Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. David Mathayo David (37 total)

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, lakini naipongeza Wizara hii kwa kuwa makini katika kufanya kazi katika sekta hii ya nishati na madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza maswali
mawili ya nyongeza ningependa kuwapa pole wananchi wa Jimbo la Same Magharibi, hususan kata ya Hedaru ambao wamepoteza nyumba nyingi pamoja na mifugo na mazao kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataallah, aweze kutupa mvua za kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuuliza
maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, katika Mradi wa REA Awamu ya Pili, mkandarasi ambaye anaitwa SPENCON alishindwa kufanyakazi na kwa hiyo, vijiji vingi pamoja na vitongoji vingi vya Jimbo la Same Magharibi hususan vijiji 48, umeme haujakamilika kutokana na kwamba, mkandarasi huyo alishindwa kazi.
Je, REA Awamu ya Tatu, vijiji hivi ambavyo vilikosa umeme pamoja na vitongoji vyake, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kwamba, vitongoji vyote vinapata umeme na vijiji vyangu vyote vya Jimbo la Same Magharibi katika Awamu hii ya Tatu ya REA?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili la Bajeti kuongozana na mimi kwenda katika Jimbo la Same Magharibi, ili akajionee mwenyewe vijiji na vitongoji ambavyo havina umeme katika Jimbo langu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, awali ya yote niungane na Mheshimiwa David kuwapa pole wananchi wake kwa tatizo walilopata.
Mheshimiwa Nibu Spika, kulingana na maswali yake mawili ni kweli kabisa katika utekelezaji wa REA Awamu ya Pili, Mikoa miwili ya Kilimanjaro na Singida haikukamilika ipasavyo na ni kweli kabisa mkandarasi SPENCON hakufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kutoa taarifa pia ya hatua za Serikali ambazo zilichukuliwa kutokana na kutofanya kazi vizuri kwa mkandarasi huyo.
Hatua ya kwanza tulichukua asilimia 10 ya mkataba wake ambayo ni retention kimkataba kabisa. Hatua ya pili, kazi hiyo sasa atapewa mkandarasi mwingine ili aikamilishe vizuri na wananchi wa Same waendelee kupata umeme. Lakini hatua ya tatu, tunaendelea sasa kuchukua hatua za kisheria, ili Wakandarasi wa namna hiyo sasa wapate fundisho waache kuwakosesha miundombinu wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David kwamba wananchi wa Same, vijiji vyako vyote 48 vitapata umeme. Naelewa viko vijiji vya milimani kwa Mheshimiwa Dkt. David kijiji cha Muhezi, Malaloni kule Malalo pamoja na kwa Hinka, vitapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika naelewa vile vijiji 48 anavyosema Mheshimiwa, yapo maeneo kama kule Hedaru, yako maeneo kule ambako Mheshimiwa tumesema Chekereni, Mabilioni pamoja na Jificheni Mabilioni, pamoja na kijiji cha Njiro vyote vitapata umeme. Hivyo, ninakuhakikishia kwamba vijiji ambavyo havijapata umeme kwenye REA II, sasa vyote vitapata umeme. Siyo vijiji tu hata vitongoji vyake na taasisi za umma pamoja na maeneo mengine muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili la kuongozana naye, kwanza kabisa niko tayari, ninaweza nikasema utakaponikaribisha utakuwa umechelewa,
ukichelewa sana utanikuta kwenye Jimbo lako, kwa hiyo, niko tayari kutembelea kwenye Jimbo lako.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawwili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wangu wa Kata za Kisiwani, Vumari na Mji Mdogo wa Same wamebanwa sana na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi; na kwa kuwa Mwenyezi Mungu wakati anaumba dunia alimuumba binadamu akamwambia atawale viumbe vyote viishivyo kwenye maji na kwenye nchi kavu; na kwa kuwa wakati wa uhuru tulikuwa na idadi ya watu milioni 10.3 na sasa hivi tuko takribani milioni 50, tulikuwa na ng’ombe milioni nane sasa hivi milioni 28; tulikuwa na mbuzi milioni 4.4 sasa hivi ni milioni 16.6; tulikuwa na kondoo milioni tatu na sasa hivi ni milioni tano, tulikuwa na nguruwe 22,000 sasa hivi ni milioni mbili, astaghfilillah nimetaja nguruwe wakati ni mwezi wa Ramadhani, mnisamehe sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza je, Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo, TAMISEMI pamoja Ardhi ili waweze kutathmini eneo na idadi ya watu pamoja na mifugo wanayofuga ili kusudi kama kuna uwezekano maeneo ya hifadhi za misitu pamoja na Hifadhi za Wanyamapori zipunguzwe ili binadamu waweze kupata maeneo ya makazi pamoja na mifugo na kilimo?
Swali la pili, kwa kuwa Botswana, Afrika ya Kusini na Namibia wameweza kuzuia wanyamapori kutoka kwenye mapori kwenda kwa binadamu ama kwenye wanyama wanaofugwa, je, Serikali iko tayari sasa kuandaa mpango rasmi wa kuweka fence ili wanyamapori wasiweze kwenda kwenye makazi ya watu kuwasumbua na kuwaletea madhara ikiwa ni pamoja na vifo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge anazungumzia upungufu wa ardhi kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu hasa kwa ajili ya faida ya kiuchumi na kijamii, akihusisha na uhaba au upungufu wa rasilimali ardhi kwa ajili ya shughuli hizo zinazotokana na ongezeko la binadamu na wanyama kama ambavyo amewataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi Serikali inatambua na kwa kweli ni dhamira ya Serikali kuwafanya wananchi waweze kufanya kazi za kuzalisha mali kwa sababu ni kwa kufanya hivyo tu peke yake ndiyo hata madhumuni makubwa kabisa ya Serikali ya kuiondoa nchi kutoka katika uchumi wa chini kwenda uchumi wa kati yatafanikiwa, ni kwa kufanya kazi tu peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi waweze kufanya kazi lazima waweze kuwa na ardhi au wawe na maeneo ya kufanyia kazi. Kabla hatujaanza kusema kwamba maeneo tunayoyatumia hayatoshi ni lazima kwanza tuone maeneo hayao yanatumikaje hivi sasa, kwa hiyo, hapa ndipo ambapo tunazungumzia juu ya suala la mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Kuhusu swali lake tutashirikiana vipi na Wizara nne zile alizozitaja ukweli ni kwamba Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba tayari tunayo Kamati ya Kitaifa ya Wizara alizozitaja ambayo iko kazini inashughulikia suala hilo na baada ya utafiti wa kitaalam, baada ya kujiridhisha kitaalam tutapitia upya sheria na kuona katika kila eneo kama kweli suluhisho pekee la kuweza kuwafanya wananchi kupata eneo la kufanya shughuli za kibinadamu kama suluhisho pekee ni kugawa maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa faida ambazo tunazifahamu ziko lukuki, basi Serikali itazingatia mwelekeo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kutajitokeza ukweli kwamba bado maeneo tuliyonayo tunaweza kuyatumia vizuri