Contributions by Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa (12 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumshukuru Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa wakati wa akizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina shaka kuwa majadiliano ya hotuba hiyo hapa Bungeni yamedhihirisha umakini wa namna Waheshimiwa Wabunge walivyoielewa hotuba ile na umakini uliotumika katika kutayarisha na uwasilishaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Spika na wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa jinsi ambavyo mmesimamia mjadala huu. Aidha, kwa pekee kabisa, nampongeza Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge ambaye alipata fursa ya kusimamia mjadala wa hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nachukua nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia mjadala huu wa hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Aidha, nawashukuru kwa kuunga mkono maeneo mbalimbali yaliyobainishwa katika hotuba hiyo. Kitendo cha kuunga mkono kimeipa Serikali nguvu ya kutekeleza ushauri wa michango mizuri iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwadhihirishia kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge yote kwa ujumla itasaidia sana Serikali kutekeleza ufanisi zaidi, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, itasaidia kutekeleza pia Mpango wa Miaka Mitano, kutoka mwaka 2016/2017 kwenda mwaka wa fedha 2020/2021 na Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 171 wamechangia mjadala huu, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhitimisha hoja hii, siyo nia yangu kujadili tena hoja moja baada ya nyingine kama ilivyotolewa wakati wa Waheshimiwa Wabunge wakichangia hotuba ya Mheshimiwa Rais, bali nitajielekeza katika ujumla wake. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri tayari wameshatoa maelezo ya maeneo muhimu na ambayo yanayotakiwa kuzingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya awamu ya tano imeweka msisitizo katika kuhakikisha inarejesha nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa kuweka mkazo katika misingi ya uadilifu, uwajibikaji, kutoa huduma kwa wakati na kuchukua hatua za haraka dhidi ya watumishi wote wanaokwenda kinyume na misingi ya utendaji kazi Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali ya awamu ya tano kwa kuzingatia falsafa ya Hapa Kazi Tu, ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, itaendelea kuhakikisha kwamba inawakumbusha kuwa kila Mtanzania anatumia muda wake katika kufanya kazi zaidi na kila Mtendaji Serikalini anatimiza wajibu wake na pia Serikali itahakikisha inachukua hatua dhidi ya wote watakaokiuka maadili ya kazi na sheria zilizowekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusisitiza kuwa kila mtumishi mahali popote alipo ni lazima atimize wajibu wake ipasavyo. Tunataka kujenga utumishi wa umma wenye kuzingatia uadilifu unaowajibika na watumishi wanaofanya kazi kwa bidii na maalifa na kamwe hatutavumilia mtumishi mzembe na anayefanya kazi kwa mazoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mjadala wa hotuba ya Mheshimiwa Rais, zipo hoja zilitolewa na Waheshimiwa Wabunge ambazo utekelezaji wake utahitaji kufanya maandilizi ya kutenga Bajeti ya Serikali. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara, mawasiliano, uchukuzi, ikiwemo bandari pamoja na miundombinu ya usambazaji wa maji na nishati.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ipo miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa nchini katika sekta za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, mifugo, maliasili, madini na kadhalika na sekta za huduma ya jamii, kama vile elimu na afya ambayo inahitaji pia kukamilishwa wakati huu sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali itajitahidi kupanga vipaumbele vyake vya Mpango na Bajeti kwa kuzingatia ahadi za Mheshimiwa Rais kuanzia mwaka huu wa fedha na kuendelea. Maoni na hoja za Wabunge zitazingatiwa wakati wowote wa utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi ni kuomba ushirikiano wa wananchi wote ili utekelezaji uwe wa ufanisi na tija. Ili kutimiza azma ya kutekeleza miradi yote hiyo, Serikali itahakikisha inasimamia ukusanyaji wa mapato yake ipasavyo ili kuwahudumia Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya kilimo, Waheshimiwa Wabunge wameeleza changamoto nyingi zinazowakabili wakulima ikiwemo kupatikana kwa pembejeo, uchelewaji wake wa kuwafikia pia wakulima wetu. Tatizo la ununuzi wa mazao hasa tumbaku, pamba, kahawa na korosho na huduma chini ya Stakabadhi Ghalani, Serikali imepokea ushauri wa Wabunge na utazingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kueleza kuwa kutokana na baadhi ya maeneo katika nchi yetu kukumbwa na uhaba wa chakula, uliotokana na aidha uzalishaji hafifu katika msimu uliopita ama kutokana na mazao ya vyakula kusombwa na mafuriko, Serikali inaendelea kutumia akiba yake ya chakula kuhakikisha kwamba waathirika wote wanapata chakula.
Nachukua fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kusimamia kikamilifu ugawaji wa chakula hicho ili kuwafikia walengwa bila ya upendeleo na bila ya kuchepusha na kukipeleka mahali pengine. Aidha, chakula hicho kigawanywe hadharani ili kuondoa malalamiko ya wananchi ili kuhakikisha walengwa wa chakula cha msaada wanafikiwa na kuhudumiwa pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wakuu na watendaji wa Serikali katika ngazi zote, watoke maofisini kwenda vijijini ili kuhakikisha kwamba kila mwananchi anajishughulisha na shughuli za kilimo kwa lengo la kuzalisha chakula zaidi kwa ajili ya matumizi ya msimu ujao. Wakulima katika maeneo yaliyopata mafuriko wapatiwe mbegu za mazao yanayokomaa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu usambazaji wa pembejeo, Halmashauri zote zihakikishe kuwa pembejeo zinafika mapema katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za masika na zipelekwe kwa walengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limesisitizwa vizuri na Waziri wa Kilimo lakini pia Serikali itaendelea kuangalia mfumo bora wa kusambaza pembejeo hizo za ruzuku ili kuondoa malalamiko ya wakulima. Halmashauri na Wizara ya Kilimo wakae kuondoa tozo za ushuru zenye kero kwa mazao yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji ni changamoto ya nchi nzima. Ili kuboresha huduma ya maji Serikali itajitahidi sana kutumia mbinu zake zikiwemo kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ili yatumike wakati wa kiangazi. Aidha, Serikali imepanga kuhakikisha kwamba fedha kwa ajili ya miradi ya maji ambayo haijakamilika, zinapatikana na kutumwa kwa wakati katika maeneo husika. (Makofi)
Vilevile Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa wakandarasi wanaopewa kazi za kujenga miradi ya maji, wana uwezo wa kutosha ili miradi hiyo iwe na ubora unaotakiwa na itaendelea kulipa madeni ya wakandarasi na wataalam washauri kama ambavyo imeelekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo yanayoikabili sekta ya maliasili na utalii yakiwepo ya ujangili wa wanyamapori na nyara, migogoro ya mipaka kati ya vijiji na hifadhi na upotevu wa mapato yanayoshughulikiwa kwa wakati ili kuifanya Serikali hii muhimu kuchangia katika uchumi wa Taifa na kuhifadhi rasilimali hii kwa ajili ya kizazi kijacho. Ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wote utazingatiwa na wadau wote pia ili kuhakikisha wanyamapori hususan tembo na faru hawaendelei kuuawa na majangili.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala haya ya uvuvi yataimarishwa kwa kuwatafutia wananchi na wadau wa sekta ya uvuvi nchini na kuhakikisha kwamba wanapatiwa vifaa vya kisasa vya uvuvi; kuwatafutia masoko na kuongeza kasi ya uwekezaji katika viwanda vya mazao ya samaki hususan katika ukanda wa bahari kuu na maziwa makuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanya uvuvi katika maeneo ya bahari, maziwa na mito unakua endelevu, usimamizi na doria utafanyika kwa nguvu zote ili kukabiliana na uvuvi haramu. Serikali pia itaendelea kuhimiza wananchi kuanzisha ufugaji wa nyuki kwa kutumia mizinga ya kisasa, lakini pia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata mizinga ya kisasa kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuzingatie sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa mtazamo wa kibiashara zaidi na viwanda kwa lengo la kuwa na viwanda vya kisasa vya kuongeza thamani ya mazao yake. Mkazo utakuwa katika kuanzisha viwanda ambavyo sehemu kubwa ya malighafi itatoka ndani hususan kwenye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, madini na maliasili nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro ya ardhi nchini; na malalamiko katika maeneo mengi nchini yanahusu matumizi ya ardhi. Maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa ni kati ya wakulima na wafugaji, wananchi kuhodhi maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza, mipango miji na ujenzi katika maeneo ya wazi. Serikali imepokea michango mbalimbali ya Wabunge na namna bora ya kumaliza migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwahakikishia kwamba Serikali kupitia michango yenu itasimamia utekelezaji wa ushauri wenu ili tupate kupunguza migogoro iliyopo. Wizara zinazohusika zitashirikiana na wadau wa sekta ya ardhi nchini ili kubaini vyanzo vya migogoro hiyo na kuipatia ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inayo dhamira ya dhati kuona migogoro hii inakwesha. Wito wangu ni kuwa watumiaji wote nchini lazima waheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwenye matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimeona nielezee haya kwa kifupi kama njia ya kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge wote na wale wenzangu wa upinzani ambao kwa hulka yao waliamua kufanya waliyofanya, lengo letu sote ni kujenga nchi yetu na kuleta maendeleo ya nchi yetu. Tunalo jukumu la kufanya kama wadau ikiwemo Serikali. Sisi kama Wabunge na wananchi wote, tuna wajibu wa kuishauri Serikali jukumu letu ni kuwaongoza wananchi na kutekeleza yaliyomo katika hotuba ya Mheshimiwa Rais. Nawaomba sana Wabunge wenzangu wa vyama vyote vya siasa na wananchi wote nchini, kutambua wajibu wetu na kwa umoja wetu, kujenga nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sababu na wala siyo busara kubeza juhudi za kila mmoja wetu ambazo zinasaidia sana kujenga nchi yetu. Nawaomba tuunge mkono na tuungane pamoja katika juhudi za kuwaendeleza wananchi na maendeleo yao. Michango yetu na mawazo yenu ndani na nje ya Bunge ndiyo kielelezo chetu kama Wabunge wenye mtazamo wa mbele kwa Watanzania waliotupatia dhamana ya kuwaongoza na kwamba tutatekeleza wajibu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayoyafanya hapa Bungeni yawe yanalenga maslahi ya Taifa. Hivyo basi, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge hasa wenzangu wa Kambi ya Upinzani kwamba tunalo jukumu la kufanya jambo ambalo tumepewa deni na wapigakura wetu waliotuchagua, tujitahidi sana kuondoa tofauti zetu kwa maslahi ya Watanzania.
Aidha, sisi wote ni Watanzania, hivyo hatuna budi kufanya juhudi za dhati kudumisha upendo, amani, mshikamano na kusaidiana kwa masilahi ya Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wote, baada ya kusema hayo, namshukuru tena Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kunipa nafasi hii ili kusema hayo ambayo nimeyasema kufuatia michango iliyotokana na hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kupitia hotuba hii, nimeridhishwa na michango yenu na sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipa afya njema hadi leo ninapohitimisha majadiliano ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka huu wa fedha 2016/2017. Ninakushukuru sana wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Mheshimiwa Spika ambaye kwa sasa hayupo Mezani na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia kwa umakini mkubwa majadiliano ya hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwashuhukuru Waheshimiwa Mawaziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Possi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini, Makatibu Wakuu wote watatu, Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi zote za Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitumie nafasi hii pia kuwashukuru watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kunipa ushirikiano mkubwa wakati wote katika utumishi lakini pia katika kuandaa shughuli hii ambayo leo tunaihitimisha hapa mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa ujumla wenu, kwa namna ya pekee kwa michango yenu ya kina ambayo imefanikisha kwa kiasi kikubwa kuboresha mipango na kazi ambazo zimekusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kutoa majibu, maelezo mbalimbali ya wachangiaji, nitumie nafasi hii kupitia Bunge lako Tukufu kutoa pole kwa wananchi wetu waliokumbwa na maafa makubwa kule Mkoani Morogoro, Wilaya ya Kilosa lakini pia Wilaya za Rombo na Moshi Vijijini Mkoani Kilimanjaro. Taarifa si nzuri sana kwa sababu Wilayani Rombo tumeweza kupoteza kwa vifo Watanzania wenzetu wanne, Moshi Vijijini Watanzania watatu lakini pia kuna uharibufu mkubwa wa nyumba, mali, ikiwemo mashamba na vyakula. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwapa pole wote na wale ambao wametangulia mbele za haki tumwombe Mwenyezi Mungu aweke roho zao mahali pema peponi. Serikali itafanya jitihada za kuokoa wale ambao bado wamekwama na janga hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kuwapa taarifa Watanzania kwamba Taasisi yetu ya Hali ya Hewa imeendelea kutupa tahadhari kubwa kwamba kipindi kilichobaki kufikia mwanzo mwa Mei, mvua zitaendelea kunyesha kwa kasi kubwa.
Kwa hiyo basi, wale wote ambao wako maeneo hatarishi waanze kuondoka katika maeneo hayo waende maeneo salama ili kuepusha majanga yanayoweza kujitokeza tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa nimetoa salamu za shukrani pamoja na pole kwa waliopata maafa, sasa nijikite katika mjadala huu ambao ulichangiwa na jumla ya Wabunge 93; Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa maneno ni 80 na waliochangia kwa maandishi 13. Wote hawa wameweza kutoa mchango wao kwa kina kupitia bajeti yetu ambayo leo hii niko hapa kwa ajili ya kuhitimisha. Napenda niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa hoja zao nzuri. Hata hivyo, kutokana na muda, naomba nisiwataje kwa majina lakini naomba majina yao yaingizwe katika Hansard.
Serikali imejibu hoja hizo kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri lakini hoja zilizosalia zitajibiwa kwa maandishi. Aidha, na mimi nitatumia nafasi hii kutoa ufafanuzi wa hoja chache huku nikijua kwamba kwenye hotuba yangu nilizungumzia sekta mbalimbali za Wizara za Kisekta lakini pia nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba sekta zote ambazo zimechangiwa zitajibiwa vizuri na Wizara husika, mimi nitajikita kwenye maeneo ya kisera kupitia sekta hizo zote ambazo zimeweza kuzungumziwa.
Aidha, napenda nitumie nafasi hii ya awali kuwashukuru tena Wabunge wote kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, kwa utendaji wao na kasi nzuri waliyonayo katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru wote wale ambao wameonesha nia ya dhati ya kuunga mkono jitihada hizi za viongozi wetu wakuu katika kutekeleza kauli mbiu ya hapa kazi tu. Ni dhahiri kwamba wananchi wengi wamemuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais. Hivyo, ni wajibu wetu sisi kama viongozi na wawakilishi wao kuonyesha njia bora ya kutekeleza kauli mbiu hiyo na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mimi naamini kabisa kuwa mijadala yote iliyowasilishwa hapa itatusaidia sana kuwa makini zaidi katika kukidhi matarajio ya wananchi wetu katika Serikali ya Awamu ya Tano. Pongezi mlizozitoa Waheshimiwa Wabunge, zimetutia moyo sana na kutupa nguvu zaidi kama Serikali katika kuimarisha utendaji wetu katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa hoja ambazo zilitolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 99(13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016, naomba sasa nichukue nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya maeneo ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kama zilivyojitokeza. Katika ufafanuzi huu Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mawaziri walijikita kujibu hoja zilizochangiwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, sikusudii kurudia ila nataka tu niweke nyongeza ya majibu ya Mwanasheria Mkuu juu ya kipengele cha instrument. Eneo hili lina mchakato mrefu, pamoja na uwezo na mamlaka aliyonayo Mheshimiwa Rais ni kwamba Mheshimiwa Rais anaendelea kuiunda Serikali yake, alianza na Mawaziri na Makatibu Wakuu ambao ndiyo watendaji wa Serikali wameteuliwa mwanzoni mwa Januari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia lazima kuwe na utaratibu wa kila Wizara baada ya kuwa Mheshimiwa Rais ameziunganisha Wizara mbalimbali ili sasa kupata uwezo mzuri wa kuweza kutengeneza hiyo instrument ambayo taratibu zake zimeendelea. Instrument hiyo baada ya kuwa imekamilika na hawa watendaji lazima itangazwe na Gazeti la Serikali. Taratibu zote zikiwa zimeshakamilika ni lazima sasa itangazwe kwenye Gazeti la Serikali lakini utangazaji wa Gazeti la Serikali hauwi kama ilivyo kwenye magazeti yetu ya kawaida ambayo yanatangazwa kila siku, ni baada ya kuwa tumeshapata hoja za kutosha zilizo kwenye Gazeti la Serikali ndiyo unaweza kulitangaza ili wananchi waweze kuona.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwape faraja kwamba instrument za Wizara zote zimeshakamilika na zimesainiwa tarehe 20/04/2016 sasa tunasubiri kutangaza, wakati wowote Mheshimiwa Rais atakapoamua kutangaza zitakuwa zimetoka. Kwa hiyo, Mawaziri walioko kazini sasa wanafanya kazi kwa mujibu wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais lakini pia na Ilani ya Chama kinachotawala ambacho kimeunda Serikali hii. Kwa hiyo, nataka niwape faraja kwamba instrument ipo na imeshasainiwa na watendaji wetu wanafanya kazi kwa mujibu wa instrument hiyo. (Makofi)
Naomba sasa nianze na maeneo ya jumla yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na kama muda ukiruhusu nitaelezea machache pia ya kisekta kama ambavyo nimeeleza. Nianze na hoja ambayo imezungumzwa sana ya kuitaka Serikali iilipe MSD deni la shilingi bilioni 1.13 ili iweze kuendesha shughuli za kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini. Nataka nieleze kwamba taarifa iliyotolewa ya MSD kwamba Serikali inadaiwa na jumla ya shilingi bilioni 134 na siyo ile shilingi bilioni 1.34 kama ilivyokuwa imechangiwa. Hata hivyo, nataka nilipe taarifa Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeshaanza kushughulikia deni hilo kwa kumwelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhakiki deni hilo. Mpaka sasa CAG ameshahakiki madeni jumla ya shilingi bilioni 67 na kazi ya uhakiki inaendelea na malipo yatakuwa yanatoka kadri ambavyo CAG atakavyokuwa anaweza kuhakiki ili tuone madai haya na uhalisia wake. Ndiyo mkakati tulionao katika kuhakikisha deni hili la MSD linamalizika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ilikuwa ni ununuzi wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI lililochangiwa na Wabunge kadhaa pamoja na Kamati ya Bunge ya masuala ya UKIMWI. Kama nilivyoeleza katika hotuba yangu Serikali inao mpango wa kuendelea kununua dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa kutumia vyanzo vya ndani na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache Barani Afrika zinazoweza kuwanunulia wananchi dawa hizo kwa kutumia fedha zake za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanikisha mpango huo, Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya kupunguza utegemezi wa wahisani katika ununuzi wa dawa za ARV na mfuko huo unachangiwa sana na Serikali na sekta binafsi. Hivyo naziomba sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia mfuko huo. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 imeshatenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa ajili ya dawa za ARV.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni suala la vibali vya kuagiza mchele kutoka nje. Limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge, napenda pia kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya nafaka hapa nchini imeendelea kuwa nzuri kila msimu. Takwimu za uzalishaji mpunga zinaonesha uwepo ongezeko katika kipindi cha miaka sita iliyopita na takwimu zinaonesha kwamba kiasi cha uzalishaji wa mpunga kimeongezeka kwa tani 1,669,825 kutoka mwaka 2009/2010 hadi kufikia tani 1,936,000 kwa mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 14.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ambayo tunaifanya sasa Serikali ni kuhakikisha kwamba kupitia Wizara ya Kilimo tunaweka mkakati wa uzalishaji wa nafaka zaidi ili tuweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa. Ninayo matumani pia kwamba kwa sasa tunayo hifadhi ya kutosha ya chakula kwenye maghala yetu na mkakati huo unaendelea ili tuweze kuwa na akiba ya kutosha kwenye maeneo yetu. Kutokana na mwelekeo mzuri huu wa uzalishaji wa mchele hapa nchini, Serikali imesitisha kutoa vibali vya uagizaji wa mchele kutoka nje kwa lengo la kuleta unafuu lakini pia uthamani wa mchele ulioko ndani na kuimarisha masoko yaliyoko ndani kwa zao hili la mchele. Kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kwamba hatutakuwa na vibali vya kuagiza mchele kutoka nje.
Hata hivyo, napenda pia kuagiza vyombo vya dola kuendelea kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu yote hasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi ili kuzuia uingizwaji holela wa mchele wa magendo kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda wafanyabiashara na mchele ambao tunao ndani uweze kuingia kwenye masoko tunayoyakusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hili, naomba kuzungumzia suala la upungufu wa sukari nchini. Ni kweli kwamba uzalishaji wa sukari nchini upo chini ya kiwango cha mahitaji. Mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000 na kiwango cha uzalishaji nchini ni tani 320,000 na kweli tuna upungufu wa tani 100,000 na sasa hivi tumeanza kuona upungufu wa sukari.
Nataka niwaambie sukari iliyokuwepo kwenye maghala yetu na viwanda vyetu imepungua lakini tumeshaiagiza na baada ya muda mfupi kutoka sasa sukari itakuwa imeingia nchini. Sukari ambayo tumeiagiza ni ile tu iliyopungua kwa lengo la kuzuia kuingiza sukari nyingi ikadhoofisha viwanda vyetu tulivyonavyo nchini huku tukiwa tumeshaweka malengo ya uzalishaji wa ndani ya nchi ili kuweza kufikia mahitaji ya Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuwaeleza wananchi kwamba sukari itaingia baada ya muda mfupi. Nawasihi wafanyabiashara wote wenye sukari, wenye maduka, waitoe sukari waliyonayo kwa sababu takwimu tuliyonayo sasa hivi nchini tuna tani zisizopungua 37,000 ambazo tunaamini zinaendelea kuuzwa na hii itakapoingia itaweza kukamilisha na kuzuia upungufu wa sukari tulionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kauli hii, natoa agizo kwa Maafisa Biashara kwenye Halmashauri za Wilaya, wafanye ufuatiliaji kwenye maduka yetu kuona kwamba sukari haifichwi kwa lengo la kuuza kwa bei ya juu ili sukari iuzwe kwa bei elekezi ambayo imetolewa na Serikali ili wananchi waweze kupata sukari wakati wote wanaohitaji. Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba Watanzania na wafanyabiashara wote, sukari hii ambayo tunajua tunayo nchini itatolewa nje ili wananchi waweze kununua kwenye maduka yetu tena kwa bei ileile elekezi kwa sababu upungufu huo unaotamkwa hauko kwa kiwango hicho lakini hata hivyo ule upungufu ambao tunao tayari taratibu za uagizaji wa sukari umeshakamilika na wakati wowote itaingia kwenye soko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni ile hoja ya mfumo wa stakabadhi za ghala, ambao umechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na Serikali. Mfumo huu ulianzishwa kwa zao la korosho kwanza, kwa nia ya kuwawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa utaratibu wa ushindani baada ya kuyakusanya katika maghala ya Vyama vya Ushirika vilivyo kwenye maeneo yao. Hii ilikuwa inalenga kuwawezesha wakulima kupata kipato zaidi ikilinganishwa na mifumo mingi iliyokuwepo huko nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nakiri kwamba mfumo huu umeleta changamoto nyingi na malalamiko mengi. Nataka niwahakikishie Watanzania na wakulima wa zao la korosho nchini, kwamba mfumo huu ni mzuri, lakini changamoto zake ni zile ambazo zimesababishwa na Watendaji wetu, nami nikiri kwamba tunao usimamizi mbovu wa Vyama vya Ushirika (AMCOS), lakini ia usimamizi mbovu wa Vyama vyetu Vikuu pamoja na Bodi yenyewe. Vilevile uwepo wa makato holela ya hovyo, pia kunakuwa na riba za juu za mabenki yetu ambapo yote haya kwa pamoja yanapelekea mkulima kuwa na pato dogo ambalo pia wakulima wamekuwa wakilalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ambao sasa tunafanya mapitio ya mazao yetu yote makuu nchini ya kuondoa matatizo yaliyojikita kwenye maeneo haya ikiwemo kuyaondoa makato ya hovyo hovyo yaliyopo kwenye mazao haya. Kwa mfumo huu wa Stakabadhi Ghalani ambao umeanza kwenye zao la Korosho, tumebaini pamoja na upungufu niliousema ya usimamizi mbovu, lakini tuna makato tisa ambayo mkulima huwa anakatwa na yote haya yanamsababisha mkulima kupata pato dogo na hatimaye wakulima kulalamika. Mpaka sasa tumeshafanya vikao vya pamoja, Wizara pamoja na Bodi, tumekubaliana na Serikali imeondoa makato sita kati ya tisa ili kuweza kumfanya mkulima aweze kupata tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, makato tuliyoyaondoa ni gharama ya usafirishaji ya zao la mkulima kutoka nyumbani kwake mpaka kwenye maghala na kazi hiyo tumewaachia Vyama vya AMCOS vyenyewe na viko Vyama vya AMCOS vimenunua magari yao, watanunua matrekta yao, watasafirisha wenyewe kwa gharama zao wenyewe badala ya kuwakata kutoka chama kikuu cha ushirika kwa thamani ya shilingi 50. Tumesema kuanzia sasa, minada yote itafanywa kwenye maeneo ya wakulima ili wakulima wenyewe washuhudie minada yao. Badala ya kuipeleka minada eneo la mbali, linamfanya mkulima anashindwa kujua mnada uliofanywa ni wa kiasi gani na una uhalali wa kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hii itaweza kumdhihirishia mkulima kuona wanunuzi na kusikia kila mnunuzi ananunua kwa kiasi gani na watafanya maamuzi ya kuwaachia korosho au lah ili waweze kupata tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kato la pili ni ushuru wa maghala unaotozwa kule ambapo korosho zinatunzwa. Tumeondoa ushuru huu kwa sababu kila Chama cha Ushirika kimejenga ghala lake. Wakulima walishachangia ujenzi wa ghala lao na korosho zao zitatunzwa kwenye ghala lao na mnada utakaofanywa kwenye eneo lao, hautamlazimisha mkulima kukatwa shilingi 50/= ya kulipa kwenye maghala. Kwa hiyo, makato hayo tumeyaondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, makato mengine ni ya mkulima kulipa Chama Kikuu. Mkulima hana mahusiano na Chama Kikuu zaidi ya kwamba chenyewe ndiyo kinaratibu. Chama Kikuu kimeundwa na AMCOS na kwa hiyo, Chama Kikuu kitatoza mchango kwa AMCOS na kwa hiyo, Chama Kikuu hakiwezi kumtoza mkulima. Tumefuta mchango huo na badala yake fedha ile itarudi kwa mkulima ili iweze kuongeza tija yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na malipo yanalipwa Sekretarieti ya Mkoa, asilimia moja. Fedha hizi ni nyingi kwenda Mkoani, watu wa Mkoa watafanya kazi zao kwa mujibu wa ajira yao ya kufuatilia mwenendo wa zao la Korosho na wala hakuna sababu ya mkulima kuichangia Ofisi ya Mkoa shilingi moja, hiyo ilikuwa ni kupunguza mapato ya mkulima. Tumeiondoa na sasa hivi mapato haya hayatakuwepo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na makato ya unyaufu wa zao la korosho. Sheria ya Unyaufu inatekelezwa tu pale ambapo korosho itakaa zaidi ya miezi sita na siyo mwezi mmoja. Kwa hiyo, zao hili lilikuwa linakatwa asilimia 0.5 ya unyaufu ambayo tunasema sasa tumeiondoa na fedha hiyo itarudi kwa mkulima mwenyewe, tukiamini kutoka siku mkulima anapeleka ghalani mpaka siku ya mnada haiwezi kuchukua muda wa miezi sita. Kwa hiyo, makato hayo tumeyaondoa na mkulima atapata hela yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kato lingine ambalo tunaanza kuliangalia sasa ni riba ya benki ambapo AMCOS huwa zinakopa benki. Mfumo wa Stakabadhi Ghalani haulazimishi AMCOS kwenda kukopa benki. Unapokwenda kukopa benki inashawishi viongozi wa AMCOS kugawana kwanza na hawalipi na badala yake malipo hayo hulipwa na mkulima. Kwa hiyo, tunaanza kuangalia uwezekano wa AMCOS kukopa benki au mkulima apeleke mazao, asubiri siku ya mnada ili aweze kuuza apate fedha yake yote, badala ya utaratibu wa sasa wa kulipa kidogo kidogo. Wanalipa malipo ya kwanza, malipo ya pili, hiyo haitakuwepo tena kama AMCOS itapeleka mazao hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati huu unaacha malipo yafuatayo tu; mchango wa Halmashauri wa mazao wa 3% mpaka 5%; Mfuko wa Wakfu ambao tumeupa kazi ya kununua magunia na mbolea na kuhakikisha kwamba mkulima anapata pembejeo; na mkulima kuichangia AMCOS yake iliyopo kwenye eneo lake na siyo Chama Kikuu. Kwa hiyo, makato hayo ndiyo pekee ambayo mkulima sasa atakuwa anachangia na kwahiyo, tumeondoa zaidi ya shilingi 360 ambazo alikuwa anakatwa mkulima bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea na zoezi hili la kufanya mapitio ya kila zao maarufu ikiwemo la pamba, kahawa, chai pamoja na tumbaku ili kuhakikisha kwamba wakulima wa mazao haya, wanapata unafuu. Na mimi nitalisimamia mwenyewe kwa kupita kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kutoa huduma kwa wananchi na Mikoa, lakini pia kulikuwa na changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge walizionyesha kwamba Benki ya Kilimo ina mtaji mdogo ikilinganishwa na mahitaji na kwahiyo, Serikali iliombwa iweke utaratibu mzuri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba benki hii inapata unafuu wa kuweza kuhudumia wakulima nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika hotuba yangu, Serikali ilizindua Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuendeleza na kukuza shughuli za kilimo nchini. Kitaalam kilimo ni pamoja na shughuli za kilimo cha mazao, uvuvi, mifugo na maliasili, hivyo naamini kuwa hata wavuvi na wafugaji waliopo katika Jiji la Dar es Salaam, wanastahili kutumia huduma za mikopo kutoka benki hii.
Kwa mara nyingine tena niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo ili kuongezea benki hii mtaji wake; lakini bado Serikali pia imeongeza benki nyingine inaitwa TIB Maendeleo na TIB Ushirika (TID Development na TIB Corporate). Zote hizi nazo tumeziongeza kwenye mifumo ya mikopo kwa ajili ya kilimo. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wakulima wote nchini, tunayo fursa kubwa sasa kukopa kwenye Benki ya Kilimo, lakini pia na TID Development na TIB Corporate ili kuweza kuongeza mtaji wa shughuli za kilimo.
Kulikuwa na suala la hifadhi ya jamii nalo pia ni jambo ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi walichangia. Kwenye eneo hili Wabunge waliomba Sera ya Uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na kupunguza idadi ya mifuko hiyo iweze kuangaliwa tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetoa miongozo ya uwekezaji iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi ya Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Benki Kuu ya Tanzania. Aidha, kaguzi za mara kwa mara zinafanyika kuhusu uwekezaji wa mifuko hii ya jamii. Sambamba na hatua hizo, Serikali imekwishatoa maelekezo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuona namna itakavyoshiriki katika sekta ya viwanda ili kuchangia katika uchumi wa viwanda, kuongeza fursa za ajira na hatimaye kujipatia wanachama wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kupunguza idadi ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ushauri uliotolewa umepokewa na ni mzuri na tayari Serikali inakamilisha utafiti wa kina kuhusu hali ya mifuko na namna ya kupunguza idadi ya mifuko iliyopo. Kwa sasa hatua inayoendelea ni kupokea maoni ya wadau ili kuwezesha mabadiliko husika kufanyika kwa wakati muafaka. Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba mawazo yenu tutaendelea kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ilikuwa ni mchakato wa kura za maoni na Katiba Iliyopendekezwa. Ilitakiwa Serikali itoe tamko kuhusu maandalizi ya utekelezaji wa mchakato wa kura za maoni katika Katiba Iliyopendekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013 mchakato wa kura za maoni kuhusu Katiba Iliyopendekezwa unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa Tanzania Bara na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa upande wa Tanzania Zanzibar. Zoezi hilo lilipangwa kufanyika tarehe 30 Aprili, 2015 lakini likaahirishwa kwa sababu zifuatazo:-
Moja, kutokamilika kwa zoezi la kuandikisha wapigakura wakati muda wa kura ya maoni ukiwa umekaribia.
Pili, mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa ni sawasawa na mchakato wa uchaguzi, kwahiyo, Tume zisingeweza kuendesha kura ya maoni pamoja na Uchaguzi Mkuu kwa pamoja. Hivyo njia pekee ilikuwa ni kuahirisha kura ya maoni ili ikuendesha uchaguzi wa mwaka 2015 kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia haya, kwa kuwa Tume hizi mbili ndizo zilizoahirisha mchakato huo kwa sababu zilizoelezwa na pia ndizo zenye dhamana ya kuendesha zoezi hilo, napenda kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kuwa taarifa na ratiba mpya ya kura za maoni zitatolewa na Tume hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya ratiba ya uchaguzi iliyotakiwa Serikali iweke utaratibu mpya wa ratiba ya upigaji kura ili kuwezesha chaguzi zote za Rais, Wabunge, Madiwani na Serikali za Mitaa zifanyike kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nieleze tu kwamba uendeshaji wa usimamizi wa Uchaguzi Mkuu ambapo Rais, Wabunge na Madiwani ndio unawahusu na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unasimamiwa na kuratibiwa na kuendeshwa kwa sheria na mamlaka mbili tofauti kama ifuatavyo:-
Moja, uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani unasimamiwa na sheria mbili ambazo ni Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 na uchaguzi huo husimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unasimamiwa na sheria mbili ambazo ni Sheria ya Mitaa, Mamlaka ya Wilaya Sura Namba 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka za Miji Sura Namba 288. Uchaguzi huu usimamiwe na Wizara yenye dhamana na masuala ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huo uliwekwa ili kutowachanganya wananchi katika upigaji kura, kwani kwa kufanya chaguzi hizo zote kuwa pamoja, zingeweza kusababisha karatasi za kura kuwa na picha rundo au nyingi kiasi kwamba mpigakura angeshindwa kuweza kutambua kwa haraka. Pamoja na maelezo haya, Serikali imepokea mapendekezo na nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaendelea kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na suala la uhakiki wa majina ya wapigakura ya kwamba Serikali iongeze muda wa uhakiki wa majina kabla ya kupiga kura ili kuwawezesha wananchi wengi waweze kupiga kura.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekamilisha zoezi la tathmini baada ya uchaguzi (post-election evaluation) na inakamilisha uchambuzi wa tathmini hiyo na matokeo ya tathimini hiyo yatawezesha kuboresha maeneo mbalimbali likiwemo suala la uwekaji wazi daftari la kudumu la wapiga kura.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na utafiti wa wananchi ambao hawakupiga kura nalo pia lilijitokeza na Waheshimiwa Wabunge walichangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria za Uchaguzi; kujiandikisha na kupiga kura ni haki na hiyari ya mwananchi. Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanya tathmini za uchaguzi, pamoja na mambo mengine na kubaini sababu za baadhi ya maeneo wananchi kujitokeza wachache kupiga kura. Uchambuzi wa taarifa hiyo utakapokamilika, Tume itabainisha sababu ya baadhi ya wananchi kutokujitokeza kupiga kura pamoja na mapendekezo ya hatua za kuchukua ili wananchi wengi waweze kujitokeza kwenye chaguzi zijazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na mchango wa Waheshimiwa Wabunge juu ya vigezo vya kugawanya Majimbo ya Uchaguzi. Eneo hili ni kwamba vigezo vinavyotumika kugawa majimbo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ni pamoja na wastani wa idadi ya watu, hali ya kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, hali ya kijiografia, upatikanaji wa mawasiliano, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, lakini mazingira ya muungano wenyewe, uwezo wa ukumbi wa Bunge na idadi ya Viti Maalum vya Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015 Tume ilipokea maombi 77 ya kuanzishwa au kagawa majimbo ambapo Halmashauri 37 ziliwasilisha maombi ya kugawa majimbo ya uchaguzi na maombi 40 yalitoka katika Majimbo yakiomba kugawanywa. Kati ya maombi yaliyowasilishwa, maombi 35 yalikidhi vigezo na yalistahili kugawanywa.
Hata hivyo, kutokana na ongezeko la Halmashauri mpya ambazo kisheria ni majimbo ya uchaguzi, ongezeko la idadi ya Wabunge wanawake na Viti Maalum na uwezo wa ukumbi wa Bunge, Tume iliamua kutumia vigezo vitatu ili kupata idadi ya majimbo yanayoweza kugawanywa. Vigezo hivyo ni hivi hapa wastani wa idadi ya watu, mipaka ya kiutawala na uwezo wa ukumbi wetu wa Bunge kwa kutumia vigezo hivyo vitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ilianzisha Majimbo 25 kwa mchanganuo ufuatao; majimbo 19 yalitokana na ongezeko la Halmashauri mpya na majimbo sita yalitokana na kigezo cha wastani wa idadi ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia pia maombi ya kugawa majimbo katika Wilaya ya Chemba na Sumbawanga, natarajia kwamba kwa kuzingatia vigezo vilivyotajwa hapo juu, Tume itaangalia uwezekano wa kugawa majimbo hayo iwapo yanakidhi vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa sasa hatutaweza kutamka maeneo mapya ya utawala, hii ikiwemo na maombi ya Wilaya, Halmashauri hata Mikoa. Hii ni kutokana na mamlaka zile mpya ambazo tumezipa maeneo mapya bado hatujakamilisha kuzijenga na kuzipa uwezo wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwenye maeneo mapya. Baada ya kuridhika kwamba tumeshakamilisha hayo, tutawapa taarifa na jambo hili tutaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na jambo la miradi ya REA kutaka miradi ya usambazaji umeme vijijini ikamilishwe na leo nimefurahi nimemsikia Naibu Waziri hapa akitoa ufafanuzi. Kwa ufafanuzi ule, niwahakikishie tu kwamba vile vijiji vyote ambavyo vilishaingia kwenye Mpango wa REA, kazi hizo zinaendelea, lakini Awamu ya Tatu Itakapoanza vijiji vyote vilivyobaki tunatarajia vitaingia kwenye mpango ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakamilisha. Malengo yetu vijiji vyetu nchini vipate umeme na wananchi wetu wote wapate umeme wa kutosha kwenye maeneo yao. Uwezo huo tunao na tunawaahidi kwamba Serikali itakamilisha jambo hili kwenye maeneo yetu kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la uwezeshaji wananchi vijijini ambapo pia ilitakiwa Serikali iweke utaratibu wa vigezo vitakavyozingatiwa kwa wananchi kabla ya kutoa Shilingi milioni 50 zile ambazo zinaenda vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili, niseme tu kwamba mradi unalenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutenga shilingi milioni 50 kwa kila kijiji kama Mfuko wa uwezeshaji kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa katika vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni 59 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo. Ili kuwapatia mikopo wakopaji, masharti yafuatayo yatatumika katika kutekeleza mpango huu. (Makofi)
Moja, ni kikundi cha kifedha kiwe kimesajiliwa na Halmashauri na Tume ya Ushirika; pili, kikundi kiwe na Katiba, uongozi uliochaguliwa kidemokrasia na kupata mafunzo ya mikopo; tatu, kikundi kiwe chini ya asasi ya kiraia inayotambulika na yenye uzoefu wa shughuli za mikopo; nne kikundi kionyeshe uzoefu wa kukopeshana kwa muda wa mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa historia ya urejeshaji wa mikopo hiyo kwa asilimia kuanzia 95.
Pia dhamana ya Serikali itakuwa kwenye kiasi cha msingi cha mkopo na siyo kwenye kiasi ambacho kimechanganywa na riba. Sita, kikundi kitaweka amana akiba ya fedha benki katika akaunti maalum; asilimia 10 ya mkopo ndani ya kikundi, hautazidisha riba zaidi ya asilimia 11, lakini mkopo wa SACCOS itafuata Kanuni ya Sheria ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013. Kwa hiyo, ni vyema sasa Waheshimiwa Wabunge tukaendelea kuhamasisha kwenye maeneo yetu ili vikundi mbalimbali vianze kusajiliwa na viweze kuingia kwenye utaratibu huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ilikuwa ni suala la CDA kutokuwa na Sheria ya Makau Makuu, hili limejibiwa vizuri na Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama kwamba sheria imekamilika, bado taratibu zinaendelea ili kuweza kuifanya CDA sasa kuwa kwenye sheria iliyo kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo lilichangiwa ni suala la uchakavu wa meli ya MV Serengeti ya Ziwa Victoria; Waheshimiwa Wabunge hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Nataka niwahakikishie, hata nilipokuwa Mkoani Kagera niliwahakikishia wananchi kwenye mkutano wa hadhara kwamba ahadi hii ya kupata meli mpya itatekelezwa, itakayoweza kufanya safati zake kwenye Ziwa Victoria. Kwa hiyo, wananchi waendelee kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho tunaendela kuomba bajeti hapa. Na mimi nawaomba Waheshimiwa Wabunge tupitishe hii bajeti ili tuendelee kufanya kazi za Serikali ikiwemo na ahadi ambazo Mheshimiwa Rais ameahidi katika maeneo mbalimbali nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo lilikuwa limehitaji mchango lakini na majibu, ni uwepo wa Makau Makuu wa Wilaya ya Nyang‟hwale, ambapo sasa kumetokea na mkanganyiko kule. Nataka niwahakikishie Wana-Nyang‟hwale wote kwamba bado Serikali inatambua kuwa Makao Makuu ya Wilaya ni Karumwa, ambayo ilipendekezwa na ninyi wenyewe na sisi wajibu wetu sasa ni kuanda certificate au cheti kwa ajili ya kuthibitisha uwepo wa Makao Makuu hayo.
