Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nape Moses Nnauye (73 total)

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utaratibu wa kuweka ‘X’ kwenye nyumba au shughuli ambazo zinafanywa na wananchi kwenye maeneo ambayo Serikali inataka kuweka miundombinu ni utaratibu ambao sasa umezagaa nchi nzima. Kwa kweli unaathiri sana maendeleo ya wananchi wetu kwa kuwa utaratibu huu unazuia wananchi kuendeleza
maeneo yao na inachukua muda mrefu kwa Serikali kuanza kutekeleza mipango yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa, je, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kuubadilisha utaratibu huu wawe wanapanga mipango yao wakikamilisha ndiyo waende kuzungumza na wananchi kwenye maeneo husika? Mfano mzuri ni kwenye maeneo ya Jimbo langu la Mtama ambako inasemekana utapita mradi wa reli, zimewekwa ‘X’ kwa muda mrefu. Kama Serikali itakubaliana na utaratibu huu wa kubadilisha sasa utaratibu watoe tamko hapa niwaambie wananchi wangu wapige chokaa waendeleze maeneo yao. Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama mtagundua sasa hivi kila barabara inayojengwa tunaweka mawe mita 30 kila upande ili tusisubiri wakati wa kupanua barabara. Watu wajue toka mwanzo kwamba barabara hifadhi yake ni mita
30 kila upande. Tatizo lililojitokeza siku za nyuma hizo alama zilikuwa haziwekwi kwa hiyo watu walikuwa wanavamia hifadhi ya barabara wengine kwa kujua na wengine kwa kutokujua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sasa ni kweli baada ya kupitishwa hii sheria mwaka 2007 tumeamua kuweka alama mita 30 kila upande na yeyote aliye katika eneo hilo tunamwekea ‘X’ ajue kwamba yupo ndani ya hifadhi ya barabara na hivyo anatakiwa aondoke. Sio suala la kufidia,
wale wenye haki ya kufidiwa, wanakuja kufidia wakati kutakuwa na mradi maalum utakaopita mahali hapo na hatimaye fedha zinapopatikana. Hiyo ndiyo dhana ya kuweka alama hizi za mita 30 na tumefanya hivyo nchi nzima.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pamoja na kazi nzuri ambayo imeanza kufanywa ya kusaidia kuongezeka kwa bei ya zao la korosho kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani ambao ni wakulima wazuri wa korosho, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuweka kiwango cha elimu kwa viongozi wanaoongoza Vyama vya Msingi, kwa sababu ni moja ya changamoto kubwa sana ambayo imesababisha migogoro mikubwa kwenye Vyama vya Msingi na inasababisha hasara kubwa kwa wakulima wakorosho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, moja ya changamoto kubwa kwenye biashara ya korosho ni utaratibu wa wanunuzi wa korosho kutengeneza cartel, kutengeneza muungano wa pamoja ambao unakwenda kuathiri bei ya mnada kwenye ununuzi wa korosho. Sasa Serikali inachukua hatua gani kukomesha utaratibu huu? Kwa sababu kwa kweli, kwa namna moja ama nyingine umeathiri sana wakulima wa zao la korosho na bei inaendelea kushuka kila kunapokucha na hata sasa ambapo bei imekwenda vizuri, msimu ujao mpango huu wa cartel ukiachiwa ukaendelea, wakulima wetu wataendelea kupata umaskini na nchi yetu haitasonga mbele.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuungana na Mheshimiwa Nape kwamba zao la korosho ni zao la muhimu sana kwa mikoa inayolima hususan Mikoa ya Lindi na Mtwara. Katika msimu uliopita mikoa sita inayolima korosho, kwa uchache waliweza kuingiza shilingi bilioni 700 katika kipindi kifupi kwa ajili ya kuuza korosho. Yote imetokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ya kuendeleza zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, kiwango cha elimu kwa Watumishi wa Vyama vya Ushirika, ni kitu kikubwa. Kimsingi tunategemea kurekebisha sheria ili kuweza kuongeza kiwango hicho, lakini tunasisitiza vilevile kwamba elimu pekee siyo kigezo, tunahitaji watu waadilifu, lakini zaidi watu ambao wanafahamu taratibu za tasnia ya korosho inavyoendeshwa. Kwa hiyo, tutaleta marekebisho, lakini vilevile tutaangalia vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na namna ya kudhibiti cartel, kwa kutambua kwamba huko nyuma wanunuzi walikuwa wanatumia utaratibu huo wa cartel kuharibu bei ya korosho, kwa sasa tunaendesha minada kwa uwazi zaidi ili isitokee watu wakatengeneza utaratibu na watumishi wa Ushirika, vilevile na wa Vyama vya Ushirika wasio waaminifu ili kujitengenezea utaratibu ambao wanunuzi ni hao hao na hivyo kuweza kuharibu bei.
Kwa hiyo, kwa sasa kuna utaratibu wa kuuza korosho kwa uwazi zaidi, lakini vilevile pale mnunuzi atakaposhinda zabuni ya kununua korosho inatakiwa aweke dhamana ili baadaye asije akaacha kununua ili baei ije ishuke. Kwa hiyo, utaratibu huo unashughulikiwa.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la kutokamilika kwa miradi ya maji kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara linaonekana kuwa sugu na moja ya chanzo chake ni wakandarasi kutokaa site; na mfano mzuri Naibu Waziri anajua ni miradi ya maji ya Jimbo langu, maeneo ya Ingawali, Linoha, Nyangamala, Namangale na maeneo mengine; tatizo kubwa ni kwamba hawa Wakandarasi hawakai site; wanakwenda mnapokwenda kufanya ziara. Msipoenda na wao wanarudi Dar es Salaam, ndiyo maana miradi hii haikamiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni hatua gani mnachukua ambazo zitasaidia hawa wakandarasi wakae site ili miradi ikamilike kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea kwenye Jimbo lake na huo mradi mkubwa niliutembelea na siku nilipokuwepo pale ni kweli mkandarasi alikuwepo. Kama kuna hilo tatizo la mkandarasi kutokukaa kwenye eneo la kazi yake na mkataba tunao na vifungu vya mkataba viko ndani ya mkataba, wasiwasi wangu ni kwamba wale wanaosimamia mkataba hawachukui hatua za kimkataba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge nitawasiliana nawe ili tumpigie Mkurugenzi simu tumwulize kama hilo linatokea. Nami vifungu navijua kwa sababu nimesimamia mkataba, tumwelekeze kitu cha kufanya.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Mtama ni baya kuliko ilivyo katika Jimbo la Mbulu Vijijini, kwa sababu katika Tarafa tano; Tarafa tatu mawasiliano ya simu ni tabu sana, wakati mwingine inabidi upande juu ya mnazi au juu ya kichuguu ili uweze kuwasiliana. Tulianza kupata matumaini baada ya Kampuni ya Viettel kuanza kusambaza minara, tukadhani hali itarekebishika, lakini inaonekana kama kazi ile kama imesimama hivi.
Sasa ni lini kazi ile itakamilika ili wananchi wangu waweze kufaidi matunda ya kazi nzuri ya mawasiliano ya simu katika Jimbo la Mtama?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, haikubaliki kati ya tarafa tano, tarafa mbili tu ndiyo zipate mawasiliano ya uhakika, hiyo haikubaliki. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutalifuatilia hili, nini hasa kimesababisha ujenzi wa minara katika maeneo hayo kusimama na baada ya hapo tutaangalia namna ya kushughulikia.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri juu ya process ya Miji Midogo na kwa kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya kufungua barabara ya lami kwenda Msumbiji inayopita katikati ya Jimbo la Mtama na ile inayokwenda Tunduru mpaka Songea, Miji ya Kiwalala, Mtama na Nyangao kasi yake ya kukua ni kubwa na hizo sifa ambazo Mheshimiwa Waziri alikuwa akizieleza zote tunazo.
Ni lini Serikali itakamilisha sasa mchakato wa kuitangaza miji hii midogo kuwa mamlaka kamili ambayo inajitegemea, badala ya kutaka tujumlishe yote kwa pamoja kama ambavyo Waziri anaeleza, nadhani twende case by case na kwa wale ambao wamekamilisha vigezo wapewe badala ya kusubiri wote kwa ujumla wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kama tulivyosema pale awali, concern ya Mheshimiwa Nape ni kwamba ikiwezekana twende case by case, naomba nikuhakikishie kwamba tulivyoenda kufanya tathimini ya maeneo yote, maana yake hata tumefika sehemu nyingine kwa ajili ya watu wametu-invite makusudi kwenda kuangalia hiyo Miji Midogo. Tulipofanya hiyo ziara ndiyo maana tukatuma hiyo timu; na bahati nzuri hiyo timu imefanya kazi kubwa sana. Siyo muda mrefu sana, ile kazi ikikamilika sasa na baada ya kujiridhisha na haya mambo ambayo Mheshimiwa Waziri aliyazungumza kwamba suala zima la kuangalia vigezo vya kiuchumi eneo lile, basi tutatangaza maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuvute subira tu, kwa sababu kila jambo lina utaratibu wake na mchakato wake, kwa hiyo, tuvute subira tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo ambalo alizungumza, ni kweli linakua sana, basi tutaangalia jinsi gani tutafanya maeneo yatakayokuwa tayari, basi yatatangazwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri atakumbuka kwamba walipokwenda kuzindua REA III kwa Mkoa wa Iringa, walifanya assumption kwamba ndiyo wamezindua na Mkoa wa Njombe, lakini hii mikoa ni mikoa miwili tofauti, inawezekana TANESCO mnaona kama ni Mkoa mmoja lakini hii ni Mikoa miwili tofauti. Je, ni lini mtakwenda kuzindua REA III kwa Mkoa wa Njombe specific kwa Mkoa wa Njombe badala ya kuunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Iringa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; vipaumbele vya kusambaza umeme wa REA III katika maeneo mengi, katika vijiji vimefanyiwa ofisini na Watendaji wa TANESCO bila kushirikisha viongozi kwenye maeneo husika na hasa kwa Mkoa wa Lindi hasa katika Jimbo la Mtama. Yapo maeneo mengi ukiangalia vijiji vilivyowekwa, vipaumbele vyake nadhani vimezingatiwa zaidi ofisini bila kujali hali halisi ya mazingira. Je, ni lini hawa Watendaji wa TANESCO pamoja na Wakandarasi watakaa na viongozi kwenye maeneo husika ili wakubaliane vipaumbele wapi tuanzie na wapi tuishie wakati wa awamu mbalimbali zinazoendelea za kusambaza umeme kwenye maeneo yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Nape kwa jinsi ambavyo anatupa ushirikiano katika Jimbo lake la Mtama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la uzinduzi, tumefanya uzinduzi ambao kwa kweli katika miaka ya nyuma tulikuwa hatufanyi na mantiki kubwa ilikuwa ni kuwatambulisha Wakandarasi pia kuwajulisha viongozi pamoja na Waheshimiwa Wabunge ili waweze kushiriki ipasavyo kwenye zoezi zima. Kwa hiyo, nataka tu kusema kwamba, katika Jimbo la Mtama hata katika Mkoa wa Njombe, katika Mkoa wa Njombe kimsingi tulifanya uzinduzi Kesamgagao lakini kama ikibidi tutarudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kazi yetu ni kuwafikishia umeme wananchi wa Njombe. Kwa hiyo, niseme tu kwamba wala halina shida, tutapanga siku na tutarejea ingawa Mkandarasi ameshafika site. Kwa hiyo, niwape faraja wananchi wa Njombe, tutaendelea kulifanyika kazi, watatualika tutakwenda pia kuwazindulia rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na vipaumbele niseme tu, kazi ambayo Mkandarasi anatakiwa kuifanya na hili nitoe kama tangazo kwa Wakandarasi pamoja na TANESCO wanaowasimamia, utaratibu wa kwanza kwa Mkandarasi yeyote kabla hajaanza kazi anatakiwa kwanza awashirikishe Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo husika na Viongozi wa maeneo hayo na kutofanya hivyo tutachukua hatua kali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya hivyo kwa sababu tunataka kuepuka vijiji muhimu kurukwa, maeneo ya vipaumbele kurukwa, pamoja na taasisi za umma. Kwa hiyo, nitoe angalizo, nakushukuru Mheshimiwa Nape lakini nachukua nafasi hii kuwatangazia rasmi kuwatangazia rasmi Wakandarasi pamoja na TANESCO kuhakikisha wanawashirikisha Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Viongozi wa maeneo husika ili kuhakikisha kwamba hakuna maeneo, vijiji wala taasisi za umma zitakazorukwa. Hilo ni angalizo nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Nape wakati wa uzinduzi wa Lindi ni kweli hakuwepo lakini vijiji vyako vya Rondo Mheshimiwa vitapata umeme, Nyangamara watapata umeme, Chiwerewere watapata umeme, kwa hiyo bado Mheshimiwa Nape wananchi wake wa Mtama awape uhakika huo.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ufufuaji wa viwanda vya korosho kwa Ukanda wa Kusini ni ukombozi mkubwa kama ufufuaji huo utafanyika kama ulivyokusudiwa. Kama lilivyoulizwa swali la msingi, ufufuaji huo hasa kwa wale wawekezaji waliopewa viwanda hivi, tunadhani wanafanya chini ya kiwango.
Mheshimiwa Spika, mfano mzuri ni kiwanda cha Kubangua Korosho cha Mtama. Sisi Wanamtama haturidhiki na mwekezaji alivyowekeza na kukiendesha kile kiwanda. Tunaamini anafanya chini ya kiwango ambacho alitakiwa kufanya. Sasa Serikali iko tayari kwenda kufanya ukaguzi kujiridhisha kama uwekezaji ule ndiyo waliokubaliana naye?
Kama siyo, wako tayari kuvunja na kumpa mtu mwingine ili tufaidike na uwekezaji wa viwanda vya korosho na hasa kiwanda chetu cha korosho cha Mtama?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge na Wadau wote wa korosho katika mikoa 11 inayolima korosho. Korosho imewekwa katika mazao ya kipaumbele matano ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu; mimi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tunafuatilia. Navijua viwanda vyote kwenye ncha ya vidole, najua tasnia nzima ya korosho; nimezunguka dunia nzima natafuta masoko ya korosho. Siyo viwanda tu, najua tatizo la industry. Wataalam wangu wako site kwenye viwanda vyote 10 tunafuatilia. Nina mawasiliano ya mtu mmoja mmoja.
Mheshimiwa Spika, kwa mamlaka niliyonayo, watu wa Treasury Registrar, mtuletee majibu nije nikae na watu wa Newala na watu wa Lindi, nije niwaeleze kwa nini kiwanda hiki kinakwama? Suala siyo kiwanda kuanza, suala ni kiwanda kuwa endelevu. Kuna mambo zaidi katika tasnia ya korosho na ndiyo tunayahangaikia.
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya mambo ya msingi nimezungumza. Nimezungumza mambo ya branding humu, tunapigana kutengeneza brand ya korosho ya Tanzania. Brand ya korosho huwezi kuitengeneza mpaka uzalishe wewe mwenyewe. Tunafanya kazi, lakini kwa Newala na Lindi nimewaagiza wataalam.
Mheshimiwa Spika, kwanza mwekezaji aliyechukua Kiwanda cha Mtama nimweleze Mheshimiwa Mbunge, yuko tayari kukiachia yeye mwenyewe. Kwa hiyo, nawaagiza wataalam wangu waje Jumanne watueleze. Yule mwekezaji, yeye si anataka kukiachia, tumemwambia aje akiachie, tusaidiane na Mheshimiwa Mbunge ili tutafute mwekezaji mwingine.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, utaratibu wa kuanzisha miradi ya scheme ya umwagiliaji na kutoimaliza sasa unaonekana kama ni utaratibu wa kawaida, ukiacha kwamba uzalishaji hautafanyika lakini pana pesa ile ambayo ndiyo imeanzisha hiyo miradi, hiyo pesa itapotea. Mfano mzuri ni miradi ya umwagiliaji katika Jimbo la Mtama, katika Vijiji vya Utimbe, Kiwalala na Mbalala ambayo imeanzishwa karibu miaka mitano mpaka saba iliyopita, imeishia katikati na haijamalizwa. Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha kuimalizia miradi hii ili tufaidike na miradi hii? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ipo miradi mingi ambayo ilikuwa imeanzishwa na haikukamilika. Huko nyuma miradi hii katika Program ya Maendeleo katika Sekta ya Kilimo, sehemu kubwa ya miradi ile ilikuwa inaendelezwa na wafadhili kwa fedha za nje. Sasa tumeona kwamba ni lazima sisi kama Serikali tuwekeze fedha za ndani na kusimamia ili miradi iweze kukamilika na ndio maana tumeunda Tume ya Umwagiliaji ili iweze kusimamia miradi ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuunda Tume hii, mwaka huu tumeamua kwanza kuipitia miradi yote na kuainisha mahitaji yake. Kwa hiyo, Serikali itatenga fedha kulingana na yale mahitaji yatakayokuwa yameainishwa ili miradi hii ambayo tumeipanga iweze kutekelezwa.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri anakiri kwamba hili tatizo la watendaji wasiokuwa na sifa ni moja ya tatizo kubwa sana kwenye zao la korosho na Serikali inatambua kwamba msimu wa korosho uliomalizika tumepata upotevu mkubwa sana wa pesa.
Sasa Serikali haioni wakati umefika wa kubadilisha sifa zinazotumika za kuwapata hawa watendaji? Nasema hivyo kwa sababu kiwango hicho kidogo cha elimu ni moja ya sababu ya wao kuzungukwa na watendaji wa mabenki na watendaji wengine wanaohusika katika mfumo na matokeo yake pesa nyingi sana zinapotea na wakulima wanapata hasara. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema, kwamba mara nyingine elimu na uwezo mdogo wa watendaji wa Vyama vya Ushirika inaweza ikawa kikwazo kikubwa cha wao kuweza kufanya kazi kwa ufanisi, hasa pale kiwango kikubwa cha fedha kikiwa kinahusika. Naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria haisemi kwamba ni lazima mtu awe na elimu ya kidato cha nne, inasema kuanzia. Kwa hiyo maana yake, hata kama kunakuwa na waombaji wa nafasi zile wana elimu zaidi bado wanaweza kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize kitu kimoja, kuwa na elimu kubwa mara nyingine siyo kigezo cha uadilifu na tabia njema. Leo hii tunafahamu Vyama vyetu vya Msingi ni vyama vya wakulima, vinashughulikia maslahi ya watu wa kawaida, ukija kupeleka wataalam, wanaweza wakawa wataalam wana elimu nzuri lakini vilevile wakawa wataalam wa kupiga. Kwa sababu hata huko Serikali Kuu na maeneo mengine unasikia kwamba mara nyingine wapigaji ni watu ambao elimu zao ni kubwa. Kwa hiyo, tutaendelea kuangalia ni namna gani ya kuboresha mazingira ya utendaji wa Vyama vya Ushirika, lakini kwa sasa sheria haimkatazi mtu mwenye degree au masters kuwa Mtendaji wa Chama cha Msingi. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa chanzo kikubwa cha migogoro kati ya wananchi na wawekezaji wanaoenda kuwekeza kwenye sekta hii ya uchimbaji wa madini ni utaratibu unaotumika wa kumalizana na wawekezaji kitaifa na kutowashirikisha vizuri wale wa Wilayani na pale kijijini penyewe ambapo utafiti au uchimbaji unakwenda kufanyika na mfano mzuri ni katika Jimbo langu la Mtama, Kata ya Namangale kuna utafiti unafanyika wa graphite na Kampuni ya Nachi Resources lakini mgogoro uliopo ni kwamba wananchi wa eneo lile hawaelewi kinachoendelea na hivyo kubaki na malalamiko mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itabadilisha huu utaratibu na kuwasaidia wananchi wangu wapate uelewa wa kinachoendelea ili waone ushiriki wao utakuwaje?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Nape tumekuwa tukishirikiana sana katika hili na wananchi wa Mtama nadhani ni mashahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii nisema utaratibu unaotumika ni kwamba mwekezaji yeyote anayepata leseni, hatua ya kwanza akishapata leseni ni kuonana na uongozi wa Halmashauri au uongozi unaohusika wa wilaya na kama hilo halifanyiki ni uvunjivu wa sheria na sisi tutalisimamia.
Lakini pia nichukue nafasi hii kusema kwamba tutapita katika maeneo ya kero, tumeshapanga utaratibu, kuanzia tarehe 02 Agosti, 2017 tunashughulikia matatizo hayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Nape hata kwake tutafika. Ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwenye Kijiji cha Mnara, Kata ya Mnara, Tarafa ya Rondo Jimboni Mtama kwa kupindi cha miaka mitatu sasa imepita tumekamilisha jengo zuri la kisasa la Mahakama, lakini kwa kipindi chote hicho Serikali imekuwa kwa namna moja ama nyingine pengine inapiga chenga kufungua na kuruhusu jengo hili litumike.
Mheshimiwa Spika, Mbunge aliyepita alisaidia ujenzi, ameomba Serikali tulifungue, lakini mpaka leo Serikali haijafungua. Sasa ni lini Mheshimiwa Waziri Serikali itaruhusu jengo hili litumike ili haki itendeke kwa watu wangu hawa kupata huduma karibu na maeneo yao.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana yeye pamoja na wananchi wa Jimbo lake kwa kupata jengo la Mahakama zuri, lakini mimi mwenyewe nasikitika kwamba mpaka sasa halijaweza kuzinduliwa.
Naomba nitoe ahadi kwamba tutakapotoka tu hapa, tena nataka niwe mbele yake, nitampigia Mtendaji Mkuu wa Mahakama, tuhakikishe kweli hili jengo linaanza kutumika. Kwa sababu huko ndiko kusogeza huduma za Mahakama kwa wananchi. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, Serikali imekiri kwamba baadhi ya sheria tulizonazo zinadumaza maendeleo ya wanawake na hasa watoto wa kike na kwa kuwa, tatizo la watoto wa kike wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kukatisha masomo yao kutokana na mifumo ambayo mingine imepaliliwa na Sheria hizi mbovu tulizonazo.
Je, Serikali inachukua hatua gani kuwanusuru hawa watoto ambao sasa wanaendelea kupoteza fursa ya kusoma na kufanikiwa katika masomo yao kutokana na sheria hizi mbovu tulizonazo?