zaidi bila kuathiri maeneo yaliyohifadhiwa basi hatutakuwa na haja ya kupunguza maeneo ya hifadhi isipokuwa tutajiimarisha zaidi katika kutumia vizuri zaidi maeneo ambayo hayajahifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili juu ya kuweka fence, kuweka uzio kwa ajili ya kuzuia wanyamapori kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya binadamu, kwa ajili ya maeneo ya makazi ya binadamu na maeneo ambayo binadamu wanafanya shughuli za kibinadamu za kiuchumi na kijamii; napenda tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba huko ambako anazungumzia kwamba udhibiti umefanikiwa njia iliyotumika siyo hii tu peke yake ya kuweka fence, njia ya kuweka fence ni njia mojawapo na inatumika tu pale ambapo ni lazima kuweka fence kwa sababu njia hii ni ya gharama kubwa na si rafiki pia kwa mazingira hata kwa wanyama wenyewe na hata kwa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kwa sasa hivi ni kwamba Serikali inalichukua suala hili na kwa kweli tumekuwa tukilifanyia kazi muda mrefu kuweza kuona ni namna gani tunaweza kudhibiti kiwango na kasi ya Wanyamapori kutoka kwenye maeneo yao na kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi hapa vilevile na binadamu na wenyewe tusiendelee na utaratibu ule wa kwenda kukaa kwenye maeneo ambayo aidha ni njia za wanyapori au ni maeneo ya mtawanyiko ya wanyamapori.
MHE. MATHAYO D. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza.
Aidha, napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa kujibu maswali yake vizuri na kitaalam. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Benki Kuu imepunguza riba ya mabenki ya biashara yanapokopa kutoka kwenye Benki Kuu hadi kufikia asilimia tisa na kwa kuwa pia, imepunguza amana kutoka asilimia kumi hadi asilimia nane ya kiwango cha fedha ambazo mabenki haya ya biashara yanatakiwa yahifadhi Benki Kuu. Je, Benki Kuu imefuatilia na kuona kwamba, mabenki ya biashara yanatoza riba nzuri au yametoa punguzo zuri la riba kwa wananchi ambao wanakopa kwenye mabenki hayo?
Swali la pili, kwa kuwa katika nchi zinazoendelea asilimia 70 ya fedha zinakuwa mikononi mwa wananchi na asilimia 30 inakuwa kwenye mabenki pamoja na Serikali. Je, Benki Kuu imefanya utafiti na kuona, kwa sababu sasa hivi tukiangalia fedha katika mzunguko kwa wananchi wa kawaida zimepungua sana.
Je, Benki Kuu imefanya utafiti na kujua kwamba, fedha hizi ziko wapi ili waweze kutunga Sera ambazo zitarudisha fedha hizi kwenye mabenki ya biashara pamoja na wananchi ili maisha yaweze kuwa mazuri, lakini wananchi pia washiriki vizuri katika shughuli za kujenga nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumeshusha kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi na kwa sasa tunafanya ufuatiliaji kuona kwamba, riba zinazotozwa na benki zetu za biashara pamoja na taasisi za kifedha zinashuka ku-respond katika jitihada hizi ambazo zimefanywa na Serikali kupitia Benki Kuu. Tutakapomaliza ufuatiliaji huu na sasa hivi tuko katika vikao mbalimbali na mabenki haya kuona ni jinsi gani sasa wanaweza kurejesha riba chini ili wananchi wetu waweze kukopa, tutaleta taarifa katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, napenda kumwambia Mheshimiwa Mathayo kuwa ni sahihi kwamba asilimia 30 tu ya pesa ndiyo iko benki, asilimia 70 iko kwa wananchi. Kinachoonekana kwa sasa ni kwamba Serikali tumeimarisha mfumo wetu wa ukusanyaji wa kodi. Yule mfanyabiashara aliyekuwa akifanya biashara bila kulipa kodi akijidanganya ile ni faida yake, sivyo ilivyo kwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono tuweze kukusanya kodi inavyostahiki na ili Watanzania sasa tuishi katika uchumi ambao Taifa letu na wananchi wanastahili kuishi. Kiuhalisia fedha bado iko ya kutosha katika mikono ya wananchi kama alivyokiri yeye Mheshimwa Mbunge aliyeuliza swali kwamba asilimia sabini ya pesa yetu iko kwa wananchi na uchumi wetu unaendelea vizuri.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza na pili nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutupa majibu ya matumaini. Hata hivyo, napenda kusahihisha kidogo wakati wataalam wamekuja mwaka 2015/2016 nilikuwepo na tuliona maeneo mawili ya malambo kwa ajili ya kujenga malambo na maeneo mawili kwa ajili ya majosho na sehemu moja ya kisima kirefu, lakini jibu la Waziri hapa linazungumzia lambo. Kwa hiyo naomba hiyo irekebishwe kwamba ni miundombinu hiyo niliyoitaja.
Mheshimiwa Spika, sasa naelekea kwenye swali la kwanza, je, ni kiasi gani ambacho kimetengwa kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya miundombinu hiyo ambayo nimeitaja katika Jimbo la Same Magharibi na hususani Kata ya Ruvu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa millioni 100 zinaweza zikatosha malambo mawili na majosho mawili kama kazi hii itasimamiwa na Wizara, lakini kazi hii kama itasimamiwa na Halmashauri milioni 100 inaweza ikatosha josho moja au lambo moja. Je, Serikali sasa iko tayari kwa sababu yenyewe ndio inatoa hizi fedha isimamie kusudi miundombinu hiyo ikamilike kwa bajeti ya mwaka huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu wa usahihi wa nilichokisema ambapo amesema anarekebisha tutaenda kuangalia kuhusu makubaliano yale, lakini kimsingi hakuna kitu kilichoharibika, tutaenda kutekeleza kadiri tulivyoahidi wakati tulipokwenda Jimboni kwake.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuhusiana na ni kiasi gani cha fedha ambacho kimetengwa, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa inakuwa ni vigumu kuwa na takwimu sahihi lakini anaweza akanifuata baadaye nikamweleza na ombi lake la kwamba Wizara yenyewe ndio inasimamia ujenzi ule, vilevile tutalichukua na ukweli wa mambo fedha zinazotolewa mara nyingi na Wizara kwa ajili ya kujenga miundombinu huwa tunahakikisha kwamba tunazisimamia ili ifanye kazi iliyoelekezwa.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawwili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wangu wa Kata za Kisiwani, Vumari na Mji Mdogo wa Same wamebanwa sana na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi; na kwa kuwa Mwenyezi Mungu wakati anaumba dunia alimuumba binadamu akamwambia atawale viumbe vyote viishivyo kwenye maji na kwenye nchi kavu; na kwa kuwa wakati wa uhuru tulikuwa na idadi ya watu milioni 10.3 na sasa hivi tuko takribani milioni 50, tulikuwa na ng’ombe milioni nane sasa hivi milioni 28; tulikuwa na mbuzi milioni 4.4 sasa hivi ni milioni 16.6; tulikuwa na kondoo milioni tatu na sasa hivi ni milioni tano, tulikuwa na nguruwe 22,000 sasa hivi ni milioni mbili, astaghfilillah nimetaja nguruwe wakati ni mwezi wa Ramadhani, mnisamehe sana. (Kicheko)

MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza je, Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari kushirikiana na Wizara ya Kilimo, TAMISEMI pamoja Ardhi ili waweze kutathmini eneo na idadi ya watu pamoja na mifugo wanayofuga ili kusudi kama kuna uwezekano maeneo ya hifadhi za misitu pamoja na Hifadhi za Wanyamapori zipunguzwe ili binadamu waweze kupata maeneo ya makazi pamoja na mifugo na kilimo?
Swali la pili, kwa kuwa Botswana, Afrika ya Kusini na Namibia wameweza kuzuia wanyamapori kutoka kwenye mapori kwenda kwa binadamu ama kwenye wanyama wanaofugwa, je, Serikali iko tayari sasa kuandaa mpango rasmi wa kuweka fence ili wanyamapori wasiweze kwenda kwenye makazi ya watu kuwasumbua na kuwaletea madhara ikiwa ni pamoja na vifo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge anazungumzia upungufu wa ardhi kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu hasa kwa ajili ya faida ya kiuchumi na kijamii, akihusisha na uhaba au upungufu wa rasilimali ardhi kwa ajili ya shughuli hizo zinazotokana na ongezeko la binadamu na wanyama kama ambavyo amewataja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi Serikali inatambua na kwa kweli ni dhamira ya Serikali kuwafanya wananchi waweze kufanya kazi za kuzalisha mali kwa sababu ni kwa kufanya hivyo tu peke yake ndiyo hata madhumuni makubwa kabisa ya Serikali ya kuiondoa nchi kutoka katika uchumi wa chini kwenda uchumi wa kati yatafanikiwa, ni kwa kufanya kazi tu peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wananchi waweze kufanya kazi lazima waweze kuwa na ardhi au wawe na maeneo ya kufanyia kazi. Kabla hatujaanza kusema kwamba maeneo tunayoyatumia hayatoshi ni lazima kwanza tuone maeneo hayao yanatumikaje hivi sasa, kwa hiyo, hapa ndipo ambapo tunazungumzia juu ya suala la mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Kuhusu swali lake tutashirikiana vipi na Wizara nne zile alizozitaja ukweli ni kwamba Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba tayari tunayo Kamati ya Kitaifa ya Wizara alizozitaja ambayo iko kazini inashughulikia suala hilo na baada ya utafiti wa kitaalam, baada ya kujiridhisha kitaalam tutapitia upya sheria na kuona katika kila eneo kama kweli suluhisho pekee la kuweza kuwafanya wananchi kupata eneo la kufanya shughuli za kibinadamu kama suluhisho pekee ni kugawa maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa faida ambazo tunazifahamu ziko lukuki, basi Serikali itazingatia mwelekeo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kutajitokeza ukweli kwamba bado maeneo tuliyonayo tunaweza kuyatumia vizuri zaidi bila kuathiri maeneo yaliyohifadhiwa basi hatutakuwa na haja ya kupunguza maeneo ya hifadhi isipokuwa tutajiimarisha zaidi katika kutumia vizuri zaidi maeneo ambayo hayajahifadhiwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili juu ya kuweka fence, kuweka uzio kwa ajili ya kuzuia wanyamapori kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya binadamu, kwa ajili ya maeneo ya makazi ya binadamu na maeneo ambayo binadamu wanafanya shughuli za kibinadamu za kiuchumi na kijamii; napenda tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba huko ambako anazungumzia kwamba udhibiti umefanikiwa njia iliyotumika siyo hii tu peke yake ya kuweka fence, njia ya kuweka fence ni njia mojawapo na inatumika tu pale ambapo ni lazima kuweka fence kwa sababu njia hii ni ya gharama kubwa na si rafiki pia kwa mazingira hata kwa wanyama wenyewe na hata kwa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kwa sasa hivi ni kwamba Serikali inalichukua suala hili na kwa kweli tumekuwa tukilifanyia kazi muda mrefu kuweza kuona ni namna gani tunaweza kudhibiti kiwango na kasi ya Wanyamapori kutoka kwenye maeneo yao na kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi hapa vilevile na binadamu na wenyewe tusiendelee na utaratibu ule wa kwenda kukaa kwenye maeneo ambayo aidha ni njia za wanyapori au ni maeneo ya mtawanyiko ya wanyamapori.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini niwashukuru pia kwamba sasa wataanza kuchimba kisima kirefu kwa ajili ya wafugaji wa Ruvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi hii ya Serikali ni ya mwaka 2012/2013 na mwaka 2015 wataalamu walikuja Kata ya Ruvu na kubainisha maeneo ya majosho na malambo pamoja na visima virefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa imeshakuwa ni muda mrefu na wafugaji wale wa Kata ya Ruvu wanahangaika sana kuhamisha mifugo huku na kule. Je, Serikali haioni kwamba kwa sasa na hasa kwenye bajeti hii inayokuja ya mwaka 2020/2021 wakatenga fedha za kutosha ili waweze kukamilisha ahadi yao ambayo ilishakubalika mwaka 2012/2013 ili wananchi hao wa Ruvu waweze kupata hii huduma ya malambo na majosho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea Wilaya ya Same na kuona maeneo ambayo yanahitaji miundombinu ya mifugo kusudi wafugaji wale waweze kupata miundombinu hiyo na mifugo iweze kupata huduma hiyo kama inavyotakiwa?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa David Mathayo ambaye ni Waziri Mstaafu wa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, na kwamba nijibu maswali yake mawili kama alivyouliza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari kufanya ziara jimboni kwake mara tu baada ya Bunge hili kumalizika na kwenda kukutana na wafugaji wa maeneo hayo na kukagua miundombinu yao na kutafuta namna ya kuiboresha ili waweze kupata sehemu nzuri ya kunyweshea mifugo yao lakini pamoja na kuogeshea mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nakubaliana na yeye kwamba katika bajeti hii inayoanza tutaingiza mradi wa lambo katika jimbo lake; ambao umekuwa wa muda mrefu sana kama alivyoeleza mwenyewe, tangu yeye mwenyewe akiwa Waziri na mpaka leo hii ahadi hiyo haijatekelezwa. Sasa safari hii tutaitekeleza kwa kuweka bajeti kwenye mpango wetu wa Serikali ambao tutauanza hivi karibuni.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawili ya nyongeza lakini kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka msukumo kwenye mradi huu. Pia niipongeze Serikali kwa maana ya Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kufanya kazi vizuri na kufuatilia vizuri mradi huu na kuondoa wakandarasi ambao ni wazembe ambao wanachelewesha huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la nyongeza, kwa kuwa Desemba ni mbali kwa mahitaji ya maji katika Mji Mdogo wa Same kata za Njoro, Kisima, Stesheni pamoja na Same Mjini; na kwa kuwa Serikali hivi sasa inachimba visima viwili virefu, je, visima hivi vitakamilika lini ikiwa ni pamoja na kuweka pump kusudi wananchi hawa waweze kupunguza makali ya ukosefu wa maji kabla ya Desemba kufika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana nami baada ya Bunge hili ili twende tukakague kata kwa kata, kijiji kwa kijiji, kitongoji kwa kitongoji kuhusiana na utekelezaji wa mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tunafahamu kwamba Desemba ni mbali na maisha lazima yaendelee. Sisi Wizara ya Maji tuko imara kabisa kuhakikisha kwamba tatizo sugu la maji tunakwenda kulishughulikia kwa haraka sana. Wizara tumejipanga vyema chini ya Jemedari wetu Mheshimiwa Jumaa Aweso ambapo katika Mji wa Same kisima kipya kimeshachimbwa eneo la Stelingi chenye kina cha mita 200. Kazi hii ilianza Oktoba 2020 na itakamilika mwezi huu Februari 2021. Kama Quick-win program ya kuongeza uzalishaji wa maji katika Mji wa Same utahudumiwa na visima virefu viwili vilivyopo Stelingi na Kambambungu pamoja na chemichemi mbili za Mahuu na Same Beach.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la kuongozana na wewe Mheshimiwa Mbunge usiwe na hofu, hiyo ndiyo shughuli yangu. Mheshimiwa Mbunge nitampa upendeleo mara baada ya Bunge hili tutakwenda, tutahakikisha wananchi wa Same Magharibi wanapata maji ya kutosha na hilo tatizo litabaki kuwa historia. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na napenda kumjulisha tu Mheshimiwa David kwamba timu kubwa ya club kubwa ya pale Msimbazi iko humu ndani basi na kesho tunakukaribisha. (Makofi/Kicheko)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa daraja hili linaunganisha Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Kilimanjaro na hivyo ku-facilitate kusafirisha mifugo pamoja na mazao ya kilimo kwenda mikoa mbalimbali kutoka mikoa ya Kati kwenda Kaskazini. Kwa kuwa kuwepo kwa daraja hili kutafupisha safari ya kutoka Kilimajaro kwenda Dodoma kwa kilometa 172. Kwa kuwa fedha zinazotengwa TARURA ni ndogo sana na haziwezi zikatosheleza ujenzi wa daraja hili kwa haraka. Je, Serikali, Wizara ya TAMISEMI, haioni kwamba umefika wakati sasa wa kushirikiana na TANROADS au Wizara ya Ujenzi kwa sababu imekuwa inafanya hivyo katika projects mbalimbali ili kuweza kunusuru wananchi katika maeneo mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wakati huu ni wakati wa amani na kwa kuwa Jeshi letu la Wananchi limekuwa linafanya kazi nzuri sana ya ujenzi wa miundombinu, je, katika madaraja haya ambayo yametajwa na Waheshimiwa Wabunge asubuhi ya leo pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haioni kwamba inaweza kushirikisha Jeshi ili liweze kusaidia kujenga madaraja haya ili wananchi waweze kupita kwa urahisi na shughuli za uchumi zikaendelea vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Daraja hilo la Mto Pangani ni muhimu sana kwa sababu linaunganisha mikoa miwili; Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Kilimanjaro. Ni kweli kwamba bajeti ya kawaida ya kuhudumia Halmashauri ya Same haiwezi kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kubwa; na hivyo katika utaratibu wa Serikali kuna ujenzi wa taratibu za kawaida lakini pia kuna ujenzi maalum kwa maana ya kutenga bajeti maalum kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu korofi kama ilivyo daraja hilo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mbinu hizi mbili za matengenezo ya muda wa kawaida kwa maana ya utaratibu wa kawaida na matengenezo maalum hutumika pale ambapo madaraja yanahitaji fedha kiasi kikubwa kuliko bajeti ya halmashauri husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili TARURA tumeendelea kushirikiana kwa karibu sana na TANROADS kuona namna bora ya kushirikiana ili daraja hilo liweze kupata suluhu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ushirikiano huu unaendelea vizuri na tunaamini kwamba katika mwaka wa fedha ujao tutakuwa tumefikia hatua nzuri ya utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la Jeshi kushiriki katika kujenga madaraja hayo, mara nyingi Serikali katika madaraja ambayo yanahitaji ujenzi wa dharura kutokana na maafa mbalimbali kama mafuriko, sote tumekuwa mashahidi kwamba majeshi yetu yamekuwa yanafika na kufanya matengenezo hayo kwa haraka na kwa wakati ili kurejesha huduma kwa wananchi. Jambo hili litaendelea kutekelezwa kadri ya matukio hayo hayavyojitokeza.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, ninadhani kwamba majibu haya kidogo sijaridhika sana, lakini niseme ni mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, faru weusi pamoja na wanyama wengine wanapatikana katika Hifadhi za Taifa tatu tu katika nchi hii zikiwemo Serengeti, Ngorongoro pamoja na Hifadhi ya Mkomazi. Upande wa Kenya wana kiwanja cha ndege pale Tsavo, upande wa Kenya Hifadhi ya Tsavo ndiyo inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, na hivyo wanapata watalii wengi kwa sababu wao wana kiwanja cha ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile umbali wa kutoka Arusha na KIA ni mkubwa sana ukizingatia na uhitaji wa watalii kuja kuona faru weusi walioko kwenye sanctuary pale Mkomazi National Park. (Makofi)

