Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Nape Moses Nnauye (20 total)

MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:-
Tanzania ni mwenyeji mkubwa kati ya nchi zilizounda Umoja wa Afrika Mashariki, hivyo basi, hupelekea au hupaswa Watanzania kufaidika na soko la Afrika Mashariki:-
(a) Je, Serikali inawashauri nini wananchi wake wanapokwenda kibiashara kwenye nchi zinazounda umoja huo?
(b) Je, pindi wanapopata matatizo au vikwazo katika nchi husika ni wapi watapeleka malalamiko?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mbunge wa Micheweni, napenda kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimendoleana ushuru wa forodha mipakani, hatua ambayo inapanua soko la bidhaa za Tanzania kufikia Wanaafrika Mashariki takribani milioni 143 katika nchi tano Wanachama wa Jumuiya za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Hivyo ni dhahiri kuwa, endapo soko hilo litatumika kikamilifu litachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Taifa na kupunguza umaskini wa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inawashauri wananchi kuzichangamkia fursa za kibiashara, ajira, uwekezaji na kadhalika zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kujiharakishia maendeleo.
Pili, Serikali inawashauri wananchi kuzitambua taratibu za kufuatwa katika kuzitumia fursa za kibiashara zilizopo katika Jumuiya kama nchi wanachama zilivyokubaliana ikiwa ni pamoja na kuwa na cheti kinachobainisha kuwa bidhaa imezalishwa ndani ya Jumuiya yaani cheti cha uasili wa bidhaa- EAC certificate of Origin na vibali/nyaraka kutoka mamlaka husika kutegemeana na aina ya bidhaa mfanyabiashara anazotaka kuuza au kununua.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa katika kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, vikwazo visivyo vya kiforodha hujitokeza kwa wafanyabiashara wetu kinyume na makubaliano ya nchi wanachama. Napenda kutoa rai kwa wafanyabiashara kuwasiliana na Wizara yangu pindi wanapopata matatizo au vikwazo vya kibiashara katika Jumuiya, Balozi zetu au Vyama vya Wafanyabiashara kama vile Tanzania Chamber of Commerce Industry and Agriculture (TCCIA), Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Tanzania Exporters Assosiation (TANEXA) na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Wizara imeweka mabango makubwa yani double sided billboards yenye ujumbe wa taratibu za kufuatwa na wafanyabiashara wadogo, wa kati, wa kuuza au kuagiza bidhaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mipaka ya Horohoro, Rusumo, Kabanga, Namanga, Sirari na Mtukula na vilevile imeweka Maafisa wake katika mipaka ya Rusumo, Mtukula, Namanga na Sirari kwa ajili ya kuwasaidia au kutatua changamoto za wananchi wanapofanya biashara na nchi wanachama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha wananchi katika Majimbo yao kuzitumia fursa zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y. MHE. MARTHA J. UMBULLA) aliuliza:-
Ujenzi wa senta ya Michezo ya riadha katika Mkoa wa Manyara hususani Wilaya ya Mbulu imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa viongozi na wananchi wa eneo husika kutokana na vijana wengi kuwa na vipaji katika mchezo wa riadha na michezo mingine:-
(a) Je, ni lini Serikali itasikiliza kilio cha muda mrefu na kujenga senta ya michezo ya riadha Mkoani Manyara ili vijana wengi wenye vipaji waweze kunufaika?