Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka (19 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Awali ya yote, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuwepo jioni hii kuchangia mjadala huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kutoa shukrani za dhati kwa Wanaliwale kwa kuniamini na niko tayari kuwatumikia. Vilevile napenda kuwapongeza wapiga kura Wanaliwale kwa kuiweka CCM kuwa Chama cha Upinzani Jimboni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mjadala wangu nitaulekeza katika maeneo yafuatayo. Kwanza kabisa, msingi wa Mpango. Msingi wa Mpango tumeambiwa ni amani, utulivu lakini nataka nitoe angalizo hapa ni lazima tutofautishe uvumilivu wa watu wachache na amani. Nataka nitumie neno ukondoo, ukondoo wa Wazanzibar tusiuchukulie kama ni kigezo cha amani. Nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba ukondoo huu tusitegemee kwamba utakuwa ni wa kudumu. Kama tunakusudia huu Mpango utuletee matunda tunayokusudia ni lazima tuhakikishe kweli tunapambana kuhusu suala la amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu tumeambiwa kuna kuimarisha elimu, mimi nitajielekeza kwa upande wa elimu. Hatuwezi kuimarisha elimu tukiwasahau walimu. Walimu wetu maisha yao ni duni sana. Hapa nataka niongelee jambo moja. Walimu wanapewa kazi nyingi sana, mimi naomba tufike mahali hawa walimu tuwapunguzie kazi. Nitoe mfano walimu hawa ndiyo wasimamizi wa uchaguzi nchi hii inapofika kwenye uchaguzi na madhara wanayoyapata ni pale ambapo Chama cha Mapinduzi hakijapita, huyu mwalimu aliyesimamia, aidha ni Mratibu au Mwalimu Mkuu ajira yake iko hatarini. Natoa mfano huu katika Jimbo langu la Liwale leo hii wako walimu ambao waathirika kwa matukio haya. Sasa hatuwezi kuboresha elimu iwapo walimu hawana utulivu, walimu wanaidai Serikali, naomba tuliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye sekta ya afya. Tusitarajie mpango huu unaweza ukafanikiwa iwapo watu wetu hatujawajenga kiafya. Kwa upande huu wa afya nafikiri siasa imekuwa nyingi kuliko utekelezaji. Kama ambavyo watangulizi walivyosema nchi yetu watu ni wapangaji wazuri sana na mimi nasema huu Mpango tukiamua kuuza kwa nchi yoyote wakiutekeleza miaka mitano ijayo watakuwa mbali sana, lakini kwa Watanzania Mpango huu hatuwezi kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nchi yetu imekuwa na mipango mingi sana na kitu kikubwa sana nachokiona mimi ni kwamba nchi yetu inaongozwa na mawazo ya watu wachache. Leo hii tukibadilisha Waziri hapa Wizara hiyo itabadilika kwa kila kitu, hatuna common goal kwamba nchi inataka kwenda wapi, hilo ndiyo tatizo letu. Leo hii tukibadilisha Rais anakuja na mambo mengine. Mheshimiwa Mkapa alikuja na Mtwara Corridor baada ya Mkapa kuondoka Mtwara corridor ikafa. Mheshimiwa Kikwete alikuja na maisha bora na yenyewe sijui kama itaendelea. Pia alikuja na Bandari ya Bagamoyo na sijui kama kwa utawala huu kama hiyo bandari bado ipo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Sasa kwa mtindo huu hatuendi kwamba kila Waziri, kila Rais atakayekuja na la kwake hatuna common goal kama Taifa. Hili limeshatuletea matatizo sana, nitoe mfano kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki tulipozungumzia habari za reli tulilalamika hapa, sisi tulikuwa walalamishi wakubwa sana, watu wa Uganda na Rwanda walipoamua kuondoka kujiunga kutengeneza reli tukaanza kulalamika, mnalalamika nini? Mnachelewa wenyewe halafu mnategemea wao wawasubiri hatufiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwa upande wa reli, sidhani kama kweli tuna dhamira nzuri kuhusu hiyo reli ya kati. Hivi unampaje mtu kusimamia reli ya kati ana malori ya usafirishaji zaidi ya 5000, hayo malori ayapeleke wapi? Ana malori ya usafirishaji 5000 halafu mnamwambia asimamie reli ijengwe halafu yeye malori apaleke wapi akafugie kuku? Tuache utani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka Mheshimiwa Rais alipokuwa kwenye Bunge hili kama Waziri wa Miundombinu alisema Sera ya Taifa letu ni kuunganisha mikoa yetu kwa barabara za lami. Nisikitike kusema sisi Mkoa wa Lindi hasa Wilaya ya Liwale inaitwa Wilaya ya pembezoni, kwa mawazo yangu nikajua Wilaya ya pembezoni maana yake ni Wilaya inayopakana na nchi nyingine, lakini ndani ya Tanzania kuna Wilaya za pembezoni. Sisi Liwale tunapakana na Mkoa wa Morogoro, Ruvuma niambieni kama kuna barabara inayotoka Morogoro kuelekea Liwale, hakuna. Hatuongelei barabara za lami tunaongelea hata barabara za changarawe, kutoka Liwale kwenda Tunduru hakuna barabara. Wilaya ya Liwale leo iko pembezoni inapakana na nchi gani? Halafu mnasema tunaweza kwenda sambamba na huu mkakati, huu mkakati nasema kwamba hauwezi kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye upande wa amani, tumewapa kazi Polisi kwamba wao ndiyo walinzi wa amani, lakini nipende kusikitika kwamba hao polisi tunaowategemea wanaishi kwenye viota na mtaani. Hivi wewe polisi unakaa mtaani mwanangu anauza gongo utamkamata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale imekuwa Wilaya mwaka 1975 mpaka leo hawana Kituo cha Polisi. Kituo cha Polisi cha kwanza kilikuwa kwenye gofu la mkoloni, NBC walipojenga nyumba yao wakahamia huko, ile nyumba ilikuwa ni ya mtu binafsi leo hii inamwaga maji kila mahali, mafaili yanafunikwa na maturubai halafu polisi hao hao ndiyo tunategemea walinde amani, hapo tunacheza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nijielekeze kwa upande wa sekta ya viwanda. Sekta ya viwanda hasa kwa sekta binafsi huku ndiyo tumekwama kabisa. Kama tumefika mahali tunawaacha vijana wetu wahangaike na hawa matajiri wakubwa, eti ndiyo wa-bargain mishahara. Mimi nasikitika jambo moja, sielewi imekuwaje. Zamani nilisikia wale ma-TX walikuwa na vibali vya kuishi miaka miwili leo hii tuna ma-TX kwenye viwanda vya watu binafsi mpaka wafagizi na madereva, sijui Uhamiaji wanafanya kazi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mpaka naingia hapa Bungeni nina miaka 30 kwenye sekta ya watu binafsi, nimetembea zaidi ya viwanda sita, usiniulize kwa nini nimebadilisha viwanda vyote hivyo, ni kwa sababu nilikuwa sitaki kunyanyaswa. Haiwezekani leo hii tuna ma-TX, mtu ana cheti cha uinjinia ni dereva, ana cheti cha uinjinia anasimamia upakizi wa mizigo kiwandani, hii nchi imeoza, ni kama vile haina mwenyewe. Ndiyo maana nikasema kama ni kutunga sheria sisi tunaongoza kwa kutunga sheria nzuri sana na kama kwa mipango sisi tunaongoza lakini utekelezaji zero. Kama walivyotangulia kusema wenzangu, Waheshimiwa Mawaziri mliopewa dhamana nafuu msikilize Wabunge wa Vyama vya Upinzani wanasema nini, lakini mkiwasikiliza wa huko mtapotea na kama majipu ninyi mtakuwa wa kwanza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze upande wa kilimo. Kilimo ndugu zangu hakiendeshwi na ngojera hizi za kilimo kwanza wala kilimo uti wa mngogo, tuna matatizo ya masoko. Nikupe mfano Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Liwale, sisi tunalima korosho, ufuta, mbaazi lakini wakulima wetu sasa hivi bado wanahangaika. Mwaka juzi mbaazi ilipanda bei watu wakajikita huko, mwaka huu korosho zimepanda bei, ufuta umeshuka. Kwa hiyo, watu bado wanahangaika yaani wanalima kwa kubahatisha kwamba ukilima ufuta ikikuangukia bahati umepanda bei ndiyo unanufaika, ukivuna korosho mwaka huu imepanda bei ndiyo umenufaika. Hizi ngonjera za Kilimo Kwanza bila kutafuta masoko ya mazao yetu hatutakwenda huo mkakati ni wa kufeli. Mimi sijaona kwenye mpango huu wapi kumeelezwa suala kuimarisha masoko. Natoa angalizo hatuwezi kuimarisha kilimo kwa ngojera ya kilimo kwanza wala kilimo uti wa mngogo ni lazima tufanyekazi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nitoe shukurani kwako wewe kwa kunipa nafasi ili niwe mchangiaji mmojawapo asubuhi hii ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwenye Mpango huu ni kama ifuatavyo; Serikali yetu hii ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ni Serikali ya kupanga mipango mizuri sana. Hii ni mara ya pili nalisema hili ndani ya Bunge lako Tukufu, lakini tatizo letu kubwa liko kwenye utekelezaji wa ile mipango tunayoipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sijui hizi takwimu mnazokuja nazo, hizi za ku-copy na ku-paste zinaletwa kwa sababu ipi? Tunakuwa tumedhamiria nini tunapoleta takwimu ambazo hatuna uhakika nazo na wala hazitekelezeki. Hatuwezi kuwa na mipango na ikatekelezeka iwapo hatuna mikakati iliyowazi ya kuonyesha namna gani tutatekeleza mipango hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano takwimu ambayo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati, anasema sera ya nchi yetu ilikuwa kuunganisha mikoa yetu na imekamilika na akaitaja baadhi ya mikoa na akasema ni mikoa michache tu ambayo imebaki haijaunganishwa. Hata hivyo, nashangaa Mkoa wa Lindi - Morogoro haijatajwa katika mikoa ambayo haijaunganishwa. Kwa sababu Mkoa wa Morogoro unapakana na Mkoa wa Lindi kupitia Wilaya ya Liwale lakini hakuna barabara. Mkoa wa Lindi unapakana na Ruvuma katika Wilaya ya Liwale hakuna barabara lakini takwimu hapa zinaonyesha kwamba mikoa hiyo tumeshaunganishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Sera ya Taifa inasema kila kata kuwe na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na zahanati. Lengo hili halijafikiwa kama ambavyo Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani amesema, tunadiriki vipi kwenda na mpango wa pili wakati hii mipango yetu ya kwanza haijakamilika, tena imekamilika kwa asilimia 26 tu. Katika Jimbo langu tuna kata 20 lakini tuna kituo cha afya kimoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii hapa tunajitapa kwamba tunao uwezo wa kutekeleza mipango hii kwa kutumia rasilimali zetu ambazo nina hakika kabisa hazisimamiwi kama inavyotakiwa.
Ubadhirifu wa rasilimali zetu umekuwa ni mkubwa sana. Tunavyo viwanda, hivyo ambavyo sasa tunasema tunataka kuvifufua, Mkoa wa Lindi kulikuwepo na viwanda vya korosho vikabinafsishwa na havifanyi kazi mpaka leo lakini leo hii tunapokuja kufufua viwanda napata wasiwasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi sasa hivi unazalisha ufuta na korosho lakini kama nilivyosema tuna matatizo ya barabara. Hivi ni mwekezaji gani atayekuja kuwekeza Lindi mahali ambapo hakuna barabara, mahali ambapo hatujajiandaa na miundombinu yoyote? Nitoe mfano halisi, sasa hivi barabara ya Jimboni kwangu imeshafungwa, huwa inapitika kiangazi tu lakini sisi Mkoa wa Lindi ndiyo tunaoongoza wa kuzalisha korosho na ufuta lakini hatuna kiwanda hata kimoja. Mimi siwezi kumvutia mwekezaji yeyote aje kuanzisha kiwanda Liwale wakati ambapo hatuna barabara, umeme wala miundombinu yoyote, huku ni kudanganyana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sijajua Serikali inavyokuja na hizi takwimu au maelezo ya juu juu wanakuwa wamedhamiria nini kwamba tupitishe tu ili mradi siku ziende au kweli tuko committed na hayo tunayoyaongea au tunayoyadhamiria? Kwa mfano, hapa tumesema malengo yamekamilika kwa asilimia tano, hivi ni kweli? Yaani mpango wa kwanza umetekelezwa kwa asilimia tano au asilimia 26 tunaingia kweli kwa kifua mbele kwa mpango wa pili, mimi sijaelewa na wala sishawishiki kuona kama tuko serious na jambo hili. Hivi tunawezaje kwenda na Mpango wa Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kikao kilichopita nilisema hapa kwamba hatuko serious. Mpango ule wa kwanza wa kujenga reli tulitekeleza kwa asilimia 5 tu na nikawaambia hapa kwamba hii haifanywi kwa bahati mbaya ila kwa makusudi kwani kuna watu wanataka wafanye biashara za malori, nikasema hapa wakaanza kulalamika. Mipango hii tunayokwenda nayo haiwezi kwenda kama hatuko serious. Mimi naomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi kama hamko serious na nchi hii mtuachie na watu wako tayari kutuachia lakini ninyi hamtaki kutoka. Kwa mipango hii hatuwezi kwenda. Tumekuwa wepesi sana wa kuainisha vipaumbele lakini si watekelezaji wa vipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja upande wa kilimo, tangu Uhuru tumekuja na sera nyingi za Kilimo Kwanza, Kilimo Uti wa Mgongo lakini hivi kweli hiki kilimo kinaweza kikaimarishwa kwa njia hii na hakuna mkakati wowote wa kuimarisha masoko. Leo hii Waziri anakuja hapa anasema kwamba anataka kushusha bei mazao ya kilimo ina maana wakulima waendelee kuteseka, hiyo ndiyo mipango ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mtuachie nchi hii kwa sababu mimi ninavyofahamu huwezi kuimarisha kilimo kama haujaimarisha masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwetu tunapata shida, nitolee mfano wa Jimboni kwangu, tunalima korosho na ufuta lakini wananchi wangu wanahangaika kila mwaka. Mwaka huu wakivuna korosho, ufuta unapanda bei, mwakani wanavuna ufuta, korosho zinapanda bei hawajui kinachoendelea.
Leo hii tunakuja hapa na Mpango kwamba tunaanzisha viwanda hatujui hivyo viwanda vilivyokuwepo awali vilienda wapi, wale walioharibu viwanda hivi wamechukuliwa hatua gani hatujui, tunakuja tunavurugana vurugana hapa tu ndani kwamba tuna mipango endelevu.
Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze, utekelezaji wa Mpango huu hizo hela anazipata wapi? Kwa sababu mipango iliyopita, Serikali ni hii hii, watu ni wale wale imetekelezwa kwa asilimia tano, leo hii mnakuja kutuambia kwamba mnaweza kutekeleza angalau asilimia 50, huo uwezo mnaupata wapi? Au ndiyo kama nilivyosema jana hapa tupo tu kwa ajili ya kuonekana kama sisi tupo Bungeni tunajadili mustakabali wa nchi yetu ili mradi siku ziishe lakini seriousness mimi sijaiona. Seriousness ya Chama cha Mapinduzi kuwahudumia watu wake sijaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaambieni Jimboni kwangu tungekuwa tumepakana na nchi mojawapo ningeshawishi lile Jimbo tuliondoe Tanzania. Hata hivyo, kwa sababu tuko katikati hatujapakana na nchi yoyote tutaendelea kubaki kisiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi nikiwa na maana halisi. Mimi kwangu hakuna barabara, Kituo cha Polisi, hospitali, maji na nikisema hakuna maji namaanisha. Liwale tumerithi Kituo cha Polisi tulichukua jengo la benki.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba ulinde muda wangu.
NAIBU SPIKA: Muda wako unalindwa, naona kuna taarifa nyingine.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pili naikataa taarifa kama ifuatavyo. Nimesema Wilaya ya Liwale haina barabara, mimi kila tarehe 15 Septemba na tarehe 15 Julai wananchi wa Liwale wanatoka kwenda Mahenge kwa miguu wanasindikizwa na askari wa wanyamapori na wanatembea muda wa siku tatu mpaka siku nne. Nimesema Liwale hakuna barabara, nimesema Liwale kama ingekuwa vita ile ya mwaka… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka, naomba ukae kuna taarifa nyingine.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa hiyo, nakataa Taarifa yake kama ifuatavyo; nimesema na naendelea kusema Liwale sisi hatuna hospitali inayoitwa Hospitali ya Wilaya, nashukuru aliyenipa taarifa ni Naibu Waziri wa Afya atalichukua akitaka kuthibitisha. Sasa hivi katika Wilaya nzima ya Liwale tuna Clinical Officers watatu tu, siyo Madakatari Bingwa ni Clinical Officers watatu tu mahitaji ni Clinical Officers 40, nasema kwa takwimu. (Makofi)
WABUNGE FULANI: Aibu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, labda uniambie unapotaka kuunganisha mikoa ina maana kwamba tutoke Lindi - Dar es Salaam - Dodoma - Iringa, twende Songea, labda kuunganisha kwa namna hiyo. Nikisema nina hali hiyo ya kusema, nawasemea wana Liwale. (Makofi)
Kwa hiyo, narudi kwenye Mpango. Kama nilivyotangulia kusema kwamba sisi shida yetu ni uhakika wa masoko. Serikali haionyeshi mahali ambapo wananchi hawa watasaidiwa vipi kwa upande wa masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi kwa upande wa maliasili, sisi Liwale tuko kwenye Mbuga ya Selous lakini Liwale haina hoteli ya kitalii, barabara wala kiwanja cha ndege, hatunufaiki kwa chochote sisi kupakana na mbuga za wanyama zaidi ya kuendelea kupigwa na kunyanyaswa. Nimeshamletea Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili taarifa ya mgogoro uliopo Wilaya ya Liwale na Mbuga ya Selous. Sasa anapokuja Naibu Waziri akaniambia kwamba sina haki ya kuiondoa Liwale Tanzania sijamuelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunanufaikaje na maliasili? Sisi tunapakana na mbuga za wanyama lakini vilevile tulikuwa na uwanja wa ndege enzi zile za Mzee Kawawa, Mwenyezi Mungu amrehemu, tangu Mzee Kawawa amekufa na Liwale imekufa, ule uwanja wa ndege haupo tena pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo hii Serikali hii kwenye Mpango wake huu, labda Waziri atakapokuja kuniambia kama ana mpango wowote, kama kuna mpango wa kuufufua uwanja wa ndege Liwale, kama kuna utaratibu wowote ule wa maliasili, kama wanajenga hoteli au kama wanatutengenezea barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimetembea vijiji vyote vya Jimbo langu sijakuta hata choo kilichochangiwa na Selous, sijakiona! Sasa unategemea wananchi wa Liwale na Lindi wa-support mpango huu kwa kipaumbele gani ambacho wamepewa au kwa sehemu gani ambayo wamekumbukwa? Labda Waziri atakapokuja kwenye kujumuisha atakuja kunieleza kwamba Liwale au Mkoa wa Lindi kwa ujumla ameuweka katika mpango huu katika maeneo gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Liwale bado watumishi hawataki kukaa kule, mawasiliano hakuna siyo ya barabara wala simu. Ndiyo maana nikasema hapa nahitaji Clinical Officers 40, siyo kwamba hawapangwi, wanapangwa lakini hawakai kwa sababu mazingira ya Liwale siyo rafiki. Jamani Chama cha Mapinduzi mtuachie hii nchi. Tuachieni hata miaka mitano tu muone nchi inaendeshwaje. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na hayo tu ya kusema. Ahsante sana.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yangu kwenye Mpango huu yatajikita katika Wizara zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; ukizingatia mafanikio kidogo kwa ufanisi wa Mpango wa awali kwa maoni yangu tatizo kubwa linaloikabili mipango yetu mingi ni ukosefu wa uadilifu kwa watekelezaji wa mipango yetu. Ikiwa ni pamoja na nchi kukumbwa na tatizo kubwa la rushwa, ukosefu wa miundombinu bora ya reli na barabara kwa maeneo ya uzalishaji mazao ya kilimo. Hatuwezi kuwa na uchumi mzuri mpaka pale tutakapobadilisha mtazamo wetu na kuacha tabia ya uchumi wetu kutumikia siasa, badala ya siasa kutumikia uchumi. Katika kilimo tuna tatizo la masoko ya wakulima wetu, sambamba na ujenzi wa viwanda vidogo vidogo hasa pale ambapo mazao hayo hulimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu elimu; miongoni mwa sababu za mipango mingi kutofikia malengo ni mfumo mzima wa elimu yetu, elimu inayotoa wahitimu wasiokuwa na uwezo wa kuingia kwenye soko la ajira ya kujitegemea. Elimu ambayo haiwajengei uwezo wa kujitegemea na badala yake wanakuwa mzigo kwa Serikali; vyuo vya VETA pekee ndio ufumbuzi wa hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, maliasili; hatuwezi kukuza sekta ya utalii kama hatupo tayari kufufua vivutio vilivyosahauliwa kama kivutio kilichopo Liwale (Gofu la Mjerumani la vita ya maji maji lililopo Mjini Liwale) hivi ni kweli ili kuingia Selou ni lazima watalii wapitie Morogoro kwa nini Mkoa wa Lindi (Liwale) imeachwa yatima katika utalii wa ndani na nje?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawezaje kuwashirikisha wananchi kushiriki kulinda rasilimali zetu kama hawataona faida ya moja kwa moja itokanayo ya rasilimali zetu. Utatuzi wa migogoro ya mipaka ya hifadhi zetu ni moja ya kikwazo cha sekta hii kushindwa kufikia malengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu; ugawaji usiozingatia hali halisi wa miradi ya barabara nchini ni moja ya kikwazo katika Mpango huu. Mfano ni Mkoa wa Lindi ambao mpaka leo mkoa huu haujaweza kuunganishwa na Mkoa jirani wa Morogoro kupitia Liwale na Mkoa wa Ruvuma kupitia Wilaya za Tunduru na Liwale. Sio hivyo tu hata barabara ya Nangurukuru-Liwale ambayo ingeendeleza mazao ya korosho na ufuta ambayo sasa yanalimwa kwa wingi katika Mkoa mzima wa Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Afya ni sekta muhimu sana ambayo tumeshindwa hata kuboresha afya za watu wetu hasa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto. Mfano, katika Wilaya ya Liwale hakuna hadi leo hospitali yenye hadhi ya kuwa hospitali ya Wilaya. Hospitali haina miundombinu yoyote inayofanana na hospitali ya Wilaya. Wilaya nzima ina kituo kimoja tu cha afya Wilaya yenye Kata 20 na Mpango huu haujasema chochote kuhusu ni namna gani ya kupambana na changamoto hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikishwaji wa wadau ni muhimu ili mipango yetu iweze kutekelezeka, vile vile uadilifu wa watendaji. Tuongeze bidii ya kupambana na rushwa na uwajibikaji wa pamoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu na Sekta ya Ualimu. Mtiririko mzima wa kuandaa Walimu una kasoro kubwa sana hasa tangu kuchafuliwa kwao kwenda kwenye Vyuo vya Walimu kwa kuwachagua watu wenye ufaulu wa chini kuingia kwenye Vyuo vya Ualimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kitendo cha wahitimu kukaa mwaka mzima wakisubiri ajira kinavunja moyo Walimu wetu. Hata hivyo, kitendo cha Walimu kushindwa kuwapandisha madaraja kwa muda mrefu na pale wanapopanda kushindwa kuwapa stahiki zao, nako ni kuvuruga kiwango cha elimu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu kufanya kazi nje ya ajira yao, mara nyingi Walimu wamekuwa wakitumikia kwenye kazi kama vile sensa, kusimamia uchaguzi, kuwa Watendaji wa Vijiji nakadhalika. Mwalimu anaposimamia uchaguzi na Chama Tawala kikianguka kwenye Kituo husika, basi huyuo Mwalimu Mwalimu ajira yake huwa hatarini. Ninayo majina ya walimu waathirika na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Liwale ambako CCM ni Chama cha Upinzani, ushauri wangu ni kwamba tuwaache Walimu wabaki madarasani. Pamoja na changamoto nyingi tunazokabiliana nazo ili kujikwamua kutokana na umasikini uliokithiri mahitaji ya Chuo cha VETA Liwale ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na Chuo cha Walimu, kwani Walimu wanaotoka nje ya Mkoa wetu wa Lindi wanashindwa kukaa Liwale. Vilevile tunaomba Kituo cha Chuo cha Utalii ili kukuza utalii Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule za Jimbo la Liwale hazina Wakaguzi na wale wachache waliopo hawana vitendea kazi. Hawana gari hata moja la ukaguzi wala pikipiki. Tunawezaje kuwa na elimu bora, elimu ambayo haisimamiwi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupanda kwa madaraja ya Walimu kuzingatie kiwango cha elimu. Hakuna utendaji ulio bora kama Mratibu Kata ni Form IV, Mwalimu Mkuu Degree au Mkuu wa Shule Diploma, Mwalimu Degree, hapo hakuna uwiano wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu imeshusha kiwango cha elimu nchini. Leo watoto hawana mitihani ya Mid-term, mitihani ya wiki, Mock – Kata, Mock – Wilaya, wala Mock – Mkoa. Sasa hivi mtoto hupimwa mara moja tu kwa mwaka mzima. Utajuaje maendeleo ya mtoto anayefanya mtihani mmoja tu kwa mhula?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii jioni ya leo nami nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Afya. Awali ya yote, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kusimama hapa katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kutoa shukrani za dhati kwa wapiga kura wangu, Wanaliwale kwa kunikabidhi jukumu hili la kuwawakilisha na sasa hivi ndiyo hiyo kazi naifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naanza kuwaasa ndugu zangu wa Kambi yetu ya Upinzani. Kambi ya Upinzani ndiyo tuliopewa jukumu la kuishauri Serikali. Serikali hii wanasikia na wanatuelewa. Wenzetu waliobaki kule nyuma, wamepewa kazi ya kushangilia na kupitisha. Sisi ndiyo tunatakiwa tuishauri hii Serikali. Hii Serikali siyo kwamba hawasikii, tatizo la Serikali yetu ni kwamba wako nyuma sana na wakati. Mliwashauri hapa mwaka 2010 kwamba safari za Mheshimiwa Rais hazina tija; Mwaka 2015 wametekeleza; mkawashauri mwaka 2010 kuhusu ufisadi, mwaka 2015 wametekeleza; tatizo ni muda gani wanautumia kuyatekeleza haya tunayowaambia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri wa kusema ni kutazamana, ndiyo maana sisi tumetazamana na Mawaziri, wale wako nyuma, kwa sababu wanajua nini tunaongea. Nataka niwape faida moja; tunapochangia Upinzani na Mawaziri wako busy kuandika, kwa sababu wanajua sasa ndiyo wanashauriwa, kule wanasubiri kushangilia na kupitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi kwa mabosi wangu, Wanaliwale, naomba niwawakilishe. Wilaya ya Liwale ni Wilaya iliyoasisiwa mwaka 1975 na mwasisi wa Wilaya ile ni Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Rashid Mfaume Kawawa. Nakuja kwenye upande wa hospitali; sasa bahati mbaya ya wilaya ile, ina vijiji 76, tuna zahanati 30 tu. Wilaya ya Liwale ina kata 20, tuna kituo cha afya kimoja, mfu. Nasema kituo mfu kwa sababu ni mwaka wa tatu huu, vifaa vimekwenda pale vya upasuaji, viko kwenye maboksi mpaka leo. Havijafunguliwa, mchwa wanakula yale maboksi. Nimeyaona haya kwa macho yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Wilaya ya Liwale ina magari mawili ya wagonjwa; gari moja ndilo ambalo anatumia DMO kama gari la kufanyia kazi na gari moja ndiyo linalotumika kama la kusaidia wagonjwa. Bahati mbaya nyingine ya Wilaya ya Liwale, Mji ule upo; sijui nani anamjua pweza! Barabara zetu ziko mkia wa pweza, kwamba hatuunganishi kutoka kata moja kwenda nyingine, ni mpaka uende urudi, uende urudi. Nakupa mfano wa vijiji vichache vifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Nahoro kwenda Liwale ni kilomita 135, Napata - Liwale Kilomita 120, Liwale - Lilombe Kilomita 65, Kikulyungu - Liwale Kilomita 120. Hawa wanatembea hizo kilomita 120, kufuata huduma Liwale Mjini. Wakifika Liwale Mjini, hospitali yenyewe ndiyo kama hiyo, takwimu hizo nilizokupa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale kwenye zahanati zetu 30 zinahudumiwa na wale mnaita one year course…
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Medical attendant wa one year course ndio wanaohudumu kwenye hizi zahanati. Kichekesho, nimekwenda na DMO kwenye baadhi ya zahanati, tumekuta dawa zimeharibika. DMO anasema hizi dawa zimeharibika kwa sababu hawa wahudumu hawazijui. Wanataka panadol zilizoandikwa panadol. Ukibadilisha boksi siyo panadol hiyo. Hili ni tatizo!
