Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka (29 total)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Wilaya ya Liwale ilipandishwa hadhi kuwa Wilaya kamili tangu mwaka 1975, lakini ni Wilaya ya pekee ambayo haina Kituo cha Polisi wala nyumba za watumishi wa kada hiyo:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga jengo la kituo cha Polisi Wilaya ya Liwale sambamba na nyumba za watumishi ambao wanaishi uraiani kwa sasa?
(b) Je, ni lini Tarafa ya Kibutuka itapata kituo kidogo cha Polisi ili kulinda wafanyabiashara wa mazao ya ufuta wanaokuja Tarafani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, siyo kweli kwamba Wilaya ya Liwale ndiyo Wilaya pekee nchini ambayo haina Kituo cha Polisi na nyumba za watumishi. Liwale ni miongoni mwa Wilaya 65 nchini ambazo bado hazijajengewa vituo vya Polisi.
Hata hivyo, Serikali itajitahidi kujenga vituo vya Polisi awamu kwa awamu kadri hali ya kibajeti itakavyoruhusu.
(b) Mheshimiwa Spika, ili kusogeza huduma za Polisi kwa wananchi ni azma ya Serikali kujenga Kituo cha Polisi kila Tarafa, sanjari na kupeleka Wakaguzi wa Polisi kuongoza vituo hivi, hata hivyo, Kata nne ikiwemo Kibutuka, Mirui, Kiangala na Nangano za Tarafa ya Kibutuka, kuna Askari Kata ambao wanatoa huduma kwa wananchi. Aidha, katika kutekeleza azma hii tayari Jeshi la Polisi limeshapeleka Wakaguzi katika baadhi ya Tarafa. Tunaomba Mheshimiwa Mbunge kuwa na subira kwani hali ya fedha itakaporuhusu mpango huu utafika kila Tarafa ikiwemo Kibutuka.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha vijiji vya Mlembwe, Kimambi, Lilombe, Mirui, Mpigamiti, Kikulyungu na Mtungunyu vinapata miradi ya mawasiliano ya simu za mkononi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha usikivu hafifu wa matangazo ya Redio Tanzania (TBC – Taifa) katika Wilaya ya Liwale?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Mlembwe, Lilambwe, Mirui, Mpigamiti na Mtungunyu vimo katika orodha itakayofikishwa huduma ya mawasiliano na kampuni ya simu ya Halotel katika Awamu ya Nne inayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2017. Aidha, kijiji cha Kikulyungu katika Kata ya Mkutano kitafikishiwa huduma ya simu na kampuni ya simu ya TTCL kupitia mradi wa Awamu ya Kwanza B, kwa jumla ya ruzuku ya dola za Kimarekani 143,280. Mradi huu unategemewa kukamilika mwezi Machi, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Utangazaji Tanzania lina mitambo ya kurushia matangazo ya redio katika Mkoa wa Lindi kwa kutumia mitambo yake iliyopo Nachingwea eneo la Songambele na Lindi eneo la Kipihe. Hivi sasa mitambo ya redio ya masafa ya kati kilowati 100 iliyopo eneo la Songambele Wilayani Nachingwea haifanyi kazi kutokana na uchakavu. Mitambo ya Lindi eneo la Kipihe ni ya FM ambayo ni kilowati 2. Hali hii inasababisha maeneo mengi ya Mkoa wa Lindi na Mtwara kutopata usikivu mzuri wa matangazo ya redio ikiwemo Wilaya ya Liwale na mengine kutopata matangazo kabisa. Mtambo uliopo Kipihe, Lindi una uwezo wa kurusha matangazo katika maeneo ya Lindi Mjini na baadhi ya maeneo ya Lindi Vijijini. Shirika limeandaa mpango mahsusi wa kupanua usikivu nchi nzima ambao utekelezaji wake utategemea upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kujenga mitambo yenye uwezo wa kurusha matangazo maeneo yote yaliyoathirika na kutofanya kazi kwa mtambo wa Nachingwea wa kilowati 100. Mpango wa muda mrefu ni kuhakikisha kuwa TBC inanunua mitambo inayolingana na teknolijia ya kisasa katika tasnia ya utangazaji. Mpango huu utahusisha pia maeneo mengine ya nchi ambako mitambo ya masafa ya kati haifanyi kazi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) lililokuwa na matawi karibu nchi nzima na assets mbalimbali lilibinafsishwa kutokana na sera ya ubinasfishaji.
(a) Je, ni matawi mangapi yamebinafsishwa na mangapi yamebaki mikononi mwa Serikali?
(b) Je, Serikali imepata fedha kiasi gani kutokana na ubinafsishaji huo?
(c) Kati ya matawi yaliyobinafsishwa ni mangapi yanaendeshwa kwa ubia wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, lenye vipengele (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Idadi ya matawi ya Shirika la Taifa la Usagishaji yaliyobinafsishwa ni 22 na yaliyobaki mikononi mwa Serikali ni matano;
(b) Katika kubinafsisha mali za NMC Serikali imepata fedha kiasi cha shilingi 7,491,611,000; na
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika matawi yaliyobaki hakuna tawi linaloendeshwa kwa ubia kati ya Serikali na mwekezaji. Matawi hayo kwa sasa yanasimamiwa na Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko. Hata hivyo, tawi la NMC - Arusha maarufu kama Unga Limited limekodishwa kwa Kampuni ya Monaban Trading Company Limited.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Wilaya ya Liwale ina miradi mikubwa miwili ya umwagiliaji, Mradi wa Ngongowele na Mtawango lakini Mradi wa Ngongowele umesimama kwa muda mrefu sasa.
(a) Je, ni nini hatma ya mradi huu wa Ngongowele kwa sasa?
(b) Je, Serikali iko tayari kumpeleka Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ili kukagua mradi huu ambao unaonekana kuhujumiwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza wa Mradi wa Ngongowele ilianza kutekelezwa mwaka 2009 kwa kujenga banio na miundombinu yake kwa gharama ya shilingi milioni 346.1 kupitia Mfuko wa Kuendeleza Umwagiliaji ngazi ya Taifa. Awamu ya pili wa mradi ilitekelezwa mwaka 2010 kwa gharama ya shilingi milioni 400. Kazi zilizofanyika ni kuchimba na kusakafia mfereji mkuu mita 2,500; kujenga vigawa maji sita; kujenga makalvati matano; kujenga kujenga kivusha maji chenye urefu wa mita 80 na kuchimba mfereji wa kutoa maji mita 200. Awamu hii ya utekelezaji ilikumbwa na changamoto ya mafuriko makubwa yaliyotokea katika maeneo hayo na kuharibu miundombinu. Hali hiyo ilipelekea mkandarasi kuongezewa muda wa kukabidhi kazi kutoka tarehe 01.10.2011 hadi tarehe 30.10.2011. Baada ya kushindwa kukabidhi kazi kwa tarehe hiyo, Halmashauri ilianza kumkata liquidated damage ya asilimia
