa Spika, mbali ya hilo la umeme kukatika katika, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote lazima tufanye maamuzi. Tukiwa tunajenga hii miundombinu kuna wakati lazima tuzime umeme. Watu wa upande wa Ziwa Victoria kila Jumapili umeme unakatika, lakini wanatangaziwa kwamba tunajenga miundombinu ya kusafirisha umeme mwingi kutoka Iringa mpaka hapa Dodoma, tunatoka kwenye KV 220 mpaka KV 400. Tunatoka hapa Singida, Shinyanga mpaka Nyakanazi KV 400. Sasa hii tunaizindua Septemba.
Mheshimiwa Spika, sehemu zingine Tanzania nzima, hata ndugu zangu wa Arusha waliokuwa wanasema umeme unakatikakatika, tunajenga kutoka Singida kwenda Arusha KV 400, halafu kutoka Da es Salaam kupitia Tanga kwenda Arusha KV 400. Hiyo ndiyo TANESCO mpya. Ahsante.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa suala hili la Kipunguni Dar es Salaam kutokana na jibu la msingi limekuwa likileta malalamiko mengi na limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu na kwa kuwa ofisi ya Wizara hii ipo Dar es Salaam:-
Je, kwa nini Serikali hasa Mheshimiwa Naibu Waziri asitoke yeye aende Kipunguni pamoja na wataalam ili aweze kupata majibu ya kujiridhisha badala ya kumsubiri Mheshimiwa Mbunge yeye ndiyo alete majibu hapa Bungeni.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa wa Kipunguni walishafika ofisini kwetu, nikaondoka nao nikaenda kwa acting CEO wa Uwanja ule wa Ndege na baada ya kujadiliana kwa mpana ndiyo hayo majibu ninayoyatoa hapa yanatokana na vikao hivyo. Mimi mwenyewe nimekutana nao ofisini baada ya wao kuja na baadaye tulifanyia vikao Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam tukiangalia maeneo yote yale matatu ya Kipunguni, Kipawa na Kigilagila. Kwa hiyo, namhakikishia kwamba hicho nachokisema hapa ni kutokana na kile nilichokifanyia kazi. Ndiyo maana nasema huu utofauti kati yangu na Mheshimiwa Mbunge wa figure alizoleta hapa ningependa nipate ushahidi wa hicho anachokiongea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachokisema, waliobakia ni 742 na tutawalipa mara fedha zitakapopatikana, ni kutokana na kazi kubwa niliyoifanya katika eneo hilo. Hata hivyo, bado nitaendelea kuliangalia suala hilo nikishirikiana na hawa Waheshimiwa Wabunge ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Kaluwa kuhakikisha kwamba hicho tunachokisema ndicho sahihi.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo hili la maji lipo kwenye categories mbalimbali kwa nchi nzima, wapo watu ambao hawana kabisa miradi katika maeneo yao kwa sisi Wabunge hapa ndani Bungeni, lakini pia yapo maeneo ambayo miradi ipo lakini haijakamilika kutokana na sababu mbalimbali, lakini yapo maeneo katika nchi yetu ambayo maji yanapatikana lakini kumekuwa na manung’uniko ya chini chini ya wananchi kwamba jinsi bili zinavyotoka kunakuwa hakuna usawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo haya yamekuwa yakisemwa kwa wananchi kwa muda mrefu na yamekuwa takribani kila Mbunge anaposimama hapa wengi wamekuwa wakigusia kuhusu tatizo la kutokuwa na usawa wakati wa kutoa bili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara badala ya kusema kwamba wananchi au sisi Wabunge twende kwenye bodi kutoa malalamiko au wananchi waende kule kwenye taasisi za kutoa huduma ili kwenda kupeleka malalamiko yetu.
