Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka (8 total)

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nichukue nafasi hii kuwashukuru wachangiaji wote wa hoja hii tuliyoileta mbele yenu, Taarifa hii ya PAC, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote mliotoa maoni yenu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sijaambiwa napewa muda gani!
NAIBU SPIKA: Una nusu saa Mheshimiwa lakini ukitumia muda pungufu ya huo utakuwa umefanya vyema zaidi.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Muda niliopewa nusu saa na wachangiaji walikuwa zaidi ya thelathini, nikienda kwa kila mmoja, nadhani hatutamaliza leo, kwa hiyo, nitayaweka kwa mafungu kutokana na jinsi wachangiaji walivyochanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wachangiaji wote walitupongeza Kamati zetu zote mbili za PAC na LAAC, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wachangiaji wote niliowasikia wamekubali kwamba PAC bila kuwezeshwa hatutaweza kufanya kazi yetu kikamilifu. Kwanza kwa sababu tukifanya ripoti tu kama tunavyoletewa bila kuwa na muda wa kwenda kuhakiki tutakuwa hatuwatendei haki waliotutuma kazi hii.
Kwa hiyo, ni wazi kwamba PAC lazima tukiletewa taarifa tuweze pia kwenda kuhakiki. Kwa hiyo tunaomba kama Bunge lako likaridhia kama kweli PAC inahitaji kuongezewa pesa ili ziweze kufanya kazi yake kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, wachangiaji wengi walisema kwa msisitizo tena kwa masikitiko, kuhusu jicho letu Wabunge, CAG ambaye bajeti yake ni ndogo sana kiasi kwamba hawezi kwenda kutembelea ile miradi mbalimbali maana ukisema tu sisi tufanye kazi, PAC kazi zetu zinategemea CAG analeta nini. Kama CAG hawezi kwenda kufanya audit ina maana PAC hatuna kazi. Kwa hiyo tungeomba sana CAG bajeti yake iongezwe, vinginevyo tutajidanganya Wabunge hapa na kazi hazitakwenda. (Makofi)
Mifuko hii ya jamii imeongelewa sana kwa uchungu na wachangiaji, Waheshimiwa Wabunge mbalimbali na Waziri amejaribu kujibu. Hata hivyo, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri na kusema kwamba walikuwa wanahakiki wafanyakazi hewa na amesema PSPF wameshamaliza, swali langu ni kwamba kama wamemaliza kwa nini hawapeleki, hawarudishi yale madeni ya PSPF ili waendelee kulipa mafao ya wastaafu?
Wastaafu wengi wamelalamikia sana sehemu hii kwamba mafao yao hawalipwi. Wabunge wengi wanapigiwa simu, mimi mwenyewe napigiwa simu kutoka Jimboni kwangu. Kwa hiyo tungeomba, sana kama wamemaliza na wanaendelea na Mifuko mingine, basi angalau Mfuko huu wawape pesa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kuna sehemu nyingine ambazo zinahitaji msisitizo kidogo. Suala la Lugumi ni suala ambalo limetuletea matatizo sana kwenye Kamati, maswali yamekuwa mengi kabla hata haijaundwa Kamati Ndogo na bahati mbaya Kamati yetu hadidu ya rejea yetu ilikuwa inatufunga sana kwenda kuhakiki kama vile vyombo vilinunuliwa na kufungwa ndiyo tulitumwa hivyo.
Bahati mbaya hatukuwa na mkataba kwa hiyo hata kama tumekuta upungufu mengine hatuwezi kuyaingilia, lakini kibaya zaidi tulikuta vifaa vingi kweli vimelundikwa, havikufungwa sasa je, ni vya mradi huu au ni vya mradi mwingine ili tukipita vinaondolewa vinapelekwa kunakohusika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama vilinunuliwa kwa nini havikufungwa? Kwa nini kazi haikuanza? Miaka yote hiyo tangu 2011 mpaka leo miezi mitatu vifungwe? ndiyo kazi kubwa tuliyokuwa nayo. Kamati yetu wameshindwa kujibu maswali mengine tunayokutana nayo, ni sawa na mtu amefungwa miguu na mikono halafu anaambiwa kimbia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba, maswali ambayo bado Kamati ilijiuliza baada ya kupata ile Taarifa ya Afisa Masuhuli 28/10; ni je, vifaa vilivyoharibika kabla havijatumika ilikuwa ni wajibu wa nani avitengeneze ndipo vifungwe? Iweje Serikali inasema inasubiri ipate hela za bajeti za mwaka 2016/2017 ndipo ivitengeneze. Hilo ni jibu ambalo hatujalipata bado. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tulikuta vyumba ni vichafu sana, sehemu nyingi vilipowekwa hivi vyombo, je, lilikuwa ni jukumu la nani kutengeneza? Hatujui. Kwa hiyo Kamati yetu ilifanya kazi katika mazingira hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, samahani ninywe maji maana hili ni tatizo kubwa sana. Hili tatizo limeninyima usingizi, tunapigiwa simu kwamba ooh tumekatiwa chochote au tumetiwa mifukoni. Ninachotaka kusema Waheshimiwa Wabunge, kama kazi kubwa ya vifaa vile ilikuwa kuchukua picha za wahalifu pale kituoni, kuhifadhi taarifa, kwa nini hizo kazi kubwa mbili hazikufanyika miaka yote hiyo? Je, hivi vifaa vilikuwa vinafanya kazi kweli? Maana hii kazi ya kusema Mkongo wa Taifa ulikuwa haujafungwa ili kuwa na mawasiliano, hii ilikuwa stage ya mwisho, lakini ulitakiwa ukifika kituoni ukute picha, taarifa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili utusaidie sisi ambao si Wajumbe wa hiyo Kamati, haya maswali unayoyauliza saa hizi anayepaswa kujibu ni nani, kwa sababu maswali ya Wabunge wote hawa ni wewe Mwenyekiti ndiye unatoa ufafanuzi ndio waliyekuuliza. Sasa na wewe ukiuliza mimi sina majibu, mimi siyo mjumbe wa Kamati, kwa hiyo nataka kujua. Kwa sababu Serikali haitapewa tena nafasi tutaelekea kwenye mapendekezo mliyoleta kwenye hii ripoti yenu.