Kwa hiyo, sasa nawasihi wananchi kupitia pia Mheshimiwa Mbunge ambaye ataonana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kupata hicho cheti muweze kuendelea na shughuli za maendeleo kwenye Wilaya yenu ya Nyang‟hwale ikiwa chini ya Makao Makuu pale Karumwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ambazo zilikuwa mezani kwangu siyo nyingi na hivyo naomba nihitimishe hoja hizi kwa hayo yafuatayo kwamba, kama nilivyosema hapo awali kwamba muda hautoshi kujibu hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge, hata hivyo nirudie kusema kuwa Serikali yetu inayoongozwa na chama cha Mapinduzi, imejipanga vizuri sana katika kila sekta hasa za kiuchumi na kijamii, kuhakikisha kwamba wananchi wake wanajiletea maendeleo yao na Serikali hii itasimamia maendeleo hayo na maeneo ambayo yamekosa fursa, tutahakikisha kwamba tunapeleka fursa hizo ili wananchi waweze kwenda sambamba na hizo fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona juhudi kubwa za Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha tunakuwa na mapato ya kutosha kutuwezesha kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na hususan katika sekta ya kilimo, miundombinu, elimu, afya, nishati na madini. Wito wangu bado unabaki pale pale kwa watendaji wa Serikali walioko kwenye maeneo haya kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanatarajia Serikali hii kuwa itawapokea, itawasikiliza na kuwahudumia na jukumu hili Serikali imewapa watumishi wa Serikali ili waweze kutenda hayo kwa wananchi, wananchi waone kabisa wapo kwenye nchi yao na kwamba inawajali na inaweza kuwaletea mafanikio. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kupitia maombi yangu ya leo kwenu Waheshimiwa Wabunge ya fedha za maendeleo ambazo tunatarajia tuzipeleke kwenye maeneo yetu, tulikuwa na tatizo la upitishaji wa mikataba ya thamani ya mikataba yenyewe kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitumie nafasi hii sasa kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa kwa sasa Serikali imefanya mapitio na hasa kupitia Gazeti la Serikali Toleo Namba 121 la tarehe 24/4/2016 imepandisha kiwango cha thamani za mikataba inayopaswa kupitiwa au kuhakikiwa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kutoka shilingi milioni 50 ya awali hadi shilingi bilioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapitio ya mikataba hii ya shilingi milioni 50 imekuwa ikileta matatizo makubwa kwenye Halmashauri. Mradi mdogo wa shilingi milioni 50, mkataba uende kwa Mwanasheria Mkuu. Tumegundua kuna mrundikano mkubwa wa mikataba hii pale kwa Mwanasheria Mkuu. Sasa Serikali imefanya marekebisho, mikataba ya kwenye Halmashauri itakayotakiwa kwenda kwa Mwanasheria Mkuu ni kuanzia shilingi bilioni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, mikataba yote yenye thamani ya chini ya shilingi bilioni moja itahakikiwa na mamlaka yenyewe ya Halmashauri au taasisi husika kwa ajili ya manunuzi. Hatua hii itaharakisha kasi ya manunuzi na hivyo kasi ya maendeleo pia katika Halmashauri inaweza kufikiwa kwa haraka. Hata hivyo, Mamlaka za Ununuzi hazizuiliwi kuomba ushauri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mikataba ya kiwango cha chini ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujiridhisha tu kwamba walichofanya ndicho chenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watakaokuwa wanahakiki mikataba hiyo katika Mamlaka za Ununuzi (procure re-entities) watapaswa kuzingatia Sheria ya Ununuzi na sheria nyinginezo zinazohusu mikataba hiyo na maadili ya Wanasheria lazima yazingatiwe katika utumishi wa umma ili kulinda maadili sahihi ya namna ya upitishaji wa mikataba hii. Kinyume cha hapo, kama maadili hayataweza kutekelezwa, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wale watendaji wetu kwenye Halmashauri zote, pale ambapo mikataba hiyo itapitiwa na pia itaweza kupindishwa kwa mujibu wa taratibu hizi za Serikali zinavyotaka hatua kali itachukuliwa na hatutasita kuchukua hatua kwa wale wote ambao hawawezi kufanya hivyo. (Makofi)
Mwisho, narudia tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, kwamba tumeshirikiana katika siku hizi zote hapa tukiwa tunachangia hoja mbalimbali kutoa maoni ya utendaji bora wa mwaka wa fedha ujao kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na mimi pamoja na Mawaziri wangu, Makatibu Wakuu wangu, Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi pamoja na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Kwa kuwa pia niliomba na nilieleza pia utendaji wa Serikali kwenye Wizara nyingine zote, nataka niwahakikishie, bajeti hizi zinazoletwa kwenu ambazo naamini mtaziridhia kuzipitisha ili tuanze kazi tarehe 1 Julai, tutasimamia maadili, tutasimamia uaminifu, tutasimamia uwezo mzuri wa kitaalamu katika utendaji wa kazi za kila siku ili Watanzania waweze kupata tija ndani ya nchi yao. Na ninyi kama Wabunge mtatusaidia sana kuona mwenendo wa utendaji wa Serikali kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kwamba tutaendelea kushirikiana kwa pamoja, tutafanya hivyo bila kujali vyama vyetu, tutafanya hivyo kwa kujali maslahi ya Watanzania wote na tuendelee kushirikiana kwa pamoja, na mimi kama Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Serikali nitashirikiana nanyi kuhakikisha kwamba miradi yetu inafikiwa kwa kiwango kinachostahili. (Makofi)
Sasa basi nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa ujumla, tushirikiane kuivusha nchi yetu katika hatua tuliyonayo kiuchumi, tunahitaji kusonga mbele, kwani wananchi wetu wanahitaji maendeleo, na sisi ndio wenye jukumu la kuwaongoza wananchi wetu kufikia malengo tuliyoyatarajia. Naomba sana, nitakapokuja kuwaomba fedha mridhie ili tuanze kazi ile mnayotarajia tuifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndio ilikuwa kauli yangu ya msingi ya mwisho kwa Wabunge wenzangu ili tuweze kuungana kwa pamoja na sasa naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye rehema ambaye leo ameweza kutupa afya na kupata nafasi ya kuja kuhitimisha majadiliano ya bajeti yetu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe Watanzania kwamba leo ni siku ya kumbukumbu ya hayati Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Kwanza alizaliwa tarehe 1 Agosti, 1938 na kufariki tarehe 12 April, 1984 takribani miaka 23. Naamini Watanzania wote tutaendelea kuungana pamoja kumuombea Kiongozi wetu aliyetutangulia mbele za haki ili Mungu aweze kuiweka roho yake mahali pema, amina.
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba ya Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge UKIMWI na Kamati ya Kudumu ya Bajeti kwa michango yao mizuri kwenye hoja ambayo niliwasilisha mbele yako.
Mheshimiwa Spika, kipekee nakushukuru sana wewe mwenyewe, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa majadiliano ya hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa pamoja. Pia ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa pongezi zenu kwa Serikali na kwa michango yenye dhamira yenye kuboresha mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, mjadala huu umedhihirisha namna ambavyo Bunge linaendelea kuimarika na kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kuishauri na kuisimamia Serikali kikamilifu.
Nawashukuru tena Makatibu Wakuu wangu, Wakurugenzi, Makamishna, watumishi na watendaji wote ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa waliyoifanya kipindi chote cha bajeti hii katika kuratibu mambo yote muhimu.
Mheshimiwa Spika, mjadala huu leo ulichangiwa na Waheshimiwa Wabunge 148, ambapo Waheshimiwa Wabunge 99 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 49 wamechangia kwa njia ya maandishi. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja yangu, hata hivyo kutokana na muda naomba mridhie nisiwataje kwa majina lakini majina ninayo na ninaomba yote yaingie kwenye Hansard ili iweze kuwa kumbukumbu muhimu siku za baadae.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, leo hii niko mbele yenu hapa sasa kuja kuomba ridhaa yenu mtupitishie bajeti yetu tufanye kazi za pamoja kwenye maeneo yenu ya kuboresha maendeleo na kusimamia maendeleo na watendaji wetu walioko kule ili tuweze
kupata matarajio ambayo tumeyakusudia. Serikali imejibu hoja hizo kupitia Mawaziri pia Mwanasheria Mkuu namshukuru sana, Naibu Mawaziri na hoja zilizosalia zitajibiwa kwa maandishi.
Aidha, kama ambavyo mnajua kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo ofisi ambayo inafanya shughuli zote za Serikali kwa hiyo, mambo mengi ambayo mmekuwa mkichangia Waheshimiwa Wabunge yalikuwa yanagusa sana kwenye Wizara za kisekta na kwa hiyo, zipo hoja ambazo sitazijibu hapa lakini zitakuja kuzungumzwa kwa kina na Wizara husika ili muweze pia kupata mwelekeo wa utekelezaji wa jambo ambalo mmeshauri.
Mheshimiwa Spika, niendelee kusema tu kwamba utendaji wa jumla wa Serikali ni mzuri, kabla ya kuanza hoja za Waheshimiwa Wabunge, naomba uniruhusu nibainishe baadhi ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nianze kwa kumpongeza sana yeye Mheshimiwa Rais, Makamu wa
Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kwa namna wanavyoendelea kuiongoza nchi yetu kwa uzalendo uliotukuka na kwa dhamira njema isiyotiliwa shaka.
Mheshimiwa Spika, nina hakika Watanzania wote ni mashuhuda wa kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais pamoja na timu yake katika kuongoza nchi yetu kwa weledi mkubwa na kwa mipango iliyo imara ili kuboresha maisha ya Watanzania. Katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho nimeingia madarakani tumeushuhudia uongozi wake kuanza kwa miradi mikubwa na yenye tija kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kueleza moja kati ya hiyo kati ya mambo ambayo yalikuwa yamechangiwa ni elimu bure isiyokuwa na malipo. Chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ambapo watoto wote wa Tanzania wanapata elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kila mwezi Serikali inapeleka shilingi bilioni 18.77 kwenye shule zote za Serikali nchini. Aidha, chini ya Serikali hii kiasi cha shilingi bilioni 3.3 zinatolewa kila
mwezi kwa walimu wakuu, wakuu wa shule kama motisha ya Viongozi hao na kufanya jumla ya shilingi bilioni 22.7 kila mwezi ambazo tunazipeleka ikiwa ni utekelezaji wa eneo hili. Tunajua zipo changamoto ambazo zimejitokeza pamoja na idadi kubwa ya vijana walioandikishwa na kusababisha upungufu wa madawati.
Nataka nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Wabunge wenzangu, mlijitokeza sana baada ya Serikali kutoa wito wa kuchangia madawati kwenye shule zetu, mmetumia fedha zenu, mmetumia muda wenu, mmeshauri Halmashauri zenu kuweza kuchangia na leo hii tunaweza kusema tatizo la madawati limepungua sana kwenye shule zetu za sekondari na msingi. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, tuende pamoja kwa ajili ya maendeleo yetu.
Mheshimiwa Spika, pia sekta ya afya imeboreshwa sana sasa hivi baada ya mwaka mmoja huu. Bajeti yetu pia ime-reflect hilo, kwamba bajeti ya mwaka 2015/2016 zilitengwa shilingi bilioni 31 lakini leo hii tuna shilingi bilioni 251 ambazo zinapelekwa kwenye Halmashauri zetu na kufikia
leo hii kila Halmashauri imeshapokea zaidi ya asilimia 75 ya fedha hii ya bajeti kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwenye maeneo yetu, lakini tumeona pia ujenzi wa maduka ya madawa, mpaka sasa tumejenga maduka nane tunajenga maduka mengine katika kila mkoa ili kuweza kutoa huduma kwa karibu. Tumenunua magari ya ambulance 67 ambayo tunayapeleka kwenye vituo vya afya na tumeanza na Kanda
ya Ziwa ili kuanza kutoa huduma na kadri tunavyokuwa tunanunua tutajihakikishia kwamba tunapeleka kila Halmashauri kwenye vituo vya afya ili huduma iendelee.
Mheshimiwa Spika, tumeendelea kutoa huduma za mama na mtoto, tunajenga katika kila Halmashauri, tunaanza na Halmashauri 140 kwa kujenga wodi ya watoto, maabara ya damu, nyumba moja ya mganga na chumba cha upasuaji. Hiyo ndiyo kazi ambayo inaendelea kwa sasa
kwenye maeneo yetu. Pia jana Mheshimiwa Rais kama ambavyo mmepata kwenye vyombo vya habari ameshagawa vifaa vifuatavyo katika kila Halmashauri nchini.
Ametoa vitanda 25 kwenye kila Halmashauri, vitanda vitano kati ya hivyo ni vile ambavyo vinatumika katika kujifungulia, magodoro 25, mashuka 50 na vifaa tiba seti tano kila Halmashauri, huu ni mkakati wa kuboresha sekta ya afya.
Tutaendelea vizuri, nataka tuwahakikishie sekta ya afya pamoja na changamoto zake tutafikia hatua nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sekta ya uzalishaji, ujenzi wa reli ya kati, Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha reli ya kati kwa lengo la kurahisisha usafiri wa usafirishaji wa mizigo na abiria ndani ya nchi na sasa kupitia fedha tuliyotenga, trilioni moja, tumeanza utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, leo hii, tarehe 12 Aprili Mheshimiwa Rais ameweka jiwe la msingi saa tatu zilizopita tayari kwa ujenzi wa reli kwa kiwango cha standard gauge. Hii ni sehemu ya mkakati wa kuchochea maendeleo kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, pia kwenye ujenzi wa viwanda; leo hii tumeshasajili viwanda 2,169 nchini, viwanda hivi katika sekta mbalimbali na tunaamini kupitia michango yenu kwamba tuimarishe kilimo ili viwanda vifanye kazi ni wazo ambalo tumelichukua, tutalifanyia kazi ili viwanda vyetu viweze kufanya kazi. Bado tumefungua milango viwanda vije na tunaendelea kufanya hivyo. Mkoa wa Pwani kwa sasa unaongoza kuwa na viwanda vingi sana, tuna viwanda vikubwa 83 na vidogo zaidi ya 200. Tunatoa wito Halmashauri na mikoa zitenge maeneo kwa ajili ya viwanda, mikakati ambayo mmetushauri Waheshimiwa Wabunge tutaizingatia ili viwanda vyetu hivi tuweze kuvifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, tumeboresha sana sekta ya usafiri wa anga kama ambavyo tulieleza kwenye taarifa yangu ya awali nilipokuwa nawasilisha taarifa yangu kwamba tumenunua ndege mbili na nne zinakuja, lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaboresha usafiri wa njia ya ndege,
pia tunakamilisha Terminal III uwanja wa ndege ikiwa ni mpango wa uimarishaji wa viwanja vya ndege. Tunaendelea kukamilisha Uwanja wa Mwanza, ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA), Uwanja wa Songwe - Mbeya, vilevile Serikali inaendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege pale Geita, Tabora, Kigoma, Sumbawanga, tutajenga pia Lindi na Shinyanga.
Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ukarabati wa ujenzi wa viwanja vya ndege vya Musoma, Mtwara, Lindi na Songea. Kazi hii itaendelea kwenye viwanja ili ndege zile tulizonunua ziweze kusafiri kwenye maeneo yote ambayo tumeyataja ndani ya nchi lakini lengo letu hasa ni kuimarisha utalii wa wageni wa kutoka nje na watalii wa ndani ambao ni sisi wenyewe.
Mheshimiwa Spika, tumeimarisha pia barabara na Serikali inaendelea na kukarabati na kuboresha barabara ili kuunganisha nchi nzima. Kwa sasa tunakamilisha barabara za ngazi ya mikoa na maeneo yote sasa tunajenga barabara za ngazi ya mikoa na ninyi wote ni mashahidi, kule upande wa Magharibi, Kigoma, Kasulu mpaka Nyakanazi kazi zinaendelea, lakini pia Tabora – Kaliua kwenda kutokea Malagarasi – Uvinza kazi inaendelea, Rukwa kupitia Mpanda kwenda kutokea Uvinza kazi inaendelea, lakini pia hapa katikati Iringa – Dodoma mpaka Babati tumebakiza kilometa 20, 30 kazi inakamilika na huko Kusini tumejenga barabara kutoka Tunduru – Songea na tunakwenda mpaka Mbinga
tunashuka mpaka Mbamba bay ili kudhihirisha kwamba kazi hizi zinafanywa maeneo yote nchini, naomba mtuunge mkono ili tuendelee na tufanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamejadili sana kuhusu suala la madeni ya wakandarasi, wazabuni, watumishi na watoa huduma.
Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, hawa wakandarasi na watoa huduma wote ndugu zetu, makampuni ya nje, tunaendelea kulipa na wakandarasi wengine ambao wametoa huduma tunaendelea kuhakiki madeni yao, tunataka tuhakikishe kwamba tunalipa huduma
zote. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge muendelee kutuunga mkono ili tuhakikishe kwamba jambo hili hatupati tena lawama kutoka kwa wenzetu ambao wanatoa huduma Serikalini.
Mheshimiwa Spika, suala lingine Bunge lako tumetoa fedha, najua Waheshimiwa Wabunge walikuwa na mashaka juu ya huduma za Bunge. Bunge hili tumeliongezea fedha, shilingi bilioni 21 ili liweze kufikia tarehe 30 Juni, kwa hiyo, Bunge hili halina mashaka litafika. Lakini maombi ya bajeti mpya tumepandisha mpaka bilioni 121 ambazo pia zitafanya Bunge lijalo liweze kuendelea kwa mwaka ujao wa fedha.
Kwa hiyo, nataka niwahakikishie kwamba Serikali yetu ni sikivu, tumewasikia vilio vyenu, ushauri wenu na sasa tunatekeleza. Tunaomba ridhaa yenu leo ili fedha hii tuweze kuitoa na Bunge letu liweze kufanya kazi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kujibu hoja mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuzitoa na nianze na ya kiongozi mwenzangu, Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mbunge lakini pia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani. Najua swali lake la kwanza limejibiwa na
Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nataka niongeze pale aliposhauri kwamba sasa Serikali itoe maelekezo kwa Halmashauri ili kuongeza ajira angalau 20,000 kila mwaka katika miradi mbalimbali ndani ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, nataka kukuambia kwamba tayari natoa maelekezo na kwa maelekezo haya sasa nataka Halmashauri zote zizingatie mwongozo wa bajeti ya Serikali unaotolewa na Hazina kila mwaka unaozitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara na taasisi zote kubainisha fursa za ajira zinazotarajiwa kupatikana kila mwaka kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Vilevie mwongozo huo unazitaka sana taasisi hizo kutoa taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo ili pia na sisi tuweze kutoa taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge wajue kinachoendelea kupitia Halmashauri zao.
Mheshimiwa Spika, tulikuwa na hoja ya pili ya hali ya upatikanaji wa chakula nchini. Kama ambavyo nilisema kwenye Hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka 2017/2018 ipo ukurasa wa 21. Katika msimu wa kilimo uliopita wa mwaka 2016/2017 hali ya upatikanaji wa mvua haikuwa nzuri kwenye mikoa, hasa ile ambayo inapata mvua wakati wa vuli na hali ya mavuno katika baadhi ya maeneo hayo iliyumba kwa sababu hakukuwa na mvua za vuli, leo hii tunaendelea kupata mvua, tulichokifanya ni kusisitiza wafanyabiashara wetu wa ndani waendelee kusafirisha vyakula kutoka vinapopatikana mpaka eneo ambalo lina upungufu mkubwa na tulibaini zile Wilaya zetu 55, taratibu zinaendelea na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anasimamia upatikanaji wa chakula kwenye maeneo hayo kupitia wafanyabiashara wetu wa ndani.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa mvua zinazoendelea sasa, maeneo mengi mvua zinanyesha tujitahidi basi kupanda mazao ya muda mfupi ili yaweze kuiva katika kipindi kifupi ili msimu ujao wa mavuno tuweze kufanya tathmini, je, tumepata chakula cha kutosha, tuna upungufu wapi, ile akiba tuliyonayo tutaona namna ambavyo tunaweza tukaisambaza kwenye maeneo yetu.
Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge ambaye alitoa hoja hii, Serikali imejipanga kwa utaratibu huo na tutaisimamia kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, hoja ya tatu ilikuwa ni kuwa na mipaka mingi yenye vipenyo vingi pamoja na ukanda mrefu wa bahari ambao umefanya udhibiti wa uingizaji wa dawa za kulevya kuwa mgumu sana. Serikali imeshauriwa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa kutoa elimu kwa jamii zinazoishi mipakani ili zishirikiane na vyombo vya dola kwenye maeneo hayo ili kudhibiti hali hiyo. Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya imeshaanza kutoa elimu kwa Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo ya mipaka ya Tunduma, Kasumulo, Namanga, Horohoro na Mtukura ili kuweza kutoa elimu ya juu ya athari za dawa za kulevya kwa jamii inayoishi mipakani.
Aidha, elimu hii itatolewa kwa wananchi kadri hali inavyoruhusu ili wananchi wote kwa pamoja washiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya badala ya kuviachia vyombo vya dola peke yake. Kwa hiyo, kazi hiyo inaendelea ili tuweze kuimarisha maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kulinda watoa taarifa na pendekezo la kutaifisha mashamba ya bangi. Tatizo la dawa za kulevya ni janga kubwa, tumelizungumza mara nyingi na linaathiri sana ustawi wa nchi yetu. Serikali imedhamiria kwa dhati kabisa kupambana na mtandao wa dawa za kulevya nchini. Mafanikio katika mapambano ya dawa za kulevya yanahitaji sana ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi, hivyo napenda sana kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba watoa taarifa za wahusika wa dawa za kulevya watalindwa na wanaendelea kulindwa kwa mujibu wa sheria za kulinda watoa taarifa na mashahidi ambao wanatoa ushahidi wa kesi hizi na kwa mujibu wa sheria ile ya mwaka 2015 (Whistleblowers and Witness Protection Act, 2015).
Mheshimiwa Spika, Serikali inalipokea pendekezo hili kutaifisha mashamba ya bangi na litaendelea kutafakari utekelezaji wake vilevile. Pale ambapo tutajiridhisha kuwa adhabu hii itatosha inaweza kutoa fundisho kwa wananchi wanaojihusisha na kilimo cha bangi, Serikali haitasita kuleta Bungeni Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ili pia tuweze kupata mwongozo mwingine zaidi kutoka kwako.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya tano ya kuongeza kituo cha tiba za methadone na sober houses za Serikali angalau moja kila mkoa. Uanzishwaji wa vituo vya tiba kwa kutumia methadone unategemea ukubwa wa tatizo la matumizi ya dawa za kulevya na uwepo wa
miundombinu ya msingi katika mkoa husika. Hadi sasa kuna vituo vya methadone katika Hospitali za Muhimbili, Mwananyamala na Temeke Mkoani Dar es Salaam, vilevile Serikali inakusudia kufungua vituo kama hivyo katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani na Tanga. Kwa kuwa matibabu ya methadone yanasaidia sana watumiaji wa dawa za kulevya aina ya heroin tu pekee, Serikali inatarajia kuanzisha nyumba ya upataji nafuu (sober house) kila mkoa, huduma hii itakuwa ni kwa ajili ya kuwasaidia warahibu wengine wa aina zote za dawa za kulevya badala ya kuwaachia watu binafsi ambao mpaka sasa wanaendesha nyumba 17 za upataji nafuu nchini.
Hata hivyo, niwasihi sasa wale wote waendelee na kazi hiyo na kama wapo wadau wengine wataendelea kutuandalia nyumba za aina hiyo, tutazipokea na tutazisajili lakini Serikali inaendelea kuandaa mwongozo wenye lengo la kusimamia na kuratibu hizo nyumba zote za watu binafsi.
Mheshimiwa Spika, tulikuwa na hoja nyingine ambayo Serikali ilishauriwa iongeze vituo vya afya, vifaa tiba, wahudumu wa afya wenye weledi wa kupunguza umbali wa kupata huduma za wanaoishi na virusi vya UKIMWI; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Sera ya Maendeleo ya Afya ya Msingi inaelekeza Serikali kuboresha huduma za afya ya msingi kwa kjenga zahanati kila kijiji, kituo cha afya kila kata na Hospitali
ya Wilaya kila Wilaya.
Aidha, Serikali ina mkakati wa kuongeza idadi ya wataalam wa afya nchini kote. Jambo hili limezungumzwa na Wabunge wengi wakiuliza maendeleo ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya, zahanati na vituo vya afya. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kadri
tunavyopata fedha na kuzitenga katika bajeti tutaendelea pia kuhamasisha wananchi kuanzisha miradi ya ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na Serikali itaendelea kuunga mkono kwa lengo la kila kijiji kuwa na zahanati yake, kila kata iwe na kituo cha afya na Wilaya ziweze kuwa na Hospitali za Wilaya na yale majukumu yote ya Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI yataendelea kuimarishwa ili maeneo yote yawe
yanapata huduma ikiwemo na uwepo wa watumishi wa afya. (Makofi)
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ushauri wenu kwenye eneo hili tumeupokea, nataka niwahakikishie kwamba tutaufanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine ambayo inataka Serikali itoe elimu ya kujikinga na VVU kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo elimu kwa njia ya sinema na kuanzisha vilabu vya mapambano dhidi ya VVU katika shule zote kuanzia msingi hadi sekondari na kuandaa mitaala ya elimu ya UKIMWI katika ngazi zote za elimu ya msingi hadi Vyuo Vikuu. Nia ya Serikali katika hili ni kuona elimu ya UKIMWI
inawafikia wote wanaostahili nchini. Serikali ina magari ya sinema katika mikoa yote 20 ya Tanzania Bara ambayo pia hutoa elimu ya UKIMWI kwa njia ya sinema. Mkakati tulionao sasa pia na mikoa mitano ya Tanzania Visiwani nayo itapata magari ya sinema ili kuendelea kutoa huduma nchini kote.
Wizara ya Elimu kwa pamoja na Wizara ya Elimu ya Zanzibar imetoa mitaala kufundisha wanafunzi kuhusiana na elimu ya UKIMWI kwenye shule zetu. Serikali inatoa wito pia kwa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuyatumia ipasavyo magari hayo na kuhakikisha kwamba walimu wapya wanapitishwa vema katika mitaala hiyo pamoja na kuanzisha clubs za kuhamasisha mapambano
dhidi ya UKIMWI katika shule, vyuo vyote nchini na mahali pote ambapo kuna mikusanyiko ya watu.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na ushauri unaosema Serikali ibuni chanzo mahsusi cha kutunisha Mfuko wa UKIMWI (Aids Trust Fund) kama ilivyo kwa mifuko mingine mfano REA na maji ili kufanikisha mapambano dhidi ya UKIMWI. Kupitia Bunge lako napenda kuwahakikishia kwamba ushauri huu uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge umepokelewa na Serikali itaufanyia kazi. Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba
mfuko huu tukiuanzisha, tukiutunisha huduma zote zinaweza kuwafikia mpaka walioko vijijini, kwa hiyo, jambo hili Waheshimiwa Wabunge tumelipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulikuwa na hoja pia ya kuweka utaratibu wa kufuatilia fedha zinazotolewa na wafadhili kwenye Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali zinazojihusisha na masuala ya UKIMWI. Utaratibu wa kufuatilia fedha zinazotolewa kwenye NGO’s upo na tumekuwa tukisisitiza
ufuatwe vizuri. Mathalani nilipofanya ziara mkoani Arusha hivi karibuni nilirudia wito wa kuzifanyia kaguzi za mara kwa mara NGO’s zinazofanya kazi nchini. Hivyo, ushauri wangu wa Kamati kuhusu hitaji la kufanya ukaguzi kwenye NGOs zinazoshughulikia UKIMWI utaendelea kuzingatiwa kama ambavyo tumetoa maelekezo. Natoa wito kwa wakurugenzi wote wa Halmashauri zetu za Wilaya nchini waendelee
kuhakikisha wadau wa UKIMWI wanaofanya kazi kwenye maeneo yao wanakaguliwa kulingana na Sheria ya UKIMWI ya mwaka 2008 na Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002, ili tuweze kujiridhisha wanapata nini kwa ajili ya huduma gani, kiasi gani kinatumika ili wanufaika waweze kuridhika kwenye huduma hii.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilikuwa imetolewa na Waheshimiwa Wabunge ni juu ya Serikali kujiridhisha kuhusu masuala ya kitaalam ya kufanya mapitio na maboresho ya sheria stahiki katika kutekeleza mpango wa kuunganisha mifuko ya pensheni; hili limezungumzwa vizuri sana na Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Jenista Mhagama.
Lakini zoezi la kuunganisha mifuko ya pensheni linafanyika kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam. Katika kutekeleza jukumu hilo mifuko yote ya pensheni imefanyiwa tathmini ambayo pamoja na mambo mengine imebainisha kuwa kuunganisha mifuko ya pensheni ndiyo njia bora ya kuimarisha sekta ya hifadhi ya jamii nchini.
Aidha, Serikali imeandaa andiko la mapendekezo ya kuuunganisha mifuko, kazi hii imefanyika kwa kushirikisha wadau muhimu katika sekta husika. Serikali itaendelea kutoa taarifa za mara kwa mara juu ya hatua iliyofikiwa kwenye mpango huo wa kuunganisha mifuko.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na ushauri mwingine kwamba mifuko ya hifadhi ya jamii inayojishughulisha kuwekeza kwenye uchumi iweze kuendelea na uwekezaji huo hasa kwenye maeneo ya viwanda. Uwekezaji ni kazi mojawapo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na lengo la
uwezeshaji ni kulinda thamani ya michango ya mwanachama pamoja na kukuza uwezo wa mifuko, kupitia na kulipa mafao kwa wanachama wake pamoja na wanapopatwa na majanga mbalimbali yanayowasababishia kukosa kipato. Majanga hayo ni kama vile maradhi, uzee na kifo, kwa msingi huo uwekezaji kwenye viwanda unavyofanywa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii sasa una manufaa makubwa sana kwani pamoja na kulinda thamani ya fedha za michango ya wanachama, uwekezaji huu unakuza mapato ya Serikali, unatoa fursa za ajira na hivyo kusaidia kuongeza idadi ya wanachama watakaoweza kuongeza michango yao kwenye mfuko husika.
Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Serikali kwa pamoja vitaendelea kuhakikisha kwamba uwekezaji unaofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii unazingatia miongozo ya uwekezaji ili mifuko hiyo isiweze kupata hasara kubwa, tunashukuru jambo hili linaendelea
na tutakuja kuwapa mrejesho.
Mheshimiwa Spika, tulikuwa na hoja ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na utoaji wa elimu ya kupiga kura. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inayo jukumu la kuboresha daftari la kudumu la kupiga kura. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaweka kipaumbele katika uboreshaji wa daftari la wapiga kura na Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa jukumu la kutoa elimu ya mpiga kura nchini kote na kusimamia na kuratibu asasi, taasisi na watu wanaotoa elimu kwa mpiga kura. Tume pia imeendelea kutoa elimu ya mpiga kura kwa njia mbalimbali ikiwemo kutumia redio, television, kukutana na wadau,
kupitia maonyesho mbalimbali pamoja na kushiriki mikutano katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, iko hoja ambayo ilizungumzia suala la mgogoro wa uongozi ndani ya Chama cha CUF.
Jambo hili limezungumzwa kwa hisia kali na sisi tumelipokea lakini nataka niseme tu kwamba hoja hii kwa namna ambavyo imejadiliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wameweza kuijadili sana. Serikali haifurahishwi na migogoro ndani ya vyama vya siasa kwani inadumaza demokrasia nchini na kusababisha mifarakano isiyokuwa na tija. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kama mlezi wa vyama vya siasa imekuwa ikishiriki sana kikamilifu katika kuhakikisha kwamba migogoro ndani ya vyama vya sisa inatatuliwa kwa majadiliano.
Mheshimiwa Spika, katika hili mgogoro uliopo ndani ya Chama cha CUF, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilitoa ushauri kulingana na taratibu zilizopo, hata hivyo wakati usuluhishi ukiendelea, baadhi ya wanachama wa CUF ambao hawakuridhika na usuluhishi uliofanywa na Msajili walipeleka shauri Mahakamani ili kudai haki yao kwenye mhimili ya Mahakama ikiwa ni pamoja na suala la ruzuku ambalo Mahakama imetoa zuio la muda mpaka shauri la msingi lililoko Mahakamani litakapotolewa uamuzi. Kwa kuwa masuala haya yapo Mahakamani na kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge mnataka jambo hili lingepata nafasi ya kuzungumzwa basi ni vizuri tukaiacha Mahakama ifanye kazi yake halafu tuje tulizungumze. Hiyo ni rai yangu na namna nzuri ya kuweza kutatua mgogoro (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu kwa jambo ambalo limezungumzwa sana hapa ndani, suala la
usalama na kutokuwa na uhakika wetu Waheshimiwa Wabunge. Jambo hili kama ambavyo Mwanasheria amelieleza, Serikali inalifanyia kazi na hapo baadae tutakuja kutoa taarifa ya Serikali kwenu kwa sasa tunawasihi Waheshimiwa Wabunge tuache vyombo vyetu vifanye kazi, vifuatilie ni nini hiki kinaendela, nani anaendelea nacho, malengo ni nini ili tuje tujiridhishe kama je, matendo haya yanayozagaa huko ni matendo ambayo yanakubalika?
Kimsingi hayakubaliki, lakini taarifa rasmi tutakuja kuileta Bungeni Waheshimiwa Wabunge wenzangu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa leo ulinipunguzia muda na niliona nitumie muda huu kuzungumza haya machache, nashukuru nimefika mwisho wa maelezo yangu ili nirudi tena kwa Waheshimiwa Wabunge kuomba ridhaa yao ya fedha tuweze kutekeleza na yale ambayo mliyasema ambayo sijayajibu lakini nina uhakika kwa maelekezo ninayoyatoa kwa Wizara ni lazima waje wafafanue vizuri ya hoja zote ambazo mlizitoa Waheshimiwa Wabunge ili tupate mwelekeo. Nataka niwahakikishie kwamba ushauri wenu tumeuchukua ili tuufanyie kazi katika kipindi cha mwaka mmoja wa fedha kinachokuja baada ya ninyi kuridhia maombi yetu ambayo tunayo hapa.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo awali,muda usingeweza kutosha kujibu hoja zote zilizotolewa, Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja, tumejifunza mengi sana kutoka kwenu, kwenye kupitia michango yenu na tuko tayari kuendelea kujifunza zaidi kutoka kwenu Waheshimiwa Wabunge na ni jukumu letu kuwasikiliza na kupokea ushauri wenu.
Mheshimiwa Spika, nchi hii ni yetu sote na kila mmoja wetu anaowajibu wa kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu, kila mchango wa Mheshimiwa Mbunge una thamani kubwa sana kwetu na ninawashukuru sana kwa ushauri, maangalizo na mafunzo mliyotupa.
Nataka niwahakikishie ushauri huu wakati mwingine tunautekeleza tunapokuja kwenye Majimbo yenu, nitaendelea na ziara zangu kwenye maeneo yenu ili kutekeleza na haya ambayo mmetushauri. Bado tuko pamoja, nataka niwahakikishie ushirikiano ambao tutawapa wakati
wote katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao. Endeleeni kutoa ushauri kwa Serikali hata kwa maandishi tu wakati wowote siyo lazima Bungeni, popote ili tuweze kufikia hatua nzuri ya maendeleo, na sisi tutapokea ushauri huo na kuona namna bora ya kuufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania mkiwemo Waheshimiwa Wabunge mnawajibika kuiacha Tanzania ikiwa ni nchi bora zaidi ya tulivyoikuta. Ili kuifikisha azma hiyo inabidi tuanze kuwa tayari kujinyima mambo mazuri tuliyoyazoea angalau kwa muda ili kuimarisha misingi ya ujenzi wa
Tanzania yetu. Ninawasihi sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu muielewe dhamira ya Serikali na mtuamini katika kusimamia rasilimali ya nchi yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo. Serikali imejipanga vizuri katika kulinda maslahi ya nchi hii na wananchi wake. Hivyo nawaomba muendelee kutuunga mkono kwa kupitisha bajeti yetu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo leo hii iko mbele yenu na tunaomba ridhaa
yenu ili tufanye kazi kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapohitimisha hoja yangu tena katika siku ambayo Taifa letu kama ambavyo nimeeleza ninalazimika kuwakumbusha Watanzania wote tuendelee kumuenzi mpambanaji huyo wa haki za wanyonge kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za
kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Tumuombe tena Mwenyezi Mungu aendelee kumpumzisha Hayati Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu Awamu ya Tatu. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, amin.
Mheshimiwa Spika, nirudie tena kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu, niko chini yenu kuomba ridhaa yenu kwenye mpango ambao tutauleta.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba kutoa hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza sina budi kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya njema hadi leo ninaposimama katika kikao hiki cha sita cha Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge lako hili Tukufu kwa ajili ya kuhitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2018/ 2019. Naungana na wenzangu walionitangulia kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameendelea kukupa afya njema na kurudi hapa kuendelea na kazi yako ya kuongoza Bunge hili Tukufu Mungu ni mkubwa na aendelee kukupa afya njema zaidi. (Makofi)
Aidha, nikushukuru sana wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kuendelea kusimamia Bunge hili kwa michango iliyotolewa Waheshimiwa Wabunge, majadiliano na hasa hoja ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii pia kuwashukuru Wenyeviti na Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI kwa taarifa nzuri walizoziwasilisha maoni na ushauri waliotoa kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa majikumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge.
Vilevile nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa pongezi maoni, ushauri na hoja mbalimbali mlizozitoa wakati wa kuchangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa Serikali hii ya Awamu ya Tano imepokea kwa mikono miwili pongezi zenu na michango yenu ambayo naamini itakuwa chachu ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa naomba niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa kisekta kwa maelezo ya ufafanuzi waliyoyatoa kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Jenista Johakimu Mhagama (Mbunge) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Antony Peter Mavunde (Mbunge) Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Vijana na Mheshimiwa Stella Alex Ikupa, (Mbunge) Naibu Waziri watu wenye Ulemavu kwa maelezo mazuri wakati wa kufafanua hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge zilizoelekezwa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie pia fursa hii kuwapongeza sana Makatibu Wakuu wangu Mama Maimuna Tarishi, Profesa Kamuzora na Bwana Eric Shitindi kwa pamoja na Wenyeviti wa Tume wa Uchaguzi, Tume ya TACAIDS, Kamishina Jenerali, Madawa ya Kulevya, Msajili wa Vyama vya Siasa, Wakurugenzi wote na watendaji wote walio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ya uratibu wa hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge ambazo sasa tumeanza kuzijibu.
Mheshimiwa Spika, katika mjadala huu uliotumia siku tano Waheshimiwa Wabunge 124 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 50 walichangia kwa njia ya maandishi.
Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote mliochangia hoja yangu, hata hivyo kutokana na muda kutokuwa rafiki sana naomba nisiwataje kwa majina, lakini naomba majina yote ya Waheshimiwa Wabunge yaingizwe katika Hansard na ninayo hapa.
Mheshimiwa Spika, wakati wa kuchangia hoja Waheshimiwa Wabunge wengi wanakiri na kupongeza mafanikio yaliyopatikana kutokana nautendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo napenda nitumie nafasi hii ya awali kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein Rais wa Serikali za Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Naendelea kutoa rai kwa viongozi na watendaji kuendelea kuifanyia kazi na kutekeleza kwa dhati falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosema hapa kazi tu. Kwa mantiki hiyo viongozi, watendaji na wawakilishi tunaowajibu mkubwa sana wa kuwatumikia wananchi kwa kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia kama namna bora kabisa ya kutekeleza falsafa hiyo ya Mheshimwia Rais na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pongezi mlizozitoa Waheshimiwa Wabunge kwa hakika si tu zimetutia moyo na kutupa nguvu zaidi ya kusonga mbele, bali pia zinatoa mwelekeo mzuri hususani pale zinapoainisha mafanikio muhimu ya kitaifa na kimataifa ambayo yamepatikana ndani ya kipindi cha takribani miaka miwili na nusu ya utendaji wa Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na michango maoni ushauri napongezi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge naomba uridhie nitoe maelezo ya jumla kwa maeneo yafuatayo ambayo baadhi yetu walihitaji kujua faida za kwa nini tumetumia fedha kutekeleza miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, mradi wa kwanza ni ule mradi wa usimikaji wa mfumo wa rada. Mnamo tarehe 2 Aprili, 2018 Mheshimiwa Rais alizindua mradi wa usimikaji mfumo wa rada nne kwa ajili ya kuongoza ndege kwenye viwanja vyetu hapa nchini ambavyo ni vinne; uwanja wa Julius Kambarage Nyerere - Dar es Salaam, uwanja wa KIA kule Kilimanjaro, uwanja wa Mwanza na uwanja wa Songwe kule Mkoani Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, miradi hii yote imegharimu jumla ya shilingi bilioni 67.3. Hivi sasa nchi yetu rada moja tu ya kiraia iliyoko kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Saalam ambayo uwezo wake wa kuona ndege ni asilimia 25 tu ya eneo ambalo linatakiwa kuona ndege. Aidha, uwezo wa rada hiyo ambayo ilinunuliwa mwaka 2002 ili itumike kwa miaka 12 kwa sasa imepungua uwezo wake kutokana na uchakavu ulionayo. Hali hiyo imesababisha baadhi ya mashirika ya ndege nchini kuhairisha kuja Tanzania kwa sababu hayaonwi, hakuna mawasiliano moja kwa moja na mahali petu Dar es Salaam, kwa maana Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mradi huu wa rada ni sehemu ya mipango ya Serikali ya kuimarisha usafiri wa anga nchini na ambao utakuwa na manufaa mwengi kwa Taifa letu. Miongoni mwa manufaa hayo sasa ni kuimarisha usalama wa nchi yetu kwa kuongeza uwezo wa kuhudumia anga yetu kutoka asilimia 25 ya sasa mpaka asilimia100 pindi zitakapokamilika na kuanza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nataka tuanze kurejesha imani na mashirika ya ndege ambayo yaliahirisha kuingia nchini hiyo pia ni jambo muhimu. Lakini nataka turahisishe pia shughuli za kuongoza ndege zinazoingia hapa nchini kwa kuongeza pia mapato ya nchi yetu kutokana na tozo ambazo tutakuwa tunatoza kwa ndege zile kuingia na kuhudumiwa na rada zetu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge hiyo ilikuwa ni faida za kwa nini mradi ule tumeutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mradi wa pili ni kufufua Shirika la Ndege la Tanzania, ununuzi wa ndege hizi ni mipango ya Serikali ya kufufua shirika letu la ndege ambalo lilishakufa kabisa. Kama tulivyoshuhudia tarehe 2 Aprili, 2018 Mheshimiwa Rais akiongoza wana Dar es Salaam kwa niaba ya Watanzania kupokea ndege yetu ya tatu aina ya Bombardier Dash 8 Q400. Ni mwelekeo wa kulifufua shirika letu ambako sasa Serikali tumenunua ndege sita, ndege tatu zimeshaingia ndege tatu zingine zitaingia ambazo tunataka zitoe huduma ndani na nje ya nchi kwa lengo la kukuza na kama kichocheo cha ujenzi wa uchumi wa viwanda hususani viwanda vya usindikaji wa mazao kama vile matunda, usafirishaji wa maua, mbogamboga, samaki, na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, aidha, usafiri imara wa anga na wenye uhakikia utasaidia sana kukuza sekta ya maliasili na utalii. Kama ambavyo mnafahamu Watanzania wote kwamba watalii wengi zaidi ya asilimia 70 wanatumia usafiri wa ndege kuingia nchini na nchi yetu ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kuwa na vivutio vingi ambavyo watalii wanavipenda sana. Kwa hiyo, tunataka moja kati ya malengo ni kuongeza idadi ya watalii nchini kutoka watalii milioni 1.3 ya sasa na ikiwezekana kuifikia milioni tano ifikapo mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nataka tuimarishe usafiri wa anga ndani ya nchi na ndiyo sababu sasa tunajenga viwanja vingi vya ndege katika kila mkoa ili kuwezesha ndege zetu kutua kila mkoa na kuweza kusafirisha vile ambao watakuwa wanaweza kusafiri. Lakini pia tunataka tufungue fursa za utalii kwenye mikoa hiyo ili watalii wetu waweze kusafiri kwa ndege wafike kwenye maeneo yetu, tuna vivutio vingi; Kigoma tuna eneo la sokwe ambako sasa wanaanza kufika kwa sababu ndege inakwenda sasa mpaka Kigoma na maeneo mengine mengi ambayo yana vivutio vya aina hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hili tunataka tukuze sekta nyingine ambazo zinahitaji usafiri wa ndege sekta ya kilimo lakini sekta ya mifugo, uvuvi. Lakini pia nataka tuongeze ajira nyingi ili wengine wafanye kazi kwenye shirika letu la ndege kwa kupitia maeneno yote ambayo tuliyonayo. Kwa hiyo, mradi wa ufufuaji wa shirika la ndege ulikuwa na malengo hayo kwa kifupi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, uko mradi mwingine wa kuanzisha uzalishaji wa umeme kwa wingi hii imetolewa maelezo mazuri sana na Waziri wa Nishati kwa nini tunaanzisha vyanzo vingi vya kuzalisha umeme na vyanzo hivi ni vingi tunataka kwenye maji, kwenye gesi asilia lakini kwenye upepo kwa kutumia hata pia takataka, uko uwekezaji unakuja muda mfupi wa kutumia takataka zetu kuzalisha umeme.
