Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi) (11 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2016/2017. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili, nachukua nafasi hii kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ambao walinipa kura za kishindo ili niweze kuwawakilisha vyema katika vikao hivi vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawashukuru sana wanawake wenzangu wa Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nachukua nafasi hii kuwashukuru wapigakura wote wa Mkoa wa Ruvuma ambao wamehakikisha kwamba Chama cha Mapinduzi kinashinda Majimbo yote ya Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala la umeme. Kwa kuwa kwenye Mpango huu kimsingi tumejipanga kuhakikisha kwamba tunakua kiuchumi hasa kupitia viwanda; na kwa kuwa viwanda vyetu haviwezi kuendeshwa bila kuwa na umeme wa uhakika; sijaona mpango mzuri ambao umewekwa kuhakikisha kwamba umeme wa grid ya Taifa kutoka Makambako kuelekea Songea unasimamiwa vizuri ipasavyo na kuhakikisha kwamba mradi huu wa umeme unatekelezwa kwa haraka ili kurahisisha ujenzi huu au Mpango huu wa Viwanda ambao Taifa kwa ujumla limejipanga hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mashaka yangu ni kwamba, inawezekana kabisa Mkoa wa Ruvuma tukaachwa nyuma kwa kuwa bado umeme huu wa grid ya Taifa haujafika huko. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati ahakikishe kwamba katika bajeti hii, suala la kuhakikisha kwamba umeme wa grid ya Taifa unafika Mkoani Ruvuma ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba nizungumzie suala la maji. Kwa kuwa suala la maji ni muhimu sana katika ustawi wa maisha ya binadamu hasa wananchi wetu na kwa ujumla nchi nzima, naomba leo niongelee eneo moja la shida ya maji ambayo inaukumba Mkoa wa Ruvuma. Katika Wilaya ya Tunduru, Namtumbo, Songea Mjini, Songea Vijijini, Madaba, Wilaya ya Nyasa pamoja na Wilaya ya Mbinga, kiukweli kuna shida kubwa sana ya maji. Katika Mpango huu wa utekelezaji wa mwaka 2016/2017 sijaona mkakati madhubuti ambao utapelekea kupunguza adha ya maji kwa wanawake wa Mkoa wa Ruvuma.
Kwa hiyo, nadhani ni vizuri Wizara hii ya Maji ione umuhimu katika kuhakikisha kwamba endapo hakutakuwa na uwezekano wa kupata maji ya mtiririko kwa mwaka huu, basi wanawake wale waweze kuchimbiwa hata visima virefu wakati wanaendelea kusubiri mpango wa maji ya mtiririko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, kimsingi Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma zina shida hiyo na wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ni wanawake ambao ni wajasiriamali, lakini pia ni wakulima. Kwa hiyo, wanatumia muda mwingi sana kwenda kufanya shughuli ya kutafuta maji badala ya kwenda kufanya shuguli zao za kilimo na hata nyingine za ujasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee pia suala la bandari kama Mpango ulivyoainisha suala la kuboresha bandari. Katika Wilaya ya Nyasa tuna ziwa Nyasa lakini pia kuna gati la Ngumbi. Zabuni ya ujenzi wa Gati ya Ngumbi ulikamilika tangu Januari, 2015, lakini ujenzi mpaka sasa hivi haujaanza na wala hakuna matumaini yoyote. Katika Mpango huu sijaona kama kuna fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya mwendelezo huo, ni maneno tu yanaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Mpango huu wa ujenzi wa Gati hii ni wa muda mrefu sana takribani miaka 20 sasa. Kwa kuwa katika Mpango huu pia bado halijaingizwa hili suala, ni mashaka yangu kwamba inawezekana tunaingiza vitu kwa maana ya mpango lakini utekelezaji unakuwa sivyo. Naomba sana, Gati hili la Jimbo la Nyasa litengewe fedha kwa ajili ya utekelezaji na siyo maneno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la kilimo. Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa ambao unashika nafasi ya nne Kitaifa kwa suala la kilimo. Pamoja na mazao mengi yanayozalishwa katika Mkoa wa Ruvuma, lakini leo naomba niongelee zao ambalo linazalishwa katika Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma ambalo ni zao la mahindi. Hili ni zao la chakula katika Mkoa wetu lakini pia ni zao la biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mpango Mzuri wa Serikali wa kuhakikisha kwamba unatoa Ruzuku ya Serikali kwa ajili ya pembejeo za kilimo kwa maana ya voucher, niseme tu kwamba vouchers hizi kimsingi hazimnufaishi mwananchi wa kawaida wa pato la chini. Badala yake kumekuwa na vurugu, yaani kutokuelewana baina yao wenyewe; wananchi wao kwa wao pamoja na wanaosimamia. Tatizo ni kwamba voucher ni kidogo na hitaji ni kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiria kwamba ni vizuri basi Mpango huu wa Serikali ungekuja na Mkakati maalum namna gani unamwezesha mwananchi ili aweze kupata pembejeo za kilimo kwa bei nafuu baada ya kuondoa kodi ili kila mwananchi aweze kuchukua pesa yake kununua pembejeo za kilimo kwa bei nafuu badala ya kuwa baadhi wanapata voucher na wengine hawapati. Matokeo, mnatusababishia ugomvi ambao siyo muhimu kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani Mpango huu ungekuja na Mkakati wa kuona namna gani kodi inaondolewa na wananchi wale waweze kufikiwa, mmoja baada ya mwingine aweze kujikimu mwenyewe kununua pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mpango Mzuri wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wananchi wanawezeshwa kwa maana ya Shilingi milioni 50 kila Kijiji na kila Mtaa, ni mpango mzuri sana wa kuhakikisha kwamba uchumi wa mwananchi mmoja mmoja unakua. Naipongeza sana Serikali kwa kuona umuhimu wa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango huu pia sijaona mkakati madhubuti ambao umewekwa kuhakikisha pesa hii inayoenda kwa ajili ya kumwinua mwananchi mdogo, inatengeneza mazingira ya kumwondolea kodi zisizokuwa za lazima au ushuru usiokuwa wa lazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, pesa hii inalenga kabisa kuwainua watu wafuatao: kwa mfano, vijana, mama lishe, bodaboda, wauza matunda na wauza mboga mboga. Sasa ushuru ambao wanatozwa kwenye masoko yao ni ushuru mkubwa. Haiwezekani mtu ana fungu tano za nyanya anatozwa Sh. 1,000/= kutwa! Hiyo ni shida! Kwa hiyo, Mpango huu uende na mkakati wa kuona ni namna gani wataondoa huo ushuru usiokuwa na umuhimu ili kumfanya mwananchi huyu, kweli kile anachokipata aweze kukizungusha na kujikimu katika maisha yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Benki ya Kilimo. Ni jambo jema Serikali kuanzisha Benki hii ya Kilimo, lakini ndani yake nimeona kuna vitu ambavyo siyo sahihi. Benki hii imeanzishwa kwa madhumuni ya kumwinua mkulima, lakini kwenye utekelezaji iko ndivyo sivyo kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma vizuri kwenye mapendekezo ya Mpango huu na nimeona kwamba kuna baadhi ya mikoa ambayo imetengwa kwa ajili ya majaribio na imeshaanza kupelekewa fedha. Baadhi ya hiyo Mikoa ni Iringa; sina shida, wananchi wa Iringa wanalima, lakini pia Mkoa wa Njombe sina tatizo nao, wanalima vizuri tu; Mkoa wa Morogoro nao pia ni wakulima wazuri; hata Pwani, wanalima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vitu vya kushangaza sana eti Mkoa wa Dar es Salaam nao umepangwa kwa ajili ya watu kupata pesa ya kilimo. Jamani, tuseme ukweli, hivi Dar es Salaam kuna mashamba ya kulima? Mbona hatujaona hayo mashamba, wanalima wapi? Ina maana kuna mashamba Mikocheni, Oysterbay na hapo Sinza Mori? Haya ndiyo mambo ambayo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayataki na ndiyo anayamulika. Haya ni sehemu ya majipu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli Serikali imejipanga kumwinua mkulima wa kawaida wa hali ya chini, ni vizuri basi malengo haya yakaenda moja kwa moja kwenye maeneo ambayo wananchi wapo na wanalima kweli, badala ya kwenda kuwanufaisha tu watu wamekaa tu maofisini, wengine wamekaa kwenye magari yao, full viyoyozi, wanapata pesa za kilimo ilhali hawalimi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee kuhusu suala la Uwekezaji. Mpango wa Serikali juu ya suala la uwekezaji naona ni mzuri, lakini pia nadhani uende sambamba na kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo yalikuwa yamechukuliwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza viwanda kwa maana ya ardhi ya wananchi ambayo imechukuliwa, basi Mpango huu wa Serikali wa kuendeleza viwanda uende sambamba na kulipa fedha za fidia kwa wananchi ambao wamechukuliwa maeneo yao, ikiwemo eneo la Mwenge Mshindo katika Wilaya ya Songea Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu sana wawekezaji hawa EPZ wamechukua maeneo makubwa sana ambayo mpaka sasa hivi inakaribia miaka 15 au 16 wananchi hawajalipwa pesa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba kwenye suala la miundombinu, barabara inayotoka Makambako kwenda Songea…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ngonyani!
MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Nayo pia ifanyiwe marekebisho ni mbaya sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ngonyani, muda wako umekwisha.
MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na anaendelea kuifanya. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia Mawaziri wote kwa Wizara mbalimbali kwa jitihada zote ambazo mnaendelea nazo kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Hongereni sana, kazi mnayofanya inaonekana na Mungu awajaalie kila la kheri, awape wepesi ili muendelee kudunda kazi kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimeona ni vizuri nikaenda moja kwa moja kwenye eneo la afya. Katika Manispaa yetu ya Songea, kituo cha afya cha Mjimwema ambacho hivi karibuni kinatarajia kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya pana shida kwani hakuna vifaa vya upasuaji. Leo hii tunakwenda kupitisha hii bajeti ya TAMISEMI, labda Mheshimiwa Waziri ataniambia katika eneo hili kuna pesa ambazo zimetengwa? Nimejaribu kuangalia hapa sijaona na kama nilichokiona bado ni kidogo na ndiyo maana kama vile sijaona. Kwa hiyo, niombe katika kituo hiki cha afya ambacho kinakwenda kupandishwa hadhi mwezi wa saba basi kuwe na umuhimu kuhakikisha kwamba vifaa vya upasuaji katika chumba cha upasuaji vikamilishwe ili inapopanda kuwa Hospitali ya Wilaya iwe pia imetekelezwa kwa kiasi hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende pia kwenye eneo hilo hilo la afya katika Wilaya ya Mbinga. Katika Hospitali ya Wilaya kuna tatizo kubwa la mortuary ambayo haijapewa vifaa vinavyostahili ikiwemo fridge. Sifa ya mortuary ni kuwa na fridge na kama haina fridge basi hiyo sio mortuary. Kwa hiyo, niombe kupitia Waziri wa TAMISEMI afanye kila linalowezekana kuhakikisha kwamba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbinga kunakuwa na vifaa ambavyo ni fridge na vifaa vingine ambavyo vinastahili katika mortuary hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende pia kwenye eneo la kilimo. Juzi nilisema hapa lakini pia naomba leo niseme labda nikisema sana itaeleweka. Kwenye eneo hili la kilimo katika mkoa wetu nimeshasema sana na nadhani hata Waziri wa Kilimo anafahamu kwamba Mkoa wetu wa Ruvuma ni mkoa ambao unazalisha mazao kwa wingi sana hasa mazao ya chakula. Kwa hiyo, ni vizuri mkoa huu ukapewa kipaumbele kwa kupatiwa pembejeo za kilimo kwa maana ya vocha zikawa nyingi zaidi ya zile ambazo zinapelekwa huko kwa sababu zilizopo bodi hazikidhi. Pia nipongeze mpango huu wa Serikali wa kuhakikisha kwamba unatoa pembejeo za kilimo kwa mpango wa vocha ili kuwawezesha wananchi kujikimu katika shughuli hizi za kilimo ili waweze kuzalisha zaidi. Chagamoto zilizopo ni pamoja na ufinyu huo wa pembejeo lakini pia ni pamoja na kuchelewa kwa pembejeo ambazo zinapelekwa kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo hilo kuna changamoto kubwa ambayo imekuwa ni kero sana, wakulima wanakwenda kulima na wanalima vizuri kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa maana ya kilimo kwanza na wamekuwa wakizalisha sana. Shida inakuja wamepata pembejeo na wengine wanajiwezesha wenyewe kwa kununua pembejeo kwa bei ghali hatimaye sasa inafika mwisho wa siku anaporudisha mazao yake kutoka shambani ni tatizo kubwa, ushuru umekuwa ni kero. Kumekuwa na kero kubwa sana ambayo inasababisha hata watu wanaona shida kulima. Mtu analima labda kata fulani, anapotoa mazao kutoka kata hiyo kwenda kwenye kata nyingine katika Wilaya hiyo hiyo kunakuwa na barrier lukuki. Kwa mfano, katika Wilaya ya Namtumbo, ukitoka Mputa kwenda Hanga pana barrier, ukitoka Hanga kwenda Msindo pana barrier, ukitoka Msindo kwenda Lumecha pana barrier, hii ni kero. Pia kuna barrier kati ya Mwanamonga na Mwengemshindo, ni kata hizo hizo tu kunakuwa na barrier karibu 30 katika Wilaya moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali na Waziri wa TAMISEMI ajaribu kuona namna ya kuweka mikakati ya utafutaji wa pesa kuziwezesha halmashauri zake siyo kuwakamua wananchi. Kwa sababu unapokwenda kumkamua mwananchi ambaye amehenya miezi sita ili aweze kupata mazao halafu mwisho wa siku anakuja anakamuliwa kwa kukatwakatwa huu ushuru nalo si jambo jema. Ni sawaswa na mtu una mgonjwa unamuongezea damu huku upande mwingine unampachika mrija wa kumnyonya damu, hii haina mashiko na wala haina afya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuniamini na kunipa kura za kishindo. Nawashukuru pia wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa namna ambavyo wamekipa Chama cha Mapinduzi kura za kishindo na hata Majimbo yote sasa ya Mkoa wa Ruvuma ni ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye Benki ya Kilimo. Nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuona umuhimu wa kuanzisha Benki ya Kilimo ili kuweza kuchochea hali ya kilimo katika nchi yetu na kuwafanya wananchi wake waweze kujiwezesha kwa ajili ya kukopa na kuendeleza kilimo mmoja baada ya mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na shughuli hiyo inayofanyika kwa maana ya kilimo, naomba niseme tu kwamba katika Mkoa wetu Ruvuma kuna mazao mengi ambayo yanalimwa katika Mkoa huo, lakini leo hii naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, aone umuhimu wa kupeleka Benki hii ya Kilimo sasa katika Mkoa wa Ruvuma kwa sababu Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa ambao katika shughuli zake asilimia 90 wananchi wote wanategemea kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Benki ya Kilimo ipelekwe huko ili iweze kuwarahisishia wananchi kuweza kukopa na kuendeleza shughuli zao za kilimo, wakiwepo wanawake ambao ni wakulima na wafugaji wanaotokana na Wilaya ya Mbinga, Wilaya ya Nyasa, Wilaya ya Songea Vijijini, Wilaya ya Namtumbo na Wilaya ya Tunduru. Hawa wote wanahitaji wapate pesa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo bila kusahau Halmashauri ya Madaba, nao pia kuna wanawake ambao wanahitaji wapate pesa kwa ajili ya shughuli za kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kusema sana kwenye eneo hili, lakini naomba tu endapo Waziri mwenye dhamana atanikubalia kupeleka benki hii kule katika Mkoa wa Ruvuma, azma yangu ya kuondoa shilingi katika bajeti hii nitaiondoa. Vinginevyo nitaondoa shilingi ili anihakikishie kwamba benki hii sasa inakwenda kuhakikisha kwamba wale ambao ndio wanashughulika na shughuli za kilimo, ndio ambao wanasogezewa mahitaji haya. Kwa sababu Benki hii katika Mikoa mitano ambayo ni ya mfano ambao wameanza nayo ni pamoja na Mkoa wa Njombe.