Ninaomba Serikali iangalie uwezekano wa kukarabati Uwanja wa Ndege wa Same ili watalii hao waweze kufika kwa urahisi na kuongeza Pato la Taifa kama Mheshimiwa Rais alivyosema jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ninaomba inapowezekana Mheshimiwa Waziri aje pale Same ili aweze kuona mazingira hayo ninayozungumzia, kwamba uwanja upo unahitaji marekebisho ili tuweze kukuza uchumi kupitia utalii. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuleta wazo zuri sana ambalo kimsingi siyo la Same Magharibi peke yake, hili ni jambo la Kitaifa.

Ninaomba nitumie nafasi hii kumuelekeza Katibu Mkuu Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Uchukuzi, awatume wataalam wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege waende Same Magharibi wafanye tathmini, tuangalie cost implication ili kiwanja hiki kikarabatiwe mapema iwezekanavyo, fedha itakapopatikana kupitia watalii katika eneo hili itasaidia kuboresha hotuba nzuri ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya jana ya kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kabla Bunge hili halijaisha naomba kibali cha Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Waziri Mkuu, twende Sa me kwa sababu kuona ni kuamini, tushuhudie hali halisi na tuongeze maelekezo ya ziada. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kunipa nafasi hii lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kutupa majibu yenye matumaini kwa Jimbo la Same Magharibi na Wilaya nzima ya Same, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa hii ni ahadi ya Waziri Mkuu kujenga Hospitali ya Wilaya ya Same na kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Same ipo katika barabara kuu inayokwenda Arusha ambapo ajali nyingi sana zinatokea na watu wote wanaopata matatizo haya wanategemea kupata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Same na kwa kuwa eneo limeshatengwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Same.

Je, Serikali inapoanza kujenga hospitali mpya 43; Wilaya ya Same itapewa kipaumbele ili iweze kujengwa hospitali na kuletwa vifaa tiba pamoja na wafanyakazi wa kutosha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Sera ya Serikali ni kuwa na zahanati angalau kwa kila kijiji na kituo cha afya kila kata; na kwa kuwa katika Jimbo langu tumejenga zahanati za kutosha takribani asilimia 80 lakini hatuna wafanyakazi na hatuna vitendea kazi.

Je, Serikali ni lini itapeleka watumishi wa afya kwenye zahanati hizo ili tuache kuzifunga zianze kutumika kusaidia wananchi wa Wilaya ya Same?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa David Mathayo David kwa juhudi zake za kuhakikisha mara kwa mara anawasiliana na Serikali kuhakikisha Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Same inajengwa; na mimi nimuhakikishie Serikali itaendelea kushirikiana naye lakini na wananchi wa Same kuhakikisha katika vipaumbele hivi tunakwenda kujenga Hospitali ya Wilaya ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, hii ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na kama ilivyo ada ahadi za viongozi wetu wa Kitaifa zinapewa kipaumbele; na mimi naomba nimuhakikishie kwamba Serikali tayari imeshaainisha ahadi zote za kitaifa za viongozi wetu wa kitaifa na zinakwenda kufanyiwa kazi kwa awamu na hospitali hii ya Same ikiwemo.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, ni kweli tuna sera ya zahanati katika vijiji na vituo vya afya katika kata, lakini tumeamua kufanya mapitio ya sera ile ili tuwe na ujenzi wa zahanati kimkakati zaidi, lakini pia ujenzi wa vituo vya afya kimkakati zaidi badala ya kuwa kila kijiji na kila kata. Lakini nimhakikishie vituo hivi vyote ambayo vimejengwa Serikali inaendelea kuajiri na watumishi hao 2,726 walioajiriwa wapo ambao watapelekwa Same na katika awamu nyingine za ajira tutahakikisha tunapeleka watumishi Same. Ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru majibu ya Mheshimiwa Waziri kidogo yanaleta matumaini kwa mbali, lakini kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne japo haijawahi kuwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi; lakini kwa kuwa TANROADS kila mwaka inapoteza mabilioni ya fedha, kwa mfano mwaka huu barabara hii imetengewa shilingi bilioni mbili, lakini vifusi vipowekwa baada ya mvua kunyesha usiku mmoja tu, kifusi hiki kinazolewa na maji ya mvua na wananchi wa milimani ambapo ni asilimia zaidi ya 65 ya wakaazi wa Wilaya ya Same wanakosa mawasiliano na pia Serikali inaingia hasara: -

Je, upembuzi yakinifu wa barabara hii utafanyika lini ili Serikali isipoteze mapato lakini wananchi wa Mwembe, Mbaga, Bonja mpaka Mamba waweze kupata mawasiliano pale mvua zinaponyesha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Tunafahamu kwamba Sera ya Serikali ni kuunganisha mikoa kwa mikoa na Wilaya kwa Wilaya; vile vile nchi hii na Wilaya hizi za nchi hii kuna tofauti ya mazingira, kwa mfano Wilaya ya Same kuna malima mingi sana, Lushoto kuna milima mingi; Mbinga kuna milima; Kagera na maeneo ya Arusha kuna milima mingi sana: Sasa kwa nini Serikali isichukue ikafanya upembuzi yakinifu wa barabara zote za milimani kusudi wananchi wa milimani waweze kupata usafiri wakati mvua zinanyesha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwenye maeneo ya miinuko vifusi huwa vinasombwa na maji. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna barabara za lami na za changarawe na za udongo. Azma ya Serikali ni kuwa na barabara zote za lami, lakini uwezo huo bado hatujakuwa nao na kwa hiyo Serikali inatengeneza barabara kwa kiwango cha lami, kila mwaka tunatenga fedha ili barabara hizo ziweze kutumika.

Mheshimiwa Spika, bajeti aliyoisema ya bilioni mbili siyo tu kuweka kifusi, ni pamoja na kutengeneza mifereji, madaraja pamoja na makalavati ili barabara hiyo iweze kutumika kwa mwaka mzima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema, tunatafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na hatimae usanifu wa kina.