TAARIFA
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Kuchauka keti kidogo....
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zuberi unaikubali taarifa au unaikataa?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Taarifa yake naikataa, kwa sababu zifuatazo: Waziri Mkuu wa kwanza Tanganyika huru ni Mwalimu Nyerere, lakini Waziri wa Kwanza wa Tanzania ni Mzee Kawawa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee Kawawa ni Waziri Mkuu wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, uwezo wake wa kuifahamu historia haiwezi. (Kicheko/Makofi)
MWENYEKITI: Endelea!
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Hiyo ni historia fupi tu ameshindwa kuielewa. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa na kiti kinakulinda, uko sahihi! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa Afya, watu wengi wamewasifia na wanaendelea kuwasifia, nami naendelea kuwasifia, lakini nawapa pole. Nawapa pole kwa sababu jukumu mlilonalo ni kubwa, mazingira ya kazi ni magumu, kwa bajeti hii kwa kweli dhamira yenu ni nzuri, nami nataka niwaambie kwamba ili muweze kuonekana angalau mmetekeleza kidogo, mnahitaji kufanya kazi ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama takwimu zinavyosema, bajeti ya Serikali imeongezeka kwa trilioni sita point something, lakini bajeti ya Afya imepungua kwa asilimia 11. Sasa mwone hiyo kazi mliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narejea kule kule Liwale. Liwale sisi tunayo matatizo, sisi tuna upungufu wa Clinical Officer 40. Mheshimiwa Waziri atakapokuja naomba anieleweshe, hivi DMO anaruhusiwa kutibia? Anaruhusiwa kuingia ofisini kutibu watu? Maana DMO wangu yeye ni mtawala, hajawahi kuingia ofisini kutibia. Sasa sijaelewa, mimi kwa sababu siyo mtaalam sijaelewa. Hapo mtakapokuja, mtanielewesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, jiografia ya Wilaya ya Liwale kiutendaji kuwa na gari moja la wagonjwa ni tatizo. Gari lile likiondoka, watu wengine huku nyuma hawana usafiri tena na ni kilomita kama hizo nilizokupa. Liwale hospitali ile, mimi nimeingia haina X-Ray mwaka mmoja uliopita.
Namshukuru Naibu Waziri, nilikwenda ofisini kwake akanisaidia, akanipa njia ya kupata mtaalam, nikampata mtaalam nikapeleka X-Ray ile ikatengenezwa. Kama Waswahili wanavyosema, “Siku ya Kufa Nyani, Miti yote Huteleza.” Ile X-Ray sasa hivi ni nzima lakini haina mhudumu. Mpiga picha hatuna, kwa hiyo, tumerudi pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Liwale haina ultrasound. Mwezi Januari kuna dada mmoja alikwenda pale kwa lengo la kujifungua, wale akinamama wakaenda kumpima, wakampapasa wakamwambia njoo wiki ijayo. Wiki ijayo yule mama hakufika, tumbo likawa la njano wamemrudisha pale yule mama kafa. Hospitali ya Wilaya ya Liwale!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wanamwambia Mheshimiwa Waziri, njoo kwetu, njoo kwetu, mimi sisemi aje Liwale; naomba atusaidie Liwale. Akiona namna ya kuweza kuja, karibu Liwale, aje ajionee haya ninayoyasema. Ile Wilaya imesahauliwa, ni ya siku nyingi, lakini ukienda ukiiangalia utafikiri ni Wilaya ambayo imezinduliwa juzi. Hayo ndiyo matatizo tuliyonayo Wilaya ya Liwale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati napita kuomba kura niliwaambia, sitakubali kuona akinamama wakienda kujifungua wanakwenda kama wameachika; anakwenda na beseni, ndoo, carpet; maana hizi mackintosh wao hawana, kule wanatumia hizi carpet za kawaida. Anakwenda na carpet, ndoo, beseni, wembe, kanga, gloves na sindano. Nikasema sitalikubali hilo. Kwa kuonesha mfano huo, nimepeleka, mackintosh 5,000 mwezi uliopita. Nimeona nianzie hapo, lakini hali yetu ni mbaya, tunaomba msaada wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye upande wa MSD. MSD ni tatizo jamani. Nakumbuka siku moja tulikwenda MSD nikiwa kwenye Kamati ya UKIMWI; yule Mkurugenzi alituambia kwamba tatizo la Halmashauri wanatupa order haraka. Wanatupa order leo, kesho wanataka hela, lakini hii siyo kweli. Sisi Liwale tumepeleka pesa Desemba, shilingi milioni 35. Dawa tulizopata mpaka leo ni za shilingi milioni 20, inaonekana dawa tulizopewa siyo zile tunazozihitaji. Tumepewa dawa zile ambazo MSD wanazo. Mkurugenzi alisema kwamba mkileta pesa, baada ya wiki mbili au wiki tatu mtakuwa mmepata, lakini hii siyo kweli. Huo ndiyo ukweli halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye CHF. Tarehe 8 Januari, Mkoa wa Lindi ulizindua CHF Kitaifa na mimi mwenyewe nimechangia watu 100 kwenye Jimbo langu, lakini CHF imenitia kitanzi, kwa sababu nimehamasisha Wanaliwale, kabla ya uzinduzi tulikuwa asilimia 10 ya wanajamii wa Liwale, lakini mpaka namaliza tarehe 30 Aprili, tulikuwa tayari tumefika asilimia 46.4 na nikawaahidi Wanaliwale, kufikia Agosti tukiuza ufuta tunataka tusahau masuala ya CHF. Tunataka tuchangie asilimia mia moja. Sasa hiyo imenitia kitanzi. Imenitia kitanzi mimi na Madiwani wangu kwa sababu tuliwaambia, mkienda dirishani mkikosa dawa, njooni kwetu. Sasa vyeti vyote vya dawa vinakuja kwetu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti vyeti vyote vya dawa vinaenda kwa Diwani, vinaenda kwa Mbunge kwa sababu tuliwaahidi mtoe pesa mtapata dawa; dawa hazipo! Tunawaomba Mheshimiwa Waziri, CHF inatutia kitanzi. Nashukuru mwenzangu Mheshimiwa Bobali aliona mbali, akawaambia wasichange kabisa. Sasa mimi nimeji-commit kwamba tunachanga na kweli wananchi kwa sababu wananikubali, nikiwaambia wanatekeleza. Mwezi Agosti Mheshimiwa Waziri alituahidi tutakuwa tumefikia asilimia mia moja. Naomba Mheshimiwa Waziri, mnitoe kwenye hiki kitanzi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye hivi mnasema Vituo vya Saratani ya Mlango wa Kizazi. Lindi kuna vituo vinne, Liwale hatuna. Hivi Liwale kuna nini? Jamani, tuoneeni huruma, hata Mzee Kawawa hamumwenzi, simba wa vita! Jamani nawaombeni mtukumbuke na sisi tumo. Kwenye mchango wetu, pato la Taifa tumo! Tunalima korosho kwa wingi, tunalima ufuta kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kwenye masuala ya UKIMWI sasa, nakuja kwenye masuala ya UKIMWI. Takwimu zinaonesha wanaotumia dawa za ARV mpaka mwaka 2015 ni watu 700,000 na inakadiriwa mpaka mwisho wa 2016, wanafika watu 900,000, lakini pesa iliyotengwa ni ya watu 200,000. Maana yake mpaka sasa hivi tunasema watu 500,000 hawana dawa. Hiyo ni takwimu sahihi kabisa zinazohusiana na mambo ya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri hili suala la UKIMWI tulipe kipaumbele. Kama kweli dhamira yetu ni kuwasaidia watu wetu, hili suala la UKIMWI tulipe kipaumbele. Vile vile narudi tena kwenye upande wa MSD. MSD hata hizo dawa chache wanazozileta, kwa jiografia ya Liwale na Mkoa wa Lindi ha… (Makofi)
MWENYEKITI: Basi.
MHE.ZUBERI M. KUCHAUKA: Nashukuru kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo na mimi nitoe mchango kwenye Wizara hii. Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha mimi kusimama jioni hii ya leo nikiwawakilisha Wanaliwale, nikifikisha vilio vyao Wanaliwale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda huko naomba nitoe utangulizi kidogo maana nasikia watu wanalalamika reli, reli, reli, reli. Mbona haijengwi, mbona haijengwi. Nataka niwape faida moja, tatizo la Serikali yetu ni kutanguliza mipango kabla ya nia au dhamira. Sisi kwenye uislamu tunaamini kwamba, mtu unatakiwa utangulize nia, kwanza nia iwepo utende jambo; haiwezekani katika karne ya 21 Tanzania unasafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma kwa gari! Unasafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara kwa gari! Bandari Mtwara ipo haiwezekani! Hivi Wajerumani wakati wanajenga ile reli tuliwaona wendawazimu? Wamechukua tu nchi wakajenga reli, sisi leo karne ya 21 tunategemea malori, miaka 54 ya Uhuru hapa hatuendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wakandarasi mnaowapigia kelele, mnawalalamikia wanajenga barabara, maana gari likipiga kona na barabara nayo inapiga kona! Hawa tutaendelea kuwalaumu, hata aje malaika ajenge hiyo barabara kwa malori yale yanayopita kwenye hizo barabara haziwezi kudumu, cha msingi tubadilishe mindset zetu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalalamika kwamba, wenzetu sijui Kenya, sijui Rwanda, sijui nani, wameamua kufanya kazi! Wale wameamua kufanya kazi wametoka maofisini wanafanya kazi. Ndugu zangu Watanzania leo hii Mtanzania ukikabidhiwa mradi cha kwanza ni kutafuta kiwanja, cha kwanza ni kuagiza gari, tunakwenda wapi? Hatuwezi kwenda! Tena basi kama wewe ni Meneja wa Mradi, mradi unakwisha huna nyumba, huna gari, jamii inakucheka, unaonekana wewe fala! Tubadilishe mindset zetu, tuondoe ubinafsi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niwaambie reli hii kama Waziri huyu aliyekuja leo anadhamira ya kujenga mimi nitaiona. Huwezi kupingana na hawa wafanyabiashara wa malori, mtu ana malori 2000, 3000, 5000, hivi unayapeleka wapi? Nani atakubali reli ijengwe? Tuache kubabaishana, turudi kwenye uhalisia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye viwanja vya ndege. Mheshimiwa Waziri mimi sielewi Mzee Kawawa aliacha usia gani kwa Wilaya ya Liwale, ile miradi yake yote iliyokuwepo yote imefutwa. Sijaelewa kabisa, kabisa tatizo ni nini! Pengine Waziri atakapokuja atanieleza pengine kuna maagizo special Mzee aliyaacha ile Wilaya muisahau kwa kiwango hicho. Sisi Liwale kulikuwa na kiwanja cha ndege leo hii kuna miti unaweza kuchuma hata matunda ule uwanja wa ndege haupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye upande wa mawasiliano ya simu. Mawasiliano ya simu kwa Wilaya ya Liwale jamani tunaomba mtutoe kisiwani. Mimi namuomba Mheshimiwa Waziri kwa heshima na taadhima muitoe Liwale kisiwani, Liwale kuna tatizo la barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Rais aliyepo madarakani, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, amekuwa muadilifu. Aliulizwa hapa habari za barabara Nangurukulu – Liwale akasema haiko kwenye mpango wa kujengwa kwa lami na kwa kulikumbuka hilo alipokuwa anaenda kuomba kura Liwale hakuja, alijua kwa sababu wameshakataa kwamba hiyo barabara hatowajengea kwa kiwango cha lami na kweli hakujenga na alipoenda kuomba kura hakuenda Liwale kuomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namshukuru pengine angekuja nisingekuwa hapa sasa hivi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hakuna barabara mimi naomba Mheshimiwa Waziri ututoe Liwale kisiwani. Tuna barabara ya Nachingwea – Liwale, kilometa 120, sijaiona kwenye hotuba yako yote. Kuna barabara ya Nangurukuru – Liwale kilometa 230 sijaiona kwenye mpango wako wote, tunakosa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa jinsi Liwale ilivyo na rasilimali za kutosha, tunazo mbuga za wanyama, tunayo mazao ya misitu, tunao wakulima wanalima ufuta, wanalima korosho. Tungekuwa na barabara Liwale tusingekuwa walalamikaji kama tunavyolalamika leo upande wa afya, tunaolalamika upande wa elimu, tungeweza kujenga hospitali zetu. Hizi zahanati tungeweza kuziwezesha kwa mapato ya Halmashauri, leo Liwale imefungwa, Halmashauri inapata wapi mapato?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namuomba Waziri atusaidie, atuokoe, atuondoe kisiwani. Nimeona kwenye mpango kuna barabara inatoka Mtwara – Newala – Masasi – Nachingwea inarudi Nanganga; nikupe umbo la hiyo barabara ina “U”, chini ya hiyo “U” ndio kuna Liwale, hebu muone Liwale ilivyotengwa. Yaani umechora “U”, umetoka huku umekwenda ile “U” chini ndio kuna Liwale, wameiacha huko chini! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi watu wale wakiona kwamba CCM haiwataki, wana haki au hawana haki? Mmetengeneza “U”, inatoka Mtwara – Newala – Masasi – Nachingwea inarudi Ruangwa – Lindi, Liwale iko chini! Tunawatendea haki watu wale na tunawahitaji?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba kwa heshima na taadhima uiondoe Liwale kutoka kisiwani. Tatizo kubwa ninaloliona hapa, tatizo kubwa, Chama cha Mapinduzi tangu Uhuru mnaongoza hii nchi, lakini hii nchi kila siku inazaliwa upya! Kila tunapobadilisha uongozi nchi inazaliwa upya. Kwa maana ya kwamba, kila Rais anayekuja ana vipaumbele vyake, hatuwezi kufika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuja Mheshimiwa Mkapa na Mtwara Corridor, Mheshimiwa Mkapa kaondoka na Mtwara Corridor imekufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kama ipo tena?
Mheshimiwa Mwenyekiti, atakuja huyu na lake, mimi nafikiri, sijui tuseme waongoze milele, sijui kama Rais mmoja abaki tu, sijui tufanyaje? Maana kila tunapobadilisha pamoja kwamba chama ni kile kile, watu ni walewale, lakini mikakati yao ni tofauti kabisa. Utafikiria aliyekuja ni tofauti yaani utafikiri ni chama kingine na nchi ni nyingine...
