Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi) (8 total)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Kumekuwa na changamaoto kubwa katika Mkoa wa Ruvuma ambapo vocha na pembejeo za kilimo zinazotolewa zimekuwa hazitoshi na wakati mwingine kuleta mgogoro kwa wananchi wenyewe kwa wenyewe:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza pembejeo za ruzuku katika Mkoa wa Ruvuma?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isiondoe kodi kwenye pembejeo ili wananchi waweze kununua wenyewe pembejeo hizo kwa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Ruvuma umekuwa ukipata ruzuku ya pembejeo za kilimo tangu msimu wa 2003/2004 hadi sasa ambapo takribani kaya 80,000 kila mwaka zimekuwa zikinufaika na ruzuku hiyo mkoani humo. Kutokana na changamoto za mfumo wa utoaji wa ruzuku za pembejeo kama vile kuchelewa kwa pembejeo, ubadhirifu, bei kubwa na kadhalika wakulima wachache wamekuwa wakinufaika na ruzuku hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuweza kuwafikia wakulima wengi zaidi katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Ruvuma, Serikali inaangalia upya utaratibu wa kutoa ruzuku bila kujali makundi ambao utawezesha wakulima wengi zaidi kunufaika na ruzuku ya pembejeo. Utaratibu huo utakapokamilika umma wa Watanzania utajulishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kodi za import na excise duties zimefutwa kwa pembejeo za kilimo zinazoagizwa kutoka nje ila bado kuna tozo za bandari na taasisi mbalimbali kama vile TBS, SUMATRA, Taasisi ya Mionzi na kadhalika ambapo baadhi ya tozo hizo ndani yake kuna VAT. Aidha, Halmashauri bado zinatoza cess kwenye mbegu zinazozalishwa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha bei za pembejeo zinakuwa nafuu, Serikali inaangalia uwezekano wa kuondoa au kupunguza tozo mbalimbali kwenye pembejeo zote za kilimo ili kuwawezesha wakulima wengi kununua pembejeo hizo kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inaendelea kuweka msisitizo kwa wawekezaji wa nje na wa ndani kuanzisha viwanda vya mbolea na pia kuwekeza katika mashamba ya kuzalisha mbegu hapa nchini. Lengo kubwa likiwa ni kuwapatia wakulima pembejeo za kutosha na kwa bei nafuu ili kuongeza uzalishaji.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Katika Ilani ya CCM 2016/2017 Serikali imeahidi kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja:-
Je, ni lini Serikali itaanza kutoa fedha kiasi cha shilingi 50,000,000 kwa kila Kijiji au Mtaa ili kuwasaidia wananchi kuboresha mitaji yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 59.5 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 chini ya Fungu 21, kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 ya kupeleka shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Fedha hizo zitatolewa baada ya kukamilisha taratibu mahususi zinazolenga kuhakikisha uwepo wa tija, katika matumizi ya fedha hiyo. Hivyo namwomba Mheshimiwa Mbunge Jacqueline, asubiri utekelezaji wake kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017. Mara baada ya kukamilika kwa mfumo na muundo wa utekelezaji wa zoezi zima, ambapo kazi hii imeshaanza kufanyika.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Wilaya sita zenye Majimbo tisa ya uchaguzi, unakabiliwa na tatizo kubwa la maji:-
Je, ni lini Serikali itapeleka maji safi na salama katika Mkoa wa Ruvuma?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa utekelezaji wa miradi ya maji vijijini ulioanza mwaka wa fedha 2006/2007, Mkoa wa Ruvuma ulipangiwa vijiji 80. Kati ya vijiji hivyo, vijiji 76 vilipata vyanzo vya maji na Vijiji vinne vya Mchoteka, Nakapanya, Mtina na Muhuwesi katika Halmashauri ya Tunduru vilikosa vyanzo. Miradi ya maji katika vijiji 43 imekamilika na miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Mkoa wa Ruvuma umetengewa jumla ya shilingi bilioni 13.17 kwa ajili ya miradi ya maji vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea na mipango ya kuboresha huduma ya maji katika Miji ya Songea, Mbinga, Namtumbo na Tunduru ya Mkoa wa Ruvuma. Kwa Mji wa Songea, Serikali imekamilisha mradi wa ukarabati wa chanzo cha maji cha Mto Ruhila Darajani kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6 ambapo umeongeza kiasi cha maji lita milioni sita kwa siku. Mradi huo umekamilika mwezi Februari, 2016 na sasa upo kwenye majaribio. Kukamilika kwa mradi huo kumewanufaisha wakazi 164,162 wa Manispaa ya Songea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango wa muda mrefu Serikali imekamilisha usanifu wa kina na uandaaji makabrasha ya zabuni kwa ajili ya uboreshaji huduma ya maji katika Miji ya Tunduru, Namtumbo na Mbinga. Utekelezaji wa miradi hiyo utagharimu Dola za Marekani milioni 7.3 kwa Mji wa Tunduru, Dola milioni 12.08 kwa Mji wa Namtumbo na Dola milioni 11.86 kwa Mji wa Mbinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA (K.n.y. MHE. JACQUELINE
N. MSONGOZI) aliuliza:-
Barabara ya Makambako - Songea yenye urefu wa kilometa 295 imeharibika sana na inahitaji kufanyiwa matengenezo.
