Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Josephine Tabitha Chagulla (1 total)

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na nipende kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa sana na nzuri inayoifanya katika kupeleka umeme Jimbo la Bukoba Vijijini. Pamoja na hayo nina maswali mawili madogo ya nyogeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Jimbo la Bukoba Vijijini ni kubwa sana, lina vijiji 94 na vitongoji kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri vitongoji 515 na vitongoji ambavyo vimepewa umeme ni nusu ya vitongoji vilivyopo.

Je, hawaoni kwamba ni vyema katika mgao ujao Bukoba ipewe kipaumbele badala ya vitongoji 15 vipewe 60 au 100 kusudi watu wapate umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunafahamu kwamba kufunga umeme vijijini ni shilingi 27,000 kwa nyumba, lakini watu wangu wanaombwa 300,000/400,000 badala ya shilingi 27,000 na ni vijijini, je, ni kwa nini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kuhusiana na kupeleka umeme kwenye vitongoji ambavyo bado havina umeme, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tayari kuna miradi inaendelea katika Jimbo la Bukoba Vijijini na tunatarajia kuwa na mradi mkubwa wa kupeleka umeme pia kwenye vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya yanatofautiana, na ni kweli kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge takribani nusu ya vitongoji havina umeme. Tutaendelea kushirikiana na Taasisi yetu ya Wakala wa Nishati Vijijini kuhakikisha kwamba maeneo ambayo kwa kweli miradi ya vitongoji ipo nyuma yanapewa jicho la kipekee ili kuhakikisha kwamba nayo yanapanda kidogo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, miradi ipo ambayo inafanyika, lakini na kwa miradi inayokuja tutaendelea kuhakikisha Bukoba Vijijini tunaingalia kwa jicho la kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili la maeneo ya vijiji ambayo yanakuwa-charged shilingi 321,000. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na ni kweli kwenye baadhi ya maeneo yake ambayo ni vijiji kuna baadhi ya eneo kama moja au mawili yanakuwa-charged shilingi 321,000. Kwa niaba ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati nimwelekeze Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuyapitia maeneo haya ambayo ni vijiji na kwa namna moja ama nyingine yanakuwa-charged zaidi ya bei ambayo Serikali imetoa mwongozo, ahsante.