0.15 ya thamani ya mkataba wa siku kwa muda wa siku 100 hadi tarehe 15.02.2012 na baadaye ilivunja mkataba kutokana na mkandarasi huyo kushindwa kukabidhi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa mradi huo kwa wananchi wa Ngongowele na Taifa kwa ujumla, Serikali kupitia mradi wa kuendeleza skimu ndogo za wakulima itatenga fedha katika mwaka wa fedha 2018/ 2019 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi huu ili ufanye kazi. Aidha, Serikali itafuatilia utekelezaji wa Mradi wa Ngongowele na endapo itabainika kuna hujuma katika utekelezaji wa mradi huo hatua stahiki zitachukuliwa.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Mji wa Liwale unakuwa kwa kasi lakini una chanzo kimoja cha maji ambacho kwa sasa hakiwezi kukidhi mahitaji hivyo kusababisha uhaba mkubwa wa maji.
• Je, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuwaondolea wananchi adha ya upatikanaji wa maji?
• Je, mradi wa kumwagilia wa Ngongowele utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha huduma ya maji ili kuwaondolea adha wananchi wa Mji wa Liwale, Serikali katika mpango wa muda mfupi imepanga kukarabati na kupanua mtandao wa majisafi, kununua na kufunga dira za maji kwa wateja, kukarabati chanzo cha maji na kukarabati matenki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hizo zinatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka wa fedha 2017/2018. Kiasi cha shilingi milioni 300 kimetengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kazi hizo.Taratibu za kumpata mkandarasi atakayetekeleza kazi hiyo zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.5 katika bajeti wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni katika Miji Mikuu ya Wilaya nchini ikiwemo na Mji wa Liwale. Taratibu za kumpata mtaalam mshauri atakayetekeleza kazi hizo zinaendelea. Kukamilika kwa upembuzi na usanifu wa kina kutatoa gharama halisi ya utekelezaji wa mradi mkubwa katika Mji wa Liwale pia idadi ya Kata zitakazonufaika na mradi huo wa maji zitajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ya umwagiliaji ya Ngongowele iliyopo Kata ya Ngongowele, Wilayani Liwale iliibuliwa mwaka 2008. Ujenzi wa skimu hii ulifanyika kwa awamu tatu kati ya mwaka 2009 na 2012 kwa kujenga banio, vigawa maji, kivusha maji, vivuko vya watembea kwa miguu, pamoja na kuchimba mifereji miwili yenye urefu wa jumla wa mita 4,800 ambapo mita 1,080 tayari zimesakafiwa. Aidha, kwa miaka miwili mfululizo 2010/2011 na 2011/2012 skimu hii ilikumbwa na mafuriko makubwa na kusababisha uharibifu wa baadhi ya miundombinu ambayo hata hivyo baadhi imefanyiwa marekebisho ili kudhibiti uharibifu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na mapitio ya miradi yote ya umwagiliaji hapa nchini ili kubaini mahitaji na gharama za ukarabati ama kujengwa upya. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Liwale ni Wilaya ya zamani hapa nchini lakini hadi leo haina jengo la Mahakama zaidi ya jengo lililorithiwa toka iliyokuwa Mahakama ya Mwanzo Liwale.
Je, ni lini Serikali itajenga jengo la Mahakama Liwale sambamba na nyumba za watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba ni kweli Wilaya ya Liwale haina jengo la Mahakama ya Wilaya. Aidha, kama alivyoainisha Mheshimiwa Mbunge ni kweli jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Liwale Mjini ambalo linatumika sana kutolea huduma za Mahakama ya Wilaya na ya Mwanzo ni chakavu na hivyo kuhitaji kujengwa upya. Katika mpango wa ujenzi, tumepanga kujenga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Liwale kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambalo pia litatumika na Mahakama ya Mwanzo Liwale Mjini, sambamba na ujenzi wa nyumba ya Hakimu kutegemea upatikanaji wa fedha.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa mpaka kati ya Wilaya ya Liwale na Wilaya ya Kilwa:-
Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro huo ili kuleta amani katika Wilaya hizo kabla amani haijatoweka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kilwa ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na. 91 la tarehe 16 Mei, 1947 na Wilaya ya Liwale ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Na.185 la tarehe 5 Desemba, 1980. Hadi hapo hakukuwa na mgogoro wowote. Tangazo la Serikali Na. 134 la mwaka 1983 lilianzisha Halmashauri za Wilaya ambapo Mirui iliorodheshwa kama kata na kijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale na haikutajwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inautambua mgogoro huo unaohusu mkanganyiko ulioko kati ya Kitongoji cha Mirui katika Kijiji cha Nanjirinji A, Kata ya Nanjirinji, Wilayani Kilwa kwa upande mmoja na Kijiji cha Mirui katika Kata ya Mirui Wilayani Liwale kwa upande wa pili.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mgogoro huo ni sehemu ya migogoro mingi inayoshughulikiwa na Serikali chini ya uratibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nashauri Mbunge na wananchi wa maeneo husika wawe na subira wakati huu ambapo Serikali imetuma wataalam kwenye eneo hilo la mgogoro wanaofanya mapitio ya kina ya matangazo ya kuanzisha wilaya zote mbili na tangazo la kuanzisha halmashauri zote mbili kwa lengo la kuhakikisha mgogoro huo unapatiwa ufumbuzi wa kudumu ndani ya mwaka 2018/2019.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Msitu wa Nyera – Kipelele ni miongoni mwa misitu ya asili iliyopo Wilaya ya Liwale. Serikali imekuwa ikiandaa taratibu za uvunaji wa mazao ya msitu huo.

