Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi) (8 total)

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ambayo kimsingi sijaridhishwa nayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo, nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Ruvuma una wakazi zaidi ya watu 150,000 na ruzuku/vocha zinazotolewa kwa maana ya pembejeo za kilimo ni karibu kwa watu 80,000 ni wazi kuwa hazikidhi haja. Swali langu, naomba anieleze leo ni lini Serikali itaondoa angalau ushuru kwa maana ya cess kwa wakulima ili pale wanapotoa mazao yao shambani wasitozwe tozo yoyote ile?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mawakala wa pembejeo za kilimo ambao wamehudumia kwa maana ya kuikopesha Serikali kwa msimu wa mwaka 2015/2016 mpaka sasa hawajalipwa pesa zao. Naomba Waziri anipe majibu mazuri na ya kina kwamba ni lini Serikali itawalipa mawakala hawa ambao wamehudumia wananchi katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma za Nyasa, Mbinga, Songea, Namtumbo pamoja na Ruvuma ikiwepo pia hata maeneo mengine yote ya nchi yetu ya Tanzania? Hawa watu wanafanya biashara kwa kukopa kwenye benki na sasa hivi imefika mahali wanashindwa kurejesha mikopo yao. Naomba anipe majibu ya kina.
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini Serikali itaondoa ushuru, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Finance Bill inayotegemewa kuja katika Bunge hili tumependekeza kwa Wizara ya Fedha, baadhi ya hizo tozo ziondolewe. Kwa hiyo, tunategemea tutakapoleta Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze tu kwamba kuna tozo nyingi ambazo zimekuwa zikiongeza bei ya pembejeo kwenye mjengeko wa jumla ambazo nyingi kwa kweli zinaleta matatizo kwa wakulima na tutahakikisha nyingi zitaondolewa. Vilevile tufahamu kwamba suala la kodi ni la kisheria, kwa hiyo, kuna baadhi ya kodi ambazo tutaziondoa taratibu lakini kimsingi Wizara yangu ipo kwenye utaratibu mzima wa kuhakikisha kwamba baadhi ya hizi kodi zinaondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la mawakala ambao hawajalipwa, nikiri kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna mawakala ambao hawajalipwa mpaka sasa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kuwa tayari Wizara imejipanga kuhakikisha kwamba tunamaliza madeni yote ya mawakala ili wasiendelee kupata vikwazo kama wanavyopata, wengi wanauziwa mali zao kutokana na mikopo. Tunawasihi mawakala wote wapeleke certificate zao kwa sababu tayari utaratibu wa kuwalipa unaandaliwa. Nashukuru sana.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la gati lililopo katika Wilaya ya Geita linafanana kabisa na tatizo la gati lililoko katika Wilaya ya Nyasa. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Gati ya Ngumbi katika Ziwa Nyasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani nadhani ni Ndumbi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:Mheshimiwa Naibu Spika, gati linaloongelewa kama ambavyo mmeona linamuhusu sana Naibu Waziri anayehusika na masuala ya Elimu; na kwa kweli nilishuhudia mwenyewe wakati nilipoenda kukagua ile gati ambayo inatumika kupakia mkaa wa kutoka Ngaka kwamba tunahitaji kufanya mambo mazito pale ili ile biashara ambayo tayari imeshapanuka iweze kufanyika kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, anafahamu Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Jacqueline Msongozi kwamba katika bajeti hii ambayo nawashukuruni sana Waheshimiwa Wabunge; na mnisamehe jana nilipa matatizo kidogo kuona kwamba mmeniwezesha kuanza kujenga reli na miundombinu mingine nikatoa kwa sauti kubwa sana kuunga mkono bajeti, nanyi mkapitisha; pamoja na hii gati ambayo ipo ina bajeti tutaisimamia kuhakikisha inakamilika na kile tunachokusudia kitendeke pale Ndumbi kiweze kukamilika.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza, Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa yenye wananchi wengi sana na katika vijiji ambavyovimeainishwa kwa ajili ya kupewa mikopo hiyo, kila kijiji kina wastani wa wananchi 5,000 ambao wana uwezo wa kufanya kazi za uzalishaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa mikopo yenye tija wananchi hao?