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kujenga senta ya michezo Manyara itaweza kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wa Mkoa huo na maeneo jirani kama Singida, Arusha na Dodoma ambako kuna vipaji hivyo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Manyara na Wilaya zake una vijana wenye vipaji vya riadha na michezo mingine. Aidha, Serikali inatambua pia umuhimu wa kuwa na kituo kikubwa cha michezo hasa ya riadha ambacho pamoja na mambo mengine kitasaidia kuibua, kukuza na kuviendeleza vipaji vya vijana ikiwa ni pamoja na kuwapatia ajira vijana mkoani humo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Massay, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mkoa wa Manyara imepanga kujenga kituo cha michezo cha mkoa mara baada ya kukamilisha mazungumzo na kukubaliana na wananchi wanaomiliki ardhi katika eneo ambalo mkoa wamekubaliana. Aidha, kwa kipindi hiki ambacho uongozi wa mkoa hauna kituo cha michezo, mkoa umepanga kutumia kambi ya michezo ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa muda, wakati wanasubiri kupatikana kwa eneo la kudumu la mkoa. Hii ni kutokana na sababu kuwa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ina hosteli na viwanja vya michezo vya kutosha.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kujengwa kwa kituo hiki katika mkoa kutaongeza ajira, kutapanua shughuli za kibiashara na hata kukua kwa uchumi wa Mkoa wa Manyara. Serikali inaendelea na mazungumzo na wananchi wamiliki wa eneo husika, yakikamilika na pesa zikipatikana ujenzi wa kituo hiki cha michezo utaanza.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. HAFIDH ALI TAHIR) aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, katika Bunge la 2005 – 2010 kulitokea hoja ya TFF kujiunga katika Shirikisho la Mpira la Kimataifa (FIFA) bila ridhaa ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; hoja hiyo ilipelekea aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda kuunda Kamati Maalum yenye Wajumbe kutoka ZFA na TFF ili kuondoa utata huo:-
(a) Je, ni nini matokeo ya Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kutopatikana muafaka au uamuzi uliofikiwa kwa pamoja ni kuchelewesha agizo la Waziri Mkuu?
(c) Je, Serikali inasemaje kuhusu ubabaishaji unaofanywa na TFF?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir, Mbunge wa Dimani, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kufuatia majadiliano na vikao kadhaa vilivyofanyika katika kipindi cha mwaka 2005/2010 kumbukumbu zinaonyesha kwamba suala zima la uanachama wa TFF na ZFA lilifanyiwa kazi kwa ukamilifu na Serikali za pande zote mbili kwa ushirikiano na vyama vyote viwili.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa ZFA kupata uanachama wa FIFA, mwaka 2010 Ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ukiongozwa na aliyekuwa Naibu Waziri Kiongozi Mheshimiwa Juma Shamhuna pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Joel Bendera walikwenda Zurich-Switzerland ambako walikutana na Rais wa FIFA wa wakati huo. Aidha, katika msafara huo walifuatana na viongozi wa TFF na ZFA. Madhumuni ya safari hiyo ilikuwa ni kuwasilisha maombi ya ZFA kupewa uanachama wa FIFA.
Mheshimiwa Spika, mwezi Juni 2011, FIFA iliiandikia ZFA ikiwajulisha kuwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo isingewezekana Zanzibar kupata uanachama wa FIFA kwa kuwa uanachama wao ni nchi zinazotambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyoelezwa katika aya ya 10 ya Katiba hiyo.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa maelezo haya, ni dhahiri kuwa suala la usajili wa TFF na ZFA linafahamika vyema ndani ya Serikali ya Mapinduzi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa uanachama wa TFF katika FIFA upo kwa mujibu wa muafaka wa pande zote mbili.
(c) Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia utaratibu huo wa FIFA kuhusu suala hilo, Wizara yangu imewaelekeza TFF na wako tayari kufanya maridhiano na ZFA ili kukamilisha utaratibu wa wazi wa kukidhi mahitaji ya Zanzibar kushiriki katika masuala ya FIFA kupitia TFF bila kuathiri ushiriki wa klabu za Zanzibar katika mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika yaani CAF.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y MHE. HASSAN E. MASALA) aliuliza:-
Redio ya Taifa (TBC) haisikiki Wilayani Nachingwea, pamoja na kuwepo kituo cha kurusha matangazo katika eneo la Stesheni.