(a) Je, taratibu hizo zitakamilika lini?

(b) Je, Serikali imepata manufaa gani kutokana na uhifadhi wa msitu huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Msitu wa Nyera – Kipelele ni hifadhi ya msitu ulio chini ya umiliki wa usimamizi wa Serikali Kuu (Wakala wa Misitu wa Huduma Tanzania). Misitu hiyo ipo katika Wilaya ya Liwale, Mkoa wa Lindi, Msitu wa Kipelele ulitengwa kuwa hifadhi ya Serikali Kuu katika Tangazo la Serikali Na. 79 la mwaka 1956 ukiwa na eneo la hekta 98,423. Msitu huo umezungukwa na vijiji tisa, ambavyo ni Kichonda, Nyera, Kimambi, Mtawatawa, Kitogoro, Litou, Legezamwenda, Kipelele na Naujombo.

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za kuandaa uvunaji wa mazao ya msitu katika msitu huo zimekamilika mwaka 2018, baada ya kuandaliwa kwa mpango wa usimamizi wa msitu (Management Plan) na mpango wa uvunaji (Harvesting Plan). Kwa mujibu wa mpango wa usimamizi, kiasi cha hekta 59,053 katika msitu huo zina miti ya kuweza kuvunwa. Aidha, miti ya ujazo 19,970 zimepangwa kuvunwa kuanzia mwaka
2019/2010 kwa kufuata mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu.