Mheshimiwa Spika, malengo yetu ni kupata umeme wa kutosha ili sasa uende sambamba na matakwa yetu ya kuboresha viwanda nchini ambavyo vitakuwa vinaendeshwa na umeme. Lakini pamoja na hiyo tunataka pia tuhakishe kwamba tunasambaza umeme tunapata umeme wa kutosha ili miradi yetu ya usambazaji wa umeme kwenda vijijini tupeleke umeme wa kutosha, umeme wa uhakika na umeme ambao tutakuwa tunajiridhisha kwamba tunao tunaweza pia kutumia umeme huo kwa wajasiliamali kutengeneza ajira nyingi hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia utatupatia mapato ya Serikali kupitia tozo hizo kidogo ambazo tutakuwa tunazipata kutokana na matumizi ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nieleze kwa kifupi sana kuhusu ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme ambao toka mwaka 1970 ndiyo ulikuwa umebuniwa na hakukua na mafanikio lakini azima yetu ya kuboresha eneo hili ndiyo kwa sababu tumeamua tutumie bonde lile la Mto Rufiji au maporomoko ya Mto Rufiji kuwa ndiyo maeneo ya kuzalishia umeme mwingi wa kutosha. Eneo hili tukishalianzisha kama alivyosema Mheshimiwa Waziri tutaongeza kiwango cha maji ambacho wanyama wetu kule msituni wataweza kutumia vizuri, lakini pia itasaidia kwenye umwagiliaji kwenye miji ambako watu wanaishi uko Ikwiriri na maeneo mengine ya Wilayani Rufiji na eneo lote linalopita mto huo pamoja na kuongeza mazalia ya samaki ambayo pia tunayo, na kuongeza sasa ubora wa hifadhi yetu ya Selous ambayo pia itakuwa inaembelewa na watalii wengi na maeneo haya yatakuwa ni kivutio. Kwa hiyo, miradi hii ikiwemo na huu wa maporomoko ya Mto Rufiji malengo yetu hasa ni hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna mradi mwingine ambao Waheshimiwa Wabunge walitaka kujua unafaida gani, ujenzi wa reli ya kisasa. Hatuna ubishi kwenye ujenzi wa reli ya kisasa kwamba reli hii kwa miaka mingi ilikuwa inapoteza uwezo wake lakini sasa kwa kuanzisha mradi huu wa reli ya kimataifa (standard gauge) utaweza kusafirisha mizigo na abiria kwa haraka zaidi na kwa sababu tunatumia umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia kupitia mradi huu ambao tulitaka tujenge kwa kilometa 1219 utaweza kurahisisha pia kufanya biashara ya uhakika na nchi jirani kama Rwanda, Congo, Burundi na nchi yoyote ile ambayo itahitaji kutumia reli yetu kusafirisha mizigo yake. Kwa hiyo, tunauhakika kwamba kupitia reli hii tutaweza kupata fedha kupitia tozo mbalimbali za watumiaji wa reli hiyo kutoka nje ya nchi na ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia mnafahamu kwamba tunayo reli ambayo sasa inatumika tunaendelea kuiboresha ili iendelee kutoa huduma kwa sasa mpaka hapo tukapofanya mabadiliko na tunaendelea kupanua wigo kwa kuipeleka Tanga, tunaboresha kutoka Segera mpaka Arusha na kupitia Moshi na tunaendelea pia kuijenga/kuidumisha reli hiyo kutoka Tabora kuelekea Mpanda; na sasa nataka tuende mpaka Ziwa Tanganyika kule mpakani kabisa ili iendelee kutoa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapoanza sasa reli hii mpya itakuwa na uwezo wa kubeba mizigo zaidi ya tani 10,000 sawa na malori 250 ya tani 40/40 ambayo tutaondoa kwenye barabara. Kwa hiyo, faida nyingine kwamba tunataka tuimarishe barabara yetu iweze kutumika muda mrefu ili pia iweze kutumika na wengi. Lakini pia kupitia mradi huu sasa tunazalisha ajira za kutiosha ambazo tumeanza kuona Watanzania wengi wakienda kupata ajira na utakapokamilika tunatarajia takribani ajira 30,000 za moja kwa moja na nyingine 600 kwa ajili ya wajenzi, walinzi na sekta zote ambazo zinahitaji kuhudumia njia hiyo ya reli.
Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao Waheshimiwa Wabunge walihitaji kujua kwa nini tumeutekeleza, ni ukuta kuzunguka Mradi wa Mererani.
Mheshimiwa Spika, wote mnajua kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuhakikisha kuwa inalinda raslimali zetu, maliasili na madini. Ujenzi huu ambao umeshakamilika na umezinduliwa utasaidia sana kuhifadhi kulinda na maliasili ambazo ziko pale na Mheshimiwa Rais amefanya hili ilikuwa ni azma na hasa alidhamiria kufanya hivyo pale alipofanya ziara Mkoani Manyara na alikuwa anazindua barabara kutoka KIA kwenda Mererani na alipopata malamiko akaona ni muhimu sasa hayatekeleze.
Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie ukuta huo wa kilometa 24.5 ambao umekamilika sasa utawezesha sasa mali zote kuzitambua pale ndani. Na ikumbukwe kwamba kabla ya ujenzi inakadiliwa kuwa kwa mujibu wa taarifa za Wataalam wetu inakadiliwa kuwa zaidi ya asilimia 40 ya uzalishaji ilikuwa inapotea tulikuwa hatuna manufaa nayo. Kwa hiyo, madini yetu ya Tanzanite sasa tunauhakika kwamba tunaweza kuyadhibiti na tukapata mapato yanayokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushahidi katika kipindi hiki kifupi ambacho tumeweka utaratibu wa ulinzi na huku ukuta unajengwa kuanzia Januari mpaka mwezi Machi, 2018 tumeingiza pato la milioni 714 kwa miezi mitatu tu ukilinganisha na pato ambalo tumelipata kuanzia Januari mapaka Disemba ya mwaka 2017 la milioni 147.1. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo muone namna ambavyo tulikuwa tunapoteza fedha nyingi na sasa ambavyo tunatarajia kupata pia fedha. Kwa hiyo, ukuta huu unafaida sana na tutaendelea kuimarsha na katika kuboresha tmeridhia ukuta ule na Mheshimiwa Rais ameridhia tumekaribisha Watanzania na wale wachimbaji na yoyote ambaye yuko kule jirani kuweka uwekezaji kule ndani, tutakuwa na maduka na nyumba ambazo za kupumuzika ili eneo lile kulifanya kuwa eneo la kivutio tutakuwa na nyumba za kufanyia mauzo ya hiyo Tanzanite kwenye eneo ambalo litakuwa kidogo linapandisha uchumi hata wenyeji wetu wa pale Mererani nao wataweza kunufaika na ujenzi wa ukuta huu wa pale Mererani.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na issue ya utambuzi wa mifugo, wengi walipoona kwenye risala yetu hawakuelewa tulikuwa tunalenga nini.
Waheshimiwa Wabunge, wote mnajua kwamba nchi yetu iliingia kwenye migogoro mingi sana ya wakulima na wafugaji na kukawa na ongezeko kubwa sana la mifugo nchini na mifugo mingine ilikuwa inatoka nje kuja kulisha ndani na kurudi nje ambayo sisi ilikuwa haitupi tija. Kwa hiyo, ili kudhibiti pia hata maliasili zetu zitumike na watanzania wenyewe kwanza, zoezi la kutambua mifugo maana yake linatuwezesha kutambua tuna mifugo mingapi, wapi na inamilikiwa na nani ili pia tuweze kuipangia utaratibu mzuri wa malisho wa namna nzuri ya huduma ya madawa lakini na huduma nyingine ikiwemo na jitihada tunazozifanya sasa za ujenzi wa viwanda ambavyo vitataka Watanzania wanufaike kupeleka ng’ombe, wauze, wapate fedha za kutosha ili waweze kujiendesha maisha yao. (Makofi)
Kwa hiyo, zoezi hili tumeendelea, lina faida nyingi na nawasihi tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuendelee kushirikiana ili tukomeshe mauaji ya wakulima na wafugaji ambayo kwa sasa kumetulia kidogo na tungependa utulivu huu uendelee kwa kutokana na zoezi hili ambalo tunaendelea nalo.
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge niseme tumepata faraja sana kuona utulivu huu, mauaji tena ya wakulima na wafugaji yamepungua na tutaendelea kuyadhibiti kadri ambavyo tutaweza kulisimamia zoezi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kujibu hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge nao pia waliweza kuzieleza na sisi tulizichukua sasa ni muhimu kuzitolea majibu na baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa Serikali zimejibiwa na Waheshimiwa Mawaziri wa kisekta, lakini Naibu Mawaziri nao wamejibu na zile hoja zilizosalia zitajibiwa kama ambavyo tumeendelea, ziko nyingine ambazo tutazijibu kwa maandishi na hoja ambazo pia zina mwelekeo wa kisekta zitatolewa ufafanuzi na baadhi ya Wizara ambazo zitakuja hapa kuja kuwasilisha bajeti zake na tayari tumewaagiza maswali yote na hoja zenu zote waziweke ili waje wazitolee majibu wakati wa hoja zao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la mwaka 2016 naomba sasa nitumie fursa hii ili kujibu sambamba na kutolea ufafanuzi kuhusu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo zimetolewa.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walitaka Serikali kudhibiti zabuni za ujenzi wa miradi ya maendeleo kwamba zabuni hizi za ujenzi wa miradi ya maendeleo zitolewe kwa uwazi. Lakini kipaumbele kitolewe kwa makampuni ya ndani ya nchi ya wakandarasi yanayokidhi vigezo na uwezo wa kutekeleza, kukamilisha miradi kwa wakati na kwa mujibu wa mikataba ya miradi husika.
Mhesghimiwa Spika, nataka nieleze kwa Watanzania kwamba tumeimarisha utoaji wa zabuni. Zabuni zetu zinatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 ambayo wote wanapata zabuni zile ni wale wenye makampuni yaliyosajiliwa, yana sifa zote na yana uwezo wa kutekeleza miradi na zabuni hizi ni za wazi na mara nyingi tunashindanisha kwa makampuni ambayo yanahitaji kuomba nafasi hizo. Lakini pia tumeanza kutoa mwongozo wa ushirikishwaji wa Watanzania ili kupata zabuni zile (local content). Kwa hiyo, tuna uhakika sasa kwa utaratibu tuliojiwekea Watanzania wenye makampuni wataendelea kunufaika na zabuni za ndani ili pia waweze kufanya kazi za ndani tuweze kuwajengea uwezo wa kufanya kazi hizo na kuongeza kazi nyingi zaidi.
Mheshimiwa Spika, na tumeanza kushuhudia makampuni mengi ya Kitanzania yakifanya kazi hizo, lakini pia hata Serikali imetoa nafasi ya kuzungumza na private sectors (sekta binafsi) ili kusikia changamoto wanazozikabili na sisi kuwaambia yale ambayo wanatakiwa waboreshe ili tuendelee pia kuimarisha kwenye maeneo hayo. Lengo letu la kukutana nao ni kutaka tu kuhakikisha kwamba na wao wananufaika na zabuni za ndani ya nchi ili fedha ambayo inalipwa iendelee kubaki nchini na pale ambapo inabidi kupata makampuni ya nje mara chache ndiyo wanaweza kupata nafasi kwa kadri ya ushindani utakavyojitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ambayo Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI iliitoa inayotaka Serikali kuimarisha ukusanyaji wa mapato, udhibiti wa matumizi ya Serikali na ufuatiliaji wa miradi yetu ya maendeleo. Wanataka Serikali ihakikishe kuwa fedha zote za miradi ya maendeleo zinatumika kwa tija na kwa kuzingata thamani ya fedha ya miradi husika (value for money).
Mheshimiwa Spika, lakini pia wanataka Serikali iweke mpango mkakati wa kupata vyanzo zaidi vya mapato ili viweze kutekeleza miradi yote ya maendeleo. Kwenye hoja hii nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imepokea maoni haya na kwamba tutaendelea kuyafanyia kazi kupitia mkakati ambao tumeuweka wa kwanza, kubainisha vyanzo vyote vya mapato kwa kila sekta. (Makofi)
Mbili, ukusanyaji wa mapato hayo na kwenye ukusanyaji wa mapato haya tumetaka ukusanyaji wote uwe wa kielektroniki ili kudhibiti mianya ya kupoteza fedha na tumeanza kuona tija kwa kutumia elektroniki tunapata mabadiliko makubwa sana ya fedha ambayo tunaikusanya. Lakini pia baada ya kuwa tumekusanya fedha hizi, tumeweka mfumo wa kudhibiti matumizi yake na tumesisitiza kwa watumishi wenye dhamana ya matumizi ya fedha hizi za umma ni lazima wawe waadilifu na waaminifu na tumesimamia hili pia kwa kupeleka kaguzi za mara kwa mara kuona kama fedha hizi kweli zinakusanywa, zinatumika vizuri baada ya kuwa tumeetoa maelekezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na hii pia tumeelekeza hata kwenye Halmashauri zetu. Halmashauri zote zibainishe vyanzo vya mapato, Halmashauri zijikite katika kukusanya mapato yake, lakini baada ya mipango kupitia Baraza la Madiwani lazima tusimamie matumizi na tumewaasa Baraza la Madiwani lisimamie kikamilifu matumizi ya fedha hizi badala ya kuwaachia Wakuu wa Idara pekee na pale kwenye uovu taarifa itolewe na kupitia kaguzi za ndani na wakaguzi wa nje nao watabaini na pale ambako kuna tatizo tunachukua hatua mara moja kwa wale wote ambao siyo waaminifu katika kuhifadhi fedha hizi na kuzitumia.
Mheshimiwa Spika, na Halmashauri tumezipa malengo. Tunataka kila Halmashauri mwishoni mwa mwaka wawe wamekusanya kwa asilimia 80. Mkakati huu bado unaendelea na kwenye Halmashauri zetu mtakapoingia kwenye Mabaraza ya Madiwani endeleeni kusisitiza na kwa kufanya hilo inawapa fursa Waheshimiwa Wabunge kupanga mipango ya maendeleo kwenye Halmashauri zenu vilevile na Waheshimiwa Madiwani.
Kwa hiyo, tuungane pamoja katika kudhibiti jambo hili la ukusanyaji wa mapato lakini pia namna ya kutumia fedha zile na zote tuhakikishe zinakwenda kweye miradi ya maendeleo ya wananchi ambayo italeta tija kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja inayohusu usimamizi na matumizi ya fedha za umma ambayo nimeieleza vizuri na mimi nasema kwenye eneo hili tumeanza kupata report ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Ndani za Serikali ambayo ilikabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais hivi karibuni na tutakuja kuileta Bungeni ili pia tuweze kufanya mapitia kwa pamoja. Nataka niwahakikishie hiyo ni njia mojawapo ya kudhibiti matumizi haya ya fedha za umma na tutaendelea kudhibiti matumizi ya umma na tumeendelea kuchukua hatua kwenye maeneo ambayo udhibiti wake una udhaifu.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumepata taarifa na wote mnajua kwenye ukaguzi wa mwaka wa fedha 2016/2017 Kurugenzi tatu tu ndiyo zimepata hati chafu nchini kati ya Halmashauri zote 180 na ngapi na hatua kali zimechukuliwa dhidi yao na hilo ni fundisho kwa Wakurugenzi wengine kwamba lazima wasimamie matumizi sahihi ya fedha za Serikali na Waheshimiwa Madiwani waendelee kutusaidia kubainisha matatizo ya matumizi ya fedha kwenye Halmashauri hizo na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na ninyi ni sehemu ya wategemewa wetu kwamba mtatuambia wapi kuna tatizo na ili tuweze kuchukua hatua kwa lengo la kunusuru fedha hizi za umma ziende kwa wananchi kutekeleza miradi wanayoitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine ya miradi ya maji vijijini, hoja imeitaka Serikali ikubali kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini pamoja na kuongeza tozo za shilingi 50 kwenye mafuta ya petroli na dizeli ili kutunisha Mfuko wa Maji kwa lengo la kutatua tatizo la maji ambalo linagusa maneo mengi hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza nieleze kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kuhakikisha kwamba tunatoa huduma za maji kwenye miji yetu na vijijini na Mheshimiwa Rais katika hili amewekea msisitizo na amehakikisha kwamba maeneo yote ya miji na vijijini kunakuwa na miradi ya maji na ameanzisha kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampeni hii maana yake ni kuhakikisha kila kijiji wanakuwa na eneo la kuchota maji ili kumwezesha mwanakijiji asizagae hovyo bila kujua wapi mahali pa kupata maji. Kwa hiyo, Wizara ya Maji imeendelea kufanya vizuri sana, Waziri na Naibu Waziri wanafanya kazi yao vizuri, Katibu Mkuu na wote kwenye Ofisi ile kuhakikisha kwamba miradi yote inaratibiwa vizuri na inakwenda vijijini na kwa bahati nzuri na mimi nimefanya ziara kwenye maeneo niliyopita kila Halmashauri ya Wilaya ina miradi ya maji. Mahitaji ya maji ni makubwa, lakini nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba zoezi letu la kuhakikisha tunatoa huduma ya maji linaendelea. Malengo yetu kufikia mwaka 2020 maeneo ya miji yawe yamefikia asilimia 95 na maeneo ya vijijini angalau tuwe tumefikia asilimia 85 ya huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaenedelea kutafuta vyanzo zaidi vya kuhakikisha kwamba tunaanzisha miradi mingi ya maji kwa ajili ya matumizi ya vijijini. Kwa hiyo, wazo lenu la Serikali iendelee kutafakari kwa makini namna ya kupata fedha hasa kwa kuingiza tozo ya shilingi 50 kwenye mafuta ya petroli na dizeli tunaendelea kutafakari na tutawaambia hatua tuliyoifikia baada ya kuona miradi hii tuliyoiweka, miradi ambayo tumeipanga na tumeipeleka vijijini; tumeshapeleka vijiji vingapi, miji mingapi na miji mingapi na vijiji vingapi bado havijapata huduma ya maji na gharama ya miradi inayotakiwa ni ya kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa kila Halmashauri tumeagiza kila kijiji kifanyiwe upembuzi yakinifu kuona wapi tunaweza kupata chanzo cha maji ili tutoe huduma ya maji kwenye Hamashauri hiyo.
Mheshimiwa Spika, eneo la nne, ni elimu msingi bila malipo. Utekelezaji wa mpango huu bila malipo toka ulipoanzishwa tumeanza kuona mafanikio makubwa. Moja imeongeza idadi ya usajili, imepunguza kero za wazazi za kuchangia ile michango ile holela holela, hapa tunazungumzia ile michango holela na michango ile ingawa pamoja ilikuwa ina tija, Serikali ilichofanya ni kupeleka fedha badala ya kuwachangisha wananchi na tumeshaeleza mara kadhaa na hapa narudia tu kueleza kwamba tunaendelea kutuma fedha kwenye Halmashauri zetu na zinaenda kwenye shule za msingi na sekondari na jumla ya bilioni 18.5 zinakwenda pamoja na fedha ambazo tumezipeleka sasa fedha majukumu kwa ajili ya Maafisa Elimu, Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata nazo pia zinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai mwaka 2017 mpaka mwezi Machi 2018, jumla ya shilingi bilioni 187 zimetumika kupeleka kwenye shule zetu ili kuendelea kuwapunguzia wazazi wa kuchangia ile michango midogo midogo. Suala la michango limeratibiwa vizuri, hatujazuia michango kwa wananchi, lakini tumeliondoa kwenye ngazi ya shule kwa sababu ya kuogopa kuwa huru wa kuchangisha michango mingi kwa kisingizio kwamba wamekaa na kamati za shule, wamekaa na bodi za shule na hatimaye kurudisha tena kero kwa wazazi badala yake michango hii sasa itaratibiwa na Mkurugenzi kwenye Halmashauri. Mkurugenzi anayo fursa au kwa kuanzisha Mfuko wa Elimu kwenye Halmashauri na kuwataka wazazi wachangie ili kupeleka huduma kwenye maneo mengine inaweza kuwa miundombinu au vinginevyo.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia sana suala la upatikanaji wa chakula kwenye shule zetu ambazo wanafunzi wetu wanahitaji kupata chakula. Jambo hili linaweza kuratibiwa vilevile lakini lazima lisimamiwe na Mkurugenzi kwa sababu tunapokuwa na shule mbili jirani kwenye kijiji, shule moja imekuwa na ubunifu wamepata chakula, shule nyingine hawana ubunifu, hawana chakula tunaleta mgongano pale kijijini na ndiyo maana tumesema Mkurugenzi aratibu vizuri michango. Suala la chakula shuleni ni muhimu kwa hiyo muhimu zaidi ni kwamba Wakurugenzi wote waendele na ubunifu, watenge fedha kwenye bajeti zao za halmashauri, wajue wana shule ngapi zinahitaji kuhudumiwa kwa chakula na hasa zile ambazo ziko pembeni sana na vijiji ambazo hazimuwezeshi mwanafunzi kurudi nyumbani. Kwa hiyo michango yote sasa itaratibiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ili ngazi ya shule waendelee na kazi yao ya utoaji wa taaluma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kuimarisha kutoa huduma kwa kupeleka fedha kadri tunavyozipata na kwa kadri ya mahitaji kule shuleni ili jambo hili tuweze kuwaondolea kero wazazi walioko kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, eneo la tano, ni uzalishaji wa mazao ya biashara ambayo tumezungumza mara kadhaa na utekelezaji wake tumeuona, manufaa kadhaa tumeyaona, lakini tulianza na mazao matano; kahawa, chai, tumbaku, korosho na pamba. Tumesimamia kutoka kilimo chake mpaka masoko yake, lakini siyo kwamba ndiyo mwisho, tunaendelea kuratibu mazo mengine. Tunatambua tuna alizeti, ufuta, mbaazi, karafuu kule Zanzibar, tuna mazao mengine kama ya jamii ya kunde, mazao haya yote yanaendelea kuratibiwa na Wizara ya Kilimo na mimi nawataka Wizara ya Kilimo sasa muharakishe uratibu wa mazao haya ili nayo pia yaingie kwenye mpango bora wa kilimo na tukashirikisha Maafisa wa Kilimo wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nini tumekifanya Serikali? Kwanza tumeimarisha ugani kwenye ngazi za vijiji na Kata na kupitia ugani pia tumeimarisha vyuo vya utafiti ili viweze kutafiti mazao haya kutoka ardhi inayofaa kupandwa kwenye maeneo haya lakini namna ya kulihudumia zao lenyewe.
Mheshimiwa Spika, lakini mwisho, tunaendelea kuimarisha ushirika kwa maana ya sekta ya masoko ili kuweza kuweka mfumo mzuri wa kumwezesha mkulima kuuza mazao yake na tuna uhakika maeneo haya tutayaimarisha. Lakini tuna zao la mkonge ambalo pia nalo sasa linaanza kutuletea tija na lina bei inapanda juu ambalo linalimwa maeneo machache hasa Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro maeneo Same na maeneo machache sana kama mkoani Morogoro. Tumeendelea pia nalo kuratibu vizuri na tumeshaoweka Afisa Zao la Katani ndani ya Wizara ili ashirikiane na wakulima wa mzao haya ambayo kilimo chake kinahitaji zaidi ya ukubwa wa hekari tano, 10 na kuendelea. Kwa hiyo, tumeimarisha mfumo wa kilimo kwa ujumla wake na mimi nina uhakika hatua tunayoifikia sasa itatusaidia sana kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata tija.
Mheshimiwa Spika, kwa wafanyabiashara kwenye eneo hili nao pia hatujawaacha nyuma, tumeendelea kukaa nao vikao mbalimbali kuwaonesha njia nzuri ya kupata uwezo wa kununua mazao yetu ili mazao haya yapate masoko mazuri. Najua saa hizi tunahangaika na soko la mbaazi ambako ni nchi pekee ambayo inatumia mbaazi kwa wingi ni nchi ya India na India kwa miaka yote hiyo walikuwa wanalima zao hilo na kwa bahati nzuri kwao na mbaya kwetu, ilipofikia mwaka 2017 walikuwa wamezalisha mbaazi zaidi ya asilimia 30 ya uwezo wa kawaida, kwa hiyo, wamezuia kuingiza mbaazi kutoka nchi nyingine kwa sababu wana mbaazi nyingi zinatosha. Hata hivyo tunaendelea kuzungumza nao na tuliwahi kusema hapa mbele yenu bado niendelee kuwahakikishia kwamba mazungumzo yanaendelea ili kuhakikisha kwamba tunapata masoko ya mazao yetu ili yaweze kupata tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wa sita ambao kwangu mimi nahitaji kuueleza ni hii miradi mikubwa; ni namna ambavyo Serikali inatakiwa kuimarisha ajira kwa Watanzania kupitia miradi ambayo tunaitekeleza.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujihakikishia kwamba fursa hizi za kuanzisha miradi hii mikubwa ni fursa ambazo pia zitatoa nafasi ya ajira kwa Watanzania na tumejiwekea malengo kwenye miradi hii mikubwa, idadi ya wageni ambao wanatakiwa kufanyakazi katika maeneo yale. Tunajua tuna wataalam na tunajua pia na sisi tumekosa utalaam baadhi ya maeneo, kwa hiyo, tumetoa fursa kwa wageni lakini kwa uratibu mzuri sana kuona ni wangapi na utaalamu gani unatakiwa ambao sisi hatuna ndiyo tunawpaa fursa, vinginevyo idadi kubwa ya waajiriwa ni watanzania wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna miradi mikubwa mingi tu ila yote niliyoitaja awali; reli, viwanja vya ndege, ujenzi wa mitambo ya umeme, lakini hata bomba pia la Tanga - Hoima nayo ni sehemu ya ajira na litachukua sehemu kubwa sana, kwa hiyo, tuendelee kuwapa matumaini Watanzania kwamba tunahitaji sasa kupanua wigo wa kupata ajira. Na kwa taarifa tulizonazo sasa kwenye miradi hii zaidi ya asilimia 80 ya kila mradi uliopo ni Watanzania wenyewe kwahiyo tunaleta faraja, nataka niwahakikishie tutaendelea kuimarisha/kuongeza idadi ya miradi ili watanzania wengi wapate fursa ya kuweza kuajiriwa na kufanyakazi waweze kupata vipato vyao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kusisitiza tu kwamba miradi hii mikubwa, moja kati ya faida kubwa tunayoipata ni kupunguza kilio cha ajira na uzuri wa miradi hii yote inachukua ajira za watu wa ngazo zote, za elimu zote; asiyesoma kabisa, wa darasa la saba, kidato cha nne mpaka hao waliomaliza ma-degree wanapata fursa ya kufanyakazi kwenye sekta hizo. Na Serikali pia imeandaa utaratibu au programu maalum ya kitaifa ya kukuza ujuzi, kuwawezesha Watanzania kufanyakazi kwenye maeneo hayo ili wawe na sifa na programu hizi zinaendelea na Serikali imetenga fedha za kugharamia mafunzo hayo, lakini tumehamasisha wale Watanzania wanaoendesha miradi hii au wanaoendesha sekta za kibiashara kuwapokea Watanzania wetu kwenda kupata ujuzi kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, na mafunzo haya tumeyapa asilimia 60/70 wanatumia mafunzo kazini zaidi halafu asilimia 40/30 wanatumia kwa kupata maelekezo na tumeanza kushuhudia vijana wetu wakimaliza wanapata ujuzi wanapata na ajira pia. Kwa hiyo, tumetengeneza utaratibu ambao Watanzania wanaendelea kupata ajira kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya saba inayotaka Waziri Mkuu kufanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu nitafanya ziara mikoa yote nchini na si tu kwenye mikoa, nataka nifike kwenye Wilaya na majimbo yenu nakuja kuona kazi zinazoendelea, kuja kuona changamoto zilizopo, lakini kutatua changamoto zilizopo na maeneo tuliyopita tumefanya haya.
Kwa hiyo, wale ambao mikoa yao bado sijagusa baada ya Bunge tunakuja kuona miradi yenu na hizi ziara hizi ndio zinaongeza na nani kwenu kwa hiyo tutaendelea kuja kuwatembelea ili muweze kupata fursa ya kuonyesha miradi mliyoitekeleza katika kipindi chote ambacho mpo na tutaendelea kuwaunga mkono kuhakikisha kwamba mnafanya kazi vizuri wakati wote kwenye majimbo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja ya nane Waheshimiwa Wabunge walisema Serikali iendelee kusimamia amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Jambo hili ni muhimu sana na ninapolizungumza niseme tu kwamba tutaendelea kusimamia kwamba nchi hii inaendelea kuwa na amani, umoja na mshikamano wa kitaifa na tunapotumia kupata nafasi hizi ni lazima tuendelee kukumbushana Watanzania wote kwamba nchi hii ili tupate maendeleo ambayo tunayalilia ambayo Waheshimiwa Wabunge wanaelezea wanaruhusu fedha zitumike kwanza lazima tuwe na amani ili pia tuweze kufanya hayo maendeleo ambayo tunayahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia maendeleo ya maji lazima tuwe na amani, elimu tuwe na amani, kilimo tuwe na amani nchi zote zenye vita watu hawana nafasi ya kuoga hamna mtu anafuata maji kila mmoja anakimbia huko anakojua alikotizama hajui kama huko kuna huduma au la ilimradi ameokoa maisha yake. Mmeshuhudia nchi mbalimbali tena nchi nyingi zinakimbilia Tanzania, sasa je, Watanzania tukianza kukurupushana hapa ndani tunakimbilia wapi? Kama wao wanakuja hapa sisi tunaenda wapi? Kwa hiyo, ni muhimu sana tukasimamia amani yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa wito kila mmoja kwa nafasi yake aendelee kuimba amani, aendelee kuimba msisitizo na utulivu wa nchi ili tuweze kufanya maendeleo ambayo tunakusudia. Nitoe wito kwa kila mmoja kutekeleza adhima hii ili pia tuweze kusimamia amani yetu hapa nchini ni jambo muhimu sana tupambane na yale yote ambayo yanaleta uchokozi wa amani wa kuvunja amani nchini ili pia kila mmoja aweze kuwajibika namna ambavyo tunataka tuweze kuimarisha amani ambayo tunayo kila mmoja ajaribu kuepuka matatizo yanayopelekea nchi hii kuwa isitawalike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo ambalo limezungumzwa sana jana kwa masikitiko makubwa ni suala la Muungano nieleze sana masikitiko yangu juu ya mjadala ulioendelea jana sikuridhika sijaridhishwa na mjadala wa jana najua ziko hoja, lakini mjadala wa jana kwa namna nilivyojifunza ni migogoro ya mtu na mtu, kundi na kundi jambo ambalo halileti tija wala afya hapa kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, natambua kwamba Muungano wetu unaendelea vizuri, lakini natambua pia yako mapungufu na viongozi wetu wote Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali za Mapinduzi Zanzibar wote wameapa kusimamia Muungano huu na sisi jukumu letu pia kuhakikisha kwamba tunaunga mkono ili tuulinde Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba kutokana na kuingia madarakani na sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ina miaka miwili, yako maboresho Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yako maboresho. Maboresho haya yanaweza kuathiri mfumo wa kawaida ambao tulianza nao ambao tunaumaliza kupitia vikao ambavyo tulivyonavyo, inawezekana jambo hilo baada ya mabadiliko linahitaji harmonization ya kisheria. Kwa hiyo, jukumu hilo ni jukumu la Kamati ambayo inasimamiwa na Makamu wa Rais ambaye pia naye ndio anahitisha kikao cha pamoja ili tuweze kuzungumza. Lakini kwa namna ambavyo mjadala umeendelea jana na watakao na niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu hakuna afya kwenye mjadala kama ule wa jana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuzuii Mbunge yeyote kuuliza swali lolote juu ya ufafanuzi juu ya mwenendo wa Muungano lakini majibishano ya mtu mmoja na mmoja hayo hayana afya. Lakini tumeanza kulifanyia kazi na hatutatoa mwanya wa Wabunge kujibishana kupeana maneno makali kwa sababu ya mwenendo wa Muungano Serikali tumejipanga vizuri tutasimamia Muungano wetu, tutatoa kero zetu ili tuende vizuri pande zote mbili tuweze kufurahia Muungano wetu ambao sasa tunao.
Mheshimiwa Spika, mimi niseme tu kwamba Muungano wetu ambao huwa tunakutana mara kadhaa katika kujadili vitu ambavyo vinahitaji kufanyiwa mabadiliko Makamu wa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ndio Mwenyekiti wetu na sisi watendaji wa chini, mimi ni mjumbe na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ni mjumbe na Mawaziri walioko kwenye Wizara zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa tumefanya mabadiliko kadhaa ndani ya Serikali na namna ya kuendesha sekta mbalimbali ni kweli yako maeneo ambayo yanahitaji kubadilisha pia na sheria na vitu vingine, mijadala yetu inaendelea na tarehe 28 hapa tunakutana na tunafanya/ tunaendelea na mjadala huu wa maeneo yote ambayo yanaweza kuleta manung’uniko. Kwa hiyo, nawasihi Waheshimiwa Wabunge wenzangu jambo hili tuliendeshe kwa lugha nzuri za kiistarabu si vyema tukafanya tukarudia tena kama ilivyotokea jana, haifurahishi kundi moja likakasirika lakini kwa sababu mtu mmoja au wawili kuwakasirisha watu wengine jambo hili si jema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini yote hii imetokana na issue ya sukari na mimi nataka nieleze nchi yetu inahitaji sukari kwa sababu hatuna viwanda vinavyotosha kuzalisha sukari. Zanzibar tunahitaji sukari, Bara tunahitaji sukari; na kwa kuwa Zanzibar wana kiwanda kimoja, Bara tuna viwanda vitano, viwanda hivi vitano vyote havitoshi kupeleka sukari hata kule Zanzibar kutoka huku mpaka kule Zanzibar hata kila Kiwanda cha Mahonda kiwe na uwezo wa kuzalisha sukari ikatosha Zanzibar pia na huku kwa hiyo tunachofanya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Biashara ndio inayoratibu uletaji wa sukari Zanzibar na Serikali ile inatoa fursa wafanyabiashara kuleta sukari nchini pale Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, huku Bara tumeunda chombo kinaitwa Bodi ya Sukari ndio inaratibu kuleta sukari iwe kutoka ndani kupitia viwanda vyetu au kutoka nje ya nchi sasa sukari ya Bara kupitia viwanda vyake na huu ni mkakati wa kitaifa wa kulinda viwanda vya ndani, tunapolinda viwanda vya ndani tumebana uingizaji holela wa sukari ndani ya nchi ili tusije tukaathiri uzalishaji wa ndani. Huku tukiwa tunaendelea ku-harmonize kodi zake na nini, utakuta sukari ya nje inayoingia nchini ni ya bei rahisi kuliko sukari inayozalishwa ndani ya nchi na kwa maana hiyo kiwango cha sukari inayozalishwa ndani gharama yake inakuwa kubwa viwanda vya Bara hata kila cha Zanzibar gharama yake ni kubwa, kwa hiyo, ukileta sukari kutoka nje maana yake sukari ya ndani haiwezi kuuzika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa jambo ambalo najua Mawaziri tunahitaji pia tuwe tunawapa taarifa Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wakiwepo ni kwamba mpango wa sukari kwa Tanzania Bara hata ile gape sugar tuwe tunapotoa matangazo kutaka watu na kuwapa vibali walete hatuchagui kama tumempa kibali ni wa Bara au wa Zanzibar wote wanapata sukari, nataka niwaambie mimi ndio natoa vibali mwaka 2016 tulipoingia madarakani tulikuwa na gape sugar ya tani 140000 kwenye tani 140000 kati ya wafanyabiashara ambao tumewapa vibali wa Zanzibar wawili na watanzania Bara watatu lakini kiwanda hicho cha Mahonda nilikipa kibali kikaingiza tani 390. Naeleza hili ili muone kwamba tunafanya kazi kwa pamoja mwaka 2017 sukari ambayo tumeingiza gape sugar ni tani 140000 walioleta sukari Tanzania ni Wazanzibar wawili na wa Bara wawili. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, muone namna ambavyo tunashirikiana na wale Wazanzibar mmoja ni agent wa hiyo Mahonda. Nataka niwaambie ukweli ili muone kwamba tunapotoa vibali hivi hatuangalii sura, hatuangalii huyu mtu anatoka wapi, ili mradi mfanyabiashara Mtanzania tunatoa vibali. Ni mwaka huu tu sasa tume-improve zaidi tumesema sukari mwaka huu ebu tuwape wazalishaji wenyewe na kibali cha gape sugar ya tani 135,000 tumewapa viwanda vyenyewe na tayari wameshaagiza na sasa sukari imeshaanza kuingia tulitaka tuwahi hata Mfungo wa Ramadhani ili nchi nzima iwe na sukari ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hasa mwaka huu peke yake ndio haijafanya Wazanzibari kuingia wala Watanzania kupata vibali wafanyabiashara wengine kwa sababu inaletwa na viwanda vyenyewe. Kwa hiyo, kama kuna malalamiko yaliyopitia hapa Bungeni yakaletwa hapa kwamba hakuna vibali ni kutokana na nature hiyo. Na mimi naamini wakati huo tunafanya majaribio, lakini mkakati wetu tunavitaka viwanda hivi vizalishe sukari ya kutosha ili nchi ijitegemee yenyewe na tukiruhusu sukari nyingi kuingia kwa uingzaji holela viwanda hivi sukari yao itabaki viwandani haitanunulika kwa sababu sukari ya ndani ina gharama kubwa kuliko sukari ya nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kauli hii Mawaziri wa biashara wote wa Bara na Visiwani kama tutaiangalia vizuri hata kule Zanzibar kiwanda cha Mahonda hicho kiwango cha uzalishaji wake ile gape sugar ndio tutoe vibali badala ya kuacha watu wanaingiza holela vitafunika soko la ndani.
Mheshimiwa Spika, mimi nilishafika Zanzibar nimeshazungumza na Waziri wa Biashara, nimeshazungumza na Waziri wa Kilimo wakati ule Mheshimiwa Hamad Rashid, yule mfanyabiashara wa Mahonda amekuwa na matatizo mengi sana, miwa yake mara nyingi imekuwa ikichomwa, haifikii uzalishaji na leo kiwanda kile kimefungwa hakizalishi.