(a) Je, ni tatizo gani linasababisha kutosikika kwa Redio ya Taifa katika Jimbo la Nachingwea?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kukifanyia ukarabati kituo cha kurushia matangazo Nachingwea ambacho pia ni chanzo cha ajira kwa wakazi wa jirani na kituo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, matangazo ya Redio ya Taifa katika Jimbo la Nachingwea yalikuwa yakisikika maeneo yote ya Wilaya ya Nachingwea na Mikoa ya Kusini kwa ujumla kupitia mtambo wa masafa ya kati (medium wave) wa kilowati 100 ambao tangu tarehe 01/01/2012 haufanyi kazi kutokana na uchakavu. Kwa hivi sasa eneo la Nachingwea Mjini ndilo linalopata matangazo ya Taifa kwa kutumia mitambo miwili midogo ya redio, FM ya watt 230 (TBC- FM) na watt 100 TBC-Taifa, ambayo imefungwa katika kituo cha redio kilichopo eneo la Songambele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali, ni kufunga mitambo mpya na ya kisasa ya FM yenye nguvu kubwa ya kilowati mbili pale fedha zitakapopatikana.
Mtambo huo utakuwa na uwezo wa kurusha matangazo yatakayowafika wananchi sehemu mbalimbali. Ufungwaji wa mitambo hiyo utaenda sambamba na ukarabati wa majengo ya mitambo, Ofisi na miundombinu mbalimbali ya kituo cha Nachingwea.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Wananchi wa Tarafa za Hagati, Mbuji na Mkumbi hawapati matangazo ya Redio ya TBC kutokana na Kituo cha TBC- Songea kutokuwa na uwezo wa kurusha matangazo na badala yake wanapata matangazo ya redio toka nchi jirani ya Malawi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza uwezo wa kurusha matangazo ya kituo cha TBC- Songea ili wananchi wa Tarafa hizo wapate habari kupitia TBC?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martin Alexander Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, matangazo ya Radio ya Taifa kupitia mtambo wa masafa ya kati yaani Medium Wave yenye nguvu ya Kilowati 100 yalikuwa yakisikika vizuri katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma wakati mtambo huo ulipokuwa ukifanya kazi. Tangu mwezi Julai, 2013 mtambo huo haufanyi kazi kutokana na uchakavu na hivyo kuathiri usikivu wa matangazo ya TBC katika maeneo kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa wananchi kupata matangazo, TBC ililazimika kuhamisha mitambo yake miwili ya Radio yenye uwezo wa Kilowati moja kwa kila mmoja iliyokuwa imefungwa eneo la Mshangano - Songea na kuifunga eneo la juu la mlima wa Matogoro (Songea) ili angalau usikivu wake usambae eneo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kufunga mitambo hiyo, matangazo ya TBC- Songea yameboreshwa. Hata hivyo, kutokana na uwezo mdogo wa mitambo ya FM inayotumika kwa sasa mawimbi yake ya sauti hayafiki mbali sana ukilinganisha na yale ya mitambo ya Medium Wave iliyokuwa ikitumika wakati wa awali ambayo yanafika eneo kubwa zaidi la Mkoa wa Ruvuma zikiwemo Tarafa za Hagati, Mbuji, na Mkumbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kukabiliana na changamoto za usikivu hafifu katika maeneo kadhaa Mkoani Ruvuma, TBC imeshafanya upembuzi yakinifu wa kufunga mitambo ya FM yenye uwezo wa kilowati moja katika eneo la Mbamba Bay lililopo Wilaya ya Nyasa ili kuongeza usikivu wa redio na TBC. Katika bajeti ya mwaka wa 2016/2017, Wizara yangu imetenga fedha za maendeleo kwa ajili ya kufunga mtambo eneo la Mbamba Bay. Kazi hiyo ya uboreshaji wa matangazo katika eneo hilo itaanza mara tu fedha za kununua na kufunga mitambo zitakapotolewa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:-