Mheshimiwa Spika, manufaa yanayopatikana kutokana na uhifadhi wa msitu huo ni makazi ya wanyamapori aina tofauti wakiwemo tembo, uboreshaji wa mifumo ya kiikolojia ikiwemo hifadhi ya hewa ya ukaa. Aidha, ni vyanzo vya maji katika Vijiji vya Mtawatawa, Kitogoro, Legeza mwendo, Kipelele na vilevile hifadhi hiyo ni chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Mgogoro wa mipaka kati ya Kijiji cha Kikulyungu na Hifadhi ya Selous ni wa muda mrefu:-

Je, Serikali itamaliza lini mgogoro huo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa mgogoro wa mpaka kati cha kikulyungu na poro la Akiba Selous umekuwepo kwa muda mrefu. Chanzo cha mgogoro huo ni wananchi wa kijiji hicho kufutiwa kibali cha kuvua samaki katika bwawa la kihurumila ambalo limo ndani ya Pori la Akiba Selous baada ya wananchi wa kijiji hicho uanza kuvua kwa njia zisizo endelevu au haribifu ikiwemo kutumia sumu. Baada ya kufutiwa kibali wananchi wa Kikulyungu walianza kulalamika na kudai kuwa mpaka wa Selous na kijiji hicho upo mto Matandu jambo ambalo ni kinyume na Tangazo la Seriklai Na.475 la Mwaka 1974.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uhakika wa mipaka imekamika na taarifa imewasilishwa Wizarani kwangu. Aidha, zoezi la kuhakika mipaka hiyo lilienda sambamba na uwekaji wa alama za kudumu baada ya maridhiano ya pande zote kwa kuzingatiwa tangazo la Serikali kuanzishwa kijiji cha Likulyungu, Tanganzo la Serikali kuanzishwa pori la Akiba la Selous GN. Na. 275 la 1974 na Tanganzo la Serikali la kuanzishwa pori tengefu Kihurumila Na.269 ambalo pia ni la mwaka 1974 lililopo kati ya kijiji cha Likulyungu na pori la Akiba Selous.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uhakiki huo umefanywa na wataalam kutoka Wizara yenye dhamana ya ardhi na kushirikisha pande zote zilizohusika katika mgogoro huo, ni imani kuwa mgogoro huo umemalizika.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuimarisha utalii wa picha badala ya utalii wa uwindaji kwenye Mapori yetu ya Akiba nchini: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na lango la utalii wa picha kwenye Pori la Akiba la Selous kwenye Ukanda wa Kusini kwenye Wilaya za Tunduru na Liwale?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohammed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Niabu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imendelea na jitihada za kupanua wigo wa mazao ya utalii kulingana na rasilimali zilizopo. Mazao hayo ni pamoja na utalii wa uwindaji, utalii wa picha, utalii wa utamaduni na utalii wa fukwe na namna ambayo itanufaisha Taifa na Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa azma hiyo, tarehe 26 Julai, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akiwa katika ziara yake ya kikazi kwenye uzinduzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Nyerere, alitoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa sehemu ya Pori la Akiba Selous ipandishwe hadhi kwa kuanzisha Hifadhi Taifa Nyerere. Azimio la kuanzisha Hifadhi ya Taifa Nyerere lilipitishwa na Bunge lako Tukufu kwenye kikao cha tarehe 9 Septemba, 2019 na kuridhiwa na Mheshimiwa Rais kwa GN. No. 923 ya mwaka 2019. Kwa mujibu wa Sheria, shughuli za utalii zinazoruhusiwa kwenye hifadhi za Taifa ni zile za kuangalia na kupiga picha tu na uwindaji hauruhusiwi.

Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa, kufuatia kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa Nyerere, Wilaya za Tunduru na Liwale ni miongoni mwa wilaya zitakazonufaika na fursa za moja kwa moja za utalii wa picha katika maeneo hayo. Aidha, tathmini itafanyika ili kuona sehemu ya kuweka lango la kuingilia katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere itaweza kuwekwa kuendeleza utalii.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Shule ya Msingi Kambarage ni shule pekee katika Wilaya ya Liwale inayochukua watoto wenye mahitaji maalum (walemavu); lakini shule hiyo haina walimu wenye taaluma hizo na vilevile miundombinu ya shule hiyo sio rafiki kwa watoto wenye ulemavu:-