Sasa jamani Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, hivi kutoka Njombe na kufika Songea mbona ni kama pua na mdomo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, pamoja na kazi nzuri anazozifanya, wananchi wanatambua na wana imani kubwa sana na wewe, hasa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, wanawake wa Ruvuma, naomba sana jambo hili ungelitilia mkazo ili tuweze kupata benki na wananchi waweze kufanikiwa kwa ajili ya mahitaji hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Ruvuma pia tunalima mahindi, kahawa na korosho, ndiyo maana ninaona umuhimu wa kusisitiza, kwa maana mazao yote haya ndiyo yanayoipatia pato kubwa sana nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, umuhimu wa kupeleka benki ni mkubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye suala la zao la tumbaku. Zao la tumbaku ni shida; kila mmoja ameongea hapa! Maeneo mengi sana ni wahanga wa jambo hili. Hata kwetu katika Mkoa wa Ruvuma katika Wilaya Namtumbo kuna shida hiyo. Tunaomba sasa kuhusu gawio ambalo linagawiwa na Wizara kupeleka maeneo ambayo watu wanalima tumbak, basi na Wilaya ya Nambumbo ipewe kipaumbele ili waweze kupata gawio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, kwa kuwa mahitaji ya tumbaku duniani yameshuka, ni vizuri sasa Serikali ikajipanga kuhakikisha kwamba zao hili la tumbaku linalimwa hapa hapa ndani ya nchi yetu na wanunue zao hili ndani ya nchi yetu, badala ya kununua tumbaku hii nje ya nchi, kwa mfano, sasa hivi inanunuliwa maeneo mengine ya nje ya nchi ikiwemo Uganda; naomba sana kwa kuwa eneo hili mahitaji yameshuka, basi mazao yatakayozalishwa juu ya suala la tumbaku, nadhani yatakidhi haja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye suala la mawakala wa pembejeo za kilimo. Kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kupeleka huduma hii ya voucher kwa wananchi wetu, baadhi yao wananufaika na wengine hawanufaiki, lakini najua Serikali yetu ni sikivu, wataona umuhimu wa kufanya marekebisho juu ya jambo hili ili wananchi wote mwisho wa siku waweze kufikiwa na huduma hii. Mawakala wetu kwenye maeneo mbalimbali katika nchi yetu hii ya Tanzania, wamejitoa muhanga kuhakikisha kwamba wameikopesha Serikali kwa kuwapa wananchi pembejeo na baadaye wanakuwa wanaidai Serikali. Wamejitolea!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuwapongeza sana. Naomba sasa Serikali na Wizara kwa ujumla mwone mchango mzuri ambao mawakala hao wameutoa ili kuwezesha zoezi la utoaji wa voucher uweze kwenda kwa wakati. Kwa misingi hiyo, naomba niwasemee leo mawakala wa pembejeo za kilimo. Waheshimiwa Wabunge wengi waliosimama hapa, mimi naona wamewasahau kabisa kuwasemea; ni watu ambao wamejitoa, lakini mpaka sasa hivi hawajalipwa pesa zao. Wanadai pesa nyingi na wale ni wajasiriamali ambao wanaendesha biashara zao kwa kutumia mikopo mbalimbali; wanakopa kwenye mabenki, SACCOS na maeneo mengine mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika wakati sasa hivi, wale wajasiliamali wamekauka midomo. Hali ni mbaya na wengine wanadaiwa sana na hatimaye wengine tayari wanaweza hata wakafilisiwa mali zao, ikiwemo hata kuuziwa nyumba zao.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati unajipanga vizuri kuhakikisha unatekeleza ipasavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye eneo la kilimo, naomba uwatazame kwa jicho la huruma sana wajasiriamali waliopo katika Mkoa wa Ruvuma, katika Wilaya zote zinazojumuisha Mkoa wa Ruvuma, tukianza na Tunduru, tukaja Namtumbo, nikaja Songea na hatimaye Mbinga na hata Nyasa. Wote wanahitaji walipwe pesa zao ili waweze kuendelea kujikimu katika maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii niongelee suala la zao la samaki katika Ziwa Nyasa. Naomba nimwambie tu Mheshimiwa Waziri kwamba katika maziwa yote ambayo yanatoa samaki katika nchi hii, hakuna samaki watamu wanaoshinda Ziwa Nyasa. Ziwa Nyasa linatoa samaki watamu sana na wenye virutubisho sana na ndiyo maana ukimwangalia Mheshimiwa Jenista Mhagama, amenawiri, yuko vizuri; ukimwangalia Sixtus Mapunda naye yuko vizuri hata ukinitama mimi niko vizuri kwa sababu ya samaki wazuri na watamu wanaotokana na Ziwa Nyasa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Uvuvi naomba uelekeze macho yako katika Ziwa Nyasa. Ziwa hili linatoa dagaa wazuri mno haijapata kutokea! Naomba uelekeze nguvu huko! Naishauri tu Serikali kwamba hebu oneni umuhimu... (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Kwanza kabisa nianze kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali imara, yenye Sera nzuri zinazokubalika na zinazotekelezeka. Niipongeze sana Serikali yangu ya Awamu ya Nne iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Katika Wizara hii ya Miundombinu ilikuwa na Jemedari wetu ambaye sasa hivi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Pombe Magufuli. Serikali hii imefanya kazi nzuri ya kuhakikisha ya kwamba mikoa yetu inaunganishwa na barabara za lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana hata kama huna masikio, lakini hata macho hayaoni? Amesimama mlevi mmoja hapa, mimi namuita mlevi, amesimama mlevi akisema kwamba eti Serikali ya Chama cha Mapinduzi hamna chochote inachokifanya. Barabara hizi zimejengwa kwa 31% kwa miaka 15! Safari ni hatua, kama imefikia 31% ina maana Serikali inafanya kazi na inaendelea kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumtia moyo Waziri wa Miundombinu na Naibu wake pamoja na delegation yake yote, endeleeni kuchapa kazi, sisi tuko nyuma yenu, tunaendelea kuwaombea. Kazi mnayofanya ni nzuri na inaendelea kuonekana kwa hiyo, ungeni pale ambapo Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Dkt. Magufuli walipoishia ninyi endelezeni pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu kwamba, hakuna mwanamke yeyote yule atakayeweza kumsifia mke mwenzake hata siku moja. Mke mwenza ni mke mwenza tu na kama ikitokea ukamsifia mke mwenzako basi wewe kidogo utakuwa fuse down. Hali kadhalika, debe tupu ndilo lenye kelele, debe lililokuwa na ujazo mzuri halipigi kelele. Tunawashukuru wananchi wetu wa Tanzania ambao wameona umuhimu wa kukipa Chama cha Mapinduzi kura za kishindo na wakiwa na imani na Serikali yao kwamba ina sera nzuri na zinazotekelezeka na sasa hivi Chama cha Mapinduzi kiko mtamboni kitaendelea kutekeleza majukumu yake. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye nyumba za Serikali. Nyumba za Serikali zilizokuwa zinasemwa hapa ni nyumba ambazo ziliuzwa wakati wa Rais wa Awamu ya Tatu akiwepo Waziri Mkuu ambaye ndiye mwaka jana alikuwa miongoni mwa watu wa mabadiliko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Sumaye ndiyo ambaye alikuwa Waziri Mkuu kwa wakati huo na ndiye aliyesimamia. Kama alifanya kazi mbaya basi muone kwamba mabadiliko mliyokuwa mnaenda kuyafanya ni mabadiliko hovyo…
MHE. JACQUILINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu hata ambaye alipewa ridhaa ya kuipeperusha bendera ya CHADEMA kwa mwaka jana naye ni hovyo, fisadi aliyepindukia na pia ukija na Mheshimiwa Sumaye naye ni tatizo! Ndiye aliyeuza nyumba hizo kwa mipango mibovu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisiharibiwe muda kwa sababu sindano zinapoingia na wao watulie kama wao walivyokuwa wanaingiza sindano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua lazima Wananchi watambue wazi kwamba, hata katika suala ambalo kwa mfano tunachangia humu ndani, upande mwingine ni kelele maana yake ni madebe matupu na upande mwingine wanatulia kwa sababu wana hoja. Na niseme tu kwa upande wa wenzetu wa Upinzani kwa wanawake wanaoweza kujenga hoja ni watu wawili, Mama Sakaya na Upendo, lakini wengine the rest hamna kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye hoja ya msingi sana. Pamoja na kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa na Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, naomba niende moja kwa moja kwenye barabara yenye urefu wa kilometa 124, barabara ambayo inatoka Likuyufusi kuelekea Mkenda. Barabara hii ni ya muda mrefu, Waheshimiwa Wabunge waliopita, Mheshimiwa Jenista Mhagama, dada yangu Stella Manyanya na