Kwa nini Serikali isifute michezo Tanzania?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Methuselah Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimtambue Mheshimiwa Venance Mwamoto kama mwanamichezo ambaye amewahi kucheza mpira wa miguu katika timu ya ligi daraja la kwanza wakati huo, sawa na ligi kuu Tanzania kwa sasa, yaani timu ya Majimaji ya Songea na RTC ya Kagera lakini pia timu ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, hapa Bungeni Mheshimiwa Venance Mwamoto ndiye Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kufuatia sifa hizo za Mheshimiwa Venance Methuselah Mwamoto, binafsi naamini kuwa swali lake limelenga kupata maelezo ya kwa nini michezo haiendelei kwa kasi wanayotamani wapenda michezo wengi hapa Tanzania na wala siamini kuwa anayo nia ya kutaka Serikali ifute michezo kwa kuwa anafahamu fika umuhimu wa michezo kwa Taifa paoja na wananchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania haiwezi na wala haina nia ya kufuta michezo nchini kwa sababu yoyote ile, badala yake nia ya Serikali ni kuiendeleza sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa hili kwa kuwekeza katika miundombinu ya michezo, elimu ya michezo ya kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa sekta ya michezo inaendelezwa ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge lako Tukufu kushirikiana na Serikali kuhimiza maendeleo ya michezo katika majimbo yetu. Aidha, tunashauri na kuhimiza wadau wote wa michezo ikiwemo Serikali za Mitaa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Waheshimiwa Wabunge, sekta binafsi na wadau wengine kuibua vipaji vya michezo kwa watoto kuanzia umri mdogo na kuviendeleza.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara na Taasisi zake itaendelea kutenga fedha kupitia bajeti yake na vyanzo vingine kadri inavyowezekana kila wakati ili kuendeleza michezo katika ngazi mbalimbali.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA aliuliza:-
Kila jamii ina mila na desturi zake; hapa nchini wanamuziki wamekuwa hawavai mavazi ya staha au utu wa mwanamke umekuwa ukidhalilishwa kutokana na kuvaa nguo zinazoonesha maungo yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti mavazi yasiyo na staha kwa wanamuziki wa kike?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) imekuwa ikitoa elimu kwa wasanii mara kwa mara kupitia vyombo vya habari, makongamano, semina na warsha juu ya umuhimu wa maadili katika sanaa na namna ya kubuni kazi za sanaa zenye ubora na zinazozingatia maadili, elimu imekuwa ikitolewa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo E fm Radio, EATV, Magic FM, Azam TV, Channel Ten, Clouds Entertainment na TBC.
Mheshimiwa Spika, kwa wasanii wanaokiuka maadili kwa kuvaa mavazi au kubuni kazi za sanaa zinazomdhalilisha mwanamke hatua za kinidhamu na kisheria kama vile kufungia kazi zao, kuwafungia wao wenyewe na kuwatoza faini zimekuwa zikichukuliwa.
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2014/2015 mpaka sasa wasanii watatu wa kike na msanii mmoja wa kiume na kikundi kimoja cha kanga moko walipewa maonyo na wengine kufungiwa kabisa kwa kudhalilisha utu wa mwanamke. Aidha,kwa mwaka 2016/2017 msanii mmoja wa kiume alipewa onyo na kutozwa faini.
Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997 imeeleza wazi kwamba kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda mila na desturi zetu sambamba na kuhakikisha maadili yanalindwa na mwanamke hadhalilishwi wakati wa shughuli za sanaa. Wizara yangu inapenda kutoa wito kwa kila Mtanzania kuhakikisha kwa namna moja au nyingine anatunza na kulinda maadili na utamaduni wa Mtanzania.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -

Je, lini minara ya mawasiliano itajengwa katika Kata za Endanywish, Endagulda, Gidurdagaw, Yaeda Ampa, Hayeda na Endanilay?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kKuna mnara umejengwa katika kata ya Bashay kijiji cha Bashay kwa lengo la kutoa huduma katika kijiji cha Bashay na baadhi ya maeneo ya Yaeda Ampa. Hata hivyo, baada ya ujenzi wa mnara kukamilika, bado ilionekana kuwa Vijiji vya Arri na Hayeseng kutoka Kata ya Yaeda Ampa bado havipati huduma nzuri ya mawasiliano na hivyo viliingizwa katika orodha ya miradi ya Tanzania ya Kidigitali ambapo zabuni ya mradi huu inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni mara idhini ya benki itakapotolewa.