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi ni kwamba tatizo hili la watoto wa kike kutomaliza masomo yao au kukatisha masomo yao kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara ni kubwa sana na hasa katika Jimbo la Mtama. Moja ya sababu kubwa ni hizi sheria tulizonazo ambazo zinapalilia matendo kama hayo ya watoto hawa kupewa mimba na kukatishwa masomo yao na wengine kuolewa wakiwa bado wanaendelea na masomo na mengine wazazi wanasukuma watoto wao wafanye vibaya ili wafeli waende wakaolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni kwamba Serikali inachukua hatua gani kuwanusuru hawa watoto ambao kwa kweli wanaendelea kupoteza fursa katika maisha yao?
NAIBU WAZIRI AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba arudie swali lake kwa ufupi. Swali hasa analotaka nijibu.

NAIBU WAZIRI AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Vizuri!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Nape kwa swali lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yetu kama Serikali ni kwamba, kama nchi tulipitisha Sheria hapa Bungeni mwaka jana tu, 2016 na tulifanya mabadiliko kwenye Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, kwenye kile kifungu cha 60(A).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kifungu hicho tuliamua kupandisha umri wa mtoto kuolewa mpaka kufikia miaka 21, lakini pia kuzuia mtoto yeyote yule ambaye anasoma primary school ama secondary school asiolewe kwa mujibu wa sheria na tukaweka adhabu pale. Kwa maana hiyo, suala hili kama Serikali tunalichukulia kwa ukali kama lilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa suala hili hauwezi kupigiwa mfano kwa sababu, ni jambo linalohusu maisha ya kizazi cha nchi yetu huko tunakoelekea. Kwa hiyo, rai yangu ni kwamba wazazi wote washiriki kikamilifu katika kuwalea watoto wetu na kuwasomesha ipasavyo kwa mujibu wa sheria; na wa watambue kwamba ni kosa kisheria kumwoza binti ambaye anasoma ama ni kosa kisheria kumpa mimba binti ambaye anasoma. Yule atakayefanya hivyo, awe mzazi, awe ndugu, awe mlezi, atachukuliwa hatua za kisheria kama itathibitika kwamba imekuwa hivyo. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa tatizo la nyumba hizi za kukaa wahudumu wa afya hasa maeneo ya vijijini hasa Mikoa ya Lindi na Mtwara na Jimbo la Mtama ni kubwa sana. Pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Taasisi ya Benjamin Mkapa ya ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kulishughulikia tatizo hili ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa maeneo ambayo yana changamoto kubwa sana ya afya. Mheshimiwa Nape ni shahidi kwamba katika jambo ambalo amekuwa akilipigia kelele sana ni hili la sekta ya afya na nimpongeze sana katika utekelezaji wa Ilani last week alienda kukabidhi ile ambulace, nadhani wananchi wa Mtama wana-appreciate kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili alilotoa ni wazo zuri kwa sababu sasa hivi tunatumia fedha za Local Government Development Grants kwa ajili ya kuhakikisha miradi mingi hasa viporo inakamilika hasa katika ujenzi wa majengo mbalimbali ya afya na elimu. Ndiyo maana katika mpango wa bajeti ya mwaka huu tumetenga karibuni shilingi bilioni 251.18, lengo kubwa ni kuwezesha upatikanaji wa makazi kwa wataalamu wetu.
Kwa hiyo, jambo la kuanzisha mfuko, nadhani kwa sasa tutumie huu mfumo tuliokuwa nao lakini wazo ni zuri tutalifanyia kazi kama Serikali kuona nini tufanye, lengo kubwa tuweze kutatua matatizo ya afya kwa Watanzania wote kwa ujumla wetu.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kutatua tatizo la umeme kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara, baada ya mateso makubwa tuliyoyapata katika kipindi hiki cha miezi miwili/mitatu cha kukosa umeme kwa zaidi ya siku nne. Serikali inaambatanishaje juhudi hizo na ukarabati wa miundombinu hasa nguzo, kwenye yale maeneo ambayo nguzo zake ni mbovu. Kwa hiyo, hata wakikamilisha uzalishaji bado usambazaji wa umeme kwenye haya maeneo ambayo nguzo zake ni mbovu bado itakwama.
Sasa Serikali imejipangaje kuambatanisha juhudi hizo mnazoendelea nazo na ukarabati wa nguzo kwenye yale maeneo ambayo nguzo zimechoka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Lakini niwape pole sana Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kipindi ambacho Mheshimiwa Nape amezungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli zipo juhudi za makusudi ambazo sasa tunachukua kama Serikali, tuliporekebisha umeme katika Mkoa wa Mtwara tarehe 16 mwezi uliopita tuliacha feeder mbili ambazo matengenezo yake yanaendelea. Wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa sasa wanapata umeme kutoka kwenye sub station ya Maumbika. Sasa sub station ya Maumbika marekebisho ya engine yake yanakamilika kesho. Kwa hiyo wananchi wa Mtwara, Lindi na maeneo mengine yategemee kupata umeme kuanzia kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nguzo kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amezungumza, tumeagiza nguzo mpya kutoka hapa nchini, tumeacha sasa kuleta nguzo kutoka nje ambazo zilikuwa zinakaa kwa muda mrefu mipakani. Nguzo zitakuwa mpya, kwa hiyo, niwahakikishie wananchi watapata nguzo na ukarabati utaendelea vizuri. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali chini ya Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayofanya ya usambazaji wa umeme vijijini, hasa hii REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, kwa kuwa gharama za kuunganisha umeme wakati mradi unaendelea katika eneo ni Sh.27,000 na mradi ukishapita ni Sh.177,000; na kwa kuwa idadi nzuri na kubwa ya watumiaji wa umeme ni biashara nzuri kwa TANESCO, kwa nini sasa bei hii isiwe moja hiyohiyo ya 27,000 badala ya bei kupanda baada ya mradi kwisha? Kama haiwezekani, basi REA hawa waendelee na kazi ya usambazaji wa nguzo na miundombinu na TANESCO wafanye kazi moja tu ya kupeleka umeme na kukusanya kodi yao baada ya kupeleka umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, Kaka yangu Nape Nnauye. Ni kweli bei ya kusambaza umeme ya vijijini ni Sh.27,000 kipindi cha mradi na hii ni hatua ya Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwamba, imegharamia gharama zote za uunganishwaji kwa umeme huu na kwamba mwananchi yeye gharama yake ni analipia VAT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wazo alilolisema kwamba, mara baada ya mradi kukamilika na miundombinu kukabidhiwa TANESCO ni kweli wananchi wanaunganishwa kwa bei ya Sh.177,000, lakini hata hivyo niseme hata hii bei pia, Sh.177,000 nayo ina mchango wa Serikali kwa sababu, mijini kwa bei hii wanaunganishwa kwa Sh.321,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wazo alilosema linapokelewa na litafanyiwa kazi na ni la msingi kwa sababu, Wizara yetu na Shirika letu la TANESCO na wadau wengine wa nishati kwamba, tunauza bidhaa ya umeme. Kwa hiyo, ni vema zaidi kwamba, tunapoiuza tupate wateja wengi, ili tupate mapato na kuendesha shughuli mbalimbali na uwekezaji mpya wa maeneo ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, nimelipokea na Serikali itaona utaratibu gani wa kufanya ili iweze kurahisisha. Ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji katika Mikoa ya Lindi na Mtwara bado ni mbaya sana na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji ambaye sasa ni Waziri wa Maji alipotembelea Mikoa ya Lindi na Mtwara alikagua baadhi ya miradi ambayo inaendelea katika Jimbo la Mtama, Mradi wa Maji wa Nyangamara na pengine hakufika lakini Mradi wa Maji wa Namangale na alituhaidi kwamba certificates za miradi hiyo zikifika Wizarani mara moja pesa zitalipwa, mpaka sasa huu ni mwezi wa pili au wa tatu certificates hizo zimefika Wizarani na hazijalipwa.
Je, ni lini Serikali italipa pesa hizi za hawa wakandarasi ili miradi hii ipate kukamilika wananchi wangu wapate maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha na Mipango jana ametupatia shilingi bilioni 12. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba hizo certificates kama zimeshaletwa wiki ijao tutahakikisha tumezilipa ili mkandarasi aendelee kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza
kwa niaba ya wananchi wangu wa Mtama na Mkoa wa Lindi kwa wakulima wa ufuta. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ongezeko la uzalishaji wa zao la alizeti kasi yake inafanana sana na
ongezeko la uzalishaji wa ufuta katika Mkoa wa Lindi na hasa katika Jimbo la Mtama na kwa kuwa ubora wa mafuta ya ufuta ni mzuri kuliko yale ya alizeti. Sasa Serikali ina mpango gani wa kusaidia uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo vya kukamua mafuta ya ufuta kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wangu wa Mtama na Mkoa wa Lindi ambao wanalima ufuta na kuinua uchumi wao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jibu langu, napenda niseme mafuta yote ya alizeti na yale ya ufuta yote ni mazuri.
Kwa hiyo, wananchi waende kuyatumia, ilimradi yazalishwe Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda vidogo vidogo, namshauri Mheshimiwa Mbunge awasiliane na SIDO.
Nina Meneja mzuri wa SIDO, Lindi na kwa sababu hili liko kwenye mamlaka yangu, mradi wa SME Guarantee Scheme unahusisha na Mkoa wa Lindi.
Kwa hiyo, Mkurugenzi wangu anayeshughulikia mpango huu, ahakikishe na Lindi inakwenda kule kwa sababu Tanzania tunaagiza mafuta mengi ya kula. Tunaconsume tani 400,000 kwa mwaka, lakini karibu 70%
tunaagiza nje. Mafuta ya kula ni commodity ambayo inachukua pesa za kigeni ikiwa ni namba mbili baada ya
mafuta jamii ya petroli.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, unalisaidia Taifa lako, tukamue mafuta hapa, tujitosheleze, tuokoe pesa za kigeni.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na mjomba wangu Profesa Kabudi na timu yake kwenye Wizara ya Katiba na Sheria, itakumbukwa mwaka mmoja na zaidi uliopita niliuliza hapa na kuiomba Wizara itusaidie tufungue jengo la Mahakama ambalo tumeshalijenga, tumelikamilisha ni zuri na la kisasa, nikaahidiwa hapa kwamba Serikali itasaidia kukamilisha utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana, sasa ni mwaka na utaratibu haujakamilika. Sasa kama jambo hili limeshindikana Serikali ituambie ili tubadilishe matumizi tufanye shughuli nyingine kwenye lile jengo la Mahakama ambalo nia yetu ilikuwa ni kusogeza huduma za kimahakama kwa watu wetu.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Nape swali hilo nilichukue nilifanyie kazi, kwa sababu amesema ni mwaka mmoja na nusu na mimi leo ni mwezi wangu wa Kumi wa Uwaziri. Naomba anisaidie tuonane nilifuatilie ili tuone jengo hilo linatumika kwa Mahakama.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na kutambua na kupongeza kazi nzuri ambayo inafanywa katika kuboresha viwanja mbalimbali vya ndege hapa nchini, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa nilizonazo ni kwamba uwanja wa ndege wa Lindi umeshafanyiwa upembuzi na usanifu. Sasa, Serikali iko tayari kuanza kutenga fedha za ndani badala ya kutegemea fedha za nje kwa ajili ya kuanza ukarabati wa uwanja huu wa ndege ikizingatiwa uwanja ulivyokaa kimkakati, lakini historia ya uwanja huu na mahitaji ya uwanja huu kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba avute subira wakati wa bajeti ataona kwamba tumeweka fedha za kutosha kupitia mapato ya ndani. Ile asilimia ya fedha ambazo tumetenga kupitia mapato ya ndani ni kubwa. Kwa hiyo, ilikuwa sio vema nizungumze hapa lakini labda kama baadaye tunaweza tukaonana nimwoneshe, lakini wakati wa bajeti tutaonesha namna ambavyo Serikali imedhamiria kuboresha viwanja vyake kupitia mapato ya ndani. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nipongeze juhudi na kasi kubwa inayofanywa na Serikali ya kufufua viwanda vile ambavyo vilikuwa vimekufa, lakini pia kuvutia uwekezaji wa viwanda vipya. Sasa swali langu, ufufuaji wa viwanda vya korosho katika Ukanda wa Kusini hasa katika Jimbo la Mtama na maeneo mengine umefanyika lakini kuna kusuasua kwa ukamilishaji wa baadhi ya maeneo ili ubanguaji wa korosho uweze kufanyika kwa kiwango kikubwa na hasa hapa nazungumzia Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Nachingwea, kwa kuwa Mwekezaji ambaye amefufua Kiwanda cha Mtama, ndiye ambaye amepewa kazi pia ya kufufua Kiwanda cha Nachingwea. Ni lini sasa kazi hii itakamilika ili wakulima wa korosho wapate mahali pa kuuza korosho yao na thamani ya zao la korosho ipate kuongezeka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU - K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kwamba inafufua viwanda vyote na ndiyo maana Wizara inafanya kazi ya karibu sana na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na TIRDO, lengo lake ni kuhakikisha kwamba viwanda hivi vinafufuliwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa upande wa Mikoa ya Kusini kule Mtwara, Lindi na kwingineko wanakolima korosho, tulikuja na model ambayo tumeiita BOOT ambayo Build on Operate na Transfer na hii ndiyo ambayo tuliitumia hata pale Mtama kwa kumtumia huyu Mwekezaji wa kutoka China ambaye anaitwa Sang Shin industry alifanya hivyo Mtama na ndivyo hivyo tutafanya katika maeneo mengine hasa Nachingwea kuhakikisha kwamba viwanda hivi vya korosho vinaweza kufufuliwa.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa katika jitihada za kupunguza mzigo mkubwa unaobebwa na Hospitali ya Lindi, Serikali iliingia makubaliano na hospitali za mission kwa mfano Hospitali ya Nyangao pale Jimbo la Mtama kwa ajili ya kusaidiana nao katika kutoa huduma za afya ili tupunguze mzigo mkubwa katika Hospitali ya Lindi. Lakini utekelezaji wa makubaliano hasa upelekaji wa fedha na watumishi kwa ajili ya kufanya kazi katika hospitali hizi ambazo mmekubaliana nazo hautelekezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali sasa itaanza kupeleka pesa kama walivyokubaliana pamoja na watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nape, naomba tulichukue hilo kwa sababu kuna hizi ahadi najua kwamba katika hospitali mbalimbali zinatekelezeka na nikijua kwamba kweli kuna shida kubwa na ndiyo maana kutokana na kesi ile ya kwako tumeona kwamba pale Kituo cha Nyangarapa ambao kituo cha afya kwenda kukiboresha zaidi kama tulivyokubali pale mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tutaenda kukiboresha kituo hiki lakini suala zima la commitment za hizi taasisi ambazo za dini au vituo mbalimbali vya dini au vituo mbalimbali binafsi ambao Serikali imeingilia nazo, kama kuna scenario ambayo kwa Wakilindi iko tofauti kidogo upelekaji wa fedha hauko vizuri tunakwenda kuufuatilia kuangalia jinsi gani tuuboreshe wananchi waweze kupata huduma vizuri.