Je, Wizara hii haioni sasa umefika wakati kuchukulia tatizo hili kwa ukubwa wake kama tatizo la kitaifa, kuunda timu maalum itakayopita kila maeneo na kuweza kujua kwamba maeneo haya yana matatizo haya tuweze kuyatatua vipi na eneo hili matatizo yake tuweze kutatua vipi? (Makofi). Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lucy Mayenga ameuliza swali zaidi ya moja; anazungumzia habari ya matatizo ya upatikanaji wa maji, lakini pia anachanganya tena na masuala ya bili. Sasa ni vitu viwili tofauti. Masuala ya upatikanaji wa maji, Serikali inaendelea kutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili la matatizo ya bili nimeshalitolea majibu, labda nirudie kwa kuweka msisitizo. Ni kwamba Wizara inatambua yapo maeneo ya mtu mmoja mmoja kulalamikia bili, siyo kwamba kila mmoja analalamikia bili. Sasa nasema, kama ni isolated cases, hatuwezi kuchukulia kama ni tatizo la Kitaifa. Hili ni tatizo la mtu mmoja ambaye ana tatizo, amepewa bili ya miezi mitatu hajapata maji.
Sasa hili naomba tulifuatilie kwa maana ya kwa huyo mtu ambaye anatuletea ni isolated case tuishighulikie. Siyo jambo la kusema tulitolee mwongozo kama Taifa kwa maana ya kwamba tumeshakubaliana kwamba maji ili yawe endelevu, upatikanaji wake ni lazima tuchangie.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kulipa bili ni lazima ili tuwe na uhakika wa kuwa na maji. Sasa kama kuna matatizo mahali, tutayashughulikia kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara hii imekuwa ikijitahidi sana kwenye suala zima la usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali kupitia miradi ya REA pamoja na taratibu nyingine.
Je, Wizara hii iko tayari sasa kuweza kuwasaidia wananchi wetu wa Wilaya ya Shinyanga Mjini na hasa Jimbo langu la Shinyanga ambako natoka ambapo tunakabiliwa na tatizo kubwa sana la kukatika sana sana kwa umeme; kwa taarifa nilizonazo ni kwamba kituo cha kusambazia umeme cha Ibadakuli kimezidiwa nguvu.
Je, Serikali ipo tayari sasa kuweza kusaidia kituo hiki kukiongezea nguvu ili umeme wa uhakika uweze kupatikana? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Ni kweli kufuatia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa msongo wa KV 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga, mradi ule una taratibu za upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoozea umeme kimojawapo ikiwa ni Ibadakuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo kile pamoja na kuzidiwa, mradi huu wa kukikarabati na kukiwezesha kutoka kwenye KV 220 na kufika KV 400 utakwenda kutatua tatizo la wananchi wake wa Shinyanga ambako amekuwa akifuatilia sana mahitaji wa umeme. Ahsante.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikipata takribani shilingi bilioni 5 kutokana na meli za nje zinazoingia Tanzania kwa ajili ya kufanya uvuvi mkubwa. Je, Serikali sasa na hasa Wizara hii iko tayari kuanzisha bandari maalum ya uvuvi kwenye Bahari ya Hindi ambayo itakuwa inasaidia meli kubwa kutoka nje zinazokuja kwa ajili ya uvuvi ziweze kufanya kazi ili Serikali iweze kupata faida? Kwa sababu sasa hivi meli hizi kubwa zimekuwa zinapata takribani shilingi bilioni 500 na nchi yetu imekuwa ikipata shilingi bilioni 5 tu. Je, Serikali iko tayari kuchukua wazo hili kuanzisha bandari hiyo ili nchi yetu iweze kufaidika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tuko tayari kuchukua wazo hilo na tutashirikiana kwa karibu sana na Wizara ya Uvuvi na Mifugo kuhakikisha kwamba wanatuonesha maeneo stahiki kwa ajili ya kujenga bandari hizo.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Watumiaji wa madawa ya kulevya hivi sasa Serikali kutokana na jitihada kubwa na nzuri za mapambano dhidi ya madawa sasa hivi wamegeuza kibao wameanza kutumia dawa kama pethidine, benzodiazepine dawa hizi zimekuwa zikisabisha kwamba watu ambao wanatumia madawa kulevya madawa hakuna wanatumia dawa hizi. Je, Serikali iko tayari sasa kuleta sheria ambazo zitakuwa kali sana ili kuweza kudhibiti usambazaji na manunuzi ya dawa hizi ili zifanane na jitihada kubwa na nzuri zinazofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali zuri la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya awali tumeanza kuona ongezeko