Swali la pili, kama wanakijiji watapata shilingi 1,000 kila mmoja itakayotokana na shilingi milioni 50. Je, watawekeza kwenye biashara gani ili wapate faida kwenye uwekezaji huo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kumpongeza sana huyu Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma kwa kazi nzuri na jitihada kubwa anayoifanya ya uwakilishi ndani ya Bunge na hasa kuwawakilisha Watanzania wote, lakini hasa hasa wanawake wa Mkoa wa Ruvuma nampongeza sana. Mheshimiwa Mbunge ameniuliza maswali mawili la kwanza ameonyesha idadi ya watu jinsi ilivyo, katika maeneo mbalimbali kwenye Vijiji vya Mkoa wa Ruvuma, akitaka kujua kama tuna mpango mahususi katika Serikali wa kuhakikisha vijiji hivyo vinapata mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, wakati tukipitisha bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Fungu 65 mradi namba 49, 45 pamoja na hiyo milioni 50. Hata hivyo, Serikali imetenga fedha nyingine bilioni moja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vijana na akina mama wanapata mikopo katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Hata hivyo, Serikali pia kupitia Halmashauri zetu itaendelea kutenga asilimia tano ya mapato kwa ajili ya akinamama na vijana. Kwa hiyo, namhakikishia kwamba nguvu hizo zote zitasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili la nyongeza amesema, pia anakadiria wastani wa shilingi 1,000 kama Mfuko huo utakopeshwa kwa wananchi, kwa idadi ya wananchi ambao wanaweza kuifanyia kazi. Namwomba Mheshimiwa Mbunge asubiri kama nilivyosema, tunatengeneza utaratibu na mfumo mzuri ambao utasaidia kuhakikisha kwamba wakopaji watapata fedha yenye tija na wataweza kufanya kazi na biashara ambazo zitainua kipato kwa familia zao na Taifa zima kwa ujumla.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuuliza Waziri wa Maji, kumekuwa na miradi ya World Bank ambayo ilianza mwaka 2013 na miradi hii baadhi yake huwa inatolewa ripoti kwamba tayari imekamilika ilhali maji hayatoki katika maeneo hayo. Napenda kuainisha maeneo ambayo maji hayatoki ikiwa ni pamoja na kumwomba Waziri mwenye dhamana akubaliane nami baada ya Bunge hili twende pamoja kwenye maeneo hayo ili akajionee yeye mwenyewe adha ambayo wanaipata wanawake kuhusiana na miradi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya ni yafuatayo: Litola na Kumbara ni baadhi tu ya maeneo katika Wilaya ya Namtumbo; Wilaya ya Mbinga kuna mradi wa Mkako na Litoha; Wilaya ya Tunduru kuna Nanembo na Lukumbule; lakini pia katika Manispaa ya Songea kupitia SOWASA Kata ya Ruvuma, Subira, Luwiko, Bombambili, Msamala na Matalawe ni maeneo ambayo maji hayapatikani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningependa baada ya Bunge hili tuweze kuongozana akaone mwenyewe kwa macho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la piliā€¦
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Nahitaji Waziri niongozane na yeye akaone mwenyewe.