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na kwamba kwa kweli, Naibu Waziri nadhani hili swali la Mbunge wa Tarime amelinanihii. Pamoja na dinosaur Mikoa ya Lindi na Mtwara ina utajiri mkubwa wa utamaduni ambao unaweza kutumika kama sehemu ya utalii na kufaidisha watu wa Kusini. Je, ni lini Serikali au Wizara itaamua kuanza kuwekeza kenye utamaduni wa Kusini ili utumike kama utalii wa watu wa Kusini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli Kusini ni sehemu ya maeneo yaliyoko nchi nzima, Tanzania nzima ambayo yana utajiri mkubwa wa kihistoria hasa Historia ya Utamaduni wa Mtanzania katika makabila yote tuliyonayo na kwamba, eneo hilo pia, ni kivutio cha kutosha kabisa chenye sifa ya kuweza kuwa maeneo ya shughuli za utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nirudie tu kama ambavyo nimejibu swali kama hili mara nyingi nikiwa nimesimama hapa, mbele ya Bunge lako Tukufu. Ni kwamba, Halmashauri zote, ikiwemo ile ambayo Mheshimiwa Mbunge ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani waharakishe kutekeleza Agizo la Serikali la kuorodhesha maeneo yote ambayo yako kwenye maeneo yao, Halmashauri zao, ambayo yana sifa hizo tunazozizungumzia, ili tulete Wizarani yaweze kupitiwa, yachambuliwe, ili kuweza kuwekwa katika viwango na kuweza kuona namna gani mahitaji yake yakoje, ili tuweze kuendelea katika kuvitangaza na badaye kuwavutia watalii kwa ajili ya shughuli za utalii.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nipongeze kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii, inaonekana wanakwenda kwa kasi nzuri, lakini miradi mingi ya mabwawa na miradi ya umwagiliaji mingi inaanzishwa lakini haikamiki, aidha, kutokana na upungufu wa fedha au kuwa imekuwa designed vibaya. Mfano mzuri ni miradi ya vijiji vya Utimbe, Runyu na Longa katika Jimbo la Mtama.
Sasa Serikali haioni kwamba ni vizuri wakaacha kubuni miradi mipya wa-concentrate na kumalizia miradi hiii ambayo kwa miaka mingi hawajaimaliza na pesa zimezama kwenye miradi hii?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba changamoto hiyo tumeiona katika Wizara yangu kwamba miradi mingi ilibuniwa lakini haikukamilika na haikukamilika kwa sababu miradi mingi imekuwa inatekelezwa na hela za wafadhili ambao wao wenyewe walikuwa wanachagua miradi, lakini pia wanaweka ceiling ya fedha na wanalazimisha kwamba mradi huo lazima utekelezwe kulingana na design kwamba ile hela iliyotolewa haiwezi kufanya mradi sasa ukawa umekamilika na kuweza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri na Kamati yangu imeliona hilo, tumelijadili na kuanzia sasa tunataka kuweka utaratibu maalum kwamba kama kuna fedha haitoshi, hakuna haja ya kutekeleza huo mradi. Lazima tuweke fedha ambazo tukishauanzisha mradi, tuchimbe bwawa, tuweke na scheme ili wananchi waendelee kufaidi matunda ya Serikali yao. Hilo Mheshimiwa Mbunge tumeshaliona na tunalifanyia kazi.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru ka kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa msimu uliopita soko la mbaazi lilisababisha kuanguka kwa bei ya mbaazi kutoka shilingi 2,000 kwenda mpaka shilingi 150, Serikali ilihaidi hapa Bungeni kwamba itahakikisha inahangaika kupata soko la kuaminika la zao hili. Sasa ni msimu wa kilimo hicho, Serikali imefikia wapi kupata soko hili na kama hali bado haileweki tuwashauri wananchi wetu waachane na mbaazi badala yake wajikite kwenye mazao mengine ambayo yana soko la uhakika?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni kweli kabisa katika msimu huu ulioisha kulikuwa na hali isiyopendeza katika soko la mbaazi, hiyo ni kutokana na kwamba wadau ambao tulikuwa tunawategemea sana katika biashara hiyo ilikuwa ni wenzetu kutoka India. Niseme tu kwamba mbaazi ni chakula kizuri, mbaazi ni chakula ambacho kina protini na hata sisi wenyewe tunaweza tukala siyo kuwategemea tu watu wa maeneo mengine. Kama tunaavyosema kwamba biashara ni ushindani na kila watu wanajitahidi kuhakikisha kwamba wanakidhi soko lao la ndani, upande wa Tanzania tunaendelea kutafuta soko wakati huo tunaendelea kusisitiza kwamba hata wenyewe tupende kutumia mbaazi.
Mheshimiwa Spika, nimepita hapa katika masoko yetu kwa mfano soko la hapa Dodoma, nilipofuatilia nilikuta kwamba mbaazi zinauzwa mpaka shilingi 1,800 kwa kilo. Soko la pale Dar es Salaam kwenye supermarket mbaazi inauzwa mpaka shilingi 2,400 kwa kilo. Kwa hiyo, tusitegemee tu soko kutoka nje hata ndani ya nchi bado kuna watu ambao wananweza kula mbaazi na mimi mwenyewe ni mtumiaji wa mbaazi, vilevile tunategemea kwamba hata kupitia shule zetu tutaweza pia kuhamasisha na kuweza kupeleka chakula cha aina hiyo wakati masoko mengine ya nje yakiendelea kutafutwa.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea Kilwa ni suala la Ilani ya Uchanguzi wa Chama cha Mapinduzi lakini pia ni ukombozi mkubwa kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara na mapinduzi kwa kilimo chetu. Mwaka jana Serikali ilitoa ahadi kwamba mchakato unaendelea vizuri, nataka kujua mchakato huo umefikia wapi kwa sasa.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wakati najibu swali la msingi kama Mheshimiwa Nape hakunisikiliza vizuri; ni kwamba nilisema tayari kuna wawekezaji ambao wameshaonesha nia wa Makampuni ya HELM na FERROSTAAL wa Ujerumani, kwa hiyo mchakato unaendelea katika mazingira hayo.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Serikali kupitia Bodi ya Korosho waliingia mkataba na baadhi ya wakulima kuzalisha mbegu za korosho na miche hii hawa wakulima wakaisambaza lakini mpaka sasa tunavyoongea wakulima hawa hawajalipwa na hii ni baada ya Bodi ya Korosho kuchukua kazi iliyokuwa inafanywa na Mfuko wa Pembejeo ambao walikuwa wakizalisha watu wanalipwa kwa wakati.
Sasa ni lini Serikali itaisimamia Bodi ya Korosho kuhakikisha inawalipa hawa wazalishaji wa mbegu za korosho waliofanya kazi ya kizalendo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli Serikali tunaelewa kwamba zao la korosho ni mojawapo ya zao la kimkakati na ni kweli kabisa kwamba kuna wakulima hawa ambao wanaidai Bodi ya Korosho. Hata hivyo Serikali tumejipanga kwamba pesa hizi zinafuatiliwa na wakati wa bajeti Mheshimiwa Nape ataelewa majibu haya ya uhakika na ya kweli tunaweza kumpatia, ahsante. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika kuziimarisha tawala za mikoa ni pamoja na kuziruhusu na kuzipa uwezo wa kufanya maamuzi yake zenyewe, ikiwemo kuwapangia vituo watumishi wapya ambao wanaajiriwa. Hata hivyo, lakini hivi karibuni Serikali mmebadilisha utaratibu, wanaoajiriwa hasa walimu mnawapangia vituo kutoka makao makuu, wenyewe, badala ya kupangiwa kule kwenye halmashauri ambako ndiko wanakojua mahitaji ya Walimu katika maeneo yao. Kwa nini Serikali wamepora madaraka ya Tawala za Mikoa, hasa Halmashauri, kupanga vituo vya watumishi? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliokuwa unatumika zamani ulikuwa ni kwamba Serikali ikishaajiri basi lile rundo la waajiriwa au idadi ya waajiriwa inapelekwa katika halmashauri. Hapo inakuwa ni kazi ya halmashauri kuwapangia mahali pa kwenda kufanya kazi au vituo vya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopatikana kutokana na utaratibu huo ambao wenzetu walipata shida sana kuudhibiti ni vi-memo, vikiwemo vi-memo vya Wabunge. Akishapelekwa katika halmashauri fulani ki-memo kinafuata bwana huyo ni wa kwangu kwa hiyo msimpangie mbali na mji. Kwa hiyo unakuta Walimu wengi walipangiwa katika maeneo ya Makao Makuu ya Wilaya, katika maeneo ya miji hasa wanawake, sitaki kueleza sababu kwa sababu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Nnauye kwamba baada ya kupata changamoto hiyo sasa Serikali imeamua kwamba tunapowapeleka; kwa sababu Maafisa Elimu wanakuwa wameleta yale mahitaji ya kila shule katika halmashauri yake; tunajua kwamba Yaleyale Puna wana Walimu saba, tunajua kwamba Pemba Mnazi wana Walimu watatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunajua kwamba kutoka makao makuu tupeleke Walimu watano Pemba Mnazi na tupeleke Walimu wawili Yaleyale Puna ili kusudi shule za pembezoni nazo zipate Walimu badala ya kupeleka vi-memo kwa Afisa Elimu. Ki-memo cha Mbunge kina nguvu sana kwa Afisa Elimu lakini ukileta ki–memo kwangu kinadunda tu, wala hakiwezi kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Nape Nnauye wala asipate wasiwasi, tunafanya hivyo kwa ajili ya kuangalia kwamba kunakuwa na usawa mkubwa kwa wale ambao wana uhitaji mkubwa wa kupewa Walimu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mwaka jana Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea Jimbo la Mtama alikuta tunajenga Kituo cha Polisi pale Mtama na akaahidi kwamba tukimaliza ujenzi wa kile kituo atatupatia gari kwa ajili ya kusaidia huduma za usalama katika lile eneo. Ni lini sasa ahadi hii ya Waziri Mkuu itatekelezwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Nape kwa ufuatiliaji wake wa masuala ya jimboni kwake. Niseme tu kwamba ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni maelekezo na sisi tutafanyia kazi maelekezo hayo.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itakubaliana nami kwamba uanzishwaji wa Vituo vya Utafiti wa Mazao ya Kilimo, vilianzishwa vingi kwa kanda na lengo lilikuwa zuri, lakini utendaji wa vituo hivyo umeanza kusuasua hivi karibuni kwa sababu ya kutokupata fedha za kutosha za kusimamia shughuli zake. Mfano mzuri ni Kituo cha Utafiti wa Mazao ya Korosho pale Naliendele. Ni lini Serikali sasa itapeleka fedha za kutosha ili vituo hivi vianze kufanya kazi kama vilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa mkwe wangu Nape Nnauye, Mbunge wa Jimbo la Mtama, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Vituo vingi vya Utafiti vya Wizara yetu ya Kilimo, vinasuasua lakini kama tunavyoelewa kwamba vituo hivi na sisi kama Wizara tumewaambia pia wajiongeze zaidi hata wao, si tu kutegemea pesa ya Serikali kwa sababu vituo vyetu vya utafiti vinaweza pia vikaandika proposal kwa ajili ya kuweza kupata fedha pia kutoka kwa wafadhili mbalimbali ili viweze kufanya kazi yake vile inavyotakiwa. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kuboresha mazingira ya kilimo ni pamoja na upatikanaji wa mbegu bora au miche bora ya zao husika, na kwa kuwa wazalishaji wa miche ya korosho imechukua muda mrefu sana kulipwa pesa zao na wengi wao walikuwa wamekopa fedha kwenye vyombo vya fedha. Je, Serikali pamoja na kuwalipa malipo yao ya stahiki, wako tayari sasa kuwalipa fidia ya ziada kutokana na hasara iliyotokana na mikopo waliyochukua kwenye vyombo vya fedha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anachoouliza, tumeshafanya uhakiki wa miche milioni kumi na tatu mpaka sasa hivi. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu, pesa ya kuwalipa wananchi hawa ipo tayari, lakini suala la fidia halipo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Katika sekta iliyoathirika sana wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti, suala zima la vyeti fake ni sekta ya afya. Jimboni Mtama baadhi ya zahanati tumelazimika kuzifunga kabisa kwa sababu watu wameondolewa.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa nini Serikali isichukue hatua za dharura kwenye haya maeneo ambayo zahanati zimefungwa badala ya kusubiri process hii ya kuajiri watumishi wapya wa afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo nilifanikiwa kupita na kuona kazi nzuri ambayo imefanyika katika suala zima la ujenzi wa vituo vya afya ni pamoja na Jimbo lake la Mtama, kwanza naomba nimpongeze.
Mheshimiwa Spika, tukiwa hapa ndani bungeni Mheshimiwa Mkuchika alitoa taarifa kwamba kama yuko Mbunge yeyote, wa eneo lolote ambalo tumelazimika kufunga zahanati au kituo cha afya kwa sababu ya ukosefu wa watoa huduma aandike barua ampelekee ili tatizo hili lisiweze kutokea.
Mheshimiwa Spika, naomba kama Mheshimiwa Mbunge hakuwepo siku hiyo atumie fursa na bahati nzuri yeye yuko jirani sana na Mheshimiwa Mkuchika ili hicho anachokisema kisiweze kutokea.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.
Pamoja na kazi nzuri ambayo inafanywa na Wizara ya Nishati katika kusambaza umeme vijijini, lakini zipo taarifana hali halisi ndivyo ilivyo kwamba REA Awamu ya Tatu inasuasua sana kwa madai kwamba wakandarasi hawajalipwa pesa zao. Sasa ni lini Serikali itawalipa pesa zao ili wakandarasi hawa waongeze kasi ya kusambaza umeme kama ambavyo Serikali imeahidi hapa ndani ya Bunge?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na napenda nimthibitishie Mheshimiwa Nape kwamba wiki mbili zilizopita Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Benki Kuu ilifungua Letter of Credit kwa makampuni zaidi ya 18 kiasi cha shilingi bilioni 260. Naomba nilithibitishie Bunge lako tukufu kwamba kuanzia sasa miradi ile itashika kasi kwa sababu tatizo la ufunguaji wa Letter of Credit limekwisha na Benki Kuu imefanya kazi yake na ninapenda niishukuru sana. Ahsante. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza pamoja na maelezo mazuri ya Serikali itakumbukwa kwamba siku nne tano zilizopita Mheshimiwa Waziri Mkuu alikiri kwamba zoezi la uhakiki limegubikwa na vitendo vya rushwa. Sasa ni hatua gani zimechukuliwa na Serikali kuwachukulia hatua wale ambao wameshiriki zoezi hili na kujihusisha na vitendo vya rushwa, ambayo kwa kweli kwa sehemu kubwa ndiyo imevuruga zoezi hili na kulikosesha maana na matokeo yake wakulima wameathirika sana.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kabla ya kujibu hili swali, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kwa kuniteua katika nafasi hii na kuniamini kwamba naweza kufanya kusaidia katika maendeleo.