la madawa ya hospitali ama prescription drugs zikianza kutumika ndivyo sivyo kama mbadala wa madawa haya ya kulevya. Sisi kama Wizara tumeanza kuchukua hatua na ni mambo ambayo tunaendelea kuyafanya kama ndani ya Serikali. Kuanza kutoa elimu kama ambayo nimeitoa hapa kwamba hizi dawa zinatakiwa zitumike kwa malengo ambayo yamekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili tumeanza sasa kuweka utaratibu mzuri wa kufanya udhibiti wa hizi dawa kuhakikisha pale tangu zinapoingia mpaka kwa mtumiaji wa mwisho. Niseme kwamba uratibu huu tumeshauanza ndani ya Wizara na tutaendelea nao. Sheria tulizonazo za matumizi ya madawa ya kulevya zinaongelea vilevile hizi dawa za prescription drugs na sheria ni nzuri tu zinajitosheleza kwa adhabu.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza kabisa ninaomba niipongeze sana Serikali kwa hatua yake ya kuamua sasa kutuma timu ya Wataalamu kufanya tathmini ili kuweza kuendeleza Bwawa hili lakini nilikuwa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hawa Wakandarasi katika nchi nzima wako Wakandarasi ambao wamekuwa wakijenga Mabwawa na wengine wamekuwa wakitudhalilisha na kutusababishia matatizo na kusababisha pesa nyingi za Wananchi na pia vilevile pesa kutoka kwa Wafadhili kuonekana kwamba ni nchi ambayo ni kama vile kuidhalilisha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamekuwa wanajenga vitu ambavyo haviko katika viwango na wengine wamekuwa wakishindwa kumaliza,

Je, Serikali iko tayari sasa kufanya tathmini nyingine upya ili hawa Wakandarasi ambao baadhi yao wakiharibu Mkoa mmoja anaenda kwenye Mkoa mwingine waweze kuchukuliwa hatua ikiwemo kushindwa kabisa kupewa kazi na ikiwezekana kutokupewa kazi kabisa katika nchi ya Tanzania ili kuendeleza heshima tuliyonayo kama nchi na kuweza kulinda pesa za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kabla ya tathmini je Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kuweza kujionea kwa macho yake athari zilizoko pale katika eneo lile ambalo limesababisha kwa kiwango kikubwa wakinamama wanapata shida walikuwa wanalima lakini sasa hivi hawalimi maji walikuwa wanapata eneo la karibu lakini sasa imekuwa wanapata eneo la mbali, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) Mheshimiwa Spika, kwanza naomba unipe nafasi nimpongeze Mheshimiwa Lucy kwa jinsi anavyowapigania Wakulima wote wa Mkoa wa Shinyanga na akishirikiana na Mbunge wa Jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, kwanza Serikali tuko tayari na tulishaanza kufanya tathmini ya kina na ndiyo maana tuwaarifu Waheshimiwa Wabunge wanaona Miradi mingi ya Umwagiliaji imechelewa kupelekewa fedha kwa sababu Serikali tumejipa jukumu la kupitia Miradi yote ili kubaini ubadhirifu na jinsi ya kutathmini thamani ya fedha ya Miradi hiyo kabla hatujaanza kupangia fedha nyingine kwa ajili ya kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, zoezi hilo la kudumu na tutaendelea na Miradi yote Tanzania kabla hatujaanza kuipatia fedha nyingine. Swali lake la pili, niko tayari kuambatana na yeye baada ya Bunge hili nitaanzia Mkoa wa Shinyanga kwenda kutembelea Mradi huo ili kubaini changamoto hizo tuweze kutafutia ufumbuzi.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali katika sekta hii ya madini kuhakikisha kwamba tunapata faida. Je, Serikali sasa iko tayari kukaa kwa Wizara nne; Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuweza kutoa kikwazo cha dola 300 za viza ya biashara kwa wafanyabiashara wa Congo ambayo imekuwa ni kikwazo kikubwa cha kusababisha nchi yetu kukosa dhahabu licha ya kufungua biashara ya dhahabu hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika,ni kwamba sisi tunapokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na kweli hata sisi tunaona kwamba ni vizuri sasa kutoa viza kwa watu wanaotoka Congo. Vilevile tumeanzisha masoko katika mikoa yote ikiwa ni pamoja na mikoa ambayo ipo mipakani mwa nchi yetu pamoja na Kigoma ambapo ni karibu na Congo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa tulipo sasa hivi ni kwamba tumetoa zile tozo ambazo zilikuwa zinakuwa charged katika Wizara yetu ya Madini kwamba mtu anapoingiza madini ni lazima alipe kiasi fulani, tumekwishakutoa hiyo ni moja ya hatua lakini vilevile tupo tayari kushirikiana na hizi Wizara kama alivyosema

