Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Selemani Said Bungara (2 total)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-
Mradi wa ujenzi wa Barabara ya Singino/Kivinje maarufu kama Barabara ya Kwa Mkocho ni ahadi ya Serikali iliyotolewa na Rais Mstaafu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, karibu miaka 10 iliyopita. Aidha, kwa kipindi chote cha miaka 10 ujenzi wa barabara hiyo umekuwa wa kusuasua ingawa barabara hiyo ni kiunganishi kwa wananchi hasa wagonjwa wanaokwenda kutibiwa hospitali ya wilaya:-
(a) Je, ni nini kauli ya Serikali ya Awamu ya Tano juu ya ukamilishwaji wa ahadi hiyo?
(b) Je, Serikali inatoa maelezo gani kwa wananchi juu ya kuchelewa kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kipindi cha miaka 10 sasa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Singino/Kivinje – Kilwa ni barabara inayohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Katika mwaka 2012, Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne aliahidi kutenga fedha kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ili barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ilisaini mkataba na kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 1.478. Hata hivyo, mradi huo haujakamilika na mkandarasi amekimbia eneo la mradi. Wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi, kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya mahitaji ya fedha zinazotakiwa ili kuendelea kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii yamefanyika na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii unatarajiwa kuanza pindi fedha zitakapopatikana.
MHE. SELEMANI S. BUNGARA aliuliza:-
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kilwa kina upungufu mkubwa wa vitanda na hata vichache vilivyopo vimechakaa sana kwani vilinunuliwa tangu mwaka 1969. Mahitaji halisi ya vitanda vinavyohitajika chuoni hapo ni zaidi ya vitanda 50 (double decker):-
Je, Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vitanda pamoja na samani nyingine chuoni hapo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Said Bungara, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) kwa ajili ya kuandaa rasilimali watu watakaotumika katika viwanda ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025. Vyuo hivi vitasaidia kuongeza fursa ya mafunzo ya ufundi stadi sambamba na elimu ya wananchi (folk education). Aidha, vitasaidia kuwaandaa vijana kwa kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa vyuo hivyo, Serikali imetoa kandarasi kwa vyuo vitatu ambavyo ni Taasisi ya Teknolojia Dar-es-Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya ili vifanye uchambuzi wa kina wa hali halisi ya miundombinu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia, pamoja na samani katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kikiwemo Chuo cha Maendeleo cha Wananchi Kilwa Masoko. Taratibu za ukarabati zitaanza baada ya kukamilika kwa zoezi hili. Aidha, Wizara inafanya zoezi la kubaini mahitaji ya watumishi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, zoezi linalotarajiwa kukamilika Julai, 2018.