Marehemu John Komba na wengineo walisimama imara sana kutetea hii barabara ili iweze kujengwa, lakini mpaka sass hivi barabara hii haijajengwa, ni barabara ambayo inaunganisha Msumbiji na Tanzania. Naomba Waziri mwenye dhamana, barabara hii iweze kuanza kujengwa kwa kipindi hiki cha mwaka 2016/2017, utakapokuja hapa wakati una-wind up tafadhali naomba ueleze bayana barabara hii inaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye barabara ya Morogoro - Ruvuma; mimi hizo kelele hazinibabaishi kwa sababu ninyi kwetu, kwa lugha ya kwetu tunawaita mazindolo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ambayo inaunganisha mkoa wa Morogoro na mkoa wa Ruvuma, na sisi kwetu hatuna aibu Wangoni hawana aibu hata kidogo kwa hiyo, barabara hiyo inatoka Kidatu – Ifakara – Lupilo – Malinyi – Londo – Lumecha mpaka kufika Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia kupata uzima siku hii ya leo, nikushukuru pia wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza na suala la ujenzi wa zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali ni jambo ambalo lilikuwa limelenga kabisa maendeleo yetu ili yaweze kufanikiwa ni lazima kwanza wananchi wetu wawe na afya bora na hapo ndipo tutakapoweza kufikia uchumi wa kati, lakini pia katika kufanikisha malengo ya milenia kufikia uchumi huu wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiulize Serikali leo ni lini itakamilisha ujenzi wa vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali za Wilaya ili tuweze kufikia sasa uchumi huu wa kati, kwa sababu tusipokuwa na afya njema ni wazi kabisa Taifa litakuwa na wananchi ambao ni goigoi, watashindwa kufanya kazi vizuri ili kuweza kufikia uchumi huu. Hivyo, Serikali iniambie lini ujenzi huu utakamilishwa katika vituo vile vya afya, zahanati pamoja na hospitali za Wilaya ambazo hazijawa tayari kwa maana ya kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuainisha hizo zahanati ambazo zipo katika Wilaya ya Mbinga, Mbinga Mjini kuna zahanati karibu 15 ambazo zinahitaji kumaliziwa, lakini pia Mbinga Vijijini kuna vituo vya afya na zahanati ikiwemo katika Kata ya Kilimani kuna zahanati, Lipilipili, Luwahita, Luhaga, Mikatani na Kihuka. Pia katika Wilaya ya Nyasa pana shida kubwa sana kwa maana ya hospitali ya Wilaya imeanza na haijakamilika, ni lini Serikali itakamilisha ili tuweze kupata wananchi ambao watakuwa na afya bora tuweze kufikia malengo ya milenia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya hiyo hiyo ya Nyasa kuna zahanati ya Chiwanda, Ngindo, Liweta, Mpotopoto, naomba pia nazo zitiliwe uzito zitengewe pesa kwa ajili ya kukamilisha. Tunduru pia kwenye eneo hili kuna wodi ya wanaume katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru, watoto wa kiume wanaenda kulala kwenye wodi ya akina mama, hii ni hatari sana kiafya lakini pia hata kimaadili. Wodi ya wanaume kule Tunduru inatakiwa imaliziwe, lakini pia kuna wodi ya wanawake nayo pia imaliziwe katika Wilaya ya Tunduru nikienda sambamba na zahanati za Masonya, Sisi kwa Sisi, Cheleweni, Njenga na Fundimbanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Madaba pia naomba mfahamu mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Madaba na jitihada ambazo anaendelea kuzifanya ili kuhakikisha kwamba, Jimbo la Madaba litakuwa na hospitali ya Wilaya lakini pia na vituo vya afya pamoja na zahanati ili nao pia waingia katika malengo ya milenia. Hali kadhalika na katika Wilaya ya Namtumbo zahanati na vituo vya afya ni muhimu. Zahanati na vituo vya afya vikikamilika ni wazi kabisa tutakuwa tuko vizuri na afya zitaboresheka na hata hivyo tutafikia hizo asilimia saba za uchumi wa Tanzania ambao tunautarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuondoa tozo zisizokuwa na tija kwenye mazao ya korosho, kahawa na tumbaku, naipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma bajeti hii na maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii kwa maana ya bajeti ya Serikali maelezo ni matamu na hata uchambuzi wake ni mzuri mno. Hii inaonyesha wazi ni namna gani Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba inakuza uchumi wa ndani kwa kukusanya mapato pia inafikia hatua ambayo Serikali sasa itaacha kuwa tegemezi na itaenda kujitegemea yenyewe. Naipongeza sana Wizara hii kwa kujipanga vizuri kwenye eneo hili. Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake mko vizuri pamoja na delegation yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia kwenye eneo hili iangalie sekta zile ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa sana kwa maana ya kuingiza mapato mengi katika nchi yetu ikiwemo sekta ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya utalii kumekuwa na jambo moja ambalo lilikuwa kama vile wenzetu ambao walikaa kwa maana ya mahusiano haya ya East Africa wakakaa kwa pamoja Mawaziri wa Fedha wakiwa na lile jambo ambalo kwa mfano, labda wanasema kwamba, kuna chakula cha mgeni na chakula cha wote. Kilichofanyika hapa ni kama hivi changa la macho.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Kenya mara ya kwanza walikuwa wameingia kwenye suala la kutoza VAT kwa watalii wanaoelekea Kenya. Baada ya hapo wakaona kwamba ile VAT haitawasaidia na kwamba imeshusha sana kiasi cha mapato yanayopatikana katika utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 Mawaziri hawa walipokaa walikubaliana vizuri kilichojitokeza ni kwamba, mwaka 2015 Kenya ilipata watalii 3,000,000 na waliingiza dola za Kimarekani bilioni 1.5. Tanzania iliingiza watalii milioni 1,100,000 ilipata dola za Kimarekani bilioni 2.5. Sababu kuu ilikuwa ni kwamba Tanzania ililenga kuwa na watalii wakubwa tu ambao wana uwezo wa kulipia hoteli, lakini Kenya walikuwa wamelenga wapate watalii wadogo wadogo pamoja na kutoza kodi kwa hiyo mapato yao yalishuka. Baada ya kugundua hilo sasa wamerudi na habari nyingine wakasema kwamba, wao ni vizuri wakaondoa kodi kwa hiyo, tumebaki sisi ambao kimsingi tumeenda kujiingiza kitanzi wenyewe, tunaenda kujikaba wenyewe ili tujinyonge na hatimaye tushindwe kuongeza mapato kwenye eneo hili la utalii. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge wenzangu, niwaombe sana kwenye jambo hili tushirikiane, tufike mahali tukubaliane kama wamoja tuondoe VAT kwenye eneo hili la utalii ili utalii uendelee kuingizia mapato Serikali, kinyume na hivyo maana yake tutakosa hizi dola za Kimarekani bilioni mbili na point zake, badala yake wenzetu Kenya wanaenda kufanikiwa sisi tunabaki tuko tunabembea tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Wabunge kama nilivyosema nisingependa kurudia pia nitakuwa sijatenda haki endapo kama sitaongelea kodi ya Wabunge. Kwenye suala hili kwa kweli mmegusa pabaya, panaumiza kweli kweli ukizingatia kwamba Mbunge hata sasa mshahara wake bado anatozwa kodi kila mwezi Mbunge anakatwa shilingi milioni moja na laki tatu na kadhalika mpaka itakapofika miaka mitano maana yake kunakaribia milioni 50 ambayo Mbunge anakatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niwaambieni mimi kama Mbunge toka asubuhi mpaka sasa hivi hapa niliposimama nina simu 30 zinatoka kwenye Jimbo langu la Mkoa wa Ruvuma, wananchi wana mahitaji mbalimbali na ukizingatia kwamba Wabunge wa Viti Maalum hatuna Mfuko wa Jimbo, tunafanyaje kwa kile tunachokipata? Kile tunachokipata kidogo ndiyo kinaenda kusaidia hata ukaenda kufanya hili, ukafanya lile na hata kuwezesha vikundi mbalimbali. Ninaomba Waziri atakapokuja tena, aje na maelezo mazuri kuhusu eneo hili ili tuweze kwenda sambamba, vinginevyo hatumuelewi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kwa kifupi nichangie hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukataji miti hovyo ni chanzo kikubwa sana kinachochangia mabadiliko ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na nchi yetu kuelekea kuwa jangwa. Uchomaji wa mikaa hovyo nao pia unachangia sana mabadiliko ya hali ya hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na uharibifu mkubwa sana juu wa vyanzo vya maji kutokana na matumzi mabaya ya ardhi. Kwa nini:-
(a) Halmashauri zetu zinaruhusu wananchi kujenga ndani ya vyanzo vya maji, sheria ifuate mkondo wake.