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena kwa kujisifia kabisa kwamba Tanzania inazaliwa upya! Inazaliwa upya kwa kuyaacha yale ambayo yalipangwa awali.
TAARIFA....
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo sijaipokea kwa sababu zifuatazo; amesema Mtwara Corridor bado ipo, anaweza kuniambia Mtwara Corridor ilikuwa ni mradi wa miaka mingapi? Na uliishia wapi? Na ulitengewa fungu kiasi gani? Na ni kwa miaka mingapi? Na utekelezaji wake leo umefika wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara Corridor ilikuwa inatuunganisha sisi mpaka Msumbiji, leo hii huyu mchangiaji aliyetoka hapa anaongelea suala la kutuunganisha na Msumbiji. Eti mtu anakuja anasema Mtwara kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua hili ni tatizo la watu kutokujua jiografia ya Tanzania. Watu jiografia ya nchi hii hawaijui na ndio maana leo hii ukiongelea barabara ya Kusini mtu anakwambia daraja la Rufiji! Mimi nataka niwaambie daraja la Rufiji halina tofauti na daraja la Ruvu kwa sababu mtu leo anadai barabara ya Kigoma unamwambia daraja la Ruvu, inaeleweka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio hicho mnachokifanya! Maana tukiwaambia jamani tunahitaji barabara ya Kusini, aah, ninyi Kusini sijui mmetengenezewa daraja la Mkapa. Daraja la Mkapa ndio nini sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuanzia leo hii Kigamboni nako wamepata daraja lile huku Kimbiji, Gezaulole, nani, hawaitaki tena barabara kwa sababu, wanadaraja la Nyerere. Tunakwenda wapi? Mbona tunakuwa wavivu wa kufikiri? Mbona tunakuwa wavivu wa kufikiri! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri tunahitaji kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kufanya kazi nchi hii, tunahitaji watu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umeisha, naomba ukae tafadhali.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kwanza jioni hii ya leo kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Nishati na Madini. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, bado ananiwezesha kusimama kwenye Bunge lako Tukufu, nikitoa mchango wangu katika Wizara mbalimbali; ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu aliyenifanya nisimame hapa niwawakilishe Wanaliwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema ukweli, sina wasiwasi na dhamira ya Waziri wa Nishati na Madini. Kwanza nakubaliana naye kwa taaluma yake, masuala ya uweledi na ufanisi hilo sina ujuzi nalo, lakini kwa taaluma yake namfahamu vizuri. Wasiwasi wangu ni kwenye utekelezaji, na uwezo wa kuyatekeleza haya ambayo yameanishwa kwenye hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuweka rekodi sawa nataka niwaeleze Waheshimiwa Wabunge walioko humu ndani, wasione Wabunge wa Kusini wamekuwa walalamikaji sana humu ndani, kwamba kila Mbunge wa Kusini akisimama analalamika kama vile tumeonewa! Kwa kuweka rekodi sawasawa nataka niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge, Reli ya Tanga – Dar- es-Salaam iling‟olewa kutoka Mtwara– Nachingwea, wakati ule Mkoa wa Lindi tulikuwa tunalima pamba, mkonge, karanga pamoja na korosho. Wajerumani wakatuwekea ile reli, ili kuharakisha maendeleo, lakini tulivyopata uhuru reli ile ikang‟olewa, ndipo umaskini wa watu wa kusini ulianzia pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapokuja kulalamika tumeona Mwenyezi Mungu ametupa neema hii ya gesi, sasa ni lazima watu ambao tumeshafanyiwa huko nyuma tuwe waoga. Ndio maana mtu wa Kusini akisimama leo hapa, haiamini hii Serikali ya Chama cha Mpinduzi kwa sababu, wameshatufanyia mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye madini. Sera ya Madini bado sijaielewa, hata wananchi wangu wa Liwale nafikiri bado hawajaielewa Sera hii imekaakaaje, hasa pale ambapo ardhi ya wanakijiji inapokuja kugundulika pana madini; hawa wananchi wa ardhi ile bado hawaelewi hatima yao na nafasi yao katika rasilimali ile iliyopatikana pale kwenye ardhi yao. Kwa sababu, ninavyofahamu mnufaika wa kwanza wa rasilimali inayopatikana ni lazima awe yule inayomzunguka pale alipo. Pamoja na kwamba, hizo rasilimali ni za kitaifa, lakini mnufaika wa kwanza anapaswa awe yule inayomzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii kwa Liwale imekuwa ni kinyume chake, sisi Liwale tuna machimbo ya madini yako kwenye Kata ya Lilombe, katika Kijiji cha Kitowelo. Pale wanachimba madini ya sapphire na dhahabu, lakini Ofisi ya Madini iko Tunduru, ndiko mahali ambako kinapatikana kibali cha uchimbaji. Aidha, wachimbaji wadogo ili kupata leseni inabidi uende Tunduru, sasa unafikaje huko Tunduru, sielewi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu ukishapata hicho kibali, unakwenda moja kwa moja msituni, machimbo, wanachimba, wakishachimba wanakwenda moja kwa moja Tunduru kwenye mauzo; Halmashauri ya Kijiji na Wilaya haina habari! Nilivyofika kule kwenye machimbo nikalazimika kumtuhumu hata Mkurugenzi wa Halmashauri, pengine naye anajua chochote. Haiwezekani madini yatoke pale Lilombe, wana Lilombe hawajui, Halmashauri haijui, haipati hata thumni! Sasa leo nimesikia ofisi hii imesogezwa imepelekwa Nachingwea!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Lilombe mpaka Liwale Mjini ni kilometa 60, kwa hiyo, hayo yanayofanyika Lilombe Halmashauri haijui! Sasa hii Sera ya Madini, Mheshimiwa Waziri, atakapokuja nitaomba ufafanuzi kidogo, hii inakuwaje kuwaje? Hawa wachimbaji wadogo tunawasaidiaje? Kwa sababu, nimekwenda mimi kwenye yale machimbo nimemkuta mmiliki mmoja, mchimbaji mdogo, kuna bwana mmoja pale, nafikiri yule alikuwa IGP, Mheshimiwa Mahita! Yeye ana vitalu vyake pale, lakini yeye mwenyewe hayupo pale yupo Tunduru!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana wale wachimbaji wakipata madini wanampigia simu, anakuja kuchukua anakwenda au pengine wampelekea ananunua anakwenda, lakini Halmashauri pale haipati chochote, wala kijiji kile hawapati chochote, wanaachiwa mashimo tu na ile ardhi ipo pale! Sasa hapo Waziri atakapokuja naomba anisaidie, hii Sera ya Madini ikoje kwa sababu, sisi ndiyo kwanza tunaingia kwenye hiyo fani kwa sababu, mgodi wetu ule ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirejee kwenye umeme. Wilaya ya Liwale ilibahatika kupata umeme miaka ya 77, ndiyo Wilaya ya kwanza kwenye Kanda za Kusini na Nyanda za Juu Kusini kupata umeme wakati ule Mzee Kawawa akaambiwa umeme amefunga kwenye mikorosho, lakini umeme wenyewe ni ule wa mwisho saa nne, mpaka leo miaka 40 bado umeme ni ule ule wa mafuta!
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa wametuonea huruma wakachukua ile mashine kutoka Ikwiriri wakaipeleka Liwale, mashine kuukuu iliyotoka Ikwiriri wakaipeleka Liwale ku-subsdise ile mashine ya zamani ya Mzee Kawawa; lakini kulingana na jiografia ya Liwale, umeme ule wa mafuta, masika kama saa hizi Liwale hakufikiki na mafuta hakuna! Kwa hiyo, mafuta yanapokosekana Liwale inabaki giza, lakini siyo hivyo tu, kutoka Liwale kuja Nachingwea ni kilomita 120. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna hii Miradi ya REA; umeme wa REA katika Wilaya ya Liwale, ambayo ina vijiji 76 sisi tuna vijiji vitano tu! Tuna Mangirikiti, Kipule, Likolimbora, Mihumo na Darajani, hivi vipo ndani ya kilomita tano kutoka Liwale Mjini, lakini nje ya hivyo zaidi ya hapo hakuna kingine tena kinachopata umeme. Siyo hivyo tu, umeme huu wa gesi umeishia Nachingwea! Nachingwea Liwale kilomita 120, lakini mpaka leo sijaelewa huu mradi wa umeme wa kutoka Nachingwea kufika Liwale umefikia hatua gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembea kutoka Liwale kuja Nachingwea katika Vijiji vya Kiangara, Vibutuka, Nagano mpaka Mikunya; nguzo zimewekwa pale, zingine zimechimbiwa, zingine huku zinaanguka huku zinachimbiwa, haieleweki, haielezeki, ukimuuliza meneja hakuna anachosema! Mara pesa bado, hajaleta mkandarasi, hapo alipofikia bado hajalipwa, sijui imekuwa kuwaje, haieleweki ile REA pale Liwale mwisho wake ni lini? Hivi sisi tutabaki gizani mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka niseme, kama ingekuwa enzi zile za zamani kwamba, ukitoa shilingi inaleta reflection yoyote, ningekuwa natoa shilingi kila Wizara hapa, maana sioni Wizara hata moja ambayo nikasema Wizara hii ina nafuu kwa Liwale. Hata hivyo, hata nikitoa shilingi haina maana yoyote kwa sababu, tumeona hapa mambo yenyewe yanavyokwenda mwisho wa yote tunapiga kura wape, wape, basi; haina maana yoyote!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, namwomba Mheshimiwa Waziri, kweli atutendee haki, atuondoe gizani; sisi umaskini wetu umechangiwa na haya mambo ya barabara na haya mambo ya umeme, huu ndio unatuletea umaskini, leo hii Liwale hakufikiki, huu umeme wa mafuta magari hayaendi! Hivi huu umeme wa mafuta utafika lini? Halafu umeme wenyewe mwisho saa nne!
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wetu ndiyo huo!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini kama ilivyowasilishwa leo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Madini nchini bado haijaeleweka hasa kwa wananchi wengi wa vijijini, jambo linalowafanya wananchi wengi kunyanyasika hasa pale ardhi yao inapogundulika kuna madini na wao kutakiwa kuhama pengine bila ya hata kujua stahiki zao, zaidi ya kuambulia mashimo. Sambamba na hilo, hata utaratibu wa upatikanaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo, hauko wazi hasa kwa watu waishio vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Liwale katika Kijiji cha Lilombe kuna machimbo ya madini ya dhahabu na sapphire, lakini wachimbaji wadogo wanapotaka leseni, hulazimika kwenda Tunduru Mkoani Ruvuma ambako ndiko kuna Ofisi ya Kanda.