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeziingiza Kata za Endahagichan yenye Vijiji vya Endadubu, Miqaw na Endahagichan, Kata ya Eshkesh yenye Vijiji vya Domanga na Endagulda, kata ya Geterer yenye Vijiji vya Magong na Mewada, Kata ya Haydarer yenye Kijiji cha Gidbiyo, Kata ya Masqaroda yenye Kijiji cha Harbanghet, na Kata ya Yaeda Chini yenye Kijiji cha Endajachi katika mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambao kama nilivyosema zabuni yake inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata za Endanywish, Endagulda, Gidurgadaw, Hayeda na Endanilay tathmini ilifanyika na maeneo hayo yalionekana yana changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano na hivyo yataingizwa katika orodha ya miradi ambayo zabuni yake itatangazwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Kata za Ikoma, Roche, Gobire na Bukura zilizopo mpakani mwa Tanzania na Kenya?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Bukura Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeingia makubaliano na Kampuni ya Simu ya Halotel tarehe 30 Agosti, 2022 kwa ajili ya ujenzi wa mnara katika Kijiji cha Kirongwe kilichopo katika Kata ya Bukura. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa Kata za Ikoma na Roche zilizopo katika Jimbo la Rorya zimejumlishwa katika kata 763 ambazo zabuni ya kata hizo kwa ajili ya kupeleka huduma za mawasiliano inatarajiwa kutangazwa mapema mwezi Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata ya Gobiro, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umepokea changamoto hiyo na kwamba eneo husika litafanyiwa tathimini na litaingizwa kwenye zabuni za miradi ya mawasiliano itakayotangazwa kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuiwezesha TTCL kuunganisha Wateja wengi kwenye Mkongo wa Taifa kwa punguza gharama za kuunganisha?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba, 2021, Wizara iliingia mkataba wa ushirikiano na TANESCO kwa ajili ya matumizi ya pamoja ya miundombinu inayojengwa. Kupitia mkataba huo, miundombinu inayojenjwa kwenye nguzo za TANESCO nchi nzima zinazojumuisha nyaya za mawasiliano zitatumiwa kwa pamoja. Hivyo, kupitia ushirikiano huo, utawezesha TTCL kuunganisha wateja maeneo ya biashara na nyumbani (fiber to X) kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa gharama nafuu kwa kuwa gharama za uwekezaji zitapungua. Aidha, Serikali inaongeza uwezo wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano kutoka kiwango cha 200G hadi 800G. Kuongezeka kwa kiwango hiki kitasaidia kupunguza gharama, hali itakayopelekea kuwaunganisha wateja wengi zaidi.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine wa Serikali ni kuondoa Wizarani shughuli zote za mkongo wa Taifa wa mawasiliano na kupeleka TTCL. Suala hili litawezesha TTCL kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi ya kibiashara kwa haraka zaidi inayojumuisha masuala ya kuwaunganisha wateja kwenye mkongo huo. Aidha, Serikali inaongeza kiwango cha internet band width kinachotumiwa na taasisi 312 za Serikali, taasisi za utafiti na elimu ya juu kutoka 2.1G kwenda 20G. Hii itapunguza gharama za internet kwa taasisi hizo pamoja na nyingine zitakazounganishwa.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuhimiza mashirika mengine ya simu kujiunga na mpango wa M-Mama kwani umekuwa msaada kwa wajawazito wengi?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mfumo wa M-mama unatekelezwa na kusimamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Vodacom, USAID, Vodafone Foundation, Pathfinder International na Touch Foundation. Mfumo huu unalenga kusaidia upatikanaji wa usafiri wa dharura kwa mama mjamzito, mama aliyejifungua na mtoto mchanga kote nchini.

Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya mfumo kwa haraka na kwa kuwafikia walengwa wengi zaidi, kuna haja ya wadau mbalimbali kuongeza nguvu kwa kushirikiana katika utekelezaji wakiwemo watoa huduma wengine wa mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kuwaalika mashirika binafsi wakiwemo watoa huduma wengine wa mawasiliano pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo wajitokeze kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mfumo wa M-mama hapa nchini.