Je, ni lini Serikali itakarabati barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuifanyia ukarabati kwa kiwango cha lami barabara ya Makambako hadi Songea yenye urefu wa kilometa 295 ili kupunguza gharama na muda wa kusafiri kwa watumiaji wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania –TANROADS, tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na utayarishaji wa nyaraka za zabuni. Lengo la kazi hiyo ni kuikarabati barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kazi hii imefanyika kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati kwa kiwango cha lami barabara ya Makambako hadi Songea. Aidha, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania inaendelea kuifanyia matengenezo barabara hii kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ili iendelee kupitika wakati Serikali inatafuta fedha za kuifanyia ukarabati kamili.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Wakati Rais akiwa katika kampeni aliahidi kuwa ataondoa ushuru na kodi ndogo ndogo zinazoleta usumbufu kwa wajasiriamali wadogo wadogo kama vile machinga, wachuuzi wa mboga mboga na matunda, mama lishe, waendesha bodaboda na kadhalika, lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya uamuzi wa kufuta ushuru unaotozwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi wakiwemo mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mboga mboga, ndizi na matunda. Vile vile, wafanyabiashara walio nje ya maeneo maalum ya kibiashara wenye mitaji chini ya shilingi 100,000 hawaruhusiwi kulipa ada, tozo na kodi za aina yoyote.
Mheshimiwa MWenyekiti, uamuzi huu umeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 1 Julai 2017 baada ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2017 iliyotangaza kufuta ushuru na kodi kero kwa wafanyabiashara wadogo wadogo. Hatua inayoendelea sasa hivi nikuwatambua wafanyabiashara wadogo wote ili kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya. Hivyo, Serikali imetekeleza kwa vitendo ahadi hii iliyoko katika Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2015 inayolenga kuwapatia unafuu wa maisha wananchi wa hali ya chini kiuchumi ili waweze kukua na kuchangia vizuri katika uchumi wa Taifa lao. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Kiwanda cha SONAMCU kilichopo Songea Mjini?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuwaongezea gawio la uzalishaji wa tumbaku wananchi wa Wilaya ya Namtumbo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania ambayo ni msimamizi wa vyama vya Ushirika Tanzania imewezesha kukamilisha mkataba kati ya mnunuzi mwingine wa Tumbaku Kamouni ya Premium Active Tanzania Limited na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Songea na Namtumbo (SONAMCU Ltd.) wa miaka saba na mkataba huu umeboreshwa zaidi kwa kuweka kipengele cha tumbaku yote inayozalishwa Songea lazima isindikwe katika Kiwanda cha Tumbaku kilichopo Songea Mjini. Mkataba huu tayari umeshasainiwa na umeshaanza msimu huu wa mwaka 2018/2019 ambao utadumu kwa miaka saba hadi mwaka 2025/2026. Vyama vyote vya msingi vimeingia mkataba na Chama Kikuu cha Ushirika (SONAMCU) ili kudhibiti tumbaku yote itakayozalishwa Songea na Namtumbo kusindikwa katika kiwanda cha tumbaku kilichopo Songea Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi huu wa Februari, kampuni hii itawaleta wahandisi wawili kutoka nchi ya Italia ambao watafika Songea na kushirikiana na Mkoa ili kuandaa gharama halisi za ukarabati na mtambo mwingine utakaoagizwa Italia ili tumbaku yote itakayozalishwa kuanzia msimu huu wa 2018/2019 isindikwe katika Kiwanda cha Songea Mjini. Serikali ina matumaini kuwa kiwanda hiki kitafunguliwa na kuanza upya kazi ya usindikaji wa tumbaku ifikapo mwezi Julai, 2018 hivyo kuwezesha kutoa ajira kwa wananchi zikiwemo ajira za kudumu na za msimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa ununuzi wa tumbaku uliopo sasa kati ya SUNAMCU na Premium Active Tanzania Limited umeanza kuongeza uzalishaji wa tumbaku kwa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo kutoka kilo 250,000 za mwaka 2017/2018 hali kufikia kilo milioni moja kwa mwaka 2018/2019. Aidha, mkataba unaonesha kila mwaka kutakuwa na ongezeko la uzalishaji wa tumbaku kutoka kwa mnunuzi aliyeingia mkataba kufuatana na ubora na mahitaji ya soko la nje ya nchi.
