Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Josephine Tabitha Chagulla (11 total)

MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Vijana wengi wa Mkoa wa Geita hawana ajira kutokana na ukosefu wa viwanda na hasa ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya uchumi wetu unategemea kilimo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda vya kusindika mazao katika Mkoa wa Geita?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI, alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Thabita Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kuchangia ukuaji wa nchi, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia mkakati unganishi wa maendeleo ya viwanda (Integrated industrial Development Strategy), lengo ni kuhamasisha wananchi na wadau kuwekeza katika kuanzisha viwanda. Viwanda hivyo ni pamoja na viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa vyenye lengo la kuzalisha bidhaa zinazotokana na rasilimali zinazopatikana hapa nchini zikiwemo zile za kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini zitakazounganisha nchi nzima pamoja na Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati huo pia unazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa na Miji kutenga maeneo ya uwekezaji katika viwanda hadi ngazi ya Kata ambayo itatumika kuanzisha Mitaa ya Viwanda kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo husika. Wizara itakuwa na jukumu la kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kuanzisha viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara inamfuatilia mwekezaji ambaye ni bingwa wa kutengeneza juice akichukua kati ya namba tano mpaka saba duniani ili ajenge kiwanda mkoani Geita. Ujenzi wa kiwanda hicho utaenda sambamba na uwekezaji katika kilimo cha kisasa ambapo makubaliano yatafikiwa kwa kuwa na nuclear farm na wakulima wanaomzunguka kuweza kupatiwa huduma (outgrowers). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Wizara kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) itaendelea kushirikiana na wadau Mkoani Geita kuibua miradi kupitia program ya Wilaya Moja, Bidhaa Moja, (One District One Product-ODOP) kwa lengo la kuanzisha na kukuza viwanda katika ngazi ya Wilaya na hivyo kuleta ajira kwa vijana vijijini. Hatua hiyo itasaidia kupunguza wimbi kubwa la sasa lililopo la vijana kukimbilia Mijini sambamba na kuongeza pato binafsi na pato la Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane katika kuhamasisha na kuvutia sekta binafsi kuwekeza na kutumia fursa zilizopo katika Mkoa wa Geita.
MHE. JOSEPHINA T. CHAGULA aliuliza:-
Hivi sasa kumeibuka wimbi kubwa la wagonjwa wa kisukari na miongoni mwa waathirika ni wanawake na watoto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kisukari katika Zahanati na Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephina Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, dawa za ugonjwa wa kisukari zinapatikana katika ngazi zote za huduma za afya kwa kupitia utaratibu wa Bohari ya Dawa (MSD). Kwa wananchi walio kwenye Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) wanapata dawa hizo kwa kupitia bima zao. Watoto chini ya umri wa miaka mitano wao wanapata dawa hizi bila malipo yoyote kupitia Mpango wa Taifa wa Kisukari. Kwa wale watu wazima ambao hawamo kwenye NHIF, wao wanazipata kupitia utaratibu wa kuchangia huduma za afya (cost sharing).
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeongeza bajeti ya fedha za kununulia dawa kutoka shilingi bilioni 33 mwaka 2015 hadi 2016 hadi kufikia shilingi bilioni 251.5 kwa mwaka wa Fedha 2016/2017. Hivyo ni matarajio yetu kuwa upatikanaji wa dawa utaongezeka ikiwa ni pamoja na dawa za kutibu magonjwa ya kisukari.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Wilaya ya Nyang’hwale ni moja kati ya Wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni ili kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuwezesha kujenga ofisi na nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya eneo la Karumwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Halmashauri mpya ya Nyang’hwale ilipokea shilingi milioni 450 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa ofisi katka Makao Makuu ya Wilaya iliyoko Karumwa. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 177.7 zimetumika kumlipa Mtaalam Mshauri ambaye ni BJ Amili Limited kwa ajili ya kuandaa michoro, upembuzi yakinifu na usanifu wa eneo lote zinalojengwa ofisi. Kiasi kilichobaki kinajumuishwa katika fedha zilizoombwa mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri hiyo imetengewa shilingi milioni 850 kwa ajili ya kuendela na ujenzi majengo ya Makao Makuu ya Halmashauri katika eneo la Karumwa. Azma ya Serikali ni kuhakikisha ofisi na nyumba za watumishi zinajenwa katika Wilaya na Mikoa mipya kwa awamu ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Serikali ilipandisha hadhi Kituo cha Afya Kharumwa kuwa Hospitali ya Wilaya Nyang’hwale.