MHE. TASKA R. MBOGO, aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Mkongo wa Mawasiliano katika eneo la Sikonge hadi Inyonga?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na uendelezaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kuwa ni muhimili wa mawasiliano hapa nchini. Katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuanzia Tabora – Sikonge – Inyonga – Majimoto – Kizi wenye urefu wa Kilomita 369.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hadi sasa Serikali kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imesaini mkataba na Mkandarasi kwa ajili ya kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika maeneo hayo. Hatua za utekelezaji zimeanza ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2024.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika Kata za Karambi, Mubunda, Ngenge na Rutoro katika Wilaya ya Muleba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) K.n.y. WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Disemba, 2021 Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ilifanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Karambi, Mubunda, Ngenge na Rutoro.

Mheshimiwa Spika, Kufuatia tathmini hiyo, kata tajwa zilibainika kuwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na hivyo zimejumuishwa katika zabuni inayotarajiwa kutangazwa kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 kukamilika, ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu ya mawasiliano katika Kata za Idete, Kiyowela, Maduma, Idunda, Makungu na Ihowanza?

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inatekeleza miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata za Idunda na Ihowanza, Wilayani Mufindi ambapo ujenzi wa minara unaendelea na utakamilika ifikapo Julai, 2022. Mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali itafikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Idete na Maduma. Aidha, Kata za Kiyowela na Makungu zitafanyiwa tathmini ya kiufundi kubaini changamoto halisi iliyopo ili kutatuliwa.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -

Je, lini Kata za Bwakila Juu, Singisa pamoja na Mkulazi, Morogoro Vijijini zitapatiwa mawasiliano ya uhakika?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ilitoa ruzuku kwa watoa huduma za mawasiliano ya simu kwa ajili ya ujenzi wa minara mitatu katika Kata ya Mkulazi katika awamu tofauti. Vodacom ilijenga mnara katika Kijiji cha Mkulazi, Halotel - Kijiji cha Chanyumbu na TTCL - Kijiji cha Usungura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kwa upande wa Kata ya Bwakila Juu, UCSAF iliingia makubaliano na TTCL kwa ajili ya kupeleka huduma katika kata husika na utekelezaji unaendelea. Kwa upande wa Kata ya Singisa Kampuni ya Airtel itajenga minara mitatu kwa ajili ya kuhudumia Vijiji vya Nyamigadu ‘A’, Nyamigadu ‘B’, Lumba Juu, Lumba Chini, Ntala, Singisa na Kitengu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itafanya tathmini ya hali ya mawasiliano ya simu katika maeneo husika baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa miradi inayoendelea hivi sasa na kuchukua hatua stahiki endapo kutatokea na maeneo yatakayokuwa hayana mawasiliano ya kuridhisha.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza tatizo la mtandao wa simu kwenye baadhi ya maeneo katika Jimbo la Tabora Mjini?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imejenga minara ya mawasiliano ya simu saba katika Jimbo la Tabora Mjini. Minara hiyo ilijengwa na Vodacom na Halotel katika Kata za Itetemia, Kabila, Kalunde, Ndevelwa, Tumbi na Uyui kupitia awamu mbalimbali za miradi iliyotekelezwa kati ya 2017 na 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Ifucha na Kiloleni zitajengewa minara na Kampuni ya Honora (Tigo). Kwa upande wa Kata ya Kakola, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeingia mkataba na TTCL kwa ajili ya kujenga mnara katika kata hiyo. Utekelezaji wa mradi huu ni wa miezi 24 kuanzia tarehe 13 Mei, 2023, mkataba uliposainiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa miradi hii, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itafanya tathmini ya hali ya mawasiliano katika Jimbo la Tabora Mjini ili kubaini mahitaji halisi ya mawasiliano ya simu na kuchukua hatua stahiki kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kukomesha wizi wa mtandaoni?