Mheshimiwa Spika, ni jukumu letu sisi kuhakikisha tunamlinda mwekezaji yule na mtaji aliouweka pale ili aweze kupata mtaji hakuna sababu Waheshimiwa Wabunge kulumbana hapa suala la sukari, sukari imeratibiwa vizuri, lakini uratibu huo tunalinda viwanda vya ndani, tunataka viwanda hivi vizalishe, viongeze uwezo, viongeze mtaji ili viweze kutosheleza mahitaji ya ndani tunaweza kusema nchi nzima tuna viwanda sita tu Kilombero, Kagera Sugar, Mtibwa, Manyara Sugar lakini pia tuna hiyo Mahonda ni viwanda hivyo tu tunaongeza kiwanda kimoja Bagamoyo Sugar wameshaanza kujenga, tunaongeza kiwanda pale Mbigili, Mkulazi malengo yetu tuongeze sukari. Tuna shamba Kigoma kubwa sana tunataka tulime sukari, pale Manyara tunataka tupanue lile shamba nimeshakwenda pale kiwandani kuona wana eneo kubwa tu wanaweza kupanua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi yetu sasa ni kuwezesha viwanda hivi na wawekezaji kupata mtaji wa kupanua viwanda ili sukari iingie hapa ndani yaani tuzalishe ndani, ijitosheleze hapa ndani. Kwa hiyo, nataka niseme Waheshimiwa Wabunge msigombane bure, sukari tumetaka viwanda vya ndani viwe na uwezo wa kuzalisha vifikie malengo, hatuhitaji kuagiza mara kwa mara, kwanza sukari nyingi tukiileta watu wa TFDA wanasema rudisha kwa sababu labda inakosa ubora na vitu vya namna hiyo. Lazima tujiridhishe sukari inayoingia nchini ina ubora, kwa hiyo, naamini baada ya kauli hii mgogoro huu wa sukari sitousikia tena hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nakaribisha maoni ya namna ya kuboresha sekta hii na bado Wizara ya Kilimo itakuja kwa hiyo, mnaweza mkatoa pia maoni yenu si tutakuwa hapa tunasikiliza tutapokea maoni yenu Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, jambo hili la sukari lisivuruge Muungano wetu, jambo hili la migogoro mingine, mapungufu mengine kwenye Muungano wala lisiwe jambo kubwa kwa sababu Kamati ipo na sisi tuko tayari tutasimamia mapungufu yote, tutayaondoa Bara na Zanzibar ni nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila mmoja, ni kila mmoja ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa kusema haya nadhani kwenye eneo hili ambalo nimetumia muda mrefu nitakuwa nimeeleweka na naomba niwasihi mnielewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba baada ya kusema haya sasa naomba nihitimishe na nikiri kwamba hoja zote za Waheshimiwa Wabunge zilizowasilishwa na kuzungumzwa moja kwa moja hapa Bungeni na zile za maandishi zote ni za msingi na ni muhimu na hivyo Serikali inazipokea na tutazifanyia kazi. Kama nilivyoeleza katika hotuba yangu ya bajeti Serikali imeadhimia kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba utekelezaji wa miradi kuimarisha utendaji, usimamizi makini wa rasilimali na nidhamu ili kukidhi dhumuni rasmi la Serikali katika kuwafikishia wananchi huduma za kuwaletea maendeleo hili tutalisimamia kikamilifu, tunataka watanzania wanufaike na huduma zote za nchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea pia kutenga fedha ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta zote na msukumo utawekwa katika kusimamia utekelezaji wa mageuzi yaliyobaki katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, mifugo, uvuvi, maji na miradi mikubwa yote ya kielelezo ili ikikamilika na ikamilike kwa haraka na ianze kuleta mafao ambayo tunayatarajia kuyapata au manufaa tunayotarajia kuyapata ikiwemo na ajira kutoka kwa Watanzania, muhimu pia hapa ni kukumbuka kuwa bajeti ni chombo muhimu cha kutekeleza sera na malengo yaliyowekwa kupitia Serikali iliyopo madarakani na mimi naamini kama ilivyotangulia kuelezwa hapo awali muda hautoshi kujibu kila hoja ningeweza kutoa ufafanuzi yote lakini yote yameelezwa menigne yote yameelezwa na Wabunge na kwa sababu tuko hapa miezi mitatu kadri jambo linapozaliwa mko huru kuja kwa consultation halafu tuweze kutoa ufafanuzi.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tuendelee kuunga mkono jitihada za viongozi wetu na hasa kiongozi wetu Mkuu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake kubwa anazozifanya katika kuimarisha ulinzi wa rasilimali za Taifa ikiwemo madini na tumeongeza ukusanyaji wa mapato ambayo yametuwezesha sasa kutekeleza mafanikio haya ambayo tumeyaeleza kwenye hotuba yetu yote na yale ambayo yatakuja kuzungumzwa na sekta husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusisitiza tena kwamba suala la kuwahudumia Watanzania, kuwaletea maendeleo pamoja na kuhakikisha nchi yetu inafikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda mafanikio yake hayo yatatoka mikononi mwetu sisi sote. Kwa hiyo, ni muhimu sana sasa wote tuunge mkono jitihada za Serikali ili tuweze kuwafikia wananchi wetu huko waliko kwa kuwapelekea miradi ya maendeleo ni muhimu sana pia kwa wadau wote kufanya kazi zaidi kwa kuwa na nidhamu zaidi katika kila jambo umnalolifanya ili uweze kupata matokeo mazuri, na hii sasa tuendelee sasa kuunga mkono falsafa hii ya awamu ya tano ya hapa kazi tu ndio italeta majibu ya haya yote tunayosema.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kutupa afya njema na kutujalia kukutana tena kwenye Kikao hiki cha Sita cha Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuhitimisha mjadala huu kuhusu hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziuri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kutoa shukrani za dhati kwa makundi mbalimbali kama yalivyotamkwa na Mawaziri wote walionitangulia, nami sikusudii kurudia ila nitayapitia kwa makundi lakini wote waamini kuwa natambua mchango wao mkubwa katika kuwezesha Ofisi hii kutimiza wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, natoa shukurani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa michango yao mizuri kwenye hoja ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nawashukuru sana Mheshimiwa Spika, wewe Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa mwenendo mzima wa majadiliano ya hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge pia kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri waliochangia hoja pamoja na Naibu Mawaziri, Ofisi ya Waziri Mkuu; Makatibu Wakuu; Naibu Makatibu Wakuu; Wakuu wa Idara; Mashirika; Wakala na Taasisi zote za Serikali pamoja na watumishi wengine katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa waliyoifanya na ushrikiano walionipa katika kipindi chote cha mjadala wa bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa pongezi zenu kwa Serikali na kwa michango yenu yenye dhamira ya dhati kabisa, michango yenye hoja za kuboresha mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa mwaka wa fedha mwaka 2019/2020. Mjadala huu umeendelea kuthibitisha uimara na umakini wa Bunge katika kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba na kuishauri na kuisimamia Serikali kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mjadala huu Waheshimiwa Wabunge 142 walichangia hoja Ofisi ya Waziri Mkuu. Kati ya hao, Waheshimiwa Wabunge 98 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa 44 walichangia kwa maandishi. Ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda, naomba uridhie nisiwataje, aidha, majina yao yote yaingingizwe katika Hansard. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejibu hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge kupitia Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, halikadhalika hoja zilizosalia zitajibiwa kwa maandishi. Vilevile baadhi ya hoja zenu zitatolewa ufafanuzi wa kina na Waheshimiwa Mawaziri ambao watajipanga vizuri kuzitolea ufafanuzi wa kutosha wakati wa kuwasilisha bajeti zao za kisekta.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kuwa kuna msuala muhimu yameibuliwa wakati wa majadiliano haya. Kadhalika mtakubaliana nami kwamba mjadala ulikuwa wa kina na wa kiwango cha juu na umakini unaostahili. Ninakiri kuwa michango ya Waheshimiwa Wabunge na hoja zao zilizoibuliwa zina uhusiano wa moja kwa moja na utendaji wa kazi za Serikali. Aidha, masuala muhimu hususan usafiri wa anga, utalii, bandari, maji, makusanyo ya kodi na uwekezaji ndiyo ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni kitovu cha mjadala mzima wa michango ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kabla ya kuingia moja kwa moja katika kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge, naomba nitolee ufafanuzi baadhi ya masuala muhimu yaliyoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye hoja hii ya Waziri Mkuu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ilikuwa suala la bniashara na uwekezaji. Serikali imeendelea kujenga mazingira wezeshi na rahisi ya kufanya biashara na uwekezaji bila kuathiri ubora na viwango, sambasamba na kufuata sheria, kanuni na miongozo iliyopo. Hata hivyo, licha ya azma hiyo nzuri ya Serikali, bado kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji kama walivyoeleza Waheshimiwa Wabunge wakati wa kuchangia hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ufafanuzi kwa yale masuala yaliyogusa vyombo vya udhibiti kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka nyingine za udhibiti pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, OSHA, BRELA, Taasisi ya Mionzi na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu Mamlaka hizi na namna ya utendaji kazi wake, miongoni mwa kero hizo ni mchakato wa muda mrefu wa kupata leseni za biashara, gharama za usajiri wa bidhaa zinazotozwa na TFDA, suala la viwango vya TBS, madai ya kuwepo kwa unyanyasaji unaofanywa na TRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi dhidi ya wafanyabiashara, umbali wa Makao Makuu wa Maabara za Taasisi za Mionzi na eneo wanalofanyia kazi kama vile bandari, viwanja vya ndege na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa ni hatua ya kuondoa kero hizo, katika nyakati tofauti Viongozi wetu wa Kitaifa wamekuwa wakichukua hatua za makusudi kuzungumza na wafanyabiashara pamoja na wawekezaji. Mazungumzo haya yamekuwa yakijielekeza zaidi katika kupokea kero na kuzitafutia ufumbuzi kero hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ameweza kukutana na wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji zikiwemo taasisi za Serikali, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wachimbaji wa madini na wakulima katika nyakati tofauti. Aidha, nami nimekutana na wawakilishi wa wafanyabiashara wadogo na wafanyabiashara wa kati tarehe 28 Februari, 2019 Jijini Dar es Salaam. Kadhalika tarehe 6 Machi, 2019 nilitembelea Shirika la Viwango vya Taifa Tanzania na Mamlaka ya Chakula na Dawa na kufanya mazungumzo na viongozi na watendaji wa taasisi hizo akiwemo Mkemia Mkuu wa Serikali na baadaye tarehe 16 Machi 2019 tulikutana tena kwa pamoja na TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazungumzo hayo, nilielekeza viongozi na watendaji wa mamlaka hizo za udhibiti kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uadilifu na weledi wa hali juu huku wakijiepusha na vitendo vya rushwa, kuhamisha mafaili ya ofisi, ofisi za wafanyabiashara na kukusanya komputa na kuondoka nazo. Badala yake watumie nafasi hiyo kuwaelimisha wafanyabiashara ili kuwafahamisha nini kinabadilika? Nini kinatakiwa? Hasa katika kufuata utaratibu, kanuni na sheria na miongozo mbalimbali inayohusu biashara na uwekezaji na kuondoa urasimu na mianya ya rushwa katika kutekeleza majukumu ya taasisi hizo kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo imeonekana kuwa kikwazo cha biashara na uwekezaji ni mwingiliano wa majukumu ya taasisi hizo. Kwa mfano, uwepo wa majukumu yenye kufanana kwa TFDA na TBS na Mkemia Mkuu, Bodi ya Maziwa, Bodi ya Nyama, Baraza la Mifugo, EWURA, SUMATRA na TANROADS ni kikwazo kikubwa katika kurahisisha mazingira ya kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari nimeshatoa maelekezo na yameanza kufanyiwa kazi kwa Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta hizo zote chini ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu, kwamba wakae pamoja kupitia sheria na mganyo wa majukumu yao kwenye taasisi zao za udhibiti ili kuondoa mkanganyiko uliopo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Mamlaka ya Mapato na Taasisi zake, nawaelekeza tena Mawaziri husika kuhakikisha kuwa wakuu wa taasisi hizo wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia sheria bila kuwabughuzi wafanyabiashara na wawekezaji hapa nchini. Kwa upande wa wawekezaji, nao pia natoa rai wahakikishe kuwa wanazingatia sheria na kanuni ili pande zote ziweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzisisitiza mamlaka hizi za udhibiti kupanua wigo wa shughuli zao hususan maeneo ya mipakani, kuimarisha matumizi ya kielektroniki ili kuondoa urasimu kukabiliana na mianya ya rushwa na hasa katika utoaji huduma zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, liko jambo limezungumza upande wa Uhamiaji. Kama ambavyo nimeeleza kwenye hotuba yangu, Serikali pia imeendelea kuboresha taratibu za Idara ya Uhamiaji kwa kutekeleza awamu ya pili ya mradi wahamiaji wa mtandao. Mradi huo wenye kuhusisha utoaji wa VISA na vibali vya ukazi vya kielektroniki utarahisisha zaidi shughuli za utalii, biashara na uwekezaji hapa nchini kwa kuondoa urasimu hususan muda mrefu unaotumika kufanya maombi hayo ili kupata vibali hivyo kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hatua thabiti za kuvutia uwekezaji zinazochukuliwa na Serikali, haikunishangaza kwa Tanzania kuibuka kinara katika kuvutia uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki ambapo tulivutia mitaji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.18. Hii ni kwa mujibu wa report ya mwaka 2018 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya biashara na maendeleo. Tunaendelea kuvutia mitaji zaidi ya uwekezaji na ninaamini tutafikia malengo tunayokusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuwavutia wawekezaji kujenga viwanda nchini hususan vyenye kutumia nguvu kazi kubwa na malighafi zinazozalishwa hapa nchini kwa lengo la kutengeneza ajira, kuongeza tija kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma na kuipatia Serikali fedha nyingi za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie Sekta ya Utalii. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge pamoja na kuipongeza Serikali kwa hatua za kuboresha Sekta ya Utalii hususan ununuzi wa ndege mpya, pia wametoa mapendekezo ya ndege hizo kufanya safari katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu na maeneo ya kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia fursa hii kuwafamisha Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali itaendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Utalii. Uboreshaji wa usafiri wa anga unakwenda sambamba na utangazaji na utajiri mkubwa kwa vivutio vya utalii tulivyonavyo kama vile, uoto wa asili, wanyama, fukwe, malikale, tamaduni za makabila yetu yasiyopungua 120 na vinginevyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutoa msukumo kufungua kanda za Kusini katika maendeleo ya utalii kwa kuviendeleza vivutio vya utalii vilivyopo kwenye ukanda huo ili vichangie kukamilisha ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi. (Makofi)
Aidha, Serikali inaendelea na mkakati wa kuunganisha na kufungua ukanda wa ziwa kwa kuendeleza Mapori ya Akiba maarufu kama BBK, yaani Biharamulo, Burigi na Kimisi pamoja na Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa. Mpaka sasa takribani shilingi bilioni nne zimeshatumika kuimarisha ulinzi, kuainisha mipaka, kujenga miundombinu ya utalii, kuweka mifumo ya kielektroniki ya utawala na ya kukusanya mapato pamoja na kuendeleza vivutio vya utalii vinavyopatikana kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine, kuimarika kwa usafiri wa anga nako kumeendelea kuchangia vyema ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini. Mathalan baada ya kuwasili kwa ndege zetu kubwa tatu zinazojumuisha Boing 787 Dreamliner na nyingine mbili aina ya Air Bus A220-300. Shirika la Ndege la Tanzania sasa limeanza safari za kwenda nchi jirani za Zambia na Zimbabwe. Halikadhalika, muda siyo mrefu shirika hilo litaanza safari za masafa ya mbali zitakazohusisha nchi za China, India na Thailand. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kuipongeza Bodi ya Utalii nchini ambayo mwezi Novemba, 2018 iliingia makubaliano na kampuni ya Touch Road International Holding Group kwa ajili ya kutekeleza mradi huo uitwao Tour Africa the New Horizon. Mradi huo utasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka China ambapo kwa kuanzia tunatarajia kupokea watalii 10,000 kwa mwaka 2019. Aidha, mwezi Mei mwaka huu Tanzania inategemea kupokea watalii wasiopungua 300 kutoka nchini humo na tayari tumeshapokea watalii 336 kutoka nchi mbalimbali walioingia wiki iliyopita kwa njia ya meli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni ya Touch Road inayo nia pia ya kufanya uwekezaji mpya kwenye ujenzi wa hoteli, maeneo ya viwanda na kanda maalum ya uchumi wa makazi. Napenda kutoa wito kwa mamlaka na wadau mbalimbali wanaojihusisha na sekta hii muhimu ya utalii, kuliangalia vyema suala la viwango vya gharama za malazi kwenye mahoteli ya kitalii pamoja na tozo mbalimbali za kuingia kwenye maeneo yenye vivutio vya utalii. Kumekuwepo na malalamiko kuwa gharama zetu kwenye maeneo hayo ziko juu na kwa hiyo, zinasababisha utalii wa ndani kupungua kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusisitiza pia kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania wote kwa ujumla kuenzi utalii wa ndani. Aidha, Mamlaka za Utalii zote zitoe vivutio mbalimbali kwa watalii wa ndani ili nao wapate fursa kujionea utajiri wa maliasili tulizonazo hasa uoto wa asili, wanyama, fukwe, malikale na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezungumzia upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini sambamba na kuipongeza Serikali, lakini pia walikosoa utekelezaji na ubora wa baadhi ya miradi ya maji na vilevile wameonesha kutorodhishwa sana kwa baadhi ya maeneo kwa sababu hayajafikiwa na miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na usambazaji wa maji licha ya changamoto hizi. Hata hivyo, Serikali inachukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa miradi yote ya maji inayotekelezwa inatoa matokeo yanayokusudiwa. Kwa kuanzia Mheshimiwa Rais aliunda Tume Maalum ili kupitia, kufanya tathmini na kutoa mapendekezo juu ya hatua za haraka zinazostahili kuchukuliwa. Hatua hizo zitalenga hasa kuhakikisha kuwa thamani ya fedha ya miradi hiyo inayosambazwa mikoani kote na Wilayani inapatikana na kuleta tija kwenye maeneo miradi hiyo inapotekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa tumehakiki madai ya Wakandarasi waliotekeleza miradi hiyo na kulipa shilingi bilioni 138. Aidha, hivi karibuni tutapata fedha nyingine kiasi cha shilingi bilioni 44. Sasa naielekeza Wizara husika ihakikishe kuwa Wakandarasi na Watendaji wa Serikali kufuatilia ufanisi wao kuwa unakuwa wa kiwango cha kuridhisha wakati wote.
Waheshimiwa Wabunge endeleeni kutoa ushauri kwenye Sekta ya Maji. Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunafikia mpaka ngazi ya vijiji ili wananchi wote waweze kunufaika kwa kupata maji safi na safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie maji na usafi wa mazingira. Changamoto nyingine katika eneo la maji ni uharibifu wa mazingira ambao umeshika kasi kubwa. Ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kuiepusha nchi yetu na janga hili. Katika kuhakikisha kuwa tunaondokana na janga hili, Bunge lilipitisha Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2019 yenye lengo la kuimarisha mfumo wa utoaji huduma za maji na usafi wa mazingira nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, sheria hiyo itaongeza uwajibikaji katika utoaji wa huduma ya maji, utaimarisha ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji. Kufuatia kuundwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na kuleta uendelevu kwa miradi ya maji vijijini, nawaagiza viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji kuchukua hatua za makusudi katika kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji na kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira. (Makofi)
Aidha, viongozi na watendaji watakaobainika kutosimamia ipasavyo sheria husika, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono jitihada hizi za Serikali ili kuweza kudhibiti uhalibifu wa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba mnamo tarehe 5 Mei, mwaka 2016 Serikali ilitoa kauli ndani ya Bunge lako Tukufu kuhusu dhamira ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki hapa nchini. Kuanzia wakati huo hadi sasa Serikali imekuwa ikifanya maandalizi ya kutimiza dhamira hiyo. Hivi karibuni nimemwagiza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, anayesimamia masuala ya Mazingira ikiwemo kuzungumza na wadau mbalimbali, ikiwemo wenye viwanda vya kutengeneza mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuhakikisha kwamba jambo hili linatekelezwa kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya plastiki nchini yameendelea kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo vya mifugo kwa kula plastiki, kuziba kwa mifereji mingi nchini, uchafuzi wa mazingira na kushindikana kwa kuozesha taka kwenye vituo vya kukusanya taka. Kuanzia tarehe 1 Juni, 2019 itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote. (Makofi)
(Hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu Alikohoa)
WAZIRI MKUU: Na washindwe! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie tena. Kuanzia taehe 1 Juni, 2019 itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote. Aidha, ifikapo tarehe 31 mwezi Mei mwaka huu 2019 itakuwa ni mwisho wa kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadilisha teknolojia yao, wauzaji kuondoa mizigo yao au kumaliza kuiuza yote na kadhalika. Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais, itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchukua hatua hizi, tumetambua kwamba kuna baadhi ya bidhaa lazima zifungwe kwenye vifungashio vya plastiki. Vifungashio kwa bidhaa hizo havitapigwa marufuku kwa sasa. Kwa msingi huo, katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais yatatolewa maelekezo ya kina kuhusu katazo la vifungashio la aina hii hasa katika maeneo ya uzalishaji wa viwanda, Sekta ya Afya na Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yetu kuwa utaratibu huu pamoja na kutunza mazingira, utatoa fursa kutengeneza ajira nyingi, hususan za watu wa chini kupitia utengenezaji wa mifuko mbadala ya plastiki pamoja na kutumia kikamilifu fursa ya viwanda vya karatasi vilivyopo nchini kikiwemo kiwanda cha Mgololo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia makusanyo ya kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Waheshimiwa Wabunge wameainisha maeneo kadhaa ambayo yanalenga kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania. Maeneo hayo ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuongeza wigo wa kulipa kodi na maeneo haya kuweka viwango himilivu ili kuchochea walipa kodi wengine wengi zaidi kulipa kwa hiyari na kujenga mazingira rafiki kwa walipa kodi. Serikali imepokea ushauri huo na itaufanyia kazi, ili kuondoa kero kwa walipa kodi nchini. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko makubwa na kutoa maelekezo mahususi, hivyo nawaelekeza watendaji wote kuzingatia maelekezo wanayopewa na kuacha tabia ya kutoa visingizio vinavyokwamisha utekelezaji mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa nimetoa maelezo haya ya msingi, sasa nijielekeze kwenye baadhi ya hoja ambazo zimetolewa. Ziko hoja ambazo tayari zimeelezwa na Waheshimiwa Mawaziri na Waziri wa Nchi alipokuja hapa mbele, hivyo nitapitia kwa haraka kwenye maeneo yale ya kimkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016, naomba nitumie nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, Ofisi ya Waziri Mkuu ihakikishe kwamba, vipaumbele vyake vinalenga kuboresha na kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa hapa ndani na nje ya nchi. Hatua ambayo itatengeneza ajira kwa wananchi wengi na kuongeza fursa za biashara na mapato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla wake. Serikali imepokea ushauri wa Kamati. Aidha, moja ya vipaumbele vya mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano ni kuimarisha mazingira ya biashara ya uwekezaji, ili kuwezesha uanzishaji na ukuaji wa biashara hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza hilo Serikali itaendelea kuweka kipaumbele kwenye kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile usafiri kwenye maeneo ya ujenzi wa reli, barabara, viwanja vya ndege, bandari, lakini pia huduma za umeme na maji ili kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na uwekezaji kwa wawekezaji kwa ujumla. Aidha, Serikali itaimarisha upatikanaji wa ardhi, kuendeleza maeneo maalum ya uwekezaji (Special Economic Zones) na kutekeleza programs za kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na mpango wa kuboresha mfumo wa udhibiti wa mazingira ya biashara nchini (Blue Print for Regulatory Reforms to Improve Business Environments). Vilevile Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na majadiliano na sekta binafsi kupitia Baraza la Biashara la Taifa pamoja na mikutano ya wadau wa sekta mbalimbali wa ngazi za Kitaifa, mikoa na wilaya ambapo changamoto zinazobainishwa kwenye vikao hivyo ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya pili ya Serikali ilete Bungeni haraka iwezekanavyo Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 na marekebisho yake ambapo kwa mambo mengine itawezesha, moja kuunda Tume Huru ya Uchaguzi (Tanzania Independent Electoral Commission) na yale yote ambayo pia yanaingia kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni Idara huru inayojitegemea na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Tume hiyo inatekeleza majukumu yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote kwa mujibu wa Ibara ya 74(7) na Ibara ya 74(11) ya Katiba. Aidha, ni vema ikafahamika kuwa uteuzi wa Wajumbe wa Tume hufanywa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba. Hivyo, njia inayotumika kuwateua Wajumbe au Mkurugenzi wa Uchaguzi haiathiri uhuru wa tume.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko hoja ambayo pia, imezungumzwa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi alipokuja hapa, uchaguzi wa Serikali za mitaa kwamba, uchaguzi wa Serikali za Mitaa usisimamiwe na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na badala yake usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Serikali ishughulikie jambo hili mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa imani kubwa mnayoonesha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni huru juu ya utekelezaji wa majukumu yake na kuona umuhimu wa kuiongezea jukumu la kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Hata hivyo, majukumu ya tume yameainishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo, jukumu la kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa si miongoni mwa majukumu ya tume kwa mujibu wa Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya nne ambayo pia imezungumzwa kwa upana wake juu ya Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo imeharamisha shughuli za siasa nchini na kuzifanya kuwa kosa la jinai. Hii inadhihirika kutokana na sheria hii kuwa na vifungu vingi vinavyotoa adhabu ya jamii, kifungo au vyote kwa pamoja kwa wanasiasa ili msajili na Serikali na vyombo vyake hakuna kifungu hata kimoja ambacho kinawagusa kama wakikiuka utekelezwaji wa sheria ya namna hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 3 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeruhusu uwepo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini, hivyo hakuna sheria ya nchi inayoweza kufanya siasa kuwa kosa la jinai. Adhabu zilizopo katika Sheria ya Vyama vya Siasa zinaendana na aina ya kosa linalotolewa kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na Bunge. Aidha, Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinamruhusu mtu yeyote ambaye anadhani Msajili wa Vyama vya Siasa amekiuka Sheria ya Vyama vya Siasa kwenda Mahakamani kupata haki yake. Serikali inavitaka vyama vya siasa na taasisi mbalimbali kuzingatia sheria pale zinapotekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tano ilikuwa ni kilimo cha zao la pamba nchini kwamba, bado hatujatumia zao la pamba vizuri katika kuongeza pato la Taifa na kuinua maisha ya Watanzania. Serikali ijizatiti kusimamia uwekezaji kwenye kilimo cha zao la pamba kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa viwanda vya nguo hapa nchini ili kufikia malengo na kuwa na Taifa lenye uchumi wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Sekta ya pamba na mnyororo wake wote wa thamani ni sekta ya kipaumbele ambayo pamoja na kuwahakikishia soko wakulima na kuongeza kipato chao uwekezaji katika viwanda vya nguo unatengeneza ajira nyingi kwa vijana, hivyo kuinua kipato chao na kuboresha maisha ya watu walio wengi. Kwa kutumia mkakati wa kuzalisha nguo na mavazi mbalimbali (cotton to clothing) Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwa kutumia teknolojia za kisasa na kutengeneza nguo kuanzia kuchakata pamba hadi nguo kwa kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafanyika nchini na msisitizo uwe ni utengenezaji wa nyuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya sita, Serikali itumie fursa ya uwepo wa mifugo mingi nchini kwa kuwekeza katika viwanda vya kuchakata nyama ili rasilimali ya mifugo iweze kunufaisha Taifa badala ya nchi jirani kunufaika na mazao ya mifugo inayotoka hapa nchini kwetu. Serikali inaendelea na jitihada za kuvutia uwekezaji katika mzao ya mifugo kwa ushirikiano na wawekezaji binafsi wa ndani na nje kwa ranchi za Taifa. Mfano ni uendelezaji wa ranchi ya Taifa ya Ruvu ambapo Serikali imeingia makubaliano ya awali ya kujenga machinjio makubwa ya kisasa, unenepeshaji wa mifugo na ufungashaji wa nyama. Aidha, kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018 Serikali imeweka vivutio vya kikodi kwa kupunguza kodi ya makampuni kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa viwanda na bidhaa za ngozi, pamoja na kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani kwa mitambo na vifaa vya viwanda hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya saba, Serikali iangalie namna ya kuondokana na urasimu katika kuwezesha jitihada za wawekezaji, hasa kwa wageni wanaokuja na mitaji yao kuja kuwekeza hapa nchini. Ili kuondokana na urasimu, Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1977 iliunda kituo cha uwekezaji hapa Tanzania kiitwacho TIC ambapo huduma mbalimbali ikiwemo usajili, utoaji wa vibali mbalimbali na leseni na kwa ajili ya uwekezaji unafanyika katika eneo moja (One Stop Facilitation Centre) ambapo taasisi zilizokuwepo awali ni pamoja na TRA, Ardhi, Brela, Uhamiaji na Kazi, ndizo pekee zilikuwa zinapatikana kwenye kituo hicho. Kwa sasa Serikali imeongeza taasisi nyingine ikiwemo OSHA, NEMC, TFDA, TBS, TANESCO na NIDA, hivyo vyote vinafanya jumla ya taasisi 11 kutoa huduma katika eneo moja pale kwenye kituo chetu cha uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao ili kupunguza muda na gharama katika kupata huduma kwa wawekezaji wetu hapa nchini. Vilevile Serikali imeunda Kamati ya Taifa inayojumuisha wakuu wote wa taasisi zinazotoa huduma kwa wawekezaji kwa lengo la kujadili maeneo ya kuboresha na urahisishaji wa upatikanaji wa vibali na leseni. Serikali imeongeza huduma za uwekezaji kwa kuanzisha Ofisi za TIC katika kanda zote hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya nane ilikuwa Serikali ifanye tathmini na kuangalia vikwazo vinavyokwamisha harakati za uwekezaji nchini, ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mpya, kurekebisha baadhi ya sheria, ili kuendana na mahitaji ya Blue Print. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi mwaka 2017 ilifanya tathmini ya kina na kuandaa Blue Print ambayo imebainisha masuala yote muhimu yanayokwamisha uwekezaji na kuainisha maeneo yote muhimu yanayohitaji kurekebishwa ikiwemo sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uwekezaji hapa nchini na kwa kila taasisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hatua hiyo huduma zimeainishwa kwa kuanzisha mifumo ya kielektroniki ambapo wawekezaji sasa wataweza kufanya maombi ya vibali mbalimbali wakiwa popote bila kulazimika kufika kituoni kwetu. Mifumo hii itaondoa urasimu na kuhakikisha utoaji wa vyeti vya uwekezaji, leseni na vibali mbalimbali na hatua hizi zitapunguza gharama na muda wa mwekezaji kufuatilia vibali na leseni kupitia katika kila taasisi na badala yake anavipata kwenye eneo moja. Aidha, Kituo cha Uwekezaji Tanzania hivi sasa kina ofisi saba za kanda, Mwanza, Dodoma, Moshi, Kigoma, Mtwara, Mbeya na Dar-es-Salaam, lengo ni kuendelea kusogeza huduma karibu kwa wawekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tisa, ni juu ya hali ya chakula kwa wananchi na wakulima wa Musoma kwamba, sio nzuri kutokana na mvua kutonyesha za kutosha na Serikali ijiandae kuwapelekea chakula na msaada wa njaa. Serikali inatambua uwepo wa mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha upungufu wa mvua katika maeneo mbalimbali nchini. Hali hii ilitabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kipindi kilichoanza mwezi Novemba, 2018 hadi Juni mpaka mwaka 2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia utabiri huo mamlaka za mikoa na wilaya husika zimeelekezwa kuchukua hatua za tahadhari, ikiwemo utunzani wa chakula, upandaji wa mazao ya muda mfupi na yanayostahamili ukame. Hivyo, nitoe wito kwa maeneo yanayopata mvua kwa sasa ni vyema kutumia vizuri mvua hizi zinazopatikana kwa kulima mazao yanayostahili, yasiyohitaji kiasi kikubwa cha mvua ili kuyawezesha mazao hayo kuweza kuiva na hatimaye kujihakikishia kuwa tunakuwa na kiwango kizuri ha chakula hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa nimetoa hoja hizi, naomba kuhitimisha hoja yangu kwa kueleza kuwa nimesikiliza na kufuatilia kwa umakini sana mjadala kuhusu Hotuba ya Waziri Mkuu. Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 mpaka Mwaka 2020 inatekelezeka vema chini ya jemadari Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Mwelekeo wetu ni mzuri, suala la msingi lililopo mbele yetu ni kuongeza umakini na kasi kwa malengo yote tuliyojiwekea ambayo dhamira ni kuwaletea maendeleo wananchi wote kwa Taifa na kwa ujumla yaweze kufikiwa na yaweze kuwafikia wananchi wote popote walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 7 Aprili, mwaka huu wa 2019 tuliadhimisha miaka 47 ya kumbukumbu ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar na terehe 12 mwezi huu, kwa maana ya keshokutwa tutaadhimisha miaka 35 ya kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, hayati Edward Moringe Sokoine. Watanzania tutaendelea kuwakumbuka viongozi hao kwa mchango wao mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya hapa nchini, kutetea wanyonge na kudumisha misingi ya amani, mshikamano na umoja wa Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na misingi imara iliyoachwa na viongozi tunaoendelea kuwakumbuka, Tanzania imeendelea kung’ara duniani katika eneo la amani na usalama. Kwa mfano, report ya The Global Peace Index 2018, inaonesha kuwa Tanzania imeendelea kuwa kinara wa amani kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na pia tunayapiku pia hata mataifa makubwa ambayo pia yenyewe yanasimamia amani kwa nchi changa. Amani tuliyonayo ni hazina kubwa tuliyoachiwa na viongozi wetu hawa. Wito wangu ni kuwa tuienzi na kuilinda amani ya nchi yetu ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada za waasisi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawakumbusha Waheshimiwa Mawaziri, viongozi wateule wa Serikali na watendaji wote kuwa, wananchi wamejenga imani nasi baada ya Rais kutupa majukumu ya kumsaidia, hivyo kila mmoja wetu hana budi kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Tufanye kazi kwa bidii, tuache mazoea ya kiurasimu, tuchape kazi kwa maslahi ya Taifa na kwa maslahi ya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa namalizia kufafanua hoja zangu napenda kuwakumbusha tena Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kuwa zimebaki siku tano tu kufikia tarehe 14 Aprili, mwaka 2019, siku ambayo Taifa letu litaweka historia kupitia timu yetu ya vijana, Serengeti Boys, itakayozindua mashindano ya mpira wa miguu, maarufu AFCON Under 17, dhidi ya timu ya Nigeria ikitafuta tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia. Uzinduzi wa michezo hiyo utakaofanyika Uwanja wa Taifa tarehe 14 Aprili, siku ya Jumapili ni muhimu kwetu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwenda Uwanja wa Taifa kushuhudia na kuwashangilia vijana wetu ili waweze kushinda vizuri. Timu yetu imeandaliwa vizuri, tunahitaji kushinda michezo miwili tu ili tuweze kucheza Kombe la Dunia, sasa ni zamu yetu, Mungu ibariki Serengeti Boys, Mungu ibariki Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme haya mawili yafuatayo: Wakristo duniani kote wanaendelea na kipindi cha toba ambacho ni muhimu katika imani kuelekea siku ya sikukuu ya pasaka. Niwasihi kuwa maisha mnayoishi katika kipindi hiki yalingane na maisha yetu ya kila siku. Kadhalika, kuelekea kumalizika kwa kipindi hicho niwatakie Watanzania wote heri na baraka ya Pasaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nao unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu wa 2019. Napenda kutumia fursa hii pia, kuwatakia Waislam wote nchini mfungo mwema na wenye mafanikio, ili kila atakayefanya ibada hiyo aifanye kikamilifu na kama inavyoagizwa katika Quran Tukufu ili tuweze kufuata misingi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zilizo chini yake na Mfuko wa Bunge, kama nilivyowasilisha katika hoja yangu ya tarehe 4 mwezi huu wa Aprili, 2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kusema kwamba sote tunajua wajibu wetu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha pia kukutana hapa kwenye kikao hiki muhimu, Kikao cha Saba cha Mkutano wa Kumi na Tisa wa Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuhitimisha mjadala wa hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka huu wa 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, aidha, ninakushukuru sana na Mheshimiwa Naibu Spika kwa pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge, Katibu wa Bunge na timu yako kwa umahiri mkubwa uliouonyesha katika kusimamia mwenendo mzima wa majadiliano yetu ya hoja hii ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, vilevile natoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge na Bajeti na Masuala ya UKIMWI kwa michango yao mizuri sana kwenye hoja hii ambayo imetolewa hapa kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kadhalika nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wenzangu mliochangia hoja, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu wote, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala wa Taasisi zote za Serikali pamoja watumishi wote kwa ushirikiano mkubwa walionipa katika kipindi chote cha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, ingawa niliwahi kuwashukuru Mawaziri ambao nafanya nao kazi, lakini nalazimika pia kurudia tena kuwashukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki, Waziri wa Nchi ambaye anashughulikia Uwekezaji. Pia ninaye Naibu Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini pamoja na Mheshimiwa Stella Ikupa, Mbunge na Naibu Waziri anayeshughulikia Walemavu.
Mheshimiwa Spika, bila kuwasahau Makatibu Wakuu ambao wanasimamia na kuratibu shughuli zote za Ofisi ya Waziri Mkuu, Bwana Tixon Nzunda, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu; yuko pia Mama Mwaluko, naye pia ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Bwana Massawe ambaye pia tunashirikiana naye vizuri sana akishughulikia eneo la Kazi; bila kuwasahau Watendaji wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu ambao pia tunafanya nao kazi kwa weledi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, pia nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa pongezi zenu kwa Serikali na kwa michango yenu yenye hoja za kuboresha mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali, hasa katika mwaka wa fedha ujao wa 2020/2021. Mjadala huu umeendelea kuthibitisha uimara na umakini wa Bunge letu katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, lakini pia kuishauri Serikali na kusimamia vizuri Serikali yetu ili iweze kufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Spika, pia nataka niendelee kutumia nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia na kuipongeza Serikali, pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais; na pia sisi wasaidizi wao ambao tunaendelea kushirikiana nanyi Waheshimiwa Wabunge katika kutekeleza shughuli mbalimbali za Serikali. Nami nataka nitumie nafasi hii kuwahakikishia kwamba salamu hizi nitazifikisha kwa Mheshimiwa Rais na Makamu wa Rais ili waendelee kuchapa kazi yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii ni bajeti ya mwisho ya miaka mitano, binafsi napenda kukushukuru wewe binafsi na timu yako ya Bunge. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango yenu hasa katika kuchangia mambo yote muhimu ambayo tuliyafikisha mbele yenu na kwa kitendo chenu cha kupitisha bajeti zote zilizopita zile nne. Bajeti zote zimefanya kazi yake na nyie wenyewe mmeona matokeo ya bajeti hizo kwa miradi mikubwa na mingi yenye thamani ya kutosha, ambayo pia inaendelea kutumika na wananchi. Ni matumaini yangu kwamba kwa spirit hiyo hiyo, basi mtaniunga mkono pia kwenye bajeti hii kwa kuipitisha kwa kishindo. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja hii ya Waziri Mkuu imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge 80. Kati yao Waheshimiwa Wabunge 62 walichangia kwa kuzungumza moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa 18 walichangia kwa njia ya maandishi. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda ninaomba uridhie nisiwataje majina, kwani tayari majina yao yameingia kwenye Hansard.
Mheshimiwa Spika, Serikali imejibu hoja nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge kupitia Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri hapa mbele yetu jioni hii. Aidha, kutokana na ufinyu wa muda pia, hoja nyingine zitajibiwa kwa maandishi na kutolewa ufafanuzi kwa kina na Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kuhitimisha bajeti za kisekta.
Mheshimiwa Spika, kupitia Waheshimiwa Mawaziri, wamejibu karibu maeneo mengi ambayo tumeyakusudia kuyajibu leo hii. Nami ninayo maeneo machache sana ambayo nitayakamilisha ili kuweza kutosheleza mahitaji ya ushauri, maeneo ambayo yanahitaji ufafanuzi kwenye mambo muhimu ambayo inabidi yatolewe leo ili yasaidie pia kuongoza katika upitishaji wa bajeti yetu ambayo tunayo leo.
Mheshimiwa Spika, moja ya jambo kubwa ambalo limezungumzwa wakati wa michango yetu ilikuwa ni suala la maafa. Suala la maafa yaliyojadiliwa hasa ni kutokana na uwepo wa mvua nyingi sana msimu huu ambazo zimenyesha na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali zikiwemo barabara, nyumba za wananchi, miundombinu ya taasisi zinazotoa huduma za jamii na pia imesababisha vifo. Haya niliyaeleza nilipokuwa nawasilisha hoja yangu siku ya mwanzo na kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba Serikali inaendelea kuchukua za kurejesha hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini za uharibifu wa miundombinu mbalimbali na pia kuainisha mahitaji ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, tumekubaliana kwamba tutafanya hivyo baada ya msimu wa mvua kukamilika au kwisha ili sasa tathmini ziweze kufanywa na kujua kiwango halisi cha mahitaji kwenye maeneo hayo yaliyoharibika ili tuweze kufanya urejeshi wa miundombinu hiyo.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeweka kwenye mipango yake ya utekelezaji wa suala la urejeshaji wa hali ya miundombinu kwa vipindi vya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kwa kuzingatia mahitaji husika. Aidha, Kamati za Maafa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji zitaendelea kusimamia suala zima la kuzuia, kujiandaa kukabilina na maafa na kurejesha hali pale ambapo wana uwezo napo.
Mheshimiwa Spika, pale ambapo uwezo umewazidi kiasi, basi, taratibu za kawaida kufika Ofisi ya Waziri Mkuu inayoratibu maafa itaambiwa na yenyewe itachukua hatua stahiki ili kushirikiana na Mikoa, Wilaya, Kata, pamoja na Vijiji kwenye maeneo husika. Baada ya tathmini katika kila eneo Wizara za Kisekta zitaendelea kushughulikia athari zilizojitokeza kwa rasilimali zilizopo kwa kuzingatia mipango na bajeti ambayo tumejipangia.
Mheshimiwa Spika, niendelee kutumia nafasi hii kuelekeza Viongozi na Watendaji wote kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya, mpaka Vijijini kusimamia ipasavyo upangaji na utekelezaji wa mipango na matumizi ya ardhi katika ngazi ya Mikoa, Wilaya na Vijiji. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wanatambua maeneo salama kwa ajili ya makazi na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara pia na shughuli za uwekezaji ambazo zipo kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, niendelee kusisitiza kuwa Wakala wa Barabara Nchini, TANROADS na TARURA kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara za madaraja na barabara zetu ili kuchukua hatua kwa wakati na hivyo kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwenye maeneo yetu. Aidha, wananchi wote wachukue tahadhari kwa kuhama sehemu za mabondeni na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinapotolewa na mamlaka hiyo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka za hali ya hewa, itatusaidia pia kuchukua tahadhari kabla ya maafa haya kutokea. Kwa sasa tunaendelea kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Pwani, eneo la Wilaya ya Rufiji na Kibiti kupitia Mheshimiwa Mbunge ambaye pia tunaye hapa, Mbunge wa Rufiji, kuona namna ya kuweza kusaidia yale maeneo yaliyopata athari hasa kwenye mafuriko yanayoisha sasa. Tunatambua kuwa mafuriko yamesambaa nchini kote, lakini tutaangalia wapi ambako yamezidi kiasi na athari kubwa zimejitokeza kama vile Rufiji ambako pia kumejitokeza tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naendelea kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha kwamba maeneo haya tunaendelea kuyasimamia vizuri. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuomba Mungu, mvua tunazitaka, lakini pale ambapo kuna madhara yanajitokeza, basi tuendelee kushirikiana kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo napenda nilizungumzie ni lile ambalo Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama amelizungumza. Yeye amezungumzia Tume ya Uchaguzi, mimi nataka nizungumzie uchaguzi wenyewe utakaofanyika mwaka huu mwezi Oktoba.
Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kwamba mwezi Oktoba mwaka huu nchi yetu itafanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Hivyo, tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba, Serikali inatoa wito kwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi kuzingatia katiba, sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika kuendesha shughuli za uchaguzi katika Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa.
Mheshimiwa Spika, lengo hapa ni kuhakikisha tu kwamba nchi yetu inaendelea kulinda na kuenzi tunu yetu ya amani, umoja, upendo na mshikamano wa Kitaifa, kama tulivyoachiwa na waasisi wetu wa Taifa hili. Nami nataka niendelee kuunga mkono kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba uchaguzi ujao utakuwa wa huru na wa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano kama ilivyokuwa na watangulizi wake itaendelea kulinda amani hiyo, mshikamano wetu na demokrasia yetu tuliyonayo katika nchi yetu. Kwa hiyo, niwasihi viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa na wananchi kwa ujumla kuendelea kulinda sasa amani ile na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili kla mmoja apate haki yake ya kuchagua na kuchaguliwa.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu wa 2020 yanaendelea vizuri. Hivi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inajiandaa na awamu ya pili ya maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanayotarajiwa kuanza wakati wowote ule mwezi huu. Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya majadiliano na wadau, maazimio mengi yamekubalika na yamefikiwa. Sasa ni jukumu la Tume kutekeleza makubaliano yale. Lengo la majadiliano yale ilikuwa ni kuwezesha Tume kujipanga, kupata vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu ya Covid 19.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatangaza ratiba ya uchaguzi kwa kuzingatia matakwa ya katiba na sheria. Kwa sasa bado ratiba haijatangazwa. Nalisema hili kwa sababu tumeona kwenye mitandao watu wakitamka Ratiba ya Tume ya Uchaguzi. Hiyo iliyotoka kwenye mitandao siyo sahihi. Wananchi wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali waendelee kujitokeza, nanyi Waheshimiwa Wabunge mliomo ndani ya Bunge hili, nami naungana nanyi na pia nawaombea sana na ninaendelea kuwaombea muweze kurudi tena baada ya uchaguzi ujao wa mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo ambalo pia ningependa nilizungumzie ambalo limezungumzwa sana na viongozi wetu au Waheshimiwa Wabunge hapa ndani ni homa kali ya mapafu (Corona).
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, nami naungana nanyi kueleza kwamba hali ya ugonjwa huu Duniani ni mbaya na kwamba wote mnakubaliana nami kuwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona umekuwa na athari kubwa kijamii lakini pia na kiuchumi Duniani kote. Aidha, katika kipindi hiki tumeshuhudia changamoto mbalimbali kutokana na hatua zinazochukuliwa na baadhi ya nchi katika kukabiliana na ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maambukizi ya virusi vya Corona kuingia nchini kwetu na hata kabla ya kuingia nchini, Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli alilitangazia Taifa kuwa ugonjwa huu ni hatari na Watanzania tujiandae na tahadhari kadhaa zilianza kuchukuliwa ndani ya Serikali ili kukabiliana na ugonjwa huu pindi utakapokuja kwa wakati huo. Lakini baada pia ya ugonjwa huu kujitokeza nchini, Serikali pamoja na mambo mengine, tulianza kujipanga vizuri kuanza kukabiliana na ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, kwanza tuliunda Kamati za Kitaifa, moja ya Kamati ya Kitaifa inayoratibu mapambano yote ya virusi vya UKIMWI ikisaidiwa na Kamati ya Makatibu Wakuu na Kamati ya wataalam. Kamati hizi ni za Kitaifa kwamba zinasimamiwa pia na Serikali mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, jukumu mojawapo la Kamati hizo ni kuwezesha nchi kupunguza madhara makubwa ya Kijamii lakini na kiuchumi ambayo yanaweza kusababishwa na ugonjwa huu wa homa kali ya mapafu.
Mheshimiwa Spika, upande wa kijamii tunaendelea kutoa elimu na upande wa kiuchumi kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameeleza ameunda timu ya wataalam, wachumi, wanaendelea kufanya mapitio ya athari zinazoweza kujitokeza katika kipindi hiki kufuatia tatizo hili. Tunajua biashara nyingi zimezorota na zinaendelea kuzorota lakini pia shughuli za kiuchumi nyingi nyingine zimeanza kusimama na kwa hiyo lazima tathmini ifanyike hatimaye Serikali itatoa muelekeo.
Mheshimiwa Spika, vile vile kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, elimu kuhusu namna ya kujilinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona inaendelea kutolewa kote nchini katika sehemu mbalimbali pamoja na kuwahusisha kwa karibu zaidi viongozi wa dini, wadau mbalimbali wa sekta na wataalam wenyewe wa Sekta. Niendelee kusisitiza Wizara, Mikoa, Wilaya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutoa elimu kwa jamii yetu kupitia watendaji wa Serikali walioko kwenye maeneo hayo na wananchi wote wapate kujua nini namna gani wanaweza kujilinda na maambukizi ya ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia leo tarehe 6 Aprili, tunao wagonjwa 24, mpaka asubuhi ilikuwa wagonjwa 22 lakini baada ya vipimo vya waliochukuliwa vipimo jana na kufikishwa kwenye maabara zetu mchana huu tumepata taarifa kwamba wagonjwa wawili wameongezeka, mmoja Tanzania Bara na mmoja Zanzibar na kufanya wagonjwa wote kuwa 24. Na hao ndiyo wamethibitika kuwa na ugonjwa huo. Kati ya wagonjwa hao, watatu wamepona na kuruhusiwa kutoka katika hospitali na mmoja amefariki dunia wakati wagonjwa 18 wanaendelea vyema na matibabu.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya kitaalam yanaonesha kuwa virusi vya Corona vinaweza kusambaa endapo mtu anagusa majimaji kama mafua, mate na makohozi ya mtu alie na virusi hivyo na kisa kujigusa kwenye mdomo, macho au pua. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imeendelea kuwafuatilia watu wote ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa karibu sana na wagonjwa hao. Hadi sasa watu 685 walikuwa wanafuatiliwa ambapo watu 289 wamemaliza siku 14 za kufuatiliwa na vipimo vyao vimethibitisha kuwa hawana maambukizi ya virusi vya Corona. Watu wengine 396 waliobaki wanaendelea kufuatiliwa ili kujiridhisha kuwa iwapo wana maambukizi ya virusi hivyo basi waweze kujitenga kwa kukaa kwenye maeneo maalum yaliyopangwa.
Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona ni pamoja na kudhibiti mipaka yetu, kufanya ukaguzi au screening kwa wageni wote wanaoingia nchini kutoka nje pamoja na kuwaweka katika uangalizi wa siku 14 kwenye maeneo maalum. Aidha, ndege za nje zinazoingia nchini zimeshajifuta zenyewe kwa sababu kwenye nchi wanakotoka wamefunga mipaka na kwamba hakuna kuingia wala kutoka kwa ndege.
Mheshimiwa Spika, pia, ndege zetu nazo tumezizuia kufanya safari za nje, kwa hiyo ndege zetu sasa zinafanya safari za ndani pekee. Tumezuia wafanyakazi kwenda nje ya nchi, tumeimarisha mipaka, sambamba na kuhakikisha wasafiri wote wanaoingia nchini wanalazimika kuwekwa chini ya uangalizi wa lazima kwa siku 14 kwa lengo la kudhibiti mienendo ya wasafiri nchini chini ya ulinzi kwa masaa 24.
Mheshimiwa Spika, nimetoka kuzungumza leo mchana huu na Wakuu wa Mikoa wote tena, nilizungumza nao wiki iliyopita lakini pia leo nimefanya tathmini ya kazi hiyo inavyoendelea na nimepata taarifa ya kila Mkuu wa Mkoa namna ambavyo wamechukua jambo hili kwa umakini mkubwa na kila mkoa umeshatenga maeneo haya na hasa kwenye wilaya zilizoko pembezoni kwenye mipaka yetu ambako abiria wengi sasa wanatamani kuingia kupitia barabara. Maeneo yote yameimarishwa, lakini pia tumetenga na maeneo ya kuhifadhi, kuwatenga hawa wote wanaoingia nchini kwa siku 14 na ujumbe huu utakapofika naamini wao hawatakuja tena nchini.