Kwa hiyo utusaidie vizuri ili baadaye Bunge hili litakapokuwa linafanya maamuzi kwenye yale mliyopendekeza humu liwe na taarifa za kutosha. Utusaidie tu hicho Mwenyekiti kwa sababu Bunge hili linawategemea ninyi. Sasa ukiuliza maswali na sisi hatuwezi tena kujijibu; inabidi utujibu wewe mwenyewe.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na nilikuwa nihitimishe hivyo, kwamba ndiyo maana tumesema! Umeniwahi tu. Ndiyo maana tumesema hatuwezi kutoa majibu yoyote hapa kwa taarifa tuliyoletewa tarehe 28 mwezi Oktoba; wakati tunafunga taarifa yetu mpaka tutakapoweza kuhakiki kama kiti chako kilivyotuambia kwamba, tuhakiki hivi vifaa kama vimefungwa.
Kwa hiyo, ndiyo maana nilitaka kwamba hii ajenda haijafungwa, huu mjadala haujafungwa, tutakwenda kipindi kinachofuata kuhakiki, kwa hiyo tutaweza kuleta taarifa kamili; hivyo ndivyo ilikuwa nihitimishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kulizungumzia ni suala la TIB. Labda niseme tu kwa ujumla kwamba majibu ya Mawaziri nimeyapata mengine yameniridhisha kiasi, maana kasema hizi hoja tutakutana nazo wakati CAG atakapopitia yatakuja. Hata hivyo, mahali ambapo bado pamenipa utata ni ukiangalia jibu ambalo alilitoa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kwamba kuna sheria ambayo inakataza mabenki kutoa taarifa za wateja wao.
Nikajiuliza kama hivi ndivyo, hivi hii taarifa ya TIB tuliletewa kwenye Kamati ili iweje? Imeletwa kwa minajili gani? Kupewa taarifa watu wamepewa hela, watu hawalipi, leo nahoji tujue zile kampuni ambazo zimepewa hela hizi, miaka hawalipi tunaambiwa hapana, hamuwezi kufanya hivyo, hawawezi kutoa siri za wateja. Hizi pesa kwanza ni za nani? TIB inawajibika kwa nani?
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema Spika amefanya makosa kutojua hiki kifungu kwa vile ameshawaandikia TIB kwamba watuletee hizo taarifa za yale mashirika sugu yanayodaiwa ambao hawajataka kuleta hizo taarifa tukaziona ili Bunge lako likatoa maagizo kwamba wachukuliwe hatua gani. Je…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, umemtaja Spika, hapo kwamba pengine hakukijua hicho kifungu; kifungu anakijua, maagizo aliyotoa haimaanishi ninyi mtaletewa hiyo taarifa moja kwa moja ndio utaratibu ambao tunautumia siku zote. Kwa hiyo si kwamba kifungu hakikujulikana ama hakukiona, anakifahamu kifungu na ametumia sheria nyingine kuitisha ile taarifa. Itakapomfikia yeye ataangalia namna bora ya kuileta kwenu kama ni taarifa ambayo inapasa kutolewa basi atawaletea. Kama ni ile ambayo haipaswi kutolewa basi hatoileta; tuendelee.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini naomba uniache kwa vile Kamati… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inaniwia ngumu kwa sababu kwa maelezo yako wewe ndio unatusaidia tufanye maamuzi na maamuzi lazima tufanye leo. Sasa nikisema nitapata muda wa kujibu baadaye sina na wewe ndio unayetusaidia ili tufanye maamuzi baadaye, Bunge zima hili linakutegemea wewe tu ndiyo mwenye hoja hii.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Sitaki kubishana na kiti, lakini nimeshapata taarifa, lakini pia nilikaa nikajiuliza ambalo labda litaingia huko. Hivi wateja sugu wanapotolewa kwenye magazeti kwamba hawalipi maana yake nini? Nafikiri Waheshimiwa Wabunge, hiyo hoja tuiache, tusubiri Spika atakapotuletea ile barua na majibu yake tutajua tufanye nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kuhusu suala la na SACCOS. Mheshimiwa Mhagama amelijibu, nafikiri alikuwa anawajibu wale Waheshimiwa Wabunge waliosema kwamba NSSF isitoe mikopo kwa SACCOS; amelijibu vizuri. Kamati yetu tatizo lake lilikuwa si hilo, Kamati yetu tumesema tatizo hapa ni kwamba NSSF imeweka utaratibu wake kwamba, mkopaji au atakayekopeshwa atumie vigezo hivi. Kwanza imeweka ceiling kwamba kukopa ni kuanzia minimum ni milioni 50, maximum ni bilioni moja. Pia wakasema collateral lazima ionekane kwamba iwe ni 50% ya ile amount unayotaka kukopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tatizo letu lilikuwa je, wale waliopewa zaidi ya bilioni moja mpaka bilioni mbili na laki tano, ni sawa sawa hiyo? Si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa wale ambao wamepewa mikopo ambao hesabu zao zilikuwa hazijakaguliwa, lakini wakapewa mikopo, tukasema si sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, tukasema wale ambao hawajarejesha mikopo ile, maana pesa hizi ni za kulipa mafao ya wastaafu, hivyo si sahihi na ndiyo maana sisi tumesema, tunaomba CAG aende akahakiki akafanye ile kazi ili atuletee taarifa kamili. Nani wamelipa na nani hawajalipa, nani wamefanya kinyume ili iletwe katika Bunge lako au katika Kamati tuweze kuleta katika Bunge ili lichukuliwe hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ya kuzungumza ni mengi nimerukia kwa Manaibu, ndiyo nilikuwa nakwenda nikiangalia hizi responses zilizotoka kwa wenzangu mbalimbali ambao wamechangia. Sasa naweza nikarudi nyuma kidogo kuzungumzia mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema; ili kwamba hata muda ukiisha tutakuwa angalau zile important areas tumezipitia.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengine wamezungumzia kuhusu tatizo la bandarini kuhusu zile meli, kweli wamesema kama sisi tulivyosema kwamba inakuwaje meli iingie mpaka itoke miezi 18 taarifa zake hazijajulikana, hawajalipa. Hilo limezungumzwa na sisi tuliliweka katika taarifa yetu. Kwa hiyo tumesema kwamba bandari yetu inatakiwa iangaliwe kwa ukaribu sana ili iweze kufanya kazi zake kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la TRA na misamaha ile ya kodi, pia tumeleta katika Bunge lako ili ijulikane kwamba TRA wapewe maagizo ili wafanye kazi zao. Kuhusu ile misamaha hewa watuambie wale ambao wana misamaha hewa wamechukuliwa hatua gani? Ndiyo maana tumeleta hilo ili nalo kama Kamati yetu ilivyopendekeza tupewe majibu kwamba wamechukuliwa hatua gani kwenye misamaha ile ambayo hawakukidhi, wengine ni misamaha hewa, ifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine kwa kweli in general yamezungumzwa sana hayo ya kuhusu