Contributions by Hon. Josephine Tabitha Chagulla (4 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu katika hotuba hii iliyoko mbele yetu. Nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama hapa leo nikiwa mzima wa afya ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza na kumpongeza Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Nimpongeze pia Waziri Mkuu, lakini pia nipongeze sana Baraza lote la Mawaziri kwa jinsi walivyojipanga kufanya kazi nzuri, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu sasa na sekta ya afya. Utafiti uliofanyika mwaka 2015, Mkoa wa Geita unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi sana wa malaria. Katika Hospitali zetu za Wilaya ya Geita zote zimejaa wagonjwa wa malaria. Hii ni kutokana na mashimo mengi yaliyoachwa wazi na wachimbaji wa madini. Akina mama na watoto wadogo wa chini ya umri wa miaka mitano wanakufa sana na ugonjwa wa malaria. Niiombe sana Serikali iweze kuona ni namna gani itaweza kumaliza tatizo hili, tatizo hili ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri, niiombe sana Serikali iweze kuja na sheria ambayo itawataka pia wachimbaji hawa wa madini waweze kufukia mashimo kabla ya kuanza tena kuchimba mashimo mengine ili tuweze kunusuru maisha ya wananchi wa Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa ujenzi wa vituo vya afya katika kila kata na ujenzi wa zahanati katika kila kijiji utapunguza sana msongamano katika Hospitali zetu za Wilaya. Hivi sasa Hospitali zetu za Wilaya zimejaa wagonjwa wengi sana lakini niiombe sana Serikali iweze kujitahidi kila kata iweze kuwa na kituo cha afya na kila kijiji kiweze kuwa na zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya katika vituo vyetu vya afya na zahanati. Unakuta katika kituo cha afya kimoja kina daktari mmoja na muuguzi mmoja, hii kwa kweli sio sawa, huyu mtu atafanyaje kazi? Kazi hii ni ngumu inahitaji angalau watu wawe na shift. Niombe Serikali iweze kuajiri watumishi wengi katika sekta hii ya afya ili vituo vyetu viweze kuwa na watumishi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuongelea kuhusu kauli mbovu na chafu kwa baadhi ya watumishi wa afya. Hivi karibuni tumeshuhudia vitendo vya kinyama vilivyofanywa na baadhi ya wauguzi hadi kusababisha vifo vya watoto mapacha na mama yao. Hii kwa kweli inauma, Serikali ijipange na kukemea kabisa kwa nguvu vitendo hivi visijirudie tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye sekta ya maji. Nianze mchango wangu wa sekta ya maji na tatizo kubwa la maji katika Mkoa wa Geita. Mkoa wa Geita umezungukwa na Ziwa Viktoria lakini tatizo la maji ni kubwa mno huwezi kuamini. Bado akinamama ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa hili wanahangaika kutwa nzima kutafuta maji tu. Bado wanatembea kilometa nane mpaka kumi kutafuta maji tu.
Mheshimiwa Spika, niiombe sana Serikali iweze kutatua tatizo hili ili akinamama hawa waweze kushiriki vizuri katika ujenzi wa Taifa lao. Ipo haja sasa ya Serikali kutoa kipaumbele kwa wawekezaji binafsi kama ilivyo katika sekta ya elimu ili tuweze kutatua kabisa tatizo hili la upungufu wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile miradi ielekezwe vizuri kuliko sasa hivi, kuna miradi mingi inaanzishwa lakini inasuasua na mingine haiishi kabisa. Kuna mradi wa maji katika Wilaya ya Nyang‟hwale. Hivi sasa ni mwaka wa tano lakini haijulikani kama mradi huu utakwisha au la! Kutokamilika kwa miradi kama hii kunasababisha sehemu kama vituo vya afya, zahanati, hospitali, kukosa maji safi na salama hivyo kuwa na mazingira hatarishi kwa mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu. Niombe sana Serikali ijipange vizuri katika kutatua tatizo hili la ukosefu wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la elimu, nimpongeze tena Rais wetu mpendwa na kumshukuru sana kwa kutuletea elimu bure kutoka Chekechea mpaka Kidato cha IV. Pia niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kujenga shule za Sekondari za Kata nchi nzima. Sasa hivi tuna uhakika watoto wetu watafika angalau Kidato cha IV.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, changamoto iliyopo sasa ni upungufu wa vyuo vya ufundi pamoja na VETA. Mkoa wa Geita ni mpya, tunahitaji kupata chuo cha ufundi na chuo cha VETA, lakini siyo Mkoa wa Geita tu bali ni mikoa yote. Naomba Serikali ijipange ili tuweze kuwa na vyuo vya ufundi nchi nzima ili watoto wetu hawa wanavyomaliza Form Four waweze kuingia vyuo vya ufundi na vyuo vya VETA.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema na kuniwezesha kuwa hapa Bungeni leo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya. Nimpongeze Waziri na Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanazozifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inafanya jitihada kubwa za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama lakini bado kunahitajika jitihada za ziada katika suala hili la maji. Naishauri Serikali ili suala hili la maji liende vizuri iweke ukomo kama ilivyoweka TANESCO kwamba ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote vitapata umeme. Kwa hiyo, Wizara ya Maji nayo itamke muda rasmi wa kumaliza tatizo la maji kwa vijiji vyote nchini, hii itasaidia miradi kukamilika kwa wakati.