(a) Je, ni lini shule hiyo itapatiwa walimu wenye taaluma husika ili kukidhi mahitaji ya shule?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya shule hiyo ili iweze kukidhi mahitaji ya watoto hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Kambarage ina wanafunzi 1,283 wavulana wakiwa 636 na wasichana 647. Shule inatoa elimu changamani ambapo wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wapo 10, wenye ulemavu wa akili kwa maana ya mtindio wa ubongo wapo watano na wenye ulemavu wa ngozi wapo watatu. Uwiano wa walimu na mwanafunzi unatofautiana kulingana na aina ya ulemavu wa wanafunzi. Ulemavu wa akili mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano, ulemavu wa kusikia mwalimu mmoja kwa wanafunzi tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Kambarage ina walimu watatu wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia na mwalimu mmoja kwa wenye ulemavu wa akili. Kwa uwiano huo walimu na wanafunzi ni wazi kuwa hakuna upungufu wa walimu kwa wanafunzi kwenye mahitaji maalum katika shule hiyo.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya tathimini ya miundombinu katika Shule ya Msingi Kambarage na kubaini kuwa kiasi cha shilingi milioni 50 kinahitajika kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu kwenye Shule ya Msingi Kambarage. Naielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Liwale kutenga fedha hizo kwenye bajeti zake zinazotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kufanya ukarabati na ujenzi wa miundombinu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Wakati Jeshi la Polisi likitekeleza majukumu yake kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na hata uvunjifu wa Katiba kwa kisingizio cha maagizo kutoka juu:-

(a) Je, ni mamlaka gani iko juu ya sheria?

(b) Je, maagizo hayo yanapopingwa na sheria za nchi na kukiuka haki za binadamu nini hukumu ya yule aliyetendewa kinyume cha sheria?

(c) Je, huyu anayekutwa na kadhia hii hana haki ya kumjua huyo mwenye mamlaka ya juu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi hutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo kwa msingi huo Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 inampa mamlaka polisi kutumia nguvu ya wastani anapokuwa anatekeleza kazi yake kulingana na mazingira yaliyopo. Aidha, hakuna mamlaka ya juu katika Jeshi la Polisi iliyo juu ya sheria kiasi cha kuvunja sheria.

(b) Mheshimiwa Spika, nchi yetu inafuata misingi ya Demokrasia na Utawala Bora ambapo mtu yeyote anao uwezo wa kwenda kutoa malalamiko yake kwenye chombo chochote cha kisheria na hauta stahiki zikachukuliwa.

(c) Mheshimiwa Spika, hakuna mamlaka inayomzuia mtu kumuona mtu ambaye anadhani atamsaidia kutatua tatizo Lake Linalomsibu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Wakazi wa Liwale waliathirika na vurugu za Uchaguzi wa mwaka 2020 na mali za wananchi na Serikali zilichomwa moto:-