Mheshimiwa Spika, nchi zote jirani zimefunga mipaka yake, hawaingii wala hawatoki kwa hiyo, automatically hatuwezi kupata mtu yeyote anayeweza kuja. Hata hivyo, wale wote wanaokuja wanaendelea kuwekewa kwa siku 14 na kufuatiliwa afya zao na tumeimarisha ulinzi wa maeneo hayo ili kuzuia hao walioko kwenye ulinzi huo kutoka au watu wengine kuingia kwa maana ya kuja kufanya mawasiliano na walioko pale ndani.
Mheshimiwa Spika, vilevile kutokana na umuhimu wa kuwatenga watu wanaofuatiliwa, Serikali imeagiza mikoa yote nchini kutenga maeneo maalum ambayo leo wametoa taarifa na uangalizi kuimarisha na waimarishaji wote na wafuatiliaji wa afya zao wote wapatiwe vifaa maalum ili kuendelea kufanya kazi hiyo bila kuwa na athari zozote zile za maambukizi kwao.
Mheshimiwa Spika, hatua hii ni muhimu katika kudhibiti kuenea zaidi kwa maambuzi ya virusi vya Corona na kati ya wagonjwa hawa, walio wengi ni wale waliotoka nje yaani watu wa Mataifa ya nje lakini na Watanzania ambao walisafiri kwenda nje ya nchi na kuja hapa ndani na maeneo haya yaliyotengwa yatatumika na kila mmoja bila kujali wadhifa wake na nalitamka hili kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza hali iliyoko kule visiwani.
Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikuwa na Waziri ambaye alitakiwa kwenda kwa matibabu, alikataa baadaye akaenda Mnazi mmoja kwa matibabu na baadaye akatakiwa kwenda kujitenga bado alikataa, lakini Serikali ilichukua hatua na ikamtoa na kumpeleka sehemu ya kutengwa, kwa sasa yuko eneo la kutengwa. Na narudia kutamka hili ya kwamba maeneo haya ya kutengwa yamewekwa kwa madaraja kadri ya uwezo wa anayetengwa. Tumetafuta mabweni ambayo watu wanalala bure, kwa hiyo, asiyekuwa na uwezo wa kulipa atalala huko. Tumetafuta maeneo ambayo yanaweza kulipiwa lakini ya hadhi tofauti tofauti kwa hiyo yeyote anayehitaji kwenda lakini yote yameteuliwa na yanasimamiwa na sio maeneo mengi, ni machache ili kurahisisha usimamizi na kwa hiyo kila mtu atakwenda eneo hilo kulingana na uwezo wake. Tumetafuta watu ambao watatoa huduma ya chakula ilia pate chakula kwa gharama ambayo anaweza kuimudu na maeneo haya yana ulinzi kama ambavyo nimeeleza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kila mmoja anayetakiwa kujitenga ameenda maeneo ambayo yameandaliwa rasmi kwa gharama ambazo yeye anaweza kuzimudu. Tunafanya hili ili kuondoa manung’uniko yaliyokuwa yamejitokeza awali kwamba watu walikuwa wanapelekwa maeneo ya gharama kubwa wakiwa hawana uwezo. Kwa hiyo, tumeimarisha hilo na sasa malalamiko haya yamepungua.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaimarisha maabara mbalimbali nchini ili ziweze kutoa huduma za upimaji ikiwemo maabara zilizopo kwenye mikoa na mikoa hiyo ni kama vile Arusha tunayo maabara inaweza kupima sasa vipimo vyote vya Kanda ya Kaskazini, Dodoma, hapa katikati ya nchi, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani pamoja na Tanga. Maeneo haya yote yana maabara na kwa hiyo itarahisisha kupeleka vipimo kwa umbali mfumo na kupata majibu kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na vipimo vyote ni lazima ithibitishwe na Mganga Mkuu wa Serikali na atakayetoa taarifa ni Waziri wa Afya pekee. Kwa hiyo, natambua mchango wako Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani juu ya watu kutoa Taarifa kiholela, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, kila mmoja anatamka anavyotaka. Tumetoa maelekezo kwamba Taarifa zote za ugonjwa huu zitatolewa na Waziri wa Afya. Kama ni lazima atatoa Waziri Mkuu, kama ni lazima sana, basi atatoa Makamu wa Rais au Rais mwenyewe. Utaratibu huu utasaidia kuleta taarifa za uhakika zilizothibitishwa na watoaji hao ndiyo ambao watahusika. Kwa hiyo, tutalisimamia hili ili tuondoe utamkaji holela wa kila mmoja kadri anavyojisikia.
Mheshimiwa Spika, vipimo hivi pia vinapimwa na hospitali zote za Rufaa, Kanda, za Mikoa nazo zinaratibiwa kutoa huduma za upimaji sambamba na maeneo ya mipakani. Shughuli hizi za upimaji zinafanyika kwa usimamizi wa maabara kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa lengo la kuthibitisha ubora na vipimo hivyo kuratibiwa na utoaji wa matokeo pia nao umeratibiwa.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu pia imeendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Afya Duniani, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika katika kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu na kwa hiyo tunabadilishana mawazo lakini pia tunapeana mbinu mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, yako malalamiko ya baadhi ya Watanzania wakitaka tuchukue hatua ambazo zinachukuliwa na nchi nyingine. Lakini nataka niseme kwamba watu lazima tutambue kwamba nchi hizi zina mazingira tofauti. Tanzania ina mazingira tofauti na nchi nyingine ambazo watu wengi wanazilinganisha na umuhimu ni kwamba Taifa lazima tujipange tuhakikishe kwamba tundhibiti maambukizi kusambaa nchini na hatua tuliyoifikia sasa tunafurahi kwa sababu tunaona tunaanza kupata ushirikiano na wananchi, pindi ikionekana kuna mtu ametoka nje ameingia nchini bila kupitia kwenye vituo vya uhifadhi tunapewa taaarifa na sisi tunachukua hatua za kuwafuata popote walipo na pale ambako kuna mtu ana hisiwa kuwa na tatizo la Corona ili kuitaka Serikali iweze kuthibitisha basi wananchi wanatupigia kwa namba ile 199 na Serikali inachukua hatua ya kuwafuatilia na kuwafanyia vipimo na ikithibitika tunawatenga mahali rasmi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nieleze tu kwamba nchi yetu iko makini na Serikali inafanya kazi hiyo kwa umakini na tutaendelea kuwahusisha pia wadau mbalimbali ambao watasaidia pia kuungana nasi katika kukabiliana na pambano juu ya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na maandalizi kadri ya hali ilivyo kulingana na mazingira tuliyonayo kama ambavyo tumeyaeleza lakini Serikali inaendelea pia kufanya tathmini za kila wakati kuhusu changamoto zinazoweza kusababishwa na ugonjwa huu wa Corona na namna ambavyo tunaweza kuzitatua. Tunajua kuna changamoto za kiafya ambako wananchi wetu wengi wanapata madhara haya. Lakini pia kuna changamoto za kiuchumi ambayo nimeeleza mwanzo na Waziri wa Fedha ameeleza yote haya ni yale ambayo tunaendelea kuyafanyia tathmini. Na tathmini hizi zinafanywa na zile Kamati tatu ambazo tumeziteua. Moja, Kamati ya Kitaifa ambayo inasimamiwa na Waziri Mkuu, ya pili Kamati ya Makatibu Wakuu ambayo inasimamiwa na Makatibu Wakuu Viongozi wa Bara na Visiwani pamoja na Kamati ya Wataalam ambao pia kuna madaktari kutoka pande zote mbili ili kuweza kubadilishana. Kwa hiyo, kadri tathmini inavyofannywa, tukipata matokeo tunachukua hatua. Hatuwezi kwenda na hatua zote tunaweza tukaleta mkanganyiko ndani ya nchi. Muhimu zaidi ni kujiridhisha kwamba maambukizi haya hayaendelei.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tunaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali na Serikali kushirikiana na wadau wengine imeendelea kutafuta fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu ili kuweza kumudu kupambana dhidi ya maambukizi. Vilevile Serikali imeendelea kupokea michango ya mtu mmoja mmoja kutoka Taasisi mbalimbali kwa lengo la kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa huu. Wiki mbili zilizopita nilipokea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali yenye thamani ya bilioni 1.8 na tarehe 8 wadau kadhaa wamejitokeza kwa hiyo, tutapokea tena misaada hapa Dodoma kwa kila ambaye ameamua kuchangia watakuja watachangia pale Ofisi ya Waziri Mkuu na tutawatangaza rasmi kwa mchango wao na michango hii yote inayochangwa na wadau hawa itatumika kama ambavyo imekusudiwa. Tunaendelea kuratibu kwa kupata vifaa mbalimbali ili kuwezesha watendaji wetu au wataalam wetu kufanya kazi hiyo bila kuwa na madhara wakati wote wanapohudumia ndugu zetu ambao wamepata madhara hayo.
Mheshimiwa Spika, niendelee kusisitiza kuwa viongozi wa mikoa na wilaya waendelee kusimamia kwa karibu, Kamati za Maafa ziendelee kushirikiana kwa pamoja na madaktari wetu kuhakikisha kwamba wanasaidia kupambana dhidi ya maambukizi haya na kama ambavyo nimewaeleza, nimezungumza na Wakuu wa Mikoa, tumewasisitiza na kuwapata muelekeo wa namna ya kufanya kazi zao kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kuwa suala hili ni mtambuka nitoe wito kwa waajiri, wafanyakazi, wafanyabiashara, wavuvi, wakulima, wasafirishaji na wananchi wote kwa ujumla kuchukua tahadhari zaidi kwani sote tunao wajibu wa kujilinda na kuwalinda wengine ambao wako kwenye mazingira hatarishi. Kadhalika maeneo ya huduma kama vile masoko, hospitali, vituo vya mabasi na vyombo vya usafiri kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima na kuchukua tahadhari ikiwemo kutumia vifaa vya kinga. Haya ni mambo ambayo pia tumeyatolea msisitizo na pia tumewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia, kila mmoja kwenye mkoa wake kupitia wilaya zake na wananchi nao waelimishwe ili waweze kujua njia zote sahihi za kujikinga na maambukizi.
Mheshimiwa Spika, ugonjwa huu hadi sasa umeonesha kutokuwa na dawa na unaleta madhara makubwa Duniani. Hata hivyo, tukiangalia hali ilivyo nchini mwetu hatuna bdi pia kila mmoja kuchukua tahadhari ya kutosha na tunaendelea kuwatahadharisha wananchi wote kwamba ni muhimu kufuata maelekezo ya wataalam wetu, madaktari wetu na maelekezo ambayo tunayatoa wakati wote.
Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii kushukuru sana vyombo vya habari kwa namna ambavyo wanafanya kazi yao katika kuelimisha wananchi wetu. Pia niwashukuru wasanii ambao pia wameaanza kutunga hata nyimbo za kufikisha ujumbe wa kuchukua tahadhari huku wakitoa elimu kwa wananchi namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona. Lakini pia tuendelee kuzingatia miiko ambayo tumeitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, fursa ambayo tumeitoa kwenye maeneo machache ni kuwezesha kupata huduma lakini fursa hiyo isitumike vibaya kama vile kuendesha shughuli za kidini, tunataka tu siku za Ijumaa, Jumamosi kwa Sabato na Jumapili kwa wale wanaokwenda kwenye ibada za Jumapili na sio makongamano ya Kidini, hiyo tumezuia. Tunasema watu wakasali na watumie nafasi hiyo kuliombea Taifa. Lakini pia wanapokuwa huko, wazingatie ile miiko yote ya kukaa umbali na tumesema kama nyumba ni ndogo basi wengine wapate nafasi ya kukaa nje kwa nafasi ile ile ili mradi ule muda unaotumika kwa sala au swala utumike huo na watu waondoke waende maeneo yao. Tutaendelea kutathmini hali hiyo kadri siku zinavyokwenda tukiona maeneo hayo yana madhara makubwa, tutakuja kutamka vinginevyo kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, suala la usafiri tulidhani tukiacha watu wasafiri kutoka eneo moja mpaka lingine linaweza kusaidia na tumeelekeza mabasi yote yasijaze abiria, watu wakae kwenye viti, wasafiri wafike, inaweza kutusaidia zaidi na wakiwa kwenye mabasi kila mmoja azingatie. Tumeanza kuona baadhi ya wasafirishaji wanajali na wengine waendelee kujali na kwa kufanya hivyo itatusaidia zaidi kujikinga na maambukizi kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki ambacho tunaendelea kufanya tathmini ya hali ilivyo, Serikali inasisitiza wananchi kuweka umuhimu wa kufuatilia haya ambayo pia tunahitaji yafanyiwe kazi na watu wote kila mmoja aweze kuzingatia sheria na miongozo ambayo tumeitoa na tahadhari za kitaalam ambazo pia zimetolewa na watu wetu.
Mheshimiwa Spika, wakati tunapokea hoja, kwenye eneo hili nataka niendelee kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kupokea ushauri wenu na ushauri huo tutauangalia kwa kupitia Kamati zetu za Tathmini ambazo tatu zimeundwa ili tuweze kuchukua hatua kadri tunavyokwenda. Lakini tunashukuru sana kwa michango yenu na ndiyo hasa mijadala yetu hapa kwenye awamu hii ilichukua nafasi kubwa. Kila aliyechangia anazungumza suala la Corona na anazungumzia pia suala la mradi.
Kwa hiyo, tumelichukua hili kama jambo muhimu na ni jambo la Kitaifa, lenye madhara ya Kitaifa na tumeona namna ambavyo tumeshirikiana wote bila kujali utofauti wetu kiitikadi, kidini, kisiasa lakini tumeendelea vizuri na sisi tumepokea mawazo yenu tutahakikisha tunayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, baada ya hoja hii kuwahakikishia Watanzania kwamba Serikali imeendelea kuwa makini nayo na kuchukua tahadhari zote na tunaratibu vizuri. Hoja nyingine ilikuwa ni hoja iliyojadiliwa na baadhi ya Wabunge kuhusu Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa kwamba ihakikishe inasimamia mwenendo wa vyama vya siasa kwa kuendelea kuchunguza na kufuatilia mienendo ya vyama hivyo ili vizingatie sheria, kanuni, taratibu na weledi kwa ustawi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili Serikali imepokea ushauri wa Kamati lakini pia Waheshimiwa Wabunge. Serikali inaahidi kuufanyia kazi kwa kuiwezesha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kusimamia utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha kwamba vyama vyote vya siasa vinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni zilizokubalika kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, pia mwaka huu 2019/2020, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilichunguza na kuvitaka baadhi ya vyama vya siasa vilivyotuhumiwa kuvunja sheria kufuata utaratibu. Maelekezo ya msingi yalitolewa na Msajili, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba maelekezo yale yatazingatiwa. Katika kuhakikisha kwamba vyama vya siasa vinakidhi na kutekeleza matakwa ya sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ofisi inaendelea kufanya uhakiki wa vyama vya siasa kuhusu utekelezaji wa masharti hayo na matakwa mengine ya kisheria ili vyama hivyo viweze kufuata sheria hiyo ikiwemo na Sheria ya Gharama za Uchaguzi hasa kipindi hiki tukielekea kwenye chaguzi.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilijitokeza ni ile inayosema Serikali iangalie upya taratibu za utoaji wa vibali vya kazi na ukaazi kwa wataalam kutoka nje ikiwemo kuzingatia wataalam ambao hawana elimu rasmi lakini wana ujuzi katika sekta kama vile ukataji wa vito sambamba na kupunguza gharama za vibali vya kazi ili kuvutia wawekezaji. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mavunde ameitolea ufafanuzi hoja hii lakini naomba niseme machache juu ya hili kwamba utoaji wa vibali vya kazi kwa raia wa kigeni unazingatia matakwa ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008. Sera hiyo inabainisha kuwa ajira za wataalam wa kigeni hulenga zaidi katika kuziba pengo la ujuzi adimu na teknolojia. Kwa msingi huo, Serikali imeendelea kuzingatia vigezo muhimu vyenye kuhusisha elimu, ujuzi na uzoefu wa kazi husika katika utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni ambao wanaingia hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kuhusu gharama za vibali vya kazi, Serikali inaendelea na kukusanya maoni kwa lengo la kuifanyia mapitio sheria husika ambapo masuala ya ada pia yanaweza kuangaliwa. Hata hivyo, changamoto kubwa kwa wawekezaji si kiwango cha ada bali ni muda mrefu ambao umekuwa ukitumika kuomba kibali hicho hadi kutolewa. Tumefanya maboresho ili pia vinapoombwa vibali hivi viweze kutolewa kwa muda mfupi zaidi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakamilisha mfumo wa TEHAMA kwa ajili ya utoaji vibali vya kazi ili kurahisisha utoaji wa vibali hivyo kwa kipindi kifupi sana. Hivi sasa kazi ya kuweka miundombinu stahiki inaendelea na utaratibu wa kuzindua mfumo huo utafanywa siku za karibuni ili mfumo huo uanze kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni Serikali iboreshe miradi ya umwagiliaji pamoja na miundombinu yake ili kuongeza uzalishaji wa chakula hapa nchini. Ni kweli kwamba nchi yetu tunategemea sana mvua badala ya kuimarisha umwagiliaji katika kilimo na kwa maana hiyo mwaka ambako hakutakuwa na mvua nchi yetu inaweza kuingia kwenye baa la njaa. Serikali inatambua tulikuwa na Taasisi ya Umwagiliaji ambapo awali ilikuwa chini ya Wizara ya Maji. Hatua ya kwanza tumeiondoa kutoka Wizara ya Maji tumeipeleka Wizara ya Kilimo, Wizara ambayo inahusika na suala la kilimo ili iweze kuiratibu kwa ukaribu. Bado Tume ipo na inaendelea kufanya kazi yake, tumefanya mabadiliko kadhaa ndani ya Wizara ya Kilimo ikiwemo na kuondoa Wakurugenzi saba ambao awali walikuwa wanaratibu kutokana na matatizo mbalimbali yaliyojitokeza kwenye Tume hiyo na sasa tumeunda timu.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumefanya maboresho ya ufunguzi wa ofisi zake ambapo awali ilikuwa ipo Makao Makuu peke yake na kwenye Kanda. Sasa tumefungua ofisi za mikoa 26 ambazo zitakuwa na Maafisa wa Umwagiliaji lakini tumepeleka Maafisa Umwagiliaji 34 kwenye ngazi za Wilaya na kwenye Wilaya ambazo zina miradi ya umwagiliaji na wanaendelea kufanya kazi yao ili waratibu kwa ukaribu miradi hiyo chini ya usimamizi wa Halmashauri za Wilaya wakishirikiana na Afisa Kilimo.
Mheshimiwa Spika, lengo ni kuhakikisha kila mradi wa umwagiliaji uliopo katika Halmashauri, unapata msimamizi mtaalam ambaye ni kutoka Tume ya Umwagiliaji. Tayari wataalam wa umwagiliaji wamenza kupelekwa maeneo yote na kazi zimeanza. Hatua hizo zinalenga kuiwezesha Tume hiyo kusimamia ipasavyo shughuli za umwagiliaji nchini ili kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 475,056 za sasa hadi hekta 1,000,000. Malengo yetu ifikapo mwaka 2025 tuwe tumefikia hatua hiyo.
Mheshimiwa Spika, nikiwa nahitimisha hoja yangu, hayo ndiyo machache ambayo yamejitokeza, yapo mengine machache kama vile eneo la ushirika ambalo lilichangiwa na Mheshimiwa Mbunge kutoka Mkoa wa Kagera alipokuwa anaonesha kutoridhishwa na ushirika uliopo Mkoani Kagera. Nikiri kwamba ushirika huu toka awali haukuwa na mwelekeo mzuri. Ushirika baadaye iligeuka na kuwa ni maeneo ya watu wanaopata nafasi ya kuongoza kuwa ni maeneo ya kula.
Mheshimiwa Spika, tulichofanya ni kufanya mapitio ya ushirika huo na kufanya maboresho lakini pia kufanya uhakiki wa kina katika kila ushirika kuona ushirika ulikuwa na nini na maboresho yake na hatimaye kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa ushirika. Kwa sasa, baada ya uhakiki wa maeneo yote ya Vyama Vikuu vya Ushirika na kubaini kwamba kulikuwa na ubadhirifu mkubwa ikiwemo na WETCO -Mkoani Tabora, NCU - Mkoani Mwanza, KNCU - Mkoani Kilimanjaro lakini pia KBCU ya kule Kagera.
Mheshimiwa Spika, pia hapa karibuni tumeenda kwenye mkonge; maeneo hayo tumefanya uhakiki na kugundua kwamba zipo mali nyingi za ushirika zimetoweka au zimechukuliwa na watu bila utaratibu na kukatisha tamaa wakulima kujiunga kwenye ushirika huo. Baada ya hatua hii, tumeanza kusimamia ushirika huu kurudi kwenye nafasi yake. Kwa hiyo, tumeendelea kuboresha ushirika huo ikiwemo na kusimamia Tume ya Ushirika ambayo inaratibu ushirika.
Mheshimiwa Spika, upo ushirika kwenye maeneo mengi; upo ushirika kwenye mazao ya kilimo ambapo pia kuna Vyama Vikuu vya Ushirika vya Mazao ya Kilimo lakini kuna ushirika wa fedha ambao unasimamiwa na taasisi za fedha, wote upo chini ya Tume ya Ushirika. Kwa sasa tupo kwenye mjadala na wadau wa kuiondoa Tume ya Ushirika kutoka Wizara ya Kilimo ikae ama Ofisi ya Waziri Mkuu au Ofisi ya Rais ili iweze kufanya kazi ya kusimamia ushirika wote ulipo katika Wizara zote ikiwemo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na maeneo mengine na kupata mafanikio makubwa zaidi badala ya kuuweka kwenye Ushirika tukiwa tunajua kuna wana ushirika waliojiwekea fedha za akiba na kukopa kwenye sekta ya fedha. Hayo ni malengo ya kuboresha ushirika kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, sasa ushirika wa mazao ambao tulioupata hapa ni kwamba kazi yao wao ni kusimamia biashara ya mazao lakini pia ushirika huu unatakiwa usimamie kuanzia maandalizi ya kilimo mpaka masoko yake. Kasoro zote zilizojitokeza zinaendelea kurekebishwa ili ushirika huu uwe na tija kwa wakulima na tumeanza kuona manufaa kwenye maeneo mengi ambayo ushirika huu unaanza kusimamiwa, masoko ya mazao mengi yaanza kufikiwa vizuri pamoja na kasoro hizo lakini tunaendelea kuimarisha. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ambao pia ni Wajumbe wa Ushirika kwenye maeneo yenu au mnao wana ushirika wenye malalamiko kwenye maeneo yenu, endeleeni kuwa na matumaini kwamba mwisho wa zoezi la kuimarisha ushirika huu, tutakuwa na ushirika ambao utakuwa unaringiwa na wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna sekta ya ajira ambayo ilizungumzwa vizuri kwenye hoja yangu nilipokuwa nawasilisha. Naomba tu nifanye marejeo ni kwamba Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa anaingia madarakani moja ya kilio cha Watanzania ilikuwa ni kukosekana kwa ajira. Alipokuja na kauli mbiu ya kuboresha uchumi kupitia viwanda; moja kati ya mkakati ni kufungua milango ya ajira kwenye viwanda vinavyojengwa. Leo hii tunashuhudia viwanda vingi vinavyojengwa nchini vinatoa nafasi za ajira za Watanzania bila kujali elimu. Wapo wanaoajiriwa wasiokuwa na elimu kabisa, elimu ya kati mpaka elimu ya juu na ndiyo malengo yaliyokuwepo ya uanzishwaji wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia ajira tumeifungua kwa kuanzisha miradi mingi ya kimkakati. Miradi yote ya kimkakati imetengeneza ajira kwa kuajiri vijana wanaosaidia kufanya kazi lakini wataalam, bado kuna wajasiriamali, wafanyabiashara na wenye makampuni wamepata ajira kupitia miradi hii mikubwa. Hata ile ya ujenzi wa vituo vya afya, hospitali, miradi ya maji nayo pia imetengeneza fursa za ajira kwa wale ambao wapo kwenye maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la ajira ni pana na ni endelevu kama nilivyosema wakati nawasilisha hoja. Hata hivyo, tunachofanya pia, tumeweka programu ya kuwapa ujuzi Watanzania wasiokuwa na ujuzi ili waweze kuajirika kwenye sekta mbalimbali lakini pia waweze kujiajiri kwa kutumia ufundi walionao.
Mheshimiwa Spika, pia tumetoa fursa za Ofisi za Serikali kushiriki kikamilifu katika kuboresha ajira hizi kwa kutengeneza mifumo itakayowapatia mtaji vijana au makundi mbalimbali ili nao pia waweze kujiajiri kwa kuanzisha biashara mbalimbali au miradi mbalimbali ambayo itaweza kuwapatia vipato. Katika kuhakikisha tunahamasisha eneo la ajira, tumetoa fursa kwa kuzungumza na taasisi za fedha kutoa mikopo mbalimbali kwa wajasiriamali ili wawe na mitaji ya kuanzisha biashara zao ikiwa ni sehemu mojawapo la ajira.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo la ajira ni sehemu ya ajenda yetu, ni eneo endelevu na tunaendelea kuweka mikakati kadiri siku zinavyokwenda kuhakikisha kwamba tunawatoa vijana wengi kwenye maeneo ya kukaa na kucheza pool bila sababu kwa kukosa ajira na kila mmoja ashiriki kwenye maeneo haya. Leo hii tumeanza kushuhudia vijana wengi nchini wameachana na kucheza pool, kila mmoja anafanya kazi yake na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu” imesaidia kuwafanya vijana hawa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali za ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiwa nahitimisha naomba nieleze suala la ziara za Viongozi wa Kitaifa ambazo zimefanyika nchini kote kwamba Serikali yetu tuliweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunawafikia wananchi. Tulikuwa tunaweka msisitizo wa kila mtumishi wa Serikali lazima ajenge tabia ya kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano iliweka juhudi za kipekee za kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika sekta ya umma kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi katika kuwahudumia wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha kuanzia Julai 2019 hado Februari, 2020, ziara mbalimbali zimefanyika zikihusisha viongozi wa Kitaifa, Mawaziri katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara lakini pia hata Visiwani. Lengo la ziara hizo zilikuwa ni kukagua miradi ya maendeleo na shughuli mbalimbali za kiuchumi na jamii; kuzungumza na watumishi wa umma; kusikiliza malalamiko na kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali kwa viongozi na watendaji husika ili waendelee kuwahudumia Watanzania kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, ziara hizi zimeleta tija sana kama ifuatavyo. Moja, tumeongeza pia hata nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika ngazi mbalimbali. Watumishi wameongeza ari ya kuwatumikia wananchi, kusikiliza malalamiko, kero na kutoa ufafanuzi lakini kubwa zaidi kuwahudumia wananchi bila ya urasimu. Hili litaendelea kusimamiwa wakati wote ili kujenga nidhamu ya utendaji ndani ya nchi, hasa ndani ya Serikali ya kuwahudumia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mbili, tumeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya huduma za jamii ikiwemo miradi ya elimu, afya, maji pamoja na miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na umeme. Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi kwamba Serikali yetu imeyafanya haya na tunaendelea kufanya haya ili kuleta ustawi wa jamii yetu.
Mheshimiwa Spika, tatu, tumeongeza kwa kasi ukusanyaji wa mapato ya Serikali Kuu na mapato ya ndani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kutokana na uhimizaji wa matumizi ya mashine za kielektroniki pamoja na mwitikio wa wafanyabiashara, wafanyakazi na wananchi kulipa kodi na ushuru kwa hiyari bila shuruti. Naona sasa Watanzania wengi wanapenda kulipa kodi kwa sababu kodi ile inaratibiwa vizuri na inarudi kwao kwa kuwajengea miradi. Kwa hiyo, ari imeongezeka na tunaamini ari itazidi kuongezeka ya kila mmoja kujua kwamba wajibu wake ni kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna ongezeko la uzalishaji na tija ya mazao mbalimbali ya kilimo cha biashara na chakula katika maeneo mengi. Pia sekta ya mifugo na uvuvi imepata mabadiliko makubwa. Vilevile na tunaendelea kuwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula na kuongeza mapato ya kuchochea maendeleo ya viwanda. Pia tunaendelea kuimarika kwa hali ya usalama, amani na utulivu nchini pamoja na kuongezeka kwa kasi ya mshikamano ndani ya Taifa ili pia tuweze kufanya kazi hiyo kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, najua tuna kazi kubwa ya kupitia bajeti yetu na mimi naomba nihitimishe kwa kusema kuwa sote tumekuwa tukifuatilia kwa karibu mjadala huu kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu. Aidha, wakati wa kuwasilisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nilitumia nafasi hiyo kueleza kirefu mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha takribani miaka hii minne na tunaingia sasa wa tano. Hivyo, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi kote nchini kwa ujumla kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 imetekelezeka vema chini ya Jemedari wetu, Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Naomba tu niendelee kwa kusema kuwa tutaendelea kuwahudumia Watanzania na Watanzania waendelee kuiamini Serikali yetu, Rais wetu na wasaidizi wa Mheshimiwa Rais kuwa tupo kwa ajili yao na tutaendelea kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwezi huu wa Aprili una matukio makubwa kidogo. Moja tarehe 7 Aprili, 2020 yaani kesho tutaadhimisha miaka 48 ya Kumbukumbu ya Kifo cha Hayati Mzee wetu Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar. Pia tarehe 12 Aprili, 2020 tutaadhimisha miaka 36 ya Kumbukumbu ya Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Hayati Edward Moringe Sokoine.
Mheshimiwa Spika, ndugu zangu Watanzania tuendelee kuwakumbuka viongozi hawa. Kesho itakuwa ni siku ya dua maalum kwa ajili ya kumuombea baba yetu Hayati Sheikh Abeid Amani Karume. Kwa hiyo, kila mmoja kwa dhehebu lake atumie nafasi hiyo kumuombea Mzee wetu Rais wa kwanza wa Zanzibar. Pia itakapofika tarehe 12 Aprili, 2020, nako pia familia inaandaa dua. Kwa hiyo, kila mmoja kwa dhehebu na imani yake aendelee kumuombea aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Moringe Sokoine na tuendelee kumuomba Mungu aendelee kuweka roho zao mahali pema peponi, Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Mawaziri, viongozi wateule wa Serikali na watendaji wote kutekeleza wajibu wetu ipasavyo. Tufanye kazi kwa bidii zaidi, tuache mazoea, tuchape kazi kwa lengo la kuwa hudumia wananchi wetu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Wakristo wote duniani wataendelea na kipindi cha toba ambacho ni muhimu katika imani kuelekea sikukuu ya Pasaka. Niwasihi kuwa maisha mnayoishi katika kipindi hiki yalingane na maisha yetu ya kila siku. Kadhalika kuelekea kumalizika kwa kipindi hiki, niwatakie Watanzania wote kheri ya Pasaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwezi huu pia tuna Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nao unatarajiwa kuanza wakati wowote ule kuanzia katikati ya mwezi huu. Napenda kutumia fursa hii pia kuwatakia Waislamu wote nchini mfungo mwema na wenye mafanikio ili kila atakayefanya ibada hiyo, aifanye kikamilifu na kama inavyoagizwa katika mafundisho ya Quraan Tukufu basi naamini kila mmoja takuwa anafuata imani hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya mapato na matumizi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge letu kama ilivyowasilishwa katika hoja yangu siku ya tarehe 1 Aprili, 2020.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwa utamaduni uleule na tabia ileile ya ushirikiano wa dhati na kwamba kama ambavyo mmekuwa mkipitisha bajeti zote nne zilizopita, naamini pia pamoja na bajeti hii ya tano inayolenga kuhudumia Watanzania wote, ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtaniunga mkono kwa kuipitisha kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutujaalia afya njema tunapoelekea kuhitimisha hoja ya kujadili Hotuba ya Mheshimiwa, Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, tarehe 13 Novemba, 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii pia kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi pamoja na Mheshimiwa Spika kwa namna ambavyo mmesimamia vyema mjadala huu uliotuchukua siku 4. Hali kadhalika napenda kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumshukuru Mheshimiwa, Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa hotuba yake nzuri aliyoitoa wakati wa kuzindua Bunge la Kumi na Mbili la Jamhuri ya Muungnao wa Tanzania siku hiyo ya tarehe 13 Novemba, 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 169 wamechangia mjadala huu. Hivyo natumia nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia mjadala huu na kuunga mkono maeneo mbalimbali yaliyobainishwa katika hotuba ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia michango ya Waheshimiwa Wabunge, kwanza nakiri kupokea salamu za pongezi, salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nami nawahakikishia kwamba nitazifikisha baada ya kufunga hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, michango ya Waheshimiwa Wabunge itasaidia sana Serikali kutekeleza kwa ufanisi maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025 sambamba na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano kutoka mwaka 2021/2022 - 2025/2026 ambao utawasilishwa kwenye mkutano huu na Waziri wa Fedha na Mipango kuanzia wiki ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge sambamba na kutekeleza ushauri na michango mizuri waliyoitoa wakati wa kuchangia hoja hii. Nitumie fursa hii pia kuwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri kwa kutoa maelezo ya ziada na ufafanuzi mzuri kwenye sekta zote zilizochangiwa na kushauriwa kuelekea kwenye utekelezaji mzuri. Maeneo yote yaliyoshauriwa ni muhimu ambapo Serikali haina budi kuyazingatia katika utekelezaji wa mipango na vipaumbele vyake kwa kipindi kijacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyoona wakati wa mjadala huu, masuala na hoja nyingi zimetolewa maelezo na ufafanuzi wa kina kutoka kwa Waheshimiwa Mawaziri ambao wamemaliza muda mfupi uliopita. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali itazingatia maelekezo na ahadi za Mheshimiwa Rais katika kupanga vipaumbele vyake vya mpango wa bajeti katika kipindi chote hiki cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuibuliwa kwa hoja nyingi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wakati wa mjadala wa Hotuba ya Mheshimiwa Rais ni kielelezo tosha kwamba hotuba hiyo imegusa maeneo muhimu na yenye maslahi ya moja kwa moja kwa wananchi wetu. Miongoni mwa maeneo yaliyosisitizwa na Waheshimiwa Wabunge ni kuimarishwa kwa sekta za miundombinu na usafiri na usafirishaji ambapo taasisi zetu za TARURA na TANROADS nazo pia imeshauriwa namna ya kuziboresha. Sekta ya maji imeguswa, elimu na ujuzi nayo imesisitizwa, uongezaji thamani kwenye bidhaa zetu hususan za kilimo nayo pia imeguswa, uzalishaji mali, masoko, nishati, afya na huduma za kifedha na shughuli za kiuchumi uwekezaji ukiwemo na ujenzi wa viwanda nazo zimeguswa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote hayo yamefafanuliwa kinagaubaga kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo hoja yake tunaihitimisha leo. Kadhalika wakati nawasilisha hoja hii, nililiarifu Bunge lako Tukufu kuwa tayari utekelezaji wa maelekezo na ahadi za Mheshimiwa Rais ulishaanza mara tu alipowasilisha hotuba yake siku ya tarehe 13 Novemba, 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwenye wiki ijayo tutapata nafasi ya kuchangia hoja ya Waziri wa Fedha na Mipango ambayo nitasheheneza mjadala ninaohitimisha leo. Kama ambavyo unafahamu maandalizi ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/2022 yanaendelea. Hivyo basi, kutokana na ukweli kuwa maeneo hayo ya vipaumbele yanahitaji kupangiwa fedha za bajeti kwa ajili ya utekelezaji wake, kupitia mijadala na hoja zote mbili, hotuba yangu ya kuhitimisha Mkutano huu wa Bunge nitatoa mwelekeo wa namna ambavyo tutakwenda kutekeleza yale yote ambayo yameshauriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa maelekezo kwa Wizara na taasisi nyingine za Serikali kuhakikisha kwamba vipaumbele hivyo vinapangiwa fedha kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022. Kwa msingi huo, nitumie fursa hii kurudia tena kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba maoni na hoja zenu zitazingatiwa wakati wote kwa utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali. Vilevile kwa ile miradi inayoendelea kutekelezwa nchini katika sekta za uzalishaji mali ikiwemo kilimo mifugo, maliasili, madini na sekta za huduma ya jamii kama vile elimu na afya zitakamilishwa kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imekuwa ikifanya juhudi kubwa katika kuandaa mpango pamoja na mipango ya bajeti na kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali vya Serikali vyenye lengo la kuwaletea maendeleo wananchi. Hata hivyo, awali tulikuwa na changamoto ya baadhi ya viongozi na watendaji kutowajibika na kusababisha kudorora katika kuwahudumia wananchi ipasavyo. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano ilijikita katika kuhakikisha inarejesha nidhamu katika utumishi wa umma kwa kuweka mkazo katika misingi ya uadilifu, uwajibikaji, kutoa huduma kwa wakati na kuchukua hatua za haraka dhidi ya watumishi wote wanaokwenda kinyume na misingi ya utendaji wa kazi ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyote mtakubaliana nami kwamba kuimarishwa kwa nidhamu ya viongozi na watendaji Serikalini imekuwa chachu ya kufikiwa kwa malengo mengi tuliyojiwekea. Aidha, baada ya kufuatilia kwa karibu michango ya Waheshimiwa Wabunge, nami napenda kusisitiza masuala machache kwa viongozi na watendaji wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni suala la utoaji wa taarifa kwa umma kwa wakati kuhusu miradi na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali. Katika hili, nirejee kauli ya Mheshimiwa Rais mpendwa aliyoitoa tarehe 4 Juni, 2018 wakati akizindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Nchini (ASDP II) kwamba viongozi na watendaji wa Serikali wanao wajibu wa kueleza kwa kina mambo yanayotekelezwa na Serikali kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote ni mashuhuda kwamba yako mambo mengi ya kujivunia yametekelezwa na yanaendelea kutekelezwa na Serikali yetu. Kwa msingi huo, Watanzania wanayo haki ya kuhabarishwa na kufahamu mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu. Nitoe wito kwa viongozi na watendaji kwenye ngazi mbalimbali kuzingatia eneo hilo la mawasiliano kwa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulisisitiza ni viongozi na watendaji kuwafikia wananchi kwenye maeneo yao kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi. Katika ziara zangu zote nimekuwa nikisisitiza kuwa viongozi na watendaji wawafuate wananchi kwenye maeneo yao, wawasikilize na kuwahudumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe tu viongozi na watendaji wote kwamba tunao wajibu mkubwa kwa wananchi kutokana na dhamana waliotupatia, hivyo, tunapaswa kuwajibika kwao badala ya kusubiri ziara za viongozi wakuu wa kitaifa. Natumia fursa hii kuwaambia viongozi na watendaji wote wa Serikali kuwa tutapima utendaji wenu kwa namna mnavyotatua kero za wananchi kwenye maeneo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa upande wetu itahakikisha inachukua hatua dhidi ya wote watakaokiuka sheria, kanuni na taratibu za kazi na kwamwe hatutamvumilia mtumishi mzembe na mwenye kufanya kazi kwa mazoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali, hotuba yangu ya kuhitimisha mkutano huu itajumuisha mijadala yote miwili; huu ambao tunahitimisha leo na ule wa Mpango wa Wizara ya Fedha ambao utaanza kujadiliwa kuanzia Jumatatu. Nimalizie maelezo yangu kwa kuwasihi Waheshimiwa Wabunge kwamba tunao wajibu wa kuishauri Serikali sambamba na kuwaongoza wananchi katika kusimamia utekelezaji wa ahadi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais yaliyomo katika hotuba yake ya kuzindua Bunge la Kumi na Mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuimarisha ushirikiano wa wananchi na mamlaka mbalimbali za Serikali hususan Serikali za Mitaa kwa lengo la kuhakikisha kwamba wanaunga mkono Serikali na hivyo kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niseme ni kwamba nimevutiwa sana na michango ya Waheshimiwa Wabunge wakati wote wa kuchangia hoja hii. Nimepokea ushauri wenu kama ambavyo nilieleza wakati tunawasilisha hoja hii na sasa narudia kwamba tutaendelea kushirikiana katika kuboresha yale yote ambayo mmechangia kwenye hoja hii ya kujadili hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo aliitoa tarehe 13 Novemba, 2020 wakati akifungua Bunge la Kumi na Mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, niungane na wenzangu kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana kwenye Kikao hiki cha Kumi na Moja cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Mbili kwa ajili ya kuhitimisha mjadala kuhusu Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana wewe, Mheshimiwa Naibu Spika kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa mwenendo mzima wa majadiliano ya Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2021/2022. Nazipongeza na kuzishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa kazi nzuri na michango yenye tija kwenye Hoja ya Waziri Mkuu. Nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa sekta ambao pia wamekuwa hapa wakisikiliza hoja hizi mbalimbali na Naibu Mawaziri lakini pia kupitia vipindi vya maswali na majibu wamekuwa wakijibu maswali na hoja kadhaa wamekuwa wakizipitia na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali. Kadhalika, nawashukuru Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uratibu wa pamoja na ushirikiano walionipa katika kipindi chote cha mjadala wa bajeti hii yetu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa pongezi zenu kwa Serikali na kwa michango yenu ambayo ni muhimu katika kuisaidia Serikali kutekeleza kikamilifu vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/2022. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilipokuwa nawasilisha Hoja siku ya tarehe 13 nilianza maelezo ya utangulizi mazuri ambayo sitaraji kuyarudia tena yaliyogusa maeneo mengi. Sasa tunaendelea na hoja ile ile ya kufafanua hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wote hapa wakati wa mjadala wetu.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mjadala wa Hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2021/2022 umeenda vizuri sana na umethibitisha uimara na umakini wa Waheshimiwa Wabunge kupitia Bunge lako Tukufu katika kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba kwa kuishauri na kuisimamia Serikali kikamilifu. Serikali, imepokea maoni na ushauri wote uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge na wakati wote tutauzingatia katika kutekeleza majukumu yetu.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala hapa tulikuwa na Wabunge waliochangia 121 kati yao Waheshimiwa 109 walipata nafasi ya kusema moja kwa moja hapa Bungeni na Waheshimiwa Wabunge 12 walichangia kwa njia ya maandishi. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote mliopata nafasi ya kuchangia kwenye hoja hii ya Waziri Mkuu. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda naomba uridhie nisiwataje na kwamba majina yao yaingizwe moja kwa moja kwenye Hansard. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mjadala huu, Serikali kupitia kwa Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wameendelea kujibu hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge. Kutokana na ufinyu wa muda hoja zitakazosalia zitajibiwa kwa maandishi. Vilevile, Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kuwasilisha hoja zao kwenye sekta zao watatoa ufafanuzi wa yale yote yaliyogusa sekta zao. Walikuwa hapa wame-take note yale yote wanayopaswa kujibu na bajeti yao itakapokuja mbele ya Bunge lako Tukufu kila mmoja atalazimika kufafanua yale yote yanayogusa sekta yake.
Mheshimiwa Spika, wakati wa majadiliano kuhusu Hoja ya Waziri Mkuu yako masuala mengi na muhimu yameibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Aidha, wakati wote wa Hoja ya Waziri Mkuu tumekuwa na mjadala wa kina na wenye msisitizo wa kiwango cha juu kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na kujenga hoja zenye ubora na umakini unaliostahili unaoifanya Serikali kuweza kuzingatia kwa umakini kwa ajili ya utekelezaji wake.