Mheshimiwa Mbunge alivyotoa ushauri, basi tuangalie namna ya kuweza kurahisisha biashara kufanyika katika masoko haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi unaweza ukaleta madini katika masoko yetu na hatuulizi madini unayatoa wapi, wewe leta katika masoko yetu tutaangalia pale, tuta-charge sisi mrabaha wetu pamoja na clearance fee, utafanya biashara, wanunuzi utawakuta pale utaweza kufanya biashara yako vizuri na tumeweka mazingira mazuri.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa muda mrefu kwenye kundi hili la watu wenye matatizo ya akili baadhi yao wamekuwa wakipata matatizo ya kisheria na kuweza kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kufungwa, lakini kwa sababu tiba hii na ugunduzi wa watu wa aina hii huwa inachukua muda mrefu sana, kwa maana ya kwamba, mtu anakuwa na matatizo ya akili, lakini uthibitisho kwamba, huyu anakuwa na matatizo ya akili unachukua muda mrefu. Je, Serikali sasa iko tayari kwa kundi hili maalum kwa matatizo haya waliyonayo wakaongeza muda wa jinsi ya kuwahudumia watu hawa, hasa wafungwa, lakini zaidi waweze kuwa na kitengo maalum cha kuhudumia watu hawa, ili badala ya kuteseka muda mrefu kwenye jela na mahabusu, basi waweze kupata huduma mapema ili kuweza kuchukuliwa hatua mapema?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa la nyongeza, lakini naomba kuongezea kidogo pale mwanzo kwenye vyanzo vya sababu zinazosababisha ugonjwa wa afya ya akili, ili ikibidi na sisi wenyewe tuwe mabalozi wa kuweza kudhibiti hivi vyanzo maana vingine ni vya kawaida kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, zimetajwa sababu za kibaolojia ambazo ni vinasaba vile ambavyo mtu amekuwa ameumbwa navyo. Unaweza ukawa unavyo lakini usifikie stage ya kuweza kupata huu ugonjwa kutokana na mazingira unayoishi nayo katika jamii yako na wewe mwenyewe yanavyokuandaa kupata au kutokupata. Naweza nikatoa mifano hai hapa kuhusu matumizi ya vilevi kupita kiasi mfano bangi au pombe kupita kiasi, kama mwili wako katika maumbile yake unavyo vile vinasaba unaweza ukajikuta unaangukia kwenye ugonjwa wa kukosa akili. Kwa hiyo, inabidi jamii yetu tunakokwenda huko tuishi vizuri, matumizi ya kila kitu ni kwa kiasi, yasije yakakusindikiza kwenye kupata ugonjwa huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna watu wanawafanyia wenzao ukatili. Ukatili ukianza kufanyika kwenye maisha ya binadamu katika hatua zake zote siyo jambo jema. Sisi kama Waheshimiwa Wabunge ni mabalozi wazuri wakuweza kukemea vitendo vya ukatili maana vinaweza vikawapeleka kupata msongo hatimaye kupata ugonjwa huu wakawa hatari kwenye taifa letu na kwenye jamii yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna masuala jinsi gani mwanadamu anachukulia maisha yake, zile changamoto, watu wanasema wana ugumu wa maisha, hili nalo ni suala la kukaa na jamii iweze kuchukulia positive changamoto mbalimbali na siyo kujiwekea msongo wa mawazo kufika huko kusikotakiwa. Dunia imeendelea sana nayo ni shida kwa watoto wetu wanapoangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala lile lingine la pili naomba nilipokee, kweli umuhimu huo upo. Tutajipanga kama Wizara kuona jinsi gani tunatoa huduma hiyo ya kuharakisha hayo mashauri yaishe yanayotokana na afya ya akili. Ahsante.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa usambazaji wa umeme kwa kutumia REA umekuwa ukitumia transfoma za KV 50 lakini Serikali kwa ujumla na kama Taifa tumekuwa tukihamasisha sana shughuli za uzalishaji. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuendelea kutumia umeme huu wa KV 50 wakati idadi ya watu na shughuli za uzalishaji zinaongezeka baadaye kuonekana kwamba umeme huu hautoshi. Kwa nini Serikali isianze sasa kubadilisha badala ya kuweka KV 50 ianze kwa maeneo kidogo kidogo kuweka KV 100? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa tunapeleka umeme tunaangalia na kuzingatia mahitaji ya wananchi walio katika maeneo hayo. Transformer ya KV 50 ni transformer kubwa inaweza kuhudumia wateja zaidi ya 200 katika eneo moja. Kwa hiyo, kadri wateja wanavyoongezeka na sisi tutazidi kuboresha na kuongeza ukubwa wa transformer tunazoziweka katika maeneo husika.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma imekuwa ikihudumia wagonjwa wengi sana hasa kutokana na kwamba idadi kubwa ya wananchi wamehamia hapa Dodoma, lakini huduma za afya katika hospitali hii haziridhishi sana kwasababu kwa mfano sasa hivi ultra sound katika huduma za kawaida, wale wagonjwa wa kawaida ultra sound haifanyi kazi kwa muda mrefu, wananchi wamekuwa wakilalamika, lakini pia vitu vingi sana vina kasoro mimi nilikuwa naomba kuuliza.

Je, ni lini Wizara hii itaweka mkakati wa kuwa wanaiangalia hospitali hii kwa karibu zaidi ili kuhakikisha inatoa huduma kama ambavyo wananchi wanataka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mikakati na inaitekeleza mikakati ya kuhakikisha kwamba hospitali zetu zote kuanzia Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya lakini hata Hospitali za Kanda na ya Taifa zinatekeleza utoaji huduma bora kwa wananchi kwanza kwa kuhakikisha kwamba vifaa tiba vyote vinapatikana.

Kwa hiyo ninaomba nimhakikishe kwamba Hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa nayo ni moja ya hospitali ambazo zinasimamiwa kwa karibu na tutaendelea kuhakikisha tunasimamia kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini changamoto ya vifaa tiba kama ultra sound naomba hili nilichukue tulifanyie tathmini kwa haraka tuone kwa nini ultra sound haifanyi kazi na kama kunahitajika ultra sound mpya basi Serikali itaweka mipango mizuri ya kununua mapema iwezekanavyo ili wananchi waweze kupata huduma bora. (Makofi)
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Shinyanga Mjini licha ya kuwepo kwa umeme wa kutosha kutoka kwenye gridi ya Taifa, lakini kumekuwa na tatizo kubwa sana la kukatikakatika kwa umeme. Je, Serikali ipo tayari sasa kuja na hasa Mheshimiwa Naibu Waziri, yupo tayari kuongozana na mimi kwenda kule Shinyanga Mjini kusikiliza wananchi jinsi wanavyoathirika kibiashara pamoja na kijamii?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mayenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namruhusu Mheshimiwa Naibu Waziri kufuatana naye katika Jimbo lake kwa siku alizotaja. Hata hivyo, tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Shinyanga inatokana na matengenezo yanayofanyika kwa sasa katika line ya Segese ya umbali wa kilometa 12. Kwa hiyo mara nyingi tunataoa matangazo kurejesha hali ya umeme katika hali yake ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Shinyanga unapata umeme kutoka substation ya Ibadakuli yenye megawatt 182 ambapo mahitaji ya Mkoa wa Shinyanga ni Megawatt 123. Kwa hiyo umeme wa Mkoa wa Shinyanga unatosha, isipokuwa kwa sasa wananchi tunaomba radhi katika maeneo yote yanayopitiwa ikiwemo Ngokoro na maeneo mengine kwa sababu ya matengenezo ya line ya Segese. Ndani ya 14 matengenezo yatakamilika na umeme utarejea katika hali yake ya kawaida.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika Kata ya Itilima, Wilaya ya Kishapu kuna Kijiji cha Mwamala na katika Kata ya Mwaduiluhumbo kuna kijiji cha Nyenze, katika Wilaya hii ipo miradi ya skimu za umwagiliaji ambayo Serikali ilitoa pesa lakini baada ya kutoa pesa zile hazikutosha, katika Jimbo hili la Kishapu wakinamama katika maeneo haya wanapata shida sana kutokana na hali halisi ya ukame katika maeneo haya.

Je, ni lini Serikali itatupatia pesa katika skimu hizi mbili za Nyenze pamoja na Mwamala ili wananchi waweze kufaidika? Kwa sababu skimu hizi za umwagiliaji endapo kama zikikamilika maji yatasaidia mifugo pamoja na binadamu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji amekuwa akifanya ufuatiliaji mara kwa mara ofisini kwetu na ninamuahidi kwamba katika bajeti yetu ambayo tutaisoma mwezi ujao tutaainisha miradi ambayo itafikiwa na miradi hii pia tutaifikia. (Makofi)
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wizara hii kwa Mheshimiwa Ummy ameitendea haki sana kwa kufanya kazi kubwa sana; na kwa kuwa akina mama wengi wale ambao wanajifungua kwa operation wamekuwa wakilalamika kuhusu maumivu makubwa sana kutokana na zile sindano ambazo wamekuwa wakichomwa mgongoni; na kwa kuwa kuna pesa hizi Shilingi bilioni 460 za World Bank; na kwa kuwa Mheshimiwa Ummy nakuamini una wataalamu na watafiti wa kutosha: -

Je, kwa nini Serikali isifanye utafiti na kujua ni nini hasa kinachosababisha akina mama hawa wapate maumivu ambayo almost yatasababisha ulemavu mara baada ya kujifungua hapa Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Shinyanga kwa swali lake lakini kwa jinsi anavyowapambania wanawake wa Mkoa wa Shinyanga ikiwemo akina mama wajawazito.

Mheshimiwa Spika, nalipokea swali la Mheshimiwa Lucy Mayenga, ndiyo maana nimesema, Rais Samia ameruhusu mradi huu wa investing in people na focus yake ni afya ya uzazi, mama na mtoto. Fedha zote hizi tutazipeleka katika kuboresha huduma za uzazi. Kwa hiyo, hiyo sindano ambayo wanachomwa akina mama wajawazito ni dawa ya usingizi ili waweze kufanyiwa upasuaji. Tutafanya tathmini kama alivyoshauri.

Mheshimiwa Spika, pia nataka kuwaahidi, tunakwenda kuhakikisha tunatumia huduma za ubingwa za uzazi katika mradi huu ambao tunautekeleza. Vile vile tutajenga hospitali ya mama na mtoto katika Mkoa wa Dodoma ya kwanza ya Kitaifa ili kujenga uwezo wa afya ya uzazi, mama na mtoto katika nchi ya Tanzania. Kwa hiyo, suala hili tunalibeba, tutalifanyia kazi. (Makofi))
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, masuala mazima ya Mfuko wa Jimbo kwa wananchi wetu ni katika nia ya kuongeza maendeleo na mipango mizima ya kuinua uchumi wa wananchi wetu. Lakini Mheshimiwa Waziri katika Wizara yako kama utakumbuka Novemba mwaka jana Mheshimiwa Rais alipokuwa Glasgow alihutubia nchi tajiri na akaziomba kuongeza ufadhili wa fedha kwa nchi maskini ili kuweza kusaidia masuala mbalimbali ya kulinda mazingira. Fedha hizi zimekuwa nyingi sana, zimetolewa nyingi sana, lakini mbona Wizara hii iko kimya kutoa idhibaki (accreditation) kwa taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kwa sababu tunafahamu kwamba nchi hii ikipata pesa hizi maendeleo yatapatikana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru sana dada yangu Lucy Mayenga kwa ufatiliaji wake na kwa kweli katika mkutano uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana kule Glasgow, Scottish; Mheshimiwa Rais alizungumza mambo makubwa sana. Naomba niwaambie Watanzania katika mkutano ule hii image ya Tanzania imekuwa kubwa sana kwa Rais wetu katika kushughulikia masuala mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo alilouliza halihusiani na Mfuko wa Jimbo isipokuwa kama Serikali katika masuala ya miradi ya maendeleo ndio maana pale ofisini kwetu sasa hivi tunafanya kazi kubwa ya uandishi wa miradi. Na mtakumbuka mwaka huu itakapofika tarehe 5 Juni tutazindua mpango mkakati wa kutekeleza maeneo mbalimbali ambao mpango huo ndani yake una jinsi gani tunafanya resource mobilization ya upatikanaji wa fedha kushughulikia changamoto za kimazingira katika maeneo mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1998 Serikali ilitaifisha viwanda vikiwemo vya nguo na vingine. Mwaka 2017 viwanda hivi vilirejeshwa Serikalini katika Bajeti ya Viwanda na Biashara ya mwaka jana, Waziri alisimama hapa akasema viwanda hivi vitatangazwa kwa wawekezaji wenye uwezo ili waweze kuvifufua. Wananchi wetu na hasa vijana wanalalamika ajira, kwa nini Wizara iko kimya mpaka leo?