(b) Uchimbaji wa mchanga na kokoto navyo vinachangia uharibifu wa vyanzo vya maji, sheria ifuate mkondo wake.
(c) Shughuli za kilimo ndani ya vyanzo vya maji nalo ni tatizo kubwa, sheria ifuate mkondo wake.
(d) Shughuli za ufugaji ndani ya vyanzo vya maji zidhibitiwe ili vyanzo vyetu visiendelee kuharibiwa.
(e) Tusiruhusu nchi jirani kuingiza mifugo katika nchi yetu, ni hatari sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono michango ya TANAPA kwa jamii na nawapongeza kwa dhati na niombe taasisi au mawakala wengine wa Serikali kama TANAPA watoe mchango kwa jamii kama TANAPA wanavyofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya hali ya hewa. Hili ni janga la kidunia, tukiwa kama nchi ambayo ina misitu na maliasili nyingi yafaa tuendelee ku-maintain misitu, uoto wa asili, vyanzo vya maji, tusichanganye mifugo na wanyamapori kama ambavyo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakichangia kwamba maeneo ya hifadhi nao wachunge ng‟ombe. Napinga vikali jambo hilo, tena nasisitiza sana kuwa sheria itumike ili waamue kupunguza mifugo na wakipunguza mifugo watafuga kwa tija badala ya sasa ng‟ombe kibao lakini ukiwatazama ng‟ombe hao wana uzito sawa na bata. Ni wazi kuwa ng‟ombe huyu hatamsaidia mfugaji, ni kero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa kiwanda cha Baraghashi – Sao Hill. Hiki kiwanda kinapata gawio la misitu 60% bado wanapata bei punguzo. Jambo la kusikitisha ni kwamba kiwanda hiki kinazalisha karatasi ngumu, anasema finishing anakwenda kufanyia Kenya, jambo ambalo sio kweli, anachokifanya huyu mwekezaji ni kukwepa kodi ya Serikali. Nashauri afuatiliwe kwa ukaribu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wafanye kazi yao badala ya kujiingiza kwenye biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja na naomba mchango wangu uingie kwenye Hansard.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi kukushuru kwanza kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia Kamati ya Huduma ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, pamoja na Ardhi, Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kupongeza uchaguzi uliopita tarehe 22 Januari, 2017 ambapo Chama cha Mapinduzi kiliwafunga wapinzani wetu wana UKAWA goli 22 kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana unajua tunajuana humu ndani wapo wanaokula msuba asubuhi, mchana na jioni kwa hiyo hainipi shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niende kwenye suala la kilimo kwa maana ya ubora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba hiyo kazi wanayoifanya ndiyo iliyowaleta humu ndani na hawana kazi nyingine kama wangekuwa na kazi wangekuwa watulivu wasikilize nini kinachochangiwa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Kilimo wawe makini sana kwenye suala la ubora wa mbegu. Mbegu zinazopelekwa kwa wakulima siyo mbegu sahihi, wakati mwingine mbegu zile huwa zinakuwa zina shida, hata kama ni mbegu ambazo zinatolewa kwa mtindo wa ruzuku lakini bado hazimsaidii mwananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisema kwamba kunai le hali ya mimba za utotoni, kwenye mbegu hizi nyingine nazo ni staili ya mimba za utotoni. Kuhusu hizi mbegu unakuta wakati mwingine mbegu zinakuwa ni fupi haziwezi kuzalisha kadiri ambavyo inastahili, kwa hiyo Wizara ya Kilimo tunaomba muwe makini. Pia niseme endapo mbegu hizo zisizokuwa na ubora zinaletwa, mwisho wa siku mwananchi anapokuwa amepata hasara, hasara hii inafidiwa na nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee suala la mawakala wa pembejeo. Mawakala wa pembejeo hili ni jambo ambalo tumekuwa tukiliimba kila siku. Mawakala wa pembejeo ambao kimsingi waliikopesha Serikali, walifanya kazi ya kusambaza mbolea na mbegu mbalimbali kwa ajili ya kuikopesha Serikali mwisho wa siku mawakala hawa mpaka leo hawajalipwa. Toka mwaka 2014, mwaka 2015, mwaka 2016, ni lini Serikali hii itawalipa hawa mawakala? Wamekuwa na shida na wengine mpaka sasahivi wameshapoteza maisha na wengine wanadaiwa na mabenki, walikuwa wazima wakati wanakopesha mbolea hizi kwa wananchi, sasa hivi unakuta tayari wameshanunua magonjwa kama pressure. Naiomba Serikali iwe serious ili kuwasaidia hawa wananchi wajasiriamali ambao waliweza kuikopesha Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia kwenye Benki ya Kilimo. Wakati tunapitisha bajeti hapa mwaka jana mwezi wa sita, bajeti ya kilimo, Waziri alikuwa amesema kwamba angeweza kufikisha Benki ya Kilimo katika Mkoa wetu wa Ruvuma, lakini nashangaa mpaka sasa hivi bado haijafika, sijui ndiyo bado upembuzi yakinifu au ni nini? Mpaka sasa hivi hakuna dalili zozote zile za kufikisha benki hii ya kilimo! Niombe Waziri wa Kilimo tafadhali kwa kuwa mkoa wa Ruvuma ni mkoa ambao wananchi wake wanashugulika na kilimo kwa asilimia 92, naomba sasa benki hii iende ili iweze kuwasaidia wananchi hawa waweze kukopa na kuweza kufanya uzalishaji wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la uvuvi; tunalo Ziwa Nyasa katika Mkoa wetu wa Ruvuma. Mimi naomba nishauri jambo hapa, uvuvi katika Ziwa Nyasa samaki walioko pale wangeweza kuwa wengi zaidi na uvuvi ule ukawa na tija endapo kama Serikali ingeweza kufanya kama wanavyofanya wenzetu wa Malawi, kwa sababu ziwa hilo moja liko upande Malawi na upande mwingine wa ziwa upo upande wa Wilaya ya Nyasa kwa maana ya Tanzania. Kwa hiyo, wenzetu wa Malawi wanachokifanya wanalisha chakula kwenye lile ziwa, samaki wanakwenda kwenye upande wa Malawi kwa sababu kuna chakula. Wenzetu wa Malawi sasa wanapata mavuno mengi kutokana na hili Ziwa Nyasa. Sisi tunaambulia patupu, ziwa lipo tunaambulia kuangalia tu mandhari ya ziwa lilivyo lakini hatuna faida nalo yoyote ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali ione umuhimu kama tuko serious na suala hili la uvuvi, basi walao tufanye huo utaratibu wa kuwa tunalisha chakula ili tuweze kupata samaki wazuri ambao tutawauza na watatupatia pato…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Jacqueline.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na Kamati ya UKIMWI. Namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenipa uhai ili niweze kusimama hapa siku hii ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la elimu bure. Nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kuthubutu kuweza kutekeleza elimu hii bure. Dhamira ni njema, lakini katika mpango huu bado kumekuwa na changamoto nyingi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la elimu napenda kuzungumzia kwamba elimu bure sawa inatolewa, lakini pia ukienda kwenye shule zetu za primary na za secondary kumekuwa na changamoto ya upungufu wa madarasa; lakini bado katika Mkoa wangu wa Ruvuma kuna changamoto katika Wilaya ya Namtumbo katika sekondari ya Nungu Kata ya Hanga.