Pia nichukue nafasi kuwashukuru viongozi wengine wote wanaomsaidia Mheshimiwa Rais lakini pia, wewe Mwenyewe Mheshimiwa Spika kwa malezi mazuri, ambayo ndiyo yamenifanya nifikie katika nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nimjibu Mheshimiwa Nape Nnauye kama ifuatavyo, ni kweli kabisa kwamba wakati tunaendelea na hili zoezi la uhakiki katika maeneo mengi kumekuwa na maneno katika baadhi ya maeneo kwamba baadhi ya viongozi na baadhi ya wafanyakazi ambao wako kwenye Kamati za uhakiki wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa. Sisi kama Wizara tuliposikia tu hatukusubiri tupate ushahidi, tuliposikia baadhi ya wafanyakazi wanashiriki kwenye rushwa tumechukua hatua na naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwenye upande wa Wizara na bodi zake.

Mheshimiwa Spika, wafanyakazi wanne tumeshawachukulia hatua tumeshawasimamisha na hivi sasa tunakusudia kuwapeleka Mahakamani kutokana na kudhihirika kwamba wamejihusisha na vitendo vya rushwa. Lakini pia kuna baadhi ya wafanyakazi ambao wako TAMISEMI ambao tunawasiliana ndani ya Serikali ili nao waweze kuchukuliwa hatua zinazokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kusema kwamba Serikali haitavumilia wafanyakazi wote ambao watakuwa wanajihusisha na vitendo vya rushwa na pale ambapo Waheshimiwa Wabunge mnazo takwimu au mmepata taarifa kwamba mfanyakazi wetu yeyote anajihusisha na rushwa tunaomba mtupatie hizo taarifa na kama Serikali tutachukua hatua mara moja. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa reli ya Mtwara ambao ulipangwa kupita kwenye baadhi ya maeneo ya Jimbo la Mtama, Kata ya Nyangao, Mtama, Kiwalala, Mnolela kuelekea Mtwara maeneo ambayo reli imepangwa kupita wananchi walizuiwa kufanya uendelezaji mpaka pale watakapofidiwa; na kwa kuwa, sasa huu ni mwaka karibu wa nne na hatuoni dalili za ujenzi wa reli hiyo, kwa nini wananchi hawa sasa wasiruhusiwe kuendeleza maeneo yao mpaka pale Serikali itakapokuwa tayari kuyachukua kwa ajili ya ujenzi wa reli na ikafanya tathmini upya na kufidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Nape atakubaliana nami kwamba, ujenzi wa reli hii ni kitu muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi na ni muhimu kwa ajili ya wananchi wenyewe. Kwa hiyo, nataka nimwombe tu avute subira kwa sababu, tunavyotambua kwamba, kuna mradi utapita hapa, ni vema sasa kwamba, wananchi wakaona wasije wakaweka vitu ambavyo vitakuwa na gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuchumi kama tutawaruhusu wafanye vitu vya maendeleo halafu baadaye tukabomoa kwa ajili ya kuweka miundombinu muhimu kama hii ya reli, tutakuwa tunabomoa ile dhana nzima ya ukuaji wa uchumi. Kwa hiyo, niwaombe tu wananchi wasiweke vitu vya thamani kubwa, reli ni kwa ajili yao, reli ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, tushirikiane tu, lakini Serikali inaendelea kusukuma jambo hili ili tuweze kupata hii reli ambayo itatupa manufaa makubwa katika nchi yetu.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Halmashauri ya Lindi Vijijini na hasa Jimbo la Mtama tulipanga mwaka huu wa fedha kuchimba visima virefu 25 na fedha zipo, tumeomba kibali toka kibali toka mwezi wa Nane mwaka jana, tukaandika barua kukumbusha mwezi wa Kumi na Mbili lakini mpaka sasa hatujibiwi chochote, tatizo la vibali hivi ni nini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mbunge, Mheshimiwa Nape, nimefanya ziara katika Jimbo la Mtama, ni mmoja kati ya Waheshimiwa Wabunge wanaofanya kazi nzuri sana katika majimbo yao. Sisi kama Wizara ya Maji hatuko tayari kukwamisha jitihada anazozifanya. Nimwombe tu baada ya Bunge tuweze kukutana na Katibu Mkuu ili tuweze kupata vibali hivyo ili wananchi wake waweze kupata huduma ya msingi.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya msingi, kwenye swali la Kivukoni, mimi ni moja ya product ya Kivukoni. Kwa kuwa historia ya Chuo hiki kilikuwa ni Chuo cha ku-train Viongozi na kutokana na changamoto tunazoziona katika utekelezaji wa majukumu yao hasa Viongozi kwenye Local Government, wilayani, Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa.

Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kukirudishia chuo hiki kazi yake ya msingi ya kufundisha viongozi skills za namna ya kutekeleza majukumu yao kwenye maeneo yao na nakubaliana na uamuzi wa Serikali wa kutokukipandisha hadhi badala yake tukibadilishie sasa majukumu kitoke kwenye ku-train social sciences kiende
kwenye ku-train viongozi wetu kwa sababu kwa kweli changamoto ya utekelezaji wa majukumu yao kwenye maeneo yao imekuwa ni kubwa sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NASERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA - K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba nimjibu Mheshimiwa Nape Nnauye swali lake la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kwamba Chuo hiki kimeanzishwa kwa majukumu aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge na yataendelea kufanyika hivyo, sasa kama kuna upungufu umeonekana, hilo ni jambo la kulichukua na kwenda kulifanyia kazi, lakini tunaamini kwamba kazi ya msingi iliyoanzishwa kwayo inaendelea kufanyika. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na kupongeza ziara nzuri ya Mheshimiwa Rais Magufuli kwa baadhi ya Mikoa ya Kusini ambayo inalima korosho, Serikali itakubaliana na mimi kama ilivyotokea kwenye kahawa mabadiliko ya mfumo wa ununuzi wa korosho yameathiri mapato ya Halmashauri ambazo zilikuwa zinategemea ushuru wa korosho. Halmashauri nyingi kwa asilimia 70 mpaka 80 zilikuwa zinategemea mapato haya. Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya madhara yatakayojitokeza baada ya maagizo ya Mheshimiwa Rais kwamba pesa hizi zisidaiwe na hivyo kuangalia namna ya kufidia ili hizi Halmashauri zisiathirike zaidi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nape, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la msingi anasema kwamba, je, Serikali ipo tayari kufanya tathmini ya athari zilizopatikana kwa kushuka mapato ya Serikali ya Halmashauri? Kwanza nichukue nafasi hii kusema kwamba Serikali haijabadili mfumo wa ununuzi wa korosho hapa nchi. Kama mnavyofahamu tuliingia kwenye mfumo huo baada ya wakulima wenyewe kukataa kuuza katika mnada uliokuwa halali kwa wanunuzi wale kutokana na bei ambayo haikuwavutia zaidi ya minada mitatu minne. Kama Serikali tusingeweza kuangalia hali ile iendelee ndiyo maana tuli- intervene ili kuhakikisha wakulima hawa wanapata bei nzuri wanayostahili. Wakati ule tunaingia tulikuwa tunafahamu bei ni ndogo lakini tulienda kuwalipa wakulima bei ya Sh.3,300 ambayo ilikuwa huwezi kuipata mahali popote duniani zaidi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali lake la kama tupo tayari kufanya tathmini, napenda kusema kwamba tupo tayari na tumeshaanza kufanya tathmini hiyo lakini mapato yale ya Halmashauri ni ya Serikali na iliyolipa ni Serikali, kwa hiyo, Serikali haiwezi kumlipa Serikali mwenzie. Msimu ujao tutajipanga vizuri na mfumo utakuwa kama ulivyokuwa, mapato ya Halmashauri watayapata kupitia mfumo utakaokuwepo.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa katika jibu la msingi la Serikali kwenye suala la pembejeo tunakiri kwamba moja ya sababu ya kupanda na kuongezeka kwa gharama ni kwa sababu pembejeo zinaagizwa kutoka nje. Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, katika Mpango wa Serikali, kulikuwa na ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea Kilwa Mkoani Lindi. Serikali imefikia wapi kukamilisha ahadi hii ya Ilani ya Uchaguzi ili kusaidia upatikanaji wa pembejeo?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naomba nijibu kidogo swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliweka ahadi ya kuhakikisha kwamba tunajenga kiwanda cha kuzalisha mbolea pale Kilwa. Naomba nimhakikishie tu kwamba hatua za ujenzi wa kiwanda hicho tuko katika hali nzuri sana. Mpaka sasa hivi wiki mbili zilizopita wataalam kutoka Pakistan, Ujerumani na Morocco wamekuja kwa ajili ya kuangalia na kufanya tathmini ya mwisho na kufanya mazungumzo na Serikali ili kuhakikisha kwamba kiwanda hiki cha mbolea kinajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba baada ya muda mfupi, kiwanda hiki kitaanza kujengwa sambamba na maeneo mengine ya viwanda ambavyo vitajengwa ili kuweza kupunguza gharama za pembejeo hapa nchini. Nashukuru.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami naulize swali dogo la nyongeza. Katika jitihada za kuboresha miundombinu ya elimu Mkoani Lindi, kwa misimu miwili, mitatu iliyopita tulikubaliana kukata fedha kutokana na malipo ya korosho ya shilingi 30/= kwa kila kilo ili kukarabati miundombinu na kujenga miundombinu mipya. Sasa iko miundombninu ambayo ilianza kujengwa kwa sababu ya hali ambayo sote tunaijua, miundombinu hiyo sasa imesimama kwa sababu hiyo fedha haikupatikana.