Mheshimiwa Spika, pengine nitoe maagizo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro aweze kuainisha yale maeneo yote korofi na yenye miinuko mikali ili tuweze kufanyia matengenezo surface dressing ama hata kujenga barabara hizo kwa zege kama ilivyofanyika maeneo mengine kama Mikoa ya Manyara, Ruvuma, Kigoma, ukienda Morogoro; maeneo ambayo ni korofi basi barabara zinajengwa kwa kiwango hicho.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mikoa, ni kwamba kama tulivyoainisha kwamba tunaunganisha mikoa na mikoa kwa kiwango cha lami, hiyo ndiyo sera ambayo tunayo, lakini wazo la maeneo kwenye miinuko, basi tulichukue na tukiona kama fedha itatosha, basi Serikali itafanya hivyo. Azma ni kuhakikisha kwamba barabara zote zinajengwa kwa kiwango cha lami bila ya kujali eneo eneo na eneo. Ahsante. (Makofi)
MHE. MATHAYO D. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, Kata ya Vudee na Kata ya Mshewa katika Jimbo la Same Magharibi, ni miongoni mwa Kata za kujengewa vituo vya afya vya kimkakati: Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Kata ya Vudee na Kata ya Mshewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mathayo David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mbunge kwamba Serikali iliainisha kata zote za kimkakati kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na tutakwenda kujenga vituo vya afya hivyo kwa awamu ikiwemo kata hizi za kimkakati katika Jimbo la Same Magharibi. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia niipongeze sana Serikali kwa kupunguza riba katika hati fungani kwenye level tofauti. Ningependa kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika swali la kwanza; kwa sababu sasa hivi Serikali inafungua uchumi, inafungua nchi na kila mtu anatakiwa ashiriki katika suala zima la uchumi. Je, Serikali inaonaje kwamba ipunguze idadi ya minada ya hati fungani kusudi mabenki ya biashara yaweze kufanya biashara yaweze kupata wawekezaji, ili tuweze kuongeza mzunguko wa fedha nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; ningependa kuiomba Serikali miaka saba iliyopita Serikali ilikuwa inapitisha fedha zake kwenye mabenki ya biashara na zile fedha zilikuwa zinakaa pale muda mrefu, kwa hiyo kulikuwa na mzunguko mkubwa wa fedha na wananchi walikuwa wanaweza kukopa na hata riba zilikuwa zimepungua kwa sababu kulikuwa na fedha nyingi kwenye mabenki ya biashara. Je, Serikali haioni muda umefika sasa wa kufungua tena kwamba fedha zake ziwe zinakaa kwenye mabenki ya biashara kusudi wananchi waweze kukopa, mzunguko wa fedha uongezeke lakini pia na riba ziweze kushuka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. David Mathayo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupunguza idadi ya riba katika hati fungani ni swali la kisheria, lakini Serikali imelichukua na tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Dkt. Mathayo alileta ombi kwamba minada iwe inapungua mwenendo wake wa riba, basi nalo Serikali imelichukua na tutalifanyia kazi.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kunapokuwa na taa za barabarani kwanza kuna kuwa na usalama wa wasafiri lakini vile vile wananchi wanafanya shughuli zao za uchumi mpaka usiku kwa sababu kuna usalama.

Je, ni lini Miji ya Hedaru, Makanya, Mji mdogo wa Same, Njoro Kisiwani pamoja na Mwembe watawekewa taa za barabarani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa David Mathayo David, Mbunge wa Same, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miji aliyoitaja, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro ameshawasilisha maombi na tunategemea fedha itaenda mwaka huu ili miji hiyo iweze kuwekewa taa kwa ajili ya usalama lakini pia na kupendeza miji aliyoitaja, ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ningependa kujua mradi mkubwa wa maji tambarare ya Mwanga mpaka Same unakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Mathayo, Mbunge wa Same kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mradi huu ni mradi mkubwa, utekelezaji wake unaendelea, pamoja na changamoto zake, Wizara inaendelea kuona tunafanya kila linalowezekana mradi uweze kukamilika na lengo la matumizi haya kwa wananchi wa Same, Mwanga mpaka Korogwe yaweze kukamilika.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri zetu nchini zina mazingira tofauti. Kuna Halmashauri ambazo zina mazingira magumu sana kiasi ambacho walimu wanapoajiriwa wanaripoti halafu wanaenda kutafuta sababu za kuhama kwenda kwenye maeneo mengine kwa kutoa hata sababu za kusema wanaumwa ili waende maeneo ya mjini.

Mheshimiwa Spika, Je, Serikali inatoa motisha gani kwa walimu ambao wapo kwenye mazingira magumu kwa sababu watoto wetu wanapomaliza Kidato cha Nne na Darasa la Saba wanapata mitihani sawa na wale ambao wana walimu wa kutosha sasa tutaendelea kuwa na watoto ambao hawafaulu, wanafeli kwa sababu walimu wanakimbia mazingira magumu, tunaomba Serikali itueleze inandaa mazingira gani mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili Utumishi inachelewa kutoa vibali vya kuajiri walimu na hasa walimu wanapokuwa wamestaafu ama wanapofariki ama wanapoacha kazi kutokana na sababu mbalimbali. Je, ni lini Serikali italeta sheria ibadilishwe au Muswada tutengeneze sheria kwamba TAMISEMI iruhusiwe kuajiri walimu wa kuziba mapengo moja kwa moja badala ya kuomba vibali Utumishi kwa ajili ya kuziba mapengo ya walimu ili kuweza kuokoa elimu katika nchi yetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. David Mathayo Mbunge wa Same Magharibi.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kutoa pongezi zangu za dhati kabisa kwake yeye Mheshimiwa Mbunge Dkt. David Mathayo wa Same Magharibi kwa maana amekuwa akifuatilia sana maslahi ya Watumishi wa Umma hasa wale wa Jimboni kwake Same Magharibi.

Mheshimiwa Spika, sasa nikienda kwenye swali lake la kwanza la motisha kwa Watumishi wa Umma hasa walimu wale waliopo pembezoni. Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele sana cha kuona ni namna gani bora ya kuweza kutoa motisha kwa watumishi wanaoenda pembezoni kutoa huduma kwa Watanzania. Ndiyo maana hata jana nikiliarifu Bunge lako hili tukufu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ametoa maelekezo pale ofisini kwetu kwa watumishi housing cooperation kuweza kuhakikisha kwamba wanajenga nyumba pembezoni ambazo ni affordable kwa ajili ya watumishi hawa waweze kuweza kupata nyumba kwa gharama nafuu katika maeneo wanayofanyakazi lakini vilevile waweze kulipia kupitia mshahara wao.

Mheshimiwa Spika, ukiacha hilo huwa tunawaasa sana na kuwataka waajiri yaani halmashauri zetu nchini kuhakikisha wanatenga bajeti katika mapato yao ya kuweza kutoa motisha kwa watumishi hawa, hasa wale wapya ambao wanaenda kuripoti. Kuna baadhi ya Halmashauri nchini ambazo zimefanya hivyo wale wanaoripoti kazini wanapewa magodoro, wanapewa baiskeli na vifaa vingine vya kuweza kuwaongezea motisha ya kazi pale wanaporipoti.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili kuhusu ajira mbadala. Tatizo si Ofisi ya Rais, Utumishi. Tatizo linakuwa kwa ajili wenyewe kuto-focus mbele kujua wangapi wanastaafu katika kipindi cha mwaka wa fedha fulani, wangapi ambao wamefariki katika kipindi cha mwaka wa fedha fulani ili waweze kuomba vibali vile vya ajira mbadala kwa wakati. Kwa hiyo, unakuta mara nyingi wanasubiri mwaka wa fedha unapita wanasema kwamba ni utumishi iliyokwamisha vibali vile lakini unakuta hawavi-compile kwa wakati kuvipeleka TAMISEMI ili nao TAMISEMI waweze kuvileta katika Ofisi ya Rais, Utumishi kuweza kuvitoa.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi Ofisi ya Rais, Utumishi tunapopata maombi ya vibali vya ajira mbadala huwa Katibu Mkuu anavitoa palepale kwa sababu tayari mshahara wao upo, bajeti yao ipo lakini tunahitaji tupate maombi yale kwa wakati.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Kata ya Makanya katika Jimbo la Same Magharibi kimechakaa sana na ni cha zamani sana.