Kwenye hiyo sekondari ambayo sasa imeanza kidato cha tano; na changamoto iliyoko hapo inafanana kabisa na changamoto iliyoko katika Wilaya hiyo hiyo katika sekondari ya Nasulu Wilayani Namtumbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu sekondari hizi zilipoanzishwa kwa kidato cha tano hawajapelekewa pesa kwa ajili ya chakula. Kwa hiyo niombe, tunapoamua kutoa elimu bure ni vizuri basi tukajikita kwenye mambo ya msingi. Kwa mfano; mtoto hawezi kuendelea kusoma na akajituma vizuri zaidi na kuweza kuwa msikivu katika masomo kama hatakuwa amepata chakula. Wazabuni ambao wamejitokeza kutoa huduma katika shule hizi wameshafanya kwa kiasi walichoweza, lakini imefika mahali wanakwama kwa sababu hawajawezeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Walimu pia unachangia kwa kiasi kikubwa. Hili ni eneo ambalo wajumbe wenzangu wengine Waheshimiwa Wabunge wamechangia; kwamba bado maboresho dhidi ya Walimu hawa yanatakiwa ili Walimu waweze kuwa na moyo wa kuendelea kutoa huduma hii ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende pia kwenye suala la afya katika Wilaya hiyo hiyo ya Namtumbo. Hospitali hiyo inajengwa kwa takribani miaka mitano sasa na haijakwisha. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza, hospitali hii ya Wilaya ya Namtumbo bado ina jengo la OPD tu, hakuna wodi wala hakuna theatre.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Namtumbo ni wilaya kubwa sana na imejumuisha kata nyingi, zaidi ya kata 23, bado wilaya hii inahudumia pia mji mdogo wa Lusewa; Wizara ingefanya jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba hospitali hii ya Wilaya inakwisha ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa sababu akinamama wengi wajawazito wanapata shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hizi kata zilizopo pale katika Wilaya ya Namtumbo nyingi zimekuwa kwenye maeneo ya mbali. Unakuta kutoka kwenye kituo au Makao Makuu ya Wilaya kwenda kwenye maeneo ya pembezoni, maeneo mengine yanafikia kama kilometa 100, kilometa 70 na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwenye Wilaya hii ya Namtumbo, kwa maana ya Hospitali ya Wilaya, angalau ingekamilishwa wodi ya akinamama ili kuweza kuwafanya akinamama waweze kujifungua salama. Kwa mfano; kuna kituo hiki cha Lusewa; Kituo hiki cha afya cha Lusewa kimekuwa kikihudumia wanawake ambao wakati mwingine wakizidiwa wanajikuta wanalazimika kwenda katika hospitali ya Mbesa ambayo iko karibu kilometa 150 kutoka Wilayani Namtumbo na usafirishaji wa akinamama hawa wakishakuwa kwenye hali mbaya mara nyingi wamekuwa wakibebwa na pikipiki. Yanatengenezwa matenga huku nyuma, wanawekwa kwenye matenga ili waweze kusafirishwa ili kufikishwa kwenye hospitali ya Mbesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, mama yangu Ummy, naomba asikie kilio hiki cha wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ili waweze kusaidiwa kwenye eneo hili ambalo imekuwa ni eneo tete sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende pia kwenye Wilaya ya Tunduru katika zahanati ya Legezamwendo. Zahanati ya Legezamwendo ni zahanati ambayo imezungukwa na vijiji karibu sita; zahanati hii bado haijakamilika na sasa hivi tayari inakaribia miaka minne. Niombe basi zifanyike jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba fedha zinakwenda ili zimalizie zahanati ile ili iweze kutoa huduma kwa wananchi ambao kimsingi baadhi yao tayari wameshapewa hata zile kadi za CHF ili waweze kuzifanyia kazi hizo kadi zao na waweze kupata huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru. Hospitali ya Wilaya ya Tunduru ni ya muda mrefu sana ambayo inahudumia karibu Halmashauri mbili zenye zaidi ya Kata karibu 54; na unapoambiwa Kata zaidi ya 54 kwa Wilaya ya Tunduru ni eneo la kilometa za mraba nyingi mno kiasi ambacho kutoka kituo kimoja mpaka kufika Hospitali ya Wilaya ni parefu mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Tunduru iweze kuboreshwa ili wale wote wanaopata huduma katika hospitali ile waweze kupata huduma stahiki. Ingawaje sasa katika hospitali hiyo kumekuwa na mrundikano mkubwa sana wa wagonjwa kiasi ambacho hospitali inazidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati tunaendelea kufanya miundombinu mingine, nadhani tuanze na hii Hospitali ya Wilaya tuiangalie ili tuweze kupata theatre; theatre ipo lakini ipanuliwe zaidi ili kuendelea kuboresha huduma hizi. Pia madawa na vifaa tiba viongezeke mara dufu ya vile vinavyotolewa sasa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
The Finance Bill, 2016
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Muswada wa Sheria ya Fedha 2016. Nimefurahi sana baada ya Serikali kuona umuhimu wa kukusanya kodi ya majengo na kutokuziachia Halmashauri zetu ziendelee kukusanya. Ni wazi kwamba hata wenzangu watakuwa ni mashahidi pesa nyingi sana zilikuwa zinapotea zilizokuwa zinatakiwa kukusanywa kwenye majengo hasa zilipokuwa zinakusanywa na Halmashauri, kwa sababu Halmashauri zetu zilikuwa zinatumia utaratibu wa kuweka wazabuni ambao wanakusanya pesa. Kimsingi wazabuni ndiyo walikuwa wananufaika na kuziacha Halmashauri zetu zikiwa mbavu za mbwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kidogo kwenye eneo hili kwa maana ya maboresho, ukiangalia katika marekebisho haya namna ambavyo nimeona kwenye ukurasa wa nne, kipengele cha sita imeeleza bayana kwamba TRA ndiyo itakayokwenda kukusanya hizi pesa. Pesa hizi zitakapokuwa zimewekwa kwenye Mfuko Maalum mwisho wa siku zitarudishwa kama zilivyo kwenye miji yetu kama ilivyokuwa imeanishwa au kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili naomba niseme yafuatayo:-
Ukiangalia katika miji mikubwa mfano Mji wa Dar es Salaam, ni mji ambao unakua kwa kutegemea michango ya kodi za maendeleo kutoka katika Mikoa mbalimbali ya Pembezoni. Mikoa ya pembezoni ni watu ambao wanakusanya kodi kupitia aidha kilimo, wengine kwa shughuli nyinginezo. Kwa Mkoa wetu wa Ruvuma, wakulima wa korosho, tumbaku pamoja na mahindi ndiyo ambao wamekuwa wakichangia hata ikafikia Mkoa wa Dar es Salaam sasa unaweza kuwa na miundombinu mizuri. Kwa mfano tunajenga fly over, lakini pia tumejenga daraja lile la Kigamboni pamoja na barabara zilizopo katika Mkoa wa Dar es Salaam na miradi mingine yote mikubwa inajengwa pale kwa sababu ule ndiyo Mji Mkuu wa Tanzania, kwa hiyo, lazima uwe na sura nzuri ambayo inavutia wawekezaji kwenda kuwekeza katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kodi hizi zinazokusanywa kutoka katika maeneo mbalimbali kwenye mikoa yetu ndiyo zinawezesha Jiji la Dar es Salaam kupata wawekezaji wengi na kuonekana kwamba, Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam ndiyo zitakusanya pesa nyingi sana kwenye maeneo haya ya kodi ya majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukusanya pesa hizo wao wataendelea kustawi, Halmashauri zao zitaendelea kustawi, wakati Halmashauri zingine za pembezoni zitakuwa zinasinyaa kwa sababu zenyewe chanzo chao cha mapato kinategemea hasa kilimo na miundombinu yake bado haijawa wezeshi ili kuwezesha aidha kuweka viwanda, aidha kuvutia wawekezaji wa aina mbalimbali kuja kuwekeza kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sasa Serikali ifanye yafuatayo kwa maana ya ushauri wangu. Nadhani kwamba baada ya TRA kukusanya pesa na zikawekwa kwenye Mfuko, basi pesa zile zikagawiwe sawa kwa sawa kwenye Halmashauri mbalimbali katika nchi yetu, ili kuziwezesha Halmashauri nyinginezo ambazo zina hali duni, ziweze na zenyewe kuchipua, ziweze kufikia hatua ambayo itawavutia wawekezaji kwenda kuwekeza kwenye maeneo yao, kwa sababu tayari wataweza kutengeneza miundombinu ambayo itakuwa wezeshi na miundombinu ambayo itakuwa ni kivutio kwa wawekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisisitize sana kwenye eneo hili, ukizingatia katika Wilaya yangu ya Tunduru, wamekuwa wakizalisha na pato kubwa sana linatokana na zao la tumbaku, halikadhalika Namtumbo wamekuwa wakizalisha tumbaku, wanapata pato kubwa sana ambayo inawezesha katika Serikali hii, lakini pia hata wenzetu wanaolima mahindi Songea Mjini, Songea Vijijini nao pia wamezalisha sana kupelekea hili pato kuendelea kukua na kuendesha mikoa mingine. Halikadhalika…
NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa…
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, haya yakizingatiwa itapendeza sana. Naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Muswada wa Sheria wa Upatikanaji wa Habari wa mwaka 2016.
Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wenzetu Kamati ya Katiba na Sheria ambao waliona umuhimu wa kuleta sheria hii ili tuweze kuichanganua kadri tutakavyoweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba pia niwapongeze sana wadau wote walioshiriki kuchakata sheria hii wakiwemo Chama cha Wanasheria, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Sekretarieti ya Msaada wa Sheria, Baraza la Habari Tanzania na wadau wengine wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba ni jambo jema sana ambalo limeletwa kwetu kwa misingi ya kwamba kutokana na hali halisi juu ya upatikanaji wa habari ambao umekuwa ukiendelea katika nchi yetu, kumekuwa na haja kubwa sana ya kuleta sheria hii na kuweza kuifanyia marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa habari sasa hivi katika nchi yetu umekuwa ni wa kiholela tu, kila mtu anajiamulia kadri anavyoweza na anaweza akaamua tu akaanzisha habari yoyote ile isiyokuwa na uhakika; lakini pia Taifa letu tayari limeshaingia kwenye hali ya kuwa kila siku kunakuwa na habari zinaibuka na hatimaye tunakuwa na kazi ya kukanusha kanusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachelea kusema habari ambazo zinakuja kinyume na utaratibu ambazo hazijahakikishwa na hatimaye kutolewa, unaweza kusema ni sehemu ya umbea tu. Kwa sababu imeonekena kwamba habari nyiungi sana za kulipuka zinatupiwa kwenye magazeti, zinawafanya watu waweze kuuza magazeti tofauti na hali halisi ambayo inatakiwa iende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii itakwenda sasa moja kwa moja kumbana mtoa habari. Itakwenda kumbana mtu ambaye anayekwenda kutoa taarifa ambayo siyo. Kwa mfano, labda niseme tu, siyo muda mrefu kama mwezi mmoja na nusu au miwili imepita, nadhani wenzangu watakuwa mashahidi, kulikuwa na habari ambayo ilitupiwa kwenye mtandao kwamba Jerry Muro amekuwa ni Kaimu Mkurugenzi Ikulu, lakini ni jambo ambalo lilikuwa siyo la kweli. Hatimaye akasema kwamba amekuwa Kaimu Mkurugenzi na Greyson Msigwa amekuwa Mkurugenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hizi zilikuwa siyo za kweli, badala yake sasa Serikali ikaanza kufanya kazi ya kukanusha jambo hilo. Sasa hatuwezi kuwa na Taifa ambapo kila siku ni kupeleka habari, mtu anaamua tu; kesho yake mtu anaanza kukanusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni jambo ambalo kimsingi limempata dada yangu Mheshimiwa Magdalena Sakaya. Leo hii mmeshuhudia yeye mwenyewe anakanusha hapa. Wameshatengeneza habari kwamba amefukuzwa Chama cha CUF, jambo ambalo siyo kweli.
Kwa hiyo, tutakapokwenda kuitengeneza hii sheria na tukaiweka sawa sawa, itakuwa inasimama pande zote mbili; hakuna ambaye ataathiriwa na Sheria hiyo. Endapo tu kama mtu ataona yeye anahitaji kufanya hivyo, basi atakuwa ameamua yeye kwa makusudi na sheria itakuwa inachukua mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nataka tu niwakumbushe wenzangu; juzi tumepata habari nyingine, eti Makamu wa Rais anataka kujiuzulu. Yaani ni mtu ameibuka tu anaanzisha kitu from no where. Kwa hiyo, 81
nadhani hii sheria ni vizuri tukaenda kuipitisha wote kwa pamoja ili kuepuka vitu ambavyo mtu anaweza akaibuka tu akajifanyia bila sababu za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeshuhudia juzi hapa tunaambiwa kwamba Mheshimiwa Freeman Mbowe ametolewa vitu vyake National Housing, jambo ambalo halina ukweli kwa sababu yeye mwenyewe amekuja amekanusha. Eti kwamba anadaiwa shilingi bilioni 1.6. Amekanusha na akasema kwamba anaenda mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sheria hii tukiisimamia vizuri, itacheza pande zote mbili ili kuwafanya watu katika nchi yetu tusiwe na ile hali ya kulipuka, kila mmoja anaamua from no where tu, mtu aanzisha habari yake, halafu tunarudi kwenda kukanusha; na tuone hii adha kwamba, badala ya kufanya shughuli nyingine basi tunaanza kuingia kwenye shughuli za kukanusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba naomba nikubaliane na kipengele ambacho kinasema, Sheria ya Usalama wa Taifa isiguswe. Mtu akitoa taarifa upande wa Usalama wa Taifa, mimi nikubaliane na kipengele hiki kwa Sheria ya mwaka 1970, chini ya Ibara ya (6) kwamba mtu huyu kwa kweli achukuliwe hatua za kisheria na aweze kufungwa miaka 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye amendment kwamba imefanyiwa marekebisho, badala ya kiama 20 na 15, basi mtu anaweza akafungwa kifungo cha miaka mitatu mpaka mitano. Mimi napendekeza miaka 15 na 20 ibaki pale pale badala ya kupunguzwa. Kwa sababu watu wengine watafanya kwa makusudi. Anakwenda kwa makusudi kutoa taarifa za usalama wa nchi ili nchi yetu iingie kwenye janga kubwa; na watu wengine wako tayari hata kujitoa mhanga. Kwa hiyo, miaka mitatu au miaka mitano ni kitu kidogo sana. Naomba kama inawezekana, hili jambo libaki pale pale na hii adhabu ibaki pale pale kwa maana ya miaka 15 mpaka miaka 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kumshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo imefika mahali ambapo sisi na wenzetu watani wetu tuko pamoja humu ndani. Ni jambo ambalo niseme tu wenzetu hawa tuliwa-miss sana na waliporudi sisi tuna amani na kimsingi wao wenyewe waliamua kuziba na baadaye wamezibua wenyewe.