TR na kuelezea jinsi ambavyo Kamati yetu imependekeza kwamba TR awezeshwe ili na yeye aweze kufanya kazi yake vizuri. Tunampongeza sana kwa kweli ameisaidia sana Kamati yetu na hivyo tunaamini kwamba atakavyozidi kupewa nguvu ataweza kuendelea kufanya kazi nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu haya Mashirika yetu ya EWURA, SUMATRA kwa kweli tumesisitiza na Waheshimiwa Wabunge wameliongelea kwamba zile tozo wanazoleta kule Serikalini hazikubaliki, kwamba wapunguze administrative expenses zao ili waweze kutoa tozo linalokubalika Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengine samahani kidogo mnisamehe, maana yameingiliana na ya wenzetu, ya LAAC lakini at the end of the day tunakubali kwamba, pesa za maendeleo kwa kweli Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni vizuri ziende kama zinavyopitishwa na Bunge, otherwise nchi yetu tutapiga kelele hapa, lakini hatutapiga hatua, zipelekwe kwa wakati. Ili zile bajeti zinazopitishwa hapa zihakikishwe kwamba zinafika kule zinakotakiwa ziende.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Kilimo amejitahidi sana kuelezea aliyoyaelezea na kuhusu ile ya wafanyakazi kwamba wanaangalia sababu nyingine na kwamba hawakusimamishwa tu kutokana na yale mahindi mabovu, kwa hiyo, tunajua kwamba tutapata taarifa kamili katika ukaguzi ujao ili tuweze kujua hatma yao imekuwa ni nini. Hayo maghala aliyoahidi naamini yatajengwa ili yafanye kazi vizuri na nguvu ya wakulima isipotee bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri nimejitahidi ku-cover maeneo mbalimbali na naamini kwamba eneo kubwa la hii taarifa yetu masuala yake yalikuwa yamewekwa katika mafungu hayo niliyoyataja ndiyo maana nimeya-sum up.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kwamba Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kukubali taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali pamoja na mapendekezo yaliyomo katika taarifa hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii maana nimeona mara nyingi hata nikileta maombi ya kuchangia sichaguliwi, lakini leo umenichagua ninakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kusema kwamba, kutokana na tamko la Kiongozi wetu wa Kambi ya Upinzani kuhusu uvunjaji wa Katiba ambao unawanyima wananchi wetu kufuatilia haya yanayotendeka hapa Bungeni ningeomba nisubiri mpaka tupate ufumbuzi wa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jina naitwa Naghenjwa au wale waliozoea wananiita Naghe Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupatiwa nafasi hii kutoa mawazo au maoni yangu machache kutokana na hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Kwanza kabisa niseme kwamba Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi tunamfurahia kwa approach yake ya kwanza aliyoifanya alipokutanisha wafugaji wa Wilaya ya Same na Jimbo la Mlalo na wa kutoka sehemu zingine za Mkoa wa Tanga, akakaa na wafugaji, akaongea nao vizuri takribani wiki tatu, nne zilizopita. Amevunja rekodi na wafugaji wale walifurahi sana kwa mara ya kwanza kuweza kukutana na Waziri na kueleza matatizo yao na Waziri akawasikiliza na akaahidi kufuatilia na kuwapa ushirikiano mkubwa. Sioni kama kuna ubaya wa kumsifu mtu ambaye amefanya kitu kizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi nataka tu niseme machache maana mengi yamesemwa katika Kambi ya Upinzani ambayo yalikuwa katika yale niliyotaka niyaulizie. Kwa uchache huo ninalotaka kuuliza ni kwamba naomba Waziri ajaribu kunieleza kwa vile Serikali yetu inaangalia kukuza viwanda na ninaamini kwamba sustainability ya viwanda inatokana na malighafi ya ndani ya nchi. Je, kumekuwa na mawasiliano na Wizara ya Viwanda kuona jinsi ambavyo viwanda vile vitakavyotumia malighafi, yale maeneo yatakayotoa malighafi wale wakulima wanasaidiwa ili kuwe na mikataba maalum ya kuonyesha kwamba watatoa mazao yatakayoweza kufaa katika viwanda vile ili viwanda vyetu viweze kuboreshwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza hivyo kwa mfano, nikianza na viwanda vya ngozi, kwanza tunaona kiwanda kile cha Kawe kilikufa hatujui kama kuna mpango wa kukifufua ama vipi lakini wafugaji wameshaandaliwa ili waweze kufuga ng‟ombe wazuri watakaotoa ngozi nzuri itakayotumika katika viwanda vyetu? Maana kama hakuna uwiano au mahusiano ya kupanga mikakati kati ya Wizara hii na Wizara ya Viwanda sioni jinsi ambavyo viwanda vyetu vitafanikiwa kama Wizara ya Kilimo na Mifugo haikufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika upande wa mazao yale kama pamba, kama tunataka kuanzisha viwanda vya nguo, je, wakulima wa pamba wameangaliwa jinsi ya kusaidiwa kwanza kulima, kuhifadhi na kusafirisha mazao yale kwenda kwenye viwanda? Tumeshuhudia viwanda vya Mwatex, Kilitex, Urafiki vyote vikifa au vikisuasua na sasa tunataka kuanzisha viwanda ambavyo sijui kama vinaangalia hayo yote. Maana wenzangu wachumi watanisahihisha kwamba lazima tuwe na backward na forward linkages otherwise kila Wizara ikifanya kitu chake parallel hakika lengo hili halitafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, for example nimeona Kambi Rasmi wakitoa maelezo kwamba ukame umeathiri upatikanaji wa mazao kipindi kilichopita. Je, Wizara ya Maji inahusishwa katika sehemu ile itakayowekwa viwanda ili maji yapelekwe kwenye zile malighafi tusitegemee kilimo cha mvua? Wenzetu wa Israel wanatumia sana teknolojia ya drip ambayo inatumia maji kidogo sana lakini inahakikisha mazao yao yanakuwa bora sana. Je, Wizara ya Kilimo ina mpango wa kuongea na Wizara ya Maji ili wawekewe maji kule ambako wanataka kuboresha mazao yale ili system ya drip angalau ifanyiwe utafiti na sample kama kutengeneza model ya shamba ambalo linatumia drip na kuona wale ambao hawatumii system hii na wale wanaotumia nani ambao wanapata mazao zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa kwamba Wizara hii ni nyeti na kubwa sana ambapo Watanzania wengi wanaitegemea. Tunaamini kwamba hata wale wanaojiita mabaunsa bila chakula hawawezi kuwa mabaunsa, kwa maana hiyo njaa haina baunsa. Kwa hiyo, naamini kwamba Wizara hii itaongezewa fedha ili kusudi iweze kufanya vizuri na itatoa mchango mkubwa ambao utakuwa input katika Wizara zetu nyingine kama zile za Afya na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kwamba muda si rafiki, napenda tu nijue kuhusu kiwanda cha tangawizi kule kwenye Jimbo letu la Same Mashariki ambacho kimekuwa hakianzi kufanya kazi pamoja na Rais wa Awamu iliyopita kwenda kukifungua mwaka 2012. Matokeo yake wakulima wengi wa tangawizi ambao waliongeza sana kilimo cha tangawizi wamepata hasara kubwa sana na kule sasa hivi tuna makaburi mengi ya tangawizi kuliko ya wananchi waliofariki kutokana na kwamba wakulima hawakuwa na jinsi bali kuzika zile tangawizi zao. Sasa tunapowaeleza wakulima waongeze kilimo wakati hatujui jinsi ambavyo viwanda vyetu vitawahudumia hatuoni ni kuwasumbua wakulima bure?