Vile vile soko la madini wanayoyapata hulazimika kwenda kuyauzia Tunduru, hivyo Halmashauri ya Liwale haina mapato yoyote yatokanayo na machimbo hayo. Maeneo ya machimbo hayo ni ardhi inayomilikiwa na Kijiji cha Lilombe, lakini inapotolewa leseni wananchi hawa hawashirikishwi katika lolote. Hivyo kuweka mgogoro kati ya wachimbaji hao na Halmashauri ya Kijiji. Nini kauli ya Serikali juu ya mgogoro huu? Kwa nini kusifunguliwe Ofisi ya Madini Liwale? Kwa nini wachimbaji wasilipe ushuru kijijini ili kijiji kipate mapato yatokanayo na ardhi yao badala ya kuachiwa mashimo na mapato yaende mkoa mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Liwale iko kilometa 120 toka Wilaya ya Nachingwea ambako kuna umeme wa gesi asilia, lakini kwa masikitiko makubwa hadi leo Liwale inategemea umeme wa mafuta (generator) ambao kutokana na ukosefu wa barabara kuna wakati Liwale hubaki gizani kutokana na kukosa mafuta. Vile vile generator hilo kwa sasa limezidiwa na watumiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu wa REA kwa Wilaya ya Liwale ni wa kusuasua sana hasa baada ya kukosekana kwa umeme wa uhakika. Wilaya yenye vijiji 76 ni vijiji vitano tu vyenye umeme wa REA. Njia kuu ya umeme kutoka Nachingwea hadi Liwale ujenzi wake haujapewa msukumo unaostahili. Kumekuwepo na visingizio vingi, haijulikani kikwazo ni nini na nani kati ya Mkandarasi, TANESCO au Serikali. Namwomba Waziri mwenye dhamana kuhakikisha mradi huu unakamilika ili kusukuma maendeleo ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi (LNG – LINDI) ni bora ukaharakishwa sambamba na kulipa fidia kwa wale waathirika wa ujenzi huo. Vile vile ni jambo la kuzingatia kuwa vijiji vyote vinavyopitiwa na bomba hili la gesi ni lazima vipatiwe umeme sambamba na kuwalipa fidia watu wote ambako bomba hili limepita. Hakuna dhambi kubwa itakayofanywa na Serikali hii kama mtawanyima umeme wanavijiji Mikoa ya Lindi na Mtwara. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunisimamisha tena hapa nikichangia Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nataka niendelee kuwaasa ndugu zangu wa Kambi yetu hii ya Upinzani, hii Serikali tuendelee kuishauri wale kule tusiwape miongozo wala taarifa, wale ni washangiliaji tuwaache waendelee kushangilia. Sisi tuendelee kuishauri Serikali pengine Mwenyezi Mungu anaweza akawajalia wakaweza kuyasikia na wakayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kama ifuatavyo. Kwanza sijaelewa Watanzania tuna matatizo gani? Mwenyezi Mungu atupe nini tufike mahali tuseme Alhamdulillah tumepata tutoke hapa twende mbele? Kwetu sisi madini dhambi, mifugo hatari, kila kitu hatari! Nchi za wenzetu ardhi ni maliasili muhimu sana kwa maendeleo ya mwanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni rasilimali kubwa sana ingeweza kututoa hapa tulipo lakini ardhi hii sisi tunaifanyia nini na kwa nini tunaingia kwenye matatizo ya umaskini wakati ardhi tunayo? Inawezekana kwa sababu ya wingi wetu wa ardhi unatufanya tusijue thamani ya hiyo ardhi. Kwa sababu nchi za wenzetu kuwa na angalau heka 10 tu wewe ni tajiri, unakopesheka, taasisi zote za fedha wanakukopesha lakini ni Mtanzania gani anamiliki ardhi inayomsaidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumefika hapa? Tunatengeneza sera ambazo naona hazina maandalizi. Nitoe mfano pale kwenye Jimbo langu la Liwale, tulipata mwekezaji akajenga shule ya Kiislamu nzuri tu, lakini kupata usajili wa shule hiyo leo ni mwaka wa tano kwa sababu hawana hati miliki. Wakienda kwenye Ofisi ya Ardhi wanaambiwa kijiji ulichojenga hakijaingia kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa hiyo huwezi kupata hati miliki, tunakwenda wapi? Mtu unaandaa mradi, unakwenda kijijini unatafuta ardhi, wanakijiji wanakupa ardhi, unajenga shule ama zahanati, umeshamaliza sasa unatafuta usajili ukifika Ofisi za Ardhi unaambiwa hicho kijiji hakijapimwa, hakiko kwenye mpango bora wa ardhi, kwa hiyo hatuwezi kukupa hati, hao ni Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Wizara ya Ardhi naweza kusema ni kama Wizara mtambuka. Kuna Sera za Wizara kibao zimeingia hapa, mkanganyiko ni mkubwa, hatuelewi tunakwenda wapi. Kuna Sera ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Madini na Wizara inayoshughulika na Misitu, hawa watu wote wanavurugana tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mwingine, pale kwenye Jimbo langu walikuja hawa jamaa wa TFS, watu wa misitu, wamewapimia watu mpaka kwenye nyumba zao, kwa sababu maskini wale hawajui utaratibu ukoje, walikuja pale wakadanganywa, wakapima mpaka unakosa hata mahali pa kuchimba choo, ukitoka kidogo unaambiwa hapa ni kibao cha TFS. Hapa ndiyo mchanganyiko sasa wa makazi na misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kitu kinachonishangaza hizi taasisi ni za Serikali. Hivi inawezekanaje taasisi ya Serikali inakwenda kijijini inawadanganya wananchi, wanaingia mkenge baada ya miaka miwili, mitatu ukienda kuuliza unaambiwa ni ninyi wenyewe wanakijiji ndiyo mlipitisha hii. Tulipitisha hatukujua hilo na ninyi ni taasisi ya Serikali mlitakiwa mtoe elimu. Sasa inafika mahali wananchi wanakosa mahali hata pa kukata kuni, wanaambiwa Mwenyekiti wenu wa Kijiji ndiyo alisaini lakini alijua hilo? Ndiyo hapo unapopata mkanganyiko kwamba jamani hii Serikali tunakwenda wapi, kwa nini hii neema ya ardhi isiwe ndiyo neema kwetu iwe ni majanga? Kitu gani ambacho tunaweza tukakipata tukakiona kwamba hiki kwetu ni neema? Namwomba Mheshimiwa Waziri ashirikiane na Mawaziri wenzake waangalie hizi sera, hii mikanganyiko inatoka wapi? Wananchi wetu hawa kwa nini tuwadhulumu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee katika upande huo huo wa ardhi. Kule kwangu nimewahamasisha vijana wameunda vikundi vya ufugaji na vya kilimo, lakini wale watu wakiandika andiko watafute wafadhili wanatakiwa wapate hati, mfadhili huyo watampataje? Matokeo yake vijana wale wamekwama, hawana wanachofanya, wakija mjini mnawafukuza, sasa wafanye nini, nani mwenye jukumu la kupima hii ardhi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye viwanja. Liwale bei ya kiwanja ni ghali sana. Nimekwenda nikamuuliza Mkurugenzi kwa nini hii hali ipo hivi? Akaniambia mimi sina wapimaji, nawachukua Nachingwea. Kwa hiyo, nikiwachukua Nachingwea wanakuja hapa nawalipia hoteli na kadhalika, kwa hiyo gharama ya kupima viwanja ipo juu, watu wanashindwa kumudu kununua viwanja. Sasa hili jukumu la kupima viwanja ni la nani? Hivi unawezaje ku-hire wapimaji kutoka sehemu nyingine kwenda sehemu nyingine halafu unakuja kwa mwananchi unamwambia bwana gharama ya kiwanja imekuwa kubwa kwa sababu tuna-hire wapimaji kutoka maeneo mengine, Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu zote wananchi wetu wako mbele ya maendeleo kuliko Serikali na ndiyo hapo mgogoro unaanza. Mtu anakaa pale kesho na kesho kutwa unamhamisha eti panataka kujengwa hospitali sijui amekaa kwenye makazi yasiyo bora sijui pamefanyaje, mlikuwa wapi? Huyu mtu anaweka nguzo ya kwanza mpaka anamaliza tofali la mwisho anahamia mlikuwa wapi? Ndugu zangu, namtakia kila la kheri Waziri mwenye dhamana, lakini nataka tu nimtahadharishe kwamba uwepo wa ardhi nyingi Tanzania imeonekana hatuithamini, kama tungekuwa tunathamini ardhi leo tusingekuwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye majengo kujengwa chini ya kiwango. Naamini Shirika la National Housing lina Wahandisi wengi wa kutosha inafikaje mtu unajenga jengo linakuwa chini ya kiwango, hii ni rushwa! Mkandarasi kuipata hiyo tenda anatumia zaidi ya nusu ya fedha aliyotenda. Hivi ni injinia gani atakwenda kumsimamia yule mkandarasi kumwambia hili jengo umejenga chini ya kiwango wakati tayari ameshachukua hela kutoka kwake, anaupata wapi ujasiri wa kumkemea?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii kwa kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri kwa mikakati yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kawaida ya Serikali yetu tatizo kubwa linaanzia pale ambapo Serikali inaposhindwa kutoa fedha zilizotengwa katika bajeti hii. Wizara ya Ardhi kwangu mimi ni kama Wizara mtambuka kwani migogoro mingi husababishwa na maingiliano ya sera kama vile sera ya kilimo, sera ya mifugo, sera ya madini na kadhalika ambazo zote zinaihusu ardhi lakini ni nani anasimamia sera ya ardhi kwa upana wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi na umaskini wa watu wetu. Watanzania wengi hasa wa vijijini wanakuwa maskini kutokana na kushindwa kwa Serikali kuwamilikisha ardhi. Hivyo watu hawa hushindwa kuaminika na taasisi za kifedha, hawakopesheki na pale mwananchi anapoomba kupimiwa ardhi yake ili aweze kuwa na hati miliki gharama huwa ni kubwa sana na kuwa na milolongo mingi inayosababishwa na rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wanashindwa kuwekeza vijijini kwani kikwazo kikubwa ni vijiji vingi kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi. Kijiji ambacho hakijapimwa kwa matumizi bora ya ardhi kinakosa wawekezaji eti kwa kuwa kijiji husika hakijaingia kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi. Mfano ni jimboni kwangu Liwale wawekezaji wengi wameshindwa kusajili biashara zao kwa kuwa vijiji walivyowekeza havijapimwa kwa hiyo hao wawekezaji kukosa leseni za biashara zao. Yuko mwekezaji ameshindwa kusajili shule kwa kukosa hati miliki ya ardhi kutokana na kijiji kukosa matumizi bora ya ardhi. Vilevile kuna mwekezaji ameshindwa kusajili zahanati kwa kuwa kijiji hakijaingia kwenye matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba mkubwa wa watumishi wa kada hii kunafanya gharama ya kupima ardhi na viwanja kuwa ghali sana. Mfano Mji wa Liwale hulazimika kukodi wapimaji toka Wilaya jirani ya Nachingwea hivyo kufanya bei ya viwanja kuwa juu sana na watu kuendelea kukaa maeneo yasiyopimwa. Namuomba Waziri atuongezee watumishi ili kuhakikisha upimaji wa ardhi Jimboni Liwale unafanyika ili kuharakisha maendeleo ya Halmashauri yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro wa ardhi. Wilaya ya Liwale ina mgogoro wa muda mrefu kati ya wanakijiji cha Kikulyungu na Hifadhi ya Mbuga ya Selous. Mgogoro huu umeshaleta maafa tayari watu wanne (4) wamepoteza maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upimaji wa vijiji; Serikali iharakishe upimaji wa vijiji ili wawekezaji wanapokwenda vijijini wakute kijiji tayari kimeshafanya mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Maliasili. Wizara ya Maliasili ni Wizara ambayo nilikuwa naisubiri kwa hamu sana kwa sababu asilimia 60 ya Wilaya ya Liwale ni Mbuga ya Selous. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina wasiwasi na weledi, ufahamu na nia ya Mheshimiwa Waziri. Tunalo tatizo kama Watanzania, tunazo fursa nyingi sana Watanzania, lakini maisha yetu fursa hizi hazijawahi kutusaidia. Hivi najaribu kujiuliza nini tatizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufahamu wangu mdogo tatizo la Watanzania ni kwamba tumepoteza uzalendo wa nchi yetu, tumetawaliwa na ubinafsi. Hii ndiyo sababu kubwa inayotufanya tushindwe kufikia malengo yetu pamoja na kuwa na rasilimali za kutosha katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye vivutio vya utalii hasa malikale. Hapa tunalo tatizo la Watanzania kupoteza historia ya nchi yetu. Tunashindwa kutambua vivutio vilivyopo kwenye nchi yetu ni kwa sababu watu tumepoteza historia ya nchi yetu, hatujui historia ya nchi yetu, tumepoteza hata jiografia ya nchi yetu. Natoa wito kwa Waziri wa Elimu aimarishe somo la historia na jiografia pengine vizazi vijavyo vitaweza kukumbuka haya ninayoyasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuisahau Liwale kama utaikumbuka vita ya Majimaji. Lipo boma pale la Mjerumani linaitwa Boma la Mdachi, boma lile pale mpaka leo ziko picha za wahanga wa vita ya Majimaji, ziko sanamu za wahanga wa vita ya Majimaji. Nani analikumbuka Boma la Liwale leo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Liwale tunao mlima ule tunauita Mlima Lukundi, uko Lilombe, mlima ambao ulikuwa na volcano iliyolala, nani anaijua hii? Tumepoteza historia. Naomba turudi kwenye historia, tutaweza tu kuzikumbuka hizi rasilimali zetu kama tutakwenda na historia ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hifadhi ya Selous, asilimia 60 ya Wilaya ya Liwale imezungukwa na Mbuga ya Selous katika vijiji vya Mpigamiti, Barikiwa, Ndapata, Kimambi na Tukuyungu, lakini kuwepo kwetu Selous hakujatusaidia chochote. Nimezunguka katika vijiji hivi nilivyovitaja hatuna alama yoyote kuonesha kwamba sisi tuko karibu na Selous. Hatuna hoteli, hatuna barabara, hatuna miundombinu yoyote wala hatuna kiwanja cha ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie kwa Kusini nzima kwa upande wa utalii tumeiacha nyuma. Lindi hakuna hoteli, Mtwara hakuna hoteli. Mtwara ndiko kuna uwanja wa ndege, lakini siyo ule wa Kimataifa kama ambavyo viwanja vingine vipo. Sasa tunategemea ile rasilimali ya Kusini, ule utalii wa Kusini ni nani atakuja kuukumbuka? Kama Mjerumani anaijua Kusini kwa nini Watanzania tusiijue?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mji wa Liwale kuna kumbukumbu ya Mikukuyumbu, pale ndipo ambapo mmisionari wa kwanza kuja Pwani ya Afrika Mashariki waliuwawa pale. Mpaka leo Wafaransa wanakuja Liwale, wanakuja Mikukuyumbu kuzuru pale, lakini Watanzania hatuna habari hiyo, tumepoteza historia yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu askari wa wanyamapori, mimi nina wasiwasi na askari wa wanyamapori, aidha kwa sababu ya kutokutunzwa vizuri wanafanya haya mambo makusudi kuwachonganisha Serikali na wananchi. Kwa sababu vitendo wanavyovifanya askari wa wanyamapori havilingani na ubinadamu. Mimi nasema hivyo kwa ushahidi, ninayo picha hapa, huyu ni Mwenyekiti wa Kitongoji wa Kijiji cha Kichonda, hana mkono wa kulia, amekatwa mkono mnamo tarehe 08 Septemba, 2015 tukiwa kwenye kampeni na kesi yake imefutwa tarehe 08 Februari, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi hii kisa chake ni nini, huyu amekatwa mkono akiwa nyumbani kwake. Askari wa wanyamapori wametoka porini wamemfukuza mtu na pikipiki wamesema ameingia pale kijijini wanataka kwenda ku-search. Wanakivamia kile kijiji kufanya searching nyumba kwa nyumba. Mwenyekiti wa Kitongoji akatoka akawauliza, ninyi mmekujaje hapa? Mbona hamna kibali cha polisi? Mbona hamjasindikizwa na polisi? Mbona hamjaja ofisini? Imekuwaje muwaingilie watu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni kosa lake lililomfanya akose mkono na file la kesi yote ninalo hapa. Hii kesi imefutwa na Wakili wa Serikali. Wakili wa Serikali anasema silaha zile zilikuwa ni zaidi ya moja, kwa hiyo, haijulikani katika zile silaha ni ipi iliyomjeruhi huyu mkono, yule mshtakiwa ameshindwa kumtia hatiani kuona kwamba je, ni bunduki yake au bunduki nyingine? Ndiyo kesi ikafutwa hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hawa askari wa wanyamapori wana ajenda ya siri na Serikali yenu, inawezekana hamuwahudumii vizuri, wanafanya mambo kuwachonganisha ndiyo maana watu wengine wote hapa watasema, utampaje adhabu mtu afanye mapenzi na mti ina uhusiano gani? Tunaomba hawa askari waangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upande wa TFS. Jamani TFS ni taasisi ya Serikali, lakini hii tuiangalie, hawa TFS kwa jinsi nilivyowaona wao kazi yao ni moja tu, kufanya udalali wa mbao na mali za misitu, hawana kazi nyingine wanayoifanya. Ukiwauliza mna mikakati gani ya kuendeleza misitu, hawajui chochote. Wao kazi yao ni kugonga mbao, kugonga mali za misitu, basi wamemaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala hili la kitanda. Tunaomba hili suala la kitanda mliangalie. Kwa nini Kusini leo hii tumetengeneza vijana wajiajiri, wana viwanda vyao vidogo vidogo vya mbao, lakini havina soko. Ukinunua kiti Liwale, ukinunua kiti Kusini huwezi kukisafirisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hatujui kwamba zile mbao zote wanazotengeneza furniture ni za wizi, maana haiwezekani? Watu wanakwenda mpaka kwenye majumba, kwenye paa. TFS wanafuata mbao kwenye paa zinashushwa. Sasa mbao zimefikaje kule? Hili ni suala ambalo tunatakiwa tuliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mgogoro kwa upande wa Liwale. Mgogoro ule umetengenezwa kati ya Hifadhi ya Selous pamoja na Kijiji cha Kikulyungu, huu mgogoro ni wa muda mrefu sana. Tatizo lake ni kwamba huu mgogoro wakati walikuja kutengeneza barabara wakasema tutengeneze barabara ili tuweze kufanya patrol, lakini badala yake leo wanasema ule ndiyo mpaka wa Selous. Hata GN hawana, lakini ukienda kuwauliza hakuna wanachofanya zaidi ya kupiga watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie hiki Kijiji cha Kikulyungu leo askari hakuna anayekanyaga, hivi vijiji nimevitaja hapo zaidi ya vitano, ina maana vijiji vyote hivi vikifunga njia Selous askari wa wanyamapori hawaingii. Tutafikia huko iwapo huu mgogoro hautaweza kutatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi sasa kwenye wanyamapori, tembo, simba pamoja na nguruwe. Kule kwetu ukisikia njaa Liwale imeletwa na nguruwe, ukisikia njaa Liwale imeletwa na tembo, simba kule Liwale ni kama mbwa au kama paka wako wengi sana, tunaomba mje mtusaidie. Tunapokwenda pale kituoni kuomba msaada tunapovamiwa na simba wanatuambia usafiri hawana. Hawana askari wakutosha, watu wetu wanateseka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kabla sijaja Bungeni nilikwenda kwa Mhifadhi wa Kanda anaitwa Salum, nikamwambia Salum kinachokubakiza hapa ni uvumilivu tu wa hawa watu, siku watakapokataa huna kazi hapa. Haiwezekani watu wanauwawa, haiwezekani watu mazao yao yanaliwa wewe unakuja hapa unaleta nahau. Nikamwambia Salum tafadhali, siku nitakayokuja kusema nimechoka, huna salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtusaidie, Mikoa ya Kusini mtuwekee hata Chuo kimoja cha Misitu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mchango wangu nianze katika sekta ya utalii. Juhudi ya Serikali katika kutengeneza vivutio vya utalii bado siyo wa kuridhisha kwani kuna vivutio vingi bado hatujaweza kuvitambua na kuvitangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malikale, ukanda wa Kusini kuna vivutio vya malikale kama vile Boma la Mdachi (Wajerumani) lililojengwa miaka ya 1904 -1907 wakati wa vita vya Majimaji Mjini Liwale. Ndani ya boma hili kuna mabaki ya sanamu na michoro ya watumwa kwa ajili ya biashara ya utumwa.