Je, ni lini Serikali itaongeza majengo kwa ajili ya wodi
za wagonjwa na wodi za wazazi katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA SERIKALI ZA MIKOA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri ya Wilaya ya Ngang’wale ilitengewa ruzuku ya maendeleo isiyokuwa na masharti (LGDG) kiasi cha 533,822,000 kwa ajili ya ujenzi wa miradi, ikiwemo sekta ya afya. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 186.6 zimeshapokelewa. Fedha hizo zinapaswa kutekeleza miradi ambayo ni kipaumbele cha halmshauri kilichowekwa na wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeongeza ruzuku ya maendeleo hadi shilingi bilioni 1.038 sawa na ongezeko la asilimia 95. Vipaumbele vya matumizi ya fedha hizo ikiwemo ujenzi wa wodi, vitapangwa na halmashauri zenyewe kwa kuzingatia fursa na vikwazo vilivyopo.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu benki haziwafikii, pia hawana mafunzo maalum ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya kufikia huduma hiyo ya kukopeshwa:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa akina mama hao mafunzo maalum yatakayowasaidia katika kujipanga kukopa?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma
ya benki vijijini ili wanawake wa huko waweze kupata mikopo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mageuzi ya Pili ya Mfumo wa Sekta ya Fedha (Second Generation Financial Sector Reforms) Benki Kuu ilipewa jukumu la kusimamia uundwaji wa muundo wa utoaji elimu ya masuala ya fedha nchini. Muundo huu ulikamilika mwaka 2015 na kuzinduliwa mwaka 2016 mwezi wa pili na una maeneo makuu matatu ambayo ni mkakati wa elimu ya fedha, ikijumuisha makundi maalum, aina ya elimu na namna itakavyotolewa, mfumo wa usimamizi wa utoaji elimu na namna ya kupima utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa elimu ya fedha inahusisha wadau mbalimbali ikiwemo Serikali na Taasisi zake, Benki Kuu inaratibu uanzishwaji wa Taasisi ya Kitaifa itakayokuwa na jukumu la kuratibu, kuwezesha na kusimamia utoaji wa elimu ya fedha. Baada ya kuunda Taasisi ya Kitaifa ya Uratibu wa Elimu ya Fedha, kutakuwepo na mfumo rasmi nchini wa utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo akina mama wa vijijini.
Hata hivyo, taasisi za fedha zina utaratibu wa kutoa elimu ya fedha kwa wateja wao wakiwemo wanawake ili kuhakikisha kwamba wateja wao wanaendesha biashara zao kwa ufanisi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa wananchi kupata huduma za kibenki karibu na maeneo yao. Pia Serikali inatambua umuhimu wa taasisi hizo katika kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi. Hata hivyo, kufuatia mabadiliko ya mfumo wa kifedha nchini kuanzia mwaka 1991 Serikali ilijitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kibenki. Uanzishwaji wa huduma za kibenki unafanywa kwa sehemu kubwa na sekta binafsi na hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia uwepo wa faida kwa pande zote mbili, yaani benki na wananchi na hii hutegemea vigezo kadhaa ikiwa ni pamoja na hali ya uchumi wa eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua pia mabenki mengi huendesha shughuli zake mijini kwa sababu ya urahisi wa upatikanaji wa miundombinu muhimu kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kibenki. Kwa kuzingatia hilo, Serikali inajitahidi kuboresha miundombinu kama vile teknolojia ya mawasiliano, barabara, ulinzi, umeme na maji katika maeneo ya vijijini, ili kuweka mazingira bora yatakayovutia wawekezaji katika sekta binafsi kupanua huduma za kibenki kwenye maeneo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imetoa Mwongozo wa Uwakala wa Huduma za Kibenki. Utaratibu huu wa Uwakala unapanua wigo wa huduma za kibenki ili kuwezesha huduma hii ya kibenki kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwa gharama nafuu, hasa katika maeneo ya vijijini. Aidha, mabenki yameshaanza kuweka mawakala maeneo mbalimbali na wananchi wa maeneo husika wameshaanza kufaidi huduma za kibenki zinazotolewa na Wakala wa Huduma za Kibenki.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Hospitali ya Mkoa wa Geita inakabiliwa na kero mbalimbali kama vile ukosefu wa Madaktari Bingwa wa akinamama na watoto, dawa, vifaa tiba pamoja na uhaba wa majengo ya wodi za wazazi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutatua kero hizo katika Hospitali ya Mkoa wa Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabitha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mkoa wa Geita ina Daktari Bingwa mmoja wa upasuaji. Madaktari wengine watatu wako masomoni akiwemo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akina Mama na Watoto. Ukosefu wa Madaktari Bingwa unasababishwa na uchache wa Madaktari ukilinganisha na uhitaji wetu. Katika kibali cha mwaka wa fedha 2017/2018 cha kuajiri watumishi 2,058 kilichokuwa na Madaktari 46, Hospitali ya Mkoa wa Geita imepangiwa jumla ya Madaktari wanne ambao wamesharipoti na wameanza kazi, naamini Madaktari hao watapunguza uhaba uliopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa dawa, Mkoa wa Geita umepanga kuanzisha duka la dawa kwa kutumia mkopo wa shilingi milioni 160 kutoka NHIF. Wagonjwa watapatiwa dawa na vifaa tiba kwa gharama nafuu zaidi ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kutatua tatizo la uhaba wa miundombinu mkoa unaendelea na ujenzi wa Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Geita. Ujenzi upo katika hatua za msingi kwa majengo manne ambayo ni jengo la upasuaji, wagonjwa wa nje, jengo la mionzi na jengo la kufulia nguo. Kazi hii inatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Kumekuwepo na tatizo kubwa la ukosefu wa maji safi na salama katika Mkoa wa Geita pamoja na Wilaya zake kama Bukombe, Chato, Mbogwe na Nyang’hwale.