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imechukua hatua kadhaa kwa ajili ya kuweka mazingira salama kwa wananchi hususan kwenye mitandao. Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya Makosa ya Mitandao na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki kwa lengo la kutambua miamala inayofanyika kimtandao lakini pia kutambua kisheria makosa yanayofanyika kwenye mitandao ili kuweza kuchukua hatua stahiki yanapobainika makosa hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kujenga mazingira salama ya kisheria, pia Serikali imetunga Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022 ambayo lengo kuu ni kuweka utaratibu wa kuhakikisha wakusanya taarifa wote wanafuata misingi ya kulinda taarifa za mwananchi. Aidha, Serikali ilianzisha Kitengo cha Uhalifu wa Mitandao Nchini chini ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa makosa ya mitandao, ikiwemo wizi wa aina yoyote kwenye mtandao na kuandaa majalada ya kufungulia mashtaka kwa kusaidiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua nyingine, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wa simu za mkononi imeanzisha mfumo kupitia namba ‘15040’ ya kupokea na kuzifungia namba ambazo zimeripotiwa na kuthibitika kutuma ujumbe au kupiga simu za utapeli. Baada ya kuthibitisha namba hizo kufanya vitendo hivyo, namba husika hufungiwa, kitambulisho cha NIDA kilichotumiwa kusajili namba husika kufungiwa kusajili na kifaa kilichotumika (simu) pia kufungiwa ili kisifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kuongeza jitihada za kuelimisha umma namna nzuri ya kutumia TEHAMA ili kuendelea kudhibiti matukio ya utapeli na wizi wa kimtandao kupitia simu za mkononi. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga mnara wa Mawasiliano katika Kata ya Kimaha, Kijiji cha Mwaikisabi –Chemba?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Lujuo Monni, Mbunge wa Chemba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia UCSAF iliijumuisha Kata ya Kimaha katika Mradi wa Kufikisha Huduma ya Mawasiliano ya Simu uliosainiwa tarehe 13 Mei, 2023. Utekelezaji wa mradi huo unaendelea ambapo Mtoa Huduma Halotel anajenga mnara kwa ruzuku ya Serikali ya kiasi cha shilingi 145,000,000 za Kitanzania, kwa lengo la kuhudumia Vijiji vya Mwaikisabe, Chukuruma, Wisuzaje na Mwailanje. Mnara huo tayari umejengwa na kwa sasa mtoa huduma anaendelea na kazi ya kufunga vifaa vya redio. Mnara huu unatarajiwa kuwashwa mwezi Juni, mwaka huu. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya maboresho ya minara iliyojengwa na Halotel Liwale ili iweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, ilifanya tathmini katika Jimbo la Liwale na kubaini uwepo wa changamoto za mawasiliano katika Minara ya Halotel. Minara hiyo inatakiwa kuongezewa teknolojia 3G na 4G ambapo utekelezaji wake utafanyika kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Kampuni ya Halotel ina jumla ya minara nane katika Wilaya ya Liwale, ambayo ina uhitaji wa kuiongezea nguvu kutoka 2G kwenda teknolojia ya 3G na 4G. Kiasi cha ruzuku inayohitajika kuiongezea nguvu minara hiyo, ni takribani shilingi 320,000,000 za Kitanzania. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -

Je, lini Kata za Bwakila Juu, Singisa pamoja na Mkulazi, Morogoro Vijijini zitapatiwa mawasiliano ya uhakika?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ilitoa ruzuku kwa watoa huduma za mawasiliano ya simu kwa ajili ya ujenzi wa minara mitatu katika Kata ya Mkulazi katika awamu tofauti. Vodacom ilijenga mnara katika Kijiji cha Mkulazi, Halotel - Kijiji cha Chanyumbu na TTCL - Kijiji cha Usungura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kwa upande wa Kata ya Bwakila Juu, UCSAF iliingia makubaliano na TTCL kwa ajili ya kupeleka huduma katika kata husika na utekelezaji unaendelea. Kwa upande wa Kata ya Singisa Kampuni ya Airtel itajenga minara mitatu kwa ajili ya kuhudumia Vijiji vya Nyamigadu ‘A’, Nyamigadu ‘B’, Lumba Juu, Lumba Chini, Ntala, Singisa na Kitengu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itafanya tathmini ya hali ya mawasiliano ya simu katika maeneo husika baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa miradi inayoendelea hivi sasa na kuchukua hatua stahiki endapo kutatokea na maeneo yatakayokuwa hayana mawasiliano ya kuridhisha.