Je, Serikali kupitia Mfuko wa Maafa ina mpango gani wa kuwafuta machozi wananchi walioathirika na vurugu hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakiri kupata taarifa za kutokea kwa vurugu zilizosababishwa na wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale na kuleta uvunjifu wa amani, uharibifu wa vitu mbalimbali ikiwemo mali za wananchi na Serikali. Uhalifu huo umefanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020 katika Jimbo la Liwale na maeneo mengine Mkoani Lindi. Aidha, Serikali ilifanya jitihada mbalimbali za kumaliza vurugu hizo kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, kufanya vurugu za aina hii ni kosa la jinai. Hivyo, matokeo ya madhara ya vurugu hizo yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu masuala ya makosa ya jinai. Sheria ambayo inahusika kwenye masuala ya makosa ya jinai ni Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code CAP.16) ambayo imefanyiwa marekebisho mara kwa mara, lakini kwa Sheria ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2015 na Kanuni zake za utekelezaji hazina ufungamanisho wa pamoja na madai ya kijinai na hasa yahusuyo uharibifu wa mali na namna ya kulipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kuwapa pole sana wananchi wote walioathirika na kadhia hii kwa sababu si jambo zuri. Serikali pia ililipokea na kulifanyia kazi lakini tunatambua kwamba kuna uharibifu wa nyumba ambao ulifanyika, kuna uharibifu wa mali kama magari, pikipiki na vifaa vinginevyo ambapo hata timu ya mkoa tayari ilikwishakuanza kuchukua hatua za awali za kufanya tathmini ya kujua changamoto hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Lindi kuhakikisha uchunguzi kuhusu vurugu hizo unakamilika na hivyo kulifikisha suala hilo katika vyombo vya sheria ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda kuwapa pole wale wote walioathirika na vurugu hizo na kuwaomba wananchi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kudumisha amani na usalama nchini.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali haioni kuwa ipo haja ya kuwajumuisha Wenyeviti wa Halmashauri na Wabunge kwenye Kamati za kujadili na kupitisha maombi ya wavunaji wa mali za misitu kwenye Wilaya zetu nchini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi, uwakilishi wa wananchi upo katika ngazi mbili. Ngazi ya kwanza ni ambapo Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji vinavyovuna hushiriki kwenye vikao vya Kamati, ngazi ya pili ni ambapo Waheshimiwa Madiwani na Wabunge katika vikao vya Baraza la Madiwani hupata wasaa wa kujadili na kutoa ushauri juu ya taarifa za Kamati zinazohusu maombi yote ya uvunaji wa miti na tathmini ya mwenendo wa uvunaji katika Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ugawaji wa malighafi ya miti ya kuvunwa katika misitu ya asili ya Serikali unasimamiwa na Kamati ya Usimamizi ya Uvunaji katika kila Wilaya. Jukumu la kwanza la Kamati hii ni kujadili na kutoa maamuzi ya maombi ya uvunaji wa miti Wilayani katika misitu ya asili inayovunwa kwa ajili ya magogo, mbao, nguzo, fito, kuni na mkaa. Mazao hayo ni yale tu yatakayovunwa kwa ajili ya biashara. Jukumu la pili ni kufuatilia utekelezaji wa mpango wa uvunaji katika msitu husika na kutoa ushauri katika ngazi za Wilaya na Wizara pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mpango wa upandaji miti katika eneo la msitu unaovunwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya udanganyifu mkubwa kwenye mikataba ya Ushuru wa kampuni za Simu na wenye maeneo pale panapojengwa minara ya simu kiasi cha kusababisha ushuru kwenda kwa watu wasiohusika?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zubeir Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kwa mtumiaji wa mwisho huwezeshwa na minara ambayo kwa kiasi kikubwa hujengwa ardhini, lakini pia husimikwa katika majengo marefu, hususan katika maeneo ya miji mikubwa. Ardhi ambayo hutumika katika ujenzi wa minara humilikiwa na wananchi ama taasisi za umma au taasisi za kijamii ambapo hupangishwa kwa mtoa huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, katika kubaini eneo linalopaswa kujengwa mnara wa mawasiliano vigezo mbalimbali vya kitaalam hutumika kama vile uimara wa ardhi, eneo linalowezesha mnara husika kuwasilisiana na minara mingine na maeneo yanayoweza kufikiwa na mawasiliano kupitia mnara husika. Vigezo hivi na vingine ndio vinaweza kuamua mahali sahihi ambapo mnara unaweza kujengwa. Kwa utaratibu uliopo sana, eneo likibainika kukidhi vigezo vya kitaalam, mtoa huduma hufanya mawasiliano na mmiliki wa eneo husika pamoja na Serikali ya eneo hilo ili eneo hilo liweze kujengwa mnara wa mawasiliano. Mtoa huduma huingia mkataba na mmiliki wa eneo ambapo mmiliki huyo hulipwa fedha ya pango la ardhi kulingana na makubaliano yaliyofikiwa ambayo ndiyo huwekwa katika mkataba.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya minara ya mawasiliano ikiwemo kufuata taratibu katika upangishaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa minara. Vilevile Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umetoa maelekezo katika mikataba wanayoingia na Kampuni za Simu kufuata taratibu zote katika kukodi ardhi ambapo minara hiyo hujengwa kupitia halmashauri husika. Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali ipo tayari kufanya mapitio ya upimaji wa vijiji nchini kwa kuwa migogoro mingi imesababishwa na upimaji usio shirikishi wa mwaka 1970?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kabla ya kujibu swali lake la msingi kuwa kilichofanyika katika miaka ya 1970 haikuwa upimaji wa vijiji bali ilikuwa ni Operesheni Maalum ya Serikali ya kuanzisha Vijiji vya Ujamaa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 2000 Serikali ilitekeleza Programu ya upimaji wa vijiji kwa lengo la kuvifanya vijiji kuwa mamlaka kamili za usimamzi wa ardhi za vijiji. Mathalani, katika Mkoa wa Lindi jumla ya vijijii 401 kati ya vijiji 523 vikiwemo Vijiji vya Wilaya ya Liwale vilipimwa kwa njia shirikishi na kuwekewa alama za mipaka.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani Vyuo vya Serikali vimejiandaa kupokea wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatanyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) inatarajia kuongeza fursa za wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu kwa kujenga na kukaratabati miundombinu kama ifuatavyo: ujenzi wa maabara na karakana za kufundishia 108; vyumba vya mihadhara na madarasa 130; kumbi za mikutano ya kisayansi 23; mabweni 34; miundombinu ya shambani na vituo atamizi 10 kwa ajili ya kuendeleza ubunifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma programu za Sayansi kutoka wanafunzi 40,000 kwa mwaka 2020 hadi kufikia 106,000 mwaka 2026. Aidha, mradi huu pamoja na kuboresha mitaala zaidi ya 290 pia utasomesha wahadhiri 831 katika programu za kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, kwa mwaka wa masomo 2022/2023, Serikali kupitia Samia Scholarship imetoa ufadhili wa asilimia 100 kwa wanafunzi 640 wenye ufaulu wa juu waliodahiliwa katika Vyuo Vikuu kusoma Programu za Sayansi, Teknolojia, Hisabati na Tiba.