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri, ana habari kwamba Rais wa Kenya ameruhusu kilimo cha mirungi na kutenga dola za Kimarekani milioni mbili ili kilimo hiki kikuzwe. Tukizingatia kwamba tuko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, je, pamoja na kwamba sisi tumezuia kilimo hiki tunahakikishaje mirungi hii haitaingia kwetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri ni vizuri Waziri wa Kilimo akawasiliana na wenzake Kenya kuona kwa nini wao wameruhusu zao hili. Naamini kwa vile wamejua lina faida sana na ni rahisi kuzuia madhara kama ukiruhusu zao hili kuliko ukilikataza halafu watu walime kwa kificho, watalitumia vibaya zaidi. Tuna mfano wa nchi ya Holland waliidhinisha maduka fulani kuuza dawa hizi za kulevya kwa kuamini kwamba wale watumiaji watatumia kidogo kidogo kuliko wakificha halafu watumie kwa wingi kwa wakati mmoja madhara yake yanakuwa makubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme hivi, namshukuru Waziri wetu kwa mikakati hii mizuri lakini pia azingatie maoni ya upinzani maana yatamsaidia kuboresha kilimo, ufugaji na uvuvi ambao ni tegemeo kubwa sana la nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia nijue, je, Waziri wetu wa Kilimo ana mahusiano gani kupitia labda Wizara ya Viwanda na hili Shirika letu la World Trade Organisation kuona kwamba na sisi masoko yetu yanafiki katika kiwango kizuri cha juu na tukapata upanuzi wa masoko nchi za nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nisisitizie upande wa uvuvi, hizi neti ambazo ni ndogo na zinaharibiwa kila wakati, kwa nini ziruhusiwe kuwa nchini kama zinaleta madhara makubwa? Nafikiri Wizara waangalie na kuona kwamba neti hizi zisiruhusiwe ili tusitie wavuvi wetu hasara ya kuwachomea neti walizozinunua kwa gharama kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri Kivuli kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mimi naomba nizamie katika diplomasia ya kiuchumi. Naona nchi yetu tumeongelea hili tangu 2001 mpaka leo na inaelekea hata Mabalozi wetu hawajui katika diplomasia kiuchumi wanatakiwa wafanye nini. Tunaongea juu juu tu hatuzamii kusema diplomasia ya kiuchumi maana yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Waziri ni mwanadiplomasia sana lakini nasikitika kusema hotuba yake yote au sehemu kubwa imeenda katika mambo ya kisiasa kwa maana na diplomasia ya kiisiasa. Kwanza tuanzie karibu hapa nyumbani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, inasikitisha sana kuona Wabunge wetu wa Afrika Mashariki hawajui wanaripoti kwa nani au wako chini ya nani? Je wako chini ya Bunge hili au wako chini ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi hawana hata ofisi. Sasa unampaje mtu jukumu kubwa kuitwa Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini hana hata Ofisi nyumbani kwake. Nchi ndogo kama Burundi wana ofisi za Wabunge wao wa Afrika Mashariki hata Rwanda na Kenya lakini Tanzania hatuna. Hii inaonesha jinsi Tanzania ambavyo tunachukulia mambo yetu kwa urahisi rahisi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu tuangalie, angalia shilingi yetu ya Tanzania na shilingi ya Kenya. Mpaka jana shilingi yetu ishirini na mbili ya Tanzania ndiyo unapata shilingi moja ya Kenya. Hivi wenzetu wametuzidi nini na tunazungumzia diplomasia ya kiuchumi. Mabalozi wetu wa East Africa wanajifunza nini au wanatuambia kwa nini wenzetu Kenya wanapiga hatua? Wakenya wako mbali sana angalia supermarket tu hata iliyoko Dar es Salaam, Mkenya ndiyo anaiendesha hata Kenya Commercial Bank, Tanzania Kenya tuna nini, Uganda tuna nini na Rwanda tuna nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ninachoshangaa kama tunazungumzia mambo ya diplomasia kiuchumi, nakumbuka Awamu ya Pili kule Saudia walieleza kwamba wanataka mbuzi wengi kwa vile watu wakienda Hija wanatumia sana nyama ya mbuzi. Watu wakaja hapa (Waarabu), Ubalozi wetu sijui ulifanya kazi yoyote kufuatilia suala lile lakini foreign officers wakapigapiga ikaishia hapo. Sasa hivi wenzetu wa Comoro ndiyo wanapeleka Uarabuni ng‟ombe na mbuzi kutoka Tanzania. Tunaongelea diplomasia ya kiuchumi, uko wapi uchumi wetu tunaouzungumzia hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie wawekezaji, wanakuja wawekezaji sijui Foreign Ministry yetu inasaidiaje kuonyesha hawa wawekezaji kule kwao wana uwezo kiasi gani ili waweze kutushauri kwamba hao muwakubali kama wawekezaji au msiwakubali? Unakuta wawekezaji wengine wanakuja kukopa kwenye benki zetu hizi hizi, halafu unaambiwa ni mwekezaji huyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi angalieni migodi yetu wageni kutoka nje wametawala migodi yetu Watanzania tunabakia kufanya kazi za vibarua. Wizara yetu ingeshauri kwamba hawa wawekezaji labda tuwape position moja, mbili hizi nyingine zote zibanwe na Watanzania. Watanzania mali yetu (contribution) yetu iwe ardhi yetu na wale wawekezaji waje na hela ili tuwe equal partners. Leo tunaongelea uchumi wa kidiplomasia lakini migodi yetu watu wetu ni kupigwa risasi kila siku na wageni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalieni hoteli zetu mfano Hoteli ya Serena na iliyokuwa inaitwa Kilimanjaro sijui sasa hivi imeshabadilishwa jina au bado.