Mheshimiwa Spika, nikiri kuwa hoja nyingi zilizoibuliwa zina uhusiano wa moja kwa moja na utendaji kazi wa Serikali. Aidha, masuala muhimu hususan vibali vya kazi kwa wageni na uwekezaji kwa kiasi kikubwa yamekuwa kitovu cha mjadala na michango ya Waheshimiwa Wabunge walipokuwa wakichangia hii Hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Hii ni kwa sababu eneo la Uwekezaji ndiyo ambalo sasa tunaitegemea kukuza uchumi wa nchi hasa kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, madini, maliasili, maji na sekta nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, naomba uridhie japo kwa uchache nitoe ufafanuzi kuhusu baadhi ya masuala yaliyoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye Hoja ya Waziri Mkuu hususan eneo la uwekezaji na vibali vya kazi pamoja na kwamba Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi wameeleza maelezo ya awali.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 6 Aprili 2021, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wakati akiwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Wakuu wa baadhi ya Taasisi za Serikali aliweka msisitizo masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji na vibali vya kazi ikiwa ni maeneo ambayo yamekuwa na changamoto nyingi katika utowaji wa vibali hasa kwenye uwekezaji. Mheshimiwa Rais aliielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu kuimarisha Huduma za Pamoja (One Stop Centre), kushughulikia malalamiko yote kuhusu kodi, kuondoa vikwazo katika uwekezaji, kuhamasisha uwekezaji kupitia mazungumzo, ushawishi, kudhibiti rushwa na kuondoa urasimu kwenye maeneo yote ya uwekezaji ikiwemo na maombi ya vibali vya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maelekezo hayo ya Mheshimiwa Rais yenye kujali maslahi mapana ya nchi hii yalikwenda sambamba na uamuzi wake wa tarehe 31 Machi 2021 wa kuunda rasmi Wizara ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Lengo la Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kuwa Wizara hiyo inasimamia kikamilifu masuala ya uwekezaji hapa nchini, kikanda na kimataifa. Majukumu mengine ni kuratibu majadiliano ya uwekezaji wa miradi ya kimkakati, mikutano ya majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ndani na nje ya nchi lakini pia kubuni na kutekeleza mikakati ya kujenga sekta binafsi ya hapa Tanzania iliyo imara na yenye ushindani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona ushindani huu unaanza kukuwa na utatuletea manufaa makubwa. hatua hiyo, itawezesha kuvutia wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi kuja hapa nchini lakini pia hata Watanzania wenye uwezo wa kuwekeza nao sasa wanapata fursa ya wazi ya kuanza kuwekeza mitaji yao teknolojia na ujuzi ili kuongeza ukuaji wa uchumi kwa kasi na upatikanaji wa ajira na maendeleo nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nami, napenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa uamuzi wa kurejesha jukumu la uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni ishara ya wazi kuhusu imani kubwa aliyonayo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu. Nami napenda kumhakikishia kuwa sitamuangusha, nitasimamia sekta hii ili iweze kuleta mafanikio hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa tayari hatua mbalimbali za utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais zimeanza kuchukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na moja kuandaa Muundo wa Wizara ambao utaainisha majukumu na mgawanyo wa Idara na Taasisi zitakazokuwa chini ya eneo hilo la uwekezaji. Mbili, kupitia upya Sera ya Uwekezaji ya Mwaka 1996 na Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 ili kubainisha maeneo yenye kuhitaji maboresho ambapo tayari tathmini ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 imekamilika. Tatu, tunaandaa sasa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ili kuimarisha uratibu, usimamizi, uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya uwekezaji katika sekta zote hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa hatua hizo kutaiwezesha Serikali kutekeleza masuala muhimu kama yafuatayo. Moja, ni kushiriki kikamilifu katika mikutano na majadiliano ya Jumuiya za Kikanda yanayohusu masuala ya uwekezaji ikiwemo maandalizi ya Sera ya Uwekezaji ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, utungaji wa Sera za Uwekezaji kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Itifaki ya Uwekezaji ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika. Mbili, ni kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji na uchumi shindani nchini kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameendelea kusisitiza kwa kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha mazingira hayo wezeshi. Tunataka biashara ishamiri na yeyote anayekuja kuwekeza nchini apate fursa hiyo ya kuwekeza kwenye sekta yoyote ile ambayo tunayo. Tuna uhakika atapata huduma zilizo sahihi.
Mheshimiwa Spika, tatu, kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wawekezaji kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Nchi alivyokuja kueleza hapa mbele yetu. Nne, kutatua changamoto za wafanyabiashara kupitia Baraza la Taifa la Biashara ambalo sasa tunaliunda kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa ambako Mheshimiwa Rais ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo la Biashara la Taifa lenye malengo ya kuratibu majadiliano ya sekta za umma na sekta binafsi. Eneo hili tutalisimamia ili sekta binafsi nayo ipate nafasi ya kuishauri Serikali kwa ajili ya utekelezaji au uwekezaji wenye tija.
Mheshimiwa Spika, tano, kutoa elimu na hamasa kuhusu huduma zitolewazo kwenye Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre), fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta mbalimbali nazo pia ziweze kuibuliwa na kuelimisha wananchi namna ya kupata wabia na kushirikia nao katika kuanzisha na kuendeleza miradi yao kupitia Taasisi yetu ya Uwekezaji Tanzania (TIC). Sita, tunataka tuimarishe mifumo ya usajili wa miradi na kutoa Cheti cha Vivutio (Certificate of Incentives), kuunganisha mifumo inayotumika TIC na makao makuu ya Taasisi na kuboresha mfumo wa kuchakata rufaa za vibali vya kazi na ukaazi kwa njia ya mtandao ambapo kila mmoja atakuwa anaweza kuufika popote alipo ndani au nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii tena kuwakumbusha watendaji wenzangu wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kuhakikisha kuwa muundo na mifumo ya masuala ya uwekezaji inakamilika ndani ya muda ulioelekezwa na Mheshimiwa Rais. Natoa maelekezo kwa Wizara na taasisi zote zinazohudumia wawekezaji kuhakikisha wanawezesha uwekezaji katika maeneo yao kwa kutoa huduma stahiki na taarifa muhimu kwa wakati zipatikane lakini pia kuondoa usumbufu ukiwa unaambatana na maombi ya rushwa lakini na urasimu kama nilivyoeleza awali, hili nalo tutalisimamia.
Mheshimiwa Spika, aidha, nasisitiza kuwa watendaji wajiepushe na haya ambayo nimeyaeleza ya uombaji wa rushwa na urasimu usiokuwa wa lazima katika kuhudumia wawekezaji ili kujenga imani baina ya sekta ya umma na sekta binafsi ili tuweze kuzungumza lugha moja. Mwaka ujao wa fedha 2021/2022, Serikali itaimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Uwekezaji ikiwemo kuainisha ardhi ya uwekezaji (land bank) na kuendeleza miundombinu muhimu ya uwekezaji katika mikoa yote ili kuvutia uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limeibua mjadala mkubwa wakati uchangiaji wa hoja ya bajeti ya Waziri Mkuu ni vibali vyenyewe vya kazi. Mheshimiwa Waziri wa Nchi hapa ameeleza lakini changamoto kubwa iliyozungumziwa ni kuhusu kubanwa na masharti mbalimbali dhidi ya ajira za wageni ikiwemo la kwanza ukomo wa mwombaji kuishi nchini kwa muda usiozidi miaka mitano. Huu nao umekuwa kikwazo pale anapowekeza mradi mkubwa unaohitaji kuusimamia zaidi ya miaka 10. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, mahitaji ya elimu, uzoefu au ujuzi wake wa mwombaji ili aweze kupewa kibali. Hapa pia kuna mgogoro mkubwa. Tunadai mtu awe na degree lakini pia degree hiyo aweze kuifanyia kazi kwenye sekta hiyo. Kwa hiyo, tutaangalia zaidi uzoefu na ujuzi alionao, elimu itakuwa ni kitu ambacho kinasaidia ujuzi na uzoefu alionao katika kufanya kazi. Hili nalo tutaliangalia ili kurahisisha kupata watu ambao wanaweza kufanya kazi hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini tatu kigezo cha mwombaji kupata uthibitisho wa cheti chake kutoka NECTA. Mtu kasoma Norway tunataka alete cheti ili aweze kuajiriwa hapa nchini kwa kupeleka cheti hicho NECTA, NACTE au TCU. Nalo hili tutaliangalia tena vizuri kwa sababu limekuwa likikwaza kupata wawekezaji wanapokuja kuwekeza hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maeneo hayo ndiyo yenye mgogoro zaidi katika suala la utoaji wa vibali vya kazi kwa wageni. Hivyo basi, Serikali inafanyia kazi changamoto hizo kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Rais. Aidha, tayari nimetoa maelekezo kwa Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kushirikiana na Wizara zote za kisekta pamoja na watendaji wa Wizara zote za kisekta katika kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinafanyiwa kazi kwa haraka zaidi ili kuweza kuuweka uwekezaji katika sura inayotuletea watu wengi zaidi na kujenga imani ya uwekezaji hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mbali ya uwekezaji, kwa mujibu wa Kanuni ya 118(13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo ya Mwaka 2020, naomba nitumie nafasi hii pia kuendelea kufafanua hoja nyingine ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wote wa mjadala kama ifuatavyo. Tulikuwa na hoja ya kuitaka Ofisi ya Waziri Mkuu ihakikishe kwamba utekelezaji wa vipaumbele ulenge zaidi katika kuwatengenezea wananchi wa kawaida fursa za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu inalo jukumu la kuratibu, kufuatilia na kutekeleza vipaumbele vya Sera na miongozo mbalimbali ya Serikali ili kumletea maendeleo mwananchi kulingana na fursa zilizopo katika maeneo husika miongoni mwa maeneo ya kimkakati ya utekelezaji wa jukumu hilo ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja ni kuwajengea wananchi uwezo kwa kutambua fursa zinazowazunguka na kuzitumia kwa ajili ya kujiletea maendeleo. Kwa mfano, utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali, uanagenzi, urasimishaji ujuzi, kurahisisha upatikanaji mitaji na taarifa za masoko, ni miongoni mwa mkakati wa Serikali kuwafanya Watanzania wajue fursa zinazowazunguka.
Mheshimiwa Spika, pili, kuratibu ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya kiuchumi ili kuwawezesha Watanzania kunufaika na fursa zilizopo katika maeneo yao, mathalani ujenzi wa njia za usafirishaji kama vile njia ya anga, njia za maji, barabara, pia ujenzi wa madaraja makubwa, masoko, vituo vya mabasi, miundombinu ya umwagiliaji kwenye Sekta ya Kilimo, usambazaji wa umeme na pia kuimarisha mawasiliano ndani ya nchi. Hayo yote ni yale ambayo tunayasimamia.
Mheshimiwa Spika, pia tunaendelea kuratibu na kufuatilia ushiriki wa Watanzania katika utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kimkakati kupitia mpango wa local content. Lengo ni kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na utekelezaji wa miradi hiyo sambamba na uwekezaji mkubwa ulifanywa na Serikali kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfano wa miradi hiyo ni ujenzi wa reli ambao sasa unaendelea ambayo ni SGR, ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ambao pia unaendelea, bomba la kusafirisha mafuta litakaloanza hivi karibuni linalotoka Uganda mpaka hapa Tanzania, kuna suala la uchimbaji wa madini hususan uchimbaji mdogo mdogo nao tumeimarisha, ujenzi wa barabara za vijijini na barabara kuu pamoja na madaraja makubwa ambayo pia yanaunganisha eneo moja na eneo lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulikuwa na hoja ya Wizara ya Fedha inayotaka ihakikishe inatoa fedha kwa wakati ili kuwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuteleza majukumu yake ya kusimamia changuzi ndogo zinazoendelea kujitokeza kwa mujibu wa sheria. Haya yote yanaendelea kutekelezwa na tunazingatia sana sheria, Kifungu cha 122 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura 343) na Kifungu kidogo cha (120) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Sura 292).
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatekeleza hili kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha kwamba chaguzi hizi zinaendelea kufanyika kama ambavyo zinaendelea. Kwa sasa tunayo maeneo mawili ya yanayoendesha uchaguzi mdogo kule Buhigwe pamoja na Kibondo ambapo pia uratibu wake umeshanza kuratibiwa.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu iwe na mfumo mzuri utakaohakikisha Makao Makuu ya Nchi Dodoma yanaendelezwa. Hili nataka nilileleze vizuri kwa kuwaondolea mashaka au wasiwasi Watanzania wakifikiri kwamba mkakati wa Makao Makuu ya Nchi Dodoma kuwa sasa hautaweza kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mfumo mzuri sana wa kuhakikisha kwamba Makao Makuu ya Nchi yanaendelezwa kwa kujenga na kuendendelea na mipango ya maendeleo ya Jiji la Dodoma. Mfumo huo unahusisha kikosi kazi cha Taifa cha kuratibu Mpango wa Serikali kuhamia hapa Dodoma ambacho kinajumuisha Wajumbe kutoka Wizara na Taasisi zote za Serikali.
Mheshimiwa Spika, leo hii watumishi wote wapo hapa Dodoma, shughuli zote za Serikali zinafanywa hapa Dodoma na ujenzi wa miundombinu mbalimbali unaendelea hapa Dodoma. Natumia nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji, wale wote ambao wanaotamani kufanya kazi hapa Dodoma, waje. Nataka niendelee kurudia kusema kwamba Makao Makuu ya Dodoma bado itaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiki kikozi kazi kina jukumu la kushauri namna moja ya kupanga na kuendeleza Mji wetu wa Dodoma na utekelezaji huo unahusisha zaidi miradi mbalimbali ikiwemo na kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa miradi ya maji, tupate maji ya kutosha, tunajenga kiwanja cha ndege kikubwa zaidi ya hiki tulichonacho, barabara na utoaji wa huduma za jamii nao unaimarishwa na kujenga kituo cha reli kikubwa kuliko vituo vyote nchini kitajengwa hapa Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Watanzania wote kuwa Dodoma inaendelea vizuri na wale wote wanaotamani kuja, waje, fursa zipo na njia za usafiri zote zipo za barabara na anga.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja nyingine inasema Serikali iendeleze miradi yote ya awamu zilizopita ambayo inaendelea kutekelezwa na utekelezaji wake uweze kusimamiwa. Serikali tumeahidi kutekeleza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni ya Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika, miradi yote ya kipaumbele iliyoainishwa kwenye Ilani ambayo imeanza kutekelezwa na ile ambayo bado haijatekelezwa, yote itatekelezwa ili kuhakikisha kwamba tunafikia malengo ya Chama cha Mapinduzi kupitia Serikali yake kwa kutelekeza na kusimamia miradi yote hii ya kimkakati.tuna Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umeweka kipaumbele cha kuendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Hilo halina matatizo.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ipo mbele yetu na imejadiliwa sana ni ile ya Ofisi ya Waziri Mkuu ishirikiane na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuboresha utaratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuwepo na mfumo mmoja wa vyanzo vya fedha. Hatua hiyo iweze kuandamana na kuongeza usimamizi wa udhibiti wa marejesho ya fedha hizo za mikopo ambazo zinatolewa na hiyo mifuko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyofafanua katika hotuba yangu ya bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali itathimini kwa kina utendaji na ufanisi wa mifuko yote ya uwezeshaji kwa wananchi kiuchumi ikiwemo Mfuko huu wa Maendeleo ya Vijana ili kuona kuwa kuna umuhimu wa kufuta baadhi ya mifuko kuunganisha au kuanzisha mifuko mipya kwa kuzingatia mahitaji ya sheria za nchi.
Mheshimiwa Spika, aidha, wakati wote mchakato huu ukiendelea, taratibu za kuratibu marejesho ya fedha za mikopo hiyo zitakuwa zinaendelea kuratibiwa ili fedha hizi zinazokopeshwa ziweze kurudi halafu ziwe endelevu kuwakopesha vijana wengine.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilikuwa imezungumzwa kwenye mijadala hapa, ni mfuko wa uwezeshaji wa vijana wa Halmashauri kwamba uongezewe fedha kutoka 4% mpaka asilimia 10. Kama nilivyotangulia kueleza, Serikali inafanyia tathmini mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa lengo la kutaka kujua kiwango cha mikopo chenyewe kinachotolewa ikilinganishwa na mahitaji, riba za mikopo yenyewe na ufanisi wa mifuko hiyo katika kukuza uchumi wa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya tathmini hiyo, taarifa rasmi itatolewa na maombi haya yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na ushauri wao tutauzingatia kulingana na uwezo wa mfuko wenyewe kadiri tunavyoendesha ndani ya Serikali. Mfuko huu wa Halmashauri kwa sasa unaendelea kutoa 4% ya vijana, asilimia 4% kwa wanawake na 2% kwa wenye mahitaji maalum au walemavu.
Mheshimiwa Spika, yako maeneo muhimu yaliyojadiliwa kama hoja ikiwemo uboreshaji wa huduma za maji, elimu, lakini pia suala TARURA limezungumzwa sana, Sekta ya Mafuta nayo imejadiliwa sana, uimarishaji wa bandari umeungumzwa na suala la madini hasa kule Mererani imepata nafasi kubwa ya kuzungumzwa. Masuala haya yote yataratibiwa vizuri sana kupitia Wizara husika kama ambavyo nimeeleza na watafika mbele ya Bunge lako Tukufu ili kutoa ufafanuzi wa kila hoja ambayo pia imeweza kuchangiwa hapa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, hoja za Muungano zimejadiliwa sana, nazo pia zitapata ufafanuzi kupitia bajeti ya hotuba ya Makamu wa Rais. Hoja ya mfumo kununua mazao (TMX) imezungumzwa pia na Wizara ya Kilimo itazingatia hili, kwa sababu mkakati wetu sasa ni kukuza ushirika.
Mheshimiwa Spika, ushirika ni wana ushirika, tutaendelea kuwapa nafasi wanaushirika kusimamia ushirika ili tuufanye ushirika huu uweze kuwa endelevu. Mifumo mingine yote itabuniwa na kuanzishwa na Wizara yenyewe ya Kilimo inayosimamia ushirika ambayo pia inajua mwenendo wa uanzishaji wa ushirika mwenendo wa uanzishaji wa mifumo mingine inayotakiwa kusimamiwa hapo. TMX kwa sasa ni ya Wizara ya Fedha na tunaisihi Wizara ya Fedha ijiimarishe na mfumo huu, itutafutie masoko ya nje zaidi kwa mazao yaliyoko hapa ndani ili tuweze kuyauza na wanunuzi kutoka nje huko waweze kununua kwa mfumo huo wa TMX.
Mheshimiwa Spika, hoja ya mahusiano ya Vyama vya Siasa au Chama Kimoja na Serikali, imefafanuliwa vizuri na Waziri wa Nchi. Jambo hili litaangaliwa na linaendelea kuangaliwa, lakini mahusiano yetu bado ni mazuri kwa sababu tunashirikiana kwa pamojo, licha ya kuwa kuna kasoro mbalimbali ambazo pia nazo huwa zinapata ufumbuzi kupitia Baraza la Vyama vya Siasa ambapo pia huwa tunakaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni migogoro ya ardhi na mipaka ya utawala kwenye maeneo mbalimbali nchini. Tuna migogoro kati ya vijiji na vijiji, migogoro kati ya Wilaya na Wilaya, hata Mkoa na Mkoa, ukiwemo ule mgogoro wa Wilaya ya Kiteto na Kilindi ambao pia tulishautafutia ufumbuzi. Nilitoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya, nitoe wito tena kwa Wakuu wa Mikoa ya Manyara na Tanga; na Wilaya za Kiteto na Kilindi, wamalize huo mgogoro kabla sijarudi tena huko ili ufumbuzi upatikane na wananchi waweze kufanya mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiwa nahitimisha, nimesikiliza na kufuatilia kwa umakini sana mjadala huu kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania wote kwa ujumla kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 mpaka 2025 itatatekelezwa vyema chini ya Jemedari wetu, Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Saluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wakati wote tunakuwa katika Vikao vya Bunge, tutakuwa tunaendelea kushauriana na pia kuona namna nzuri ya kutekeleza maeneo haya kupitia ushauri wenu na namna ambavyo mnaweza kuisimamia Serikali yetu kupitia Kamati zetu.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanayo imani kubwa sana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kufuatia mafanikio makubwa yaliyopatikana na mwanzo mzuri aliouonyesha Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waheshimiwa Wabunge wenzangu, imani hiyo ya wananchi haina budi kuwa chachu kwetu katika kuwatumikia kwa ubora zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine mwelekeo wetu ni mzuri, suala la msingi lililo mbele yetu ni kuongeza umakini na kasi ili malengo yote tuliyojiwekea ambayo dhamira yake ni kuwaletea maendeleoo wananchi na Taifa kwa ujumla yaweze kufikiwa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa tarehe 7 Aprili, mwaka huu 2021 tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 47 ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na tarehe 12 Aprili mwaka huu, 2021 tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 37 ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Watanzania tunaendelea kuwakumbuka viongozi hawa kwa mchango wao mkubwa katika kutetea wanyonge na kudumisha misingi ya Imani, mshikamano na umoja wa Kitaifa ambao tunao. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Watanzania, turejee kauli ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa wakati huu tuendelee kushikamana, kusimama na kuwa wamoja katika Taifa, kuonyesha upendo wa undugu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu, Utanzania wetu na kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huu siyo wakati wa kuonyesheana vidole, bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele. Kwa msingi huo, tuendelee kudumisha na kuilinda amani ya nchi yetu ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada za waasisi wa Taifa hili. Tutumie muda mwingi kwa kazi zaidi na kujipatia kipato na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja kuliko vinginevyo.
Mheshimiwa Spika, nawakumbusha Waheshimiwa Mawaziri, Viongozi na Watendaji wote waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, mnalo jukumu kubwa sana kuwahudumia wananchi na kuhakikisha mnasimamia ipasavyo miradi iliyoanzishwa kwenye maeneo yenu na kushughulikia changamoto zote katika maeneo yenu na pia kusikiliza kero za wananchi kwenye maeneo yenu.
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo yanayoendana na thamani ya fedha za walipa kodi. Ndiyo namna bora ya kurudisha shukrani kwa wananchi waliotupa ridhaa ya kuwatumikia.
Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kusisitiza kuwa tukiwa watumishi wa Umma, tunao wajibu wa kuwapokea, kuwasiliza na kuwahudumia wananchi waliotupa dhamana hii ya uongozi. Kwa hiyo, tufanye kazi, tena kwa bidii zaidi, tuache mazoea ya kiurasimu ili kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile napenda kutumia nafasi hii kuwatakia Waislamu wote nchini mfungo mwema na wenye mafanikio wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani ulioanza katikati ya wiki hii. Natoa rai kwamba tutumie kipindi hiki kumwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki nchi yetu, aendelee kuwalinda viongozi wetu na Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, kadhalika, tumwombe Mwenyezi Mungu awajaalie wote kwa hekima na busara ili tuendelee kuliongoza Taifa letu kwa haki kujenga umoja na mshikamano kudumisha amani katika nchi yetu pamoja na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nihitimishe kwa kutoa tena shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, timu yote ya Bunge ikiongozwa na Katibu wa Bunge, Watanzania kwa ujumla, ndugu Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, napenda mtambue kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu muda wote ipo wazi, iko tayari, kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia. Tunaendelea kushirikiana na kila mmoja kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, kwa unyenyekevu mkubwa kabisa naliomba sasa Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili tuweze kuchapa kazi, taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge letu Tukufu kama nilivyowasilisha katika hoja yangu ya tarehe 13 mwezi huu wa Nne 2021ili tuchape kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba nimesikiliza mjadala unaogusa maeneo ya Ngorongoro na Loliondo juu ya mahitaji makubwa ya uhifadhi wa maeneo haya kwa maslahi ya Taifa. Ni kweli upo mgongano mkubwa unaotokana na sheria tulizonazo, lakini pia matakwa binafsi ya mtu mmoja mmoja.
Mheshimiwa Spika, vile vile Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo ya kukutana na ndugu zetu waliopo pale. Kazi hiyo tumeshaianza. Jumapili iliyopita nilianza na kazi hiyo nikakutana na Uongozi wa Mkoa wa Arusha, nimewasikiliza, nimekutana na Wizara pale Arusha, nimewasikiliza na sasa hatua iliyobaki ni kwenda Ngorongoro. Nitafanya mikutano na wananchi wa eneo la Ngorongoro, nitafanya mikutano na wananchi wa eneo la Loliondo ambako pia mwaka 2017/ 2018 tulifanya mikutano mingi sana kueleweshana juu ya jambo hili.
Mheshimiwa Spika, haya yote na mjadala unaoendelea hapa Bungeni wapo ambao wanaelewa mazingira yaliyopo kule, lakini wapo Wabunge ambao hawajui mazingira yaliyopo pale. Huku tukiwa tunazungumza na wananchi kule, naiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya semina siku moja kwa Wabunge wote ili Wizara iwaambie kuna nini kule Ngorongoro? Nini kilikuwepo awali na ni hali gani ambayo ipo sasa? Hii itasaidia tuwe na uelewa wa pamoja hata haya mapendekezo ya Mheshimiwa Waziri ya kutaka kuja kubadilisha sheria, mnaweza kuunga mkono au kutokuunga mkono baada ya kujua nini kinaendelea kule? Hatua hii ndiyo itawezesha kuendesha zoezi hili kwa amani kabisa kadri itakavyokuwa imeamriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo njia sahihi ambayo pia niliona nipate muda huu niweze kutoa maelekezo kwa Wizara na pia Wabunge mpate kuelewa jambo hili. Tutakwenda kwa wananchi; tumeanza kwa hatua hizo ambazo nimezieleza, tumzungumza na Wizara, tumezungumza na Mkoa ambao unasimamia jambo hili ambapo pia TAWA, TANAPA pamoja na Ngorongoro walikuwepo, na hao sasa nawataka kupitia Wizara waje hapa Bungeni wawaelimishe Wabunge, mjue mazingira yaliyopo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kumaliza jambo hili, kwa kadri ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kutatua tatizo hili bila kuwa na mgongano kati ya wananchi walipo pale na maamuzi ambayo yanaweza kufikiwa, lazima tukae pamoja ili tuweze kumaliza.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa na hayo tu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza kabisa nami niungane na wenzangu waliotangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa rehema na kutujalia siha njema na kutuwezesha kukutana hapa kwenye Kikao hiki cha Sita, Mkutano wa Saba wa Bunge la 12, kwa ajili ya kuhitimisha mjadala huu kuhusu hoja ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa Miongozo yake mizuri iliyowezeshwa ofisi ya Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake na kulifanya Taifa letu kufanya maendeleo hadi leo hii. Pia niendelee kumshukuru Mheshimiwa Daktari Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia anamsaidia kazi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan naye kwa kutoa Miongozo kwa ofisi ya Waziri Mkuu na kuwezesha ofisi ya Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake vilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru sana wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuongoza vyema mjadala kuhusu hoja ya Bajeti, ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Pia niendelee kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu yaBunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kwa kazi kubwa waliyoifanya ikiwemo kutoa michango yao yenye tija kwenye hoja ya Waziri Mkuu, nawashukuru sana Wajumbe wa Kamati zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia tena kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri wa Sekta waliyochangia hoja za Bajeti ya Waziri Mkuu, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala wa Taasisi za Serikali kwa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha hoja ya Bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, vilevile kipekee ninawashukuru sana watumishi wote wa ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri waliyoifanya na ushirikiano walioendelea kunipatia katika kipindi chote, hususan wakati wa maandalizi hadi kipindi tunapoelekea kuhitimisha mjadala wa Bajeti wa ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nitumie vilevile nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango yenu muhimu, hakika mnaendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yenu ya msingi ya kuisimamia na kuishauri Serikali, kwa kutoa michango mizuri yenye lengo la kuisaidia Serikali katika kutekeleza kikamilifu vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali napenda kuwapongeza na kuwashukuru sana tena Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa hoja na michango yenye kujenga utendaji wetu Serikalini. Niwahakikishie kwamba Serikali itazingatia maoni yenu na ushauri wenu mlioutoa katika kutekeleza majukumu yatu ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge 115 walichangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa mjadala huu. Kati yao, Waheshimiwa Wabunge 104 walichangia kwa kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge 11 walichangia kwa maandishi. Ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Aidha, kutokana na ufinyu wa muda, ninaomba uridhie nisiwataje mmoja mmoja kwa majina na badala yake majina yao yaingizwe kwenye Hansard moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mjadala wa hoja ya Waziri Mkuu, Serikali imetoa majibu ya hoja nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge, kupitia Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda Serikali itatoa majibu yenye ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zilizosalia kwa njia ya maandishi.
Mheshimiwa Spika, vilevile, wakati Waheshimiwa Mawaziri wakiwasilisha hoja za bajeti za sekta zao wataendelea kutoa ufafanuzi wa kutosha na kwa undani zaidi wa baadhi ya hoja ambazo zimeibuliwa kwenye mjadala huu chini ya ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, naomba niueleze mwaka mmoja wa Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, itakumbukwa kwamba tuna mwaka mmoja pekee tangu Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ashike hatamu za kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, katika kipindi hicho kifupi Tanzania imepata mafanikio lukuki ambayo yametufanya kuendelea kutembea kifua mbele na kujiamini.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio hayo ni kuendelea kuimarika kwa uchumi, shughuli za kijamii, ongezeko la mapato ya kodi, kurejea kwenye diplomasia na medani za kimataifa, kuongezeka kwa uwazi katika usimamizi mzuri wa sera za soko huria, sera za kiuchumi na kifedha sambamba na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, makusanyo ya kodi, usimamizi mzuri wa sera za kiuchumi na fedha sanjari na kujenga mahusiano mazuri kati ya walipa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kumechangia ka kiasi kikubwa kuimarika kwa mapato ya kodi. Kwa mfano, mwezi Desemba 2021, TRA ilikusanya Shilingi Trilioni 2.51 sawa na ufanisi wa asilimia 109 wa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 2.29 katika kipindi hicho cha Desemba. Kuvunjwa kwa rekodi hiyo ya makusanyo ya kodi ni kielelezo tosha cha kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais pamoja na Taasisi zote za ndani ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19. Afrika inamtazama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kuwa miongoni mwa viongozi waliochangia kuliweka Bara hili katika ramani nzuri ya dunia kutokana namna alivyofanikiwa kushughulikia suala la UVIKO-19.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango huu wa UVIKO-19 kwa Ustawi wa Taifa na Maendeleo dhidi ya UVIKO- 19 unaakisi dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha inaboresha sekta za jamii. Kwa mfano, sekta ya elimu, afya, maji, maliasili na utalii, pia ujasiriamali na hifadhi ya jamii kwa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie mfano wa mkopo nafuu wa Shilingi Trilioni 1.3 usiokuwa na riba yoyote kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuonesha namna Mheshimiwa Samia, Rais wetu alivyofanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za jamii pamoja na miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
Mheshimiwa Spika, huduma za afya. Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa Shilingi Bilioni 204.4 kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali za afya. Afua hizo, zinajumuisha kuimarisha huduma za dharura, huduma za wagonjwa mahututi, wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu na huduma za maabara. Kwa upande wa vifaa na vifaa tiba, Serikali imenunua mashine za CT Scan 29, MRI Nne, magari 253 ya kubebea wagonjwa kwa lugha nyingine ambulance, magari 250 kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za afya ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri zote nchini, magari manane ya damu salama na magari 30 ya kusambaza chanjo.
Mheshimiwa Spika, huduma za Elimu. Nyote mtakubaliana nami kwamba katika mwaka 2022, tumeshuhudia wanafunzi wote 907,803 waliokidhi vigezo vya kujiunga na Kidato cha Kwanza wakichaguliwa kwa mkupuo mmoja tofauti na miaka ya nyuma ilipotulazimu kuwa na machaguo mawili na wakati mwingine hadi machaguo matatu.
Mheshimiwa Spika, hali hiyo imewezekana ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya Serikali kutumia Shilingi Bilioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 12,000. Katika hatua nyingine ya kuboresha miundombinu ya elimu na kuhakikisha watoto wa kitanzania hawabaguliwi katika kupata elimu, Serikali imetumia Shilingi Bilioni 60 kujenga vyumba vya madarasa 3,000 kwenye vituo shikizi vya Shule za Msingi na hivyo kuondoa changamoto kwa wanafunzi wanaoshindwa kufika kwenye shule mama.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imepeleka Shilingi Bilioni 100.58 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari 214. Taratibu za kuanza ujenzi huo, zinaendelea kwenye Kata za Majimbo yote nchini. Aidha, Shilingi Bilioni 30 zimepelekwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari mpya za wasichana kwenye Mikoa 10, ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kujenga shule moja ya sekondari ya wasichana kila Mkoa wa Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la ufundi stadi, Serikali imeanza ujenzi wa chuo kikubwa cha ufundi Mkoani Dodoma ambapo Shilingi Bilioni 3.44 zimetumika. Ujenzi huo unakwenda sambamba na kuanza ujenzi wa vyuo vingine vinne vya ufundi stadi katika Mikoa ya Geita, Njombe, Rukwa na Simiyu ambayo haikuwahi kuwa na Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA).
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali hapa ni kuhakikisha kwamba vijana wanapatiwa stadi za kazi na ujuzi ili waweze kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya nchi hii na hivyo kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa ajira.
Mheshimiwa Spika, huduma za maji. Katika kutekeleza mpango wa kumtua ndoo mama kichwani, kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, Serikali ilitoa Shilingi Bilioni 104 kwa ajili ya kutekeleza jumla ya miradi ya maji 218 nchini. Kati ya hiyo, miradi 172 inatekelezwa mijini na miradi 46 inatekelezwa vijijini. Miradi hiyo itaongeza idadi ya wananchi wanaonufaika na huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza vilevile.
Mheshimiwa Spika, kiasi cha Shilingi Bilioni 17.5 zimetumika kununua seti 25 za mitambo ya kuchimbia maji, kwa maana ya kuchimba visima kwa Mikoa 25 ya Tanzania Bara. Aidha, Shilingi Bilioni 17.6 zitatumika kununua seti Tano za mitambo ya ujenzi wa mabwawa na vifaa vya utafiti wa maji chini ya ardhi ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ambayo hakuna vyanzo vya uhakika vya maji.
Mheshimiwa Spika, miundombinu ya usafiri na usafirishaji. Katika eneo la usafiri na usafirishaji, Mheshimiwa Rais ameibuka mshindi wa tuzo ya uwekezaji kwenye miundombinu ya usafirishaji na usafiri kwa mwaka 2020, tuzo iliyotolewa na taasisi ya Media for Infrastructure and Finance in Africa (MIFA). Maelezo yaliyotolewa na wadhamini wa tuzo hiyo ambao ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) yameonesha kutambua mchango mkubwa wa Rais wetu katika ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, uwekezaji mkubwa kwenye barabara za mzunguko kwenye Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma, ununuzi wa mabehewa mapya ya treni 1,430 pamoja na usimamizi mzuri wa Serikali unaoongozwa na uwazi wa hali ya juu imekuwa chachu ya mafanikio hayo.
Mheshimiwa Spika, hatua hizo zinazochukuliwa na Mheshimiwa Rais ni muhimu katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ujenzi wa uchumi unaoongozwa na viwanda. Ikumbukwe kwamba miongoni mwa mahitaji muhimu katika ujenzi wa viwanda na uwekezaji ni uwepo wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji, upatikanaji wa maji ya kutosha, huduma nzuri za afya na wafanyakazi wenye ujuzi.
Mheshimiwa Spika, diplomasia ya uchumi. Utekelezaji wa diplomasia ya uchumi umepiga hatua kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha Mheshimiwa Rais wetu mpendwa. Mheshimiwa Rais ametumia vema ziara zake za kikazi nje ya nchi kuhamasisha uwekezaji, kujenga mahusiano mazuri ya kibiashara sambamba na kujenga taswira ya nje ya nchi kwa nchi yetu. Ripoti ya uwekezaji iliyotoka mwezi Juni mwaka 2021, inaonesha kuwa licha ya janga la UVIKO- 19, Tanzania katika mwaka 2020 ilipokea uwekezaji kutoka nje wa takribani Dola za Marekani Bilioni Moja.
Mheshimiwa Spika, aidha, takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa katika kipindi cha Machi, 2021 hadi Februari, 2022, Serikali imeweza kuvutia na kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294. Miradi hiyo inatarajiwa kuwekeza mtaji wa thamani ya dola za Marekani Bilioni 8.13 na kutoa ajira kwa watu wasiopungua 62,000.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Mheshimiwa Rais amefanikiwa kuimarisha mahusiano yetu na nchi jirani.
Kwa mfano, kufuatia ziara yake ya Kitaifa Jamhuri ya Kenya, jumla ya vikwazo 30 visivyo vya kibiashara vilijadiliwa. Kati ya hivyo vikwazo 10 vilipatiwa ufumbuzi na kuondolewa, vikwazo vitano vilifutwa kwa sababu ya kukosa taarifa za kutosha kuweza kujadiliwa na vikwazo 15 vimewekewa ukomo wa kuvitatua ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu 2022.
Mheshimiwa Spika, kupatiwa ufumbuzi kwa vikwazo hivyo kumeimarisha shughuli za kiuchumi za kijasiriamali kwenye maeneo ya mipakani, kuinua vipato kwa wananchi wetu na kuimarisha mtangamano kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo tarehe 29 mwezi wa Tatu mwaka huu 2022 ilipokea mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa hiyo Congo sasa ni nchi ambayo pia ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwahakikishi na kuwahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa zilizotokana na kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara pamoja na ujio wa mwanachama mpya huyu wa Congo unaozidi kuimarisha soko la Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki kibiashara na kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, suala la ushirika. Ushirika umeendelea kuwa sehemu ya kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha unakuwa na tija kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na Taifa kwa ujumla. Hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha utendaji wa vyama vya ushirika zimeanza kuonesha mafanikio makubwa kama ifuatavyo: -
Moja; vyama vya ushirika kuanzisha na kufufua viwanda vidogo na vikubwa 452. Viwanda hivyo ni pamoja na viwanda vya kahawa, alizeti na pamba ikiwemo viwanda vya kuchambua pamba vilivyopo Kahama na Chato.
Mbili; kusimamia urejeshaji wa mali za vyama vya ushirika zikiwemo mashamba, viwanja, majengo, maghala na viwanda, pia nyinginezo zenye thamani ya takriban Shilingi Bilioni 68.
Tatu; kujenga imani ya wakulima katika ushirika ikilinganishwa na hapo awali. Kutokana na imani iliyojengeka, idadi ya vyama vya ushirika vyenye usajili vimeongezeka na kufikia 9,741 kufikia mwaka 2022 ikilinganishwa na vyama 9,185 mwaka 2020, sawa na ongezeko la vyama 556. Kadhalika, kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanachama 914,948 wa VVyama vya ushirika kutoka mwaka 2021 hadi mwaka 2022.
Nne; kuimarika kwa uuzaji wa mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. Hatua hii imewezesha kuimarika kwa bei ya baadhi ya mazao. Mathalan, hivi karibuni tumeona bei ya cocoa inayolimwa kule Mkoani Mbeya, Wilaya ya Kyela ikiongezeka mara dufu kutoka Shilingi 2,500 hadi Shilingi 5,000 kwa kilo baada ya kutumia mfumo wa ushirika na stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Spika, aidha, kupitia uhamasishaji wa masoko na uwekezaji katika vyama vya ushirika, mazao ya aina 10 yenye uzani wa tani 575,296 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.52 yaliuzwa kupitia ushirika kwa kipindi cha Julai 2021 hadi 2022.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kusimamia ushirika, bado kuna changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi ili ushirika uendelee kuimarika. Changamoto hizo ni pamoja na usimamizi usioridhisha wa mali za ushirika, wizi na ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika, kukosekana kwa elimu ya ushirika kwa wadau muhimu, upatikanaji wa masoko na utitiri wa tozo unaofanya bei anayolipwa mkulima kuwa ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya bei ndogo ya mazao, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutafuta masoko ndani na nje ya nchi, kuimarisha viwanda vya ndani vya kuchakata mazao pamoja na kuondoa tozo zisizo za msingi zinazosababisha bei anayolipwa mkulima kuwa ndogo.
Mheshimiwa Spika, mara zote Mheshimiwa Rais amesisitiza kufanya mapitio ya tozo kwa kuzirekebisha au kuzifuta ili kuleta unafuu kwa mkulima. Kwa kuzingatia maelezo hayo ya Mheshimiwa Rais, Tarehe 29 Machi mwaka huu 2022 nikiwa Mjini Karagwe, nilikutana na viongozi na wadau wa ushirika kwa ajili ya kutoa maelekezo na mwelekeo wa usimamizi na uendeshaji wa zao la kahawa Wilayani Karagwe, Wilaya ya Kyerwa na wilaya za jirani kama vile Bukoba Vijijini na pia Muleba na Ngara.
Mheshimiwa Spika, kupitia kikao hicho, nilitangaza uamuzi wa Serikali wa kufuta tozo 42 kati ya 47 zilizokuwa zinatozwa na vyama vya ushirika kwa zao la kahawa. Awali, mkulima alilazimika kulipa Shilingi 805 kwa kila kilo ya kahawa aliyoiuza kutokana na uwepo wa tozo hizo 47. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninatoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo kukutana na wadau wote muhimu ili kuhakikisha mpangokazi wa zao la kahawa kwa ajili ya msimu ujao wa ununuzi unaanza mara moja. Serikali kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua za makusudi kunusuru hali ya wakulima nchini ili kuhakikisha kuwa kilimo kinakuwa chachu katika kutengeneza ajira, upatikanaji wa malighafi za viwanda na kuwapatia tija kwa wakulima wenyewe. Vilevile, Serikali inafanya mapitio ya tozo zilizopo katika mazao mbalimbali ili kuufanya ushirika uwe na tija na mkulima aweze kunufaika zaidi.
Mheshimiwa Spika, suala la amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa. Itakumbukwa kuwa Tarehe 7 Aprili, 2022, ilikuwa ni kumbukizi ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza na muasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tukio hilo lilifuatiwa na mdahalo wa kumbikizi ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa muasisi mwingine wa Taifa hili Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mheshimiwa Spika, uhuru tunaoushuhudia leo, amani na umoja tunaoushuhudia leo, mshikamano wa Kitaifa tunaoushuhudia leo na kustahimiliana kuliko tufikisha hapa tulipo leo, ni miongoni mwa misingi ya uongozi uliotukuka na wenye kujali utu tulioachiwa na waasisi wetu ambao Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania ameyaamua kuuishi.
Mheshimiwa Spika, 19 Machi, 2021 baada ya kuapa kuliongoza Taifa hili, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitamka maneno yafuatayo, naomba kunukuu “… Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa, ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, undugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu na Utanzania wetu. Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini…” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tangu atamke maneno hayo, Mheshimiwa Rais ameendelea kuyaishi kwa vitendo huku akiwa kinara wa kuhubiri amani na mshikamano hapa nchini, nia yake ya dhati ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa inajionesha wazi katika kuundwa kwa kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia, kufuatia maoni yaliyotolewa katika mkutano wa wadau wa demokrasia nchini uliofanyika tarehe 15 na 16 Disemba, 2021 hapa Jijini Dodoma.
Mheshimiwa Spika, katika kuonesha nia yake ya kuleta maridhiano na amani, Mheshimiwa Rais aliwataka wajumbe wa kikosi kazi hicho kwenda kutafakari zaidi na hatimae kuwasilisha taarifa itakayoainisha njia bora za kutatua changamoto ambazo nyingine ametaka zitafutiwe ufumbuzi wa haraka hata kabla ya kufanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.
Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Rais alitaka kikosi kazi hicho kuchambua masuala yote ambayo hayaleti siasa za tija, kukwaza demokrasia na kufanya siasa kuwa chuki. Aidha, katika kudumisha amani na maridhiano ya dhati, Mheshimiwa Rais alitoa rai kwa vyombo vya habari kuwa na mahusiano chanya kati ya Serikali na vyama vya siasa bila kuwa na upendeleo.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza dhamira yake ya ushirikishwaji na usawa, Mheshimiwa Rais alitoa wito kwa vyama vya siasa kuzingatia usawa wa kijinsia, kwa kutoa nafasi kwa wanawake ili waweze kushiriki katika siasa ndani ya vyama vyao. Aidha, aliwataka wanawake kutambua wajibu wao katika vyama vyao na jamii kwa ujumla na kuhakikisha wanaelewa ipasavyo ajenda zinazowawezesha na kuwasemea wanawake wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa katika kuhakikisha tunakuwa wamoja, sambamba na kuimarisha demokrasia nchini huku akitambua kuwa umoja wetu ndiyo uhai wetu. Kwa msingi huo, jitihada tunazozifanya za kujenga uchumi imara, shindani na endelevu zimebebwa na misingi ya amani, maelewano na mshikamano.