Swali la pili, katika Kituo cha Afya cha Lipalamba hakuna maji kabisa na wananchi sasa wameshaanza kujichangisha kwa ajili ya kuchimba mitaro kwa ajili ya kutandika mipira ya mabomba. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutoa fedha kwa ajili ya kununua roll mita 30 kwa ajili ya kutandika pamoja na vifaa vyake vya kuungia?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ameomba kama niko tayari kuongoza naye kwenda kuona maendeleo ya utoaji wa huduma ya maji katika Mkoa wa Ruvuma. Nakubali ombi lake, nitafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili na katika jibu la msingi, tumesema kweli katika vijiji 80 vipo vijiji ambavyo bado miradi haijakamilika na kwamba iko katika hatua mbalimbali. Sasa kuwa na jibu ambalo ni mahususi kujua kijiji gani tumesema imekamilika na maji hayatoki, hii inabidi tuifanyie verification. Haya majibu yanayoletwa inawezekana yakawa sio sahihi, lakini naomba sana Waheshimiwa Wabunge katika vikao vya Halmashauri za Wilaya taarifa hizi za maendeleo ya huduma za maji katika maeneo yale huwa zinatolewa kila robo mwaka, naomba sana tuwe tunahudhuria vikao vile ili tuweze kujua.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kama kuna tatizo la msingi la kisera ambalo Waziri inabidi nijue, naomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuwasiliana ili tuweze kuona namna gani tutamaliza matatizo ya maji kwa wananchi wetu.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, tatizo la mradi wa umwagiliaji la Mufindi Kaskazini linafanana kabisa na tatizo la mradi wa umwagiliaji uliopo katika Halmashauri ya Songea katika Kata ya Subira na katika Mtaa wa Subira. Mradi huu ni
wa muda mrefu, umeanza tangu mwaka 2008 na mpaka sasa hivi bado haujakamilika, pesa zilizotumika mpaka sasa hivi ni shilingi milioni 585 na bado panatakiwa zaidi ya shilingi bilioni moja ili kukamilisha mradi huu. Je, Serikali imetenga kiasi gani kwa ajili ya kukamilisha mradi huu kwa kipindi hiki cha Bajeti ya mwaka 2017/2018?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi mingi ya umwagiliaji ina matatizo. Na ina matatizo kwa sababu, kwanza kulikuwa na udhaifu katika usimamiaji katika sekta hii, hii miradi ya kilimo. Na miradi mingi ilikuwa ina ufadhili wa JICA. Kwa hiyo, kulikuwa na weakness katika usimamizi, yaani ulikuwa dhaifu na ndio maana utekelezaji wake haukwenda kwenye viwango vinavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nikiri tu kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tulitenga fedha kwa ajili ya kufanyia mapitio ya miradi yote ya umwagiliaji, ili kwanza tuweze kuirekebisha iweze kufanya kazi iliyokusudiwa, hiyo ndio kazi ambayo inaendelea sasa hivi.
Lakini pili, tulikuwa tunafanya usanifu wa miradi mipya ya umwagiliaji, sasa kwa sasahivi siwezi kukwambia bajeti ya mwaka 2017 ni kiasi gani, lakini nitakapowasilisha bajeti yangu najua utaunga mkono ili kusudi tuweze kukamilisha huu mradi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kw amajibu mazuri. Pamoja na majibu mazuri hayo napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji huu bado kuna maeneo mbalimbali katika Halmashauri mbalimbali katika Mkoa wangu wa Ruvuma na maeneo mengine kwenye Halmashauri nyingine maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua kali halmashauri ambazo bado wanawanyonya kwa kuwatoza ushuru wajasiriamali wadogo wadogo wote katika Halmashauri zote zilizoko mkoani Ruvuma na maeneo mengine? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wafanyabiashara hao wadogo wadogo wanafanya biashara katika mazingira magumu sana jua la kwao, mvua ya kwao, vumbi lao. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawekea mazingira bora ili wamachinga hao waweze kuepuka adha hiyo wanayoipata? (Makofi