Hata hivyo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira na fursa ya wanunuzi wengine watakaojitokeza wenye mahitaji ya tumbaku. Ikumbukwe kuwa ongezeko hutokea endapo tu kuna mwenendo mzuri wa biashara katika soko na ongezeko la uzaishaji. Ahsante sana.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Mji Mwema katika Manispaa ya Songea kinahudumia watu zaidi ya laki mbili lakini kinapata mgao wa dawa sawa na vituo vingine vya afya:-
(a) Je, Serikali ina mpango wa kukiongezea dawa kituo hiki ili kipate mgao wa dawa na vifaa tiba kama Hospitali ya Wilaya?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha vifaa vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mji Mwema?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafanya mgawanyo wa fedha za dawa kulingana na idadi ya watu wanaopata huduma katika kituo husika. Takwimu za Wizara za mwaka 2015 zinaonesha kituo hicho kinahudumia wananchi 20,000. Kama kuna mabadiliko ya idadi ya wananchi wanaopata huduma katika kituo hiki ni vyema takwimu hizo ziletwe Wizarani na Mganga Mkuu wa Wilaya husika ili marekebisho yaweze kufanyika. Kwa kuwa hiki ni Kituo cha Afya, hakitapata mgao kama Hospitali ya Wilaya mpaka pale ambapo kitapandishwa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kukamilisha upatikanaji wa vifaa vya upasuaji wa Vituo vya Afya nchini kikiwemo cha Mji Mwema chini ya mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mpango huu ni wa miaka mitatu na umelenga kupunguza vifo vya akinamama kwa asilimia 20. Katika kipindi hicho cha 2015 – 2018, Vituo vya Afya nchini vitaboreshwa ili kutoa huduma za upasuaji hasa kwa akina mama ambao wameshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida. Serikali pia itaboresha idadi ya wataalam na upatikanaji wa dawa hasa za mpango wa mama na mtoto.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Benki ya Kilimo ipo kwa ajii ya kumwezesha mkulima wa Tanzania aweze kufanya uwekezaji wenye tija katika kilimo:-
(a) Je, ni lini Serikali itapeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma ili wananchi waweze kukopeshwa?
(b) Je, Serikali ipo tayari kupunguza riba kwa pesa anayokopeshwa mkulima kutoka katika benki hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango Kazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania wa miaka mitano (2017 – 2021), benki inakusudia kuanzisha Ofisi za kikanda katika Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini pamoja na Zanzibar. Kutokana na ufinyu wa rasilimali fedha, benki itatekeleza mpango wake wa kusogeza huduma karibu na wateja wa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia 30 Juni, 2018, Ofisi ya Kanda ya Kati itakuwa imefunguliwa ambayo pia itakuwa ni Makao Makuu ya Benki ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ufunguzi wa Ofisi ya Kanda ya Kati kukamilika, benki itafanya uchambuzi wa fursa zilizopo kikanda na hivyo kuchukua hatua na taratibu za kufungua Ofisi nyingine kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania inatoa mikopo kwa kutumia mfumo wa makundi:-
(i) Kundi la kwanza ni wakulima wadogo wadogo kwa riba ya 8% – 12% kwa mwaka;
(ii) Kundi la pili ni la miradi mikubwa ya kilimo kwa 12% – 16% kwa mwaka;
(iii) Kundi la tatu ni wanunuzi wa mazao kwa 15% – 18% ; na
(iv) Kundi la mwisho ni mikopo ya ushirika ambapo riba yake inaendana na hali ya soko na matumizi ya mkopo huo. Hata hivyo, majadiliano kuhusu kiwango cha riba yanaweza kufanyika kulingana na historia ya mkopaji.