Mheshimiwa Spika, nami nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kusisitiza kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na kwamba, kwa hakika nchi yetu itajengwa na watu wenye itikadi zote za siasa. Aidha, nitoe rai kwa vyama vyote vya siasa kuendeleza siasa za maridhiano na amani sambamba na kutumia vema haki ya demokrasia kwa maslahi mapana ya Watanzania. Katika kila sera na mipango ndani ya vyama vyetu, hatunabudi kuwatanguliza Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha kumbukizi ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kumbukizi ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tunapaswa kujiuliza tunairithisha nini, tunairithisha vipi misingi muhimu hususan uongozi iliyojengwa na waasisi hao kwa vizazi vya sasa na vinavyofuata? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa lugha nyingine, tunayo kila sababu ya kufanya tafakari kuhusu namna bora ya kuhakikisha urithi wa maisha ya waasisi wetu ambao walikuwa tayari kuacha kila kitu kwa ajili ya Taifa hili umeenziwa, unatambulika, unahifadhiwa, unasherehekewa na unajulikana kwa Watanzania wengi hususan vijana wa leo. Urithi huo ni tunu na nguzo kubwa ya Taifa letu hususan katika masuala yanayohusu maadili ya uongozi, kuimarisha muungano, kuondoa tofauti za kidini, kikabila pamoja na kuchagiza mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini.
Mheshimiwa Spika, sensa ya Watu na Makazi. Tarehe 08 Aprili, 2022, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizindua rasmi Tarehe na Nembo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Tukio hilo ni sehemu ya hatua muhimu kuelekea kukamilisha Sensa ya Watu na Makazi siku ya tarehe 23 Agosti 2022.
Mheshimiwa Spika, binafsi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amelibeba suala la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Mheshimiwa Rais amekuwa akishiriki kwa karibu katika hatua zote muhimu zenye lengo la kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Kwa mfano, tarehe 14 Septemba, 2021 katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, Mheshimiwa Rais alizindua Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ikiwa ni mwongozo wa kuhamasisha wananchi wote kushiriki zoezi la kuhesabiwa ifikapo Agosti, 2022. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile, tarehe 08 Februari, 2022, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Jakaya Kikwete (JKCC) uliopo Jijini Dodoma. Zoezi la utambuzi na kujenga mfumo wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima ni sehemu muhimu kuelekea kwenye Sensa ya Watu na Makazi vilevile.
Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi huo unaotarajiwa kutumia shilingi bilioni 28, utachangia masuala yafuatayo: -
Moja, kuifungua Tanzania kuelekea kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda (uchumi wa kidijitali) sambamba na kuimarisha biashara ya Kimataifa.
Mbili; kuimarisha Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki kufikika kwa haraka, uhakika na wepesi zaidi na hivyo, kufungua milango ya biashara Kimataifa na shughuli nyinginezo za kiuchumi.
Tatu; Kusaidia utambuzi wa maeneo ya uwekezaji wa viwanda, ufugaji na kilimo na hivyo kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi hususan baada ya kukamilika kwa uandaaji wa ramani za kidijitali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, Kuimarisha huduma za ulinzi wa usalama sambamba na kurahisisha shughuli nyingine za kijamii kwa kuwa mfumo huo unatambulisha mahali halisi ambapo mtu anaishi, mahali ilipo, biashara yake au ofisi anayofanyia kazi kwa kufuata jina la barabara na mitaa, namba ya nyumba au jengo pamoja na Postikodi.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha viongozi na watendaji wote hususan Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kusimamia ipasavyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kwamba kazi ya kuweka mfumo wa anwani za makazi na postikodi itekelezwe kwa haraka na kuhakikisha inakamilika ifikapo mwezi 30 Mei, 2022.
Mheshimiwa Spika, ninalishukuru Bunge lako Tukufu kwa kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 215.6 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi. Aidha, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuhamasisha wananchi wote katika Majimbo yetu ili washiriki ipasavyo katika zoezi la kuhesabiwa kwa kutoa taarifa sahihi za kijamii, kiuchumi na mazingira wanayoishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwaomba viongozi wetu wa dini na kimila ambao wamekuwa bega kwa bega na Serikali tangu kuanza kwa zoezi hili, waendelee kutusaidia kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ili kuwawezesha makundi yote ya jamii kushiriki zoezi hilo. Aidha, nitoe wito kwa viongozi na watendaji wa umma na sekta binafsi kutumia Nembo ya Sensa kwenye shughuli zote za umma na shughuli binafsi pia hadi pale zoezi la sensa ya watu na Makazi litakapokamilika mwezi Agosti, 2022.
Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana na mimi kwamba idadi yetu ndiyo mtaji wetu. Hivyo, kufanikiwa kwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 ambalo hivi sasa limefikia asilimia 79 kutaiweka nchi yetu kwenye ramani nzuri kimataifa na kuiwezesha kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa kwenye nyanja za kiuchumi na maendeleo.
Mheshimiwa Spika, ndugu zangu Watanzania, ninawasihi tukahesabiwe na tutoe ushirikiano wa kutosha kwa Makarani na Wasimamizi wa sensa siku ya Tarehe 23 Agosti, 2022 watakapotutembelea katika kaya zetu. Zoezi hili ni muhimu kwani linakuwa ndiyo msingi wa taarifa ambazo zitatumika kwenye mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.
Mheshimiwa Spika, majibu ya hoja ambazo zimeletwa mbele yetu. Kwa mujibu wa Kanuni ya 118 (13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020, naomba nitumie nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge zilizoibuliwa wakati wa mjadala huu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ilikuwa ni Serikali iweke utaratibu mzuri wa kutembelea miradi ya maendeleo ili kuepuka kutembelea miradi mingi kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Spika, usimamizi wa miradi ya maendeleo umeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali, katika kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaakisi thamani ya fedha za umma. Sambamba na hilo, Serikali itaendelea kutumia ziara za viongozi kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa miradi na kuchukua hatua stahiki dhidi ya ubadhirifu wa aina yoyote utakaojitokeza. Kwa upande mwingine, Serikali itaandaa utaratibu mzuri ikiwemo kutenga muda wa kutosha wakati wa ziara za viongozi ili kuhakikisha kwamba miradi na shughuli muhimu za kijamii zinafikiwa.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeandaa Mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo unaoainisha majukumu na wajibu wa kila mdau katika usimamizi wa miradi. Pamoja na mambo mengine, mwongozo huo unazielekeza taasisi zote za umma kuandaa mpango wa mwaka wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi (Monitoring and Evaluation Plan).
Mheshimiwa Spika, tayari mwongozo huo umeshasambazwa katika Wizara, Halmashauri na Taasisi zote za Serikali na utaanza kutumika katika mwaka wa fedha 2022/ 2023. Nitumie fursa hii kusisitiza taasisi zote za umma kuhakikisha zinaandaa mipango ya ufuatiliaji na tathmini ya mwaka ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mwongozo huo.
Mheshimiwa Spika, ili mwongozo huo ulete matokeo tarajiwa, ninaelekeza viongozi na watendaji walio katika Mikoa, Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba, wanatembelea mara kwa mara na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi katika maeneo yao. Aidha, wawatembelee wananchi katika maeneo yao, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi badala ya kusubiri ziara za viongozi wa Kitaifa. Serikali ihakikishe wananchi wanashirikishwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ilikuwa ni Serikali ihakikishe wananchi wanashirikishwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, hapa jibu ni kwamba Mwongozo wa Taifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi umeainisha umuhimu wa kushirikisha wananchi katika hatua zote za utekelezaji wa miradi. Lengo la Serikali kupitia mwongozo huo ni kuongeza uelewa, umiliki, uwajibikaji na thamani ya miradi inayotekelezwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua zote hizo ili kuhakikisha kwamba wananchi wanaibua changamoto halisia za maendeleo katika maeneo yao, kwa kufanya hivyo, wanaingia moja kwa moja katika mnyororo mzima wa utekelezaji wa miradi inayotoa fursa za maendeleo, kuimarisha huduma za jamii, ajira na kujiongezea kipato.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuzingatia ushiriki wa jamii ikiwa ni kigezo muhimu katika kuidhinisha miradi na hivyo kuibua uhalisia wa malengo ya utekelezaji wa miradi hiyo katika kutatua kero na changamoto za wananchi.
Mheshimiwa Spika, kampuni za ndani zitambuliwe, ziwezeshwe na kupewa fursa za kushindana na Makampuni ya nje katika zabuni zitakazotangazwa kupitia Miradi ya Ujenzi wa Bomba la Mafuta la Hoima (Uganda) – Tanga (Tanzania), hatua hii itasaidia kuongeza ajira kwa wazawa. Hii ilikuwa ni hoja nyingine ya kwamba kampuni za ndani zitambuliwe, ziwezeshwe na kupewa fursa za kushindana na makampuni ya nje katika zabuni zitakazotangazwa kupitia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima (Uganda) – Tanga (Tanzania). Hatua hii itasaidia kuongeza ajira hususani kwa wazawa.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya Serikali ni kwamba, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba wazawa kupitia kampuni zao wanapata fursa ya kushiriki katika miradi ya kimkakati na uwekezaji. Aidha, katika kuhakikisha tunawafikia kwa urahisi, tarehe 04 Oktoba, 2021 Serikali ilizindua kanzidata ya watoa huduma, wawekezaji na wasambazaji bidhaa wazawa. Kanzidata hizo, zinawawezesha watoa huduma na wasambazaji bidhaa wazawa, kupata taarifa ya zabuni zinazotangazwa na wawekezaji mbalimbali ndani na nje ya nchi. Hatua hizo zinawezesha watoa huduma na wasambazaji bidhaa ambao ni wazawa kutambua na kuunganishwa na fursa zinazotolewa na wawekezaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, katika kukuza Ushirika wa Watanzania kwenye mradi wa East African Crude Oil Pipeline (EACOP), Serikali imekutana na kampuni za wazawa na wajasiriamali kwa nyakati tofauti, katika Mikoa nane ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lengo la kukutana na wadau hao katika Mikoa ambayo bomba la mafuta linapita ni kuwafahamisha tu kwamba fursa zilizopo katika ujenzi wa bomba hilo ni za kwao ili waweze kuzitumia kikamilifu. Mikutano hiyo, pia ilishirikisha Taasisi za fedha ambazo zilipata nafasi ya kueleza fursa za mitaji zitolewazo na taasisi zao.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia kongamano la EACOP lililofanyika tarehe 23 Septemba, 2021 imeendelea kuwajengea uwezo watoa huduma na wasambazaji bidhaa wazawa. Kongamano hilo lililenga kuongeza uelewa wa kampuni za wazawa kwa wajasiriamali juu ya hali ya mradi wa EACOP, pamoja na fursa zinazopatikana katika awamu ya ujenzi wa kwanza wa bomba hilo, ikiwemo fursa ya ajira na zabuni za manunuzi.
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa wito kwa kampuni, watoa huduma na wasambazaji bidhaa wazawa kujisajili, katika kanzidata ya watoa huduma na wasambazaji bidhaa wazawa katika sekta ya mafuta na gesi ili kupata fursa zitakazotokana na mradi wa EACOP.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni Serikali iangalie ni jinsi gani inaweza kushusha bei za mafuta, ikiwezekana kwa kutoa ruzuku, kutenga bajeti maalum ya kufidia bei ya mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na swali hili ambalo limechukua maeneo mengi juu ya upandaji wa bidhaa mbalimbali, kati ya mwaka 2019/2020 hadi mwaka 2021/2022 bei za bidhaa nyingi zimekuwa zikipanda kutokana na matukio mbalimbali yanayoikumba nchi yetu na dunia kwa ujumla. Baadhi ya matukio makubwa yaliyoikumba dunia katika kipindi hicho ni pamoja na janga la UVIKO-19, mabadiliko ya hali ya hewa kama vile ukame, uzalishaji mdogo wa bidhaa kwenye viwanda vyetu na maeneo mbalimbali na mashambani na ukosefu wa malighafi. Lakini pia, uwepo wa tukio ambalo linaendelea kwa sasa nchini Ukraine na Urusi la vita.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mwingiliano wa kibiashara, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Mataifa mengine, matukio hayo vilevile yamekuwa na athari za moja kwa moja na wakati mwingine zisizokuwa za moja kwa moja katika uchumi wa maisha ya watu wetu.
Mheshimiwa Spika, janga la UVIKO-19 lilisababisha shughuli nyingi za kiuchumi kusimama duniani. Hali hiyo ilipelekea baadhi ya bidhaa muhimu ikiwemo mbolea, sukari na mafuta ya kula kupanda bei.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nchi yetu, hatua madhubuti zilichukuliwa na Serikali ikiwemo kuruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kiuchumi kuliufanya pia uchumi wa nchi yetu kuendelea kuwa na shughuli za uzalishaji zikituhakikishia usalama wa chakula ikilinganishwa na maeneo mengine ambako hawakuchukua hatua kama ambazo sisi tulichukua.
Mheshimiwa Spika, wakati nchi ikiendelea kuponya majeraha ya kiuchumi yaliyosababishwa na UVIKO-19, mwezi Februari 2022 kulizuka mgogoro mwingine duniani ulioingiza nchi ya Urusi kwenye vita dhidi ya Ukraine. Kama ambavyo mnafahamu, Urusi ni mzalishaji mkubwa wa bidhaa za mafuta akiwa ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa watatu duniani. Kadhalika, nchi ya Urusi na Ukraine ni wazalishaji wakubwa wa bidhaa za ngano duniani. Kwa upande wa Tanzania, takriban asilimia 57 ya ngano inayotumika hapa kwetu nchini imekuwa ikitoka kwenye ukanda wa Ukraine na Urusi.
Mheshimiwa Spika, kufuatia vita hiyo, nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani ziliamua kuiwekea vikwazo Urusi ikiwa ni pamoja na kutafuta vyanzo mbadala vya mafuta na gesi ili kuachana na ununuzi wa bidhaa hizo kutoka Urusi.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba vikwazo dhidi ya Urusi vimechangia kupungua kwa kiwango cha uzalishaji wa mafuta duniani, bidhaa za ngano vilevile zimepungua pamoja na mbolea na hivyo kusababisha ongezeko la bei ya bidhaa hizo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kueleza, Tanzania ikiwa ni sehemu ya dunia nasi tumekuwa sehemu ya waathirika kiuchumi kufuatia kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa za mafuta na ngano kutoka kwenye nchi hizo za Urusi na Ukraine. Kwa mfano, tumeshuhudia kupanda kwa bei ya mafuta japo bado nchi yetu ina unafuu mkubwa ikilinganishwa na baadhi ya maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, Tanzania kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine duniani, Serikali yetu naendelea kuwahakikishia Watanzania kwamba bidhaa hizo zinazopatikana katika masoko yote nchini, sambamba na kuchukua hatua madhubuti zenye kuleta unafuu kwa wananchi zitaendelea kuangaliwa kwa ukaribu na ufuatiliaji wake kwa ukaribu zaidi.
Mheshimiwa Spika, tarehe 11 Aprili, 2022 Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Mbunge, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, pamoja na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango, walifanya mkutano na wadau mbalimbali wazalishaji. Kupitia mkutano huo, Waheshimiwa Mawaziri walieleza hali halisi kuhusu mwenendo wa bei na hatua ambazo Serikali inachukua katika kukabiliana na hali hiyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Mawaziri, ambao pia waliungwa mkono na wazalishaji, napenda kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kufanya yafuatayo: -
Moja; kuhakikisha kwamba, bei ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi zinakuwa himilivu na kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi Serikali kupitia Kamati za bei za Mikoa na Wilaya itaendelea kufanya tathmini ya kuona namna ya kuleta unafuu katika masoko kila Mkoa na kila Makao Makuu ya Wilaya kupitia Kamati hizo za bei. Kamati hizi zinazoongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndizo zenye wajibu wa kupita kwenye masoko yetu kuona bidhaa zilizopo, zile zinazozalishwa ndani ambazo hazina sababu ya kupandishwa bei zitakuwa zinadhibitiwa na kamati ya bei ya ngazi ya Wilaya na Mkoa.
Mbili; kuendelea kushirikiana na sekta binafsi hususan wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa hizi, ili kupanga viwango vipya vya kodi vitakavyoleta unafuu kwa mlaji, kama vile kupunguza kodi ya baadhi ya bidhaa, pia kuhakikisha kwamba bidhaa hizo nazo zinapatikana kwenye maeneo hayo.
Tatu; kupunguza gharama za vifaa vya usafiri na usafirishaji ambazo zimekuwa na athari ya moja kwa moja kwenye kupanda bei ya bidhaa. Kupungua kwa gharama hizo kunategemewa kushusha gharama na bei ya bidhaa nyingine ndani ya masoko yetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba, inaimarisha uzalishaji wa bidhaa za viwandani, hasa bidhaa za chakula zinazoingizwa kwa wingi kutoka nje ikiwemo ngano, mafuta ya kula na sukari kwa kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji hapa ndani, kwa kutoa vivutio stahiki kwa wawekezaji wetu. Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa uwekezaji wa ndani kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali ili kukabiliana na aina hii ya mtikisiko wa kiuchumi. Pia, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya kisera za kibiashara ili kuona maeneo yanayoweza kuleta unafuu kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, ninaielekeza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali kwenye soko na kuchukua hatua stahiki kwa wakati, sambamba na kusimamia vema mfumo wa kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo usioridhisha wa bei za bidhaa sokoni. Kamati za bei na biashara za Mikoa na Wilaya zihakikishe zinafuatilia kwenye masoko na kujiridhisha na uhalisia wa kupanda kwa bei za bidhaa kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, vilevile, ninazielekeza Mamlaka na Serikali za Mitaa, Taasisi za Serikali zilizopewa dhamana ya kusimamia mienendo ya masoko ya bidhaa kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kwa umakini mkubwa sambamba na kudhibiti vitendo vya upandishaji bei holela wa bidhaa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia, kukemea vitendo vya baadhi ya wazalishaji na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kupanga bei, kufanya mgomo, kukubaliana katika manunuzi na kuuza kwa bei ya juu, mbinu ambazo wakati mwingine zimekuwa chanzo cha kupanda kwa bei za bidhaa. Wale wote watakaobainika kufanya michezo hiyo, hatutosita kuwachukulia hatua za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Watanzania kwanza kuendelea kuwa wamoja na tuendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuufanya uchumi wa nchi yetu kuwa shindani na wa viwanda kwa maendeleo ya watu. Serikali kwa upande wake itaendelea kuhakikisha kuwa hakuna uhaba wa bidhaa nchini wakati ikiliangalia vizuri suala la bei na kuona namna ya kutoa unafuu kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, niendelee kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali imejipanga vizuri kupitia Kamati za Bei, kama nilivyoeleza awali na kutoa agizo kwa wakuu wa mikoa kuziimarisha kamati hizo na kuzifanya kamati hizo ziwe zinafanya kazi mpaka kwenye ngazi ya Wilaya zikiongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na kupita kwenye masoko kukagua bidhaa zote na kuona gharama zake kama ni halisia au la, lakini pia kukaa na wafanyabiashara wa maeneo haya ya biashara kufanya mapitio ya gharama za bidhaa hizo ili kuona uhalisia wa bei na hatimae tuhakikishe kwamba, wananchi wanaopata huduma kwenye maeneo hayo wanapata unafuu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ya tano; wanasema fedha nyingi zinatumika kwa ajili ya shughuli za mbio za mwenge wa uhuru. Je, Serikali haiwezi kuja na mbinu mbadala ya kuenzi mwenge wa uhuru badala ya kuukimbiza kila mwaka?
Mheshimiwa Spika, jibu la swali hili ni kwamba, tangu kuasisiwa kwa Taifa letu, uhuru na umoja umeendelea kuwa nguzo ya amani na mshikamano wetu. Ukweli huo unajidhihirisha katika itikadi na falsafa za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, zilizojikita katika kuhakikisha kunakuwepo na usawa na utu wa ubinadamu kwa binadamu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, falsafa hizo zimeendelea kuitambulisha Tanzania katika medani za Kimataifa kuwa ni nchi yenye kupinga ukandamizaji, unyonyaji, unyanyasaji na mifumo ya kitabaka yenye kudhalilisha utu wa binadamu. Hali hiyo inajionesha waziwazi katika kauli aliyoitoa Baba wa Taifa kabla nchi yetu haijapata uhuru, mwaka 1958 aliposema, naomba kunukuu, “Sisi Watu wa Tanganyika tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tangu kipindi cha uhuru, Mwenge umeendelea kuwa miongoni mwa alama tano za nchi hii, ikiwa ni pamoja na Bendera, Twiga, Wimbo wa Taifa na Ngao ya Taifa pamoja na Mwenge wenyewe. Hivyo, tumeendelea kuutumia Mwenge wa Uhuru kuhamasisha ujenzi wa Taifa lenye watu wenye amani, upendo, matumaini na kuheshimiana kwa misingi ya utu na usawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vijana Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuwa kielelezo cha ukakamavu na uzalendo walionao katika ulinzi na ujenzi wa Taifa hili. Pia, Mwenge wa Uhuru umekuwa sehemu ya kuhamasisha wananchi kubuni na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika nyanja za kilimo, ufugaji, uvuvi, uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji, umeme na huduma za jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2010- 2021, jumla ya miradi 15,212 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 9.19 iliyotokana na michango ya wananchi, Serikali Kuu, Halmashauri na wahisani ilikaguliwa na mingine kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi. Mbio za Mwenge wa Uhuru pia zimekuwa zikitumika kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya lishe bora, jinsi ya kupambana na rushwa, dawa za kulevya, maradhi yanayotishia ustawi wa jamii ya watu wetu kama vile UKIMWI, Malaria, UVIKO -19 na magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, kuna umuhimu wa kuendelea na Mbio za Mwenge wa Uhuru kila mwaka kwani lengo lake kuu ni kuwakumbusha Watanzania wote na vizazi vijavyo juu ya jukumu lao la kulinda uhuru, umoja na amani ambavyo vimekuwepo ili viweze kuendelea na kudumu wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapoelekea kuhitimisha maelezo yangu, nirudie tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango yenu yenye kuonesha ni jinsi gani tupo pamoja katika kuwatumikia Watanzania sambamba na kusimamia mwelekeo wa sera za Chama cha Mapinduzi zenye lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi imara, unaojitegemea na shindani, lakini Wabunge wenzangu naomba basi na ninyi mfikirie namna ya kupitisha bajeti hii, ili tuendelee kufanya kazi kwa pamoja kupitia Majimbo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie pia fursa hii kuwasihi viongozi na watendaji wote hususan katika sekta za umma, kuiishi ndoto ya Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuona Watanzania wanafikiwa kwenye maeneo yao, na wanapofika kwenye ofisi za umma wanapokelewa, wanasikilizwa na kuhudumiwa kikamilifu. Eneo hili ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu na maendeleo ya haraka.
Mheshimiwa Spika, niwatake viongozi wenzangu kuendelea kufuatilia kwa karibu na umakini mkubwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yetu ili kuhakikisha inalingana na thamani ya fedha inayowekezwa kwenye maeneo yetu. Kadhalika, niendelee kuwasihi ndugu zangu Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili kazi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ninawasihi Watanzania kutumia vyema kipindi hiki cha toba cha Kwaresma na mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuiombea nchi yetu iendelee kuwa tulivu, yenye amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kuwaombea viongozi wetu ili waweze kutekeleza wajibu wao na majukumu yao kwa jamii yetu hasa katika kuinua uchumi na mafanikio makubwa. Aidha, nichukue nafasi hii kuwatakia heri ya sikukuu ya Pasaka kwa ndugu zetu wote wakristu na mfungo mwema waislamu n ahata huko mwisho kutakapokuwa na Iddi yote haya tunawatakia kila la heri kwa sherehe hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, sasa, naomba Bunge lako Tukufu, narudia tena. Naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake ikiwemo na Mfuko wa Bunge kama nilivyowasilisha katika hoja yangu ya tarehe 06 mwezi huu wa Nne, 2022. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa fadhila zake ambazo zimetuwezesha kukutana kwenye Kikao hiki cha Sita cha Mkutano wa Kumi na Moja wa Bunge la Kumi na Mbili kwa ajili ya kuhitimisha mjadala kuhusu Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, mbili, kipekee nakushukuru sana wewe binafsi, pia Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuliongoza kwa umahiri Bunge lako Tukufu wakati wa mjadala kuhusu Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2023/2024 tangu nilipowasilisha hoja hii.
Mheshimiwa Spika, tatu, natoa shukrani zangu za dhati kwa Wajumbe wa Kamati za Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba. Pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini pia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki na Kamati ya Kudumu ya Bunge, Ustawi na Maendeleo ya Jamii chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kwa kazi kubwa waliyoifanya ikiwemo kutoa michango yenye tija kwenye hoja ya Waziri Mkuu, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nne nitumie fursa hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri wa Sekta na Naibu Waziri waliochangia hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu, kadhalika nawashukuru Makatibu Wakuu na Naibu Katibu Mkuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano wao mkubwa wa kujitoa kwao katika kufanikisha Hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu, Taasisi zake pamoja na Mfuko wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, tano, vile vile niwashukuru kwa dhati watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri waliyoifanya na ushirikiano wanaoendelea kunipatia katika kipindi cha maandalizi hadi tunapoelekea kuhitimisha mjadala wa Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sita, napenda pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, wenzangu wote kwa hoja na michango yenu muhimu yenye nia ya kuimarisha utendaji wa Serikali. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kuwa michango yenu itakuwa chachu katika kutekeleza kikamilifu wajibu wetu wa Kikatiba na vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wote kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge 101 wamechangia Hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa mjadala huu kati yao Waheshimiwa Wabunge 10 walichangia kwa njia ya maandishi.
Mheshimiwa Spika, natoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Aidha, kutokana na ufinyu wa muda naomba uridhie nisiwataje mmoja mmoja kwa majina na badala yake majina yao yaingizwe moja kwa moja kwenye Hansard. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati nikiendelea na mjadala wa Hoja ya Waziri Mkuu. Serikali imetoa majibu ya hoja nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge, kupitia Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda Serikali itatoa majibu yenye ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zilizosalia kwa maandishi, lakini vile vile Waheshimiwa Mawaziri, wataendelea kutoa ufafanuzi wa kutosha wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa kwenye mjadala huu wakati wakiwasilisha hoja ya bajeti za sekta zao.
Mheshimiwa Spika, pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 4 Aprili, 2023 katika Mkutano wake wa Kumi na Moja, Kikao cha Kwanza, Bunge lako Tukufu liliazimia kwa pamoja kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuimarisha demokrasia na kukuza diplomasia ya uchumi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, nami nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitaungana na Waheshimiwa Wabunge, wenzangu kumshukuru kwa mara nyingine tena Mheshimiwa Rais, kwa juhudi zake katika kuhakikisha kuwa ustawi wa demokrasia nchini sambamba na kuhimarisha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kuwaletea maendeleo Watanzania.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia falsafa yake ya maridhiano, ustamilivu, mageuzi na mabadiliko ameonyesha wazi na tena kwa vitendo nia yake ya kuifanya Tanzania kuwa moja, salama na bila kundi lolote kuwa nyuma katika kufurahia demokrasia ya kweli hapa nchini. Kwa lugha nyingine amefanikiwa kuendeleza misingi aliyoipokea kutoka kwa watangulizi wake na Waasisi wa Taifa hili ya kukaa pamoja na kushirikiana katika kutafakari, kujadili na kutafuta suluhu ya mambo yanayotuhusu na hivyo kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Mheshimiwa Spika, nasi tukiwa wawakilishi wa wananchi tumefanya jambo la msingi kutumia jukwaa hili adhimu kabisa katika kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, katika kuimarisha demokrasia nchini. Niendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tuendelee kuenzi mfumo wa kujadiliana, kukosoana na kutumia Bunge hili Tukufu kuibua mijadala kitaifa pamoja na kuikosoa na kuirekebisha Serikali pale inapobidi.
Mheshimiwa Spika, vile vile nikishukuru Kituo cha Demokrasia Nchini (TCD) kwa kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, katika kuimarisha demokrasia pamoja na kutatua changamoto za maendeleo ya demokrasia hapa nchini. Sambamba na (TCD) inalishukuru sana pia Baraza la Vyama vya Siasa Nchini kwa kuendelea kuhimiza siasa za kistaarabu zinazozingatia sheria na maslahi ya nchi kwa ujumla na kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Vyama vya Siasa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, tangu kuundwa kwake mwaka 2009, Baraza la Vyama vya Siasa limefanya mambo mengi katika kuhakikisha kunakuwa na siasa za kistarabu zinazozingatia sheria na maslahi ya nchi kwa ujumla na kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Vyama vya Siasa. Aidha, Baraza limekuwa kiungo muhimu katika kufanikisha kuundwa kwa kikosi kazi cha Mheshimiwa Rais, ili kushauri masuala mbalimbali ya kuboresha demokrasia ya vyama vingi hapa nchini kwetu.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kutoa rai kwa Baraza la Vyama vya Siasa, kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Serikali Kuu na wadau wengine wa Demokrasia ya Vyama vingi ikiwemo Taasisi zisizokuwa za Serikali na zile za Serikali kama Jeshi la Polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na Bunge. Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wote muhimu katika kujenga mustakabali mwema wa demokrasia yetu Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nianze kuzungumzia huduma za elimu. Nyote mtakubaliana nami kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya marekebisho ya mazingira kujifunzia na kufundishia kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu. Sote tumeshuhudia maboresho makubwa yaliyofanywa katika shule zetu za sekondari, vyuo vya kati na vile vya elimu ya juu hususani katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu na upanuzi wa taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa upande wa sekondari kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imefanikiwa kujenga vyumba vya madarasa elfu ishirini na kuwezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa mkupuo mmoja kwenda shule. Licha ya mafanikio hayo kwa upande wa elimu ya sekondari katika kipindi cha hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia uwepo wa changamoto za msongomano wa wanafunzi wa shule za msingi kwa baadhi ya maeneo, mathalani kati ya shule za msingi 17,000,182 zilizosajiliwa shule 10,000,804 sawa na asilimia 62.87 zina msongamano mkubwa wa wanafunzi.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie mpango wa Serikali kuboresha elimu kwenye shule za msingi. Kufuatia hali hiyo Serikali imeanza kutekeleza mpango wa maboresho makubwa ya elimu msingi. Pamoja na mambo mengine mpango huo unalenga kuondoa changamoto ya msongamano wa wanafunzi kwenye shule za msingi na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Hadi kufikia Machi, 2023, Serikali imetoa shilingi bilioni 230 kwa halmashauri zote nchini kwa ujenzi wa shule mpya za msingi 302, ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa 3,338 kwenye shule za msingi zenye msongamano mkubwa wa wanafunzi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine maboresho haya yameenda sambamba na ukarabati wa shule nane za msingi na ujenzi wa nyumba 41 za Walimu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia ili waweze kutimiza zao na falsafa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Serikali imetenga shilingi bilioni saba kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vilivyoboreshwa vya mafunzo ya elimu ya awali na mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu wa madarasa ya awali. Kupitia mpango huu madarasa 7,000 ya elimu ya awali yatashehenezwa na vifaa mbalimbali na Walimu zaidi ya 34,000 wa elimu ya awali watajengewa uwezo kuhusu matumizi ya vifaa hivyo pamoja na mbinu bora za ufundishaji.
Mheshimiwa Spika, hatua hizo zinatekelezwa sanjari na mpango wa miaka mitano ya mafunzo endelevu ya Walimu kazini (MEMKWA). Lengo ni kuboresha utendaji wa Walimu darasani na ujifunzaji wa wanafunzi ambapo Walimu wote wa shule za msingi watanufaika na mpango huo.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kutoa majibu ya hoja mbalimbali. Kwa mujibu wa Kanuni ya 118 kipengele cha 13 cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Februari, 2023, naomba nitumie nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge zilizoibuliwa wakati mjadala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ilikuwa ni Wakurugenzi wa Halmashauri wanazitumia fedha za Mfuko wa Jimbo kinyume cha sheria. Fedha hizi hazitumiki kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo hasa Maafisa Manunuzi kuzuia ununuzi wa vifaa vilivyopendekezwa na Mheshimiwa Mbunge kununuliwa. Je, Mfuko wa Jimbo ni wa Mbunge au ni wa Mkurugenzi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jibu hapa ni kwamba, moja ya hoja iliyoibuka wakati wa kuchangia Bajeti ya Waziri Mkuu ni kuhusu fedha hizi kutokutumika kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo hasa kutokana na Maafisa Manunuzi kuzuia ununuzi wa vifaa vilivyopendekezwa kununuliwa.
Mheshimiwa Spika, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba, Fedha za Mfuko wa Jimbo zinasimamiwa na Sheria ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, Sura Na.99 na imeeleza kinagaubaga kuwa usimamizi wa fedha za Mbunge wa Jimbo utafanyika kupitia Kamati ya Mfuko wa Jimbo hilo ambayo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hilo na Katibu wake ni Afisa Mipango wa Halmashauri husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa lugha nyingine Mheshimiwa Mbunge, ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Jimbo inayoratibu miradi na shughuli zitakazoelekezwa kupitia Mfuko huo na pia ndiye mwenye mamlaka ya kuitisha vikao vya Kamati hiyo. Kwa upande wake Kamati inalo jukumu la kupokea, kujadili na kupitisha vipaumbele vya matumizi ya fedha za Mfuko huo wa Jimbo kama ilivyokubaliwa na hakuna kikao ambacho kitakaliwa nje ya Mwenyekiti ambaye ni Mbunge wa Jimbo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ni Afisa Masuuli na anao wajibu wa kusimamia na kuhakikisha kwamba fedha za Mfuko za Jimbo zinaelekezwa kwenye vipaumbele vilivyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo ambayo Mwenyekiti ni Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kadhalika sheria inataka ununuzi wa bidhaa, kazi na huduma kwa kutumia fedha za mfuko ufanyike kwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi, Sura Na.410 na kwa msingi huo nitumie nafasi hii kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuheshimu na kuzingatia vipaumbele vinavyopitishwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo pamoja na kuhakikisha matumizi ya fedha hizo yanazingatia Sheria ya Mfuko wa Jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia ipo Sheria ya Fedha za Umma, Sura ya 348 na Sheria ya Manunuzi, Sura 410. Aidha, nimemwelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa Maafisa Manunuzi kwenye Halmashauri hawawi vikwazo katika kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vya matumizi ya Fedha za Mfuko wa Jimbo hususani upatikanaji wa vifaa kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Pia halmashauri isifanye maamuzi yake nje ya Uenyekiti wa Mbunge ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ni Mikopo kwa Makundi Maalum. Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge kuhusu kiasi kidogo cha fedha za mikopo kinachotolewa kwa Makundi Maalum ya Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu kutokidhi matakwa ya kuyainua makundi hayo kwa kufanya shughuli za uzalishaji au biashara. Aidha, kumekuwa na changamoto kwenye baadhi ya halmashauri kutoa fedha hizo kwa Watumishi wa Halmashauri au wakati mwingine vikundi hewa badala ya walengwa na kusababisha fedha za mikopo hiyo kutorejeshwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia malalamiko hayo na maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu matumizi mabaya ya fedha hizo, nazielekeza sasa halmashauri kote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo hiyo zitakazotokana na makusanyo ya kuanzia mwezi Aprili hadi Juni mwaka 2023, wakati Serikali inajipanga kwa mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo utakaoelekezwa kabla ya mwezi Juni mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni Serikali kuwa tayari kuchukua hatua pale majanga yanapotokea kama ilivyoainishwa kwenye sheria kuendana na uhalisia.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Kujiandaa Kukabiliana na Maafa kwa mwaka 2022 ambao umezingatia viashiria vya maafa nchini, mifumo ya kitaasisi, mahitaji na maendeleo katika shughuli za kujiandaa na kukabiliana na majanga kitaifa. Mpango huu umewezesha utekelezaji wa shughuli za kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa kuzingatia taasisi yenye jukumu la msingi na ushirikiano wa sekta na taasisi zisizokuwa za kiserikali kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Tawala za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinahimizwa kushughulikia maafa katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kujumuisha katika Mipango ya Bajeti zao hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa kukabiliana na maafa kwa mujibu wa sheria husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni Serikali iweke mkakati maalumu wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye program ya Taifa ya Kukuza Ujuzi chini ya program nyingine ili kuhakikisha kuwa fursa kwa wenye ulemavu zinaimarishwa.
Mheshimiwa Spika, jibu hapa ni kwamba Serikali imeandaa mwongozo wa utekelezaji, ujumuishwaji na uimarishwaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu wa mwaka 2022 kwa lengo la kuhakikisha ujumuishwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu kwenye programu, miradi na mipango mbali mbali ya maendeleo katika sekta zote za uchumi na kijamii.
Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa programu ya Taifa ya kukuza ujuzi, watu wenye ulemavu wamekuwa wakijumuishwa kwa kuhakikisha kuwa matangazo yote ya fursa za mafunzo yanatafsiriwa kwa lugha rafiki na kupelekwa kwenye vyama vya Watu Wenye Ulemavu na kwa Maafisa wa Ustawi wa Jamii na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii waliopo katika Halmashauri na Vyombo vya Habari. Mathalani katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya vijana walemavu 1,171 wamenufaika na programu za kukuza ujuzi zinazoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na masuala ya ujuzi, Serikali inahakikisha watu wenye ulemavu wanapewa upendeleo maalum katika masuala ya ajira pamoja na kuimarisha miundombinu mbalimbali na kuifanya kuwa rafiki kwa mahitaji yao. Kwa mfano, katika kutekeleza mpango wa maboresho ya elimu ya msingi kwa mwaka 2022/2023 Serikali inajenga vyumba vya madarasa 41 kwa watu wenye mahitaji maalum.
Mheshimiwa Spika, vilevile chini ya Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 Serikali yetu imetumia Shilingi Bilioni 3.46 kwa ajili ya ukarabati wa Vyuo Vinne vya Ufundi Stadi na marekebisho ya Rwanzari kule Mkoani Tabora, Sabasaba Mkoani Singida, Mtapika Mkoani Mtwara na Yombo Mkoani Dar es Salaam. Ukarabati huo umewezesha vyuo hivyo kuongeza uwezo wa udahili wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka 407 kabla ya ukarabati na kufikia 800. Aidha fani zilizokuwa zinatolewa awali zimeongezeka kutoka Tatu hadi 10.
Mheshimiwa Spika kama utakavyoona Serikali imeendela kutoa fursa za upendeleo maalum kwa watu wenye mahitaji maalum, katika kuingia kwenye programu ya Taifa ya kukuza ujuzi, chini ya programu nyingine ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni juu ya hoja kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), itakumbukwa kuwa Tarehe 29 Machi, 2023 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliwasilisha kwa Mheshimiwa Rais, Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2022. Uwasilishwaji huo ni takwa la Kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 143 kipendele cha (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sura Na. 418.
Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliainisha baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa na viashiria vya usimamizi usioridhisha wa mali na fedha za umma. Maeneo hayo ni pamoja na matumizi mabaya ya mikopo ya Halmashauri, kasoro za utekelezaji wa miradi na baadhi ya mifumo kutosomana.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa hoja ya Waziri Mkuu ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali ya mwaka 2022/2023 na mwelekeo wa kazi zake kwa mwaka 2023/2024. Waheshimiwa Wabunge wenzangu sambamba na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya hawakuweza kuficha hisia zao kuhusu mwenendo usioridhisha wa uwajibikaji kwa baadhi ya Viongozi na Watendaji ndani ya Serikali, kama ilivyoonesha katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 06 Aprili 2023, taarifa hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliwasilishwa hapa Bugeni ikiwa ni utekelezaji wa takwa la Kikatiba linaloielekeza Serikali kuwasilisha Bungeni taarifa hiyo ndani ya siku Saba za kazi kuanzia siku ya Kikao cha Kwanza cha Bunge tangu kuwasilishwa kwake kwa Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, binafsi ninatambua hisia za Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla, kuhusu ubadhilifu wa mali na fedha za umma uliobainishwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Aidha, sote tulishuhudia hisia na namna Mheshimiwa Rais alivyoonesha kutoridhishwa na ubadhilifu uliobainishwa katika taarifa hiyo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo na wakati huu ambapo Bunge lako tukufu linaendelea na taratibu zake za kufanyia kazi hoja zilizowasilishwa katika taarifa hiyo, nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa Bungeni, tayari Serikali kwa upande wake imeanza kuifanyia kazi mara moja.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni kuhakikisha kuwa Maafisa Masuuli wote wanaandaa majibu ya hoja kama inavyoelekezwa katika Sheria na Kanuni za Ukaguzi wa Umma na kusisitizwa na Mheshimiwa Rais. Aidha, nitumie fursa hii kuiwakumbusha Maafisa Masuuli wote kuzingatia maelekezo ya Mhehsimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba wanapitia kwa kina taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kujibu na kuchukua hatua za haraka juu ya hoja zote zilizoibuliwa kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, vilevile naahidi kuwa pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali, taarifa ya kina katika maeneo yaliyobainishwa kuwa na hoja katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali itawasilishwa katika Bunge lako tukufu kwa kuzingatia Kanuni husika. Aidha, nilihakikishie Bunge na wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitamfumbia macho yeyote atakaebainika katika ripoti hiyo kuwa amehusika katika matumizi mabaya ya fedha na mali za umma na kuwa hatua kali zitaendelea kuchukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyojadiliwa mbele yetu ni changamoto ya mmomonyoko wa maadili na vitendo vinavyokwenda kinyume ya mila, desturi na tamaduni za Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, wakati tunaendelea na mjadala wa hoja hii ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha kukerwa na uwepo wa matukio mbalimbali yanayokinzana na tamaduni, mila na desturi zetu. Matukio na matendo haya yamekuwa yakihatarisha uimara wa ustawi wa familia zetu na msatakabali wa Taifa kwa ujumla. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa nchi yetu inazo sheria kali tu na sheria zetu zote zinasimamia kila eneo, pia zinakataza bayana vitendo hivyo na zimeweka adhabu mbalimbali kwa makosa ya namna hiyo na yale ya udhalilishaji kwa watoto ikiwemo ulawiti. Pia sheria zinazokataza kuweka kwenye mtandao maudhui yanayochochea mahusiano ya jinsi hiyo au maonesho ya sanaa yanayochochea vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili yetu.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura Namba 16 ya Sheria ya Tanzania, ambayo inatamka bayana kwamba vitendo vya mapenzi ya jinsia moja au kinyume na maumbile iwe kwa faragha au kwa makubaliano ni kosa la jinai. Sheria hiyo pia inakataza udhalilishaji wa watoto kwenye matendo yanayofanana na hayo, pamoja na kuweka adhabu kwa kosa la kujaribu kufanya vitendo vilivyokatazwa chini ya sheria husika.
Mheshimiwa Spika, Mbili; Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni chini ya Tangazo la Serikali Na. 538 la mwaka 2020, linakataza kuweka mtandaoni maudhui yenye kuonesha mahusiano ya jinsia moja sambamba na adhabu zake. Tatu; ipo Sheria ya Makosa ya Kimtandao Sura Namba 22, inazuia kutangaza au kusababisha machapisho ya ngono au matusi kupitia mfumo wa kompyuta au mfumo mwingine wowote wa kiteknolojia na Kanuni nyingnine ni Kanuni ya Baraza la Sanaa la Taifa za mwaka 2018 zinaweka masharti kwamba hakuna kazi ya sanaa itakayopelekwa sokoni kwa walaji kabla ya kupewa kibali cha kuthibitisha kuwa maudhui yamezingatia maadili.
Mheshimiwa Spika, aidha Baraza katika kuhakiki maadili na maudhui linajiridhisha kuwa kazi ya sanaa haishawishi wala kuhamasiha vitendo vya ngono, ushoga, usagaji au matumizi ya dawa za kulevya wakati wote sanaa hiyo inapowasilishwa kwa jamii.
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imepokea hoja na michango mbalimbali iliyowasilishwa na itaielekeza Tume ya Marekebisho ya Sheria kuzipitia sheria hizo, kuzifanyia utafiti wa kina na utafiti wa kitaalam ili kubaini mapungufu yaliyojitokeza katika utekelezaji na kufanya maboresho yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, aidha nitoe wito kwa Taasisi zote zilizo na wajibu wa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu tulizojiwekea kama vile Jeshi la Polisi, BASATA, TCRA, kutosita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakaebainika anavunja sheria hii inayogusa maeneo haya ya kukiuka mila, desturi na utamaduni wetu na kukiuka misingi ya taratibu zetu tulizojiwekea.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hoja na hisia za Wabunge kuhusu matendo haya, watoto wetu pia wamekuwa ni miongoni mwa wahanga wakuu, kutokana na hali hiyo Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili.
Mheshimiwa Spika, mathalani, kutokana na matukio ya unyanyasaji wa watoto yaliyoripotiwa hivi karibuni Serikali imechukua hatua Madhubuti, zikiwemio kutoa waraka kwa wamiliki wote wa shule nchini unaoelekeza kuwa kuanzia tarehe 1 Machi, 2023, kuanza utaratibu wa uwepo wa wahudumu wa jinsia ya kike na wa jinsia ya kiume kwenye magari yanayobeba wanafunzi kuelekea na kutoka majumbani mwao.