Je, Serikali iko tayari kusaidia kumalizia miundombinu hii katika Mkoa wa Lindi hasa upande wa elimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ni nia ya Serikali kuendelea kukamilisha miundombinu ya elimu na hasa ile ambayo imeanzishwa na wananchi na ndiyo maana tumepeleka fedha za kiutawala mwezi Januari, tumepeleka fedha za maboma karibu shilingi bilioni 29.9. Kwenye bajeti hii ambayo imepitishwa, zaidi ya shilingi bilioni 90 inaenda kusimamia miundombinu ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipokee maombi ya Mheshimiwa Mbunge, tutazingatia maoni yake. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na majibu ya Serikali, kuna mkanganyiko mkubwa na mlolongo mrefu kwa watu hawa kupata haki zao.

Sasa kwa kuwa Benki Kuu ndiyo guarantor wa hizi benki, kwa nini Serikali isimalizane na hawa wateja kwa niaba ya hii benki halafu Serikali sasa ibaki ikishughulika na benki hii wakati wananchi wakiwa wanaendelea na shughuli zao, hasa ikizingatiwa kuwa ziko taarifa kwamba, wamiliki wa benki hii wametushitaki, wameishitaki Serikali kutokana na hatua walizochukua?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, benki inapofilisika, benki inaponyang’anywa leseni yake ya kufanya kazi, hatua zote za ulipaji wa wateja wa beki hiyo au taasisi hiyo ya kifedha, imetajwa katika sheria ya mabeki na taasisi za fedha kifungu cha 39(2) na (3), ambako kuna maeneo mawili.

Mheshimiwa Spika, kwa wale ambao wana amana zilizo chini ya 1,500,000 hulipwa fedha zao zote, kwa wale ambao amana zao ni zaidi ya hiyo, hulipwa kwa kutumia sasa sheria ya ufilisi baada ya kujiridhisha na madeni na mali halisi ya benki hiyo au taasisi ya kifedha kama ilivyoelezwa.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba niliambia Bunge lako Tukufu kwamba, siyo kwamba wamiliki wa benki ndiyo walioishitaki Serikali, hapana, waliostopisha mchakato huu ni Central Bank ya Cyprus, ambayo wao wanaona wana mandate ya kuweza kulipa wateja wote wa benki hii, wakisahau kwamba kulingana na sheria ya uanzishwaji wa mabenki, wanaotakiwa kulipa ni kule ambako benki hiyo ilikuwa na makao makuu, na makao makuu ya benki hii ya FBME yalikuwa Dar es Salaam lakini shughuli zake nyingi zilikuwa zinafanyika nchini Cyprus.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, mwezi wa nne tarehe 5 mwaka 2019, Serikali mbili zimekutana nchini Cyprus na tayari makubaliano yamefikiwa ya jinsi gani ya kuhakikisha wateja wote wa iliyokuwa benki ya FBME Tanzania na FBME Cyprus wanapata haki zao bila kupoteza chochote katika mchakato huu.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtama, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kuamua kutupa watu wa Mtama Halmashauri yetu. Sasa je, Serikali iko tayari kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kujenga barabara za Mji wa Mtama na kuzikarabati zile ambazo zimeharibiwa na mvua ili Mji wa Mtama sasa uwe na hadhi ya kubeba Halmashauri hii ambayo Mheshimiwa Rais ametupa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Nape na Halmashauri zingine zote kwamba Serikali ipo tayari kutenga fedha za kutosha kujenga barabara katika Makao Makuu ya Halmashauri mpya na zile za zamani, pia na kujenga majengo muhimu katika maeneo hayo ili huduma ziweze kutolewa kwa uhakika zaidi. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Pamoja na shukurani za wananchi wa Jimbo la Mtama kwa miradi kadhaa inayoendelea ya maji katika Jimbo hilo baada ya Mji wa Mtama kupewa hadhi sasa ya kuwa Halmashauri mahitaji ya maji yameongezeka sana katika Mji huu. Je, Serikali sasa iko tayari kwenye bajeti ya mwaka huu kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu na upatikanaji wa maji katika Mji huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, Kaka yangu Mheshimiwa Nape.

Mheshimiwa Nape anafanya kazi kubwa na nzuri na alishakuja katika Ofisi yetu ya Wizara ya Maji, tukakaa mimi, yeye, Waziri pamoja na Katibu Mkuu. Hakuna haja ya kusubiri mpaka bajeti fedha tumekwishatuma 1.3 billion kwa ajili ya utekelezaji. Mheshimiwa Mbunge asimamie mradi ule uanze haraka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtama niishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutupa bilioni 1.5 kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya. Pamoja na shukrani hizi mwaka 2017 Waziri Mkuu alifanya ziara jimboni Mtama katika Kata ya Mtama na majengo ambayo ina idadi ya watu wengi sana na mpaka sasa tuna zahanati alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya. Sasa je, Serikali haioni umefika wakati wa ahadi hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu itekelezwe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Nape Nnauye na wananchi wake wa Mtama kwa kazi kubwa waliyoifanya ya uimarishaji wa kituo cha Afya cha Mnazi Mmoja na hali kadhalika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo tumewapelekea fedha. Lakini tukijua wazi kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa ahadi sehemu hii ni jukumu letu la Serikali kwamba tutafanya kila liwezekanalo maeneo yote ambayo viongozi wetu wa kitaifa wametoa ahadi tutaweza kuyashughulikia. Sambamba na hilo hata kule mkoani Kigoma kwa Peter Serukamba kuna scenario kama hiyo zote tunaenda kufanyia kazi kwa kadri tutakavyokuwa tumejipanga, hakuna shaka.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hoja ya msingi hapa ni kwamba tunayo changamoto siyo tu katika Jimbo hili, lakini katika Majimbo mengine pia ya namna ya kusaidia hasa watoto wa kike kuwapunguzia suluba wanayoipata ya kwenda shuleni na kurudi, ndiyo maana hawa wananchi wa Msalala wakawekeza fedha kwa ajili ya kujenga mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu la Serikali ni kwamba mnasaidia kwenye shule ambazo zinachukua wanafunzi wa kitaifa. Hawa ambao wako wengi kwa nini Serikali haioni iko haja sasa ya kuwekeza hata kwenye hizi shule ambazo zinachukua katika eneo dogo lakini kwa lengo la kuwasaidia mabinti zetu wapate mahali pa kukaa na kupata masomo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; uwekaji wa miundombinu katika hizi shule na hasa suala la umeme kwa maeneo mengi kwa miradi ya REA imekuwa kama ni hisani ya Wakandarasi, kwa sababu wanaambiwa wakipata nafasi waweke. Maeneo mengi ushahidi unaonesha kwamba hawafanyi mpaka ambapo panakuwa na msukumo maalum. Serikali haioni umefika wakati sasa suala la kuweka umeme kwenye shule liwe ni suala la lazima kwa Wakandarasi waliopewa miradi ya REA na iwe ni kazi ambayo inafanyika bure badala ya kuwa sasa hivi inafanyika kama hisani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba nia njema ya Serikali kama tungekuwa na uwezo mkubwa tungepeleka mabweni ama mabwalo katika shule zetu hizi za kutwa. Tumesema hizi shule za kutwa zipo karibu na makazi ya wananchi na tumeelekeza pia Waheshimiwa Wabunge, wananchi wengine na wazazi waendelee kuchukua tahadhari juu ya kulinda watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza na hizi shule za mabweni za Kitaifa kwa sababu wanafunzi wanatoka maeneo ya mbali sana katika makazi yao huku majumbani kwao kwenda katika hizi shule. Naomba tupokee ari ya Mheshimiwa Mbunge na maoni yake; tukipata uwezo wa kutosha tutafanya kazi na tungependa pia watoto wetu waendelee kusoma vizuri. Ni kweli kwamba kumbukumbu zinaonesha watoto wengi wa kike hawamalizi shule kwa sababu wanapewa mimba wakati wa kutoka nyumbani kwenda shuleni na wakati wa kurudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anazungumzia habari ya umeme kupelekwa katika shule zetu za sekondari za Umma. Ni kweli kwamba tumepata malalamiko mengi katika maeneo mbalimbali, nami nimefanya ziara maeneo hayo. Walimu wetu, Wenyeviti, wazazi, viongozi, Madiwani na Wabunge wanalalamika kwamba kunakuwa na bill kubwa pia ya kuunganisha umeme katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumesikia mara kadhaa Mheshimiwa Waziri wa Nishati akitoa maelekezo. Tupokee wazo hili pia, tuongee na viongozi wenzetu wa Wizara ya Nishati ili ikiwezekana umeme upelekwe kwenye maeneo ya Umma tena iwe ni bure kwa sababu hii ni huduma ya Serikali. Shule za Serikali, vijana wa Kitanzania, Serikali ni ya kwetu, ipo namna ya kulifanya jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tungependa unapopeleka umeme katika maeneo ya shule za jirani, hata vijana ambao wanakaa maeneo ya jirani, hata wakati wa usiku wanaweza wakajisomea kujiandaa na mitihani yao na kufanya discussion mbalimbali hata kutoka shule mbalimbali za jirani katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makazi katika kushughulikia makazi, tunayo changamoto ya waajiriwa wapya, watumishi wapya na hasa wale wa kipato cha chini kumudu makazi bora hasa katika mazingira ambayo wamiliki wengi wa nyumba za kupangisha wanataka kodi ya miezi sita mpaka mwaka mzima jambo ambalo watumishi hawa hawawezi kumudu na hivyo kusababisha mazingira ya wao sasa kujihusisha na rushwa ili wapate fedha za kulipia kodi. Sasa Serikali haioni umefika wakati wa kuleta sheria itakayoharamisha kitendo cha wamiliki wa nyumba kudai kodi ya zaidi ya mwezi mmoja? (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye, Mbunge wa Jimbo la Mtama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli jambo hili linaleta kero sana na kama Wizara tumeshalitolea maelekezo mara kadhaa kwa mujibu wa sera, Waziri wa Ardhi na Makazi ana uwezo wa kutoa maelekezo fulani fulani au kuweka kanuni zitakazoweza kutawala masuala haya yote yanayohusiana na makazi. Mimi nimeshawahi kutangaza na kupiga marufuku utaratibu huu kwa sababu sio wa kiungwana wala sio wa kisheria. Ni kweli kwamba watu wanalazimisha wapangaji kulipa miezi 12, si vijana wanaoanza kazi tu, hata wanafunzi wanaokaa kwenye hostel wanalazimishwa kulipa miezi 12, hili jambo halikubaliki hata kidogo. Serikali haitaingilia gharama ya upangishaji, upangishaji ni makubaliano ingawa iko katika utaratibu wa kuweka regulatory authority ambayo itaangalia na viwango vyenyewe vya upangishaji ili kulinda haki za wenye nyumba na haki za wapangaji vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili la kulazimisha mpangaji alipe miezi 12 au sita halikubaliki! Ila ni kweli kwamba ushauri wa ndugu Nnauye tunauchukulia maanani wakati tunasubiri Real Estate Regulatory Authority na sheria kuja Bungeni, tutaweka Kanuni kidogo itakayowabana hawa wasiosikia. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu Katiba inatambua uwepo wa Serikali za Mitaa na uwepo wa Serikali Kuu. Serikali za Mitaa kwa juu zinaanzia kwenye ngazi ya Halmashauri. Je, Serikali haioni kwamba, umefika wakati sasa wa kuunganisha uchaguzi wa Madiwani na uchaguzi wa vijiji, vitongoji na mitaa ili Serikali za Mitaa wafanye uchaguzi pamoja na Serikali Kuu kwa maana ya Bunge na Rais, uchaguzi wao uwe pamoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, hili jambo ni jambo la kisheria. Tunayo Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura Namba 287 na Sura Namba 288, lakini pia tuna uchaguzi wa Serikali Kuu, Wabunge na Madiwani na Mheshimiwa Rais; tupokee wazo hili tulifanyie kazi, ni jambo la mchakato, kama itawezekana kufanya hivyo ni jambo jema tutalifanyia kazi, lakini hili ni jambo la kisheria tunalipokea na kulifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu zetu. Ahsante.
MHE. NAPE M. MNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kama ilivyo kahawa, korosho ni zao la mkakati na bila shaka ndio zao linaloongoza kuingiza kipato kwa nchi yetu. Sasa hali toka msimu umeanza hali ya upatikanaji wa magunia ni mbaya sana, hili jambo limezungumzwa na kuzungumzwa. Hivi asubuhi ya leo imefikia mahali kwa sababu ya kukosekana kwa magunia viongozi wa vyama vya msingi wameanza kutishiwa maisha, wengine wanafungiwa ofisini, wakulima wanapewa magunia mawili, gunia moja. Serikali inatoa tamko gani ku-rescue hali hii kwa sababu, ikiachiwa ikaendelea hivi zao hili tunaliua tena?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kamba, kuna changamoto ya magunia na Serikali tumeiona na yeye anafahamu wenye jukumu la kuagiza magunia walikuwa ni vyama vya ushirika na ndio hao ambao waliagiza magunia. Baadaye tulivyoona kwamba, inasuasua Serikali tumeingilia kati, tumeshaongea na yule msambazaji, mpaka sasa magunia zaidi ya 2,400,000 yako bandarini. Na mpaka hivi tunavyozungumza ameshatoa zaidi ya magunia laki saba, jana amepakia zaidi ya magunia 258,000 kupeleka huko mikoa ya Kusini. Na leo hivi ninavyozungumza tunaendelea kupakia magunia 255,000 na usiwe na wasiwasi na tumeshamuelekeza maalum apeleke zaidi ya magunia 30,000 pale Lindi Mwambao.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mtama lina shule za sekondari mbili ambazo zinapokea vijana waKidato cha Tano na Kidato cha Sita. Shule ya Sekondari Nyangao na Shule ya Sekondari Mahiwa. Mwaka jana Naibu Waziri wa Elimu alipotembelea Jimboni Mtama alipoenda kuiona Shule ya Sekondari Mahiwa alikuta majengo yake yamechoka na yamekuwa ya muda mrefu na akaahidi kwamba Serikali itatoa fedha kusaidia ukarabati wa majengo hayo.