Vilevile katika ukanda wa Liwale kuna milima ya Rondo yenye misitu na vipepeo ambao hawapatikani popote duniani. Tunayo pia bwawa la Mlembe na Kiulumila. Haya ni mabwawa yenye mamba na viboko wenye kuwasiliana na wazee wa mila zetu.
Kuhusu ulinzi wa misitu yetu siyo wa kuridhisha. Kuna Mamlaka ya Uvunaji wa Mali ya Misitu (TFS). Taasisi hii imekuwa kero kubwa kwa watu wanaokaa karibu na hifadhi zetu. Badala ya kuwa na wastawishaji wa misitu wamekuwa waharibifu wakubwa wa misitu yetu. TFS wanatuhumiwa kila mahali kuwa wao ndiyo waharibifu wakubwa wa misitu yetu. Kazi kubwa inayofanywa na watu hawa ni kugonga mihuri tu na kusafirisha mazao ya misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya mipaka, kumekuwa na migogoro mingi ya mipaka kati ya hifadhi zetu na wanavijiji. Hali hii huchangiwa sana na watendaji wa hifadhi kusogeza mipaka bila kushirikisha jamii husika. Mfano mgogoro wa kijiji cha Kikufungu Wilayani Liwale uliosababishwa na wahifadhi kuhamisha mpaka wa hifadhi bila kushirikisha jamii. Mgogoro huu una zaidi ya miaka kumi sasa. Hadi sasa zaidi ya watu wanne wamepoteza maisha na kuharibu kabisa mahusiano ya askari wa hifadhi na wanakijiji. Aidha, kijiji cha Ndapata wako watu wawili wamepoteza maisha kwa sababu ya mgogoro huu wa mipaka.
Kijiji cha Kichonda Mwenyekiti wa Kitongoji mwezi wa 8 mwaka 2015 amekatwa mikono na askari wa wanyamapori hadi leo hakuna kesi wala fidia juu ya kadhia hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Lindi sehemu kubwa ni sehemu ya Selous lakini kwa masikitiko makubwa Mkoa huu hauna manufaa yoyote na Selous. Mkoa wa Lindi hasa Wilaya ya Liwale hakuna hoteli ya kitalii Mkoa wa Lindi pia kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Lindi hakijapanuliwa na kuwa na hadhi ya kuwezesha ndege kubwa kutua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nangurukuru - Liwale ndiyo barabara ingewapeleka watalii kwenye hifadhi hiyo. Kanda ya Kusini haina Chuo cha Misitu Kanda nzima. Eneo kubwa la Hifadhi ya Selous ipo Mkoa wa Lindi Wilaya ya Liwale. Kuhusu ulinzi shirikishi, Serikali imeweza sana kwenye ulinzi wa silaha na mabavu kama njia pekee ya kulinda hifadhi zetu, jambo ambalo halina tija kubwa zaidi ya kuongeza uhasama baina ya wahifadhi na jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika hili Serikali ijikite zaidi katika kutoa elimu juu ya ulinzi shirikishi sambamba na kuwaonyesha wananchi faida itokanayo na hifadhi zetu. Kwa mimi nadhani walinzi wa kwanza wawe wale watu wanaozungukwa na hifadhi husika badala ya kutumia silaha zaidi na kuendelea kuua watu na kuongeza uhasama. Mkoa wa Lindi hatujaona faida ya moja kwa moja inayotokana na hifadhi ya Selous zaidi ya kushuhudia mauaji.
Kuhusu uhaba wa watumishi na vitendea kazi, kwa Wilaya ya Liwale uhaba wa watumishi wa wanyamapori kumesababisha hasara kubwa sana kutokana na wanyama kuharibu mashamba ya wakulima. Ukienda kutoa taarifa watakujibu hawana gari au watumishi wa kwenda kuwasaidia watu hao wa vijiji vya Mpigamiti, Barikiwa, Kimambi, Kikulyungu na Ndapata wanakabiliwa na njaa mara kwa mara kutokana na mazao yao kuliwa au kuharibiwa na wanyama kama tembo na nguruwe. Nguruwe wamekuwa ni tishio kubwa sana kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la watu kuliwa na simba Wilayani Liwale ni kubwa sana hasa baada ya watu kunyang‟anywa silaha zao kwenye Operesheni Tokomeza. Wizara ifikirie namna bora ya kuanza kurudishiwa silaha watu wale ili zisaidie kuimarisha ulinzi vijijini hasa zile silaha ndogo ndogo. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii kwa dakika tano hizi. Nami nichangie Wizara hii ya Maji. Sina wasiwasi na dhamira ya Mawaziri wote wawili wa idara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu ni hizi takwimu. Takwimu hizi tunazoletewa, nina wasiwasi nazo kwa sababu hapa takwimu inasema kwamba, wanaopata maji safi na salama imefikia asilimia 72, hapo ndipo wasiwasi wangu unapoanzia, ndipo hapo unapokuja umuhimu wa kuwepo na Mamlaka ya Maji Vijijini, kwa sababu najua hizi takwimu siyo wao wamezileta ila wao wameletewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano; kwenye jimbo langu tunapata maji kwa asilimia 47 katika mradi wa Vijiji 10, vile ambavyo World Bank walitoa fedha, sisi tumefanikiwa kupata vijiji vitatu tu ambavyo sasa maji yanapatikana. Katika vijiji 76, tumepata vijiji vitatu tu, ambavyo ni Vijiji vya Mpigamiti, Mbaya na Barikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kulikuwa na mradi wa kutafuta chanzo cha maji kwa ajili ya maji ya Liwale Mjini. Palitolewa pesa, shilingi milioni 200, lakini katika zile pesa, mpaka sasa hivi shilingi milioni 55 zimeshatumika na bado chanzo mbadala cha maji hakijapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 20 zimetumika katika kutafuta chanzo cha maji katika Mji wa Makunjiganga lakini maji hayajapatikana. Shilingi milioni 35 zimetumika katika Kijiji cha Mikunya, pale kumepatikana maji ya lita 5,000 kwa saa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya Wilaya ni lita 25,000 kwa saa. Kwa hiyo, Mkandarasi Mshauri akasema, pampu ile sasa ifungwe kwa ajili ya Vijiji vya Mikunya na Liwale „B‟. Kwa hiyo, chanzo cha maji katika Liwale Mjini bado ni kitendawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tulikaa kwenye kikao cha Halmashauri, tukawashauri, badala ya hizi pesa kuendelea kutafuta vyanzo, zitakwisha shilingi milioni 200 bila kupata chanzo mbadala. Tukaiagiza Halmashauri sasa ifanye utaratibu mwingine labda tutafute kuchimba mabwawa; labda tuvune maji kwa mabwawa badala ya kuendelea kutafuta vyanzo mbadala kwa sababu hakuna mahali ambapo itachimba, utapata maji yenye ujazo wa lita 25,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tuna Vijiji vifuatavyo ambavyo kwa shida ya maji iliyopo Liwale, watu wanahama kuanzia asubuhi wanarudi jioni na ndoo moja. Vijiji kama Kichonda, Kipule Magereza, Kiangara, Mbumbu, Nangano, Kikulyungu, Mkutano, Miluwi na Makata; hivi vijiji watu wanaamka asubuhi, wanarudi jioni na ndoo moja. Sasa ninapoambiwa kwamba kuna asilimia 72 ya watu wanaopata maji, napata wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye miradi ya umwagiliaji; tunayo miradi miwili ya umwagiliaji katika Jimbo langu. Kuna mradi wa Ngongowele. Ule mradi wa Ngongowele umeshakula pesa zaidi ya shilingi bilioni moja mpaka sasa hivi zimeteketea na ule mradi umesimama. Tulipokwenda kuwafuata pale, Mkandarasi Mshauri anasema ili huu mradi uweze kuendelea, panatakiwa bilioni nne ili uweze kutumika masika na kiangazi. La sivyo, utumike kwa masika tu, panahitajika shilingi milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mradi kutumika masika tu, wanakijiji hawako tayari. Wanasema kama mradi unatumika masika tu, sisi masika tunalima. Sisi tulivyokubali huu mradi lengo lilikuwa utumike masika na kiangazi. Kwa hiyo, hata kama zitapelekwa shilingi milioni 800 leo, ule mradi wanakijiji hawako tayari kuupokea kwa sababu hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi wa Mtawango, nashukuru Alhamdulillah kwamba sasa hivi unaendelea vizuri, umefikia asilimia 95. Ushauri wangu, kama ambavyo wachangiaji waliotangulia walisema, kweli tunahitaji Mamlaka ya Maji Vijijini kwa sababu hawa Wakandarasi na Wasimamizi wa miradi hii Vijijini hakuna wasimamizi wa kutosha. Kwa ilivyo jiografia ya Liwale, juzi nilikuwa naongea na Naibu Waziri, nafikiri; ameshindwa kufika Liwale kukagua ile miradi miwili kwa sababu ya jiografia ya Liwale, hakufikiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Liwale tunakwenda sisi tunaokujua, lakini kwa watu kama Mawaziri kama ninyi kufika Liwale inakuwa ni shida. Sasa itakapoundwa hii Mamlaka ya Maji nafikiri hawa ndio wanaweza kufanya usimamizi huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hivyo tu, katika Halmashaui ya Wilaya ya Liwale, tunao uhaba wa mafundi kwa maana ya wataalam. Mtaalamu aliyepo pale mwenye cheti ni mmoja tu, wengine wote waliopo ni mafundi wa spana tu wa mitaani. Kwa hiyo, hili nalo ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii miradi ya vijiji hivi vitatu nilivyovitaja, kuna kijiji kimoja kisima kimechimbwa; Kijiji cha Kiangara, kijiji hiki maji ni ya chumvi, hayatumiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri, nimeona kuna shilingi milioni 300 nyingine zimetengwa hapa. Naendelea kusisitiza kuhusu usimamiaji wa hizi fedha. Kama tusipopata usimamizi wa kutosha, kitakachotokea ni hiki hiki ambacho kimetokea kwenye hizi shilingi milioni 200 za awali na hii miradi ya kwanza Vijiji 10 na badala yake tukaambulia vijiji vitatu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naomba kwa sababu nilipewa tu dakika tano na shida yangu ilikuwa ni hiyo tu, naomba niishie hapo. Ahsanteni sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii jioni hii. Naomba niende moja kwa moja kwenye mchango wangu nikiangalia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye huu mpango. Nimesoma vipaumbele vyote vilivyotajwa sijaona kipaumbele cha kilimo na sisi tunajitangaza kwamba tunataka kwenda kwenye Taifa la viwanda. Lakini kwenye miradi hii ambayo imetekelezwa, hakuna mradi hata mmoja wa kilimo uliotajwa hapa. Nikifika na kwenye miradi ambayo inatekelezwa nako vilevile sijapata mradi hata mmoja wa kilimo unaotekelezwa zaidi ya kuona kuna Kijiji cha Kilimo Morogoro. Sasa je, hilo shamba ni la mazao gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu, ulaji wetu kama Watanzania sasa hivi umebadilika, sasa hivi tunakula sana kwenye mazao ya chakula (ngano) kuliko mazao ya mahindi au mchele kama tulivyozoea. Lakini kwenye mpango huu sijaona mahali popote ilipotajwa kuendeleza hili zao la ngano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mashamba ya ngano NAFCO, yale mashamba sijui yamepotelea wapi. Na hapa nataka ni-declare interest, mimi ni msindikaji wa nafaka. Ngano hii kiwanda kimoja cha Bakhresa peke yake anasindika tani 2,700 per day na hizi tani 2,700 anazosindika kwa siku zinatoka nje a hundred percent, Tanzania tumelala. Leo hii tunakuja tunasema kwamba tunataka kuimarisha viwanda, hapo napo sijapaelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nirejee kwenye takwimu, hizi takwimu za Mheshimiwa Mpango bado hazijanishawishi. Kwa sababu kwenye akiba ya fedha, pesa za kigeni, tunasema tunayo akiba ya pesa kuendesha miezi 4.1, hapohapo mwisho kabisa anasema kwamba hii ni zaidi ya lengo la chini kabisa ambalo ni la miezi minne. Huko kuongeza tu kwa pointi moja tayari ni sifa kwetu kuona kwamba tumepiga hatua, lakini je, hizi takwimu zinalingana na takwimu za ongezeko letu Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana unaweza kujisifu kwamba wewe ni mtu wa kwanza darasani kwa kupata asilimia 30, ndiyo hiki ninachokiona hapa, lakini kama kweli tuna nia nzuri ya kuwatendea haki Watanzania, naomba kabla hatujafika kwenye mpango huu turejee kwanza kwenye sensa ya watu waetu ili huu mpango na haya maendeleo tunayojisifu kwamba uchumi wetu unaimarika, unalingana na idadi ya watu tulionao unaowahudumia huu mpango? Ndiyo maana leo hii Serikali inasema uchumi umeimarika, lakini kwa watu tunaokaa nao wanaona hakuna kitu kinachofanyika, ni kwa sababu ule uchumi unaowahudumia ni wengi kuliko hivyo mnavyotarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka nijielekeze kwenye kufungamanisha maendeleo ya watu na uchumi, hapa napo mmetuacha mbali sana. Leo hii tunaposema hivi, tumeacha vijana wanahangaika, kilimo ambacho