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Same ili kukarabati kituo cha afya cha Makanya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa David Mathayo Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Makanya ambacho amekitaja Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ya vituo ambavyo ni chakavu na Serikali inaendelea kuweka mpango mkakati wa kuvikarabati. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aamini kwamba Serikali imetambua hilo, tunaweka mpango endelevu wa kukarabati na kituo hiki kitapewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kero za Muungano zimechukua muda mrefu sana na sasa hivi tuko Awamu ya Sita lakini bado kuna kero na zingine mpya zinajitokeza. Ningependa kuuliza ni mambo gani ambayo yanakwamisha kukamilika kwa kero zote za Muungano?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Sheria Mama ni Katiba na katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania suala la uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi vimeorodheshwa kama masuala ya Muungano na jibu la Serikali linaonesha kwamba changamoto hii imemalizika. Je, suala hili kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano limefutwa kwa sheria gani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mbunge na Watanzania kwa ujumla kwamba suala la utatuzi wa changamoto za Muungano halijakwama wala halijasuasua, ni suala ambalo linakwenda kwa sababu mpaka hivi tunavyozungumza asilimia ya changamoto zilizotatuliwa ni nyingi tofauti na zilivyokuwa. Vile vile, katika orodha ya mambo yaliyotatuliwa yapo mengi, tulikuwa tuna changamoto nyingi, lakini sasa hivi kama atarejea kwenye jibu langu la msingi jumla ya changamoto 22 zimekwishatatuliwa. Zilizobakia ni changamoto ambazo Kamati zinazohusika ziko mbioni na zinakaa kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hizi na Muungano huu uendelee kudumu kama kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, ni kweli kwamba suala la utafutaji na uchimbaji wa gesi asilia lilikuwa ni changamoto, ilifika wakati lilikuwa Iina mvutano kidogo, lakini kwa sababu ya busara ya viongozi wetu wanaosimamia Muungano huu na Kamati zilizoundwa zikiwemo Kamati za Makatibu Wakuu, Kamati za Wataalam na Kamati zile za Mawaziri, zimefikia mahali pazuri katika kulitatua jambo hili, tena limetatuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zote na sasa hivi tayari Zanzibar iko vizuri na Muungano unakwenda vizuri katika suala hili la mafuta na gesi.(Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hii ni mara ya tatu kama siyo ya nne tunauliza swali hili tunaambiwa kwamba Serikali itatafuta fedha. Tunaomba kauli ya Serikali, ni lini fedha itapatikana? Hii ni ahadi ya Rais toka mwaka 2005 mpaka leo fedha za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina hazijapatikana? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Kata ya Mhezi, Mshewa na Msindo, barabara hii inaponyesha mvua kidogo inaharibika sana kiasi ambacho magari hayapiti kabisa. Kwa hiyo, mawasiliano yanafungwa kati ya Kata hizo na Same: Je, ni lini Serikali itaweka zege katika barabara hiyo kwa maeneo hayo niliyoyataja kabla ya upembuzi yakinifu na upembuzi wa kina kukamilika ili barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi, tunatambua umuhimu wa barabara hii na ndiyo maana katika jibu la msingi nimesema tunaendela kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri barabara hii mimi nimetembelea yote na tulishatoa maagizo na tayari tumeshaainisha maeneo yote korofi likiwemo eneo hilo la Msindo, Mshewa na Mhenzi. Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro ameshatengeneza bajeti na hivi ninavyoongea amesha-submit kwa Mtendaji Mkuu wa TANRIOAD ili aweze kutoa fedha kujenga hayo maeneo korofi ama kwa lami nyepesi ama kwa zege ili barabara hii iweze kupitika yote kwa mwaka mzima, ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, barabara za milimani zinapowekewa kifusi, mvua inavyonyesha kifusi kinazolewa kwa hiyo Serikali inapoteza fedha nyingi sana. Je, ni lini Serikali itaweka zege katika barabara ya Chome – Tae na Yavumali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara za milimani kwa kweli tukizijenga kwa kifusi mara nyingi baada ya msimu wa mvua barabara zinaharibika kabisa na hivyo thamani ya fedha inapotea na ndiyo maana Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tumefanya tathmini ya aina ya barabara kulingana na hali ya kijiografia ya maeneo husika ikiwemo Halmashauri ya Same, ambayo ina milima mingi.

Mheshimiwa Spika, moja ya solution ambayo tumeitafuta, ni kuanza kujenga barabara hizo kwa kutumia mawe. Kwa sababu mara nyingi maeneo yenye miinuko yana mawe pia, lakini pili kutumia zege. Kwa hiyo, kwa hizi barabara ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, naomba tuzichukue, tufanye tathmini, halafu tuone uwezekano wa kujenga kwa kiwango cha changarawe, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Napenda kujua kama ratiba ya kukamilisha mradi mkubwa wa maji kutoka Mwanga kwenda Same mpaka Korogwe imebaki pale pale mpaka mwaka kesho mwezi wa Nne wananchi wa Same wanapata maji kutoka Mwanga?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa sasa hivi wananchi wangu wa Same hawana maji: Serikali ina mpango gani wa dharura kuchimba visima virefu katika Kijiji cha Ishire, Kitongoji cha Kavambuhu, Majevu, Kirinjiko, Makanya pamoja na Mabilioni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza. Wizara tutafanya kila jitihada kuhakikisha mradi huu unakamilika ndani ya wakati kadiri tulivyosaini mkataba na mkandarasi.

Mheshimiwa Spika, kwa suala la dharura, maeneo yote yenye dharura kama Same Mjini na hasa maeneo haya aliyoyataja Mheshimiwa Mathayo, tutafanya kila jitihada kuona mashine ambazo Mheshimiwa Rais ametununulia tuweze kuondoa changamoto hii, basi tutakwenda kuchimba hivi visima. Lengo ni wananchi kupata huduma kwa wakati.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, Kata za Suji, Vudee na Mshewa ni Kata za kimkakati; je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Kata hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza kujenga vituo vya afya hivi vya kimkakati katika maeneo ambayo ameyataja. Nitoe wito na kusisitiza kwamba ni wajibu wa halmashauri kupitia Wakurugenzi na Mabaraza ya Madiwani kuanza kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kuanza ujenzi huu na Serikali Kuu itachangia kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, napenda kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo: -

Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Kata ya Vudee na Siji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya Mundee na Suji kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tuna vijiji zaidi ya hivyo ambavyo amevitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa mfano vijiji vya Gundusini, Mabilioni, Gavao, Saweni, Rwinndini, Ruvu, Jiungeni, Mferejini, Duma, Emugule na Endevesi vyote hivi havina umeme. Sasa Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari tutembelee vijiji hivi ili aone hali halisi kuliko kwamba zinawekwa nyumba mbili halafu tunaambiwa Kijiji kimewekewa umeme? Hilo halitakubalika.

Mheshimiwa Spika, la pili. Je, Serikali iko tayari kutoa kwa Wabunge orodha ya Wakandarasi wale wanaokwenda kuweka umeme katika maeneo yao ili nao waweze kufuatilia? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru Waheshimiwa Wabunge jana wametupitishia bajeti kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi na ahadi ambazo tumezitoa. Pia nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kuambatana naye kwenda jimboni kwake baada ya Bunge kuisha ili kuona vijiji hivyo ambavyo havijafikiwa na umeme. Kama tulivyosema viko tisa na ni kweli hata jana tumesoma kwenye bajeti, tunatambua kwamba sio wananchi wote na vitongoji vyote vimepata umeme, lakini jitihada na hatua zimeanza na tunaamini tutakamilisha. Ifikapo Desemba, 2023 hatutarajii kuwa na kijiji ambacho hakijafikiwa na miundombinu ya umeme.