Je, Serikali iko tayari kutekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Jimbo la Mtama?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba nilitembelea Jimbo la Mheshimiwa Nape na ni kweli kwamba alinisihi nimsaidie shule yake iweze kupata miundombinu ili iweze kuwa bora na hatimaye kuwa shule ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita. Naomba niendelee kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imepanga kupeleka fedha katika Awamu ya Nane ya Mpango waEP4R, kwa hiyo, ahadi yetu iko palepale na itatekelezwa.(Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na kutambua nia njema ya Serikali katika kusitisha kuongeza maeneno mengine mapya ya utawala hasa kwa maeneo ya mikoa na wilaya na halmshauri ambazo pengine gharama ya kuanzisha ni kubwa lakini kule chini kwenye kata na vijiji na mitaa hali ni mbaya sana na gharama yake sio kubwa kiasi hicho, badala kuyabeba yote pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali kwa nini isifikirie hasa tunapokwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwenye mitaa, kwenye kata na vijiji kwenda kuongeza maeneo ya kiutawala kwa sababu hali halisi inakataana na huo msimamo wa Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema ni kweli kuwa tunaangalia gharama ni kubwa lakini naomba nikubaliane na maoni ya Wabunge walio wengi humu kwamba tuangalie kama nilivyomjibu Mheshimiwa Massare tuangalie kama kuna maeneo ambayo hatutakuwa na gharama kubwa tuyazingatie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu lengo la Serikali nikusogeza huduma karibu na wananchi na kuna maeneo kwa kweli wanatembea km 40, 30 kwenda kuomba barua ya mtendaji wa kata kitendo ambacho sio sawa sawa. Kwa hiyo, tulipokee hili kwa niaba ya Bunge hili Tukufu na kwa niaba ya Serikali tumelifanyia kazi kwa pamoja na tutashirikisha Wabunge wa maeneo husika namna kuweza kulifanya hili kutekelezeka. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niiulize wali dogo la nyongeza. Kwanza nimpongeze sana mdogo wangu Ulega inaonekana shuleni alifanya vizuri kwenye somo la biolojia, na ni mfano mzuri nimefuata ule ushari wake ndiyo maana kitambi changu kimepungua. Serikali inajitahidi kupambana na magonjwa mbalimbali nchini hivi karibuni kuna ugonjwa wa homa ya Dengue ambao hali yake sasa ni mbaya na vimeanza kuripotiwa vifo kutokana na jambo hili. (Makofi)

Sasa Serikali inachukua hatua gani kwa kuhakikisha jambo hili linakwisha kwa sababu tukiendelea kulinyamazia vifo vitaendelea kuongezeka watu wanaendelea kumwa na hali ya Jiji la Dar es Salaam kwa sasa ni mbaya?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye Mbunge wa Mtama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa hapa karibuni imeibuka ugonjwa wa Dengue na hasa katika Jiji la Dar es Salam, Serikali inafahamu juu ya tatizo hili na imeanza kuchukua hatua za makusudi.

Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote na watanzania. Moja katika jambo kubwa ililoligundua Serikali ni kuwa gharama kubwa zinazolipwa na watanzania wanaopata matatizo hayo katika sehemu za kutolea huduma za afya. Sasa katika Serikali jitihada inayofanyika hivi sasa ni kuhakikisha matibabu ya Dengue yanakuwepo na yanapatikana kwa bei zilizokuwa nafuu ili kuweza kuwasaidia watanzania. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kutambua jitihada za Serikali katika kuboresha mawasiliano na uchukuzi katika nchi yetu na hasa maboresho yaliyofanyika katika Shirika la Ndege la Tanzania sasa hivi kumeanza kujitokeza tatizo la ucheleweshaji wa ndege. Kila mara unaposafiri ndege inasogezwa, inasogezwa, inasogezwa na hili jambo linakera sana. Chanzo cha tatizo hili ni nini na Serikali mnachukua hatua gani kurekebisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika siku za karibuni kumetokea changamoto ya uchelewaji (cancelation) kwa Shirika letu la Ndege la Tanzania. Tatizo hili limetokana na sababu mbalimbali za kiufundi ambazo zimerekebishwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya kuhitimisha bajeti yetu tulitoa maelekezo Menejimenti na Bodi ya ATCL kwamba kama kutakuwa na cancelation yoyote au delay ya zaidi ya nusu saa tupate taarifa ya maandishi ya sababu zilizobabisha hiyo ndege ichelewe kuondoka kwa zaidi ya nusu saa. Hilo limeshaanza kufanyika na huwa tanapata taarifa.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuwasisitiza ATCL kwamba wateja ndiyo watu wa thamani sana. Kwa hiyo, delay ambazo hazina sababu ya msingi ziepukwe sana.

Mheshimiwa Spika, nikutaarifu wewe na Bunge lako kwamba sasa hivi marekebisho yameshaanza kufanyika. Sasa hivi ATCL wameshaanza kwenda vizuri, delay na cancelation ambazo sio technical hazitokei tena.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Kiwanda cha Dangote, lakini yale magari makubwa ya Dangote yanapita barabara ya kutoka Mtwara kuja Mnazi Mmoja kwenda Mtama - Masasi. Ile barabara hali yake haikutengenezwa kubeba magari makubwa ya kiasi kile kwa hiyo hali yake imekuwa mbovu sana. Kila mara unafanyika ukarabati na barabara inaendelea kuwa mbovu. Sasa Serikali inachukua hatua gani kumaliza tatizo hili la ubovu wa hii barabara kwa kila mara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii imekuwa ikifanyiwa matengenezo lakini Mheshimiwa Nape atakubali kabisa kwamba hii barabara ni ya zamani, hii barabara ina zaidi ya miaka 30 na imekuwa ya muda mrefu na hata ukisoma kibao pale imeandikwa T2 (T Namba 2) na uone hata kwenye usajili wake ni kati ya barabara ambazo ni za zamani sana kwa maana hiyo iko haja sasa ya kufanyia rehabilitation kwa maana ya matengenezo makubwa na wiki iliyopita nilijibu hapa kwamba Serikali tumejipanga kwa ajili ya kuijenga upya barabara hii kutoka Mtwara kuja Mnazi Mmoja na kutoka Mnazi Mmoja kwenda Masasi kwa ufadhili wa World Bank.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Nape vuta subira ule utaratibu wa kawaida wa kifedha na kimanunuzi unaendelea. Tutakwenda kuifumua barabara hii na kuitengeneza kabisa ili iwe mpya kwa hiyo niwahakikishie wananchi wa Mtama, wananchi wa Mtwara, wananchi wa Lindi na Watanzania kwa ujumla kwamba tunakuja kufanya maboresho makubwa ya barabara hii.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kila baada ya miaka 10 tumekuwa tukifanya sensa ambapo sensa hii pamoja na mambo mengine inaonesha mtawanyo wa umri na kwa hiyo, ni rahisi kufanya maoteo ya watoto wanaoingia shuleni. Kwa kuwa, tatizo hili la mawati limekuwa likitokea kila mwaka inapotokea tunaanza msimu mpya wa masomo, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kutumia takwimu zinazotokana na sensa kujiandaa vizuri kulimaliza tatizo hili badala ya kutokea mwaka hadi mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimuondoe hofu, Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inatumia takwimu sahihi kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto za madawati na wanafunzi mashuleni. Ndiyo maana nimeeleza katika moja ya mpango wa Serikali ambao sasa hivi upo ni kwamba kila darasa linavyokuwa linajengwa ni lazima liwe na madawati ama kama ni shule lazima iwe na miundombinu yote. Kwa hiyo, hiyo ni sehemu tu ya kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto ya madawati mashuleni.

Mheshimiwa Spika, lakini pili na kwa kifupi ni kwamba sisi tuna huo mpango na nimhakikishie kabisa kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano, hiyo kero ya madawati mashuleni tunayo na tutaieleza katika mpango wetu wa bajeti wakati utakapofika.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa kuwa Serikali imekiri kwamba matumizi ya bandari ya Dar es Salaam yalisababisha uharibifu wa barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Lindi kwenda Mtwara na hali ya barabara hiyo kwa sasa kwa kweli ni mbaya pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais aliagiza ikarabatiwe, lakini hali ni mbaya tunasafiri mpaka masaa saba badala ya masaa manne.

Je, Serikali iko tayari sasa kutenga fedha ya kutosha kuikarabati barabara hii kwa kiwango kinachotakiwa ili turudie hali yetu ya zamani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la msingi ilikuwa ni bandari lakini ilikuwa linahusianisha na uharibifu wa barabara kwa sababu magari mengi yanaendelea kutumika. Naomba tu niseme baada ya hapa kwa sababu halikuwa swali la msingi, nitaomba nionane na Mheshimiwa Nape ili niweze kuona namna ambavyo Serikali imetenga fedha kwa sababu ni utaratibu wa Serikali kutenga fedha kufanya matengenezo kwenye barabara zote na hasa barabara muhimu kama hizo.

Lakini figure kamili sina, ila fedha inatengwa kwa kila barabara kuhakikisha kwamba hiyo barabara inatumika. Ahsante. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, tunajua kwamba Serikali ilisitisha uongezaji wa maeneo ya utawala lakini Serikali ilitoa ahadi hapa Bungeni kwamba yale maeneo ambayo hayatakuwa na gharama za uanzishwaji wake na hasa maeneo ya kata, kwa sababu kata zetu hizi ni kubwa mno katika baadahi ya maeneo. Je, Serikali itaanza kutekeleza ahadi hii lini ili kusogeza huduma karibu na wananchi wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara hizi ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezizungumzia hapa zimekuwa zikiharibika mara kwa mara na hasa wakati huu wa kipindi cha mvua. Uwezo wa TARURA kuendelea kuzikarabati hizi barabara unaonekana unapungua siku hadi siku kwa sababu ya mgao mdogo ambao wanaupata kutoka kwenye fedha za Bodi ya Barabara. Je, Serikali haioni umefika wakati sasa wa kuanzisha chanzo maalum cha fedha kupelekwa kwenye TARURA badala ya kutegemea hisani kutoka kwenye Mfuko wa Barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali ina mpango na dhamira ya dhati ya kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi kwa kuanzisha maeneo ya utawala ambayo hayatakuwa na gharama kubwa. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, naomba nimhakikishie kwamba dhamira hiyo ya Serikali ipo na utaratibu wa kuomba maeneo hayo unafahamika na nishauri kwamba pale ambapo tunaona kuna kila sababu ya kuanzisha maeneo hayo yanayofuata maelekezo ya Serikali ya kuzingatia kutokuongeza gharama, basi maombi yawasilishwe kwa mujibu wa taratibu Ofisi ya Rais TAMISEMI ili yaweze kufanyiwa kazi kwa kadri ya taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye ni kuhusiana na barabara zinazohudumiwa na TARURA. Ni kweli Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini ina jukumu kubwa la kuhakikisha miundombinu ya barabara inapitika mwaka mzima. Wakala huyu ana mtandao wa barabara zipatazo kilometa 108,496 ambazo hufanyiwa matengenezo mara kwa mara na pale inapobidi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba bado bajeti ya TARURA haitoshelezi lakini Serikali imekuwa ikiongeza fedha mwaka hadi mwaka ili angalau kuendelea kuboresha utekelezaji wa wakala huyu. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, bajeti ya TARURA ilikuwa shilingi bilioni 241, lakini kwa mwaka 2020/2021 bajeti ya TARURA ni shilingi bilioni 275 ikiwa ni ongezeko la takribani shilingi bilioni 34. Ni kweli Serikali inaona sababu ya kutafuta vyanzo vingine vya kuongezea uwezo TARURA ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa zaidi na jambo hili linaendelea kufanyiwa kazi.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu wa kipande cha Ifakara – Kihansi chenye kilometa 125 umekamilika. Je, Serikali iko tayari kuanza kutenga fedha ya kujenga hiki kipande katika mwaka huu wa fedha?

Mheshimiwa Spika, swali la pili barabara ya Lutamba- Chiponda-Mnara-Nyengedi inayounganisha Halmashauri ya Mtama na Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ambayo pia inaunganisha barabara ya Mkoa ya kwenda Ruangwa lakini pia ya kwenda Masasi kwa maana ya Mkoa wa Mtwara, ni barabara ya muhimu sana kwa uchumi wa eneo hili, lakini hii barabara imekuwa chini ya TARURA kwa muda mrefu na TARURA kwa kweli hawana uwezo wa kuendelea kuijenga. Je, Serikali iko tayari kuipandisha hadhi barabara hii sasa ianze kuhudumiwa na TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Nape, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoiuliza ya Mheshimiwa Kunambi ni barabara ambayo inaunganisha Mkoa na Mkoa na kwa kuwa usanifu wa kina umekamilika, tunaamini katika bajeti ijayo Serikali itaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Nikiri Mheshimiwa Kunambi kila anaposimama imekuwa akiipigia sana kelele barabara hii. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi kwamba katika bajeti tunazoanza kuzitekeleza kwa mwaka ujao naamini itatengewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Nape Mbunge wa Mtama sitazitaja barabara zake zimekuwa ni nyingi Lutamba-Chiponda-Mtama-Lindi na kwamba ni barabara za TARURA, naomba Mheshimiwa Nape nimshauri waweze kupitia kwenye taratibu za kawaida za kupandisha hadhi hizi barabara kutoka TARURA kwenda TANROADS ambapo lazima watakaa na Bodi ya Barabara ya Mkoa halafu itakwenda kwenye Kamati ya Ushauri ya Mkoa na baadaye zinakuja kwenye Wizara kwa ajili ya kuziangalia kama zinakwenda kupandishwa hadhi. Kwa hiyo kama zitakuja kwa utaratibu huo nadhani kuna utaratibu zitafikiriwa na Serikali itaona namna gani ifanye ili kuzipandisha hizo hadhi. Ahsante. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mtama tulipokabidhiwa Halmashauri hii na Mheshimiwa Rais alituahidi kwamba ujenzi wa mjengo yake utaanza mapema na hivi karibuni Waziri Mkuu alifanya ziara Jimboni Mtama na kutuahidi kwamba hizi fedha za ujenzi zitakuja.

Sasa je, Serikali iko tayari kuanza kuleta hizi fedha hata kama ni kwa awamu ili ujenzi huu na ahadi ya Mheshimiwa Rais ianze kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imedhamiria kuhakikisha inakamilisha au inaanza ujenzi wa majengo ya utawala katika Halmashauri zile mpya ambazo miongoni mwao ni Halmashauri hii ya Mtama.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi bilioni 80.42 zimetengwa na zitaanza kutolewa wakati wowote kuanzia sasa na taratibu zinaendelea ili zile Halmashauri ambazo kwanza zilipata fedha za kuanza ujenzi zipate fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo lakini zile ambazo zinahitaji kuanza ujenzi ziweze kupata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo ya utawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili katika mwaka wa fedha ujao pia Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha shughuli hizo za ujenzi wa majengo ya utawala zinakamilika. Kwa hivyo, naomba nimhakikishie Mbunge wa Mtama, Mheshimiwa Nape kwamba Serikali inatambua uhitaji wa kuanza ujenzi wa jengo la utawala katika Halmashauri ya Nape hiyo ya Mtama na tutahakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya kutoa Elimumsingi Bila Malipo kwa miaka mitano mfululizo, kuna changamoto ambazo zimejitokeza kutokana na zoezi hili. Moja ya eneo kubwa ni kwamba vigezo vinavyotumika kupeleka fedha kidogo vinasumbua, hasa kwa shule ambazo zina wanafunzi wachache wakati baadhi ya mahitaji hasa ya utawala yanafana. Je, Serikali haioni umefika wakati wa kupitia upya vigezo hivi na kuona namna bora ya kupeleka fedha hasa kwenye eneo la utawala ili kutatua tatizo hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Elimumsingi kwa definition ambayo imekuwa ikitolewa ni kuanzia Chekechea mpaka Kidato cha Nne. Hapa pana Kidato cha Tano na cha Sita ambapo hakuna facility na Elimu ya Juu kuna mikopo.