Haya Hyatt. Hawa wenzetu wanapewa grace period kwamba msilipe kodi muangalie kwanza biashara, miaka mitano wakimaliza wanabadilisha jina leo Sheraton, kesho Serena sijui keshokutwa wataitwa nani? Tumekaa kimya, hiyo diplomasia kweli ya uchumi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie wawekezaji wanapewa umiliki wa mashamba kwa muda wa miaka 99, mwananchi sisi mpaka na watoto wetu hamna atakayekaa kushuhudia mkataba umeisha, tunawapa wawekezaji. Huko nchi za nje, je, kuna Mtanzania anakwenda apewe ardhi miaka 99? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa kwamba tumejivunia tunaletewa msaada wa pikipiki na Wachina, jamani juzi sijui miaka kumi iliyopita tuliletewa baiskeli wanakuja ku-assemble pikipiki kiwanda chetu cha jeshi pale Nyumbu ambacho kilikuwa kinatengeneza magari pale Kibaha, kingeombewa hela wangekuwa mbali siye tunarudi kwenye pikipiki. Pikipiki zitabeba mizigo gani, ndiyo diplomasia ya uwekezaji huo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu vyuo vya ufundi, tumeenda kuomba hela, wakati nafanya Danish Embassy tulitengeneza Chuo cha Chang‟ombe na Dodoma kwa grant leo tunaenda kuomba mikopo kurudi tena kutafuta technical assistance kutoka nje. Tunajivunia Italia wanatusaidia, hivi Engineers wetu wote kutoka chuo kikuu kutoka iliyokuwa technical college wameshindwa kusaidia kutengeneza VETA kweli mpaka twende tukaombe huko Italia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba USD milioni 55 kujenga maghala, maghala mangapi tunayo yamewekwa uchafu hayawekwi hata mazao? Leo tunaomba USD milioni 55 msaada wa kujenga maghala, hivi kweli hata kujenga maghala jamani tushindwe nchi hii? Wenzetu wanatengeneza ndege wako mbali sisi bado tunatafuta msaada wa kujenga maghala? Hii diplomasia ya kwamba tuna marafiki siyo urafiki siye ni ombaomba, hakuna urafiki na ombaomba. Ukiwa na rafiki kila siku yuko mlangoni kwako anaomba utasema huyo ni rafiki yangu siyo rafiki. Tumekuwa nchi ya ombaomba hata vile vitu tunavyoweza kutengeneza wenyewe, inatuaibisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Mengi yameshasemwa, lakini napenda ni-concentrate katika mambo mawili au matatu. La kwanza, nilikuwa naangalia ripoti hii ya wenzetu, ni nzuri sana, Kamati inawapa pongezi mmeiweka ripoti vizuri. Nilipokuwa napitia ukurasa wa 42 kuhusu ukuaji wa Sekta ya Kilimo na kwamba asilimia 70 ya nchi yetu wananchi wetu wanategemea kilimo na kwamba sekta hii ndiyo inaweza kuondoa umaskini hasa vijijini na kweli vijijini ndio kwenye hii asilimia kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaanza kujiuliza, hii slogan ya Kilimo Kwanza tumeisikia muda mrefu sana, slogan hii sikuona ikiwekewa mikakati ya jinsi ambavyo ingeweza kutekelezwa. Nilikuwa nikipitia, nikiangalia jinsi ambavyo Kilimo Kwanza kingetekelezwa wakati kila sekta inafanya bajeti yake, Sekta ya Maji imegeukia kulia, Sekta ya Kilimo imegeukia kushoto na sisi tunaongelea Kilimo Kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama priority ilikuwa katika umwagiliaji, kwa akili ya kawaida ungetegemea hizi sekta mbili ziweze kufanya assessment, ni maeneo gani basi tunakwenda kuyaboresha, je, tunakwenda kwenye Bonde la Rufiji, kulikojaa maji, yale maji tunayatoaje pale? Ili bonde lile liweze kuilisha Tanzania na nchi za jirani, hilo hulioni. Hiyo slogan imekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuja slogan ya viwanda nayo naiangalia, hivi priority ya viwanda vyetu ni ipi, tunaangalia vyuma au tunaangalia kilimo ambacho tunajua kwanza ndiyo uti wa mgongo ili tuwe na ile backward and forward linkage tuweze kuoanisha kwamba kama basi tunataka viwanda priority yetu iko kwenye moja, mbili, tatu. Kwa hiyo, wakulima wetu wawezeshwe katika kilimo hiki na pesa nyingi iwekwe hapo, hasa katika umwagiliaji na ninyi muangalie ili tusitegemee mvua, huvioni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza hivi viwanda navyo vitakuwa kama Kilimo Kwanza, nchi yetu kwenda kwa slogans tu? Kama tunakwenda kwa slogans hivi tunamdanganya nani. Ningetegemea basi hata Wizara hii ya Fedha na Mipango waite hizi sekta Ministries wakae pamoja wawe focused, waangalie kwamba tunaomba pesa nyingi iwekwe katika sekta hizi mbili, tatu, ili tuweze kupata azma tuweze kufikia lengo letu la viwanda, kinyume cha hapo hii slogan nayo itapita kama ilivyopita ya Kilimo Kwanza. I am sure ukiangalia unaona kilimo kimewekwa pembeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Kamati wametuwekea vizuri sana kwamba hii sekta itategemea umwagiliaji, sasa kama umwagiliaji Wizara ya Maji na Umwagiliaji wameweka mikakati ya kufanya sensa kwamba ni sehemu gani kuna maji mengi yanayoweza kutumika kwa umwagiliaji ili iweze ku-demarcate yale maeneo kwamba yatamwagiliwa na kwa malengo gani, kwamba tuta-produce kiasi gani? Nilishangaa wakati mmoja, nafikiri ilikuwa mwaka jana, Waziri wa Kilimo alivyozungumza, alipokuwa Soko la Kibaigwa kwamba ameshangaa mazao yamekuwa mengi sana na storage hamna, kwa hiyo yapo nje yananyeshewa yanaharibika, Waziri wa Kilimo anashangaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tunasema tuna upungufu wa chakula, kwa kweli ukiangalia ni utani, ingekuwa hizi Wizara zinaendeshwa na Wapare na Wachaga ningesema hawa ni watani wa jadi, lakini unaona watu tuko serious, tunakaa hapa Waziri anasema ameshangaa mavuno ni mengi hamna pa kuweka, hii inaniambia kwamba hatufanyi kazi kwa kuweka malengo au malengo yetu tunaweka madogo sana, hatuwi realistic, hatutumii wataalam wetu kufanya projections, matokeo yake tunashangaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachonishangaza zaidi, wakulima na wafugaji wote wako chini ya Wizara moja na kila siku kuna vita kati ya wakulima na wafugaji. Hivi hiki Kilimo Kwanza ambacho sasa Kamati hii inatilia mkazo kitakuwaje kama mtu amelima kesho ukiamka wanyama wameingia wamekula mazao yako yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaangalia Wizara moja mmeshindwa kuja na mikakati ya kuona mifugo yetu itunzweje, kilimo chetu kitunzweje. Bado wafugaji wetu ni wale wa kuswaga, zile artificial insemination centers zimekufa wakati ukiangalia hizi Sekta za Kilimo, Ufugaji na Utalii zingeweza kutoa nchi hii katika umasikini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaambiwa tuna ng‟ombe wengi, viangalie ving‟ombe vyetu vilivyokondeana, uliza anatoa lita ngapi per day, tunaringa katika Afrika Tanzania ni ya pili ikifuatiwa na Ethiopia, yet miaka yote hii hatuna mikakati. Unamwambia mfugaji punguza mifugo humpi target, huyu anafuga 2,000, huyu 10,000, huyu 500, huyu 200, unamwambia apunguze, apunguze kutoka wapi kwenda wapi, akipunguza anapeleka wapi, kama anamuuzia Mheshimiwa Profesa Maghembe ni palepale si ndiyo, mifugo inatoka hapa inakwenda pale, hatuna viwanda vya nyama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anapunguza anapeleka wapi, unatoa mzigo kichwani unaweka begani ndiyo kupunguza huko? Kibaya zaidi humpi alternative, unaboreshaje ng‟ombe wako, tuwe na shamba darasa weka ng‟ombe kumi tukuonyeshe jinsi ya kuwaboresha vis-a-vis ng‟ombe wako 1,000, mfugaji ataweza kuelewa. Hufanyi hivyo unamwambia punguza, amuuzie nani, kiwanda kiko wapi?
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Sasa nasema kwa kweli kama nchi yetu inge-concentrate Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anapunguza anapeleka wapi, unatoa mzigo kichwani unaweka begani ndiyo kupunguza huko? Kibaya zaidi humpi alternative, unaboreshaje ng‟ombe wako, tuwe na shamba darasa weka ng‟ombe kumi tukuonyeshe jinsi ya kuwaboresha vis-a-vis ng‟ombe wako 1,000, mfugaji ataweza kuelewa. Hufanyi hivyo unamwambia punguza, amuuzie nani, kiwanda kiko wapi?
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Sasa nasema kwa kweli kama nchi yetu inge-concentrate na kilimo tungekwenda mbali sana. Ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiaw Mwenyekiti, kwanza niwapongeze wenzetu wa Kamati zote kwa kazi nzuri walizofanya. Najua ukiwa wa mwisho itakuwa point zako nyingi zimechukuliwa lakini nimebaki na chache ili nisirudie rudie zile ambazo wenzetu wamezisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa tu nataka ni-observe mambo mawili, kwamba katika nchi yetu nafikiri tunatakiwa tuongeze uzalendo zaidi maana naona kwamba kila wakati tunasema tukaangalie wawekezaji kutoka huko nje. Hatuweki misingi ya kusema tujenge uwezo wa watu wetu wa ndani. Kama wenzangu waliotangulia waliosema Wachina, nakumbuka hata kile kisiwa cha Hong Kong wakati wazungu wale wa Uingereza wakitakiwa waondoke, 10 years before, waliwawezesha watu wao wawe na mitaji mikubwa waweze kuwekeza kwenye vie viwanda vikubwa na wawe board members ili waweze kujifunza na kupata uzoefu, ndiyo maana wenzetu mpaka leo China wamekwenda mbele sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwetu tunajua kwamba kuna aliyesema 50 percent ya mafuta yanaingizwa kutoka nje, infact ni 70 percent ya mafuta ya kula wakati alizeti zinalimwa sana na infact tungeongeza pressure au misaada kwa wakulima wetu wa zile alizeti tungehakikisha kwamba hatu-import mafuta ya kula. Wenzetu kutoka Kenya wanakuja kuchukua vitunguu hapo Singida wanavi-re-export, sisi tunabaki tunaangalia wakati vitunguu vinatoka kwetu. Tunadharau vitu vidogo vidogo, lakini tungeangalia bottom up tungejikuta tunasaidia wakulima zaidi as a result tukaboresha na umaskini tukauondoa katika level ile ya chini kwa kuweza kuunganisha viwanda vyetu na malighafi kutoka kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tunaangalia institutions zetu, tuna TEMDO, CARMATEC, CBE, Dar Tech, Arusha Technical; wote hawa wanafanya kazi ambazo wangewekwa pamoja, wakasaidiwa, wangeweza ku-invent vitu vizuri na ushauri mzuri kwamba tu-invest kwenye nini na waweze kuweka utaalam wao pale. Hivi vyote vimewekwa pembeni tunaangalia watu wa nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabalozi wetu wametumwa nje, wanaambiwa muangaie wawekezaji, samahani sikumbuki labda imesemwa hiyo; lakini ningetegema nchi iwe ime-identify ni mazao gani tunaweza ku-export ili kila Balozi anayekwenda nchi fulani tumwambie atuangalilie soko la kitu hiki na kile na kile. For example, vitu vinavyolimwa Tanzania ambavyo tunaweza kupeleka nje ni vitu kama nini? Tunaweza kusema ni mzaha mzaha lakini tangawizi ambayo tunaweza kuiboresha, ni nchi yetu ina-produce tangawizi the best katika Afrika, lakini hivyo vyote hatuviangalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaangalia maziwa tuna-import mengi, kwa nini hatuboreshi viwanda vyetu watu wakasaidiwa, wafugaji wakazalisha maziwa kuliko ku-import maziwa, viwanda vile vikakuzwa. Unaona kuna ASAS Iringa, kuna kiwanda cha maziwa cha Tanga hatutaki kuviboresha badala yake tuna-import maziwa ya unga, yanakuwa imported sijui madawa gani kutoka South America yanakuwa packed, tunapata maziwa ya hovyo hovyo. Sasa kuna mambo mengi sana, kwamba bado uzalendo wetu haupo kuangalia kwamba tukuze from the bottom up halafu tuwe na inward looking badala ya kila siku tunasema kalete wawekezaji, wawekezaji ambao wakija wanatunyanyasa. Tunajua kuna viwanda watu wamewaweka huko hawajui hata Kiswahili sasa ndiyo tunayoyataka hayo. Mimi nafikiri ifike high time ambayo tutaweza kuangalia kwamba tunasaidiaje watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie suala la mitaji, banks zinaweka riba kubwa sana kwa nini tusiwe na strategic plan ya kuona kwamba tuna-identify viwanda gani ambavyo tuwaboreshe watu wetu na tuwape…….