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hilo la maji kwa wananchi wa Mkoa wa Geita na Wilaya zake?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Geita kwa kutekeleza miradi mbalimbali. Kwa upande wa maji vijijini Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) kwa Halmashauri zote za Mkoa wa Geita kama ilivyo katika Halmashauri zote hapa nchini. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2018 Serikali imetekeleza miradi 66 katika vijiji 217 vilivyopo katika wilaya za Mkoa wa Geita zikiwemo Wilaya za Bukombe, Chato, Mbogwe na Nang’hwale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maji mijini, Serikali imeendelea na juhudi mbalimbali za kuboresha huduma ya maji ambapo imekamilisha upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji na jumla ya kilometa 101.3 za mabomba zimelazwa. Mradi huo umewanufaisha wakazi 14,300 wa Mji wa Geita. Kwa upande wa Mji wa Ushirombo katika Wilaya ya Bukombe, Serikali imekamilisha usanifu wa uboreshaji wa huduma ya maji ambapo mradi huo unawanufaisha wakazi 10,722. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2018, taratibu za kumpata mkandarasi wa mradi huo zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwa lengo la kuwapatia wananchi wengi zaidi huduma ya maji safi na salama.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y JOSEPHINE T. CHAGULA) aliuliza:-

Hospitali ya Mkoa wa Geita haina jenereta la dharura pindi umeme unapokatika na hivyo kusababisha vifo vingi kutokea:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka jenereta la dharura katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jenereta lililokuwa linatumika katika hospitali ya Mkoa wa Geita lilipata hitilafu na hivyo kufanya hospitali ya Mkoa wa Geita kutokuwa na jenereta la dharura.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hospitali ya Mkoa wa Geita imepata jenereta mbadala lenye ukubwa wa KVA 400 ambalo linakidhi mahitaji yote ya hospitali. Jenereta hili lilipatikana kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita kupitia Mgodi wa GGM.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULLA aliuliza:-

Mkoa wa Geita hauna Chuo cha Serikali hata kimoja:-

Je ni lini Serikali itajenga Vyuo Mkoani Geita ikiwemo vya Afya na Madini?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa elimu inayotolewa katika ngazi ya vyuo katika kujenga ujuzi unaochochea maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Hivyo, ni azma ya Serikali kujenga na kuboresha vyuo vilivyopo katika mikoa mbalimbali nchini ili viweze kutoa elimu bora kwa wanafunzi wengi zaidi. Kwa sasa mkoa huu una Chuo kimoja cha Serikali cha Uuguzi ngazi ya kati (Geita School of Nursing). Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vingine viwili vya VETA. Wizara pia imepokea maombi kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita ya kukikabidhi Chuo cha Ujasiliamali kiitwacho Magogo ili kiwe chini ya Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA). Serikali imeridhia ombi hilo na taratibu za makabidhiano zinaendelea. Kwa kuwa vyuo hivi vimezungukwa na migodi, pamoja na fani zingine, Serikali itaangalia pia uwezekano wa kuanzisha fani ya madini.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Geita pia kuna tawi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambacho hutoa masomo kwa ngazi ya elimu ya juu. Kwa kuwa masomo ya ngazi ya elimu ya juu ni suala la kitaifa, kwa sasa wananchi wa Geita wanashauriwa kuendelea kutumia vyuo vikuu vingine vilivyopo nchini.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka walimu katika shule za sekondari na msingi Wilayani Nyang’hwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023 Serikali iliajiri Walimu 13,130 ambapo Walimu 20 wa shule za msingi na 55 wa shule za Sekondari walipelekwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale. Serikali inatambua mahitaji ya Walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale na maeneo mengine. Hata hivyo, kila mwaka Serikali inaendelea kupunguza mahitaji ya walimu katika sekta ya elimu na hivi karibuni Serikali itatangaza ajira za walimu baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi kukamilika na kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka Watumishi pamoja na Vifaa Tiba katika Hospitali ya Mkoa wa Geita?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Tabitha Chagula, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mkoa wa Geita ina jumla ya watumishi 349. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imepeleka watumishi 22 wa kada mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita. Pia Serikali imepeleka vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.