Je, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuhusisha kidato cha tano na cha sita kwenye elimumsingi ili nao wapate elimu hii ambayo imekuwa ikitolewa na Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli alichoeleza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina vigezo vyake ikiwemo idadi ya wanafunzi na ndiyo mfumo ambao tunautumia kupeleka hiyo ruzuku ya fedha katika shule zote nchini. Bahati mbaya sana kwenye zile shule ambazo wanafunzi wake ni wachache tumekuwa tukipeleka fedha kulingana na mahitaji ama kulingana na idadi yao ambayo ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa na nia njema na ndiyo maana moja ya nia njema yake ni kuanzisha Elimu Bila Malipo. Kutokana na hiyo nia njema, sasa hivi nafikiri ninyi nyote mmejua, moja ya jitihada kubwa ya Serikali ilikuwa ni kuboresha miundombinu hususan katika yale maeneo ambayo shule nyingi zimekosa uhitaji na Wabunge wote ni mashuhuda sasa hivi, Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni, mabwalo pamoja na maabara. Ndiyo maana nimeeleza kwenye jibu langu la msingi kwamba, kulingana na bajeti na mahitaji tutaendelea kutenga fedha. Hata hivyo, hiyo changamoto anayoielezea Mheshimiwa Mbunge tunaipokea na kutaifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita ambao Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba hawahusiki na Elimu Bila Malipo. Moja nipokee, lakini hili ni suala la kisera; na kwa sababu Serikali ipo hapa ndani, tumelipokea hilo na tutalifanyia kazi tuone mahitaji yake kulingana na mazingira tuliyonayo. Ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na commitment nzuri ya Serikali ya kuboresha vituo hivi, tunayo changamoto moja kubwa ya Maafisa Ugani wengi wanaopelekwa kwenye baadhi ya maeneo yetu kutokuwa na ujuzi wa kuhudumia mazao ya maeneo husika. Mfano mzuri ni kwenye korosho wapo Maafisa Ugani wanapelekwa wakulima wa korosho wanakuwa wanajua zaidi kuchanganya madawa kuliko hao Maafisa Ugani. Serikali ina mpango gani wa kutumia Vituo hivi vya Utafiti kutoa mafunzo ya ziada kwa Maafisa Ugani wanaowapeleka kwenye maeneo mbalimbali ili wawe na ujuzi wa ziada wa kuhudumia mazao ya maeneo husika badala ya huu ujuzi wanaopewa wa jumla ambapo wakija kule inakuwa ni usumbufu badala ya kuwa msaada.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba kuna gap kubwa ya Maafisa Ugani ambao wanakwenda kuhudumia mazao na aina ya mazao wanayoyahudumia kuhusu suala la uelewa na mabadiliko ya teknolojia imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kama Wizara katika programme ambayo tunaianza sasa hivi na mwezi ujao tutaanza training ya kwanza ya Maafisa Ugani 245 wa Ukanda wa Kati na kituo hicho kitakuwa hapahapa Bihawana kwa ajili ya kuwa-training kuhusiana na mazao yaliyoko katika Ukanda huu wa Kati. Kwa ukanda wa maeneo anayetoka Mheshimiwa Nape na yeye mwenyewe nilikuwa naye kwenye ziara hivi karibuni, tumekubaliana mwezi wa 10 kwa kuwa Vyuo vya MATI vinakuwa vimefungwa tutawachukua Maafisa Ugani kutokana na halmashauri husika na ekolojia yake na mazao yanayozalishwa pale na kitu chetu cha TARI Naliendele kitatoa training maalum ya wale Maafisa Ugani kutokana na zao katika eneo husika analotoka Afisa Ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nilihakikishie Bunge lako na Watanzania wote kwamba katika mwaka huu wa fedha suala la ku-train Maafisa Ugani ni priority namba moja ya Wizara ya Kilimo. Kwa kuwa bajeti yetu mlishatupitishia sasa hivi wataalam wetu wanaandaa manual za ekolojia tofauti tofauti ili tuanze kazi hiyo ya ku-train Maafisa Ugani as we go on. Nashukuru.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya kugharamia elimu kutoka chekechea mpaka kidato cha nne na utaratibu unaofanywa na Serikali wa kutoa mikopo kwa elimu ya juu bado hapa vijana wa kidato cha tano na sita kuna tatizo la kugharamia elimu.

Ni lini Serikali itaweka sasa utaratibu ili kuwahusisha vijana wa kidato cha tano na sita katika utaratibu wa elimu bila malipo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Naibu Spika, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nape kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli vijana wetu wa kidato cha tano na sita wanatakiwa kugharamia kwa maana ya ada kwa wale wa kidato cha tao na sita ambao kwa wanafunzi wetu wa bodi kulipa shilingi 70,000 na wale wa
day kulipa shilingi 35,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii tunaiona kwamba ni affordable au inaweza sana Watanzania wengi kuilipa lakini kwa vile Mheshimiwa Mbunge ameielezea hapa acha basi tulibebe jambo hili tuweze kwenda kuliangalia kwa kina kama Serikali, kwa vile Serikali sasa imeanza kutoa elimu bila malipo kutoka elimu ya awali mpaka kidato cha nne basi na hili tuliingize kwenye mjadala tuweze kuliangalia katika kipindi kijacho kama tunaweza kama Serikali tukaweza ku-wave na kuweza kuondoa ada hii kwa upande wa kidato cha tano na sita, aHsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa umilikaji halali wa ardhi utaisaidia Serikali katika kukusanya mapato kwa sababu wamiliki halali watalipa kodi vizuri na kwa kuwa kwa uzoefu uliooneshwa kutokana na shida ya uhamishaji wa umiliki unaonesha kwamba wananchi wa kawaida wanashindwa kumudu gharama. Je, Serikali iko tayari ikiwezekana kufuta kabisa gharama za kuhamisha umiliki ili wamiliki waweze kumiliki na kulipa kodi kwa Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa maombi ya wananchi wa Mtama walifuta umiliki wa shamba la Maumbika lililoko Jimboni Mtama na kulikabidhi kwetu, lakini tukiwa katika utaratibu wa kuligawa kwa wananchi, Serikali hiyo hiyo ili-reverse uamuzi wake. Je, Serikali iko tayari sasa kutumilikisha shamba hili ili wananchi waweze kulitumia kwa sababu limetelekezwa kwa muda mrefu na mmiliki wa shamba hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka tu nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii ni sikivu na kila mara wananchi wanapotoa kilio chao, Serikali hukaa na kuanza kuangalia upya kuweza kuona ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia. Kwa hiyo katika suala zima la kusema kwamba pengine gharama ya uhamishaji miliki iweze kufutwa ili watu waweze kumiliki wengi bila tatizo lolote, naomba niseme tu Serikali hii inaendeshwa kwa kodi za wananchi. Sasa ukishaanza kuzifuta kodi ambazo pengine ni ndogo na ni token ukiziangalia, mwisho wa siku utakuta Serikali haina njia nyingine yoyote ya kupata mapato na kujikuta kwamba tunakwama. Tunachofanya kama Serikali ni kuendelea kupunguza zile kodi ambazo pengine zina kelele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nikizungumzia suala la muuliza swali ambaye aliuliza swali la msingi, Mheshimiwa Stella Manyanya kwenye eneo lake hata zile tozo wanazotoza katika masuala mazima ya ardhi ziko chini sana. Ukiangalia kwenye makazi walikuwa wanatozwa shilingi 15 lakini sasa hivi wanatozwa shilingi 11 ambazo ni kidogo sana. Kwenye maeneo ya biashara ilikuwa shilingi 30, sasa hivi wanatozwa shilingi 21, hata shilingi 100 haijafika. Ni ndogo ndogo ambazo wananchi wakiweza kulipa kwa hiari ni pesa ambazo unaweza ukazikusanya na zikafanya kazi kubwa katika Taifa hili. Kwa sababu wazo limetolewa, naomba tulipokee na sitaweza kulitolea maamuzi sasa hivi kwa sababu ni lazima mchakato uweze kupita.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameongelea suala la shamba la Maumbika kwamba Serikali ilifuta umiliki wake kwa kushindwa kulimiliki halafu baadaye pengine maamuzi yakabadilika. Naomba niseme kwamba, wakati mwingine tunapotoa ilani kwa ajili ya kubatilisha milki za watu, tunaangalia hatua iliyofikiwa lakini halmashauri husika ndiyo inayoleta notice au maombi yake kwa Waziri kuomba shamba lile lifutwe kwa sababu wameshindwa kutimiza masharti lakini wakati huo wanakuwa wamempa notice ya siku 90 ili aweze pengine kujitetea kwamba kwa nini hakuweza kumudu au kufuata masharti yale yaliyowekwa. Kwa hiyo utetezi unapokuwa wakati mwingine una uhalali na mantiki ndani yake, Serikali pia huwa inabadili mtazamo wake na kuweza kumrudishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa suala hili la Maumbika ambalo amelizungumza lazima kuna kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika hilo kwa sababu sikuweza kuliangalia kwa undani wake kuweza kujua ndiyo amelitoa sasa hivi. Basi kama lina maelezo ya ziada zaidi ya hizi taratibu za kisheria, niko tayari kumjibu baadaye. (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana na ya uhakika ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka tu kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba nchi hii kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Na. 5 Ardhi ya Vijiji na Na. 4 Ardhi ya Jumla tunatoa hati mbili. Kuna hati ambayo ndiyo hiyo inayosababisha wanyonge wananchi wanamiliki, tuna hati ya kimila ambayo inatolewa kwa mujibu wa sheria ambayo zaidi ya asilimia 90 ya hao wanyonge wa nchi hii wanapewa hati za kimila na ndizo zilizo nyingi kuliko hizi hati za mjini. Hawatozwi pesa ya kuanzia wala ada ya kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka niwaambie kwamba Serikali kupitia Bunge hili mlitunga sheria nzuri sana inayowatambua wanyonge. Wanyonge wote wanaomilikishwa zile ardhi wanazozitumia kwa shughuli zao za uzalishaji wa kila siku hawatozwi lolote, hawana kodi ya uhamishaji wala hawana kodi ile la land rent ya kila mwaka na hawana ukomo. Ana miliki leo, hana miaka 33 wala miaka 99 kama hati za mjini. Kwa hiyo suala la wananchi maskini wametambuliwa kwa mujibu wa sheria na waendelee. Hivi sasa Bunge lako halijawahi kutunga tozo yoyote kwa wananchi maskini wanaomiliki ardhi kwa mujibu wa sheria hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la Maumbika, nalijua vizuri. Tulikuwa na makusudi ya kufuta na ni kweli yule mwekezaji ametelekeza lile shamba. Nataka uwaambie wananchi wa Jimbo lako la Mtama, leo nakupa ahadi, nitakapokuwa naosma bajeti hapa, nitakupa barua nataka lile shamba limilikiwe na Halmashauri ya Wilaya ya Mtama ili wananchi wa pale waliendeleze iwe sehemu ya mapato yao. Walime korosho kwa sababu lile shamba ni la korosho, mmiliki alilitelekeza siku nyingi, tuko kwenye hatua za mwisho za kuliondoa, lakini kwa sasa ningeomba watu wa halmashauri waendelee kuliangalia angalia, kama kuna korosho humo waanze kuokotaokota. Barua kamili ya umiliki wa shamba lile kurudi halmashauri nitaitoa hapa wakati nitakapokuwa nawasilisha bajeti yangu. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025, Chama cha Mapinduzi kiliahidi kwamba Serikali itaweka utaratibu sasa wa kuanza kununua chokocho au mabibo yaliyokaushwa: Je. Serikali iko tayari kuanza kununua mabibo hayo kwa msimu huu wa Korosho unaokuja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahadi iliyowekwa katika Ilani ni kuhakikisha kwamba mkulima wa Korosho anauza Korosho, anauza Bibo na ikiwezekana hata product ambazo zinatokana na zao la Korosho ikiwemo Siagi na vitu vingine. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie tu kwamba, TARI Naliendele wameshamaliza tathmini ya namna gani ya wakulima wataweza kuvuna Korosho na Ijumaa mkihudhuria kikao mtaona Mheshimiwa Dkt. Kapinga anafanya presentation ya kwanza ya namna ya kuvuna kwa kutumia Neti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatarajia kwamba Serikali haitanunua Mabibo, bali tutahakikisha Mabibo yanavunwa kwa ubora unaostahili ili yaweze kununuliwa na wafanyabiashara na yaweze kuongezewa thamani.

Mheshimiwa Spika, Kongwa vile vile Korosho zako ulizoanza kuvuna hivi karibuni ndani ya kipindi cha miaka hii mitano, Bibo na lenyewe litapata soko. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na kumwalika Naibu Waziri aje kutembelea msitu wa hifadhi wa Rondo, maeneo ya Tarafa ya Rondo, Rutamba, Milola na Kiwawa yamekuwa yakiathiriwa sana na Wanyamapori hasa tembo; na kwa kuwa idadi ya askari wanaohusika na ulinzi wa eneo hili ni kidogo.

Je, Serikali iko tayari kutoa mafunzo na kuwawezesha vijana wa maeneo haya washirikiane na wale askari katika kusaidia kulinda mali na Maisha ya wananchi wa eneo hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Spika, ahsante. Ni kweli kumekuwa na matukio mbalimbali ya uvamizi wa tembo. Hii tukumbuke tu kwamba tunaishi maeneo mengi ambayo kihistoria ilikuwa ni mapito ya Wanyamapori wakiwemo tembo. Wizara kwa mara nyingi imekuwa ikipata hizi taarifa na kutoa ushirikiano kwa wananchi ikiwemo kupeleka maaskari kuwaondoa hao tembo.

Mheshimiwa Spika, Serikali iko tayari kushirikiana na vijana wakiwemo kwenye maeneo husika hasa kuanzisha WMA ambazo huwa zinashirikiana na Wizara katika kuhakikisha kwamba zinatunza maeneo husika lakini pia tunashirikiana kudhibiti hawa Wanyama wakali. Hivyo niko tayari kuongozana na Mheshiniwa Nape Nauye kwenye Jimbo lake kuhakikisha kwamba suala hili tunali-solve kwa Pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuongeza nguvu kwenye uchumi wa bahari, Serikali wakati ikijibu swali la Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, Mbunge wa Mchinga katika Bunge lililopita iliahidi kuwasaidia wavuvi wa ukanda wa bahari ya Mkoa wa Lindi vifaa vya uvuvi na hasa boti ya kusaidia uvuvi wao.