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Na mimi niungane na wenzangu kutoa pole sana kwa wafiwa wote waliofiwa na watoto wetu wale waliofariki kule Arusha kwa ile ajali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nielekeze mchango wangu katika upande wa umwagiliaji maana najua hapa ndio kwenye maisha yetu Watanzania wote. Ukiangalia tafiti ambazo zimefanyika za REPOA na ESRF zote zimeonesha kwamba, Tanzania kama tunataka kutoka katika umaskini lazima msisitizo uwe katika kilimo cha umwagiliaji, kama hatukuweka msisitizo katika kilimo cha umwagiliaji hata tukitengeneza barabara kiasi gani tutakuwa tunajidanganya, maana nchi ambayo haiwezi kujilisha haina heshima yoyote hapa duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata Jarida la Economist la 2012 linatueleza jinsi ambavyo Tanzania ni nchi ya kumi na moja duniani ya kuwa na maji mengi ambayo ni maji yale tunasema maji ya baridi au maji ambayo hayana chumvi. Ukiangalia Ziwa Tanganyika peke yake lina asilimia 17 ya maji yote masafi katika ulimwengu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiweka na Mito ya Pangani, Rufiji na Maziwa mengine tuliyonayo hakika utajua kwamba Tanzania tuna utajiri mkubwa sana wa maji. Licha ya maji tuna mabonde makubwa sana yanayofaa kwa umwagiliaji. Tafiti pia zimeonesha na Mheshimiwa Waziri amezungumza, kwamba tuna mabonde hekta milioni 29.4 yanayofaa kwa umwagiliaji. Lakini inasikitisha kwamba mpaka sasa ni hekta 468 tu ambazo zimejengewa miundombinu, na hiyo ni kama asilimia mbili tu ya sehemu yote ambayo imejengewa miundombinu ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunauliza hivi kweli Watanzania tunatakaje kuondokana na umaskini wakati hatutilii mkazo zile sekta ambazo zitatutoa kwenye umaskini? Unaangalia unajua je, ni kwamba hatutaki kutumia akili zetu tuko tayari tukaombe misaada kutoka nje, tukachukue misaada kutoka nje? Tungekuwa kama nchi za huko Ethiopia, Sudan, hivi nchi hii si tungekuwa tumeshakufa wote. Kwa hiyo, ninachosema, ni kwamba nchi yetu bado hatujatumia busara, hekima na akili Mungu alizotupa kwa ajili ya kuona vipaumbele vyetu viwe katika nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kilimo kwa mwaka 2010 kilikua kwa asilimia 2.7 lakini mwaka jana kimeshuka hadi asilimia 1.7, tatizo unaambiwa uhaba wa mvua, ni aibu. Maji yamejaa tunazungumzia uhaba wa mvua kwa nini akili zetu zote tunapeleka kwenye mvua? Haya mambo ya kilimo cha umwagiliaji tumezungumza miaka nenda, rudi tangu kilimo kwanza, lakini mpaka leo tuna tatizo hilo, sijui tusemeje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija Jimbo la Same Mashariki Mungu ametujalia tuna mito mikubwa ukichukulia Nakombo, Hingilili, Saseni, Yongoma lakini mito yote hii inakwenda baharini, mito yote inapita kwenye vichaka. Tumeomba tujengewe mabwawa ili akinamama ambao wengi ndio wanaolima wapate nafuu, akinamama ndio watekaji maji wengi ndio wanahangaika. Watoto wetu wa shule wako wengine boarding wanafuata maji kilometa nzima au mbili, ugonjwa wa UTI haupungui kwenye boarding schools, ugonjwa wa kuharisha watoto, akinamama kila siku wako hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba bajeti ya Wizara ya Afya iongezwe. Tunasema hapa Wizara ya Afya iongezewe pesa kumbe yote inaenda kutibu kuharisha, matumbo, kwa nini tusingeboresha maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nasema, nchi yetu tukiendelea kwa mtindo huu, tusipojali maji na hasa tuseme maji ya kumwagilia akina mama, mboga mboga, akina baba mashamba, vijana wetu hasa kule Jimbo la Same Mashariki kilimo cha tangawizi ambapo LAPF wanataka wajenge kiwanda kikubwa, hakiwezi kufanya kazi kama tangawizi haitapata maji ya umwagiliaji. Kwa hiyo naomba wenzetu walione hilo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishuke kuangalia nini kinachotufanya Tanzania tunarudi nyuma. Hata tukisema bajeti ya Wizara ya Maji iongezwe, ambavyo naunga mkono, je, ubadhirifu ambao uko katika Wizara ya Maji nao tutaufanya nini? Ukiangalia ukaguzi wa ufanisi wa ujenzi wa miradi ya maji hasa ya mijini kwa mwaka 2010/2011 na mwaka 2013/2014 imeonesha katika miradi tisa, miradi nane iliongeza gharama zake kuanzia asilimia 10 mpaka asilimia 229 sawa na ongezeko la shilingi bilioni 30. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa je, Wizara ikiongezewa bajeti sasa hivi itatuhakikishiaje kwamba haya maji yatawafikia hasa akina mama ambao katika Tanzania wako asilimia 51 na na kati yao asilimia 60 wako vijijini? Tupunguze bajeti ya kwenda huko kwenye miji ili asilimia 30 iende mjini, 70 iende vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nasisitiza kwamba tungeanzisha Wakala wa Maji Vijijini badala ya Mfuko wa Maji ili tuwe na uhakika maji kweli yanaenda vijijini na kwamba maji yatawafikia wananchi vijijini. Kinyume cha hapo fedha itawekwa kwenye mfuko halafu hela zitakwenda ndivyo sivyo. Kwa hiyo, ningeomba sana, hata kama tukisema tunaweka umeme mwingi, barabara za lami kama akina mama vijijini watakuwa wanahangaika na maji, hakika nchi hii hatutaendelea. Akina mama ndio wenye uchumi mkubwa katika nchi hii, ndio wakulima wadogo wadogo. Tume-fail katika mambo mengi lakini hebu tuwape akinamama chance, tupeleke maji vijijini, tuanzishe huu Wakala wa Maji Vijijini ili tuwe na hakika hela kweli inaingia huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo.
Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mimi nitachangia kwa kutaka baadaye nije nipate ufafanuzi zaidi hasa kuhusiana na Chemist Professionals Act.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia majukumu ya Baraza pamoja na mambo mengine ni kupitisha vile vyuo ambavyo vitafundisha hawa ma-professionals. Siku za nyuma tumeona matatizo ya vyuo hivi binafsi ambavyo vimekuwa havifuati maadili na kwa ajili hiyo vimekuwa vinatoa mafunzo na vyeti ambapo watumishi wake wakienda kwenye kazi wanakuwa substandard katika utumishi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba katika majukumu ya Baraza litusaidie kuangalia vile vyuo vyenye intergrity ambavyo vinaweza kuruhusiwa kutoa hao wataalamu. Nasema hivi kwa sababu vyuo vingine vya binafsi vinapenda vifaulishe na kutoa watu ambao kwa kweli wakienda sehemu za kazi hawafanyi sawasawa na vyeti vile. Nia yao ni kutoa vyeti hivyo ili waweze kuendelea kuonekana wanafanya kazi. Nimeshuhudia sehemu mbalimbali ambapo wataalamu wamekuwa wakitoa majibu ya utafiti waliofanya na kuonesha ni vitu viwili tofauti sana wakati wako qualified.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nataka nizungumzie matumizi ya hivi vyeti ambavyo hao wataalamu watapewa wakishaandikishwa na Baraza hili. Wataalam hao kwa vile hawako wengi utakuta mtaalam mmoja amejiandikisha katika sehemu tatu au nne za kufanyia kazi na cheti chake kinatumika katika sehemu hizi mbalimbali. Utakuta maabara hasa za hospitali binafsi zinatumia vyeti vya wafanyakazi ambao hawafanyi kazi pale, wamelipwa ili wakija wakaguzi wanaona vile vyeti viko pale na wanaona kweli hii maabara iandikishwe maana ina wataalam na kumbe vile vyeti vilivyotumika wale wataalamu hawafanyi kazi katika maabara zile.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa labda Baraza na Kamati zitakazoundwa zitusaidie kusimamia kanuni za maadili na mwenendo wa wataalamu wawe na uhakiki wa kuonesha kwamba kweli mtaalam ambaye ameandikishwa katika maabara ile ndiyo yuko pale na anafanya kazi pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine ninaloliona katika maabara zetu siyo nyingi, lakini relatively za hali ya juu maana nimepita maabara nyingi kwa sababu zangu mwenyewe, unakuta mkemia yule anayefanya kazi pale anaweza kutumia reagents ambazo zimepitwa na wakati. Mara nyingi hizi reagents zinatumika kwa vile mwenye maabara hataki kupata hasara. Hawezi kusema hapana hizi tusizitumie kwa vile zime-expire matokeo yake zinatoa majibu ya analysis ambayo siyo sahihi. Sasa tujue hizi Kamati zitakuwa na jukumu la ku-inspect kila wakati kuona reagents zinazotumika kufanya analysis katika sampuli mbalimbali zinakuwa hazijapitwa na wakati ili tusitoe majibu ambayo sio sahihi kutokana na reagent ambazo zime-expire. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kwa vile mara nyingi ina tatizo la ukatikaji wa umeme na reagents nyingine zinatakiwa zikae katika temperature fulani na majenereta ya sehemu zile za kazi hayafanyi kazi zile reagent huwa zinabadilika matokeo yake hata yule analyst akifanya kazi atapata majibu ambayo sio sahihi.
Naomba Kamati hizi zitakazoundwa pamoja na Baraza lenyewe liwe na majukumu ya ziada ya kufanya inspection ambayo ni ad-hock maana tumeshaona wakitoa ratiba kwamba leo wanapita kunawekwa mambo ya ajabu ajabu, wanaletwa wataalam ambao hawapo katika maabara ile na kuoneshwa kwamba yuko pale, siku hiyo zitakuwa displayed reagent ambazo ni nzima na wakati mwingine maabara nyingine wanakodisha vyombo kutoka makampuni mengine inspection ikishapita vile vifaa vya maabara vinarudishwa kwa wenyewe.
Kwa hiyo, ningeshauri Muswada huu pia uzingatie haya ninayozungumza hapa ili utafiti utakaokuwa unafanyika katika maabara zetu na hata tukiwa na wataalam ambao ni wasomi zifanywe kwa uhakika na yapatikane majibu ambayo ni ya kisayansi na sio ya kulipua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.