Mheshimiwa Spika, Mbili; kusimamia ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mabasi ya shule ili kuhakikisha kwamba utekelezaji wa agizo hilo na uwepo wa wahudumu wa jinsia ya kike na kiume kwenye magari hayo unazingatiwa. Tatu; kuthibiti nyimbo na video zisizo na maadali kuchezwa au kuoneshwa kwenye magari ya wanafunzi yanapofanya safari zake. (Makofi)
Mhehsimiwa Spika, pamoja na hatua hizo tumeendelea kuimarisha mifumo ya ushirikishwaji jamii ili kurahisishwa upatikanaji wa taarifa pindi jamii inapobaini uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na ukiukwaji wa mila, desturi na tamaduni zetu na kuchukua hatua mbalimbali za kisheria kwa wale wanaobainika kuvunja sheria hizo za nchi.
Mheshimiwa Spika, mtakubaliana nami kuwa suala la malezi ya watoto na utunzaji wa mila, desturi na tamaduni zetu ni jukumu la kila mmoja hivyo sote tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na kizazi salama chenye kuzingatia sheria, mila, desturi na tamaduni. Tamaduni hizi ni zile ambazo tunaziheshimu ambazo pia zinaleta utu na kuimarisha mshikamano wa Kitaifa.
Mheshimiwa Spika, nami nitumie fursa hii kuwaasa Watanzania wenzangu kuendelea kuienzi misingi yetu ya mila, tamaduni na desturi zetu nzuri na kuendelea kuzingatia sheria za nchi. Aidha, nitumie Bunge lako tukufu kuwasihi wafuatao: -
Wazazi na walezi; imarisheni uhusiano na urafiki wa watoto wetu ili kupata taarifa za viashiria wa uwepo wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Jengeni utamaduni wa kutenga muda wa kuwasilikiza watoto ili kujua kinachoendelea katika maisha yao ya nyumbani, mtaani na shuleni vilevile na kuchukua hatua stahiki ikiwemo za kisheria pale inapotokea kuna ukiukwaji wa misingi yetu ya maadili ya malezi ya watoto wetu.
Viongozi wa dini; endeleeni kuwakumbusha waumuni wetu kuzingatia maadili na kushiriki kikamilifu katika kuwalea watoto wetu kiroho, kuwahimiza kuwa waadilifu na kuepuka vitendo visivyokubalika katika jamii. Tumeshuhudia karipio lenu kupitia mikutano yenu, endeleeni kukaripia jamii yetu ili kila mmoja azingatie maadili yetu ya Kitaifa. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge wenzangu; endeleeni kuiunga mkono Serikali katika suala la ulinzi wa mtoto wa Kitanzania na usimamizi wa maadili yetu, sote kwa nafasi zetu tuendelee kuhimiza jamii na kuwa mfano katika kutekeleza sheria tulizozitunga wenyewe, kutunza mila, desturi na tamaduni zetu.
Wito kwa Wizara za kisekta; kusimamia kikamilifu sheria tuliojiwekea Kanuni tulizoziweka na miongozo tulionayo pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale watakaobainika kufanya vitendo kinyume cha sheria na maadili ya Taifa letu.
Asasi za Kiraia; kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa vibali vyao vya usajili kwa Taasisi zitakazobainika kwenda kinyume na malengo ya usajili ikiwemo kuhamasisha mmomonyoko wa maadili na vitendo vinavyokinzana na mila za nchi hii, utamaduni wa nchi hii na desturi zetu tutachukua hatua kali za kisheria dhidi ya Taasisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiwa naelekea kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, naomba uniruhusu nitumie jukwaa hili kuzungumzia kwa uchache kabisa kuhusu masuala mawili kama ifuatavyo: -
Suala la kwanza ni pongezi kwa timu yetu ya mpira wa miguu ya Fountain Gate kwa kutwaa Ubingwa Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake wa Shule za Sekondari Barani Afrika. Nikiwa mdau wa michezo nanyi mkiwa wadau wa michezo mmefurahi leo kwamba asubuhi tuliwapokea hapa Bungeni mabingwa wa soka la wanawake wa Shule za Sekondari Barani Afrika kwa mwaka 2023. Shule ya Sekondari ya Fountain Gate iliyoko Jijini Dodoma, ambao wameambatana na wanafunzi wenzao. Mafanikio yao yanaifanya Fountain Gate kuwa mfano wa kuigwa wa shule na vituo mbalimbali katika kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo kwa watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii hatuwezi kuzungumzia mafanikio ya soka la wanawake nchini bila kuitaja Fountain Gate. Kwa mfano, katika kikosi cha Timu cha Wanawake wa Serengeti Girls kilichoshiriki katika fainali za Kombe la Dunia za Soka la Wanawake nchini India mwaka 2022 na kuingia hatua ya robo fainali, Timu ya Fountain Gate ilikuwa na wachezaji Saba katika kikosi hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tumekuwa nao hapa Bungeni, mashujaa wetu, mabinti zetu wa Fountain Gate, baada ya kupata mafanikio makubwa na kutwaa ubingwa wa michuano ya CAF kwa shule za Sekondari Barani Afrika na kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kutwaa kombe lililoandaliwa na CAF. Hongereni sana Fountain Gate. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuipongeza Wizara ya Utamaduni na Michezo kwa kusimamia vema utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika michezo kwa maslahi ya Taifa. Pia napenda kuipongeza Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa kusimamia kikamilifu uendeshaji wa shughuli za michezo shuleni, kutoka shule za msingi na mashindano ya UMITASHUMTA na shule za sekondari kwa mashindano ya UMISETA. Vilevile napongeza Baraza la Michezo Tanzania kwa utendaji mahiri ambao umekuwa chachu ya mafanikio kwenye tasnia ya michezo ikiwemo mpira wa miguu wa wanawake.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji uliofanywa na mmiliki wa Fountain Gate wa Jijini Dodoma ni miongoni mwa vielelezo vya mafanikio katika utekelezaji wa sera ya maendeleo ya michezo nchini. Hivyo basi, nitoe wito kwa wadau wa michezo kuiunga mkono Serikali katika kuimarisha miundombinu ya michezo, kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo mbalimbali. Aidha, niwapongeze tena mabinti zetu wachezaji mahiri, mashujaa wanafunzi wa Fountain Gate kwa historia waliyoiweka katika soka la Afrika na kulitangaza Taifa letu duniani. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukio la pili ni baadhi ya kumbukizi muhimu katika kipindi cha Aprili kwa Taifa letu. Itakumbukwa kuwa tarehe 7 Aprili mwaka huu, tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 51 tangu kitokee kifo cha Muasisi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mzee wetu Hayati Sheikh Abeid Aman Karume. Aidha leo tunaadhimisha mwaka wa 110 tangu kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jana tarehe 12 Aprili mwaka huu wa 2023 kumeadhimishwa kumbukizi ya miaka 39 tangu kitokee kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine, Waziri Mkuu wa Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana na mimi kwamba kumbukizi za viongozi hao ni urithi muhimu kwa Taifa kutokana na uzalendo, uwajibikaji na utumishi wao uliotukuka katika Taifa hili, kwa mantiki hiyo, tukiwa Taifa linalothamini na kuenzi utendaji wa Viongozi wetu tunao wajibu siyo tu kuwakumbuka lakini pia kurithisha urithi huo kwa vijana wetu wa sasa na vizazi vijavyo. Kwa kufanya hivyo, tutasaidia vijana wetu na vizazi vijavyo kuyaiga, kuyaenzi na kuyaishi matendo bora yenye tija waliotuachia viongozi hawa na hivyo kuimarisha umoja na mshikamano wa Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa napoelekea kuhitimisha hoja yangu, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuendelea kuiunga mkono Serikali yetu kupitia Bunge hili Tukufu ikiwa ni pamoja na kutoa mapendekezo ya kujenga umoja, kuimarisha mshikamano wa Kitaifa kusaidia Serikali kuwahudumia ipasavyo wananchi wake na kuikosoa pale inapobidi. Aidha, katika maeneo yetu ya uwakilishi tuimarishe ushirikiano na wananchi katika kuhakikisha kwamba miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yetu inaleta tija iliyokusudiwa na kuhakikisha thamani ya fedha ya umma ambayo imetumika kwenye miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Watanzania wenzangu niwaombe kuendelea kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumjaalia afya njema, maono, hekima na busara katika kuliongoza Taifa hili na kufanikisha azma yake ya kuliletea maenedeleo.
Mheshimiwa Spika, kadhalika niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba Serikali kwa upande wetu itaendelea kutoa ushirikiano stahiki kwa wananchi na wadau wote muhimu, katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzingatia mustakabali na maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
WAZIRI MKUU: Ahsante, shukurani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nataka nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima wa afya hata leo tumeweza kukutana kwenye Kikao hiki cha Sita cha Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge la Kumi la Mbili kwa ajili ya kuhitimisha mjadala kuhusu hoja ya bajeti ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Mbunge na Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge ya Dunia kwa namna ambavyo analiongoza Bunge letu kwa umahiri mkubwa. Nashukuru na kukupongeza sana wewe binafsi pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge kwa Uongozi wenu imara na thabiti. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana nami kuwa wameweza kuongoza vyema kipindi chote cha mjadala kuhusu hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru na kuwapongeza sana Wenyeviti na Wajumbe wote wa Kamati za Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa michango yao muhimu ambayo wameitoa mbele ya Bunge lako Tukufu. Nikiri kwamba maoni na ushauri wao wakati wote umekuwa ukileta tija kubwa kwenye hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa hoja na michango yenu yenye tija katika kipindi chote cha mjadala wa hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Nataka nitumie nafasi hii kuwahakikishia kwamba Serikali wakati wote itazingatia maoni yao na ushauri walioutoa katika mipango na utekelezaji wa majukumu yake kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri wa Sekta na Naibu Mawaziri waliochangia hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kuwashukuru Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Taasisi na Wakala wa Serikali kwa ushirikiano mkubwa walioutoa na kufanikisha hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge. Nawapongeza sana Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika hatua zote za maandalizi ya hotuba ya bajeti hadi tunapoelekea kuhitimisha mjadala wa hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Vilevile nawashukuru kwa ushirikiano walionipa ambao wakati wote ambao umeniwezesha kutimiza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, salamu za pole; wakati tukiendelea na Mkutano huu wa Kumi na Tano wa Bunge lako Tukufu, mnamo tarehe 9 Aprili, 2024 tuliondokewa na mpendwa wetu Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana nami kuwa Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil alikuwa ana uwezo mkubwa na ushawishi wa kipekee ndani ya Bunge hili na mchango wake utakumbukwa daima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kutoa salamu za pole kwa wana CCM wote, familia, ndugu na jamaa wa marehemu, wananchi wa Jimbo la Kwahani na Watanzania wote kwa ujumla. Niwaombe Watanzania wote tumwombee marehemu kwa Mwenyezi Mungu apumzike mahali pema peponi.
WABUNGE FULANI: Amina.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni wapo Watanzania wenzetu waliopatwa na majanga mbalimbali yakiwemo ajali za barabarani, mafuriko na mengine yaliyosababisha vifo na uharibu wa mali. Kwa masikitiko makubwa naungana tena na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa salamu za pole kwa waathirika wote wa majanga hayo. Nitumie nafasi hii kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliowapoteza wapendwa wao kutokana na majanga hayo. Tumwombe Mwenyezi Mungu awajalie uponyaji wa haraka majeruhi wote na kuwapa pumziko la amani marehemu wote.
WABUNGE FULANI: Amina.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mjadala huu ukiendeshwa, Waheshimiwa Wabunge 129 wamechangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kati yao Waheshimiwa Wabunge 119 walichangia kwa kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge 10 walichangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutumia nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia Hoja ya Waziri Mkuu. Ningependa kuwataja majina yao, lakini kutokana na ufinyu na muda naomba uridhie nisiwataje na badala yake majina yao yaingizwe kwenye Hansard.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wametoa ufafanuzi wa hoja nyingi zilizowawasilishwa na Waheshimiwa Wabunge wakati tukiendelea na mjadala wa Hoja ya Waziri Mkuu. Sikusudii kuzirudia, lakini nataka nishukuru kwa michango yao tena na kwamba tutaendelea kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa Waheshimiwa Mawaziri wataendelea kufafanua zaidi baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye mjadala huu wakati wakiwasilisha hoja za bajeti za sekta zao. Kadhalika kama ilivyo ada Serikali itatoa ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zilizosalia kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Waheshimiwa Wabunge wanavyofahamu kwamba tayari tumetimiza miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni jambo la kujivunia kuwa katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya uongozi wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Taifa letu. Sisi sote ni mashahidi kwamba amekuwa kinara katika Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020. Mheshimiwa Rais wakati wote amekuwa akionyesha busara, uhodari mkubwa, uzalendo, usikivu, uwajibikaji na kuwa mfano wa kuigwa ndani na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutumia nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu kumshukuru kwa uzalendo wake na namna anavyojitoa kulitumikia Taifa letu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Miradi hiyo inahusisha Sekta za Maji, Elimu, Afya na Miundombinu ambayo niliieleza wakati nilipokuwa nawasilisha hoja yangu. Naomba sasa nieleze kwa uchache mafanikio mengine yaliyopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni kuleta maridhiano ya kisiasa, amani na utulivu wa kidemokrasia hapa nchini. Niendelee kutokuwa na mashaka na Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana nami kuwa Mheshimiwa Rais ni kinara katika kuimarisha demokrasia vilevile haki za binadamu na utawala bora. Katika kipindi hiki cha uongozi wake tumeshuhudia utekelezaji wa falsafa yake ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuilding). Kwa lugha ya Kiswahili ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Mabadiliko ambayo kwa hakika yamekuwa chachu ya kuimarisha siasa za ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na utashi wake, mwelekeo wa mitazamo na uendeshaji wa masuala ya kisiasa umebadilika na kuchagiza siasa za kistaarabu. Sote ni mashuhuda kuwa nchi yetu inaendelea kuwa na mshikamano, amani na umoja wa kitaifa. Hii inatokana na msisitizo wake kuhusu utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, utawala bora na demokrasia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza masuala ya demokrasia kwa vitendo, tumeshuhudia maboresho mbalimbali ya upande wa mifumo, sheria na uendeshaji wa shughuli za kisiasa hapa nchini. Licha ya hayo tumeshuhudia pia uwepo wa fursa zaidi za mijadala na maridhiano miongoni mwa makundi ya wadau wa demokrasia na masuala ya siasa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni maboresho ya mfumo wa utoaji haki na Taasisi za Hakijinai katika kuhakikisha mfumo wa utoaji haki unaboreshwa. Mnamo tarehe 31 Januari, 2023, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliunda Tume Maalum aliyoipa jukumu la kushauri namna njema ya kuboresha mfumo wa utendaji kazi katika taasisi zinazohusika na hakijinai.
Mheshimiwa Naibu Spika, tume hiyo ilipokea maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine wa hakijinai na kutoa mapendekezo ya maboresho yanayohitajika kufanyika. Tangu tume ilipowasilisha mapendekezo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za maboresho ya mfumo wa utoaji wa hakijinai, ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa Taasisi za Hakijinai. Licha ya hayo Serikali inaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa kwa lengo la kuhakikisha kuwa, wananchi wanapata haki zao kwa wakati ili waweze kuendelea kufanya shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa zima kwa ujumla. Hii ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kukidhi kiu na matarajio ya wananchi katika utoaji wa hakijinai kuanzia hatua ya uchunguzi, ukamataji watuhumiwa hadi utoaji wa hukumu yenyewe pale inapofanyika haki mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ni matumizi ya TEHAMA na Lugha ya Kiswahili mahakamani. Katika hatua nyingine Serikali ya Awamu ya Sita, imeendelea kufanya jitihada kubwa ya kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kutokana na mapinduzi ya nne ya viwanda hapa duniani. Jitihada hizo zimeanza kuleta mafanikio katika utendaji wa Serikali kwa kuunganisha Serikali yote (Wizara, Idara, Wakala na Taasisi zake) ili ziweze kusomana kwa kimfumo. Tumeanza kupata mafanikio tukianza na Mahakama ya Tanzania, ambapo mifumo mbalimbali ya TEHAMA imejengwa ili kurahisisha na kuhakikisha utoaji wa haki kwa wananchi unaimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo hiyo ni pamoja na mfumo wa usajili, uendeshaji na usimamizi wa mashauri kwa ajili ya kurahisisha, kuharakisha na kuokoa muda wa mwenendo wa shauri mahakamani. Mfumo mwingine ni wa unukuzi na tafsiri ya mienendo ya mashauri mahakamani kwa lengo la kuwa na suluhu ya kudumu, ili kuwawezesha Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kuondokana na adha ya kuandika kwa mkono mwenendo wa mashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatua kubwa sana katika mfumo huu unaorekodi sauti na kupeleka kwenye maandishi. Vilevile unaweza kutafsiri Lugha ya Kiswahili au Kiingereza kulingana na uhitaji na kwa upande mwingine Kanuni za Mahakama zimeanza kutafsiriwa sambamba na uandaaji wa mihtasari ya hukumu katika Lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni mafanikio kwenye Sekta ya Uzalishaji ambako kuna kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda. Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuinua sekta ya uzalishaji. Kama tunavyofahamu uzalishaji kupitia Sekta ya Kilimo umeendelea kuongezeka na kuiwezesha sekta hii kuchangia 26% ya Pato la Taifa kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada zinazofanywa na Serikali ni katika kuhakikisha kuwa, Sekta ya Kilimo inaendelea kutoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa ajira, malighafi za viwandani, kuleta fedha za kigeni kutokana na mauzo ya nchi za nje, pamoja na kulihakikishia Taifa letu usalama wa chakula. Jitihada mbalimbali zinazofanywa zimewezesha nchi yetu kuwa na utoshelevu wa chakula kwa 124%.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina shaka Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kuwa, Mheshimiwa Rais amefanya jitihada kubwa kuimarisha Sekta ya Uvuvi. Utekelezaji wa ujenzi wa Mradi mkubwa wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko unaogharimu zaidi ya bilioni 289.5 ni kielelezo tosha cha dhamira yake njema ambayo pia Mheshimiwa Rais ameionesha hadharani. Tayari ameshatoa ridhaa ya matumizi ya shilingi bilioni 106.2 za kuendeleza ujenzi wa bandari hiyo, ambayo itachochea ukuaji wa Sekta ya Uvuvi na kuongeza pato la Wananchi kama ilivyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Sekta ya Mifugo, vilevile tumeshuhudia ikiendelea kuimarika na kuwezesha kutoa ajira kwa wananchi milioni 4.5. Aidha, kutokana na jitihada zilizopo mchango wa sekta katika pato la Taifa umefikia 7.1% kwa mwaka. Uwekezaji kwenye viwanda umeongezeka, ili kuzalisha bidhaa kwa mahitaji ya ndani na kupata masoko ya bidhaa nje ili kuongeza pia pato la kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo Mheshimiwa Rais amelieleza ni mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Amelifafanua vizuri zaidi, lakini nataka nieleze tu kwamba, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kupambana na tatizo la dawa za kulevya hapa nchini. Hii inatokana na ukweli kwamba, kundi la vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa linalotarajiwa kuwakilisha maendeleo, ndiyo linaathirika zaidi na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini. Licha ya tatizo la dawa za kulevya kuendelea kuwepo hapa nchini, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika kipindi kifupi, imefanya kazi kubwa sana. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua anazozichukua za kuiwezesha mamlaka hii kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka inafanya kazi kubwa na nzuri, katika hili natoa rai kwa Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Mashirika ya Dini, Taasisi zisizokuwa za Serikali na Washirika wa Maendeleo na wananchi wote kwa ujumla, kutoa ushirikiano kwa mamlaka ili iweze kutimiza majukumu yake. Vilevile namwomba kila mmoja kwa nafasi yake, ashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa ya kulevya. Taasisi inaendelea kufanya kazi nzuri ya kudhibiti uzalishaji, usafirishaji, uuzaji na utumiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana pia Waheshimiwa Wabunge kwa michango waliyoitoa kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, umoja ni ushindi. Hivyo basi, Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote tushirikiane katika mapambano ya dawa za kulevya, kwa pamoja tutashinda, mapambano bado yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nieleze kidogo juu ya utekelezaji wa sera na fursa za kujikwamua kiuchumi. Serikali imeendelea kutekeleza sera mbalimbali za uwezeshaji wa makundi maalum ya wanawake, vijana na wenye ulemavu. Lengo likiwa ni kuhakikisha makundi haya yanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hapa nchini. Utekelezaji wa sera hizo unafanywa kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi, ambayo imeendelea kunufaisha makundi yote, wakiwemo wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, fedha kiasi cha shilingi bilioni 743.7 zimetolewa kwa wanufaika zaidi ya milioni sita kupitia Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Katika utekelezaji wa sera ya ushirikishwaji Watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini, wanawake na vijana wameendelea kunufaika kupitia miradi ya kimkakati na uwekezaji. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya Watanzania 162,968 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuratibu masuala ya uzalishaji wa fursa za ajira nchini kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, fursa za ajira 2,489,136 zimezalishwa sawa na wastani wa ajira mpya 829,712 kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuwezesha vijana ili waweze kujiajiri kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuchangia pato la Taifa. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, kiasi cha shilingi bilioni 3.19 kimeshatolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambazo zilitumika kutoa mikopo kwa ajili ya kuwezesha miradi 148 katika Sekta za Kilimo, Viwanda na Biashara katika halmashauri 62.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, kurasimisha na kuendeleza biashara kwa vijana katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI hivi karibuni itatoa taarifa ya mfumo utakaotumika kutoa mikopo ya 10% kutoka katika halmashauri zetu nchini ili wajasiriamali waweze kuendesha shughuli zao za kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utunzaji wa mazingira, sote tunatambua kuwa uhifadhi wa mazingira una umuhimu mkubwa katika maisha yetu ya kila siku, kwa kuwa unatuwezesha kupata mahitaji muhimu ikiwemo maji, chakula, madawa, malighafi za viwandani, pamoja na nishati ya umeme itokanayo na maji. Ni ukweli usiopingika kuwa upatikanaji wa mahitaji haya, unaharakisha maendeleo yetu ya kiuchumi na kijamii, hivyo, tuna kila sababu ya kutunza mazingira ili nayo yaweze kututunza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu huo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa faida yetu na vizazi vijavyo. Vilevile, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mara kwa mara amekuwa akitukumbusha kuhusu utunzaji wa mazingira yetu. Nitumie nafasi hii kuungana na viongozi wetu, kuzungumza kwa uchache kuhusu uhifadhi wa mazingira hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao kimsingi unasababishwa na ukataji wa miti hovyo kwa matumizi ya nishati. Kilimo kisicho endelevu kinachofanyika kwa kukata miti na kuchoma mashamba ikiwa ni njia ya kurahisisha maandalizi ya shamba. Sababu nyingine ni ufugaji holela usiozingatia uwezo wa eneo la malisho, ambao umesababisha mifugo kuharibu ardhi na maeneo mengine yaliyohifadhiwa ikiwemo vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kuwa athari za uharibifu wa mazingira ni mbaya kwa kuwa, huathiri masuala ya kijamiii na kiuchumi mathalani mara kadhaa tumeshuhudia vifo vya mifugo kutokana na ukame na uhaba wa maji, vilivyotokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira. Vilevile mvua nyingi kupita kiasi zimeendelea kusababisha athari kubwa nchini, ikiwemo mafuriko, vifo, na uharibifu wa miundombinu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, nitumie fursa hii kusisitiza masuala yafuatayo:-
(i) Viongozi wote kuanzia ngazi za vijiji hadi mikoa, wasimamie kikamilifu utunzaji wa mazingira na suala hili liwe ajenda ya kudumu katika vikao vyote katika ngazi hizo; (Makofi)
(ii) Viongozi wa Mikoa na Wilaya wasimamie utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu athari za kuchoma misitu hovyo, pia kufuga bila kuangalia uwezo wa maeneo ya kulishia, kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kuondokana na tabia ya kukata miti hovyo;
(iii) Halmashauri zote nchini, zisimamie kikamilifu sheria ndogo za uhifadhi wa mazingira na kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya uharibifu wa mazingira yetu;
(iv) Taasisi za Uhifadhi wa Misitu (TFS) na halmashauri ziandae vitalu vya miti inayoendana na ikolojia ya maeneo yao, kuigawa kwa wananchi na kuhakikisha inapandwa na kukua. Hatua hii iendane sambamba na kusimamia upandaji wa miti kwa kila kaya. Vilevile TANROADS na TARURA wahakikishe wakandarasi wanapanda miti pembezoni mwa barabara katika kila mradi wa ujenzi wa Barabara. Kwa kufanya hivyo itasaidia upandaji na utunzaji wa mazingira; (Makofi)
(v) Wananchi tuendelee kushirikiana na Serikali katika uhifadhi wa mazingira ili kuepusha madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia mabadiliko ya hali ya hewa. Kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani inaendelea kuongezeka kila mwaka na athari zake zimekuwa kubwa. Tathmini ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani, limeonesha kuwa wastani wa ongezeko la joto kwa 2023 ulifikia nyuzi joto 1.4 kwa kipimo cha selsiasi (Celsius) na kuvunja rekodi ya kuwa mwaka wenye joto kubwa zaidi katika historia ya dunia. Kwa upande wa Tanzania, wastani wa ongezeko la joto kwa mwaka 2023 ulifikia nyuzi joto 1.0 kwa kipimo cha selsiasi. Pia ulivunja rekodi kwa kuwa mwaka wenye joto kubwa zaidi katika historia ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la joto limesababisha uwepo wa El-Nino ambayo imeambatana na mvua kubwa na mafuriko hapa nchini. Oktoba hadi Desemba, 2023 kulikuwa na ongezeko kubwa la mvua, ambapo jumla ya milimita 534.5 zilipimwa ikilinganishwa na milimita 227.2 kwa mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la 135.5%. Vilevile ongezeko hilo la mvua limeshuhudiwa katika kipindi cha Januari hadi Aprili, 2024 na kwa mujibu wa Taasisi ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mvua zitaendelea kunyesha hadi mwezi Mei, 2024 kwenye Mikoa ya Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, Ukanda wa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania na Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwa nchi mbalimbali duniani, nchi yetu imeendelea kupata mvua nyingi zaidi ya wastani kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamesababisha maafa mbalimbali. Maafa hayo ni pamoja na vifo, uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli. Kama mnavyofahamu maeneo mengi yameathirika na mvua. Mikoa ambayo imeathirika kwa sasa ni Mikoa ya Arusha, Lindi, Manyara, Kigoma, Morogoro, Pwani na Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Maafa Kitaifa kwa kushirikiana na Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya, zimeendelea kuchukua hatua mbalimbali kurejesha hali katika maeneo yaliyoathirika ikiwemo Wilaya ya Rufiji, eneo la Muhoro; Wilaya ya Kibiti, eneo la Delta; Newala, Lindi Mjini, Liwale, Arusha, eneo la Kisongo; Mkoani Morogoro Malinyi, Wilaya ya Kilombero; kule Mrimba maeneo ya Masagati na Utengule na kule Mbeya kulikotokea maporomoko ya udongo kutoka milimani eneo la Kawetere.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizo ni pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika, kurejesha miundombinu iliyoathirika, kutoa elimu kwa jamiii kuhusu kujikinga, kuchukua tahadhari na kuendelea kufanya tathmini ya kina ya athari na vyanzo vya maafa hayo. Kamati za Maafa za Kitaifa kwa kushirikiana na Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya, zinaendelea kufanya tathmini kwenye maeneo yote yaliyopata athari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua kadhaa tena za haraka na za dharura ikiwemo uokoaji, kutoa chakula, maji, makazi ya muda, dawa, mbegu na huduma za unasihi, katika maeneo yaliyopata athari kubwa za mvua ambazo zinaendelea hivi sasa. Tunatoa pole kwa ndugu zetu walioathirika na mvua hizo na naomba wananchi wote kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini. Niwasihi sana wananchi, waendelee kuwa na subira pale wanapoona maji mengi yanapita hususani barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa waendesha vyombo vya moto vya usafiri na wavuka kwa miguu, kuchukua tahadhari ya kutovuka mahali popote wanapoona maji yanakatiza barabara, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kama ambavyo imetokea eneo la kisongo kule Mkoani Arusha, kwa gari la wanafunzi kutumbukia kwenye shimo, kwa dereva kupinga, kukaidi na kupita kwenye eneo ambalo maji yanavuka bila kujiridhisha kama eneo hilo lina maporomoko au la.
Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADS, TARURA na Shirika la Reli waendelee kuchukua hatua za haraka wakati uharibifu wa miundombinu ya barabara na reli unapoendelea kujitokeza. Hatua hizo ziendelee sambamba na kutoa taarifa kwa watumiaji wa miundombinu hiyo, kuweka alama za tahadhari na kuweka kambi maalum za matengenezo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizikumbushe mamlaka za upangaji kuzingatia mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kusimamia upangaji wa makazi kwa kuzingatia sheria ya mipango miji. Aidha, Wizara ya Maji kwa kushirikiana na sekta mtambuka, waendelee na mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ikiwemo mabwawa na kuyahifadhi kwa ajili ya huduma za jamii na uzalishaji ikiwemo kilimo, pia majosho ya kunyweshea mifugo ili kupunguza athari za uharibifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe watendaji wote wa Serikali kusimamia uratibu wa maafa kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na kanuni zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa mwaka 2022 umeweka bayana majukumu ya kukabiliana na maafa kwa kuanzia ngazi ya kijiji au mtaa, kata, shehia, wilaya, mkoa na Taifa, kupitia Kamati za Usimamizi wa Maafa zilizopo katika ngazi husika. Hivyo basi, nasisitiza kuwa, Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote ziendelee kuweka mipango madhubuti ya kutekeleza majukumu ya usimamizi wa maafa katika ngazi hizo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ya kutoishi maeneo ya mabonde ili kuepusha kutokea kwa maafa kama ambavyo sasa tunashuhudia kwenye maeneo yaliyoathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia mwelekeo na mwenendo wa maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo. Tarehe 3 Aprili, 2024 wakati nawasilisha Hotuba yangu ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na mwelekeo wa kazi zake kwa mwaka wa fedha 2024/2025, nililieleza Bunge lako Tukufu kuhusu mchakato wa maandalizi ya Dira Mpya ya Maendeleo ya Taifa. Niruhusu niwapitishe Waheshimiwa Wabunge katika mafanikio yaliyopatikana katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 pamoja na maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, umewezesha Taifa letu kuwa na mafanikio yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni kuboresha hali ya maisha ya Watanzania ikiwemo utoshelevu wa chakula, kuimarika kwa huduma za jamii hususan afya, elimu na upatikanaji wa maji, ongezeko la idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi na utawala katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kuongezeka kwa umri wa kuishi kwa Watanzania na kupunguza kiwango cha umaskini wa kutupwa kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuimarika kwa mazingira ya amani, usalama na umoja, ikiwemo kuzingatiwa kwa utii wa sheria na utawala wa kisheria kulikowezesha kupungua kwa matukio ya uhalifu wa aina mbalimbali, hususan mauaji, wizi wa watoto, unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi katika barabara kuu, uhalifu wa kifedha na dawa za kulevya. Yale ambayo yanajitokeza yanaendelea kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuimarika kwa utawala bora ikiwemo utaratibu wa makabidhiano ya kiuongozi na kiutawala kwa amani na utulivu. Kuongezeka kwa kiwango cha haki za msingi za binadamu na kuendelea kupungua kwa kiwango cha rushwa hapa nchini. Kuwepo jamii inayoelimika vema na inayojifunza ambapo idadi ya Watanzania wanaopata elimu rasmi imeongezeka katika ngazi mbalimbali ikiwa ni ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu. Aidha, kumekuwa na ongezeko kubwa la nyenzo na fursa za kuwezesha kuendelea kujifunza kupitia uwepo wa majukwaa ya mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, uchumi wetu kuweza kukabiliana na ushindani katika nchi nyingine kulikochangia kuongezeka kwa mpango wa pamoja wa Sekta ya Viwanda, Ujenzi na Uzalishaji wenye pato la Taifa. Kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi kupitia Sekta Ndogo ya Uzalishaji na kuhimili kiwango cha mfumuko wa bei kwa chini ya tarakimu moja. Ongezeko la pato la Taifa kwa mwaka kwa wastani wa 6.7%, kati ya mwaka 2000 na 2021, kuimarika kwa miundombinu ya msingi na ya kiuchumi, hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, huduma za mawasiliano na huduma za umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, matarajio yetu kwa Dira Mpya ya Taifa ni mafanikio yaliyopatikana yanayotokana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo itafikia tamati ifikapo Juni, 2026. Sasa, tuko kwenye mchakato wa maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo inayotarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2026/2027. Ni matarajio yetu kuwa, utekelezaji wa Dira Mpya utawezesha nchi yetu kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dira Mpya pamoja na mambo mengine itazingatia masuala muhimu yafuatayo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na sekta za uzalishaji; Kuimarisha upatikanaji wa data kwa sekta isiyo rasmi ili kuweza kurasimisha shughuli na kutambua mchango wake katika ukuaji wa Uchumi; Kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini; Kuwepo kwa utaratibu jumuishi wa programu mbalimbali za utekelezaji wa Dira Mpya; Kutoa kipaumbele katika ufanisi wa Mashirika ya Umma wakati wa utekelezaji wa Dira Mpya; Kuimarisha ushiriki wa Sekta Binafsi ndani na nje ya nchi pamoja na kuwawezesha wenyeji kuwa na utayari wa kupokea na kushirikiana na wageni wanaokuja kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini; na Kuweka mkazo zaidi katika suala la Maadili ya Taifa na kubainisha mapema viashiria hatarishi na namna ya kukabiliana navyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine natumia nafasi hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya Dira yetu Mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano. Wakati tunaelekea kutimiza miaka 60 ya Muungano wetu, sote ni mashahidi kwamba, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umedumu na umekuwa ni wa kipekee na wa kuigwa Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Vilevile, sote tunatambua kwamba, jitihada kubwa zimefanyika katika kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Tunu ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matunda ya Muungano wetu yanajumuisha kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili za Muungano. Aidha, kuingiliana kwa kuoleana pia nako kumeimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendelea kuutunza Muungano wetu ulioasisiwa na kuenziwa kwa manufaa ya Watanzania kwa kizazi cha sasa na baadaye, Serikali ilizindua kitabu kinachoelezea chimbuko la historia hiyo, misingi na maendeleo ya Muungano. Vilevile, elimu kwa umma kuhusu muungano imekuwa ikitolewa kupitia vipindi vya redio na television. Tumepeleka magazetini semina, warsha, makongamano, Maonesho ya Kitaifa, ziara za viongozi, machapisho mbalimbali na mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa terehe 26 Aprili, 2024, nchi yetu itaadhimisha Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Maadhimisho hayo yataongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matukio yaliyopangwa kufanyika ni pamoja na uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Muungano ambayo yalifanyika tarehe 14, jana, kule Zanzibar. Matukio mengine ni uzinduzi wa maonesho ya Muungano yatakayofanyika tarehe 19 Aprili katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam. Kutakuwa na Tukio la Dua na Sala ya kuliombea Taifa letu siku ya terehe 22 Aprili, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri hapa Jijini Dodoma. Natumia fursa hii kuwajulisha Watanzania kuwa, maandalizi yanaendelea vizuri na wote mnaalikwa kushiriki katika matukio hayo muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matukio hayo ni muhimu katika kuimarisha Muungano wetu, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaenzi waasisi wa Muungano ambao ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa pumziko la amani waasisi hawa wa Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wanafahamu kwamba Taifa letu mwaka huu litakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uchaguzi huu ni muhimu sana kutokana na ukweli kwamba, viongozi wa Serikali za Mitaa ni msingi imara katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa letu. Licha ya hayo, Viongozi wa Serikali za Mitaa ni wasimamizi wa karibu wa shughuli za maendeleo ya wananchi na pia, wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi katika maeneo yao. Kutokana na umuhimu huo, napenda kusisitiza kuhusu masuala yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni Watanzania wenzangu bila kujali jinsia watumie haki yao ya Kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa. Wale wenye uwezo wajitokeze kugombea nafasi za uongozi pamoja na kushiriki kikamilifu siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Watanzania wote wajitokeze kwa wingi ili kushiriki katika hatua zote za uchaguzi huo, ikiwemo Maboresho ya Daftari la Mpiga Kura.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, ni viongozi wa Serikali watumie kila fursa zikiwemo semina, warsha na mikutano kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huo. Waweke mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili waweze kuwajulisha wananchi kufahamu haki zao na wajibu wao katika kuchagua viongozi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, ni wamiliki wa vyombo vya habari waweke mkakati wa kuhamasisha umma wa Watanzania kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Waandae makala maalum na vipindi maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie utambuzi au kutambua mchango wa watumishi wa umma. Watumishi wa umma wana mchango mkubwa katika kutafsiri na kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais. Mafanikio tunayoshuhudia sasa katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya Taifa ni kutokana na kazi nzuri inayofanywa na watumishi wa umma. Natumia nafasi hii kuwapongeza kwa dhati watumishi wote wa umma kwa kujitoa kwao na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, nawakumbusha watumishi wenzangu kuimarisha ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi na kutekeleza kikamilifu wajibu tulionao. Watumishi wote tujikite katika kutatua changamoto na kero za wananchi, tuwafuate kwenye maeneo yao tukawasikilize na kutoa majawabu yanayohitajika. Kwa kufanya hivyo wananchi wataishi kwa amani na utulivu na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nifafanue baadhi ya hoja ambazo zilichukua nafasi kwenye mijadala yetu. Hoja ya kwanza ilitolewa na Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Sumve, Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum na Mheshimiwa Janejelly Ntate James, Mbunge wa Viti Maalumu. Hoja ilikuwa ni Serikali kufanya maboresho ya ulipaji wa mafao ya wafanyakazi kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na kwamba, Serikali iongeze wigo wa utoaji elimu ya kanuni mpya za mafao kwa watumishi, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kanuni mpya ya ulipaji wa mafao iliyoanza kutumika tarehe Mosi Julai, 2022 kwa kuzingatia tathmini ya uhimilivu na uendelevu wa Mfuko iliyofanyika katika kipindi husika. Serikali imesikia ushauri na kupokea maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Vyama vya Waajiri na wafanyakazi wenyewe. Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao kwa wastaafu na itaendelea kufanya tathmini ya kuzingatia sheria za kazi ili tuweze kufikia hatua nzuri ambayo haitazua malalamiko mengi. Aidha, kuhusu utoaji wa elimu ya kanuni za mafao kwa watumishi, Serikali itaendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa jamii ikiwemo na mafao kwa watumishi kupitia njia mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kumtaka Waziri wa Kazi na Ajira asimamie kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya mafao kwa watumishi kwa lengo la kujenga uelewa wa kutosha pamoja na mjadala ambao wanaendelea nao juu ya uwepo wa kikokotoo ambacho sasa kimekuwa kinatolewa ushauri na makundi mbalimbali ya wadau.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ilitolewa na Mheshimiwa Ahmed Shabiby, Mbunge wa Jimbo la Gairo, Serikali ihakikishe inaweka mikakati ya kuwezesha upatikanaji wa vyanzo vingi vya mapato ili kuwezesha upatikanaji wa Bima ya Afya kwa wananchi vijijini. Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023, imeanzisha Mfuko kwa ajili ya kugharamia Bima ya Afya kwa watu wasio na uwezo na kubainisha vyanzo vya fedha vya Mfuko huo. Serikali itaendelea kupokea mapendekezo ya uendeshaji wa mfuko, ikiwemo vyanzo vya mapato na kufanya maboresho kadri inavyofaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya wanyamapori kuvamia maeneo ya wananchi pamoja na mauaji ya watu kwenye hifadhi, iliyotolewa na Mheshimiwa Esther Nicholaus Matiko, Mbunge wa Viti Maalum. Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya wanyamapori kuvamia makazi na mashamba na kusababisha madhara kwa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi; madhara hayo ni pamoja na ulemavu, vifo na uharibifu wa mali. Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya kukabiliana na wanyama waharibifu, uanzishaji wa Vituo vya Ulinzi kwa Maafisa Wanyamapori. Kwa upande mwingine, kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi na kusababisha migogoro baina yao na Askari wa Hifadhi, changamoto ambayo pia imekuwa ikisababisha majeruhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kuwakumbusha wasimamizi wa hifadhi kuzingatia taratibu wakati wa kushughulikia changamoto za uvamizi wa hifadhi. Kwa upande mwingine, nawasihi wananchi kuheshimu mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuacha tabia ya kuingia hifadhini kiholela, kuingiza mifugo, kufanya shuguli za kilimo ndani ya hifadhi na uwindaji haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni ya Mheshimiwa Kasalali, Mbunge wa Sumve ya utekelezaji wa ahadi za Mawaziri. Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025 na ahadi za viongozi katika maeneo mbalimbali kupitia mipango ya bajeti ya kila mwaka. Utekelezaji unafanyika na unaendelea mpaka mwezi Juni, 2025 ambapo ndio mwisho wa mwaka huu wa fedha kwa hiyo, ahadi zote ambazo zimetolewa zinatarajiwa kutekelezwa katika kipindi hiki kwa zaidi ya 90%.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hitimisho. Wakati nahitimisha Hoja hii ya Waziri Mkuu, naomba nitumie nafasi hii kuzungumzia masuala yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikiko kwenye sekta ya michezo; sote ni mashahidi, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita...
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naongeza dakika 30.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya michezo imepata mafanikio makubwa. Michezo inapendwa na Watanzania walio wengi na imekuwa ni chachu ya maendeleo na nguzo muhimu kwa ustawi wa jamii pamoja na kuitangaza nchi yetu Kimataifa na kuliletea sifa Taifa letu. Wabunge watakubaliana nami kwamba, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mpenda michezo na amekuwa mstari wa mbele kusimamia ukuaji wa Sekta ya Michezo, maono na maelekezo yake yameleta mchango mkubwa na mafanikio katika sekta hii. Aidha, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara katika kuongeza hamasa kwa wanamichezo wetu. Suala ambalo limechangia kuimarika kwa nafasi ya Taifa kwenye michezo mbalimbali ya Kimataifa hususan kwenye ngumi, riadha na mpira wa miguu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa hamasa kubwa anayoitoa katika Sekta ya Michezo pamoja na kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia timu zetu, ili ziweze kufanya vizuri. Kama mtakumbuka, kupitia “Goli la Mama” mafanikio makubwa yamepatikana katika Mchezo wa Mpira wa Miguu. Katika hili, Mama amefanya mambo makubwa na kwa lugha ya sasa, “Ameupiga Mwingi na Apewe Maua Yake”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, jitihada za Mheshimiwa Rais zimewezesha Vilabu vyetu vya Mpira wa Miguu kuendelea kung’ara Kimataifa. Katika Msimu wa Ligi wa 2023/2024, Tanzania imekuwa nchi pekee iliyoingiza timu mbili kwenye hatua ya Robo Fainali ya Mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika. Hatua hii ni ya kupongezwa na kujivunia kama Taifa. Hongera sana wachezaji wetu, hongera sana viongozi wa vilabu, hongera sana timu zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kuvipongeza Vilabu vya Yanga na Simba kwa kufikia hatua ya robo fainali. Nawapongeza sana kwa kucheza mpira wa viwango vya hali ya juu. Michuano yote ilikuwa mikali na kwa yeyote anayefahamu mchezo wa mpira wa miguu atakubaliana nami kwamba, wachezaji wetu walionesha umahiri mkubwa, viwango vya hali ya juu na waliweza kukonga mioyo ya washabiki wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao, ama kwa hakika wanalitendea haki jukumu la kuishauri Serikali, la kuwawakilisha wananchi pamoja na kuhakikisha kwamba, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025 imetekelezwa kama ilivyoelekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kutoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali yake. Dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Mama Samia ni safi ambayo ni kuwaletea maendeleo ya haraka Watanzania wote. Jitihada kubwa anaendelea kuzifanya hivyo basi, Watanzania wote tumpe ushikiano unaohitajika ili aweze kufanikisha utekelezaji wa maono, mipango na mikakati ya kuinua ustawi wa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo yote, sasa naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zilizo chini yake na Mfuko wa Bunge kama ilivyowasilishwa katika Hoja yangu ya tarehe 3 Aprili, 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)