Kwa kuwa ahadi hiyo imechukua muda mrefu na muda unakwenda, wakati Serikali ikijipanga kuitimiza ahadi hii, je, iko tayari kuwasaidia walau mashine ndogo ndogo ziwasaidie kuboresha uvuvi wao wavuvi wa eneo hili hasa wanaotoka Jimbo la Mtama?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko tayari, tutapeleka mashine kwa wavuvi wa Mchinga na Mtama. Nataka tu nimhakikishie kwamba tunao mpango mkubwa zaidi wa kuwawezesha wavuvi wa Ukanda wa Pwani In Shaa Allah katika bajeti yetu hii ya 2021/2022 mambo yatakuwa mazuri sana katika kuhakikisha kwamba wanafanya vizuri katika shughuli zao za uvuvi.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na jitihada ambazo zinafanywa na Serikali, Wizara imekuwa ikisema kwamba upandaji wa pilipili kwenye maeneo ambayo yanakaribiana na vijiji una uwezo wa kuzuia tembo kuingia vijijini. Sasa, je Serikali hiko tayari kupitia TANAPA na taasisi zake wakapanda wao hizi pilipili ili wawasaidie wananchi wetu wasihangaike, mazao yao yasiliwe na wao wasiuliwe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape, Mbunge wa Mtama, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tulishabuni mbinu mbadala za kuhakikisha kwamba hawa wanyama wakali wanapunguza kasi ya kuathiri wananchi ikiwemo pilipili lakini pia kuna mizinga ya nyuki ambao ni njia bora zaidi ya kuwafanya hawa wanyama wasiweze kusogelea makazi ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, tunalipokea wazo lake, lakini kulingana na gharama Serikali itaendelea kuangalia tathmini na tunaweza tukafanya kwa awamu, kwenye maeneo ambayo yameathirika Zaidi. Hata hivyo, niwaombe tu Waheshimiwa tuendelee kushirikiana kwenye hizi mbinu ambazo tunaendelea kuzielekeza wakati Serikali sasa inaangalia mbinu ya kudumu ambayo inaweza ikasaidia wanyama hawa kuishi katika maeneo yao na wananchi wakaishi kwa amani.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara hii ya Kusini liko serious kuliko namna ambavyo Serikali wanafanya kulijibu hapa na niwasihi sana Serikali hayo majibu mnayoyatoa hapa si sawa; ni kuwakejeli wananchi wa Kusini. Hii barabara imeharibika sana, kuna fedha mnapeleka kwa kweli ni uhujumu wa uchumi wa watu wa Kusini. Mtakumbuka mpaka ilifikia wakati Rais Magufuli akaja akafukuza watu yaani mpaka Rais anakuja anapita anaona ubovu anafukuza watu.

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea kwenye ukarabati ni kuongeza ubovu ndani ya ubovu yaani kwa kweli Kusini kwa sasa kumefungika.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni kwamba ni lini Serikali watakuwa serious waache kutumia rasilimali za nchi hii kuharibu zaidi ile barabara badala yake waende kufanya jambo la kuonyesha wako serious na kukarabati hii barabara badala ya majibu haya mnayotoa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimesikiliza sana, sana hoja zilizojengwa na Wabunge na hasa katika eneo la Ujenzi wa barabara hii inayokwenda huko Kusini (Mtwara - Lindi) na inafika mpaka huko kwenye Mkoa wa Ruvuma kwa jiografia yake.

Mheshimiwa Spika, na ninaendelea kukumbuka na kurejea maelezo ya Serikali na hasa viongozi wa juu ambavyo walikuwa na concern kubwa na barabara hiyo na hiki ambacho Waheshimiwa Wabunge wanakieleza kwa sasa ndani ya Bunge lako tukufu, ninaomba sana jambo hili tulichukue turudi ndani ya Serikali, tukafanye majadiliano na kwenda kufanya tathmini ya kina ya kujua nini kinachofanyika na hii itatusaidia kuokoa fedha za wananchi wa Tanzania walipa kodi katika kutekeleza miradi ambayo hailingani na thamani ya fedha na uhalisia unaotakiwa katika eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hapa hatuwezi kupata nafasi ya kufanya haya majadiliano ya kina na kutoa tathimini ya uhakika naomba uridhie tulichukue Serikali na tukalifanyie kazi. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara hii ya Kusini liko serious kuliko namna ambavyo Serikali wanafanya kulijibu hapa na niwasihi sana Serikali hayo majibu mnayoyatoa hapa si sawa; ni kuwakejeli wananchi wa Kusini. Hii barabara imeharibika sana, kuna fedha mnapeleka kwa kweli ni uhujumu wa uchumi wa watu wa Kusini. Mtakumbuka mpaka ilifikia wakati Rais Magufuli akaja akafukuza watu yaani mpaka Rais anakuja anapita anaona ubovu anafukuza watu.

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea kwenye ukarabati ni kuongeza ubovu ndani ya ubovu yaani kwa kweli Kusini kwa sasa kumefungika.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni kwamba ni lini Serikali watakuwa serious waache kutumia rasilimali za nchi hii kuharibu zaidi ile barabara badala yake waende kufanya jambo la kuonyesha wako serious na kukarabati hii barabara badala ya majibu haya mnayotoa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimesikiliza sana, sana hoja zilizojengwa na Wabunge na hasa katika eneo la Ujenzi wa barabara hii inayokwenda huko Kusini (Mtwara - Lindi) na inafika mpaka huko kwenye Mkoa wa Ruvuma kwa jiografia yake.

Mheshimiwa Spika, na ninaendelea kukumbuka na kurejea maelezo ya Serikali na hasa viongozi wa juu ambavyo walikuwa na concern kubwa na barabara hiyo na hiki ambacho Waheshimiwa Wabunge wanakieleza kwa sasa ndani ya Bunge lako tukufu, ninaomba sana jambo hili tulichukue turudi ndani ya Serikali, tukafanye majadiliano na kwenda kufanya tathmini ya kina ya kujua nini kinachofanyika na hii itatusaidia kuokoa fedha za wananchi wa Tanzania walipa kodi katika kutekeleza miradi ambayo hailingani na thamani ya fedha na uhalisia unaotakiwa katika eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hapa hatuwezi kupata nafasi ya kufanya haya majadiliano ya kina na kutoa tathimini ya uhakika naomba uridhie tulichukue Serikali na tukalifanyie kazi. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo mazuri ya Serikali ikumbukwe kwamba maeneo haya yalichukuliwa karibu miaka sita iliyopita kwa upande wa Jimbo la Mtama, ikafanyika tathmini wananchi hawakulipwa fidia kwa hiyo maisha yao yamesimama kwa miaka sita. Huu mchakato umeendelea unakwenda unarudi na wananchi hawajui wafanye nini. Serikali iko tayari kutoa fidia pamoja na ile ambayo ilifanyika lakini fidia hii ya miaka sita ambapo maisha ya wananchi hawa yamesimama hawaendelei na maisha yao ya kawaida wakisubiri fidia kwa miaka sita? Serikali iko tayari sasa kutafuta namna ya kuwafidia au vinginevyo tufute wananchi waendelee na maisha yao.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tukubali kwamba mambo haya yalifanyika wakati wa transition ambapo Sheria ya Madini ilikuwa inabadilika. Ni kweli kwamba jambo hili lilionekana kama linaleta hofu na wawekezaji walirudi nyuma. Pia sheria inatoa muda wa kwamba kama fidia imefanyika na ikapita miezi sita basi fidia hiyo inaweza kurudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu sasa mazingira yanaboreshwa tutawaomba tena tufanye fidia upya ili wananchi hatimaye waweze kulipwa. Nadhani hilo liko katika utaratibu wa sheria na hivyo sisi tutahimiza sheria ifanye sehemu yake ili fidia iweze kurudiwa na hatimaye wananchi waweze kulipwa na mradi uweze kuanza. Ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushkuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa pamekuwa na tatizo la matumizi ya hizi fedha za mikopo kwa maeneo mengi, na hasa maeneo mengine zimekuwa zikipelekwa kutumika kwenye maeneo yasiyo kusudiwa baada ya kukopwa.

Je, Serikali haioni wakati umefika sasa badala ya kutoa fedha, tutoe vifaa vinanyoendana na biashara husika au shughuli husika ambao inakopewa. Kwa sababu hivi vifaa tunahakika vitakwenda kufanya shughuli iliyokusudiwa, mfano, matrekta au vifaa vya uzalishaji badala ya kutoa fedha kama fedha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye Mbunge wa Mtama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, Serikali inatambua kuna mikopo ambayo inatolewa kwa maada ya fedha taslim kwenye vikundi, pia kuna mikopo ambayo sasa tumeboresha utaratibu wa kutoa vifaa vitakavyowawezesha wajasiriamali kutekeleza shughuli zao; Kwa hivyo wazo lake ni zuri sana. Na sisi kama Serikali tumelichukua tumeanza kulifanyia kazi, kuna vikundi ambavyo kimsingi vinahitaji vifaa, na kuna vikundi ambayo vitahitaji fedha kwa ajili ya aina ya shughuli zake, na hili nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kulitekeleza. Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa tatizo hili limekuwa kubwa na kwa miaka sasa linazungumzwa na hoja ni hizi hizi na majibu ni haya haya, Serikali haioni umefika wakati wa kutunga sheria iwe ni kosa kumkaimisha mtu kwa muda mrefu. Kwamba tutunge sheria ifikie ukomo kwamba mwisho wa kukaimu ni hapa na baada ya hapa mtu akipitiliza tuchukue hatua ili tuondokane na hili mtu anakaimu miaka Tisa na hakuna mtu anachukuliwa hatua. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishasema awali tatizo hili tunalifahamu na tayari tukishakuwa na kanzidata ya watu wenye sifa hii changamoto inaenda kuisha kwa sababu tutaanza ku-post moja kwa moja watu kwenye nafasi hizi zilizo wazi. Commitment yetu ni kwamba tutaendelea kulifanyia kazi na kuhakikisha kwamba nafasi zote zinazokaimiwa zinakuwa na watu wenye sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilihakikishie Bunge lako kwamba muda si mrefu tutakuwa tayari tuna watu wenye sifa kwenye nafasi zao. Vilevile, nichukue fursa hii kuwaasa na kuwaagiza watumishi wote nchi nzima kuhakikisha ifikapo mwisho wa mwezi huu, walete majina yote ya watu ambao wanakaimu nafasi zao bila kibali cha Katibu Mkuu Utumishi. Vilevile, ifikapo tarehe 30 ya mwezi huu, walete majina ya wote wanaokaimu kwa vibali vya Katibu Mkuu Utumishi ili tuweze kuwafanyia upekuzi na kama wao wanafaa kuwa kwenye nafasi hizo, basi tuwaache hapohapo kwenye nafasi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sisi Kusini nadhani magonjwa haya kwa sababu ya korosho hayapo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya aliwahi kutembelea kusini. Katika ziara yake, tulimpa maombi ya kusaidiwa kukarabati kituo cha afya kikongwe kuliko vyote katika Jimbo la Mtama ambacho kinahudumia zaidi ya kata sita na ahadi hiyo ilitolewa. Sasa nataka kujua ni lini tutapata fedha ili tusaidie kuboresha huduma katika eneo hili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kama ambavyo amesema tulikwenda na vilevile baada ya hapo aliandika barua kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya na Mheshimiwa Waziri wa Afya aliwasiliana na TAMISEMI. Nataka kumhakikishia kwamba kituo hicho kimeingizwa kwenye bajeti na kimetengewa shilingi milioni 500 na baada ya fedha kupatikana kazi itaanza. Nami baada ya kumaliza Bunge, twende pamoja ili tusisitize na mambo mengine ambayo tuliyapanga wakati ule kuyafanya. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge wa Mchinga amesema, yeye kwake ni tarafa mbili, mimi nina tarafa tano. Kati ya tarafa tano tarafa tatu hazina mawasiliano kabisa. Na utaona hapa sisi wa Lindi tunazungumzia Tarafa, siyo Kijiji, ni tarafa nzaima ambayo ina kata kadhaa na vijiji kadhaa.

Mheshimiwa Spika, swali langu kwa Serikali, Serikali haioni sasa umefika wakati wa kuja kukomboa Mkoa wa Lindi na suala la mawasiliano kwa sababu pamekuwa na ahadi za miaka nenda, miaka rudi kulimaliza hili jambo?

Hii habari ya kusema tutakuja kutembea ndio majibu yamekuwa haya kila siku. Nataka commitment ya Serikali kuja kutusaidia Mkoa wa Lindi tuondokane na tatizo hili.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Nnauye Mbunge wa Mtama kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nape Nnauye kwa sababu amekuwa akitoa taarifa ya changamoto ya mawasiliano ya wananchi wake wa Jimbo la Mtama. Na kwa bahati nzuri nimekaa naye sana na tayari tumeshakubaliana mimi na yeye tutatoka hapa kwenda mpaka Mtama kwenda kujiridisha tukiwa na wataalamu wote kiasi kwamba sasa hili tatizo pindi ambapo tutajua kwamba tatizo lipo wapi ili tuweze sasa kuingiza katika mpango wa utekelezaji wa mwaka ujao. Ahsante sana.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na kupongeza kazi nzuri sana inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini Rais Samia ya kufufua uchumi wa Mkoa wa Lindi ikiwemo kufufua mazungumzo ya Mradi wa LNG, lakini pia na utengaji wa shilingi billion 50 kwa ajili ya kujenga Bandari ya Uvuvi Kilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni lini mchakato huu wa ujenzi wa hii bandari ambao ni ukombozi mkubwa wa ukanda wetu utaanza? Kwa sababu ahadi iliyokuwepo ni kwamba mchakato huu ungeanza mapema pamoja na kumshukuru Mama Samia kwa kazi hii nzuri lakini lini mchakato huu utaanza wa kujenga bandari hii kwa ajili ya uvuvi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nape Moses Nnauye Mbunge wa Mtama Mkoa wa Lindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze sana kwa swali hili zuri na la kimkakati. Ujenzi wa bandari ya Uvuvi umetamkwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025, nasi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kwake na msukumo wake wa kuhakikisha kwamba mradi huu wa kimkakati wa ujenzi wa bandari unafanikiwa na hatimye kuweza kwenda sambamba na ile zana ya uchumi wa blue. Tayari wataalamu wetu wameshafanya hatua zote za mwanzoni na imekubalika kitaalamu ya kwamba bandari ile itakwenda kujengwa pale Kilwa Masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa wataalam wapo katika hatua za mwisho kabisa ya kuweza kuli-demarcate kuliweka sawa lile eneo linalokwenda kuwekwa bandari ile. Na tunashukuru sana kwa kuwa eneo hili ni eneo la kimkakati la kuelekea kule katika bahari kuu. Hivyo kile kilio cha muda mrefu cha Wabunge wengi na Watanzania wengi cha kwamba nchi hainufaiki ipasavyo na bahari yetu sasa kinakwenda kupata muarobaini wake. Kwa kweli tunamshukuru Mheshimiwa Rais hata kwa zile pesa za kununua meli nane ambapo sisi Tanzania bara tutapata meli nne zitakazo kwenda kuvua upande wa bahari kuu. Ninashukuru sana. (Makofi)