kinaajiri watu wengi bado ni kilimo chetu kilimo cha mkono. Zipo taasisi zinakopesha matrekta kwa ajili ya kilimo, lakini hizi taasisi sharti la kwanza uwe na hatimiliki ya shamba. Leo hii nani mkulima wa kijijini anaweza ku-access kupata hatimiliki ya shamba, tunawaacha wapi hawa vijana, na hii tunaposema tunafungamisha maendeleo ya uchumi na watu wetu tumewaacha wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, turejee kwenye sekta binafsi, sekta binafsi sasa hivi ndiyo imechukua ajira kubwa sana, lakini hivi asubuhi hapa nimeuliza swali, ni asilimia ngapi ya Watanzania wana hudumu kwenye hivyo viwanda. Lile swali nimeuliza asubuhi hapa sasa nina messages zaidi ya 100 kwenye simu yangu, watu wanasema kweli wanateseka. Nimepigiwa simu kutoka Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, watu wanalalamika, hivi viwanda wanahudumiwa na watu wa nje tu, hakuna Mtanzania anakwenda pale akapata ajira, lakini Watanzania bado tunasema tunahimiza uwekezaji. Lakini je, tunapohimiza uwekezaji tupo tayari kufuatilia hawa wawekezaji kwamba wanakidhi masharti ya nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kwa upande wa umiliki wa ardhi. Kumiliki ardhi hapa kwetu tatizo ni kubwa sana na hakuna mtu ambaye anaweza ku-access, mtu wa kijijini akaweza kupata hakimiliki. Upimaji sasa hivi wanasema kwamba eka moja ni shilingi 300,000, kitu kama hicho. Sasa hivi mtu wa kijijini ili aweze kupata shamba la eka 10, 20 atahitaji pesa kiasi gani na atazipata wapi? Kwa hiyo, naona huu mpango, pamoja na kwamba nia ni nzuri, lakini utekelezaji wake na upangaji wake haufanani na hali halisi ya watu wetu wanavyoishi huko vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwa upande wa…
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na mchango wangu kwa kuangalia vipaumbele vya mpango wenyewe kuelekea Tanzania ya Viwanda. Nilitegemea kuona kilimo kikipewa kipaumbele katika mpango huu, lakini imekuwa kinyume chake sijaona mahali popote pakitajwa kama kipaumbele kwa kilimo cha mazao kama korosho, pamba, katani, ufuta na kadhalika ilikuwa malighafi katika viwanda hivyo. Hata hivyo, sijaona zao la ngano likitajwa popote wakati sasa ulaji wa watu nchini sasa umebadilika kwani sasa ngano huliwa zaidi kuliko mchele, mahindi na mazao mengine ya chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano katika hili kama ifuatavyo:-
Kampuni ya Bakhresa peke yake kwa siku wanasindika tani 2700 za ngano ambazo zote zinatoka nje ya nchi. Katika miradi iliyotekelezwa hakuna mradi wa kilimo zaidi ya kuona mradi wa kuendeleza Kijiji cha Kilimo Mkoani Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda sijaona kiwanda chochote kilichotajwa katika viwanda vinavyotarajiwa kukuza uchumi zaidi ya General Tyre na makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga. Katika fungamanisha maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya watu hakuna uhalisia kwani hatujawaandaa vijana nchini kushiriki katika uchumi wa kilimo wala viwanda. Wakulima wetu wanashindwa kuondokana na jembe la mkono kwa kuwa hawakopesheki katika taasisi za fedha. Kwani gharama za kupata hati ya kumiliki mashamba bado ziko juu sana kwani hilo nalo sharti kuu kwa taasisi zinazokopesha vifaa ya kilimo kama tractor, hivyo kuwafanya wakulima kushindwa kulima kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilwa sasa imeanza kutoa madini ya gypsum ambayo sasa yanatumiwa na viwanda vyote vya cement nchini. Hata kusafirishwa kwenye nchi za Zambia, Malawi na Afrika Kusini, lakini sijaona mahali ilipotajwa katika mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa ya Waziri wa Fedha kwa robo ya kwanza, sekta yenye ukuaji mdogo ni sekta ya usambazaji wa maji safi na udhibiti wa maji taka, pamoja na chakula na malazi, hivyo basi kutarajia kupata maendeleo toka kwa jamii yenye huduma hafifu kiafya ni sawa na kukamua ng‟ombe bila malisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu yetu bado ni ya kutegemea ajira kutoka Serikalini au sekta binafsi kwani wahitimu wetu wameshindwa kupata stadi za maisha kulingana na elimu wanayoipata. Vilevile kama hatutakuwa tayari kuboresha maisha ya Walimu na badala yake kuendelea kuwadhalilisha Walimu kwa kuwapa adhabu mbalimbali kama vile kuwapiga viboko mbele ya wanafunzi hakuinui ari ya Walimu hawa ya kufundisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda; mlundikano wa viwanda katika Mji wa Dar es Salaam hasa kwa viwanda vinavyotegemea malighafi toka nje ungeweza kupunguzwa na kusambaza viwanda hivyo mikoa mingine ya nchi yetu. Ikiwa wawekezaji wangeondolewa kodi kwa wale watakaowekeza nje ya Dar es Salaam ili gharama zilingane na yule aliyewekeza Dar es Salaam. Kwa kiwanda kinachofanana kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kupanua ajira kwa vijana wa mikoa mingine kwa upatikanaji wa ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, sensa ya watu ni muhimu sana kwa sasa kwani takwimu tunazoletewa leo hazina uhalisia ukilinganisha na idadi ya watu. Hayo maendeleo ya kukua kwa uchumi tunayapima kwa kigezo gani wakati hatuna takwimu halisi ya idadi ya watu wetu. Ndio maana matamko mengi ya Serikali kuhusu huduma za jamii yanakosa uhalisia kwa wananchi wa hali ya kawaida. Haingii akilini mtu kuambiwa uchumi unakua wakati kipato cha mtu mmoja mmoja kinashuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshauri Waziri mwenye dhamana ni bora akazingatia ushauri wa Wabunge ukizingatia ndiyo wawakilishi wa wananchi. Tunashauri kwa niaba yao kulingana na hali halisi ya maisha ya Mtanzania wa hali ya chini wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie kwenye hotuba hizi mbili. Awali ya yote nichukue fursa hii kuwashukuru sana Wenyeviti wa Kamati kwa hotuba nzuri walizotuletea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mchango wangu niuelekeze kwanza kwenye upande wa maji. Asubuhi nimeuliza swali la nyongeza hapa jibu nililolipata ni tofauti na matarajio. Mimi nimeongelea Mradi wa Ngongowele nimejibiwa mradi wa kijiji kingine tofauti kabisa na mtaa wangu. Mradi wa Ngongowele umegharimu shilingi bilioni nne mpaka sasa hivi hauna maendelezo yoyote yale na hautegemei kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika Mji wa Liwale kuna mradi wa World Bank pale kutafuta chanzo mbadala cha maji umegharimu shilingi milioni 200 nao mpaka leo hii unasuasua mradi huo haujaendelea. Kwa hiyo, kwa ujumla wake katika Halmashauri ile kuna shilingi 4,200,000,000, naomba Kamati inayohusika hebu nendeni mkaangalie ili muweze kuishauri Serikali nini cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika ule mradi wa maji wa vijiji kumi, Liwale nimepata vijiji vitatu tu, kijiji cha Barikiwa, Namiu na Mpigamiti lakini kuna miradi ambayo mpaka sasa hivi imesimama na hakuna kinachoendelea ambayo ni miradi ya kijiji cha Kipule, Kiangara, Mikunya, Mpengele, Kimambi, Nangorongopa, Nahoro na Kitogoro. Kwa hiyo, naiomba Kamati hii kama itapata wasaa hebu iweze kutembelea Jimbo lile la Liwale muone pesa za nchi hii zinavyoharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda Idara ya Maliasili. Nimeshasimama hapa mara nyingi na nimeshaongea sana, lakini nataka niongelee mgao wa asilimia 25. Kwenye Jimbo langu la Liwale hatujapata huu mgao wa asilimia 25 pamoja na kwamba hatujui asilimia 25 inatokana na mauzo gani lakini walituambia kwamba Halmashauri zote zinazozunguka Hifadhi tutapata mgao wa asilimia 25 kutoka kwenye Serikali Kuu kama ruzuku inayotokana na mauzo ya maliasili ya misitu lakini mpaka leo hii jambo hili halijatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye upande wa Maliasili nikiongelea upande wa malikale. Sisi pale tuna jengo lile la Wajerumani ambalo ni kumbukumbu ya Vita ya Majimaji mpaka leo hii yapo majina kwenye zile kuta, lakini Mheshimiwa Waziri nilisikitika sana nilipouliza hili swali akaniambia kwamba Halmashauri ndiyo tuifanye hiyo kazi ya kuendeleza lile jengo ili kuweka kumbukumbu. Sijui ana maana kwamba sisi tufungue website yetu, tuutangaze utalii wa Liwale kwa kutangaza maliasili ile, mimi sijaelewa. Kwa hiyo, naomba Waziri mwenye dhamana hebu atueleze ile malikale inayopotea pale mpango wake kwa Serikali hii ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye upande wa kilimo ambapo tuna tatizo la pembejeo, wengi wameshaliongea kwanza haziji kwa wakati. Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Liwale kwa ujumla wake safari hii tumepata viatilifu fake ambavyo vimetupelekea kupata mazao hafifu ya korosho. Ukienda kwa mawakala wale wanaouza pembejeo za kilimo, utakuta ana stock mbili; maana kule kiatilifu kikubwa ni sulphur, anakwambia hii ni sulphur ya ruzuku na hii hapaya kununua. Ukichukua ile sulphur ya ruzuku ni kwamba umeumia, lakini ukichukua ile sulphur ambayo inauzwa cash ndiyo inaweza ikakuletea mazao mazuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika,
ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo ili na mimi
niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo ada, naomba
nijielekeze moja kwa moja kwenye hotuba hii nikilenga
kwanza hii Taasisi ya Uvunaji wa Misitu (TFS). Kama ambavyo
unafahamu 60% ya Wilaya ya Liwale inazungukwa na misitu, kwa hiyo, uchumi mkubwa wa watu wa Liwale unategemea
sana maliasili za misitu pamoja na wanyama. Kwa hiyo,
naomba moja kwa moja nianzie huko.
Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri Mkuu au
Wizara inayohusika walete hapa marekebisho ya Sheria ya
TFS. TFS kutupatia sisi Halmashauri 5% ya uvunaji wa mazao
ya misitu kwa kweli ni kutokututendea haki. Ukienda kuangalia
Liwale jinsi magogo yanavyovunwa pale, miti inavyohama
na faida wanayoipata Wanaliwale wale kwa 5%, tena hiyo
5% yenyewe namna ya kuipata ni kwa shida kwelikweli.
Naomba hii sheria iletwe hapa irekebishwe, 5% ni ndogo
sana.
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba niuelekeze
mgogoro wa Hifadhi ya Selou pamoja na Wanakijiji wa
Kikulyungu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa nini nauelekeza
mgogoro huu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu? Ni kwa sababu
kwenye Wizara husika naona mgogoro huu umeshindikana.
Kwa hiyo, naomba moja kwa moja kwa nafasi hii niuelekeze
mgogoro huu kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu pengine tukapata
msaada ili wale wananchi wa Kikulyungu wakaepukana na
adha wanayoipata leo hii ya kupigwa vibaya na Askari wa
Wanyamapori.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba
nijielekeze kwenye upande wa takwimu. Sensa ya mwaka
2012 kwa kweli sisi Wilaya ya Liwale imetuathiri sana.
Imetuathiri kwa maana ya kwamba, imeonesha wakazi wa
Wilaya ile ni kidogo sana. Nitoe mfano ufuatao. Wilaya ya
Liwale kwenye Basket Fund tunapata Sh.8,000,000/=, Wilaya
ya Nachingwea Sh.18,000,000/=, Wilaya Kilwa Sh.17,000,000/
=, Wilaya ya Ruangwa Sh.21,000,000/=. Basket Fund, Liwale
350, Ruangwa bilioni 1, Kilwa milioni 600, Nachingwea milioni
800 lakini sisi hii idadi tuliyonayo sio kweli kwamba Wilaya ya
Liwale yenye Kata 20 ina watu 92, siyo kweli, hii takwimu sio
sahihi.
Mheshimiwa Spika, nashindwa kuwaelewa hawa
watu wanaosimamia hizi takwimu. Katika Mkoa wa Lindi, Hospitali pekee inayoona wagonjwa wengi kwa mwezi ni
Hospitali ya Wilaya ya Liwale lakini ndio hospitali pekee
inayopata mgawo mdogo. Naomba nilielekeze hili kwenye
Ofisi ya Waziri Mkuu ili liweze kupatiwa ufumbuzi.
SPIKA: Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, kuna taarifa.
TAARIFA...