Kuna mradi wa maji katika Wilaya ya Nyang’hwale leo ni mwaka wa sita tangu uanzishwe, wananchi wanateseka na haijulikani lini watapata maji. Niiombe sana Serikali iweze kumaliza mradi huu wa maji ili wananchi wa Nyang’hwale wapate maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya maji katika Mji wa Geita na vitongoji vyake ni makubwa sana ukilinganisha na maji tunayoyapata, mahitaji halisi ni lita 15,000,000 kwa siku lakini tunayopata ni lita 4,000,000. Kwa hiyo, kuna upungufu wa lita 11,000,000 kwa siku sawa na asilimia 29 ya maji tunayopata. Niiombe sana Serikali iongeze uwezo wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Viktoria ili tuweze kupata maji ya kutosha kulingana na mahitaji yetu ya maji kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa uchimbaji visima virefu 16 katika Halmashauri ya Mji katika vijiji 16 tofauti tofauti ambapo mpaka sasa mkandarasi amechimba visima vyote 16 na visima saba tu ndiyo vimefanikiwa kupata maji. Pamoja na vyanzo hivyo kuchangia kiwango hicho cha maji lakini bado huduma ya maji ni changamoto. Hivyo tunaiomba Wizara kuchukua hatua za makusudi katika kuhakikisha upanuzi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria unafanyika ili kukidhi mahitaji ya maji kwa siku katika Mji wa Geita na vitongoji vyake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa katika Idara ya Maji Geita nayo ni kukosa usafiri kwa ajili ya kufuatilia miradi ya maji iliyopo pembezoni mwa halmashauri. Tunaomba tupatiwe gari kwa ajili ya watendaji wetu ili waweze kumudu vizuri shughuli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa hapa leo, pia kwa kutulinda sisi sote Wabunge na kuwa hapa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana anazofanya. Ninamuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumuongoza, amlinde, amtunze na ampe maisha marefu. Nimpongeze Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Baraza lote la Mawaziri kwa kazi nzuri sana wanazozifanya. Nimpongeze sana Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Ndalichako kwa hotuba nzuri. Pia nimpongeze Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Naibu Waziri na watendaji wote wa wizara kwa kazi nzuri sana wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo naomba nichangie sasa kuhusu elimu katika Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuweza kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati shule kongwe hapa nchini. Kazi iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika kukarabati shule kongwe hapa nchini ni nzuri mno na inafaa kupongezwa na kila Mtanzania anayependa maendeleo. Hongera sana Serikali, hongera sana TAMISEMI na hongera sana Wizara ya Elimu kwa kuweza kusimamia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee upungufu wa walimu katika Mkoa wangu wa Geita. Katika Mkoa wa Geita shule nyingi za msingi hazina walimu wa kutosha hivyo kupelekea walimu wachache sana na sera yetu ya elimu inasema mwalimu anatakiwa afundishe wanafunzi 45, lakini kwa mapungufu yaliyopo katika Mkoa wa Geita mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 100 mpaka 150. Kwa hiyo, kwa kweli ni changamoto, niombe sana Serikali iweze kutupatia walimu wa kutosha kulingana na mahitaji yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika shule zetu za sekondari za kata kuna mapungufu makubwa sana ya walimu na hasa walimu wa sayansi. Hatuwezi kufikia uchumi wa kati bila kuwa na walimu wa kutosha wa sayansi. Hivyo niombe sana Serikali iweze kuliona hilo watupatie walimu wa kutosha katika Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu wa nyumba za walimu na mabweni, changamoto hii ni kubwa sana. Mwalimu anapokuwa mbali na kituo chake cha kazi hukupelekea kuchelewa kufika kazini, matokeo yake shule huwa chini ya kiwango. Niombe sana Serikali, mimi nishauri kwa nini tusitumie Shirika letu la Nyumba kuweza kujenga nyumba za walimu pamoja na mabweni ili kuondoa kabisa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo lingine la walimu kutopanda madaraja. Kuna walimu morale ya kufundisha inashuka kutokana na kutopanda madaraja kwa wakati. Mwalimu anapokaa kwenye daraja moja mwaka mmoja mpaka miaka mitano bila kubadilishwa kwa kweli inakatisha tamaa, matokeo yake walimu wanashindwa kufundisha vizuri. Mimi niombe Serikali iweze kuona inafanyaje ili walimu hawa waweze kupandishwa madaraja kwa wakati unaofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA:Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya TAMISEMI. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema lakini pia kuweza kusimama hapa leo jioni hii. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa hotuba yake nzuri, lakini pia tumpongeze sana kwa kazi nzuri anazozifanya. Vile vile niwapongeze Manaibu Waziri, niwapongeze watendaji wote wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri wanazozifanya, lakini vile vile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Utumishi na Utawala bora, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, nimpongeze Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa jinsi wanavyotekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi. Hongera sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nianze kutoa mchango wangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa jinsi ilivyojipanga kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika vizuri. Kwa kweli Serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa sana kuweza kujenga hospitali za wilaya, hospitali za mkoa lakini pia kujenga vituo vya afya, zahanati, kununua vifaa tiba vya kutosha na kikubwa zaidi kupata madawa ya kutosha kwa nchi nzima. Haya yote ni matunda mazuri ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, tunamshukuru sana, tunampongeza mno na tunamtakia kila lililo la kheri katika maisha yake hapa duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wangu wa Geita tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunaishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi tumeweza kupata billion 5.9 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya rufaa na kwa sasa tumeshapata bilioni 3.7 na mkandarasi yupo kazini anaendelea. Tunaishukuru sana Serikali na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, palipo na mafanikio lazima kuna changamoto; changamoto yangu ya kwanza ni upungufu wa Wauguzi katika zahanati zetu, kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika zahanati zetu, unaweza ukakuta zahanati moja, ina Muuguzi mmoja,anafanyaje kazi. Sasa niiombe sana Serikali iweze kuona ni namna gani itaweza kutupatia Wauguzi wa kutosha katika zahanati zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili ni upungufu wa Madaktari katika vituo vyetu vya afya. Hili pia ni tatizo, huko kwenye vituo vya afya tunapofanya ziara, kuna vituo vya afya vingine utakuta daktari mmoja na muuguzi mmoja. Kituo cha afya ni wananchi kata nzima, wananchi hawa ni wengi mno kuweza kupewa huduma na mtu mmoja, niiombe sana Serikali iweze kuona ni namna gani itaweza kutupatia Madaktari wa kutosha katika vituo vyetu vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto yangu ya tatu ni kukosekana kwa Madaktari Bigwa katika wilaya, niiombe sana Serikali yangu iweze kupeleka Madaktari Bigwa kwa watoto na akinamama katika hospitali zetu za wilaya. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu kumekuwa na msongamano mkubwa mno kwenye hospitali zetu za rufaa kwa sababu ya wagonjwa wengi kwenda kwenye rufaa, lakini Madaktari Bigwa wakiwa kwenye hospitali za wilaya tutapunguza huo msongamano na wananchi wetu watakuwa hawapati shida kama hivi sasa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kuliona hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tena, katika Mkoa wangu wa Geita wananchi wamehamasika sana kujenga maboma kwa ajili ya vituo vya afya lakini pia, Zahanati kwa maana hiyo tunamaboma mengi sana ambayo yamesimama na nimpongeze sana Mkuu wangu wa Mkoa wa Geita kwa jinsi alivyosimamia ujenzi huo, niombe sasa Serikali iweze kuunga mkono jitihada za wananchi hawa ili maboma hayo yaweze kukamilika kwa kuezekwa na wananchi hawa waweze kupata huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza hayo, naomba kuunga mkono hoja.Ahsante.(Makofi)