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote ni mashuhuda kwamba, Sheria hii ilipitishwa na Bunge lako Tukufu na kwa vyovyote vile hakuna kisingizio chochote ambacho kinaweza kikatolewa na halmashauri eti kwa sababu, wakidhani kwamba, sheria ndogo ambazo wao hawajazipitisha zinakuwa zinakinzana kwamba hazitawaletea mapato. Naomba niwasihi Wakurugenzi wote Halmashauri zote, na jambo hili hata Mheshimiwa Rais amekuwa akilirudia, naomba niliseme kwa mara ya mwisho; Mkurugenzi yeyote wa halmashauri iwayo yoyote ambaye atapingana na maelekezo haya na sheria aambayo imetungwa na Bunge lako Tukufu, sisi kama Serikali hatutasita kumchukulia hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anaulizia namna ya kuwawekea mazingira mazuri wafanyabiashara wadogo wadogo. Ni dhamira ya Serikali na ndio maana tunaanza kwa kuwatambua kwa kuwapa vitambulisho ili tuhakikishe kwamba, wanatengewa maeneo mazuri ili wafanye kazi katika mazingira yaliyo mazuri kwa ajili ya kuongeza kipato cha nchi.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyoko katika Jimbo la Manonga linafanana kabisa na changamoto iliyoko katika mkoa wangu wa Ruvuma. Katika mkoa wa Ruvuma kuna changamoto ambayo itaenda sambamba na tatizo la kubadili mita za maji kutokana na mfumo wa kupata maji kwa maana ya mita ibadilike kuwa wananchi wapate maji kwa mfumo wa unit. Sambamba na hilo, iko miradi ambayo nilikuwa nikisema hapa mara nyingi katika mkoa wangu wa Ruvuma ambayo kimsingi inaonekana kwamba imekamilika laikini haitoi maji, na miradi hiyo inataokana na World Bank.
Mheshimiwa Mwenyekiti, World Bank wamefanya hiyo kazi na miradi inaonekana kwamba sasa tayari inatoa maji, lakini katika miradi hiyo kuna mradi wa maji wa Mkako (Mbinga), Ruhuwiko (Songea Mjini), Matemanga na Ndembo (Tunduru), Litola (Namtumbo)...
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani ya kuhakikisha miradi hii inafanyiwa marekebisho ili iweze kutoa maji na wananchi waweze kufaidika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema kwamba miradi imekamilika lakini maji haitoi kwa wananchi. Lengo la Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji na fedha zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ile. Lakini cha kushangaza miradi imekamilika haitoi maji. Labda nimuombe Mheshimiwa Jacqueline kwamba baada ya Bunge tuongozane pamoja tukaone sababu gani zinazosababisha mradi ukamilike lakini hazitoi maji? Kama kuna mtu ambaye anasababisha au kukwamisha ili maji isitoe tutalala naye mbele ili wananchi wetu waweze kupata maji.
MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza yenye seheu (a) na (b).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa tumbaku unategemea sana upatikanaji wa mbegu, mbolea, madawa kwa wakati muafaka. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati unaotakiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni nini faida na hasara ya kumruhusu mnunuzi kupeleka mbolea kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kama inavyofahamika kwamba zao hili la tumbaku limekuwa na mchango mkubwa sana katika uchumi wa nchi yetu. Kwa misingi hiyo, Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kwamba pembejeo zinapatikana na zinawafikia walengwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nini tatizo la kumfanya mnunuzi aweze yeye kupeleka mbolea. Mnunuzi mzuri anapopeleka mbolea kwa tija ili mwananchi huyu apate hiyo mbolea kwa tija huwa hakuna tatizo lakini kuna wanunuzi ambao ni wanyonyaji ambao wanapeleka mbolea na kumwambia mwananchi kwamba ukishapata hii mbolea yangu na mazao yako yote lazima uniuzie mimi kwa bei anayoitaka yeye, huo ni unyonyaji na mnunuzi wa aina hiyo huwa tunakuwa hatumtaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana sasa hivi kupitia maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa, katika mazao makuu matano ya nchi hii yanawekewa utaratibu maalum ili kuhakikisha kwamba vyama vya ushirika viwe na nguvu na kusaidia kuwawezesha wananchi ili wasiendelee kunyonywa.