Mheshimiwa Spika, katika eneo lingine, tuko tayari na tulishafanya hivyo na tutafanya tena kuhakikisha kila Mbunge anamfahamu Mkandarasi wake na scope yake na wale wanaosaidia katika usimamizi. Nikitoka hapa nitapitia kwa Mheshimiwa Mbunge nimpatie pia wale wa kwake wanaofanya kazi kwenye maeneo yake ili aweze kuwa na nafasi nzuri ya kufanya ufuatiliaji yeye mwenyewe.
MHE. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Same Magharibi, Kata za Milimani kuna shida sana ya mitandao. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kuziangalia Kata hizo za milimani vilevile, ziletewe huduma ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mathayo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Same Mashariki pamoja na Magharibi nilifanya ziara katika maeneo yote ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Ni kweli kuna changamoto lakini habari njema kwa wananchi wa Same ni kwamba, Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika Kata zaidi ya 12 katika Wilaya nzima ya Same. Kwa hiyo, naamini kwamba katika maeneo ambayo yatakuwa bado yana changamoto tutatuma wataalam wetu waende wakajiridhishe. Kama tutahitaji kuongeza nguvu ya minara iliyopo tutafanya hivyo, kama tutahitaji kuweka minara mipya basi tutafanya hivyo, lengo likiwa ni kutatua changamoto ya mawasiliano kwa wananchi. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo la Same Magharibi maeneo ya milimani hasa Kata za Msindo, Mshewa, Vudee, Tae, Suji, Chomi, Muhezi na Ruvu kuna shida kubwa sana ya Walimu na kwa sababu pengine mazingira magumu ya milima. Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa kutosha katika kata hizo za milimani na kuwapatia motisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itapeleka Walimu katika mgao huu wa hawa 13,130, Wilaya ya Same nayo itapata Walimu hawa kwenda kufanya kazi kule na tutaendelea kuajiri kadri ya bajeti itakavyoruhusu kwa ajili ya kuweza kupeleka Walimu kwenye maeneo yote yenye upungufu hapa nchini, ikiwemo kule kwa Dkt. Mathayo, Wilayani Same.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru sana Serikali kwa kuendelea kujenga vituo vya afya na vingine vile zamani kukarabatiwa lakini ningependa kujua ni lini Serikali sasa itapeleka vifaatiba vya kutosha katika Vituo vya Afya vya Hedaru, Kisiwani, Makanya, Ruvu na Shengena?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; zahanati nyingi katika Jimbo la Same Magharibi hususan katika Tarafa ya Mwembembaga, Chemesuji na Same, zahanati zimekamilika lakini hazina watumishi. Je, ni lini Serikali sasa itapeleka watumishi wa kutosha na waganga katika zahanati hizo ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Dkt. David Mathayo David.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu upatikanaji wa vifaatiba katika Jimbo la Same Magharibi. Niseme tu kwamba Serikali tayari imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika vituo vya afya vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same. Vilevile, shilingi milioni 100 kwa ajili ya zahanati zilizokuwepo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same katika Mwaka wa Fedha wa 2023/2024. Hivyo nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo tutaanza utekelezaji wa bajeti mpya kwenye mwaka wa fedha unaokuja, tutaweka kipaumbele hizi fedha ziweze kwenda haraka kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivi tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la zahanati hizi kukosa watumishi kule Halmashauri ya Wilaya ya Same. Serikali imeajiri watumishi wa afya zaidi ya 8,070 katika mwaka huu wa fedha ambao tupo na tunaenda kuumalizia. Tutaangalia ni wangapi ambao wamepangiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Same ili zahanati hizi nazo Mkurugenzi nae aweze kufanya allocation ya hawa watumishi wapya watakaokwenda kwenye zahanati alizozitaja Mheshimiwa Mathayo.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya milimani ya Vudee ni fupi sana, lakini kila mwaka Serikali inamwaga kifusi na mvua inaponyesha, basi inazolewa na maji: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kwamba tukimaliza Bunge twende Vudee milimani ili akaone barabara hii inayokwenda mpaka Ndolwa ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami au zege ili Serikali isipoteze fedha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubalina na Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo ya milimani kwa kweli yana changamoto kubwa. Kwanza nitoe maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro aitembelee hiyo barabara. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge twende tukaipitie, lakini twende wakati mtaalam ameshapita ili tuwe tayari tuna taarifa za awali kuhusu changamoto ambazo ziko kwenye hiyo barabara. Kwa hiyo nakubali, tutakwenda kuitembelea hiyo barabara, ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kufanya upembuzi yakinifu wa barabara ya milimani ya Mwembe – Mbaga – Mamba – Ndungu ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Je, barabara hii ya Mwembe – Mbaga ya milimani ni lini itatengewa fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakuwa shahidi barabara hii mimi tayari nimeshaitembelea na kuiona na kuona changamoto zake. Moja ya vitu ambavyo Serikali tunavifanya kwa nature ya barabara yake, tumemuagiza Meneja wa TANROADS hata kabla ya kuanza kufikiria kuijenga yote kwa kiwnago cha lami, aainishe maeneo yote korofi ambayo kipindi cha masika hayapitiki ili Serikali iweze kuyajenga na kuhakikisha kwamba mwaka wote barabara hii inapitika. Lakini taratibu zipo kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara yote aliyoitaja ya Mwamba – Miamba – Ndungu ili kufanya maandalizi kwa ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)

MHE. DKT. MATHAYO D. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Jimbo la Same Magharibi.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Hedaru na Kituo cha Afya cha Kisiwani, ni vituo ambavyo vinahudumia watu wengi sana lakini vina upungufu wa vifaa tiba. Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba Kituo cha Afya Hedaru na kile cha Kisiwani kinapata vifaa tiba vya kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mathayo David Mathayo, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi kama ifuatavyo: -

Katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwenye hospitali za halmashauri zilizokamilika na vituo vya afya vilivyokamilika vya awamu ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kama vituo hivi vipo awamu ya kwanza nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vitapata vifaa tiba lakini kama viko awamu ya pili na ya tatu basi vitapata awamu itakayofuata, ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza; ningemuomba Mheshimiwa Waziri pengine baada ya Bunge tuweze kutembelea katika skimu hizi ili tuweze kuziona zile ambazo kwa kweli ndizo zinazotakiwa zitengewe fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Spika, la pili, katika Kata ya Makanya kuna korongo ambalo wakati mvua inanyesha ndilo linategemewa sana katika umwagiliaji. Ningeomba Serikali, hasa Waziri tuweze kutembelea naye pamoja ili aweze kuliona hilo Korongo ili na lenyewe liwekwe katika mpango wa kufanyiwa upembuzi yakinifu ili wananchi wa Makanya waweze kupata chakula kwa mwaka mzima. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Dkt. David Mathayo David, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kutembelea skimu hizo kuziangalia na ukarabati ambao unahitajika. Vilevile kwa sababu nia yetu ni kuhakikisha hatupotezi maji, Kata ya Makanya kwenye eneo ambapo kuna korongo kubwa ambalo linatuamisha maji tutakwenda pia kuona. Lengo letu ni kuyatumia maji ipasavyo kwa ajili ya kilimo cha nchi yetu.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, jana Tarehe 06 Novemba, 2023 kulikuwa na tatizo kubwa la mtandao wa Vodacom. Shughuli nyingi za kutuma fedha zilikwama, mambo mengi yalikwama kabisa, mawasiliano hata kutuma miamala ya fedha kwenye benki na kwenye simu.