Mheshimiwa Saibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani kuirejeshea Halmashauri ya Liwale fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati iliyorudishwa Hazina ili iweze kujenga Stendi ya Kisasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa stendi ya kisasa ya Liwale ni moja kati ya miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato kwa Halmashauri, ambapo mwaka 2018 Serikali iliingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Mkoani Lindi kutekeleza mradi huo kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.2.

Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa. Hivyo, kutokana na umuhimu wa mradi huu, katika mwaka 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imetengewa Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya kisasa ya Liwale. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI inahimizwa kukamilisha taratibu za maombi ya fedha na kuwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango. Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa visima vitatu katika Kijiji cha Turuki utakamilika kwa ajili ya kupeleka maji Liwale Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Liwale katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali imechimba visima vitatu katika Kijiji cha Turuki. Visima hivyo kwa pamoja vina uwezo wa kuzalisha lita 1,008,000 kwa siku na vitaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita 1,200,000 kwa siku hadi kufikia lita 2,208,000 kwa siku.

Mheshimiwa Spika, usanifu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji hayo ulikamilika mwezi Machi, 2023 na ujenzi umepangwa kutekelezwa na kukamilika katika mwaka wa fedha 2023/2024. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ulazaji wa mtandao wa bomba umbali wa kilomita 78 na ujenzi wa matanki mawili (2) yenye ujanzo wa lita 1,300,000.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itafungua Ofisi ya Madini Liwale?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa ofisi ya madini unazingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uwepo wa shughuli kubwa za madini katika eneo husika. Kigezo hiki kinalenga katika kuhakikisha kunakuwa na usimamizi na udhibiti madhubuti wa rasilimali madini inayoanzishwa katika eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Lindi, pamoja na kuwa na Ofisi ya Madini ya Mkoa iliyopo Nachingwea pia Wizara imefungua ofisi ndogo iliyopo Lindi Mjini ili kurahisisha uratibu wa shughulil za madini katika maeneo mengine katika mkoa huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za uchimbaji katika Wilaya ya Liwale zipo chini ukilinganisha na Wilaya za Ruangwa, Kilwa na Nachingwea. Kwa sasa wachimbaji wa madini katika Wilaya ya Liwale wanashauriwa kutumia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi ya Nachingwea pamoja na ofisi ndogo ya madini iliyopo Lindi Mjini. Hata hivyo, Wizara itaendelea kuboresha huduma kwa wadau wake kwa kadiri itakavyopata fedha za kutekeleza jukumu hilo.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, lini barabara ya Ulinzi ya Hifadhi ya Mwalimu Nyerere inayojengwa toka Liwale hadi Mahenge itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiulinzi na kijamii na inayounganisha Mikoa ya Lindi na Morogoro, katika mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shilingi milioni 143.04 zimetengwa kwa ajili ya kazi za upembuzi yakinifu wa awali. Kazi ya upembuzi yakinifu wa awali itakapokamilika katika barabara hii inayopita katika Hifadhi ya Mbuga ya Wanyama ya Selous, itaonesha iwapo mradi unakidhi vigezo vya uhifadhi mazingira ili kuwezesha kujengwa, ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za ujenzi wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Liwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imetoa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 10,000 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi pamoja na nyumba za makazi ya askari. Tathmini ya makadirio na michoro kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi, daraja B umeshafanyika na kiasi cha Sh.768,024,734/= kinahitajika. Fedha hizo zitatolewa kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo katika mwaka wa fedha 2023/2024, nakushukuru.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kufanya mapitio sheria ya Manunuzi ya umma kwa kuwa ni kikwazo kwa utekelezaji wa miradi katika Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imefanya mapitio ya Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 na kuandaa mapendekezo ya kutunga upya sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo hayo yamekamilika na muswada wa kutunga upya sheria ya ununuzi wa umma unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Kumi na Mbili.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kuzijenga kwa kiwango cha lami barabara nyingi nchini zilizokwisha kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuzijenga kwa kiwango cha lami barabara zote zilizokwishafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Mpango huo unatekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaingia ubia na Wakala wa Nyumba Tanzania (TBA) kuwajengea nyumba walimu nchini na kisha kuwakata mishahara yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Jimbo la Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mahitaji ya nyumba kwa ajili ya walimu ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2021 hadi 2023 zimejengwa nyumba 562 zenye uwezo wa kuchukua familia 1,124 kwa thamani ya shilingi 56,325,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa pendekezo la Mheshimiwa Mbunge ni la msingi na linahusisha ujenzi wa nyumba ambazo itabidi Walimu wazilipie kupitia mishahara yao, Serikali itakaa kwanza na walimu ili kulijadili na endapo wataafiki wazo hilo litawasilishwa kwa Wakala wa Nyumba Tanzania (TBA) kwa ajili ya makubaliano.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, Serikali ipo tayari kuleta wataalamu Liwale kufanya utafiti kujua chanzo cha ugonjwa wa majani ya mikorosho kunyauka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeanza kufanya utafiti wa kina ili kutambua chanzo cha ugonjwa majani kunyauka unaoikumba mikorosho katika Wilaya ya Liwale. Utafiti huo ulianza kufanyika mwaka 2023 na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania kupitia Kituo cha TARI Naliendele kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya awali ya utafiti huo yamebaini kuwa chanzo cha mnyauko wa majani ya mikorosho katika Wilaya ya Liwale ni fangasi aina ya Fusarium oxysporum f. sp na ikajulikana kuwa ni kimelea kinachoishi kwenye udongo ambacho husababisha ugonjwa wa mnyauko fusari (fusarium wilt) na ugonjwa huu ni tishio kwa kuwa unasababisha kukauka kwa mikorosho. Serikali imeanza kutoa elimu kwa wakulima na wataalamu wa kilimo kuhusu mbinu za awali za kukabiliana na ugonjwa huo. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE K.n.y. MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Je, upi mpango wa Serikali wa kuipatia gari la Zimamoto Wilaya ya Liwale ili kukabiliana na majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na jitihada za kuliimarisha na kuliboresha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha taratibu zote za mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya Dola za Marekani milioni 100 kutoka Taasisi ya Abu Dhabi Export Credit Agency iliyopo Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya kupata vitendea kazi mbalimbali, ikiwemo upatikanaji wa magari 150 ya zimamoto na uokoaji yatakayosambazwa kwa nchi nzima, ikiwemo Wilaya ya Liwale.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:

Je, Serikali ina mpango gani wa kuyauza magari mabovu yaliyopo kwenye halmashauri zetu nchini na kwenye Ofisi za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa miongozo iliyopo ya ufutaji na uondoshaji wa mali chakavu ikijumuisha vyombo vya moto katika halmashauri na taasisi za Serikali, Wizara ya Fedha ina jukumu la kuhakiki na kutoa vibali vya ufutaji na uondoshaji wa mali chakavu. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Fedha ilitoa jumla ya vibali vya kuondosha mali chakavu 160 katika Halmashauri na Ofisi za Serikali. Kati ya vibali hivyo, kulikuwa na vibali vya magari chakavu 976 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.4. Aidha, magari chakavu 223 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 yaliondoshwa kwa njia ya mnada kwa taasisi 54. Vilevile ufualitiaji na tathmini ya magari ya miradi ulifanyika na kubaini magari 339 yenye thamani ya shilingi 479,565,000 kuwa ni chakavu na taratibu za uondoshaji wake zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya Julai na Agosti, 2024 vibali 70 vya uondoshaji wa magari chakavu vimetolewa kwa halmashauri na Ofisi za Serikali. Aidha, Septemba, 2024 Wizara ya Fedha itaratibu na kusimamia minada kwenye taasisi 54 ya uondoshaji wa vyombo vya moto 150 katika mikoa tisa ambayo ni Dar es salaam, Mbeya, Arusha, Morogoro, Mtwara, Njombe, Lindi, Pwani na Dodoma, ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya maboresho ya minara iliyojengwa na Halotel Liwale ili iweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, ilifanya tathmini katika Jimbo la Liwale na kubaini uwepo wa changamoto za mawasiliano katika Minara ya Halotel. Minara hiyo inatakiwa kuongezewa teknolojia 3G na 4G ambapo utekelezaji wake utafanyika kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Kampuni ya Halotel ina jumla ya minara nane katika Wilaya ya Liwale, ambayo ina uhitaji wa kuiongezea nguvu kutoka 2G kwenda teknolojia ya 3G na 4G. Kiasi cha ruzuku inayohitajika kuiongezea nguvu minara hiyo, ni takribani shilingi 320,000,000 za Kitanzania. (Makofi)