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika,
ahsante. Napokea taarifa yake kwani haijapingana na
nilichokieleza lakini bado narejea palepale, kama takwimu
za hospitali zinaletwa kila mwezi kwamba katika Mkoa wa
Lindi hospitali inayoona wagonjwa wengi ni ya Wilaya ya
Liwale. Sasa ni mwenye akili gani timamu hiyo hospitali
inayoona wagonjwa wengi akaipa mgawo kidogo? Napata
wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze kwenye
upande wa hiyohiyo takwimu inatuathiri vilevile kwenye
mgawo wa wafanyakazi kwa maana ya ikama ya
wafanyakazi. Ikama ya wafanyakazi kwa upande wa elimu,
ikama ya wafanyakazi kwa upande wa afya, tuna matatizo
sana. Mpaka leo hii ninavyoongea kwenye Bunge hili Tukufu,
Liwale hatuna daktari bingwa, tuna uhaba wa madaktari,
tuna uhaba wa walimu wa sekondari, lakini ukiuliza
unaambiwa kwamba wale waliopo ndio wanafanana na idadi ya watu walioko kule wakati sio kweli. Naomba hizi
takwimu zirekebishwe, kama ripoti unaletewa ya idadi ya
wanafunzi iweje sasa ushindwe kuitumia ripoti hiyo uende
mwaka 2012? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naingia kwenye vyama vya
ushirika. Vyama vya ushirika naomba iletwe sheria hapa ili
tufanye marekebisho, vyama vya ushirika wawekewe
masharti namna ya kuajiri wahasibu. Tumepata matatizo sana
mwaka huu, kwenye Chama Kikuu cha Lunali hawajawahi
kupatiwa fedha kama mwaka huu lakini wamevurunda
mpaka sasa hivi vyama vya ushirika wameshamaliza pesa
lakini wakulima hawajapata hela. Sawa, wale viongozi wa
vyama vya msingi tutawapeleka Mahakamani watafungwa
au watafilisiwa lakini bado mkulima aliyepeleka korosho
yake mwezi wa 10 mwaka jana mpaka leo hajapata hela.
Kufungwa au kupelekwa Mahakamani kwa huyu mtu
mkulima yule imemsaidia nini?
Mheshimiwa Spika, leo hii mwezi wa Nne tunaandaa
mashamba lakini mtu amepeleka korosho mwezi wa 10
mpaka leo hajapata pesa. Ombi langu ni kwamba, Sheria
ya Vyama vya Ushirika iletwe hapa, tuwaundie sheria ili ajira
za vyama vya ushirika ziendane na taaluma. Kwa sababu
tatizo kubwa tulilolipata safari hii ni watu hawana taaluma
ya uhasibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye Sera ya Wazee.
Sera ya Wazee imetungwa nafikiri tangu mwaka 2003 lakini
mpaka leo Sheria ya Wazee haijawahi kuletwa kwenye Bunge
hili, sijui mmekwama wapi? Naomba niwaambie
Waheshimiwa Wabunge hapa ndani sisi wote hapa ni wazee
watarajiwa. Tunapolichelewesha hili tunajichelewesha sisi
wenyewe na waathirika wakubwa ni sisi, leo vijana, kesho ni
wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza sana
wenzetu Zanzibar pamoja na uchumi wao kuwa hafifu lakini
wamewakumbuka wazee angalau hata kuwapa Sh.200/=.
Leo hii Tanzania Bara tumenyamaza, hata hiyo Sh.10,000/= tuliyoambiwa watapewa mpaka leo haijulikani, tutafikaje
huko hata sheria yenyewe haijaletwa hapa? Naomba sana
Sheria hii ya Wazee iletwe hapa ili tuone wazee sisi watarajiwa
huko mbele tumejiwekea akiba gani?
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napenda
nizungumzie kuhusu bajeti. Watu wengi sana
wamezungumzia kuhusu upelekaji wa fedha kwenye miradi
ya maendeleo, kwenye OC, siyo mzuri. Jamani, hapa tatizo
siyo upelekaji, hela hakuna! Mimi sidhani kama Serikali wana
pesa halafu hawapeleki! Tuseme kweli kwamba pesa hizo
hazipo, makusanyo hayo hayapo! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri wa Fedha
anieleze pengine mimi kwa sababu ya elimu yangu ndogo
sielewi. Hizi figure hizi zinazokuja hapa kila mwaka ambazo
hata 50% tunashindwa kuzifikisha zina maana gani? Kuna
tofauti gani leo hii tukasema kwamba hii bajeti yetu ni ya
shilingi trilioni 18 badala ya kuweka 30? Shilingi trilioni 18
tunaweza tukaifikia! Kwa nini tunaweka shilingi trilioni 31
ambayo mwisho wa siku hata shilingi trilioni 20 hatufiki! Kuna
sababu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Waziri
mwenye dhamana anisaidie ili na mimi nipate uelewa ili siku
nyingine nisije nikasimama tena hapa nikauliza kuhusu jambo
hilihili. Kwa nini tunaletewa hizi figures kubwa kubwa ambazo
hazina mwisho?
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naomba
niongelee walimu. Kuna tatizo kubwa sana la matokeo.
Matokeo ya elimu mwaka huu, kwa mfano kama Mkoa wa
Mtwara, Mheshimiwa Spika shahidi, Mkuu wa Mkoa
ametimua watu, amepunguza watu lakini mimi nasema hii
siyo solution, solution ni kuangalia maisha ya walimu.
Mheshimiwa Spika,
walimu wetu tumewasahau na kama tumesahau walimu
na elimu nayo tunaisahau. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kuchauka.
Tupelekee salamu kule Liwale Mjini pale Makunjiganga,
Nangano, Kimambi unapoelekea Kilwa, Kikulyungu
unapoelekea Nachingwea, Mtawatao kwenye mpunga,
Ndapata unapopakana na Selou, Barikiwa. Liwale sio ya
kwako peke yako bwana. Mheshimiwa Kakunda.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii niwe mchangiaji wa kwanza na mimi mchango wangu utajikita sana kwenye hii Taasisi ya Utafiti wa Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno ya utangulizi, Watanzania tumekuwa Wataalam wazuri sana wa kutunga sheria kama ambavyo tuko wataalam wazuri sana wa kupanga mipango, tatizo letu kubwa liko kwenye upande wa utekelezaji, kwamba ni nani anaingia kwenye utekelezaji. Kwa hiyo, kuja na Muswada huu, Serikali imeleta Muswada huu ni mahali pake kabisa kama ambavyo kauli mbiu inavyosema kwamba tunakwenda kwenye nchi ya viwanda na hatuwezi kwenda kwenye nchi ya viwanda kama tukisahau kilimo na hatuwezi kufanikiwa kwenye kilimo kama hatukuweza kufanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema, tatizo langu ni matumizi ya hizi tafiti. Je, tuko tayari kutumia hizi tafiti? Je, tunao wataalam wa kutosha wa kutafsiri hizi tafiti? Je, tuna mikakati ya kufikisha matokeo ya hizi tafiti kwa walengwa? Hapo ndipo ambapo napata ukakasi kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu muundo wa Bodi ya Utafiti wa Kilimo, hapa naona pana upungufu kidogo, sijawaona watu wa Bodi za Mazao, kwa sababu hawa watu wa Bodi za Mazao ndiyo hasa mara nyingi wako na wakulima wa mazao husika, lakini hapa kwenye Bodi hii hawa Watafiti wa mazao sijawaona, badala yake nimekuta hapa hii namba 5(2) kuna Mkurugenzi wa Halmashauri, nafikiria badala ya kumweka huyu Mkurugenzi wa Halmashauri tungemweka Mwakilishi yeyote kutoka kwenye Bodi ya Mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Namba Nne, unakutana na kazi za taasisi, moja ya kazi za taasisi nimeona hapa wameandika kuhamasisha matumizi ya mbegu bora. Matumizi ya mbegu bora ni lazima yaende sambamba na matumizi ya pembejeo za kilimo, sasa nazo hapa sijaona, Ningependekeza kazi mojawapo hawa Watafiti angalau wangepewa ni hii ya kuhamasisha matumizi bora ya mbegu na viuatilifu kama mbolea na pembejeo nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye muundo tumeambiwa patakuwa na Baraza, hili Baraza nalo sijaona katika wawakilishi sehemu hii namba 12, sijaona Mwakilishi hapa kutoka Bodi ya Mazao, bado wanaendelea kusahaulika hawa na hawa mara nyingi wana vikao vya Bodi vinakaa at least kila mwaka kufanya tathmini ya mazao mbalimbali. Ningetegemea kwamba pangekuwepo na ripoti ya utafiti ikaletwa kwenye vikao hivi vya Bodi vikatusaidia, lakini hapa napo sijaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu matokeo ya utafiti. Sijaona mkakati kwenye Muswada huu ni namna gani matokeo ya utafiti yatawafikia walengwa ambao ndiyo hasa wazalishaji. Kwa sababu tunayo matatizo, nikitolea mfano, mimi ni mdau wa zao la korosho, kwenye zao la korosho tunayo matatizo na hawa watu wa utafiti, mara ya mwisho tuliambiwa pembejeo, viuatilifu wanasema vile vya maji ni bora zaidi kuliko vile vya unga. Tukaja tena tukaambiwa lakini vile viuatilifu vya kimiminika (maji) vinatumika masika, wakati korosho sisi tunapulizia kiangazi, sasa bado tunapata mkanganyiko na mkanganyiko huu ulitakiwa tupate majibu kutoka kwa hawa Watafiti wanatusaidiaje, lakini utaona kwamba chain ya kutoka kwa Watafiti mpaka kwa watumiaji sijaiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea hapo kwenye korosho, tumeletewa mbegu tukaambiwa hizi mbegu ni za muda mfupi. Ni kweli baada ya miaka mitatu hii mikorosho huwa inazaa lakini tatizo lake iko kwenye lifetime ya mkorosho. Ile mikorosho yetu ya asili hata miaka 20 unavuna tu, lakini hii mikorosho ambayo imeletwa na hawa watafiti bado inatupa shida. Utakuta kwamba tunakosa watu sasa wa kuja kututafsiria au kutuelekeza kwamba hii mikorosho itakaa kwa muda gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye jedwali namba moja, sehemu ya tatu. Kuna hawa Wajumbe wa Bodi, inasemwa kwamba pakiwa na mgongano wa maslahi, kuna neno limetumika hapa kwamba ikiwezekana, sijaelewa unaposema ikiwezekana maana yake nini, kwamba it is optional, anaweza aka-declare au la. Mimi naona hapa kipengele hiki nacho kingeweka wazi ili na sisi watumiaji wa hii sheria tuweze kupata ufafanuzi unaoridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utafiti, nimeangalia kwenye huu Muswada wote, mkazo kwenye utafiti wa masoko sijauona na tatizo kubwa la mazao ya kilimo ni masoko. Kwa sababu hata ukiangalia upungufu wa uvunaji au uzalishaji unategemeana na soko. Mfano kule kwetu tunalima sana korosho, ufuta na mbaazi, haya mazao yana matatizo ya kubadilishana masoko. Mwaka ambao soko la korosho limepanda, basi mwaka unaofuata litashuka na mwaka ule likishuka watu wanalima mbaazi, mbaazi nazo zikishuka watu wanalima korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo watu wetu hawako stable. Sasa na hawa watu wa utafiti nao sijaona, sijui kwa sababu sasa hivi ndiyo wamesema kwenye Muswada huu kwamba tutaimarisha hiki kitengo cha utafiti, lakini bado naona tuna matatizo, tuna-base sana kwenye utafiti wa mazao, kuongeza ubora na wingi labda hivyo, lakini bado kwenye upande wa masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeona kwenye huu Muswada, kipengele hiki cha maeneo ya utafiti, sehemu ya Nane, kipengele (l) nafikiri ndiyo kimegusia kidogo kuonesha kwamba, yaani kama kuna masoko. Ningetegemea hivi vitu vyote viwili vingeenda sambamba, unapozungumzia utafiti wa kilimo moja kwa moja hapohapo lazima uingie kwenye utafiti wa masoko kwa sababu tatizo kubwa tunalo hapo kwenye upande wa masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla basi ningependekeza kwamba ili tuweze kwenda sambamba na utafiti wa kilimo, basi ni lazima twende sambamba na utafiti wa masoko, tena hili la masoko kwenye hii sehemu ya maeneo ya utafiti, yaani imetupwa mbali sana kuonekana kwamba hatuko tayari. Vilevile, tukirudi kwenye utafiti nafikiri kwamba watu wanaoweza kututafsiria hizi tafiti na kutuletea hizi tafiti…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Kuchauka.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia Muswada huu kwa kuishauri Serikali yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mwandishi wa habari kutoandika habari za kiuchunguzi au zile zilizoko mahakamani ni kuwanyima watu kupata habari za kina, kwani ni waaandishi wa habari ndio mara nyingi huibua uozo mwingi katika jamii na mara nyingi hata TAKUKURU hutumia taarifa hizi katika kufanya uchunguzi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo napendekeza kifungu hiki kifanyiwe marekebisho kwani mara zote watendaji kwenye Taasisi za Umma utoaji wa habari ni wasiri sana, hawako wazi hata kwa habari za kawaida. Kuwepo kwa vyombo viwili katika sheria moja kutaleta mgongano wa kiutekelezaji kwani kazi za Bodi ya Wanahabari ingeweza kufanywa na Baraza la Wanahabari ambako ndiko kuna watu wenye taaluma ya habari, lakini si hivyo tu, kuwepo kwa wateule wa Waziri au Rais hakuwezi kukifanya chombo anachokiongoza kuwa huru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, adhabu kwa mwanahabari aliyekutwa na kosa, kunyang’anywa leseni ili asifanye tena kazi ya uandishi wa habari ni adhabu kubwa sana. Lengo la adhabu hii si kutoa funzo ama kumrekebisha mtenda kosa, adhabu hii inakusudiwa kuwatia woga wanataaluma hawa wasifanye kazi kwa uhuru, hivyo kushindwa kuibua maovu yatakayofanywa na watu wenye mamlaka makubwa Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema hayo mambo yanayotajwa kama ni mambo ya siri, uchochezi, uhuru binafsi, faragha yakawa wazi kwani watu wenye mamlaka wanaweza wakatumia mwanya huu kuwazuia waandishi kupata habari kwa kigezo kuwa ni siri na mambo mengine kama hayo. Vilevile kitendo cha masharti ya leseni kuachwa kwa mtu mmoja (Waziri) kunaweza kuwafanya watu wengi kukosa au kufutiwa leseni hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uingizaji wa machapisho nchini. Mamlaka aliyopewa Waziri katika kifungu hiki yasipofanyiwa marekebisho Waziri anaweza akayatumia vibaya. Hivyo mamlaka hayo yakabidhiwe kwenye Bodi ya Huduma ya Habari/Baraza la Habari kuepuka Waziri kuzuia machapisho kwa maslahi binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Makosa Mbalimbali; mtu aliyefanya kosa kwa makusudi kumpa adhabu sawa (moja) na mtu aliyefanya kosa kwa uzembe si sawa kwani huyu wa pili hakukusudia kufanya kosa, hivyo adhabu ni bora zikatofautiana.