Je, Vodacom jana ilipatwa na changamoto gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Kata hizi ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja zimefikia hatua gani, katika utekelezaji wake, maana wameshazipitia tayari, zimefikia hatua gani ili wananchi wa Kata hizi za Ruvu, Msindo, Mshewa, Vudee, Mhezi na Suji waweze kupata mitandao ya simu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na kipengele cha kwanza ni kweli kabisa, jana kumekuwa na changamoto kupitia mtandao wa Vodacom, tunasema kwamba kulikuwa na technical hiccups. Technical hiccups maana yake kwamba, ilitokea katika network service ambapo iliathiri masuala ya kupiga, sms, pamoja na kutuma pesa kwa mtandao wa M-Pesa, lakini wenzetu wametoa taarifa wanaendelea kuifanyia kazi na leo tumeona kuna improvement, pia wateja ambao waliathirika ni Watanzania milioni 1.8. Kwa hiyo, tunaamini kwamba wanaendelea kulifanyia kazi na baadae watatupatia mrejesho wa hatua ambayo wameifikia na tunaamini kwamba hili tatizo litakuwa limeisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kata za Ruvu, Msindo, Mshewa, Vudee, Mhezi pamoja na Suji ukiachilia hili suala la Kata ya Tae ambayo tutaiingiza katika mpango wa utekelezaji wa minara mingine inayokuja, hizi Kata ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza naomba uniruhusu nitoe ufafanuzi kidogo hapa. Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla tumekuwa na maswali mengi sana kuhusiana na minara hii 758, tulichokifanya pale mwanzoni ni kubainisha Kata ambazo zina changamoto ya mawasiliano, lakini hatukubainisha maeneo ya kwenda kujenga minara hii. Kwa hiyo, tunachokifaya ni kuhakiksha kwamba tunaenda kubainisha maeneo sasa ambapo tunaenda kujenga minara na baada ya kufanya hivyo tunaenda kuhakikisha kwamba sasa tunaomba vibali. Wakati haya yote yanaendelea labda nikupe takwimu kidogo kwamba, mpaka sasa Airtel kati ya maeneo 188 mpaka sasa ameshaainisha maeneo 140 ambayo ni zaidi ya asilimia 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna TTCL yeye ameshamaliza maeneo yote pia ameshaingia mikataba na wahusika wa maeneo. Tigo kati ya maeneo 137 tayari maeneo 133 yameshakamilika. Halotel maeneo 22 yote ameshakamilisha kulingana na mkataba wake lakini Vodacom maeneo 133 kati ya 137. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba kuna hatua ambazo Waheshimiwa Wabunge hawatoziona kule zinatokea katika Majimbo yao ni kwa sababu kuna hatua ambazo ni za kiufundi na ni lazima tuzifuate na ni lazima zikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tunahitaji minara hii ijengwe kwa kasi, lakini ni lazima tuhakikishe kwamba, tunafuata utaratibu ambao hautakuja kuingiza Taifa katika janga la minara ambayo itajengwa halafu idondoke. Kwa hiyo ni lazima haya yafanyike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba, kampuni zote mpaka sasa zimeshaandika kuomba vibali na wakati wanaandika kuomba vibali bado wameagiza vifaa kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo, kuna hatua mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyika kuhakikisha kwamba minara hii itakapokuja kuanza kusimamishwa, nakuhakikishia kwamba inaweza ikasimama kwa pamoja na Watanzania, Waheshimiwa Wabunge, wote tutashangilia kazi kubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini kwa ndugu yangu wa Same, bahati nzuri yeye yuko katika minara ya Halotel ambapo wao kazi kubwa imeshafanyika, Halotel wameshaanza kujenga minara mitano. Katika minara hiyo mitano kuna mmoja ambao unajengwa katika Kata ya Mheshimiwa David Mathayo David. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza hapa. Kwanza, ningependa kujua katika maeneo haya ambayo yanafanya utafiti wa gesi na mafuta ni leseni ngapi zimetolewa kwa ajili ya uchimbaji wa gesi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, napenda kujua Serikali ina mkakati gani wa kuendelea kunadi vitalu hivi ili kupanua wigo wa uwekezaji na kuweza kuthibitisha zaidi kiasi cha rasilimali hizi ambazo tunazo nchini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hadi sasa kwa maeneo haya 84 ambayo tunafanya tafiti, tunazo jumla ya leseni 11 ambapo leseni nane ni za utafutaji na leseni tatu ni za uzalisahaji wa gesi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, kwa sasa hivi Wakala wa Udhibiti wa Mkondo wa Juu Wa Petroli (PURA) akishirikiana na Wizara tunao mkakati wa kuendelea kufanya maandalizi ya kunadi zabuni za vitalu kwa ajili ya kuleta wawekezaji zaidi ili kufanya tafiti na kuthibitisha rasilimali hii, ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza. swali la kwanza; tumekuwa na kampeni kwa miaka mingi iliyopita, kuelimisha na kuwezesha mtoto wa kike, tukasahau mtoto wa kiume. Sasa je, Serikali ina mikakati gani kuwapa upendeleo maalum watoto wa kiume ili waweze kupata elimu nzuri na kujiamini ili baadaye waweze kuoa wanawake waliosoma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kumekuwa na kuvunjika kwa ndoa, siku hizi ndoa zinavunjika sana na watu wanaachana sana kiasi ambacho kunakuwa na watoto ambao hawana wazazi wawili wa kuwalea. Je, Serikali ina mikakati gani katika kuelimisha, kutoa elimu kwa Watanzania hasa kuonesha majukumu ya akina mama na majukumu ya akina baba katika ndoa ili watoto hawa waweze kulelewa na wazazi wawili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Serikali kupitia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 inatoa haki sawa kwa watoto wote wa kike na wa kiume wakiwemo wenye ulemavu. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi kujenga madarasa katika kila mkoa kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata elimu na waweze kufikia malengo ambayo wamekusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023 inatambua umuhimu wa ushiriki wa wanawake na wanaume akiwemo mtoto wa kiume kama wakala muhimu wa kuleta mabadiliko na kuimarisha maendeleo ya familia nchini. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo wa kuweka zege kwenye barabara za milimani kwa sababu wanapoweka vifusi pindi mvua inaponyesha barabara zile zinazolewa na tunatia hasara Serikali na wananchi wanashindwa kupita, hata hivyo na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Barabara za Msanga – Chome – Ikokoa – Makanya – Tae – Suji na Barabara ya Kisiwani hadi Msindo zina maeneo makorofi mengi sana, je, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kutenga bajeti ya kutosha kusudi barabara hizi zitengenezwe kwa kiwango cha zege ili tuweze ku-save hela za Serikali zinazotokana kumwaga vifusi ambavyo vinazolewa na mvua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini yuko tayari kutembelea Jimbo hili na kuziona hizi Barabara za Chome, Barabara za Makanya – Tae pamoja na Kisiwani – Msindo ili aweze kuona umuhimu wa kutenga fedha za kutosha haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutetea wananchi wake. Kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ameuliza baadhi ya barabara Serikali ina mkakati gani wa kuzijenga kwa tabaka la zege na hasa kwenye maeneo korofi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Msanga – Chome – Ikokoa katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024 zimetengwa shilingi milioni 267.15 kwa ajili ya kujenga meta 100 kwa kiwango cha zege kwenye eneo korofi, lakini pia kwenye eneo hatarishi la Mlima wa Chome imejengwa strip concrete ya meta 350, lakini katika mwaka wa fedha ujao 2024/2025 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 74.9 kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha zege meta 180 kwenye eneo hatarishi la Mlima Ikokoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu Barabara ya Makanya – Tae – Suji Serikali imetenga katika mwaka wa fedha 2024/2025 milioni 161.18 kwa ajili ya kujenga kwa tabaka la zege urefu wa meta 100 kwenye eneo la Mgwasi – Tae, lakini pia ujenzi wa driffs nne za meta 32 na kwenye Barabara ya Kisiwani – Msindo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitumia shilingi milioni 250 kwa ajili ya kujenga meta 500 za strip concrete. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga kwa kiwango cha zege kwenye maeneo hatarishi, kwenye barabara zake hizi ili ziweze kupitika kipindi chote cha mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa mimi na yeye tutazungumza, tutapanga ratiba vizuri nipo tayari kutembelea Jimboni kwake kuangalia miundombinu hii ya barabara ili tuweze kuona umuhimu wa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuzikarabati na kuzijenga vizuri. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Mwaka huu 2024, Januari Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alikuja Same kushughulikia matatizo ya ardhi na mipaka katika Kata za Ruvu, Makanya na Bangalala na alituma wataalam wakaangalia matatizo yalivyo. Je, Mheshimiwa Waziri atarudi lini tena Same kwenye Kata za Bangalala, Makanya na Ruvu ili kushughulikia matatizo hayo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba tarehe 26 Januari, 2024 nilifika Wilaya ya Same kwenye Jimbo la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo. Kweli timu imeshakwenda na taarifa wameshaniwasilishia, na ninamwomba subira Mheshimiwa Dkt. David Mathayo, amekuwa akifuatilia kwa karibu sana, na pia nawaomba subira wananchi wa Jimbo la Same Magharibi, pindi nitakapomaliza bajeti yangu mwisho wa mwezi huu, Juni mwanzoni nitaongozana na Mheshimiwa Mathayo, tutaenda kutoa taarifa hiyo kwa wananchi, naomba wawe wavumilivu. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, mwaka 2023 Serikali iliahidi kuchimba visima 12 katika Jimbo la Same Magharibi kwenye Kata ya Ruvu, Station, Makanya, Mabilioni, Hedaru na Bangalala, lakini gari la Mkoa wa Kilimanjaro lilikuja likachimba visima viwili tu.

Je, hilo gari la Mkoa wa Kilimanjaro lililotolewa na Mama Samia Suluhu Hassan, litarudi lini Same ili kukamilisha visima 10 vilivyobaki ?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba Mheshimiwa Rais alitoa fedha kwa ajili ya kununua gari hizi. Shida iliyopo ni kwamba bajeti yake kidogo ilikuwa na changamoto. Sasa mwongozo umeshatolewa, kwamba magari haya yatarudi katika maeneo husika na kuendelea na uchimbaji wa visima vya maji ili wananchi wapate huduma ya maji. Ahsante sana.