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Lucy, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli viwanda ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa na vikawa havifanyi kazi jumla viwanda kama 20 vilikuwa vimerejeshwa Serikalini. Kati ya hivyo 10 tutavitangaza, notice ilishatangazwa mwaka jana, lakini sasa tunaendelea na mchakato wa kupata wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, vingine ambavyo tunadhani ni muhimu kama Serikali tuendelee kuviendeleza, vitakuwa chini ya Mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwemo NDC, maeneo yale ya uwekezaji kwa ajili ya wananchi EPZA, na kadhalika. Kwa hiyo, Serikali inaendelea na mchakato wa kuona tunapata wawekezaji mahiri, hatutaki tena kwenda haraka tukapata wawekezaji ambao badala ya kuendeleza viwanda watavidhoofisha zaidi kama ambavyo ilitokea huko nyuma. Kwa hiyo tunaendelea na mchakato huo kuhakikisha tunavitangaza viwanda hivyo kwa wawekezaji wenye tija na wenye nia ya kuendeleza viwanda hivyo. (Makofi)
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kituo cha Afya cha Kambarage kilichopo Manispaa ya Shinyanga Mjini ambacho ni tegemeo kubwa sana kwa wananchi na hasa akinamama kwa kuwa kinazalisha akinamama takribani 330 kwa mwezi, kinakabiliwa na tatizo kubwa sana la ukosefu wa generator. Kiasi cha shilingi milioni 290 ambayo ilitolewa katika mpango wa Serikali kuboresha vituo vya afya ilitolewa na ikakabidhiwa MSD, vifaa tiba vingi vimekuja kasoro generator, wananchi wanalalamika. Je, ni lini generator litakuja kama sehemu ya vifaa-tiba katika Kituo hicho cha Afya cha Kambarage? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimetembelea hicho kituo na nimekuta Mheshimiwa Mbunge alichangia milioni 18 kwa ajili ya ujenzi wa hicho kituo, lakini ninachoweza kusema ni tukishamaliza maswali hapa, tukutane mimi na yeye, tutashirikiana na mwenzangu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ili tuweze kuhakikisha kwamba, vifaa hivyo vinafika kwa sababu, kama fedha zimepelekwa, basi ni kupeleka kile ambacho kinatakiwa kufanyika. Tukae mimi na yeye tuhakikishe generator limeenda.
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sababu kubwa ambayo inasababisha wananchi waweze kushindwa kujenga nyumba bora ni gharama kubwa ya vifaa vya ujenzi, lakini vifaa hivi ni suala ambalo haliko Wizara ya Ardhi, liko Wizara ya Viwanda na Biashara.

Je, Wizara hii iko tayari sasa kukaa na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuangalia zile sababu zote zinazofanya vifaa kuwa bei kubwa ikiwemo matamko ya viongozi, gharama kubwa za kodi na changamoto nyingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa mawazo yake mazuri, lakini nataka nimhakikishie tu kwamba yako maelekezo toka kwa Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kukaa na Wizara zote zinazohusika katika eneo hili la ujenzi wa nyumba ikiwemo Wizara ya Ujenzi, ili kuhakikisha kwamba gharama zinakuwa nafuu katika ujenzi, lakini pia katika vifaa na kuhakikisha mazingira yanakuwa mazuri ya upatikanaji wa nyumba zilizo bora na salama.