Karibuni sana ndugu zetu, tuendelee kuchakata hizi sheria ili tuendelee kuwa pamoja, tuendelee kushirikiana kwa mustakabali wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye amenijalia kusimama hapa siku hii ya leo. Pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii adhimu ili nami niweze kuchangia Muswada wa Sheria ya Kuanzishwa Taasisi ya Kilimo ambayo inaitwa TARI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu, nashauri kwamba Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa pamoja tukubaliane ili tuweze kupitisha sheria hii iweze kuanza kufanya kazi ili watafiti waweze kunufaika na sheria hii.
Lengo la Muswada huu, kwa maana ya sheria hii ni kusimamia tafiti zote za kilimo Tanzania nzima. Kwa kuwa sheria hii ilikuwa haijaundwa, basi ilikuwa inapelekea, watafiti wanapoanzisha utafiti, mwisho wa siku wanashindwa kufika mwisho na utafiti ule ulikuwa hauzai matunda yoyote. Kwa hiyo, ulikuwa haumnufaishi mwananchi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme tu, utafiti uliokuwa ukifanywa ulikuwa siyo mzuri kiasi ambacho kwenye maeneo mbalimbali tumeshuhudia. Kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Ruvuma, mbegu ambazo zimeletwa kwa maana ya uzalishaji wa mahindi ni mbegu za ajabu sana. Unashangaa kuona kwamba mhindi unakuwa kufikia futi moja na nusu eti ndiyo unachanua. Sasa huo muhindi unaochanua hivyo ni wazi kwamba unakwenda kubeba kipande cha mhindi kidogo sana. Kwa hiyo, hizi mbegu nyingi ambazo zimekuwa zikiletwa kwetu siyo nzuri, hazifai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nadhani kwa kufanya maboresho na kwa kupitisha sheria hii sasa itakwenda kuhakikisha kwamba tunapata watafiti ambao watakwenda kufanya utafiti mzuri na kuweza kuongeza mapato katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia imeonekana kwamba Maafisa Ugani wapo tu jina, hawana kazi yoyote ambayo wanaifanya ya kuweza kuboresha mazao katika maeneo yetu ambayo tunaishi. Wapo wapo tu, wanapokea mishahara lakini kazi zile za msingi sisi hatuzioni. Kwa sababu kama mbegu ya mhindi inaletwa inafikia futi moja halafu inabeba mtoto pale; ni sawa sawa hata sisi akinamama, mwanamke ambaye anaweza akatotoa mtoto mzuri kweli kweli ni yule ambaye angalau anakuwa na urefu kiasi fulani, ingawa hata yule mfupi anaweza akatoa mtoto ambaye anafaa; lakini niseme tu kwamba mbegu ambayo inakuwa imekua kwa maana ya mahindi, ndiyo ambayo inaweza ikabeba mtoto mzuri. (Minong’ono)
Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sana, sina maana mbaya kwa wale wafupi, ni kwa ajili tu ya kuchambua ili nieleweke kwenye eneo hili la suala la mbegu. Tupo pamoja, naomba Waheshimiwa Wabunge wasinielewe vibaya. (Makofi/Kelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na Maafisa Ugani, Maafisa Kilimo na wenyewe wapo lakini hizi mbegu zinakuja feki hawasemi chochote, wapo tu wamekaa. Kwa hiyo, suala la utafiti ni muhimu, naomba tupitishe hii sheria ili tuweze kupata mazao mengi na mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme faida ya kuhakikisha kwamba tunapitisha hii sheria, maana yake, uzalishaji utaongezeka. Pia teknolojia mpya dhidi ya kilimo zitagundulika kutokana na utafiti huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Taasisi ya Uvuvi kwa maana ya TAFIRI. Hapa kwenye suala la uvuvi utafiti huu utasaidia kuongeza uzalishaji wa viumbe hai kwenye mito, maziwa au bahari. Ni utamaduni ambao umezoeleka, watafiti wetu mara nyingi sana walikuwa wanajikita kwenye bahari na kwenye maziwa, lakini sijaona watafiti wanafanya utafiti wa uzalishaji wa samaki kwenye mito; sijaona watafiti wamejikita kisawasawa kwenye uzalishaji wa samaki kwenye mabwawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watafiti wakijipanga vizuri, zao la uvuvi wa samaki linaweza likatusaidia kwa asilimia kubwa sana kuinua kipato katika nchi yetu. Niseme tu, kule kwetu huwa tunachimba na visima hivi vya maji; lakini unaona kisima wamekichimba kienyeji tu, baada ya miezi mitatu ukienda kusafisha unakuta kambale wamejaa kibao. Hivi hawa kambale, au hawa watafiti wetu hawawezi kuingia huko wakafanya utafiti wa kina wakatengeneza mazingira, hatuwezi kupata samaki wengi jamani? Hatuwezi kuinua kipato! Kwa hiyo, niseme tu huu utafiti na hii sheria tukiipitisha, itakwenda kuwasaidia watu wetu wafanye utafiti wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile mito iliyopo; Tanzania tunasema ni nchi tajiri ambayo ina mito na mabonde. Mito mingine jamani kwa haki ya Mungu imeamua tu sasa ijikaukie tu, kwa sababu hakuna jambo lolote linalofanyika dhidi ya hiyo mito, ipo tu. Zipo nchi ambazo, yaani mtoto anatolewa darasani kupelekwa kwenye mto ili awe kama anatembelea mto aone unafananaje; lakini huku kwetu hatua 20 mto, ukienda kilometa ngapi, mto; lakini ile mito imekaa tu, haifanyiwi utafiti wowote, hakuna kitu chochote ambacho inazalisha, mwisho wa siku inaamua ijikaukie tu. Nao uumbaji wa Mwenyezi Mungu kama huutumii, basi inaamua ijikaukie tu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani sheria hii tukiipitisha itaongeza mazao katika suala la uvuvi, lakini pia itaongeza kipato na itaongeza lishe. Pia niseme, mimi sio daktari, lakini utafiti umeonesha kwamba samaki anaongeza afya nzuri sana, lakini pia inasaidia hata ukuaji wa ubongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukilalamika hapa tunasema watoto wengine hawana afya bora, nadhani kama tutaboresha na watafiti wetu wakafanya utafiti wakaona ni samaki wa aina gani, kama tukiwatunza vizuri, tukaona labda katika Nyanda za Juu Kusini kwamba ni samaki wa aina gani wazalishwe; haya, wakaenda labda kwa mfano, kwenye centre hii tuliyopo hapa Dodoma ni samaki wa aina gani wazalishwe ili samaki hawa sasa wawe wanazalishwa kila maeneo kwa ajili ya kusaidia lishe, hasa kwa watoto wetu ambao ndiyo tunatarajia kwamba ndiyo zao la watoto wetu wanaoanza sasa waweze kupata samaki wale, ili waanzie hapo sasa kuboresha afya zao na kukuza vizuri kwa ufasaha zaidi ubongo wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu tunachokihitaji siyo tu uwezo wa kufaulu darasani, lakini tunataka mtoto mwenye akili ambaye anaweza akafanya utafiti mzuri kwa kutumia ile akili yake. Kwa hiyo, kama ukitaka tu kwa kufaulu, mtu mwingine anaweza akachungulia kwa mwenzake akafaulu. Tunataka watoto ambao kweli wana afya bora kwa kupitia huu uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani pia katika sheria hii iundwe panel ili iweze kwenda kusaidia kuwasimamia hao watafiti watakaokuwa wanaenda kufanya utafiti. Badala ya kujifanyia utafiti tu kiholela, ikafika mahali mtu ameshapiga mpunga wake, ameweka mfukoni, hana haja ya kuendelea na utafiti, anasema tu kwamba nimeishia hapo na wala hakuna sheria ambayo atachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme hii panel itakayokuwa inasimamia itatazama mwenendo wa wale watafiti, mwisho wa siku kabla hawajamaliza utafiti wao, wanaweza wakafikia nusu na wakaambiwa kwamba kwa utafiti wenu huu, tumeona kwamba hamtoshelezi na…
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri.