Answers from Prime Minister to Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa (280 total)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kumuuliza Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, wewe ukiwa kama Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni na wewe ukiwa kama mwanasiasa mzoefu, nina hakika unatambua kwamba ujenzi wa demokrasia ni gharama na ni mchakato wa muda mrefu. Nina hakika utakuwa utajua vilevile kwamba nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kujenga jamii inayoheshimu demokrasia, inayoheshimu Sheria na inayoheshimu Katiba ya nchi. Katika muda mfupi tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, yapo mambo matano makubwa yaliyotokea ambayo yanaashiria, aidha Serikali hiyo haiheshimu kukua kwa demokrasia katika Taifa ama pengine ina dhamira ya kuondoa lengo kubwa hilo lililowekwa na Katiba ya Taifa.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo hayo ni pamoja na baada tu ya uchaguzi wa mwaka 2015, Jeshi la Polisi limeweka makatazo nchi nzima kwa Vyama vya Siasa kufanya kutokufanya kazi zake za kisiasa, haki ambayo ni haki ya kikatiba.
Leo tayari ni miezi mitatu na siku tatu katazo hilo linaendelea na katazo hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu uliliunga mkono na kulisisitiza katika mkutano wako uliofanywa katika Jimbo lako la Ruangwa, kwamba wenye haki ya kufanya ni wale walioshinda, lakini Vyama vya Siasa haviendelei kuruhusiwa kufanya kazi hiyo ya siasa. (Makofi)
Swali langu sehemu (a) ni kama ifuatavyo; Mheshimiwa Waziri Mkuu unataka kuithibitishia Bunge hili, nchi hii na dunia hii, kwamba wewe kama Kiongozi Mkuu wa Serikali una kusudio la kuendelea kuzuia Vyama vya Siasa kufanya kazi zake za kisiasa ambayo ni haki yao ya Kikatiba? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu, tukiendelea hapo hapo unatambua vilevile kwamba urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ni haki ya Kikatiba ya wananchi kupata taarifa na Shirika la Habari la Taifa ni shirika la umma, lakini ndani ya Bunge kuna taarifa zilizo rasmi kabisa kwamba Serikali yako imetoa kauli hapa kuzuia urushaji huo wa matangazo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na uzuiaji wa urushaji huo wa matangazo kumeendelea kuwepo matumizi makubwa ya majeshi yetu kuanzia Zanzibar hadi hapa na Zanzibar katika kupinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar ambao ulikuwa ni uamuzi wa wananchi?
Mheshimiwa Waziri Mkuu unaiambia nini dunia kwamba Awamu yako ya Tano sasa imekubali kuwa na utawala wa kijeshi kwa mgongo wa utawala wa kidemokrasia? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme namshukuru sana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwa maswali yake mawili ambayo yanahitaji ufafanuzi na Watanzania waweze kujua, kwamba uongozi huu wa Awamu ya Tano ni uongozi ambao unaongoza kwa kufuata demokrasia, kanuni, sheria na taratibu kadri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo mambo yanajitokeza na tunapojaribu kutoa maelekezo ya kimsingi ya kuweza kufuatilia na kwa sababu ya utaratibu wa mazoea tu yanaweza kutafasiriwa vinginevyo. Suala lako la makatazo ya Vyama vya Siasa kufanya mikutano, ni jambo ambalo naweza kusema msemaji wa kwanza kabisa hakutumia nafasi yake ya uandishi kuandika kwa mfululizo kwa sababu ni mimi ndiye ambaye nilikuwa nimefanya ziara kwenye Jimbo langu kusalimia wapiga kura wangu.
Mimi ni Mbunge kama nyie na ninapokuwa Ruangwa sivai koti la Waziri Mkuu bali nakuwa Mbunge nazungumza na watu wangu. Nimekuwa na vikao mbalimbali vya makundi mbalimbali nikiwashukuru binafsi kwenye Jimbo langu ambako najua tuna utamaduni wetu. Nimepita pia kwenye Kata ambazo pia Madiwani wetu ni wa Vyama vya Upinzani, lakini tumeweka msimamo wa vyama vyote katika Jimbo lile kwamba lazima sasa tufanye kazi za maendeleo kwenye Jimbo letu.
Mheshimiwa Spika, kama mwandishi yule angeweza kuweka mtiririko wa ziara zangu na matamko yetu ndani ya Wilaya yangu kwa Jimbo langu, angeweza kunitendea haki, kwa sababu nilichotamka mimi kilifuatiwa na kauli zilizotamkwa na Madiwani kwenye Kata ambako nimetembela wakiwemo wa upinzani, ambao walisisitiza na kutoa msimamo kwamba sasa Jimbo hili tunataka tufanye kazi suala la siasa tunaliweka pembeni na tunaondoa tofauti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya yanazungumzwa na Madiwani wenzangu wa vyama vingine. Kwa hiyo, ni jambo jema wanapolitamka kwa wananchi kwa maana ya kuweka msimamo wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtiririko ule tulizungumza pia na Baraza la Madiwani, nimezungumza na wafanyakazi wa Halmshauri, nimezungumza na Baraza la Wazee, nimezungumza na akinamama na pia nikazungumza na Jeshi la Polisi, wale ni sehemu ya raia walioko kwenye Jimbo langu. Mimi nimefanya kazi nyingi kwao na wao wamefanya kazi nyingi sana kwangu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kauli yangu ilikuwa inatokana na mazingira yale, kama mwandishi angeamua kufanya kazi yake vizuri kwa kueleza shughuli zangu hata nilipotamka kwamba kuanzia sasa sisi tumeamua tufanye kazi, bila kuzingatia itikadi za vyama vyetu na kwamba sasa mambo ya siasa tuache pembeni. Wale wote ambao sasa wangetakiwa kupita kwenye maeneo ya walioshinda ni wale tu ambao wameshinda kwenye maeneo yao. Kwa hiyo jambo lile kama lingekuwa limeelezwa, limeripotiwa kwa mtiririko ule wala lisingeweza kuleta tafsiri ambayo imekuja kutolewa.
Mheshimiwa Spika, najua utawala wa sheria, najua Vyama vya Siasa vina haki yake, najua nchi inatambua kwamba chama cha siasa kinaweza kufanya mkutano. Pia kama msingi ule wa kauli ya Wanajimbo wa Ruangwa unaweza kufuatwa na watu wengine unaweza kuwaletea tija pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hayo niliyosema, niseme tu kwamba, jambo lile lilitokana na mazingira ninamoishi na sikulitamka kama Waziri Mkuu, nilitamka kama Mbunge wa Jimbo na lilitokana na matamko ya sisi wawakilishi wa Vyama vya Siasa kutoka kwenye Jimbo lile Mheshimiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni lile ambalo Mheshimiwa ametaka kujua suala la kauli ya Serikali juu ya TBC kuacha kutangaza siku nzima na badala yake watatangaza vipindi vya maswali na majibu, lakini baada ya hapo wataendelea na shughuli zao na huku waki-record ili waweze kututangazia baadaye.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amelifafanua vizuri sana jana kwenye kipindi maalum na naamini Watanzania wametuelewa. TBC haijaacha kutangaza, walichofanya ni kubadilisha ratiba. Matangazo ya Bunge yataendelea kutangazwa, lakini tumebadilisha muda, badala ya muda ule ambao wao wangeweza kufanya matangazo ya kibiashara na matangazo mengine, suala la Bunge waandishi wao wako, TBC ina wawakilishi Dodoma, watafanya recording, halafu baadaye watatafuta muda mzuri ambao pia tunaamini Watanzania wengi watapata muda mzuri wa kuweza kuyasikiliza matangazo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huo ni mpango wa Taasisi yenyewe wa ndani, unaotokana na kazi wanazozifanya, wanajua matatizo na faida wanazozipata ndani ya Taasisi. Kwa hiyo, wanapoishauri Wizara, wanapoieleza Wizara na kwa kuwa walishaanza kutekeleza na Watanzania waliona mkatiko wa matangazo, lakini pia kulikuwa na mwongozo ulitolewa hapa. Kwa hiyo, tukasema jambo hili ni lazima sasa tulieleze kesho yaani lazima kuwe na kauli ya Serikali kwa Watanzania kwa sababu Mwongozo ulitolewa na mmoja kati ya Wabunge wetu anataka kujua kwa nini kuna mkatiko wa matangazo. Kwa hiyo, ndivyo ilivyokuwa na huo nadhani ni msimamo wa TBC na ndiyo msimamo wa Serikali.
SPIKA: Tunaendelea na Mheshimiwa Kiongozi wa Upinzani swali la nyongeza!
MBUNGE FULANI: La majeshi bado.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa ametaka pia kujua matumizi ya Majeshi. Majeshi yetu yapo kwa malengo kwamba lengo kuu ni kutunza amani na utulivu ndani ya nchi. Wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha kwamba watu kwa maana ya Watanzania kwa Majeshi ya Tanzania, wajibu wake ni kuhakikisha kwamba watu wetu wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu na wako nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jukumu lao ni kumlinda Mtanzania popote alipo bila ya kukiuka misingi ya jambo ambalo anatakiwa kulifanya wakati huo. Wapo Zanzibar, wapo pia Tanzania Bara na wote hao kazi yao na jukumu lao ni lilelile. Sasa wanaweza kulazimika kutumia nguvu pale ambapo wanaona utaratibu uliowekwa eneo hilo unakiukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo kazi ya Jeshi la Polisi, kwamba wataendelea kutunza amani ili Watanzania waliokuwa kwenye eneo hilo kila mmoja afanye shughuli yake. Kila mahali kuna utaratibu wake na kila mahali kuna msingi wake na tunatarajia katika eneo, wote walio kwenye hapo, wanaofanya jambo hilo, wafanye jambo hilo kwa msingi unaofanana, usiokiuka taratibu za eneo hilo.
Kwa hiyo, Jeshi la Polisi lipo na litaendelea kufanya kazi yake kwa uaminifu, kwa uadilifu na naomba sana tuwasaidie Jeshi la Polisi kufanya kaziWAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa ametaka pia kujua matumizi ya Majeshi. Majeshi yetu yapo kwa malengo kwamba lengo kuu ni kutunza amani na utulivu ndani ya nchi. Wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha kwamba watu kwa maana ya Watanzania kwa Majeshi ya Tanzania, wajibu wake ni kuhakikisha kwamba watu wetu wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu na wako nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jukumu lao ni kumlinda Mtanzania popote alipo bila ya kukiuka misingi ya jambo ambalo anatakiwa kulifanya wakati huo. Wapo Zanzibar, wapo pia Tanzania Bara na wote hao kazi yao na jukumu lao ni lilelile. Sasa wanaweza kulazimika kutumia nguvu pale ambapo wanaona utaratibu uliowekwa eneo hilo unakiukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo kazi ya Jeshi la Polisi, kwamba wataendelea kutunza amani ili Watanzania waliokuwa kwenye eneo hilo kila mmoja afanye shughuli yake. Kila mahali kuna utaratibu wake na kila mahali kuna msingi wake na tunatarajia katika eneo, wote walio kwenye hapo, wanaofanya jambo hilo, wafanye jambo hilo kwa msingi unaofanana, usiokiuka taratibu za eneo hilo.
Kwa hiyo, Jeshi la Polisi lipo na litaendelea kufanya kazi yake kwa uaminifu, kwa uadilifu na naomba sana tuwasaidie Jeshi la Polisi kufanya kazi yao bila ya usumbufu ili wasionekane wanafanya kazi nje ya utaratibu wao. Hilo ndiyo jibu la msingi. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kuuliza swali kwako Mikoa ya Kanda ya Magharibi, Mkoa wa Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma, ni Mikoa pekee ambayo hayaijaunganishwa barabara kwa kiwango cha lami. Mikoa hii inazalisha chakula kwa wingi, kwa bahati mbaya bado miundombinu kuwasaidia wananchi wa Mikoa hii ambayo walisahaulika kwa kipindi kirefu toka uhuru? (Makofi)
Naomba kupata majibu ya Serikali juu ya umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami na ukizingatia Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, amewaahidi wananchi hao na mkoa wake wa kwanza wakati wa harakati za kuomba kura za Urais alianzia Mkoa wa Katavi na kutoa ahadi nzito, Serikali ina dhamira ipi ya kukamilisha miundombinu hiyo? (Makofi)iko duni na kuwafanya wananchi wa mikoa hii kudumaa kiuchumi.
Je, Serikali ina mpango gani ya kuunganisha hii mikoa ili iweze kupata barabara za lami, kwa maana ya barabara kutoka Sumbawanga kuja Mpanda, barabara kutoka Mpanda kwenda Kigoma, barabara kutoka Mpanda kupitia Wilaya ya Mlele-Sikonge kwenda Tabora, halikadhalika kumalizia barabara ya Tabora kwenda Kigoma. Serikali ina mpango gani
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mkoa ule hatujamudu kuunganisha maeneo yote na mikoa yote ya jirani. Hata hivyo, Mheshimiwa Mbunge anajua jitihada ambazo Serikali hii inafanya sasa za kuimarisha miundombinu na hasa barabara kwa miradi tuliyonayo nchi nzima, yenye malengo ya kuunganisha mikoa yetu tuliyonayo. Tayari ipo miradi inaendelea Mkoani Katavi ya kuunganisha na mikoa ya jirani, ikiwemo Katavi kwenda Mbeya. Pia upo mpango wa ujenzi wa barabara kutoka Katavi kupitia Sikonge mpaka Tabora na tunaimarisha barabara kutoka Katavi kwenda Kigoma kupitia Uvinza na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, miradi hii ambayo sasa inatekelezwa nchi nzima, inawezekana yako maeneo ambayo tumeanza na mengine tunaendelea, lakini mengine yapo kwenye mpango wa uendelezaji. Kwa hiyo, nataka nimpe imani na hii niwaambie wananchi wote walioko mikoa ile kwamba Serikali inayo nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba tunaunganisha mikoa yetu yote kwa barabara za kiwango cha lami. Kazi tunayoifanya sasa ni kuhakikisha tu kwamba, tunatenga fedha kwa barabara ambazo zinaendelea, lakini zile ambazo hatujaanza kabisa, tunapeleka wataalam kwa ajili ya upembuzi yakinifu ili tuanze michoro na kazi hiyo tuweze kuanza. (Makofi)
Kwa hiyo, tutaendelea pia kushirikiana na wananchi wa Mkoa wa Katavi kuhakikisha kwamba barabara zao zote tunaziunganisha, kama ambavyo sasa tunaendelea kuunganisha mikoa mingine kama Mkoa wa Dodoma na Manyara, Dodoma na Iringa, Dodoma tumeshaanza kwenda Singida sasa tunakwenda Tabora kupitia Manyoni. Kwa hiyo jitihada hizi ni za nchi nzima na wote ni mashahidi kwamba kazi hizi zinaendelea vizuri.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kazi hiyo inaendelea na Katavi pia watanufaika pia na mpango wa Kitaifa wa kuunganisha mikoa yetu.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni Serikali imetoa Waraka katika Halmashauri zetu kuhusu elimu bure na Waraka wenyewe ni wa tarehe 6 Januari, 2016.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waraka huu umezua sintofahamu katika sehemu ya chakula cha wanafunzi katika shule zetu. Mfano, Waraka huu unasema kwamba wanafunzi wanaosoma day wazazi walipe chakula, lakini wanafunzi wanaosoma shule za bweni ambao wazazi wao wana uwezo hata wameweza kuwafikisha katika shule hizo, hawatakiwi kulipa hata chakula, Serikali itapeleka chakula.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali inasemaje katika hali hii ambayo imezua mtafaruku kwa wazazi kuona kwamba wamebaguliwa wale ambao hawana uwezo na Serikali imewaongezea uwezo wale ambao kidogo wana uwezo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philip Gekul, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini kama ifuatavyo:-
Ni kweli kwamba ipo mikanganyiko imejitokeza sana hasa baada ya kuwa tumeanza kutekeleza mfumo wa elimu bure. Hata hivyo, nataka niwajulishe Watanzania wote maeneo ambayo Serikali imejikita, kuwa ni ya bure.
Moja, kwa upande wa sekondari, tulikuwa na ada ya shilingi 20,000/= kwa mwaka kwa shule za kutwa, eneo hilo sasa hawatalipa. Eneo la sekondari za bweni, wazazi walikuwa wanalipa shilingi 70,000/= kwa mwaka eneo hilo halilipiwi, ni bure. Eneo la tatu, kwa shule za msingi na sekondari mitihani yote ya darasa la nne na kidato cha pili, iliyokuwa inafanywa kwa wanafunzi kuchangia, eneo hilo sasa wanafunzi hawatachangia. Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mitihani hiyo ya kidato cha pili na darasa la nne, watafanya bure.
Mheshimiwa Spika, eneo la lingine kwa shule za sekondari za bweni ambazo wanakula chakula tunaendelea na utaratibu wa kuwalipia, kuwagharamia. Sasa mkanganyiko unaojitokeza kwa uelewa wangu, Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote, ni pale ambako zipo shule za kutwa, ambazo kisera shule za kutwa, ni za mtoto anatoka nyumbani anaenda shuleni, anasoma anarudi kula nyumbani. Hizi sasa ndiyo ambazo zimeleta mkanganyiko hasa kwa wazazi ambao walikuwa wamejiwekea mpango wao, wao wenyewe ili kuweza kuwafanya vijana wetu waweze kupata lishe shuleni.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili nikiri kwamba pamoja na mkanganyiko ikiwemo na hili, Wizara sasa inaandaa utaratibu mzuri wa maelezo mazuri ya namna tutakavyotekeleza kwenye eneo hili halafu tutatoa taarifa, kwa sababu ndiyo tumeanza kutekeleza mwezi Januari, hizi changamoto zimeanza kujitokeza, yako maeneo mengine wanaendelea kuchangisha. Kwa hiyo, tunataka tutoe Waraka ambao sasa utaweka wazi kila kitu na Waheshimiwa Wabunge, tutawaletea nakala ili mtusaidie katika kuratibu jambo hili. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza naishukuru Serikali yako kwa kuondoa tozo kadhaa kwenye zao la korosho. Swali langu ni je, pamoja na kuondoa tozo hizo, Serikali imeendelea kumnyonya mkulima kwa kukata asilimia 15 ya bei ya soko. Je, Serikali ina mkakati gani kuendelea kumwondolea mkulima tozo hii ambayo ni kubwa sana?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katani, Mbunge wa Tandahimba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Katani pamoja na Wabunge wote wanaotoka mikoa inayolima korosho kwa kazi kubwa waliyoifanya kubainisha matatizo makubwa yanayowapata wananchi wanaolima korosho na hasa wanapolalamikia mfumo ulio bora na imara, lakini kutokana tu na kuwa na tozo nyingi, kama ambazo Mheshimiwa Mbunge amezisema.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya maamuzi ya kupunguza tozo zote za hovyo ambazo zilipangwa tu kwa lengo la kutaka kuvuruga mfumo na hatimaye wananchi wakachukia kutumia mfumo ambao unawaletea tija kwenye zao lao la korosho. Hii ni pamoja na tozo za asilimia 15 ambazo zipo miongoni mwa zile tozo, lakini tozo hii ya asilimia 15 kwenye orodha ya zile tozo, ilikuwa iko kwenye eneo la manunuzi ya vifungashio. Vifungashio; kuna magunia ambayo bei yake ni ya juu kidogo, pamoja na nyuzi.
Mheshimiwa Spika, tozo hii sasa itakuwa imeondoka kwa kuwa tumeupa Mfuko unaoitwa Mfuko wa WAKFU, ambao unasimamia maendeleo ya zao la korosho. Mfuko huu umeundwa na wadau wenyewe na unachangiwa na tozo za korosho zinazouzwa nje ya nchi. Inaitwa Export Levy, ambayo inachangiwa kwa asilimia 65 na tozo hii huwa inatozwa na TRA.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mfuko wetu wa WAKFU kwa asilimia zile 65, sasa hivi wana hela nyingi sana kwa ajili ya kukamilisha madhumuni ambayo yamepangwa na wadau ikiwemo na kuhakikisha kwamba, masoko ya zao la korosho yanapatikana. Pili, kuhakikisha kwamba, wananunua pembejeo kwa maana ya mbolea na mbegu, kusimamia uboreshaji wa mbegu hizo na kupanua mashamba ya korosho; pamoja na kugharamia tafiti mbalimbali ambazo zinatakiwa ziwe zinafanywa kwa ajili ya kupata ubora wa zao la korosho.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Katani na Wabunge wote wanaotoka mikoa ya korosho, tozo hii iko sasa kwenye Mfuko wa WAKFU ambao umeingia kwa ajili ya kununulia vifungashio na kwa hiyo, mkulima kwa sasa hana tozo hiyo.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu; katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na migogoro mingi sana baina ya wafugaji na wakulima kwa upande mmoja, kugombea maeneo; lakini pia baina ya wakulima, wafugaji na maliasili, kwa upande mwingine. Hii ni katika maeneo mengi ya nchi. Sasa kwa kuwa katika Ilani ya Uchaguzi yako maelekezo kwamba Serikali itapima maeneo mapya kwa ajili ya wakulima na wafugaji hususan kuongeza eneo la wafugaji kutoka hekta milioni moja hadi milioni tano:-
Swali, je, ni lini Serikali itateua Kamati ya Kitaifa ambayo itapitia maeneo yote na kutoa mapendekezo yatakayotekelezwa ili kuondoa migogoro hii na watu waendelee kuishi kwa amani? Hii kazi inahitaji msaada zaidi. Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakunda Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba sasa hivi tunayo migogoro mingi sana ya wafugaji na wakulima, lakini pia hata migogoro ya ardhi yenyewe tu baina ya jamii zetu; mtu mmoja mmoja lakini pia na jamii na jamii. Migogoro hii tumefika wakati sasa tunatakiwa kuitafutia ufumbuzi. Jambo ambalo amelieleza Mheshimiwa Mbunge ni miongoni mwa mikakati ambayo sisi tunayo pia.
Mheshimiwa Spika, moja, tumeanza kutafuta njia sahihi ya kuondoa migogoro ya ardhi na hii inatokana na kuongezeka kwa matumizi na mahitaji ya ardhi na thamani ya ardhi. Pili, kumetokana na matatizo makubwa yaliyojitokeza kwenye maeneo yale ya mipaka kutokana na mahitaji ya kupanua eneo; kuongezeka kwa mifugo mingi; lakini wakati mwingine ni utendaji wa hovyo tu wa Watendaji wetu wa Serikali ambao tumewapa dhamana kwenye maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tunao wawekezaji ambao wanaingia kinyemela kwenye maeneo yetu na wanapoingia kule wanajichukulia ardhi na kuongeza maeneo bila ridhaa ya wananchi wenyewe na kusababisha migogoro mingi. Kwa hiyo, jukumu la Serikali ambalo pia Mheshimiwa Mbunge amesema, ni kweli tuliamua tuunde task force inayounganisha Wizara tatu; Wizara ya Ardhi yenyewe, Wizara ya Maliasili, pamoja na Wizara ya Kilimo ili tuweze kubaini mipaka yote, tuweze kubainisha maeneo haya ili kila mmoja ajue anakaa wapi na vinginevyo, kwa kupima maeneo haya na kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi yanayobainisha maeneo ya wafugaji, wakulima, viwanda na maeneo ya makazi ya kawaida. Kwa hiyo, task force hii kwanza tumezipa Wizara zenyewe majukumu.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili ituambie kwenye maeneo yale na ukomo wake, wanaishia wapi. Wizara ya Kilimo nayo watuoneshe wananchi wanaishia wapi na kilimo wapi baadaye sasa tumwite Waziri wa Ardhi wakae pamoja, tuweze kuweka mipaka mipya. Hii ikiwemo na kuongeza maeneo ya wafugaji kama ambavyo sasa tumeamua wafugaji wote sasa kuwatengea maeneo, kutumia ranch zetu za Taifa na mkakati huu ni ule wa kuboresha mifugo yetu.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanaofuga kawaida, watakuwa wanapeleka mifugo yao kwenye maeneo ambayo tumewatengea kama ranch ambayo mimi mwenyewe nimetembea; nimekwenda Mkoa wa Kagera kuona kule Misenyi, Karagwe lakini pia nimekwenda na Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ufumbuzi wetu ni kuwapeleka wafugaji kwenye maeneo yale, tunataka tuwamilikishe kwenye zile blocks. Wafugaji wote wenye mifugo mingi wakae kwenye maeneo yale ili sasa waweze kulisha, kuogesha, wanenepeshe, waweze kuuza maeneo ya nje. Huku vijijini kutakuwa na ng‘ombe hawa wachache ambao watakuwa wanaenda ranch kwa kuwapa maeneo hayo ya wafugaji, baada ya kuwa tumeweka mpango bora wa matumizi.
Kwa hiyo, Tume ile itakapoundwa, tutaileta maeneo hasa yenye migogoro. Simiyu nimekwenda nimeona migogoro mingi, kwa hiyo, maeneo kama hayo yatapata kipaumbele katika kuanza na zoezi hili.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Serikali yetu ya Tanzania ilisaini na kuridhia ule Mkataba wa Kimataifa wa 2006 kuhusu haki za watu wenye ulemavu, uliridhiwa, yaani ulikuwa ratified mwaka 2009. Utaratibu ni kwamba baada ya miaka miwili baada ya kuridhia, Serikali inatakiwa kuandika State Report na kuiwakilisha kwa ile Kamati ya Umoja wa Mataifa inayosimamia utekelezaji wa huo mkataba.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Serikali yetu haijaandika hiyo State Report, sasa ni miaka minne overdue. Ni kwa sababu gani, Serikali yetu haijapeleka State Report kuhusu huo Mkataba wa Watu Wenye Ulemavu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Macha, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeridhia mikataba mingi sana, kwa lengo la kuunganisha Taifa letu na matakwa yetu na Mataifa na Taasisi mbalimbali za Kimataifa ili kuweza kufungua milango ya huduma mbalimbali, mahitaji mbalimbali ya nchi na Mataifa ya nje ikiwemo na jambo ambalo Mheshimiwa Macha amelieleza.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu imedhamiria kufungua milango na kutoa huduma na kuweza kuwafanya ndugu zetu wenye mahitaji maalum kuwa ni sehemu ya wachangiaji wakubwa wa shughuli mbalimbali za maendeleo nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumefungua milango hiyo, Serikali ya Awamu ya Tatu, Serikali ya Awamu ya Nne imeweza kuwashirikisha kikamilifu Watanzania wote ambao wana mahitaji maalum na katika kuweza kuona katika kupata mchango wao ili pia waweze kutoa mchango wao kikamilifu, ikiwemo na mikataba hii. Mikataba hii baada ya kuwa tumeunda Serikali yetu, tutafanya mapitio ya kazi zote zile za Awamu ya Nne ambazo zilikuwa zimefikiwa na sasa tuweze kuunganisha na mkakati ambao Mheshimiwa Rais ameuweka wa kuunda Wizara inayoshughulikia eneo la hilo na baadaye itafanya mapitio na imeshaanza kufanya mambo mengi ya kuweza kuridhia mikataba yote au kupitia mikataba yote ambayo tunadhani inaweza kuwaunganisha Watanzania wote kuweza kuridhia jambo ambalo tumekubaliana nalo. Kwa hiyo, hili ni pamoja na lile ambalo Mheshimiwa Macha amelieleza.
Mheshimiwa Spika, kwa mkakati tulionao, Mheshimiwa Dkt. Possi ameanza kukutana na wadau wenyewe kuanza kupitia mikataba ile kuona kama ina tija kwa Taifa, ina tija kwa ndugu zetu Watanzania ili sasa tuweze kuridhia. Kwa hiyo, taratibu zinaendelea na pindi itakapokamilika, tutaweza kukushirikisha Mheshimiwa Mbunge.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo imenadiwa na Mheshimiwa John Pombe Magufuli mwaka 2015; moja ya ahadi kubwa ambayo ilitolewa kwa Watanzania ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami. Naomba kufahamu kupitia Serikali yetu, imejipanga vipi katika kutekeleza ahadi hii ambayo kimsingi inasubiriwa na Watanzania walio wengi?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masala, Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Mkoani Lindi, kama ifuatavyo:-
Kwanza, nataka niwaambie Watanzania kwamba Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015 imefafanua mambo mengi ambayo tumeamua tuyatekeleze katika kipindi cha miaka mitano. Jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua utekelezaji wake ni lini, nataka nimhakikishie kwamba ahadi zetu zote zilizoahidiwa na Chama cha Mapinduzi zitatekelezwa kama ambavyo zimeahidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumedhamiria kujenga barabara zetu kwa kiwango cha lami na tumeanza na mkakati wa kuunganisha barabara za ngazi za Mikoa, zinazounganisha Mikoa kwa Mikoa; tukishakamilisha hizo, tunaingia kwenye barabara zinazounganisha ngazi za Wilaya na barabara zote ambazo zimeainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa awamu hii ni barabara ambazo zitakamilishwa kupitia bajeti ambayo sasa mnaipitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi itakapokuja hapa, naomba niwashawishi Waheshimiwa Wabunge kuweza kuipitisha ili tuanze kazi ya kukamilisha barabara ambazo nimezitaja. Pale ambapo barabara za Mikoa hazijakamilika, tunataka tuzikamilishe. Tukishakamilisha hizo zote, tunaanza ngazi za Wilaya ili tuendelee.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie Watanzania wote kwamba ahadi zote zilizotolewa na Mheshimiwa Rais kwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 zitakamilishwa kama zilivyoahidiwa. Ahsante sana.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami kwa niaba ya wananchi wa Temeke niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunatambua kwamba mmiliki wa ardhi ya nchi hii ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kimsingi Serikali imekuwa iki-enjoy mamlaka hayo kwa kuchukua baadhi ya maeneo kwa ajili ya kukaribisha uwekezaji. Hili ni jambo zuri sana kukaribisha uwekezaji. Isipokuwa inasahau kitu kimoja, pale ambapo inawakaribisha hao wawekezaji, haizifanyi Halmashauri husika kuwa sehemu ya uwekezaji ule kwa maana ya uanahisa. Je, Serikali yako imejipangaje sasa kubadilisha mwelekeo huu ili kila unapowekwa uwekezaji ile Halmashauri iwe sehemu ya mwanahisa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mtolea, Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu imefungua milango kwa wawekezaji nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali kulingana na matakwa ya mwekezaji. Uwekezaji huu unafanywa na unajikuta upo kwenye mamlaka zetu za Halmashauri ya Wilaya, Manispaa na maeneo mengine. Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kama Serikali imejipangaje na Halmashauri hizi kuweza kunufaika na uwekezaji huu?
Mheshimiwa Spika, ni kweli. Sasa uwekezaji huu uko wa aina mbili; kuna uwekezaji ambao tumeutaka upitie kwenye Taasisi yetu ya Uwekezaji (TIC) ambapo TIC inayo Benki yake ya Ardhi na kwa kuwa ardhi ni ya Serikali, kwa hiyo TIC tumeweza kuwapa ardhi ambapo wao sasa wakipata mwekezaji mkubwa, wanaweza kwenda kuwekeza mahali. Kwa uwekezaji huu, wanapokwenda kuwekeza kwenye eneo lolote lile Halmashauri ndiyo ambayo itakuwa imetoa ardhi hiyo lakini kupitia TIC na uwekezaji huo, Halmashauri wanaweza kunufaika kwa tozo ya ile ardhi.
Mheshimiwa Spika, pia Halmashauri inaweza kunufaika pia kwa mwekezaji huyo kushiriki kikamilifu kwenye mipango ya maendeleo ya Halmashauri kwa kuchangia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yale. Pia kama kuna tozo nyingine na manufaa ya uwepo wa mradi wenyewe kama kuna bidhaa zinatengenezwa tunatarajia eneo hilo linaweza kunufaika kwanza kwa gharama nafuu kupitia uwekezaji ule.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji mwingine ni ule ambao Halmashauri yenyewe inakuwa na Benki yake ya ardhi ambayo inaamua sasa kutafuta wawekezaji ili kufanya maendeleo. Hii inanufaika zaidi kwa sababu kwanza atapata tozo ya ardhi, lakini pili, naye anaweza kuwa ni sehemu ya mwanahisa wa mradi wenyewe kulingana na utaratibu atakaotumia; lakini atanufaika na manufaa yale yote ambayo nimeyataja kwamba mwekezaji anatakiwa atambue kwamba yeye yupo pale na wananchi waliopo maeneo yale watanufaika kupitia mradi wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namna ambavyo Serikali tunasimamia jambo hili, kwanza tunahakikisha wawekezaji tunawatambua na uimara wao, ubora wao katika uwekezaji na tunawaunganisha na maeneo hayo ili waweze kujenga mshikamano katika kuwekeza ili pia na yeye aweze kupata security na Halmashauri kwenye maeneo hayo ziweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uwekezaji wa aina mbili; uwekezaji ambao wananufaika zaidi ni ule ambao Halmashauri yenyewe imetengeneza mpango wa matumizi ya ardhi lakini wametenga maeneo ya uwekezaji ili mwekezaji anapokuja, anakwenda kuwasiliana na Halmashauri. Kwa hiyo, pale wana-negotiate, wanaweza kukubaliana yale mambo ya msingi ili kuweza kupata tozo mbalimbali ikiwemo na Halmashauri yenyewe kutumia ardhi yake kuwa mwanahisa wa ardhi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakuta kuna tofauti kati ya ardhi inayomilikiwa na TIC, Taasisi ya Uwekezaji ambayo inakwenda kumpeleka mwekezaji ili awekeze chini ya Taasisi ya Uwekezaji na ile ardhi ambayo mwekezaji anakwenda kwa uwekezaji chini ya Halmashauri yenyewe. Kwa hiyo, maeneo haya yote utofauti wake ni kama ambavyo nimeweza kuutofautisha na namna ambavyo unaweza kunufaika.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, mvua zimenyesha pasipo kueleweka, zimekwenda kuua mazao mengi sana katika maeneo mbalimbali, hali ambayo inaonesha kabisa kuna viashiria vya njaa huo mbele tunapokwenda. Je, Serikali yetu imejipanga vipi katika kukabiliana na janga kubwa la njaa ambalo linaweza kuja baadaye kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kisangi, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kupitia swali hili kwanza naomba nitoe pole kwa wananchi wote ambao wamekumbwa na matatizo makubwa ya mafuriko. Mafuriko haya yameleta madhara makubwa ya vifo, uharibifu wa mali, lakini pia mashamba yetu yote yamesombwa na maji. Nilisema hapa nilipokuwa nahitimisha hoja yangu wiki iliyopita kwa kuwatahadharisha Watanzania baada ya kuwa tumepata taarifa kutoka chombo chetu cha hali ya hewa kwamba mvua hizi bado zinaendelea. Natoa pole kwa watu wa Kilosa, natoa pole kwa watu wa Moshi Vijijini na Rombo ambako pia ndugu zetu wengi wamepoteza maisha na madhara hayo ambayo nimeyataja.
Mheshimiwa Spika, Serikali imejipanga kuwahudumia Watanzania wote wanaopata madhara na mpango huu upo kwenye Ofisi yangu kupitia Kitengo cha Maafa. Tunaendelea kufanya tathmini na tathmini hii inafanywa kwanza na Halmashauri zote zote za Wilaya ambazo ndiyo zimeunda Kamati ya Maafa kwenye maeneo yao. Wakishafanya tathmini, Mkoa unafanya mapitio na mahitaji yao halafu wanatuletea ofisini kwetu; nasi tunapeleka misaada kadiri walivyoomba kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tuna hifadhi ya chakula, yaani tunacho chakula cha kutosha cha kupeleka kwenye maeneo hayo na tayari tumeshaanza kupeleka chakula kwenye maeneo yote yaliyopata maafa. Tumejiimarisha tena kwa ajili ya maafa haya yanapoweza kutokea hapo baadaye na kutumia msimu huu wa kilimo kwa maeneo ambayo hayajapata madhara.
Nataka nitoe wito kwamba tulime sana, tupate chakula kingi tuweze kutunisha hifadhi yetu ya chakula ili pia tunapopata tatizo la mahitaji ya chakula, basi chakula hicho tuweze kukipeleka maeneo yote yenye maafa.
Mheshimiwa Spika, pia kitengo hiki sasa tunakiboresha, tunaanza mazungumzo ndani ya Serikali kuifanya kuwa agency ambayo itakuwa inaratibu shughuli zote za maafa popote nchini, ambapo tutakuwa tunatengea fedha ziweze kutafuta maturubai au vibanda vya kujihifadhi kwa muda mfupi lakini pia kununua vyakula, madawa na mahitaji mengine ili yanapotokea tu maafa kama haya, basi kitengo chetu kiende mara moja.
Kwa sasa tumejiimarisha vizuri, maeneo yote yenye maafa tumeshayapitia na wataalam wetu wapo huko kwenye maafa ili kunusuru maisha ya Watanzania wenzetu ambao sasa wamepata mahangaiko kutokana na mvua nyingi ambazo zimenyesha.
Mheshimiwa Spika, pia tahadhari kwa wale wote ambao wako kwenye mabonde, narudia tena, nataka niwasihi Watanzania wote ambao wako kwenye maeneo hatarishi wapishe maeneo hayo, watafute maeneo mazuri. Viongozi wa Serikali za Vijiji, Kata na Wilaya wawasaidie Watanzania hao kuwapeleka maeneo sahihi ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza itakapotokeza mvua nyingi kunyesha tena ambazo zinaendelea kwa sasa.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa na mimi nimwulize Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni dhahiri kwamba wanafunzi hawatakiwi kufanya siasa Vyuoni, lakini kumekuwepo na ama mkakati au maelekezo ambapo Menejimenti ya Vyuo inawanyanyasa wanafunzi wanaokuwa hawapendezwi na siasa ya Chama cha Mapinduzi. Je, ni kweli kwamba kuna hayo maelekezo? Kama hakuna maelekezo, Serikali inazieleza nini sasa Menejimenti za Vyuo kuhusu hii tabia ambayo imejengeka ya kuwanyanyasa vijana na hata kuthubutu kuingilia Uongozi wa Serikali za Wanafunzi? Mojawapo ya Chuo ambacho kimekithiri ni Chuo Kikuu cha Dodoma.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo:-
Kwanza nataka nikanushe kwamba siyo kweli kwamba kuna maelekezo kwenye Vyuo vyote vya Elimu ya Juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, hakuna unyanyasaji wowote unaofanywa kwenye Vyuo kwa wanafunzi ambao...
Mheshimiwa Spika, narudia tena. Hakuna unyanyasaji wowote wa Vyuo...
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, Watanzania wote wanao uhuru wa kujiunga na vyama vyovyote wanavyovitaka, lakini kila eneo limeweka utaratibu wake. Hakuna zuio la wafanyakazi kujiunga na vyama vyovyote lakini liko zuio la mtumishi anapokuwa kazini kuendesha siasa. Hakuna zuio la mwanafunzi yeyote kama Mtanzania kujiunga na Chama anachokitaka yeye, lakini zuio ni kwamba hutakiwi kufanya siasa wakati wa masomo ili u-concentrate na masomo yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inaweza kutokea labda vijana wawili wenye itikadi tofauti huko wakafanya mambo yao, wakatofautiana huko, huo siyo utaratibu wa Serikali, ni utaratibu wao wao wenyewe. Kwa hiyo, nawaomba sana niwasihi Viongozi wa Vyama vya Siasa, tusilione hili kama ni msimamo wa Serikali, badala yake tulione hili kama ni mapenzi ya watu wengine, kama ambavyo vijana wafanyabiashara huko wanavyoweza kukorofishana mahali pao, lakini haina maana kwamba yule wa Chama Tawala anapokorofishana na mtu mwingine wa Chama cha Upinzani huko kwenye biashara zao tukasema labda soko lile, Chama Tawala kimepeleka watu wake kuzuia watu wa Vyama vingine wafanye vurugu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, niwasihi Watanzania wote; Tanzania hii ni yetu sote na tunahitaji maendeleo ya Watanzania wote. Kila mmoja anao uhuru wa kupenda Chama anachokitaka. Kama kuna maeneo yanabana kisheria na kwa utaratibu wa matumizi au matakwa hayo kuyapeleka maeneo hayo, lazima yazingatiwe. Serikali hii itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila kujali Vyama vyao; tutaendelea kuwahudumia Watanzania wote bila kujali Vyama vyao; pia tutatoa elimu kutoka ngazi ya awali mpaka elimu ya juu bila kujali mapenzi ya Chama chako. (Makofi)
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikusihi tu uamini bado kwamba Serikali hii haina jambo hilo wala haina maagizo hayo mahali pa kazi na uwe na amani. Nami nasema Watanzania hawa ni ndugu, wanaishi pamoja na bado tunapenda washiriki kikamilifu katika masomo yao. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali ya utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilitimiza malengo yake ya kusaidia kupigania uhuru nchi za Afrika na hivyo kupelekea nchi zote kupata uhuru; nchi hizo wakati zikiwa hapa zilijenga makambi ambayo yalitumika kwa ajili yao katika sehemu tofauti; na kwa kuwa makambi hayo yametumika baada ya kuondoka kama Vyuo na Sekondari na pia kufanya wao waendelee kukumbuka kwa yale ambayo tumeenzi:-
Ni lini Serikali sasa, itabadilisha makambi ya wapigania uhuru hawa ambayo yametumika kama Magereza na matumizi mengine yasiyofaa, ili waendelee kukumbuka sehemu ambazo walikaa kwa ajili ya kupigania uhuru wetu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la kwanza kabisa la Mheshimiwa Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba nchi yetu ilishiriki sana kuwakaribisha wapigania uhuru wa nchi mbalimbali, kuendesha harakati zao za kisiasa hapa nchini. Maeneo yote waliyokuwa wamekaa, waliweza kujenga miundombinu mbalimbali na yanatambulika kama makambi ya wapigania uhuru.
Katika kumbukumbu zangu, Morogoro kuna eneo linaitwa Dakawa ambalo sisi tunatumia kama Sekondari, lakini pia Mazimbu pale kwenye Compus ya SUA na maeneo mengine, nakumbuka kule Nachingwea kuna eneo la Matekwe na eneo lile lililotumika ni kama vile Pashule; na kuna eneo pale Msata, hapa jirani Chalinze pale ambako jeshi linatumia sana kama sehemu ya mazoezi. Pia kuna makambi mengine, nakumbuka nikiwa Naibu Waziri nilikuja kwako Kilolo, eneo moja kati ya maeneo ya makambi pale Kilolo ndiyo wanatumia kama Magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maeneo haya baada ya kuwa shughuli za wapigania uhuru kumaliza kazi zao, Serikali ilifanya maamuzi kutumia miundombinu ile kwa shughuli mbalimbali ikiwemo elimu. Eneo lingine kama hilo la Msata, Jeshi na pale Kilolo, Magereza. Maeneo hayo yote, kutokana na nature ya miundombinu iliyopo, maamuzi haya yalifanywa ili kutumia kwa umuhimu wa mahitaji ya nchi. Kwa hiyo basi, eneo kama Kilolo ambalo limetumika kama Magereza, suala la Magereza siyo suala la matumizi yasiyokuwa muhimu, ni muhimu pia kwa sababu ni sisi wenyewe ndio tunaenda kuishi pale na ni maeneo ya mafunzo, lakini pia ni eneo ambalo tunawahifadhi wale ambao wamepatikana na hatia kadhaa na kwenda kutunzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambako tumetumia miundombinu ile kwa shughuli nyingine nje ya elimu, basi napenda kutumia nafasi hii kuwasihi Halmashauri za Wilaya, pamoja na wananchi kujenga miundombinu mingine kwa ajili ya kutumia kwa matumizi ya elimu na haya maeneo mengine yanayotumika kwa elimu yataendelea kutumika kama ambavyo imepangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumbukumbu hizi sasa ukiangalia kwa sehemu kubwa, makambi yale yote yaliyotumika, mengi sana yanatumika ni kwa matumizi ya elimu zaidi na maeneo machache ndiyo kama hayo mawili niliyoyataja, kule Msata na Kilolo ndipo ambako yanatumika kwa Jeshi pamoja na Magereza. Yote haya ni mambo muhimu kwetu sisi, ni lazima tutumie miundombinu ile ili pia badala ya kuwa tumeyaacha tu, bora yatumike ili huduma mbalimbali ziweze kutolewa katika maeneo hayo.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini sasa nielekeze swali langu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza lengo lake la sera za fedha na sheria kwa kupeleka maendeleo vijijini na hasa kwa kuwapelekea fedha za miradi ya maendeleo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo, zinafika katika Halmashauri kwa wakati ili kuhakikisha wanatekeleza shughuli za maendeleo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka nia ya dhati ya kupeleka fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu, Wizara na Taasisi za Umma ili kufanya kazi za maendeleo. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, mwaka huu kupitia bajeti yetu hii ambayo sasa tunaendelea nayo, tumefanya mabadiliko makubwa ya kutenga na kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo kutoka asilimia 27 mpaka asilimia 40. Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba miradi yote ya maendeleo, yale yote ambayo tunahitaji yafanyiwe maboresho, yanatekelezwa kama ambavyo imekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mikakati kadhaa, moja ni kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato, lakini pia tunadhibiti mianya ya ukwepaji kodi ili kuweza kujiongezea pato zaidi, lakini kubwa zaidi ni kusimamia fedha hizi ambazo tunazipeleka kwenye Taasisi za Umma kwamba zinatumika kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali bado tunaendelea kuwataka watumishi, pindi fedha hizi zitakapokusanywa na baada ya Bunge hili, tutaanza kupeleka fedha kwenye mamlaka zetu za Serikali za Mitaa na Taasisi na Wizara. Nataka nitumie nafasi hii kuwaambia Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kupokea fedha na kusimamia matumizi, kuhakikisha kwamba fedha hii iliyotengwa inatumika kama ambavyo imekusudiwa; na kwamba hatutasita kuchukua hatua kali kwa yeyote ambaye atathibitika kupoteza fedha hizi nje ya matumizi ambayo tumeyakadiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni mkakati wetu pia kuhakikisha kwamba baada ya makusanyo tuzipeleke fedha zote. Wajibu mwingine ni kuhakikisha kwamba miradi inayotekelezwa inakuwa na thamani ya fedha iliyopelekwa kwa ajili ya matumizi ya maeneo hayo. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itasimamia jambo hili, lakini pia tushirikiane Wabunge wote, nyie pia ni Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani kwenye maeneo yenu. Kwa hiyo, tusaidiane tukishirikiana, mkakati wa Serikali wa kupeleka fedha kwa wakati na mkakati wa Serikali wa kutaka kuongeza fedha ili kupeleka kwenye maendeleo uweze kufikiwa na hatimaye Watanzania waweze kuiona tija.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ina sera nzuri, ina sheria mbalimbali juu ya elimu ambazo zinapelekea wanafunzi wa Kidato cha Nne waliofaulu, wanachaguliwa na kwenda Kidato cha Tano. Mara nyingi kwa maarufu wamesema huwa kunakuwa na selection.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna habari ambazo zinazagaa kwamba mwaka huu Serikali haitachukua wanafunzi kutokana na sababu ambazo bado hazijaeleweka. Sasa je, Mheshimiwa Waziri Mkuu, jambo hili lina ukweli gani? Kama lipo, Serikali inatoa kauli gani juu ya suala hilo?
imiwa Mbogo, Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nikanushe kwamba Serikali haina mpango wa kuwapanga vijana wetu waliomaliza Kidato cha Nne kwenda Kidato cha Tano. Najua tuna makundi mengi ya watu wanapenda kupotosha tu habari, ikiwemo na hii, lakini nataka nitumie nafasi hii kuwahakikishia wanafunzi wote waliomaliza Kidato cha Nne, wanaopaswa kwenda Kidato cha Tano, lakini na wazazi pia wa vijana wetu hawa kwamba Wizara ya TAMISEMI yenye dhamana na Sekondari, kwa pamoja na Wizara ya Elimu, kazi ya upangaji wa vijana wanaokwenda Kidato cha Tano inaendelea na wakati wowote ule mwishoni mwa mwezi huu majina hayo yatakuwa yametoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazofanywa sasa, nyie wote mnatambua kwamba mwaka uliopita wanafunzi hawa walikuwa wanapangwa kwa mfumo wa GPA na sasa tumebadilisha GPA kwenda division. Kwa hiyo, kazi ambayo Wizara ilikuwa inafanya ni kubadilisha ule mfumo wa GPA kwenda division ili uweze kuwapanga vizuri kwa division zao na sifa ambazo zinatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upangaji halikuwa ni kwa ajili ya Kidato cha Tano peke yake, kuna wale ambao tunawapeleka Vyuo kama Afya, Kilimo na maeneo mengine, nao pia wanatakiwa wapangwe kwa mfumo wa division na wote hao unapowapanga Kidato cha Tano, ili wengine waweze kupangwa, zoezi hili lazima lifanywe kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi hii inakamilika, itatoka muda mfupi ujao na kwa hiyo, baada ya hapo Serikali itatoa majibu haya wiki mbili kabla ili kuwawezesha wazazi kujipanga vizuri kuwapeleka vijana wao kwenye maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na kazi ya sensa ya kuhakikisha tuna shule ngapi za Kidato cha Tano ili tuweze kuwapeleka vijana wetu wote. Kwa sababu mwaka huu ufaulu ni mkubwa zaidi, kuliko mwaka jana, 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuhakikishe tunawapeleka vijana kulingana na uwezo wa shule ili tujue tumewapeleka wangapi na wanaobaki wangapi wenye stahili ya kwenda Kidato cha Tano ili nao wapate nafasi ya kupangiwa maeneo mengine kwa stahili ile ile ya Kidato cha Tano ili waziweze kupoteza ile stahili yao waliyokuwanayo ya Kidato cha Tano; kama vile kuwapeleka kwenye course za miaka mitatu za Diploma ambapo miaka miwili huitumia kwa ngazi ya Kidato cha Tano na cha Sita, wakishafaulu wanaingia kwa profession, kama ni afya, kama ni kilimo, kama ni sekta nyingine; kwa mfano Ualimu, ili waweze kuendelea na stahili yao ya Kidato cha Sita. Kwa hiyo, kazi hiyo itakapokamilika, tutaweza kutoa taarifa mapema.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, nami niweze kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali ambalo nimeona kuna umuhimu wa kuliuliza kwa sababu jana nilisikia ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Rais, lakini bado nimeendelea kupokea message kutoka kwa watu mbalimbali wakiuliza kuhusu swali hilo. Suala hilo ni kwamba, kumekuwepo na taarifa katika mitandao ya kijamii na mitaani kwamba Serikali imefuta ajira hali ambayo imesababisha tahamaki na taharuki miongozi mwa wahitimu mbalimbali waliokuwa wanatarajia kuajiriwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, taarifa hizo za mitandaoni na mitaani zinasema pia kwamba Serikali haitafanya tena promotion wala kupandisha madaraja, hali ambayo pia inawafanya Watumishi wa Umma kwa namna fulani morali yao kushuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kusikia ukweli halisi ni upi katika suala hili. Je, ni kweli kwamba Serikali haitaajiri tena? Ni kweli haitapandisha madaraja tena? Nakushukuru.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu swali la Mheshimiwa Mbogo, ni kwamba sasa hivi kuna watu wengi hupenda kusema maneno ambayo siyo sahihi na hili pia napenda nikanushe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana kwenye hotuba yake ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Benki Kuu, ametoa ufafanuzi mzuri sana. Nami nataka nitumie nafasi hii kurudia tu yale ambayo Mheshimiwa Rais ameyasema kwa kuwahakikishia Watumishi wa Umma na wale ambao wanatarajia kuajiriwa kwamba Serikali haijasitisha ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imesimamisha kwa muda kuajiri kwa sababu tunaendelea na zoezi la uhakiki wa watumishi hewa. Kazi hii ilishaanza, sasa hivi tunaikamilisha. Katika ukamilishaji huu, tunataka tujue sasa watumishi hewa ni akina nani kwa kila idara na kila sekta na watumishi walioko sasa kazini ni akina nani; ili tuweze kujua idadi ya watumishi waliobaki na pengo yaliyopo ndipo sasa tuweze kuajiri kwa ajili ya kusheheneza mahitaji ya watumishi kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali inafanya mapitio ya Miundo ya Utumishi kwa lengo la kuboresha. Tunaposema kuboresha, maana yake sasa tunataka tupate tija zaidi kwa watumishi. Kwa hiyo, naomba niwasihi Watumishi wote wa Umma kwamba zoezi hili halilengi kuwakandamiza watumishi; kazi hii hailengi kuathiri utumishi wao na madaraja yao, bali kuboresha watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie Watumishi wa Umma kwamba Serikali hii inawapenda sana na inajali mchango mkubwa ambao watumishi mnautoa kwa Serikali hii. Ili tuweze kufanya kazi kwa motisha, Serikali hii imeona ni muhimu sasa kuboresha zaidi miundo mbalimbali na maslahi mbalimbali, lakini pia kuona idadi ya watumshi tuweze kutumia fedha inayotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka muwe na amani kwamba kazi hii inayoendelea ni ya muda mfupi sana. Itakapokamilika, ajira zote ikiwemo na elimu, afya, majeshi, ambazo pia zilikuwa tayari zianze karibuni, zote zitarudishwa na watu watapelekwa kwenye vituo vya kazi kwenda kuanza kazi zao na madaraja mapya yatakuwa yameshatolewa.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, Sera na Mifumo ya Kisheria tuliyonayo sasa inaruhusu kuwaenzi waasisi pamoja na viongozi wa n hi hii, lakini siku za hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu, imejidhihirisha wazi kwamba baadhi ya viongozi wameingia katika dimbwi la wizi, ubadhirifu wa mali za Umma na ukiukwaji wa maadili:-
Je, ni lini Serikali itafanya mapitio ya Sera, Sheria na kubadilisha mifumo ili sasa wale wezi wote waweze kuchukuliwa hatua kali za Kisheria na watakaobainika hivyo dhidi ya ukiukwaji wa maadili ya nchi hii? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kudhibiti vitendo vya wizi, kukosa uadilifu, kukosa uaminifu mahali pa kazi na Watumishi wa Sekta ya Umma. Serikali inafanya hilo bila kujali ngazi ya mtumishi huyo, awe ni kiongozi wa ngazi ya juu, wa kati, hata wale watumishi wa kawaida, ilimradi Serikali imetoa dhamana ya kuwatumikia Watanzania, tunatarajia kila mtumishi atakuwa mwadilifu, mwaminifu, lakini pia atakuwa mchapakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaokiuka, dhidi ya wale wote ambao hawatumii vizuri madaraka yao, dhidi ya wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa popote pale nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ametaka kuona ni hatua gani zinachukuliwa; kwanza, tunaendelea kutoa elimu kwa watumishi ya kwamba kila mtumishi anatakiwa kufuata maadili ya utumishi, ikiwemo na uaminifu, uadilifu na uchapakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali inaendelea kuboresha kwa kuunda; na tumeshaunda Taasisi ya Utumishi wa Umma, Taasisi ya Maadili ya Watumishi ambayo yenyewe inajiridhisha kwamba kila mtumishi anatangaza mali zake na kuendelea kufuatilia mara kwa mara mabadiliko ya mali hizo ili tuone kama mali hizo amezipata kwa utumishi wake huu alionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Serikali imeendelea kuimarisha taasisi mbalimbali ikiwemo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo pia inafuatilia maeneo yote; kwa Watumishi wa Umma na hata raia wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafanya mapitio ya lile jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema la Sera yetu na Sheria, Kanuni ili ziweze kuendana na mabadiliko ya wakati. Hii pia, ili kuisaidia Serikali kudhibiti tabia hii, sasa Serikali kupitia Bunge hili, siku mbili tatu zijazo mtapitisha Muswada wa kuanzisha Division ya Mahakama ya Mafisadi ili kuweza kupambana nao kwa lengo la kudhibiti vitendo vya Watumishi wa Umma wenye tabia ya kuiba fedha mahali pa kazi, lakini wale wenye vitendo vya ufisadi ili wote hao waweze kuchukuliwa hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa mbinu hizi, kwa njia hizi zote, tutaweza kuwa na Watumishi wa Umma wenye maadili mema na wenye kutumia madaraka yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, malengo yetu Serikali ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanahudumiwa vizuri na Watanzania wawe na uhakika na Watumishi waliopo kwa kutekeleza wajibu wao kwa Watanzania wote bila kuwa na vitendo ambavyo vinaweza kuathiri utendaji wa kila siku.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Waziri Mkuu, nami nichukue nafasi hii kukupongeza wewe na Serikali yako kwa kazi nzuri mnayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, viwango vya VAT sasa hivi Tanzania ni 18% na viwango hivi havitofautishi biashara, kati ya katikati, kubwa na za chini. Je, Serikali haioni sasa ikipunguza viwango vya VAT kwa biashara za chini, compliance ya watu wa biashara za chini, wengi wataweza kulipa VAT hii kwa kiwango cha chini na kuiongezea mapato Serikali kwa kiwango kikubwa sana. Naomba kujua kama Serikali inaweza ikapokea ushauri huu na kulifanyia kazi na kuhakikisha kila mtu alipe VAT kwa kiwango cha shughuli ya biashara anayofanya.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukienda Super Market sasa hivi ukinunua chochote, unalipa 18%. Kwa hiyo, inaongezea mzigo kwa wale wachache ambao wanalipa kodi hii, lakini kodi hii ikishushwa kwa viwango, 18, 14, 10 na labda na tano itafanya compliance ya wananchi wote ambao wanafanya biashara waweze kulipa kodi hii na Serikali kujiongezea mapato. Naomba majibu yako Mheshimiwa Waziri Mkuu.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala, kama ifuatavyo:-
Swali hili, pia nimewahi kupata bahati ya kukaa na wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuwatia moyo wa kufanya biashara zao zaidi.
Moja kati ya mambo ambayo yalijitokeza kwenye vikao vile ni mjadala ambao leo umeuliza swali linalofanana sana kama ambavyo walikuwa wameomba. Pia tuliweza kuwaeleza wafanyabiashara na naomba nijibu swali lako kama ambavyo tuliweza kujibu, kwamba, VAT ya 18% mara nyingi huwa inatozwa kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara kuanzia milioni arobani na kuendelea kwa mwaka au wanaopata pato la milioni kumi ndani ya miezi mitatu na miezi minne. Chini ya hapo hawausiki na VAT.
Mbili, kuruhusu biashara zote za aina zote zile kutoza 18%, kuna matatizo mengi. Moja, ni ngumu sana kumwacha Afisa wetu wa TRA kwenda kutoza VAT kulingana na biashara aliyonayo hasa kwa sababu ni ngumu pia kiutawala katika kutambua thamani ya jambo hilo, halafu pia, menejimenti yake inakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Spika, pia unaweza kutengeneza mianya ya rushwa ya wale watendaji wetu wanapofanyakazi ya kufanya tathimini ya biashara hizi za aina mbalimbali, lakini unapoweka 18%, wewe unaangalia tu pato lake la jumla kwa mwaka au kwa miezi mitatu, unafanya calculation ya 18%, kuliko kuanza kupitia biashara yenyewe ukubwa wake, unapata shilingi ngapi kwa mwezi, inakuwa ngumu sana.
Kwa hiyo, tumefanya study maeneo mengi na nchi mbalimbali tumegundua kwamba, njia nzuri ni ya kuweka flat rate, kwa biashara hasa kuanzia ile milioni arobaini kwa mwaka na milioni kumi kwa miezi mitatu, minne; inakuwa rahisi zaidi, hata menejimenti yake pia inakuwa ni nzuri.
Kwa hiyo, tumegundua kwamba jambo hili linaweza likasumbua hata wafanyabiashara, linaweza likawasumbua pia hata watendaji wetu wa TRA. Kwa hiyo, tunaendelea kukutana na wafanyabiashara, kupeana mawazo zaidi, lakini jambo hili sasa linahitaji utafiti wa kina, tutakapokuja kufanikiwa, tunaweza pia tukalitambulisha, lakini kwa kuwa tumejifunza pia na nchi za jirani jambo hili lina matatizo haya ambayo nimeyaeleza.
MHE. FREEMAN A. MBOWE:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu maswali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu unatambua kwamba sasa hivi nchi ina uhaba mkubwa wa sukari. uhaba huu wa sukari umesababishwa na amri iliyotolewa na Mheshimiwa Rais mwezi Februari mwaka huu ya kuzuia uagizaji wa sukari bila kufuata utaratibu ama kufanya utafiti wa kutosha kuhusiana na tatizo zima ama biashara nzima ya uagizaji na usambazaji wa sukari katika Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunatambua kwamba nchi yetu inazalisha takribani wastani wa tani milioni 300 na zaidi ya tani 180 hivi zinaagizwa kutoka nchi za nje na sasa hivi wewe mwenyewe umetoa kauli kwamba Serikali imeagiza sukari.
Sasa swali langu ni hili; maadam sukari ina utaratibu maalum wa uagizaji ambao unasimamiwa na Sheria ya Sukari ya mwaka nafikiri Sugar Industry Act ya mwaka 2001 na kwamba Bodi ya Sukari inatoa utaratibu maalum wa uagizaji wa sukari hii na biashara ya uagizaji sukari sio tu uagizaji kwa sababu ya fedha ni pamoja na muda maalum, circle maalum wakati gani agizo hili isingane na uzalishaji katika viwanda vya ndani ambavyo Mheshimiwa Rais alidai alikuwa na
nia ya kuvilinda ambalo ni jambo jema.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa unaweza ukatuambia hiyo sukari uliyoagiza umeiagiza kwa utaratibu gani? Anaiagiza nani? Inategemewa kufika lini? Ni kiasi gani? Na itakapofika haitagongana na uzalishaji katika viwanda vyetu local baada ya kuisha kwa msimu wa mvua na hivyo kusababisha tatizo la sukari kwa mwaka mzima ujao?
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbowe, Mbunge wa Hai na Kiongozi wetu wa Kambi ya Upinzani kwa kuuliza swali hili kwa sababu tulitaka tutumie nafasi hii kuwaondoa mashaka Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wakati wote anapotoa tamko ni kutokana na mwelekeo na mpango wa Serikali ambao umepangwa kwa lengo maalum. Sukari nchini ni k
weli kwamba inaratibiwa na Bodi ya Sukari ambayo pia imewekwa kisheria na moja kati ya majukumu yao kufanya utafiti, lakini pia kusimamia viwanda vinavyozalisha kwa lengo la kusambaza sukari nchini na iweze kutosha.
Mheshimwia Spika, kwa miaka mitatu, minne ya nyuma, sukari imekuwa ikiletwa kwa utaratibu ambao baadaye tuligundua kwamba unavuruga mwenendo wa viwanda vya ndani na viwanda vya ndani havipati tija. Kwa hiyo, Serikali hii ilipoingia madarakani moja kati ya mikakati yake ni kuhahakikisha kwamba viwanda vya ndani vinalindwa, unavilindaje? Ni pale ambako sasa sukari inayoingia ndani lazima idhibitiwe lakini pia kuhamasisha viwanda hivyo kuzalisha zaidi sukari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000. Sukari ambayo inazalishwa nchini ni tani 320,000 na upungufu ni kama 100,000 hivi. Tani 100,000 hii kama hatuwezi kuiagiza kwa utaratibu na udhibiti mzuri kunaweza kuingia kwa sukari nyingi sana kwa sababu kwenye sukari tuna sukari za aina mbili, sukari ya mezani ile ambayo tunaitumia kwenye chai na sukari ya viwandani na haina utofauti mkubwa sana kwa kuingalia na sukari ya viwandani na ya
mezani ni rahisi sana kwa mwagizaji kama hatuwezi kudhibiti vizuri unaweza kuleta sukari nyingi ya mezani halafu kukajaa sokoni.Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kauli ya Mheshimiwa Rais ni katika mpango wa kulinda viwanda vya ndani kama ambavyo umekiri, lakini jukumu la Bodi sasa ya Sukari baada ya kauli ile inatakiwa sasa iratibu vizuri. Kwa hiyo, sukari imeratibiwa vizuri na bodi ya sukari na mahitaji ya sukari ile ya tani 100,000 na
mahitaji ya sukari ambayo inatakiwa kuingia ili isivuruge uzalishaji ujao ni kazi ambayo inafanywa Bodi ya Sukari.
MHE. SAUMU H. SAKALA:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, katika nchi yetu kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara wa mazao kuwalazimisha wakulima kufunga mazao yao kwa mtindo wa lumbesa jambo ambalo licha tu ya kumdidimiza mkulima huyu na kumnyanyasa lakini pia linaifanya Serikali inakosa mapato.Mheshimiwa Spika, sasa ni nini kauli ya Serikali juu ya suala hili ambalo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu sasa licha ya makemeo mbalimbali yaliyokuwa yanatokea?
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saumu, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli wako wafanyabiashara hasa wa mazao wamekuwa na tabia ya kuwalazimisha wakulima kununua kwa gunia lililofungwa kwa mtindo wa kuwekwa kile kichuguu maarufu lumbesa, kwanza hilo ni kosa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeshatoa maelekezo kupitia Wakala wa Vipimo ambao ni wasimamizi wakuu wa kuhakikisha kwamba biashara yote ya mazao ya kilimo nchini yanauzwa kwa vipimo vya kilo na siyo kwa kufunga gunia likawa lumbesa. Lakini pia kwa mazingira ya vijijini ambako hakuna mizani imejitokeza sana hilo Mheshimiwa Mbunge la kwamba watu wanafunga gunia mpaka lumbesa ndiyo inakuwa kama gunia moja. Lakini gunia letu sisi limepimwa limeshonwa viwandani kwa vipimo sahihi na lazima lishonwe kwa uzi
juu ndiyo linakuwa gunia na wala siyo ile lumbesa.
Mheshimiwa Spika, sasa jukumu la Serikali ni kuendelea kusimamia na mimi nataka nitoe wito tena kwa Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Halmashauri zao za Wilaya na Maafisa Biashara walioko kwenye Halmashauri hizo kusimamia kwamba biashara hii haiwanyonyi wakulima wadogo wanaouza mazao ya mahindi, vitunguu, viazi na kitu kingine kwa kufunga magunia kwa njia ya lumbesa. Jambo hili wala siwaachii Wakuu wa Wilaya peke yao nawaagiza pia Wakuu wa Mikoa kupitia Kamati zao za Ulinzi na Usalama kwenye Mikoa, zisimamie agizo ambalo lilishatolewa na Serikali na leo
Mheshimiwa Mbunge umeliuliza inawezekana mambo hayo bado yanafanyika huko na Serikali isingependa ione mnunuzi anakwenda kununua kwa mkulima na kumlazimisha amfungashie kwa lumbesa halafu anunue kwa bei ndogo ya gunia na lumbesa siyo gunia kwa sababu gunia ni lile limeshonwa kiwandani, lina vipimo na linahitaji kushonwa pale juu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikiri kwamba wako Wafanyabiashara wajanja wajanja na sisi Serikali tuko macho na sasa kupitia agizo hili kwa wafanyabiashara kwenye Halmashauri za Wilaya na maeneo yote lakini pia lishuke mpaka chini kwa Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata pale ambapo kuna biashara ya mazao kwenye maeneo
yao, waendelee kudhibiti kwamba ufungashaji wa mizigo hiyo na ununuzi haununui kwa kigezo cha lumbesa badala yake ununue kwa vigezo vya kilogram au kwa gunia ambalo ni
rasmi kutoka viwandani . (Makofi
MHE. HASSAN S. KAUNJE:
Mheshimiwa Spika, nishukuru kupata nafasi ya kuuliza swali la moja kwa moja kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza tunafahamu kwamba maji ni uhai na Sera ya Taifa ya Maji inahitaji kila mwananchi kuweza kuyafikia maji ndani ya umbali wa mita 25. Je, Serikali ya Awamu ya Tano imejipangaje kuhakikisha maji haya yanawafikia wananchi especially
wananchi wa Mkoa wa Lindi ambao wanatatizo kubwa sana la maji?
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini kama ifuatavyo:-
Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kaunje, amekuwa anafuatilia sana mwenendo wa maji na hasa alipoweka kule mwishoni hasa wananchi wa Mkoa wa Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Sera ya Maji nchini imetamka wazi kwamba Serikali itasambaza maji kwa wananchi wake kote nchini mpaka ngazi za vijiji tena kwa umbali usiozidi mita 400 hiyo ndiyo sera na wakati wowote Wizara ya Maji inapofanya kazi yake inafanya kazi kuhakikisha kwamba sera hiyo inakamilika. Iko mipango mbalimbali na nadhani Wizara ya Maji itakuja na bajeti hapa ikiomba ridhaa yenu muipitishe Waheshimiwa Wabunge ili tukaendelee kutekeleza hiyo sera ya kusambaza maji, na mikakati yetu sisi, maji
lazima yawe yamefika kwenye ngazi za vijiji kwa asilimia mia moja ifikapo mwaka 2025 na ikiwezekana kufikia mwaka 2020 hapa kwa zaidi ya asilimia tisini huo ndiyo mkakati wetu. Mkakati huu utatokana tu kama tutaendelea kupata fedha nyingi Serikalini na kuzipeleka Wizara ya Maji ili Wizara ya Maji waendelee na mkakati ambao wanao.
Kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa malengo haya tunakusudia kusambaza maji kwenye maeneo yote ya vijiji na maeneo ya miji ili wananchi wetu waweze kupata tija ya maji kwenye maeneo haya. Kwa miradi ambayo ipo, ambayo imeelezwa kwamba ipo inaendelea kutekelezwa, tunaamini miradi hiyo kwa watu wote ambao tumewapa kazi hiyo wataendelea kutekeleza kadri ambavyo tunawalipa fedha zao ili waweze kukamilisha.
Waliokamilisha wakamilishe miradi ambao hawajakamilisha tunaendelea kuwapelekea fedha ili waweze kukamilisha ili maji yaweze kutolewa na kila mwananchi aweze kunufaika na sera hiyo ya Serikali.
MHE. LUCY S. MAGERELI:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la moja kwa moja kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu , Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano ni kuipeleka Tanzania kuwa Tanzania ya viwanda na ziko changamoto zinazokabli mpango huo na moja ni namna ya kuwawezesha wazalishaji na wafungashaji wadogo katika level za Halmashauri kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Tunafahamu uwepo wa GS1 ambayo inalengo la kuwasaidia wazalishaji na wafungashaji hao kupata barcodes ili waweze kuuza bidhaa zao. Mwaka jana Waziri Mheshimiwa Mizengo Pinda alitoa maelekezo ya maandishi akielekeza TAMISEMI iagize halmashauri zote zitoe
ushirikiano kwa GS1 ili waweze kuwasaidia hao wazalishaji na wafungashaji wadogo kupata barcodes kitu ambacho kinge-stimulate uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo...
SPIKA:
Mheshimiwa Lucy sasa swali.
MHE. LUCY S. MAGERELI:
Mheshimiwa Spika ahsante, ningetemani nimalizie, anyway.
Nini sasa Kauli ya Serikali hasa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu katika kusimamia na kutekeleza maelekezo haya ambayo tayari yalishatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu aliyepita ili kuwasaidia wazalishaji na wafungashaji wadogo hawa?
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Ni kweli kwamba Serikali inayo mkakati, tunaendelea kuhamasisha wajasiriamali wadogo kujiendeleza kupitia viwanda vidogo vidogo na msisitizo huu wa Serikali wa viwanda unajumuisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo kwa lengo lile lile la kumtaka Mtanzania aweze kunufaika na hasa katika kuongeza thamani ya mazao ambayo tunayazalisha nchini.
Tumeendelea kuwa na mipango mbalimbali ambayo Serikali inaunga mkono jitihada za wazalishaji wadogo ikiwemo na uwekaji wa barcodes ambayo pia inamsaidia kupata bei na thamani nzuri ya mazao ambayo mjasiriamali anajihusisha katika kuchakata kwenye michakato ya awali kwa maana processing hii ya awali.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu bado unaendelea na tumeagiza utaratibu huu wa
barcodes uendelee lakini pia tumehusisha TBS, TFDA kuhakikisha kwamba chakula tunachokizalisha kinakuwa na ubora ili tukikipa barcode, Taifa liweze kuuza bidhaa hiyo nje ya nchi na ndani ya nchi ambako tunaweza kupata fedha nyingi na wajasiriamali waweze kunufaika zaidi.
Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie tu kwamba utaratibu huo bado unaendelea ili kuweza kuipa thamani mazo yetu lakini kuwapa uwezo mkubwa wa kusafirisha bidhaa zao nje na kuzipa soko ili ziweze kuwaletea tija Watanzania na tutaendelea pia kusimamia jambo hilo kuwa linaendelea kukamilika. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. MAHAWE:
Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, sera ya elimu ya nchi yetu sasa inasema ni kupata elimu bure lakini hii bure ina maana inalipiwa na Serikali. Lakini kumekuwa na kundi dogo la wazazi wengine ambao kwa kuchangia kupitia kodi zao ndizo ambazo zinatumika kusomesha watoto wao ama kugharamia elimu lakini kundi hili limekuwa likilipa kodi zote zinazotakiwa kulipwa lakini wamekuwa wakichajiwa mara mbili (double taxation) kupitia watoa huduma wa elimu katika taasisi binafsi.
Je, nini kauli ya Serikali ili kwamba na hawa wananchi amba tayari walikwisha kulipa kodi na kuchangia elimu bure na wenyewe waweze kufurahia keki hii ya elimu bure? (Makofi)
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo umesema, kwamba swali limechanganywa sana haliko wazi mno na haya ni maswali ya papo kwa papo inatakiwa liwe-clear ili na mimi niweze kujibu kitu halisi ili pia naye aweze kunufaika na majibu lakini pia Watanzania ambao wanasikia kipindi hiki waweze kujua jambo gani limeulizwa na jambo gani ambalo linatakiwa kujibiwa.
Lakini pia, amezungumzia suala la elimu bure na ni jambo ambalo watu wengi limekuwa likiwachanganya na wengine kupotosha, naomba nitoe ufafanuzi huu ufuatao ili Watanzania wajue kwamba elimu bure ni mkakati unaolenga Kurugenzi ya Msingi na Sekondari na hasa katika kuwapunguzia mzigo wazazi wa kuchangia changia michango mbalimbali shuleni.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumeanza na maeneo ambayo tumeona wazazi walikuwa wanakwazwa sana. Tumezungumza mara kadhaa lakini narudia kwamba moja kati ya maeneo hayo tumeondoa yakle malipo yaliyokuwa yanaitwa ada kwa sekondari, shilingi 20,000 na shilingi 70,000. Pia kulikuwa na michango ya ulinzi, maji, umeme pale shuleni michango ile yote ile sasa Serikali imetenga fungu kwa ajili ya kuipa shule ili iweze kulipia gharama hizo, lakini suala la mitihani mbalimbali nayo pia ni eneo Serikali imeamua kulichukua kwa sababu gharama za mitihani zitafanywa na Serikali ili wazazi
wasiingie kwenye michango hiyo.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tunaendelea kuona ni maeneo gani mengine ambayo wazazi yanawakwaza zaidi katika kuchangia, sasa kama kuna mzazi anachangia huku nje hata kama analipa kodi maeneo mengine, ni jukumu tu la kuona kwamba kuna umuhimu wa kuchangia sekta ya elimu na kwamba yeye kama Mtanzania anayo nafasi ya kuchangia mahali popote bila kujali kama mchango huo pia unagusa kodi ambazo alikuwa anazilipa kule awali.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, tutoe wito kwa Watanzania, kwanza tupe subira Serikali kuona maeneo mengine zaidi ambayo tunaweza tukaboresha ili kumpunguzia mzazi mzigo wa kuweza kusomesha watoto hawa.
Sasa lawama inakuja pale ambako tumetoa nafasi hizi tumegundua kwamba kuna watoto wengi wa Kitanzania walikuwa hawapelekwi shuleni na kwa kuondoa hizi gharama, gharama watoto wengi wanapelekwa shule na sasa tumeanza kuona uzoefu wa kwamba watoto wengi wameendelea kusajiliwa shuleni, idadi imekuwa kubwa na kumekuwa na changamoto nyingine kama madawati na vyumba vya madarasa.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishi e Watanzania, kwamba Serikali inaendelea kuweka utaratibu wake kwa ajili ya kuongeza madawati lakini pia miundombinu ya vyumba vya madarasa ili watoto wetu ambao sasa tumebaini kuwa wamekuwa wengi waweze kupata mahali pa kukaa na chumba ambacho wanaweza kupata taaluma yao. Lakini hatuzuii mlipakodi yeyote wa sekta nyingine kuchangia kujenga madarasa kwa haraka ili watoto wetu waingie ndani, kutoa madawati kama ambavyo tumeona Watanzania wengi
wamejitokeza, makampuni mengi yanachangia lakini pia hata baadhi ya Wabunge tumeona mkitoa mchango wenu, na mimi nataka nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Wabunge ambao pia mmeanza kuunga mkono jitihada za Serikali kuchangia madawati. Jambo hili ni letu sote, watoto ni wetu sote hebu twende pamoja, tutoe elimu hiyo ya kuchangia kwa namna mtu anavyoweza kwenye madawati, kama una uwezo wa kujenga chumba cha darasa ili watoto wetu waweze kusoma ndani, lakini Serikali inaendelea na mkakati pia
wa ujenzi wa maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ningependa nitamke hili ili wale wote wanaodhani kulundikana kwa watoto sasa ni jambo la makusudi, hapana, ni jambo ambalo tuliona ni muhimu tupunguze michango, lakini Wazazi ambao walikuwa wanashindwa kuleta watoto nao wapate kupeleka watoto, wamepeleka watoto wengi ni jukumu letu sasa kujenga vyumba na kupeleka madawati. (Makofi
MHE. VENANCE M. MWAMOTO:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali ya utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilitimiza malengo yake ya kusaidia kupigania uhuru nchi za Afrika na hivyo kupelekea nchi zote kupata uhuru; nchi hizo wakati zikiwa hapa zilijenga makambi ambayo yalitumika kwa ajili yao katika sehemu tofauti; na kwa kuwa makambi hayo yametumika baada ya kuondoka kama Vyuo na Sekondari na pia kufanya wao waendelee kukumbuka kwa yale ambayo tumeenzi:-
Ni lini Serikali sasa, itabadilisha makambi ya wapigania uhuru hawa ambayo yametumika kama Magereza na matumizi mengine yasiyofaa, ili waendelee kukumbuka sehemu ambazo walikaa kwa ajili ya kupigania uhuru wetu?
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la kwanza kabisa la Mheshimiwa Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba nchi yetu ilishiriki sana kuwakaribisha wapigania uhuru wa nchi mbalimbali, kuendesha harakati zao za kisiasa hapa nchini. Maeneo yote waliyokuwa wamekaa, waliweza kujenga miundombinu mbalimbali na yanatambulika kama makambi ya wapigania uhuru.
Katika kumbukumbu zangu, Morogoro kuna eneo linaitwa Dakawa ambalo sisi tunatumia kama Sekondari, lakini pia Mazimbu pale kwenye Compus ya SUA na maeneo mengine, nakumbuka kule Nachingwea kuna eneo la Matekwe na eneo lile lililotumika ni kama vile Pashule; na kuna eneo pale Msata, hapa jirani Chalinze pale ambako jeshi linatumia sana kama sehemu ya mazoezi. Pia kuna makambi mengine, nakumbuka nikiwa Naibu Waziri nilikuja kwako Kilolo, eneo moja kati ya maeneo ya makambi pale Kilolo ndiyo wanatumia kama Magereza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maeneo haya baada ya kuwa shughuli za wapigania uhuru kumaliza kazi zao, Serikali ilifanya maamuzi kutumia miundombinu ile kwa shughuli mbalimbali ikiwemo elimu. Eneo lingine kama hilo la Msata, Jeshi na pale Kilolo, Magereza. Maeneo hayo yote, kutokana na nature ya miundombinu iliyopo, maamuzi haya yalifanywa ili kutumia kwa umuhimu wa mahitaji ya nchi. Kwa hiyo basi, eneo kama Kilolo ambalo
limetumika kama Magereza, suala la Magereza siyo suala la matumizi yasiyokuwa muhimu, ni muhimu pia kwa sababu ni sisi wenyewe ndio tunaenda kuishi pale na ni maeneo ya mafunzo, lakini pia ni eneo ambalo tunawahifadhi wale ambao wamepatikana na hatia kadhaa na kwenda kutunzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambako tumetumia miundombinu ile kwa shughuli nyingine nje ya elimu, basi napenda kutumia nafasi hii kuwasihi Halmashauri za Wilaya, pamoja na wananchi kujenga miundombinu mingine kwa ajili ya kutumia kwa matumizi ya elimu na haya maeneo mengine yanayotumika kwa elimu yataendelea kutumika kama ambavyo imepangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumbukumbu hizi sasa ukiangalia kwa sehemu kubwa, makambi yale yote yaliyotumika, mengi sana yanatumika ni kwa matumizi ya elimu zaidi na maeneo machache ndiyo kama hayo mawili niliyoyataja, kule Msata na Kilolo ndipo ambako yanatumika kwa Jeshi pamoja na Magereza. Yote haya ni mambo muhimu kwetu sisi, ni lazima tutumie miundombinu ile ili pia badala ya kuwa tumeyaacha tu, bora yatumike ili huduma mbalimbali ziweze kutolewa katika maeneo hayo.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini sasa nielekeze swali langu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa Serikali inatekeleza lengo lake la sera za fedha na sheria kwa kupeleka maendeleo vijijini na hasa kwa kuwapelekea fedha za miradi ya maendeleo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo, zinafika katika Halmashauri kwa wakati ili kuhakikisha wanatekeleza shughuli za maendeleo?
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka nia ya dhati ya kupeleka fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu, Wizara na Taasisi za Umma ili kufanya kazi za maendeleo. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, mwaka huu kupitia bajeti yetu hii ambayo sasa tunaendelea nayo, tumefanya mabadiliko makubwa ya kutenga na kuongeza kiwango cha fedha za maendeleo kutoka asilimia 27 mpaka asilimia 40.
Malengo yetu ni kuhakikisha kwamba miradi yote ya maendeleo, yale yote ambayo tunahitaji yafanyiwe maboresho, yanatekelezwa kama ambavyo imekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mikakati kadhaa, moja ni kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato, lakini pia tunadhibiti mianya ya ukwepaji kodi ili kuweza kujiongezea pato zaidi, lakini kubwa zaidi ni kusimamia fedha hizi ambazo tunazipeleka kwenye Taasisi za Umma kwamba zinatumika kama ilivyokusudiwa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali bado tunaendelea kuwataka watumishi, pindi fedha hizi zitakapokusanywa na baada ya Bunge hili, tutaanza kupeleka fedha kwenye mamlaka zetu za Serikali za Mitaa na Taasisi na Wizara.
Nataka nitumie nafasi hii kuwaambia Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kupokea fedha na kusimamia matumizi, kuhakikisha kwamba fedha hii iliyotengwa inatumika kama ambavyo imekusudiwa; na kwamba hatutasita kuchukua hatua kali kwa yeyote ambaye atathibitika kupoteza fedha hizi nje ya matumizi ambayo tumeyakadiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni mkakati wetu pia kuhakikisha kwamba baada ya makusanyo tuzipeleke fedha zote. Wajibu mwingine ni kuhakikisha kwamba miradi inayotekelezwa inakuwa na thamani ya fedha iliyopelekwa kwa ajili ya matumizi ya maeneo hayo. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itasimamia jambo hili, lakini pia tushirikiane Wabunge wote, nyie pia ni Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani kwenye maeneo yenu. Kwa hiyo, tusaidiane tukishirikiana, mkakati wa Serikali wa kupeleka fedha kwa wakati na mkakati wa Serikali wa kutaka
kuongeza fedha ili kupeleka kwenye maendeleo uweze kufikiwa na hatimaye Watanzania waweze kuiona tija.
MHE. RICHARD P. MBOGO:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ina sera nzuri, ina sheria mbalimbali juu ya elimu ambazo zinapelekea wanafunzi wa Kidato cha Nne waliofaulu, wanachaguliwa na kwenda Kidato cha Tano. Mara nyingi kwa maarufu
wamesema huwa kunakuwa na selection.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna habari ambazo zinazagaa kwamba mwaka huu Serikali haitachukua wanafunzi kutokana na sababu ambazo bado hazijaeleweka. Sasa je, Mheshimiwa Waziri Mkuu, jambo hili lina ukweli gani? Kama lipo, Serikali inatoa kauli gani juu ya suala hilo?
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbogo, Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nikanushe kwamba Serikali haina mpango wa kuwapanga vijana wetu waliomaliza Kidato cha Nne kwenda Kidato cha Tano. Najua tuna makundi mengi ya watu wanapenda kupotosha tu habari, ikiwemo na hii, lakin
i nataka nitumie nafasi hii kuwahakikishia wanafunzi wote waliomaliza Kidato cha Nne, wanaopaswa kwenda Kidato cha Tano, lakini na wazazi pia wa vijana wetu hawa kwamba Wizara ya TAMISEMI yenye dhamana na Sekondari, kwa pamoja na Wizara ya
Elimu, kazi ya upangaji wa vijana wanaokwenda Kidato cha Tano inaendelea na wakati wowote ule mwishoni mwa mwezi huu majina hayo yatakuwa yametoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazofanywa sasa, nyie wote mnatambua kwamba mwaka uliopita wanafunzi hawa walikuwa wanapangwa kwa mfumo wa GPA na sasa tumebadilisha
GPA kwenda division. Kwa hiyo, kazi ambayo Wizara ilikuwa inafanya ni kubadilisha ule mfumo wa GPA kwenda division ili uweze kuwapanga vizuri kwa division zao na sifa ambazo zinatakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upangaji halikuwa ni kwa ajili ya Kidato cha Tano peke yake, kuna wale ambao tunawapeleka Vyuo kama Afya, Kilimo na maeneo mengine, nao pia wanatakiwa wapangwe kwa mfumo wa division na wote hao unapowapanga Kidato cha Tano, ili wengine waweze kupangwa, zoezi hili lazima lifanywe kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi hii inakamilika, itatoka muda mfupi ujao na kwa hiyo, baada ya hapo Serikali itatoa majibu haya wiki mbili kabla ili kuwawezesha wazazi kujipanga vizuri kuwapeleka vijana wao kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na kazi ya sensa ya kuhakikisha tuna shule ngapi za Kidato cha Tano ili tuweze kuwapeleka vijana wetu wote.
Kwa sababu mwaka huu ufaulu ni mkubwa zaidi, kuliko mwaka jana, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuhakikishe tunawapeleka vijana kulingana na uwezo wa shule ili tujue tumewapeleka wangapi na wanaobaki wangapi wenye stahili ya kwenda Kidato cha Tano ili nao wapate nafasi ya kupangiwa maeneo mengine kwa stahili ile ile ya Kidato cha Tano ili waziweze kupoteza ile stahili yao waliyokuwanayo ya Kidato cha Tano; kama vile kuwapeleka kwenye course za miaka mitatu za Diploma ambapo miaka miwili huitumia kwa ngazi ya Kidato cha Tano na cha Sita, wakishafaulu
wanaingia kwa profession, kama ni afya, kama ni kilimo, kama ni sekta nyingine; kwa mfano Ualimu, ili waweze kuendelea na stahili yao ya Kidato cha Sita. Kwa hiyo, kazi hiyo itakapokamilika, tutaweza kutoa taarifa mapema.
MHE. COSATO D. CHUMI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, nami niweze kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali ambalo nimeona kuna umuhimu wa kuliuliza kwa sababu jana nilisikia ufafanuzi kutoka kwa Mheshimiwa Rais, lakini bado nimeendelea kupokea
message kutoka kwa watu mbalimbali wakiuliza kuhusu swali hilo. Suala hilo ni kwamba, kumekuwepo na taarifa katika mitandao ya kijamii na mitaani kwamba Serikali imefuta ajira hali ambayo imesababisha tahamaki na taharuki miongozi mwa wahitimu mbalimbali waliokuwa wanatarajia kuajiriwa na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, taarifa hizo za mitandaoni na mitaani zinasema pia kwamba Serikali haitafanya tena promotion wala kupandisha madaraja, hali ambayo pia inawafanya Watumishi wa Umma kwa namna fulani morali yao kushuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kusikia ukweli halisi ni upi katika suala hili. Je, ni kweli kwamba Serikali haitaajiri tena? Ni kweli haitapandisha madaraja tena? Nakushukuru.
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu swali la Mheshimiwa Mbogo, ni kwamba sasa hivi kuna watu wengi hupenda kusema maneno ambayo siyo sahihi na hili pia napenda nikanushe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana kwenye hotuba yake ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Benki Kuu, ametoa ufafanuzi mzuri sana. Nami nataka nitumie nafasi hii kurudia tu yale ambayo Mheshimiwa Rais ameyasema kwa kuwahakikishia Watumishi wa Umma na wale ambao wanatarajia kuajiriwa kwamba Serikali haijasitisha ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imesimamisha kwa muda kuajiri kwa sababu tunaendelea na zoezi la uhakiki wa watumishi hewa. Kazi hii ilishaanza, sasa hivi tunaikamilisha. Katika ukamilishaji huu, tunataka tujue sasa watumishi hewa ni akina nani kwa kila idara na kila sekta na watumishi walioko sasa kazini ni akina nani; ili tuweze kujua idadi ya watumishi waliobaki na pengo yaliyopo ndipo sasa tuweze kuajiri kwa ajili ya kusheheneza mahitaji ya watumishi kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali inafanya mapitio ya Miundo ya Utumishi kwa lengo la kuboresha. Tunaposema kuboresha, maana yake sasa tunataka tupate tija zaidi kwa watumishi. Kwa hiyo, naomba niwasihi Watumishi wote wa Umma kwamba zoezi hili halilengi kuwakandamiza watumishi; kazi hii hailengi kuathiri utumishi wao na madaraja yao, bali kuboresha watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie Watumishi wa Umma kwamba Serikali hii inawapenda sana na inajali mchango mkubwa ambao watumishi mnautoa kwa Serikali h
ii. Ili tuweze kufanya kazi kwa motisha, Serikali hii imeona ni muhimu sasa kuboresha zaidi miundo mbalimbali na maslahi mbalimbali, lakini pia kuona idadi ya watumshi tuweze kutumia fedha inayotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka muwe na amani kwamba kazi hii inayoendelea ni ya muda mfupi sana. Itakapokamilika, ajira zote ikiwemo na elimu, afya, majeshi, ambazo pia zilikuwa tayari zianze karibuni, zote zitarudishwa na watu watapelekwa kwenye vituo vya kazi kwenda kuanza kazi zao na madaraja mapya yatakuwa yameshatolewa.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA:
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, Sera na Mifumo ya Kisheria tuliyonayo sasa inaruhusu kuwaenzi waasisi pamoja na viongozi wa nchi hii, lakini siku za hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu, imejidhihirisha wazi kwamba baadhi ya viongozi
wameingia katika dimbwi la wizi, ubadhirifu wa mali za Umma na ukiukwaji wa maadili:-
Je, ni lini Serikali itafanya mapitio ya Sera, Sheria na kubadilisha mifumo ili sasa wale wezi wote waweze kuchukuliwa hatua kali za Kisheria na watakaobainika hivyo dhidi ya ukiukwaji wa maadili ya nchi hii? Ahsante.
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kudhibiti vitendo vya wizi, kukosa uadilifu, kukosa uaminifu mahali pa kazi na Watumishi wa Sekta ya Umma. Serikali inafanya hilo bila kujali ngazi ya mtumishi huyo, awe ni kiongozi wa ngazi ya juu, wa kati, hata wale watumishi wa kawaida, ilimradi Serikali imetoa dhamana ya kuwatumikia Watanzania, tunatarajia kila mtumishi atakuwa mwadilifu, mwaminifu, lakini pia atakuwa mchapakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaokiuka, dhidi ya wale wote ambao hawatumii vizuri madaraka yao, dhidi ya wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa popote pale nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ametaka kuona ni hatua gani zinachukuliwa; kwanza, tunaendelea kutoa elimu kwa watumishi ya kwamba kila mtumishi anatakiwa kufuata maadili ya utumishi, ikiwemo na uaminifu, uadilifu na uchapakazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali inaendelea kuboresha kwa kuunda; na tumeshaunda Taasisi ya Utumishi wa Umma, Taasisi ya Maadili ya Watumishi ambayo yenyewe inajiridhisha kwamba kila mtumishi anatangaza mali zake na kuendelea kufuatilia mara kwa mara mabadiliko ya mali hizo ili tuone kama mali hizo amezipata kwa utumishi wake huu alionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Serikali imeendelea kuimarisha
taasisi mbalimbali ikiwemo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
ambayo pia inafuatilia maeneo yote; kwa Watumishi wa Umma na hata raia
wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafanya mapitio ya lile jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema la Sera yetu na Sheria, Kanuni ili ziweze kuendana na mabadiliko ya wakati. Hii pia, ili kuisaidia Serikali kudhibiti tabia hii, sasa Serikali kupitia Bunge hili, siku mbili tatu zijazo mtapitisha Muswada wa kuanzisha Division ya Mahakama ya Mafisadi ili kuweza kupambana nao kwa lengo la kudhibiti vitendo vya Watumishi wa Umma wenye tabia ya kuiba fedha mahali pa kazi, lakini wale wenye vitendo vya ufisadi ili wote hao waweze
kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa mbinu hizi, kwa njia hizi zote, tutaweza kuwa na Watumishi wa Umma wenye maadili mema na wenye kutumia madaraka yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, malengo yetu Serikali ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanahudumiwa vizuri na Watanzania wawe na uhakika na Watumishi waliopo kwa kutekeleza wajibu wao kwa Watanzania wote bila kuwa na vitendo ambavyo vinaweza kuathiri utendaji wa kila siku.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kumuuliza Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo nchini sasa hivi kiuchumi, kuna mdororo mkubwa wa uchumi, na katika mdororo huu wa uchumi ambao tuna imani kabisa katika hatua za baadaye utaathiri bajeti ya Serikali, wawekezaji wengi wanasita kuwekeza katika nchi kwa sababu ya kutokuwa na uhakika kuwa Tanzania ya kesho itakuwaje. Kuna kuporomoka sana kwa deposits ama amana zinazowekwa katika benki zetu za biashara, mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, mizigo katika Bandari ya Tanga, mizigo katika border posts za Namanga, Sirari, Horohoro na Tunduma imepungua kwa zaidi ya asilimia 60.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, baadhi ya makampuni ya usafirishaji kwa zaidi ya asilimia 40 yamefunga kazi zao au vyombo vyao vya usafirishaji, kwa maana ya malori makubwa yamesitisha safari na makampuni mengine yamehamia nchi nyingine za jirani kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa hali ya ndani.
Je, hali hiyo kama Serikali mnaijua? Na kama mnaijua mnachukua hatua gani za makusudi za kurekebisha hasa ikizingatiwa kwamba uchumi unapoporomoka, kama ilivyo Tanzania leo mazao ya wakulima kama mbaazi, nafaka, mpunga nao unaanguka bei na tayari umeshaanguka bei kwa kiwango kikubwa?
Mheshimiwa Waziri Mkuu, mna mkakati gani wa makusudi wa kurekebisha hali hii? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nianze leo kwa kujibu swali la Mheshimiwa Mbowe, Mbunge na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwa swali lake muhimu kwa sababu linagusa hali ya uchumi ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumia hali ya uchumi tunazingatia mambo mengi na nikiri kwamba maeneo yote uliyoyatamka ni sehemu kubwa ya mchango wa hali ya uchumi nchini. Na kwa kutambua kwamba uchumi unashuka, inabidi tufanye tathmini ya kutosha, ingawa maeneo uliyoyatamka kwamba yamepungua sana nayo pia kuna haja ya kujiridhisha na kupata takwimu sahihi za miaka iliyopita na hali tuliyonayo sasa ili tujue kama je, kiwango cha kushuka kimesababishwa na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali haitaweza kulala, malengo ya Serikali wakati wote ni kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unaongezeka. Moja ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kwamba uchumi unakua kupitia nyanja zote pamoja na maeneo uliyoyatamka. (Makofi)
Kwa hiyo, kupungua kwa mizigo bandarini kumekuwa kunazungumzwa na watu wengi na juzi juzi Kamati yetu ya Bunge ya Viwanda na Biashara ilikuwa bandarani kupitia hayo na wamekaa na wadau. Lakini wadau peke yao hawatoshi, ni lazima tupate pia taarifa kutoka ndani ya Serikali na mwenendo wa uendeshaji wa bandari, mipaka yetu, lakini pia mazao yetu ndani ya nchi na mwenendo wake mzima. (Makofi)
Kwa hiyo, niseme kwa sasa kukupa takwimu halisi za kuporomoka au kutoporomoka si rahisi sana, lakini nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwamba Serikali itafanya jitihada wakati wote kuhakikisha kwamba uchumi wake unapanda. Serikali itakubali kukutana na wadau kuzungumzia hatma ya uchumi nchini, Serikali itapokea ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge kwa namna ambavyo wanaona kwamba kuna udhaifu mahali ili tuweze kuhakikisha kwamba uchumi unaongezeka na pia bajeti ya mwakani inapata mafanikio makubwa ukilinganisha na bajeti ambayo tunaitekeleza sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi bado nirudie kukuhakikishia kwamba Serikali haitalala katika hili kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unapanda na kwa hiyo, kama changamoto ya maeneo ambayo umeyatamka tutafanya mawasiliano na Wizara ya Fedha lakini pia na Benki Kuu ili tuweze kupata takwimu halisi za hali ya uchumi nchini na tutakuja kulijulisha Bunge letu ili Wabunge wajue na wapate nafasi ya kutushauri. Kamati yetu ya Kudumu ya Biashara na Viwanda ipo, bado ina nafasi nzuri ya kuweza kutushauri kama Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Nami nikushukuru na vilevile nikutakie afya njema na kila zito Mwenyezi Mungu afanye jepesi kwa upande wako.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali hii isingekuweko madarakani bila kuwepo wananchi na wananchi ndiyo Serikali na Serikali ni wananchi, hata Mheshimiwa Waziri Mkuu wewe mwenyewe bila kuweko wananchi usingepata Uwaziri Mkuu hata Mheshimiwa Rais pamoja na sisi Waheshimiwa Wabunge wote humu ndani.
Mheshimiwa Spika, swali, afya huwezi kupata bila kupata chakula, mwanzo upate chakula ili upate afya. Hivi sasa kumekuwa na harufu inaweza ikawa nzuri au ni mbaya.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upungufu wa chakula ikiwemo bidhaa muhimu ya sukari, na sijui kama Serikali mmefanya utafiti gani kuliangalia suala hili. Msemo wa Waswahili husema, usipojenga ufa, hutajenga ukuta. Mmechukua jitihada gani kama Serikali kuangalia hali ya sukari na mchele ilivyo sasa? Na wanaoumia ni wananchi na ukizingatia kesho kutwa tuna sikukuu na inahitaji sukari kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Je, kuna harufu Serikali imeagiza sukari. Ni kweli suala hilo kwa ajili ya kuwajali wananchi wake?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ameeleza maneno mengi lakini muhimu ni kwamba kuna harufu ya upungufu wa bidhaa ya sukari nchini. Ni kweli huko nyuma tulikuwa na tatizo la sukari nchini kote na Serikali ikafanya jitihada ya kutambua mahitaji ya nchi, na yale mapungufu tuliyafanyia kazi kwa kuagiza sukari nje ya nchi na kuleta ndani kwa kiwango ambacho hakitaathiri uzalishaji wa ndani ili tuweze kuendelea kutoa huduma hiyo. Tumeendelea kufanya hilo mpaka pale ambapo tumeridhika kwamba viwanda vyetu vya ndani vimeanza kuzalisha na kuona uzalishaji ule na sukari ambayo tumeingiza vinaweza kutufikisha tena msimu ujao wa uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, suala la sukari hatujaishia tu kuwa na maazimio ya kuagiza toka nje. Mkakati mkubwa tuliofanya ni kuhakikisha tunaimarisha viwanda vya ndani viweze kuzalisha. Tumekutana na wazalishaji wote wa sukari, TPC, Kilombero, Kagera pamoja na Mtibwa kupata picha ya uzalishaji kwenye viwanda vyao na mkakati walionao kuendeleza uzalishaji. Lakini bado tumegundua kwamba viwanda vyetu havitakuwa na uwezo kwa kipindi cha miaka minne ijayo kuzalisha sukari ikatosheleza nchini. Lakini pia kumekuwa na wasiwasi wa takwimu za mahitaji ya sukari nchini kwa sababu nchi jirani ya Kenya yenye watu milioni 45 mahitaji ya sukari ni tani 800,000, lakini tathmini ya Idara yetu ya Kilimo nchini kwa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 45 ile ile wanatuambia takwimu zile zinahitaji tani 420,000; kwa hiyo utaona tuna upungufu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, tulichokifanya; kwanza tumeagiza Wizara ya Kilimo ifanye utafiti wa kina kuona mahitaji ya sukari nchini, lakini pili kutokana na maelezo tuliyopata kutoka kwa viwanda tumewapa maelekezo ya kuzalisha zaidi ili tuongeze sukari, na tumekubaliana hilo. Tatu, tumeamua kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda na uhamasishaji wa kilimo cha miwa ili tuweze kuzalisha sukari inayoweza kutosheleza mahitaji ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tayari tumeshapata wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza kwenye ulimaji wa miwa pamoja na uzalishaji wa sukari nchini ili na sisi tufikie kiwango ambacho kitakwenda kutambulika baada ya Wizara ya Kilimo kufanya sensa yake. Lakini wakati wote huu Serikali itahakikisha kwamba nchi haikosi sukari na wananchi wanaweza kupata kinywaji ambacho kinahitaji sukari, uendeshaji wa sukari kwenye viwanda kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayohitaji sukari ili tuweze kuhakikisha kwamba biashara hii na zao hili linatosheleza kwa matumizi ya ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia Mheshimiwa Jaku ametaka kuzungumzia upungufu wa chakula na jana Mheshimiwa Keissy aliomba Mwongozo wa kutaka maelezo ya hali ya chakula nchini na bado Serikali tumeahidi kutoa taarifa hapa Bungeni kabla ya mwisho wa wiki hii ya hali ya chakula nchini na mkakati wa taifa kama kuna upungufu huo wa kiasi hicho ili sasa kila mmoja wetu nchini aelewe nafasi tuliyonayo ili tuweze kushirikiana kwa pamoja kuondoa tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo taarifa ambayo itatolewa na Wizara ya Kilimo juu ya hali ya chakula ikiwemo na zao la sukari inaweza kusheheneza mahitaji ya uelewa kwenye eneo hili ahsante sana. (Makofi)
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu swali langu linahusu suala la zao la korosho.
Mheshimiwa Spika, Serikali hivi karibuni ilifanya maamuzi mazuri ya kuhakikisha wakulima wa korosho wanaondolewa tozo na kero kubwa ambazo zilikuwa zinawasumbua kwa muda mrefu na hizo tozo tano zilitolewa maamuzi ambayo mpaka sasa hivi hajatoa tamko zuri ambalo litawafanya wananchi wale waweze kufarijika na hilo suala.
Swali langu Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama mdau wa korosho na sisi wengine ambao ni wadau wa korosho, na mikoa mingine ya Tanzania nzima ambao ni wadau wa korosho wanataka wapate tamko lako la kuhusu suala la korosho.
Je, katika msimu huu wa korosho utaweza kusimamia na kuhakikisha zile tozo tano zinafutwa ili wananchi wafarijike? Ukizingatia kwamba hali ya sasa hivi ni mbaya, mazao ya mbaazi yako majumbani, ufuta uko majumbani, kunde ziko majumbani, njugu mawe ziko majumbani, njegere ziko majumbani, choroko ziko majumbani? Mwenyezi Mungu akikujalia kusimamia na kutupa tamko lako hapa ndani ya Bunge utawafariji Watanzania. Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lulida, Mbunge na mdau wa korosho kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba zao hili la korosho limekuwa na matatizo mengi hasa kwenye masoko kufuatia mfumo unaotumika wa kuuzia zao hili wa Stabadhi za Mazao Ghalani. Lakini pia zao hili linaendeshwa kwa mfumo wa ushirika ambao una viongozi kutoka ngazi za vijiji, Chama Kikuu cha AMCOS na badaye kuundiwa Bodi.
Mheshimiwa Spika, zao la korosho lilikuwa na tozo zake za kisheria lakini pia wanaushirika waliongeza tozo nyingine nyingi za hovyo, na mimi ndiye niliyetamka kusimamia mazao yetu ya biashara kote nchini kuhakikisha kwamba tunafanya mapitio ya kina na kwamba tunaondoa makato ya hovyo hovyo yaliyoingizwa tu na wanaushirika kwa maslahi yao na hatimaye kupelekea wananchi wanaolima mazao haya kukata tamaa kuendelea na uzalishaji wa zao husika likiwemo zao la korosho.
Mheshimiwa Spika, Serikali baada ya kutoa tamko jukumu letu sasa ni kusimamia na tumeshatoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wa ushirika, lakini pia hata viongozi wa taasisi yenyewe Bodi ya Korosho kuhakikisha kwamba wanasimamia maelekezo ya Serikali ya kuondoa zile tozo.
Mheshimiwa Spika, zao hili baada ya kuwa tumetoa maelekezo wajibu wa Serikali sasa ni kuhakikisha kwamba yale tuliyoyaagiza yakiwemo na yafuatayo yanaweza kukamilishwa:-
(i) Tunataka zao hili linapokusanywa na kupelekwa kwenye maghala, maghala yote ya vijijini lazima sasa yatumike kuhifadhi korosho hizo badala ya kupeleka kwenye ghala kuu ambayo yalikuwa yanatengenezewa ushuru, huku wakulima wenyewe wakiwa wameshajijengea maghala yao; na kwa hiyo kila maeneo ya Wilaya watabaini maghala ambayo yatatunza korosho hizo ili kuwapunguzia tozo ya gharama ya ghala kwenye maghala makuu.
(ii) Kumekuwa na minada inayopelekwa makao makuu ya mkoa pekee, na kuwanyima wananchi kusimamia na kuona mwenendo wa minada. Tumeagiza kuanzia sasa minada yote itafanywa kwenye ngazi ya Wilaya ili wananchi waende kushuhudia minada hiyo. (Makofi)
(iii) Kulikuwa na wanunuzi wanaoenda kwenye minada wakiwa hawana fedha. Sasa ili kujihakikishia kwamba mnunuzi ananunua na analipa lazima aweke dhamana ya kiwango cha fedha benki ambacho bodi itaamua, ili tuwe na uhakika kwamba anayekuja kuweka zabuni ya kununua zao la korosho ana fedha za kulipia; kwa sababu tumegundua watu wanakuja kutafuta zabuni hawana fedha halafu wanakimbia.
Kwa hiyo, Serikali itaendelea kusimamia haya kuhakikisha kwamba mkulima anapata fedha yake kwa kipindi kifupi sana baada ya mnada na mnunuzi awe na fedha na fedha ikishatolewa inaingizwa kwenye akaunti ya benki halafu wakulima waweze kupelekewa mahali walipo. Kwa hiyo, hiyo ndizo jitihada ambazo Serikali itahakikisha kwamba yale maelekezo yanasimamiwa na tutashuhudia kwamba yanatekelezwa vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu, utaratibu wa kibajeti unaanzia kwenye Serikali za vijiji mpaka inamalizikia Bungeni ndio tunapitisha bajeti ya Serikali. Lakini mpaka hapa ninapoongea kuanzia mwaka 2014 kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuna vijiji vitatu vilisimamishwa na Ofisi ya TAMISEMI visifanye uchaguzi ingawaje vilishatangazwa kuwa vijiji. Vijiji hivyo viko katika kata ya Mofu ambapo ni Miomboni, lakini Kata ya Namohala ni Idandu na Chiwachiwa. Lakini kwa maelezo ya Serikali kwamba yale maeneo ni ya uwekezaji kwa hiyo hakuna uchaguzi wa vijiji utakaofanyika.
Je, Waziri Mkuu nini kauli ya Serikali kuhusu hatma ya vijiji hivyo na wananchi katika hilo Jimbo la Mlimba na kata na vijiji nilivyovitaja? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Susan Kiwanga kwa eneo lile la kisera zaidi badala ya kujikita kwenye ngazi za vijiji na hasa alipokuja kutamka kwamba kuna mwelekeo wa kibajeti kwenye ngazi za vijiji mpaka Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mchakato wa bajeti huanza kwenye ngazi za vijiji inaenda kwenye Kata, Wilaya na hatimaye Mkoa na baadaye unakuja kwenye Wizara. Hii inatoa nafasi kwa kila eneo kutengeneza mpango wake wa matumizi ya kifedha ili kuboresha masuala mbalimbali yakiwemo na mambo ya maendeleo. Na kama lipo tatizo ndani ya Halmashauri ya Wilaya linalogusa vijiji na wamekosa nafasi ya kuweka bajeti zao ngazi ya juu inawajibika kuweka bajeti ya maeneo hayo ambayo hayajapewa uongozi unaosimamia utengenezaji wa bajeti kwenye eneo hilo ili na wao waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, na kwa hiyo basi kama vijiji vile vitatu havijapata nafasi ya kuunda uongozi utakaoweka bajeti ya maendeleo yao ngazi ya kata ambako kuna Diwani ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ndiye atakayewajibika kuviingiza vijiji vile kuvitengenezea bajeti kwenye kata yake na diwani atabeba kupeleka kwenye Halmashauri ya Wilaya na atalazimika kuviingiza kwenye mpango wa bajeti wa Halmashauri ya Wilaya vijiji hivyo ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma. Hata kama vijiji hivyo havijapewa nafasi kwa sababu tu eneo hilo ni la uwekezaji. Bado Serikali inatambua kuna wananchi pale na ni lazima wahudumiwe kwa hiyo bajeti lazima pia ioneshe kwamba wananchi wale watahudumiwa kadri wanavyokwenda mpaka hapo jambo hilo litakapopata utatuzi wake.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mchakato wa kibajeti unahusisha Watanzania wote, hata kama kwenye maeneo hayo kuna upungufu wa viongozi waliopo wanayo dhamana ya kutengeneza bajeti. Kwa hiyo basi, Wizara ya TAMISEMI na bajeti yao yote ya nchi nzima lazima vijiji hivyo viweze kushughulikiwa.
Mheshimiwa Spika, lakini suala la mgogoro wa vijiji hivyo sasa, na Waziri mwenye dhamana yuko hapa atakuwa ameshachukua jambo hilo na atawajibika sasa kufuatilia kule Ifakara na aweze kukupa jibu katika kipindi hiki cha Bunge ili utakaporudi nyumbani uwe na majibu ya hatma ya vijiji hivyo na uwekezaji uliopo maeneo hayo. (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumeendelea kuwa na mauaji ya mara kwa mara katika nchi yetu hasa askari pamoja na wananchi wa kawaida, hasa katika mikoa ya Mwanza, Tanga, Vikindu, je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na vitendo hivi vinavyosababisha mauaji makubwa kwa wananchi wasiokuwa na makosa yoyote?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Ngonyani, Mbunge wa Korogwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba hapa karibuni tumepata matukio mengi ya mauaji ya raia, lakini pia hata askari wetu nao wameuawa katika mfululizo wa matukio hayo hayo kwenye maeneo ya Tanga, Mwanza na hivi karibuni pale Vikindu.
Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kwanza kutoa pole kwa wananchi wote ambao ndugu zao wamepoteza maisha kupitia mauaji hayo yaliyotokea kwenye maeneo haya yote. Lakini pili, ningependa niwahakikishie Watanzania kwamba Serikali imesikitishwa sana na jambo hili ambalo linaonekana kuna Watanzania wachache wasingependa maisha ya wenzao yaendelee na kuamua kukatiza kwa njia ya mauaji ambayo Serikali haijaridhishwa, na Watanzania wengi wamepata uoga katika hili kwamba linaweza kuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, nataka niwatoe wasiwasi huo Watanzania kwamba Serikali iko macho, na imeendelea kuwasaka wale wote waliohusika kwenye mauaji haya, na tutahakikisha tutawakamata wote popote walipo ili tuwatie mikononi na hatimaye mkondo wa kisheria uweze kuchukua nafasi yake.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo hili kwa masikitiko ambayo nimeyaeleza napenda tuwahakikishie Watanzania kwamba vyombo vya dola viko macho, na tutaimarisha ulinzi maeneo yote, kutoka ngazi ya vitongoji na maeneo yote ambayo wananchi wanavyokuwa wanaishi na wanahitaji amani ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili niombe wananchi wote washirikiane sana na vyombo vya dola katika kuhakikisha kwamba kwenye maeneo yetu kama kuna jambo ambalo tunalitia mashaka, kama kuna mtu ambaye tunamtilia mashaka tushirikiane na vyombo vya dola kuvipa taarifa ili vyombo vya dola viweze kuchukua tahadhari kabla ya mauaji hayo hajawahi kujitokeza.
Kwa hiyo, kauli ya Serikali katika hili ni kuhakikisha Watanzania kwamba usalama wa nchi hii utaendela kwa kuhakikisha kwamba tunathibiti matukio matukio yote ya hovyo yanayopelekea wananchi kusitisha maisha yao kama ambavyo imetokea kwa askari, lakini pia kwa wananchi wetu ambao wametangulia mbele za haki kwa matukio haya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo bado nirudie kwamba Serikali itaongeza ulinzi katika nchi yetu kwenye maeneo yote, na ndio hiyo ambayo tulikuwa tunaijadili hapa juzi kuona kwamba tumeimarisha ulinzi zaidi; polisi wako wengi wanaangalia usalama katika nchi hii unaendelea. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie kwamba nchi itaendelea kuwa salama na wale wote waliohusika katika matukio haya tutaendelea kuwasaka ili kuhakikisha tunawapata na kuwachukulia hatua. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali kwa Waziri Mkuu. Kwa kuwa Serikali ina mifumo, sheria, miongozo na taratibu ya upelekaji wa fedha za maendeleo katika Halmashauri zetu mara tu baada ya bajeti ya Serikali kwisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kuwa sheria hizi na miongozo hii haifuatwi na kupelekea Halmashauri zetu kupelekewa robo tu ya fedha au nusu tu ya fedha zikiwemo Halmashauri zangu za Mkoa wa Tabora ambazo zote saba hazijawahi kupata fedha kamili. Hii inaleta taharuki kubwa ndani ya Halmashauri zetu. Je, Mheshimiwa Waziri Mkuu unatoa kauli gani kuhusu ucheleweshwaji wa fedha za bajeti kwenda kwenye Halmashauri zetu kwa wakati muafaka?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijaanza kujibu swali, uridhie kuwakumbusha Watanzania kwamba leo hii Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatimiza siku ya 365 kwa maana ya mwaka mmoja. Naamini Watanzania wote tumeona utendaji wake na hasa mwelekeo wake wa kuiongoza Serikali hii kwa mafanikio. Jukumu letu ni kumwombea Mheshimiwa Rais aweze kuendelea vizuri na kuiongoza nchi yetu na wananchi wote tuungane pamoja kila mmoja kwa dhehebu lake kuiombea Serikali hii iweze kupata mafanikio makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nianze kujibu swali la Mheshimiwa Munde kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu baada ya bajeti inawajibika kutekeleza maamuzi ya Bunge letu hasa katika kupeleka fedha za bajeti zilizopangwa. Hata hivyo, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mnajua kwamba baada ya Bunge kuridhia na kutoa mamlaka ya matumizi ya fedha, Serikali hii tulianza na majukumu muhimu; moja, ilikuwa kwanza kujiridhisha kuwepo kwa mifumo sahihi ya makusanyo ya mapato na matumizi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbili kwa upya wake tulianza kupeleka watumishi watakaosimamia shughuli za usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na matumizi yake kwenye Halmashauri zote nchini. Kazi kubwa ya tatu ilikuwa ni kuratibu na kutathmini miradi yote iliyokuwa imeanza halafu ilikuwa haijaendelezwa na ile miradi mipya ili tuweze kutambua pamoja na thamani zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwa tumejiridhisha sasa tumeanza kupeleka fedha kwenye Halmashauri zote nchini. Kwa mujibu wa kumbukumbu kutoka Hazina ambazo wakati wote tunapewa taarifa; ofisini kwangu pia napewa taarifa; kufikia mwezi Oktoba tumeshapeleka zaidi ya shilingi bilioni 177 za miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge watabaini wiki hizi tatu tumeanza kuona kwenye magazeti yetu mengi matangazo mengi ya zabuni kutoka kwenye Halmashauri mbalimbali. Hii ina maana kwamba tayari miradi ile ambayo ilikuwepo na ile ambayo inaendelea na mipya imeshaanza kutengewa fedha na kuanza kutangazwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba sasa Serikali itaendelea na upelekaji wa fedha kwenye Halmashauri kwa ajili ya shughuli zetu za maendeleo kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado msisitizo umebaki pale pale kwamba Halmashauri ziendelee kukusanya mapato ya ndani ili kuongezea bajeti kwa fedha za Serikali ambazo tunazipeleka na tumesisitiza ukusanyaji huo uwe ni wa mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti mapato ambayo tunayapata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tumeendelea kusisitiza matumizi sahihi ya fedha ambazo tunazipeleka kwenye Halmashauri kwamba fedha hizi ni lazima zitumike kadiri ilivyokusudiwa kwa miradi iliyoandaliwa kwenye Halmashauri zenyewe.
Waheshimiwa Wabunge, sisi wenyewe ni Wajumbe wa Baraza letu la Madiwani kwenye Halmashauri zetu; niendelee kuwasihi kusimamia na kufuatilia matumizi ya fedha tunazopeleka kwenye Halmashauri ili ziweze kutekeleza miradi ile kikamilifu. Serikali itaendelea kutuma fedha kwenye Halmashauri zetu kadri miradi ile ilivyoweza kuratibiwa. Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nampongeza kiongozi wa Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa swali zuri ambalo wewe mwenyewe Naibu Spika, umesaidia kuiua CCM humu ndani. Watu wataamini hizo hela mmekula, bora ungeacha ajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nimwulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nitatumia maneno ambayo watawala wanapenda kuyasikia kwamba Serikali hii haijafilisika kabisa na Serikali hii ina mikakati mizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi katika Ubunge wangu wa muda mfupi huu, ile Sheria ya Mfuko wa Jimbo ndiyo sheria ambayo nimeona imekaa vizuri kweli kweli kwa sababu ni fedha ambazo Mbunge anapewa kwa taarifa tu zinaingia kwenye Halmashauri halafu Kamati yake inakaa, miradi inaibuliwa halafu wanapanga inaenda kwa wananchi moja kwa moja, Mbunge hagusi hata shilingi mia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali haijafilisika, tangu bajeti ya Serikali yenu hii ya Awamu ya Tano imepitishwa, Waheshimiwa Wabunge hawajapewa fedha hii ya Mfuko wa Jimbo. Sasa naomba unieleze, kama Serikali haijafilisika, Waheshimiwa Wabunge wameahidi miradi mbalimbali katika maeneo yao ya kiuongozi na wananchi wakawa wanasubiri miradi ile, Waheshimiwa Wabunge wanaonekana waongo kwa sababu fedha hazijaenda na Wabunge hawawezi kufanya maamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini kauli yako juu ya hili? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimwambie kwamba Serikali hii haijafilisika. Mfuko wa Jimbo wa Mbunge ni miongoni mwa fedha zilizoandaliwa kwa bajeti ambayo tuliipitisha mwezi Julai, lakini Mfuko huu unapelekwa mara moja kwa mwaka kwenye Majimbo yetu. Nawe ni shahidi kwamba toka tumemaliza Bunge sasa tuna miezi mitatu. Bado tuna miezi kama saba ili kuweza kuhakikisha kwamba fedha yote tuliyokubaliana hapa inaenda kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo yana kipaumbele chake, yapo yale ambayo yanaweza kutekelezwa ndani ya mwaka mzima, lakini nataka nikukumbushe kwamba mfumo wa fedha zetu ni cash budget, tunakusanya halafu pia tunapeleka kwenye miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe Mheshimiwa Mbunge faraja kwamba suala la Mfuko wa Jimbo bado unatambulika na fedha tutazipeleka kwenye Majimbo na Waheshimiwa Wabunge wote tutawajulisha tumepeleka kiasi gani ili sheria zile ziendelee kutumika na Mheshimiwa Mbunge kama Mwenyekiti wa Mfuko wa Jimbo utaendelea kuratibu mipango yako ya Jimbo lako na fedha ambayo tutaipeleka. Kwa hiyo, endelea kuwa mtulivu, fedha tutazipeleka na tutawajulisha Wabunge wote. Ahsante sana.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu, hakuna Serikali yoyote duniani ambayo haitozi kodi. Ni lazima tulipe kodi ili tupate madawa, watoto wasome, tupate maji na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi kirefu sana, wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kunyanyaswa na baadhi ya Maafisa wa Kodi na wengine wakikadiriwa kodi isiyostahili na mbaya zaidi kuna wazabuni ambao wanaidai Serikali yetu. Je, nini kauli ya Serikali kwa jambo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabati, Mbunge wa Iringa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba nimepata malalamiko na baadhi ya wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali. Mimi nimekuwepo kwenye ziara ya kawaida Mkoani Mbeya na kwenye kikao changu na wafanyabiashara, wamewahi kueleza matatizo yanayowapata chini ya chombo chetu cha TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wao niliwahakikishia, naomba nirudie tena kwamba Serikali hii inaheshimu na kuwathamini wafanyabiashara wote, wawekezaji wote na wadau wote walipa kodi ndani ya nchi hii, kwa sababu maendeleo yetu katika nchi yataletwa na sekta ya wafanyabiashara na wawekezaji wakiwa ndio walipa kodi wakubwa, wazuri nchini na uchumi wetu unategemea sana kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo ndani ya chombo chetu cha TRA, tumeendelea kufanya vikao nao, kuwasisitiza na kuwataka wafuate kanuni na taratibu za ukusanyaji wa kodi na kuwasisitiza watumie lugha zenye busara pale wanapotakiwa kwenda kuonana na mfanyabiashara kuzungumzia jambo lolote au kukusanya kodi wanapofika kwenye duka lake au sehemu yake ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka niwasihi wafanyabiashara, popote ambako unadhani hutajendewa haki na mtumishi wa TRA; TRA yetu inacho chombo cha nidhamu na maadili cha TRA ambacho kinapokea malalamiko mbalimbali dhidi ya watumishi ambao hawafuati kanuni na hawana maadili katika kutekeleza jukumu lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, mfanyabiashara yeyote, mwekezaji yeyote, mlipa kodi yeyote ambaye pia atakuwa na malalamiko yoyote yale, bado anayo nafasi ya kwenda kwenye chombo chochote cha usalama kutoa taarifa ya jambo ambalo limemkwaza ili pia tuweze kutafuta dawa sahihi ya baadhi ya watumishi ambao hawafanyi kazi yao vizuri kwenye chombo chetu cha TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kuwahakikishia wafanyabiashara, wawekezaji na walipa kodi wote, Serikali hii itaendelea kuwapa ushirikiano wa dhati. Serikali hii ambayo sasa tunahitaji kupanua Sekta za Biashara itaendelea kuwaunga mkono kwenye jitihada zenu za kibiashara ili tuweze kupata mafanikio ya maendeleo na kuinua uchumi wetu katika Taifa letu. Ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nina swali moja kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu napata ufahamu kulikuwa na sera katika nchi yetu ya wataalam, wafanyakazi wale wa nje, zamani walikuwa wanaitwa ma-TX. Wafanyakazi wa nje, kulikuwa na sera kwamba wanafanya kazi kwa kupata kibali kutoka uhamiaji cha miaka miwili, wakitegemewa kwamba kipindi hicho wana-recruit Mtanzania kwenye kampuni au kwenye kiwanda hicho na baada ya miaka miwili tunatarajia kwamba yule TX atakuwa ameshamhitimisha yule kijana au yule mfanyakazi atakuwa amehitimu na kibali chake kitakoma. Kama huo ujuzi utakuwa bado unahitajika, yaani hapana mtu aliyehitimu, ataongezewa tena miaka miwili kutimiza miaka minne. Je, Mheshimiwa Waziri Mkuu, hiyo sera bado ipo? Kama ipo, bado inatekelezwa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kwamba, sera ile bado ipo na Serikali tunaisimamia. Msingi wa jambo hili wa kuwapa muda mfupi hawa watalaam wenye ufundi maalum nchini kwetu katika sekta za kazi, ilikuwa ni kujenga wigo mpana kwa Watanzania kupata ajira na kuweza kusimamia maeneo haya ambayo yanahitaji pia utalaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya hili kutoa nafasi kwa watumishi wa nchi za nje kuja nchini Tanzania kufanya kazi ambazo hapa ndani tunakosa utalaam; ndiyo tunapofuata utaratibu huo. Tunawapa miaka miwili ya kwanza, tukiamini kwamba Watanzania waambata watakuwa wameshajifunza utalaam ule na baada ya miaka miwili wanaweza kuondoka. Pale ambapo inaonekana kuna uhitaji zaidi, sheria inawaruhusu kuwaongezea miaka miwili ili tuendelee, lakini mwisho tunaweza kumwongezea mwaka mmoja na kufanya miaka mitano ya mwisho. Baada ya hapo, tunaamini Watanzania watakuwa wameshaweza kupata ile taaluma na kusimamia sekta za kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka niwahakikishie, mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunafungua milango ya ajira kwenye sekta zote ikiwemo na utaalam, tutaendelea kuusimamia utaratibu huu wa kupokea watalaam kutoka nje wenye utalaam ambao nchini kwetu haupo ili kutoa nafasi kwa Watanzania kujifunza na baada ya miaka miwili tutataka wale wa kutoka nje warudi nchini kwao ili nafasi zile ziendelee kushikiliwa na Watanzania. Tutaendelea kusimamia Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wakati tunaelekea kwenye msimu mwingine wa kilimo na mvua zimeshaanza kunyesha kwenye maeneo mengi ya nchi yetu likiwemo Jimbo langu la Mbeya Vijijini, lakini pembejeo za ruzuku za kilimo bado hazijawafikia walengwa. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa hizo pembejeo za ruzuku zinawafikia wakulima kwa muda muafaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:- (Makofi/ kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya kilimo imeweka utarabu wa kusambaza pembejeo kwenye maeneo yetu kote nchini, pembejeo za mbegu na mbolea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeamua msimu huu wa kilimo, kuanzia mwaka huu, kutumia taasisi inaitwa Tanzania Fertilizer Cooperation Company ili kupeleka mbolea, lakini pia mashirika mengine kusambaza pembejeo za aina nyingine. Mashirika haya tayari yameshakaa na Wizara ya Kilimo kwa pamoja ili kuweza kuratibu vizuri usambazaji wa pembejeo mpaka kwenye ngazi za vijiji na kuweza kuwafikia wakulima kabla ya msimu wa kilimo kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwezi uliopita tumeshatoa fedha kwa ajili ya kununua pembejeo na tumekabidhi taasisi zote ambazo nimezitaja ambazo pia zenyewe zinaweza kupata Mawakala kwenye ngazi ya Wilaya kule ili kuwafikishia wananchi kwenye ngazi ya vijiji na msimu huu wa kilimo utakapoanza, wakulima waweze kupata hizo pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote ambao kweli tumejikita kwenye kilimo kwamba, Serikali itaendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati na hasa wakati huu ambao mvua zimeshaanza kunyesha katika baadhi ya maeneo, kabla ya mazao husika kulimwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kusimamia na tutaendelea kutoa fedha zaidi ili tuweze kupeleka mbolea, mbegu za mazao ambayo yako kwenye orodha ya pembejeo kama ambavyo tumekusudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona lakini nilisikitika kwamba unadai hujaniona, lakini nashukuru umeniona hatimaye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali la msingi la kisera.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni siku ambayo Taifa letu linaadhimisha siku ya Haki Duniani. Tunapoadhimisha siku hii ya Haki Duniani ambayo nina hakika leo Spika wetu yupo Dar es Salaam kwa ajili ya jukumu hilo akiungana na viongozi wengine wa Kitaifa akiwemo Mheshimiwa Rais na Jaji Mkuu. Ni miezi mitatu kamili tangu Mheshimiwa Godbless Lema, Mbunge wa Arusha akamatwe nje ya geti la Bunge na kupelekwa kizuizini kushtakiwa kwa kesi inayoitwa ya uchochezi ambayo ina dhamana, lakini miezi mitatu leo hajaweza kupata dhamana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo tuna Mbunge mwingine wa Kilombero, Mheshimiwa Lijualikali ambaye anatumikia kifungo cha miezi sita katika Gereza la Ukonga kule Dar es Salaam na kazi ngumu; wakati huo huo, tuna zaidi ya Madiwani sita wa Chama cha CHADEMA ambao wamefungwa kwa makosa yenye misingi ya kisiasa; tuna viongozi kama Mwenyekiti wa Chama wa Mkoa wa Lindi aliyefungwa miezi nane kwa kufanya kazi yake ya kisiasa. Tuna viongozi wa ngazi mbalimbali zaidi ya 215 aidha wamefungwa ama wanaendelea na mashtaka mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona namna Serikali inavyotumiwa mawakala na vibaraka wake kukigawa na kukidhoofisha Chama cha Wananchi (CUF) ikiwemo kumtumia Msajili wa Vyama vya Siasa kudhoofisha Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, maadam Mheshimiwa Rais alishatangaza kwamba kusudio lake ni kufuta vyama vya upinzani kabla ya mwaka 2020, haya yanayoendelea katika Awamu ya Tano ambacho ni kinyume na utamaduni na mazoea yetu kama Taifa, ni sera au utekelezaji wa sera hiyo ya kuua upinzani; na ni sera chini ya Serikali yako na Mheshimiwa Magufuli?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nikanushe kwamba Mheshimiwa Rais hajawahi kutangaza kuvifuta Vyama Vya Upinzani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Spika umesema kwamba Watanzania wote wanajua kwamba nchi hii inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu, lakini pia tunajua katika kuendesha nchi tunaendesha kwa mihimili mitatu. Iko Serikali, Mahakama na Bunge. Hakuna mhimili unaoweza kuingilia mhimili mwingine. (Makofi)
Tatu, Watanzania wote wanajua kwamba jambo lolote ambalo liko Mahakamani haliwezi kuzungumzwa mahali pengine popote. Kwa hiyo, siwezi kutumia nafasi hii kuzungumzia mambo yote yaliyoendelea chini ya sheria na yaliyoko Mahakamani. Ahsante sana.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nina swali moja kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa waziri Mkuu, kwa kuwa mwaka 2016 miezi kama hii kulitokea upungufu mkubwa wa sukari nchini na Serikali ya Awamu ya Tano ilifanya jitihada kubwa sana kukabiliana na hali ile na hatimaye nchi yetu ikapata utulivu mkubwa katika suala zima la sukari.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nikupongeze wewe na Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa mliyofanya mwaka 2016 katika suala zima la upungufu wa sukari nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kipindi hiki, viwanda vyetu vya ndani vinakamilisha msimu, vingine vinamaliza mwezi wa Tatu, vingine vinamaliza mwezi wa pili; na kwa kuwa vikikamilisha msimu, uzalishaji unaanza tena mwezi wa sita na kuendelea. Je, hali ilivyo sasa ya sukari nchini ikoje? Serikali imechukua juhudi gani kuhakikisha kwamba yale yaliyotokea mwaka 2016 hayatatokea?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saddiq, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka niwahakikishie Watanzania kwamba hakutakuja kutokea upungufu wa sukari, kwa sababu viwanda vyetu vya ndani vilishaanza uzalishaji na sasa vinaendelea na uzalishaji. Tunavyo viwanda vitano ambavyo tumevitembelea, tumehakiki utendaji kazi wake na uzalishaji upo na sukari ambayo inatumika nchini inatokana na uzalishaji huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaaamini kufikia mwishoni mwa msimu ambapo ni mwezi wa tatu mwaka huu wa 2017 tunaweza kuwa tumezalisha na kufikia malengo. Kwa sababu kwa taarifa za mwisho, mpaka mwishoni mwa Januari, uzalishaji kwa malengo waliokuwa wamejiwekea wamefikia asilimia 86. Asilimia iliyobaki inaweza kuzalishwa kwa kipindi kifupi kilichobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kama itajitokeza upungufu kwa sababu ya mahitaji ya sukari, pia kutozuia upandaji wa bei, Serikali itakuwa iko tayari kutafuta namna nzuri ya kupata sukari tukishirikiana na viwanda vyenyewe ikiwa ni mkakati wa kuvilinda viwanda vya ndani vinavyozalisha sukari ili viweze kuongeza uwezo wa uzalishaji wa sukari nchini. Huo ndiyo mpango wa Serikali.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa mujibu wa taratibu za kisera tulizonazo, Serikali ina wajibu wa kuangalia hali ya chakula nchini. Kwa taarifa ya Serikali, Halmashauri 55 zina upungufu wa chakula. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuleta chakula ili kupunguza mfumuko wa bei ulioko sokoni sasa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la chakula limeelezwa vizuri sana na Waziri wa Kilimo kupitia taarifa Bungeni juzi na taarifa yake imefafanua vizuri na hatua ambazo Serikali inazichukua za kuhakikisha kwamba Watanzania wanaendelea kuwa na akiba ya kutosha kwenye maeneo yao ili Watanzania waweze kuwa na uwezo wa kuendelea na uzalishaji mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sikusudii kurudia maelezo ya Mheshimiwa Waziri, lakini Serikali inaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara wa ndani pia kutumia nafasi hii kufanya biashara kutoka Wilaya moja ambayo ni kwenye mazao mengi kwenda maeneo mengine ili kuweza kuongeza idadi ya chakula na kupunguza bei kwenye masoko na tunao ushahidi wa kutosha kwamba Mikoa ya Rukwa, Mbeya Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma bado ina chakula cha ziada, lakini pia hata kwenye soko letu la Kimataifa - Kibaigwa kuna mahindi ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wafanyabiashara wa ndani watumie nafasi hiyo kuweza kuchukua chakula na kupeleka kwenye maeneo ambayo yana upungufu. Hata jana tulikuwa tunazungumza pia na Mheshimiwa Mathayo, Mbunge wa Same Mashariki namna ambavyo Same imekuwa kame wakati wote, hata msimu ambao tunakuwa na mvua nyingi, kuona namna nzuri ambayo tunaweza kuwasaidia kupata chakula kwa kutumia pia hata wafanyabiashara wa ndani zaidi ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeanza kushuhudia kuona mvua zikinyesha ingawa siyo nyingi za kutosha, lakini basi pale ambako tunapata mvua angalau mara moja, mara mbili, tunawahamasisha wakulima kulima mazao ya muda mfupi ili yaweze kuiva kwa kipindi kifupi pia tuweze kujipatia chakula kwa msimu ujao wa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kutakuwa na tatizo lolote lile, Serikali hii iko bado inajua na inafuatilia mwenendo wa hali ya chakula na ufumbuzi tutaupata kupitia Serikali yenyewe.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Mheshimiwa Waziri Mkuu nafikiri una hakiki kutokana na vyanzo vyako mbalimbali kwamba Taifa katika wakati huu linakumbwa na sintofahamu, hofu na taharuki nyingi zinazosababishwa mambo kadhaa.
Mheshimiwa Spika, moja na la msingi ambalo napenda kukuuliza ni kwamba kuna hofu kuhusu haki ya kikatiba ya kuishi na kupata hifadhi. Kuna hofu kuhusu haki ya kikatiba ya kupata na kutoa habari ambayo inaweza kuchagizwa kwa kiwango kikubwa na kukosekana kitu kama
uhuru wa Bunge kusikika kwa wananchi ambao wametutuma mahali hapa.
Mheshimiwa Spika, kuna hofu kuhusu watu kupotea, watu kutekwa na jambo hili limetawala sana kwenye mijadala katika mitandao na vyombo vya habari na mfano halisi ukiwemo kupotea kwa msaidizi wangu Ben Saanane ni miezi sita sasa Serikali haijawahi kutoa kauli yoyote, haielezi ni nini kinafanyika jambo ambalo linapelekea pengine kuamini aidha, Serikali haitaki kufanya uchunguzi ama imeshindwa kufanya uchunguzi. Mheshimiwa Waziri Mkuu unalipa Taifa kauli gani kuhusu hofu na taharuki hii ambayo imelikamata Taifa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kwamba Taifa lina hofu ya kikatiba kwenye maeneo kadhaa lakini pia amerejea michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge iliyokuwa inazungumzia suala la usalama wa nchi kwamba Taifa na Watanzania wana hofu na kwamba bado Serikali hatujatoa kauli.
Mheshimiwa Spika, kupitia majibu yangu lakini pia wakati wa bajeti yangu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, jambo hili mara lilipojitokeza tulitoa taarifa ya awali na mimi niliwasihi Watanzania kwamba Taifa letu kwanza ni Taifa ambalo kwa miaka mingi limekuwa na utamaduni mzuri wa watu kuheshimiana, watu kufuata misingi, kanuni, sheria na taratibu. Pia tunatambua kuwa kumetokea matukio mbalimbali kwa miaka mingi huko na matukio haya tumeendelea kuyaachia vyombo vya usalama kufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa jambo ambalo limejadiliwa sana na Waheshimiwa Wabunge na hofu ambayo imekuwa ikielezwa kwamba Watanzania wana hofu, nilitumia nafasi yangu kuwasihi Watanzania kwanza waiamini Serikali yao kwamba moja kati ya majukumu ya Serikali yetu ni kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa amani na kwa uhakika wa ulinzi wa wao wenyewe na mali zao wakati wote. Pia hata Serikali yetu nayo imeweka azma hiyo na kwamba jambo hili tunaendelea kuliimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kupitia michango hiyo pia hata Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alieleza na mimi nikarejea kuimarisha hili kwamba Watanzania tunaomba mtupe muda, vyombo vyetu vinaendelea kufanya kazi ya kuchunguza ili tuweze kubaini ni nini hasa sasa kinatokea na ni kwa nini Watanzania wanafikia hapo kuwa na hofu. Haya yote huwezi kutoa matamko hadharani zaidi ya kuwasihi Watanzania kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa Taifa na kwamba vyombo vyetu vinapofanya kazi kama tutaweza kueleza haraka maazimio yetu tunaweza tukapoteza njia nzuri ya kupata vyanzo vya kwa nini kasoro hizi zinajitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nirudie tena na nimsihi sana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwamba Serikali ipo na imesikia haya kutoka kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge. Naomba niwasihi tena Watanzania kuwa na imani na Serikali yenu kwamba tunaendelea na ufuatiliaji wa matukio yote yaliyozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge tuone kwa nini yanajitokeza, nani anasababisha kwa sababu vyanzo vya matatizo haya ni vingi na vinahitaji uchunguzi wa kina ili tuweze kujua hasa dosari iko wapi na tuweze kudhibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wito wangu kwa Watanzania, tuendelee na utamaduni wa kutoa taarifa kwa vyombo vyetu pindi tunapojua kwamba hapa kuna jambo au linaandaliwa au limetokea na aliyesababisha ni fulani ili tuweze kuchukua hatua za papo kwa papo ili tuweze kunusuru watu wengine wasiweze kukubwa na matukio hayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge mwenzangu na Kiongozi mwenzangu hapa Bungeni tuendelee kuipa muda Serikali kufanya ufuatiliaji wa jambo hili na baadaye tutakapogundua kabisa tutakuja kuwapa taarifa ili Watanzania wawe na uhakika na shughuli zao wanazoendelea nazo. Ahsante sana.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ushahidi wa kutosha kabisa kuhusiana na wizi unaofanyika kwenye biashara yetu ya korosho hasa katika Mikoa ya Mtwara na Lindi kutokana na kazi iliyofanywa na TAKUKURU iliyobainisha kwamba kumekuwa na upotevu wa kiasi kikubwa sana cha fedha ambacho ni takribani shilingi za Kitanzania bilioni 30 kutoka kwenye Bodi ya Korosho. Hata hivyo, mimi binafsi na naamini na wengine hawajasikia tamko lolote juu ya jambo hili kutoka Serikalini. Je, leo Serikali inatuambia nini kuhusu ubadhirifu huu uliotokea hapa nchini kwetu hasa kwa wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kwa sababu jambo hili linaweza kutokea sehemu yoyote ndani ya nchi yetu? Naomba majibu ya Serikali.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwenendo wa vyama vyetu vya ushirika nchini umeweza kuanza kuonyesha dalili ambayo si nzuri kwa sababu ya upotevu mkubwa wa mapato ya fedha za ushirika ambayo pia inapelekea kukatisha tamaa wakulima wetu kote nchini. Ni kweli kwamba Serikali imechukua hatua thabiti kufanya mapitio ya vyama vyote vya ushirika kwa mazao yetu makubwa ambayo yanatuingizia pato kubwa nchini na yanaleta manufaa kwa wakulima wetu. Tulianza na zao la korosho baada ya kupata tuhuma hizo tulipeleka wakaguzi COASCO na baadaye tukapeleka TAKUKURU kwa uchunguzi zaidi lakini kupitia vikao mbalimbali vya wadau wa mazao yenyewe huwa wanabainisha kasoro zinazojitokeza kwenye uendeshaji wa mazao hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa kumbukumbu zangu na kwa kuwa mimi mwenyewe pia ni mdau wa zao la korosho tulikuwa na kikao Bagamoyo ambacho pia kilitoa taarifa ya ubadhirifu wa shilingi bilioni 30 kwa Bodi yetu ya Korosho Mkoani Mtwara. Serikali iliunda timu maalum pamoja na TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi, lakini baadaye uchunguzi ulibaini kwamba hasara ile ni ya shilingi billioni sita na siyo shilingi bilioni 30 kwa Bodi ya Korosho na hasara ile haikusababishwa na Bodi ilisababishwa na Vyama Vikuu pamoja na Vyama vya Ushirika vilivyoko kwenye ngazi za kijiji na kata. Hatua kadhaa zimechukuliwa kwa watendaji wote ambao wamehusika kwenye ubadhirifu. Vyama vya msingi na vyama vikuu vyote vilifanyiwa uchunguzi na hatua thabiti zimeanza kuchukuliwa na nyingine zitaendelea kuchukuliwa kadiri tunavyoendelea.
Mheshimiwa Spika, lakini nataka niwaambie Watanzania kwamba jambo hili la ushirika haliko kwenye zao la korosho pekee liko pia kwenye mazao kama tumbaku, pamba, kahawa, chai na mazao mengine yote makuu. Tumeanza kufanya mapitio ya kaguzi za kina kwenye ushirika wa mazao haya kubaini ubadhirifu ili tuweze kufanya marekebisho ya namna nzuri ya kuendeleza mazao haya ili wakulima waweze kupata tija. Kwa sasa tunaendelea na zao la tumbaku, ukaguzi unaendelea na tumeanza na chama kikuu sasa tunaenda kwenye AMCOS tukishamaliza tutaenda kwenye mazao mengine yakiwemo pamba, kahawa, chai na yale yote ambayo yameunda ushirika kwa lengo la kuwalinda wakulima, kuhakikisha kwamba fedha za wakulima zinawafikia wakulima wenyewe na hii ni pamoja na kuondoa tozo ambazo zimewekwa na vyama vyenyewe ambavyo pia vinamletea hasara mkulima.
Mheshimiwa Spika, naomba kusisitiza tu kwa Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua hizi zinaendelea kuchukuliwa na tutaendelea kuhakikisha kwamba ushirika nchini unaimarika na unaongozwa na watu waaminifu ambao hawatawaletea hasara wakulima wetu, ahsante.
MHE: GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kunipa nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu jitihada za Serikali ya Awamu hii ya kupigania sera ya Tanzania ya viwanda ambalo ni jambo muhimu sana kila mtu mwenye akili timamu analipongeza. Hata hivyo, ili suala la viwanda liweze kuwa ni la uhakika na kweli ni lazima investors ama wafanyabiashara wawe na mazingira huru na mazingira yasiyokuwa na mashaka katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku za biashara ili kuelekea katika investment hizo za viwanda.
Mheshimiwa Spika, Tanzania Revenue Authority (TRA) wamekuwa wakitesa na kusumbua sana wafanyabiashara hasa wa mikoa mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya. Katika kila mkoa na hasa mimi nakotoka Arusha, TRA wamekuwa wakitumia Polisi, Usalama wa Taifa na TAKUKURU kuwasumbua wafanyabiashara, kuwatishia mpaka kesi za money laundering kwenye masuala yanayohusu kodi. Sasa ili wafanyabiashara hawa waweze kufanya kazi zao kwa uhakika na waweze kuwa na confidence ya uwekezaji katika Taifa hili, nini kauli ya Serikali juu ya mfumo wa TRA unaotumika sasa wa kusumbua na kuwapa taabu wafanyabiashara katika shughuli zao za kila siku?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Lema, Mbunge wa Arusha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba tunacho chombo ambacho kinawajibika katika ukusanyaji wa kodi kutoka kwa walipa kodi wetu wakiwemo wafanyabiashara. Pia wafanyabiashara hawa pamoja na haki yao ya kulipa ambayo kila mmoja ni wajibu wake kulipa tunatambua kwamba wako wafanyabiashara ambao wana madeni sugu. Jambo ambalo nalieleza nimelishuhudia pia hata kwenye televisheni na tuliwahi kupata taarifa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha pale ambapo TRA kupitia chombo chake Makao Makuu kiliunda task force ya ufuatiliaji wa madeni sugu kwa wadaiwa sugu na wadaiwa sugu wale si wote lakini wachache hawataki kabisa kulipa pamoja na kwamba wanajua wao ni wadaiwa sugu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, task force ilikuwa na mkakati wa kuwapitia wadaiwa sugu wale wachache ili waweze kulipa madeni yao. Sasa ile task force iliundwa kwa pamoja na TRA wenyewe, kulikuwa na Jeshi la Polisi pamoja na TAKUKURU ili kuona kuwa wanapokwenda kule hakutumiki vitendo ambavyo havikubaliki kama vile utoaji wa rushwa ili madeni hayo yasilipwe au namna nyingine yoyote ambayo pia mfanyabiashara anaweza kuona kwamba si sahihi kwake. Kwenye msafara ule tuchukue mfano wa Arusha tulipata taarifa kwamba Polisi walikuwa wanatembea na silaha lakini si kwa lengo la kumtisha mfanyabiashara ni kwa sababu ya utaratibu ambao jeshi inao hasa wanapokwenda kufuata fedha kama zinaweza kulipwa papo kwa papo. Kwa hiyo, ile ilileta mtikisiko kidogo kwa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii pia kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwamba aliita wafanyabiashara pamoja na TRA na kueleza kwanza umuhimu wa ulipaji kodi kila mmoja atambue na walipaji sugu watambue kwamba ni haki yao kulipa kodi kwa biashara ambayo wameifanya. Pia alieleza vyombo vyetu zile silaha iwe ni kwa ajili ya kulinda tu ule msafara kwa sababu pia wanahusika kukusanya fedha lakini sio kwa ajili ya kumtisha mfanyabishara. Kwa hiyo, aliweza kurudisha amani na kuondoa mashaka waliyonayo wafanyabiashara na kuwafanya wafanyabiashara na TRA kuwa marafiki na huo ndio msisitizo wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nataka niwaambie wafanyabiashara kwamba TRA inao utaratibu wa wafanyabiashara ambao wanadhani wanatendewa sivyo. TRA imeunda dawati ambalo liko katika kila mkoa la kusikiliza kero za wafanyabiashara pindi inapotokea kuna vitendo ambayo si sahihi. Kwa hiyo, watumie madawati hayo kupeleka malalamiko yao na tunaamini madawati hayo yatafanya vizuri. Jambo la msingi kwa wafanyabiashara na walipa kodi wote ni kufahamu kwamba ni muhimu kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie kwamba Serikali inaheshimu wafanyabiashara, Serikali inatambua wawekezaji wote pamoja na wale wanaoendesha viwanda na maeneo mengine na tutawapa ushirikiano, waendelee kutambua umuhimu wao wa kulipa kodi na sisi tutaheshimu kodi yao wanayotupa na kila mmoja ajue wajibu wake. TRA yetu kama ambavyo tumesema iendelee kutoa elimu kwa wafanyabiashara na walipa kodi wote ili tuweze kupata kodi kwa njia ambayo haimpelekei hofu mfanyabiashara. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, nami naomba nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa moja ya sababu ambazo zilipelekea wananchi wengi kutoa ridhaa kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuongoza ilikuwa ni ahadi nzuri ambazo zilitolewa. Pamoja na kuwa ahadi hizo nyingi zimeanza kutekelezwa lakini kulikuwa kuna kilio kikubwa sana cha wafanyakazi kwa ujumla kutokana na malimbikizo ya madeni na mishahara yao na hasa walimu. Serikali inasemaje kuhusu suala hili ili waweze kupata moyo wa kuona kweli zile ahadi ambazo walipewa na mgombea wa Chama cha Mapinduzi zimetekelezwa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Mwamoto Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali tunao watumishi wengi walimu wakiwemo na kama watumishi kwa sababu wanafanya kazi zao za kila siku na nyingine zinahitaji kulipwa malipo ya ziada mbali na malipo ya mshahara, nikiri kwamba tunadaiwa na watumishi wetu ikiwemo na walimu pia. Hata hivyo, Serikali yetu imeahidi kumaliza kwa kiasi kikubwa kero hii ya madeni kutoka kwa watumishi wetu wa Serikali walimu wakiwemo. Hatua ya awali ambayo tumeichukua ni kufanya mapitio ya madeni yetu yote tunayodaiwa na watumishi ikiwemo na walimu.
Mheshimiwa Spika, madeni ya walimu yote yalishakusanywa na yalihakikiwa kwanza na Wakaguzi wa Ndani wa kila Halmashauri mahali walipo lakini madeni yale pia yameendelea kuhakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa maana ya timu ambayo imeundwa pamoja na Wizara ya Fedha ili kuona uhalali wa madeni hayo baada ya kuwa tumegundua kuwa baadhi ya madeni yamepandishwa kwa kiasi kikubwa ambayo sio halali. Kwa hiyo, kila hatua tunayoifikia ya kukusanya madeni na kuyahakiki tukishapata kiwango tunaendelea kulipa. Kwa hiyo, Serikali imeendelea kulipa madeni ya wafanyakazi na inataka iwahakikishie wafanyakazi kwamba madeni yao yatalipwa na hiyo ndiyo stahili yao na kwa sababu tumeanza kulipa, tunaendelea kulipa kadri ambavyo tunamaliza kuhakiki ili tuweze kuondokana na madeni haya. Pia Serikali haijaishia hapo. Tumeweka utaratibu wa kudhibiti uzalishaji wa madeni kwa watumishi wetu na kusisitiza watu wafuate Kanuni na taratibu za eneo linazozalisha madeni ili tuweze kuondoa madeni ambayo sio muhimu wakati mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nataka nitumie nafasi hii pia kusema kwamba baadhi ya madeni ambayo hayana viwango vikubwa yanaweza kulipwa kwenye Halmashauri zenyewe mbali ya kulipwa na Serikali Kuu. Lazima nimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha ambaye kupitia mapato yake ya ndani na kupitia Baraza lake la Madiwani waliweza kulipa madeni ya watumishi wao hasa walimu ya zaidi ya shilingi milioni mia moja na zaidi. Kwa hiyo, mfano huu ni mzuri kwa Wakurugenzi wengine kwenye Halmashauri nyingine ili kuondoa kero kwenye maeneo yao. Wanaweza kutenga fedha kupitia mapato yao ya ndani kulipa watumishi wao wakiwemo walimu ili kuondokana na ule mlolongo ambao tunatakiwa tuuhakiki. Wakishahakiki wakijiridhisha na hasa baada ya kuwa tumedhibiti madeni na wao wanaweza kuruhusu kazi fulani zifanywe, wazitengenezee bajeti ili waweze kulipa moja kwa moja kuondokana na kero zinazoweza kupatikana kwa wafanyakazi.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kumuuliza Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Bunge kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63(2), ndicho chombo kikuu chenye mamlaka na wajibu wa kuisimamia na kuishauri Serikali. Katika Bunge hili, Bunge la Kumi na Mabunge mengine kadhaa, Bunge limekuwa linatoa Maazimio kadhaa kuitaka Serikali itoe taarifa na Serikali imekuwa inaahidi kutoa taarifa, lakini taarifa nyingi ambazo ni Maazimio ya Bunge yamekuwa hayatekelezwi na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna Maazimio ya Bunge kuhusiana na Tokomeza mpaka leo Serikali haijaleta majibu. Kuna Maazimio ya Bunge kuhusiana na ESCROW na IPTL, Serikali mpaka leo haijatoa majibu. Kuna Maazimio ya Bunge kuhusu mabilioni ya Uswis, Serikali mpaka leo haijatoa majibu na Maazimio mengine mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu unaliambia nini Bunge na unaliambia nini Taifa. Wewe kama Kiongozi wa Serikali Bungeni, utapenda kusema kwamba Serikali inalidharau Bunge ama Serikali haina majibu ya kutoa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe, Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nikuhakikishie kwamba Serikali inaheshimu sana Mhimili wa Bunge na inathamini sana maamuzi ya Mhimili huu wa Bunge na tutaendelea kushirikiana na Mhimili wa Bunge katika kupata ushauri na namna nzuri ya kuendesha Serikali kwa mapendekezo ambayo yanatolewa na Waheshimiwa Wabunge kupitia chombo cha Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua vikao kadhaa huko awali kumekuwa na Maazimio yanayoitaka Serikali ilete maelezo, lakini baadhi ya maeneo ambayo yanatakiwa kuletwa hapa ni yale ambayo yanahitaji uchunguzi wa kina na uchunguzi huu unapokamilika ndipo unapoweza kuletwa Bungeni.
Sasa yapo ambayo tunaona upo umuhimu wa kuyaleta ni pamoja na hayo uliyoyasema, nataka nikuahidi kwamba haya ambayo umeyatamka kwenye maeneo yanayogusa Wizara kadhaa ambazo zinatakiwa kuleta taarifa nitafanya ufuatiliaji, pale ambapo tutakuwa tumekamilisha uchunguzi wetu, nitayaleta kwa utaratibu ambao Bunge utakuwa umetoa maelekezo yake. Ahsante sana.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa umakini na utendaji wake na kilichonivutia zaidi anapotoka hapa akienda ofisini kwake haifiki hata dakika, watu anaokutana nao njiani anasalimiana nao ni jambo la kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri bila kujali itikadi ya chama. Ninakupongeza sana, mara nyingi huwa nikikaa nje pale na nikienda kunywa chai ninakuona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakaribiwa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kama wiki mbili tu panapo majaaliwa tukifika, hali ya kusikitisha ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, sukari inahitajika kwa wingi matumizi yake. Hata wananchi wa Ruangwa na Peramiho wanahitaji sukari. Mwenyezi Mungu alitupa mtihani wa mvua, viwanda vyetu vya ndani havikuweza kuzalisha sukari ya kutosha na uchunguzi au harufu niliyoipata tunahitaji kama tani laki moja na ushee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha kwa taarifa niliyo nayo ni kuwa mmetoa vibali vya tani 30,000 na baya zaidi kuna msemo Waislamu husema nguo ya Ijumaa hufuliwa Alhamisi na mvua hii pengine isikauke. Sasa hawa mliowapa vibali, sukari yao navyotegemea hata ikifika Ramadhani itakwisha, itawasaidia nini wananchi? Mnatumia utaratibu gani kuwapa vibali hawa watu, wanarudia ndiyo wale wale au na wengine? Kuna formula gani ili kuokoa hatua hii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu uko tayari kuleta watu angalau mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani wakaingiza sukari kwa kipindi hiki ili kuokoa hii hali na janga hili lilivyo? Hii sukari mliyowapa vibali hata ikifika Ramadhani itakwisha, itasaidia nini kwa wananchi?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, najua amezungumza mengi na yaliyotengeneza maswali mengi sana. jambo la msingi alilotaka kuzungumza hapa ni kupungua kwa sukari na mahitaji ya sukari nchini kwa sasa. Napenda niwathibitishie Watanzania kwamba Serikali iko macho na inajua maeneo gani yanahitaji kuboreshwa kulingana na mahitaji ambayo yanahitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la sukari ni kweli nchi yetu hatuna uzalishaji wa kutosha wa sukari kutosheleza mahitaji ya Watanzania. Katika mwaka wa kilimo, mahitaji ya sukari nchini ni zaidi ya tani 420,000, lakini uzalishaji tulionao hapa nchini ni tani 320,000; kwa hiyo tunakuwa na mapungufu ya sukari inayohitajika ya tani laki moja na ikiwezekana zaidi kwa sababu ya ongezeko la watumiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka tunao utaratibu wa kuagiza sukari na mwaka huu pia tumesahafanya hilo, tumeshaagiza sukari na mwaka huu tumeagiza sukari tunataka tuagize sukari ya tani 131,000 kwa mujibu wa takwimu zilizofanyiwa utafiti na Bodi ya Sukari, kati ya hizo tayari tumeshaagiza tani 80, kati ya tani 80 tayari zimeshaingia tani 35 na nyingine ziko bandarini. Hizi tani 35 tumeshaanza kuzigawa kwenye maeneo yote ya nchi ili ziweze kufika kwa wananchi ziweze kusaidia kupunguza gharama na bei.
Mheshimwa Naibu Spika, pia kwa kuwa, tunakabiliwa na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo watumiaji ni wengi, utaratibu wa kuagiza sukari zaidi kufikia malengo umeshaandaliwa. Watanzania tushirikiane kuwasihi wafanyabiashara ambao sasa hivi wamepandisha bei bila sababu na hii inaumiza sana Watanzania kwa sababu bei zilizopandishwa hazina umuhimu wowote kwa sababu uzalishaji tulionao na hii sukari pengo tunavyoleta nchini inataka tu bei zile ziendelee kuwa ambazo zinaweza kuhimilika na Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, iko mikakati ya kuongeza uzalishaji kufikia malengo. Natambua tuna viwanda vinne, Kagera Sugar, Kilombero, TPC na Mtibwa, tuna kiwanda cha tano kilichoko Tanzania Visiwani, Mahonda navyo pia vinasaidia uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa tatizo la kuagiza sukari nje ya nchi, tumejiwekea utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara wenye viwanda na kuwasihi kuongeza uzalishaji na tumeona jitihada kadhaa ambazo zinafanywa na wazalishaji. Bahati nzuri sana wiki moja iliyopita nilikuwa Mkoani Kilimanjaro, nimepata nafasi ya kutembelea kiwanda cha TPC ambacho kimeonesha mafanikio makubwa ya uzalishaji zaidi. Mwaka jana walizalisha tani 100,000 na sasa wameongeza tani 20,000, kwa hiyo, sasa hivi wamefikia uwezo wa kuzalisha tani 120,000 na msimu huu wa kilimo wataongeza tani nyingi zaidi, hivyo hivyo na viwanda vingine kama Kilombero na Mtibwa Sugar.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilipofanya ziara Mkoani Manyara, nilitembelea Manyara Sugar, kwa hiyo viwanda vingi vinaendelea kujengwa na sasa tunakamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkoani Morogoro kuna eneo la Mbigiri kwa ushirikiano na Magereza pia na eneo la Mkulazi ambalo linaandaliwa na Taasisi ya NSSF na PPF kwa pamoja na wawekezaji ambao pia wako tayari kutuunga mkono katika uzalishaji wa sukari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaondoe mashaka Watanzania kwamba sukari ipo na wakati wa Ramadhani sukari ya kutosha itakuwepo wala hakuna sababu ya kuongeza bei, tutafanya hivyo na pia ufuatiliaji kuona bei haziongezeki ili kuwakera Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kumuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu imekuwa na sera nyingi sana, sera ambazo mara nyingi utekelezaji wake ama ni pungufu au hazitekelezwi kabisa. Sera hizi mara zote kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi zimekuwa zikirudiwa rudiwa mara nyingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo swali langu litaenda kwenye Sera ya Maji ya mwaka 1991 ambayo lengo kubwa ilikuwa wananchi wetu waweze kupata maji kwa umbali wa mita 400, utekelezaji wa sera hii mpaka ifikapo mwaka 2002, siyo hivyo tu, Julai 2002 hiyo baada ya ile sera kuwa haijafikiwa, ikafanyiwa mapitio tena, ikatambua kwamba maji ni uhai, maji ni siasa, maji ni uchumi, vilevile ikaingizwa rasimu ya kwamba maji na mazingira.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, mpaka leo hii wananchi wetu wamekuwa na janga kubwa la maji. Ni nini kauli ya Serikali juu ya utekelezaji wa sera hii?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kwamba sera hiyo tunayo na huo ndiyo msisitizo wetu na hata bajeti ambazo Waheshimiwa Wabunge huwa mnazipitia kila mwaka zinalenga kufikia hatua hiyo. Nataka niwahakikishie kwamba pamoja na mipango ya Serikali ya usambazaji wa maji, pamoja na kutenga bajeti ambazo tunazo huku ndani, bado tunapata tatizo kubwa nchini la kupatikana kwa vyanzo vya kutosha vya maji vinavyoweza kutosheleza kusambaza maji kwa kiwango ambacho tumejiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sera ni malengo na malengo yetu tunataka tuyafikie, tunapata changamoto kwenye utekelezaji kama ambavyo nimeeleza. Sasa hivi nchi imekumbwa na uharibifu mkubwa sana wa mazingira na nimelieleza mara kadhaa. Maeneo haya yamesababisha kukosekana upatikanaji wa maji na miradi mingi ambayo inatakiwa itekelezwe ni ya gharama kubwa kwa sababu inatakiwa tufuate maji kwenye umbali mkubwa ambapo gharama zake ni kubwa, hiyo sasa inakuja kugongana na mahitaji pia ya bajeti. Waheshimiwa Wabunge sasa hivi tuko kwenye Bajeti ya Maji ambayo mnaendelea kujadili na kushauri Serikali na Serikali kwa usikivu tulionao tutaendelea kuwasikiliza na kuyachukua yale yote muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutumia nafasi hii kuwasihi Waheshimiwa Wabunge tushirikiane sana katika kuhakikisha mazingira yetu nchini yanalindwa ili tuwe na vyanzo vya kutosha, Serikali imudu kuchimba visima hata vya urefu wa kati au urefu mfupi ili kuweza kumudu kusambaza maji kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ambalo tunalipata sasa ni hilo la kukosekana kwa vyanzo sahihi vya maji. Lakini pia nitumie nafasi hii kuwasihi Watanzania, tuendelee kuvitunza vyanzo vyetu vya maji ili Serikali isitumie gharama kubwa kutafuta mradi ambao maji yake hayatoshi na kama unayapata ni ya muda mfupi kwa sababu huku juu kote kuko kweupe na jua linavyopiga maji yote hukauka.
Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie kwamba Ilani yetu inayosema katika kipindi cha miaka mitano tunataka tufikie hatua fulani, tutaitekeleza. Serikali ya Awamu ya Tano sasa tuna mwaka mmoja na tunaomba ridhaa yenu mwaka wa pili wa utekelezaji, mpaka kufikia mwaka 2020 kama miaka mitano ya ahadi zetu, tunatarajia sehemu kubwa ya nchi kwenye vijiji, kata na miji mikubwa tuwe tunapata maji kwa kiwango ambacho tumejiwekea commitment kwenye sera ya kufikia mita 400 kila mmoja aweze kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumemuona Makamu wetu wa Rais, Mama Samia Suluhu akipita kuzindua miradi mingi sana, naomba sasa mtupitishie bajeti yetu ambayo tunaijadili hapa ili tuendelee kutoa huduma za maji. Tunajua tuna changamoto, inaweza kuwa fedha kidogo lakini tutaendelea kuwa na miradi mingi sana ambayo tutaifungua. Juzi tumefungua mradi mkubwa sana Tabora, unaotoa maji Shinyanga, Ziwa Victoria, tunasambaza Tabora na Wilaya zake zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea na miradi mikubwa kama hiyo, tutaendelea kuzungumza na marafiki zetu ambao pia tunapata miradi ili tuweze kusambaza miradi hii kwenye vijiji na kwenye umbali ambao tumeuweka kwenye sera yetu. Ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunapoingia kwenye chaguzi vyama pamoja na wagombea huwa wanawaahidi wananchi ili waweze kuwaamini na kuweza kuwapa nafasi katika nafasi mbalimbali wanazogombea. Mnamo tarehe 5 Oktoba, 2015 mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia katika uwanja wa Barafu Manispaa ya Dodoma alikutana na mabango mbalimbali ya wananchi wa Manispaa ya Dodoma wakilalamikia suala la CDA na mgombea Urais Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliwaahidi wakazi wa Manispaa ya Dodoma endapo watampatia kura za kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jukumu lake la kwanza ni kuifuta CDA.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakazi wa Manispaa ya Dodoma wanapenda kujua ni lini ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itakwenda kutekelezwa? Ahsante
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika naomba kujibu swali la Mhesimiwa Kunti, Mbunge wa Dodoma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa anafanya ziara maeneo mbalimbali amekuwa akitoa ahadi kadhaa. Nataka nirudie kusema tena kwa Watanzania kwamba ahadi ambazo Mheshimiwa Rais ameziahidi tutajitahidi kuzitekeleza kwa kiasi kikubwa ikiwemo na uboreshaji wa Mji wa Dodoma, pia moja ya ahadi yake ilikuwa ni kwamba katika awamu yake hii kufikia mwaka 2020 atahakikisha Serikali inahamishia Makao yake Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ikiwa ni moja kati ya mambo ambayo aliyaahidi na tumeyatekeleza, mbili kwa kuwa tayari Serikali imehamia Dodoma lazima sasa tuandae utaratibu wa uboreshaji wa mazingira ya Mji wa Dodoma ili utawala wake, uendeshaji uweze kuwa rahisi ikiwemo na kupitia sheria mbalimbali zilizoiunda CDA, kuzifanyia mapitio na kuziboresha ili tuweze kuachana na CDA tuwe na mfumo ambao utatoa nafasi kubwa ya kukaribisha watu wa kawaida, wawekezaji na kuitumia ardhi iliyopo kwenye Manispaa katika kuwekeza au vinginevyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa nikiri kwamba kwa Sheria ya CDA huwezi kuleta mwekezaji hapa kwa sababu ni CDA pekee ndiyo imepewa ardhi hii na wao ndiyo waliopewa hati na ardhi Makao Makuu. Kwa hiyo wao wasingeweza kutoa hati kwa wananchi wanaojenga au wanaowekeza hapa, ili kuwapa nafasi wananchi kuwa na hati ya umiliki wa ardhi lazima tufute Mamlaka ya CDA ili tuweze kutumia Sheria ya Ardhi katika kutoa ardhi iliyopo hapa ili tuweze kukaribisha wawekezaji na uboreshaji wa mpango ambao sasa tumeukamilisha kuhamia Makao Makuu Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikutoe wasiwasi kwamba sasa tunafanya mapitio na Mheshmiwa Rais ameshatoa maagizo Tume imeshaundwa inafanya mapitio ya namna bora ya kuifuta CDA lakini kupitia sheria zilizoiweka CDA, hiyo ndiyo hatua ambayo tumeifikia na katika kipindi kifupi tutakuwa tumeshatoa taarifa. Ahsante.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, hapo nyuma kidogo Serikali ilitoa agizo kwa nia njema kabisa ya kutaka kutunza na kuboresha mazingira yetu, agizo lenyewe lilitutaka wananchi maeneo mbalimbali katika nchi kuhakikisha kwamba mwishoni mwa wiki tunafanya usafi wa mazingira.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, jambo hili ni jema sana na sisi wananchi tulilipokea vizuri sana katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Jambo hili limesababisha kero na usumbufu mkubwa kwa wananchi, hasa kwa kufungwa huduma muhimu wakati wanapokuwa wanazihitaji, huduma kama vile vituo vya afya, zahanati hata mahospitalini asubuhi ya siku ya Jumamosi wananchi wamekuwa hawapati huduma ipasavyo, migahawa pia katika maeneo ya miji imekuwa ikifungwa.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, Serikali ipo tayari sasa kutoa ama kuboresha agizo hili ili wananchi wale waendelee kupata huduma ipasavyo wakati huu wa asubuhi wa mwisho wa wiki?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka msisitizo wa nchi yetu kuwa safi kwenye maeneo tulimo, kwenye makazi, maeneo ya jumuiya, maeneo ya utoaji huduma ili kuifanya nchi kuwa safi kama ambavyo sasa tunaona maeneo kadhaa yana usafi unaoridhisha lakini bado tunatakiwa tuongeze nguvu. Utaratibu ambao tumeutoa ni kwamba tumekubaliana nchi nzima kila Jumamosi moja ndani ya mwezi mmoja kadri Mikoa ilivyojipangia au Wilaya ilivyojipangia ni kwamba Watanzania wote lazima tujihisishe kwenye usafi wa maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika makazi yetu lakini na maeneo ya jumuiya kama vile vituo vya mabasi, hospitali na maeneo mengine. Utaratibu unaendelea, Mheshimiwa Mbunge ameomba kujua utaratibu unaotumika na baadhi ya maeneo wa kufunga maeneo muhimu, nasi tumesisitiza kwamba viongozi wa maeneo hayo ambao wanatambua kwamba eneo hili ni la utoaji huduma za jamii ambao ni muhimu, waweke utaratibu mzuri wa namna ya utoaji huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu suala la usafi ni kuanzia saa 12.00 na tumesema angalau mpaka saa 4.00 asubuhi, kwa hiyo ni kwa saa manne tu. Kama eneo hilo linaweza kuvumilika kusitisha kwa muda fulani ili kuruhusu kufanya usafi ni vizuri, lakini kama eneo hilo lina mahitaji makubwa ya utoaji wa huduma basi Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Kijiji na viongozi wa maeneo hayo waweke utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wanaosimamia zoezi hili waangalie umuhimu wa utoaji huduma wa maeneo ya jumuiya kama ni lazima yafungwe kwa saa manne hayo au vinginevyo ili kuruhusu kufanya usafi. Kwa mfano maeneo ya hospitali hatuwezi kuyafunga hili eneo lazima liwe wazi wakati wote kwa sababu tunazo dharura zinaweza kutokea wakati wowote. Hivyo muhimu zaidi ni kuweka utaratibu wa usafi wake kwanza kabla ya siku ya Jumamosi ili Jumamosi huduma ziweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya migahawa yenyewe wakati wote yanatakiwa yawe safi hata bila kuwa na Jumamosi, ni muhimu zaidi wale waendesha migahawa wahakikishe maeneo hayo yanafanyiwa usafi vizuri na siku ile ya Jumamosi kama kiongozi wa eneo hilo anaona kuna umuhimu wa eneo hilo kutofunga ili shughuli ziendelee basi tujiridhishe kwamba eneo hilo liko safi, kwa vile usafi ule unajumuisha wananchi wote kwa pamoja kutoka kwenye eneo hilo, watumishi wa eneo hilo waingie kwenye usafi kwa pamoja ili waweze kushiriki kikamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu zaidi ni kiongozi wa eneo hilo kuona umuhimu wa eneo hilo na mahitaji yake, aweke utaratibu mzuri kwa ajili ya kufanya kazi bila kuzuia huduma nyingine kuendelea. Ahsante.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa ni sera ya Serikali kuboresha kilimo hapa nchini, ikizingatiwa kwamba kilimo kinatoa ajira kwa Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80 na kilimo kimekuwa kikihudumia Watanzania kwa maana ya kujitosheleza kwa chakula, lakini kwa kuwa pia ni sera Serikali iliamua kuja na mikakati ya kuboresha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kutoa majukumu kwa mawakala wa pembejeo hapa nchini ili waweze kutoa huduma hizo za pembejeo kwa wakulima wetu hapa nchini.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, mawakala wa pembejeo wamefanya kazi yao kwa uadilifu mkubwa toka mwaka 2014/2015; 2015/2016 lakini mpaka sasa hivi mawakala hao hawajalipwa fedha zao.
Je, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni sera ya Serikali kuwarusha mawakala ambao wamefanya kazi yao vizuri?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba nitumie nafasi hii kutoa pole kwa Watanzania, pia kwa Kambi ya Upinzani inayoongozwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe, kwa kifo cha kiongozi wetu wa kisiasa toka Kambi ya Upinzani toka Chama cha CHADEMA Mheshimiwa Philemon Ndesamburo ambaye jana alitangulia mbele za haki, nitoe pole pia kwa mke na watoto wa marehemu, nitoe pole pia kwa Wabunge wenzangu kwa sababu Mheshimiwa Marehemu Ndesamburo tulikuwa naye hapa ndani ya Bunge. Nitoe pole pia kwa Watanzania wote kwa sababu tumempoteza kiongozi ambaye alionesha uwezo mkubwa wa kulitetea Taifa, alionesha uwezo mkubwa wa kusemea Watanzania kwa ujumla wake. Sote kwa pamoja tumuombe marehemu Mzee wetu Ndesamburo ili Mwenyezi Mungu aweze kuiweka roho yake mahala pema.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Minja, Mbunge wa Morogoro kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sera ya Serikali, moja kati ya mambo muhimu ni kuboresha kilimo na Serikali za awamu zote zimeendelea kufanya vizuri kwenye eneo hili kwa kusisitiza kilimo na Serikali tunatambua kwa asilimia zaidi ya 80 ya Watanzania tunategemea kilimo. Hata mpango wetu wa sasa wa Tanzania ya viwanda na uchumi wa viwanda unategemea kilimo zaidi ili kuendesha viwanda vyetu. Nikiri kile ambacho umesema Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapata msaada sana na Watanzania ambao wanajitoa katika kuunga mkono jitihada za Serikali kwa usambazaji wa pembejeo, kufanya kazi mbalimbali za kilimo na namna ambavyo wanajitahidi kuwa wavumilivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakiri kwamba ni kweli wanatudai, lakini katika hili nataka niseme ukweli kwamba tulipoanza mfumo wa utoaji wa pembejeo kwa njia ya vocha na kuwatumia hawa mawakala kutupelekea pembejeo hizi kwa wakulima kule vijijini, zipo dosari kadhaa ambazo tumeziona. Moja ya dosari kubwa ambayo tumeiona ni kwamba baadhi ya mawakala, wachache wamekuwa siyo waaminifu sana. Kwamba walikuwa wanashirikiana na watendaji wetu wa vijiji kule katika kuorodhesha majina ya wakulima ambao si wakulima na hawapo, wamewapa mbolea, madawa na kudai fedha nyingi sana ambazo hazipo na tukajikuta tuna deni ya zaidi ya shilingi bilioni 65. Ninazo kumbukumbu kwa sababu hao mawakala wote nimekutana nao, tumekaa nao hapa tumejadili namna nzuri lakini tuliwaambia dosari hii kwa wachache wao na kwamba tumewahakikishia Serikali itawalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka tufanye jambo moja lazima tujiridhishe tuende kwenye vijiji kupitia watendaji ambao ni waaminifu kufanya uhakiki wa kama kweli pembejeo hizi ziliwafikia wakulima ili tueze kujua deni halisi. Nataka nikuhakikishie baada ya kuwa tumeanza uhakiki huo maana yake tumeshafanya uhakiki awamu ya kwanza. Kati ya shilingi bilioni 35 zilizoonekana kwenye orodha ya madeni ya awali tulipata shilingi bilioni sita tu ambazo Serikali inadaiwa. Lakini bado tuna shilingi bilioni 30 nyingine ambazo sasa na kwa mujibu wa mazungumzo yangu na mawakala wote ambao walikuja hapa wiki mbili zilizopita tumekubaliana. Kimsingi kwanza, tumewasihi waendelee kuwa wavumilivu pia tumeshukuru kwamba wamekuwa wavumilivu kwa kiasi hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu tufanye huo uhakiki ili tujue Serikali hasa inadaiwa kiasi gani ili tuweze kuwalipa. Nataka nikuhakikishie kwamba kazi hiyo inaendelea na tuko kwenye hatua za mwisho na tutawalipa madeni yote. Kila aliyefanya kazi vizuri kwa uaminifu, deni lake atalipwa kwa sababu hiyo ni stahili yake na kweli umefanya kazi nzuri ya kufikisha pembejeo kwa wakulima na tunatambua mchango wao na tutaendelea kuheshimu mchango wao. Ahsante sana.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, baadhi ya walimu wenye ulemavu kutegemeana na ulemavu walionao wanahitaji vifaa maalum vya kujifunzia na kufundishia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Vifaa hivyo ni pamoja na mashine za maandishi ya nukta nundu, shime sekio pamoja na vifaa vingine. Natambua kazi nzuri iliyofanywa ofisi yako pia Wizara ya Elimu kwa kutoa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. Bado tatizo lipo kwa walimu hasa kwa kuzingatia kwamba sio walimu wote wenye ulemavu wanaopangiwa kwenye shule zenye mahitaji maalum ambazo shule hizo zina vifaa hivi.
Je, wewe kama Baba na hasa kwa kuzingatia masuala haya ya watu wenye ulemavu yako chini ya ofisi yako, nini kauli yako ili kuhakikisha kwamba walimu hawa wanatekelezewa mahitaji yao na kutimiza majukumu yao pasipo matatizo yoyote?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina uratibu mzuri sana wa kuhahakisha kwamba Watanzania wenzetu wenye mahitaji maalum wanapata huduma stahiki ili waweze kukamilisha shughuli zao za siku katika nyanja mbalimbali. Moja kati ya ushahidi kwamba jambo hili limeratibiwa vizuri Serikali zote zilizopita pamoja na hii ya Awamu ya Tano tumeweza kutenga Wizara inayoshughulikia Watanzania wenzetu ambao wana mahitaji maalum. Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo mimi mwenyewe nipo, ndio hasa Wizara ambayo inashughulikia kwa ujumla wake, lakini tuna Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) zote hizi zinaratibu kwa namna ambavyo tumepanga utaratibu wa kufikisha huduma hii mahali hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hawa wote ambao wana mahitaji maalum, tunatambua kwamba wakati wote wanahitaji kujielimisha, kupitia taasisi na shule mbalimbali na kule wako waelimishaji ambao wanafanya kazi hiyo kila siku. Sisi tuna utaratibu kwenye maeneo haya ya vyuo, taasisi na shule mpango wa kwanza tumepeleka fedha za kuwahudumia pale ambapo wanahitaji huduma kulingana na mahitaji yake. Wako wale ambao hawana usikivu mzuri, uono hafifu, ulemavu wa viungo, wote hawa tumewaandalia utaratibu kwa kupeleka fedha kwenye Halmashauri ili waweze kuhudumiwa. Pia walimu ambao wanatoa elimu hii nao pia tumeweza kuwawezesha kwa kuwapa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kulingana na aina ya mahitaji ambayo tunayo.
Pia walimu hawa tunawapeleka semina mara nyingi kuhakikisha kwamba na wao pia wanapata elimu ya kisasa zaidi ili kuweza kuwahudumia vizuri hawa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lini Serikali itajiimarisha katika kutoa huduma hii ni kwamba Serikali imeandaa kituo cha Msimbazi Center kuwa ni eneo la kukusanyia vifaa ambavyo tunavisambaza kwenye shule na taasisi zote ili viweze kutumika katika kufundishia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie pia Jumanne wiki ijayo napokea vifaa vingi sana vya elimu kule Dar es Salaam ambavyo vimeletwa kwa ajili ya kupeleka kwenye shule zetu za msingi. Miongoni mwa vifaa ambavyo pia tutakabidhiwa siku ya Jumanne ni pamoja na vifaa vya Watanzania wenzetu walioko vyuoni, kwenye shule ambao wana mahitaji maalum.
Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Amina Mollel na tunajua jitihada zako za kusemea sana eneo hili kwamba Serikali iko pamoja, Serikali inaendelea kuratibu vizuri na niendelee kukuhakikishia kwamba Serikali itaendelea kuratibu na kuhakikisha kwamba vifaa vya kujifunzia na kufundishia vitapatikana na hawa waelimishaji wanapata elimu ya mara kwa mara ili waweze kuwasaidia hawa wenzetu ambao wana mahitaji maalum. Ahsante sana.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Naomba kwanza kabla sijauliza swali langu niipongeze Serikali chini ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi ilivyoshughulikia suala zima la vyeti fake pamoja na watumishi hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Serikali ilifanya maamuzi ya kuzuia kusafirisha mchanga wa dhahabu nje ya nchi, katika kufanya hivyo Serikali itakuwa imepoteza dira katika demokrasia ya kiuchumi duniani, lakini si hivyo tu itakuwa pia imeleta mahusiano ambayo si mazuri na nchi mbalimbali duniani. Nini tamko la Serikali kuhusu jambo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sasa tuko kwenye matarajio ya kupata taarifa iliyo kamili kwenye sakata la mchanga na nataka nizungumzie eneo ambalo umehitaji zaidi la nini Serikali inatamka juu ya hili ili kuwaondolea hofu wawekezaji wetu wale waliowekeza kwenye maeneo ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni Watanzania wenyewe walionesha hofu kubwa kwa kipindi kirefu, hata Waheshimiwa Wabunge katika michango yenu mbalimbali kwa miaka iliyopita, hata pia katika kipindi hiki cha Serikali hii ya Awamu ya Tano mmeendelea kuitaka Serikali ichukue hatua thabiti na kutaka kufanya uchunguzi wa kina juu ya mchanga unaotoka nchini kupeleka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli amelitekeleza hilo pale ambapo alinituma mimi mwenyewe kwenda Kahama, kwenda kuona zoezi la ufungashaji wamchanga na kuuona mchanga huo, lakini nilipomletea taarifa akaamua kuunda Tume na aliunda tume mbili, moja ya kwenda kuukagua mchanga wenyewe na kujua ndani kuna nini, lakini ya pili, ni ile Tume ambayo inahakiki, itatoa taarifa ya madhara ya kiuchumi, lakini pia madhara ya kisiasa kwa ujumla na mahusiano kwa ujumla wake. Mpaka sasa tumepata taarifa moja na bado tunasubiri taarifa ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nataka nitumie nafasi hii kuwasihi wawekezaji wote, kwanza wasiwe na mashaka kwa sababu, lengo la Serikali ni kujiridhisha tu kwamba, je, mchanga huu unaosafirishwa kwenda nje una nini? Na wala hatubughudhi uzalishaji wao. Baada ya kuwa tumepata taarifa ya kwanza, bado hatua kamili hazijachukuliwa, tunasubiri taarifa ya kamati ya pili, baada ya hapo sasa Serikali itakaa chini na kutafakari kwa kupata ushauri kutoka sekta mbalimbali za kisheria, za kiuchumi na maeneo mengine hatua gani tuchukue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kuwatoa hofu wawekezaji wale walioko kwenye sekta ile ya madini wawe watulivu. Hatuna jambo ambalo tumelifanyia kazi dhidi ya hatua ambazo tumechukua ndani ya nchi kwa watu wetu ambao tunao ambao tuliwapa dhamana ya kusimamia hilo, lakini wawekezaji wote waendelee na shughuli zao za uwekezaji kama ambavyo tumekubaliana, wale ambao wako kwenye mchanga kwa sababu juzi wameambiwa watulie, watulie, hakuna jambo ambalo litafanywa ambalo halitatumia haki, ama litaenda nje ya haki au stahili ya mwekezaji huyo na kila kitu kitakuwa wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pia nitoe pia rai hata kwa Watanzania wawe watulivu. Tumeona watu wanatoa matamko wakidhani labda kuna uonevu, hapana! Watu watulie wasubiri majibu ya Serikali ambayo yatalinda haki ya kila mwekezaji, lakini na sisi pia Watanzania ambao tunaona tuna rasilimali zetu, hatuhitaji hizi rasilimali zipotee hovyo, lazima tuwe na uhakiki. Katika hili naomba mtuunge mkono Serikali kwa sababu kazi tunayoifanya ni kwa manufaa ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki huu ni kwa manufaa yetu Watanzania, ili tuwe na uhakika wa matumizi sahihi ya rasilimali zetu nchini. Kwa kufanya hilo tutakuwa tunajua tunapata nini na pia tujue tunaratibu matumizi yake na sisi Wabunge nadhani ndio hasa wahusika kama wawakilishi wa wananchi, twende tukawatulize wananchi waache kutoa matamko wasubiri Kamati zile. Pia tuzungumze na wawekezaji wetu ili nao pia wawe watulivu, bado Kamati ya pili haijatoa taarifa, baada ya hiyo maamuzi yatafanyika. Ahsante sana.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali la kwanza.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, wewe ndiye Kiongozi wa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ndani ya Bunge, lakini pia ndiye kiranja mkuu wa Serikali hii ya Awamu ya Tano. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama unavyofahamu kuna wazabuni wengi katika Halmashauri zetu tunakotoka ambao sisi ni wawakilishi wao pamoja na Serikali Kuu, walifanya kazi ya kutoa huduma katika taasisi za Serikali na Serikali yenyewe kwa muda mrefu, wengine wana miaka miwili, mitatu, wengine mpaka mitano, lakini mpaka sasa hawajalipwa stahiki zao.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ukizingatia mnamo tarehe 01 Juni ndani ya Bunge hili, uliliambia Bunge hili kwamba malipo yanachelewa ni kwa sababu wanafanya uhakiki, ambalo ni jambo zuri, kuwagundua wale ambao wanastahili kulipwa…
SPIKA: Swali Mheshimiwa Mgumba, moja kwa moja!
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Spika, nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu, watu hawa wamesubiri kwa muda mrefu na ukaguzi umeshafanyika zaidi ya mara tano, nini kauli ya Serikali, watawalipa lini wazabuni wote waliotoa huduma ndani ya Serikali?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgumba, Mbunge wa Morogoro Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba, Serikali inadaiwa na wazabuni wetu waliokuwa wanatoa huduma kwenye maeneo mbalimbali. Wako ambao wametoa huduma kwenye Halmashauri za wilaya kwa maana ya huduma kwenye shule, kwenye magereza, lakini pia wako ambao wamefanya kazi za kutoa huduma kwenye Wizara mbalimbali. Na kwa mara ya mwisho nilikuwa hapa nilipata swali la aina hii linalowahusu wadai/wazabuni wa pembejeo, wote hawa ni watoa huduma ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumeweza kugundua kwamba baadhi ya madeni na baadhi ya wadai wachache miongoni mwao wametuletea taarifa za madai ambayo si sahihi sana. Na kweli, tulichokifanya tulitoa maagizo kwenye maeneo yote, ili kuhofu kupoteza fedha, kulipa fedha ambayo haikufanyiwa kazi kwa madai yale.
Kwa hiyo, tumeendesha zoezi la uhakiki chini ya Wizara ya Fedha na taasisi yetu kupitia CAG, hasa kule kwenye madeni makubwa ili kujiridhisha viwango vinavyotakiwa kulipwa kwa wazabuni hawa.
Mheshimiwa Spika, tuliweka utaratibu kwamba angalao kufikia mwishoni mwa mwezi huu tuwe tumemaliza hilo zoezi la uhakiki halafu tuanze kulipa madeni haya. Kwa hiyo ni matarajio yangu kwamba Wizara ya Fedha watanipa taarifa, na Wizara zile zote ambazo zina madeni ya watoa huduma zitatoa taarifa ya viwango vya fedha, halafu sasa tusimamie Wizara ya Fedha kuweza kuwalipa hawa watoa huduma.
Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii, kwanza niwashukuru kwa uvumilivu wao wadeni wote wanaotudai, lakini pili tuwasihi waendelee kutuvumilia na taratibu hizi kwa lengo lilelile nililokuwa nimelieleza awali la kuokoa fedha ambazo zinalipwa kwa watu ambao hawakutoa huduma. Hata hivyo bado tutaendelea kuwatumia watoa huduma kutoa huduma ndani ya Serikali kwenye maeneo ambayo wameendelea kutoa huduma na tuwahakikishie tu kwamba tutawalipa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kama wako watoa huduma kwenye eneo lako endelea kuwahakikishia kwamba Serikali tutlipa madeni. Ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya uhakiki wa watumishi ambao wana vyeti fake. Sasa baada ya uhakiki huo wengine wameacha vituo vya afya na zahanati zetu kule.
Sasa swali langu, je, lini mtaajiri sasa, ili watu wetu kule wapate huduma, hasa kwenye maeneo ya afya ambako watumishi wameshaacha kazi kutokana na kwamba, walikuwa wana vyeti ambavyo havistahili kuendelea kuwepo? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumepitisha zoezi hili la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wetu na uhakiki huu baada ya kuwa tumekamilisha tulipata makundi matatu. Kundi la kwanza ni wale wenye vyeti fake moja kwa moja, kundi la pili ni wale wenye vyeti vinavyotumika na zaidi ya mtu mmoja, lakini kundi la tatu uko utata wa majina ambao umejitokeza kwenye vyeti hivi ambavyo wao wamepata nafasi ya kukata rufaa. Sasa wote hawa wameacha pengo kwa sasa, na ndilo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelizungumzia, lini tunatoa ajira.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ametoa nafasi za ajira zaidi ya 50,000 ili kuziba mapengo haya ambayo yamejitokeza kwa wenye vyeti fake, lakini vilevile ili kuongeza tu ajira kwenye sekta nyingine kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwenye sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, tayari vibali vimeshatolewa na Wizara ya Utumishi, tumeanza na idara ya elimu, tumesha ajiri walimu wa masomo ya sayansi wamekwenda kwenye vituo, tumetoa pia nafasi kwenye sekta ya afya na vibali hivi vitaendelea kutolewa kadri ya nafasi ambazo Mheshimiwa Rais ameahidi kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, ninaamini Rais wetu mpendwa kwa ahadi yake nafasi hizi ataendelea kuzitoa ili tuzibe mapengo na kuboresha pale ambako kuna upungufu mkubwa. Na sasa ajira hizi zitaenda kitaaluma zaidi, ili kuweza kuleta ufanisi mkubwa kwenye sekta y ajira. Ahsante.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ahsante; na mimi nashukuru kupata nafasi ili nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa, tarehe 15/05/2017 Serikali ilitangaza rasmi kuivunja Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma na majukumu yake kuhamishiwa Manispaa ya Dodoma, kwa hilo naipongeza Serikali. (Makofi)
Lakini kwa kuwa baadhi ya wananchi hata Waheshimiwa Wabunge pia walikuwa tayari wameshalipia viwanja na walikuwa hawajakabidhiwa. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu jambo hili? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Mlata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais alitoa agizo la kuvunja Mamlaka ya CDA na mamlaka hiyo na majukumu yake kuyahamishia Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kupitia Manispaa ya Dodoma. Kazi hiyo imeshafanywa na zoezi linaloendelea sasa kwanza wale watumishi wote wa CDA watahamishiwa Manispaa ya Dodoma, lakini tutafanya mchujo kidogo, wale ambao walikuwa na malalamiko, wanalalamikiwa na wananchi wale wote tutawaweka pembeni, kwa sababu tunataka tupate timu mpya ambayo inafanya kazi vizuri.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, mbili, tunaendelea sasa na uhakiki na ukaguzi wa kina kwenye masuala ya fedha na utumishi wenyewe ili tuweze kuanza vizuri, tujue CDA ilipoacha iliacha na fedha kiasi gani na shughuli zake zilifikia hatua gani halafu pia kuweza kuendelea, lakini majukumu yote yanabaki kama yalivyokuwa na CDA yataendelea kufanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Kinachobadilika pale ni maandishi, kama kwenye risiti zilikuwa zinasomeka CDA, sasa zitasomeka Manispaa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha utaratibu huu mpango kazi wote utaendelea kama ulivyokuwa. Kama kuna mtu alilipa nusu anataka kumalizia, wataendela kukamilisha malipo yao, kama kuna mtu alishakamiliha hajapata kiwanja, ataenda kukabidhiwa kiwanja chake na namna yoyote ya utendaji wa kawaida utaendelea. Sasa hivi akaunti zote zimefungwa kwa hiyo, huwezi kulipa mpaka hapo tutakapofungua malipo.
Mheshimiwa Spika, tutamuagiza Mkurugenzi sasa wa Manispaa, atoe maelezo sahihi kwa Wana Dodoma na kwa Wananchi, Waheshimiwa Wabunge mkiwemo ili kila mmoja aweze kujua, lakini kwa kauli hii ndio usahihi wa taarifa ya CDA kwa namna ambavyo tumeivunja na tumehamishia Mamlaka pale Manispaa ya Dodoma na watumishi wote sasa watawajibika kwa Mkurugenzi wa Manispaa na hakutakuwa na chombo kingine pale.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ambayo tumewaelekeza sasa pale CDA kwenye Idara ya rdhi, kwenye lile jengo lisomeke Idara ya Ardhi - CDA na huko ndani tume- plan sasa Wizara ya Ardhi ipeleke mtu anayeandika Hati. Tunataka pale ndani iwe One Stop Centre. Ukienda kuomba ardhi, ukishapimiwa, ukishalipia, hati unapata humo humo kwenye hilo jengo. Kwa hiyo, tunataka turahisishe upatikanaji wa hati na viwanja kwenye jengo hilohilo moja, ukiingia ndani ukitoka unatoka na hati yako badala tena kwenda mahali pengine. Ahsante.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni Serikali imetoa tamko la kutosafirisha chakula nje ya nchi, lakini kuna baadhi ya mikoa ambayo imezalisha chakula cha kutosha cha ziada kinachoweza kusafirishwa hata nje ya nchi. Je, Serikali inatoa ufafanuzi gani kuhusiana na utekelezaji wa tamko hilo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Iringa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jambo hili nimelizungumza siku ya Idd Mosi nikiwa kwenye sherehe ya Idd kwenye Baraza la Idd kule Mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Nilizungumza kwa msisitizo kwamba tumedhibiti na tumezuia usafirishaji wa chakula na hasa mahindi nje ya nchi kwa sababu historia yetu sisi kuanzia mwaka wa jana mwezi Novemba, 2016 mpaka Februari, 2017 nchi yetu ilikosa mvua za msimu unaotakiwa na tutapata usumbufu mkubwa ndani ya nchi kwa maeneo mengi kukosa chakula cha kutosha.
Mheshimiwa Spika, na chakula kikuu sasa nchi Tanzania naona utamaduni umebadilika, nilikuwa nazungumza pia na Mheshimiwa Mbatia hapa kwamba utamaduni umebadilika, Wachaga, Wahaya sasa badala ya kula ndizi wanakula ugali. Wamasai waliokuwa wanakula nyama tu pekee sasa wanakula ugali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utakuta mahindi yanatumika sana kuwa ni chakula kikuu nchini na kwa hiyo lazima tuweke udhibiti wa utokaji wa mahindi ili yaendelee kutusaidia kama chakula kikuu hapa nchini kwetu.
Kwa hiyo tumeweka zuio, na hasa baada ya kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa Kilimanjaro ilitoa taarifa kwamba kuna utokaji wa mahindi mengi kwenda nchi za nje kwenye mipaka yetu. Na siku ile nilipokuwa Kilimanjaro malori kumi yalikamatwa yakiwa na mahindi yakivushwa kwenda nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lazima tuweke utaratibu na ninyi wote ni mashahidi kwamba uzalishaji huu haukuwa wa uhakika sana kuanzia mwezi Machi mpaka mwezi Mei, kwa miezi mitatu. Maeneo machache yamezalisha sana kama ulivyosema Mheshimiwa Ritta Kabati lakini maeneo mengine hayana chakula. Juzi nilikuwa Mwanza nikiwa pale Usagara, Kigongo Ferry nilisimamishwa na wananchi, moja kati ya tatizo walilolieza ni upungufu wa chakula. Nimeona, hata Sengerema mahindi yote yamekauka, Geita mahindi yote yamelimwa yamekauka. Kwa hiyo, bado tuna tatizo la upungufu wa chakula. Pia bei za chakula chetu iko juu sana hatuna namna nyingine ni kudhibiti chakula chetu.
Mheshimiwa Spika, na nilieleza kwamba nchi nyingi za jirani hazina chakula. Sisi tuna barua hapa kutoka Congo, South Sudan tumepata kutoka Somalia na nchi za jirani wanaomba kupewa msaada wa chakula kutoka Tanzania wakati sisi wenyewe hatuna chakula cha kutosha. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa Serikali na wananchi mkatuunga mkono katika hili, kudhibiti utokaji wa chakula, na hasa mahindi yanayokwenda nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, nimeeleza kwamba sisi tulichofanya ni kudhibiti kutoa mahindi nje bila kibali. Na kama kuna umuhimu wa kupeleka mahindi nje basi tunataka yasagwe ndani ili yapelekwe, kwa sababu ukisaga tunafaida zake, pumba tunazipata, tunazitumia kwa chakula cha mifugo lakini pia mashine zetu ambako tuna msizitizo wa viwanda vitafanya kazi ya kusaga, tutakuwa na ajira, lakini tunapotoa mahindi maana yake tunatoa kila kitu huku ndani tunakuacha tupu. Kwa hiyo, lazima tuwe na mpango ambao utasaidia sasa, sisi wenyewe Watanzania kunufaika kupitia zao hili.
Mheshimiwa Spika, bado msimamo ni ule ule kwamba tumezuia mahindi kutoka nje ya nchi na kama ni lazima basi aende Wizara ya Kilimo akaombe kibali kama ni lazima Wizara ikiona inafaa utapata kibali, lakini kibali hicho ni cha kutoa unga na si mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wote ni mashahidi, jana tumepata taarifa malori zaidi ya 103 kwa siku nne kutoka siku ya Idd mpaka leo hii, malori 103. Je, kwa mwezi mzima tutakuta na mahindi hapa ndani?
Mheshimiwa Spika, tunazo taarifa kupita Kamati za Ulinzi na Usalama kwamba wengi wanaofanya biashara kuja kuchukua mahindi Simanjiro, Kibaya kwa maana ya hapa katikati maeneo ya Kongwa ni watu kutoka nje ya nchi ndio wanaokuja kuchukua. Kwa hiyo hatuna faida sana hao kuingia zaidi ya kwamba wanatuachia fedha. Hivyo tunaitengeneza shida ambayo tutakuja kuanza kuuliza tutapateje chakula ndani ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Watanzania kwa jambo hili naomba mtuunge mkono kwa sababu tunachofanya ni kwa maslahi ya nchi, hatimaye bei zitapanda tutashindwa kununua mahindi na wote mnajua angalau sasa mahindi yamepungua kwenye masoko
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuendelee na hali hiyo ili chakula kiwe cha kutosha baada ya kuwa tumefanya tathimini tukijiridhisha kwamba chakula cha ndani cha kutosha kipo na tuna akiba kutoka kwenye maeneo yanayozalisha sana basi vibali hivyo vinavyotolewa kwa utaratibu vitaendelea kutoka, na wale ambao wanataka kufanya biashara nje ya nchi wataendelea kupata fursa ya kufanya biashara nje ya nchi. Lakini kwa sasa tumezuia; na ninataka nimpongeze sana Mkuu wa Mkoa ya Kilimanjaro mama Anna Mghwira na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kusimamia.
Mheshimiwa Spika, tumeona malori yale agizo limebaki pale pale, mahindi yale ambayo yatakuwa yamaekamatwa; na tumejihisi kwamba yalikuwa yamekwenda nje ya nchi, yote yataingizwa kwenye hifadhi ya taifa, na hayo malori yanyofanya biashara hiyo yote yatabaki kituo cha polisi. Lakini pia kwa namna ambavyo wanaendelea na waendelee kwa utaratibu wote na maagizo yetu yatabaki vilevile ili tuweze kuwahudumia Watanzania ndani ya nchi.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Waziri Mkuu swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu nina imani utakubali kwamba usalama wa nchi na mahusiano mema miongoni mwa raia ni tunda la mahusiano mazuri kati ya vyama vya siasa, Serikali na vyombo vyote vya dola.
Mheshimiwa Spika, siku za karibuni kumekuwa kuna mwendelezo wa matukio mengi yanayovunja usalama huo, yanayovunja amani na yanayojenga chuki miongoni mwa vyama vya siasa na kuharibu utengamano wetu wa kitaifa.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa nia ya kuua kwa Mheshimiwa Tundu Anthipas Lissu, Mbunge na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni limezua hofu kubwa sio tu kwa Taifa ila katika Bara zima la Afrika na Jumuiya ya Kimataifa. Nina hakika taharuki hiyo imeharibu sana sura ya Taifa, heshima tuliyokuwa nayo kama Taifa na hatujaona kama Serikali inachukua hatua zozote kujaribu kufanya jambo hili lisiendelee kuharibu image yetu kama Taifa.
Mheshimiwa Spika, aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu atakumbuka kwamba hapo nyuma vimetokea vifo vya kisiasa. Alifariki Mwenyekiti wetu wa Mkoa wa Geita, Bunge na Serikali tulilizungumza hapa na Serikali ikasema inafanya uchunguzi, hadi leo hakuna hatua iliyochukuliwa.
Mheshimiwa Spika, akapotea msaidizi wangu Ben Saanane, nikakuomba Waziri Mkuu na Serikali yako iruhusu uchunguzi wa kimataifa ili kutatua tatizo hili, ukasema vyombo vyetu vya ndani vina uwezo hadi leo hakuna lililopatikana. Tumeomba vilevile kushambuliwa kwa Mheshimiwa Tundu Lissu kuchunguzwe na vyombo vya uchunguzi vya kimataifa vilivyo huru, visivyofungamana na upande wowote, bado Serikali inaonekana ina kigugumizi katika jambo hili.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, unatupa kauli gani sisi kama chama, Wabunge na Taifa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nieleze kwamba amani yetu na utulivu ndani ya nchi ni jambo ambalo Watanzania wote lazima tushikamane na tushirikiane katika kulidumisha. Ndilo ambalo linaendelea kutupa heshima duniani kwa sababu Watanzania wote tunashirikiana katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo matukio yanajitokeza, Mheshimiwa Mbowe umezungumzia upande wa siasa lakini pia matukio haya yapo kwa ujumla wake nchini kwenye maeneo kadhaa kwa ngazi ya familia, lakini pia na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko, na watu wengine pia. Wapo wenzetu ambao hawana nia njema nchini wanajitokeza katika kutenda matendo hayo.
Mheshimiwa Spika, na hata hili analolisema la Mheshimiwa Tundu Lissu si Mheshimiwa Tundu Lissu pekee ingawa hatupendi mambo kama hayo yatokee, lakini pia tumepoteza Watanzania wengi. Hata mnakumbuka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji tumepoteza watu wengi. Hata hivyo pia hata siku za karibuni Kamanda wetu wa Jeshi la Ulinzi nchini (JWTZ) naye alipigwa risasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuyazungumze haya kwa ujumla wake na tunapoyazungumza haya kwa ujumla wake, na kwa utamaduni ambao tumeujenga wa nchi hii katika kujilinda wenyewe na kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwa salama, nataka nikuhakikishie kwamba vyombo vyetu vya dola vinaendelea kufanya uchunguzi wa haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na uchunguzi huu hauwezi kuwa wa leo leo ukapata ufumbuzi kwa sababu wanaotenda matendo haya wanatumia mbinu nyingi za kujificha. Kwa hiyo, na sisi lazima tutumie mbinu zetu za kutambua hao waliotenda matendo hayo katika kila eneo ili pia baadaye tuweze kutoa taarifa ya jumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niendelee kukuhakikishia pia kwamba vyombo vya dola haviko kimya, vinaendelea. Nataka nikuhakikishie vilevile kwamba vyombo vyetu vya dola vinao uwezo wa kusimamia usalama ndani ya nchi, ni suala la muda ni wakati gani wanakamilisha taratibu na hatua gani zichukuliwe. Sasa hilo linategemea na waliotenda matukio na namna ambavyo wamejificha na namna ambavyo na sisi tunatumia njia mbalimbali za kuweza kuyapata haya na kuweza kujua na kutoa taarifa kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nikusihi na familia zote ambazo zimepata athari na zimeripoti polisi na wameripoti kwa vyombo vya dola na vinaendelea kufanya kazi kwamba, pale ambapo tutakamilisha uchunguzi tutatoa taarifa kwa ngazi ya familia ambazo pia zimepata athari au ndugu au jamaa kupata athari hiyo na kuwaambia hata hatua ambayo sisi tunaichukua pia. Kwa hiyo, nataka niwasihi kwamba jambo hili tuendelee kujenga imani kwa vyombo vyetu vya dola vitakapokamilisha kazi zake vitatoa taarifa.
MHE. MUNDE A. TAMBWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuuliza swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu umekuwa mfuatiliaji mzuri wa mazao ya wakulima huko mikoani ili waweze kupata tija. Umekuja Tabora mara kadhaa, umetoa maelekezo kadhaa kuhusu suala zima na kero za tumbaku, lakini agizo kubwa ulilolitoa la kuhakikisha tumbaku iliyopo ndani ya wakulima na kwenye magodauni ya msimu uliopita inunuliwe, ambayo mpaka leo hii ninavyoongea tumbaku hiyo bado haijanunuliwa. Hii imesababisha adha kubwa kwa wakulima wa tumbaku wa Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ni msimu wa kulima tumbaku nyingine lakini tumbaku iliyopo ni ya mwaka wa jana na haijanunuliwa; na tumbaku hii ikikaa kwa muda mrefu inashuka grade ambapo ubora wa tumbaku unapungua na inateremka uzito. Mpaka sasa ma-godown mengi yanavuja na tumbaku hiyo kuvujiwa na kusababisha hasara kubwa na tahaluki kubwa kwa wakulima wa tumbaku Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Tabora wana imani kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano na leo wanakuomba sana, wanakusihi wapo chini ya miguu yako wameniagiza; wanaomba utoe tamko.
Je, Serikali inatoa tamko gani leo kuhusu kununua tumbaku ya msimu uliopita ambayo bado haijanunuliwa, iliyopo kwenye magodauni ya wakulima wa Mkoa wa Tabora?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Munde, Mbunge wa Tabora kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la zao la tumbaku ni jambo ambalo Serikali tumelifanyia kazi kweli kweli, na zao la tumbaku ni miongoni mwa mazao ambayo tunataka sasa yapate mabadiliko ya kilimo chake, lakini pia na masoko yake. Moja kati ya tatizo ambalo lipo sasa ni lile aliloeleza mheshimiwa Mbunge la masoko ya tumbaku na Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wanaotoka kwenye maeneo ya tumbaku wanajua jitihada za Serikali zilizofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la tumbaku upo utamaduni wa kila mwaka wa wakulima wetu na makampuni yanayonunua kufunga mikataba ya kiwango cha tumbaku kitakachonunuliwa na makampuni na ndicho kiwango ambacho wakulima wanapaswa kulima.
Mheshimiwa Spika, jambo lililojitokeza mwaka huu ni kwamba wakulima wamelima zaidi ya kiwango kilichowekewa mikataba ya kununuliwa kwenye msimu. Kwa hiyo, tumbaku ambayo imebaki sasa ni ile ya ziada ya msimu ya bajeti ambayo makampuni yanayonunua yalitaka yanunue tumbaku. Ile tumbaku yote ambayo ilikuwa kwenye bajeti ilishanunuliwa, hii ni ile ya ziada.
Mheshimiwa Spika, Serikali ziada hii hatujaiacha kama ambavyo tunaona sasa, ni kwamba makampuni yenyewe tumekaa nayo, tumeyasihi yaweze kununua tumbaku. Wameeleza kwamba walikuwa nje ya bajeti na walikuwa wanaendelea kuzungumza na vyanzo vyao vya fedha ili waje kununua tumbaku yote iliyobaki. Mjadala huo umeendelea na sasa upo mjadala wa bei kwa kuwa sasa imekuwa ni ziada ya mahitaji yao wao wanalazimisha na wanataka wanunue kwa kiwango cha chini, lakini Serikali tunataka wanunue angalau kwa bei dira ya zao lile.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo bado tumeendelea na jitihada za kutafuta nchi mbalimbali zinazoweza kununua tumbaku. Tumeenda Indonesia, China, Misri na Iran na nchi zote hizi zimeonyesha nia ya kuinunua tumbaku iliyopo sasa kwenye maghala yetu. Nchi ya Indonesia imefikia hatua nzuri, wanajadili kiwango cha tumbaku watakachochukua na sasa wanajadili kwenye eneo la bei. Watakapokamilisha mjadala wa kujua kiwango gani watanunua, Serikali sasa itaridhia.
Interest yetu Serikali ni kuona kwamba mwananchi ananufaika kwa kuuza tumbaku yake kwa bei nzuri ili sasa kila mkulima aweze kuendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawasihi sasa Waheshimiwa Wabunge wenzangu, lakini pia wakulima wote wa zao la tumbaku, jana nimeona pia kwenye TBC tumbaku ipo pale Kaliua, nimemwona Mwenyekiti wa Halmashauri akieleza madhara yanayojitokeza kama ambavyo umeeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka tu nieleze kwamba jitihada za kilimo zitakapokamilika tutawapa taarifa ya hatua nzuri tuliyoifikia na hatua nzuri kwetu ni kutaka kununua tu hiyo tumbaku iliyobaki. Kwa hiyo, tunaendelea na bei tutawapa taarifa.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni sera ya Serikali kulinda raia na mali zao. Lakini mnamo tarehe 24 na tarehe 25, askari wa FFU katika Kambi ya Ukonga, Mombasa, walifunga barabara wakapiga akina mama, vijana na wazee na wakawatesa sana abiria na kuleta madhara makubwa.
Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba nipate tu, na wananchi wangu wasikilize, Serikali inatoa kauli gani juu ya matukio kama haya ambayo yanafanywa na viongozi na vijana ambao kimsingi tunatakiwa tuishi kama ndugu na kushirikiana kwa ajili ya kulinda raia na mali zetu? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Waitara, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunazo taarifa kwamba pale Ukonga kulikuwa na mgongano mkubwa kati ya Jeshi letu la Polisi na raia, na mgongano huu umesababisha pia kuuawa kwa askari mmoja na watu wengi kupigwa, lakini hatua nzuri zimechukuliwa. Mkuu wetu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Mjema, aliingilia kati na kuchukua hatua ya kuunda tume ambayo inafanya ufuatiliaji kuona chanzo na madhara yaliyojitokeza na wahusika katika jambo hili. Baada ya tume kumaliza kazi yake, ikibainika nani ametenda kosa hatua kali zitachukuliwa.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu wewe ni Mbunge wa eneo lile lazima utashirikishwa pia katika kupata taarifa za matokeo ya tume iliyoundwa na Mkuu wetu wa Wilaya ya Ilala, Mama Sophia Mjema.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika Serikali ya Awamu ya Nne nchi hii ilitumia mabilioni ya fedha kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kukusanya maoni ili kuandaa Katiba Mpya na hii ilikuja baada ya kugundua kwamba Taifa hili linahitaji Katiba Mpya ili kutibu changamoto nyingi ambazo zinaikabili katika maeneo mbalimbali ikiwemo kulinda rasilimali, uwajibikaji, haki za binadamu, tunu za Taifa na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuanzisha mchakato ule, pamoja na changamoto ambazo zilijitokeza baadaye.
Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ya Awamu ya Tano toka imeingia madarakani, leo miaka miwili tayari imepita haijafanya jambo lolote la kuendeleza mchakato ule ili zile ndoto za Watanzania za kupata Katiba Mpya ziweze kutimia. Zaidi tumekuwa tukisikiliza kauli mbalimbali za kwenu viongozi na za viongozi wa Chama chenu cha Mapinduzi ambazo hazioneshi nia ya kukamilisha mchakato huo wa Katiba Mpya.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba awaambie Watanzania leo, nini mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kutimiza ndoto za Watanzania kupata Katiba Mpya?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mtolea, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali ya Awamu ya Nne ilianza mchakato wa Katiba Mpya na kupitia hatua zote za kuunda Tume, ikapita kukusanya maoni na sisi kama Waheshimiwa Wabunge tulikuwa miongoni mwa Wajumbe ambao tulishiriki katika kuweka misingi ya Katiba hiyo. Suala la Katiba Mpya linahitaji gharama kubwa ya fedha na zinatokana na mapato yanayokusanywa ndani ya nchi lakini kila mwaka wa fedha una vipaumbele vyake na sisi tumejikita katika kutoa huduma za jamii kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishuhudia Watanzania wanahitaji maji kwenye vijiji, kumekuwa na mahitaji ya huduma za afya, tunahitaji kuimarisha elimu, miundombinu, ili kuwawezesha Watanzania kuendelea na maisha yao. Katiba ni mwongozo ambao unaelekeza mambo kadhaa. Sasa hivi tunayo Katiba ambayo pia ina miongozo ile ile ingawa tumekusudia kuibadilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunayo Katiba inaendelea na miongozo ipo, na haya ni mapendekezo ya kufanya marekebisho ya maeneo kadhaa; lakini mchakato wake kwa sababu unahitaji gharama kubwa na kipaumbele cha Serikali ni kutoa huduma ya jamii kwa Watanzania; kwanza tumeanza kuimarisha makusanyo ya ndani ili tuweze kumudu kutoa huduma za wananchi, Watanzania. Pale ambapo tutafikia hatua nzuri ya mapato huku tukiendelea kutoa huduma hiyo na matatizo haya yakipungua kwa kiasi kikubwa, tutakuja kuendesha mchakato huo pale ambapo inaonekana tunaweza tukaufanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua hayo yote lakini pia tumeona muhimu zaidi tuanze na huduma za jamii ili Watanzania waendelee kufanya kazi zao za kuboresha uchumi wao ili wapate nafasi ya utulivu waje waangalie jambo lingine, kwa sasa tutatumia Katiba iliyopo. Ahsante sana.
HE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa na mimi niweze kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingikakwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano imefanya mambo mengi sana; tumeona imepunguza matumizi mengi, uchumi unakwenda vizuri, Sekta ya Madini inakwenda vizuri.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, watumishi wa Serikali au watumishi wa Umma wana malalamiko muda mrefu sana, na malalamiko yao makubwa ni juu ya mishahara. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu ninapenda nikusikie uwaambie Watanzania ni lini Serikali itapandisha mishahara ya watumishi? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, na mimi nakiri kwamba wafanyakazi wanahitaji kuboreshewa maslahi yao, eneo hili la mishahara likiwa ni moja kati ya maeneo muhimu. Kama ambavyo tumekuwa tukitoa majibu kwenye maswali ya msingi kupitia vipindi vyetu kwa Mawaziri husika, lakini pia nyakati kadhaa kueleza nia ya Serikali ya kuboresha maslahi ya watumishi. Maslahi ya watumishi ni pamoja na kuweka stahili zao za kila siku, madeni yao, kupanda kwa madaraja na malimbikizo yao pamoja na nyongeza ya mishahara ni miongoni mwa mambo ambayo Serikali imedhamiria kuyafanya.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kuboresha maslahi ya watumishi wakati wa sherehe ya Mei Mosi na aliwaambia wafanyakazi wote. Sasa Serikali kuanzia mwezi wa sita tunaendelea kuhakikisha kwamba tunakamilisha taratibu za kimsingi ambazo zitaiwezesha sasa Serikali kuanza kutoa malipo kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, lakini eneo la kwanza ni lile la madeni, eneo la pili kwa muda mrefu tulisitisha madaraja ambalo sasa tumeanza kuwapandisha madaraja watumishi ambao hawakupanda madaraja kwa muda mrefu tunawafikisha mahali pao, na tunapobadilisha madaraja haya inabidi tulipe malimbikizo yake. Pia kuna ambao walishapanda, walikuwa hawajalipwa malimbikizo, sasa tunaanza uratibu. Na hapa juzi tumetenga shilingi bilioni 147 kwa ajili ya kulipa na Mheshimiwa Rais alishaeleza nia ya kulipa maslahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukishakamilisha haya, ni pamoja na yale mambo ambayo tulianza nayo, uhakiki wa watumishi, vyeti fake, ili kuondoa watumishi tusije tukawalipa watu ambao sasa hawastahili. Eneo hilo tumelimaliza, madeni tumeendelea kuhakiki, na kwa sababu madeni yanaendelea kila siku nayo tunaendelea kuyahakiki lakini yale ya muda mrefu tayari, na tumeanza kulipa. Na madeni haya yanalipwa kupitia mishahara yao. Tusingependa tuwe tunatangaza leo tumelipa, hii inaweza ikaleta athari kwenye eneo la mabadiliko ya kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, lakini Serikali inalipa ingawa inalipa kwa awamu, lakini tutahakikisha kwamba madeni yote ya watumishi tunamaliza, waliokosa kupanda madaraja kwa muda mrefu tunawapandisha na kulipa stahili yao mpya halafu sasa tuje tuongeze mishahara. Tutakuwa tayari Serikali tunajua tuna watumishi wangapi, tutahitaji fedha kiasi gani za kulipa nyongeza ya mshahara, na wakati huo itakapokuwa imekamilika, nataka niwahakikishie watumishi tutaendelea na uboreshaji likiwemo na eneo la uongezaji wa mishahara.
Mheshimiwa Spka, kwa hiyo nawasihi sana wafanyakazi wenzetu kote wawe na imani na Serikali yao na huku tukiendelea kuratibu vizuri. Tunachotaka sisi tusije tukapoteza fedha tukawalipa watu ambao hawastahili, lakini pia lazima tujiridhishe ni kiwango gani cha fedha kinahitajika kulipa kwenye eneo hili ili kila mtumishi apate stahili yake na kila mtumishi tunapoboresha mishahara apate kima ambacho angalau kinaweza kukidhi mwenendo wa maisha ya kila siku na huo ndiyo utaratibu ambao Serikali imejiwekea. Ahsante sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imekuwa ikitoa kauli na matamko mbalimbali kwa wakulima wa mbaazi kote nchini kwamba Serikali inafanya mazungumzo na Serikali ya India ili wakulima hawa wapatiwe soko. Hata hivyo hadi sasa mazungumzo hayo hayajakamilika na wakulima wamebaki na mazao yao.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nifahamu, kwa nini Serikali isione ni busara kuwatangazia wakulima wa mbaazi kote nchini kwamba wameshindwa kuwapatia soko na wasiende kulima katika msimu huu wa kilimo ambao unakwenda kuanza sasa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hata juzi wakati tunapeana maelekezo ya msingi jambo hili la matatizo ya masoko ya mazao yetu lilijitokeza, mbaazi ikiwemo. Ninachoweza kusema hatuwezi kuwaambia wakulima msimu huu wasijiandae kulima kwa sababu suala la masoko, awali zao la mbaazi tulikuwa na soko la uhakika la nchi ya India na ndio wanunuzi wakuu wa zao hili. Huku kwetu sisi mikoa yote inayolima imeendelea kulima kila mwaka na tumeendelea kufanya biashara na nchi ya India bila tatizo lolote lile.
Mheshimiwa Spika, lakini pia hata hivi karibuni Waziri Mkuu wa India alipokuja nchini, aliweza kusisitiza pia tulime mbaazi nyingi na wao pia wanalima na sisi tumelima. Sasa tulipofikia hatua ya kuuza kwa bahati mbaya au nzuri kwao nchi ya India imeweza kuzalisha mbaazi kwa asilimia 30 zaidi na kwa maana hiyo wana mbaazi ziada na kwa hiyo, walisitisha utaratibu wa kununua mbaazi kutoka nchi za nje kuingiza kwao mpaka hapo akiba yao watakapoifikiria vinginevyo. Kwa kufanya hilo wametuathiri kwa sababu soko pekee la mbaazi kwetu sisi ilikuwa ni nchi ya India.
Mheshimiwa Spika, sasa nini jukumu la Serikali kwa sasa; tunaendelea kutafuta masoko na ndiyo sababu tumewasihi wakulima wa mbaazi nchini kote, na ni mikoa mingi inayolima sana mbaazi, tumeendelea kuwasihi kwamba waendelee kutusubiri kwa sababu Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo inashughulikia mbaazi pia sasa inaendelea kutafuta masoko, likiwemo na lile zao la tumbaku ambalo nimelieleza muda mfupi uliopita.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jitihada hizi zitakapofikia hatua nzuri, tutauza. Kwa sasa hatuwezi kuwaambia kwamba tutauza kwa sababu bado negotiations zinaendelea na mataifa ambayo yatataka kununua zao hili la mbaazi ikiwemo na India yenyewe kwa sababu ya ile commitment ambayo ilikuwa imeshatolewa kati yetu na wao; na ndiyo utaratibu wa kawaida kwa nchi ambazo tunafanya nao biashara za mazao. Pale ambapo kunatokea tatizo lazima na sisi tupate taarifa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii ni taarifa kwa wakulima wote wa mbaazi kwamba kwa sasa wawe watulivu, tunaendelea na utaratibu huu wakati wowote tutawapa taarifa. Ni kweli tunajua wanaathirika sana lakini ni muhimu pia taarifa hii kuwa nayo na uvumilivu ni muhimu pia kuwa nao.
MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize swali Mheshimiwa Waziri na kwa kuwa umeshasema hakuna nyongeza sasa itabidi niunganishe hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linasema hivi; Serikali imeandaa Sera na kutunga sheria ili kuruhusu wageni kufanya kazi na kurithisha ujuzi kwa Watanzania. Je, wageni hawa wanatakiwa waruhusiwe kufanya kazi kwa muda gani?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bulembo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli maswali yanayohusu takwimu ni ngumu kupata takwimu halisi kwa sasa kwa sababu maandalizi yetu ni ya kisera zaidi. Nchi inao utaratibu wake, iko Sheria ya Ajira na iko Sheria inayohusu waajiriwa wa ndani ya nchi na nje ya nchi na kwa bahati nzuri jambo hili liko kwenye ofisi yangu, Ofisi ya Waziri Mkuu. Sheria namba moja ya mwaka 2015 ndiyo ambayo hasa inagusa kwenye mambo ya ajira na inapotokea ajira zinahusisha sekta za kitaalam na zinahitaji wageni kutoka nje ya nchi tumeweka ukomo. Tunayo ile ratio ya 1:10 kwamba kwenye Watanzania kumi kunakuwa na mgeni mmoja.
Mheshimiwa Spika, tunachokifanya; tunatoa kibali cha kufanya kazi nchini. Ukomo wetu ni miaka miwili na katika hiyo miaka miwili, moja kati ya jukumu kubwa analolifanya huyu mgeni mwajiriwa ni kurithisha, kufundisha utaalam kwa Mtanzania ili anapomaliza miaka miwili basi Mtanzania awe ameshajua kazi ile ili Mtanzania aweze kuendelea na ile kazi.
Mheshimiwa Spika, pale ambapo tunaridhika kwamba ule utaalam bado Watanzania hatujapata vizuri, sheria pia inaruhusu kumpa fursa ya kuwaomba tena kuongezewa muda wa miaka miwili mingine. Tunaamini katika vipindi hivyo viwili vya miaka miwili miwili Mtanzania anaweza kuwa sasa ameshazoea kazi ile ambayo alikuwa anaifanya mgeni ili kuwapa uwezo Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili makampuni yote yanayokuja nchini na wataalam hao tumeyapa sheria ya kwamba, kampuni inapoendesha sekta za kitaalam lazima waweke kipengele ambacho kinatoa mafunzo kwa Watanzania. Lengo ni kwamba, wanapomaliza muda wao, basi Watanzania kupitia mafunzo yale, wawe wameshazoea kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, masharti hayo yanatofautiana kwa hao ambao na wao wanaajiriwa kama wafanyakazi, lakini pia wakati mwingine sheria inabadilika kama kunakuwa na mwekezaji anakuja kuanzisha kampuni yake na pia inahitaji utaalam. Kwa hiyo tunaangalia mazingira hayo na huwa tunatoa fursa ya mwekezaji huyo kufanya kazi nchini na kiwanda chake au aina ya uwekezaji ambayo pia Watanzania nao watapata ajira zaidi.
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo ambayo tunapenda zaidi kuwakaribisha wawekezaji kujenga, kuwekeza, ili tuweze kufungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania. Kwa hiyo msisitizo hapa ni Watanzania kuendelea kupata nafasi za ajira nyingi za kutosha pamoja na kupata utaalam ambao hatukuwa nao kupitia hao wawekezaji. Huo ndiyo utaratibu wa nchi.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ili na mimi niweze kuuliza swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 inatamka wazi kuwezesha mazingira bora kwa wanafunzi wote kwa maana ya wanafunzi wa kike na wa kiume bila kujali jinsia. Hata hivyo, kuna utafuti uliofanywa na Tanzania Gender Network Program, unaonesha kwamba watoto wa kike hukosa masomo kati ya siku tatu mpaka saba kwa mwezi na hivyo huathiri ufaulu wao. Ni kwa nini sasa Serikali haioni umuhimu wa kutoa mwongozo kwa zile pesa za ruzuku zinazokwenda shuleni kutamka wazi kwamba kiasi fulani kitengwe kwa ajili ya taulo za kike ili watoto hawa waweze kuhudhuria masomo siku zote?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kweli tunayo Sera ya Elimu na sera yetu tunasisitiza watoto wote wa Kitanzania wasome (wa kiume na wa kike) na tunaendelea kusimamia uwepo wa idadi kwa idadi kwanza iwe idadi nzuri ya wasichana na wavulana kwenye elimu.
Mheshimiwa Spika, sasa yako haya mambo ya ndani ambayo tunaingiza zaidi kwenye Sekta ya Afya na Wizara ya Afya ambayo pia inalishughulikia hili kwa ujumla wake nayo pia tumeipa jukumu la kuratibu shughuli zote zinazohusu afya. Hata hivyo, kwenye shule zetu hatukuweza kuitamka hiyo wazi kwa sababu tunaamini kwamba mwanafunzi anapopata tatizo hilo haliwezi kuwa public, ni jambo binafsi.
Mheshimiwa Spika,Sasa mambo hayo binafsi ingawa yanaweza kuathiri kipindi cha masomo lakini tunaamini kwamba tunaweza tukawa tunawatunza watoto wetu pamoja na ndiyo sababu katika kila shule tumeamua kuwe na Walimu wanawake ili waweze kumsaidia mtoto wa kike kwa hayo mambo ambayo ni ya ndani, ya usiri, hatuwezi kuyaweka wazi. Pale ambapo tutaona kuna umuhimu zaidi wa kuhakikisha kwamba tunaweza kuandaa sera ya namna hiyo kwa ajili ya kuwakinga akinamama, tunaweza kufanya hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Matrons wetu walioko shuleni wanaendelea kukaa nao watoto wetu ili kumfanya nae pia kuendelea kuwa na confidence ya kusoma pamoja na wenzake bila kuibua hizo hisia ambazo tunasema ni mambo ya usiri na ya ndani ingawa pia ni muhimu nalo katika kuliweka kwenye utaratibu huo ambao tunadhani ni muhimu pia kuufanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa swali la Mheshimiwa Mbunge, ni suala muhimu lakini linazungumzika ndani ya Serikali ili tuweze kulifanyia kazi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa nchini tunazo Sera za Ugatuaji wa Madaraka. Hii Sera ya Ugatuaji wa Madaraka lengo ilikuwa ni kufikisha huduma hizi kwa jamii kwa karibu zaidi na usimamizi wa karibu wa miradi yetu ya maendeleo inayoibuliwa katika Halmashauri zetu na vijiji.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ili sera hii iweze kutekelezwa ni kwamba Serikali inapeleka pesa nyingi kwenye Halmashauri zetu ili kuweza kutekeleza miradi hiyo na kutoa hizo huduma. Hata hivyo, kada hii, wasimamizi wakubwa wa kwanza kabisa wa fedha hizi ambazo Serikali tunapeleka ni Watendaji wetu wa Vijiji na Watendaji wa Kata.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa hivi nchi yetu inakumbwa na tatizo kubwa sana katika Halmashauri zetu kutokana na uhaba wa Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji wakati hao ndiyo tunaowategemea kwamba ndiyo wangekuwa wasimamizi wa kwanza wa fedha hizi.
wali langu ni kwamba mkakati wa Serikali ya Awamu ta Tano unasema nini katika kutatua tatizo hili ambalo limekuwa sugu, linasababisha Halmashauri zetu kupata hati isiyo salama?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kuchauka ambalo limezunguka zunguka lakini msingi wake ni Serikali inatumia utaratibu gani kuhakikisha kwamba kunakuwepo na rasilimali watu ambao pia wataweza kudhibiti rasilimali fedha kama ambavyo nimekuelewa kwa mzunguko mzima wa swali lako.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na watumishi wa kutosha kwenye kada zote. Kwa sasa tunaendelea kushuhudia kupungua kwa rasilimali watu kwenye sekta zetu na hatimaye kusababisha rasilimali fedha hizo kutotunzwa/ kutosimamiwa vizuri. Kwa Serikali ya Awamu ya Tano, jambo hilo linaweza kuwa limetokana na mazoezi mawili ambayo tumeyaendesha; ya kubaini watumishi hewa na watumishi wenye vyeti ambao hawana stahili sahihi ya kufanya kazi walioajiriwa. Sasa zoezi hili limepunguza idadi ya watumishi na ni kweli kwamba tunaweza tukawa tunapeleka fedha halafu zisipate watu wa kuzisimamia vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwenye eno hili, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ametupa nafasi za ajira zaidi ya 52,000 na tumeanza kuajiri kwa sababu anatupa vibali kadiri tunavyohitaji na tunaendelea kuhakiki kwamba wanaokwenda ni watumishi wenyewe na wamefika vituoni wanafanya kazi yao. Kama ambavyo mmeshuhudia tumeajiri kwenye Sekta ya Elimu, Afya na juzi Majeshi na tunaendelea kuajiri.
Mheshimiwa Spika, sasa kada hizi za Watendaji wa Kata na Vijiji hizi ni kada ambazo pia tumezipa mamlaka halmashauri zenyewe kuajiri pale ambapo wanaona kuna upungufu ili kuziba mapengo haya. Kwa hiyo ni halmashauri yako na Mheshimiwa Mbunge wewe pia ni Mjumbe wa Baraza la Madiwnai pale, kwa hiyo unayo fursa ya kupata takwimu za Watendaji wa Kata na Vijiji waliopo na kujua wangapi wamepungua ili muamue na muweze kuziba ninyi wenyewe pale kwa lengo la kuweza kudhibiti fedha zilizopo na zilizopelekwa kwa ajili ya miradi kwenye ngazi hizo za vijiji.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Waziri Mkuu nchi yetu imekuwa inakumbwa na majanga mbalimbali kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Tumeshuhudia watu wengi wakipoteza maisha, lakini miundombinu ikiharibika, lakini pia hata hali halisi ya mvua zimekuwa hazinyeshi kwa ukamilifu kutokana na kwamba, kuna mabadiliko ya tabianchi ambayo ni suala la kidunia. Mheshimiwa Waziri Mkuu Serikali yetu imejipanga vipi kimkakati kupambana na janga hili la tabianchi katika nchi yetu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sakaya, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya tabianchi yaliyoikumba dunia yote, Tanzania ikiwemo, tunaendelea pia kukabili changamoto hiyo huku tukiwa tunaweka mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba, tunakabiliana nayo mabadiliko hayo. Moja tumejiimarisha kwa sheria zinazohifadhi mazingira yetu, ili kuhakikisha kwamba, mazingira yanabaki yanasaidia pia, kufanya mabadiliko ya hali ya hewa ndani ya nchi yanabaki kuwa ya kawaida yanayowezesha binadamu au Watanzania walioko huku ndani au viumbe hai vyote kufanya kazi zao vizuri na kupata mahitaji vizuri.
Mheshimiwa Spika, pia, Serikali tumeendelea kusimamia Sheria za Mazingira ambazo pia zinakinga maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na misitu, mito na maeneo mengine yote ili kuhakikisha kwamba tunakabiliana na hili. Pia, Serikali tunaendelea kuweka utaratibu wa kutoa elimu kwa jamii kuwaelimisha Watanzania umuhimu wa kuhifadhi mazingira yetu kwa ujumla, lakini pia hata Taasisi za Kimataifa nazo zimeshiriki kikamilifu na Mataifa makubwa nayo yameshiriki kikamilifu katika kupambana na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini kwamba, kadri ambavyo dunia na nchi zote duniani zinakabiliwa na jambo hili na Serikali yetu nchini pia, tumeshiriki katika kuhifadhi mazingira huku ndani hiyo ikiwa ni moja ya mapambano ya mabadiliko ya tabianchi duniani. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Watanzania kwamba, mabadiliko ya tabianchi kama tutaendelea kuharibu misitu yetu, kuharibu vyanzo vyetu, tunaweza kukosa huduma za jamii ambazo zinatokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni muhimu sana tukashirikiana kwa pamoja kupitia wataalam ambao wanatoa elimu na wananchi na kila mmoja ambaye ana dhamana kwenye eneo lake, ili tuweze kushiriki kwa pamoja kuhifadhi mazingira yetu, ikiwa ni moja kati ya mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Ahsante sana.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ni Sera ya Serikali kulinda usalama wa watu na mali zao. Mheshimiwa Waziri Mkuu, mwezi wa Saba Jeshi la Polisi lilifanya shambulio Msikitini katika Jimbo langu na ikasababisha kifo cha Sheikh Ismail Bweta na kuondolewa jicho kwa Sheikh Abdallah Nakindabu, lakini Serikali iko kimya. Je, Serikali iko tayari kulipa fidia kwa watu hawa? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza sina uhakika kama Jeshi la Polisi lilimshambulia huyo unayemtaja kwa jina na kumtoa jicho, kama ambavyo umedai, lakini jukumu la vyombo vya dola, Jeshi la Polisi likiwemo, ni kulinda usalama wa raia wake na mali zao. Sio jukumu la Polisi kwenda kumshambulia mtu na hatimaye sasa tuanze kufikiria kulipa fidia kwa sababu ya shambulio lililofanywa na Polisi.
Mheshimiwa Spika, kama kuna askari au yeyote kutoka chombo cha dola ambaye ametenda tendo hilo yeye mwenyewe, ikiwa ni nje ya majukumu yake ya kila siku, hilo atakuwa ametenda kosa binafsi na atachukuliwa hatua za kisheria kama yeye aliyetenda kosa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali haiwajibiki kulipa fidia ikiwa si sehemu ya maagizo na wala si jukumu la majeshi ya vyombo vyetu vya dola, bali ikithibitika kama mmoja kati ya watumishi wetu wa vyombo vya dola ambaye ametenda kosa hilo na ikathibitika yeye mwenyewe atawajibika kuchukuliwa hatua kali ili sasa kama kutakuwa na fidia itakuwa ni moja kati ya hukumu ambazo atapewa na vyombo vinavyotoa hukumu kutokana na tendo ambalo limeshatendwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba, Serikali wala vyombo vyake vya dola havilengi kufanya kazi ya kuweza kwenda kuwatendea makosa wananchi, bali kulinda kama ambavyo nimesema, kulinda amani na mali zao ili tuweze kufanya kazi kama ambavyo tumejipanga kufanya kazi zetu vizuri. Ahsante sana.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa fursa hii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni na ni muda mrefu sasa kumekuwa na migogoro ya hifadhi na maisha ya wananchi wetu kwenye majimbo mbalimbali Na hivi karibuni kumekuwa na matangazo ya kuwakataza wananchi wetu wasiendelee na shughuli za uzalishaji na waweze kuondoka kwenye maeneo hayo. Je, Serikali inatamka nini juu ya maeneo ambayo asilimia kubwa ni hifadhi, lakini vijiji vyake vimeandikishwa kwa maana vina GN? Ahsante sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nchi yetu tuna mapori ambayo tumeyahifadhi kisheria na yana mipaka yake rasmi kwa mujibu wa ramani zilizochorwa zinzolindwa na sheria hizo. Mapori haya yako katika kila eneo na ni budi kila Mtanzania kushiriki kuyahifadhi. Sasa kumetokea uvamizi ambao unafanywa na walio jirani kwenye maeneo hayo, lakini mbili, maeneo hayo yamekuwa na migogoro mingi kati ya mapori
yetu na vijiji, kati ya mapori na wananchi ambao wanapeleka kufanya shughuli za kijamii huko ndani ambako pia, haturuhusu kufanya shughuli za kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kutokana na migogoro hii ya muda mrefu nilitoa agizo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya mapitio ya mipaka hiyo na kuweka alama kwenye mipaka ya mapori yote, lakini tumekuja kugundua kwamba, pia kwenye mapori hayo viko vijiji vimesajiliwa na ni Serikali tumesajili.
Mheshimiwa Spika, pia kulianza migogoro pale ambapo wale wataalam wanapita kuweka mipaka ile ili kutambua mipaka, tulichowasihi wananchi walio kwenye vijiji vilivyosajiliwa hata kama viko kule ndani kwenye misitu ile kwamba, wawaache wataalam wafanye mapitio na waweke alama hizo zinazobainisha mipaka hiyo kwa mujibu wa ramani.
Baada ya hapo tutakuja kuona ni kijiji gani kiko ndani na je, pale palipo kijiji malengo yetu ya uhifadhi yamefikiwa na bado ni mahitaji sahihi? Ili baadaye tuje tufanye maamuzi ya au kupunguza maeneo ambayo tunaona kwa sasa kwa uhifadhi huo hauna tija kwenye maeneo hayo, ili kuondoa migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi hiyo inaendelea na nimewaagiza kufikia mwezi wa 12 tarehe 30 wawe wamekamilisha mapori ambayo bado. Baada ya hapo sasa tutakwenda kuona ni vijiji vingapi vilisajiliwa na Serikali viko kwenye hifadhi hiyo na kama vijiji hivyo, bado viko kwenye maeneo ambayo yana tija kwa malengo ya uhifadhi au hayana tija kwa malengo ya uhifadhi, tufanye maamuzi mengineyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nitoe wito kwa wananchi wote ambao wako kwenye hifadhi ambazo zimetambuliwa baada ya kuwa wanaweka alama hizi, wawaache wataalam wetu waweke zile beacons, wamalize zoezi hilo hata kama kijiji hicho kimejikuta kiko ndani ya
beacon hizo, wawaache watulie wafanye kazi zao. Baada ya kazi hiyo tutakuja kufanya mapitio katika vijiji hivyo, ili sasa tufanye maamuzi na tutafanya maamuzi kwa maslahi ya nchi. Inaweza kuwa labda kufuta kijiji au kukiacha na kubadilisha mipaka na kuchora ramani mpya. Kuanzia hapo sasa tutakuwa tunaenda vizuri na wananchi watashiriki pia katika kuhifadhi misitu hiyo. Ahsante sana.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Siku ya Jumatatu tarehe 4 Februari, 2019, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa majumuisho ya Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Miundombinu na Kamati ya Viwanda na Biashara alitoa kauli ndani ya Bunge lako iliyomaanisha kusema Serikali imejidhatiti kukuza mitaji yake yenyewe ili kuacha kutegemea mitaji ya uwekezaji na misaada kutoka nje na alitamka akisema wawekezaji wengi ni wezi na wana mikataba ya kinyonyaji. Je, huo ndiyo msimamo wa Serikali kuhusu wafadhili na wawekezaji wa nchi hii?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba sina uhakika kama Naibu Waziri wetu aliwahi kutoa kauli hiyo kwa sababu huo siyo msimamo wa Serikali. Msimamo wa Serikali ni kukaribisha wawekezaji kuwekeza kwenye sekta zote za kibiashara na tunatoa fursa hiyo kwa mwekezaji yeyote wa ndani mwenye uwezo na wale wa nje wanakaribishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali tumefanya kazi kubwa ya kujenga mazingira ya uwekezaji mzuri hapa nchini. Tuna ardhi ya kutosha na tumetoa maelekezo katika Halmashauri zote kutenga ardhi kwa ajili ya kufungua milango ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya ardhi lakini pia tuna madini na sekta nyingi ambazo kila moja anayetaka kuwekeza anao uhuru wa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jukumu letu Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza mifumo rahisi ya kumwezesha mwekezaji kuwekeza biashara yake na kufanya biashara yake katika mazingira rahisi. Pia Serikali inajitahidi kukutana na wawekezaji wakati wowote kuzungumza nao ili kusikia changamoto ambazo zinawakabili kwenye uwekezaji wao. Ndiyo sababu Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ameendelea kutoa wito wa ujenzi wa uchumi wa Tanzania kupitia viwanda na sehemu kubwa ya viwanda vinawakaribisha wawekezaji ili waweze kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wawekezaji wote nchini na wale wa nje kuja Tanzania kuwekeza; sekta za uwekezaji ziko nyingi, Serikali inajenga miundombinu, tumejenga barabara nzuri za kufanya biashara zao, tunaendelea kuboresha reli, Shirika la Ndege na usafiri wa majini, malengo yetu ni kumwezesha mwekezaji na mfanyabiashara huyu kufanya biashara yake katika mazingira rahisi. Kwa hiyo, huo ndiyo msimamo wa Serikali wa kuhamasisha uwekezaji na kwamba tutawalinda wawekezaji wale wanaojenga viwanda vya ndani na tutalinda viwanda vya ndani ili viweze kufanya biashara yake vizuri zaidi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu natamani sana kujua mpaka sasa Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha kwamba tunaboresha na kurahisisha mazingira ya kufanya biashara nchini?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sannda, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake haliko mbali sana na swali la Mheshimiwa Lucy ambalo alitaka Serikali itoe msimamo wa namna ambavyo inaboresha biashara na kutoa fursa ya uwekezaji kuwekeza hapa nchini. Swali hili la mpango au mkakati wa Serikali wa kuboresha biashara, kama ambavyo nimesema kwenye swali la awali kwamba Serikali imejenga mazingira mazuri ya kuwezesha kufanya biashara.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba wafanyabiashara ndiyo wanaochangia pato la Serikali hapa nchini. Katika kuchangia pato la Serikali lazima tuhakikishe wafanyabiashara wote; wafanyabiashara wakubwa, wa kati, wadogo wakiwemo wamachinga, mamalishe tuwape fursa ya wazi, pana ya kuweza kufanya biashara hiyo kwa sababu wao wanachangia pato hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika uchangiaji wa pato hilo maana yake lazima Serikali sasa tuendelee kuwahamasisha wafanyabiashara, tunaendelea kuhakikisha tunajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara maeneo yote. Watanzania wote ni mashahidi, Mheshimiwa Rais wetu pia kama ambavyo nimesema awali mmeona juzi jitihada za kutoa vitambulisho kwa ajili ya kuwatambua wafanyabiashara wadogo ili waweze kuratibiwa maeneo yao na wafanye biashara vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia wafanyabaishara wa kati nao uko mpango unaendelea na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha kwamba wanakutana na Waziri kujua mwenendo wa biashara kwenye maeneo yao na hivyo hivyo kwa wafanyabiashara wakubwa. Wote mnajua kwamba tunalo Baraza la Wafanyabiashara ambalo pia Mwenyekiti ni Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na wafanyabiashara mara kadhaa ili kusikiliza matatizo wanayokutana nayo katika uendeshaji wa biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mkakati wa kujenga mazingira mazuri ya kibiashara unaendelea ikiwemo pia na upanuaji wa sekta zinazowasaidia wafanyabiashara kufanya vizuri wka maana ya kujenga miundombinu, barabara zote nchini kama nilivyosema awali zimepanuliwa na zinaunganisha mikoa. Kwa hiyo, mfanyabiashara ana uwezo wa kufanya biashara kutoka Katavi mpaka Dar es Salaam akipita kwenye barabara nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumenunua ndege, wale wote ambao wanataka kufanya biashara za ndege za ndani na mpango wetu kwenda nje wanayo fursa ya kufanya hilo. Pia usafiri majini, Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria tunajenga meli mpya ili ziweze kusafirisha abiria na wafanyabiashara kutoka eneo moja mpaka lingine. Kwa hiyo, jitihada zote hizi lengo letu ni kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanafanya biashara katika mazingira mazuri na huo ndiyo mpango wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie wafanyabiashara kuendelea kupanga mipango mizuri kwenye mpango wa biashara zao, Serikali inaandelea kuwaunga mkono na pale ambapo wanapata matatizo yoyote kwenye biashara tutaendelea kukutana pamoja na Waziri yupo lakini pia Ofisi yangu iko wazi tunawakaribisha kuja kuzungumzia changamoto ambazo zipo. Muhimu ni tufuate kanuni na sheria na taratibu ambazo zinakuruhusu kufanya biashara. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi kuuliza swali kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kutokana na songombingo iliyoipelekea zao la korosho kwa msimu uliopita ambao sasa hivi tunaendelea nao kukosa soko jambo lililopelekea Serikali kuingilia kati na kutangaza kwamba inakwenda kununua korosho za wakulima. Hata hivyo, hadi leo wakulima walio wengi hawajapata fedha zao wakati korosho tayari zimeshachukuliwa na Serikali. Siyo hivyo tu, kuna baadhi ya wakulima wameanza kulipwa kidogo kidogo lakini kinachoshangaza wakulima wengi wanalipwa Sh. 2,600 kwa kilo kinyume na Mheshimiwa Rais alivyotangaza kwamba korosho anakwenda kuzinunua kwa Sh. 3,300 kwa kilo.
Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali kulingana na hii sarakasi inayoendelea sasa hivi kwenye zao hili la korosho? Kwa sababu sasa hivi msimu wenyewe unakwenda kuisha lakini wakulima malalamiko ni makubwa sana? Nini kauli ya Serikali? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-
Mheshiiwa Spika, katika kipindi hiki cha Bunge cha wiki mbili hizi suala la korosho limezungumzwa sana na Wizara kwa maana Serikali imetoa ufafanuzi sana namna ambavyo tunaendelea kufanya malipo ya zao la korosho kwa wakulima wanaolima zao hili walioko kwenye mikoa hii mitano ya Ruvuma, Mtwara, Lindi, Pwani na Tanga ambako sasa wako kwenye masoko. Tunachosema zao la korosho siyo kwamba lilikosa soko bali lilikosa bei nzuri, wanunuzi wapo lakini lilikosa bei nzuri. Pale ambapo wanunuzi walikuwa wananua kwa bei ya chini sana kuliko hata ile bei ya kwenye soko la dunia na ilikuwa haimletei faida mkulima. Kwa nia nzuri ya Mheshimiwa Rais akaamua korosho hizi sasa tutanunua kwa Sh.3,300 bila makato yoyote yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipotoa kauli sasa Bodi ya Mazao Mchanganyiko yenye dhamana kisheria ya kununua mazao na kutafuta masoko popote pale na hasa kwa mazao ambayo yanaonekana yanasuasua kupata masoko ilianza kazi yake. Imetafuta fedha, baada ya kufanya tathmini ilishajua kiwango cha korosho kitakachozalishwa na gharama zake, wana uwezo nalo, wameanza kazi hiyo na sasa wanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tamko la Mheshimiwa Rais kununua kwa Sh.3,300 kwa kilo maana yake anazungumzia standard grade ile bei kwa korosho ya daraja la kwanza. Zao la korosho lina grade I, II, iko sheria inayoongoza Bodi ya Korosho kwamba korosho za daraja la II zitauzwa asilimia 80 ya bei ya daraja la I. Kwa hiyo, bei iliyotamkwa ni ya daraja la I, unapokuwa na korosho daraja la II maana yake sasa unarudi kwenye sheria yetu mkulima huyu atalipwa kwa bei ya daraja la II ile asilimia 80 ya bei ya daraja la I. Kwa hiyo, ndicho ambacho kinafanyika, hiyo Sh.2,600 ni calculation ya asilimia 80 ya bei ya daraja la I. (Makofi)
Mheshimiwa Spoika, lakini malipo haya yanaendelea vizuri na kama vile tulijua swali litakuja tena na wakati wote kwa kuwa timu iliyoko kule Mtwara inaendelea kutoa taarifa mpaka jana tumewaongezea tena shilingi bilioni 100 na sasa inafanya zaidi ya shilingi bilioni 500 kulipa na mahitaji yetu sisi ni shilingi bilioni 700. Kwa hiyo, wakishamaliza tunaongeza na kuhakikisha tunamaliza na kama ambavyo unajua niliingilia kati mchakato mzima na kuwapa tarehe ya mwisho ya kulipa wakulima ambayo ni tarehe 15, tuna uhakika kufikia siku hiyo tutakuwa tumefikia kiasi kikubwa cha malipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie wakulima kwamba malipo yanaendelea na sehemu kubwa ya wakulima tumeendelea kuwalipa na hasa wale walioko chini ya kilo 1,500 lakini sehemu kubwa ya malipo ambayo yanakuja sasa ni wale wa zaidi ya kilo 1,500, uhakiki umeshafanyika na wanatambulika na sasa utaratibu wa kulipa ambao unaendelea ndiyo ambao utawafanya wakulima sasa kila mmoja aweze kupata fedha yake. Nataka niwahakikishie wanunuzi wa korosho na wakulima wa korosho kwamba korosho zote kama ambavyo tumetamka mara zote kwamba tutazinunua kama ambavyo imekubalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini taratibu zinazoendelea ni ili tujue kwa uhakika zaidi mkulima anayelipwa kuwa ndiye mwenye mali na ndiyo anayelipwa, huo ndiyo mkakati ambao unaendelea kwa sasa. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wenzangu na hasa mnaotoka kwenye maeneo ya korosho muwe na amani kabisa, Serikali inaendelea na utaratibu wa kulipa na tutawalipa wakulima wote kwenye maeneo yote. Wakulima wenyewe wawe na imani na Serikali yao na mpango ambao unaendelea kwamba kila mkulima aliyepima korosho zake atafikiwa na atapata malipo yake. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kumuuliza swali moja Mheshimiwa Waziri Mkuu linalofanana kidogo na swali alilouliza Mheshimiwa Kuchauka.
Mheshimiwa Spika, wiki mbili zilizopita Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa Mkoani Mtwara na akatoa maagizo kwa timu zote zinazofanya uhakiki wa kupitia mashamba ya wakulima ziwe zimekamilisha zoezi lile ifikapo tarahe 5 Februari, 2019. Leo tunapongea tarahe 7 Februari, 2019 wakulima wengi wenye korosho zinazoanzia tani moja na nusu na kuendelea bado hawajafikiwa na zoezi hili la uhakiki.
Mheshimiwa Spika, nataka kupata majibu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kwa kuwa mpaka leo bado watu hawajafikiwa na uhakiki, nini kauli ya Serikali kwamba inaongeza siku za uhakiki au kwamba zoezi ndiyo limefikia mwisho ili wakulima waweze kujua kwa sababu hawaoni hizo timu za uhakiki zikiwaendea kwenda kuwahakiki? Nakushukuru sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mchakato wa uuzaji wa zao hili la korosho kulikuwa na eneo ilikuwa ni lazima tufanye uhakiki hasa wale wenye korosho zaidi ya kilo 1,500 na ili kuwatambua ilikuwa ni lazima tujiridhishe kama korosho ni zake kwa kufanya uhakiki? Awali utaratibu huu ulikuwa unafanywa na Bodi ya Mazao Mchanganyiko pekee jambo ambalo lilihusisha watumishi wengi lakini bado walikuwa hawakidhi mahitaji ya ukubwa wa maeneo ya wakulima wa korosho.
Mheshimiwa Spika, baada ya kugundua kwamba kulikuwa na tatizo hilo, nilipokuwa Mkoani Mtwara nilitoa maelekezo mapya na nilikuwa na tarehe 27 na ndipo nilitoa maagizo kwamba utaratibu wa uhakiki ushuke chini uhusishe Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa maana ya Halmashauri ambako pia tunajua tuna Mkuu wa Wilaya mwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama lakini tuna Mkurugenzi ana Afisa Ushirika na Maafisa Kilimo waunde timu zifanye kazi ya uhakiki baada ya kuwa wamepewa majina ya watu wao wenye kilo zaidi ya 1,500 kwenye maeneo yao. Hizi wilaya zina utofauti wa ukubwa na idadi ya wakulima, kwa hiyo kuanzia tarehe 28 kama walikuwa wameshaanza kujipanga mpaka tarehe 5, inaweza kuwa baadhi ya wilaya ambazo ni kubwa sana kama ambavyo unasema Mheshimiwa hawajakamilisha lakini zoezi hilo halikomi na kuwaacha ambao hawajahakikiwa kuwa wasihakikiwe. Tarehe ile ilikuwa ni ya kimkakati wahakikishe wanafanya kwa haraka, wanawafikia wakulima ili kila mmoja awe ameshahakikiwa.
Mheshimiwa Spika, lakini uzuri ni kwamba wilaya kadhaa ambazo zina idadi ndogo ya wakulima waliolima korosho na kufikia kilo 1,500 zoezi limekamilika na sasa wanasubiri ulipwaji. Wilaya zile kubwa kama Tandahimba, Nanyamba, Newala, Masasi, Nanyumbu, Liwale, Nachingwea karibu wilaya nyingi, kama vile Rufiji, ni wilaya kubwa na kama Bodi ile ilikuwa na idadi ndogo ya watu wa uhakiki kuna uwezekano wakaongeza. Sisi tunasema muhimu zaidi wakulima wahakikiwe kila mmoja aweze kupata haki yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kupitia kwako nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kila mkulima atahakikiwa lakini naamini mpaka tarehe 5 idadi kubwa kwa sababu ya msisitizo watakuwa wameshafikiwa na wote watalipwa. Kwa hiyo, wale wote ambao hawajafikiwa watafikiwa na watafanyiwa uhakiki kwa haraka zaidi kwa sababu tumeshusha kazi hii ifanywe sasa na Halmashauri za Wilaya, Mkuu wa Wilaya na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama anaweza kuhusisha mpaka Watendaji wa Kata ili kuwatambua wakulima waliolima kiwango kikubwa cha korosho. Kwa hiyo, kazi hiyo inaendelea vizuri. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kutoa shukrani ya dhati kwa kunipatia fursa hii ili niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na hali ya kusuasua katika utekelezaji wa Miradi ya REA kufikisha umeme vijijini. Hivi Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba miradi hii sasa inakwenda kwa kasi ili wananchi wa vijijini waweze kupata umeme, kwani umeme ni maendeleo? Naomba jinsi Serikali ilivyojipanga na kuhakikisha kwamba sasa Miradi hii ya REA itakwenda vizuri katika nchi yetu. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tuna Miradi ya REA na inatekelezwa nchi nzima. Wizara ya Nishati kupitia TANESCO ilishapata wakandarasi na imewasambaza wanafanya kazi hizo maeneo yote. Malengo ya Serikali ni kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa kila eneo kadri tulivyokubaliana na mikataba na wale wakandarasi wanaofanya kazi hiyo. Pia sisi na Mheshimiwa Waziri tunapopita huko tunafuatlia mwenendo wa utekelezaji wa miradi hiyo ili tujiridhishe vijiji vyote vilivyoingia kwenye orodha viweze kupata umeme kadri tulivyokubaliana na wakandarasi wetu.
Mheshimiwa Spika, lakini tutambue kwamba hapa katikati kulikuwa na migogoro kidogo kati ya wazalishaji nguzo na wamiliki wa mashamba yanayozalisha nguzo ambapo walikuwa wanatofautiana kuhusu kodi. Jambo hili nilipolipata mezani kwangu nililifanyia kazi kwa kuita mamlaka zote ili kupata maelezo ya msingi ili kuhakikisha kwamba kazi hii inaendelea. Nashukuru sana Mikoa ya Iringa na Njombe pamoja na na Wilaya zote kwamba tatizo walilokuwa wanabishana nalo la ulipaji kodi ambalo hasa lilikuwa linagusa kwenye tafsiri ya sheria lilikwisha na kazi inaendelea vizuri, wazalishaji nguzo wanaendelea kuzalisha nguzo na wale wakandarasi wanaendelea kupelekewa nguzo kwenye maeneo yao na kazi inaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu na hasa Mheshimiwa Mbunge uliyetaka majibu na Watanzania wote kwenye vijiji ambavyo vimewekwa kwenye mpango kwa ajili ya kupelekewa umeme, tutahakikisha unakwenda kwenye maeneo yote. Serikali inayo fedha kuwalipa wakandarasi, wakandarasi nao wanawajibika kutekeleza kwa mujibu wa mikataba na wale wote ambao tumesaini mikataba ya kuzalisha nguzo waendelee na kazi hiyo, pale ambako wanatakiwa kutekeleza masharti maeneo wanayozalisha nguzo wafanye hivyo kwa sababu uzalishaji huo na malipo yote ni ya kisheria. Kwa kuwa wameendelea kutekeleza jambo hili tumemuachia kazi Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuhakikisha kuwa wazalishaji wanaendelea vizuri na kazi yao na wakandarasi wanaoingia kwenye Wilaya hizo wanapewa mizigo yao na wanasafiri kwenda kwenye maeneo yote ili kazi iweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, zoezi la usambazaji umeme linaendelea na kama kuna tatizo la kusuasua huko Waheshimiwa Wabunge mtupe taarifa ili Mheshimiwa Waziri na yeyote mwenye dhamana anaweza kwenda kuona tatizo liko wapi ili tutatue tatizo hilo. Malengo ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunapata umeme maeneo yote ili Watanzania mpaka kwenye ngazi ya vijiji, kama ambavyo mmsesikia sasa uwekaji wa umeme tunaweka kwenye nyumba zote ya bati, isiyokuwa ya bati ili Watanzania wapate mwanga. Malengo yetu tunaamini yatakamilika na pale ambako kutakuwa na tatizo tutashughulikia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge uwe na amani. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Suala la kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma siyo suala la utashi wa mtu bali ni suala la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, Na.8 ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni zake za 2003. Ni lini sasa Serikali itaacha kukiuka sheria hii kwa kutopandisha mishahara kwa watumishi wa umma na ituambie rasmi ni lini itapandisha mishahara kwa watumishi wa umma?
SPIKA: Hiyo sheria inasomekaje?
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ni Sheria ya Utumishi wa Na.8 ya mwaka 2002 ambayo inaeleza kupandisha mishahara pamoja na stahiki mbalimbali za watumishi wa umma.
SPIKA: Si ungetusomea basi hiyo sheria inavyosema. Siyo kila mtu ana nakala hata Mheshimiwa Waziri Mkuu hana nakala, hawezi kukariri sheria zote. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, swali kwa ufupi linahusu kupandisha mishahara watumishi wa umma, ndiyo logic sasa ya swali hili. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali hajakiuka sheria unayoitaja, kama inasema hivyo, kwa kutolipa nyongeza ya mishahara. Serikali lazima iwe na mipango na mipango ile iliyonayo Serikali lazima imnufaishe mtumishi au yeyote ambaye anapata stahiki hiyo. Nia ya Serikali kwa watumishi ni njema bado ya kuhakikisha kwamba wanapata mishahara na stahiki zao na wanalipwa madeni yanayozalishwa kutokana na utendaji kazi wao. Hiyo ndiyo nia njema ya Serikali na tunatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kwenye eneo la mishahara hili Watanzania wote na wafanyakazi mnajua kwamba nchi hii tulikuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi na wengine hawakuwa wafanyakazi kwa mujibu wa orodha na wote walikuwa wanalipwa mishahara na posho mbalimbali. Kwa hiyo, ili kutambua nani anastahili kupata mshahara kiasi gani na kwa wakati gani Serikali ilianza na mazoezi makubwa mawili. Moja, tulianza kwanza kuwatambua watumishi halali na hewa. Baada ya kuwa tumekamilisha zoezi hili baadaye tulikuja kutambua watumishi wenye vyeti stahiki vya kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa mazoezi yote yamekamilika huku pia tukiendelea kulipa na madeni ya watumishi ambao tumewatambua pia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameunda Tume ya Mishahara Mishahara na Motisha. Baada ya kuwa tumemaliza kutambua watumishi stahiki sasa Tume ile inafanya mapitio ya kada zote za utumishi wa umma na viwango vya mishahara yao ili kutambua stahiki ya mshahara huo na kada hiyo baada ya kugundua kwamba ziko tofauti kubwa za watu wenye weledi wa aina moja, wamesoma chuo kikuu kimoja, lakini wanapata ajira kwenye sekta mbili mmoja anapata milioni 20 mwingine milioni 5, jambo hili kwenye utumishi halina tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nia ya Mheshimiwa Rais kuunda ile Tume ni kufanya tathimini nzuri ya kutambua weledi wa kazi lakini pia itahusisha na uwajibikaji mahali pa kazi na tija inayopatikana mahali pa kazi ili alipwe mshahara unaostahili. Kwa hiyo, jambo hili inawezekana limechukua muda katika kuhakikisha kwamba tunafikia hatua hiyo, inawezekana Mheshimiwa Mbunge ukasema kwamba Serikali haijatimiza Jukumu lake lakini nataka nikuhakikishie kwamba kwa taratibu hizi tunalenga kuhakikisha kila matumishi anapata mshahara kulingana na weledi wa kazi yake au daraja lake ili kuondoa tofauti ambazo zipo za kiwango cha mishahara ambazo zinapatikana kwenye maeneo haya watu wakiwa na weledi wa aina moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakapokamilisha kazi hii, kwa bahati nzuri ile Tume tayari imeshawasilisha taarifa Serikali na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma inaendelea kuipitia, wakati wowote tunaweza kupata taarifa za matokeo ya Tume ile. Kwa hiyo, niwahakikishie watumishi wote nchini kwanza muendelee kuwa watulivu, mbili muendelee kuiamini Serikali yetu na tatu Serikali inayo nia njema ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba watumishi wote wanapata haki zao stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana Mheshimiwa Rais wetu amekutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi, ameeleza vizuri haya na viongozi wamepata nafasi ya kueleza changamoto zilizopo kwenye sekta ya umma na Serikali tumechukua hizo changamoto zote na tunazifanyia kazi. Kwa bahati nzuri mjadala wetu na vyama vya wafanyakazi unaendelea vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ambaye pia umewazungumzia wafanyakazi uendelee kuwa na imani na Serikali, utaratibu wetu ni mzuri na unalenga hasa kuleta tija kwa mfanyakazi ili aweze kufanya kazi yake vizuri. Kwa hiyo, wakati wowote kazi itakapokamilika tutatoa taarifa kwa wafanyakazi. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali moja. Nchi yetu imepata bahati ya kuandaa Mashindano ya Vijana ya Afrika (AFCON). Kwa sababu kutakuwa na wageni wengi akiwemo Rais wa Mpira wa Dunia na wageni tofauti ambao wanakuja kuangalia wachezaji wa nchi mbalimbali, kwa hiyo, tutakuwa na ugeni wa kutosha, nilitaka kujua tumehusishaje mashindano haya na utalii wa nchi yetu ili kuutangaza na kuwafanya wageni hao wawe mabalozi watakaporudi kwao? Pia mmehusishaje na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha kwamba…
SPIKA: Swali moja tu.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Kuhakikisha kwamba usalama unakuwepo? Naomba nijibiwe swali hilo.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwamoto, Kocha wa Timu yetu ya Bunge, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, nataka nitumie nafsi hii kuipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, kwa kazi nzuri waliyofanya ya ushawishi kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani ili kuleta mashindano haya kwetu nchini Tanzania. Pongezi hizi pia zifikie chombo chetu au Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kwa jitihada zake za kuratibu vizuri jambo hili kutoka tulipopata dhamana hiyo mpaka hatua tuliyoifikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Tanzania kupitia Serikali hii ya Awamu ya Tano imeridhia mashindano hayo kufanyika hapa Tanzania na yanafanyika mwaka huu wa 2019. Katika mashindano hayo vijana wetu wanapata fursa ya kushiriki kutoka ngazi ya awali mpaka fainali kama timu zetu zitafika fainali na ndiyo tunaomba taimu yetu ifike fainali ili sisi kama mwenyeji tuweze kufika kwenye fainali na ikiwezekana pia tuchukue kombe la dunia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali imejiandaa kupokea wageni wote wanaokuja kushiriki mashindano haya hapa nchini na inaendelea na maandalizi hayo kwa kushawishi sekta zote zitakazonufaika na uwepo wa wageni hao kuja hapa nchini kujiandaa. Vikao mbalimbali vinafanywa na Wizara pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na wadau mbalimbali wanashirikishwa na Serikali tunajua kazi kubwa inayoendelea kufanywa na tunatambua kwamba tutapokea wageni wengi akiwemo Rais wa FIFA hapa nchini na tunaendelea kujenga mazingira kuwapokea wageni wengi zaidi kadri watakavyopatikana. Huduma tunazo, tunazo hoteli, maeneo ya kutoa vyakula lakini pia usafiri wa ndani tunao, kwa hiyo, ni maeneo ambayo tumeendelea kuimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kupitia mashindano haya tumehamasisha mikoa ya jirani na maeneo ambako viwanja vitatumika na tunaambiwa viwanja vitatu vitatumika wakati wote wa mashindano Dar es Salaam na maeneo mengine, Shirikisho la Mpira litatupa taarifa baada ya kuwa wamekamilisha maandalizi, kwa hiyo, pia na mikoa hiyo nayo itaweza kunufaika. Kwa hiyo, maandalizi ya maeneo yote hayo yanaendelea kufanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kupitia swali la Mheshimiwa Mbunge niwahakikishie Watanzania kwamba ujio huu kwetu ni muhimu sana. Kwa hiyo, sote tunatakiwa tushirikiane kuhakikisha kwamba tunapata mafanikio kwa wageni hawa kuingia, kuishi hapa na kurudi makwao wakiwa salama. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuhakikisha kwamba tuko salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Shirikisho la Soka Tanzania liendelee kuimarisha maandalizi ya timu yetu ambayo itashiriki kwenye mashindano haya ili hatimaye tuweze kuibuka kidedea. Sisi Watanzania wote tunawajibika sasa kuonesha uzalendo kwa timu yetu itakayofanikiwa kuingia ili kuipa moyo. Kwa hiyo, mchango wa kila mmoja wa namna yoyote ile unahitajika katika suala hili. Kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kwamba mashindano tunayapokea, tuko tayari kuwapokea wageni wake na tutaendelea kushindana kwa sababu na sisi tuna timu ambayo itashindana na naamini tutafanikiwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali lifuatalo:-
Kwa kuwa Dira ya Maendeleo ya Nchi yetu ya Mwaka 2015 ni kufikia uchumi wa kati na uchumi wa viwanda ni kigezo kimojawapo; na kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejielekeza kwenye uchumi wa viwanda na imejitahidi kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji ili waweze kuja kuwekeza; hata hivyo, wawekezaji wengi wanakwamishwa na kusumbuliwa sana:-
Je, nini kauli ya Serikali kuhusu suala hili? Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasmine kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli nchi yetu imejikita katika kuboresha uchumi wake kupitia viwanda ambapo tumetoa fursa kwa Watanzania kwa mtu yeyote kutoka Taifa lolote kuja kuwekeza hapa nchini. Suala la uwekezaji tumelipa nafasi muhimu sana kwenye uwekezaji hasa kwenye viwanda.
Awali tulikuwa tunatumia tu Taasisi ya Uwekezaji nchini, lakini Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye uwekezaji pale ambapo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli alipoianzisha Wizara Maalum ya Uwekezaji na kumteua Mheshimiwa Angellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), kumteua pia Katibu Mkuu ili kusimamia uwekezaji kwa ukaribu zaidi.
Mheshimiwa Spika, lengo hapa ni kuhakikisha kwamba tunaondoa usumbufu ambao wanaupata wawekezaji hao ili kuweza kuwekeza kwa urahisi zaidi. Hata hivyo, kwenye uwekezaji sasa tumefikia hatua nzuri sana. Kwanza tumetengeneza andiko maalum (blueprint) ambayo imeonyesha njia rahisi za uwekezaji hapa nchini kwa lengo la kuondoa usumbufu kwa wawekezaji wetu. Kwa hiyo tumetengeneza mazingira rahisi ya uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, pili, tumeboresha kituo cha uwekezaji kwa kukaribisha Wizara zote zinazoguswa na uwekezaji kwa kuwa na mtu wao pale kwenye Taasisi ili mwekezaji anapokuja, huduma zote kama mtu alitakiwa kwenda Wizara ya Ardhi, mtu wa ardhi yuko pale; akitaka kwenda BRELA, mtu wa BRELA yuko pale; anakwenda sijui TFDA; mtu wa TFDA yuko pale. Kwa hiyo, tuna idara kama 10 au 11 ambazo ziko pale za kumhudumia mwekezaji.
Mheshimiwa Spika, badaa ya kuwa Wizara ile imeletwa Ofisi ya Waziri Mkuu, tumeanzisha mfumo wa kielektroniki ambao mwekezaji sasa anaweza kuomba leseni kutoka popote alipo. Tunatambua kuna wawekezaji wako nje ya nchi, haimlazimishi yeye kuja moja kwa moja Tanzania kuanza kujaza makaratasi. Anajaza huko huko Marekani kuomba nafasi, kupata ardhi, kupata ithibati ya uwekezaji hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumetengeneza hayo yote kurahisisha mfumo wa uwekezaji kwa lengo la kupanua wigo wa uchumi hapa nchini kupitia viwanda, kilimo, madini na kila eneo ambalo mwekezaji anataka kuwekeza, sasa Tanzania imefungua nafasi, imetengeneza mazingira rahisi ya uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa wito kwa Watanzania, kwa yeyote kutoka Taifa lolote kuja kuwekeza nchini Tanzania, fursa tunazo na ardhi tunayo. Fursa hizi sasa tumezikaribisha hata kwenye Mikoa na Wilaya kutenga ardhi kwa ajili ya kukaribisha wawekezaji ili pia kuendelea kuongeza mapato ya Halmashauri yenyewe, Mkoa wenyewe na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Suala la vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo wadogo imekuwa ni kero kubwa sana katika maeneo mbalimbali nchini na limekuwa ni kero kubwa zaidi kwa wajasiriamali wale wanaouza mboga mboga kama mchicha, nyanya, tembere, maandazi na vitumbua. Kibaya zaidi, maeneo mengine hata wale wanaotoka shambani, amechuma mchicha wake, anaambiwa naye ni Mjasiriamali aweze kutoa shilingi 20,000/= apewe kitambulisho.
Mheshimiwa Spika, suala hili kwa mtazamo wangu mimi naona kama vile halijatafsiriwa vizuri kule chini hasa wale wanaolitekeleza kwa sababu maeneo mengine pia hata wapiga debe na walimu maeneo mengine wanaambiwa kwamba ni wajasiriamali waweze kulipia vitambulisho vya shilingi 20,000/=.
Mheshimiwa Waziri Mkuu sasa swali langu: Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka hili jambo lingeweza kusitishwa kwanza ili tuweze kufanya tathmini na kupanga vizuri kwamba hasa ni watu gani ambao wamelengwa na wenye mitaji ya namna gani? Kwa sababu kuna wengine wana mitaji ya shilingi 1,000/= wengine shilingi 2,000/=, lakini wanaambiwa walipe shilingi 20,000/= kwa ajili ya vitambulisho vya ujasiriamali?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwalimu Haonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka utaratibu mzuri sana wa kuwafanya wajasiriamali wadogo kuweza kuchangia pato la Taifa; na Mheshimiwa Rais alibuni njia nzuri ambayo inawatambulisha hawa wajasiriamali. Hata hivyo, wajasiriamali hawa tumewaweka kwenye madaraja yao. Wako wale wadogo, wako wafanyabiashara wa kati na wale wajasiriamali wakubwa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais aliwalenga Serikali imewalenga hawa wadogo ambao kipato chao kutokana na kazi wanayoifanya hakizidi zaidi ya shilingi milioni nne kwa mwaka ili nao wapate nafasi ya kuweza kuchangia pato la Taifa lakini kuwaondolea usumbufu kwenye maeneo wanayofanya biashara kwa kutozwa kodi kila siku ambayo pia na yenyewe inasaidia kupunguza mapato wanayopata kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, sasa vitambulisho vile vilipotolewa kwa Wakuu wa Wilaya, tambua kwamba kuna maeneo mengine utekelezaji wake siyo mzuri, kwa sababu wako wengine wanalazimisha watu badala ya kuwaelimisha namna ya kupata vitambulisho hivyo. Yako maeneo wanapewa hata wale wajasiriamali wakubwa wenye pato la zaidi ya shilingi milioni nne, linawafanya na wao wanashindwa kuchangia kulingana na biashara wanazozifanya kwa sababu wao kwa category yao wanachangia TRA moja kwa moja, lakini wale wadogo hupitia vile vitambulisho.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maelekezo ambayo tumeyatoa tena baada ya kuwa tumepata malalamiko kutoka kwenu Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa watumie muda wao kuelimisha nani anapaswa kuwa na kitambulisho badala ya kutumia wakati mwingine nguvu au kwenda kulazimisha au kuwapa wajasiriamali wakubwa wenye mapato zaidi ya shilingi milioni nne na kuondoa maana ya uwepo wa vitambulisho? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kupitia Mheshimiwa Mbunge Serikali tumeipokea hiyo. Tunaendelea kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya watumie nafasi hiyo kuelimisha zaidi kuliko kulazimisha, ni nani wanatakiwa wapate kitambulisho hicho ili kuwaondolea usumbufu wa kuwa wanatozwa fedha tena shilingi 200/=, shilingi 500/= kila siku anapoendelea kufanya biashara yake ya mchicha, maandazi, wale wanaokimbiza mahindi vituo vya mabasi.
Mheshimiwa Spika, watu wa namna hii ndio ambao Mheshimiwa Rais aliwalenga ili nao waone uchangiaji wa uchumi, pato la nchi ni sehemu yao lakini pia waendelee kufanya biashara yao bila kusumbuliwa ndani ya mwaka kwenye Halmashauri zao. Kwa hiyo, niseme tu, tumeipokea tena hiyo na tutaifanyia kazi zaidi ili kuleta utendaji ulio sahihi na wajasiriamali waweze kujitoa kuchangia kwenye nchi yao.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu katika swali lake amesema pia kwamba walimu wanalazimishwa wapewe vitambulisho vya wajasiriamali. Sijui hilo nalo unasemaje Mheshimiwa Waziri Mkuu?
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Sawasawa, hilo limetokea Jimboni kwangu.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la swali la Mhehsimiwa Mwalimu Haonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, inawezekana pia uko utekelezaji usio sahihi. Mwalimu kama Mwalimu ni miongoni mwa watu wenye pato la zaidi ya shilingi milioni nne kwa mwaka. Kwa hiyo, mwalimu anapofanya biashara, ile biashara anayoifanya kama yenyewe haimfikishi kwenye pato hilo, Mkuu wa Wilaya ambaye yuko kwenye eneo hilo, anajua mwenedno wa pato la huyo mtu ambaye yuko pale.
Mheshimiwa Spika, sasa suala la mwalimu na mfanyakazi mwingine, muhimu zaidi ni ile biashara anayoifanya, lakini pia namna ambavyo anaweza pia akachangia pato kupitia biashara hii anayoifanya ambayo uzalishaji wake haifikii kiwango hicho cha shilingi milioni nne kwa mwaka.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Swali langu ninapenda kufahamu, kwa kuwa takwimu za Taifa kwa sasa zinaonyesha kuwa kila mwaka watu 82,000 wanaambukizwa virusi vya UKIMWI hapa nchini na ni-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na Dawa za Kulevya.
Mheshimiwa Spika, kati ya hao wanaoambukizwa ni kuanzia miaka 15 mpaka 64 na asilimia kubwa inaonyesha kwamba vijana ndiyo wanaoongoza hivi sasa kwa asilimia 40 na kati ya hao vijana, watoto wa kike ndiyo ambao wanaoongoza kwa asilimia kubwa.
Mheshimiwa Spika, watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa sasa, takwimu za Taifa…
SPIKA: Sasa swali Mheshimiwa Mollel.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, swali langu; nilipenda kufahamu mkakati wa Serikali, tamko la Serikali juu ya hali hii kwa sababu hali ni mbaya. Nini tamko la Serikali katika kusaidia Taifa na hasa vijana ambao ndiyo tunawategemea katika nguvu kazi ya Taifa?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Mollel, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tatizo la UKIMWI nchini limekuwa likiratibiwa vizuri sana na Serikali toka tulipoanza kampeni ya kupambana na maambukizi ya UKIMWI kwa kushirikisha Wizara zote ambazo zinahusika katika kulinda afya ya Mtanzania. Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo hasa inasimamia suala la mapambano dhidi ya UKIMWI kwa kuwa tumeshaunda Taasisi inayoitwa TACAIDS. Tunafanya kazi kwa pamoja na Wizara ya Afya ambayo ndiyo ina wajibu wa kusimamia afya ya Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, pia Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ambayo inashughulikia masuala ya UKIMWI nayo pia imekua ikishiriki kikamilifu. Kwa hiyo, mkakati huu wa pamoja ndiyo unaowezesha sasa kupambana na maambukizi ya UKIMWI ambayo sehemu kubwa yanaathiri sana maisha ya vijana kama ambavyo umeeleza na takwimu ambazo unazo mezani kwako.
Mheshimiwa Spika, muhimu zaidi ni kwamba mkakati wetu sasa ambao tunao ni kuhakikisha kwamba wale Watanzania wote kwanza tunatakiwa kupima ili kujitambua afya yetu na malengo yetu kufikia mwaka 2020 kila Mtanzania awe ameshapima. Ndiyo maana tumeweka kampeni ya upimaji karibu maeneo yote na kila mahali wanapokutana, wananchi zaidi ya 100 lazima pawe na eneo la kupimia ili kutoa fursa kwa Watanzania kwenda kupima. Kwa hili pia tuna kampeni kubwa, tumegundua wanaopima sana ni akina mama kuliko wanaume, nami ni Balozi wa wanaume wa upimaji. Kwa hiyo, tunahamasisha kwa ujumla wake watu wapime.
Mheshimiwa Spika, pili, wale wote waliopima na wamegundulika kuwa na maambukizi, kufikia mwaka 2020 tunataka wote wawe wameshaanza kutumia dawa za kufubaza hivyo virusi vya UKIMWI. Tunataka kufikia mwaka huo kila ambaye amepima, akishajitambua aanze kutumia dawa. Malengo yetu ni wale wote ambao wamepima na kukutwa na virusi wawe wameanza kutumia dawa, ifikapo mwaka 2020 tupate idadi kubwa ya watu ambao tayari wamefubaza virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, nini ujumbe hapa? Ujumbe ni kwamba Serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapunguza kwa kiasi kikubwa maambuki ya UKIMWI nchini kupitia Kampeni, Kupitia Programu zetu ambazo tunazo, pia tunaendelea kuwaelimisha Watanzania kuendelea kutambua afya zao pale ambako wanajikuta wana maambukizi waende wakapime moja kwa moja na hasa vijana ambao umewalenga wa kati ya miaka 18 mpaka 25 ambayo sehemu kubwa ndio waathirika wakubwa hao ndio tunafanya kampeni.
Mheshimiwa Spika, hiyo kama haitoshi, tumeendelea kutoa elimu hii kwenye shule za msingi na sekondari ya maambukizi ya UKIMWI na kuwataka watoto sasa, vijana wetu kwenye shule za msingi na sekondari wawe na tahadhari ya maambukizi, waaache kujiingiza katika maeneo ambayo yana maambukizi ili waendelee kuwa salama na wao ndio wawe Walimu wa Watanzania wengine katika kujikinga na maambuki ya UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo programu za kujikinga na UKIMWI zinaendelea na Serikali inaendelea na mpango wa kuwahamasisha Watanzania na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kupitia Kamati kazi nzuri wanayoifanya kuisaidia Serikali ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanatambua umuhimu wa kupima, kupata madawa na umuhimu wa kujilinda wakati wote hapa tunapoendelea na shughuli zetu. Ahsante sana.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, hivi karibuni nchi yetu ilipata heshima kubwa ya kuandaa mashindano ya AFCON, lililotokea Watanzania wote wameshuhudia lakini tumejifunza mambo mengi. Sasa kwa kuwa tumepata heshima nyingine tena ya kuandaa mashindano ya watu wenye ulemavu ya Afrika Mashariki. Je, Serikali sasa inasemaje ili watuondoe kimasomaso?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba nchi yetu sasa tumeanza kushuhudia na kuona mwamko wa Watanzania kushiriki katika michezo mbalimbali. Pamoja na mwamko huu tuliokuwa nao tumeanza kuona pia hata mashirikisho mbalimbali duniani na Afrika wanaendelea kututambua Watanzania na kutupa heshima ya kuendesha mashindano mbalimbali. Leo hii nchini tunayo mashindano ya vijana wetu wa umri chini ya miaka 17 yanaendelea nchini na sisi tulipelekea timu yetu, hatujafanya vizuri lakini tumejifunza mambo mengi kupitia mashindano haya.
Mheshimiwa Spika, pia nafurahi kusikia kwamba nchi yetu pia imepata heshima ya kuendesha Mashindano ya Walemavu ya Afrika Mashariki. Jambo hili kwetu kama Tanzania ni tunu kwa sababu tunaanza kuona mashirikisho mbalimbali ya michezo duniani na Afrika yakitupa hadhi ya kusimamia mashindano hayo, maana yake ni nini? Maana yake nchi yetu inatambulika au kwa upande wa usalama au uwezo wa kusimamia pia inatutengenezea fursa kwa Watanzania kutumia mashindano hayo kuboresha pia masuala ya uchumi. Hili litatufanya pia na sisi sasa tuondoke hapa tulipo kimichezo katika michezo mbalimbali na tuweze kufikia hatua nzuri ya kuweza kushindana mpaka ngazi ya dunia.
Mheshimiwa Spika, mashindano ambayo yanaendelea na hayo ambayo yatakuja, tutaendelea kujifunza na kuandaa vizuri timu zetu za ndani zinapokwenda kushiriki zipate kombe lililotarajiwa na ambalo tumeletewa hapa nchini ili tuweze kuboresha. Vile vile Serikali sasa tumeanza kusimamia michezo hii ikichezwa kutoka umri mdogo kwenye shule za msingi na sekondari, kwenye vyuo ili kuweza kupata kuunda timu za Kitaifa ambazo sasa tunaanza kuona mwelekeo huo mkubwa. Hiyo ndiyo ilifanya hata mashindano haya ya vijana wa umri chini ya miaka 17 kuruhusu vijana wote wa shule za msingi, sekondari walioko likizo na Watanzania wote kuingia bure kwenda kushuhudia michezo inayochezwa kwa lengo la kujifunza zaidi kwenye michezo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hadhi na heshima ambayo tunaipata Serikali ni pamoja na kupata fursa za kuongeza uchumi, kutangaza nchi, kuboresha sekta ya utalii na kila mmoja hasa watoa huduma kupata fursa ya kuweza kutoa huduma. Nitoe wito kwa Watanzania, tuanze sasa kuona michezo kuwa ni fursa kwetu na tuendelee kuungana pamoja kuhakikisha kwamba michezo inachezwa katika maeneo yote na michezo yote, tuunde vilabu, tuvisimamie vizuri, viingie kwenye mashindano na kila shirikisho la kila mchezo lishawishi kwenye ngazi yake ya Afrika, ngazi ya Dunia michezo iweze kuchezwa hapa ili fursa zile sasa ziwewe kunufaisha Watanzania. Kwa hiyo kwa kupitia michezo sasa Serikali na Watanzania tunaweza kunufaika zaidi. Ahadi ya Serikali kwenye hili ni kusimamia michezo. Ahsante sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kumekuwa na matukio ya uhalifu katika maeneo ya mipakani na ni kutokana na mwingiliano wa wageni kutoka nchi jirani. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na kuimarishwa na kudhibiti hali ya usalama katika mipaka yote nchini hususan katika maeneo ya Mkoa wa Kigoma ambako kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya uhalifu ambayo yanahusisha matumizi ya silaha za moto?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katimba, Mbunge wa vijana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la ulinzi na usalama nchini ni jukumu letu sote, suala la ulinzi na usalama nchini napenda kuwahakikishia Watanzania na wote ambao wanakuja nchini Tanzania kwamba, ulinzi na hali ya amani na utulivu nchini inaendelea vizuri kwa sababu vyombo vyetu vya ulinzi vinaendelea kufanya kazi katika maeneo yote na kuhakikisha kwamba Tanzania inabaki kuwa salama.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge amezungumzia wasiwasi wake wa hali ya ulinzi na usalama kwenye mipaka na ameeleza hasa Mkoani Kigoma ambako natambua yeye pia anatoka Mkoani Kigoma. Nimefanya ziara Mkoani Kigoma, yako matukio kadhaa yameripotiwa, lakini hasa matukio haya ni kutokana na mchanganyiko tulionao na hasa kwenye mikoa yote iliyoko pembezoni.
Mheshimiwa Spika, nimeenda Kigoma, Kagera na Mkoani Kilimanjaro nimeona dalili hizo na taarifa za Jeshi la Polisi, lakini sehemu kubwa ni salama. Nini tahadhari ya maeneo haya, ni kutokana na mwingiliano wa nafasi ambazo tunazo na nchi jirani ambazo zinazunguka kwenye maeneo haya, tahadhari kubwa imechukuliwa. Nataka pia nitumie nafasi hii kuwasihi Watanzania hasa wale tulioko mipakani kushiriki kikamilifu katika kulinda mipaka yetu na kubaini vyanzo vyote vinavyoashiria kuleta uvunjifu wa amani nchini tukishirikiana na vyombo vya dola ambavyo vyenyewe vina nafasi ya moja kwa moja kwenye ulinzi wa usalama hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, tunachokifanya ni nini kwenye mipaka? Kwanza, tumeimarisha mipaka hiyo kwa kuweka maeneo maalum ya wanaoingia nchini ili kuweza kuwatambua wote wanaoingia na kukagua wamengia na zana gani kwa lengo la kudhibiti uingiaji wa silaha ambazo haziruhusiwi kuingia hapa nchini. Pia vyombo vyetu vya ulinzi vimeweka tahadhari kubwa sana na nchi jirani ambazo sasa tunashuhudia huko kuwa na migogoro mingi ya ndani, kwamba migogoro hiyo kwenye nchi hizo jirani isihamie kwenye nchi yetu.
Kwa hiyo, Majeshi yetu na vyombo vyote vya dola vinaendelea na umakini huo ikiwemo na Mkoa wa Kigoma ambako tunapakana na nchi jirani zisizopungua mbili, tatu, nne ambazo na zenyewe pia tunaendelea kujenga mahusiano ya kiulinzi kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine anaweza kuhamishia migogoro nchi nyingine ili kufanya nchi hizi kuendelea kuishi kwa umoja, mshikamano pia kuwa na ulinzi wa pamoja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nataka niwahakikishie wananchi wote wanaoishi maeneo ya pembezoni matukio yote madogo yanayoripotiwa yanachukuliwa hatua lakini udhibiti wa mipaka hiyo unaendelea kuimarishwa lakini nitoe wito sasa kwa Watanzania wenyewe tushirikiane, tushikamane katika kubaini viashiria vyote vinavyoleta uvunjifu wa amani nchini kwa lengo ya kuifanya Tanzania kuendelea kuwa salama, kwa lengo la kuifanya Tanzania kuwa ni kimbilio la wale wote wanaopenda amani, kwa lengo la kuwafanya Watanzania wenyewe kufanya shughuli zao za maendeleo wakiwa na uhakika wa maisha yao, wakiwa na uhakika wa shughuli zao.
Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba vyombo vya usalama vinalinda maeneo yote ili kuhakikisha kwamba nchi inabaki salama. Ahsante sana.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa fursa hii niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu natambua na ninapongeza juhudi za Serikali juu ya upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA. Vilevile natambua na ninajua faida za vitambulisho vya NIDA kwa kutambua mtu mmoja mmoja kama Mtanzania na sababu za kiusalama. Hata hivyo kwa sasa hivi kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa namba hizo za NIDA kwenye vijiji na miji. Nini kauli ya Serikali kwasababu wananchi sasa wanapata mkanganyiko speedna upatikanaji nini kauli ya Serikali?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika,naomba kujibu swali la Mheshimiwa Obama Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo:-
Upo ukweli kwamba Watanzania wengi tulikuwa hatujawafikia kuwapa vitambulisho maarufu vya NIDA mpaka ngazi ya vijiji na kule vitongojini; jambo hili Serikali imelifanyia kazi. Kwanza tumeongeza idadi ya watumishi kwenye ngazi za halmashauri ili kuwezesha kufika mpaka kwenye vijiji na vitongoji na kufanya kazi hiyo.
Mbili, tumeongeza pia na mitambo ya kufanyia kazi ili baadaye tuweze kupata vitambulisho; na idadi hii ya watumishi hawa ambao tumeongeza nimpaka Makao Makuu, ili kuweza kuharakisha kutoa vile vitambulisho vyao.
Mheshimiwa Spika, tunachokifanya sasa, ili Watanzania waweze kupata huduma yeyote ile inayohitaji kitambulisho cha NIDA Serikali imeridhia kila yeyote anayetaka kitambulisho cha NIDA kwa mwananchi; na kama mwananchi atakuwa hajapata kitambulisho cha NIDA basi atumie namba aliyopewa ili kuweza kuhalalisha kupata huduma yeyote ile ambayo inahitaji kitambulisho huku akiwa hana kitambulisho. Hiyo ni njia ya kwanza ambayo tumeitumia kurahisisha kuwafikia Watanzania.
Mheshimiwa Spika, lakini mbili, inawezekana pia namba hii ni ngumu kwa mwananchi huyo aliyeko kijiji kuipata. Tumetoa maelekezo kwa watendaji wetu wa NIDA walioko kule kwenye ngazi ya halmashauri kwamba sasa watoe orodha ya wale wote waliowaandikisha kwenye vituo vyao na namba zao ili angalau mwananchi aweze kufika pale kwenye kituo aone orodha na namba yake sasa imuwezeshe mwananchi huyu kupata huduma popote panapohitaji kitambulisho cha NIDA kwa kupeleka namba tu; hiyo ndiyo njia ambayo tumeirahisisha ili kuwafikia Watanzania wote mpaka vijijini na kuhakikisha kwamba sasa uzalishaji wa vitambulisho makao makuu kule Kibaha iende kwa haraka na vitambulisho vipelekwe mpaka vijijini kwa haraka ili kila Mtanzania aweze kupata vitambulisho.
Mheshimiwa Spika, lakini natambua kwenye eneo hili, naomba nizungumze jambo moja, kwamba yapo maeneo tumeongeza umakini mkubwa, na hasa maeneo ya mipakani, kwa lengo la kuzuia wananchi wa nchi jirani kujipatia kitambulisho cha NIDA nchini Tanzania halafu akafanya mambo yake huku ndani kupitia kitambulisho cha nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwahiyo mtaona kunaweza kuwa kuna ucheleweshaji huko kwenye miji iliyoko mipakani na nchi jirani za Tanzania. Kwasababu tunafanya zoezi hili kwa umakini kwa lengo la kutoa kitambulisho kwa Mtanzania tu. Na nitoe wito kwa Watanzania mtusaidie kuwatambua ambao siyo wakazi wa nchi wanaokuja kuchukua vitambulisho vyetu kwa lengo la kudhibiti hali ya ulinzi na usalama ndani ya nchi. Kwahiyo kama kunaweza kuwa kuna kuchelewa maeneo kadhaa hasa mipakani; natambua Mheshimiwa Mbunge unatoka Buhigwe. Buhigwe iko karibu na nchi ya Burundi, kwahiyo pale tumeongeza umakini sana pale ili tusiweze kutoa vitambulisho kwa ndugu zetu wa nchi jirani.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuuliza swali kwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu Tanzania ni nchi ambayo inaendelea kwa kasi kubwa katika uchumi wa viwanda hususan Serikali ya Rais Joseph John Pombe Magufuli; ambayo imejikita sana kwenye uchumi wa viwanda mpaka ambapo muda huu tunaviwanda zaidi ya 3,700; si jambo dogo. Lakini maendeleo haya ya kasi kubwa ya uchumi yanabidi yaendane na maendeleo ya wananchi. Je Mheshimiwa Waziri Mkuu mnamkakati gani kama Serikali kuhakikisha maendeleo ya kasi kubwa ya uchumi wa viwanda na kuhakikisha maendeleo ya watu vinakwenda sambamba?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde Mbunge wa Mkoa wa Tabora kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu inayoongozwa na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli imeelekeza kuboresha uchumi wake kupitia viwanda pia. Viwanda hivi baada ya kufanya study ya kuweza kuwafikia Watanzania na kuwapatia maendeleo; tunajua mchango wa viwanda popote palipo na kiwanda lazima kitumie mali ghafi na malighafi hizi ziko kwenye sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili pia hata madini. Kwa hiyo panapokuwa na kiwanda kinachohitaji malighafi hiyo obvious malighafi hiyo na wale wote wanaozalisha malighafi hiyo watakuwa wameboreshewa uchumi wao kwasababu tayari wanauhakika wa soko pale kwenye kiwanda. Ule uhakika wa soko tayari tunapeleka tunaunganisha manufaa ya uwepo wa kiwanda na hali na maisha ya wananchi wanaopata huduma hiyo kwenye kiwanda hicho.
Lakini viwanda hivi navyo vinavyofaida nyingine nyingi ambazo pia tunaunganisha na maendeleo ya mtu mmoja mmoja. Leo mgogoro wetu wa kukosekana kwa ajira, Rais weru alikuwa na muono wa mbali sana. Viwanda hivi sasa vinaajiri Watanzania kwenye maeneo kilimo; na wote mnajua kwamba hata kwenye ajira tumeweka tumebana kidogo mianya ya watu wengi kutoka nje kuajiriwa badala yake tumefungua milango kuajiriwa kwa Watanzania wenyewe. Kwahiyo viwanda vingi vinaajiri Watanzania kwahiyo angalau tumepunguza mgogoro wa kutokuwepo kwa ajira.
Lakini mbili kwa uwepo wa viwanda hivi tunapata kodi, kodi hizi ndizo ambazo zinatuwezesha leo kujenga zahanati, kujenga shule, kujenga miundombinu ya barabara na maeneo mengine. Kwahiyo tunaufanya uchumi wa viwanda tunaupeleka pia kwa jamii. Hatujaishia hapo tu viwanda hivi sasa vinazalisha malighafi ambazo leo tunakuwa na uhakika nazo kwa uzalishaji wake na ubora wake, lakini pia kwa gharama nafuu na upatikanaji wa karibu kuliko kuagiza vitu kutoka nje zaidi. Kwahiyo tumetengeneza uwepo wa soko la ndani la uhakika ambako sasa uchumi huu tunaupeleka sasa kwa wananchi. Kwahiyo kufungamanisha kwa viwanda na uchumi wa mtu mmoja mmoja hasa kumejikita kwenye maeneo hayo, namna ambavyo viwanda vinaleta tija kwa uwepo wake na kwa wananchi walioko jirani na kwa Tanzania nzima. Tunaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda ili watanzania waweze kunufaika na uwepo wa viwanda hivyo.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Watanzania, tunaendelea kuhamasisha na kuita wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi tuendelee kuwekeza kwenye viwanda ili tuboreshe pia uzalishaji na kupata masoko wa malighafi inayotakiwa viwandani. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAKU HASHIM AYOUB:Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, na vilevile nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara yake aliyoifanya Tanzania nzima bila kujali mvua, jua wala kula, nami ni shahidi upande wa kula; hasa kwa upande wa pili wa Muungano; Mheshimiwa nikupongeze kwa dhati kabisa, ni Waziri Mkuu wa Tanzania ikiwemo Zanzibar na kama kuna kitu kilichonivutia Mheshimiwa Waziri Mkuu ziara uliyoifanya katika …
SPIKA: Swali lako Mheshimiwa Jaku.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, ahsante ziara uliyoifanya katika Kiwanda cha Sukari cha Mahonda, umeiona hali ile na ukatoa maagizo. Yale maagizo uliyotoa Mheshimiwa Waziri Mkuu ni sawasawa na maagizo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuwa sukari ile inunuliwe pale, ikiisha ndipo waruhusiwe watu kuagiza nje yaani ni maagizo sawasawa uliyoyatoa wewe. Lakini kelele za mlango hazimkeri mwenye nyumba, wewe ndiyo mwenye nyumba zile kelele ulizozikuta pale zisikushughulishe soko kubwa la walaji liko Tanzania Bara.
Je, ni lini mtafikiria angalau ile bidhaa kama zinavyotoka hapa ni saruji ikiwemo Tanga cement, Twiga, Dangote, kiboko na mabati yanakwenda katika soko dogo la Zanzibar angalau nusu yake likaja katika soko lile…?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jaku, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa kutambua jitihada kubwa tunazozifanya. Si mimi bali ni Serikali yetu; imeweka huo mpango na utaratibu wa kuwafikia wananchi popote walipo. Kwa hiyo ziara zangu ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuwafikia wananchi kule waliko.
Mheshimiwa Spika,ni kweli nimefanya ziara kwenye Kiwanda cha Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja; na nimepita ndani ya kiwanda nimeona, nimeenda mpaka Bohari tumekuta sukari nyingi bado imebaki. Kiwanda kile kinao uwezo wa kuzalisha tani 24,000 na sasa hivi kinazalisha tani 6,000. Mahitaji ya Unguja na Pemba ni tani 36,000. Hata hivyo nimeikuta sukari ghalani na bado mwekezaji wetu analalamika kwamba hana soko. Kwa kweli nililazimika kuwa mkali kidogo.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali inahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza hapa na tumewahakikishia kuwa na masoko na kuwalinda, lakini bado hatumpi masoko; na hatumpi masoko kwa sababu tunakaribisha sukari nyingi ya nje kuingia halafu ya ndani inabaki. Kwa kufanya hilo tutakuwa hatumtendei haki yule mwekezaji.
Mheshimiwa Spika, ni vyema; umesema kwamba unahitaji soko pia na Bara, lakini palepale ilipo inapozalishwa sukari mahitaji ni tani 36,000, lakini hizo tani 6,000 hazijanunuliwa zimebaki bohari, mwekezaji anahangaika, anatafuta masoko, haiwezekani!
Mheshimiwa Spika, na mimi nilitumia lugha ile kwamba mpango huu si sahihi, mbovu kwa sababu kwanza tungehakikisha hizi tani 6,000 za ndani zinanunuliwa halafu uagize nyingine. Kama tani ni 36,000 ndiyo mahitaji ya eneo, kwanza tani 6,000 zingetoka; na wale waagizaji basi wangepewa masharti ya kwanza kuinunua sukari ya ndani halafu unawapa kibali cha kuweka top up.Sasa kuagiza sukari yote ya nje iwe inakuja ndani haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi kama Waziri Mkuu mwenye wajibu pia hata kwa chama changu kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi; mimi kwa pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ndio wenye jukumu la kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Suala la viwanda liko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ninapaswa kwenda popote Tanzania kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, sina mipaka. Sasa leo ninapokuta mahali Ilani haitekelezeki lazima niwe mchungu na nitaendelea kuwa mchungu kwa kiasi hicho.(Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, lazima tuweke mpango wa kuwalinda wawekezaji wa ndani na kuwahakikishia masoko, na masoko tunayo. Pale naambiwa waagizaji wako watatu, kwa nini usiwape masharti angalau rahisi, ndio mpango mzuri. Waambie kwanza nunua tani 20,000 chukua tani 10,000 lete na mwingine, na mwingine, 6,000 tumezimaliza. Lakini unaagiza zote kutoka nje halafu huyu atauza wapi? Haiwezekani, haiwezekani. Halafu mtu anasema nimewachefua Wazanzibar; nimewachefua Wazanzibar au nimewachefua wanunuzi? (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, kwenye hili naomba nilieleze zaidi kile Kiwanda pale Mahonda kinawanufaisha wale wananchi wa Kaskazini Unguja kwa sababu wenyewe wanalima miwa, na soko lao ni kile kiwanda. Ukichukua sukari ya nje kama hainunuliwi wale wananchi miwa wanayolima haiwezi kupata soko unawaumiza Wazanzibar. Kile kiwanda kiko pale kinaajiri watumishi 400, wanufaika ni wale walioko Kaskazini Unguja; lakini leo usipouza huyu hawezi kuajiri, hawezi kulipa mishahara kwa sababu sukari iko bohari, haiwezekani! Leo kile kiwanda kiko pale kinalipa kodi, kodi ndiyo ile ambayo imeniwezesha kwenda kuona Kituo cha Afya kule Bambi, kituo cha afya kule Kizimkazi nimeona maabara nzuri imejengwa yenye viwango pale Bwejuu, nimeenda pia Unguja, Kaskazini Pemba nimekuta VETA inajengwa nzuri kwa sababu ya fedha ya kodi ya viwanda!Haiwezekani! (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, mimi naamini Watanzania walinielewa na Watanzania hawa hata wenzangu wa Zanzibar nilichosema ni sahihi. Hao wanaotamka kwamba wamechefuliwa ni wanunuzi, na wala wasio wazanzibari. Sera yetu ni moja ya kuwalinda Watanzania, na tutaendelea kufanya hilo; tutakuwa wakali pale ambapo mambo hayaendi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika awamu ya nne na tano iliazishwa uboreshaji wa Serikali za Mitaa ambayo tuliita ugatuaji wa madaraka au tulikuwa tunaita D by D.
Mheshimiwa Spika, tangu wakati huo Serikali imeendelea kufanya kazi lakini ugatuaji wa madaraka haujaenda sawa sawa. Kwa mfano Serikali imechukuwa vyanzo vikubwa vya mapato vya Serikali za Mitaa; kodi ya majengo na kodi ya mabango. Je, hatua hii ambayo ilikuwa ituwezeshe Serikali za Mitaa kwa rasilimali na fedha inakinzana na dhana nzima ya ugatuaji wa madaraka?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mollel, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunazo Serikali za Mitaa zinayomajukumu yake na Serikali Kuu ambayo inawajibika pia hata kuihudumia hata Serikali ya Mitaa. Kuanzia mwaka 2014 uliousema na kufika sasa tumejifunza mambo mengi katika uendeshaji wa Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, hasa katika utoaji wa huduma za jamii. Yapo maeneo yanahayo mafanikio, yapo maeneo yana udhaifu. Kwahiyo ni jukumu la Serikali kujiwekea taratibu wa kutibu udhahifu huu ili kuwafikia wananchi katika kuwapa huduma. Lakini bado wajibu wa kumuhudumia mwananchi kule tumewakabidhi Serikali za Mitaa ili wafanye kazi ile kwa ukaribu. (Makofi)
Sasa swali lako ni pale ambapo baadhi ya vyanzo tumepeleka Serikali Kuu kwa usimamizi bado Serikali Kuu inalo jukumu la kusimamia na hasa kwenye mapato. Serikali yetu tumeamua kudhibiti ukusanyaji wa mapato na mapato haya yarudi tena kwa wananchi, tunaporudisha kwa wananchi tunawapelekea hao hao Serikali ya Mitaa kwa mahitaji yao ili watekeleze hilo jambo, hatujawaondolea mamlaka ya kusema tunahitaji darasa, tunahitaji kituo cha afya, tunahitaji uboreshaji wa miundombinu; bado mamlaka ile tunayo.
Mheshimiwa Spika, na tumeongeza hata kuunda kwa TARURA ili isimamie miundombinu. Sasa hivi tunaenda kwenye maji isimamie utoaji wa maji. Pale ambapo kuna mahitaji Serikali za Mitaa iseme inahitaji shilingi ngapi kwa ajili ya nini, tunawapelekea. Ndiyo sababu leo tunaona huduma zinatekelezwa mpaka vijijini kwa sababu tunashirikiana na Serikali za Mitaa katika kuratibu. (Makofi)
Kwa hiyo, ule udhaifu wa usimamizi wa makusanyo, usimamizi na matumizi yake ambao ulikuwa umejitokeza sasa tunaendelea kuutibu; na ndiyo sababu unaona wakati wote tunapokwenda huko kwanza tunauliza ukusanyaji na kama makusanyo yoyote yameifadhiwa na matumizi yake, na pale ambapo matumizi yanakuwa si sahihi tunachukuwa hatua. Kwa hiyo tunakwenda tunafanya marekebisho kwa namna ya kutunza rasilimali za Watanzania zinazokusanywa kwenye maeneo haya lakini pia na matumizi yake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mollel awe na amani kabisa kwamba tunafanya kazi kwa ushirikiano kati ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu kwa kuwapelekea rasilimali fedha, rasilimali watu ili ziweze kuhudumia Watanzania walioko kwenye Serikali za Mitaa huo ndio utaratibu tunaoutoa. Lakini hatujaondoa huo wajibu wa kuwahudumia wale wananchi kupitia Serikali za Mitaa. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziru Mkuu.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwambaSerikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya kazi kubwa katika sekta ya elimu na wananchi wameunga juhudi hizo kwa kuchangia ujenzi wa madarasa. Hata hivyo kuna maelfu ya wanafunzi waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza hadi leo hawajaripoti shuleni kwaajili ya upungufu wa madarasa
Mheshimiwa Spika, nilitaka kujuwa ni nini kauli ya Serikali?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Komanya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sasa tunayo idadi nzuri na kubwa ya wanafunzi wanaofaulu darasa la saba kwenda Sekondari. Serikali msimamo wake ni kuwapeleka wanafunzi wote waliofaulu kwenda Sekondari kwa asilimia mia. Serikali imetoa maelekezo kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha kwanza unafanya sense kupitia mfumo wa elimu ambao unaweza kuutabiri halmashauri hii inaweza kutoa wanafunzi wangapi kwenda Sekondari na kujipanga katika kuboresha katika miundombinu tayari kwa kuwapokea vijana hawa.
Kazi hiyo inafanywa kila halmashauri kwa usimamizi wake na wanapofaulu tunataka wote waende waanze kidato cha kwanza kwa wakati. Hata mwezi wa Disemba nilitoa kauli nikiwa mkoani Lindi kwamba kila halmashauri ihakikishe wanafunzi wote wanaenda awamu moja badala ya kuwaweka awamu mbili kwa sababu awamu mbili wale awamu ya pili wanakosa baadhi ya topics za kusoma na kwahiyo syllabus hawawezi kwenda pamoja; na kwamba kila Halmshauri isimamie hilo. Kwahiyo, usimamizi huu ni lazima uzingatiwe
Mheshimiwa Spika, na tumewapa deadline kufikia tarehe 31 mwezi huu wa kwanza wanafunzi wote wawe wamekwenda shule. Kwahiyo tufanye subira mpaka tarehe 31 tupate taarifa, inawezekana pia kuna wasiwasi wa awali, kwamba wanafunzi wengi hawajaenda lakini kutokana na maelekezo tuliyoyatoa, na muda tuliowapa mpaka tarehe 31 unaweza ukawa umekamilika; kwahiyo baada ya tarehe 31 tutatoa taarifa na swali lako litapata majibu mazuri. Kwa sasa msimamo wa serikali ni kuwapeleka wanafunzi wetu wote wanaosajiliwa. Awe anakwenda chekechea, anaingia darasa la kwanza, anaingia kidato cha kwanza, anaingia kidato cha tano, wote lazima waingie darasani kwa wakati na waanze kusoma kadiri syllabus inavyoeleza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2019 uligubikwa na dosari nyingi sana, ikiwemo wagombea kutoka vyama vya upinzani kunyimwa fomu, ofisi kufungwa kwa muda wote, hivyo kusababisha baadhi ya wagombea, hasa wa upinzani kushindwa kupata fursa kuweza kugombea.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni kwamba ni vema uchaguzi wa wa Serikali za Mitaa uweze kurudiwa sambamba na Uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haonga, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, chaguzi hizi zote zinasheria zake na kanuni zake; na hata kanuni za Serikali za Mitaa vyama vyote vya siasa vilishirikishwa katika kutengeneza kanuni zao. Moja kati ya kanuni hizo ni pale ambapo inatoa fursa kwa yeyote ambaye hajaridhika huko anakogombea, kwamba anaweza kukata rufaa, na atakapoona rufaa hiyo kwenye ngazi inayofuata haikutendeka haki aende mahakamani. Kwa hiyo kulichukuwa hili kwa ujumla ujumla si sahihi sana kwasababu kila mmoja alipo alikuwa na mamlaka yake inayoratibu na anayo fursa ya kwenda kwenye mamlaka kukatia rufaa pale ambapo hajaridhika na utekelezaji wa jambo hilo. Vyama vyote vilishiriki kwenye hii kanuni ya kukata rufaa, kwa hiyo ni wajibu wa huyo mgombea kwenye eneo hilo kwenda kukata rufaa.
Mheshimiwa Spika, na kama kulikuwa na dosari kama ambavyo nimeeleza bado zilikuwa zinaweza kuelezwa huko huko kwenye ngazi hiyo, kwa hiyo, huna sababu ya kutengua uchaguzi wote wakati mgombea mwenye malalamiko ana fursa huko huko aliko kwa kukata rufaa na hatimaye hukumu itachukuliwa. (Makofi)
MHE. CASATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kumuhuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali, katika siku za karibuni dunia imekumbana na majanga makubwa mawili; la kwanza ni ule ugonjwa ambao uko rafiki ya China unausababishwa na virus wa aina ya corona.
Mheshimiwa Spika, la pili ni baa la Nzige ambao tayari wameshafika katika baadhi ya nchi jirani na hasa za Afrika Mashariki. Nilikuwa napenda kufahamu, Serikali imejipangaje katika kukabiliana na kudhibiti masuala haya mawili ambayo kwa namna moja ama nyingine yasipodhibitiwa yanaweza yakaadhiri ukuaji wa maendeleo ya taifa letu na wananchi wetu na hasa ukizingatia kwamba kuna biashara kubwa kati ya nchi yetu na China?
Vilevile ukizingatia kwamba kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki wenzetu jirani wameshakubwa na baa la Nzige?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Chumi Mbunge wa Mafinga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba nchini China kuna ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona ambao unapoteza maisha ya watu; na sasa tumeanza kuona hata nchi za jirani yake nazo pia zimepata maambukizi hayo. Lakini pia hili la pili la nzige tumepata taarifa kupitia mitandao na vyombo vya habari kwamba hapa nchi jirani ya Kenya mazao yao yanashambuliwa na hao nzige.
Mheshimiwa Spika, sasa tuanze na hili la corona, corona iliyopo nchini China, China ni nchi rafiki na Tanzania, Watanzania wengi wapo China, lakini pia wapo wachina walioko nchini Tanzania. Tunayo maingiliano mengi kati ya Tanzania na China. Wakati huu wa uongonjwa huu, kwanza tumewahakikishia Watanzania kwamba Tanzania haina tatizo hilo la corona; na jana Waziri wa afya pamoja na Naibu Waziri wa afya wametoa taarifa kwa Watanzania, na nimeona leo kwenye gazeti limetoka hili, sasa jukumu letu ni kuwa na taadhari tusije tukapata tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, sasa kwenye tahadhari Serikali imejipanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja tumeimarisha mawasiliano na Balozi yetu iliyoko China kujua hali huko China inaendeleaje; na Mheshimiwa Mbelwa Kairuki anafanya kazi hiyo ya kutupa mrejesho kila siku na hali iliyoko kule. Baalozi Mbelwa anaendelea kazi nzuri ya kuendelea kutoa elimu kwa Watanzania kwanza ametafuta madaktari wa Kitanzania ambao wamejifunza ugonjwa huo na kuendelea kuwaelimisha Watanzania walioko nchini China namna ya kujikinga.
Mheshimiwa Spika, na balozi kule kwa Tanzania walioko China amewakanya watanzania wasiwe na mizunguko mingi sana kwa sababu ugonjwa huo maambukizi yake ni pale ambapo watu wanakutana. Hiyo moja.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumewataka Watanzania wale wanapohitaji labda kurudi Tanzania, na kwa sababu watatakiwa kusafiri kwenye ma treni, mabasi wafanye mawasiliano na Balozi juu ya namna nzuri ya kusafiri. Wasisafiri kwenda ubalozini Beijing ulipo Ubalozi na badala yake watumie mawasiliano ya kimtandao kupata ridhaa hiyo na kuambiwa hali ikoje ili wapate vibali vya kurudi.
Ndugu Watanzania tunatambua kuna wazazi wana watoto wetu wanasoma nchini China, na wengine wamesharudi likizo. Tunawasihi watoto hawa wasiende kwanza nchini China mpaka hapo tutakapopata taarifa za kidiplomasia.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Nje Tanzania inaendelea kufanya mawasiliano na Balozi zote mbili, Balozi ya China Nchini Tanzania na Balozi Tanzania Nchini China kuona mwenendo wa ugonjwa huo. Pale ambapo Serikali itaridhika kwamba kule hali imepungua tutatoa tamko kwa Watanzania walioko likizo hapa kurudi nchini China kuendelea na masomo, na vinginevyo ikiendelea sana basi Serikali itatafuta utaratibu mwingine.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo, nitowe wito kwa Watanzania kama ambavyo Wizara imetoa kwamba kila Mtanzania awe makini na wageni wanaoingia mpakani na hasa wale wote ambao tumewaweka mpakani kuhakiki wanaongia nchini kupitia vifaa vyetu ambavyo vinaweza kutambua magonjwa mbalimbali kuvitumia vifaa hivyo kikamilifu ili kubaini hao ambao wana dalili ya magonjwa hayo ili kudhibiti kuingizwa ugonjwa huu wa corona hapa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la nzige, kama ambavyo nimesema majirani zetu mazao yanaharibiwa. Nzige ni wadudu hatari sana, wakiingia hapa watamaliza mazao yetu. Tumechukuwa taadhari, Wizara yetu ya Kilimo inaendelea kuwasiliana na Wizara ya Kilimo nchini Kenya kuona mwenendo na ukuwaji wa tatizo hilo, na sisi huku tunajipanga kwa namna ambavyo tunaweza kushiriki kikamilifu; lakini Serikali yetu inashiriki pia kusaidia nchini Kenya kupoteza wadudu hao ili wasiongezeke tatizo hili likawa kubwa nchini Kenya lakini pia lisije likaamia huku nchini kwetu.
Mheshimiwa Spika, sasa bado nitowe wito kwa mikoa na wilaya na vijiji vilivyoko mpakani kuwa makini na hao wadudu nzige.Pale ambapo watawaona wakiingia watowe taarifa haraka sana kwenye mamlaka zao ili hatua kamili iweze kuchukuliwa.
Sisi tumejipanga kudhibiti hali hiyo na tutaendelea kudhibiti hali hiyo ili tusije tukapata tatizo hilo la kuwa na nzige hapa nchini kwetu. Ahsante sana.
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa niweze kumuuliza Mheshimiwa Wazir Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli imejinasibu kuhamasisha ujenzi wa viwanda vikiwemo viwanda vya kuchakata nyama na mazao mengine yanayotokana na mifugo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wafugaji wanatengewa maeneo ya malisho na malisho hayo yanaendelezwa kwa kujenga na kukarabati mabwawa, kuchimba visima vya maji na kuwekewa miundombinu mingine muhimu ili kuboresha afya ya mifugo ili waweze kukidhi haja ya hivi viwanda kwa ajili ya ng’ombe hawa wanapokuwa wameongezewa thamani, wafugaji watapata bei yenye tija? Ahsante sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa Mbunge wa Longido kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli, kama ambavyo nimesema awali kwamba Serikali yetu imejikita katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda kwa lengo la kukuza uchumi wetu; na nimeeleza vizuri sana mwanzo manufaa ya viwanda ikiwemo na kuendeleza sekta yenyewe. Kwa kiwanda cha nyama kuwepo kwake Wilayani Longido tuna uhakika wafugaji wetu watapata faida kubwa kwa kufuga kisasa, kwa kupata masoko ya uhakika lakini pia na sisi tutanufaika kwa kupata nyama iliyopitia kiwandani yenye ubora ambao na sisi tumeuona kwamba ni ubora uliohakikiwa na taasisi yetu.
Kwahiyo, uwepo wa kiwanda kile na mwekezaji huyo, Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi imeweka utaratibu mzuri sana sasa; kwamba wale wote waliowekeza viwanda tumewaunganisha na taasisi yetu ya NARCO kwa kuwapa maeneo yaliyotengwa kama ni maeneo ya malisho, kwa kuwapa eneo la kuhifadhia ng’ombe wao, kuwakuza ng’ombe wao na zile taratibu zote zile za mifugo ili ziweze kukamilika kabla hajaingia ndani ya kiwanda kwa lengo la kutoa nyama iliyo bora kwa ajili ya chakula kama ambavyo tumetaka iwe.
Kwa hiyo tumebaini kwamba ranchi zetu zote nchini au maeneo yote ya malisho nchini. Hawa tumewapa maeneo hayo kwanza wale wenye viwanda lakini pili wafugaji wakubwa na tatu tumewatambua pia na wafugaji wadogo ambao wana ng’ombe kuanzia 100 na kuendelea, ambao tumesema tusiruhusu kuwa na ng’ombe 100 vijijini kwa sababu kunakuwa na migogoro mingi ya mifugo kula mazao, mifugo kuharibu miundombinu mingine. Kwa hiyo tumewatengea maeneo kwenye hizo Rachi zetu au kwenye maeneo hayo ya malisho.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa utaratibu huu tumetambua jitihada za wafugaji na kuboresha namna ya ufagaji wao na mahali pa kuuzia, kwa maana ya soko kwenye kiwanda. Mwekezaji naye sasa naona lengo la nchi la kumlinda mwekezaji wetu kwa kumpa maeneo ya kuhifadhia ng’ombe wake halafu awapeleke viwandani. Tunatarajia kuendelea kutenga maeneo mengi zaidi ya malisho na kutoa fursa nyingi zaidi kwa wafugaji wetu wa ngazi zote; wakubwa, wa kati na wadogo ili waendeshe shughuli zao za mifugo vizuri.
Mheshimiwa Spika, Waziri wetu pamoja na Naibu Waziri wake na Makatibu Wakuu wa Wizara hii wanafanya kazi hiyo kila siku, unawaona hata kwenye vyombo vya habari wakiendelea kuratibu maeneo haya ya malisho kwa lengo la kuboresha ufugaji nchini na pia kwa lengo la kukuza sekta ya nyama, kwa maana ya kuwa na viwanda vinavyotengeneza nyama hizi, zinazo-process nyama hizi kwa ajili ya chakula cha ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge aendelee kuhamasisha na kuhakikishia wapiga kura wake kwamba Serikali yetu imejikita katika kuhifadhi na kulinda wafugaji wetu wote na kuhakikisha kwamba tunawatengenezea fursa za kupata pia na masoko yake. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni miaka minne sasa tangu Serikali yenu imeweka zuio kwa vyama vya siasa kufanya wajibu wake kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi. Na tunachozungumza leo Mheshimiwa Waziri Mkuu ni siku 262 zimebaki kufika tarehe 24, 25 Oktoba siku ambayo nchi yetu itafanya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa busara zako binafsi na ni Serikali ambayo wewe ni kiongozi mwandamizi, mnafikiri ni lini mtaruhusu vyama vya siasa vifanye wajibu wake wa uenezi kujiandaa kwa uchaguzi Mkuu?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili Serikali ina mpango gani wa kuwezesha Taifa kupata Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itahakikisha kwamba uchaguzi huu unakuwa huru wa haki na wa halali? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbowe Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza Mheshimiwa anaomba kujua ni lini vyama vya siasa vitaruhusiwa kufanya shughuli zake za kisiasa. Vyama vya siasa havijazuiwa kufanya shughuli zake, ila tumeweka taratibu muhimu unaowezesha vyama kufanya shughuli zake za kisiasa kama ambavyo tumetoa, kumekuwa na uhuru pia wale wote wanasiasa wote ambao waliomba ridhaa kwenye maeneo yao wakapata ridhaa hiyo kuendelea kufanya shughuli na maeneo yao ambayo wamepata ridhaa. Kama vile Madiwani, Wabunge wanaendelea kufanya shughuli zao za siasa kwenye maeneo yao kama ambavyo wao wanapaswa kufanya shughuli hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amezungumzia lini tunajiandaa kwa ajili ya uchaguzi, ratiba za uchaguzi zitatolewa na ratiba hizi zitaeleza kuanzia lini shughuli za kampeni zitaanza mpaka lini ili vyama viende sasa kama chama kikaeleze sera zake kwenye maeneo yote ili sasa wananchi waweze kupata fursa ya kuendelea kufanya maamuzi ya sera ipi ya chama gani, inafaa kutuletea maendeleo nchini. Kwa hiyo hilo linaendelea na wote mnajua hata kulipokuwa na chaguzi ndogo pale ratiba ilipokuwa inatolewa kila chama kilikuwa kinaendelea kushiriki na huo ndio utaratibu ambao unaifanya hata nchi kuwa imetulia na watu wote kufanya shughuli zao kama kawaida na tutaendelea kufanya hivyo kwa vyama vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu suala la Tume Huru. Jambo hili hata Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu juzi alitoa maelezo hapa, na mimi nataka nirudie tu; kwamba tume hii imeundwa kwa mujibu wa Katiba wa sheria, na kwa mujibu wa Katiba ya nchi kipengele 74 (7), (11), (12) inaeleza kwamba hiki ni chombo huru.
Kimeelezwa pia kwenye Katiba pale kinaundwaje; na chombo hiki hakipaswi kuingiliwa na chombo chochote; iwe Rais wa nchi, iwe chama chochote cha kisiasa au Mamlaka nyingine yoyote ile haipaswai kuiingilia. Kama ni chombo huru kwa mujibu wa Katiba ndiyo Tume huru. Sasa kunaweza kuwa kuna tofauti ya neno huru hili linataka litambulike vipi lakini chombo kipo kinajitegemea kinafanya kazi yake bila kuingiliwa na mtu yoyote, kwa mujibu wa Katiba yetu ya Mwaka 1977. Hayo ndiyo maelezo sahihi na ndiyo ambayo yapo kupitia Katiba na sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri Mkuu TARURA imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya barabara mijini na vijijini. Na kwa kuwa umuhimu wa barabara hizi ndizo zinazochangia kwa kiasi kikubwa uchumi katika usafirishaji. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa bahati mbaya sana TARURA wanakumbwa na bajeti ndogo. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kuiongezea bajeti TARURA ili iweze kutekeleza majukumu yake haya makubwa ambayo imekabidhiwa? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chatanda Mbunge wa Korogwe Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunacho chombo kinachosimamia ujenzi na ukarabati wa barabara vijijini; TARURA kwa sasa; ambacho tumekipa mamlaka ya kufanya kazi karibu kwa pamoja na Mamlaka ya Serikali za Mtaa kwa maana ya halmashauri za wilaya. Sasa kila TARURA iliyoko kwenye halmashauri hiyo jukumu lake ni kufanya mapitio ya barabara zote zilizopo ndani ya wWilaya hiyo kuona mahitaji ya ujenzi wake, ukarabati wake na matengenezo ya kila siku pale ambako panahitaji ukarabati huo na kutenga fedha na kuomba fedha kulingana na mahitaji yake. Kwa hiyo kila TARURA katika kila halmashauri inayo bajeti yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana pia TARURA Wilaya ya Korogwe haitoshelezi mahitaji ya ukarabati wa barabara zake. Si rahisi kupata bajeti yote kwa asilimia 100 kulingana na mahitaji hayo lakini bado kipindi tulichonacho sasa mwezi wa pili tukiwa tunaelekea kwenye Bunge la Bajeti kuanzia mwezi wa nne basi TARURA ile kwenye halmashauri husika ioneshe mahitaji ya fedha kulingana na mahitaji ya barabara zao ili sasa tuanze kuingiza kwenye mpango wa fedha kwa ajili ya matumizi ya mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme Serikali iko tayari kupokea maombi ya TARURA zote nchini za mahitaji ya fedha halafu tutazigawa sote kwa pamoja; na kupitia Kamati yetu ya Miundombinu inaweza kusimamia pia TARURA kupata fedha ya kutosha ili iweze kujenga barabara zake kwenye maeneo yake kama ambavyo halmashauri inahitaji kuboresha barabara zake. Ahsante. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kunipa nafasi nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu swali. Ni sera na ni azma ya Serikali yetu kuwapatia wananchi maji salama lakini kwa bei nafuu pia kwa sababu maji ni huduma si biashara. Niipongeze Serikali yetu kwa kufikia azma hiyo hiyo mijini kwa zaidi ya asilimia 80 na vijijini kwa asilimia 70.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana EWURA walipandisha bili za maji kote nchini, jambo ambali limesababisha wananchi wengi kushindwa kulipa bili hizo. Serikali pamoja na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu mlituahidi hapa Bungeni kwamba EWURA wacheki upya mchakato wao ili waona kama hizi bili zinaweza zikashuka ili wananchi waweze kulipia. Naomba nifahamu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni lini mchakato wa EWURA utakamilika ili hizi bili zishuke kwa sababu wananchi wengi wameshindwa kulipia; mfano wananchi wa Babati Mjini? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gekul Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimewahi kupokea malalamiko haya kutoka hapa Bungeni, kutoka kwenye mikutano ninayoifanya kwenye maeneo mbalimbali nchini juu ya upandaji wa bei za maji holela na kukwaza wananchi kumudu kupata huduma hiyo ya maji. Kwanza nataka niwahakikishie Watanzania kwamba Serikali yetu imejipanga kutoa huduma za maji mpka kuingia vijijini kama ambavyo tumeeleza na kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza. Kwamba tunahitaji sasa angalau kila kijiji kiwe na angalau kiwekwe kisima kama ni kifupi tupate maji ili wananchi wawe na uhakika wapi watapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo inaendelea vizuri na Wizara yetu ya maji inasimamia kuhakikisha kwamba huduma za maji zinapatikana kwa ujenzi wa miradi ya visima vifupi, vya kati lakini pia hata miradi mikubwa ambayo wakati wote tumekuwa tukiieleza. Maji haya Serikali hailengi kufanya biashara kwa wananchi wala hatuhitaji faida kutoka kwa wananchi, muhimu wa utoaji huduma ya maji kwa wananchi ni kufikisha maji kwa wananchi wayapate maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeunda Kamati zinazosimamia maji kwenye maeneo husika; na pia tumeunda mamlaka ya jumla ambayo inasimamia utoaji wa huduma ya maji kwenye ngazi ya Wilaya RUWASA; kwenye ngazi ya Kitaifa tuna zile mamlaka ambazo zinachukua unaweza ukawa ni Mikoa miwili au mitatu au Kanda kusimamia utoaji huduma lakini pia na ujenzi wa miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hizi tumezitaka zifanye mapitio ya huduma ndogondogo zinazohitaji kwa ajili ya ukarabati wa kuendesha mradi huo kwenye maeneo yao; kama vile kununua tap na kufanya mabadiliko ya bomba lililotoboka. Hiyo tumeiachia zile Kamati ziratibu na sasa Kamati hizi zinahitaji angalau wananchi wachangia huduma ya maji kwenye eneo lao. Huduma hii hatutarajii kusikia mwananchi analipa gharama kubwa inayomshinda na lile ndilo tuliloagiza kwa Wizara. Tumeweka utaratibu EWURA wafanye mapitio ya maeneo haya kuona kwamba gharama haziwi zaidi ya mapato ya mwananchi kwenye eneo lake ili kuongoa usumbufu au dhana ya kwamba tunatoa huduma ya maji kama vile biashara, hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeweka utaratibu EWURA wafanye mapitio ya maeneo haya kuona kwamba, gharama haziwi zaidi ya mapato ya mwananchi kwenye eneo lake, ili kuondoa usumbufu au dhana ya kwamba, tunatoa huduma ya maji kama vile biashara, hapana. Agizo limeshatolewa na Wizara ya Maji imeshatekeleza. kwa hiyo nitamuagiza Waziri wa Maji atupe taarifa ya hatua waliyoifikia ili sasa tuone kuwa huduma hii inatolewa huko kwa namna ambazo mwananchi anaweza kupata maji akaendelea kuhudumiwa. Vilevile kama kijiji, kata, waendelee kufanya ukarabati mdogomdogo ili kufanya mradi huo kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wake. Asante sana. (Makofi)
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwea kunipa nafasi ya kuweza kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali; na nianze kwa kutoa pole kwa waathirika wote wa mafuriko.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba; Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumeshuhudia mvua zinazonyesha na zinazoendelea kunyesha. Tumeshuhudia maafa mbalimbali, vifo, watu kukosa maeneo ya kuishi, kupoteza mali zao, kuharibika kwa miundombinu, lakini pia watu wale hawana vyakula. Je, Serikali sasa ina mkakati gani wa kuweza kuwasaidia watu hao ambao wameathirika na mafuriko hayo na pia, kuboresha miundombinu nchini kwetu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu Vulu, Mbunge Mkoa wa Pwani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nami niungane na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa pole kwa waathirika wote a mafuriko nchini kwa maeneo yote ambayo yamekumbwa na tatizo hili la mafuriko. Pia Mheshimiwa Mbunge na yeye ametioa pole ni jambo zuri, jambo jema kwa sababu, wako Watanzania wamekumbwa na hali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa bahati nzuri jana nilikuwa Mkoani Lindi, Wilaya ya Kilwa ambako kulikuwa na mafuriko pia. Nimetembelea kwenye maeneo yote nimeona hali ilivyo, ingawa angalao sasa maji yamepungua kwenye maeneo yale yamebaki tu yanayotiririka kwenye mito.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli uharibifu mkubwa umejitokeza, kwanza wenzetu wametangulia mbele za haki na kwa kweli tuungane na Watanzania wote, Mungu aweke roho zao mahali pema peponi, amina. Mbili, tumeona watu wamepoteza nyumba, vyakula na miundombinu mbalimbali imeharibika ikiwemo na barabara na njia nyingi zimejifunga. Nataka niwaambie Watanzania, kwamba mwaka huu mvua ni nyingi sana, na Taasisi yetu ya Hali ya Hewa imeendelea kutuhabarisha kwamba, mvua ndio zinaanza. Sasa kama ndio zinaanza kwa hali hii tutarajie tutakuwa na matukio mengi makubwa zaidi ya haya ambayo tumeyapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapopata taarifa za wingi wa kiasi cha mvua mwaka huu sisi wenyewe tunatakiwa tuchukue tahadhari. Wale wote waliokaa kwenye maeneo hatarishi, na kwa kiwango hiki cha mvua na hali ambayo tumeiona na wanasema mvua bado inakuja; uko umuhimu na kweli nitoe wito; watu waondoke kwenye maeneo yale ya mabondeni. Kule iwe ni kazi za kilimo na kulishia mifugo, tusifanye maeneo hayo kuwa ni maeneo ya makazi kwa sababu kuna hatari tena ya kupoteza maisha ya wenzetu, nyumba, vyakula na athari nyingine inaweza kujitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hawa ambao tayari wamekumbwa kwenye maeneo yao kama vile huko Lindi, Kilwa, Liwale, Lindi Vijijini; pia Pawaga kule Iringa, Chikuyu Wilayani Manyoni, Magu Mwanza, Sengerema pamoja na Buchosa. Hayo maeneo yote ninayoyataja yana matatizo ya mafuriko. Kwa hiyo maeneo ni mengi na bado kuna mikoa sita ambayo mvua zitaanza kunyesha kwa wingi. Kamati za Maafa za Kata, Wilaya na Mikoa zipo zinafanya kazi yake na zinaendelea kutoa huduma kwa uwezo wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale ambapo Kamati ya Maafa Mkoa inapokuwa na jambo kubwa sana wanatoa taarifa kwa Kamati ya Maafa ya Taifa ambayo iko Ofisi ya Waziri Mkuu nayo pia itasadia katika kuratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na haya jambo hili ni la muda mfupi; muhimu zaidi tuanze kujiepusha kukaa kwenye maeneo hayo hatarishi ili kupunguza mzigo mkubwa ambao tutaupata. Haya yaliyotokea haya kamati za maafa zinafanya kazi nzuri, wakuu wa wilaya, viongozi wa kamati za wilaya, wakuu wa mikoa, kamati za mikoa, wameendelea kushirikiana na wale wote waathirika kuona mahitaji yao katika kipindi hiki kifupi na kazi inaendelea vizuri na taarifa tunaendelea kuzipokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ambao pia mnatoka kwenye maeneo haya tunawapa pole na wananchi wetu tunawapa pole, lakini tuwahakikishie kwamba, kamati zetu za maafa zilizoko kwenye maeneo yale zinaendelea kushirikiana na wananchi huku tukiendelea kutoa wito wananchi wasirudi kwenye maeneo walikotoka ili kupunguza athari hii. Asante sana. (Makofi)
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Waziri Mkuu swali:-
Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na mpango mzuri wa Serikali wa kuhakikisha kwamba, kila kijiji kinapelekewa umeme katika nchi yetu. na kwa kuwa, Serikali imejitahidi sana kupeleka nguzo nyingi na nyaya katika maeneo mengi ya nchi yetu, lakini bado nguzo hizo zimeendelea kulala chini na nyingine hazijafungiwa umeme. Na kwa kuwa mpango wa REA Awamu hii ya Tatu ni kwamba, lazima uishe mwezi wa sita, lakini katika mwenendo wa utekelezaji wa mradi wenyewe inaonekana mpaka mwezi wa sita kuna miradi ambayo itakuwa haijakamilika.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba, mradi huu wa utekelezaji wa REA katika vijiji vyetu unakamilika mwezi wa sita kama ambavyo Serikali ilipanga?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo miradi hii ya REA ambayo inapeleka umeme vijijini ambayo kwa kweli kazi zinaendelea vizuri. Tumeenda maeneo mengi; na sasa tumefikia zaidi ya asilimia 60 na kitu katika kuweka umeme kwenye vijiji vyetu vingi ambavyo vimekusudiwa. Mkakati huu unalenga kila kijiji huko kwenye maeneo yetu tunakotoka. Wizara ya Nishati imejipanga vizuri, imeshasambaza wakandarasi kila halmashauri, wakandarasi ambao wamesaini mkataba kukamilisha kazi hiyo kwa muda na kwa kuweka umeme katika kila kijiji kwa awamu hii ya tatu, awamu ya kwanza na kwenye awamu ya tatu kuna awamu ya kwanza na ya pili na zote hizi zitatekelezwa, ili kuhakikisha kwamba, umeme unapelekwa kwenye ngazi ya vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo ambayo nimeeleza kwamba inaendelea na ni nzuri inaanza sasa kupeleka umeme kwenye vijiji vyetu vingi; na vijiji vyote vilivyobaki viendelee kuwa na uhakika kwamba, umeme utafikishwa. Sasa suala la kufika mwezi wa Juni inategemea hapa katikati kama kunaweza kuwa na jambo lolote lile linaloweza kumfanya mkandarasi akashindwa kukamilisha kazi yake vizuri. Sisi ndani ya Serikali tunahakikisha mtiririko wa fedha za malipo kwa mkandarasi unakwenda, tunahakikisha kwamba, vifaa anavipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa bahati nzuri sasa vifaa vya kutengenezea kazi hizo vinapatikana hapahapa nchini. Nguzo zinapatikana nchini, transformer zinapatikana hapa nchini, nyaya zinapatikana hapa nchini. Kwa hiyo tuna matumaini kwamba, tunaweza kukamilisha kazi hiyo kwa kipindi ambacho tunatarajia, na kwa kuwa, wakandarasi wako kazini na tumetoa pia mamlaka kwa TANESCO zetu maana TANESCO na REA ni taasisi mbili zilizo kwenye Wizara moja, ili TANESCO sasa wasimamie kazi za REA kuwa zinakamilika kwenye maeneo ambayo wanayasimamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumini yangu kwamba kazi za uwekaji umeme kwenye vijiji itakamilika. Mheshimiwa Waziri wa Nishati ameelza hapa, kwamba sasa tunakwenda mbali zaidi mpaka kwenye vitongoji vikubwa navyo tunapeleka umeme. Kwa hiyo wananchi wawe na matumaini na wajiandae sasa kutumia fursa ya kuwa na umeme kwenye maeneo yao kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali zinazohitaji umeme, asante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali ya Awamu ya Tano imehamasisha sana shughuli za kilimo na wananchi wamehamasika sana, lakini hivi karibuni limetokea tatizo kubwa sana la ufungaji wa mazao kwa mtindo wa lumbesa lakini pia kuwepo na vifungashio ambavyo havina viwango stahiki. Jambo la kusikitisha sana ni kwamba Mamlaka za Serikali, hasa Wakala wa Vipimo na Mizani, pia Serikali katika ngazi za Halmashauri, Wilaya na Mikoa zimeshindwa kabisa kudhibiti tatizo hili la ufungaji wa mazao kwa mtindo wa lumbesa. Je, Serikali ipo tayari kuanzisha operesheni maalum nchi nzima kudhibiti tatizo hili ambalo kwa kweli linawanyong’onyeza wakulima na kuwaletea lindi la umaskini? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo kule Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeendelea kusisitiza wakulima wetu nchini wanapolima mazao yao waweze kunufaika kutokana na masoko yaliyo sahihi. Tunaanza kuona baadhi ya wanunuzi kutofuata sheria, kanuni na taratibu za manunuzi ya mazao hayo pindi wanapokwenda kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, nimefanya ziara Wilaya ya Karatu eneo maarufu linalozalisha mazao la Lake Eyasi, eneo la Eyasi kule chini. Moja kati ya malalamiko ambayo wakulima waliyatoa ni kama ambavyo Mheshimiwa Shangazi ameeleza, lakini Serikali imeweka utaratibu wa mazao yote yanayolimwa na kuingia kwenye masoko, lazima masoko hayo yatumie vipimo halisi ili liweze kulipa bei stahiki na mkulima aweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaposema vipimo stahiki maana yake kuna vipimo ambavyo tunavitumia, inaweza kuwa ni kipimo cha ndoo ambazo tunajua kuna ndoo za lita tano, kumi, ishirini, na ni rahisi pia kukadiria na bei ambayo inawekwa na wakulima inakuwa ndiyo bei sahihi. Pia kuna vifungashio kama vile magunia ya kilo hamsini, kilo mia, nayo pia ni sehemu ya vipimo halisi lakini muhimu zaidi ni kutumia mizani ambayo haina utata.
Mheshimiwa Spika, sasa imetokea wanunuzi kuwalazimisha wakulima baada ya kile kipimo halisi kuongeza tena nundu inayojulikana kwa jina la lumbesa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, hii haikubaliki. Tumetoa maelekezo sahihi kwa Wakuu wa Mikoa wote, Wakuu wa Wilaya wote, Wakurugenzi na Maafisa Kilimo na Maafisa Ushirika wanaosimamia masoko kwenye ngazi hizo za wakulima wawe wasimamizi wa biashara inayofanywa na wanunuzi kwa mkulima pindi anapouza mazao yake ili kujiridhisha kwamba vipimo vyote vinatumika na siyo kuongeza nundu zaidi ya kipimo ambacho kinatakiwa, kwa sababu kufanya hivyo tunamnyonya mkulima na mkulima anapata hasara kwenye mazao hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utayari wa Serikali upo na tumeshatoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya. Kwa hiyo nirudie tena kutoa wito kwa Maafisa Kilimo, Ushirika, Wakuu Wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa kwenye maeneo yao wasimamie biashara hii na kuendesha operesheni kwenye maeneo yote ya masoko ili kujiridhisha kwamba mazao yetu yananunuliwa kwa vipimo kama ambavyo vimekubalika. Huo ndiyo msisitizo wa Serikali na tutaendelea kusisitiza wakati wote. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika miezi ya karibuni katika Mikoa mbalimbali ya nchi yetu kumekuwa na changamoto kubwa ya kupanda kwa gharama za maji bila kuzingatia uasilia, kuletewa bili zisizo sahihi, kukatiwa maji bila utaratibu na kukosa maji kwa muda mrefu kisha unaletewa bili kubwa. Kero hiyo imejitokeza katika Mikoa mbalimbali katika nchi yetu ikiwemo Mikoa ya Dar es Salaam, Manyara, Dodoma, Tanga, Mwanza na Mikoa mingine mingi na hasa katika maeneo ya Mijini.
Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi wake waliokumbwa na kero hiyo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, alichosema Mheshimiwa Mbunge, yako maeneo yanajitokeza kwamba mamlaka tulizozipa mamlaka hiyo ya kusimamia maji kwenye maeneo yao, tunazo mamlaka ambazo tunazianzisha sasa za RUWA za vijijini na kwenye ngazi za Wilaya, lakini zipo mamlaka ambazo zimechukua maeneo makubwa kwenye ngazi za Mikoa, pia tuna Kamati za Maji ambazo zinasimamia miradi hii kwenye maeneo ya vijiji na maeneo mengine yote.
Mheshimiwa Spika, kumejitokeza wimbi la mabadiliko ya bei. Ni kweli upo utaratibu ndani ya Serikali kwamba mamlaka hizo zinapoona zinahitaji kuboresha huduma zinaweza kufanya mapitio ya bei zao. Lakini kinachotokea sasa ni kwamba zipo mamlaka zinapita zaidi ya kiasi.
Mheshimiwa Spika, nimefanya ziara Mkoani Simiyu na hapa karibuni nilikuwa kwenye Wilaya ya Maswa, moja kati ya malalamiko niliyoyapokea kwa wananchi pale ni kupanda kwa bei kutoka shilingi 5,000 wanayoilipa kwa mwezi mpaka shilingi 28,000. Sasa bei hizi hazina uhalisia, hakuna sababu ya mamlaka kutoza fedha yote hiyo na kuwafanya wananchi wakose maji.
Mheshimiwa Spika, Serikali ndiyo inatekeleza hii miradi na inatoa fedha kwa lengo la kuwapa huduma wananchi ili wapate huduma ya maji. Mamlaka tumewapa jukumu la kusimamia mradi huo na kuhakikisha kwamba angalau wanaweza kufanya marekebisho, matengenezo pale ambapo kunatokea uharibifu. Kwa hiyo, gharama haziwezi kuwa kubwa kiasi hicho na wala wao hawapaswi kutoza wananchi ili kurudisha gharama za mradi kwa sababu Serikali haijadai gharama ya kuendesha mradi huo kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri jana nilikuwa na Waziri wa Maji nikimwambia hili la kwamba lazima afuatilie Mamlaka ya EWURA ambayo ina mamlaka ya kukaa na hizo mamlaka zetu za maji kufanya mapitio ya bei. Bei zinazotakiwa kuwekwa ni zile ambazo mwananchi wa kule kijijini anaweza kuzimudu lakini siyo kwa kupandisha bei kutoka shilingi 5,000 mpaka shilingi 28,000, jambo ambalo halina uhalisia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania kwa ujumla, tutaendelea kusimamia Mamlaka zote za Maji, lakini Serikali itaendelea kutoa huduma za maji, nataka tujiridhishe kila Mtanzania anapata maji kwenye maeneo yake kwa usimamizi wa mamlaka hizi, lakini hatutaruhusu na hatutakubali kuona Mtanzania anatozwa gharama kubwa za maji kiasi hicho. Huku tukiwa tunatoa wito kwamba lazima tuchangie maji ili tuweze kuendesha miradi hii pale ambapo tunatakiwa kununua diesel, tunatakiwa tununue tepu ya kufungulia maji au bomba linapopasuka, lazima mamlaka zile ziweze kufanya ukarabati huo, lakini siyo kwa kutoza fedha kiasi hicho.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, masharti ambayo yapo mnapotaka kuongeza bei ni kwamba mamlaka hizo zinapodhamiria jambo hilo ni lazima kwanza zitoe taarifa EWURA, mbili kwenye vikao hivyo lazima Kamati za Maji zihusike, Kamati ambazo zinaundwa na wananchi wenyewe, tatu ni lazima wahusishe wadau, wadau ni wale watumia maji. Kwa hiyo, wote wakikubaliana sasa kwa viwango ambavyo wananchi wake wanaweza kuvimudu ndipo mnaweza kupandisha. lakini msipandishe wenyewe na mkawaumiza wananchi na miradi yenyewe imetekelezwa na Serikali, Serikali inayotaka wananchi wapate maji halafu mnataka kuwakwaza wananchi wasipate maji waanze kuilalamikia Serikali yao. Hatutakubaliana na hili na kwa hiyo mamlaka ziwe makini, Wizara ya Maji iendelee na utaratibu na maagizo ambayo nimewapa jana.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania, licha ya jitihada hizo kuna baadhi ya Maafisa wanakwamisha wawekezaji. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa Watendaji wa aina hii?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
SPIKA: Unaweza ukajaribu kutoa hata kamfano kidogo Mheshimiwa Jacqueline, maana yupo Waziri wa Uwekezaji naye ajifunze ni ukwamishaji gani unaotokea?
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wawekezaji wanapokuja nchini unakuta labda kwa mfano anakwenda katika Mkoa wa Mwanza anataka aweke kiwanda cha usindikaji wa samaki lakini unakuta kwenye, labda Sekta ya Ardhi au kwenye Halmashauri zetu katika sekta mbalimbali wanakuwa wanaweka vikwazo mbalimbali labda kutengeneza mazingira labda ya rushwa na mambo kadha wa kadha. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Msongozi, Mbunge kutoka Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu kwa sasa tumeweka utaratibu mzuri sana wa uwekezaji na tunaendelea kuhamasisha uwekezaji nchini wa ndani na nje ya nchi. Natambua kwamba tulipoanza kutoa wito wa uwekezaji kwa yeyote mwenye nia ya kuwekeza hapa nchini tulianza katika mapito mbalimbali, watendaji, wengine walikuwa hawajajua philosophy ya Serikali, lakini pia maeneo muhimu ya uwekezaji bado ilikuwa hayajachanganuliwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imeweka utaratibu mzuri sana, kwanza kwa kuunda Wizara ya Uwekezaji ambayo sasa itashikilia Sera ya Uwekezaji kwa ujumla, pia Serikali ina chombo kinachoshughulikia uwekezaji, Taasisi ya Uwekezaji Tanzania (TIC) ambayo sasa tumerahisisha mambo yote ya uwekezaji yako hapo ndani, anayetaka ardhi anapata huko ndani, anayetaka huduma za TRA anakuta huko ndani, usajili wa kampuni anakuta huko. Sekta zote zinazogusa uwekezaji sasa zinapatikana pale TIC kwa maana tumeanzisha One Stop Center ambayo kila mwekezaji anapokuja shughuli zote zinaishia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tumeleta mamlaka kwenye ngazi za Mikoa na Halmashauri kupokea Wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye ngazi hizo na Mikoa sasa itawezesha kuhakikisha kwamba mwekezaji huyo anapata huduma ya uwekezaji na atapata maelekezo sahihi. Yako mambo yanawezeshwa hukohuko kwenye ngazi ya Halmashauri au ngazi ya Mkoa lakini mengine lazima yaende TIC na mengine lazima yaende Wizarani kukutana na Waziri kwa ajili ya Sera ya ujumla.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa utaratibu huu kama bado kuna mtendaji anakwamisha uwekezaji huyu atakuwa hana nia njema na nchi yetu. Na popote ambako wananchi, Waheshimiwa Wabunge unaona kuna Mtendaji wa Serikali tumempa jukumu la kusimamia shughuli za Serikali ikiwemo na uwekezaji, uwekezajia ambao sasa kila siku tunatoa wito watu wawekeze, tena wawekezaji wa ndani na wa nje ya nchi na anakwamisha process hiyo hatua kali dhidi yake zitachukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, bado Serikali inatoa wito wa uwekezaji. Tumerahisisha uwekezaji kwa sababu pia tumekuwa na vikao na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, wawekezaji. Mheshimiwa Rais amekutana na wafanyabiashara wengi, wawekezaji wengi na sisi watendaji huku chini tumekutana na makundi hayo mbalimbali tukapata kero zinazowagusa hao wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeandaa mfumo tumetengeneza ile blueprint kile kitabu ambacho kinaonesha mabadiliko ya mifumo mbalimbali ya uwekezaji ambayo yanarahisisha uwekezaji hapa nchini kuwa uwekezaji rahisi zaidi. Ndiyo kwa sababu sasa unaona idadi ya wawekezaji nchini inaongezeka na tunaendelea kupokea kero za wawekezaji ili tuendelee kuboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa wito kwa wawekezaji wote wasihofu kuja nchini tuna ardhi, tunazo maliasili lakini tuna rasilimali za kuendeshea kilimo uwekezaji huo kama ni viwanda au tukitaka kuchakata madini, tunayo. Muhimu zaidi ni kufuata sheria, kanuni na utaratibu wa ndani ya nchi ili uweze kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba tumesikia, tumepata ujumbe wako ndani ya Serikali tutaendelea kusimamia vizuri kwa watendaji ambao hawaelewi bado philosophy ya Serikali na malengo ya nchi kwa ajili ya kuleta uwekezaji ulio sahihi na bora. Mazingira ya uwekezaji kwa sasa tumerahisisha na tutaendelea kurahisisha zaidi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu najua unajua kwamba kwenye msimu huu unaoendelea wa pamba, zao hili limekumbwa na kadhia mbalimbali. Ningependa kujua changamoto hizi, ya kwanza, tani elfu 35 zilizochukuliwa na wanunuzi na wakulimwa wakakopwa, tani 52 elfu ambazo ziko maghalani kupitia AMCOS, ambazo pia wakulima wamekopwa hawajalipwa, tani elfu 70 zinazokisiwa, ambazo ziko majumbani bado hazijapelekwa kwenye soko.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu tungependa kujua, nini kauli ya Serikali au tamko la Serikali kuhusu wakulima wa zao la pamba ambao pamba yao iko majumbani lakini wamekopwa mpaka sasa hivi hawajalipwa? Nini kauli ya Serikali? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika naomba kujibu swali la Mheshimiwa Senator Ndassa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la pamba Serikali tumelifanyia kazi kweli kweli na kwa bahati sasa pamba inalimwa kwenye mikoa zaidi ya 11 nchini na uzalishaji tunafurahi sana kwamba umeongezeka kutoka tani 220,000 mwaka uliopita na msimu huu tumekwenda mpaka tani 300,000, tunategemea kupata tani zaidi ya 350,000.
Mheshimiwa Spika, lakini Serikali imeendelea kusikia malalamiko ya baadhi ya wakulima kwamba pamba hainunuliwi ni kweli, na sisi tumepita, mimi mwenyewe nimepita, Mawaziri wa Kilimo, Waziri mwenyewe, Manaibu wake wamepita maeneo yote kuona hali hiyo lakini na kuzungumza pia na wananchi kwenye maeneo hayo. Tumekuwa na vikao vya wadau, wadau wanaohusika ni wakulima, wanunuzi, wafanyabiashara na kwa maana ya wanunuzi, watu wa mabenki pamoja na viongozi wa Serikali wa maeneo hayo ili kuona njia sahihi ya kuondoa pamba yote mikononi mwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, nafurahi kusema kwamba, utaratibu ambao tumeuweka wiki tatu zilizopita umeanza kuleta matunda kwamba sasa ununuzi wa pamba tumeshafikia asilimia kama 80 hivi, kwa sababu tumeshanunua tani, mpaka juzi, tani ambazo tumeshanunua ni tani 235,000. Kwa hiyo, pamba ambayo bado iko ni kidogo na kwa hiyo tunaamini kwamba pamba hii yote tutaichukua.
Mheshimiwa Spika, utaratibu tuliouweka kuwahakikishia wakulima kwamba pamba hii tutaichukua, ni kwamba baada ya kuchanganua pamba iliyobaki kwa wakulima tumeigawa kwa wanunuzi maalum ambao wana uhakika wa kuinunua pamba hiyo kwa kilograms zao na tumeshafika mpaka kilograms zote mpaka laki tatu, kila mmoja ana mgao huo na Benki Kuu kupitia mabenki, wanunuzi wale wanapewa fedha za kwenda kuchukua pamba yote mikononi mwa wakulima na zoezi la kuwapa fedha hizo linaendelea na wanunuzi wanakwenda sasa kuchukua pamba.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna uhakika katika kipindi kifupi kijacho pamba yote itatoka mikononi mwa wakulima na itabaki mikononi mwa wanunuzi ili utaratibu wa kwenda kufanya mauzo uendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana juzi tulikuwa na kikao cha pamoja kati ya Benki Kuu, Mabenki na Wawakilishi wa wanunuzi na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao pia walipata fursa ya kuingia pale kwenda kusikia mpango mkakati wa kumaliza pamba yote kule kwa wananchi. Kwa hiyo, niendelee kuwahakikishia wanunuzi wa pamba kupitia Waheshimiwa Wabunge ambao mnatoka kwenye mikoa ile yote kwamba, pamba yote itachukuliwa kwa sababu mpango wa fedha kuwapatia wanunuzi, wanunuzi wakachukue pamba unaendelea na pia tumewashirikisha Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kwa kuwaambia wilaya yako inanunuliwa na fulani na mnunuzi huyo atachukua kilo kadhaa kwenye eneo hilo na tumeshampa fedha, kwa hiyo, kazi pale ni kushirikiana naye kwenda kuichukua pamba yote ili iweze kuondoka mikononi mwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie kupitia Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali Mheshimiwa Ndassa ambaye pia ni mwakilishi wa wakulima wa pamba kule Kwimba, kwamba pamba yote ambayo tumeizalisha hii, tutaitoa sasa wakati huu tunafikiria kwamba hali ya hewa inaweza kubadilika wakati wowote ili isiweze kunyeshewa na mvua, tuwahakikishie kwamba pamba yote imetoka mikononi mwa wakulima. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimia Spika, nakushukuru. Mwaka huu maeneo mengi ya nchi yetu yamekabiliwa na upungufu wa mvua ambayo imepelekea maeneo mengi kukosa chakula cha uhakika na hivyo kusababisha bei ya chakula kupanda kwa kiasi kikubwa sana. Hapa tunapozungumza maeneo mengi mahindi yanauzwa kuanzia shilingi elfu 80 mpaka laki moja.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba chakula cha bei nafuu kutoka NFRA kinapelekwa katika maeneo haya yaliyokumbwa na ukame ili wananchi waweze kumudu chakula? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kalanga, Mbunge wa Monduli kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa chakula nchini kwa maana usalama wa chakula nchini kufuatia msimu uliopita wa uvunaji wa mazoa ya chakula uko vizuri, lakini tunatambua kwamba yako maeneo kadhaa hali ya hewa haikuwa nzuri na uzalishaji wake haukuwa mzuri sana. Kwa hiyo, maeneo hayo yanaweza kuathirika kwa kuwa na bei zisizotabirika wakati wote na kusababisha wananchi kutojua hasa bei ya mahindi, chakula hicho, lakini pia ni wapi tunaweza kupata chakula hicho.
Mheshimiwa Spika, lakini nataka niwahakikishie kwamba uzalishaji wa chakula ambao umefanywa, ambao Wizara ya Kilimo imeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba maeneo yote yanapata chakula, NFRA imepewa jukumu la kuhakikisha kwamba usalama wa chakula nchini unaimarishwa kwa kuwa na chakula cha akiba kwenye maghala ili kiweze kutolewa na kuuzwa kwenye maeneo ambayo hayana chakula kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pili, kwa kuwa chakula kiko nchini na tunao wafanyabiashara ndani ya nchi, hiyo ni fusa muhimu kwao ya kupata chakula kukipeleka maeneo ambayo hayana chakula. Mheshimiwa Kalanga amezungumzia bei nafuu, bei nafuu sasa ni tumeruhusi wanunuzi mbalimbali kuingia kununua. Wanapokuwa wanunuzi wengi kunakuwa na ushindani wa ununuzi, ingawa pia bei inakuwa iko juu lakini sisi kwa sababu tuna NFRA ambayo inashughulikia usalama wa chakula, basi chakula huwa kinapatikana. Kwa hiyo, muhimu zaidi tupate taarifa, wapi kuna upungufu wa chakula, halafu tuone, tuweze kupeleka chakula ambacho tunaweza kununua kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Spika, lakini muhimu zaidi ni ule msisitizo wa kila mmoja afanye kazi na tumeanza kuona matunda kwamba chakula sasa uzalishaji ni mkubwa mpaka tunakua na ziada hapa nchini na chakula kingine tunauza pia hata nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, lakini mbili, ni hilo ambalo tumelisema la kwamba wanunuzi sasa wapite maeneo hayo waweze kuchukua mahindi kutoka eneo moja kupeleka eneo la pili ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia Mheshimiwa Kalanga NFRA inaweza ikipata taarifa na Wizara ya Kilimo inasikia hapa ni rahisi sasa kuweza kushughulikia maeneo hayo yanayokosa chakula. Kwa hiyo, kwa taarifa ambayo tumeipata sasa naamini tutaishughulikia ili kuona namna nzuri ya kufikisha chakula ambacho tunaweza kukinunua kwa bei nafuu. Ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, asante sana. Nashukuru sana kupata fursa hii ya kipekee na ya heshima kubwa sana kwangu na kwa Serikali yangu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, utendaji na utekelezaji wa Ilani ya chetu cha CCM kwa kiasi kikubwa umekuwa na mafanikio. Mheshimiwa Waziri Mkuu utekelezaji wa ilani katika sekta ya kilimo, nishati, elimu, afya, madini, n.k. kumekuwa na hatua ya kuridhisha sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa karibu kipindi chetu kinakwisha tunakaribia uchaguzi Mkuu wa 2020 naomba kuuliza Serikali, lakini kabla sijauliza niseme kwamba, mafanikio haya tuliyoyafikia leo yamefikiwa kupitia na juhudi kubwa za Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na timu yake akiwemo Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia, Waziri Mkuu wewe mwenyewe Majaliwa na watendaji wote wa Serikali ambao wamefanya kazi nzuri kufikia maeneo hayo niliyoyataja hapo juu. Sasa hivi Serikali itakamilisha lini utaratibu wa kuwawezesha Watanzania wanaoishi nchi za nje kuweza kupata nafasi yao ya kidemokrasia kupiga kura?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa anataka kujua Serikali inaandaa utaratibu upi wa kuwezesha Watanzania walioko nje ya nchi kuja kupiga kura nchini wakati wa uchaguzi mkuu na chaguzi nyingine:-
Mheshimiwa Spika, jambo hili ni la kisera na Serikali imeendelea kuona utaratibu huo kama unaweza kufaa kwa sababu, lazima kwanza tupate kujua nani wako nje ya nchi, idadi yao, wanafanya shughuli gani na kama je, bado ni Watanzania au waliomba uraia nchi za nje. Na pindi sera hiyo itakapokamilika pale ambapo itaonekana inafaa tutakuja kulijulisha wote, Bunge na Tanzania nzima. Asante sana.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni wajibu wa Serikali kuyahudumia majeshi yetu kwa kuyapatia uniform ambazo ni viatu, soksi, suruali au sketi, shati, mkanda wa suruali, mkanda wa filimbi, nembo ya cheo, lakini na kofia. Imekuwa ni muda mrefu sasa majeshi haya hayapatiwi hizi uniform badala yake wanajinunulia wao wenyewe.
Mheshimiwa Spika, mathalani Jeshi la Magereza tangu 2012 hawajawahi kupatiwa uniform, vivyohivyo kwa Jeshi la Polisi na hizi uniform wanajinunulia kwa bei ghali sana. Mathalani nguo ambazo za jungle green wananunua kwa 70,000/=, kofia 15,000/=, buti zile 70,000/= na hawa askari wetu wanafanya kazi kwa mazingira magumu sana.
Mheshimiwa Spika, ningetaka kujua sasa ukizingatia Askari Magereza kwa mfano mwenye degree analipwa sawa na Askari Magereza mwenye elimu ya kidato cha nne, shilingi 400,000 aweze kununua, ajigharamie nyumba na mambo mengine.
Ni nini sasa Kauli yako Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhakikisha kwamba, askari hawa wanapewa uniform zao, maana ni stahiki ambayo wanatakiwa kupewa, sanjari na kurudishiwa gharama zote ambazo wamekuwa wakijinunulia hizi uniform kwa kipindi chote ambacho Serikali ilishindwa kuwapa hizi uniform?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kimsingi Serikali inao wajibu wa kutoa vifaa mbalimbali ikiwemo sare kwa majeshi yetu, ili waweze kufanya kazi yao kwa urahisi zaidi. Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo inasimamia Jeshi la Polisi, Magereza pamoja na Uhamiaji pamoja na Zimamoto ni Wizara ambayo inaendelea kuratibu namna nzuri ya kupata sare na vifaa mbalimbali, ili kuwawezesha watumishi wetu askari kwenye majeshi hayo waweze kufanya kazi yao. Na sera yetu ni kwamba, bado Serikali itaendelea kuwagharamia.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ni shahidi mwaka jana tumekuwa tukijadili upande wa Jeshi la Polisi, Wizara ya Mambo ya Ndani ilipokuwa imeagiza, imetoa zabuni ya kununua sare na tukapata taarifa kwamba, kuna majora yako pale ambayo yameandaliwa kwa ajili ya kuwapa askari, hiyo ni dalili kwamba, Wizara ya Mambo ya Ndani bado inatoa huduma hizo kwa askari wake.
Mheshimiwa Spika, sasa kama kuna mahali ambako kwa Wizara upande huo wananunua hizo sare tutaweza kuwasilisna pia na Waziri mwenye dhamana, ili tuone kwa utaratibu huo ukoje na kwa nini sasa askari wanunue na kama ndio sera ya ndani ya Wizara tutaweza kujua na tunaweza tukafanya marekebisho kadiri ya mahitaji yalivyo, ahsante.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kumuuliza Waziri Mkuu, Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi katika Halmashauri zetu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na kukamilisha, lakini miradi hiyo imekuwa haitumiki kama ilivyokusudiwa kutokana na usanifu mbovu wa miradi na kutokamilika kwa miradi hiyo.
Je, Serikali ipo tayari kuchunguza na kuchukua hatua kwa wale wote watakaobainika kwamba, walisababishia hasara Serikali na kuwasabishia Wananchi kutopata huduma ambayo walikuwa wamekusudiwa kupewa na Serikali?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba, miradi yetu mingi ya maji ambayo inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali iko mingine haitekelezwi kwa viwango na kwa hiyo, haina thamani ya fedha kama ambavyo tumekusudia iweze kutekelezwa. Lakini pia kama ambavyo Waziri mwenye dhamana alipokuwa ameleta bajeti yake mbele yetu Wabunge alieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote ambayo imetangazwa na haina thamani kama ilivyokusudiwa kwa fedha iliyotolewa. Na moja kati ya hatua ambazo amezifanya, alieleza hapa kwenye hotuba yake na ndio hasa kazi ambayo inafanywa, ameshaunda timu inayopita kukagua miradi yote nchini kwa kujiridhisha miradi hiyo kupitia BOQ zake kuona matengenezo yake na kama inakidhi thamani ya fedha kwa fedha zilizotolewa kwa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, na pale ambapo sasa hakuna thamani ya fedha hizo hatua ambazo Mheshimiwa Mbunge anataka kujua zinachukuliwa. Na ninataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tumewasikia ushauri wenu kwenye sekta ya maji ikiwemo na kuchukua hatua kali kwa watendaji wetu ambao wanasimamia miradi ya maji na maji hayapatikani, lakini mradi wenywe haujatengenezwa kwa viwango kwamba, hatua kali zitachukuliwa. Na Wizara sasa imeanza kupitia, Wizara yenyewe pale Makao Makuu, na inashuka ngazi ya Mikoa mpaka Wilayani ili kujiridhisha kwamba, tunakuwa na watumishi wenye weledi wa kutekeleza miradi hiii na kusimamia thamani ya fedha kwa manufaa ya Watanzania, ili huduma ziweze kutolewa kwa Wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea na kazi hiyo na Wizara inaendelea kukagua miradi pamoja na ile tume, itakapokamilisha kazi itakuwa na majibu. Wale wote watakaothibitika hatua kali dhidi yao itachukuliwa. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu Swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu moja katika mikakati ya Serikali, ili kuinua sekta ya kilimo ni kuhakikisha kwamba, wakulima wadogo walioko vijijini wanapata pembejeo katika ubora na katika viwango vinavyokusudiwa. Na hilo litafanikiwa tu pale ambapo mfumo wa ufikishaji pembejeo kwa Wananchi ni mfumo endelevu ambao utahusisha kuwepo na maduka madogo-madogo vijijini ya pembejeo ambayo yataweza kuuza mbolea, mbegu bora pamoja na viuatilifu.
Mheshimiwa Spika, lakini imebainika kwamba, jitihada za wadau pamoja na Serikali za kuhakikisha kwamba, kunakuwa na maduka madogo-madogo ya pembejeo vijijini zinakwamishwa na gharama kubwa ya kufuzu kuwa na maduka hayo, ikiwemo gharama kubwa kwenye TOSKI zaidi ya laki moja na eneo la TPRA ambalo laki tatu na gharama nyingine ambazo zinamfanya mdau anayetaka kuwekeza kwenye sekta hiyo, lazima atumie zaidi ya 600,000 kabla hajanunua malighafi kwa ajili ya duka lake.
Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba, inapunguza au kuondoa gharama hizo, ili kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuhakikisha mkulima mdogo ananufaika kwa kupata pembejeo bora na salama kwa ajili ya uzalishaji?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhagama, Mbunge wa Madaba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali limekuwa na maelezo mengi, lakini msingi wake anataka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa, kupunguza tozo za maduka yanayouza pembejeo, ili kumuwezesha mkulima kupata pembejeo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali imepokea ushauri na vilevile malalamiko kadhaa kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo hao wanaofungua maduka ya pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli nzima za biashara. Nataka nikuhakikishie kazi kubwa inayofanywa na Serikali sasa ni kufanya mapitio ya tozo zote kuanzia kwa wakulima kwenye mazao yao, kwa wafanyabiashara wenyewe wanapofanya biashara, ili kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini, ikiwemo maduka hayo yanayosambaza pembejeo, ili kufikisha pembejeo kwa urahisi kwa mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wenye dhamana ambao wana tozo mbalimbali kwenye Wizara zao zinazokwamisha kufanya biashara katika mazingira rahisi wameshakutana. Na hata juzi nilikuwa na Mawaziri hao kupata taarifa zao kwa pamoja kuona maeneo yote waliyoyapitia na tozo zote ambazo zinataka kupitiwa upya na kazi hiyo inayoendelea sasa ikishakamilika sasa watakutana pia na Kamati ya Bajeti ya Bunge, watakutana pia na Wizara ya Fedha, ili kuona namna nzuri ya kuondoa tozo hizo, lakini badae itaenda kwenye mamlaka inayotoa ridhaa ya kuondoa kodi ikiwemo na hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jitihada za Serikali katika hiyo zimeshaanza na tutakapofikia hatua nzuri tutakagua pia na maeneo unayotaja ya maduka yanayouza pembejeo, ili kuwawezesha wafanyabiashara wa maduka hayo kupata pembejeo na kuzipeleka mpaka ngazi ya kijiji, ili wakulima waweze kupata pembejeo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mkakati wa Serikali unaendelea na niwape matumaini wafanyabiashara wote nchini kwamba, Serikali imewasikia vilio vyao na sasa tunafanya mapitio ya tozo hizo, tutakapofikia hatua nzuri tutawajulisha na tutawashirikisha katika kujua ni aina gani ya tozo ambayo tunataka tuiondoe na au kuibadilisha kwa namna moja au nyingine, ili muendelee kufanya biashara zenu katika mazingira rahisi.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa usikivu wake ilisikia kilio ambacho Wabunge pamoja na wananchi kuhusiana na migogoro ya ardhi ambayo imehusisha vijiji zaidi ya 360 katika muingiliano wa mipaka kati ya vijiji pamoja hifadhi za taifa au hifadhi za misitu au hifadhi za misitu au mapori tengefu n kupelekea hivyo Mheshimiwa Rais aliunda kamati ya Mawaziri nane wakiongozwa na Mheshimiwa Lukuvi katika kuratibu na kumshauri namna bora ya kutatua changamoto hii ya vijiji hivi zaidi ya 360, vikiwemo Vijiji vya Mataweni na Stalike katika Jimbo la Nsimbo.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua, je, Serikali ipo tayari kukaa kwa pamoja na Wabunge kupitia taarifa hiyo ikiwa ni namna ya kufanya reconciliation ili kusiwe na malalamiko tena ya baadaye kwa sababu hili ni zoezi ambalo litakuwa linatatua kwa muda mrefu. Je, Serikali ipo tayari kukaa na Wabunge kupitia kabla ya kumkabidhi Mheshimiwa Rais ripoti hiyo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbogo, Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kama ripoti ya ukaguzi wa ardhi ya Tume iliyoundwa na Mheshimiwa Rais kama inaweza kuja kushirikisha Wabunge hapa.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumekuwa tukipata taarifa mbalimbali za migogoro ya ardhi kwenye maeneo kadhaa. Wizara ya Ardhi imefanya kazi nzuri ya kupita maeneo yote yenye migogoro ya ardhi na mwisho Mheshimiwa Rais aliunda timu ya Mawaziri wanane kupita maeneo yote yenye migogoro kukagua na kusikiliza maoni ya wananchi kwenye maeneo hayo ili kuweza kuratibu vizuri na hatimaye tuweze kutoa utatuzi wa migogoro hiyo. Sasa timu ile ni ya Mheshimiwa Rais, matokeo ya ukaguzi wake yatawasilishwa kwa Mheshimiwa Rais kwanza kabla ya kupelekwa mahali pengine, kiitifaki inatakiwa iwe hivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini pia timu ile ilipokuwa inapita kwenye maeneo yale, tuliwaagiza Mawaziri watoe taarifa kwenye Mamlaka za Wilaya kule ili watu/wadau wote washirikishwe kule, tuna amini kama kulikuwa na Wabunge na wakati ule ulikuwa siyo wakati wa Bunge, mliweza kushiriki kwa namna moja au nyingine. Pia Mheshimiwa Rais ikimpendeza, baada ya kupata taarifa hiyo, anaweza kutujulisha lakini sasa kiitifaki kwanza aliyetaka tume iundwe ndiye ambaye ambaye tunaweza kumpelekea kwanza, hatuwezi kuileta Bungeni kwanza bila kumpelekea Mheshimiwa Rais mwenyewe kiitifaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo litaangaliwa na kama Mheshimiwa Rais itampendeza anaweza akaamua kutushirikisha lakini tuna amini Wabunge kwa taarifa tulizopeleka kule kwenye halmashauri zenu ili muweze kushiriki katika kutambua na kusaidia kueleza migogoro na kama ambavyo mmekuwa mkieleza hapa ndani, yale maoni yenu ya hapa ndani ndiyo yaliyochukuliwa na kwenda kuyafanyia kazi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi, nchi yetu takribani asilimia 70 ya wananchi wake wanategemea kilimo na Mheshimiwa Waziri Mkuu kilimo hiki kimekuwa na matatizo makubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo basi kilimo cha umwagiliaji kimeonekana ndiyo chenye tija na chenye uhakika wa chakula lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu utakubaliana nami kwamba kilimo hiki bado hakijapewa kipaumbele na hasa ukizingatia sasa hivi kuna maeneo mengi sana yana njaa hata Dodoma mazao yamekauka na maeneo mengine mengi.
Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba kilimo cha umwagiliaji sasa kinapewa kipaumbele ili tuwe na uhakika wa chakula lakini vilevile viwanda vyetu viweze kupata hiyo malighafi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Lyimo, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nataka nikiri kama ulivyosema kwamba hatujaona tija ya kilimo cha umwagiliaji nchini. Serikali hilo imeliona na mwenyewe nimechukua hatua wiki moja iliyopita, tumeivunja Tume ya Umwagiliaji yote, kwanini tumeivunja? Ni kwa sababu kilimo chetu nchini ambacho kinategemea sana mvua na Serikali ilipopanga kuboresha kilimo na kuongeza uzalishaji kwa kuwa na Sekta ya Umwagiliaji, tumegundua kwamba mpaka leo hii Taifa haliwezi kuringia usalama wa chakula nchini kutegemea umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, kwanza tumeiondoa Tume ya Umwagiliaji kutoka Wizara ya Maji ambayo Wizara ya Maji yenyewe inashughulikia zaidi kwa Watanzania na kuihamishia Kilimo ili napo sasa iweze kusimamia vizuri Sekta ya Umwagiliaji kwa mipango waliyonayo ya uzalishaji wa chakula nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mbili, tumegundua fedha yote tunayoipeleka pale kwa ajili ya kutengeneza miradi ya maji haijafanya kazi yake, miradi mingi ya umwagiliaji haijaleta tija, hiyo ndiyo imetusababisha tumevunja tume. Tumepitia tumegundua tuna hasara, tayari tumepeleka timu ya kuchunguza; wakurugenzi sita tumewasimamisha, watendaji 25 tumewahamisha na sasa tunaijenga upya tume ile ili iweze kuleta tija kwa maelekezo mapya kabisa ya Serikali chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie Watanzia kwamba miradi yetu yote iliyopo huko ambayo inasuasua, itaratibiwa upya na timu mpya inayoundwa sasa na Waziri atakuja kutangaza tume na bodi muda mfupi ujao ili ianze kusimamia miradi yote iliyopo nchini. Na sasa ile structure ya utawala wa Tume ya Umwagiliaji ilikuwa wanaishia kwenye kanda, tumetoa utaratibu mpya waende mpaka wilayani. Tutakuwa na Afisa wa Umwagiliaji Mkoani, atakayekuwa anasimamia wilaya zote zenye miradi lakini tutakuwa na Afisa wa Umwagiliaji kila halmashauri asimamie mradi uliopo kwenye halmashauri badala ya kuishia kanda ambako walikuwa hawana uwezo wa kutembelea kwenye wilaya zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, marekebisho haya, yanakuja kuleta tija sasa ya umwagiliaji nchini na tutasimamia kikamilifu kuhakikisha kwamba mabadiliko haya yanaleta tija kwa Watanzania, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni imani ya watanzania kuwa elimu bora ndiyo utakuwa msingi wa kuhakikisha vijana wa Taifa hili pale wanapohitimu wanakuwa na uwezo aidha wa kuajiriwa au kutumia knowledge na skills ambazo wamezipata shuleni kuweza kutambua fursa zilizopo ili waweze kujiajiri wenyewe. Sasa ni matumaini yangu Mheshimiwa Waziri Mkuu utakubaliana na mimi kuwa walimu bora ndiyo wenye uwezo wa ku-transfer au kuambukiza maarifa yaliyo bora kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu, nilitaka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha tunatumia vijana ambao wana division one na two ili wawe walimu ambao tunategemea wata-train wanafunzi ambao watakuwa competent either kutumika kwenye nchi yetu au waweze kutoka nje ya nchi kujitafutia fursa kwa ajili ya maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tweve, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba vijana wetu wakipata elimu bora wanaweza kuingia kwenye Sekta ya Ajira, ajira binafsi hata zile rasmi nje na ndani ya nchi. Na hii inatokana na uimara wa utoaji elimu tulionao nchini ambao pia tunaendelea kuuboresha kila siku ili tuweze kufikia hatua hiyo ya kuwawezesha kuona fursa na kuweza kuzitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao tumeuweka Serikalini ni kubainisha kati ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI kwa usimamizi imara kwenye maeneo haya. Wizara ya Elimu kama msimamizi wa sera, yeye ndiye mwenye uwezo na ndiyo tumempa dhamana ya kuhakikisha kwamba tunaandaa walimu bora wenye uwezo kwa madaraja uliyoyataja na vigezo vinavyotumika kupeleka walimu ni vile ambavyo vimeshafafanuliwa. Tunao walimu wa shule za msingi, walimu wa sekondari lakini pia tuna walimu wa vyuo, maeneo yote yana sifa zake na wote hawa wanakwenda kama sifa zao zinavyoeleza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, matokeo tunayoyapata sasa ni matokeo mazuri ya mipango ya Sera tuliyonayo lakini usimamizi wa utoaji elimu tumeipeleka TAMISEMI, wao ndiyo wanamiliki shule za msingi na sekondari kama elimu ya msingi kujihakikishia kwamba vijana wanaoandaliwa kwenda mpaka elimu ya juu ni vijana ambao walishapewa msingi imara wa kielimu. Kwa hiyo, kazi hii inaendelea kwa kuwa na walimu imara, bora lakini pia kuimarisha miundombinu na wote Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote ni mashahidi, tumepeleka fedha ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyumba vingine pamoja na vifaa mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mikakati hii yote inasababisha kuwa na elimu bora nchini na unapotoa elimu bora, unatoa matokeo yaliyo bora na vijana wanaopata matokeo hayo, sasa wanaweza kuziona fursa zao na kuweza kuzitumia. Kwa hiyo, mkakati wa Serikali unaendelea na tutaendelea kupokea ushauri wenu kuona naona nzuri ya kuboresha Sekta ya Elimu ili tuweze kufikia hatua nzuri, ahsante. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa niulize swali kwa Waziri Mkuu, ni azma ya Serikali yetu na ni Sera ya Serikali yetu kuwapatia wananchi maji safi na salama lakini kwa bei nafuu. Nafahamu pia mchakato wa Serikali kupandisha bili za maji kupitia mamlaka za maji kufanya public hearing na mwisho EWURA waweze kufanya maamuzi ya bili hizo.
Mheshimiwa Spika, EWURA wamemaliza mchakato bahati mbaya sana maoni ya wananchi hayajazingatiwa, bili hizi za maji kote nchini zimepanda kwa zaidi ya asilimia 80. Mfano, mtumiaji wa maji nyumbani alikuwa analipa unit 1 kwa shilingi 1,195 imepanda kuanzia hapo mpaka 1,800. Naomba nifahamu kauli ya Serikali juu ya ongezeko hili la zaidi ya asilimia 80 ya bili za maji nchini wakati wananchi waliomba kwamba bili hizi zisipande?(Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gekul, Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali katika kutoa huduma mbalimbali nchini bado ni njema na inawaangalia uwezo wa Watanzania mpaka yule mwananchi wa chini wanaweza kumudu kugharamia gharama hizo kwa uwezo wake wa kifedha. Umeeleza upo mchakato unaendelea na umeishia mahali ambapo gharama zimepanda kwa asilimia 80. Sisi Serikali tumetoa mamlaka kwenye hizi wakala ili kufanya mapitio na mapitio hayo lazima yaangalie uwezo wa wananchi wenyewe nchini ili wawezeshe wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nimepata taarifa kwamba EWURA na Wizara ya Maji kupitia wakala wamekaa vikao vyao na sasa wameshatoa taarifa ya mwisho ya gharama hizo na zimefikia kwa kiwango ulichokitaja ambacho kimepanda kwa asilimia 80 lakini utaratibu Serikalini ni kwamba baada ya kuwa maazimio hayo yamefanywa, wanatoa taarifa Serikalini. Nashukuru kwamba umetuambia hilo na tumepata taarifa kwamba hata wadau hawakuweza kupata fursa ya kusikilizwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni jukumu la Serikali sasa baada ya kupata matokeo yale, baada ya wao mjadala wao wataleta Serikalini tuone kwamba je, viwango walivyotoa vinawezesha Watanzania kupata huduma hiyo? Na tutakapogundua kwamba hawawezeshwi kupata huduma hiyo, basi Serikali itafanya maamuzi mengine dhidi ya hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikutake ufanye subira, EWURA walete matokeo ya vikao vyao na mapendekezo yao, Serikali tutafanya maamuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Maji. Tukishawapa taarifa hiyo ya mwisho ndiyo itakuwa ndiyo bei ambazo zitakuwa zinatumika na mamlaka hiyo, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tarehe 24 Oktoba, 2019 Mheshimiwa Rais alitoa agizo kwa Halmashauri za vijijini ambazo zilikuwa zinakaa mjini kwamba ndani ya siku 30 ziweze kurudi kwenye maeneo husika ili kutoa huduma karibu na wananchi. Baada ya siku 30 Halmashauri nyingi zilitekeleza agizo hilo.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwa na shida, inaonekana kama kuna kukaidi agizo la Mheshimiwa Rais, kwani wamehamisha ofisi lakini makazi bado wanarudi kulala mjini, hata kama kule walikohamia kuna nyumba na inapelekea Halmashauri kuzipa mzigo wa kugharamia mafuta kila siku ya kurudisha watumishi kwenda kulala mjini.
Je, ni nini kauli ya Serikali kwenye Halmashauri hizo ambazo zimerudi vijijini na watumishi wanarudishwa kulala mjini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua tuliyofikia leo ambapo tuko kwenye Kikao cha Tatu.
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa King Musukuma, Mbunge wa Nzela, Geita Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais alitoa maagizo kwa Halmashauri za Wilaya zote ambazo zilikuwa na Makao Makuu yake kwenye Makao Makuu ya Halmashauri za Miji kuhama mara moja na kwenda kwenye Makao Makuu huko ambako wananchi wa Halmashauri waliko, waweze kuwahudumia kwa karibu.
Mheshimiwa Spika, agizo hili Halmashauri nyingi zimetekeleza na mimi nimepata bahati ya kupita kwenye baadhi ya Halmashauri, kwa wafanyakazi wenyewe kwa kuhamisha ofisi zao na kuhamishia kwenye maeneo hayo mapya, lakini na wao wenyewe kuishi huko.
Mheshimiwa Spika, tunatambua yapo maeneo yenye changamoto; hatuna nyumba za kutosha kwa ajili ya makazi yao, lakini kuna Halmashauri ambazo zina nyumba za watumishi na wananchi wanazo nyumba ambazo zinaweza kupangishwa na hili lilikuwa agizo la Mheshimiwa Rais; na agizo la Mheshimiwa Rais ni agizo ambalo linatakiwa litekelezwe mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge Musukuma alivyosema kwamba huko kuna makazi, kutokwenda ni kuvunja amri, kukataa amri ya Mheshimiwa Rais. Ni kosa kubwa sana kwenye utumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwaagize Wakuu wa Mikoa akiwemo na Mkuu wa Mkoa wa eneo ambako Halmashauri iliyotakiwa kuhama ilipo, Katibu Tawala wa Mkoa ambaye pia ni Mtendaji Mkuu kwenye Mkoa huo, ambapo kwenye Halmashauri zenye mazingira hayo ambayo watumishi wametakiwa waondoke kwenda kwenye makao mapya hawajaenda, waondoke mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu kipindi cha kuondoka kilishatamkwa na Mheshimiwa Rais, kwa hiyo, hatuna sababu ya kuwapa muda tena. Ni kuondoka mara moja baada ya tamko hili. Endapo hawatafanya hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mkoa husika achukue hatua mara moja dhidi ya watumishi hao na hasa wale wote ambao hawataki kwenda kwenye maeneo mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa tumeagiza haya, naagiza pia Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo pia inasimamia Halmashauri hizi, kufuatilia kila Halmashauri iliyotakiwa kuhama kwenye maeneo ya zamani, kuhamia kwenye maeneo mapya ili watumishi wote waweze kuhamia na nitahitaji taarifa hizo keshokutwa Jumamosi, ofisini kwangu saa 4.00 asubihi ili nijue ni Halmashauri gani ambayo bado watumishi hawajahama, ili tuchukue hatua nyingine za kinidhamu kwa watumishi hao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, umenipa nafasi nami niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa Serikali imetoa waraka kwamba mazao aina ya choroko, dengu na kadhalika kwa msimu huu yatanunuliwa na AMCOS kwa mkopo bila bei elekezi na watapeleka kwenye minada ya TMX na hatujui lini minada itatokea; na kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Kwimba ni wakulima wadogo wadogo ambao wamezoea kuuza sokoni kwa kilo tano, kilo kumi mpaka kilo 20 na wakishauza wanapata fedha cash wanakwenda kununua mahitaji yao kama chakula na kupeleka kwenye familia zao; hawa watu wanateseka kwa sasa hivi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa wafanyabiashara wapo sasa hivi ambao kila mwaka walikuwa wananunua mazao hayo kwa cash, kwa bei ya soko na wakulima walikuwa wanapata fedha taslimu (cash), kwa nini wasiruhusiwe kuendelea kununua mazao hayo wakati AMCOS wanajiandaa kuwa na fedha taslimu ya kulipa kwa wakulima ili tupate ushindani? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mansoor, Mbunge wa Kwimba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba upo waraka unaoelekeza kununua mazao ya choroko kwa mkopo. Sina uhakika kama kweli Wizara iliagiza inunue kwa mkopo, ila ninachojua ambacho pia nimekipatia taarifa na tumeagiza pia Wizara ya Kilimo ifanyie kazi, ni pale ambapo Wizara ya Kilimo imeagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kusimamia kuwepo kwa ushirika kwa wakulima, iwe ni mahali ambapo wanaweza kuuza mazao yao kwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ambao maeneo kadhaa ambayo wananchi wake hawajapata elimu kwa ule Mfumo wa Stakabadhi Ghalani inaonekana kama vile ni mkopo.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu unawataka wakulima kukusana mazao, kuyaweka pamoja halafu kusubiri siku moja kutangaza soko. Kwa hiyo, kitendo kile cha wakulima kukusanya mazao na kuyaweka pamoja kusubiri soko, zile siku ndiyo inapotafsiriwa kwamba tayari wamekwenda kuuza na wamekopwa, kumbe mauzo bado, ndiyo mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Sasa mgogo huu nimeusikia pia Mkoani Mwanza, Simiyu, Mara kwenye mazao haya na Shinyanga kwenye zao hili la choroko.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme, kama waraka ulitoka kwenda kuwaagiza Wakuu wa Mikoa wasimamie hili, mfumo huu kabla haujatekelezwa ni lazima wakulima wapate elimu ili waweze kuelewa mfumo huu unakuwaje? Kama hakuna elimu, kunatokea malalamiko haya, kwa sababu uzoefu pia, hata kwenye mazao kama korosho, mfumo ulipoanza kulikuwa na migongano mingi ambayo ilipelekea kutoelewana na wananchi, wakaanza kuilalamikia Serikali kwa kauli hiyo hiyo kwamba wanakopwa.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naagiza sasa mikoa yote ambayo inanunua mazao haya ya choroko na dengu, zao ambalo wazalishaji wengi wanazalisha kama alivyosema kilo tano, sita, saba; ili ukusanye dengu iweze kupata mzigo mkubwa na utangaze mnada, lazima itachukua siku nyingi. Kwa hiyo, kwa zao hili ni tatizo kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema Wakuu wa Mikoa waridhie kwanza eneo hili la choroko na dengu ambalo uzalishaji wake ni mdogo mdogo, ni muhimu tukaufikiria upya kuanza kwake tofauti na mazao yanayopatikana kwa wingi kama vile korosho, chai, pamba, kahawa na mazao yale yanayozalishwa kwa wingi, yale inawezekana ukakusanya siku mbili ukapata mzigo mkubwa na kuuza kwenye mnada na kuwa na siku chache sana kufikia siku ya mauzo na mwananchi hawezi kulalamika. Ila fiwi, choroko na dengu ni zao ambalo linalimwa kwenye ekari moja, mtu anavuna kilo mbili. Sasa ukimpeleka kwenye mnada mpaka akae upate mzigo wa kutangaza mnada, lazima atalalamika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye eneo hili, naiagiza Wizara ya Kilimo ifanye mapitio tena ya waraka huo na ione mazingira ambako wananchi wanaona kama wanakopwa, lakini kumbe ni subira ya kusubiri siku ya mnada kwa uchache wa zao lenyewe ili Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, tuanze na mazao yale ambayo yanapatikana kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama kuna maeneo wameshaanza, wao waendelee kwa sababu mfumo huu umekuja kututhibitishia kwamba unaleta bei nzuri sana ya zao siku ya mnada kwa sababu mnada ule unashindanisha wanunuzi. Kila mmoja anakuja na bei yake na wakulima watakuwa na uhuru wa kumchagua mnunuzi aliyeweka bei ya juu.
Mheshimiwa Spika, kumbukumbu zetu zinaonesha, zao hilo hilo limewahi kuuzwa mpaka shilingi 600/= mpaka shilingi 700/=, lakini baada ya mnada lilienda mpaka shilingi 900/=, shilingi 1,200/= na zaidi, hasa pale Mkoani Shinyanga ambako walishaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara ya Kilimo ifanye mapitio tena kwenye eneo hili halafu tuwape mrejesho Waheshimiwa Wabunge na wananchi wajue ni nini kinatakiwa kifanyike kwenye mazao haya. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, dhana ya Serikali ya kutenga maeneo na kusimamia hifadhi zilizopo nchini kwetu ilikuwa ni kulinda rasilimali za nchi yetu. Sote tunajua wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi mbalimbali ni wahifadhi namba moja, jambo ambalo kwa sasa limebadilika kulingana na watendaji aidha ni wachache, kulingana na mambo yanayofanyika hivi sasa.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, natambua kumekuwa na kelele nyingi na malalamiko mengi kutoka kwa sisi Wabunge kwa wananchi wetu. Leo wananchi wanaozunguka hifadhi, wanaoshughulika na shughuli za kawaida ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi, imekuwa changamoto ya kupigwa, kunyanyaswa, kunyang’anywa mifugo, jambo ambalo linakwenda kuondoa ile dhana ya wao kuwa wasimamizi wa hizi hifadhi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, miongoni mwa changamoto zinazopelekea vurugu hizo ni mipaka inayobadilishwa kila siku na mipaka mingine ambayo haieleweki, kwa maana ya kwamba havijawekwa vitu ambavyo vinaonesha alama kwamba hapa ni mpaka.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujua Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kwenda kupitia upya maeneo hayo ambayo yanasababisha migogoro kwa wananchi wetu ili mipaka hiyo ieleweke; na pia wanapokwenda kutengeneza au kupima hiyo mipaka, iwe shirikishi. Napenda kujua Serikali ina mpango gani wa haraka?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunayo changamoto ya uwepo wa migogoro kati ya wananchi waliopo pembezoni mwa Hifadhi zetu za Taifa, mapori tengefu ambayo yameweka ukomo wa wananchi hao kuingia kwenda huko. Migogoro hii mara nyingi imetokana na kutoeleweka kwa uwepo wa mipaka kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili Serikali imefanya jitihada kubwa; moja, ni kutoa elimu ya wananchi walioko kwenye vijiji vilivyo karibu na mipaka hii; kwanza kutambua ukomo wa mipaka ya Hifadhi hizo za Taifa na maeneo ambayo wananchi wanaishi huku wakiendelea kupata huduma za kijamii kwenye suala la uchumi na mambo mengine, kwa mfano kilimo, mifugo na shughuli nyinginezo.
Mheshimiwa Spika, uwepo wa migogoro kwenye maeneo haya ni pale ambapo kama Mbunge alivyosema, mipaka haieleweki. Jukumu hili tumeshawapa Wizara ya Maliasili kuhakikisha kwamba wanapitia ramani zilizopo na kwenda kila mahali palipo na migogoro ili kuondoa migogoro hiyo ili wananchi waweze kuishi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameonesha kwenye Jimbo lake pia kuna migogoro ya hiyo, ndiyo sababu amekuja na swali hili. Kwa hiyo, nimuagize sasa Mheshimiwa Waziri wa Maliasili kufika Nkasi Kaskazini kuona mgogoro huo ili kutatua tatizo hilo kwa kubainisha vizuri mipaka na kuweka alama zinazoonekana zitakazomwezesha mwananchi kutokuingia kwenye eneo hilo ili kuepusha migogoro ambayo ipo. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo haya ya hifadhi, lakini pia mapori tengefu yanaendelezwa kwa malengo yaliyowekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tunatamani kuona wananchi walipo pembezoni wakiendelea na maisha yao, shughuli zao za kijamii, kilimo, mifugo na indelezwe lakini pia kwa kuzingatia mipaka ile. Kwa hiyo, kama ni tatizo la mipaka, tayari Mheshimiwa Waziri atakuwa amepokea kauli yangu na agizo langu, aende Nkasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo Nkasi tu, na popote pale ambako kuna migongano kati ya wananchi na mipaka ili tubainishe kwa uwazi kabisa na sasa zoezi hilo liwe shirikishi; wananchi walioko jirani washirikishwe na maafisa walikuwepo pale washirikishwe, wafanye kazi kwa pamoja na kila mmoja afanye kazi yake kwa amani na watu wajipange, waongeze uchumi wao kupitia fursa zilizopo kwenye maeneo yao. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Kutokana na muitikio mkubwa wa wananchi wa Tanzania kulima mazao ya kimkakati ili kukuza uchumi wa nchi yetu, upo uwezekano baada ya miaka michache tukaongeza sana uzalishaji kwenye mazao haya. Kwa sasa sehemu kubwa ya mazao haya ya kimkakati soko lake ni nje ya nchi yetu, jambo ambalo linaminya kidogo fursa za ajira, lakini pia soko likiyumba kule, inaleta shida kwa wakulima wetu na kwa uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujua, ni upi sasa mkakati maalum na mahususi wa Serikali kuhakikisha kwamba inawezesha uwekezaji kwenye viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa kwa mazao haya ya kimkakati kama zao la mkonge ili kuwasaidia wananchi wapate uhakika wa masoko na pia kuendelea kutengeneza ajira kwa wananchi wetu wa Tanzania? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -
Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, nilikuwa nae kwenye kampeni za kufufua zao la mkonge Mkoani Tanga kwenye kikao cha wadau na tulifanya ziara kwa pamoja kwa siku tatu mfululizo kupitia mashamba, viwanda, vinavyochakata zao la mkonge. Zao la mkonge ni miongoni mwa mazao yale ya kimkakati, tulianza na matano, tumeongeza mazao mawili kuwa saba na mazao hayo ni mkonge yenyewe pamoja na mchikichi ambao unalimwa sana Mkoani Kigoma na maeneo ya Ukanda wa Pwani. Tunapohamasisha kilimo cha mazao haya na kuyapa hadhi ya mkakati, mazao haya ni mazao yanayolimwa na jamii pana kwenye maeneo yake na mazao haya ndiyo yanayoleta uchumi wa mtu mmoja mmoja kwenye maeneo yanayolimwa, lakini pia hata uchumi wa kitaifa kwa kupata fedha nyingi kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, lakini bado mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tunahamasisha kilimo si tu cha mazao haya ya kimkakati pamoja na mazao mengine ya chakula na biashara tunataka pia usalama wa chakula nchini uwepo, watu wapate chakula cha kutosha, lakini pia na mazao haya ya kibiashara yakiwemo haya ya kimkakati na mazao mengine ambayo hatukuyaingiza kwenye mkakati lakini tunatamani mazao haya yalimwe ili wananchi waweze kuuza, wapate uchumi wa kutosha na sisi pia tuwe na uwezo wa kupata fedha.
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mkakati wa kutafuta masoko. Ni kweli mkakati tunao, kila zao tunajua maeneo ambako soko lipo, lakini tunapoupeleka kwenye masoko haya jambo la kwanza ambalo tunalizingatia ni kuongeza thamani ili wakulima wapate faida kubwa na mazao haya tunaposema kuongeza thamani tunakwenda sasa kwenye wito wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa ujenzi wa viwanda ndani ya nchi. (Makofi)
Kwa hiyo, moja kati ya mkakati ambao tunao ni kuhakikisha kwamba tunakaribisha uwekezaji kwa Watanzania na walioko nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye viwanda kwa sababu tuna uhakika tuna ardhi ya kutosha, lakini pia malighafi ya mazao hayo tunaweza pia na tuna labour ya kutosha nchini kwa maana ya kwamba tunaweza kutengeneza ajira nyingi kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema.
Mheshimiwa Spika, sasa mkakati huu nilipokuwa ziara ya siku tatu mkoani Tanga tumepita kwenye viwanda na tumeona na kumesikia, sehemu kubwa ya viwanda vingi vinafanya kazi, lakini pia vingine havifanyi kazi kwa sababu ya uchakavu. Tunahitaji kubadilisha teknolojia ili tuwe na teknolojia ambayo sasa inaendelea vizuri.
Pili, viko viwanda ambavyo wawekezaji wamejenga vinakwama kupata masoko mazuri kwa sababu kuna bidhaa zisizokuwa na sifa zinazoingia nchini. Ili kuendeleza uwekezaji huo, moja kati ya jambo kubwa tunalolifanya ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti bidhaa za kutoka nje ili kuwezesha uwekezaji wa ndani kukua na kuuletea manufaa makubwa kwa kupata fedha za kutosha na ajira. Hayo yote tunayazingatia ili tuweze kuhakikisha kwamba uwekezaji unakuwepo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani, mpango wetu ni kuhakikisha kwamba tunaongeza hamasa ya ujenzi wa viwanda, lakini pia tunavilinda viwanda vya ndani. Kwa mfano tuliouona kwenye zao la mkonge, tunacho kiwanda kinazalisha nyuzi nchini kupitia zao la mkonge, na kiwanda hiki inazalisha bidhaa mbalimbali za nyuzi zenye ukubwa tofauti lakini pia tunazo bidhaa za plastiki zinaingia nchini huku Tanzania tukiwa tumeshazuia kuingiza plastiki. Kwa hiyo, nimeagiza Wizara ya Kilimo kufanya mapitio kwenye viwanda vyote vinavyozalisha nyuzi za plastiki huwa tukiwa na viwanda vinavyozalisha nyuzi za mkonge tunaoulima hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulishapiga marufuku matumizi ya plastiki lakini tulisema tutaenda kwa awamu. Tulianza na plastiki za kubebea mizigo na zile za viroba. Sasa tutaenda mbali zaidi tunaingia kwenye nyuzi kwa lengo la kumlinda mwekezaji wetu aliyejengwa kiwanda nchini, lakini pia anayetumia zao letu la mkonge kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo na nyuzi lazima tumlinde ilia pate faida na sisi tunufaike kwa kupata soko zuri, kupata ajira kwa watu wetu lakini pia kuhakikisha kwamba wakulima sasa wanahamasika kulima kwa sababu ya uhakika wa soko. Huo ndiyo mpango wetu wa Serikali kwenye eneo hili. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipatia na mimi nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tangu nchi yetu imepata uhuru, Watanzania zaidi ya asilimia 75 ni wakulima kutokana na Serikali kutangaza kilimo ni uti wa mgongo lakini wakulima wetu hawa ambao ni Watanzania wameendelea kulima kilimo cha kutegemea mvua ya Mwenyezi Mungu ambacho kimekuwa hakina tija kwao wala tija kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini mkakati wa Serikali wa kuwatoa Watanzania wakulima kwenye kilimo hiki kisichokuwa na tija kwao na kwa Taifa letu kuwapeleka kwenye kilimo ambacho kitaweza kutuondoa Watanzania kwenye wimbi la umaskini na kwenda kufikia sasa kwenye uchumi wa kati ambao utakaokwenda kukidhi mahitaji ya muonekano kwa Watanzania wetu? Nakushukuru.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunty Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba Serikali yetu sasa hivi inasisitiza kilimo ili kiweze kutoa manufaa au tija kwa wale wanaolima na wito huu wa kulima mazao haya ya biashara na chakula ni mkakati ule ule wa kuongeza tija kwa kilimo chetu. Ni kweli kwamba tukitegemea kilimo kinachotegemea hali ya hewa kama mvua pekee hatuwezi kupata tija. Nini tumekifanya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina taasisi au Kurugenzi ya Umwagiliaji ambayo yenyewe tumeipa bajeti ya kuhakikisha kwamba wanahakikisha tunafufua kilimo cha umwagiliaji nchini kitakachomwezesha mkulima kulima wakati wote masika, lakini wakati wa kiangazi ili uzalishaji uwe mkubwa na mkulima anapolima apate mazao ya kutosha, akiamua kuyauza kama atapata ziada, atapata uchumi lakini pia kumhakikishia usalama wa chakula pale anapozalisha, lakini kama ni zao tu la biashara kuendelea kumtafutia masoko. Kwa hiyo, mkakati wa Serikali katika hili ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na kilimo cha aina zote mbili cha kutegemea hali ya hewa ya mvua lakini pia na umwagiliaji ambao pia tumeimarisha na tunaendelea pia kubaini maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji na kuanzisha miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano, Mheshimiwa Kunti yeye anatoka Chemba, Chemba ni eneo ambalo limepitiwa na mto mkubwa sana ambao unatiririsha maji mpaka maeneo ya Bahi. Mto ule unapitisha maji masika pamoja na kiangazi. Mkakati ambao tunao maeneo yote yanayopita maji yale kwenye mto pembezoni tunaona wakulima wapo ambao wanalima. Sasa tunawaanzishia miradi ya umwagiliaji ili wakulima hao waweze kulima kilimo ambacho kitawapatia fursa ya kutosha ili waweze kunufaika na kilimo hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, malengo yetu kilimo chetu nchini kiwe na tija kwa wakulima, kituletee mazao ya chakula ya kutosha, pale ambapo wanalima mazao ya kibiashara basi wapate mazao ya kibiashara ya kutosha. Kwa ujumla wake tutaanza kuleta tija kwa wakulima, lakini pia kwa nchi na kuifanya nchi yetu kuwa na usalama wa chakula cha kutosha kwa kulima chakula cha kutosha na ziada. Huo ndiyo mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba Serikali na wananchi wake wanalima kilimo hiki. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa Serikali imetumia nguvu nyingi sana katika kupambana na uvuvi haramu na kulinda hifadhi zetu na kama sehemu ya mafanikio ya juhudi hizi idadi ya wanyamapori imeongezeka na katika maeneo mengine wanyamapori hawa wamesambaa na kuingia katika makazi ya watu na hivyo kuathiri sana maisha ya watu na shughuli za uzalishaji. Kwa kuwa tatizo hili sasa limeonekana kuwa la kudumu, Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya suluhisho la kudumu la tatizo hili? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tadayo, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali hili linafanana sana na swali ambalo mwanzo nimetoa ufafanuzi wake kwamba yako maeneo yana migogoro kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi. Swali la awali lilikuwa linazungumzia ule mgongano wao na hili linzungumzia wanyamapori walioko.
Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo haya tuliyoyahifadhi yana hawa wanyamapori na maeneo haya ya wanyamapori pia tumeendelea kuwahifadhi na kutoa tahadhari kwa wananchi walioko jirani na maeneo haya. Mkakati wa kuzuia wanyamapori hawa kuja kwenye makazi ya wananchi upo na unaendelea pale ambapo kwanza tumetoa elimu kwa wananchi wanaokaa karibu na maeneo haya ya wanyamapori kuwa na tahadhari. Wanapofanya shughuli zao wasiingie kwenye eneo la wanyamapori, pia tumewawekea buffer ya mita kama 500 ambazo wao wananchi walioko huko hata wanapoingia eneo hili lazima wawe na tahadhari ya kutosha. Tunaamini wanyama walioko kwenye lile pori wanaweza kuja mpaka kwenye mpaka wa kijitanua kidogo wanaingia kwenye hili eneo la mita hizi 500, wanaweza wakazunguka hapo na kurudi. Inapotokea wakija huku sasa Idara ya Maliasili kupitia kikosi chao cha wanyamapori tumekiweka maeneo yale ambayo wanyamapori huwa wana tabia ya kutoka na kurudi huku kwa ajili ya kuwazuia kurudi kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, jambo hili tunalifanya kwa kushirikisha pia vijiji vyenyewe, tunawapa elimu tunaanzisha ulinzi wa kijiji ambako pia ikitokea hilo nao wanasaidia kuwarudisha. Bado tunao wanyama wanatoka wanakuja lakini bado tumeendelea kuimarisha vikosi vyetu kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo yana wanyamapori wanaotoka sana kuweka kambi dogo la kuhakikisha kwamba wanarudishwa kwenye maeneo hayo na makambi hayo tumeamua tuyaweke katika maeneo yote ambayo tunaona wanyama kama tembo ambao wameongezeka sana kwa sasa waweze kudhibitiwa.
Mheshimiwa Spika, nimeliona hili pia nilipokuwa nafanya ziara wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, nimeona pia nikiwa Bariadi Mkoani Simiyu, nimeenda pia hata Tarime na maeneo mengine ambayo nimepita, nimepata malalamiko haya na tumeshawasiliana na Wizara ya Maliasili kujiandaa vizuri kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, tumeshaanza kusambaza vikosi vyetu, kulinda maeneo hayo ili pia wananchi wasiweze kusumbuliwa.
Mheshimiwa Spika, wito kwa wananchi walioko kwenye vijiji ambavyo viko karibu na maeneo ya hifadhi, wasiingie sana kwenye mapito ya mara kwa mara ya wanyama. Tunao wanyama kama tembo ambao wao wana mapito yao miaka yote. Kwa hiyo, maeneo hayo kwa sababu tunaishi kwenye vijiji hivyo, tunayafahamu. Ni muhimu kuwa na tahadhari kwenye maeneo haya ya mapito ili tusije tukawa tunaingiliana na hawa wanyama, lakini bado mkakati wetu ni ule ule. Kwa hiyo, tushirikiane pamoja kuhakikisha kwamba tunawahifadhi wanyama wetu na madhara ambayo yanajitokeza pia tunaendelea kuyadhibiti ili yasiweze kuendelea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkakati wa kudhibiti hatari hii unaendelea chini ya maliasili kwa kuweka makamanda kwenye maeneo hayo na kila wilaya iliyoko kwenye mpaka tuna kitengo hicho ambacho pia kinafanya kazi hiyo kubaini kwenye mipaka yake kwamba wakati wote tunakuwa salama. Lengo ni kuwalinda wananchi wanaoendelea na shughuli zao, lakini pia kuwalinda wanyamapori ambao pia na wao watatupatia tija kwa shughuli za kitalii na uhifadhi wa wanyama wetu kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
MHE. HAMIS H. T. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa ziarani Mwanza katika ziara yake ya kikazi alitoa tamko kwa nchi kuhakikisha wanafunzi wote wanakwenda darasani mwisho tarehe 28 mwezi wa pili. Tamko hilo liliungwa mkono na wananchi nchi nzima na wakuu wa mikoa wakalisimamia, wakuu wa wilaya wamelisimamia tunamshukuru Mwenyezi Mungu. Majengo yamejengwa, kuna maboma mengi katika nchi hii yamekamilika.
Mheshimiwa Waziri Mkuu nini tamko la Serikali kuhusiana na pesa za kumalizia haya majengo kwa nchi nzima ili watoto wote waingie kutokana na idadi ya siku uliyokuwa umetoa tarehe 28 Februari? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tabasamu, Mbunge wa Sengerema kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uko ukweli kwamba Halmashauri zetu zimekuwa zikifanya kazi za ukamilishaji wa maboma haya kama jambo la dharura kila mwaka, lakini sasa tumefika tumeziagiza Halmashauri hizi kuhakikisha kuwa wana mpango wa muda mrefu wa kudumu unaosimamia ujenzi wa miundombinu hii ikiwemo madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu kwenye shule zetu ili jambo hili lisiwe la zima moto kila mwaka. Kwa kutumia pia takwimu tulizonazo Halmashauri zote zinajua kila mwaka zina wanafunzi wangapi wa darasa la saba wanaotaka kumaliza mwaka huo na ambao wanaweza kufaulu.
Mheshimiwa Spika, upo utaratibu walimu wanautumia kujua wangapi wanaweza kufaulisha. Kutokana na takwimu hiyo inaweza kuifanya Halmashauri ikajiandaa kujenga vyumba vya madarasa na miundombinu nyingine. Lakini pia hata kwa sekondari wanapomaliza kidato cha nne wanaweza kutabiri tutakuwa na idadi ya wanafunzi wangapi ambao wanaenda kidato cha tano. Halmashauri ikamudu kujipanga vizuri kujenga miundombinu ya kuwapokea kidato cha tano. Jambo hili sasa limeenda sambamba na agizo ambalo nimelitoa.
Mheshimiwa Spika, lakini kama ulivyosema tumekuta maboma mengi yamejengwa na wananchi hajakamilishwa na umetaka kujua mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunakamilisha majengo hayo. Bado kwanza tumetoa wito kwa Halmashauri zenyewe kupitia mapato yao ya ndani na kupitia mipango yao kukamilisha maboma yaliyojengwa na wananchi ili tuwe na miundombinu ya kutosha kila mwaka tuweze kupata nafasi ya kuingiza wanafunzi. Lakini kupitia pia bajeti inayoandaliwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo haitoshi kumaliza maboma yote huwa tunaunga mkono juhudi za wananchi na Halmashauri kwa kukamilisha maboma yaliyopo kwa ajili ya kutoa nafasi ya wanafunzi wanaojiunga upya kwenye maeneo haya ili kila mwanafunzi ambaye anapata nafasi ya kuendelea na masomo aende kwa wakati bila ya kuwa na awamu ya kwanza na ya pili na kuendelea huko mwishoni.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niseme tu kwamba pale ambapo uwezo wa Serikali unaendelea, tutaendelea ku- support, kuunga mkono jitihada za Halmashauri na wananchi katika kukamilisha maboma, lakini awali kabisa Halmashauri zenyewe zijiwekee mpango endelevu wa kuhakikisha kwamba unapata miundombinu ya kutosha ili wanafunzi hawa waweze kuingia kwenye majengo haya ili kusiwe tena na maagizo, maagizo. Kwa sababu itakuwa kila mwaka Waziri Mkuu au Makamu wa Rais au Mheshimiwa Raisa toe maagizo ya kila mwaka, jambo hili halikubaliki na sasa tumewaambia wajipange vizuri ili tuwe na miundombinu endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana Mheshimiwa Tabasamu, Halmashauri zote zimesikia na kila Halmashauri imeagizwa iwe na mpango wa muda mrefu wa kuhakikisha kwamba miundombinu inajengwa kila mwaka na kila wanafunzi wanapofaulu wanaingia moja kwa moja bila ya maagizo. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kumi zinazozungumzwa sana Barani Afrika. Ni lugha ya pili kwa kuzungumzwa na watu wengi Barani Afrika na pia ni kati ya lugha kumi zinazozungumzwa sana duniani. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha Kiswahili kinakuwa bidhaa hasa wakati wa kuchangia diplomasia ya uchumi na kuwa fursa ya ajira kwa Watanzania? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye leo ametupa uhai wa kukutana hapa na kuendelea na shughuli zetu za Bunge.
Mheshimiwa Spika, pili, niungane nawe kuwakaribisha Waheshimiwa Wabunge wenzetu kutoka Baraza la Wawakilishi kuungana nasi kwenye Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibuni sana, tutawapa ushirikiano wa hali ya juu na kwa kweli mtasaidia sana kuchangia yale muhimu na kuishauri Serikali na sisi Serikali tupo tayari kupokea ushauri wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kujibu swali la Mheshimiwa Baba Askofu Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kiswahili sasa kimepata nafasi kubwa ya kuzungumzwa kwenye mataifa mengi duniani na wala siyo kuzungumzwa tu pia hata matumizi yake yameongezeka. Tumeanza kuona nchi mbalimbali kubwa duniani zikiandaa vipindi vya Kiswahili kwenye redio na kwenye magazeti yao. Hii ni ishara kwamba Kiswahili chetu sasa kinakua duniani kote.
Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na kutengeneza fursa hata kwa Watanzania ambao ndiyo wenye Kiswahili? Kiswahili hiki hapa nchini kinazungumzwa na makabila yetu karibu yote na ndiyo lugha ambayo inatuunganisha Watanzania. Tumeanza kusambaza Kiswahili hiki kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki, tumeona nchi zote za Afrika Mashariki zinazungumza lugha hii. Wote ni mashahidi tumeona jitihada ambazo zimefanywa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kusambaza Kiswahili kwenye Nchi za Ukanda wa Kusini (SADC) pale ambapo amekutana na Marais mbalimbali kuwahamasisha na sasa tumeona Kiswahili kimeanza kufundishwa kwenye nchi zao, kwa hiyo, Kiswahili kinazidi kupanuka.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, Kiswahili nacho kinaenda mbali zaidi, utaona Ujerumani, Marekani, Uingereza na Mataifa mengine makubwa yanaendelea kutumia Kiswahili. Sisi kama Serikali tumeweza kuwasiliana kupitia Balozi zetu, kila Balozi tumeiagiza kwenye nchi ambazo Balozi yupo kuanzisha kituo cha kujifunzia Kiswahili. Malengo yetu ni kupanua matumizi ya lugha ya Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapowafikishia Mabalozi na kufungua vituo na kuwafanya wananchi wa nchi husika kujifunza Kiswahili hapo sasa tumeingiza kwenye diplomasia ya Kiswahili. Kwa kuwa sasa Kiswahili kinapendwa duniani kote na kinazungumzwa na nchi nyingi sisi Watanzania sasa tuna fursa ya kuwa walimu wazuri kwenye nchi hizo kwenye vituo vyetu vya kufundisha Kiswahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapokwenda kuwa walimu kwenye nchi hizo tayari tunafungua fursa za kiuchumi kwa kuajiri Watanzania kwenda kufanya kazi kwenye nchi hizo. Watanzania wakishapata ajira tunajua kodi kidogo inarudi nchini na tunaboresha uchumi wetu wa ndani. Kwa hiyo, tutatumia diplomasia hii kukuza uchumi wa ndani na hasa kwa kutoa fursa ya Watanzania kuajiriwa kwenye maeneo hayo kuendeleza kuboresha Kiswahili.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, swali langu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tatizo kubwa la masoko ya mazao yetu hata kama tunazalisha kwa ubora wa juu. Je, Serikali iko tayari kupeleka wataalam wake nje ya nchi na hasa kwenye nchi ambazo zimefanikiwa ili kujifunza namna bora ya usimamizi wa masoko yetu? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lugangira, Mbunge wa Mkoa wa Kagera, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la kutafuta masoko kwenye mazao yetu lakini pia Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mpango wa Serikali wa kuwapeleka wataalam wetu nje ya nchi kujifunza kutafuta masoko. Sina uhakika sana kama alikuwa anataka kusisitiza kuwepo kwa masoko au suala ni kupeleka wataalam kujifunza masoko. Hata hivyo, Serikali yetu inatambua na inao mkakati ambao sasa tunaendelea nao wa kuzalisha mazao mengi ya chakula na biashara. Kwenye mazao yote ya biashara tumeendelea kuboresha kupata masoko ya ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuwapatia nafasi nzuri wakulima wetu kuuza mazao yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, lakini pia inapoingia kwenye utaalam wa kutafuta masoko muhimu zaidi ni kujua kama mazao tunayozalisha tuna masoko huko nje? Tunachokifanya sasa kila zao kupitia Balozi hizi nazo tunazitumia kutangaza mazao tuliyonayo ndani ya nchi ili tuweze kuyauza kwenye nchi wanazotumia mazao hayo. Zoezi hili linaendelea na tunapata wateja wengi kuja kununua mazao yetu na hali hiyo imesababisha masoko yetu kuimarika.
Mheshimiwa Spika, muhimu kwetu sisi ni kutafuta mfumo mzuri unaowezesha mazao haya kujulikana na kuyauza na tupate bei nzuri. Kama ambavyo sasa ndani ya nchi tumeweka Mfumo wa Stakabali Ghalani ambao unakusanya mazao pamoja na kuwaalika wanunuzi kila mmoja anatamka atanunua zao hilo kwa shilingi ngapi kwa kilo, yule mwenye bei ya juu ndiye ambaye tunampa fursa ya kununua. Kwa hiyo, huo ni mfumo wa uuzaji wa mazao yetu ambao tumeuandaa na tutapata bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia Serikali tunao mpango wa kutafuta masoko kwenye nchi ambazo zinazohitaji mazao hayo. Juzi hapa nilikuwa na Wabunge wa Mkoa wa Rukwa wakiomba Serikali iwasaidie kutafuta masoko ya mazao yanayolimwa Mkoani Rukwa kwa nchi za Zambia, Rwanda na Burundi. Kwa hiyo, kazi ambayo Serikali inafanya sasa ni kuwasiliana na nchi ambazo ni walaji wa mazao haya ili kuhakikishia kuwa mazao haya yanapolimwa na kuvunwa tunayapeleka kwenye nchi husika. Hiyo ni njia pia ya kupata soko zuri la mazao yetu.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali kwa sasa tunaendelea kujenga masoko ya kimkakati, masoko ya kikanda, ambayo tunayajenga pembezoni mwa nchi yetu ili kukaribisha ndugu zetu walioko jirani kuja kununua. Miezi mitatu iliyopita nilikuwa Mkoani Kilimanjaro, nimekwenda pale Horohoro, tunajenga soko kubwa sana ambalo pia wananchi wa maeneo hayo wakizalisha mazao yatawekwa hapo, wa nchi jirani wote watakuja hapo. Kwa hiyo tunawapunguzia ugumu wa kuingia mpaka huku ndani kutafuta mazao hayo badala yake tunawa-allocate kwenye masoko yale.
Mheshimiwa Spika, mwezi mmoja uliopita pia nilikuwa Mkoani Kigoma kule Kagunga. Tumejenga soko zuri sana. Kwa hiyo tunawakaribisha ndugu zetu wa Burundi na Rwanda kuja kununua pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajenga soko lingine kubwa sana Mkoani Kagera pale Nyakanazi. Lengo letu wale wote kutoka Kongo, Rwanda watakuja pale Nyakanazi kwenye soko letu lile la zaidi ya bilioni 3.5 ili wapate bidhaa. Kwa hiyo muhimu kwetu sisi ni kuweka mkakati wa namna gani mazao yetu yaliyoboreshwa yaweze kupata thamani kubwa kwa lengo la kumfanya mkulima aweze kupata tija kwa kazi ya kilimo anayoifanya. Kwa hiyo Serikali inaendelea na maboresho haya, Waheshimiwa Wabunge kama mna mawazo mengine ya kuboresha masoko, tunawakaribisha ili Serikali iweze kuimarisha upatikanaji wa mazao haya na iweze kuuza mazao haya kwa bei nzuri sana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu swali lifuatalo:-
Mheshimiwa Spika, kwa vile Serikali iliona umuhimu wa kuwafikishia wananchi kule vijijini umeme kwa gharama nafuu, kwa hivyo wakaweka utaratibu wa kuunganishia nyumba umeme kwa Sh.27,000 tu. Je, Serikali haioni umuhimu kwa kuzingatia kwamba maji ni uhai na ni hitaji kubwa sana kwa kila mtu hapa duniani, kuhakikisha kwamba wanaweka utaratibu kama huu wa kuweka gharama ya kumuunganishia mtu maji?
Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa hivi kule MUWASA na RUWASA natumaini na mamlaka nyingine za maji zitatoza 350,000 mpaka 600,000 kumuunganishia mtu maji. Sasa je, mtu ataweza kweli kuvuta maji kupeleka nyumbani? Kwa hiyo watu wameamua kuanza kunywa maji ya mfereji ambapo hiyo haisaidii…
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa swali lako limeeleweka.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu wa gharama za maji kupitia Sera yetu iliyoko pale Wizara ya Maji. Utaratibu huu tumeanzisha taasisi zitakazotoa huduma za maji sasa hivi tumezipeleka mpaka wilayani tunaita RUWASA, taasisi ambazo zinashughulikia maji vijijini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na upatikanaji wa maji kupitia mahali ambako kuna vyanzo, naweza kukiri kwamba tunaweza kuwa tuna ugumu kidogo wa upatikanaji wa maji kwa ujumla wake, lakini pamoja na ugumu huo wa upatikanaji wa maji kwenye baadhi ya maeneo kwa kutokuwa na vyanzo, bado tumeweka viwango vya kawaida ili wananchi waweze kupata huduma. Malengo yetu ni kila mwananchi mpaka kwenye ngazi za vitongoji aweze kupata maji. Kwa sasa sera yetu inafika vijijini.
Mheshimiwa Spika, kazi kubwa inafanywa ya zile RUWASA kuainisha vyanzo na gharama ya kuanzisha miradi hiyo. lakini pia na Wizara ya Maji nayo kuwekeza kwenye mamlaka hizo ili kupata maji ya kutosha mpaka kwenye ngazi za vijiji.
Mheshimiwa Spika, natambua yako malalamiko ya bei ambayo pia hata wakati tulipokuwa kwenye ziara tumeona baadhi ya maeneo bei zinatofautiana kutoka eneo moja mpaka eneo lingine. Wizara ya Maji inaendelea na utaratibu wa kuona, je, tunaweza kuwa na kiwango kimoja nchi nzima kama vile ambavyo tumefanya kwenye REA kulipa Sh.27,000 ili mtu apate kuvutiwa maji?
Mheshimiwa Spika, kazi hiyo itakapokamilika, Wizara ya Maji itakuja hapa itatuambia sasa uvutaji wa maji kutoka kwenye chanzo au mahali ambapo unaweza kuunganisha kuleta nyumbani ni kiasi gani. Tutakapokuwa na maji mengi tutatamani sana kila mmoja avute bomba apeleke nyumbani kwake, lakini kwa sasa kwa kiwango hiki cha maji tunajenga vituo ili wananchi wote waweze kwenda hapo kwa ajili ya kupata maji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala litakapokamilika na kiwango cha maji kikipatikana kwa wingi sasa tutakuja kuweka viwango vya kila mmoja kuvuta maji kupeleka nyumbani kwake. Huo ndiyo mkakati wa Serikali kwa sasa. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, miongoni mwa ahadi zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na kupitia kauli za Mheshimiwa Rais, ni juu ya uboreshwaji wa maslahi ya wafanyakazi Tanzania. Wafanyakazi wa Tanzania wameendelea kuwa wavumilivu, wastahimilivu na wakijenga matumaini juu ya ahadi hii muhimu sana kwa maisha yao:-
Je, Serikali inatoa kauli gani, ni lini wafanyakazi wa Tanzania watapandishiwa mishahara yao na kuboreshewa maslahi yao? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib, Mbunge kutoka Pemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo dhamira na inaendelea na dhamira hiyo ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma. Tunalo eneo la mishahara, upandishaji wa madaraja na maeneo mengine pia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ilijifunza kwamba wakati wote tunapotangaza hadharani kupandishwa kwa mishahara kumekuwa kunatengeneza gharama kubwa kwenye masoko yetu na kusababisha ugumu wa maisha ya watu wengine. Unajua tunao wafanyakazi, lakini tuna wakulima, wafugaji, wavuvi; hayo ni makundi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa eneo la wafanyakazi peke yake ukitangaza hadharani kwamba tumepandisha mishahara kwenye masoko yetu, vituo vya mabasi na huduma nyingine zote zinapanda lakini wanapandisha hii kwa sababu ya maslahi ya kundi moja tu, tukiwa tuna makundi mengine hatuna forum za kupandisha maslahi yao. Kwa hiyo tumeona kwenye eneo hili tutumie njia ambayo si lazima twende hadharani, lakini tunaboresha maslahi ya wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maslahi ya wafanyakazi hayapo kwenye mishahara tu; kwa kuwapandisha daraja, tunawapandisha, kupunguza kiwango cha kodi nacho pia na namna mbalimbali za kumfanya mtumishi aweze kuboreshewa maslahi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wafanyakazi wengi wanasubiri kusikia kupanda kwa mishahara, lakini ukifanya hilo tayari unatengeneza ugumu wa maisha kwa sababu ya kupanda kwa vitu mbalimbali. Bado Serikali inaendelea kutafuta njia nzuri ya kuongeza maslahi ya mtumishi ambayo pia mengine yanakuwa zaidi hata ya mshahara.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amesema mara kadhaa kupitia sherehe za wafanyakazi kwamba kupandisha mshahara kwa Sh.20,000 au Sh.30,000 haina tija, lakini mara nyingi ukiamua kupunguza kodi ambayo mfanyakazi analipa kutoka kwenye double digit kuja kwenye single digit, hilo ongezeko linaweza kuwa kubwa zaidi kuliko hata hili la kupandisha mshahara kwa Sh.10,000 na kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bado Mheshimiwa Rais ameendelea kuahidi na Serikali hii imeendelea kuahidi kuboresha maslahi ya watumishi wa umma. Bado Serikali ipo na imeingia madarakani, tunatambua mchango mzuri sana unaotolewa na watumishi wa umma na Serikali yao inatambua na ndiyo Serikali sasa inapata mafanikio kwa sababu ya mchango wao mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nitoe wito kwa watumishi wa umma, wasikate tamaa wakidhani kutangaza mshahara hadharani ndiyo kunaweza kutatua matatizo. Muhimu zaidi kupitia Mabaraza ya Wafanyakazi ambayo tunakaa nayo mara kwa mara kujadiliana namna nzuri ya kuongeza maslahi, tunaendelea kukaa na zile taasisi/jumuiya za wafanyakazi kuweza kutafuta njia nzuri ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Kwa hiyo wafanyakazi wetu waendelee kufanya kazi, tuendelee kuiamini Serikali na tuendelee kutumia vyombo vyetu kwa maana ya jumuiya zetu za wafanyakazi ili kuendelea kuzungumza maeneo ambayo tunahitaji kuyafanyia kazi, kwa lengo la kuleta maslahi kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutokana na sera nzuri za Chama Cha Mapinduzi katika elimu, hususan elimu bila malipo na kutokana na kuongezeka kwa shule za sekondari za kata, enrollment ya wanafunzi imekuwa ni kubwa sana; na hii imesababisha kuonekana kwamba kuna upungufu mkubwa sana wa idadi ya Walimu katika halmashauri zetu. Wakati huohuo wapo zaidi ya Walimu 6,000 ambao ama wanastaafu au wengine wachache kufariki dunia, lakini Utumishi inachelewa kutoa vibali vya kuwaajiri Walimu wale:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha kwamba kasi ya ongezeko la wanafunzi inakwenda na uwiano sawa na kasi ya ongezeko la walimu? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumeanza kuona faida ya maazimio na maamuzi ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli ya elimu ya msingi ambayo inaanza kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne kwenda kusoma bila malipo yoyote na kuwa na ongezeko kubwa la vijana ambao sasa wanakwenda kusajiliwa darasa la kwanza, lakini pia hata kidato cha kwanza kwenda cha nne.
Mheshimiwa Spika, manufaa haya yanatokana na utaratibu wa awali ambao ulikuwa umezalisha michango mingi sana kwenye shule na kukwaza Watanzania kupeleka watoto wao shuleni. Sasa baada ya kuanzisha elimu bure tumeona pia hata wale watoto wanaotoka kwenye familia zisizokuwa na uwezo wanakwenda sasa shule kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kutoka elimu ya msingi mpaka sekondari yote hii tunaita elimu msingi ambayo mtoto ni lazima asome na amalize kidato cha nne na akipata ufaulu anaendelea kidato cha tano kwenye elimu ya juu ya sekondari. Hili pia limefanya kuwe na hitaji la ongezeko la walimu, miundombinu nayo lazima iongezwe na Serikali kote huko inafanya jitihada za kuongeza miundombinu kwa kuhakikisha kwamba kila tunaposajili wanafunzi darasa la kwanza wote waingie madarasani na wakae kwenye madawati.
Mheshimiwa Spika, wanapomaliza darasa la saba wanafaulu kuingia kidato cha kwanza tunahakikisha kwamba tunakuwa na miundombinu ya kutosha ili kidato cha kwanza wanapoanza shule waanze wakiwa darasani na kuendelea mpaka elimu ya kidato cha nne.
Mheshimiwa Spika, wote mnatambua tulitoa maagizo kwa wakurugenzi kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliofaulu mwaka huu wote waingie darasani na waanze kusoma. Ifikapo tarehe 28, Mwezi huu wa Februari, kila halmashauri ihakikishe imeshakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba za Walimu ili wanafunzi wanapoingia waweze kuanza masomo yao.
Mheshimiwa Spika, sasa ongezeko hili pia linataka mahitaji ya ongezeko la Walimu na Serikali inaendelea kuwaajiri. Hapa juzi kulikuwa na ajira za Walimu 13,000. Awamu ya kwanza tumepeleka Walimu 8,000, wiki mbili zilizopita tumeshasambaza Walimu 5,000 na bado tunaangalia tunapata ripoti za upungufu wa Walimu kwenye maeneo gani. Bado vibali vya ajira vitatoka na tutaendelea kuajiri kadri tunavyokuwa na uwezo wa kuajiri lakini na mahitaji pia ya elimu. Lengo ni Walimu hawa wawe na vipindi vichache, wawe na urahisi wa maandalizi ya masomo yao na waweze kufundisha na kusimamia vizuri ili kumsaidia mtoto kupata uelewa wa taaluma anayoipata kila siku mahali pa kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yake bado inaajiri na itaendelea kuajiri kuhakikisha kwamba kila shule inakuwa na Walimu wa kutosha kwa masomo yetu yaliyopo kwenye upande wa shule za msingi na sekondari vilevile. Lengo ni kuhakikisha kwamba, wanafunzi wetu wanapokwenda shuleni wakirudi jioni wawe wameshapata taaluma ya vipindi vyote ambavyo vimepangwa, tena kwa uelewa mpana kwa sababu Mwalimu anakuwa na nafasi nzuri ya kuweza kujiandaa. Huo ndiyo mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba ajira zinaendelea vizuri. (Makofi)
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunafahamu kabisa shughuli ya usafirishaji ni moja kati ya sekta zinazotoa ajira nyingi kwa vijana, hasa bodaboda. Pia kumekuwa na tabia hii ya askari wetu wa Jeshi la Polisi kuwakimbiza vijana wetu wa bodaboda pale wanapovunja sheria za barabarani, hali inayosababisha ajali na vifo kwa bodaboda pamoja na abiria:-
Je, ni lini Serikali itatoa tamko kwa Jeshi la Polisi kuhusu namna nzuri ya udhibiti wa sheria hizi badala ya mfumo huu wa kuwakimbiza ili kupunguza idadi ya ajali na vifo kwa bodaboda na abiria? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylivia, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, bodaboda ni miongoni mwa vyombo vya usafiri vinavyotumia moto, kwa maana ya mtambo ambao unatumia moto katika kuendesha chombo hicho. Vyombo vyote vya moto vimewekewa kwenye sheria katika uendeshaji wake. Kwanza kila dereva lazima awe na leseni; lakini pili, chombo hicho lazima kiwe na bima. Kwa chombo kama bodaboda dereva anatakiwa kuwa amevaa helmet ili aweze kuendesha. Hayo ni matakwa ya kisheria na wasimamizi wa sheria ni hawa makamanda wetu wa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, sasa nimemsikia Mheshimiwa Mbunge akisema wanawakimbiza, sina uhakika sana na hilo la kukimbiza, lakini yapo matukio kwa kamanda mmoja mmoja, inategemea na mazingira hayo yaliyowafikisha katika kukimbizana, lakini hakuna utaratibu wa kuwakimbiza madereva hata pale ambapo wanatenda makosa. Tumeweka utaratibu wa makamanda kufanya ukaguzi na ili ufanye ukaguzi wanatoa alama ya kumsimamisha yule dereva ili ajiridhishe kama vigezo vyote hivi ameweza kuvifikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunatambua watu wanaposimamishwa na makamanda wetu wengine wanapita. Sasa wanapopita hawa wanakuwa na mawasiliano na anapopita anajua anavunja sheria, kwa hiyo utakuta mtu anaongeza moto anakimbia akidhani anakimbizwa kumbe anakimbia mwenyewe halafu anapata ajali. Sasa hilo nalo pia halikubaliki sana kama imetokea mmoja akaamua kumkimbiza dereva, lakini muhimu zaidi tunahitaji madereva wote wanaoendesha vyombo vya moto kuzingatia sheria ambazo ziko na sisi Wabunge tumezitengeneza hapa na wasimamizi wetu ni hao askari polisi ambao ni trafiki.
Mheshimiwa Spika, muhimu zaidi tuendelee kutoa wito kwa waendesha bodaboda kuzingatia sheria. Serikali imeridhia bodaboda hii iwe chombo cha usafirishaji na ni fursa kwa vijana wetu kutumia kama sehemu ya mradi, kama biashara kusafirisha abiria hapa na pale; wazingatie sheria hizi ili wafanye kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumeweka utaratibu mzuri sana ambao hauhitaji vijana hawa wawe wanakurupushwa huko maeneo mbalimbali. Halmashauri zetu tumezipa maelekezo kuwakutanisha hawa vijana, kuwaandalia mazingira mazuri, kuwapa elimu na Jeshi la Polisi liko kulekule kwenye wilaya na lenyewe lihusike katika kuwapa elimu na kuona namna nzuri ya kuwahudumia ili wafanye kazi hiyo ya kusafirisha abiria na waendelee kupata mitaji yao.
Nimeona katika halmashauri mbalimbali kupitia Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi, wakiita vikao vya madereva bodaboda kuwaanzishia umoja wao, kuwaelimisha namna ya kuendesha biashara zao ili kuondokana na hayo malalamiko yanayojitokeza ya askari kukimbizwa. Hata hivyo, pale ambapo inatokea polisi anamkimbiza bodaboda, huo siyo utaratibu, badala yake ni muhimu kuendelea kutoa elimu. Tunatoa agizo kwa maaskari wetu kuendelea kutoa elimu kwa vijana wetu wanaofanya biashara ya bodaboda na wote wako kwenye maeneo hayo ili tuwe na uelewa wa pamoja katika kutekeleza sheria hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi likitimiza wajibu wake wa kutoa elimu na kusimamia sheria, lakini hawa kwa sababu ni wengi na wengi wanaanza kujifunza na wanaingia kwenye biashara, wakipata hiyo elimu nao wazingatie haya ili kupunguza hizo ajali. Nadhani tukifanya hilo tutafika mahali pazuri pa kila mmoja kufanya kazi yake kwa weledi mkubwa; Jeshi la Polisi lifanye kazi yake, bodaboda afanye kazi yake, kila mmoja atimize wajibu wake. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, natambua Serikali ina mamlaka ya kutoa ardhi kutoka kwa wananchi kwa ajili ya matumizi mbadala kama vile ya uwekezaji au matumizi mbalimbali kwa taasisi za umma na binafsi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, Sheria Na.4 Kifungu cha 3(i) na (g) kinatamka bayana kwamba pale mtwaaji anapochukua ardhi kutoka kwa wananchi lazima ahakikishe amefanya uthamini wa haki na ukamilifu, lakini zaidi ahakikishe analipa fidia kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na haya mazoea ya kufanya uthamini lakini inachukua muda mrefu sana kulipa fidia katika maeneo haya ambayo Watanzania wamechukuliwa ardhi zao, ili waweze kwenda sehemu zingine na kuweza kuanzisha makazi na kufanya shughuli za kijamii na uchumi:-
Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujua, ni nini hatua ya Serikali kuhakikisha kwamba pale tathmini inapofanyika basi hawa wananchi wanalipwa fidia zao kwa wakati ili waweze kwenda kuendelea na shughuli za kiuchumi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Mkoa wa Mara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunayo Sheria ya Ardhi na imetoa maelekezo kwa watumiaji wote. Kwa sera ya Serikali yetu nchini, ardhi ni mali ya Serikali na ni tofauti sana na maeneo mengine na kila mtumiaji wa ardhi hii ni lazima apate kibali, sisi tunaita hati, ile hati ni kibali cha matumizi ya ardhi ambacho kinaeleza umepewa ardhi hiyo kwa ajili ya nini? Mfano, kujenga nyumba; kiwanda au shamba, kile ni kibali cha Serikali kwa mtumiaji. Huo ndiyo utaratibu ambao tunao na ndiyo maana tunasisitiza kila aliyejenga nyumba, mwenye shamba, anataka kufanya biashara ya kiwanda, lazima apate hati, yaani apate kibali kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ardhi hii ni ya Serikali, inaweza kuwa na mahitaji ya uendelezaji kwenye eneo ambalo tayari watu wapo, wanafanya kazi zao za kilimo yaani wanaendelea na maisha yao ya kawaida. Pale ambapo tunahitaji ardhi hiyo na hapo pana watu wanafanya shughuli zao, ili kuwatoa tunafanya uthamini. Katika zoezi la uthamini ni lazima uende kujua eneo hilo la ukubwa huo ambako mwananchi huyo yupo; kama alipanda mazao; mazao yote yamewekwa bei maalum ya uthamini; lakini pia kama amejenga nyumba, inafanyiwa uthamini na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inapotaka kufanya jambo hilo, au yeyote anapotaka kutumia eneo hilo ambalo mwananchi yupo, suala la uthamini limezungumzwa pia na limesisitizwa na hili lazima lizingatiwe kwamba mtu anapotolewa eneo moja kupelekwa eneo lingine kwa lengo la kutumia eneo hilo iwe ni kwa uwekezaji au kufanya kazi nyingine, ni lazima uthamini uwepo. Najua yapo matatizo kadhaa katika maeneo mbalimbali, wengine huchukua ardhi bila fidia, wakati mwingine kunaweza kuwa na makubaliano, wakati mwingine wananchi wenyewe wanaamua kutoa ardhi ili shughuli muhimu ifanywe.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge kama analo eneo ambalo kuna malalamiko na yanahitaji wananchi wa eneo hilo kupata haki yao stahiki, bado una fursa ya kuonana na viongozi wa eneo hilo waanze utaratibu wa kwenda kufanya uthaminishaji ili wananchi wote waweze kulipwa fidia yao kulingana na ukubwa wa ardhi na thamani ya mali zilizopo.
Kwa hiyo, hili limesisitizwa na linasimamiwa maeneo yote ili kila mmoja apate haki yake kulingana na ukubwa wa eneo lililoachwa kwa ajili ya shughuli hiyo mpya. Huo ndiyo utaratibu tulionao ndani ya Serikali. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la kwanza. Tangu mwaka 2019, Serikali ilisitisha kutunga na kutoa mitihani kwa wanafunzi ambao walikuwa wanasoma masomo ya ufundi kwenye zile shule za msingi za ufundi na kusababisha miundombinu ya Serikali, vifaa vya kujifunzia, Walimu na samani nyingine ambazo zilikuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kutoa mafunzo haya ambayo ni muhimu sana. Je, Serikali ina mpango gani sasa kufufua shule hizi za msingi za ufundi ambazo pia ni mahitaji sana kwa Tanzania. Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali iliona umuhimu wa kutoa elimu ya ufundi kwa vijana wetu kuanzia umri mdogo na Serikali ikaanzisha mafunzo hayo kuanzia ngazi ya shule ya msingi. Hata hivyo, kwa kuwa tunazo shule nyingi za msingi, Serikali haikumudu kutoa vifaa vya ufundi kwa kada zote, kwa sababu ufundi upo maeneo mengi. Hapa ndipo Serikali ikaona ni muhimu kuanzisha mfumo wa kuwa na vyuo maalum vinavyoweza kuwapata vijana wale na kuwapeleka maalum kwenye chuo ambacho kimeandaliwa, kina vifaa na Walimu ili kuweza kuwapatia mafunzo na baadaye mafunzo hayo kuyaweka kwenye level ambayo pia inaweza kumsaidia kwenda kwenye level au ngazi nyingine. Kwa hiyo, Serikali iliamua kuimarisha VETA na ikaiondoa VETA kutoka Wizara ya Kazi na kuileta kuwa chini ya Wizara ya Elimu ambayo inasimamia sera ya elimu yote nchini.
Mheshimiwa Spika, VETA hiyo imeendelea kuchukua vijana wetu, mwanzo ilikuwa inachukua vijana waliomaliza kidato cha nne, lakini baadaye tukapanua wigo tukajenga vyuo kwenye ngazi ya mikoa yote nchini; ni zoezi ambalo limekamilika kwa sasa. Baadaye tukaona tupanue wigo huu tuweze kutoa fursa nyingi kwa vijana wetu na Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa VETA kila Wilaya, ni zoezi ambalo linaendelea sasa kwa lengo la kuwapatia vijana hawa fursa ya kwenda kusoma ufundi katika nyanja mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, wanaokwenda VETA ni wa kuanzia waliomaliza elimu ya msingi, kidato cha nne na kule sasa tumeweka level mbalimbali; hatua ya kwanza, ya pili, ya tatu na hatua zote wanafanya mitihani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali iliona ni busara kuanzisha vyuo maalum ambavyo tutaweza kuweka vifaa vya kutosha na Walimu wa kutosha ili kuweza kutoa elimu hiyo kwa urahisi na kwa uhakika zaidi, ndilo zoezi ambalo kwa sasa linaendelea nchini kote. Hata hivyo, tuliamua kutumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) navyo pia vikahamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii vikaletwa Wizara ya Elimu ili tuweze kusimamia sera ile ile ya kuwezesha vijana kuwa na ujuzi kuwa na utaalam kwenye sekta mbalimbali ili iweze pia kuchukua wanafunzi mbalimbali. FDCs pia inachukua hata wale ambao hawajamaliza darasa la saba wanajifunza uashi, useremala, sasa hivi TEHAMA, lakini pia ushonaji na karibu sekta zote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuuimarisha utaratibu huu na kutoa fursa zaidi kwa watoto wetu nchini kupata ujuzi mbalimbali. Programu hizi zinaendelea Wizarani hata Ofisi ya Waziri Mkuu nayo pia imeanzisha programu inayowachukua wote waliomaliza darasa la saba hata chuo kikuu kuwapa uwezo wa kufanya ujuzi. Wakimaliza kozi yao kwa muda huo waliopangiwa wanaweza kufanya shughuli nyingine za kujiajiri, wanaweza pia kuajirika na kuanzisha kazi ambazo zinaweza kuwasaidia wao ikiwemo na kilimo pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuliona kule chini uwezo wa kupeleka vifaa vyote katika kila shule ya msingi kwenye shule zetu 12,000 isingewezekana. Kwa hiyo, hivi vyuo sasa vinakuwa na nafasi nzuri na ndivyo hivyo ambavyo tunavijenga kwenye ngazi ya Wilaya. Hayo ndiyo malengo ya Serikali. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu kama yalivyo maeneo mengine duniani, tupo kwenye wimbi la Covid awamu ya tatu, natambua kazi ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwanza kutambua uwepo wa ugonjwa, lakini pili kuleta kinga ambayo mtu anaweza akaamua ajikinge ama la kutokana na uamuzi wake binafsi. Hata hivyo, bado kuna changamoto nyingi sana, wananchi wetu wengi wanakufa ama kwa kukosa maarifa ama kwa hospitali zetu kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha ama kwa Madaktari wetu na wahudumu wa afya kutokuwa motivated kwa sababu wanafanya kazi wanachoka kupita kiasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa kwa kuzingatia kwamba changamoto hii inapoteza maisha ya Watanzania wengi sana, hapa Mbunge mmoja mmoja ukimuuliza amepoteza ndugu au Wanajimbo ni wengi sana. Nataka tu nijue Serikali ina mikakati gani ya ziada kuweza kutatua ama kukabiliana na hii changamoto kwa mazingira ya ziada tofauti na mazingira yaliyopo sasa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Watanzania tunajua kwamba dunia nzima imekubwa na ugonjwa huu na toka tumeanza kuukabili ugonjwa huu, kila nchi imekuwa ikitafuta namna nzuri ya kuokoa wananchi wake kwa kuwahusisha wataalam katika kutoa elimu ya namna ya kujikinga ugonjwa huu. Nikubaliane naye kwamba tumepoteza ndugu zetu wale ambao wanapata tatizo hili na bado wapo wengine wanaugua wapo kwenye maeneo ya utolewaji huduma, lakini pia maambukizi bado yapo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nini ambacho Serikali inakifanya sasa ni kutoa elimu kwanza ya kujua namna ya kujikinga na ugonjwa huu; lakini pia kuimarisha utoaji huduma kwenye maeneo yetu yote ya kutolea huduma kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya, Hospitali za Wilaya, Mikoa; lakini pia na kupeleka madawa yale ambayo yanahusu lakini na vifaa vya kusaidia kutibu ugonjwa huu. Zoezi hili linaendelea nchini kote huku pia wataalam wetu wakiendelea kushauri namna nzuri ya kukabiliana na ugonjwa huu kwa ngazi ya Serikali na sisi pia tunatumia njia hiyo kuwahamasisha wananchi kuchukua tahadhari ili tuweze kukabiliana na ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, uzuri ugonjwa huu sasa tunashirikiana na Shirika la Afya Duniani, lakini pia tunapata uzoefu namna ambavyo wenzetu wanakabiliana nalo ili kuhakikisha kwamba kwanza tunapunguza na ikiwezekana kuondoa kabisa maambukizi; lakini mbili wale ambao wanapata tatizo wanahudumiwa vizuri kwenye hospitali zetu; na kuhakikisha kwamba nchi hii haiendelei kupata ugonjwa huu na kuusambaza maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, inawezekana pia kwamba hatua hii bado sio sahihi sana au haitoshelezi mahitaji ya kukabiliana na ugonjwa huu, bado Serikali inaendelea kushirikisha wataalam wetu wa ndani kutafuta mbinu mbalimbali, lakini pia tunahamasisha pia hata tiba za asili kama nazo zinasaidia. Tumewahi kufanya hayo na tumefanikiwa, lakini sisi tunaendelea pia kumwamini Mwenyezi Mungu, tunaomba na dua pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunajaribu kutafuta mbinu zote, tunajitahidi kutafuta mbinu zote ili mradi tunakabiliana na hili. Tunaendelea kuhamasisha wananchi wetu pia kushiriki kikamilifu katika namna yote inayoweza kusaidia kupunguza maambukizi kama hivyo kuvaa barakoa pale ambapo unaona upo eneo hatarishi lakini pia kutumia vitakasa mikono, maji tiririka pamoja na sabuni; ni mambo ambayo tunahamasisha.
Mheshimiwa Spika, Madaktari wameenda mbali zaidi wanatuhamasisha lishe bora ambayo itatusaidia kuongeza virutubisho mwilini na kufanya mazoezi, kuuweka mwili imara kwa wale ambao wana uwezo wa kimwili. Kwa hiyo, tunajitahidi kutafuta mbinu mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huu.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Watanzania tuendelee kushiriki pamoja katika kupambana na ugonjwa huu. Tumeona nchi mbalimbali nazo pia zinachanja na tumeona pia kuna umuhimu wa kuchanja kwa sababu chanjo inaimarisha pia kuweka virutubisho ndani ya mwili. Najua, kuna vipingamizi, watu wengine wanapinga lakini ni kwa kutoelewa na wale ambao wanapinga ni wale tu ambao hawajaguswa na tatizo hili ndani ya familia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, viongozi wa nchi hii toka ugonjwa huu ulipoingia walieleza wazi kabisa kwa Watanzania kwamba huu ugonjwa ni hatari, lakini mbinu mbalimbali zinatumika, Madaktari wanashauri pamoja na chanjo lakini tutajiridhisha kila aina ya tiba ili na sisi tuweze kuingia hapo. Nataka niwaambie Watanzania tumetumia Madaktari/ wataalam wetu wa ndani kwenda kufanya uchunguzi wa aina hizi za chanjo kama zinafaa na sisi pia kushiriki na wamefanya hivyo, wameshiriki na tuliowatumia hawa ni Madaktari ambao ni ndugu zetu, kaka zetu, dada zetu ambao wamebobea kwenye Sekta ya Afya na wanaaminika pia hata huko nje. Kwa kweli ushauri wao na sisi tumejiridhisha kwa sababu hatuamini kwamba Daktari huyu Mtanzania aliyezaliwa hapa. ana ndugu kaka, dada akamshauri achanje chanjo ambayo itakuja kumpotezea maisha yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile wote mnajua kiongozi wa nchi, Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametangulia mbele, pamoja na nyadhifa alizonazo, dhamana aliyoibeba katika nchi hii ya kuwalinda na kuwahifadhi Watanzania yeye amekuwa mstari wa mbele kuchanja na kutuhamasisha tuchanje, lakini amesema chanjo sio lazima lakini ni muhimu. Chanjo sio lazima lakini muhimu kwa sababu inaongeza kinga mwilini. Kwa hiyo, Watanzania tumeanza kuona wanajitokeza na niendelee kuwahamasisha Watanzania wajitokeze kwenda kuchanja ili tuweze kujikinga. Hizi zote ni njia za kupambana na ugonjwa huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote kwamba Serikali tutaendelea kushirikiana na Mataifa ambayo tunajua yana nia njema na sisi na yanatumia njia mbalimbali katika kujikinga, lakini pia kwa kuwatumia wataalam wetu kujiridhisha na hatua hizo kama zinafaa na sisi pia kushiriki kwa namna hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwa na usumbufu mkubwa katika mafao ya watumishi mara wanapostaafu, kukiambatana na kuchukua muda mrefu. Je, ni nini tamko la Serikali juu ya kuwawezesha hawa wastaafu wetu ambao wamelitumikia Taifa kwa juhudi kupata mafao yao kwa wakati?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala la mafao ya wafanyakazi nataka niwahakikishe wafanyakazi tumeendelea kuliratibu ndani ya Serikali kupitia Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii na wote mnatambua tulikuwa na Mifuko mingi ikaleta usumbufu mkubwa sana. Nini tumekifanya? Tumekusanya Mifuko yote ya Hifadhi tumeunda Mfuko mmoja PSSSF ambao upo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mfuko huu umeendelea kuratibu kwanza idadi ya wafanyakazi wote waliokuwa wanalipwa na mifuko ile mbalimbali na kuweka utaratibu wa wale waliostaafu ambao walikuwa hawajalipwa kuanza kuwalipa na wale ambao wanastaafu kuendelea kadiri tunavyopata fedha na wale ambao watastaafu siku za karibuni wote wanaratibiwa vizuri ili tuondoe usumbufu uliokuwepo.
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba bado kuna wachache hawajapata mafao yao kwa muda, lakini Serikali inaendelea kulipa wastaafu kadri inavyoweza kupata fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siku za karibuni hapa nilikuwa nazungumza na wafanyakazi wa TALGWU, wa Serikali za Mitaa na hiyo ilikuwa ni moja kati ya jambo ambalo wao walitaka kulijua na mimi niliwahakikishia kwamba Serikali inaendelea na mwezi wa Nne tumelipa zaidi ya bilioni 172 wastaafu na tunaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwalipa wastaafu. Pia Mfuko huu umerahisisha namna ya wafanyakazi waliostaafu kuufikia; tumefungua Ofisi ya PSSSF kila Mkoa ili wastaafu waweze kufika pale mkoani.
Mheshimiwa Spika, tumeanzisha pia mfumo wa kielekroniki wa mawasiliano kati ya wastaafu na makao makuu. Kwa hiyo, mstaafu huko alipo anaweza kuwasiliana na makao makuu kupata taarifa mbalimbali. Tutaimarisha elimu kwenye hili ili kila anayestaafu aweze kujua na aweze kulipa kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, huo ndio mkakati ambao tunaendelea nao, tunajitahidi sana na narudia tena tunatambua kwamba wapo wastaafu ambao bado hawajafikiwa kulipwa fedha zao, lakini nataka niwahakikishie tutawalipa haki yao. Huo ndio msisitizo ambao tumewasisitiza waajiri watunze kumbukumbu za watumishi wao kutoka wanapowaajiri mpaka wanapomaliza ajira zao.
Mheshimiwa Spika, huu Mfuko tumeendelea kuusimamia hata Waziri wa Nchi wiki moja iliyopita amekaa kikao na wale watumishi wa Mfuko ule kwa kujiridhisha kama je mambo yanaenda sawasawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea kulipa mafao tunatambua wengine bado hawajalipwa lakini tutawalipa. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kuwahakikishia wastaafu kwamba kila aliyestaafu atalipwa fedha yake ya mizigo kurudi nyumbani na vile vile ile pensheni ambayo ilipaswa kulipwa wakati wote anapokuwa kwenye ustaafu. Hayo ndio malengo ya Serikali. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya mikoa hapa nchini hasa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wanategemea zao la mahindi kama chanzo kikuu cha mapato. Hata hivyo, kwa miaka mitatu mfululizo zao hili limekumbwa na mdororo wa bei na masoko.
Je, Serikali mmejipanga vipi kuiwezesha Taasisi za Serikali hasa NFRA ili waweze kupunguza mlundikano wa mahindi huko sehemu zenye shida?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mikoa yetu ile saba/nane ya Nyanda za Juu Kusini inazalisha sana zao la mahindi na ndiyo tunalitegemea kwa chakula hapa nchini. Pia mwaka huu, msimu uliopita wamezalisha na ziada; na biashara ya mahindi haijaenda vizuri msimu huu kwa sababu bei imeshuka sana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ruhusa iliyotolewa na Wizara ya Kilimo ya kuruhusu watu watafute masoko popote ndani na nje ya nchi, lakini bado uzalishaji ni mkubwa sana kwa sababu pia hata hizo nchi za jirani nazo zimezalisha pia zao hili.
Mheshimiwa Spika, tulichokifanya ni kuimarisha kuboresha Hifadhi yetu ya Taifa (NFRA) ambapo sasa tumeipa fedha za kwenda kununua angalau kwa bei inayoweza kumkidhi mkulima kujiandaa kwa msimu ujao. Uwezo siyo mkubwa sana lakini tumetoa fedha. Hata juzi wamepewa tena fedha zaidi ya shilingi bilioni 15 ili waende kwenye mikoa ile kwa ajili ya ununuzi huo.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa Mkoani Katavi siku nne zilizopita, hilo nimelisikia na nimeshuhudia mlundikano wa mahindi kule. Nilikutana pia na watu wa NFRA kuona kama je, ununuzi wao pale upo na wananunua kwa kiasi gani? Bado uwezo wa kununua ni mdogo, lakini Serikali itaendelea kuwapa fedha kadiri siku zinavyokwenda ili pia waweze kununua. Pamoja na malalamiko ya wananchi wa Mkoa wa Katavi ambayo waliniambia kwamba kituo cha kununulia kipo mbali, sasa tumeamua angalau tupeleke kwenye kila Halmashauri kituo kimoja ili kiweze kukusanya mahindi kwa ukaribu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hili tutajitahidi. Tunajua Mkoa wa Ruvuma, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na Mikoa ya Iringa na sasa Tabora kidogo inazalisha sana. Kwa hiyo, tutajitahidi kukusanya mahindi hayo kupitia NFRA pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo pia tumeipa dhamana ya kununua, nao wanasaga wenyewe kupitia vinu vyao. Kwa hiyo, mashirika yetu haya mawili au taasisi hizi mbili tunazipa fedha halafu zinakwenda kununua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, na Waheshimiwa Wabunge wote mnaotoka kwenye mikoa inayozalisha sana zao la mahindi, Serikali inaendelea kuwawezesha NFRA pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kwenda kununua mahindi kwa kiwango hicho. Najua mahindi ni mengi, lakini bado tumefungua milango, yeyote ambaye anaona soko lipo Zambia, Congo, Burundi, Rwanda, Kenya na maeneo mengine kama Malawi na Msumbiji, aende. Bado ruhusa imetolewa ili mradi unaripoti kwamba nina tani hizi, nazipeleka Zambia ili viongozi wa eneo lile waratibu tuweze kujua tumeweza kuingiza fedha kiasi gani za kigeni kwa mazao yetu kupelekwa huko nje?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hiyo ndiyo taarifa ambayo kwa sasa tunayo na Wizara inaendelea na uratibu wa taasisi hizi mbili kununua mahindi kwenye maeneo hayo. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nimepata nafasi ya kuuliza swali.
Mheshimiwa Spika, maeneo makubwa sana hasa yaliyomilikiwa na makanisa zaidi ya miaka 50 walishindwa kuyaendeleza na wananchi wakaingia kufanya shughuli za kilimo. Kwa sasa wameanza kuwaondoa wananchi hao ambao wamelima zaidi ya miaka 50. Serikali itasaidia nini wananchi hawa waweze japo basi kugaiwa kidogo waweze kuendeleza shughuli zao za kilimo maana kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi mahali hapo? Ahsante. (Makofi)
SPIKA: Unaweza ukatoa mfano?
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ndiyo. Pia Waziri Mkuu alifika eneo la Ilolo Katika Kata ya Kiwira, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, anafahamu tulilizungumzia suala hilo.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba taasisi zetu za kidini nyingi ziliweza kumudu kuchukua maeneo makubwa sana kwa ajili ya kujenga nyumba zetu za ibada kwenye maeneo hayo. Maeneo kama haya wamemudu kujenga eneo dogo na maeneo makubwa yamebaki, tukiwa tunazungukwa na vijiji na wananchi wanahitaji kutumia na maeneo mengi pia wananchi wameingia humo kutumia.
Mheshimiwa Spika, bado hatuwezi kuacha kufuata Kanuni za Ardhi kwamba unapokuwa na ardhi lazima upate Hati, unapokuwa na Hati unakuwa na kibali cha umiliki wa eneo hilo. Yeyote ambaye atakuja hawezi kupata hati nyingine juu ya hati; na kama atafanya kazi hapo, ajue kwamba eneo hilo siyo lake, bali ni la yule mwenye hati.
Mheshimiwa Spika, mgogoro mkubwa uliokuwepo kwenye maeneo mengi ni huo ukubwa wake na matamanio ya watu kuingia. Mbali ya ziara yangu niliyofanya Mkoani Mbeya Kiwira, lakini nilikuwa Dar es Salaam eneo la Temeke, kuna Kanisa huko la Anglikana, lina eneo kubwa kabisa, Halmashauri wamehangaika kutafuta eneo la kujenga kituo cha mabasi hawana, wameenda.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme, kwanza zipo Taasisi za Kidini zinatambua mahitaji ya ardhi kwa wananchi wanaowazunguka na wanachofanya wanapima uwezo wao hata wa kuendeleza wanawagawia wananchi kidogo kidogo na wanawapa vibali vya muda lakini pia baadaye huko tunaona nia thabiti ya baadhi ya Taasisi za Kidini zikiruhusu wananchi kuwakatia eneo hilo na wapate Hati na kuwaachia kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, yapo maeneo yanamilikiwa bado na taasisi hizo. Wizara ya Ardhi inayo Sera yake ya maeneo haya, namna ya kuishi na hawa watu, lakini kutambua kwamba sasa hivi tuna ongezeko kubwa la wananchi na wanahitaji kupata huduma ya maeneo ya kilimo ili waweze kujikimu.
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kufuatilia mwenendo wa sheria zetu, tunaendelea kushauri wale waliochukua maeneo makubwa wapunguze maeneo hayo ili tuwaruhusu wananchi; na kwa busara za viongozi wetu wa kidini, wanakubali, wanatoa maeneo yale na kuwaruhusu wananchi waweze kulima na baadaye pia hata kurasimisha wao waweze kuchukua maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ambacho tunakifanya sasa ni Mamlaka zetu za Mitaa kule Halmashauri, wanakaa na hao ambao wamechukua maeneo makubwa na hayatumiki kwa miaka mingi ili wakubali kuyaachia na jamii iweze kunufaika. Kwa hiyo, tunaendelea kuzungumza nao ili waweze kuachia, lakini pale ambapo tutakuja kuimarisha na kusimamia sheria zetu, tutakuja kuimarisha, lakini kwanza kwa haki yake ya msingi aliyonayo, basi lazima kwanza tushauriane naye ili apunguze maeneo na hiyo inatokea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuzungumza na wenye maeneo makubwa, hasa Taasisi za Kidini lakini kwa hao wengine ambao waliita ni wawekezaji, tukakubaliana kwamba katika kipindi fulani atakuwa ameshalima, ameendeleza na hajafanya hivyo kwa miaka mingi, hao sasa Mheshimiwa Rais anatumia nafasi yake kuchukua ardhi hiyo na kuwagawia wananchi ili waweze kutumia kwa manufaa yao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea na busara zote mbili hasa kwenye maeneo ya kidini kuweza kushauriana nao viongozi wa kidini na kwa bahati nzuri wanatuelewa. Kwa hiyo, huo ndiyo utaratibu ambao tunautumia kwa sasa. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa hii nafasi, naomba kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, ipo tabia ambayo imezoeleka na sasa hivi imeota mizizi ndani ya Jimbo la Momba ambapo watu wanawakata watu mapanga kutokana na imani za kishirikina pamoja na baadhi ya migogoro ya ardhi. Katika kipindi cha miezi mitatu ambayo tulikaa hapa Bungeni kwenye Bunge la Bajeti zaidi ya watu watano waliuliwa; na siku nne zilizopita Diwani Mstaafu wa Kata ya Kapele ameuliwa kwa kitendo hicho hicho:-
Mheshimiwa Spika, ni nini tamko la Serikali ili kutusaidia kudhibiti tabia hii, ikiwezekana kuiondoa kabisa ili wananchi wa Jimbo la Momba tuweze kuishi kwa amani, upendo na mshikamano ili tuweze kujenga nchi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunayo migogoro ya jamii zetu kwenye ardhi kati ya jamii moja na nyingine, tuna migogoro ya jamii hasa walio kwenye mipaka ya hifadhi zetu, kati ya wahifadhi na wananchi, na pia kuna hiyo migogoro ya imani za kishirikina ambayo ipo sana katika jamii mbalimbali. Sasa sisi kama Serikali moja ni kusimamia; kwanza kutoa wito kwa Watanzania kuhakikisha kwamba nchi hii inabaki kuwa ya amani na utulivu na kwamba kila mmoja lazima azingatie sheria na kuzuia sana watu kuchukua hatua au sheria mkononi na kufanya mauaji.
Mheshimiwa Spika, sisi bado tunasimamia sheria. Pale ambapo linajitokeza tatizo la namna hiyo na mtu ameamua kuchukua sheria mkononi, naye tunamtia hatiani. Bado kutumia viongozi tuliowaweka kwenye maeneo hayo; Watendaji wa Vijiji kwenye ngazi ya Vijiji, Watendaji wa Kata kwenye ngazi ya Halmashauri na Wakuu wa Wilaya. Mkuu wa Wilaya ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Ugawaji Ardhi kwenye Wilaya ile na anashirikiana na Halmashauri. Wao wameendelea kuelimisha jamii umuhimu wa kila mmoja kuzingatia sheria pale anapohitaji ardhi. Hata kama pale una ardhi halafu mwingine anaingilia, ni lazima ufuate mkondo katika kutatua migogoro.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nini Serikali inakifanya sasa? Kwanza kusimamia sheria ambazo zinagusa maeneo yote ikiwemo ya ulinzi na usalama, kuhakikisha kwamba hakuna mtu anachukua hatua kwa maamuzi yake; na kama itatokea tatizo, basi hatua thabiti ya kupeleka kwenye vyombo vya sheria, hiyo lazima izingatiwe.
Mheshimiwa Spika, pili, tunaendelea kufanya marekebisho kadhaa ya migogoro hii ya ardhi kati ya mtu mmoja na mwingine, kati ya jamii na maeneo haya ambayo yamehifadhiwa ili kufanya jamii inayozunguka maeneo hayo, jamii ambazo zinashirikiana katika kufanya kazi zao kila siku ziweze kuishi kwa amani. Hatua hii ndiyo inasaidia maeneo mengi sasa hivi kuwa tulivu na migogoro yote imeendelea kuratibiwa kwa kuunda Mabaraza ya Ardhi kwenye ngazi za Wilaya, Mikoa ili pale unapopata tatizo, kila mmoja aende kwenye chombo cha sheria. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kuondoa migogoro hii.
Mheshimiwa Spika, huo ndiyo utaratibu ambao kwa sasa tunausimamia kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kufanya eneo hili kuwa la utulivu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami naomba kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kumekuwa na ucheleweshwaji mkubwa sana wa vitambulisho vya Taifa kwa baadhi ya maeneo ya nchi yetu; na jambo hili limekuwa likitokana na kutokuwepo na mtiririko mzuri unaoridhisha wa taarifa za wananchi:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunganisha Taasisi ya Serikali ya RITA, NIDA na labda Uhamiaji kidigitali ili mtoto anapozaliwa taarifa zake zianze kutunzwa na kupatiwa kitambulisho kimoja cha Taifa kitakachotumika kama cha kuzaliwa na cha Taifa? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza ameeleza usumbufu wa upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa na pia ametaka kujua kama je, tunaweza kuunganisha NIDA na RITA au Uhamiaji ili kurahisisha kuwa na chombo kimoja chenye taarifa zote?
Mheshimiwa Spika, hivi vyombo vyote vina majukumu tofauti. NIDA wanatoa Kitambulisho cha Taifa ambacho ndiyo kinachomtambulisha Mtanzania kuwa huyu ni Mtanzania. Kitambulisho hiki hakitolewi kwa yeyote ambaye sio Mtanzania. Suala la Kitambulisho hiki cha Utanzania kinaangalia mambo mengi sana hasa maslahi ya Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, RITA ni chombo kinachotoa cheti cha kuzaliwa kwamba wewe umezaliwa tarehe na eneo fulani. RITA hiyo hiyo kazi yake ni kusajili vifo. Unaweza kuzaliwa leo; wale wana utaratibu wa kuweka takwimu za waliozaliwa Tanzania, lakini pia wanatoa na vyeti vya vifo kama mtu akifariki. Kama ulisajiliwa kuzaliwa na huku umepata cheti cha kifo, maana yake wanaondoa ile, maana yake unakuwa haupo kwenye takwimu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, chombo hiki cha RITA kinaweza kutoa vitambulisho cha kuzaliwa hata kama siyo Mtanzania. Hilo nalo pia lijulikane kwamba RITA inaweza kutoa vitambulisho kwa yoyote anayezaliwa Tanzania hata kama sio Mtanzania, lakini Kitambulisho cha Taifa, hiki ni kwa ajili ya Mtanzania tu. Kwa hiyo, hayo ndiyo majukumu tofauti.
Mheshimiwa Spika, Jeshi la Uhamiaji ni katika kutoa vibali vya kuingia na kutoka nchini na majukumu kadhaa ambayo wamepewa. Sasa kuunganisha kwa wakati mmoja, yapo maeneo huwezi kuunganisha kama ambavyo tunafikiria, lakini wanaweza kupeana taarifa pale ambapo chombo kimoja kinahitaji taarifa upande wa pili. Hiyo inawezekana pia. Kwa hiyo, vyombo hivi viwili vinafanya kazi kwa utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, usumbufu ambao unazungumzwa hapa, nilipokuwa nafanya ziara hasa kwenye Mikoa ya pembezoni; nimefanya ziara Mkoani Kagera, Kigoma na Mtwara. Mikoa yote hii inapakana na nchi jirani na tumeanza kuona pia wimbi la wenzetu kutoka jirani kupenda kuishi Tanzania na wangependa kupata Kitambulisho cha Taifa.
Mheshimiwa Spika, haiwezekani kwa sababu wao sio Watanzania, lakini akiwa hapa hata kama ameingia kwa kutoroka na amekaa hapa na mke wake ana miezi, miaka akazaa mtoto, kitambulisho cha kuzaliwa anachokipata kwenye hospitali zetu pale alipozalia, siyo cha Utaifa. Kitambulisho cha NIDA ni cha Utaifa zaidi kuliko kuzaliwa. Kwa hiyo, huo ndiyo utofauti wa vyombo hivi.
Mheshimiwa Spika, sasa kwenye mikoa hii niliyopita, upo urasimu unazungumzwa kwamba wanachelewa sana kutoa vitambulisho vya NIDA. Ni kweli kwa sababu utoaji wa Kitambulisho cha Utaifa, hii inajikita zaidi kwenye usalama wa nchi. Huwezi kumtambua yeyote anayekuja hapa nchini bila kujiridhisha kwamba ni Mtanzania ukampa Kitambulisho cha Utaifa bila kujua kama yeye ni Mtanzania au la.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuchelewa kwetu kwenye mikoa ya pembezoni ambako kunaitwa kama urasimu, sisi tumeweka utaratibu mzuri wa kufanya questionnaire au maswali yanayoweza kubainisha kama huyu ni Mtanzania au sio Mtanzania? Kwa hiyo, lazima kutakuwa kuna kuchelewa kidogo. Kama kuna urasimu, ni wa aina hiyo, wa kujiridhisha kama je, huyu aliyeomba ni Mtanzania au ni mtu kutoka nje? Maamuzi yafanyike. Kwa hiyo, huo siyo urasimu, bali ni kuhakiki kwa kina ili cheti cha NIDA kitolewe kwa Watanzania tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimepata nafasi ya kuwaeleza wananchi kwenye maeneo hayo na kuwataka wafanye Subira. Acha chombo chetu cha NIDA kijiridhishe kama huyu ni Mtanzania au la. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie tu kwamba yeyote Mtanzania mwenye baba na mama Mtanzania atappata Kitambulisho cha Utanzania. Kwa hiyo, nao waendelee kuwa na subira ili wataalam wetu wajiridhishe. Huku tumejaribu kurahisisha kidogo, tumeongeza mitambo ya uchapishaji wa vitambulisho, tumeongeza pia mfumo wa vitambulisho kufika mpaka vijijini, tumeongeza idadi ya wafanyakazi kwenye NIDA ili kurahisisha upatikanaji hasa wale ambao tayari wamehakikiwa na wanapaswa kupata kitambulisho. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali ambalo limejikita kwenye usalama. Siku za karibuni hapa nchini kumekuwa na changamoto ya wimbi la ujambazi ambalo linaendelea hasahasa Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Arusha kitu ambacho kimekuwa kikihatarisha usalama wa wafanyabiashara wetu lakini mali pamoja na usalama wa wananchi wetu. Je, ipi ni kauli na maelekezo ya Serikali dhidi ya hivi vitendo viovu ambavyo vinaendelea kwenye Taifa letu?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Sanga kwa swali hili zuri na muhimu kwa usalama wa nchi yetu. Serikali inao wajibu wa kulinda raia wake kwa usalama wao, mali zao lakini pia kuhakikisha kwamba wanaendesha shughuli zao za kila siku kwa amani na utulivu. Kazi hii inafanywa vizuri na vyombo vyetu vya dola lakini pia kazi hii mara kadhaa tumewaomba Watanzania kushiriki kwenye ulinzi wa nchi yetu pale kila Mtanzania anapopaswa kujilinda yeye mwenyewe, jamii inayomzunguka na hatimaye jamii kubwa kwa ukubwa wake ili kujiridhisha kuwa usalama wa nchi unakuwa imara.
Mheshimiwa Spika, Jeshi letu la Polisi linafanya kazi nzuri sana na siku mbili/tatu hizi nimesikia kazi nzuri wameifanya Jijini Dar es Salaam na Watanzania wote wamesikia na wameona kazi ambayo wameifanya kudhibiti majambazi hawa. Nataka nikuhakikishie kwamba Serikali inaendelea na kazi hiyo ya kuhakikisha kwamba usalama wa raia na mali zao unaendelea. Watanzania wote wanajua kwamba hata Mheshimiwa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia moja ya hotuba zake Kitaifa ameweza kuwaonya wale wote wanaofikiria kwamba huu ni wakati wa kufanya maovu nchini na amewataka wale ambao walikuwa wanafikiria kufanya hivyo waache mara moja. Anapoagiza haya maana yake anaagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote ambao wanasababisha madhara ya usalama kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunashiriki kikamilifu kwenye ulinzi wa nchi na kila Mtanzania pale anapohisi/anapoona kwamba kuna dalili za upotevu wa amani ni vyema kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria ili hatua kali ziweze kuchukuliwa. Kwa hiyo, bado tunaendelea na jukumu hilo la kulinda nchi, watu wake, mali zao na usalama wao ili nchi hii iendelee kuwa na tunu yake ya amani wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwasihi Watanzania sasa kuhakikisha kuwa tunatoa taarifa pale ambapo tunaona kwamba kuna tatizo linaloweza kutokea mahali ili majeshi yetu yafanye kazi inayokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitenga mazao ya kimkakati na miongoni mwa mazao haya kahawa ni mojawapo. Hata hivyo, zao hili ambalo ni muhimu limekuwa na changamoto ya kukosa soko la uhakika, wananchi kucheleweshewa malipo pale wanapouza kahawa lakini pia wananchi kukosa pesa ya kuwasaidia pale wanapokuwa wanaelekea kuvuna. Nini kauli ya Serikali juu ya changamoto hizi ambazo zinamfanya mwananchi kukata tamaa juu ya zao hili muhimu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imedhamiria kusimamia kilimo kwa ujumla wake kwa mazao ya chakula pamoja na ya biashara. Haya mazao ya kibiashara usimamizi wake ni kuhakikisha kwamba kuanzia kilimo hiki kinapoanza kwa kuandaa shamba mpaka mavuno na hatimaye masoko yanaratibiwa vizuri. Tumejitahidi sana kufanya hivyo wakati wote ili kuhakikisha tunaleta tija kwa mkulima anayeshiriki kilimo kila siku kwenye zao ambalo linalimwa kwenye eneo lake kulingana na jiografia yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kahawa ni miongoni mwa mazao tena ni mazao ya kimkakati ambayo yanalimwa na jamii pana. Kwa hiyo, Serikali tumehakikisha kwamba zao hili nalo tunalisimamia.
Mheshimiwa Spika, zao hili kwenye masoko tunaliuza kwenye mfumo wa mnada kupitia Ushirika. Zao hili pia kwenye maeneo yote yanayolima ikiwemo na kule Kyerwa, Karagwe na maeneo mengine ya Mkoa wa Kagera lakini pia kule Ruvuma maeneo ya Mbinga, Kilimanjaro, Arusha tunaona Tarime kule Mkoani Mara zao hili linaleta manufaa sana kwa wakulima. Tunaendelea kuratibu masoko yake na kama ambavyo Wizara ya Kilimo ilivyomaliza bajeti yake juzi na kutoa maelezo bayana ya kuimarisha masoko, bado nataka niwahakikishie wakulima wa kahawa tunaendelea kusimamia Ushirika, tutaendelea kusimamia masoko yake na pale ambapo masoko haya yanaleta tija tutahakikisha mkulima analipwa kwa wakati ili aweze kupata fedha ajipange tena kwa kilimo msimu ujao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Bilakwate kwa sababu hata wakati wa Bajeti ya Kilimo hapa alisimama kueleza haya na Wizara ikamjibu. Wizara ilipokuwa inamjibu yeye maana yake ilikuwa inajibu wananchi wanaolima kahawa wakiwemo wale wa kule Kyerwa. Kwa hiyo, niwahakikishie wakulima wote kwa mazao yote ikiwemo kahawa kwamba Serikali itaendelea kusimamia bei nzuri ya mazao haya lakini pia tutahakikisha baada ya kuuzwa fedha za mkulima zinalipwa katika kipindi kifupi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuhuisha sheria na mifumo na zile Kanuni za kutoka siku ya mnada na kipindi cha kulipwa na hatimaye fedha kumfikia mkulima. Tukishafanikiwa hapo kila mmoja atafarijika kuendelea na kilimo hiki wakati wote.
Mheshimiwa Spika, nataka nisisitize tu kwamba pamoja na kuleta masoko yaliyo bora, malengo yetu hasa ni kuanzisha viwanda vya ndani ili zao hili liweze kuongezwa ubora na ubora ule ndio utakaoleta masoko. Pia zao hili mnada wake ulikuwa Moshi pekee kwa hiyo utamuona mwananchi wa kule Kyerwa, Mbinga hata waliopo kule Mbozi wanapeleka kahawa Moshi. Tumeamua sasa kuweka vituo vya karibu na wakulima hukohuko walipo ili minada hii ifanywe huko walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumefungua kituo cha mnada wa kahawa Kagera, Makambako pamoja na Mbozi ili wale wanaolima mikoa ya jirani kwenye maeneo haya waende kwenye minada ile. Minada hii itakuwa ya wazi, mtu yeyote aliyepo ndani na nje ya nchi anakaribishwa kuja kununua. Kahawa ya Tanzania ni nzuri sana na ina thamani kubwa, kwa hiyo, tunawashawishi wanunuzi wote wa kahawa kuitumia kahawa ya Tanzania ikiwemo kahawa inayolimwa kule Mkoani Kagera kwenye Wilaya ya Kyerwa na Karagwe kwa ujirani.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nimuulize Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa kuna ugumu wa kupata ajira kwa vijana hasa waliomaliza darasa la saba kwenye taasisi za Serikali hata kama wamepata mafunzo katika fani mbalimbali kwenye vyuo vyetu vya ufundi hata vinavyotambuliwa na Serikali kwa kigezo cha cheti cha form four. Vyuo hivi vinatambuliwa na NACTE na Serikali kwa ujumla, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba ina-recognize vijana wetu hawa wa standard seven ambao wanaulizwa kigezo cha form four wakati wamepatiwa mafunzo na wana uwezo wa kufanya kazi hizo? Serikali ina mkakati gani kuwatambua na kuhakikisha kwamba inawasaidia?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat, Mbunge kutoka Mkoa wa Singida, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya kawaida ni kweli upo ugumu wa upatikanaji ajira na changamoto ya ajira iko duniani kote ikiwemo na hapa kwetu Tanzania lakini kila Serikali inaweka utaratibu mzuri wa kukabiliana na changamoto hii. Kwetu nchini Tanzania kupitia Serikali yetu inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendeleza mkakati wa Awamu ya Tano wa kupanua wigo ambao unaruhusu Watanzania kupata ajira bila ya kuangalia elimu yao; muhimu ni ujuzi na hasa anapozungumzia wale wamepata ujuzi kwenye vyetu vya ufundi vinavyotambulika na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa ujenzi wa viwanda ndiyo jibu sahihi la kupunguza changamoto hii ya ajira kwa ngazi zote; uwe umemaliza darasa la saba, kidato cha nne, una degree hata ukiwa Profesa unaweza kufanya kazi kwenye viwanda kwa sababu kazi za kufanya zipo nyingi. Kwa hiyo, mkakati wetu wa ujenzi wa viwanda ni miongoni mwa njia moja muhimu ya kuwezesha kupata ajira watu wa kada zote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mbili; tunaendelea pia kuimarisha vyuo vyetu vinavyotoa ufundi stadi kwa sababu unaposoma kwenye vyuo vya ufundi stadi unapata ujuzi, ukipata ujuzi unaweza kujiajiri, unaweza pia ukaanzisha taasisi ukawaajiri wenzako na kuajirika pia kwenye sekta nyingine. Nataka niwaongezee kuwajulisha kwamba hata Ofisi ya Waziri Mkuu tunao mkakati wa kutoa mafunzo ya watu wa ngazi zote ili waweze kupata ujuzi huo wapate nafasi ya kujiajiri, kuajiriwa lakini pia na wale wanaopata ujuzi wakaanzisha kampuni yao na kuweza kuwaajiri wengine; kwa utaratibu huu tumefanikiwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika miaka mitatu iliyopita tuliwahi kukusanya vijana wa taaluma mbalimbali zaidi ya 35,000 tukawapeleka kwenye sekta mbalimbali; kilimo, madini lakini pia utoaji huduma na maeneo mengine, tumewapeleka VETA na Chuo cha Don Bosco, tumewapeleka kwenye mahoteli na maeneo mbalimbali ya utoaji huduma. Wanapokuwa kule asilimia 40 ya muda ni nadharia, asilimia 60 ya muda wao unatumika kwa ajili ya vitendo. Wanapokamilisha mafunzo hayo ya miezi sita wanakuwa tayari wana ujuzi na wengi wamepata mafanikio wameajiriwa na wengine wamejiajiri. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati ambao Serikali inautumia ili kuwezesha kila mmoja kwa ngazi yake kuweza kupata ajira.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya mbegu ya hybrid kwa mazao kama mahindi, maharage, mchele na mengine mengi yamefanya mazao hayo kupoteza ladha lakini pia yanahitaji matumizi makubwa ya mbolea na viuatilifu. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inawekeza katika uzalishaji wa mbegu za asili kibiashara ili kuwawezesha wakulima kuzinunua lakini pia kufanya kilimo cha gharama nafuu na ku-maintain afya za Watanzania?
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu, Mbunge kutoka Mkoa wa Pwani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli ameeleza kwamba yapo baadhi ya mazao ambayo tunatumia mbegu zile tunaita hybrid, zile mbegu ambazo zinakuzwa kwa kutumia madawa ambazo mazao yake yanaweza kuwa yanapoteza ladha kama ambavyo amesema. Hata hivyo, sisi ndani ya Serikali yetu kupitia Wizara ya Kilimo tumeweka Sera ya kuimarisha vitengo vyetu vinavyozalisha mbegu hizi ambazo ni za asili ambazo pia zinaweza zikazalisha kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunavyo vyuo vya utafiti vinaendelea na tafiti mbalimbali kwa mbegu hizi zinazozalishwa na kuona kuwa tunazalisha kwa kiasi kikubwa tuweze kukipeleka kwa wananchi. Pia tumehakikisha kwamba kila tunapolima zao hilo ambalo limetokana na mbegu hizi ambazo tumezitafiti na tumezilima kutokana na uasili wetu, tunatenga kiasi cha mbegu ambacho kitasaidia kulima pia msimu ujao. Tumefanya hivyo kwenye zao la pamba, korosho na mazao ya mahindi na mpunga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tusingependa sana kuingiza mbegu hizi ambazo zimekuzwa kwa mfumo mwingine kwa sababu zina athari mbalimbali kama mahitaji ya mbolea na vitu vingine. Pia bado tunaendelea kufanya tafiti ya udongo tulio nao ili tuone udongo huo kama unaweza kuzalisha bila ya kutumia mbolea nyingi ili tuweze kuhakikisha kuwa uzalishaji wetu unapanda na unasaidia pia wakulima kupata tija kutokana na mazao wanayozalisha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua ambayo tunaichukua ni ile ya kuimarisha vyuo vya utafiti na kuongeza idadi ya wataalam, kuwapa fursa ya kufanya tafiti nyingi zaidi ili kupata mbegu. Tunayo taasisi ya mbegu ambayo pia nayo tunaitumia kuhakikisha kwamba inahakikisha tunapata mbegu za kutosha kwa kila zao linalolimwa hapa nchini na vituo hivi tumeviweka vingi kwa kanda ndani ya nchi ili kila kanda waweze kutafiti mbegu zinazolimwa kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, hizi ndiyo jitihada za Serikali ambazo tunazifanya na tutaendelea kufanya hilo ili Serikali na watu wake kwa maana ya Watanzania wapate manufaa kwa mbegu ambayo tunaizalisha sisi wenyewe na kusimamia kilimo kilicho bora kitakachovuna mazao mengi zaidi kama ambavyo mmejadili hapa kwenye Bajeti ya Wizara ya Kilimo. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati wetu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa magonjwa sugu ambayo yanakuja kwa kasi ni pamoja na ugonjwa wa Kisukari. Madaktari bingwa wanapatikana kuanzia Hospitali za Mikoa, Kanda pamoja na Taifa kulingana na Sera yetu ya Afya; na wagonjwa hawa wa Kisukari wapo maeneo yote nchini:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujua, kwa kuwa wagonjwa hao wa vijijini, wengi wanashindwa kujua kwamba wana ugonjwa huo na hawana uwezo wa kutoka vijijini na kwenda mpaka Hospitali ya Mkoa; Serikali ina mkakati gani wa ziada kulingana na uzito wa tatizo hili hivi sasa kuweza kutoa huduma kwenye Hospitali za Wilaya pamoja na ngazi ya Kata?
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nami naungana naye kwamba tunayo magonjwa mengi nchini na ambayo tunaendelea kutafuta tiba sahihi ili Watanzania waendelee kuwa na afya njema zitakazowawezesha kufanya shughuli zao za maendeleo. Ugonjwa wa Kisukari ni miongoni mwa magonjwa ambayo kwa sasa yamesambaa sana nchini. Kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, ni kweli mengine yapo mpaka kwenye Vitongoji.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imepanua wigo wa utoaji huduma za afya. Wigo huu umeanzia kwenye ngazi ya huko huko vijijini ambapo kuna zahanati. Vile vile katika ngazi ya Kata kama rufaa ya zahanati, tuna vituo vya afya vinavyotoa huduma nzuri sana sasa hivi na tumejenga vituo vya afya vingi sana na tunaendelea kuvijenga. Pia tuna Hospitali za Wilaya, Mkoa na Rufaa mpaka zile za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ugonjwa wa Kisukari ni miongoni mwa magonjwa ambayo sasa tunatoa huduma mpaka kule kwenye zahanati. Kwenye Sera yetu imeelekeza zahanati na zenyewe zinunue madawa ya Kisukari ili wawe wanapata huduma kule. Pale ambapo anaweza kupimwa kwenye Hospitali ya Kata ambayo ipo kwenye maeneo hayo hayo, lakini upatikanaji wa dawa sasa unakwenda mpaka kwenye zahanati.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni jukumu la zahanati na nataka niagize Halmashauri ambazo ndiyo zinasimamia zahanati kuhakikisha kwamba wanaagiza dawa za Kisukari na ziende katika zahanati, kwenye kituo cha afya na kwenye kila ngazi ya kutoa huduma ili wale Watanzania walioko kule kijijini kabisa wapate huduma hiyo bila usumbufu wa kusafiri na kulipa nauli kwenda mahali pengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia Mheshimiwa Aida, nikuhakikishie kwamba Serikali tumejipanga vizuri kwenye sekta ya utoaji huduma kwenye ngazi zote na bado tunaendelea na maboresho ya utoaji huduma kwa magonjwa yote. Mkakati wetu sasa ni kuhakikisha tunapunguza ukali wa magonjwa haya ili Watanzania wawe na afya njema na kila Mtanzania afanye kazi yake vizuri. Tunataka tuone tija ikipatikana kwa Watanzania kuwa na fya njema.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na nitauliza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 52A, Waziri Mkuu ametajwa kuwa ndio mdhibiti, msimamiaji wa shughuli za Serikali za kila siku. Idara za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zimekuwa zikitekeleza mpango, wakati huo huo zinajifanyia tathmini zenyewe. Mfano, hai ni Wizara ya Fedha na Mipango imekuwa na kitengo cha tathmini ndani ya Idara ya Mipango.
Mheshimiwa Spika, sasa ili tuweze kuisimamia na kuidhibiti Serikali ipasavyo: Je, hatuoni haja ya kuwa na taasisi inayojitegemea ya kuisimamia Serikali na kufanya tathmini, kutunga mifumo ya ufuatiliaji na tathmini nchini?
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mbunge wa Mkoa wa Tanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo umepata shida kulielewa vizuri lakini niseme suala la tathmini na kuona mwelekeo wa kazi hiyo baada ya tathmini, mbali ya kwamba tumeipa Wizara ya Fedha na tukaiita Wizara ya Fedha na Mipango, lakini bado kila Wizara na kila sekta yenyewe tunaitengea bajeti hapa Bungeni kwa ajili ya kujiwekea mpango wake na kwenda kufanya tathmini yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanapokuja awamu ya pili, wanaweza kuweka mipango yao kutokana na tathmini waliyoifanya msimu uliopita. Kwa hiyo, hatujaishia Wizara ya Fedha na Mipango pekee, kila Wizara na kila sekta tumeipa mamlaka hiyo na utakuta pia hata kwenye maombi ya fedha ya bajeti ya miradi kuna element ya usimamizi.
Mheshimiwa Spika, tunaposema usimamizi, maana yake wanakwenda kuikagua mipango waliyoiweka katika kipindi cha mwaka na kuitekeleza ili kupata mwelekeo wa kama: Je, wamefanikiwa au hawajafanikiwa? Kama hawajafanikiwa inawawezesha kuweka mpango ule kuwa endelevu kwa msimu ujao. Kwa hiyo, hiyo tumeishusha mpaka Wizarani na kwenye sekta zetu, hatujaishia kwenye Wizara ya Fedha pekee.
Mheshimiwa Spika, nalichukua hilo, tutafanya mapitio huku kuona swali lako limetokana na nini? Je, kazi hiyo inafanywa na Wizara ya Fedha pekee? Hapo baadaye naweza kukupa majibu kwa namna nyingine ili uweze kupata uelewa mpana juu ya wajibu huo na kama huko kuna udhaifu, basi tutaangalia na kuweza kuboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake, suala la mipango na tathmini lipo katika kila sekta.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kumwuliza Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo unafahamu mwaka huu nchi yetu ilivamiwa na nzige wa jangwani na ikanipelekea kupenda kufahamu mkakati wa Serikali katika kupambana au kudhibiti majanga yanayoweza kuathiri usalama wa chakula na mazao mengine ya kiuchumi katika nchi yetu ikiwemo mifugo. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mkakati wa Serikali wa namna ya kukabiliana na majanga. Amezungumzia chakula, lakini majanga yapo mengi. Mkakati huo upo ndani ya Serikali, pale ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu kimeanzishwa Kitengo cha Maafa. Kitengo hiki ambacho kipo Ofisi ya Waziri Mkuu, tumekishusha pia kipo ngazi ya Mkoa, kiko Kamati ya Maafa; ngazi ya Wilaya tuna Kamati ya Maafa na pia ngazi ya Tarafa ina Kamati ya Maafa.
Mheshimiwa Spika, wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunaepusha utokeaji wa majanga haya. Wakati mwingine huwezi kuyaepusha, ila ni kushughulikia majanga haya yanapojitokeza. Kwa hiyo, eneo la chakula nako pia linapotokea janga ambalo linapoteza vyakula ambavyo wananchi walikuwa wanavitegemea, nayo pia tunashughulikia.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Kiruswa atakumbuka siku za hivi karibuni kule Longido na maeneo mengine tulivamiwa na nzige, nami niliwenda pale, nikaenda mpaka Monduli kwenda kuona hali ya nzige. Ndiyo majanga hayo, wadudu wamekuja kutoka huko, wameruka wanakuja kushambulia chakula, lakini tulikabiliana nao kabla hawajaanza kushughulikia chakula chetu. Kwa hiyo, hiyo ndiyo njia mojawapo ambayo tunaitumia kukabiliana na majanga. Tulienda kuwakabili kabla hawajaanza kula chakula chetu na tukamudu kuwapoteza wote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumeimarisha kitengo hiki kwa kuweka vifaa, watalaam na pia pamoja na utaalam huo tumeendelea kushusha elimu hii kwa wananchi wenyewe waanze kushughulikia majanga pindi tu inapotokea majanga haya. Vile vitengo husika na vyenyewe vikikaa na kuratibu, vinashughulikia, lakini pale wanaposhindwa ngazi ya Kata, wanajulisha Wilaya, janga linapokuwa kubwa zaidi ya ngazi ya Wilaya wanajulisha Mkoa na Mkoa unaposhughulikia janga hilo likionekana limeshindikana, wanajulishwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikifanya kazi hiyo vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kuwa na uhakika na Serikali yao na kuiamini kwamba pia tumejipanga kwenye eneo hilo la kupambana na majanga mbalimbali ili kuhakikisha kwamba shughuli zote za Watanzania zinaenda vizuri na tuweze kuwa na akiba ya kutosha kwenye chakula na pia usalama wa maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumekuwa na matatizo na vijana wetu wanaotoa huduma za usafiri mijini ikiwemo bajaji, bodaboda na daladala na hasa kutokana na kugombania ile miundombinu ya barabara. Nilichokiona sasa pale, pamoja hiyo crisis iliyopo ni kwamba kuna shida katika ku-co-ordinate namna ya kufanya kazi zetu kati ya Serikali za Mitaa na Wizara. Mzigo mkubwa…
SPIKA: Ukichukua muda mrefu, hutajikuta umeuliza swali.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Swali lenyewe lilivyo, kidogo linahitaji ufahamu. Samahani.
Mheshimiwa Spika, jinsi ilivyo sasa tunapata shida kwa sababu unakuta kwa mfano TARURA wapo TAMISEMI wakati Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ndiyo inayohusika na masuala ya ujenzi na miundombinu. Sasa unapofika wakati wa kufanya co-ordination, hawa Ujenzi wanakuwa kwa mfano wamejenga barabara kubwa imepita katikati ya mji, lakini TARURA hawakuwa aware kutengeneza alternative way kuhakikisha kwamba ule mzigo mzito wa traffic unaokuja kuingia kwenye ule mji unapitishwa kwenye barabara nyingine. Labda ni kwa sababu TARURA wapo chini ya Wizara nyingine. Haya yanatukuta pia kwenye masuala ya afya…
SPIKA: Swali lako ni nini sasa? Maana unachangia.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Haya yanatukuta pia kwenye Wizara ya Afya kwenye kupandisha hospitali zetu kutoka vituo kwenda Hospitali za Wilaya.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu ni hivi: Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuona kwamba hizi Wizara zinachukua mzigo wake mzima; kwa mfano, Ujenzi na Uchukuzi wanaichukua na TARURA, Wizara ya Afya wanachukua na vituo vyake vya zahanati ili wanapotaka kupandisha madaraja washughulike wenyewe, kusiwe na contradiction na kuleta ugumu pale katika kurahisisha kazi hiyo? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Msambatavangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake limegusa mambo mengi; limegusa bodaboda, TARURA, TANROAD baadaye akahama tena akaja kwenye hospitali. Kwa hiyo, halina mwelekeo sahihi sana, lakini nataka niseme tu, ndani ya Serikali vyombo vyote ni vya Serikali na tumetoa miongozo ya kila mmoja. Miongozo hii tumejitahidi lazima izungumze pamoja. Ninaposema lazima miongozo izungumze, maana yake mipango ya TANROADS hata kama inaenda kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, lazima pia kama ni ya kisheria iende i-fit in; iweze kuwa ndani ya mipango ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, wanapojenga barabara kukatiza humo, ni lazima barabara hiyo ijengwe kwa vipimo vilevile na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ziruhusu hawa wapitishe barabara hiyo ili iweze kutumika na wote. Hata kwenye matumizi, kila mmoja atatumia na kama barabara hiyo inahitaji kuwa na njia za waenda kwa miguu, lazima ziende hivyo.
Mheshimiwa Spika, sasa tunapokuja kwenye Sekta ya Afya na yenyewe ambayo inaongozwa na Wizara ya Afya ambapo pia miundombinu inajengwa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ni lazima Wizara hizi zizungumze, zihakikishe kwamba zinasimamia ujenzi wa miundombinu hiyo ili iweze kutoa huduma kwa Watanzania. Mwisho wa yote haya tunawahudumia hawa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, sasa tunapokuja hapa ndani ya Serikali, tunaweka sawia katika mambo ya kisheria ambapo kila mmoja atatumia miundombinu yote ya kila Wizara kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zilizopo na zinazotuongoza. Kwa hiyo, niseme tu kwamba taasisi zote hizi pamoja na kwamba zipo huko kwenye mamlaka mbalimbali, lakini lazima ziwe zinazungumza lugha moja ili Mtanzania anapotumia asiwe na mgongano wa matumizi ya maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama nilivyosema swali lako lilijikita kwenye mambo mengi, lilikuwa pana, nilichofanya ni kuchukua maeneo hayo yote na kazi wanazozifanya kuwa zote ni za Serikali na kila mmoja anapotaka kutekeleza lazima kuwe na mawasiliano na taasisi nyingine ambayo ni ya Serikali. Kwa hiyo, Serikali lazima izungumze lugha moja na utoaji huduma lazima uende wa aina moja ili wananchi waweze kupata huduma kwenye maeneo hayo, kila mmoja na eneo ambalo analolihitaji. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kwanza kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, swali langu litahusu sekta ya korosho. Mwaka huu tumepata taarifa kwamba Serikali ilijipanga kutupatia pembejeo wakulima wa zao la korosho kwa maana kwamba waje kuzilipa baadaye kwenye mjengeko wa bei. Hata hivyo, kuna taharuki kubwa kwa wakulima wetu wa korosho baada ya Bodi ya Korosho kuleta waraka kwenye Halmashauri zetu, wakiwaambia kila mkulima akipeleka zao lile kwenye mnada kila kilo moja itakatwa shilingi 110 bila kujali kwamba mkulima yule amechukua pembejeo kwa kiwango gani. Barua ile inasema kwamba jambo hili hata sisi Wabunge tumeliridhia.
Mheshimiwa Spika, sasa kuna taharuki kubwa sana kiasi kwamba mpaka…
SPIKA: Swali lako ni nini katika jambo hilo?
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, kutokana na mkanganyiko huu ni nini kauli ya Serikali ili wakulima wetu waendelee kuchukua zile pembejeo maana sasa hivi wanaziogopa.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Wizara yetu ya Kilimo imetoa miongozo kadhaa ya kuboresha masoko ya mazao nchini ili kuwanufaisha wakulima kwenye mazao wanayoyalima ikiwemo na kuwarahisishia namna nzuri ya kupata pembejeo. Zao la korosho ni miongoni mwa mazao ambayo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kufanya mapitio ya maboresho ya namna nzuri ambayo wakulima ambao kwa sasa ndiyo wapo kwenye msimu wa kutumia pembejeo ili waweze kupata pembejeo wakulima wote na waweze kushiriki vizuri kwenye kilimo hiki.
Mheshimiwa Spika, nakiri kwamba ipo taharuki kwa sababu na mimi ni mdau pia wa zao hilo lakini taharuki hii imetokana na vikao vya awali vya majadiliano ya mfumo mzuri ambao pia wakulima nao wanaweza kushiriki vizuri kupata pembejeo. Si kwamba Wabunge wameshiriki katika kutoa maamuzi, hapana, bali Wizara inaendelea kuwa na vikao vya mara kwa mara ili kufikia hatua nzuri ya kuwezesha kila mkulima kupata pembejeo. Vikao hivi bado havijakamilika na kikao kikubwa kabisa kipo tarehe 6 ambacho kinaalika wakulima, viongozi wa ushirika, viongozi wa Serikali na Waheshimiwa Wabunge pia mtaalikwa ambacho sasa tutajadili namna nzuri ya kumwezesha mkulima kupata pembejeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya awali ya kwamba kila mkulima atakatwa shilingi 110 yamesitishwa kwa muda ila wakulima wote waende kupata pembejeo zile ambazo zimepelekwa kwenye maeneo yale. Kiwango cha pembejeo kilichoagizwa kinatosha kabisa kwa kila mkulima kutokana na takwimu zilizopatikana kutoka vyama vyetu vya ushirika ili kila mkulima apate pembejeo ya kutosha kupuliza awamu zote nne kufikia kipindi cha uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kikao kile cha tarehe 6 ndicho kitakachotoa mwelekeo mzuri wa nini kitafanyika kwa pembejeo ambazo zimetolewa na wala haitakuwa kumkata kila mkulima kwa kilo aliyoipeleka sokoni kwa sababu wapo wengine wana kilo mbili, wengine kilo 10 lakini wapo wamezalisha zaidi ya tani 20, sasa huwezi kukata kwa kila kilo. Kwa hiyo, hilo linafanyiwa kazi na Wizara na ufafanuzi utatolewa siku ya tarehe 6 ambapo wadau wa zao la korosho kila mmoja atashiriki kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwasihi wakulima wa zao la korosho waendelee kupokea pembejeo zile. Serikali inaendelea kuangalia namna bora ya kumfanya mkulima aweze kupata pembejeo kwa gharama nafuu ili aweze kuendelea kulima zao hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niongezee eneo lingine ambalo pia limeleta mkanganyiko kwamba mabenki ambayo miaka yote yamekuwa yakitoa mikopo kwa wakulima, mwaka huu walisimama kutoa mikopo yao kwa hofu kwamba wakulima watakapopata pembejeo huku Serikalini hawataweza kulipa gharama ya mikopo ambayo wameikopa kwenye mabenki. Tumeruhusu mabenki yaendelee kukopesha wakulima kwa sababu bado kwenye zao la korosho kuna shughuli nyingi za kufanya; pamoja na kupilizia dawa lakini pia kuna kupalilia, kuokota na kuhakikisha zao linakwenda sokoni, yote inahitaji mtaji ambapo mkulima ambaye amelima, anajiamini kwamba atakopa na kurejesha, bado mabenki yaendelee kukopesha. Tumeshawapa maelezo hayo mabenki na wanaendelea na kukopesha. Kwa hiyo, wakulima waende wakakope kulingana na mahitaji yake ili alihudumie zao na hatimaye aweze kurejesha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuwaambia Waheshimiwa Wabunge wote wanaotoka kwenye majimbo yanayolima zao la korosho muendelee kuiamini Serikali na mifumo ambayo inaendelea kuipanga. Mifumo hii haiamuliwi tu moja kwa moja na Serikali bali inashirikisha wadau na kwa zao la korosho wadau tutakutana siku ya tarehe 6. Kwa hiyo, siku hiyo tutatoa mwelekeo wa zao hilo sote kwa Pamoja. Kwa hiyo, wawe na amani na waendelee na uratibu wa zao hili la korosho, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa mujibu wa kifungu cha 64(2)(c) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2016, sambamba na Tangazo la Serikali Na.30 la mwaka 2013 inazitaka taasisi nunuzi (procuring entity) zitenge asilimia 30 ya zabuni zake kwa mwaka kwa ajili ya vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na ulegelege katika utekelezaji wa takwa hili ambalo linawanyima fursa vikundi hivi muhimu, je, ni mkakati gani sasa ambao Serikali unauweka kuhakikisha kwamba takwa hili la kisheria linazingatiwa ili kuweza kuwapa fursa hizi vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mavunde, Mbunge wetu wa Dodoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeweka sheria inayowezesha kila taasisi kutenga kiwango cha fedha kwa ajili ya kukopesha makundi kama alivyoyataja Mheshimiwa Mbunge lakini tunatambua zipo changamoto kwa baadhi ya taasisi kutotekeleza sheria hiyo huku wakitakiwa kutekeleza sheria hiyo. Serikali inaendelea kusisitiza na kuhamasisha taasisi zetu kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na hasa kwenye eneo hili la mikopo kwa sababu tunahitaji sasa Watanzania wanaotaka kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi au masuala ya kijamii wapate uwezesho wa kumudu kutekeleza wajibu huo. Maelekezo ambayo tunayo kwa sasa ni kuhakikisha kwamba kila mtumishi wa umma aliyepo kwenye kitengo ambacho kimetakiwa kutoa mikopo hii, lazima afanye hivyo kwa sababu tayari pia Serikali huwa inatenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali na wale wote ambao wanatakiwa kupewa mikopo hiyo ikiwemo wanawake, vijana na walemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, msisitizo wa Serikali kwa kila mmoja kujishughulisha na masuala ya kiuchumi ni msisitizo ambao unatokana na malengo yaliyowekwa na utekelezaji ambao upo kwa taasisi hizo. Kwa hiyo, bado nitoe wito kila taasisi ambayo imetenga fedha hizo na sheria inamtaka kutoa mikopo hiyo bado waendelee kutoa mikopo kwa wahitaji ili kila mkopaji aweze kupata fedha hizo na aweze kuendesha miradi yake kadiri alivyojipanga.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nachotaka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kusisitiza kuhakikisha kwamba kila mmoja anatekeleza sheria ili wanufaika waweze kunufaika kwa utaratibu ambao tumejiwekea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tunatambua kwamba Serikali yetu ilizuia kabisa usafirishwaji wa makinikia nje ya nchi na kwa sasa tumeshuhudia makontena ya makinikia yakisafirishwa kupitia barabara ya Bulyanhulu – Kahama na Bandari yetu ya Dar es salaam hivyo kupelekea taharuki kwa Watanzania na kwa wananchi wa Jimbo la Msalala. Nini sasa kauli ya Serikali juu ya jambo hili? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nami nimeona pia kwenye mitandao watu wakionesha kwamba wanaona makontena ya makinikia yakisafirishwa kwenda nje. Nataka niwakumbushe Watanzania kwenye hili kwamba mwaka 2017/2018 tulizuia usafirishaji wa makinikia kwenda nje ya nchi kwa sababu yalikuwa hayajafuata utaratibu lakini pia kulikuwa na udanganyifu mkubwa. Tulipozuia makontena zaidi ya 300/400 yaliyokuwa bandarini yalikaa pale mpaka tulipoweka utaratibu. Utaratibu uliowekwa na Serikali kwanza kuwatambua ni nani wanasafirisha makinikia kwenda nje na ni nani wametoa vibali hivyo kwenda nje na tukazuia kabisa tukaanza utaratibu mpya.
Mheshimiwa Spika, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano alilisimamia na kwa kuunda timu iliyofanya uhakiki wa sekta yote ya madini ikiwemo na eneo hili la usafirishaji mchanga ambalo kwa kweli tulikuwa tunaibiwa kwa kiasi kikubwa. Ufumbuzi wa ile timu ni kuanzisha kampuni ya Watanzania kwa ushirikiano na makampuni ya nje yaliyopo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii tunayo kampuni inaitwa Twiga Minerals ambayo ni ya Watanzania kwa maana ya Serikali ambayo imeingia ubia na hao wachimbaji wakubwa wa madini kwenye mgodi kama ule wa kwako Mheshimiwa Mbunge wa Bulyanhulu lakini wa pale Kahama Mjini Buzwagi na kule Tarime North Mara. Migodi hii mitatu chini ya Barrick tumetengeneza kampuni ya pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwanza wataalam baada ya kuchimba tunapitia kujua aina zote za madini. Mwanzo tuliambiwa madini yaliyopo pale ni ya aina moja tu dhahabu lakini kumbe kule ndani baada ya ukaguzi na uchunguzi wa wataalam tumegundua tuna aina tano za madini. Kwa hiyo, leo hii kupitia Kampuni yetu ya Serikali, inauza madini ya aina zote 5 siyo moja kama zamani. Mbili; tukishapata ule udongo na ukaguzi huo na kugundua aina zote, tunayauza hapahapa ndani ya nchi, sio nje ya nchi. Makontena yote yanayosafirishwa tayari yameshauzwa, Serikali imeshapata fedha yake na fedha imeshahifadhiwa kwenye akaunti zetu kwa hiyo Watanzania hatupati hasara. Hatua inayofuata mnunuzi anakuwa huru kuyapeleka anakotaka na ndio hayo ambayo yanaonekana kutoka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Watanzania kuyaona makontena yakipita na hofu ya awali, nataka niwaondolee kuwa makontena hayo yameshauzwa tayari na huyo ni mnunuzi. Kwa hiyo, waondoe mashaka juu ya usafirishaji wa makontena hayo yenye makinikia kwa sababu Serikali iko makini sana. Inayo timu palepale kwenye mgodi ya kuhakiki lakini pia ya mauzo na kuhakikisha fedha inalipwa na hakuna kontena linatoka nchini bila kuuzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeweka timu pale bandarini kuhakikisha kwamba kila kontena la makinikia linaloingia pale lina nyaraka zote baada ya kufanya mauzo hukohuko kwenye mgodi, kwa hiyo, hakuna kontena linaibiwa. Kwa hiyo, Watanzania muondoe mashaka, Serikali ipo makini, watu wetu tuliowaweka kwenye maeneo haya kuhakiki kuwepo kwa nyaraka zote za kuuza makinikia hayo zipo makini na kwa kweli tunaingiza fedha za kutosha; sina takwimu za kutosha lakini tuna fedha ya kutosha kwa sasa. Mheshimiwa Waziri wa Madini alipokuwa anawasilisha bajeti yake hapa alitoa ufafanuzi na kuonesha namna ambavyo kwenye madini tumepata fedha kiasi kikubwa sana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali langu; sasa hivi pamekuwa na utaratibu ambapo Serikali inapopeleka fedha za maendeleo kwenye Halmashauri hasa fedha zinazopelekwa kuanzia miezi ya Machi, Aprili na Mei, fedha hizi zinapokuwa hazijatumika zote pamekuwa na utaratibu wa miaka mingi mwaka wa fedha unapoisha zinarudishwa hazina na hivyo kuathiri sana utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Natoa mfano Jimbo la Singida Magharibi na Majimbo mengi Tanzania tumepokea fedha za ujenzi wa vituo vya afya, hosteli na mabweni lakini fedha hizi zimepokelewa kuanzia mwezi wa Aprili na Mei ni wazi itakapofika mwisho wa financial year fedha hizi zitakuwa hazijatumika zitarudi Hazina na hatujui zinakwenda kutumika namna gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, je, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali yangu haioni umuhimu wa kusitisha mpango huu na kuruhusu fedha hizi ambazo tayari zinawagusa wananchi wanyonge zisirudi Hazina zaidi sana ukawekwa mpango wa kuzi-monitor? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, najua jambo hili lilizungumzwa hapa na wewe mwenyewe ulionesha interest kubwa lakini na pia kuitaka Serikali ilifanyie kazi. Nashukuru leo limerudi tena naomba kutoa ufafanuzi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hasssan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapeleka fedha nyingi sana sasa hivi kwenye Halmashauri kwa ajili ya maendeleo. Upelekaji huu ni wakati wote, toka tulipoanza mwanzo wa mwaka wa fedha na tutaendelea kupeleka mpaka mwisho wa mwaka wa fedha ili kuwafanya wananchi waweze kupata maendeleo kupitia miradi inayolengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuliliwekea sheria ambazo zinataka fedha inapofika angalau tarehe 15 ya mwezi wa Juni wa mwisho wa mwaka wa fedha kama Halmashauri haijamudu kufanya matumizi lazima zirudi halafu tuliweka utaratibu wa kama Halmashauri imepelekewa fedha na wamefika muda wa mwisho wa kushika fedha na kutaka kuzirudisha, waweze kuandika barua ya kuonesha kwamba mpaka tarehe hii bado tuna fedha ambazo hazijatumika kwa sababu ya taratibu za manunuzi labda kwa sababu pia kwenye taratibu za manunuzi unapotengeneza mradi unalipa kadiri hatua fulani inavyofikiwa.
Kwa hiyo, inawezekana kuna miradi ambayo inafikiwa mwezi Juni tarehe 15 ipo kwenye hatua labda ya lenta na haijakamilisha kwenye finishing. Utaratibu huu unawezesha pia Wizara ya Fedha kuzirudisha fedha hizi kwenda kwenye Halmashauri ingawa kuna changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameionesha hapa na Waheshimiwa Wabunge wote tumeshuhudia kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya kweli hili; niliwaagiza Wizara ya Fedha kubadilisha utaratibu na kufanya maboresho kwenye Kanuni zetu ili kuweka Kanuni ambayo angalau inaweza kuruhusu miezi kadhaa baada ya mwaka wa fedha wa bajeti ili fedha zile ziweze kukamilisha kazi hiyo. Ingawa kwenye hili, hatutahitaji mwanya wa wazembe kukaa na fedha bila kuzitumia akitegemea ataongezewa muda. Pamoja na Kanuni hiyo ambayo tutaiboresha lakini bado tutaweka kipengele kinachombana mwajiri/mtendaji wetu kule kuhakikisha kwamba kila fedha inayoingia lazima itumike kwa kipindi kinachotakiwa kwa sababu wengine wanaweza kukaa na fedha mpaka miaka miwili, sasa hilo hatutaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaangalia ni miezi mingapi inaweza kutufaa ambayo itaingia mwaka wa pili wa fedha ili fedha hii iweze kukamilisha miradi hiyo lakini kwa barua vilevile inaonesha kwamba amepata fedha tarehe fulani labda ndani ya Juni yenyewe na mradi umeshaanza kutekelezwa upo hatua fulani na lazima tukakague tuone kama kweli fedha ile imebaki na inatakiwa itumie kufikia kipindi hicho, huyo tutamridhia. Vinginevyo hatutaruhusu mtendaji yeyote akae na fedha kwa uzembe tu halafu ategemee kupata offer ya kuongezewa miezi mingine, hao watachukuliwa hatua kali ili tuweze kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha kwa sababu wananchi wanahitaji miradi na kuona fedha inatumika vizuri na Waheshimiwa Wabunge kama Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo kwenye Jimbo ni lazima na ninyi mridhike kwamba fedha iliyokwenda imetumika kwenye mradi kusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inafanya maboresho hayo na tutatoa taarifa katika kipindi hikihiki cha Bunge ili muondoke hapa mkiwa na uhakika kwamba fedha iliyotumwa kwenye maeneo yenu inaweza kutumika lakini pia imepata fursa ya kutumika kipindi kijacho cha fedha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, zao la chai lina soko kubwa sana hapa nchini na hata soko la dunia. Nini kauli ya Serikali juu ya wakulima wa chai wanaolima chai lakini chai hiyo inauzwa kwa bei ya chini sana na kuwanufaisha watu wa katikati ambao wao hawawezi kusaidia hawa wakulima wakaweza kukidhi mahitaji yao?
Naomba kauli ya Serikali juu ya bei ya chai hapa nchini Tanzania. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mazao yetu haya chai ikiwemo Serikali inaendelea kuyasimamia kuanzia kilimo mpaka masoko yake na malengo ya Serikali ni kumnufaisha mkulima aweze kupata tija ya kutosha kwa kuuza bei nzuri kwenye masoko yetu.
Nakiri kwamba tunayo changamoto kwenye masoko ya zao la chai, hata tulipokuwa kwenye kikao pale Njombe miezi miwili iliyopita tulizungumza kwa kina juu ya tatizo la soko la zao la chai ambalo kwa sasa minada yake inategemewa sana kufanywa nchini Kenya kwenye Jiji la Nairobi pekee badala ya minada ile kuendeshwa hapa nchini na kuongeza gharama za uendeshaji wa zao hili kuliko kama tungeweza kuanzisha mnada hapa. Makubaliano ambayo tumefanya pamoja na wadau ni kuanzisha soko hapahapa ndani ya nchi ili kuwezesha zao hili kupata bei nzuri kwenye masoko yetu na kuwataka wanunuzi waje nchini wanunue hapa na kwa hiyo itapunguza gharama za uendeshaji wa mkulima mwenyewe na wengi wapo kwenye ushirika na ushirika wenyewe ili bei ile iweze kumsaidia mkulima kuweza kulilima tena zao hili na kulifanya kuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, katika miaka/mitatu iliyopita tumepata changamoto sana, nimetembelea Rungwe kwa Mheshimiwa Mwakagenda, nimetembelea kwenye kiwanda lakini nimezungumza na wakulima pale Rungwe nimeona tatizo kubwa miaka hii miwili/mitatu unaotokana na ugonjwa wa Covid kwamba masoko yetu kule tumeshindwa kuyafikia na kwa namna hiyo hata wanunuzi wamekuwa hawaamini kununua mazao kwa umbali pamoja na kwamba tuna mifumo ya kielekroniki, hata hivyo bei zake zimekuwa za chini sana. Kwa hiyo, tunachofanya hapa, tunaendelea kupunguza hao watu wa kati ambao wanazidi kupunguza faida ya mkulima na kumfanya mkulima moja kwa moja kupitia ushirika wake aingie kwenye mnada ambao tumeupanga kuufanya humuhumu ndani. Hivyo ndiyo njia sahihi ambayo tunadhani inaweza kutusaidia pia kumfanya mkulima apate fedha yake moja kwa moja badala ya watu wa kati ambao wakati mwingine wanafanya thamani ya zao kupungua.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali tunaendelea kuona na kubaini masoko kupitia Balozi zetu kuona ni Balozi ipi nchi hiyo inahitaji chai ili tufanye mauzo ya moja kwa moja na nchi hiyo ili zao letu kwa kweli liweze kupata bei. Kwa hiyo, jitihada za Serikali zinaendelea na niwahakikishie Watanzania kwenye mazao yote chai ikiwemo, tunaendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba tunapata masoko ya uhakika ili wakulima wetu wote wapate faida kwenye kilimo wanachokilima na hasa kwa kutafuta mifumo mizuri ya masoko. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu imeendelea kutoa matumaini makubwa kabisa kwa wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini. Hivi karibuni tumeona mfanyabiashara mkubwa kama Dangote amejenga imani na kuahidi kuwekeza zaidi hapa nchini lakini kumekuwa na changamoto nyingi sana katika kuwekeza hapa nchini. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sasa hivi inatengeneza sheria bora na kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza zaidi hapa nchini kwetu? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabati, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba kujua mkakati wa Serikali na maboresho yake kwenye uwekezaji. Watanzania wote mtakiri kwamba Serikali yetu imeweka msisitizo wa kuhakikisha kwamba tunapanua wigo unaowawezesha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini kwa sababu fursa, malighafi na labor tunazo za kutosha. Sisi tunavutia uwekezaji kwa sababu maeneo mengi ya uwekezaji pia yanapunguza changamoto yetu ya ajira kwa Watanzania. Kwa hiyo, mfanyabiashara Dangote aliyekuja ambaye amewekeza kwenye kiwanda cha saruji Mkoani Mtwara ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini ambao pia tumetoa fursa za kupanua wigo wa uwekezaji wake.
Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya kupanua wigo wa uwekezaji? Kwanza tunafanya maboresho ya sheria na kanuni zetu kwenye uwekezaji ili kujenga mazingira mazuri wezeshi ya uwekezaji nchini ili kila mwekezaji anayekuja kuwekeza apate huduma hiyo kwa ukaribu. Tumeanzisha taasisi inaitwa Tanzania Investment Center ambapo mwekezaji atapata huduma zote kupitia taasisi hiyo tunaita One Stop Center na tunaweza kumpa ardhi na aina yoyote ya msaada ambao anauhitaji katika uwekezaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Tanzania ya leo hatuna shida ya ardhi, ardhi tunayo, umeme upo wa kutosha, maji tunayo, barabara zetu nzuri na mazingira ya uwekezaji Tanzania sasa ni mazuri. Sheria hizi ambazo tunaendelea kuzirekebisha na kuzifanya kuwa sheria wekezi zitasaidia sana wawekezaji kuja nchini kama ambavyo tunaona sasa kasi ya wawekezaji kuja kwenye maeneo haya imeongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wawekezaji wote mliopo ndani ya nchi na walio nje ya nchi kuja Tanzania kuwekeza kwa sababu mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuboreshwa. Sasa hivi tunakaribia kuweka ile sheria ambayo imekusanya changamoto nyingi ambazo zilikuwa zinawakwaza wawekezaji na mengine ni ya kisheria kwa hiyo tunafanya maboresho ya sheria ili kuondoa vikwazo vya uwekezaji Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tunataka tuainishe huduma ambazo sisi tunazitoa au fursa zilizopo Tanzania ili kuhakikisha kwamba tunafanya wawekezaji kuwa na imani nasi. Wiki iliyopita nilikuwa Mkoani Mara kwenye mkakati wa kutangaza vivutio vya uwekezaji. Huu ni mwendelezo wa kutangaza fursa za mikoa yote nchini ambapo mpaka sasa tumeshafika mikoa 24 kuhakikisha kwamba tunawaonesha wawekezaji nini kipo kwenye mkoa huo ili kila mmoja aamue kwenda mahali anapotaka. Tuna malighafi nyingi sana zinazogusa kwenye sekta ya kilimo, madini na maliasili, hizi zote pia zinasaidia uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kufanya maboresho haya mara kwa mara ya kupitia changamoto tulizonazo na tunaziingiza kwenye sheria ili tuwe na sheria endelevu ambayo pia inaweza kutusaidia kuwekeza. Yale yote ambayo yanajitokeza kwa sasa tunayachukua, tunayafanyia utaratibu wa kuyaboresha hivyo na kurahisisha uwekezaji huo kwa yeyote anayetaka kuwekeza hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hili suala la vibali vya kazi tumeendelea kufanya maboresho ili wawekezaji sasa wawe na uhakika wa kuleta watu wao kuja kuwekeza hapa na mambo mengi ya uwekezaji ambayo yapo kwenye kile kitabu kinaitwa Blue Print ambacho kina maelekezo yote ya uwekezaji. Niendelee kuwahakikishia Watanzania fursa tulizonazo zitatusaidia pia sana kunufaisha Taifa letu.
Kwanza mwekezaji akija tutapata kodi lakini mbili ushiriki wa Watanzania, tatu ajira lakini nne malighafi na mazao tunayoyalima pia yanapata soko. Kwa hiyo, jambo hili kwa ujumla wake lina faida kubwa na sisi tunalisimamia kuwa linaleta tija kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kulijibu kwa upana huo ili wawekezaji wote wanaotaka kuja nchini waje kuwekeza na sisi tunawakaribisha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ya Tanzania imeweza kusaidia baadhi ya nchi za Afrika kujikomboa katika uhuru wa nchi zao. Moja ya nchi hizo ikiwa ni Afrika ya Kusini, Angola, Zimbabwe, Msumbiji na maeneo mengine. Katika nchi yetu ya Tanzania, maeneo ambayo yalishiriki katika mkakati huo wa kuzisaidia nchi hizo ni pamoja na Kongwa, Mazimbu Morogoro, Nachingwea na maeneo mengine. Nini kauli ya Serikali kwa Mataifa haya kuhusu kuchangia maendeleo katika maeneo haya ambayo nimeyataja nchini kwetu.
Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Halamga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, najua swali hili una maslahi nalo kwa sababu Kongwa ni moja kati ya maeneo ambayo wanaharakati hawa wa kupata uhuru kwenye nchi zao waliishi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali na Taifa letu la Tanzania limefanya kazi kubwa sana kuhakikisha kuwa nchi zetu za Bara la Afrika zinapata ukombozi kwa kukaribisha hapa wanaharakati wao kuja kuweka mikakati ya kwenda kukomboa nchi zao na nchi nyingi zimefanikiwa. Mkakati huu ulisimamiwa sana na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye pia alikuwa na ndoto ya kuona Afrika imejitawala na tunaiona imefikiwa, Bara la Afrika kwa kweli sasa hivi kila nchi imejitawala yenyewe na inaendelea na shughuli zake.
Mheshimiwa Spika, sasa maeneo yaliyotumiwa na hawa wapigania uhuru kwenye nchi yetu ikiwemo na Kongwa kama alivyosema lakini pia Dakawa, Wilaya ya Kilosa, pale Mazimbu Morogoro hata kule Nachingwea Mkoani Lindi yametoa mchango mkubwa sana ya ukombozi wa maeneo ambayo wapigania uhuru walikuja hapa. Maeneo haya namna ambavyo yanaendelezwa hayana mchango mkubwa sana kutoka kwao lakini tunaendelea kufanya mawasiliano nao kwa utaratibu ule wa kujenga mahusiano na nchi hizi.
Mheshimiwa Spika, bado tuna mahusiano na nchi zote ambazo zimepata uhuru kwa kuwa na wapigania uhuru wao hapa nchini na wao wanatambua mchango huu ingawa mchango wa kuboresha maeneo haya si mkubwa sana kwa sababu ya kubadilika kwa vizazi kwenye nchi zao na kutambua umuhimu wa Tanzania kwenye ushiriki wa ukombozi wa nchi zao. Hata hivyo, tumeimarisha sana kwenye sekta ya kiuchumi, kisiasa lakini pia kijamii pale ambapo tumefungua Balozi kwenye nchi zao, tunayo mawasiliano na nchi nyingi zipo kwenye Jumuiya ya SADC ambayo pia tunakutana mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya viongozi wa nchi hizo wanapokuja Tanzania wanapata hamu ya kwenda kutembelea maeneo haya. Wote mnakumbuka mwaka 2020 kulikuwa na Mkutano wa SADC hapa na Mheshimiwa Rais Ramaphosa miongoni mwa Marais waliokuja, alipata nafasi ya kwenda Mazimbu na mimi niliandamana naye kwenda kuona eneo lile na akaambiwa changamoto zilizopo pale na ahadi ambazo amezitoa. Tunaamini viongozi hawa ambao bado wana kumbukumbu sahihi na kuona uthamani wa Tanzania kwenye uhuru wao wataendelea kuutambua mchango wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini na sisi tunayo namna ya kuwakumbusha, tunapokuwa na matukio tunawakumbusha na wao wakiwa na matukio yao ya uhuru wanakumbuka nchi yetu Tanzania. Ni vile utofauti sasa wa yule aliyeshiriki kwenye ukombozi namna alivyokuwa anathamini nchi yetu; wote mnakumbuka Mheshimiwa Mandela alipotoka gerezani nchi ya kwanza kuitembelea ilikuwa Tanzania, hii ni kwa sababu alikuwa anajua umuhimu wa Tanzania na uhuru uliopo sasa Afrika Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunatarajia pia na Marais wengine kupitia taratibu zetu za Kidiplomasia wataendelea kuitambua nchi yetu na maeneo ambayo wamepatia uhuru kwa kuungana na maeneo hayo kuyaboresha na kuweza kuyafanya kuwa endelevu kama maeneo ya kumbukumbu kwao na sisi pia. Kwa hiyo, tunaendelea kushirikiana na nchi hizo ili kujenga mahusiano ya karibu zaidi kwa Bara la Afrika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Serikali ya Tanzania imepitia Awamu Sita za uongozi; Awamu ya Kwanza ilijikita kwenye kujenga viwanda kwa ajili ya kuboresha ajira na uzalishaji, Awamu ya Tatu iliamua kubinafsisha viwanda hivi ili kuviboresha zaidi pamoja na kuongeza ajira, Awamu ya Tano ilikuja tena na Sera ya Ujenzi wa Viwanda ili kuongeza ajira pamoja na uzalishaji.
Swali langu; viwanda vilivyobinafsishwa kwenye Awamu ya Tatu vingi havifanyi kazi iliyokusudiwa, kwa mfano viwanda vya korosho Mkoa wa Mtwara, Lindi pamoja na Ruvuma. Nini msimamo wa Serikali wa Awamu ya Sita kuhusu viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifayi kazi iliyokusudiwa? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba uchumi wa nchi yetu hutegemea nyanja nyingi ikiwemo na ujenzi wa viwanda ambavyo vina faida pana kwa Watanzania na mifano yote uliyoieleza kutoka Awamu ya Kwanza mpaka ya Tatu. Awamu ya Tatu ya Serikali yetu ililenga kutoa fursa kwa Sekta Binafsi kuhakikisha kwamba nazo zinaingia kwenye mchakato wa uchumi kwa kushika viwanda na kuviendeleza. Lakini nasikitika kwamba baadhi ya waliopewa viwanda hivyo hawakufanya vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini Serikali imefanya ni kuchukua viwanda vyote ambavyo havikufanya vizuri na tuliunda Tume iliyoongozwa na Msajili wa Hazina pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya mapitio viwanda vyote vile ambavyo vilibinafsishwa na havifanyi kazi ikiwemo na viwanda vya korosho. Na kwa bahati nzuri mimi ni mdau wa korosho na natambua viwanda vyetu kule vingi hata vilivyopo Mkoani Pwani na Tanga wameshindwa kuviendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tulichofanya, tumechukua viwanda vyote na sasa vinafanyiwa uchambuzi na Serikali na timu iliyoongozwa na Msajili wa Hazina baadaye tupeleke kwenye Baraza la Mawaziri. Malengo yetu ni kutoa viwanda hivyo kwa watu ambao wana uwezo sasa kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anasisitiza pia kwamba Sekta Binafsi lazima iwe karibu na Serikali ili kuweza kupanua wigo wa uchumi kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baadaye tukipata wale ambao wana nia ya kuendesha tutawapa kwa masharti ambayo tutayaweka ili kuendeleza ule mkakati wetu wa uchumi wa viwanda hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie tu mheshimiwa Mbunge kwamba viwanda hivi ambavyo havifanyi kazi tayari vimesharatibiwa na vitatolewa kwa watu ambao wenye uwezo. Kwa hiyo, niwakaribishe Watazania wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda kuwa tayari kupokea baada ya Baraza la Mawaziri kufanya maamuzi ili waweze kuviendesha viwanda hivyo kwa ufanisi mkubwa zaidi kuliko ilivyo hivi sasa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi iliielekeza Serikali kuhakikisha kwamba usambazaji umeme vijijini unakamilika kufika mwaka 1922. Na Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni kupitia Bunge hili Waziri mwenye dhamana ya nishati amekuwa akitueleza kwamba jukumu hili litakwenda kukamilika 2022 lakini pia ametupa mpaka namba za wakandarasi ili tufuatilie mwendelezo wa usambazaji umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo masikitiko makubwa kwamba pamoja na agizo hilo, lakini sio vijiji vyote ambavyo vimeingizwa katika mpango huu; hivi tunavyozungumza wakandarasi wapo site lakini wanaruka baadhi ya vijiji kwa maana kwamba hawajapewa scope. Na zaidi ya hilo, badala ya nguzo 40 ambazo zilikuwa zinatolewa kwenye kila Kijiji sasa wanatoa nguzo 20. Sasa nilitaka kufahamu ni ipi kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2022 nchi nzima itakuwa inawaka umeme? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imeazimia kupeleka umeme kwenye vijiji vyote na bado tumeweka dhamira ya kupeleka umeme mpaka vitongojini ikiwemo na maeneo ya visiwani. Utaratibu ambao tumeuweka ndani ya Serikali kwa zoezi hilo la kusambaza umeme, tunaenda kwa awamu na sasa tupo kwenye awamu ya tatu na hii awamu ya tatu tumeigawa kwenye awamu mbili; awamu ya tatu moja na awamu ya tatu mbili. Awamu ya tatu mbili imeanza siku za karibuni na wakandarasi tumeshawasambaza kwenye halmashauri zote ili kukamilisha vijiji vyote vilivyobaki vipate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye awamu ya tatu hii mbili tumeongeza mkakati ambao nimeueleza awali wa kupeleka umeme kwenye vitongoji na kwenye visiwa kama vile kule Ukerewe, Mafia na maeneo mengine ya visiwa. Mkakati huu tayari umeshatangazwa, zabuni zimetolewa, wakandarasi wamepatikana, ujenzi wa umeme utaanza kazi mara moja. Lengo letu ni kupeleka umeme kila Kijiji na kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote ikiwemo na visiwani ambapo tunaweza tukapeleka umeme jua ili nao wapate pia umeme kwa ajili ya matumizi ya kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, dhamira ya Serikali bado imebaki palepale na nakumbuka mwezi wa pili nilikuwa Mlalo kwa Mheshimiwa Shangazi kwa hiyo inawezekana ameuliza swali hili kama alivyokuwa amechangia siku ile kwenye mkutano wa hadhara na nikamhakikishia kwamba Serikali itapeleka umeme kwenye Jimbo la Mlalo lote, vijijini mpaka vitongojini. hivyo ni pamoja na nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme vijijini uko imara na sasa hivi tume-cover sehemu kubwa sana; tumebaki na vijiji vichache sana ili tuweze kuvimaliza vijiji vyote, kazi inaendelea na kwa kweli kazi inaendelea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JUSTINE L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi za dini zimekuwa zikikumbwa na adha kubwa, vikwazo vingi na urasimu wakati wa kushughulikia misamaha ya kodi wanapopata vifaa au misaada mbalimbali kutoka nje ya nchi na kusababisha wakati mwingine vifaa hivyo kukaa muda mrefu bandarini na kuingia tena tatizo la storage charges ambazo mwisho wake wanashindwa kuvitoa.
Ni nini kauli ya Serikali kuhusu tatizo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka utaratibu wa kutoa misamaha kwa baadhi ya taasisi zinazotoa huduma za jamii, zinazolenga kuisaidia Serikali katika utoaji wa huduma hizo. Na misamaha hii ambayo inatolewa inaratibiwa na taasisi zetu zote kama inatoka nje ya nchi inakuja nchini kuanzia mahali pa forodha kama ni bandarini, airport na maeneo mengine taratibu zimeandaliwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala la urasimu ambalo Mheshimiwa Mbunge amelieleza linatokana pia na wale wenye hizo bidhaa/mali inayoingizwa nchini kwa au kutofuata utaratibu na kuratibu jambo zima bila kufuata utaratibu wake hilo pia nalo linaweza kusababisha kuwa na urasimu wa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, bidhaa hizi zinaposafirishwa kutoka nje ya nchi kuingia ndani ili ziweze kupata msamaha, hawa wenye bidhaa hiyo taasisi ya kidini au taasisi yoyote ambayo inapata msamaha ni lazima iwe imeandaa utaratibu wa kupeleka maombi lakini pia kupeleka idadi ya orodha ya mali zinazofuata.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzoefu ambao tumeupata Serikalini ni kwamba watu wanaweza kuomba msamaha lakini anachokileta nchini sio kile alichokiombea msamaha. Kwa hiyo, kunakuwa na hatua ndefu ambazo wengine wamesema kwamba hii ni urasimu wa Serikali, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito sasa kwa taasisi ambazo zinapata misamaha, kwanza kueleza kikamilifu wanataka kuleta nini ambacho kinatakiwa kipate msamaha lakini bidhaa hiyo inayoletwa kwa misamaha lazima ikidhi matakwa ya Serikali kwamba lazima iende ikatoe huduma ambayo inakusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuondoa urasimu ni lazima taratibu hizi zifuatwe mapema ili mzigo unapofika kwenye vituo basi uweze kutoka mara moja. Kwa hiyo, tunaendelea kusimamia taratibu hizi huwa zinakamilka na kwa wito nilioutoa kwa wateja wetu kuhakikisha wanafuata taratibu kwa mapema zaidi ili mzigo unapofika uweze kutoka mara moja. Tumejipanga vizuri na tumetoa maelekezo bandarini, viwanja vya ndege na kwenye mipaka yetu kote nchini ili wateja wetu wapate huduma za haraka sana ikiwemo na wanaopata msamaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa majibu hayo kwa Mheshimiwa Nyamoga. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka za Wilaya zilizokuwa na ofisi maeneo ya mjini zilizo nyingi zilitekeleza maagizo ambayo yalitolewa na Serikali ofisi zao ziweze kuondoka pale mjini ili zipelekwe katika halmashauri zao. Na kitendo hiki kilifanya halmashauri nyingi na wananchi wengi kukosa huduma bora ambazo walizoea. Lengo la kuziacha pale mjini ilikuwa wananchi waweze kupata huduma na utawala bora kama ilivyokuwa lengo kubwa lakini kwenda kule kumeongezea kwanza umbali kwa sababu lazima wafike mjini ndio waende kule lakini pia gharama inakuwa kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyojua kule vijijini usafiri ni wa mabasi, mabasi yanatoka asubuhi alfajiri yanafika na yanarudi mchana kwa hiyo akikosa huduma kwa wakati anashindwa kurudi kwa hiyo inamlazimu kulala. Je, nini kauli ya Serikali ya kuwapunguzia wananchi adha hii na kuhakikisha kwamba wanapata huduma kwa gharama nafuu na kwa utawala bora uweze kutekelezeka. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la mheshimiwa Tendega, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, anachokisema Mheshimiwa Mbunge ni agizo la Serikali la Halmashauri hasa za Wilaya ambazo zilikuwa kwenye Makao Makuu ya Wilaya zake ambapo pia waliacha wahudumiwa wako mbali na maeneo ya kutolea huduma. Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wa Awamu ya Tano alitoa maelekezo kwamba Halmashauri za Wilaya ziondoke kwenye Halmashauri za Miji walimo badala yake wajenge kwenye Halmashauri za Wilaya hukohuko ambapo wananchi walipo kwa lengo la kutoa huduma kwa urahisi ili kumuondolea gharama mwananchi aliyepo kwenye halmashauri hiyo. Kwa hiyo, lengo ilikuwa ni kumuondolea gharama mwananchi aliyepo kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wapi makao makuu hiyo inajengwa ilikuwa ni maamuzi ya wananchi wenyewe kupitia wawakilishi wao Baraza la Madiwani ambalo pia lenyewe limejadili pamoja na watalaam na kuchagua maeneo ya kujenga. Baada ya uchaguzi huo, sasa ujenzi utaanza na Serikali tulikuwa tunapeleka fedha na tumepeleka fedha; tumeanza awamu ya kwanza kugawa fedha kupeleka kwenye halmashauri mpya ili wajenge Makao Makuu ya Halmashauri; tumpeleka pia awamu ya pili na tutapeleka awamu ya tatu kwa sababu bado hatujakamilisha halmashauri zote. Lakini bado kuna halmashauri ambazo pia zina miundombinu kongwe, nazo pia tunazijengea makao makuu mpya. Kwa hiyo, tutapeleka pia na fedha kwenye halmashauri kongwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, malengo yetu ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma hizi kwa ukaribu kuondoa gharama uliyoisema kwa kupeleka mahali ambapo wao wamepanga na ndiko kunawarahisishia kupunguza gharama hizo, hayo ndio malengo. Sasa inawezekana pia huko wamepanga vinginevyo inawasababishia wengine kuwa na gharama kubwa lakini ni jukumu lao kupanga wapi wanaweza kujenga Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua yapo maeneo ambayo jiografia yake haiwezekani; Wilaya kama Uyui tulipata shida sana tulipoamua wajenge makao makuu maeneo yalipo sasa kwa sababu Halmashauri ya Uyui iko kama yai imezunguka Manispaa ya Tabora. Kwa hiyo, mtu anayetoka huku lazima apite Makao Makuu ya Mji ili aende kwenye Makao Makuu mpya. Zipo halmashauri jiografia yake ni ngumu lakini lazima tuanze mahali halafu tuende mahali vizuri. Kwa hiyo, tutaendelea kusikiliza maeneo yote yenye jiografia ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hivi karibuni nilikuwa Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma, nilikuta hiyo, Halmashauri ya Mbinga Vijijini ambayo Mheshimiwa Mbunge hapa yupo ramani/jiografia yake ni ngumu kidogo, popote utakapoweka Makao Makuu ya halmashauri, lazima kutakuwa na mgogoro lakini bado tunapokea changamoto hiyo na tutaifanyia kazi. Malengo ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma hizo ili iwarahisishie katika kutoa huduma na wananchi wapate huduma kwa ukaribu kwa gharama nafuu, hayo ndio majibu ambayo kwa sasa Serikali inayafanyia kazi. (Makofi)
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba tumekuwa na Benki ya Kilimo na Tanzania Investment Bank ambazo zimekuwa na riba kubwa vilevile mtaji wake ni kidogo. Lakini pia tumekuwa na mifuko ya kuchochea maendeleo mingi. Je, Serikali haioni kama tuna haja ya kuwa na mfuko wa kuchochea maendeleo ya kilimo na viwanda ili wananchi waweze kwenda kupata mikopo ya kujiwezesha kujiendeleza katika kilimo na viwanda kwa riba nafuu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kainja, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anahitaji kujua mkakati wa Serikali wa kuanzisha mfuko ambao unaweza kutoa mikopo kwa urahisi na kwa gharama nafuu hasa kwenye riba baada ya kuwa ameringanisha uwepo wa benki TADB na TIB. Ni kweli kwamba Serikali inaendelea kuhamasisha taasisi za fedha zote pamoja na mifuko mbalimbali inayolenga kukuza kilimo, ili iweze kuwafikia wakulima wadogowadogo, wa kati na wakubwa ambao watawekeza kwenye viwanda na mashamba yenyewe iliwaweze kupata mikopo tena kwa riba nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho kinafanyika sasa ni kwamba mazungumzo yetu kati ya Serikali na mabenki binafsi tumekubaliana mabenki haya kutoa mikopo tena wajitahidi kupunguza riba na hata Mheshimiwa Rais juzi amesisitiza benki zipunguze riba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, tukasema tuanzishe benki yetu inayoshughuikia kilimo ili iweze kutoa mikopo kwa gharama na riba nafuu. Na tunayo tayari TADB ambayo inashughulikia kilimo lakini tuna benki ambayo pia Mheshimiwa Mbunge ameitaja TIB (Tanzania Investment Bank) ambayo pia na yenyewe ina eneo linashughulikia kilimo. Wakati huohuo tunayo mifuko mingi sana imejikita kwenye maeneo mbalimbali ambayo sasa tunaishughulikia ili kuipunguza idadi kubwa ya mifuko ili tuwe na mfuko angalu mmoja utakaokuwa unashughulikia kuratibu shughuli za kilimo kwa kukopesha na kuhakikisha kwamba inahudumia sekta nzima ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hili litakapokamilika, sasa tutakuwa na mfuko unaoshughulikia kilimo ambao ni wetu wenyewe Serikali ambao pia utakuwa unaungana na Benki yetu ya Kilimo na mabenki mengine ili ihudumie wananchi wa kawaida wanaojishughulisha na kilimo kuanzia kule kwenye ngazi za vitongoji, vijiji na wale wakulima wakubwa ambao pia wanawekeza kwenye viwanda vinavyochakata malighafi za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, malengo yetu sasa ni kihakikisha kwamba Sekta ya Kilimo inakua kwa kasi na juzi nilikuwa Mkoani Singida kuzindua kampeni ya kilimo cha alizeti nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya mambo makubwa ambayo wadau walichangia ni kukosekana kwa mitaji ya kuanzisha kilimo lakini nimetoa maelekezo kwa mabenki yetu na tulikuwa na mabenki pale ikiwemo na hizi benki zetu ambazo tunazo mpaka vijijini kama vile CRDB, NMB lakini pia tuna NBC, Azania Bank na hiyo TIB na TADB yenyewe kuhakikisha kwamba inakuwa na matawi mpaka ngazi ya wilaya na inatangaza hiyo fursa ya wakulima kwenda kukopa lakini pia kila benki ihakikishe inawezekana pia inapunguza riba zao ili ziweze kuwawezesha wakulima kumudu kukopa na kurejesha kwa wakati. Wakati mwingine nao wasaidie pia namna ya kuzipata hizo fedha kwa sababu iko tabia ya kila mmoja anataka kukopa lazima awe na andiko, mwananchi wa kawaida hajui andiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumesema lazima waanzishe dawati la kusaidia kutengeneza hilo andiko na halmashauri nazo tumeziagiza na zenyewe ziwe na maafisa wanaoshughulikia namna ya kumuwezesha mkulima kuwa na andiko linalomuwezesha kupata mikopo. Haya yote yatapelekea sasa kwenda kutoa huduma kwa wakulima ili waweze kulima lakini kutoa huduma kwa wawekezaji wa sekta ya kilimo wapate mikopo na wawekezaji kwa kiwango cha kati nao wapate mikopo ili mkakati wetu wa Serikali wa kuboresha kilimo nchini uweze kushamiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, malengo yetu ya Serikali ambayo pia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza ni kuhakikisha kwamba kilimo kinashamiri nchini ili sasa maazimio ya uchumi wa mtu mmoja mmoja yatatokana na kila mmoja kujishughulisha kwenye kilimo kwa kupatiwa mitaji na vinginevyo. Kwa hiyo, Serikali tunaendelea na utaratibu huo ili tuweze kutoa mikopo kwa wakulima wetu kwa riba nafuu, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe Sita ya mwezi Aprili Mheshimiwa Rais katika shughuli ya kuapisha Makatibu Wakuu alitoa kauli ya kusikitishwa kwa jinsi wawekezaji wanavyokwamishwa kwenye vibali vya kazi. Katika kauli yake alitoa maelekezo ya Serikali kutengeneza utaratibu mzuri wa kuwasaidia wawekezaji kutopata mkwamo katika suala la vibali vya kazi ili kuweza kuboresha uwekezaji. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kauli hii imepokelewa kwa furaha sana na wawekezaji wengi na imetoa sura mpya katika sekta ya uwekezaji nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya maeneo kauli hii imechukuliwa tofauti na baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waadilifu wameanza kuleta wafanyakazi kwenye maeneo ambayo wazawa wanaweza kufanya kazi hizo. Mfano ni marubani kwenye baadhi ya kampuni binafsi za ndege. Naomba kujua kauli ya Serikali, ni nini mkakati wa kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais katika kuwaondolea vikwazo na urasimu wawekezaji kupata vibali vya kazi, wakati huohuo kuendelea kutimiza matakwa ya sheria The Non- citizens Employment Act, 2015 Kifungu cha 11(2) ambacho kinalinda ajira za Watanzania kwenye maeneo ambayo wana uwezo wa kufanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameeleza utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa alipokuwa anawaapisha Makatibu Waku una hasa katika kuboresha uwekezaji nchini. Uwekezaji nchini ni mkakati mpana kwa sababu kwanza tunahamasisha kujenga uchumi wetu na katika ujenzi wa uchumi moja ni kukaribisha wawekezaji wa nje na ndani ya nchi kwenye uwekezaji lakini wawekezaji hawa nao wanao watu ambao wanaamini wanawaamini kushiriki kwenye shughuli zao za uendeshaji wa uwekezaji wao. Sasa nasi Serikali tumeweka sheria kidogo kwa wawekezaji ambayo haipanui wigo mpana ukapoteza fursa ya Watanzania kushiriki kwenye uwekezaji huo ikiwemo na ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anapotaka kujua tunachukua hatua gani ya wale ambao wanatumia nafasi hii vibaya, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa bahati nzuri hili jambo lipo ofisini kwangu na tunalisimamia vizuri. Kwanza tunahamasisha wawekezaji wote kuja nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali kwa fursa tulizonazo lakini mbili tunawahamasisha Watanzania kushiriki kwenye uwekezaji huu ili na wao wawe sehemu ya ujenzi wa uchumi kupitia uwekezaji. Pia kwenye uwekezaji huu tumetangaza fursa zilizopo ajira lakini pia bidhaa tunazozalisha kuwa kama malighafi ya uwekezaji huo ikiwemo na kilimo na vinginevyo kwamba Watanzania washiriki huko ili waweze kunufaika na uwekezaji huu kwenye maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pale ambapo Mwekezaji anataka kuja kuwekeza na fedha yake lakini ana idadi ya watu anaotaka kufanya kazi, nalo pia tumeliangalia kwamba mwekezaji huyu asije akaleta idadi kubwa halafu akapoteza fursa za Watanzania kuingia pia kwenye ajira. Nini tunakifanya sasa tunatengeneza sheria na maboresho ya sheria zetu zinazoweza kuwafanya wawekezaji wasikwazwe kuwekeza nchini lakini na sisi Watanzania tusipoteze fursa ya kuweza kuajiriwa ili tuweze kwenda pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, matumizi ya fursa hiyo vibaya nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunasimamia vizuri na hasa maboresho ambayo tunayafanya kwenye uwekezaji. Maboresho haya yana nia njema sana hasa katika kutoa fursa kwa Watanzania kwenye maeneo mengi tu, kwamba maeneo haya yote ambayo tunayalenga yaweze kuwanufaisha Watanzania, ndiyo malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo Mheshimiwa Mbunge asiwe na mashaka maelekezo ya Mheshimiwa Rais tumeyapokea na tunayasimamia ili yasitumike vibaya na wale wenye nia mbaya kwenye maeneo haya. Haya ndiyo malengo ya Serikali kwa hiyo niendelee kutoa wito kwa wawekezaji waje nchini tuna ardhi ya kutosha, maji, umeme, malighafi ya kutosha lakini pia tuna labor inayojituma sasa ya Watanzania kwamba mwekezaji akija Tanzania hawezi kujuta kwa nini amekuja kuwekeza Tanzania. Tunaanza kuona idadi kubwa ya wawekezaji wanakuja na huduma wanaendelea na wanapata vibali kwa siku chache sana kutoka siku wanapoomba kuwekeza hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara zetu za Uwekezaji na Viwanda na Biashara lakini pia Wizara yetu ya Ardhi zote hizi zinafanya kazi kwa pamoja ili kumwezesha mwekezaji kupata huduma yake kwa haraka sana. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali la kwanza kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera yetu ya Elimu hasa elimu ya msingi imeelekeza kwamba elimu ya msingi ni bure kuanzia ngazi ya msingi; na zoezi hili lilikuwa linafanyika vizuri sana, tunaipongeza sana Serikali kwa hatua hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu nilitaka kuufahamu, ni upi mkakati wa Serikali katika Sera ya Afya angalau sasa katika afya msingi kwa maana ya zahanati na vituo vya afya kuweka eneohili tupate huduma za afya bure?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu imeandaa sera upande wa elimu na kuifanya elimu sasa ipatikane bure kuanzia elimu ya awali mpaka kiwango cha sekondari, kidato cha nne na mkakati huu unasaidia sana kuwapunguzia wazazi gharama za kumpeleka mtoto shule na huku tukiwa pia tumeweka ulazima wa kila mtoto wa Kitanzania kupata elimu ya msingi ambayo kwa sasa inaenda mpaka kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua nini mpango wa Serikali wa Sera aina ile ile ya elimu kuifanya pia kwenye sekta ya afya ili tuweze kutoa huduma za afya bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kueleza kwamba tunaendelea kufanya mapitio ya sera zetu na hasa kwenye sekta ya huduma za jamii ili Serikali yetu iweze kutoa ikiwezekana unafuu mkubwa kwenye utoaji wa huduma za jamii kwa Watanzania ikiwemo na sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pindi tutakapofanya mapitio haya na kukamilisha kuona uwezo wa kifedha wa kugharamia kwa upande mwingine, kwa maana ya kupata vifaa tiba, utafiti na maeneo mengine yote, Serikali itatoa tangazo wakati pale tutakapokuwa tumekamilisha utafiti huo ambao sasa hivi wataalam wetu wanaufanyia mapitio, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba na mimi nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu mazuri ya swali lililopita lakini naomba nimuulize juu ya changamoto ambazo zipo katika matumizi ya Sheria ya Road Traffic (Road Traffic Act), ile Cap 168 pamoja na Kanuni zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na matatizo ya matumizi ya barabara hasa kwa waendesha pikipiki/ bodaboda ambao wanakiuka sheria zilizopo katika mahitaji ya jinsi gani ya kuendesha vyombo vyao. Na sasa imezidi pale Dar es salaam hasa watumiaji wa barabara za mwendokasi, madereva wa mwendokasi wanapita kwenye taa nyekundu; hadi jana usiku saa moja na nusu wameua vijana wawili.
Ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha watumiaji wote wa vyombo vya moto barabarani wanafuata sheria na kwamba polisi/trafiki wanasimamia sheria zile ipasavyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hizi ambazo tumeziweka sisi hapa Bungeni tunatarajia kwamba kila Mtanzania atakuwa anatekeleza wajibu wake bila ya kushurutishwa. Matumizi ya barabara yameainishwa kikamilifu kupitia sheria zetu na usimamizi unaendelea pia kwa vyombo ambavyo tumevipa jukumu la kusimamia kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini usimamizi wa sheria hautakiwi usimamiwe na Jeshi la Polisi peke yake tu, kila Mtanzania anatakiwa kufuata sheria pale ambapo sheria imeshatungwa na inataka itekelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba watumiaji wa pikipiki walio wengi hawajali matumizi haya ya sheria zetu na kujali kwamba sheria hizi ni lazima zitekelezwe. Lakini pia Jeshi letu la Polisi linacho kitengo kinatoa elimu kila siku, na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mnajua kwenye televisheni zetu za TBC, ITV, Star TV lakini pia Azam tumetengewa muda na Jeshi la Polisi linafanya kazi hiyo vizuri sana, kuelimisha Watanzania kuhusu matumizi sahihi ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunasimamia sheria hizi nitoe wito kwa watumiaji wa barabara hasa watumiaji wa vyombo vya moto wote kwamba ni muhimu sana kuzingatia Sheria za Barabarani. Hii ni muhimu sana kwa sababu inalinda uhai wa Watanzania wote, kuanzia yeye mtumiaji wa chombo chenyewe cha moto, watumiaji wa njia hizo wanaotumia kwenda kwa miguu lakini pia pamoja na wale wanaotumia barabara hizi za mwendokasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu njia hii ya mwendokasi tumeshaieleza wazi, kwamba njia hii tumeitenga maalum kwa ajili ya magari ya mwendokasi, lakini pia tumetenga njia nyingine kwa ajili ya magari yetu ya kawaida. Tumejenga na njia ya pembezoni ya watembeaji wa miguu pamoja na vyombo vingine vya moto. Kwa hiyo, ni wajibu wetu Watanzania kutekeleza sheria, ikiwemo na kujali matumizi ya barabara zetu hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati wa Serikali hapa ni kuendelea kutoa elimu na kusimamia sheria. Pale ambapo tunaona kuna mtu anavunja sheria, hatua za kisheria zinachukuliwa hapohapo; huo ndio mkakati ambao tunao kwa sasa. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2017 Serikali ilikuja na utaratibu wa upigaji chapa kama eneo la kutambua mifugo nchini. Zoezi hilo lilikuwa na changamoto zake ikiwepo chapa hizo kupotea au kufutika pamoja na ngozi kukosa ubora. Kupitia Bunge lako Tukufu, Bunge liliitaka Serikali kuja na namna bora ya utambuzi wa mifugo. Mwaka huu Serikali imekuja na utaratibu mpya wa kuvalisha hereni mifugo; zoezi ambalo limeanza tarehe 17 mwezi wa Nane mwaka huu kwenye baadhi ya mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi hilo ni zuri kwa sababu lina barcode ya nchi, mkoa, wilaya na jina la mfugaji. Hata hivyo, changamoto kwenye zoezi hilo ni pamoja na gharama ya shilingi 1,750 kwa kila ng’ombe. Lakini ng’ombe huyo akipoteza hereni mfugaji analazimika tena kulipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nia ya Serikali ni njema na itakwenda kuondoa wizi wa mifugo uliopo sasa hivi. Serikali haioni kuwa ni vyema iende ikafanye tathimini upya ione namna bora kwanza kupunguza gharama lakini kuona namna bora wataweka hiyo hereni na isiweze kuondoka kwenye mifugo? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imetafuta njia nzuri sana ya kufanya maboresho ya utambuzi wa mifugo yetu, ng’ombe wakiwemo. Na mfumo huu ulitokana na tatizo kubwa sana la wizi wa mifugo hapa nchini pamoja na kukosa takwimu sahihi za mifugo yetu hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetafuta njia kadhaa za kuweza kutambua na kupata takwimu za ng’ombe hawa. Awali tulikuwa tunatumia njia ya kupiga chapa, lakini tumegundua kwa kupiga chapa tunapoteza ubora wa ngozi ambapo ngozi zetu sasa nchini Tanzania haziuziki nje; na hata tulipoanza kutumia Kiwanda chetu cha Kilimanjaro Leather kwa kutengeneza viatu, ngozi zote zilizopigwa chapa hazitumiki vizuri kwa sababu zenyewe zimepoteza ubora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumetafuta njia nzuri ya kuweza kutambua hawa ng’ombe, tukaamua kutumia njia ya kuvalisha hereni. Kwanza mwanzo tulikuwa tunatoboa lakini sasa hatutoboi bali tunaibandika. Inawezekana pia ng’ombe mmoja mmoja kutokana na kupita kwenye majani na miti hereni zinadondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia kikao cha juzi cha mifugo ambacho mimi mwenyewe nilikuwa mgeni rasmi na mjadala uliofanyika kwenye kikao kile juzi pale Jijini Dar es salaam, kwenye eneo hili Wizara ya Kilimo wameondoa hizo tozo; endapo ulinunua kwa mara ya kwanza na sasa ng’ombe amepoteza herein. Tunachofanya ni kurudi tena kwenye mtandao na kujaza zile data zote kwenye hereni mpya tunampa mfugaji ili ng’ombe aendelee kuwa na ile alama aendelee kutambulika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hatua nzuri ya kumuondolea gharama mfugaji ni hiyo ya kumrudishia tena ile hereni ili aweze kuivaa. Pili, hereni hii tumekuwa makini sana, hatutoboi tena bali tunatafuta namna ya kuigandisha vizuri pamoja na ile spring inabana vizuri kiasi kwamba hata akiwa na pilikapilika haiwezi ikadondoka kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaendelea kutafuta njia nzuri zaidi ya hiyo. Niseme sasa kwamba tumepokea mawazo yako, na uzoefu ambao tumeuona kupitia wafugaji wetu kwamba hizi zinadondoka na kunakuwa na shida tena kurudi ofisini kupata hereni nyingine, kwa hiyo tunatafuta njia nzuri zaidi ya kutambua ng’ombe hawa kwa kuweka alama ambayo haitaharibu ubora wa masikio ya ng’ombe lakini pia haitasababisha gharama tena kwa mfugaji ili gharama ile ile aliyoitumia kwa mara ya kwanza iendelee kutumika kama alama ya kumtambulisha ng’ombe huyo. (Makofi)
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi yana maeneo makubwa ya kiutawala nchini kwetu; kwa mfano, Mikoa ya Tabora, Tanga na Morogoro. Mkoa wa Morogoro una hususan wa square meter 73,000 ambazo ni kubwa sana. Sasa zile zinafanya kwamba ule mkoa ushindwe kutimiza adhma yake ya kuhudumia watu wake kikamilifu. Kwa mfano, kuna baadhi ya maeno hayafikiki kabisa huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa maeneo haya hayafikiki na huduma zinakuwa ni hafifu.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kugawa haya maeneo hatimaye huduma za jamii ziweze kufika kila eneo kwa urahisi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamguna, Mbunge kama ifuatavyo, samahani kama nimekosea jina.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo ukweli kwamba tulikuwa na nia ya kugawa maeneo mapya ya utawala, hasa baada ya kugundua kwamba kuna maeneo makubwa sana kuliko huduma ambazo zinatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Morogoro, Tanga na Tabora ni miongoni mwa mikoa mikubwa sana ambayo pia tumepata taarifa kwa maandishi lakini pia kupitia vikao mbalimbali wakiomba kuyatenga tena maeneo hayo na kuongeza maeneo ya utawala kwa lengo la kurahisisha utoaji huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tulisitisha kidogo kutoa maeneo mapya ya utawala na kutaka kuimarisha maeneo yale ambayo tumeikabidhi mamlaka hiyo, kwa maana ya vijiji, kata, wilaya hata halmashauri na mikoa mipya ili iwe na miundombinu ya kutosha na kuwapeleka watumishi wa kutosha kuweza kuhudumia maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini mpango wa Serikali kwa sasa, tunasubiri sensa hii inayokuja mwakani ya mwaka 2022 iweze kutupa takwimu halisi ya idadi za idadi ya wakazi ili pia tuone idadi ya watumishi ambao tumewapeleka kuwahudumia na miundombinu tuliyoipeleka kuhudumia wananchi hao halafu tutafanya maamuzi kulingana na ukubwa huo na vigezo hivyo ambavyo tutavitumia kuweza kutoa maeneo haya mamlaka mpya. Hii ndiyo sababu kwa sasa hatujaruhusu tena kutoa mamlaka mpya kwenye maeneo mengine mapya kwa sababu hiyo. Kwa hiyo, baada ya sensa Serikali itafanya maamuzi ya kuona umuhimu wa kugawa maeneo hayo kulingana na vigezo vile ambavyo tumeamua kuvitumia, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kumekuwepo na uhaba wa rasilimali watu kwenye taasisi za idara mbalimbali za Serikali, mathalani kada ya walimu, watumishi wa afya na kwenye majeshi yetu; Jeshi la Polisi, Magereza na JWTZ kitu ambacho kinapunguza ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi. Hata jana Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani alikiri kabisa kwamba kuna upungufu ambao unapelekea hata kufunga vituo vya polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua kwa kutangaza ajira 3,000 kwenye Jeshi la Polisi lakini kuna masharti ambayo yameambatana, kwanza wamesema ni ambao wamemaliza JKT na JKU lakini sharti namba tano na sita linaeleza kwamba ni wale vijana waliomaliza form four na form six kati ya mwaka 2017 na 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kwamba ajira zilisitishwa tangu mwaka 2015 na kuna vijana ambao wamemaliza form four na form six kati yam waka 2015/2016 na wameenda JKT na JKU na zaidi wamejenga Taifa letu kwa mfano Oparesheni Magufuli, Operesheni Makao Makuu na Operasheni Mererani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwa nini sasa Serikali isifanye rejea kwenye tangazo lao la ajira ambalo lina-limit vijana hawa wa 2015/2016 ili liweze kuwa-accommodate na wao? Kwa nini wasiseme kwamba ajira inatolewa kwa vijana wote wenye sifa kuanzia waliomaliza form four na six 2015 mpaka 2020? Mfano Iringa na Mbeya wamewakataa walivyoenda kwenye usaili. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali inaendelea na zoezi la kuajiri watumishi wa sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo na hayo matangazo aliyoyasema ya Jeshi la Polisi. Sina uhakika na vigezo hivyo na wito walioutoa kwamba wanataka waajiri vijana kuanzia mwaka gani lakini tuichukue hiyo kama ushauri kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo sasa inasimamia ajira hiyo ili waanze kufanya mapitio ya ajira hiyo na vigezo ili pia hawa waliomaliza jeshi kuanzia mwaka 2015 nao waingie halafu wachujwe wote tupate vigezo na tuweze kuwapata wale ambao wana sifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua pia tulikuwa na hilo kundi la Operesheni Magufuli na Operesheni Mererani na wote waliahidiwa kuingia kwenye orodha ya ajira na kama miongoni mwa hao walianza mwaka 2015 na kumaliza 2016 na hao walioanza kuchukuliwa 2017 mpaka sasa basi Wizara naona itatimiza wajibu wake kuwaita wote halafu iwachuje waweze kupata ajira pia. Kwa hiyo, tunaupokea ushauri wako na Waziri wa Mambo ya Ndani yuko hapa atalichukua hilo kwa ajili ya kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamekuwa na wizi wa ng’ombe uliokithiri katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Mfugaji mara nyingi anapopata tatizo lolote anatumia ng’ombe wake kumsaidia na hao ng’ombe wamekuwa wakitolewa mkoa mmoja hadi mwingine pamoja na kuwa na chapa hizi alizozijibu katika swali la mwanzo.
Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na wizi huu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti wizi wa mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote kwamba vyombo vyetu vya ulinzi nchini vimeendelea kufanya kazi kubwa sana na nzuri ya kudhibiti matukio ya uhalifu kote nchini ikiwemo la wizi wa mifugo na matukio mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la mifugo tunaendelea na udhibiti huo na tumetafuta njia rahisi ya kuweza kupunguza matukio haya. Moja, ni ile njia ambayo nimeijibu muda mfupi uliopita ya kuweka alama mifugo hii ili iweze kutambulika ni ya nani, ya eneo gani ili pale inapopotea tunaweza kuipata. Pia, tumeendelea kushirikisha wananchi kwenye ulinzi shirikishi kwa matukio yote ikiwemo wizi wa mifugo na wa namna nyingine yoyote ya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatujaishia hapo, tumeendelea pia kushirikiana na wafugaji hawa kuhakikisha kwamba tunaweza kuimarisha ujenzi wa maeneo wanayoishi mifugo hii kwa mfano maboma yao, tumekuta maeneo mengine maboma yao wanazungusha tu miiba peke yake lakini ni rahisi ng’ombe hata kuruka na kuondoka na baadaye tunasema wameibiwa lakini kumbe boma lile siyo imara sana. Kwa hiyo, tumeendelea kutoa elimu ya uimarishaji wa maeneo hayo wanayohifadhiwa ng’ombe ili kuzuia wizi na wakati mwingine ng’ombe wenyewe kutoroka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tumedhibiti sana vibali vya usafirishaji holela kutoka eneo moja mpaka eneo lingine. Kama mwizi anaiba ng’ombe eneo A anawapeleka eneo B bila ya ukaguzi inakuwa ni rahisi sana sasa tulichofanya ni kudhibiti usafirishaji wa ng’ombe kutoka eneo moja mpaka lingine. Sasa ng’ombe hawezi kuhama kutoka kijiji kimoja mpaka kingine bila ya kibali maalum kinachotambulisha mwenye mifugo na kule anakokwenda. Hii ndiyo ambayo inasimamiwa sana kwa sasa ili kuweza kupunguza wizi wa mifugo kwenye maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kutoa elimu kwa wafugaji lakini tunaendelea pia kufanya mikutano ya wafugaji kama nilivyosema ili haya mengine yote yanayojitokeza katika udhibiti wa wizi wa mifugo yaweze kupungua kwa kiasi kikubwa huku vyombo vya ulinzi vikiendelea na kazi yake ya ulinzi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa fursa ulionipatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu na kwa sasa kuna changamoto kubwa ya kupanda kwa bei ya pembejeo nchini na hii ipo kwenye pembejeo zinazohusu mazao mbalimbali ikiwemo mahindi. Suala hili limekuwa tatizo kubwa kwa nchi nzima lakini pia kwenye mikoa yetu ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo na Mufindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mfano mbolea ya DAP kwa maeneo ya kule kwetu ni zaidi ya shilingi 100,000 wakati huo bei ya mahindi ni karibu shilingi 5000 yaani inakuhitaji ubebe karibu debe 20 za mahindi ili urudi na mfuko mmoja wa mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni upi mkakati wa Serikali wa muda mrefu na muda mfupi katika kutatua changamoto hii ambayo ni kero kubwa sana kwa wananchi wetu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kihenzile, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sasa hivi tunapata tatizo kubwa la upatikanaji wa mbolea; tatizo hili sio la Tanzania tu ni duniani kote kwa sababu uzalishaji umepungua sana. Jitihada za Serikali katika kuhakikisha tunapata mbolea ya kutosha zinaendelea na mwezi mmoja uliopita nilikuwa na Waziri wa Kilimo nchini Morocco ambako pia kuna kiwanda kinazalisha mbolea nyingi inayosambazwa karibu duniani kote na tumegundua kwamba mahitaji ni makubwa mno na kwa hiyo hata bei zake nazo zimepanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bei ya mbolea sasa duniani kote iko juu lakini mpango wa muda mfupi ambao tumeutumia ili kupata mbolea angalau iweze kushusha bei ni kutoa ruhusa kwa wafanyabiashara kuingiza mbolea hapa nchini. Tunaamini kwa kuleta mbolea kwa wingi na kwa ushindani inaweza ikasaidia kidogo kupunguza bei badala ya bei hii ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge inaweza kuwa bei ya chini ya kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama njia ya muda mfupi sisi wenyewe hapa nchini tumeazimia kutoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza viwanda vya kutengeneza mbolea hapa. Mpaka leo hii tuna kiwanda kimoja tu kile cha pale Minjingu lakini bado tunazalisha kwa kiwango kidogo sana. Tumefanya jitihada za kupata wawekezaji kutoka nchi jirani ya Burundi na nimepata fursa ya kwenda kukutana na mwekezaji kulekule nchini Burundi tumezungumza na amekubali kuja hapa na tayari tumempa eneo hapa jijini Dodoma na ameanza hatua nzuri ya kuanza kuchimba msingi na ujenzi wa kiwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini uzalishaji mkubwa unaofanywa pale Burundi akija kuzalisha hapa tatizo la upatikanaji wa mbolea litakuwa limepungua sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwasihi sana wakulima kwamba Serikali inaendelea kufanya jitihada za kila namna kuhakikisha upatikanaji wa mbolea unakuwepo kwa kiwango kikubwa ili kupunguza bei ambazo mkulima anaweza kumudu kuipata na kuendelea na kilimo chake huku tukiwasiliana na nchi ambazo zinazalisha mbolea ili tuweze kupata mbolea kutoka maeneo yote. Kwa hiyo, tumetoa fursa kwa wafanyabiashara na pia Serikali kupitia Wizara ya Kilimo wanaendelea kuhakikisha kwamba tunapata mbolea ya kutosha kutoka nchi rafiki. Hizi zote ni jitihada za kuhakikisha kwamba tunapata mbolea na ikiwezekana tupate mbolea itakayoanza msimu huu wa kilimo. Huo ndiyo mpango wa muda mfupi na muda mrefu ambao tunautumia kwa sasa. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana nami kupata nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, magonjwa yasiyoambukiza; cancer, moyo na figo, yamekuwa yakitesa sana wananchi na yana gharama kubwa sana: Je, ni lini Serikali itaamua kuleta ile Bima ya Afya kwa wote ili kupunguza maumivu makubwa ambayo yanawapata kwa sababu gharama ni kubwa sana? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, Mbunge wa Mkoa wa Mbeya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba magonjwa haya sasa hivi nchini yamekuwa yanasumbua sana; cancer, magonjwa ya moyo, figo, pia hata BP, kisukari, ni miongoni mwa magonjwa ambayo Serikali kwa sasa imeyawekea msisitizo na mkazo kwamba yapewe kipaumbele katika kutoa tiba. Ndiyo maana kwenye sera yetu magonjwa haya kwenye maeneo mengi yanatolewa bure ili mgonjwa anapopata tatizo hili aweze kutibiwa bila gharama zozote.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mchakato wa kukamilisha kuanza kwa Bima ya Afya kwa Wote. Tayari hatua za awali mpaka Baraza la Mawaziri imeshapitishwa; uko upungufu kidogo unatakiwa uimarishwe. Kwa sababu tunazungumzia Bima ya Afya kwa Wote, tunaendelea kupata uzoefu na ushauri na wadau kwa sababu Serikali ilianza na Bima ya Afya ile ya jamii inaitwa CHF; yako mafanikio na pia upo upungufu. Pia, tukawa na Bima ya Afya ya wafanyakazi NHIF ambayo pia nayo tumepata mafanikio, lakini pia changamoto zipo.
Mheshimiwa Spika, tunapokuja kuzungumzia Bima ya Afya kwa Wote sasa tunaanza kupata ule uzoefu tulioupata kwenye CHF na NHIF ili tuone namna ambavyo tutapanua na kumfikia kila Mtanzania, kila mmoja kwa pembe zote nchini ili tunapoanza Bima ya Afya tusiwe na upungufu mwingi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo hatua ambayo Wizara ya Afya inaendelea nayo kwa kushirikiana wadau, wale ambao wanatoa Bima ya Afya kwenye taasisi mbalimbali nao; hizi taasisi za bima ya kawaida ambapo pia nao wanatoa huduma ya matibabu ili tuweze kuweka utaratibu ambao utatufikisha. Kwa hiyo, Serikali sasa ikishakamilisha magonjwa hay ana wenzetu ambao wanapata tatizo hili tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuhudumiwa. Kwa hiyo, nawaomba sana Watanzania mtuvumilie.
Mheshimiwa Spika, pia, Bunge letu tunaliomba lituvumilie, tukamilishe eneo hili ili tutakapokuwa tunaleta Bungeni tayari kwa kuanza, tuanze tukiwa tuna uhakika kwamba hatutakuwa na upungufu mwingi. Hiyo, ndiyo dhamira ya Serikali na tukishakamilisha hilo Muswada ule utaletwa hapa, utapitiwa na Waheshimiwa Wabunge ili tupate sasa mawazo yenu, mchango wenu na maoni yenu ya mwisho halafu tuidhinishe sasa Bima ya Afya kwa Wote iweze kuanza. Huo ndio utaratibu wa Serikali.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kumwuliza Waziri Mkuu swali. Kwa kuwa lengo la Sera ya Manejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, ilitengenezwa toleo la pili mwaka 2008 ili kuboresha utumishi wa Umma na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia watendaji wake kwa kuzingatia sifa na usimamizi unaotoa mwelekeo: Je, Mheshimiwa Waziri Mkuu…
SPIKA: Mheshimiwa naona kuna karatasi hapo mbele, kama vile unasoma. Hebu mwangalie Waziri Mkuu, halafu uliza swali.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, nilikuwa nataka kunukuu lengo la Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ambao unasisitiza kwamba watumishi wanaoajiriwa ni wale wenye sifa na ndio watakaosimamia matokeo tunayohitaji katika utendaji wa Serikali.
Na kwa kuwa tuna watumishi wengi wenye sifa katika ngazi ya kada za Watendaji wa Vijiji ambao wamefanya kazi hiyo kwa kujitolea kwa miaka mingi na kumekuwa na tatizo la kutoa vibali vya kuajiri:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaajiri ili kuondoa hiyo kero ya hawa watumishi ambao hawana ufanisi kwa sababu ni…
SPIKA: Ahsante sana. Umeeleweka Mheshimiwa.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tulianzisha mfumo ambao unaweza kuwafikia Watanzania wote katika kuajiri badala ya kuziachia sekta ambazo zilikuwa zinaajiri au kwa upendeleo au kwa namna ambayo wengi walikuwa wanalalamikia. Kwa kuunda Tume ya Ajira, tunakusanya nafasi kwenye taasisi zote zinazoombwa, tunaziombea kibali kwenye mamlaka. Tukishatoa kibali, Tume yetu inatoa tangazo Watanzania wanapata nafasi ya kuomba na kuitwa kwa ajili ya usaili halafu wanaweza sasa kuajiriwa.
Mheshimiwa Spika, hawa ambao wanafanya kazi kwa kujitolea kwenye maeneo yetu ya vijiji, kata na pia kwenye Halmashauri zetu wapo kwenye sekta kama afya na elimu, tunao. Wale wote ambao wanafanya kazi kwa weledi na wana sifa ya kuajiriwa, pindi tunapopata vibali kutoka Utumishi, tunawaajiri. Sasa hivi tumeshatoa maelekezo kwenye Halmashauri, wako vijana ambao wanafanya kazi kwenye Halmashauri zetu kwenye nafasi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwenye sekta ya elimu wako walimu wanajitolea na wana nafasi nzuri; kwenye kata, pale kwenye mapengo tunao vijana kwenye vijiji vile, wanafanya kazi yao vizuri. Hawa wote tunaendelea kuwaangalia na kukusanya taarifa zao na sifa zao. Inapotokea kuwa na vibali ambapo sasa vinaendelea kuzalishwa kuajiri kada mbalimbali, itakapofikia kwenye kada hiyo, nao pia tunawapa nafasi ya kuwaajiri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inaendelea kuwaangalia hawa wote ambao wamejitoa, wameamua kufanya kazi bila mshahara, lakini pia wanataka kuonesha uwezo wao na kuutumia muda wao vizuri kulisaidia na kulihudumia Taifa hili, wote wanapata kipaumbele kwenye ajira.
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie wale wote ambao wanajitolea, tulikuwa tunazungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, juu ya vijana wetu ambao wanafanya kazi kwa kujitolea kule kwamba, hawa sasa waorodheshwe tuwatambue ili baadaye ajira inapotokea, waweze pia kuingia kwenye orodha ya waajiriwa. Kwa hiyo, huo ndiyo utaratibu ambao tunautumia kwa sasa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika miradi ya ujenzi wa meli katika maziwa makubwa yaliyoko nchini mwetu likiwemo Ziwa Viktoria, Nyasa na sasa Tanganyika. Hata hivyo kumekuwa na ufanisi mdogo sana katika kutoa huduma kutumia meli hizo katika maziwa hayo:-
Je, ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kuwa meli hizi zilizojengwa kwa gharama kubwa zinatumika ipasavyo ikiwemo katika Ziwa Nyasa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya, Mbunge wa Mbambabay, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeimarisha sana huduma za usafiri kwenye kada zote, maeneo yote ya barabara, hewani, kwenye maji, lakini pia kwa njia ya reli. Kama ambavyo Watanzania mnajua, miradi kadhaa inaendelea ikiwemo na utengenezaji wa meli ambazo zinatoa huduma kwenye maziwa yetu na ukanda wa bahari ikiwemo na Ziwa Nyasa; na kwa bahati nzuri nimepata nafasi ya kwenda Nyasa na kuzindua meli kadhaa: -
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Mbunge anaomba kujua utoaji huduma wenye tija; ni swali pana kidogo.
Mheshimiwa Spika, utoaji huduma wenye tija, mkakati wetu ndani ya Serikali, kwanza ni kupanua wigo wa kufanya biashara hiyo na kwa kuwahudumia Watanzania. Hii ina maana ya kwamba, kama tuna vituo vichache vinavyolazimisha wananchi walioko mbali kufuata bandari, lakini kwenye maeneo walimo, tunaweza kujenga bandari. Ndiyo mkakati ambao sasa unafanywa na Mamlaka ya Bandari kwa kujenga bandari palipo na watu wengi ili kuweza kuwafikia ili huduma sasa iwe na tija. Hiyo ni moja.
Mheshimiwa Spika, pili, sisi tunafanya kazi kule Ziwa Nyasa na nchi ya Malawi. Nchi ya Malawi ni ndefu kufuata lile ziwa, lakini tuna bandari moja tu ya upande wa Malawi. Sasa ili kufanya huduma hizi ziwe zenye tija, nako pia kushawishi kuwa na bandari nyingine ili tuweze kuwapata abiria wengi ili na yenyewe iweze kuwafikia Watanzania kwenye huduma hii.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunataka tuimarishe ratiba za meli ziwe mara nyingi zaidi kuliko ratiba ambayo inawafikia wananchi mara chache. Labda kama ratiba hiyo ni mara moja kwa wiki, basi tupeleke mpaka mara mbili, mara tatu, zipite, wananchi wafanye maamuzi ya kufanya biashara yao kwa urahisi zaidi. Hiyo nayo pia inaingia kwenye tija aliyoisema Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, pia, kwa tukio ambalo limetokea kule Nyasa siku za karibuni, meli zetu ziliharibika kwa muda mrefu. Nayo pia inaweza kuwa siyo tija. Nataka niwahakikishie, tumeimarisha ukarabati wa hizi meli. Nimeenda Kyela, nimekuta meli zetu, tukaagiza wale watendaji wa TASAC waikamilishe kusimamia ukarabati wa zile meli na zianze mara moja. Taarifa ambayo tumezipata, meli zimeshaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, nayo pia inaleta tija katika utoaji huduma kwenye ukanda wetu. Kwa kufanya hilo tutaimarisha pia ukaguzi wa mara kwa mara, ili meli zisisimame wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, vile vile tunapunguza gharama za kuingia na kusafiri na kusafirisha mizigo ili kuvutia watu wengi zaidi kutumia meli hizo. Nadhani huo ndiyo mkakati ambao tunaufanya ndani ya Serikali ili kuleta tija kwa Watanzania ambao tumekusudia kuwahudumia.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Nyasa, pia tuna Mbunge hapa wa Kyela, tuna Mbunge hapa wa Ludewa, maeneo yote haya yananufaika na meli yetu kwenye Ukanda ule wa Ziwa Nyasa. Niwahakikishie Serikali itaendelea kutoa huduma kwenye maeneo hayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuuliza swali kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, sekta ya usafirishaji hasa bodaboda imekuwa ni ajira kubwa sana kwa vijana, lakini kumekuwa kukitokea ajali ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu kwa vijana wetu kutokana na kukosa elimu ya usalama barabarani. Nini mkakati wa Serikali katika kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwaepusha nguvukazi hii na ajali hizi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Toufiq, Mbunge wa Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nami nikiri kwamba sekta ya bodaboda inayosimamiwa sana na vijana wetu imeweza kusaidia sana kupunguza tatizo la usafiri wa umbali mfupi mfupi na wakati mwingine hata umbali mrefu; na tunaona vijana wetu wa bodaboda wanafanya kazi nzuri. Pamoja na changamoto zilizopo, lakini huduma yao Serikali tunaitambua na tutaendelea kuisimamia ili iendelee kuboreshwa vijana hawa waweze kufanya kazi hiyo kusafirisha watu, lakini wapate pato la mtu mmoja mmoja, linasaidia sana kwenye familia zao.
Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba zipo ajali zinazoweza kutokea au kwa bahati mbaya, lakini wakati mwingine kwa uzembe. Tunachofanya ni kuimarisha elimu. Jeshi letu la Polisi limekuwa na mpango mzuri kabisa wa kuwafuata vijana hawa kwenye maeneo yao na kutoa elimu. Watanzania tunaona baadhi ya makamanda wa Jeshi la Polisi wakiwa wako mbele za vijana wa bodaboda wanawaelimisha baadhi ya mambo ambayo wanatakiwa kuyazingatia ili wafanye kazi yao vizuri pamoja na kupunguza ajali pia.
Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana pia hata vyombo vya habari ambavyo vimekubali kutoa nafasi ya Jeshi la Polisi kwenda kutoa elimu kwa vijana wetu wa bodaboda. Tunaimarisha sasa kwa kila mwendesha pikipiki au bodaboda kwamba apate leseni na kuwahamasisha kuwa na angalau ile helmet. Yaani yale masharti yote yale ya usalama, kuendesha chombo cha moto waweze kuyakamilisha ili huduma hii iendelee kushamiri na iendelee kuwanufaisha wanaotumia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali katika hili, nafasi yetu ni kuendelea kuimarisha utoaji elimu kwa vijana wanaoshughulika na bodaboda ili wajue kwanza kazi na thamani ya kazi yao. Pili wasaidie sana kwa kuzingatia sheria kupunguza ajali. Hili jambo ni muhimu sana na tumeendelea kulisimamia hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo la bodaboda kwanza Serikali tumelitambua na tumeendelea kuliimarisha na tutaboresha zaidi kwenye eneo hili. Pili mkakati huo wa kielimu tutaimarisha zaidi na tutawafikia wananchi, hao vijana wanaoshughulikia bodaboda mpaka kwenye vituo vyao ili kurahisisha na wao kuwaondoa kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kupata elimu. Kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha eneo hili na hayo ndiyo malengo ya Serikali. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali. Tarehe 10 Julai, Soko la Kariakoo liliungua, ambapo tarehe 11 Julai, wewe mwenyewe ulikwenda Kariakoo kwa ajili ya kuwapa pole wahanga na pia kutoa maelekezo ya Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunashukuru sana Serikali kwa sababu wamechukua jitihada za kujenga upya soko la Kariakoo ambako tarehe 6 Novemba, 2021 Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI alikwenda Kariakoo kwa ajili ya kutoa maelekezo kuhusiana na kujenga Soko la Kariakoo, kulijenga upya.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ramani mpya ya Soko la Kariakoo jipya ina masoko mawili ambapo kama sasa hivi yako masoko mawili. Ramani inataka na utaratibu wa kujenga unataka soko dogo na kubwa lijengwe kwa pamoja. Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo hili linaweza kupelekea ghasia na sintofahamu kwa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wa kujenga masoko haya kwa awamu ili wafanyabiashara wa soko dogo wabaki pale ili soko kubwa lijengwe halafu baadaye wahamishiwe likamilike kwa pamoja? Nashukuru sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat, Mbunge wa Mkoa wa Singida, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tulipata tatizo la soko la Kariakoo kuungua na wote tunajua, lakini Serikali imefanya jitihada kubwa sana. Tulienda kutembelea na kuwapa pole, lakini tulitaka tujiridhishe ajali ile ilitokana na nini? Tukaunda Timu ambayo pia ilifanya kazi yake vizuri na ikatupa mrejesho wa nini kilisababisha soko lile lakini Kamati ile ilienda mbali zaidi na kutuambia madhara ya soko lile yakoje.
Sasa lile soko pale lilipo limezungukwa na nyumba za watu binafsi, lakini pia kuna soko dogo liko karibu kabisa na lile soko, usalama wa soko lile dogo haukuwa mzuri pia nao. Kwa hiyo katika maoni au mapendekezo ambayo waliyatoa ile Tume ni pamoja na kuliondoa lenyewe na kulijenga lingine jipya ambalo pia litafanya kazi yake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Rais, atatutengea shilingi bilioni zisizopungua 32 mpaka 34 ambazo zitajenga masoko yote mawili na tumeona tufanye maboresho makubwa. Hawa walioondolewa kwenye eneo lile, kimsingi hata pale baada ya kuungua, hawa waliokuwa soko dogo walikuwa hawafanyi kazi zao. Nao tuliwasihi wapishe eneo lile, ili eneo lile sasa uchunguzi upite na sasa maandalizi ya ujenzi yaendelee na tumewapeleka Kisutu pamoja na eneo la Machinga Complex na wengine wameenda kwenye masoko jirani.
Mheshimiwa Spika, wale wote wameorodheshwa, wanafahamika nani alikuwa wapi. Malengo yetu, baada ya kukamilisha katika kipindi tulichokubaliana soko likamilike, wale wote waliokuwa soko dogo waliokuwa mle kwenye soko kubwa, tunawarudisha na kuwaweka kwenye nafasi zao. Kwa kuwa sasa soko tumeliboresha, soko dogo sasa tumelijenga kwenye ghorofa, ghorofa mbili mpaka tatu, tumeongeza na wengine waliokuwa wanazagaa kule nje wakakosa mahali, sasa tunawaingiza kwenye lile jengo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yote haya ni maboresho ambayo tumeyafanya ya kuhakikisha kwamba hawa walioko hapa si kwamba wanapata shida kubwa kwa sababu wengine tumewapeleka pale Kisutu wanaendesha biashara zao na wale kwa sababu wana uhakika jengo likijengwa watarudi na watapata nafasi, naamini wanaiamini Serikali yao kwamba tutatenda hivyo na tutasimamia hilo ili kazi hiyo iweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inasimamia kwa karibu na sasa iko kwenye zabuni ili ujenzi uanze katika kipindi kifupi, wafanyabiashara warudi kufanya biashara zao. Ahsanye sana. (Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kila mwaka Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya kupeleka kwenye Vyuo Vikuu ili watoto wasiokuwa na uwezo waweze kupata mkopo na kujikimu na mahitaji yao ya chuo. Utakubaliana na mimi kama Taifa tuna uhitaji mkubwa sana wa Watanzania hasa vijana wenye ujuzi hasa ujuzi wa kati ili sasa twende kuboresha na kupanua huduma muhimu kama vile afya, elimu, nishati na miundombinu vijijini. Sasa changamoto kubwa ya hawa vijana ambao tunawahitaji ambao wako kwenye vyuo vya kati hawana access ya hii mikopo na wao hawana uwezo wa kujilipia ada hizi.
Mheshimiwa Spika, sasa nataka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha hawa vijana ambao tunawahitaji ambao wako kwenye vyuo vya kati wanakuwa na access ya kupata hii mikopo kama ambavyo tunafanya vijana wa elimu ya juu? Nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tweve, Mbunge wa Iringa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, anachosema Mheshimiwa Mbunge ni sahihi kwamba tuna kada ya elimu ya kati hawajaingia kwenye mkopo kama ambavyo mkopo huu unaendelea. Hii inatokana na sheria tuliyoiweka na ndiyo kwa sababu Bodi inaitwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Sheria iliyoanzisha Bodi hii ilianza kwa kuelekeza elimu ya juu na ndiyo ambayo sasa tunayo. Toka tulipoanza mpaka sasa tumegundua kwamba mahitaji ni mapana mno, lakini upana huu wa mahitaji utategemea pia na uwezo wa kifedha wa Serikali. Tukiwa tunaendelea kuwanufaisha Watanzania kupitia elimu ya juu kwa vyuo tu vya elimu ya juu, bado tuna mafanikio lakini tuna changamoto zake, tunaendelea nazo. Tumegundua tuna uhitaji pia wa elimu ya kati ambayo ni kada ambayo inafanya kazi kubwa sana kwenye sekta mbalimbali mpaka viwandani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kadiri tunavyokwenda Serikali tutaleta Muswada ndani ya Bunge kama pia uwezo wa kifedha nao ukiwa mzuri na tutashiriki pamoja kujadili uwezekano wake ili kufungua mlango kwa vijana wa kada ya kati wa elimu ya kati ili na wao waweze kunufaika na mikopo hii. Kwa hiyo kadri tutakavyokuwa tunapata fedha, tutakuwa tunaendelea kuboresha kupanua wigo, tukifika elimu ya kati tutashuka mpaka elimu ya juu ya kawaida huku chini kwa maana ya sekondari kadiri tutavyopata fedha. Hiyo tutaileta Bungeni, tutajadili Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Tweve najua utakuwepo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa hii nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Sera ya kuwainua wananchi kiuchumi imekuwa na mafanikio sana kwenye ile mikopo inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya akinamama, vijana na watu wenye ulemavu. Hata hivyo, kumekuwa na tatizo haswa kwa vijana, vijana wanavyopewa mikopo wakifikisha umri wa miaka 35 vijana wa kike wanaenda kwenye kundi la akinamama, vijana wa kiume wanabaki hawana cha kufanya. Sasa swali langu, ni nini mpango wa Serikali wa kuwainua wanaume kiuchumi kwa sababu sera inasema ni wananchi kwa kufanya moja kati ya haya? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimo, Mbunge wa Manispaa ya Moshi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanzisha Mifuko kadhaa ambayo inawanufaisha Watanzania kulingana na eneo lile ambalo Mfuko huo umeanzishwa. Tunatambua kwamba kundi la vijana limechanganya maeneo yote, lengo pale ilikuwa ni vijana. Hata hivyo, iko Mifuko ya wananchi wote ambao pia wananufaika na Mifuko hii, lakini pia tumejiunganisha na taasisi za kifedha ambazo yeyote yule anakuwa na fursa ya kwenda kukopa.
Mheshimiwa Spika, tuliposema vijana, wanawake, wenye mahitaji maalum, Mheshimiwa Tarimo anajua kwamba sera ya nchi yetu sasa tumeelekeza katika kumwezesha mtoto wa kike, lakini na wanawake wote kwa ujumla ili na wao waweze kuchangia pato la nchi hii kwa kufanya shughuli mbalimbali. Kwa hiyo akishapata mkopo anaweza kuanzisha biashara na Mheshimiwa Tarimo anajua, ukimwezesha mwanamke unakuwa umeliinua Taifa hili. Ukimwelimisha mwanamke unakuwa umelielimisha Taifa hili. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuliona eneo hili, kwa kuwa tunatambua kwamba ukimwezesha mwanamke unaliwezesha Taifa hili, ukimwelimisha mwanamke unaelimisha Taifa, kwa hiyo tuliona tuwawekee eneo lao ambalo wanakuwa na uhuru mkubwa wa kukopa. Anaweza kwenda kwenye Mfuko wa Halmashauri ambao una kipengele cha wanawake, anaweza kwenda Benki akakopa, anaweza kwenda kwenye Mfuko mwingine, Mifuko iko mingi, tuna Mifuko 42 ingawa sasa tutaipunguza ibaki michache, ifahamike kila mmoja aweze kwenda kukopa.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme tu bado hatujafikiria kuanzisha Mfuko wa Wanaume, lakini tayari wigo wa wanaume hao kupata mikopo upo kupitia Mifuko hiyo na taasisi za fedha. Hapo baadaye tukiona kuna umuhimu mkubwa, ama kuna udhaifu mkubwa pia tunaweza tukaanzisha kadiri itakavyowezekana. Sheria hizi na Mifuko hii tunapoianzisha tunaileta kwenye Kamati zetu za Bunge na kuona umuhimu wa kuanzisha hicho kitu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ikolojia, kilimo cha umwagiliaji hakiwezi kukwepwa katika nchi hii. Miaka michache iliyopita Serikali ilitoa mabilioni ya fedha kununua vifaa vya uchimbaji wa mabwawa, lakini mpaka sasa hivi hakuna bwawa hata moja ambalo limechimbwa na hivyo vifaa vimechakaa na kwa sasa ni kama vile spana mkononi. Sasa nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba mabwawa haya yanachimbwa na kuwekeza fedha zaidi kwenye uchimbaji wa mabwawa ili kukinusuru kilimo chetu na mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili nchi hii? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye sekta ya kilimo, miaka yote nchini tumekuwa tukitegemea sana msimu wa mvua ili kuzalisha mazao yetu. Tumegundua kwamba tunayo fursa ya kutumia mabwawa yawe ya asili au ya kuchimba na kuyajaza maji tukatumia kwa kilimo cha kumwagilia. Tumeweka msisitizo kwenye eneo hili, pale ambapo tulichimba mabwawa mengi kwenye maeneo kadhaa lakini pia kuhakikisha kwamba tunakuwa na maeneo ya kumwagilia pale ambako kuna uwezekano mkubwa au kuna mvua nyingi na mabwawa yanajitengeneza. Serikali inaendelea kusimamia jambo hili kwa sababu tumegundua tukiimarisha kwenye umwagiliaji, tunafanikiwa sana.
Mheshimiwa Spika, Serikali huko awali tulinunua mitambo hiyo ambayo Mheshimiwa Mwenisongole amesema imechakaa. Ni kweli, lakini kwa kuwa sasa tunakisimamia kilimo na maendeleo yake, Wizara ya Kilimo hapa hata walipokuja mbele yetu kuja kuomba kuongezewa bajeti, walieleza waliomba fedha ambayo Waheshimiwa Wabunge wameipitisha kwa ajili ya kuongeza mitambo mbalimbali kwa ajili ya kupanua wigo wa kilimo cha umwagiliaji. Lengo mitambo ile isambazwe kwenye kanda zetu na ifanye kazi ya kuchimba mabwawa kwenye maeneo hayo, yatumike kwa kilimo, lakini wakati mwingine pia na wafugaji watatumia kwa kunyweshea mifugo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali ilishatoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo hiyo ili kuendelea kuimarisha mitambo iliyopo kwa kununua vipuli ile iliyoharibika, lakini mipya kwa ajili ya kuendelea kuchimba mabwawa yetu. Kwa hiyo eneo hili tutaendelea kulisimamia kwa sababu tumegundua kwamba lina tija na hasa kipindi hiki ambacho tunaambiwa hali ya hewa ina badilikabadilika, kama tutakuwa na mabwawa na maeneo haya ya kumwagilia, tunaweza tukapata kilimo kizuri tu na tukavuna mazao mengi tu kama ambavyo maeneo yote yenye mabwawa yanavyoweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mwenisongole kwamba, eneo hili kwa fedha ambayo tumeitoa, tutanunua mitambo na kama haitoshi tutaona uwezekano wa kuongeza ili iweze kufanya kazi ya kuchimba mabwawa katika maeneo yote kadiri ya uhitaji kwenye maeneo haya. Ahsante sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata fursa hii ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, mradi wa kuchakata gesi unaofanywa katika eneo la Likong’o, Mkoani Lindi ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ambayo imekusudia kuinua fursa za kiuchumi katika ukanda wa Kusini na Tanzania kwa ujumla. Nini maelezo ya Serikali kuhusiana na hatua iliyofikiwa ya mradi huu mpaka hivi sasa na Watanzania watarajie nini kutokana na mradi huu. Ahsante sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna mradi huu mkubwa wa kimkakati wa LNG ambao uko Mkoani Lindi na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Kassinge anauliza swali na anayejibu ni mnufaika nambari moja. Mradi huu hatua tuliyofikia sasa ni nzuri, kwa sababu tayari TPDC wameshiriki kikamilifu kwenye hatua zote za awali ikiwemo na kulipa fidia wananchi wote waliokuwa kwenye eneo lile, wote wameshaondoka. Eneo lile sasa linaandaliwa kulima barabara mbalimbali huko ili kuligawa kwenye plots zile ambazo huduma mbalimbali zitatolewa makazi, sehemu ya kuweka mitambo na maeneo ya utoaji wa huduma nyingine.
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine muhimu zaidi ni ya majadiliano ambayo Wizara ya Nishati kupitia Waziri aliyepo sasa ameshaanzisha hiyo timu na wako Arusha kwa sasa wanaendelea ku-negotiate, kufanya majadiliano na yale makampuni. Makampuni yenyewe yako kama manne ambayo yameonesha nia ya kwenda kuwekeza pale eneo la Likong’o pale Mkoani Lindi kwa ajili ya kuchakata gesi.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ambao pia utaleta faida kwa Watanzania wote, tumeenda kuwahamasisha, nilikuwa ziarani Mkoani Lindi wiki mbili, tatu zilizopita. Nimetembelea eneo lile la huu mradi, nimekutana na wananchi na nimewaambia wananchi wajipange sasa kunufaika na huo mradi. Kutakuwa na mambo mengi, watakuja watu wengi, kutakuwa na shughuli nyingi, watu wajikite kwenye kilimo, walime mazao yatakayoweza kuuza, watu wafuge watauza, lakini na huduma nyingine hoteli na nyumba za kulala wageni, ziandaliwe. Hizo ndiyo fursa ambazo tunazipata kwa kuwa na miradi mikubwa ya kimkakati kama wa LNG.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Watanzania wategemee mafanikio makubwa kwa mradi huu ambao tayari mchakato wake unaenda katika hatua nzuri ya kwenda kuanza uchimbaji, uanzaji wa kuchimba na kuwekeza kwenye mradi huo. Kwa hiyo kwa ujumla wake miongoni mwa miradi mikubwa nchini ambayo pia ni ya kimkakati umo na mradi huu ambao utatengeneza fursa nyingi ikiwemo na ajira kwa Watanzania wote, kwa Watanzania wale ambao watapata nafasi ya kuajiriwa kwenye eneo lile. Hizo ndiyo fursa ambazo zinatarajiwa na Watanzania kupatikana kupitia mradi huo. Ahsante sana.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuuliza swali kwa Waziri Mkuu.Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Kamati ya Mawaziri Nane ya kutatua migogoro kati ya hifadhi, hususan TFC na TANAPA, lakini kuna vijiji ambavyo bado havijafikiwa vikiwemo vijiji katika Wilaya yaMbeya. Je, ni lini Kamati hii itarejea kukamilisha hilo zoezi muhimu kwa maeneo yaliyobaki nchi nzima? Nashukuru sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali iliunda timu ya Mawaziri Nane kwa ajili ya kuhakiki vijiji ambavyo vina changamoto au migogoro kati ya vijiji hivyo na hifadhi. Mnatambua Waheshimiwa Wabunge tulipata taarifa za awali za utekelezaji huo na bado kazi hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Njeza anahitaji kujua lini kazi hiyo itakamilika, ili tuweze kwenda kule Mbeya. Nataka nimhakikishie kwamba, kazi iliyofanywa awali ambayo ilibaini vijiji vipatavyo mia tisa kama 75 hivi na kati ya hivyo ilithibitika kuwa vijiji mia tisa na 20 havikuwa na matatizo na bado vilikuwa vinatakiwa kuishi huko kwenye maeneo ambayo tuliyahifadhi, lakini hayana tija. Bado Serikali inakusudia kutambua vijiji kadhaa vyenye migogoro ya aina hii kati ya vijiji na hifadhi, pale ambapo tunaona kwamba, uhifadhi wake hauna tija kwa malengo yaliyokusudiwa, vijiji hivyo vitapata nafasi ya kuendelea kushiriki shughuli za kijamii kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, pindi Kamati itakapokamilisha, tutakuja kutoa taarifa nyingine tena baada ya taarifa ya awali. Sasa, naielekeza Kamati ile pia, kuweka mpango kazi wa kwenda Mbeya Vijijini kuona huko ambako Mheshimiwa Mbunge anasema bado hatujafika, waone vijiji hivyo, lakini pia, aina ya mgogoro uliopo na nini tufanye baada ya kuhakiki. Kwa hiyo, Kamati ya Mawaziri wale nane itakapokamilisha kazi hiyo tutaipata.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito, tunatambua tuna migogoro mingi, iko migogoro ya mipaka kati ya vijiji na vijiji vyenyewe, iko migogoro ya wafugaji na wakulima, bado nielekeze kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, hususan Waheshimiwa Wakuu wa MIkoa, Wakuu wa Wilaya, lakini tunashuka chini kule kwa Watendaji wa Kata na Vijiji kuhakiki migogoro hii na tujiridhishe kuwa inakamilishwa hukohuko kwenye ngazi hiyo, badala ya kutegemea Mawaziri ambao wako hapa Dodoma wasafiri waje kwenye vitongoji na vijiji badala ya kuwa wamekamilisha kule na Mawaziri wapate unafuu wa kutekeleza hili. Ikifika hatua hiyo ya kila mmoja kuwajibika kwenye nafasi yake hii migogoro itapungua kwa kiasi kikubwa, kama sio kuimaliza kabisa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii muhimu. Kumekuwa na changamoto ya ukame kujirudiarudia nchini kwetu na matokeo yake ukame huu umeleta athari nyingi, ikiwemo mifugo kufa kwa kukosa malisho.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, Serikali ina mkakati gani wa muda wa kati na wa muda mrefu wa kukabiliana na ukame huu hususan kwenye malisho ya mifugo? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, amezungumzia ukame, anataka kujua mpango wa Serikali wa kukabiliana na ukame huu; ukame unaojitokeza mara nyingi nchini ni mabadiliko ya hali ya tabianchi ambayo yanaleta athari ya kukosekana kwa mvua na hasa pale ambapo athari hizo zinasababisha kutopata mvua kama ambavyo mwaka huu na mwaka uliopita hapa nchini kwetu, maeneo mengi yalikuwa makame kwa sababu hakuna mvua. Hii ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi, lakini pia, ukame huu unatokana na uharibifu tu wa mazingira ambao wananchi wanaufanya kwenye maeneo yetu kwa kukata misitu na maeneo ambayo tunategemea sana kuwa na mvua.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, imeendelea kutoa elimu ya wananchi kuhifadhi mazingira kwenye maeneo yao ikiwemo misitu, ili isaidie kuleta mvua kwenye maeneo hayo kuachana na ukame. Hiyo ndio njia moja muhimu ambayo mimi naiona, lakini pia umehusisha maeneo ya malisho ya malisho ya mifugo. Kutokana na ukame huu ni kweli hatupati malisho na kwa hiyo, ni lazima pia tuhakikishe kwamba, tunaendelea kuhifadhi mazingira haya tupate mvua ili malisho mengi yaweze kupatikana.
Mheshimiwa Spika, ukiondoa ukame, lakini bado hata Wizara ya Mifugo na Uvuvi wanajitahidi sana kutoa elimu kwa wafugaji kuhakikisha kuwa wanafuga kitaalam kulingana na ukubwa wa malisho waliyonayo, ili kukabiliana na upungufu wa malisho ambayo kwa sasa yanakuwa hayapatikani kwa sababu ya kuwa na mifugo mingi zaidi. Jana tumelizungumza hapa ndani ya Bunge juu ya Ngorongoro kule, uharibifu unaoendelea kule Ngorongoro itakwisha, lakini hili ni sisi wenyewe ndio tutaweza kukabiliana nalo na kwa kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuelimisha umma juu ya uhifadhi wa mazingira, lakini pia Wizara ya Mifugo inaendelea kuwaelimisha wafugaji, ili tuanze kuandaa malisho kwa kuhifadhi malisho, lakini pia tuweze kuchimba visima kupata maji ya chini na kuanza kumwagilia kwenye maeneo ambayo tumeyatenga kama maeneo ya malisho.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake kwenye mifugo tumefanya jitihada kubwa sana za maeneo yetu yale ya ranch. Tumegawa vipande, vinaitwa blocks na kuwagawia wafugaji ili kila mmoja aweze kutunza maeneo hayo na ikiwezekana pia na kupanda nyasi ikiwa ni njia ya kupata malisho mapya, ili mifugo iweze kuendelea.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito sasa kwa Watanzania, ili kukabiliana na ukame ambao unaendelea ni lazima tuungane pamoja turekebishe, tuache tabia ya kukata miti na misitu kwenye maeneo tuliyonayo ili misitu hii iweze kutusaidia kupata mvua za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoe wito pia kwa ndugu zangu wafugaji waendelee kufuga kitaalam, tuwe na mifugo michache unayoweza kuihudumia ikiwemo kupata na malisho, ikiwezekana pia hata kuboresha malisho kwa mifugo uliyonayo badala ya kuwa ng’ombe zaidi ya 2,000 ambao hauna uwezo wa kuwafuga na matokeo yake kukosa malisho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, huo ndio ujumbe wangu kwa swali ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliuliza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kumekuwepo na ongezeko la bei za bidhaa mbalimbali nchini kote, lakini hasa Mkoa wa Shinyanga, Wilaya ya Kahama, Jimbo la Msalala na hususan bidhaa hizo ni mafuta ya kula, sabuni, lakini pia vifaa vya ujenzi kama nondo, simenti. Ni nini sasa kauli ya Serikali juu ya ongezeko au mfumuko wa bei katika bidhaa hizi mbalimbali? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kumejitokeza siku za karibuni kupanda kwa bei kwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Upandaji wa bei hizi wakati mwingine ni wa makusudi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara ambao sio waaminifu, lakini pia, upatikanaji wa malighafi. Viwanda vyote ambavyo vinazalisha hapa nchini vingi miongoni mwake vinategemea malighafi kutoka hapa nchini na malighafi zipo.
Mheshimiwa Spika, nakumbuka siku tatu, nne zilizopita, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, amezungumza na Taifa kwa kuwaambia kwamba, uko mkakati wa baadhi ya wafanyabiashara waovu wasiokuwa na nia njema wa kupandisha bidhaa kwa makusudi tu; moja, kwanza wanazalisha kidogo sana ili kutengeneza upungufu mtaani ili bei ziweze kupanda. Mbili, kumekuwa na utamaduni sasa wa baadhi ya wafanyabiashara waovu kukaa pamoja na kujadili tu bei ziweje na kusababisha mfumuko wa bei. Serikali tumeligundua hilo na ndio kwa sababu, Waziri Dkt. Kijaji, ametoka hadharani kutueleza mkakati wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono kauli yake, lakini pia, natoa agizo kwa wafanyabiashara kuacha tabia hiyo ovu inayosababisha jamii kushindwa kupata bidhaa kwa gharama nafuu kwa sababu, wakati tunawekeana mikataba na wakati tunajenga mazingira rahisi ya uwekezaji nchini, lengo la kwanza kubwa ilikuwa ni kupata bidhaa kwa wingi, kwa bei nafuu, lakini pia zipatikane wakati wote, sasa wengine wanaanza kukiuka masharti yetu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ametoa ultimatum kwao, nami narudia tena, hatutasita kuchukua hatua kwa wafanyabiashara ambao wanaweka mkakati tu wa kutaka kusumbua jamii kwa kununua bidhaa kwa bei ya juu bila sababu yoyote, kwa sababu, bidhaa tunazo, malighafi tunazo na viwanda vipo, uboreshaji ndani ya Serikali wa uwekezaji tumeufanya kwa kiasi kikubwa na kila siku tunakutana nao na wanaeleza namna ambavyo tungependa Serikali iwe na sisi Serikali tunafanya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili ambalo Mheshimiwa amelieleza, Serikali itaendelea kuchukua hatua kali na tutasimamia upandaji wa bidhaa hizi usiende kupanda mara zote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niiagize taasisi yetu inaitwa FCC, ambayo inasimamia haki za wafanyabiashara katika kufanya biashara, ihakikishe inafanya ukaguzi wa kina kila bidhaa zinazozalishwa na mauzo yao, walinganishe na uzalishaji wao, uwezo wa kiwanda kwa mwaka, tuone kama je, wanazalisha kwa kiwango kilekile tulichokubaliana au wamepunguza uzalishaji kutengeneza upungufu? Pia tujue kwa nini wanapandisha bei, kati ya kiwanda na kiwanda bei zinatofautiana? Hili nalo tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niahidi kwamba, tutalifanyia kazi kupitia taasisi zetu za ndani ya Serikali, kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Waziri Mkuu swali. Mwaka 1994 aliyekuwa Waziri Mkuu, Ndugu yetu Samuel Malecela, alitoa tamko juu ya mabasi yanayosafiri usiku na kusema yasisafiri usiku. Tamko lile halikuwa na sheria wala sera. Ni nini Serikali sasa inasema kwa kuwa, nchi yetu sasa imekuwa ni nchi ya kati na uchumi unatakiwa uende mbele.
Mheshimiwa Waziri Mkuu unaonaje kwamba, mabasi hayo yaruhusiwe kutembea usiku na mchana ili tuweze kuongeza kipato, na hasa pato la Taifa kwa Watanzania wote kwa kuwa, mabasi yakifanya mchana peke yake tunalala usiku bila kuingiza fedha yoyote? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakagenda, Mbunge wa Mbeya, lakini sio Mbeya Mjini, Mbunge wa Mkoa wa Mbeya, kama ifuatavyo:- (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mara kadhaa tumekuwa tukitoa maelekezo, hasa kwenye eneo la usafiri, kulingana na hali ya usalama iliyoko nchini. Wakati huo agizo hili lilitolewa kwa sababu, mara nyingi mabasi yalikuwa yanatekwa yanaposafiri na tulikuwa tunalazimika pia kuweka jeshi la polisi kila basi linaposafiri ili kuhakikisha kwamba, wasafiri wanasafiri salama.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, sasa usalama umeimarika nchini na Serikali inaendelea kuimarisha zaidi usalama nchini. Umuhimu wa hilo jambo upo, lakini nitawasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama kuona kama, je, wamejiridhisha kwa kiasi gani kwa usalama huo, ili tuanze kuruhusu mabasi kufanya kazi wakati wote, ili kuboresha uchumi, lakini kuwafanya abiria kuwa na mipango binafsi ya kibiashara ya kusafiri kutoka eneo moja mpaka eneo lingine katika kuendesha biashara zao kwa uhuru mkubwa.
Mheshimiwa Spika, katika hili lazima pia tutoe wito kwa Watanzania; kudumisha amani na usalama na utulivu nchini ni muhimu sana kwa sababu, malengo yetu ya kuboresha uchumi wa nchi, kama nchi haiko salama hatutayafikia. Wito uliotolewa na Mheshimiwa Mwakagenda unaendelea kusisitiza na kuonesha umuhimu wa Taifa hili kuendelea kuwa salama ili wale wanaoamua kufanya biashara zao wakati wowote wafanye biashara hizo.
Mheshimiwa Spika, pia tumeanza kutoa wito hata kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa kupitia masoko yao makuu kuhakikisha kwamba masoko haya yanafanya kazi masaa 24 ili kuwaruhusu hata wanaokuwa busy mchana kutwa kwenye ofisi zao waweze kufanya hivyo wanapopata muda wa mapumziko ambao pia ni usiku kama ambavyo tunaona kwenye nchi zilizoendelea za wenzetu, watu wanaenda shopping center, biashara zinafanywa masaa 24 na sasa tunataka Tanzania hiyo pia ijitokeze kuanzia kwenye masoko yetu, kwenye usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeagiza vyombo vya ulinzi hasa Jeshi la Polisi kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya waendelee kufanya tathmini hiyo kwa haraka ili tupate taarifa hiyo tuweze kutoa vibali hivyo vya kusafiri nyakati hizo ili kazi ziendelee. Ahsante sana.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Swali langu linahusu huduma ya umeme.
Mheshimiwa Spika, natambua, nathamini na vilevile naipongeza Serikali kwa juhudi kubwa sana za kuhakikisha kwamba Taifa hili linakuwa na umeme wa uhakika. Nafahamu vilevile kwamba kumekuwa na initiatives nyingi za Serikali ikiwemo hii ambayo imetolewa tarehe 30 Juni, 2014 ambayo ni ya Electricity Supply Industry Reform Strategy and Roadmap. Katika utafiti huo inaonekana kuna matatizo makubwa ya generation, transmission pamoja na distribution.
Mheshimiwa Spika, sasa TANESCO inaonekana kuhemewa na kazi hii hasa kwa kuwa tunakwenda kuwa na umeme mkubwa kutoka Mwalimu Nyerere Hydropower Supply. Kwa hali hiyo, Serikali haioni kwamba muda muafaka sasa wa kwenda kuifumua TANESCO ili tuwe na makampuni matatu ya generation peke yake, transmission peke yake pamoja na distribution kama ilivyo katika nchi nyingine na hata majirani zetu wa Kenya, Uganda, South Africa na kwingineko? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba ridhaa yako angalau hili eneo la mwisho naweza kulitolea ufafanuzi kama ambavyo Mheshimiwa Abbas Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, mwanamichezo alivyouliza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shirika letu la umeme nchini linafanya kazi kubwa sana. Kazi hiyo kubwa ambayo inafanywa kwa sasa, lenyewe ndiyo linazalisha, lakini TANESCO pia inasafirisha umeme na inafanya kazi ya kugawa. Unapofanya jukumu hili, pia tunaangalia na maslahi ya Taifa, kwamba maeneo haya unaweza ukawa umeyakatakata ukawapa watu tofauti tofauti ikakuletea athari kwenye usalama wa nchi. Pale ambako nchi inahitaji umeme wakati wote, halafu mmoja miongoni mwao anafanya mambo anayoyataka tu, halafu ukashindwa kufikia malengo ya kupeleka umeme kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri wake. Hali tuliyonayo sasa nchini, maeneo yote yanayozalisha umeme tunaendelea kuzalisha umeme. Tuna maeneo ya maji; tunapopata mvua za kutosha kama sasa maji yamejaa, mfano Kidatu na Mtera, tunayo maji ya kutosha na uzalishaji unaendelea. Kwa hiyo, eneo hili halina matatizo. Kwenye eneo la gesi pale Kinyerezi uzalishaji unaendelea. Pia maeneo mengine tunayotumia mafuta yanaendelea pia na uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, TANESCO kwa sasa maeneo yote ya uzalishaji, uzalishaji upo. Changamoto tuliyonayo sasa ni miundombinu iliyopo kwenye maeneo hayo ya uzalishaji. Hii inasababisha pia hata sasa naona kuna baadhi ya maeneo umeme unakatika, lakini ni kwa sababu ya kukosekana miundombinu. Sasa nini mkakati wa Serikali?
Mheshimiwa Spika, moja, tumewapa kazi TANESCO kufanya tafiti. Wanaweza kuja kwenye hatua hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameipendekeza. Pale ambapo tutakuwa tumejipanga na tunaona nani tunampa jukumu la kuzalisha, nani anasafirisha lakini pia msambazaji ni nani? Zinaweza kuwa ni taasisi za Serikali ambazo pia lengo lake ni moja. Kwa hiyo, tukifikia hapo kupitia utafiti unaoendelea sasa na Shirika letu la Nmeme Nchini, tutaweza kufikia hatua nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, suala la usambazaji, kama ambavyo mmeona Serikali leo ina mkakati wa kupeleka umeme mpaka vijijini, hii hatua tutaifikia kwa sababu tumefanya kazi nzuri sana na leo umeme unapatikana mpaka vijijini. Bado kazi hiyo inaendelea na malengo yetu kufikia Desemba mwaka huu tuwe tumefikia vijiji vyote nchini kupata umeme. Kwa nini? Tuna uhakika wa uzalishaji na bado tunaendelea kutafuta maeneo mengine ya uzalishaji, bado pia shirika letu limetoa nafasi kwa taasisi kuja kuwekeza kwenye uzalishaji. Kwa hiyo, nchi yetu itakuwa na umeme wa kutosha na kwa maana hiyo, eneo la uzalishaji halina matatizo kabisa. Tutajiimarisha pia kwenye eneo la miundombinu ya kwenye eneo la uzalishaji, usafirishaji na ugawaji kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nachukua ushauri wake, tutaufanyia kazi na hivi TANESCO wanafanya kazi hiyo. Tukishakamilisha haya, tutatoa taarifa kwenu Waheshimiwa Wabunge na hasa Mheshimiwa Mbunge ambaye ametoa pendekezo hili, tutakupa mrejesho wa hatua ambayo tutaifikia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Upungufu wa watumishi katika Halmashauri zetu limekuwa ni tatizo kubwa sana; na kwa mfano tu, Halmashauri yangu ya Mkalama ina upungufu wa zaidi ya walimu 800; na kwa kuwa nchi yetu sasa haina tatizo la wataalam na vijana wengi wanasubiri ajira: -
Mheshimiwa Spika, kwa nini sasa Serikali isianze kujaza nafasi wazi mara moja pale mtumishi anapostaafu au anapotangulia mbele ya haki kwa sababu mtumishi huyo tayari yuko kwenye bajeti inayoendelea, badala ya utaratibu wa sasa wa kusubiri Halmashauri ziombe vibali jambo ambalo huchukua muda mrefu na linaongeza ukubwa wa tatizo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mkalama kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ndani ya Serikali kupitia Wizara ya Ofisi ya Rais, Utumishi imeweka utaratibu mzuri tu wa kupata watumishi katika kuziba mapengo au watumishi wapya. Pale ambapo inatokea bahati mbaya mtumishi ametangulia mbele za haki, tunao utaratibu wa kujaza pia kwa kutangaza nafasi mpya, lakini hili linafanywa baada ya kufanya uhakiki wa kina kwa vipindi vya miezi mitatu, miezi sita au mwaka ili kuona tuna upungufu wa watumishi kwa kiasi gani; na wangapi wa kada ipi wanahitajika kujazwa?
Mheshimiwa Spika, kupitia Wizara ya Utumishi, Tume ya Utumishi wanacho kitengo maalum ambayo pia wanafanya uratibu kupitia Wizara zote na mahitaji yake. Kwa hiyo, unaweza kuona tunachelewa kutangaza nafasi hizo kwa sababu kwanza lazima tupate data base ya mapengo ya watumishi wa Serikali kwa kada na Idara, ili tuone Idara hii tutakapotangaza, mahitaji ni mangapi kwa ajili ya Wizara zote; ili tutakapotangaza, tunatangaza mara moja kwamba tunahitaji watumishi 1,000 halafu wanagawiwa kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kazi hii inapofanywa katika kipindi cha miezi sita au mwaka tunaona kama inachelewa lakini inasaidia Serikali pia kutambua idadi ya wafanyakazi waliopo na mahitaji, lakini pia na kuziba, halafu tuendelee kusimamia maslahi yao wakati wote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hilo la kuziba mapengo linaendelea, kuanzisha sekta mpya na kujaza sekta hizo. Kwa ujumla vibali hivi vinapokamilika utafiti huu, tunaomba kibali kwa Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais Mama Samia tunamwona anatoa vibali wakati wote kwa ajili ya kuajiri kada mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba kazi hiyo inaendelea kufanyika na mamlaka husika hupeleka takwimu na taarifa Wizara ya Utumishi kupitia Tume ya Utumishi na zinatangazwa wakati wote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu, mwaka 2018 tulipitisha Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na lengo kuu lilikuwa kuunganisha mifuko na vile vile kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi yanaboreshwa.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupitisha sheria hiyo, matarajio ya wafanyakazi hayakuzingatiwa na matokeo yake, Hayati John Pombe Magufuli alisitisha matumizi ya sheria ile. Mpaka sasa hivi baada ya kusitishwa, ongezeko la watumishi wanaostaafu kwa hiyari limeongezeka, ongezeko la fao la kujitoa limeongezeka na mifuko imekuwa ikilemewa kulipa mafao ya wastaafu kutokana na watu kutokujua hatima yao na kuamua kuwahi kustaafu kabla ya wakati.
Je, ni lini Serikali mtaleta mabadiliko ya sheria ambayo tayari mliji-commit zaidi ya mara tatu, hamkufanya hivyo; ili sasa wastaafu wetu wawe na uhakika wa maisha yao baada ya kustaafu kwamba yamezingatiwa kwenye sheria na kile walichokitaka? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bulaya, Mbunge wa Musoma… (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ni Mkoa wa Mara, siyo Musoma, maana nitakuwa na mgogoro na Mheshimiwa Mathayo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri jambo hili liko Ofisi ya Waziri Mkuu, nafahamu mchakato wote ni kwamba kweli tulikuwa na mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii ambayo inashughulikia mafao ya watumishi waliostaafu. Tulikuwa na LAPF chini ya Ofisi ya Rais, wakati huo ilikuwa Waziri Mkuu, tukawa na mifuko mingi, lakini tukaipunguza mifuko hii tukaacha michache ili iweze kulipa vizuri maslahi kwa watumishi waliostaafu. Sasa tuna NSSF ambayo pia inashughulikia sekta binafsi na wachache sekta rasmi, na pia kuna PSSSF baada ya kuwa tumebadilisha sheria hiyo.
Mheshimiwa Spika, ulipaji wa mafao unaendelea siyo kwa kiasi kikubwa, ni kwa sababu mifuko hii ilipoanzishwa tulikuta madeni mengi na makubwa. Kazi ambayo inafanywa sasa ni kulipa madeni ya wastaafu wa muda mrefu na tunaendelea kulipa wale wanaostaafu ili angalau kukamilisha hili, tufike hatua ya kuweza kulipa madeni pindi mtumishi anapostaafu na kuendelea kulipwa mafao yao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mabadiliko ya sheria yapo na kanuni zilitengenezwa. Kwa sasa tunaangalia kama kanuni na sheria hizi zinaweza kutufikisha hatua nzuri ya kulipa mafao kwa wakati. Tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana ndio anasimamia jambo hili; na wakati wote amekuwa na vikao na mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii ili kuhakikisha kwamba inalipa kulingana na wakati aliostaafu mtumishi; wale wa zamani na walioko sasa. Ulipaji unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunayo madai, lakini pia tunaendelea kupata changamoto za kutokamilisha ipasavyo kulipa wadai wote kwa sababu ya yale madeni. Serikali iliwahi kutoa fedha kwa ajili kuongezea uwezo wa mifuko yetu ili iweze kulipa mafao na kazi hiyo inaendelea. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya mapitio ya sheria hizo na Waziri wa Nchi yuko hapa, anaendelea kusimamia. Malengo yetu ni kulipa watumishi wote wanaostaafu kwa wakati na hatua hii nina uhakika tutaifikia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, lakini nashukuru kwa kauli ya Serikali ambayo imetolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, zoezi hili la uvalishaji hereni kwa ng’ombe lilianza katika Mkoa wa Rukwa, Wilaya Nkasi, na ikafikia mahali mpaka kutishwa kwa wafugaji, na mimi Mbunge nikalazimika kwa sababu ilikuwa ni kauli ya Serikali, nikapita kuwahamasisha wafugaji kutii maagizo ya Serikali na wakatoa hiyo fedha ya shilingi 1,750. Leo kuna maeneo ambayo yalikuwa hayajafikiwa; kwa kuwa ni utaratibu mzuri mlileta ninyi upigaji chapa siyo wafugaji, Serikali ilitoa hayo maagizo na wafugaji wakalipa, leo likaja agizo lingine la uvalishaji hereni wametii.
Mheshimiwa Spika, naomba kujua, kwa kuwa ni nia njema ya Serikali, kwa wale ambao walikuwa tayari wameshalipa hiyo fedha, itakuwaje ili na wao wajione ni sehemu ya wafugaji wengine wa Tanzania?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Nkasi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hatujasitisha malipo, tumesitisha zoezi hili ambalo linalalamikiwa ili kuipa nafasi Serikali kupitia Wizara ya Mifugo kufanya tathmini ya mapungufu ya kanuni iliyowekwa ili kuweza kufanikisha zoezi hili vizuri kwa kushirikisha na wadau. Kama kutakuwa na maamuzi mengine ndani ya Wizara ya kupunguza bei, fedha, itakuwa ni baada ya mjadala huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa sasa tumesitisha tu zoezi lenyewe kuendelea, kwa sababu tangu sheria imewekwa mwaka 2010 na kanuni zake mwaka 2011, kati ya mifugo milioni 45 ni mifugo milioni tano tu mpaka leo kuanzia mwaka 2011 ndiyo imefanikiwa kufikiwa. Kwa nini? Maana yake kuna tatizo. Kama tungetekeleza inavyotakiwa leo tungefikia angalau nusu ya mifugo yote nchini kuwekwa hereni.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumesema tunasitisha kwa muda wa miezi mitatu, ili kuipa nafasi Wizara kukaa ndani ya Wizara yenyewe, kupitia kanuni zao kuona wapi kuna dosari zilizosababisha kutofanikiwa kupata mifugo mingi zaidi, lakini kupitia hayo malalamiko ambayo yanawafanya wafugaji au kukwepa au kutoshiriki vizuri au kujiunganisha vizuri na watendaji walio kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambao ndio wanatakiwa kuwatambua watu wao kila Wilaya ili sasa kuweka mfumo mzuri unaowezesha kufikia hatua nzuri zaidi na kuondoa manung’uniko yanayotokana na utekelezaji ambao unaonekana si mzuri.
Mheshimiwa Spika, baada ya januari, sasa hayo mambo yote, maazimio yote yatakayokuwa yamefikiwa, ili waweze kufanya vizuri wakati wa utekelezaji yataanza kuanzia tarehe 1 Februari, 2023. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Swali litajikita katika eneo la zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki.
Mheshimiwa Spika, ninafahamu kwamba Serikali ilipoanzisha zoezi hili ilikuwa na nia njema kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameieleza lakini sisi wananchi pamoja na hayo ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyaeleza tunatambua pia kwamba zoezi hili lingepunguza kwa kiwango kikubwa migogoro ya wafugaji dhidi ya watumiaji wengine wa ardhi, kwa sababu mifugo ingekuwa imetambuliwa.
Mheshimiwa Spika, sasa wakati Serikali imesitisha zoezi hili ili iweze kufanya tathmini kwa miezi mitatu; nini mkakati wa Serikali wa muda mfupi na wa muda mrefu wa kuhakikisha kwamba uingizaji holela wa mifugo hautoendelea na hautoweza kuathiri na kuleta migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba yako matatizo kwenye sekta ya ufugaji ambapo kwa sasa tunaona kuzagaa holela kwa mifugo yetu, lakini pia mifugo mingi kuingizwa kwenye vyanzo vilivyohifadhiwa kisheria na kusababisha madhara mengine kama ambavyo sasa tumeona vyanzo vingi vinakauka.
Mheshimiwa Spika, kusitisha kwa miezi mitatu kutaiwezesha Wizara sasa kuweka mkakati thabiti kwanza kuhakikisha kwamba wanakutana na wadau na kuelimisha namna nzuri ya ufugaji kisasa kama alivyotamka kwenye taarifa; na pili, kushirikisha mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maana ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kutambua maeneo yote yenye mifugo na mipaka yao ili sasa lengo la kuweka hereni ambapo moja kati ya malengo ya kuweka hereni yaliyokusudiwa ni kuhakikisha kwamba tunapunguza kuhamahama kwa mifugo hii kiholela kutoka eneo moja mpaka eneo lingine, kwa sababu hereni inatambulisha mahali mfugo ulipo kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa utaratibu huu tutakuja kujipanga vizuri na kesho kutwa tuna kikao cha Mawaziri wote wenye sekta zinazohusu mifugo, maji, mazingira pamoja na ardhi, pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa hapa Dodoma kuweka mkakati wa kudhibiti hali hiyo. Hiyo ndiyo moja kati ya njia ambayo tumeamua ili tuweze kufikia hatua nzuri ya kuelimisha pia na wafugaji umuhimu wa kufuga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo mnakumbuka wakati tunaendesha zoezi la wanaohama kwa hiari Ngorongoro, na watu wa Loliondo kupisha lile eneo na kuwaweka mahali pazuri na upimaji wa vijiji vyao, tuliiagiza Wizara itumie vizuri eneo la Msomera kuwa ni eneo la ufugaji kisasa la kimkakati kama pilot area ili wafugaji wengine wapate kujifunza kutoka Msomera.
Mheshimiwa Spika, wakati Wizara inaendelea na zoezi hilo la kuratibu vizuri pale Msomera, tunataka sasa mfumo huo uhamie kwenye Halmashauri nyingine zote nchini ili ufugaji sasa uwe na tija, wafugaji watambulike, mifugo tuitambue, tuwasaidie kutohama kwa umbali mrefu unaosababisha mifugo kupata shida, kutafuta malisho na huku Serikali ikijipanga kujenga maeneo ya kunyweshea na majosho. Huo ndiyo mkakati wa Serikali.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali.
Mheshimiwa Spika, naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, kwa kuwa suala la Mlima Kilimanjaro ni suala nyeti kwa uchumi wa nchi, na ni maeneo muhimu sana ambayo yanatuletea fedha nyingi pamoja na Ngorongoro na Serengeti; na Jeshi la Kujenga Taifa limeonesha uwezo mkubwa katika operesheni mbalimbali katika nchi hii: -
Je, kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kuwa hata na kambi ndogo ndogo mbili hata za wanajeshi watano au sita, kuzunguka Mlima Kilimanjaro? Kwa sababu kwenda mbele inawezekana kuna wivu mkubwa unajitokeza kwa sababu ya matangazo makubwa ambayo tunayafanya ya kuleta watalii katika nchi hii.
Swali ni kwamba je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuwa na kambi kambi ndogo ndogo mbili za Jeshi ili kulinda Mlima Kilimanjaro?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tukio hili moto Mlima Kilimanjaro linajitokeza pia na maeneo mengine na linatokana na baadhi ya watu wasiopenda mema ambao pia hawataki hata uhifadhi, huchoma moto maeneo yote yanayotakiwa kuhifadhiwa kama ambavyo ingekuwa kupitia elimu mbalimbali zinazotolewa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa tumeona tatizo hilo na katika kipindi cha muda mrefu tulikuwa hatujapata moto kiwango hicho kwenye Mlima Kilimanjaro, lipo jambo tumejifunza. Ushiriki wa majeshi yetu yote; JWTZ, Jeshi la Mgambo, Jeshi la Polisi, na wananchi pamoja na Skauti na makundi mbalimbali yaliyojitokeza kwenda kuzima moto, tayari baada ya zoezi hilo litakapokamilika, tutakaa chini kufanya tathmini.
Swali lako ambalo limeingia pamoja na ushauri, tutauzingatia ili sasa tuwe na mkakati endelevu kwenye maeneo mengi muhimu ambayo yanaweza kujitokeza tatizo la moto, ikiwemo na kuimarisha Kitengo cha Maafa na hasa kwenye maeneo ya moto. Kuwa na vifaa, kuwa na wataalam ambao pia wanapata mafunzo ya mara kwa mara ili tuweze kukabiliana na majanga haya yanapotokea popote pale.
Mheshimiwa Spika, naomba kupokea pia na ushauri aliutoa Mheshimiwa Kiswaga. (Makofi)
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali moja kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kutokana na taarifa iliyowasilishwa. Kwa mujibu wa waraka ambao unaelekeza adhabu za viboko kwa wanafunzi wenye utovu wa nidhamu, viboko visizidi vinne na ameidhinishwa Mwalimu Mkuu au Mkuu wa Shule au atakayeidhinishwa na wakuu hao kutoa adhabu hiyo. Kutokana na usimamizi au udhibiti ambao hauko sawa, imebainika taharuki kama ambavyo imejiri hivi karibuni.
Je, kwanini Serikali isirekebishe waraka huu na kuongeza kwamba wakati aliyeidhinishwa kama ni Mkuu wa Shule au mwingine aliyeidhinishwa anatoa adhabu kukawa na Kamati maalum ya usimamizi na kubariki adhabu hiyo ili kuondokana na taharuki kama hizi? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli waraka wetu wa elimu umetoa maelezo thabiti ya namna ya utoaji wa adhabu shuleni, kama nilivyosema kwenye maelezo yangu, adhabu ya viboko ni moja kati ya adhabu zinazotumika katika kumjenga mtoto na kumfanya aweze kutii sheria za shuleni na viboko visizidi vinne. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa uundwaji wa Kamati Shule zote za Msingi zina Kamati ya Shule, na Shule zote za Sekondari zina Bodi ya Shule. Pale ambako mwanafunzi hufanya kosa kubwa kuliko haya makosa madogo madogo basi mtoto huyo, kwanza hatua inayochukuliwa mzazi kuitwa kujulishwa tabia na mwenendo wa mtoto huyo ili sasa kumshirikisha mzazi katika kumjenga mtoto kinidhamu. Mbili, pale ambako adhabu hiyo inahitaji kumfukuza shule unashirikisha sasa Kamati ya Shule. Kwa hiyo, utaratibu wa utoaji adhabu umewekwa vizuri kabisa na ndiyo ambao unafuatwa mashuleni. Hili ambalo limejitokeza hivi karibuni ni tatizo la mmoja kati ya watumishi wengi kutenda bila kufuata utaratibu lakini siyo utaratibu ambao umewekwa na siyo ambao unatumika kwenye maeneo mengi. Ahsante sana.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimuwa Waziri Mkuu kwa kuwa changamoto hii ya Walimu kuchapa watoto bila utaratibu na tena kikatili, nini sasa Serikali haioni kama kuna haja ya kuwaelimisha Walimu hawa somo la maadili la namna ya malezi ya watoto na makuzi katika shule zetu za Msingi na hata Sekondari?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lemburis, Mbunge wa Arumeru kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, taasisi zote za elimu zina taratibu zake, na uendeshaji wa elimu nchini una sheria na kanuni zake ambazo zimewekwa, na ndizo zinazosaidia kuongoza wakuu wa taasisi na wale watumishi wa taasisi husika katika kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa; na ndiyo sababu unaona mambo yanaenda vizuri. Hiyo ni kuanzia elimu ya awali, ya msingi, sekondari mpaka elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo uainishaji wa sheria hizi na kanuni ndio unaoongoza watumishi walio kwenye sekta hiyo au taasisi hiyo kufuata. Ndiyo maana tunaona sasa utulivu upo na kazi zinaenda kwa sababu kila mmoja anazingatia sheria na kanuni zilizopo. Kwa hiyo hatuwezi kusema tutachukua hatua kali kwa sababu miongozo ipo pale ambapo mtumishi anakiuka taratibu na sheria, sheria ile imeelekeza na adhabu ambazo zinatolewa kwa mhusika. Kwa hiyo utaratibu huo unatumika kama ni adhabu ndogo kwa aliyekiuka utaratibu umeainishwa, kama ni adhabu kubwa imeainishwa lakini pia hata akitakiwa kwenda mahakamani imeainishwa.
Mheshimiwa Spika, lakini tuzingatie tu kwamba taaluma ya ualimu ina misingi yake na imewekea utaratibu pia chini ya Wizara ya Elimu na kwa hiyo zipo kamati za maadili mioongoni mwa walimu. Wakati mwingine vyama vya wafanyakazi kama vile CWT yenyewe inachukua nafasi pia kukaa na walimu kuwafanyia counselling pia kuwaelimisha ili kufanya mambo yanavyokwenda kama utulivu ambao sasa upo na utaratibu huo ndio ambao tunautumia kwa sasa.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, wakati Waziri Mkuu anatoa maelezo yake amesema sasa ni marufuku watu kutoa taarifa ya matokeo haya katika social media. Matendo haya yamekuwa yakifanyika na yanafichwa na wakati mwingine viongozi wahusika wanalinda waliyoyatenda. Je, Waziri Mkuu haoni kuwa kitendo cha kuwazuia watu kutotoa taarifa ambayo ilikuwa inasaidia viongozi wahusika kuchukua hatua haraka, huoni kwamba matendo hayo yataendelea kufanyika na yataendelea kufichwa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rwamlaza, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye taarifa yangu, kwamba malengo ya kutahadharisha kuleta mkanganyiko, taharuki kwenye jamii hayalengi kulinda maovu yanatotokea bali yanalenga katika kuifanya jamii iendelee kuwa tulivu. Kwa sababu gani; taratibu zibainishwe pale ambapo mtu anakiuka utaratibu basi hatua kali zinachukuliwa.
Mheshimiwa Spika, tunatambua tukio ambalo limejitokeza pale Kyelwa aliyechukua video ni mwalimu ambaye alishindwa kumwelekeza mwalimu mwenzake kwamba jambo hilo lisifanyike kwa sababu ni kiongozi wa juu kwa cheo. Lakini bado alikuwa ana uwezo wa kutoa taarifa kwa maafisa elimu wao wa kata, pia tuna afisa elimu wa wilaya na adhabu zikachukuliwa. Kwa hiyo video ile aliyochukua badala ya kuirusha kwenye mtandao angeweza kuipeleka pia kwa afisa elimu kama ushahidi wa tukio lililotokea mahali pa kazi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo bado hatusisitizi sana hilo kwa sababu limesaidia pia kutoa taarifa. Hata hivyo, katika kuzuia taharuki na kutoa picha ambayo kwa jamii juu ya matendo yanayotendeka kwenye maeneo haya tulilazimika pia kushauri kwamba ni vizuri taratibu zikaenda kwenye mamlaka husika, kwa sababu mamlaka zipo na zimeainishwa kisheria pia.
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa kuwa viboko hivi vinaleta taharuki kubwa sana kwa nini msilete mwongozo tu aidha tukafuta kabisa ama walau kutoka nne iwe moja? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge wa Kiteto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Olelekaita ametoa ushauri; na kwa kuwa hii ilikuwa ni kanuni zilizokuwa zimewekwa na zikatolewa na waraka kutoka Wizara ya Elimu na Utamaduni, basi kwa ushairi huo tunauzingatia tutaona kama inawezekana, wadau watahusishwa, wataangalia mwenendo wa nidhamu, matatizo ya nidhamu yaliyopo nchini na pia wakati tulionao, ambao ndio unaowezesha. Hata sisi Wabunge kubadilisha sheria moja na kuifanyia maboresho inatokana na wakati. Kwa hiyo nalo pia tutaliangalia kama wakati unaruhusu kuondoa viboko vinne mpaka kimoja au kuondoa kabisa basi wadau watatushauri, na Serikali tupo tayari kutekeleza pale ambako inaonekana wadau watakubaliana na hilo, ahsante sana.
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. Kwenye huo waraka nimeona tumetoa tu adhabu ya viboko, lakini tunatambua watoto wetu wengi ambao wanaonekana ni wakaidi shuleni inatokana kwa sababu wameathirika aidha na makuzi au malezi ya nyumbani. Kwa nini tusiweke pia nafasi ya watoto hawa kupewa ushauri kabla ya kutanguliza viboko; kwamba, kuwepo na ushauri kabla ya kuadhibiwa kwa viboko kwenye huo waraka? Nakushukuru.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ndingo Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye maelezo pia niliyoyatoa hapa nimetoa wito kwa walimu wetu wa shule za msingi, sekondari, lakini hii inaenda hata pia kwenye vyuo vya kati na vyuo vya juu; kwamba tuangalie ukubwa wa makosa, umri, mahali na wakati wa makosa yalipofanyika. Nataka tu nitoe taarifa kwamba kwenye taasisi zetu za elimu tuna walezi wa watoto wa kiume na wa watoto wa kike na tumeweka hii walezi kwa lengo la kutoa ushauri pale ambapo tunaona kuna umuhimu wa ushauri. Kazi hii inaendelea shule ya msingi, sekondari na tunatumia zaidi majina ya kingereza matron na patron ndio ambao wanatumika kutoa ushauri nasaha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo pale ambako mwanafunzi anatenda kosa ambalo linahitaji kushauriwa wanafanya; na ndio hii ndiyo inasaidia kupunguza pia hata mkanganyiko kwenye jamii kutokana na nidhamu za watoto hawa. Hata hivyo bado kwenye taarifa yangu nimeeleza walimu wana kazi nyingi sana wanazozifanya shuleni. Wanatumia muda wao katika kuwafanya watoto kuwajenga katika maadili, pia katika kuwafanya wadumishe mila, desturi na utamaduni tulionao huku pia wakiwapa taaluma mbalimbali. Nimetoa wito pia kwa walezi ambao ndio wana nafasi kubwa ya malezi yam toto huyu kuanzia nyumbani pia hata mwenendo wake na baadaye nimetoa ushauri kwamba ni vyema wazazi na walezi wakawa wafuatiliaji wa karibu wa mtoto huyu badala ya kuwaachia majukumu hayo waalimu pekee ili wasaidie watoto hawa kubadilisha mwenendo. Mzazi akishiriki tunaamini mtoto huyu atabadilika sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutaendelea kutumia hizo taaisisi na idara hizo za ushauri ambazo ziko katika kutusaidia pia kurekebisha mwenendo wa mtoto awapo shuleni, ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu tumekuwa tukiona jitihada zako za kuzunguka nchi nzima kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo. Lakini katika ukaguzi huo umekuwa ukikuta miradi hiyo haitekelezwi vizuri kwa maana kunakuwepo na ubadhirifu, wizi na uzembe wa aina mbalimbali na hata ripoti ya CAG imekuwa ikitoa ubadhilifu huo na wizi mara kwa mara katika ripoti hiyo.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, nini kauli ya Serikali kuhusu hali hii ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara. Ni mkakati upi wa makusudi na wa maalum ambao Serikali inachukua ili kuhakikisha kwamba wizi na ubadhirifu katika miradi ya umma haitokei kabla haijafanyika ili basi wananchi waweze ku…
SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, majibu.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lemburis, Mbunge wa Arumeru kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inao mfumo wa kufanya tathmini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo na kufanya mapitio ya mwenendo wa matumizi ya fedha na mali za umma kwenye sekta hizo. CAG ni taasisi mojawapo ambayo inakwenda kuona mwenendo wa matumizi ya mali na fedha za umma kwenye sekta zote za Serikali na ikibidi pia hata sekta binafsi ambayo ina maslahi ya moja kwa moja kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba wanapofanya kazi hiyo wanabaini mapungufu na wakati mwingine mapungufu hayo wachache wanafanya kwa makusudi na CAG anachokifanya ni kuishauri Serikali namna bora ya kudhibiti hali hiyo kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli na mimi nilipata nafasi ya kufanya ziara kwenye Halmashauri zetu, taasisi mbalimbali za Serikali na ninapokwenda wakati mwingine nakwenda na taarifa ya CAG ambayo pia inashauri Serikali namna bora ya kusimamia maeneo hayo na kuchukua hatua. Sasa namna gani nzuri ya kuendelea kusimamia.
Mheshimiwa Spika, kwanza tunatambua mchango mzuri wa taasisi hii ambao pia unatuainishia na kubainisha mapungufu hayo kwenye sekta zetu za Serikali na kazi yake ya kuishauri Serikali tunachukua ushauri huo na kuufanyia kazi, pale ambako tunauona ubadhirifu wa moja kwa moja tunachukua hatua na pale ambako anashauri namna ya kuboresha tunafanya hilo na sasa Serikali yetu imeandaa mfumo mzuri sana wa kufatilia sekta zetu kabla CAG hajafika.
Mheshimiwa Spika, ofisi yangu, Ofisi ya Waziri Mkuu, imeanzisha sasa Kitengo cha Ufatiliaji na Tathmini kwenye Sekta za Serikali ambazo zinabaini mapungufu hayo kabla CAG hajafika na kitengo hiki tumekiimarisha zaidi na kimeshaanza kazi. Sasa hivi kinapita kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, taasisi mbalimbali za Serikali ili kuona hali hiyo, kufanya tathmini, lakini pia kushauri pale ambapo kuna mapungufu kwenye sekta hiyo kabla CAG hajafika, lakini tunapokuta mapungufu tunaendelea kuchukua hatua.
Kwa hiyo, niendelee kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko makini kwenye hili, inafatilia na itaendelea kufatilia ili kuweza kudhibiti mali na fedha za Serikali, iwe ni kwa ajili ya mradi au kwa matumizi ya kwawaida kwenye ofisi yote haya ni majukumu ambayo Serikali inayafanya, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nyakati mbalimbali tumeona Serikali yetu ikitoa misamaha ya kodi kwenye bidhaa zile muhimu ili basi kupunguza gharama kwa wananchi wetu. Mwaka 2019 tuliona msamaha wa kodi kwenye taulo la kike, lakini bei ya soko haikupungua na mwaka 2021 tuliona msamaha wa kodi kwenye simu janja, lakini bei ya soko haikuweza kupungua.
Je, ni ipi mikakati ya Serikali kwenye kudhibiti bei ya soko, pale ambapo misamaha hii ya kodi inapotolewa? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika naomba kujibu swali la Mheshimiwa Swai, Mbunge wa Arusha kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba Serikali inao mfumo wa kutoa misamaha ya kodi pale ambako inajiridhisha kwamba eneo hilo linaloombewa msamaha linaweza pia kupewa msamaha huo na hiyo inatakana pia na mtizamo wetu ndani ya Serikali kwamba kunaweza kuwa kuna maslahi, maslahi hiyo inaweza kuwa ni pamoja na ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema la kupunguiza gharama ya bidhaa hiyo au ya huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, mfano hivi karibuni tumeona kupanda kwa bei ya mbolea nchini na Serikali ilipogundua kwamba gharama ya kununua mbolea ya shilingi 110,000 au zaidi ni kubwa na kwamba Watanzania hawawezi kumudu kununua na kwamba ili kuleta maslahi kwa Watanzania, Serikali ilitoa msamaha wa kodi, wakati mwingine pia na kutoa ruzuku na kuwezesha kupunguza gharama ya upatikanaji wa bidhaa hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali inaendelea na utaratibu huu pale ambako inaona kuna bidhaa au huduma yenye maslahi na tunaweza tukaamua au mtu anayetoa huduma hiyo akaomba msamaha wa kodi na msamaha ukitolewa matarajio yetu ni kuona kuwa gharama hiyo inapungua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba maeneo yote haya ambayo yanapata ruzuku, yanapewa msamaha wa kodi, tunayasimamia kuwa na maslahi kwa watumiaji, kwa Watanzania kwa sababu unaposema unatoa msamaha wa kodi lile pengo la fedha lililokuwa linatakiwa kuuzwa awali na hii ya sasa baada ya msamaha linalipiwa pia na Serikali. Kwa hiyo, gharama inabaki pale lakini Serikali inatoa mchango wake inaweza kulipia kile cha ziada ili mtumiaji aweze kupata faida.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea kuratibu hiyo na kusimamia maeneo yote ambayo tunatoa ruzuku, msamaha kuwa yanauzwa kwa bei ambayo tumekubaliana na sasa iuzwe baada ya kutoa msamaha.
Mheshimiwa Spika, ninataka niwahakikishie Watanzania tutaendelea kufatilia maeneo yote amabayo tumetoa msamaha, tutaendelea kufatilia maeneo yote tuliyotoa ruzuku ikiwemo na mbolea kama ambavyo Wizara ya Kilimo na kila kiongozi wa Serikali tunapofanya ziara kwenye Wilaya huko, tunaendelea kutoa misamaha hiyo ili kudhibiti mfumuko wa bei. Huo ndio utaratibu unatumiaka ndani ya Serikali, ahsante sana. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuchukua maeneo ya wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo pale ambapo Serikali haina eneo la kufanya miradi hiyo hasa hasa miradi kama ya shule, hospitali au kupanua maeneo ya jeshi au uwekezaji, na baada ya kuchukua maeneo hayo hufanyiwa tathmini ili watu waweze kulipwa fidia. Hata hivyo kumekuwa na tatizo la ucheleweshaji wa kulipa fidia na sehemu nyingine kuingia hata mambo yasiyokuwa ya uaminifu katika utekelezaji wa ulipaji wa fidia.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nini msimamo wa Serikali katika jambo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’enda, Mbunge wa Manispaa ya Kigoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upo utaratibu wa Serikali wa kuchukua maeneo mbalimbali ya ardhi yetu, kwa ajili ya miradi ya maendeleo pale ambapo tunaona tunahitaji kutekeleza mradi maalum kwa maslahi ya Watanzania na kwa hili naomba nianze kueleza umma wa Watanzania kuwa ardhi yetu hii ni ya umma na Mheshimiwa Rais, ndio mdhamini wa ardhi hii. Mheshimiwa Rais anaweza kuchukua ardhi popote kwa maslahi ya umma, kwa lengo la kutekeleza mradi ambao unaweza kusaidia jamii ya eneo hilo kuutumia vizuri. Lakini tunapochukua ardhi hiyo huwa tunafanya tathmini ili kulipa fidia ya mali iliyoko kwenye ardhi, inaweza kuwa labda nyumba au mazao, lazima yafanyiwe tathmini.
Mheshimiwa Spika, ni kweli mara kadhaa Serikali tumekuwa tukichukua maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya miradi ya umma na tunapokuta kuna mali imewekezwa na mtanzania huwa tunalipa fidia.
Sasa suala la ucheleweshaji ni taratibu vigezo kama havijakidhi; moja, wakati tunafanya zoezi la tathmini ni lazima tufahamu nani hasa yuko hapo na amewekeza hiyo na lazima kuwe na viambata vinavyoeleza kwamba huyu ndio mwenye eneo hili na tunampiga na picha, thamani inatambulika hapo hapo na yeye anatambua thamani yake halafu maandalizi ya kulipa fidia yanafanywa.
Mheshimiwa Spika, ucheleweshwaji unakuja kama zoezi hilo halijakamilika au kuna migogoro ya wao kwa wao, wanagombania eneo hilo kwa umiliki, hapo inaweza kuchelewa, na wakati mwingine tathmini na idara inayolipa labda kama ilikuwa inategemea bajeti kunaweza kuwa na- delay, lakini niendelee kuwahakikishia Watanzania ambao wanafikiwa maeneo yao kwa ajili ya tathmini, kwa ajili ya kutumika kwa miradi na tunafanya tathmini kama kunachelewa. Hakuna Mtanzania, hakuna mwananchi ambaye anachukuliwa ardhi na huku akiwa amewekeza, tukafanya tathmini akakosa stahiki yake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali itaendelea kusimamia maeneo hayo na kama yako maeneo labda pale Kigoma kuna eneo ambalo tathmini ilishafanyika na bado hatujalipa kutakuwa na moja kati ya haya niliyoyasema; au kuna migogoro, labda idara ilifanya tathmini hiyo na ilikuwa haijajiandaa na kama haijajiandaa tunarudi kwenye sheria yetu ile ya kwamba toka siku ya tathmini mpaka siku ya malipo ikiwa zaidi ya miezi sita lazima ifanyike tathmini tena ili kujua thamani halisi ya wakati huo ili sasa kuwezesha idara, lakini wananchi kujipanga kwa ajili ya kupata fidia yao.
Mheshimiwa Spika, hayo ndio maelezo sahihi ya Serikali ambayo yanatumika wakati wote tunaopohitaji kuchukua eneo na kufanya tathmini na kulipa wananchi. (Makofi)
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulio chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ulianzishwa kama namna mojawapo ya kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na chanzo kikuu cha mapato katika mfuko huu ni bajeti inayotengwa na Serikali kupitia Bunge hili tukufu na kwa miaka saba mfululizo, mfuko huu umekuwa hautengewi fedha zozote. Mwaka 2022 mfuko huu umetengewa shilingi bilioni moja ambayo inatakiwa kwenda kwa vijana katika Halmashauri zote 185 nchi nzima. Fedha hizi ni ndogo, hazitoshi na hivyo hata impact ya mfuko huu haionekani kwa vijana. Sasa nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inatafuta vyanzo vingine vya mapato katika mfuko huu ili kuutunisha na kuuongezea tija zaidi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba tu ridhaa yako nimjibu Mheshimiwa Ng’wasi na nataka nimjibu kwa sababu ameuliza swali ambalo liko ofisini kwangu na nalifahamu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu inayo Wizara inashughulikia vijana na kwenye eneo hili, ziko programu mbalimbali za uwezeshaji kwa vijana wetu na tumeanzisha na mfuko huo wa vijana.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwa miaka 7 haujatengewa fedha, lakini katika kipindi hiki hiki tulishatenga fedha zaidi ya bilioni moja, kumbukumu zangu nilizonazo ofisini zinaonesha mwaka 2017 tulitenga bilioni moja, hazitoshi kwa mahitaji ya vijana nchini, tukaongeza tena bilioni nane, tukawa na bilioni 1.8 na tulishaanza kuzitoa. Tunatoa kwa vijana kwenye halmashauri zetu ambao wanakidhi vigezo na vigezo kukidhi vigezo ni moja kwanza ufahamike na Ofisi ya Halmashauri, uko wapi? Unafanya nini ili unapopata ile fedha, basi Ofisi ya Halmashauri ambayo inaratibu vijana iwe inafahamu huyu kijana yuko wapi na kwa kuwa sehemu kubwa inaweza kuwa ni mikopo au support lakini tujue kwamba kama ni mkopo unaweza kuurejesha.
Mheshimiwa Spika, sasa nini kinafanyika? Kwanza tumeunda mfuko maalum huu mfuko ambao tumeunda na tunao mwongozo wa kuendesha mfuko huo. Na mfuko huu, mbali ya Serikali lakini pia huwa tunatoa fursa kwa wadau kuuchangia na sasa tumeanza kuona taasisi mbalimbali ambazo zinasaidia Serikali yetu katika kukuza uwezo wa vijana uweze ku-support.
Nini Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya, baada ya kuona kwamba kiwango hiki hakitoshi? Kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inalenga kuwawezesha vijana kumudu, kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi, sisi tumeanzisha programu ya uanangezi, programu ambayo inawachukua vijana na kuwapeleka kwenye vyuo mbalimbali nchini, ili kupata ujuzi ambao utamuwezesha yeye mwenyewe kujiajiri. Tunawapeleka VETA, tunawapeleka vyuo ufundi binafsi, lakini tunawapa pia mafunzo ya huduma, utoaji huduma, kuwapeleka mahotelini namna ya kutoa huduma kwenye hoteli mbalimbali na anapomaliza kozi yake ya miezi sita, ambayo inagharamiwa na Serikali anakuwa tayari anaweza kujiajiri au kuajiriwa na sekta mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, programu hizi zipo nyingi na tunaendelea kuziratibu na nikuhakikishie najua Mheshimiwa Ng’wasi ni Mbunge na unawakilisha vijana tunao mpango wa kuhakikisha vijana hawa wanakuwa na uwezo, lakini wanakidhi vigezo vya kuweza kupata support kupitia mfuko huu.
Mheshimiwa Spika, lakini hatujaishia hapo tu, Serikali tumeendelea pia kutoa maagizo kwa Halmashauri za Wilaya, ule mfuko unaokopesha wa asilimia nne, wenye kipengele cha vijana cha asilimia nne nao pia wananufaika, na sasa nishauri ili waweze kunufaika waunde vikundi kwenye maeneo yao. Mmoja mmoja ni ngumu, unaweza kukosa kufikia vigezo, lakini mkiwa kikundi inakuwa rahisi zaidi mtafanya shughuli ya pamoja. (Makofi)
Kwa hiyo mfuko wa halmashauri wa asilimia nne nayo inasaidia katika halmashauri zote katika kutambua vijana na kuwa-support ili waweze kufanya shughuli zao kwa lengo la kuongezea uchumi wao. Kwa hiyo, programu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, programu iliyoko Ofisi ya Rais, TAMISEMI hizi zote kwa pamoja, lakini pia michango tuliyopata kwa wadau yote hii inaimarisha katika kuwawezesha vijana kufikia katua na malengo waliyojiwekea, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, malengo ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana mwaka 1993 ilikuwa ni kuhakikisha inawapatia mtaji vijana kwa mikopo ya masharti nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi, lakini kwa muda sasa mfuko huu umekuwa ukitengewa fedha, lakini vijana wanakosa hizo fedha kwa kiasi kwa sababu ya kukosa vigezo, lakini pia tunafahamu zipo halmashauri ambazo zinakosa asilimia 10 zile ambazo ni four, four, two; nne za vijana, nne za wanawake na mbili za walemavu, kwa sababu hazina mapato ya kutosha.
Ni kwa nini sasa Serikali isitumie Mfuko wa Maeneleo ya Vijana kama equalization fund kuziwezesha zile halmashauri amabzo zina mapato machache, mapato kidogo ili na zenyewe ziweze kutoa zile asilimia nne za halmashauri ili vijana waweze kupata mitaji kama ambavyo yalikuwa malengo ya kuanzishwa Mfuko wa Maendeleo Vijana? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hanje, Mbunge wa Singida kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotoa majibu ya swali la awali linalohusu vijana kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuwawezesha vijana nchini kwa kuwatengea fedha kupitia mfuko, lakini pia kwa kutengeneza vigezo ambavyo vinaweza vikakidhi kwa ajili ya vijana hawa waweze kunufaika na mfuko wao.
Mheshimiwa Spika, eneo hili la kutunisha mfuko nimeeleza kwamba Serikali inajitahidi kila mwaka kutenga fedha kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. Tulitenga bilioni moja, tukaongeza milioni 800 na bado tutaenedelea kutenga, lakini bado hazitoshi na nimeeleza awali. Kwa kutotosha fedha hizi bado tunaendelea kuhusisha na Wizara nyingine zenye programu za vijana ikiwemo na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo imetenga mfuko na fedha kupitia mapato ya ndani asilimia 10; asilimia nne ni za vijana, lengo ni kutunisha ule mfuko.
Mheshimiwa Spika, sasa na tumefungua milango kwa taasisi binafsi ambazo na zenyewe zinashughulikia vijana na Serikali yetu tuna marafiki wengi ambao pia wanaona jitihada zetu za kuwawezesha vijana, nazo pia zinachangia na ndio kwa sababu tulianzisha mfuko ili kurahisisha pia michango yao kuingia pale, jukumu letu Serkali ni kuusimamia mfuko uweze kuleta manufaa.
Mhehimiwa Spika, lakini la pili hivyo vigezo ambao vijana wengi wanakosa vigezo, tunaposema kukosa vigezo ni pale ambako kijana anakuwa hana anwani maalum, kijana huyu ni mzaliwa wa pale Singida, lakini anakutwa yupo Dar es salaam; kule Dar es Salaam anahitaji pia kuwezeshwa ni lazima tujue huyu hapa Dar es salaam anakaa wapi? Mtaa gani anafahamika na viongozi wa mtaa huo?
Sasa sehemu kubwa ya vijana wetu wanashindwa kukidhi kigezo hicho kwa sababu na wenyewe wako mobile, wanatembea huku, wanaenda huku katika kutafuta manufaa hayo, katika kujiwezesha kiuchumi. Lakini nini tunakifanya sasa, tunaendelea kuwahamasisha vijana kwenye halmashauri zetu na tunawatambua vijana hawa kupitia Idara yetu ya Maendeleo ya Jamii kwenye halmashauri, tunawatambua vijana kwenye vijiji, idadi yao, mahitaji yao ya shughuli za kiuchumi, huku Ofisi ya Waziri Mkuu kama nilivyosema tumeandaa mpango wa mafunzo ya vijana hawa ili kuwawezesha kuwa mafundi, kuwa na uwezo wa kufanya kazi mbalimbali na mafunzo haya yanachukua miezi sita, yanagharamiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, wanaenda vyuoni wakisoma miezi sita, wanarudi wanakuwa tayari wanakuwa na vigezo vya kupata mikopo kwa sababu tayari tunafahamu anakokaa, ana ujuzi, unajua akichukua fedha anaenda kuitumia kwa ajili ya moja, mbili, tatu. Jitihada hizi zinaendela kupanuliwa wigo ili sasa tuweze kuwafikia vijana wote.
Mheshimiwa Spika, na mwisho niliishia na ushauri kwa vijana wetu, pindi wanapomaliza mafunzo haya, wanapokuwa pamoja kwa maana ya kuunda vikundi wanakuwa vizuri zaidi, huo ni ushauri na wanapofikiwa ni rahisi wao wakiwa kikundi kukopesheka kuliko wakiwa mtu mmoja mmoja.
Kwa hiyo, tunaendelea kufanya maboresho kwenye maeneo yote haya; kwanza kuwa na vigezo, lakini mbili kuweza kuwafikia na kutunisha mfuko ili waweze kunufaika. Jitihada hizi zinaendelea na tunaendelea sasa kukusanya Wizara zote ambazo zinahusika na vijana ikuwemo na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu yenyewe na wadau ambao tunao na jumuiya mbalimbali za dini na vijana zote hizi zinatumika katika kuhakikisha tunakusanya nguvu ya pamoja kuwawezesha vijana ili kuweza kuwawezesha kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, huo ndio utaratibu tunautumia kwa sasa, lakini nikiri kwamba maswali yote mawili yanaweka msisitizo kwa vijana, kwa hiyo Serikali tutapanua wigo wa kutoa huduma kwa vijana zaidi ili malengo ya vijana yaweze kufikiwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwepo na ongezeko la mizani za kupimia mizigo ya magari nchini kote na hivyo kuongeza idadi kubwa ya watumishi katika mizani hizo, ambao kimsingi hawa mikataba ya kudumu. Sasa ukosekanaji wa mikataba ya kudumu inasababisha kukosekana kwa haki yao msingi kukopa. Nini kauli ya Serikali na hasa ukizingatia ajira hizi mpya watumishi kupata ajira za kuduma?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeongeza huduma za upimaji wa uzito wa magari nchini ambako tunavyo vituo maalum vilivyojengwa, lakini pia tunazo mizani zinazotembea kwa lengo la kuhakiki uzito wa magari ili yanapopita kwenye barabara zetu tusipate uharibifu mkubwa, kwa kuongeza mizani pia tumeongeza watumishi waliopo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, sasa watumishi hawa ni sehemu ya watumishi wote ambao wanapata mikataba yao.
Mheshimiwa Spika, iko mikataba ya muda mfupi, iko mikataba ya kudumu na tunafanya hilo ili kuwezesha pia watumishi hao kuwa na stahiki zao za kimsingi. Sasa ni lini tutaweza kuimarisha mikataba hiyo ili wapate haki zao za kudumu pamoja na stahiki zingine ikiwemo mikopo na haki nyingine, hili linategemea pia na nafasi za ajira Serikali na nafasi ambazo zinapewa sekta ya ujenzi kwenye mizani ili kuweza kuwaajiri moja kwa moja watumishi hawa.
Mheshimiwa Spika, ninalichukua hilo na Waziri wa Uchukuzi yuko hapa anasikia, kwa hiyo, ni jukumu sasa la kuratibu vizuri watumishi wote wanaofanya kazi kwenye mizani wenye mikataba ya muda mfupi kuona kama wanazo sifa za kupata ajira za kudumu ili wapate mikata ya kudumu na hatimaye haki zao ziweze kusaidiwa. (Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri Mkuu ugonjwa wa malaria unasababisha vifo vya Watanzania wengi hususan wanawake wajawazito na watoto. Naishukuru Serikali iliona tatizo na wakaamua kufanya investment kubwa pale Kibaha, takriban Bilioni 46 kujenga kiwanda cha viuadudu na ikasaini mkataba na NDC kwa makubaliano kuwa watanunua zile dawa na kusambaza katika maeneo yote nchini ili tuweze kutokomeza ugonjwa huu lakini haijafanya hivyo.
Kutokana na takwimu kutoka Mpango wa Kudhibiti Malaria Nchini tunatumia takribani Bilioni 108 kwa mwaka kufanya warsha na matamasha mbalimbali na preventive measures kama net kupambana na ugonjwa huo.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu nataka kujua mkakati wa Serikali kuhakikisha tunasaini mkataba tena na NDC wa kununua na kuhakikisha tunasambaza dawa hizi nchini kuhakikisha tunatokomeza janga hili ambalo linapoteza maisha ya Watanzania wengi. Nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tweve, Mbunge wa Mkoa wa Iringa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu imefanya uwekezaji mkubwa sana pale Kibaha Mkoani Pwani, kwa kujenga kiwanda kikubwa sana kinachotengeneza viuadudu na ili kurahisisha masoko, Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais - TAMISEMI, zimeingia mkataba wa kununua viuadudu na kuvisambaza kwenye hospitali zetu, Vituo vya Afya na hospital za Wilaya, Zahanati pia maeneo kama shule na taasisi zote ambazo zinakusanya vijana wengi na kuna tatizo la mbu. Kama sehemu ya awali ya soko mbali ya soko ambalo tunauza pia nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, utaratibu huu tuliingia mikataba ya kwamba kiwanda kile moja kati ya mteja atakuwa ni Serikali yenyewe kupitia Wizara zote mbili ili kukabiliana na tatizo la malaria inayosababishwa na mbu. Ni kweli kwamba Serikali inasimamia mauzo ya dawa hizo ndani na nje ya nchi, ziko Halmashauri ambazo bado hazijatekeleza wajibu wake wa kwenda kuchukua viuadudu, lakini baadhi ya hospitali ambazo ziko chini ya Halmashauri hazijapata huduma hiyo kupitia Halmashauri hizo. Mpango wa Serikali katika hili ni kuhakikisha kwamba tunawasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri kununua viuadudu vile ili wapulize kwenye maeneo ya makazi ya wananchi kupunguza kiasi cha mbu ili kupunguza ugonjwa wa malaria. Kwa hiyo, nachukua wazo lako na swali lako kama ushauri kwa Serikali tuimarishe mikataba, tupitie mikataba ili tuweze kusambaza dawa ile itusaidie: -
(i) Itapunguza tatizo la malaria inayosababishwa na mbu;
(ii) Tunaimarisha soko ambalo tunaliendesha kupitia uwekezaji mkubwa wa fedha ambazo umezitamka Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, hivyo, naomba nitoe wito kupitia swali hili kwa Halmashauri zote nchini lakini na hospitali za Mikoa zilizo chini ya Wizara ya Afya, kuhakikisha kwamba tunanunua viuadudu vinavyozalishwa kwenye kiwanda chetu ambacho Serikali na yenyewe ina hisa ili tuweze kupuliza kwenye makazi ya watu, maeneo ya jumuiya, tuweze kuua mazalia umbu na tuwe salama ugonjwa wa malaria ambao unasabishwa na mbu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huo ndiyo utaratibu na mkakati wa Serikali kwenye eneo hili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni Serikali yetu imeonesha uwezo mkubwa sana wa kushughulika na masuala na miradi mikubwa katika hali ya dharura na kwa mafanikio makubwa sana. Mfano mojawapo ikiwa ni miradi mbalimbali iliyoendeshwa kwa hizi fedha za UVIKO na hata linaloendelea sasa hivi la kudhibiti madhara ya bei za mafuta kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu lipo tatizo la muda mrefu la uchakavu wa Shule za Msingi ambazo nyingine zilijengwa wakati wa ukoloni nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba je, Serikali haioni kwamba kwa uwezo huu ulionao kwamba sasa ichukulie suala la uchakavu wa hizi shule za msingi kwamba ni jambo la dharura ili shule hizi zikarabatiwe na elimu yetu iendelee kuwa bora.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tadayo Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna shule za muda mrefu sana na wala siyo shule za msingi tu, ziko shule za sekondari, vyuo vya elimu ya kati hata vyuo vikuu. Nakiri kwamba tunahitaji mkakati wa Serikali wa dharura lakini utaratibu wa kukarabati shule hizi kongwe tayari ulishaanza kwa kupeleka fedha kwenye shule zetu ili kukarabati miundombinu yake irudi katika hali inayoweza kutumika kisasa zaidi. Tulianza zoezi hilo mwaka 2013 kwa kupeleka milioni 50, kila shule ili kukarabati na kuongeza fedha, tukaongeza uwezo zaidi wa Serikalini, tumeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati shule za msingi kongwe, sekondari kongwe, FDC kongwe lakini pia hata VETA ambazo zilianza kujengwa muda mrefu na vyuo vikuu vyote vilivyo vikongwe nchini.
Mheshimiwa Spika, zoezi hili ni endelevu ndani ya Serikali ya Serikali. Kwa hiyo, udharura ni pale ambapo labda kutatokea madhara makubwa moja kati ya miundombinu hiyo tunaweza tukapeleka fedha, lakini kila mwaka tunatenga fedha. Hata Wizara ya Elimu jana wameshatoa bajeti zao moja kati ya fedha ambayo jana tumeitisha hapa ni ya kukarabati shule zote kongwe na taasisi zote za elimu ili miundombinu hii iweze kutumika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Waheshimiwa Wabunge wote ambao pia kwenye majimbo yenu kuna hizo shule hizo kongwe na Watanzania naona pia kuna vijana wetu wa shule, shule zotte na taasisi zote zitakarabatiwa. Waheshimiwa Wabunge mmeshapitisha bajeti zetu hapa na naomba muendelee kupitisha bajeti za Wizara zote ili Serikali ifanye kazi yake ikiwemo na ukarabati wa shule hizo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwa na changamoto nyingi sana katika Taifa letu za ucheleweshaji wa kesi Mahakamani jambo ambalo linasababisha huduma ya utoaji wa hukumu kuchelewa. Je, Serikali ina mpango gani katika kuongeza huduma za mobile za Mahakama ili kuisaidia Serikali au nchi kwa ujumla kupata huduma za Mahakama kwa muda mfupi kwa maana ya kwamba kesi ziweze kumalizika kwa kupitia Mahakama za mobile. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba muhimili wa Mahakama umetafuta njia nzuri ya kupunguza kesi au kuondoa mlundikano wa kesi kwenye kesi zilizopo nchini. Idadi ya makosa imekuwa kubwa na sasa Mahakama zetu hazitoshi kwa sababu nyingine, matatizo mengine yanatoka kwenye vijiji ambako pia hakuna huduma ya Mahakama.
Nini muhimili wa Mahakama umefanya ni kutafuta njia nyingine rahisi zaidi ya magari yanayobeba banda litakalotoa huduma za Mahakama (mobile court) kama ambavyo Mbunge amesema.
Mheshimiwa Spika, huduma hii tumeshaanza kuona kuwa unatija, kwamba magari yale yanasafiri mpaka vijiji ambako wananchi wenye uhitaji wapo ili utoaji haki ufanyike hukohuko vijijini bila wananchi hao kulipa gharama kubwa ya nauli kwenda kufuata Mahakama ya mwanzo ambazo ziko nyingi kwenye ngazi ya Tarafa au Mahakama ya Wilaya pekee. Kwa hiyo Muhimuli wa Mahakama kupitia mpango wake na Wizara ya Katiba na Sheria itakapokuja hapa itatueleza, kuongeza mobile court, au magari haya mengi yasambazwe kwenye maeneo yetu yote kwenye Wilaya ili yaweze kuwafuata wananchi kuweza kupunguza mlundikano wa kesi uliopo kwa lengo lile lile la kutoa haki kwa wale wote wanaohitaji matatizo yao kusikilizwa na Mahakama zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nichukue wazo hilo na Waziri wa Katiba na Sheria yuko hapa alichukue hilo walifanyie mkakati naamini kwenye bajeti yao lipo niwasihi Waheshimiwa Wabunge tupitishe bajeti ya Katiba na Sheria ili sasa waweze kununua mobile court nyingi ziende kwenye vijiji vyetu na maeneo yetu na wananchi waweze kupata huduma, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MWANTUM M. ZODO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali kwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwa na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, ukatili na hata wakati mwingine mauaji ya wanawake na watoto yanayoendelea nchini. Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hii? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zodo Mbunge wa Mkoa wa Tanga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, yako matukio yameripotiwa kwenye vituo vyetu vya usalama ya unyanyasaji na ukatili wa Watoto na wanawake. Siwezi kusema kwamba yanaendelea lakini tunajitahidi kudhibiti na njia ya kuendelea kudhibiti matatizo haya Serikali imeimarisha utoaji elimu wa wale wote wanaofikwa na madhira haya kwa vyombo vya sheria. Hata hivyo, tumewakaribishia huduma hiyo kwa kufungua vituo vya kwenda kupeleka malalamiko kila palipo kituo cha polisi ili iwe rahisi kwa wananchi kwenda kuripoti kwenye maeneo hayo. Kwa lugha nyingine tunasema tumefungua madawati.
Mheshimiwa Spika, pia tumeanzisha madawati hayo kwenye taasisi za elimu, shule za msingi, shule za sekondari vyuo vya kati na vyuo vikuu na tunao waalimu maalum wanashughulikia malalamiko haya ya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili kwa Watoto na wanawake pindi yanapotokea. Kwa hiyo, eneo hilo pia nalo tunapata msaada huo ili kukabiliana na tatizo hili, huku tukiwa tunaendelea na elimu kwa jamii yetu pale ambapo jambo hili linajitokeza basi jamii ituambie ni nani huyo anasababisha jambo hili na hatua kali zinaendelea kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, nataka nitumie nafasi hii kupitia swali hili la Mheshimiwa Zodo kutoa wito kwa jamii yetu pale ambako tatizo hili la ukatili wa watoto na wanawake linapojitokeza. Hatua kali zichukuliwe kwa kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili kuweza kudhibiti hali hii. Hata hivyo kwa kuwa nimeeleza kwamba tunaendelea kutoa elimu kwa jamii basi ni muhimu sana pia jamii zetu zikaona umuhimu wa kukaa na watoto na wakawake ambao ndio binadamu wenzetu kuwa tunawatendea haki katika kila jambo ambalo tunatenda nao ili na wao waweze kuweka mipango yao ya maendeleo binafsi na jamii zao. Hili linaweza likasaidia sana kuifanya jamii yetu ya watanzania kuishi kama ndugu, kuishi wamoja lakini kwa Watoto kuwalea na hatimaye waje kuchukua fursa ya kuleta maendeleo kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inaendelea na utaratibu huo wa kufatilia madawati haya kuona matukio yanayojitokeza ili tuweze kupunguza kwa kiasi kikubwa ikiwezekana tukomeshe kabisa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Waziri Mkuu. Maji ni nyenzo muhimu sana katika Maisha ya binadamu na hata katika mahitaji makuu matatu ya binadamu maji ni sehemu mojawapo. Na katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasema kwamba kufika mwaka 2025 lazima maji yawe yamefika kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hatukaribii kufikia hayo ingawa Serikali imepeleka fedha nyingi sana vijijini lakini ukiangalia maji yanafika kwenye vituo kuna umbali mkubwa sana kati ya kituo kimoja na kituo kingine. Sasa Serikali kwa nini isishushe bei za kuunganisha maji vijijini kwa wananchi wote nchi nzima iwe kama umeme wa REA ili wananchi maskini wale wafaidike na huduma hii ya maji ambayo wanatembea umbali mrefu nchi nzima kuangalia hivyo? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kuujibu swali la Mheshimiwa Mwenisongole Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, sera yetu ya maji nchini iko wazi kwamba matumizi ya maji yatakuwa yanafika mpaka vijijini tena kwa wingi na gharama nafuu. Mheshimiwa Mbunge anahitaji kujua gharama za kuvuta maji kwenye maeneo yetu. Sera yetu inaeleza kwamba wananchi watachangia kwakulipia miundombinu ya kuvuta maji kwenda mahali alipo ikiwa na umbali usiozidi mita 60 ni umbali mfupi ambao gharama yake si kubwa. Lakini pale ambapo umbali ni zaidi ya mita 60 gharama hizo zitaingiwa na Serikali. Na ndio kwa sababu Serikali sasa inatoa fedha nyingi kutoka mahali maji yanatoka kwenda kwenye eneo la makazi ya wananchi. Pale ambako mwananchi anahitaji kupeleka maji kwenye nyumba yake basi zile gharama za kutoka kwenye nyumba yake mpaka pale kwenye chanzo kama iko chini ya mita 60 ataendelea kugharamia yeye mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo Waheshimiwa Wabunge na Watanzania mnajua kwamba Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alipokuwa Makamu wa Rais Serikali ya Awamu ya Tano moja kati ya majukumu ambayo viongozi wetu wakuu, Rais na Makamu wa Rais waligawana, Mheshimiwa Makamu wa Rais ndio alipewa jukumu la kusimamia usambazaji wa maji nchini. Na akauanzishia kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani na aliweza kusimamia kupunguza gharama za maji katika upatikanaji wa gharama za maji kwa wananchi na ndio kazi ambayo sasa inafanyika kwamba kiwango unacholipia kwenye maji ni kuchangia tu gharama ambazo kamati ya maji iliyoundwa na wananchi kwenye kijiji husika ndizo zinazotumika pindi miundombinu iliyowekwa inapoharibika ili wananchi wenyewe waweze kukarabati miundombinu hiyo muweze kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumetumia utaratibu huo ambao ni rahisi kwa kuchangia maji kwa kiwango kidogo pia kuvuta maji kupeleka nyumbani kwako kwa umbali usiozidi mita 60 utaugharamia mwenyewe lakini ikiwa zaidi ya mita 60 Serikali inawajibika kuleta maji mpaka mahali ulipo. Kwa utaratibu huu sasa tunaanza kuona huduma za maji zinasambaa maeneo yote na malengo yetu kila Kijiji kipate huduma za maji kama sio kwa mtandao wa bomba unaofata makazi ya watu basi tutajenga vilura kwenye maeneo ambayo wananchi waweze kupafikia kwa ukaribu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea kuhakiki bei zetu na kwa kuwa Wizara ya Maji inaanza leo kuwasilisha bajeti yake tutapata maelezo mazuri zaidi kwenye eneo hili na Waheshimiwa wabunge mtapata fursa ya kuchangia na Serikali tunaendelea kupokea maoni yenu, ushauri wenu namna mtakavyoboresha utoaji wa huduma za maji nchini, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa nyakati mbalimbali wakati ugonjwa wa Covid 19 umeshamiri wananchi wengi waliokuwa wanaishi nje ya nchi walirejea nchini, ikiwemo wanafunzi waliokuwa wanaendelea na masomo kwenye kada mbalimbali.
Pia hivi karibuni wakati vita ya Ukraine na Urusi inaendelea hali kadhalika wananchi wakiwemo wanafunzi wamerejea nchini. Wanafunzi ambao walikuwa wanaendelea na masomo kwenye kada mbalimbali na kwenye vyuo mbalimbali nchini sasa hivi wako hapa nchini wengine wamesitisha masomo kabisa, wengine wanasoma kwa njia ya mtandao kwa mazingira magumu sana. Ni nini kauli ya Serikali kwa wanafunzi hawa ambao wamekosa masomo? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Mbunge Hai Mkoani Kilimanjaro kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna vijana wa kitanzania wanasoma kwenye vyuo mbalimbali nje ya nchi na ugonjwa huu wa Covid 19 ulipoingia nchi kadhaa ziliamua kuwarudisha vijana kwenye nchi zao wakiwemo vijana wetu wa kitanzania ambao walikuwa wanasoma huko na wamerudi. Na si tu Covid 19 hata hii vita inayoendelea nchini Urusi na Ukraine tunaona vijana wetu wengi wamerudi hapa nchini. Nini kinafanyika hapa ndani ya nchi kuokoa miaka waliyoipoteza kwenye masomo?
Mheshimiwa Spika, tulitoa tangazo kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu kwamba vijana wote wa kitanzania waliorudi kutoka nje waliokuwa wanasoma nje kuja nchini waripoti Wizara ya Elimu ambako pia Taasisi ya TCU inayoshughulikia vyuo vya elimu ya juu kwa sababu wengi wanasoma vyuo vya elimu ya juu waende wakieleza elimu yao walikuwa wanasoma course gani, wamefikia kipindi gani halafu tuone ufaulu wake huo kutoka hapo alipo mpaka alipoishia ili sasa Taasisi yetu ya TCU iweze kuchukua zile alama. Wanavyo vigezo vyao ambavyo vinatumika katika kurasimisha taaluma waliokuwa wanasoma nje na taaluma iliyoko ndani ili waweze kuendelea na vyuo vya ndani, utaratibu huo ndio tumeutumia.
Mheshimiwa Spika, sasa kama wako vijana ambao wamerudi utaratibu huu haujawapitia kuna mambo mawili. Moja atakuwa hajaenda kuripoti ili apate huduma hiyo; lakini mbili course anayoisoma kama inafanana na course ya Tanzania, course zetu zina vigezo vya kimataifa. Anaweza kuwa alikuwa anasoma chou ambacho hakifikii viwango vya vyuo tulivyonavyo nchini hawa watakuwa bado hawajapata nafasi hiyo mpaka pale ambapo watapewa ushauri wa course gani sasa anaweza kuianza hapa nchini ili aweze kuisoma.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna hayo mambo mawili ambayo Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua ya kwa nini vijana wengine ambao hawajarasimishwa kuingia kwenye vyuo mpaka leo wako nje ya vyuo.
Kwa hiyo, nitoe wito kwa watanzania wale ambao wameenda kusoma nje wamerudi nchini kwa matukio yote mawili covid 19 na vita ya Ukraine na Urusi waripoti TCU wapeleke taarifa za course aliyokuwa anazisoma chuo ili TCU ifanye ulinganisho wa course aliyokuwa anasoma na course zilizopo nchini kwenye vyuo vyetu, baada ya hapo atapata maelekezo ili kuondoa tatizo hilo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba niseme kwa niaba ya wananchi wa Tarime Vijijini kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ni Waziri Mkuu wa viwango; hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nataka nikwambie kwamba hotuba uliyotoa hapa Waheshimiwa Mawaziri na viongozi wakiifanyia kazi Wabunge hawa watafurahi sana na wananchi wetu watafurahi, ume-cover karibu kila eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu; pamoja na hotuba nzuri uliyotoa hapa, ninataka uwasaidie wananchi wa Tarime Vijijini, Serengeti, Bunda; ni lini hawa Mawaziri watakwenda kuwasikiliza wananchi wale ili kutoa elimu na kutambua ile GN ya mwaka 1968 ambayo kimsingi ndiyo kilio cha watu wangu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru Mheshimiwa Mbunge kutambua jitihada za Serikali katika kufanya utatuzi wa migogoro iliyopo kwenye Wilaya yake, Jimbo lake kule Traime Vijijini, Mkoani Mara, kwamba hatua iliyofikiwa sasa kwenye eneo lile ni kukutana kwa Mawaziri na wananchi ili kuwaelimisha, hayo ndiyo mahitaji makubwa ya wananchi wale, ili waweze kutambua kikamilifu mipaka iko wapi na wananchi wapate nafasi pia ya kuweza kuwasilisha hoja zao, mahitaji yao ili Serikali ifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nilishawaagiza waende haraka, na ilikuwa ndani ya mwezi huu, lakini kutokana na majukumu tuliyonayo ndani ya Serikali na Mawaziri hawa kuwajibika kikamilifu, nataka nikuahidi, kuanzia tarehe 02 Mei baada ya sherehe za Mei Mosi ambazo wao pia watashiriki kule Morogoro, wataanza safari kwenda Tarime. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nina uhakika kwamba kati ya tarehe 03 na 04 watakuwa Tarime. Na tukualike wewe, tuwaalike Wabunge wa Bunda wanaoguswa na eneo lile la mipaka pamoja na Serengeti kushiriki vikao hivyo kwa sababu hoja zitakazotolewa na Mawaziri zitakuwa zinagusa kwenye maeneo hayo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna mifugo, mali nyingi za wananchi zilizokamatwa kwa kuingia hifadhini, na umesema kwamba ipo haja ya kuimarisha mahusiano kati ya wahifadhi na wananchi. Kwa nini usitoe kauli hapa Bungeni kuitaka mifugo yote, mali zote za wananchi zilizokamatwa kwa sababu ziliingia kwenye hifadhi ziachiwe ili kufungua ukurasa mpya tuanze moja? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa taarifa nimeitoa hapa leo na kutoa maelekezo kwa vyombo vyote vya Serikali kuchukua hatua hizi. Hatua zote za awali, taratibu, sheria na kanuni ambazo zipo ziendelee kufuatwa ili haki iweze kutendeka kwa haraka sana kama ambavyo nimesisitiza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maelekezo yangu yamebaki, yamekuwa wazi na sahihi. Kwa hiyo, hatua hizo ziharakishwe ili wananchi waweze kutambua haki zao na upande wa Serikali uwajibike kutoa elimu kuanzia sasa na kuendelea. Ahsante.
MHE. GEORGE. R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Sera ya Ushirika ya Vyama vya Msingi ililetwa kwa nia njema ya kumsaidia mkulima wa Kahawa lakini kwa wakulima wa kahawa ya Arabica nchini sera hii imekuwa kama kaburi kwao. Kwa sababu kwenye hivi vyama vya msingi makato ni mengi, wizi na viongozi wengi wa vyama vya ushirika ni wezi na wanawaibia wakulima na imekuwa kama inamdidimiza mkulima.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa ya ku-review hii sera ili kuwaruhusu wanunuzi binafsi nao wapate nafasi kumruhusu mkulima auze kokote anakotaka? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kujibu swali la Mheshimiwa Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, niungane na Watanzania wote kuipongeza klabu yetu ya Dar young Africans. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hakika Dar Young Africans inaendelea kupeperusha vema bendera ya Tanzania na niwapongeze sana kwa matokeo ya jana. Tunawaombea sana kwa mchezo wa marudio kule Afrika Kusini mshinde kwa magoli mengi. Watanzania tuna hamu ya kuona Tanzania ikiingia kwenye mashindano haya kwenye ngazi ya fainali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia niipongeze Klabu ya Simba kwa hatua waliyofikia, tunaamini wamejifunza na wameona kutoka klabu jirani na hatua waliyofikia. Kwa hiyo, msimu ujao tunaamini vilabu vyetu viwili au zaidi vitafanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nirudi kwenye swali la msingi linalohusu ushirika. Ni kweli kwamba ushirika una malengo mazuri sana kwa wakulima, si tu kwa wakulima bali kwenye vikundi vilivyoamua kukaa pamoja. Ushirika kwa mazao yetu nchini unatazamiwa na unatarajiwa kuwakusanya wakulima, mazao hayo pamoja ili kuwaongezea nguvu ya kupata maelekezo bora ya namna ya kulilima zao lenyewe lakini pia namna ya uhifadhi, elimu ya jumla ya zao hili lakini pia kuwapa nguvu ya pamoja ya kutafuta masoko.
Mheshimiwa Spika, tunakiri kwamba tunazo changamoto kwenye ushirika kutokana na baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza ushirika kufanya mambo tofauti na misingi ya ushirika ulivyo. Kwa bahati nzuri siku tatu zilizopita Mheshimiwa Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo, alitumia muda mrefu sana kueleza faida na umuhimu wa ushirika na kwamba ushirika hauepukiki katika kuleta maendeleo ya mkulima na mazao haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja kati ya mambo makubwa ambayo yameleta udhaifu kwenye ushirika ni pale viongozi wanapoona kwamba hiyo ni fursa ya kupata kipato kupitia uongozi wao kwenye ushirika. Hiyo ni kasoro na tutaendelea kuisimamia. Tumeshuhudia viongozi wasiokuwa waadilifu kuweka makato mengi sana kwenye ushirika na kupunguza mapato ya mkulima.
Mheshimiwa Spika, tumeyaona hayo kwenye zao la korosho ambako kulikuwa na makato zaidi ya 25 tumeyapunguza na yakabaki matano na inawezekana na ndio yanayoendelea. Kwenye zao la kahawa lenyewe kulikuwa na makato 47 tumeyapuinguza tumefika makato matano mpaka sita yale ya msingi tu na kumwezesha mkulima kupata fedha nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushirika huu pamoja na changamoto hizo ambazo Serikali tunaendelea kuzifuatilia na kuzitatua imeleta pia mafanikio ya kupanda kwa bei ya mazao kwa mfano zao lenyewe la kahawa. Nitoe mfano wa mkoani Kagera ambako zao hili wakulima wake wengi walikuwa wanaamua kulipeleka nchini Uganda kwa gharama kubwa tu kwa sababu tu ya kero walizoziona. Baada ya Serikali kuingilia kati na kuzitatua changamoto hizi leo wanauza kutoka shilingi 1,200 ya awali tumeenda mpaka shilingi 1,800 mpaka shilingi 2,000 kwa sasa na kupitia usimamizi wa ushirika.
Mheshimiwa Spika, hii ina maana ya kwamba ushirika unaweza kuongeza nguvu ya wakuilima kupata soko zuri badala ya kuruhusu mnunuzi mmoja mmoja kwenda kwa mkulima nyumbani kwake na kumshawishi kununua kwa bei ambayo anaona yeye inafaa, wakati mwingine anauza kwa bei ndogo sana kuliko hata ile iliyokuwa inauzwa. Hata hivyo, tunaendelea kuangalia mifumo mizuri zaidi ya kuuza mazao yetu chini ya ushirika. Ushirika unaweza ukatoa kibali kwa watu waliolima kahawa nyingi kama soko linakuwa lina mwelekeo mzuri tunaweza kuruhusu.
Mheshimiwa Spika, nataka niwaahidi na nimwahidi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge ambao pia tunalima mazao yale makubwa yenye ushirika, kwamba tunaendelea kufanya mapitio, tunaendelea kusimamia kikamilifu ushirika ili ulete manufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha majibu ya swali hilo.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumeona Serikali imeonesha nia njema ya kuboresha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ambayo inatokana na halmashauri kwa kufanya maboresho ambayo yatafanya sasa mikopo hii itolewe kwa tija.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, mikopo hii inatolewa katika makundi ya wananwake, vijana na makundi ya watu wenye ulemavu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, Vijana inapofika miaka 35, vijana wa kike wana–qualify kuendelea na mikopo hiyo kwa sababu wanakuwa ni wananwake lakini vijana wa kiume mikopo hiyo husitishwa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika maboresho haya mazuri yanayofanyika sasa hivi, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuboresha eneo hilo kuingiza kundi la wanaume ambao kimsingi ni wapambanaji wa kiuchumi ili sasa makundi hayo yote manne, wanaume, wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waweze kupata mikopo hii waweze kuinua uchumi wao? Mheshimiwa Waziri mkuu nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo, Mbunge wa Nkenge kule Misenyi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunayo mifuko ya mikopo ikiwemo na huu wa asilimia 10 uliopo chini ya halmashauri. Mifuko hii imetoa fursa ya wale wanaohusika wanaoweza kuingia kwenye masharti ya mfuko huo kupata mikopo. Mkopo wa asilimia 10 unaosimamiwa na halmashauri kupitia mapato ya ndani umeainisha na kuwalenga zaidi wanawake, vijana na walemavu. Sawa, wanawake, vijana na walemavu haijatamka wanaume lakini kwenye category ya vijana tuna wanaume pale lakini ni vijana. Hata hivyo, haikuwabagua wanaume kwa sababu sio mfuko pekee unatoa mikopo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, tuna mifuko mingi ambayo pia inatoa mikopo kwa wote. Hata hivyo Serikali inafanya jitihada za kutoa fursa kwa yeyote yule awe mwanamke, mwanaume, kujana lakini pia wenye mahitaji maalum kupitia taasisi za fedha.
Mheshimiwa Spika, tuna NMB, CRDB, NBC, AZANIA na mabenki mengine yote ikiwemo Benki ya Kilimo ina fursa ya kwenda kukopa. Kwa hiyo, tunapoona eneo hili huna nafasi nalo nenda kwenye chanzo kingine. Nataka nifike Misenyi nione unaposema unaona vijana wanapewa wanawake tu na wavulana hawapewi sasa nataka tuone ni nini kinachotekelezwa kule Misenyi kwa sababu sisi tunaposema vijana ni wale wa kike na wa kiume wote wakapate mikopo. Kwa hiyo, naona fursa hii tunayo.
Mheshimiwa Spika, kwanza nataka niagize kwenye halmashauri, nirudie agizo langu la kwamba mapato ya kuanzia Aprili, Mei na Juni robo ya mwisho wa mwaka wa fedha, mapato haya yasikopeshwe kwanza tunataka kuyawekea utaratibu mzuri ambao pia unaondoa dosari kama hizo ambazo zinaonekana na zimejitokeza kwenye halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, tutatoa kauli tukiwa katika kipindi hiki hiki cha Bunge kwa mapato haya ya mwezi nne, wa tano na wa Sita ili tupate mfu,mo mzuri zaidi. Kama kuna ushauri tunaupokea, je, fedha hizo tutumie utaratibu upi katika kukopesha na ziende kwa maeneo yapi yanayoweza kufikiwa kwa haraka zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba tunaendelea kupanua wigo wa maeneo ya kupata mitaji kwa makundi yetu mbalimbali wanaume kwa wanawake, wazee, vijana ili waweze kusimamia miradi yao na eneo hilo liwe kama sehemu ya kupata mitaji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutumia gesi asilia. Kwa sasa takwimu zinaonesha zaidi ya magari 2000 yameanza kutumia gesi hiyo.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kusambaza huduma hii nchi nzima ili wananchi waweze kufaidika na gesi yetu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge Mkoa wa Iringa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunayo gesi asilia nchini na ni kweli tumeanza kuitumia kwenye maeneo mbalimbali. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema tunatumia kwenye magari lakini gesi hii tunaipeleka viwandani na tunao mpango wa kupeleka gesi hii majumbani.
Mheshimiwa Spika, wizara yetu ya Nisjhati imeweka utaratibu mzuri wa kupanua wigo wa matumizi ya gesi hii. Sasa hivi tunakamilisha ujenzi wa kituo cha kukusanyia gesi hii kutoka kule Mtwara - Songosongo pale Jijini Dar es Salaam ili sasa tuweke utaratibu mzuri wa kusambaza gesi hiyo iende kwa matumizi hayo tuliyoyasema.
Mheshimiwa Spika, pia tumeshirikisha sekta binafsi baada ya kuona uwezo wetu Serikali peke yetu hatutamudu kuifikisha gesi hii kwa wananchi. Pamoja na uwezo tulio nao tukiunganisha nguvu na sekta binafsi tunaamini tutawafikia kwenye matumizi haya. Iwe ni kupeleka viwandani, majumbani hata kwenye matumizi mengineyo ikiwemo na hayo magari.
Mheshimiwa Spika, tayari zabuni zimekwisha tangazwa na watu wengi wameomba. Sasa hivi wako wachache ambao wameruhusiwa kutekeleza mfumo huo na wengine mchakato unaendelea na bado tumefungua fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika mchakato wa usambazaji wa gesi.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu tumeigawa kwenye zone ambazo tutalaza mabomba kuelekea huko. Tutakwenda na bomba la kwenda Kaskazini kwa mikoa ya Kaskazini, tutakuwa na bomba linalopita Kanda ya Kati mpaka Magharibi ili kufikia mikoa ya hapa kati na tutaweka bomba kule kule Kusini ambako inatoka gesi hii kwa ajili ya mikoa ya Kusini. Lengo ni kuifikia kwa ukaribu na kwa haraka, mikoa, wilaya na kama uwezo utakuwa mzuri na sekta binafsi ikiingia ikiwekeza zaidi tunataka tufike vijijini ili wananchi walioko vijijini nao wanufaike na hii gesi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imejipanga vizuri kwenye eneo hili na ninaamini kupitia bajeti hii Wizara ya Nishati itakapokuja hapa itatoa ufafanuzi zaidi kwenye eneo hili. Pia nimwagize Mheshimiwa Waziri, sasa moja kati ya maelezo ambayo tutahitaji kwenye Bunge hili iwe ni namna ambavyo gesi itawafikia watanzania kwenye maeneo yao. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa ya baadhi ya balozi zimetangaza kwamba zitafunga ofisi zake hapa Tanzania ikiwemo Balozi ya Denmark na tumepata wasiwasi taarifa hizi zimefika mbali zaidi kwamba hakuna mahusiano mazuri baina ya Tanzania na balozi hizo. Ni ipi kauli ya Serikali juu ya jambo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chakechake, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Tanzania inayo mahusiano na nchi mbalimbali za kibalozi na tumefungua ofisi kwenye nchi hizo. Lakini na nchi rafiki nazo zimekuja kufungua balozi hapa Tanzania na hiyo Denmark ni miongoni mwa nchi ambazo zina ubalozi hapa na sisi pia kwenye nchi zao.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie kwamba Tanzania ina mahusiano mazuri sana na Denmark ya kidiplomasia, tumejikita kwenye siasa lakini pia kiuchumi, tunafanya biashara, tuna wawekezaji pia wako hapa nchini na Watanzania wachache waliowekeza nchini Denmark wanaendelea na shughuli zao. Balozi wa Denmark aliyepo nchini Tanzania ameendelea kufanya kazi yake na hana matatizo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana wiki mbili zilizopita tumekuwa tukifanya mawasiliano na Waziri Mkuu wa Denmark juu ya maboresho ya mahusiano haya. Ni kweli Dernmark imebadilisha sera zao, sera za nchi na nchi, kwamba wanakusudia kupunguza baadhi ya ofisi kwenye Bara la Afrika kwa lengo la kufikia malengo ya sera yao. Sera yao wanasema wanajikita zaidi kwenye nchi ambazo hazina usalama, nchi ambazo zina tatizo la kiusalama; Tanzania ni nchi salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya pia tulipata nafasi ya kuzungumza na Mheshimiwa Balozi wa Denmark hapa nchini, alieleza haya na sisi tuliendelea kuonesha faida inayopatikana kwa nchi zote mbili kwa mahusiano haya na wanakusudia kufanya hivyo mwaka 2024, bado wako kwenye mchakato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, kupitia viongozi wakuu yako mazungumzo yanaendelea kubadilisha mwelekeo huo ili waendelee kubaki na pawe na ofisi nchini Tanzania na sisi tuwe na ofisi Denmark ili tuendelee kuimarisha mahusiano yetu kwa ukaribu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunataka tuone shughuli zetu zote ambazo ziko kwenye makubaliano yetu zinaendelea kama zilivyo. Kwa kuwa mazungumzo yanaendelea basi tuna matumaini kwamba Denmark watatusikiliza Tanzania na watabaki nchini na sisi tuendelee kushirikiana nao na tuendelee kunufaika na yale yote yanayopatikana kupitia shirika lao la maendeleo linaitwa DANIDA.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba mpokee hilo na kwamba tuhakikshe kwamba mazungumzo yanaendelea ili kufikia hatua nzuri, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kumekuwa na malalamiko makubwa sana hapa nchini kwa ndugu zetu wafugaji waliotaifishiwa na kuuziwa ng’ombe wao katika hifadhi zetu, na wakaenda Mahakamani wameshinda kesi na Mahakama ikaamuru Serikali iwarejeshee mifugo yao hawa wananchi, sasa Serikali imekaa kimya. Nini kauli ya Serikali juu ya suala hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Cherehani Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, natambua kuwepo kwa migogoro mingi kati ya wafugaji na wakulima, wafugaji na maeneo ya hifadhi. Wiki moja iliyopita siku ya Alhamisi nilikuja hapa mbele yako kutoa ufafanuzi wa kero hii ambayo inagusa maeneo yote kwa wafugaji, wakulima lakini pia maeneo yetu ya hifadhi, nilitolea kauli hapa, hili ni eneo moja kati ya maeneo ambayo nilitolea kauli. Tunatambua na tunajua kwamba tuna kesi nyingi ambazo wafugaji wameweza kupeleka Serikali Mahakamani au hifadhi imepeleka wafugaji Mahakamani. Kwa kuwa jambo hili ni la kisheria sana na lina sheria zake, pale ambapo imeamriwa ni lazima tutekeleze kwa sababu hakuna ambaye anaweza kupinga amri ya Mahakama.
Mheshimiwa Spika, kama imetokea kuna mahali hukumu imetoka, Mahakama imeamua, halafu hakuna aliyetekeleza jambo hili tunaweza kupata taarifa ni wapi huko ili tuwaambie Serikali watekeleze mara moja kwa sababu ni hukumu na hatuwezi kupinga Mahakama. Lakini pia nitoe wito pale ambapo kuna migogoro ya aina hii Mahakama imetoa maamuzi yake uko utaratibu, kama eneo moja hilo iwe wafugaji au hifadhi hawajaridhika ni kukata rufaa badala ya kupinga moja kwa moja kutotekeleza amri hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo nitoe wito kwenye maeneo yote ambayo yana amri hii lazima tuheshimu mamlaka ya Mahakama na tutekeleze maamuzi ya Mahakama. Kwa kufanya hivyo tutajenga mshikamano zaidi kwenye mihimili yetu hii mitatu ambayo pia inafanyaka kazi kwa kuheshimiana na tunaenda vizuri. Kasoro kama hizo, tukipata mahali kuna tatizo hilo basi Mheshimiwa Mbunge atujulishe ili tuchukue hatu ili tuweze kuhakikisha kwamba kila mmoja anapata haki yake kupitia chombo kinachosimamia haki, ambayo ni Mahakama.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuumuliza swali Waziri Mkuu. Kila ifikapo tarehe 15 Mei ni Siku ya Maadhimisho ya Familia Duniani. Kwa sasa jamii inapita katika wakati mgumu sana kutokana na mmonyoko wa maadili na ukiukwaji wa haki za wanawake na watoto.
Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuitumia siku hii kama sehemu ya kuielimisha jamii na kuhamasisha umuhimu wa malezi bora pamoja na maadili ili kukabiliana na changamoto hiyo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asharose Mattembe, Mbunge wa Mkoa wa Singida kama ifuatanyo: -
Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo na changamoto ya ukiukwaji wa maadili kwenye maeneo mengi kwa watoto wadogo, wanawake wakati mwingine hata wanaume nao wanaonewa; hayao yote ni mmomonyoko wa maadili na Serikali tuko mstari wa mbele kukemea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, dunia iliamua kuwa na siku moja maalumu ya kuelimisha umma juu ya kila mmoja kuhakikisha kwamba tunapiga vita mmomonyoko wa maadili lakini pia ukatili wa kijinsia na watoto vilevile, na sisi Tanzania tumejiunga kwenye siku hiyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge anataka kujua Serikali tumejipangaje? Na sisi pia tunasheherekea siku hiyo, siku hiyo pia tunakutana, siku hiyo pia tunatoa elimu kwa umma ya namna ya kila mmoja kushiriki katika kuhakikisha kwamba nchi hii mila zetu, desturi zetu utamaduni wetu lakini maadili ya nchi hii yanazingatiwa ili kupata kizazi ambacho kitakuwa endelevu katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwamba tumejipangaje siku hii; tunajua tarehe 15 ni siku tatu nne zijazo, nitoe agizo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya chini ya usimamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia pamoja na TAMISEMI kila mkoa upange mpango thabiti wa kuwaleta pamoja wananchi kwenye siku hiyo ili haya ninayoyasema yaweze kutekelezwa. Kwanza tutoe elimu, tutoe makaripio lakini pia tuonyeshe dira ya nchi ya umuhimu wa kukinga mmomonyoko wa maadili hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo sasa huu ndio mkakati ambao tunaweza kuutumia. Lakini mkakati huo hauishii tarehe 15 tu, hili suala la kukemea kukiukwa kwa maadili na mmomonyoko ni suala endelevu kwa hiyo wakuu wa mikoa nawaagiza tena, wakuu wa wilaya nawaagiza tena. Tunataka ishuke mpaka kule chini maafisa tarafa, watendaji wa kata, vijiji mpaka vitongojini. Ni muhimu sana Taifa hili tulilinde kwa kuwa na maadili mema, tuendeleze utamaduni wetu na mila na desturi zetu ili kujenga kizazi kipya ambacho kitakuwa endelevu kwa nchi hii na wataweza kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, huo ndio mkakati wa Serikali wa namna ya kuitumia vizuri tarehe 15 mwezi wa tano siku hii ya kupinga mmomonyoko wa maadili.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipatia nafasi ili niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Spika, kupitia sera ya Serikali kupitia Wizara ya Habari na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoka kwenye mfumo wa analogia kwenda kwenye mfumo wa kidigitali, kwa kutekeleza sera hiyo Serikali imeamua kwa kuanza kwenye mfumo wa malipo kutaka wananchi kuanza kulipa kwa njia ya kielektroniki lakini mfumo huu umekuwa na changamoto kubwa sana ya makato makubwa lakini pia na mawasiliano pia mtandao kutokuwa sawa. Sasa swali langu;
Je, ni nini mkakati wa Serikali moja kupunguza makato lakini pili kuhakikisha inaboresha mfumo wake ili mfumo uweze kufanya kazi kwa uthabiti ili kuondokana na kadhia kubwa ambayo Watanzania wanaipata kwa namna ambavyo jinsi mtandao huu unavyofanya kazi?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Mbunge Mkoa wa Dodoma kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, uko ukweli kwamba Tanzania kutokana na maendeleo ya tehema na sisi tumeanza kutekeleza mifumo mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi ndani ya Serikali, ikiwemo na ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa kielektroniki.
Mheshimiwa Spika, Tananzia ni moja kati ya nchi ambazo zinaanza siku za hivi karibuni kutekeleza mifumo mbalimbali kielektroniki. Tunapitia katika nyakati kadhaa za mafanikio lakini pia changamoto tunapoelekea kujiimarisha. Ukusanyaji wa mapato yetu kielektroniki ni mfumo ambao unaendelea vizuri sasa pamoja na hizo changamoto. Sasa, ili kukabiliana na changamoto hizi yako maelekezo thabiti yaliyofikiwa na serikali yetu kupitia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, moja ameanzisha Wizara maalumu inayoshughulikia Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa lengo la kufanya mapitio ya kina kwenye mifumo hii na kuimarisha tehama hapa nchini, na kusimamia kampuni zote za taasisi na sekta binafsi ambazo zinajishughulisha na mawasiliano ili kuimarisha mifumo hii ya mawasiliano. Kwa hiyo kuna tozo kuwa kubwa lakini pia kuna mtandao kutofanya kazi vizuri suala la tozo hili ni wale walioamua tozo hiyo kuwepo. Haya tunayafanyia kazi, na tumewasikia Waheshimiwa Wabunge mara kadhaa na wananchi pia kuitaka Serikali ipitie makato mbalimbali au tozo mbalimbali ambazo zinazotozwa kwenye maeneo mbalimbali, hilo linafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Spika, suala la mtandano hili Mheshimiwa Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari atakuja mbele yetu Waheshimiwa Wabunge kuja kuwasilisha mpango
wa bajeti, mpango wa kazi ambao tutaufanya mwaka ujao na kuomba ridhaa ya fedha. Moja kati ya mambo ambayo nitamwagiza hapa ni kuja kueleza nini wizara inafanya katika kuimarisha mifumo ya mawasiliano na hasa hii mitandao kuwa imara bila kukatika. Kwa sababu hata pia upande wa Serikali tunapata hasara sana lakini baadhi ya watu ambao wanapata vitendea kazi vya kielektroniki kwa kuzima na kusingizia kwamba mtandao haupo na kujipatia mapato, pia Serikali tunapata hasara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunataka tuimarishe eneo hili ili tuwe na mfumo mzuri wa mtandao kupitia taasisi zetu zinazofanya kazi ya kusambaza mitandao lakini pia Serikali inaimarisha tozo mbalimbali ili kuleta unafuu kwa Watanzani.
Mheshimiwa Spika, malengo yetu tunapokwenda kwenya maendeleo ya tehama tuwe na tehama ambayo inaweza kumhakikishia mtanzania kuitumia katika shughuli zake binafsi na hiyo ndio mwelekeo wetu.
Mheshimiwa Spika, hayo ndio maelezo ya eneo hili ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi pia na mimi nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni sera ya nchi yetu kwamba watu wanapotimiza umri wa miaka 18 wana-qualify kupata Vitambulisho vya Taifa. Tumeona hata kwenye Sensa iliyopita idadi ya Watanzania imeongezeka.
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba kuna watu kipindi kile wanaaandikisha kwa mara ya kwanza wame-qualify na umri umeongezeka na hawajaandikishwa. Pia baadhi ya maeneo ya pembezoni mwa nchi hii wananchi walio wengi hawakupata fursa ya kuandikishwa kwenye ile round ya kwanza. Kwa hiyo wengi wamekaa bila vitambulisho ilhali vitambulisho ni requirement kubwa ambayo inatumika katika kila eneo sasa hivi ambalo wananchi wamekuwa wanahusushwa.
Je, hamuoni kwamba ipo haja ya Serikali kuanza mchakato huu upya kama tulivyofanya kipindi kile cha mwanzo ili Watanzania wengi waliofikia fursa hii iweze kuwapata na hatimaye wapate fursa kama Watanzania wanzao walio na vitambulisho wanavyoendelea kunufaika?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chiwelesa Mbunge wa Biharamulo kama ifatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inaendelea na zoezi la utoaji wa vitambulisho kupitia taasisi yetu ya NIDA. Sote tunafahamu, kwamba tulipoanza kutoa vitambulisho hivi tulipitia hatua kadhaa, na hatua hizi zimekuwa na mafanikio lakini pia changamoto. Awali tulikuwa na idadi ndogo sana ya watumishi kuwafikia wananchi kwa ajili ya kutoa vitambulisho kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kumwezesha Mtanzania kupata vitambulisho mpaka akiwa kijijini kwake. Sasa tumeongeza idadi ya watumishi na nashukuru Mheshimiwa Mbunge ameipongeza Serikali kwa mafanikio kuwa idadi ya wanaopata vitambulisho imeongezeka Lakini bado kuna maeneo kadhaa.
Mheshimiwa Spika, mimi nimefanya ziara biharamulo na Mkoa wa Kagera kwa ujumla nimepita pia Kigoma lakini pia kule Mkoani Arusha maeneo ya Longido kumekuwa na
changamoto ya watu wetu kadhaa kutopata vitambulisho kwa haraka. Nirudie tena. hapa niliwahi kupata swali hili na nikalijibu; nirudie tena kueleza kwamba inawezekana kabisa wale ambao bado hawajafikiwa na hasa wa mikoa ya pembezoni ni kuwepo kwa chngamoto ya mwingiliano na mataifa ya jirani.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu kitambulisho hiki ni cha Taifa, tunapozungumzia kitambulisho cha Taifa tunazungumzia Usalama wa Taifa letu. Tusingependa kitambulisho hiki kila mmoja awe nacho kwa sababu kitambulisho hiki ni kwa ajili ya Watanzania. Sasa pale ambako tunapakana na nchi jirani umakini unaongezeka ikiwemo na idadi ya staff ambao wanaweza kufanya kazi hiyo; na mkakati wetu kukamilisha kwa haraka sana.
Mheshimiwa Spika, Sasa hivi tumeimarisha tumepata mashine mpya. Nilipata nafasi ya kwenda nchini Korea na Mtendaji Mkuu wa NIDA kuzungumza na taasisi ambazo zina- supply machines na tulishapata mashine za kutosha vitambulisho vinatolewa. Kwa hiyo tutawafikia Watanzania katika kipindi kifupi kwa au kuwapa namba kwanza tukichapa vitambulisho au kuwafikia na vitambulisho vyenyewe moja kwa moja, kwa sababu pia Serikali tumerahisisha Watanzania ambao bado wanachelewa kupata vitambulisho basi wapewe namba na hiyo namba itumike kwenye mahitaji yao popote pale.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote ambao kwenye maeneo yao kuna tatizo hili la upatikanaji wa vitambulisho kwa haraka sana kwa wananchi kwamba Serikali tumejipanga vizuri taasisi yetu ya NIDA imejipanga vizuri na sasa kasi inaongezeka kwa sababu tumeongeza watumishi ambao wanawafikia wananchi kwenye vijiji ambao tumewaweka kwenye wilaya zetu zote. Pale ambapo kutakuwa na tatizo kubwa sana tunawaruhusu wakati huu tukiwa hapa Bungeni mje mtupe taarifa ya maendeleo ya utoaji wa vitambulisho kwenye maeneo yenu. Niwahakikishie tena kwamba kitambulisho hiki kitamfikia kila Mtanzania na si vinginevyo; na tushirikiane katika kuhakikisha kwamba kitambulisho hiki wanokipata ni Watanzania tu kwa sababu suala la kitambulisho nirudie tena ni Usalama wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba risala ya Serikali kuhakikisha kwamba inatatua migogoro kati ya wananchi na maeneo yenye hifadhi za Serikali. sasa ningependa kujua nini mkakati wa Serikali kukomesha migogoro hii katika maeneo haya niliyoyataja?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Waitara Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waitara analizungumza hili akijua kwamba tumelifanyia kazi sana pia kwenye eneo lake ambako kuna mgogoro wa wananchi na hifadhi; na tulliunda timu ya mawaziri walienda kwenye eneo lake. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie, kwamba mkakati wa Serikali wa kukomesha haya ni kushirikisha wananchi kwenye maeneo haya yote ambayo yamejitokeza na migogoro hii ili kuwa na mapitio ya pamoja ya mipaka ilipo kila mmoja ajue mpaka upo wapi. Serikali tumeagiza mamlaka hizi za hifahdi kuweka vigingi kama alama inayoonesha pande zote mbili kwamba hapa ndio ukomo wa watu kuingia kwenye upande mwingine; na vigingi hivi navyo tumesema viwe virefu siyo vile vidogodogo kirefu wapake rangi nyeupe kionekane kwa mbali ili kila mmoja apate kuelewa. Sasa jukumu hili tunapolifanya kwa kushirikiana pamoja tunaamini migogoro itapungua kwa sababu kila mmoja atakuwa anajua.
Mheshimiwa Spika, siku tatu/nne zilizopita hili limejitokeza sana kule Tarime ambako kata kadhaa na vijiji kadhaa kulikuwa na mgongano wa kutoeleweka kwa mipaka yake, na hili pia tumeona hata juzi siku mbili zilizopita kwa kutoelewana viongozi wa Serikali za vijiji walijiuzulu. Nafurahi kusikia pia jana viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tarime wameenda kuwatembelea wananchi wamewaelimisha. Nawashukuru sana viongozi wale kwamba wamerudi kwenye nafasi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie wananchi wale ambao wako kwenye migogoro si Tarime lakini maeneo mengine yote, Serikali tunajipanga kufanya mapitio ya maeneo yote ili kuhakikisha kwamba hii migogoro haijirudii, lakini kila mmoja anakuwa na uelewa kwa kushirikisha na viongozi wale ambao wamerudi moja kati ya taarifa ambazo tumezipata ni kwamba wanahitaji kupata taarifa zaidi. Kwa ile Timu ya Mawaziri iliyoenda inakamilisha taarifa yake wataileta kwangu, tutaipitia kwa pamoja, tutashirikisha kwanza ndani ya Serikali, tutakwenda sasa Mkoa Mara, Wilayani Tarime mpaka kwenye vile vijiji. Tutakuwa na mikutano kwenye vile vijiji vya kuendelea kuelimisha zaidi kwa ukaribu na kuwashirikisha ili kila mmoja awe anajua. Sisi ndani ya Serikali tunaamini kwamba vijiji vyote, wananchi wote wanaoishi pembezoni mwa mipaka hii ya hifadhi watakuwa walinzi nambari moja wa kulinda hifadhi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutawajibika kwenda kutoa elimu maeneo yote. Tunajua hata hapa Kondoa kuna Pori la Mkungunero lina mgogoro, Babati, eneo la Tarangire lina mgogoro. Tunaambiwa Bunda pale katikati, katika ya Daraja na Mji wa Bunda pale kuna eneo lina mgororo, Serengeti nako pia kuna mgogoro. Haya maeneo yote tutayapitia eneo moja baada ya moja, tutakutana na wananchi, tutawaelemisha. Tunataka Watanzania tuone umuhimu wa hifadhi, lakini na sisi wahifadhi tuone umuhimu wa raia wanaokaa pembezoni mwa hifadhi. Tukiwa na dhana hii itatusaidia sasa kutunza rasilimali zetu popote zilipo kwa pamoja zaidi, wananchi pamoja na miundombinu tuliyonayo ndani ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa swali hili na huo ndio ufafanuzi wangu. Ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nishati ya mafuta ni nishati ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu, kwanza kwa sababu ni sehemu ya ulinzi na usalama wa nchi, lakini pili pia ni sehemu ambayo inachangia kwa mawanda mapana shughuli zote za kiuchumi katika nchi yetu. Lakini miezi ya hivi karibuni kuanzia Mwezi wa Saba, Mwezi wa Nane na hata Mwezi huu wa Tisa kumekuwa na sintofahamu kwenye eneo hili la sekta ya nishati. Upatikanaji wa mafuta umekuwa ni wa mashaka pia bei zimekuwa zikibadilika bila ya kuwa na mpangilio maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hali ambayo ni ya kushangaza zaidi ni kwamba wiki moja ama mbili kabla ya kutangazwa bei ya mafuta kama utaratibu ulivyo kwamba kila Jumatano ya kwanza ya mwezi mpya bei ya mafuta zinatangazwa, mafuta huwa hayapatikani, bei ikishatangazwa tayari mafuta yanaanza kupatikana.
Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba Taifa linakuwa na mafuta wakati wote, lakini pia kuhakikisha kwamba yanapatikana kwa bei ambayo Watanzania kote nchini wanaweza kuimudu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza ninakiri kwamba tunazo changamoto za upatikanaji wa mafuta nchini, kwa sababu baadhi ya vituo kwenye maeneo mbalimbali vimekuwa vikikosa mafuta na Watanzania wanaohitaji huduma hii maeneo kadhaa tumeona wakiwa wanalalamika kukosekana kwa mafuta.
Mheshimiwa Spika, ziko jitihada kadhaa zinafanywa na Serikali kupitia mifumo yetu ya upatikanaji wa mafuta, Wizara imekuwa ikifanya jitihada pia za kuona upatikanaji wa nishati hii unakuwepo, pia hata Kamati ya Bunge ya Nishati imekaa mara kadhaa na Wizara kuona mwenendo wa upatikanaji wa nishati hii. Nasi tunajua nishati hii ina msaada mkubwa kwenye maeneo mengi na ndiyo inasaidia pia kufanya shughuli za kiuchumi ziweze kwenda.
Mheshimiwa Spika, kufuatia mabadiliko ya Mheshimiwa Rais aliyoyafanya juzi, tumeanza kumwona Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu akifanya vikao kadhaa ndani ya Wizara kukutana na wadau. Sasa kwa kuwa ameshaanza hii kazi, niendelee kumuagiza Naibu Waziri Mkuu kushughulikia hili. Muhimu zaidi nishati yenyewe ipatikane nchini, suala la bei tunajua bei zinabadilika wakati wowote, lakini kwanza nishati ipatikane kwenye vituo vyote na maeneo yote nchini. Pili Watanzania wapate hii huduma na upatikanaji huu ni muhimu kuhusisha pia taasisi zote za mafuta, EWURA na taasisi nyingine zote wale wanunuaji wa mafuta kwa bulk, lakini pia Taasisi ya Ununuaji wa Mafuta tutengeneza kikao kikubwa na Wizara kadhaa zinazohusika, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Uratibu, Ofisi ya Waziri Mkuu mkae pamoja, muone namna ya upatikanaji wa mafuta, suala la bei tutaanza kuliangalia hapo baadae kwa sababu bei zinabadilika kutegemeana na upatikanaji.
Mheshimiwa Spika, pia tupanue wigo wa waagizaji wa mafuta ili tuwe na mafuta mengi nchini kwa usalama wa Taifa letu. Kama hili litafanyika ndani ya wiki moja tutakuwa tumeshapata majibu na tutawapa taarifa Watanzania, lakini tutahakikisha kwamba nishati hii ya mafuta inapatikana na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu atashughulikia hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi hii ya kuuliza swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu kupitia Bunge hili ilitunga sheria nyingi nzuri za kulinda uhifadhi hapa nchini na hasa kuzuia uwindaji haramu kwa ajili ya kukuza utalii, kulinda ikolojia na pia kuongeza Pato la Taifa kupitia mapato yanayotokana na utalii. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu, wanyamapori hawa ambao tumewahifadhi kwa mujibu wa sheria zetu na pia kwa kuheshimu mikataba ya Kimataifa katika eneo hili wamegeuka kuwa janga kwa kuharibu mali za watu, kuvuruga miundombinu na hata kusababisha watu wengi kupoteza maisha.
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba tunapitia upya sheria hizi ambazo tuliziweka kwa ajili ya kulinda uhifadhi ili pia ziwalinde wananchi wetu na hata ikibidi kujitoa kwenye baadhi ya mikataba ya Kimataifa ambayo inatushurutisha kuweka sheria za namna hii ambazo zinawadhuru wananchi wetu na mali zao? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tadayo, Mbunge wa Mwanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kupitia vikao vyetu vya Bunge hapa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakieleza usumbufu ambao wananchi kwenye maeneo yetu wanaupata kwa wanyama waliohifadhiwa kwenye maeneo mbalimbali kwenye misitu yetu kuhamia kwenye makazi ya watu na kusababisha uharibifu wa mali, lakini pia hata maisha ya watu, na tumepata taarifa hizi mara nyingi kwenye miji iliyoko kando kando na hifadhi zetu.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunazo sheria zinazosimamia utekelezaji huu wa kuhakikisha kwamba wanyama wanabaki porini na wananchi wanaendesha maisha yao kwenye maeneo yao rasmi. Pia kumekuwa na wimbi kubwa la ongezeko kubwa la wanyama kwenye misitu yetu na hii ilitokana na jitihada tulizozifanya kupitia sheria zetu hizo hizo za kulinda uwindaji haramu, hili ndiyo limepelekea kuwa na idadi kubwa ya Wanyama.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Wizara ya Maliasili imekuwa ikifanya taratibu kadhaa kukutana na vikao na Wizara ambata zinazohusika kwenye uhifadhi wa mazingira yetu, wa misitu yetu, wanyama wetu na kuona kuwa wanyama wanabaki huko, jitihada kadhaa ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Maaskari ambao pia wameweka vituo kando kando ya maeneo haya ili kuzuia wanyama kuingia, lakini pia tumeona jitihada za kutumia hata ndege kufukuza wanyama kuingiza porini.
Mheshimiwa Spika, tunajua ziko sheria zinalinda haya na Mheshimiwa Mbunge ametaka tubadilishe sheria, lakini muhimu sasa ni Wizara kuhakikisha kuwa maeneo yote yaliyohifadhiwa kwa ajili ya kuweka wanyama yanaendelea kusimamiwa na sheria zake, lakini na taratibu hizo ambazo wamezipanga kwa ajili ya kudhibiti wanyama hawa kuingia kwenye makazi. Hii ni pamoja na kulinda ile buffer ambayo tuliitenga kilometa tano kutoka makazi kuingia kwenye msitu na baadaye tukaruhusu wananchi wafanye shughuli zao za uzalishaji mali, shughuli za maendeleo kwenye hifadhi ile ya kilometa tano, lakini sasa inaonekana pia wanyama wanavuka hifadhi hiyo na kuingia kwenye makazi ya watu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ziko jitihada zimechukuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na wameunda timu ya kufanya ukaguzi wa maeneo haya na kubaini tatizo exactly ni nini hasa kinapelekea wanyama kutoka kule kuingia huku, baada ya kamati ile kukamilisha kazi yao tutapata majibu. Kwa hiyo, niwaahidi kwamba hili ilimradi Wizara imeshaanza kuunda timu ya kwenda kukagua na kugundua tatizo ni nini, baada ya kubaini tatizo, kama tatizo hilo pia litagusa kwenye sheria basi Wizara itatuongoza katika kuleta sheria hapa tufanye mabadiliko ili tuweze kuhifadhi, lakini pia tuhakikishe kwamba wananchi wanaendesha shughuli zao na maisha yao yanaendelea kuimarishwa na kulindwa kama ambavyo tuliweka sheria hizi awali na hatukuwa na tatizo hili hapo mwanzo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilitaka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa ushauri wake kwa Serikali sisi tunauchukua, lakini kwa kuwa timu ilishaanza kazi, tuipe muda timu yetu ikamilishe kazi, halafu ije na mkakati ambao imeuweka na tutaona mkakati huo na jinsi ambavyo utaweza kulinda maisha ya watu, utaweza kulinda pia na hawa wanyamapori wakiwa kwenye maeneo yao. Hii ndiyo njia sahihi ambayo itatusaidia katika kuzuia madhara yaliyojitokeza kwenye makazi ya watu hasa yale makazi yaliyopo karibu na sehemu za hifadhi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, sera yetu ya viwanda hapa nchini imetuwezesha kupata viwanda vingi sana na kuwafanya Watanzania watumie bidhaa nyingi ambazo zinatengenezwa hapa nchini. Hata hivyo, sera hii bado haijapiga hatua kubwa katika viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya wakulima, wafugaji na wavuvi. Tunataka tuone viwanda vya maziwa, vya nyama, tunataka kuona viwanda vya kusindika samaki, dagaa, na viwanda vya kusindika matunda.
Je, ni nini mpango wa Serikali katika kuongeza viwanda vya kusindika au kuongeza thamani ya mazao ya wakulima? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’enda Kilumbe, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imeendelea kutafuta mbinu mbalimbali za kuwawezesha Watanzania wanaojishughulisha kwenye sekta zote zinazozalisha mali na kuongeza uchumi, kuhakikisha kwamba tunaongeza thamani ili mapato yawe makubwa zaidi ikiwemo na sekta ambazo Mheshimiwa Mbunge amezieleza, Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Spika, sekta hizi zimekuwa na manufaa makubwa kwa sababu sekta hizi ndiyo zina uwezekano wa kuwa na viwanda vingi kwa sababu zinakuwa na malighafi nyingi, na kwa hiyo, mkakati wa Serikali kuongeza viwanda zaidi ya viwanda tulivyonavyo, ni kuhakikisha kuwa na hili tumeshalifanya la kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini ili kuweza kuwavutia wawekezaji wanaotaka kujenga viwanda, awe Mtanzania au yeyote kutoka nje ya nchi kwa maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, pia tumefungua wigo wa kuhakikisha kuwa, wawekezaji wote wanapokuja nchini tunawahakikishia uwekezaji wao kuwa salama. Kwa hiyo suala la usalama kwa wawekezaji wetu tumelipa nafasi kubwa ili kuwakaribisha walio wengi sana. Hata hivyo, tumeimarisha miundombinu inayowawezesha wafanyabiashara wanaotaka kujenga viwanda kuendesha viwanda vyao na kupata faida, kama vile barabara na Watanzania mnaona barabara zote nchini zimejengwa na zinaendelea kujengwa, reli lakini pia njia ya anga, tumeshanunua na ndege ya kupeleka mazao nje ya nchi. Hii yote ni kuvutia wawekezaji wetu, hata pia ukanda wa bahari na maziwa tumeongeza meli ili kuwezesha kusafirisha bidhaa zao kwa ajili ya kufuata masoko. Uboreshaji wa mazingira haya ya miundombinu unamuwezesha kumpa uhakika muwekezaji kujenga kiwanda popote nchini ili aweze kutumia malighafi tulizonazo aweze kufanya biashara yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tulikuwa tunaangalia wafanyabiashara wengi, wawekezaji wengi wa viwanda wanakwazwa wapi? Tukagundua kwamba tulikuwa na tozo nyingi sana za uwekezaji. Tumepunguza tozo ili kumuwezesha yeye kufanyabiashara na kupata faida na bado mkakati wetu wa kufanya mapitio ya mara kwa mara ya uwekezaji wetu unafanywa kuvutia wawekezaji hao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nitoe wito tena kwa Watanzania wenye uwezo kujenga viwanda ndani ya nchi, malighafi tunazo kwa sababu Sekta ya Kilimo imepata mabadiliko makubwa, Mifugo nako pia tuna malighafi za kutosha na uvuvi nako pia tumeimarisha uvuvi bora na wa kisasa kwa lengo la kupata malighafi nyingi za kuendesha kwenye viwanda vyetu, lakini pia tunajaribu kuhakikisha kwamba tuna tunasikiliza kero za wawekezaji. Hii inatoa fursa sasa ya Mwekezaji kufanya maamuzi kuja nchini na ndiyo kwa sababu wakati wote tumekuwa na maonyesho ya viwanda, maonyesho ya kilimo ili kuwahakikishia kwamba viwanda vina nafasi vilivyopo na vile ambavyo vinakuja, lakini kwenye maonesho ya mazao kuonesha uwepo wa malighafi hapa nchini. Tunaendelea kufanya haya kwa kutoa wito na kufanya maboresho ya maeneo yote niliyoyatamka ili kukaribisha viwanda zaidi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mpango wetu ambao tunao wa kuwezesha kuongeza viwanda viweze kuleta faida nchini na sisi tunaamini kwamba tukiwa na viwanda kwanza tunatengeneza ajira kwa Watanzania, mbili, tunapata kodi ya hawa wawekezaji wanalipia, tatu tunahakikisha kuwa huduma mbalimbali zinazohitajika viwandani wale majirani wananufaika nazo. Hayo yote ni manufaa ambayo tunayapata na kwa hiyo wito wako uliotokana na swali lako, tutaendelea kuusimamia na kuyasimamia hayo maboresho tunayoyafanya kwa lengo la kuvutia wawekezaji zaidi wa kujenga viwanda hapa nchini. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika ahsante, zao la chikichi ni zao ambalo linaweza kuleta ukombozi mkubwa kwa Taifa katika kujitosheleza katika uzalishaji wa mafuta ya kula nchini, hasa ukizingatia kwamba kujitosheleza katika uzalishaji wa mafuta ya kula nchini kutasaidia kupunguza changamoto ya nakisi ya urari wa malipo inayotokana na uagizaji wa bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi.
Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kunakuwa na programu endelevu ya kukuza zao la chikichi katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya nchi ambapo zao la chikichi linastawi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia zao la mchikichi, ni kweli kwamba Serikali yetu tulishaanza mkakati wa kulirudisha zao hili kwa wakulima kwa kulima kisasa na kupata mbegu bora ili tuongeze uzalishaji ukilinganisha na uzalishaji tuliokuwanao awali ambao ulikuwa unatumia mbegu ambazo hazizalishi na kutoa mafuta mengi, lakini pia hata hamasa ya kilimo cha chikichi ilipungua sana.
Mheshimiwa Spika, tulipokuwa tunaanza kurudisha zao hili liwe kwenye mpango wetu wa kiserikali, inatokana na mahitaji makubwa ya mafuta hapa nchini. Kwa hiyo, mkakati wa kupata mafuta ya kula hapa nchini unatokana na mkakati wa ndani kwa mazao hayo ya chikichi na mazao mengine kama vile alizeti na mazao yote yanayotoa mafuta.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali katika kulipanua zao hili, kwanza tumeimarisha kuwa na kituo cha utafiti, na kule Kigoma tumejenga kituo cha utafiti na ndicho ambacho kimeleta mafanikio makubwa kwa kupata mbegu yetu wenyewe Watanzania kutoka kwenye vituo vyetu. Ndiyo hiyo ambayo tumeipanda na sasa inaendelea vizuri na tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara na tumethibitisha kwamba mbegu yetu inafanya vizuri.
Mheshimiwa Spika, pia utafiti huu unakwenda sambamba na kutafiti udongo unaoweza kumea mchikichi na kupata matunda, siyo tu kwa ukanda wa Ziwa Tanganyika bali na maeneo mengine yote nchini ili tulipande zao hili, liwe pana, na watu wanaoshughulika na kilimo waweze kuingia kwenye sekta hiyo wakiwa na uhakika kwamba wanapanda mchikichi kwenye ardhi ambayo inaweza kuzalisha zaidi. Hiyo ni moja.
Mheshimiwa Spika, pili, tumeanza kampeni ya zao hili na sasa imeanza kuleta matunda. Tunaona pia Mkoa wa Tabora wanalima, tumeona Mikoa ya Pwani, Mkoa wa Pwani wenyewe, Dar es Salaam, ndiyo twende Lindi, Mtwara, tunaona maeneo yote yanayopanda zao la minazi pia tunaambiwa yanaweza kustawisha zao la mchikichi. Huu ni mpango wa kupanua zao hili ili tupate mazao mengi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tunapoanza na mkakati huu kupitia kituo chetu cha utafiti na kuzalisha mbegu nyingi, tumeanza kutoa mbegu inayozalishwa bure kwa wakulima katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja ili kupanua wigo wa watu ambao wanaanzisha kilimo hiki ili waweze kupanda zao hili la mchikichi, huku pia tukiimarisha uwekaji wa viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya wachakataji, kwa sababu baada ya kuwa tumezalisha, tunahitaji sasa tuone matokeo. Hii itasaidia watu wengi kuingia kwenye kilimo na kuwezesha kulima zao hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mkakati huu wa kukuza zao hili tunausimamia toka tulipoanza kulima zao hili Kigoma, na Mkoa wa Kigoma ni watu ambao wameanza mara moja kulilima zao hili na mafanikio tunayaona na tunaona mikoa mingine nao pia wanachukua miche na upandaji tunaona maendeleo yake. Kwa hiyo, tunataka tuhakikishe kwamba zao la chikichi sasa linaanza kuchangia upatikanaji wa mafuta ndani ya nchi na mazao yake mengine na kunufaisha yeyote ambaye anaingia kwenye kilimo cha chikichi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wakulima wa zao la chikichi kwamba Serikali itaendelea kusimamia maendeleo ya zao hili na hapo baadaye litakapokuwa kubwa tunaweza tukaliundia chombo chake cha usimamizi wa zao hili ili pia liweze kusimamiwa kwa ukaribu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, malengo yetu ni kwamba tunatoa fursa kwa Watanzania wanaotaka kulima kilimo wawekeze kwenye mashamba makubwa, wanaotaka kujenga viwanda na tumehusisha pia na taasisi za umma na taasisi binafsi kulima zao hili. Kule Kigoma tuna Magereza, Magereza zote zinalima chikichi, shule za msingi nyingi zimekuwa na mashamba yao, wanalima chikichi, pia Jeshi la Kujenga Taifa, JKT Bulombora nao wana shamba kubwa zaidi ya ekari 4,000 na tunaendelea kuhamasisha taasisi zote zilime zao hili lilete manufaa makubwa.
Mheshimiwa Spika, niwahamasishe Watanzania kulima mchikichi kwa faida yao. Tulime mchikichi kwa ajili ya kupata mafuta mengi, tulime mchikichi kwa sababu na yenyewe inatoa sabuni na bidhaa nyingine ambazo pia zinaleta faida kwenye zao hili.
Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mkakati wa Serikali wa kupanua zao hili. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kumwuliza Waziri Mkuu swali. Kwa kuwa tabia za watu za uharibifu wa mazingira zimesababisha kuwa na nchangamoto za ukosefu wa mvua na hivyo kuhatarisha pengine usalama wa chakula katika Taifa letu na hivyo kusababisha pia mabadiliko ya tabianchi: Je, ni mpango gani wa Serikali sasa kuzuia kabisha shughuli za kibinadamu kwenye milima yote na vilima vyote ili sasa tuwe na mvua za uhakika na hivyo kulifanya Taifa liendelee kuwa imara katika emneo hilo? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la uhifadhi wa mazingira Serikali yetu tumeliwekea nguvu kwa sababu tunataka tulinde mazingira haya kwa misitu yetu, mito na vyanzo vya maji kwa lengo la kufanya Taifa hili kuwa endelevu na kutoa fursa za upatikanaji wa maji na pia tupate mvua za kutosha kupitia misitu.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Rais eneo la Mazingira wamefanya kazi kubwa na wanaendelea kufanya kazi kubwa kukabiliana na uharibifu wa mazingira. Kwanza ziko sheria zinasimamia uhifadha wa mazingira ambapo pia wenyewe tumeendelea kushirikisha mpaka kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa; mkoani, wilayani na kwenye halmashauri zote na vijijini ambapo ndiyo misitu ilipo, kila mmoja ashiriki katika uhifadhi wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, pia tumeendelea kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, misitu yetu pamoja na vyanzo vya maji kwa sababu vyote hivi vina umuhimu mkubwa kwenye maisha ya kila siku ya binadamu. Hata hivyo, tumekuwa tunashirikisha taasisi mbalimbali za umma na zile za binafsi kwenye uhifadhi wa mazingira na kwenye eneo hili tunaungwa mkono sana. Malengo yetu ni kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi ni programu mbalimbali zilizoko ndani ya Serikali zinazosimamia uhifadhi wa mazingira kwenye milima hiyo ya miinuko, kwenye mabonde na maeneo yote ambayo yana misitu ambayo tunaitumia kwa ajili ya kuhifadhi mazingira yetu. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Watanzania, kwanza kuona umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa maslahi yetu.
Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya kupatikana kwa mvua yanatokana na uharibifu wa mazingira ambao sasa unaendelea; pia ukosefu wa maji kwenye maeneo ambayo tulikuwa tunatarajia tupate maji kama vyanzo ili tujenge miradi ya maji inatokana na uharibifu wa mazingira. Madhara haya na madhara mengine ndiyo yanasababisha sasa kuwa na mabadiliko ya majira, kuhamahama kwa wanyama kutoka kwenye maeneo yao kuhamia kwenye maeneo mengine wakitafuta maji na aina nyingine yoyote ya usumbufu ambao tunaupata.
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, nataka niwakikishie kwamba Serikali inao mpango huo wa kuhifadhi mazingira, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na tumeipeleka hiyo mpaka TAMISEMI, tusimamie kwa pamoja tuhakikishe kwamba nchi yetu tunakabiliana na uharibifu wa mazingira. Kwa kufanya haya, tunaweza sasa tukaokoa mazingira yetu na tukaanza kunufaika na uwepo wa misitu hii, vyanzo vya maji na aina nyingine yoyote ya uhifadhi ambayo tumeiwekea sheria, na tutaendelea kuimarisha sheria zetu na kusimamia sheria zetu. Vile vile taasisi zote ambazo zinahusika katika uhifadhi zisimamie kikamilifu. Huo ndiyo mkakati wetu tulionao ndani ya Serikali, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Serikali imekuwa ikitekeleza miradi ya elimu na afya nchini kwa kujenga majengo mbalimbali, lakini pamoja na Serikali kutekeleza miradi hiyo pia wananchi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kuhakikisha wanasaidiana na Serikali katika kuhakikisha wanajenga majengo hayo kwenye maeneo yao: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanabainisha majengo yote ambayo ni maboma nchini ili yaweze kumaliziwa na wananchi waweze kuona thamani ya nguvu yao lakini na fedha ya Serikali inayokwenda kwenye maeneo yao ili wananchi waweze kutumia? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa miradi, iwe ya elimu au afya ambayo inahusisha majengo na yasipokamilika sasa yanakuwa ni maboma, ni mkakati ambao sisi Serikali tumeuelekeza zaidi kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Tuna upatikanaji wa vyanzo vya fedha wa aina mbili; moja, kutoka Serikali Kuu. Kutoka Serikali Kuu, tunapeleka fedha kwenye halmashauri za kujenga majengo haya kwa thamani ya jengo lenyewe na kwa hiyo basi, kunatakiwa kuwa na usimamizi baada ya fedha hizi kuzipokea kuhakikisha kwamba jengo lenyewe linajengwa kwa thamani ile ile ambayo wao walitoa makadirio na Serikali Kuu kupeleka fedha kwenye Sekta ya Elimu na Afya tunapojenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na majengo mengine, kwenye afya pia zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Mheshimiwa Spika, pia kuna fedha ya aina ya pili inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri zenyewe ambapo wao halmashauri hupanga mpango wa maendeleo yao kupitia bajeti yao kwenda kujenga. Maboma mengi yanatokana na mipango ya fedha hizi za halmashauri. Kwa nini mpango wa Serikali haukukamilisha maboma?
Mheshimiwa Spika, nataka niiagize sasa TAMISEMI, kwanza iendelee na utaratibu wa kubaini maboma yote ambayo wao waliyajenga na hayakukamilika na wahakikishe wanaendelea kutenga bajeti za kukamilisha maboma hayo kwa sababu yametokana na bajeti zao. Uzoefu tulioupata wakati wa ukaguzi wa miradi hii, majengo yote yaliyopelekewa fedha za Serikali Kuu yamekwenda kama yalivyo na pale ambapo hayakukamilika hatua kali zimechukuliwa. Nao wametakiwa kukamilisha fedha kwa kuwa wameshindwa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa fedha ambayo ilikuwa imepelekwa. Sasa kwa kuwa maboma mengi yanatokana na mipango yao na kushindwa kuiendeleza, bado wanatakiwa kuweka bajeti ya kukamilisha majengo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mkakati wa Serikali sasa ni kuhakikisha maboma hayo yanakamilika kwa agizo hili ninalolitoa kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kila halmashauri ifanye tathmini ya miradi yake, ione maeneo gani walianza miradi na wameshindwa kukamilisha na yamebaki maboma ambayo Waheshimiwa Wabunge sasa wanataka waone mpango wa Serikali, ili sasa wapange bajeti ya kila mwaka kuhakikisha kwamba maboma haya yanakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba zahanati ni shilingi milioni 50, vyumba vya madarasa ni shilingi milioni 20 na fedha zote zinapatikana kwenye halmashauri. Zipo halmashauri zinapata zaidi ya shilingi bilioni tatu mpaka nne kwa mwaka, hawawezi kushindwa kupata shilingi milioni 20 ya kukamilisha chumba cha darasa, au shilingi milioni Hamsini za zahanati, au shilingi milioni 300 kwa ajili ya kujenga zahanati na kituo cha afya. Kwa hiyo, agizo langu bado linabaki pale pale kwamba tunahitaji sasa halmashauri zisimamie.
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba maboma yote haya yanakamilika ili huduma zianze kutolewa kwa wananchi walioko kwenye maeneo hayo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumwuliza swali Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa nchi yetu imeamua kuongeza wigo wa diplomasia wa uchumi kwa kufungua milango ya kibiashara na kimawasiliano: Ni upi mkakati wa Serikali katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja yanayounganisha nchi kuendana na uchumi ambao sasa tunautarajia katika nchi yetu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mtenga, Mbunge wa Mtwara Manispaa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anahitaji kujua mpango wa Serikali wa kuimarisha ujenzi wa madaraja kwa lengo la kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na mawasiliano kati ya nchi yetu na nchi jirani. Mkakati wa Serikali katika kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na mawasiliano ni mkakati endelevu na hakika kwenye eneo hili lazima nimpongeze kwanza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameifungua nchi kwa kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na mahusiano na mataifa mengi duniani na tumeanza kuona manufaa ya marafiki wengi kuja nchini kuwekeza katika maeneo mbalimbali. Hii inatokana na jitihada hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mpango wa kuendelea kujenga daraja. Najua anachotaka kukiuliza ni nini? Wiki mbili zilizopita nilikuwa Mkoani Mtwara, na moja kati ya jambo ambalo yeye aliliuliza hadharani ni ujenzi wa daraja wanalolihitaji wakazi wa Mkoa wa Mtwara kwenda nchini Msumbiji. Tuna madaraja mengi. Kule Mkoani Mtwara tuna Daraja la Umoja lile linalotoka Wilaya ya Nanyumbu kwenda Msumbiji. Linaitwa Daraja la Umoja, daraja zuri, kubwa, linalounganisha hizi nchi.
Mheshimiwa Spika, pia tuna madaraja mengine; kule Mkoani Mbeya Wilaya ya Kyela tuna daraja pale Kasumulu, linaunganisha na Malawi; Ileje tuna daraja la Mto Songwe linaunganisha na Malawi pia; na kule Ngara tumefanya ziara kwenye mradi mkubwa wa umeme wa Rusumo, tuna daraja kubwa linaungfanisha na Rwanda. Tunatarajia kuimarisha ujenzi wa madaraja haya ikiwemo na Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Ujenzi kupitia Meneja wa Mkoa wa Mtwara wa TANROAD alituhakikishia kwamba liko eneo la Mtwara Vijijini ambalo ndiyo karibu zaidi na Msumbiji, karibu zaidi na maeneo ambayo yana huduma nyingi za kibiashara na mkoa mmoja unaitwa Cabo Delgado, moja kati ya mikoa iliyoko nchini Msumbiji kwamba tayari wameshaanza upembuzi yakinifu ili kujenga daraja kwenye eneo la Kikole, Kikombo ambalo pia litakwenda mpaka Msumbiji. Huo ndiyo mkakati wa kuimarisha ile diplomasia ya kiuchumi na Msumbiji na diplomasia ya mawasiliano na msumbiji kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anatoka Mkoa wa Mtwara alisisitiza kwamba Wanamtwara wanahitaji zaidi.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa daraja hili siyo kwa Wanamtwara tu, ni taifa zima, kwa sababu sisi na Msumbiji tuna mahusiano na maeneo yote yanayohitaji kujengwa daraja, maeneo yote ambayo yanahitaji kuimarishwa vivuko, na maeneo yote yanayohitaji kuimarishwa malango ya uhamiaji kwa lengo la kujenga mahusiano rahisi na nchi jirani ili kuimarisha uchumi na mawasiliano kwenye nchi hizi.
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imelichukua jambo hili na kuendeleza jitihada hizi ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wetu amezianzisha na tunataka tuone sasa Watanzania wananufaika na diplomasia hii ya kiuchumi na mawasiliano na nchi jirani na nchi zote ambazo zinajenga mahusiano mazuri na Tanzania.
Mheshimiwa Spika, huo ndiyo mkakati ambao tunao kwa sasa kwenye eneo hili la kuimarisha mahusiano na hasa kwenye maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge anahitaji zaidi Serikali ianze kujenga daraja la kwenda nchini Msumbiji, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu tuna sera ya Cooperate Social Responsibility (CSR) kwa jamii yetu inayotoka kwenye makampuni, mashirika, wawekezaji na wakandarasi mbalimbali; lakini fedha hizi zimekuwa zikifika zinacheleweshwa sana kutumika. Leo tunaomba kauli ya Serikali juu ya ucheleweshwaji wa matumizi ya fedha hizi za CSR?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabla sijaanza kujibu swali la Mheshimiwa Songe Mbunge wa Busega, Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Watanzania wenzangu mnajua leo tarehe 01 timu yetu ya Dar Young Africans ambayo inapeperusha bendera ya Taifa itaondoka muda mfupi ujao uwanja wetu wa Dar es Salaam kuelekea nchini Jijini Algiers kwa ajili ya mchezo wa pili wa fainali. Naamini sote na tuendelee kila mmoja kwa dhehebu lake tuiombee timu yetu ya Dar Young African iweze kushinda mchezo huu wa pili kwa magoli mengi ya kutosha ili Watanzania tuweze kuwa mabingwa. Timu yetu ina uwezo mkubwa, muhimu zaidi tuwaombee wachezaji wetu, na mchezo wa tarehe 03 naamini watanzania tutakuwa kwenye sceen kuiombea na tunaamini tutashinda na watarudi na kombe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hili niungane na Watanzania kwa kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ametoa usafiri wa ndege unaobeba wachezaji, viongozi na wapenzi kadhaa pamoja na viongozi wa Serikali kuisindikiza timu yetu ya Dar Young African kwenye mashindano hayo muhimu kwa Taifa letu. Tunatamani sana ushindi huu upatikane mkubwa ili tujenge historia ya kupata kombe hili kwa mara ya kwanza nchini Tanzania. Mwenyezi Mungu awajalie safari njema pia mchezo mwema, mafanikio makubwa kwenye michezo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nijibu swali la Mheshimiwa Songe Mbunge wa Busega kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali tunayo sera ya CSR fedha ambayo inapatikana kutoka kwenye mashirika, makampuni na kwa wawekezaji waliowekeza na kufanya shughuli kwenye maeneo yetu kwa kutoa sehemu ya fedha. Iko sheria imetaja na asilimia, sina kumbukumbu ya haraka, lakini fedha ile inatolewa kwenda kwenye jamii iliyoko jirani na mradi huo au uwekezaji huo ulipo kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo. Fedha hii inapotolewa inapoenda kwenye kijiji au halmashauri inapaswa kuingia kwenye mfuko wa mapato ya ndani ya kijiji au halmashauri ili iweze kuratibiwa na kupangiwa miradi ya kufanya kulingana na mahitaji ya jamii yenyewe; na fedha hii inapoingia kwenye mfuko kama mapato manake lazima inaingia kwenye bajeti, inapangiwa matumizi.
Mheshimiwa Sika, na kwa hiyo fedha ikiingia lazima itumike katika kipindi cha mwaka. Hata kama itakuwa imechelewa kuingia lakini wakati wanapofanya mabadiliko madogo ya bajeti ndogo na yenyewe lazima ziingizwe. Kwa hiyo fedha hii inapoingia inakuwa inaingia kama sehemu ya bajeti na ikiwa sehemu ya bajeti ni lazima itumike. Kwa hiyo Serikali inasimamia hili kupitia halmashauri zetu kwa sababu miradi inakuwa kwenye wilaya, vijiji; na pindi fedha hii inapoingia mamlaka husika zinazopanga matumizi lazima zipangie matumizi.
Mheshimiwa Spika, tunajua baadhi ya halmashauri zinazopata bahati kuwa mashirika haya, makampuni haya ya uwekezaji wanapopata fedha hii wanaiona kama ni fedha nje ya bajeti na kwa hiyo upangaji wa matumizi yake unachukua muda mrefu na mwisho wanaingia kwenye migogoro. Sasa nitoe maelekezo, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI yuko hapa, na wanufaika wakubwa wanakuwa ni halmashauri ya wilaya au vijiji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pindi tunapopata makampuni au wawekezaji na wanatoa gawio hili la maendeleo ya jamii na linaingia kwenye halmashauri basi fedha hii isimamiwe na maelekezo yatoke, wale maafisa masuhuli kwa maana ya mkurugenzi lazima azitambulishe kwenye Baraza la Madiwani. Baraza la Madiwani lipange utaratibu na utaratibu ule uende kwenye miradi moja kwa moja ili wananchi waweze kunufaika kwa mradi waliotamani wao kuujenga, na itaingia pia kwenye kaguzi mbalimbali. Kwa hiyo mkaguzi wa ndani wa halmashauri anawajibika moja kwa moja kufuatilia matumizi ya fedha hizo. Tukifanya hili litaanza kuleta manufaa.
Mheshimiwa Spika, na sisi Serikali tunajua fedha ikiingia huko inatumika kama ilivyokusudiwa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na mimi kunipa nafasi hii ya kuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa sana ya ujenzi wa vituo vya afya nchini. Sambamba na kazi hiyo vilevile Serikali imepeleka vifaa tiba takriban kwenye vituo vyote vya afya nchini Tanzania. Swali langu, kumekuwa na upungufu mkubwa sana wa wataalam katika hivyo vituo wa kutumia hizo mashine na vifaa tiba vilivyopelekwa na Serikali.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka wataalam kwenye vifaa vyote ili kuweza kunusuru maisha ya Watanzania?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Lusinde Mbunge wa Mvumi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naungana naye, kwamba Serikali yetu kutoka awamu ya tano na sasa awamu ya sita imefanya kazi nzuri sana kwa ujenzi wa maeneo ya kutolea huduma nchini; zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri za wilaya pia mikoa na kanda, na sasa tunaimarisha pia na huduma kwenye hospitali za kitaifa. Kazi kubwa imefanywa nataka nitumie nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake na kwa usimamizi wake, na sisi tunaendelea kuimarisha maeneo hayo ya utoaji huduma. Awamu ya kwanza ilikuwa ni kujenga miundombinu ya majengo. Kazi hiyo imefanywa vizuri, na tunataka tuwahakikishie Watanzania, kwamba tutaendelea kujenga vituo vya afya na zahanati kulingana na mahitaji kwenye halmashauri zetu na vijiji.
Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ni ya kupeleka vifaa tiba na dawa, kazi ambayo sasa inaendelea kwa kasi. Baada ya majengo sasa tunaweka vifaa vya maabara, pia dawa na vifaa vingine kama vile vitanda kwenye wodi. Kazi hii pia inaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mpango wa Serikali wa kupeleka sasa watumishi. Kwa eneo hili la watumishi kazi sasa inaendelea vizuri. Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa vibali kwa Wizara ya Afya pamoja na mamlaka Serikali za Mitaa kuwaajili ya watumishi wa sekta ya afya ili kuwapeleka kwenye maeneo haya yote, zahanati, vituo vya afya na hospitali zote ili waweze kutoa huduma. Tunajua tuna maeneo mengi ya kutolea huduma, mahitaji ni makubwa kulingana na Ikama; kwa hiyo Serikali itaendelea kuajiri kulingana na uwezo wa kifedha kwa lengo la kutoa huduma kwa Watanzania kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, wakati huo tukiwa tunapewa kibali pia huku ndani tunafanya mapitiom, kwa sababu tunajua kuna maeneo mengine kuna watumishi wengi zaidi kuliko maeneo mengine, kwa hiyo tunahamisha walikojaa na kuwapeleka maeneo na hasa kutoka maeneo ya mijini ambako kuna mrundikano wa watumishi na kwenda kwenye maeneo ya vijiji ili maeneo yote yaweze kupata huduma. Pia wale waliopo tunawaongezea uwezo kwa kuwapeleka kwenye mafunzo, semina na warsha ambazo pia zitawasaidia kuwafanya waweze kutoa huduma hii kwa urahisi zaidi. Kwa hiyo nitoe pia maelekezo kwa wakurugenzi kufanya mapitio ya kina ya idadi ya watumishi tulionao na maeneo yenye mrundikano mkubwa kuwahamisha kuwapeleka kwenye maeneo ambayo yana watumishi wachache. Malengo yetu ya Serikali huduma hizi zitolewe kwa usawa kwenye maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwakikishie Mheshimiwa Lusinde kwamba Serikali inaendelea na ajira, na ajira hizi malengo yetu ni kutosheleza watumishi kulingana na ikama inayotakiwa, na Watanzania sasa waweze kupata huduma za afya kama ambavyo Serikali inataka ione Watanzania wakinufaika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Na mimi naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu swali kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na mkakati wa kutekeleza miradi mikubwa kupitia Mtwara corridor lakini mpaka sasa wananchi hawana uelewa juu ya miradi inayojumuishwa na iliyotekelezwa angalau kwa asilimia 50;
Je, Serikali inatoa maelezo gani juu ya utekelezaji wa hiyo Miradi ya Mtwara Corridor?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Mtwara Corridor ambao pia na mimi mdau ni mradi ambao unaasisiwa na Serikali yetu. Mradi huu una maeneo mengi yanayotekelezwa ili kusheheneza mahitaji ya Mtwara Corridor. Mtwara Corridor inatazamiwa kuimarisha huduma mbalimbali kutoka Mtwara kuelekea Mkoani Ruvuma, na pale Ruvuma tuna Mkoa jirani wa Njombe kwa kutumia fursa zilizopo kwenye maeneo haya. Kwa hiyo mikoa hii minne Lindi, Mtwara, Ruvuma pamoja na Njombe ni wanufaika wakubwa wa mradi huu.
Mheshimiwa Spika, kwanza tuna mradi wa kuimarisha barabara ambayo tunayo sasa ya lami inatoka Lindi, Mtwara inafika Ruvuma kupitia wilaya zake hapa katikati za Masasi na Tunduru. Na baada ya kufika Songea Mjini Mkoani Ruvuma tuna barabara inakwenda Mbinga mpaka Mbamba Bay, na wale wenyeji mnajua na mimi nimepita huko kuona na kukagua miradi yote hiyo. Sasa tuna barabara inatoka Songea kuelekea Njombe na barabara nzuri inajengwa kutoka Njombe kwenda Ludewa na barabara kote huko tumepita na tumeona kazi nzuri inafanyika.
Mheshimiwa Spika, lakini pia eneo la pili tunaimarisha bandari zetu zilizoko kwenye maeneo haya. Tumeona na wote mashahidi Bandari ya Mtwara imeimarishwa na leo inaanza kupokea meli kubwa; na lengo bandari hii iweze kuhudumia Mikoa hii ya Lindi, Mtwara mpaka Ruvuma pia na nje ya nchi kwenda Malawi na Msumbiji. Tuna bandari nyingine mbili zimeimarishwa, ile ya Mbamba Bay tumeona imeimarishwa, na bado itajengwa kubwa; lakini pia Lihuli au Litui, moja kati ya miji hii tumeona inaimarishwa. Pia Mkoani Njombe kule Ludewa Tungi kuna bandari pale; lakini pia hata Mkoani Mbeya Wilaya ya Kyela nako pia Ziwa Nyasa kuna bandari pale tumeenda na tumejenga na meli zinatoa huduma na nchi ya jirani.
Mheshimiwa Spika, pia tunataka tuimarishe kazi kubwa ya ujenzi wa reli inayotoka Mtwara kwenda Ruvuma na kwenda Mkoani Njombe kule Liganga Mchuchuma kwa ajili ya kuchukua mawe, na reli hii pia itakwenda mpaka Mbamba Bay. Kwa hiyo hii yote hii ndio inaitwa Mtwara Corridor, chini ya program ambayo Mheshimiwa Mbunge anahitaji kujua. Kwa hiyo tumeshaanza kazi hiyo na tunaendelea.
Mheshimiwa Spika, sasa ili wananchi wajue Mtwara Corridor ni nini, sasa Serikali inajipanga, tunapoendelea kwenda kujenga SGR kutoka Mtwara mpaka mikoa ya Ruvuma pamoja na Njombe kule Mchuchuma tunaendelea sasa kujipanga kutoa elimu ya nini Mtwara Corridor inahitaji na namna gani wananchi watanufaika kwa fursa za Mtwara Corridor ili tuweze kupata maslahi mazuri kupitia program hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali tunajipanga sasa kutoa elimu, kutoa hamasa kwa wananchi kuwa tayari kupokea mpango huu wa Mtwara Korido. Kwa hiyo malengo ya Serikali bado yamebaki palepale na utekelezaji unaendelea hatua kwa hatua, na pindi utakapokamilika wananchi wote watakuwa wanajua umuhimu wa Mtwara Corridor, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi kuuliza maswali kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Waziri Mkuu naiona nia ya dhati ya Serikali kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo wadogo kwa hasa kwa kuwatafutia mitaji kwenye taasisi za kifedha hasa benki. Lakini benki hizi zinapokuwa zinawapa mikopo machimbaji wadogo wadogo zinawapa kwa masharti ambayo hayaendani na uhalisia wa biashara hii ya wachimbaji wadogo hasa ukizingatia musa wa uzalishaji na upatikanaji wa madini hayo.
Je, ni nini mkakati wa Serikali kutengeneza mazingira rafiki ya taasisi za kifedha ili waweze kuwapa mikopo wachimbaji wadogo ambayo itazingatia mazingira yao ya upatikanaji wa madini na mazingira yao ya uzalishaji wa madini?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Makamba, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua nafasi ya Serikali katika kusimamia fursa ya wachimbaji wadogo wa madini na upatikanaji wa mitaji bila ya kuathiri utendaji wao. Serikali yetu inayo sera inayoimarisha wajasiriamali, wachimbaji wadogo wa madini, kwa kutumia fursa walizonazo kwa maeneo yao panapopatikana madini kuchimba kwa uhuru na Mheshimiwa Waziri wa Madini mara kadhaa ameeleza mpango wa Serikali wa kupima viwanja kwa ajili yao na kuwasisitiza wajitokeze kushiriki kikamilifu kwenye fursa hii ya uwepo wa madini.
Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto ya wachimbaji hawa ya kukosa vifaa muhimu pamoja na mitaji ya kuanzishia kazi ya uchimbaji. Serikali tuchofanya ni kuelekeza kwenye taasisi za fedha, benki kwa maana ya sekta binafsi na wale wote ambao wanakopesha mikopo na wanaotambulika rasmi upande wa Serikali, tunazo halmashauri za mikopo midogo kwa wanawake na walemavu na tuna mifuko pia ya uwezeshaji ambayo yote hii, maeneo yote haya ni fursa kwa vijana wetu kukopa. Tunatambua ipo changamoto ya masharti mbalimbali ya hizi taasisi za kifedha.
Mheshimiwa Spika, ni nini tumefanya; ni kutoa maelekezo kwa taasisi hizi. Kwanza lazima wajue huyu anayekuja kukopa anataka kufanya shughuli gani, na shughuli hii kuanzia uwekezaji wake mpaka uzalishaji wake inatumia muda gani, na kwa hiyo masharti yale lazima yalenge utendaji wa sekta hiy,o kwa sababu kila eneo lina muda wake wa uwekezaji na uzalishaji wake na kuingia kwenye masoko. Itakuwa haipendezi kama anajua kwamba mchimbaji mdogo tangu anachimba mpaka kuuza anajua ni ndani ya miezi sita halafu unampa mkopo wa miezi mitatu, utakuwa humtendei haki. Kwa hiyo basi Serikali tunachofanya tumetoa maelekezo sahihi na thabiti kwa taasisi za fedha kuzingatia nature ya shughuli au mradi ambao mjasiriamali anaufanya ikiwemo na wachimbaji wadogo. Sisi tunajua uchimbaji mdogo unapaa paa bila ya kuwa na uhakika kwamba je, utapata madini yenyewe? Na ukipata madini yenyewe, na ukipata ile process mpaka kwenye masoko.
Mheshimiwa Spika, mara kadhaa tumeenda kuwasisitiza wajasiriamali lakini mara kadhaa tumehamasisha taasisi za fedha kufanya study ya uchimbaji mdogo na kuwafikia wachimbaji wadogo na kuwakopesha tena kwenye riba ndogo, ikiwezekana bila riba kabisa, ili kuwawezesha vijana wetu wajasiriamali kupata mikopo na kuitumia na hatimaye wapate faida. Mara kadhaa pia tumemuagiza Mheshimiwa Waziri wa Madini kusimamia sekta hii; na tumemuona akipita maeneo mbalimbali akizungumza na wajasiriamali wadogo pamoja pia na sekta za fedha ili kuhakikisha kwamba zinatenga fedha kwenye dirisha hili la wachimbaji wadogo ili waweze kupata mikopo yenye mazingira mazuri ya ukopaji na urejeshaji kwa lengo la kuwaondolea adha ya au kufungwa au kunyang’anywa mali zao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali inaendelea kukaa na taasisi za fedha na kuzihamasisha kutenga mitaji kwenye dirisha hilo kwa masharti lakini waangalie utendaji wa sekta hiyo ili wajasiriamali waweze kupata mikopo yao vizuri. Tumeendelea pia kuwataka pia hata wajasiriamali hawa kuunda vikundi vikundi. Wakiwa kwenye vikundi ni rahisi zaidi kwa sababu taasisi nyingi zinaogopa kupoteza fedha, kwa hiyo ushirika ni mkombozi sana kwao. Na sisi tunaendelea kusimamia hasa sheria zilizosajili taasisi hizi za fedha kwa masharti ambayo hawaendi kwa kuweka riba kubwa inayomfanya yule mkopaji kushindwa kurejesha na hatimaye kuuzwa nyumba, labda kunyang’anywa au kufungwa. Kwa hiyo haya yote Serikali tunazingatia. Nataka nitoe wito kwa wajasiriamali washiriki kikamilifu na kwa uhuru mkubwa na wajenge matumaini na Serikali yao kwamba tunasimamia sekta hii ili waweze kupata maslahi kwenye sekta ya madini.
Mheshimiwa Spika, nimuagize Mheshimiwa Waziri wa Madini kufatilia taasisi za fedha zinazokopesha wajasiriamali hawa, kuwa wanapokwenda kukopesha hawaweki riba kubwa inayomuathiri mchimbaji; tunataka kila mmoja afanye kazi hii vizuri na apate faida, ahsante sana.
MHE. ALLY M. KASSINGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu Serikali imekuwa ikitekeleza sera yake ya elimu bila malipo au maarufu kama elimu bure kwa misingi ya kuwapunguzia gharama wazazi au walezi wa vijana ambao wanasoma katika shule zetu za sekondari hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo bado kumekuwa na michango kadhaa katika shule zetu za umma, ikiwemo michango ya ulinzi, shajara pamoja na chakula;
Je, Serikali haioni umuhimu wa kupitia upya sera hii ili hii michango ambayo nimeainisha ambayo kimsingi inabebwa na wazazi au walezi iwe ni jukumu la Serikali kwa dhana ile ile ya kuwapunguzia gharama wazazi au walezi wa vijana wetu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini na mkuu wa wilaya mstaafu kama ifuatavyo: - (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Sera ya Elimu bila Bila Ada kwa lengo la kuwaondolea adha wazazi ya kuwa na michango mingi na ile michango holela, michango holela. Kila mwezi Serikali yetu inapeleka fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya kuwezesha shule zetu za Sekondari, wale wakuu wa shule na uongozi wa shule kuweza kutumia kwenye maeneo ambayo walikuwa wanatarajia sana kupata michango kutoka kwa wazazi ili wazazi wasichangie maeneo hayo na badala yake wazazi waendelee kusimamia maboresho ya mtoto mwenyewe kwenda shule kwa kumnunulia sare, viatu na vitu vingine.
Mheshimiwa Spika, natambua kwamba si maeneo yote yameweza kupata fedha hii hasa eneo la chakula na ulinzi, kama ulivyoeleza. Maeneo haya ambayo tumetolea fedha ni yale maeneo ambayo yanafanya ukarabati mdogo mdogo wa majengo yanayoharibika, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, vitabu, chaki na vitu vingine ili kuondoa adha ya waalimu kuwachangisha wazazi fedha.
Mheshimiwa Spika, eneo ambalo sasa tunaendelea kushughulika nalo ni maboresho sasa. Tunazo shule nyingi za sekondari ambazo wanafunzi wanaenda asubuhi na kurudi jioni na wanapokuwa shule hawapati chakula. Nikiri kwamba eneo hili Serikali bado tunaendelea kuchakata ili tuone namna nzuri ya kutoa huduma ya chakula shuleni; ingawa tumeona sekta binafsi zinashiriki, wakati mwingine wazazi wenyewe wanaweka mpango wao.
Mheshimiwa Spika, sasa, niliposema michango holela; Tunayo ile michango holela ambayo labda waalimu wanasema njoo kesho na shilingi mia mbili, elfu moja, mia tano, ambazo zinakera kwa wazazi. Hiyo tumeidhibiti na tumepiga marufuku na haipo kabisa na kama ipo, tumeshatoa maelekezo na hapa pia nitatoa maelekezo. Sisi tunaruhusu michango rasmi inayokwenda kufanya shughuli za maendeleo. Shule za msingi, shule za sekondari hizi ni shule za wananchi. Kila kijiji kina shule ya msingi na kinasimamiwa na kijiji chenyewe, na tumeunda kamati ya shule kwa shule za msingi. Sekondari ziko kwenye kata, tumeunda bodi ya shule na inamilikiwa na kata kwenye vijiji vitatu, vinne au vitano, wanasimamia na Mtendaji wa Kata ndio kiongozi wetu anayesimamia maendeleo ya shule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inapotokea labda choo kimebomoka hatuzuii wazazi kukaa na kukijenga kwa kuchangia na kujenga hiyo ni michango ya maendeleo. Ingawa michango hii pia tumeiwekea masharti kidogo kwamba anayetakiwa kusimamia michango hii ni mkuu wa wilaya pekee au yeyote ambaye mkuu wa wilaya amemchagua kusimamia. Tunaogopa sasa watu kuchangisha kule holela na ndiyo kwa sababu nilisema michango holela. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi Serikali inaendelea kufanya mapitio ya sera hii ili kuwezesha mzazi kupata unafuu zaidi wa kutoa michango kwa ajili ya maboresho ya shule zetu. Lakini pia bado hatuondoi nafasi ya uwajibikaji wa wananchi kwenye shule zao katika kufanya maboresho. Na niliposema mkuu wa wilaya mstaafu najua hili umelisimamia vizuri sana ulipokuwa mkuu wa wilaya kabla hujawa Mbunge na kwa hiyo Serikali tunaendelea kusimamia haya.
Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa wakuu wa wilaya wote nchini, kwenye halmashauri zao kusimamia kutokuwepo kwa michango holela inayokera wananchi na kushindwa kufanya shughuli nyingine na badala yake kuwa wanasababisha wanafunzi wanaondolewa shuleni; hiyo tulishapiga marufuku kabisa. Lakini pia Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kwamba wanatuhudumia hizi shule lakini na kuweka mpango mzuri kwenye maeneo ambayo yanahitaji pia Halmasjhauri isimamie kupitia bajeti zao, kama ni lazima kuzungumza na wazazi lakini wazazi wenyewe kupitia kamati zao wafanye maamuzi haya ndiyo ambayo kwa sasa tunayasimamia. Lakini niwahakikishie tu kwamba ombi la Mheshimiwa Mbunge la kufanya maboresho ya sera yetu hayo tumepokea na tunayafanyia kazi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu na mimi swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwa na mwingiliano wakati wa utekelezaji wa majukumu kati ya Wizara tatu, kwa maana Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Maliasili pamoja na Wizara ya Ardhi hasa kwenye eneo la utoaji wa GN. Kwa mfano, Wizara ya TAMISEMI wanatoa GN wakati wa uanzishaji wa vijiji, Wizara ya Maliasili wanatoa GN kwenye maeneo yao ya hifadhi lakini Wizara mama ambayo ni Wizara ya Ardhi pia inawajibika kwa mujibu wa sheria kutoa GN kwenye maeneo yote haya ya mipaka.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa utoaji wa GN wakati mwingine hupelekea mogogoro ya ardhi kwenye maeneo haya. Nilitaka nijue tu Serikali ina mpango gani madhubuti wa kuboresha Sera ya Taifa ya Ardhi ya ya mwaka 1995, ambayo pia itapelekea maboresho ya Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 ili kuondokana na kutengeneza formality ya utoaji wa GN kwa sekta moja ya Ardhi badala ya mgongano ulioko kwa sasa, nashukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, maneno yake ya awali sikuyasikia vizuri naomba arudie tena ili niweze kumjibu kwa usahihi zaidi.
SPIKA: Mheshimiwa Jafari Chege.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekua na mwingiliano wa kiutendaji wakati wa utoaji wa GN kati ya Wizara tatu kwa maana Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Wizara ya Ardhi. Nikatoa mfano Wizara ya TAMISEMI wanatoa GN wakati wa uanzishaji wa vijiji kwa maeneo fulani ambayo yanaweza yakawa ndani ya hifadhi, Wizara ya Maliasili nao wanatoa GN kwenye maeneo yao ya hifadhi wakati huo huo Wizara ambayo ni Wizara mama ambayo ni Wizara ya Ardhi nayo inawajibika kutoa GN kwenye maeneo hayo hayo. Kwa hiyo kunakuwa na mgongano wa Wizara tatu zote kutoa GN kwenye eneo moja la umiliki wa ardhi.
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine utoaji huu wa GN husababisha uzalisha mgogoro wa ardhi, hasa kijiji kinapopandikizwa ndani ya eneo moja la hifadhi na wote wakinwa na GN zinazotoka Serikalini. Nilikuwa nataka nijue sasa Serikali ina mpango gani wa maboresho wa Sera ya Taifa ya Ardhi ambayo ni ya Mwaka 1995 ambayo itapelekea maboresho pia ya Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 ili kutengeneza formality ya utoaji wa GN kwa Wizara moja ili kuondoa muingiliano wa Wizara zote tatu kutoa GN kwenye eneo moja la umiliki wa ardhi?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hizi Wizara zote zilizotajwa na Mheshimiwa Chege, Wizara ya Ardhi, TAMISEMI pamoja na Maliasili. Tunajua zinazo sheria zinazosimamia ardhi; lakini hakuna muingiliano wa moja kwa moja kwa sababu tumejitahidi kila Wizara kuwa na majukumu yake hasa katika utoaji wa GN. GN inatolewa na Wizara moja tu. Ardhi wanalo jukumu la kusimamia sera ya ardhi nchini na inayo kujumu la kupeleka watendaji wa sekta ya ardhi wenye taaluma ya ardhi kwenye mamlaka hizi hasa mamlaka ya serikali za mitaa.
Mheshimiwa Spika, mamlaka ya serikali za mitaa kwa maana ya halmashauri za wilaya wajibu wake ni kusimamia matumizi, upimaji wa ardhi kwenye maeneo yao ya halmashauri, na wao ndio wanaanzisha mchakato wa upatikanaji wa hati kwa wale wanaotakiwa kumiliki. Lakini pia halmashauri hizi ndizo ambazo zinasimamia mipaka ya kiutawala. Kijiji na kijiji mipaka yake, kata na kata mipaka yake, wilaya na wilaya mipaka yake hata mkoa na mkoa. Kwa hiyo jukumu lao liko tofauti kidogo ingawa kuna mahusiano ya kiutendaji kwa kupeana taarifa baad aya mmoja kukamilisha jukumu lake.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii wale wanahusika na maeneo ya uhifadhi maliasili zetu na uratibu wa maliasili zote nchini. Wanapokuwa na mipaka wanalazimika kwenda sasa mamlaka ya Serikali za mtaa wanalazimika pia kutoa taarifa ardhi; na mipaka hiyo inapothibitishwa na ardhi wao sasa ndio wanatoa hiyo GN. Tumefanya kazi kubwa kwenye migogoro mbalimbali ya mipaka kati ya maeneo mawili ya utawala, kati ya maeneo mawili ya utendaji kama wakulima na wahifadhi lakini ni vijiji na hifadhi. Na tunapokuwa na mgogoro hii ndiyo kwa sababu tunaita Wizara zote tatu; Wizara ya Ardhi, Maliasili, TAMISEMI kwa sababu kila mmoja ana jukumu lake, na huo ndio utaratibu ambao sasa hivi unaendelea Serikalini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utoaji GN kama vile kule Mbarali ambako baada ya muda mfupi tutatoa GN ile mpya baada ya GN 28 ambayo tumeifanyia kazi sana, hiyo ndio Wizara itahusika siyo kila Wizara tu inatoa GN, Maliasili inatoa GN, Hapana, ni Wizara moja imeshapewa jukumu la kutoa GN Wizara nyingine ina facilitate, nyingine inasimamia. Kwa hiyo Wizara zetu tatu hizi wakati wote wamekuwa wakiangalia maeneo yenye mwingiliano na wanafanya marekebisho halafu tunawawekea sheria, ili kubainisha ile mipaka ya utendaji.
Mheshimiwa Spika, tutaendela kusimamia maeneo yote yenye changamoto, yenye mwingiliano ili kubainisha majukumu ya kila Wizara ili kusiwe na muingiliano ambao unaweza kuleta migogoro ndani ya Serikali. Kwa hiyo huo ndio mkakati ambao tunao ndani ya Serikali, ahsante sana.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ni sera ya nchi yetu kuhakikisha kwamba bandari zetu zinapanuliwa na kuboreshwa na ili ziweze kuwavutia wafanyabiashara wa nchi jirani kutumia bandari zetu, na hii tumefanikiwa sana kwa Bandari ya Dar es Salaam.
Swali langu je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha wafanyabiashara wa Sudan Kusini na Uganda wanaitumia Bandari ya Tanga na wafanyabiashara wa Congo, Malawi na Zambia wanaitumia Bandari ya Mtwara? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Bismillah.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chikota, Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu kupitia Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imetenge fedha kwa ajili ya maboresho ya bandari zetu zote nchini, zile zilizoko Ukanda wa Bahari Kuu pia kwenye Maziwa Makuu ya kuimarisha miundombinu na huduma mbalimbali. Mkakati wa Serikali ambao Mheshimiwa Mbunge anataka kujua wa namna ya kuvutia matumizi ya bandari hizi kwa nchi jirani ipo na inasimamiwa pia na Wizara yetu ya Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, moja tunaongeza vifaa vinavyoweza kupakua na kupakia mizigo kwa muda mfupi ili kuwahakikishia wale wateja wetu kuwa matumizi ya bandari yanatumika kwa muda mfupi zaidi, lakini mbili, tumefanya mapitio ya tozo hasa kwa Bandari ya Tanga na kule Mtwara tumetoa fursa ya kupunguza tozo ili kuvutia kulinganisha na mahitaji ya Dar es Salaam kwa sababu Dar es Salaam wingi wa meli ni mkubwa sana kuliko Bandari ya Tanga na Dar es Salaam ambako pia hata msimu uliopita tumekuwa tukilishughulikia hili na hatimaye tukafikia hatua ya kupunguza tozo ya asilimia 30 ya meli yoyote inayokwenda Tanga kwa ajili ya kuwezesha nchi kama Somalia na Sudan ili kuweza kutumia Bandari ya Tanga na kule Mtwara kwa nchi kama Malawi, Zambia na hiyo Congo ambako pia ni rahisi kufika ili wale wateja wanaoleta mizigo kwenye Bandari hizi za Mtwara na Tanga waweze kuvutiwa zaidi..
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili tunaamini sasa tunaweza tukawavutia wengi kwasababu wakija Dar es Salaam tozo ni kubwa na pale Mtwara na Tanga tozo ni ndogo. Lakini bado tunaangalia pia kwenye eneo la ushushaji wa mafuta nako tumeimarisha vituo na zile mita za kushushia mafuta. Kwa hiyo, tunakaribisha pia na meli zinazoshusha mafuta kwenye bandari zetu za Mtwara na Tanga; na tumejenga pia na matenki ya kutosha. Kwa hiyo urahisishaji wa kazi kwenye bandari hizo ni rahisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini Mamlaka ya Bandari tumeona ikifanya jitihada mbalimbali kupitia Balozi zetu zilizoko kwenye nchi hizo kuhamasisha wafanyabiashara wa nchi hizo kutumia bandari zetu. Hili linaendelea na tumefungua pia hata ofisi za Mamlaka ya Bandari kama vile Congo na tumefungua ofisi Malawi, Zambia ili wateja wote wanaohitaji kupata huduma kupitia bandari yetu na bandari zetu zote watapata mawasiliano kwenye nchi zao bila ya kuwataka wao kuja Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na jitihada nyingine nyingi ambazo tunazifanya ikiwemo na elimu ya kuelimisha wafanyabiashara mbalimbali kutumia bandari zetu za Tanzania. Lakini wote mnajua kwamba Serikali ya Awamu ya Sita nayo inaendelea kusimamia ukamilishaji wa reli ya kati ambayo itakuwa inabeba mizigo; ukamilishaji wa barabara ambako pia magari makubwa yatapita yakiwa yamebeba mizigo haya yote tunaamini wanaelewa.
Mheshimiwa Spika, na nitoe wito kwa wafanyabiashara wa ndani ya nchi na nje ya nchi kutumia vyema bandari zetu zote zilizoko ukanda wa Pwani pia kwenye maziwa yetu tuweze kuruhusu kuongeza uchumi zaidi kwenye nchi yetu na kwa mataifa ya nje tuwahakikishie usalama. Tanzania ni nchi salama na tumeendelea kuimarisha usalama ndani ya nchi. Kwa hiyo tunawahakikishia usalama wa mizigo yao. Wao wenyewe wanapoingia lakini pia wanapopeleka mizigo kwenda kwenye nchi zao. Haya yote tunaamini wafanyabiashara kupitia forum pia za mikutano ya wafanyabiashara wa Tanzania na nchi hizo itaendelea pia kutoa elimu kwa nchi hizo kuleta mizigo na kutumia bandari yetu kuchukulia mizigo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana nchi yetu ilikumbwa na tatizo kubwa la soko la mahindi, hali iliyopelekea kwa Mikoa ya Kusini ikiwemo Ruvuma, Rukwa, Mbeya na Iringa kuuza zao hilo kwa shilingi 15,000 kwa gunia; na hii ilitokana na baadhi ya wakulima na wafanyabiashara kudhani kwamba zao hili kuna zuio la kuuza nje ya nchi.
Swali langu, nini kauli ya Serikali kuhusu zao hili kwa msimu huu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kapinga, Mbunge wa Mbinga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba nchi yetu kupitia Mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini wanazalisha sana mahindi na mimi nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wakulima wa maeneo haya. Kwa sababu leo hii nchi yetu tunaposema tuna uhakika wa usalama wa chakula kwa maana ya kuwa na kiwango kikubwa cha chakula kinatokana na jitihada zinazofanywa na wakulima nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zao la mahindi ni kweli mwaka jana tulipata tatizo kidogo kwa sababu bei ilishuka na kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema wakulima wengi walidhani kwamba tumeweka zuio la kupeleka mahindi nje katika kutafuta soko. Tumekuwa na mikutano mingi na Waheshimiwa Wabunge wa mikoa hiyo kuwahakikishia kwamba Serikali haina zuio hilo. Pia tuliwahi kutoa tangazo hapa mbele ya Bunge lako tukufu ili kuwahakikishia wakulima.
Mheshimiwa Spika, nini tunachokifanya kwenye eneo hili, kwanza lazima tujiridhishe na usalama wa chakula au kiwango cha chakula ndani ya nchi kwamba tuna chakula cha kutosha pia tunakuwa na ziada. Ile ziada ndio ambayo tunaruhusu kuuzwa nje ili ndani ya nchi tusiwe na shida ya chakula. Kwa hiyo, pia hata msimu huu uzalishaji wa chakula msimu huu pindi Wizara ya Kilimo ambayo imekamilisha bajeti yake jana ikishafanya tathmini zake na kujua kiwango cha chakula tulichonacho na kuitambua ile ziada; ile ziada tunatoa kibali cha kuuza nje ili wakulima waweze kupata masoko ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa utaratibu tunaoutumia hapa hatupeleki tu nje holela, bali yule mkulima ambaye anataka kupeleka nje kwa mfano Mikoa ya Rukwa, kupeleka Zambia, Congo na maeneo mengine omba kibali tu kwa Mkuu wa Wilaya ili Mkuu wa Wilaya ajue leo tunatoa tani ngapi nje na sisi itatusaidia pia kujua tumeingiza shilingi ngapi fedha za kigeni kupitia zao la mahindi. Kwa hiyo, utaratibu ni huo mkulima yeyote anayetaka kuuza nje atakwenda kwa Mkuu wa Wilaya kuomba kibali cha kupeleka nje na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ina Afisa wetu wa Kilimo ambaye pia anaangalia kiwango cha chakula na uzalishaji wake ziada. Kwa hiyo, na yeye pia anajua leo imeombwa kibali cha tani 10, kesho tani 20 akijumlisha anajua kwamba tunafikia kile kiwango cha ziada ambacho tunacho.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufatilia eneo hili Serikali inaendelea kufatilia mwendeno wa masoko ya nje ili kuwaruhusu wakulima waliozalisha hapa ndani waweze kupata masoko pia nje huo ndio utaratibu ambao tunautumia wa Serikali. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwa na malalamiko makubwa sana hapa nchini kwa ndugu zetu, Watanzania wenzetu waliokuwa watumishi Serikalini walioondolewa kwa kigezo cha kutokuwa na cheti cha form four.
Sasa ni lini watalipwa stahiki zao halali za kiutumishi ambazo wanadai ili waweze kupeleka watoto wao shule na wengine waweze kujitibisha? Nini kauli ya Serikali? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ulipata taarifa wiki moja iliyopita agizo ambalo lilitolewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya msamaha alioutoa kwa wale wote waliokuwa wameondolewa kwenye utumishi, waliokuwa wametambulika kama wameghushi vyeti vya kidato cha nne na wametumikia katika nchi hii kwamba sasa tufanye mapitio tuwatambue. Pia alitoa fursa la kuunda timu kutoka Wizara ya Utumishi na Utawala Bora kwa pamoja na TAMISEMI ili kuwatambua wale wote waliotumikia kwenye nchi hii na kutoa agizo kwamba walipwe asilimia tano ya pension walikuwa na mchango kwenye pension waliokuwa wanaichangia ili waweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Tume ile itakapokamilisha kazi tutayatambua haya yote, idadi yao, halafu pia wangapi, wale wote ambao wanastahili kupata hiyo asilimia tano ya mchango waliokuwa wanauchangia, lakini pia kuona makundi mengine na maelekezo yanayotolewa.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameunda Tume naomba nisitoe majibu juu ya hilo tuiache Tume ifanye kazi yake, halafu tutapata majibu sahihi. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka 2014 tulitunga Sheria ya Tozo ya Ujuzi na Maendeleo ambapo mwajiri wa sekta binafsi wenye wafanyakazi zaidi ya kumi walitakiwa kuchangia asilimia nne kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha VETA. Lakini asilimia mbili zilielekezwa kwenda kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
Kwa kuwa sasa Serikali imejenga VETA nyingi nchini; na kwa kuwa ofisi yako sasa hivi imetoa fursa kwa vijana wengi kuweza kujiunga na mafunzo haya ya muda mfupi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Ni kwa nini sasa Serikali isione ni muda muafaka wa kurejesha ile asilimia mbili ile iliyopelekwa kwenye bodi ya mikopo iweze kurudi VETA ili waweze kutumia kukopesha wanafunzi hawa vifaa ambavyo watajifunzia na baadaye waweze kuondoka navyo kwenda navyo mtaani vya kuanzia kazi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tulitunga sheria inayotengeneza mgao wa fedha ambazo pia tungependa tuzione zikitumika kwenye vyuo vyetu vya elimu hasa kwenye ufundi stadi.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mpango wa Serikali utakaowezesha vijana wanaohitimu VETA baada ya kuwa tumejenga VETA nyingi nchini namna ya kuwasaidia wanaohitimu ili waweze kuanza vizuri.
Mheshimiwa Spika, kimsingi Serikali imeanza kuimarisha sekta hii ya ujuzi kwa utaratibu, mwanzo tumeanza kujenga VETA na tulianza kujenga VETA kila mkoa, kazi ambayo tumekamilisha siku chache zilizopita; na mimi nimepata nafasi ya kupita mikoa mingi kuona maendeleo ya ujenzi; lakini pili tumeanza na programu ya ujenzi wa VETA kila wilaya zoezi ambalo sasa linaendelea. (Makofi)
Msimu uliopita tulipata fedha, Waheshimiwa Wabunge mlipitisha bajeti ya kujenga VETA 28 kazi ambayo inaenda mwishoni ili pia tuweze kujenga VETA nyingine.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme tunaenda kwa awamu, tumeanza na ujenzi wa miundombinu, lakini mbili tunatoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, halafu tuje tuone sasa tuna idadi gani ya wanafunzi wanaohitimu, tuweze kutenga fecha pamoja na hiyo tozo ambayo pia tunatoza na ile asilimia tunayoitenga tuiingize kwenye mpango huo ili kutoa vifaa vitakavyowezesha kijana huyu anayehitimu kuanza mafunzo yake na stadi yake mara tu anapohitimu. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kulifanyia kazi jambo hili ili kuona hawa vijana wetu wanaoingia kwenye vyuo hivi kwa ajili ya kupata ufundi stadi anapomaliza anaanza kazi moja kwa moja.
Kwa hiyo kadri tunavyoendelea Wizara ya Elimu ambayo ndiyo inashughulikia elimu ya ufundi kupitia VETA itaendelea kuratibu na kuomba fedha zaidi na tunashukuru mmetupitishia bajeti ya Wizara ya Elimu katika sekta mbalimbali ikiwemo kwenye eneo la ujuzi, ili tuweze kuhakikisha kwamba vijana wa Kitanzania wanakuwa na ujuzi katika fani mbalimbali ambazo wao wanazihitaji ziwasaidie pia kwenye kujitafutia ajira au pia wao wenyewe kuwaajiri wengine, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwakuwa baadhi ya maeneo yenye migogoro na hifadhi za Taifa hayajajumuishwa kwenye ile Kamati ya Wizara nane na hata mengine yaliyojumuishwa nayo uamuzi bado haujatolewa na Serikali.
Je, ni lini sasa zoezi hili litaanza rasmi na kumalizika ili wananchi waendelee na shughuli zao bila wasiwasi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtega, Mbunge wa Mbarali kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru umenipa nafasi ya kulijibu swali hili kwa sababu timu ya Mawaziri wanane kutoka Wizara zile shiriki imeendelea kufanya kazi ya kutambua maeneo yote yenye mgogoro na kazi hii tulianza mwaka 2019. Tayari tumeshaainisha maeneo yote na tulileta taarifa hapa Bungeni ya vijiji vilivyofikiwa vilivyokuwa na migogoro lakini katika kutatua migogoro hii iliyopo kati ya wakulima na wafugaji, wakulima na wananchi na hifadhi, lakini pia hata maeneo ya ulinzi tumeweza kuratibu vizuri na ile timu pia hata wiki iliyopita ilikuwa imesafiri kwenda kukamilisha hiyo kazi na kazi bado inaendelea.
Mheshimiwa Spika, migogoro hii ina ngazi mbalimbali na sisi Serikali tumeweka utaratibu; kwanza migogoro yote ya ardhi inaratibiwa na ngazi za vijiji kwanza kwenye maeneo yenye migogoro, na zile kamati zinao uwezo wa kumaliza migogoro hii kwa kukutanisha wenye migogoro, lakini pia ngazi ya Kata, ngazi wa Wilaya na Mkoa. Leo tunazungumzia Wizara nane matatizo yanayoshughulikiwa na Wizara hizi nane ni yale makubwa tu, ambayo yanahitaji pia kukutanisha wataalam wa ngazi za Wizara na ndio kwa sababu Wizara nane zote zinazunguka na kupitia migogoro ile mikubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilitaka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na kazi ya kuondoa migogoro inayojitokeza kwenye maeneo yetu na tunafanikiwa kwa kiasi kikubwa na tunaendelea kubainisha maeneo yenye migogoro yenye tija na yasiyokuwa na tija, lengo hapa ni kuwataka Watanzania kila mmoja afanye kazi yake, wale wakulima waendelee kufanya kazi zao, wanaoshughulikia mifugo, uvuvi na maeneo mengine, lakini pia hata hifadhi zetu nazo zifanye kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kwenye hifadhi wote mnatambua Serikali hii pia ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imeridhia maeneo yale ya hifadhi ambayo kwa sasa yanaonekana hayana tija tunayaruhusu wananchi wafanye shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utaratibu huu unaendele kuratibiwa na pindi watakapokamilisha tutakuja kutoa taarifa kwenye Bunge lako tukufu ili Waheshimiwa Wabunge mnaotoka kwenye maeneo hayo muwe na taarifa hiyo. Kwa hiyo tutakamilisha wakati wowote tu kwa haraka zaidi ili na nyie mpate taarifa na migogoro iishe kwenye maeneo yetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ninatambua changamoto kubwa iliyopo ya ajira kwa vijana wetu, changamoto ambayo ni ya kidunia, lakini nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa juhudi kubwa ambazo imeendelea kuzichukua kuhakikisha kwamba vijana hawa wanaweza kujiajiri ama kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu Serikali sasa inaonaje inapokuwa inatoa kibali cha ajira na kuzitangaza ajira ikawepo asilimia fulani ambayo itakuwa ni maalum kwa ajili ya vijana wenye ulemavu wenye sifa zinazotakiwa. Tofauti na ilivyo sasa hivi ambapo vijana hawa wamejikuta wanaomba ajira na kukosa na hivyo kuendelea kupelekea ugumu wa maisha kwao na hasa ikizingatiwa kwamba ulemavu na gharama? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ikupa, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu kwenye mfumo wetu wa ajira, utaratibu ambao pia unawatambua wenzetu wenye mahitaji maalum ambao pia wanaomba ajira kwenye eneo husika, tumeunda Tume, Tume inaitwa Tume ya Ajira ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais Utumishi, na tumejiwekea kanuni ambayo pia Tume ya Ajira inasimamia kanuni hii na pia tumetoa maelekezo kwenye sekta zote za ajira kwamba kila panapokuwa na nafasi ya ajira lazima tutenge asilimia tatu kati ya wajiriwa 20 iwe ni kwa ajili ya walemavu. Kwa utaratibu huu ambao tunaendelea nao sasa umewezesha wenzetu wengi wenye ulemavu kupata ajira kwenye sekta mbalimbali, muhimu ni kuwa na zile sifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna maeneo ambayo pia hata kama hana sifa, lakini ana uwezo na anaweza akafanya kazi hiyo, basi Tume huwa inatoa fursa ya kuweza kuingia kwenye ajira na maelekezo ambayo tumeyatoa kwenye eneo hili ndugu zetu wenye ulemavu wanapata nafasi ya awali hata kwenye interview (kwenye mahojiano) wao wanaanza kwanza wanakamilisha alafu wengine wanafuata. Hii yote nikutambua wenzetu ili na wao pia waweze kuingia kwenye mfumo wa ajira.
Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Ikupa kwamba Serikali kupitia utaratibu huu inaendelea kuwahakikishia wale wenzetu wote wenye mahitaji maalum au wenye ulemavu kwamba pindi tunapotoa nafasi za ajira na wao pia watapata fursa ya kuwa sehemu ya watakaoajiriwa na wote mnaona kwenye sekta mbalimbali mnaona waajiriwa wapo, hata kwenye teuzi za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu ametambua hili amefanya uteuzi kwenye ngazi mbalimbali Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Maafisa mbalimbali kwenye sekta zote, hii maana yake ni nini; kuonesha kwamba Serikali inatambua uwepo wa ndugu zetu wenye ulemavu ambao pia wanao uwezo mkubwa wa kufanya kazi kuliko hata sisi ambao tuko imara kwenye viungo vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka niwahakikishie wale wote ambao wangetamani kuomba nafasi za ajira Serikalini ambao ni walemavu wajitokeze kila wanaposikia ajira kwa sababu fursa ipo na inatekelezwa kupitia taasisi zote zinazoajiri, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kumuuliza Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, mikoa takribani 15 ya Tanzania ikiwemo Kilimanjaro, Kagera, Tanga, Ruvuma na mingineyo uchumi wake unategemea sana zao la kahawa, lakini zao hili halina ruzuku.
Ni nini msimamo wa Serikali kuhakikisha zao hili linapata ruzuku kama ilivyo kwa mazao mengine ya kimkakati? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Malleko, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kahawa ni miongoni mwa mazao yanayotegemea kupandisha uchumi kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye mikoa ambayo Mheshimiwa ameitaja; na mimi juzi nilikuwa Mkoani Kagera kushughulikia zao hilo hilo, lakini pia jana tumekamilisha bajeti ya Wizara ya Kilimo na limechangiwa sana na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa juu ya ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, upo mkakati wa Serikali kutoa ruzuku kwenye mazao mbalimbali ikiwemo kahawa na ruzuku inategemea sana kwenye zao hilo mahitaji yake makubwa kwa sababu kila zao lina mahitaji yake, lakini tunajua tuna suala la mbegu au miche wakati mwingine, lakini pia tuna madawa kwa maana ya pembejeo madawa, mbolea lakini pia namna bora ya kulisimamia zao hili hata maghala nayo pia tunaweza kuweka ruzuku kama alivyosema Waziri wa Kilimo jana. Zao la kahawa linalolimwa Kagera na kule Kilimanjaro kila eneo linategemea na mahitaji yao na hayo mahitaji ndio tunayoyafanyia ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano juzi nilipokuwa Kagera Vyama Vikuu vya Ushirika vilikuwa vinazungumzia wakulima wao kwamba kuna umuhimu wa kuongeza ruzuku kupata miche, lakini pia kuna tatizo la upungufu maghala na wanahitaji ruzuku kwa ajili ya maghala. Kwa hiyo unaweza ukaenda Mbinga nilishakwenda Mbinga wakati tunasimamia zao hili kule sehemu kubwa ilikuwa ni kupata ruzuku ya kupata mbolea kwa sababu Mbinga bila mbolea huwezi kukuza zao hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ruzuku inategemea na mahitaji ya zao na eneo hilo kwa hiyo Serikali imeweka utaratibu wa kutoa ruzuku na kwenye kahawa kama kule Kagera tumetoa ruzuku kwenye miche kupitia taasisi ya utafiti ya TACRI. Lakini pia tumeshakubaliana na Waziri na Waziri ameshaahidi kule Kagera kujenga maghala ambako pia tunaanza na mfumo wa masoko kupitia stakabadhi ghalani ambayo inahitaji kuwa na maghala. (Makofi)
Kwa hiyo ruzuku huko Mkoani Kilimanjaro na maeneo mengine tutakapokuja tutajua mahitaji ni nini na tutaona uwezo wa Serikali na mpango ambao tumeweka ruzuku basi tutatoa ruzuku kutegemea na eneo hilo na mahitaji ya zao hilo; huo ndio utaratibu ambao tunautumia kwenye mazao yetu karibu yote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna upimaji wa ardhi na maeneo mbalimbali yenye migogoro ya ardhi ikiongozwa na Wizara nane, sehemu nyingine ambazo zinapimwa ni maeneo ambayo yapo mbali na vyanzo vya maji nchini, imeleta taharuki kubwa kwa wananchi katika upimaji huu kiasi ambacho wananchi wanajua wanabomolewa nyumba zao nchini katika taharuki hii ya upimaji katika maeneo ya maji ya upimaji wa ardhi.
Je, Serikali ina kauli gani kwa wananchi kuondoa taharuki hii?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, swali linarudi tena kwa sura nyingine la migogoro kwenye maeneo, lakini natambua mara kadhaa nimekuwa nikipita Morogoro na Mheshimiwa Mbunge mara kadhaa amekuja na wananchi wanaotoka kwenye eneo lake hasa kule Mindu wakizungumzia ile amri ya ujenzi wa makazi umbali wa mita 60 na zaidi ya 60 na kule ilikuwa mita 500 kulikuwa na mgogoro wa aina hii.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza awali kwamba ile timu ya Mawaziri ambayo inaratibu migogoro ya kitaifa na kwamba Serikali imeweka utaratibu wa kutatua migogoro kulingana na ukubwa wa migogoro na ngazi ambazo tumezipanga kutoka ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na hatimaye Taifa kupitia timu yetu ya Mawaziri. Mgogoro ambao Mheshimiwa Abood mara kadhaa amekuwa akiusimamia na kuwasemea wananchi wake wa kule Mindu, bado kazi tunaendelea kuifanya na tunashirikiana na Ofisi ya Mkoa ili kuhakikisha mgogoro wa aina hii popote unapotokea ikiwepo na hapo Mindu tunaisimamia kwa karibu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tutakapoona sasa kuna umuhimu wa kuleta timu ya Mawaziri wanane tutawaleta Mheshimiwa Abood pale Mindu ili kukaa na wananchi, kuwaelimisha na kuona namna nzuri ya kuwawezesha kufanya shughuli zao za kijamii ikiwemo na kilimo na hasa eneo lile.
Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Abood swali lake hili ambalo amelizungumza kwa ujumla jumla lakini kwakuwa na mimi nimeshashughulikia tatizo la Mindu pale Morogoro niendelee kumhakikishia kwamba tunashughulikia na tutatatua tatizo lile kwa haraka sana. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imetimiza sera muhimu ya uwekezaji nchini na hasa katika sekta ya madini. Katika kutimiza azima hiyo, wawekeza wamekuwa wakichukua maeneo ya watu maeneo kama kule Kabanga, Sumbawanga na kule Nyamongo, lakini maeneo hayo imechukua muda mwingi sana ama kuchelewa kulipwa au kutokulipwa kabisa fidia za wananchi.
Mheshimiwa Spika, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa kwa muda mrefu na wawekezaji waweze kulipwa fidia yao na waweze kutimiza kupata haki yao ya kukaa katika maeneo hayo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sera yetu, sheria za ardhi pamoja na uwekezaji nchini ziko wazi. Kwamba pale inapotokea mwekezaji yeyote anahitaji kutumia ardhi, ardhi ambayo ina mmiliki halali na shughuliki yake anaifanya, labda kwa kilimo, alijenga nyumba za makazi au uwekezaji kama ulivyosema, pindi ardhi hii inapotakiwa; iwe na Serikali au mwekezaji ni lazima apate fidia.
Mheshimiwa Spika, utaratibu unaotumika, baada ya kuwa mwekezaji ameomba kulitumia eneo hilo, uthamini utafanywa na mthamini wa Serikali, gharama zitapatikana na mhusika wa ile ardhi atahusishwa. Thamani ile ikishapatikana, kama ni Serikali, Serikali italipa, na kama ni mwekezaji atapewa ile gharama ya ule uthamini uliofanywa na atapaswa kulipa.
Mheshimiwa Spika, umetamka maeneo mengi, na mimi nimepata nafasi ya kupita maeneo kadhaa, tumekuta baadhi ya Watanzania waliokuwa wanamiliki ardhi kihalali wametoa ardhi yao kwa shughuli hizo za uwekezaji. Iwe ni kwenye madini au kwa shughuli nyingine yoyote ile ili mradi ni uwekezaji hawa wote wanapaswa kulipwa. Na nitoe wito kwa Wizara ya Ardhi ambayo ndiyo inasimamia sheria, kuhakikisha kwamba Watanzania ambao wanachukuliwa ardhi yao waliyomilikishwa kihalali, ni lazima walipwe fidia ya ardhi yao ili haki iweze kutendeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na ni muhimu sasa pia hata kwa mamlaka za Serikali za Mitaa pale ambako wananchi wapo wamechukuliwa ardhi yao kwa uwekezaji, kwa shughuli nyingine yoyote ile na wanahitaji kulipwa fidia, ni lazima haki yao waipate kwa kulipwa fedha hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba inapotekea kuna madai kama bado madai yatolewe. Na hasa kama kumefanyiwa uthamini basi ile thamani ya ile ardhi au thamani ya ile mali iliyochukuliwa kwa ajili ya kupisha kwa shughuli nyingine ni lazima iweze kulipwa. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kunipa nafasi kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la vituo vya afya na zahanati nchini baada ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa fedha za UVIKO-19. Palipo na mafanikio changamoto hazikosekani. Kumekuwa na uhaba mkubwa wa watumishi wa kada ya afya.
Mheshimiwa Spika, je, ni nini mkakati wa Serikali kukabiliana na changamoto hii?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Mnzava, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba Serikali, na kwa maelekezo ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuboresha huduma za afya Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye maeneo ya kutolea huduma, zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mikoa na hospitali za kanda, lakini pia hospitali kuu kama vile Benjamini Mkapa na maeneo mengine tumepanua maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, tunatambua uwekezaji huu ni mkubwa. Tumeanza na kuweka miundombinu, tumepeleka vifaa na maeneo mengine bado vifaa vinapelekwa, na mimi nimefanya ziara maeneo mengi, nimekuta vituo vya afya, zahanati hata hospitali bado tunaendelea kupeleka vifaa. Hata hivyo, vifaa hivi lazima viende sambamba na watumishi wa kada hii ya afya ambayo umesema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi wakati wa bajeti ya Wizara ya Afya hapa tumepata taarifa kwamba Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan ameshatoa kibali cha ajira, na kibali hiki kiko kwenye sekta za afya, elimu, kilimo, fedha na utawala. Kwa hiyo, tunatarajia baada ya kibali hiki kuwa kimeshakamilika taratibu zake tutapeleka watumishi wa afya kwenye maeneo haya yote mapya ili huduma ianze kutolewa kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niungane na Watanzania wote wanamshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye sekta ya afya. Anataka kuona jamii ya Watanzania ikipata huduma kwenye maeneo yao kwa ukaribu, anataka kuona Watanzania wanatumia gharama ndogo kwa kupata huduma karibu na maeneo yao, na sisi tuendelee kumuunga mkono kama ambavyo tunamuunga mkono na tuamine kwamba mkakati huu wa Serikali wa kupeleka watumishi wa umma utakamilika katika kipindi kifupi sana kijacho. Hii ni kwa sababu tayari fedha ipo (Hapa ilikata) kwa sababu tayari fedha ipo na Waheshimiwa Wabunge mmeridhia. Jukumu letu kuanzia tarehe mwezi wa saba na kutoa fedha na ajira ipatikane na watumishi waanze kazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu inapitia katika wakati mgumu wa kuagiza mafuta ya kula nchi nyingine. Zaidi ya nakisi 250,000 mpaka 300,000 za mafuta ya kula zinaagizwa nchi zingine ambapo tunatumia zaidi bilioni 480 kuagiza nakisi hiyo.
Mheshimiwa Spika, katika kupunguza uagizwaji wa mafuta ya kula, bonde la Tanganyika, kwa maana ya Mikoa ya Rukwa, Kigoma na Katavi, ina ardhi nzuri sana ambayo ikitumiwa vizuri inaweza ikasaidia nchi katika kupunguza nakisi hii. Je, ni nini mkakati wa Serikali katika kuwakaribisha wawekezaji wakubwa ili kuweze kusaidia kupunguza nakisi ya kuagiza mafuta hayo nchini?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Makanika, Mbunge wa Kigoma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Makanika ni shahidi wa jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali sasa za kuhamasisha kilimo cha michikichi ambacho pia kinatoa mazao haya ambayo pia yanakamua mafuta kwa lengo kudhibiti nakisi hiyo tuliyonayo ya upungufu wa mafuta hapa nchini, au kupunguza kiwango cha uagizaji mafuta kutoka nje. Tayari zoezi hilo tumelisimamia vizuri na mimi mwenyewe nimekwenda Kigoma mara kadhaa, nimehamasisha kilimo, tumeanzisha kituo cha utafiti, tumezalisha na mbegu na tumesambaza kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, na sasa tumeanza kupata matumaini. Nimekwenda kwa mara ya mwisho nimekuta michikichi inaanza kuiva, kwa hiyo, tayari sasa kwa jitihada hizi. Lakini chikichi haistawi tu pale Mkoani Kigoma, pamoja na mikoa hiyo ya Katavi na Mpanda lakini na miko yote ambayo inalima zao la nazi inaweza pia kustawisha zao la chikichi.
Mheshimiwa Spika, tunaendelea kuwahamasisha wakulima waliopo maeneo hayo yanayolimwa minazi walime pia na michikichi. Tunaamini kampeni hii ambayo tunaendelea nayo ambayo pia Watanzania wanaopenda kilimo wakiendelea kupanda michikichi tutapunguza nakisi lakini pia tutaokoa na fedha tunazozitumia kuagiza mafuta nje. Sasa nini kinafanyika sasa, kwanza tunahamasisha wakulima wadogo wadogo wenye uwezeo wa kulima eka moja, mbili mpaka kumi, mia. Tunatoa wito kwa wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza nchini Tanzania. Tuna ardhi ya kutosha, hata kule Kigoma tuna ardhi ya kutosha Mpanda tuna ardhi ya kutosha, Katavi tuna ardhi ya kutosha, Sumbawanga nako pia tuna ardhi ya kutosha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunatoa wito kwa wawekezaji kuja nchini Tanzania kuwekeza kwenye kilimo cha michikichi ili tuweze kuzalisha kwa wingi, tukamue na tuweze kupata mafuta yetu sisi wenyewe, na tunaamini gharama itakuwa ndogo na zile fedha ambazo tunapeleka nje kuagiza mafuta hazitakwenda tena na badala yake zitaingia kwenye mzunguko wa uboreshaji wa miradi ya utoaji huduma hapa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba kampeni ile inayoendelea Kigoma bado inaendelea kwa kutoa wito kwa wawekezaji. Ardhi tunayo, na wakuu wa mikoa na wakurugenzi wamepata taarifa; watenge ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
Mheshimiwa Spika, lakini sasa tunaenda kwenye viwanda vya ukamuaji. Kwamba, badala ya ile teknolojia ya kushika miti wanazunguka hivi, ambayo nimeishuhudia kule Kigoma, nataka tubadilishe iwe mashine ili iweze kukamua kwa asilimia angalau 99 ya ukamuaji, badala ya ukamuaji wa sasa wa asilimia 70. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito kwa Watanzania kujitokeza kulima. Mara kadhaa nimesema, kama unataka kuwekeza kwa ajili ya manufaa ya mtoto wako ambaye yuko shule leo lima mchikichi, mpe shamba la mchikichi, mtoto huyo anapomaliza darasa la saba tayari ana shamba lake la eka mbili, tatu, nne, anapokwenda kidato cha kwanza mpaka cha nne anakuta shamba lake lipo, hata anapokwenda chuo kikuu anakuta shamba lake lipo na anaanza kuvuna yeye mwenyewe, na linavunwa lile zaidi ya miaka 30. Kwa hiyo, ni uwekezaji mzuri mkubwa na niendelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nchi nyingi duniani zimerusha satellite angani kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kupata takwimu sahihi za hali ya hewa. Katika anga la Afrika kwa sasa tuna satellite 41 na kati ya hizo 41 mbili zinatoka katika mataifa ya Afrika Mashariki. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanza na programu ya kutengeneza satellite na baadaye tuweze kuirusha katika anga letu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa anahitaji kujua maendeleo ya teknolojia kwenye mawasiliano. Ameeleza kwamba nchi nyingine tayari zimejitegemea katika kununu mitambo inayowezesha nchi husika kuboresha mawasiliano yake. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinaendelea kwa kasi katika maboresho ya TEHAMA, na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kazi moja kubwa aliyoifanya ni kuanzisha Wizara ya Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia ambayo pia ina habari mawasiliano na teknolojia ya habari ambayo pia inaendelea kufanya ufuatiliji wa maeneo ambayo tayari tunayo na maeneo ambayo bado hayapo kwa lengo la kufanya maboresho. Na Wizara, kama ambavyo inaendelea kufanya kazi yake na imeshapitishiwa bajeti yake, na Waziri hapa ameeleza maboresho makubwa yaliyofanywa nchini. Lengo hii teknolojia kufikisha kwa Watanzania mpaka vijijini. Tumeanza na teknolojia ambayo inawezesha kufanya mawasiliano maeneo yote, na tunapanua wigo huu mpaka kwenye ngazi za kimataifa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nikuhakikishie kwamba maeneo yote ambayo nchini sasa hayapo ambayo yanahitajika katika kuboreshwa mfumo mzima wa mawasiliano Serikali itafanya maboresho kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba teknolojia tunaipandisha na teknolojia inawafikia wananchi wote mpaka kule vijiji, ahsante. (Makofi)
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kwa vile nchi yetu ni ya pili katika Afrika kwa uzalishaji wa mifugo na kwa vile ina wafanyabiashara wengi wa mifugo wanaokwenda katika nchi mbalimbali kama vile Kenya, Madagascar na Comoro. Je, Serikali ina mkakati kuimarisha usafirishaji wa mifugo hiyo na bidhaa zake ili kudumisha biashara hiyo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwinyi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia sekta ya mifugo na pia ametaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha usafirishaji, na vile vile amezungumzia masoko. Ni kweli kwamba nchi yetu ina mifugo mingi sana; ina ng’ombe wengi wa kutosha, mbuzi, kondoo na wameingia kwenye soko la kuuza ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa kwenye biashara hii ambapo baadhi ya Watanzania wamejihusisha nayo kwa kusafirisha mifugo hii. Inaweza ikawa wanasafirisha mifugo hai au baada ya kuwa wamepitisha viwandani. Sasa mkakati wa kuboresha usafirishaji, wote tunajua, kuna kazi kubwa tunaifanya ya kuboresha usafirishaji kwa njia ya ndege na sasa tunajenga pia reli ambayo inakwenda mpaka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, tunachokifanya sasa ni kuhakikisha kwamba tunatafuta masoko nje ili kuwezesha kufanya biashara hii na kila mmoja atatumia usafiri ambao anauona ni rahisi kufika kwenye nchi anakohitaji kupeleka mifugo hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inachokifanya sasa, kwanza ni kuhakikisha ufugaji wa ndani unakuwa bora, unaweza kutoa mifugo yenye afya, uwezo na yenye thamani kubwa. Vile vile kazi kubwa tunayoifanya ni kuimarsiha mifugo hii iwe thamani kubwa kuhamasisha wafugaji kufuga kisasa zaidi ili mifugo hii iweze kuwa na thamani. Kwa hiyo, kazi zote ambazo tunazifanya kwa pamoja za kuimarisha ufugaji, ufugaji wa kisasa, kuhakikisha pia tunapeleka viwandani kwa wale wanaotaka kupata nyama au kusafirisha mifugo iliyo hai kupitia njia zetu za usafiri, sisi tumetoa kibali kwa Mtanzania yeyote anayetaka kuingia kwenye uwekezaji huo, afanye hilo ili iweze kumletea tija kwenye shughuli yake ya kila siku ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kutoa wito kwa wafugaji. Jana jioni nilikuwa na wafugaji kama 60 hivi tukizungumza namna bora ya uboreshaji wa mifugo hii. Kwa hiyo, naamini ufugaji kupitia Wizara ambayo imemaliza bajeti yake hapa jana, wataendelea kusikiliza maboresho yaliyotamkwa hapa ili wafugaji sasa waweze kuzalisha mifugo yenye thamani kubwa na usafirishaji upo kama ambavyo Serikali tunafanya ili waweze kutumia huduma hiyo waweze kupata tija zaidi. Huo ndiyo mkakati wa Serikali wa kuimarisha usafirishaji, pia kwenye masoko na ufugaji wa ndani wenye viwango, wenye kuleta faida kwa wafugaji, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa kuna miradi mingi ya miundombinu inayosubiri kutekelezwa kwa bajeti ya Serikali na bajeti ya Serikali; na bajeti ya Serikali imekuwa inatengwa kwa kutumia fedha za ndani na fedha za nje, lakini mfumo huu umeonesha kuchelewesha miradi na hata kupelekea gharama ya miradi kuwa kubwa:-
Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuanza kutumia mfumo wa PPP au mfumo wa EPC plus finance ambao ni mfumo wa Engineering, Procurement na Construction ambao umeonesha mafanikio makubwa sana kwa nchi za Afrika Mashariki na hata SADC ili kupunguza gharama za utekelezaji? Ahsante sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara zake, tunaleta bajeti zetu hapa na Waheshimiwa Wabunge mnapitisha bajeti hizi. Siwezi kusema kwamba bajeti hizo hazitoshi, lakini najua mahitaji ni makubwa, ni kweli tunahitaji fedha nyingi; na baadhi ya miradi tunapoitekeleza mwishoni mwa mwaka, mingine tunakuwa hatuikamilishi kwa sababu ya mwenendo wa makusanyo ambayo tulikuwa tunategemea kukusanya, kiwango hicho cha fedha ambacho tulikiomba hapa Bungeni, kinaweza pia kisitoshe.
Mheshimiwa Spika, iko mifumo mingine ambayo inawezesha pia kukamilisha bajeti zetu tunapopata fedha kutoka nje ya bajeti inayotegemea mapato ya ndani, kwa sababu bajeti zetu zinategemea mapato ya ndani, na pia tuna marafiki zetu wanaongeza mtaji na tunatekeleza majukumu yetu. Hii ndiyo tunafanya kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, sasa tunapokwenda kukusanya na tusifikie malengo, tunatafuta njia nyingine ikiwemo na hiyo ya PPP ambayo kwa muda mrefu tumeitekeleza, lakini imekuwa ngumu kidogo kutekeleza na tumebadilisha na sheria. Leo Mheshimiwa Njeza amependekeza mfumo wa EPC plus finance, najua Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ameizungumzia sana mfumo huo juzi hapa wakati wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu unatafuta mwekezaji ambaye atakuwa tayari kutekeleza mradi wa aina fulani, anautengenezea mchoro wake, tunakaa naye, tunakubaliana naye, tunampa kazi hiyo ya manunuzi, ujenzi; na tunapokwenda kujenga, gharama ya mradi anaitumia yeye, na sisi tunaupokea mradi kwa yeye kuujenga, halafu kuufanyia kazi na wakati mwingine anaweza kuurudisha kwetu tuutumie baada ya kuwa ametumia kwa kipindi fulani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, miundombinu ile inabaki kwetu sisi. BOT (Build, Operate and Transfer System), hiyo inaweza kuwa inaendelea kutumika kwa utaratibu huo. Kwa hiyo, mfumo huo tunaukubali Mheshimiwa Njeza, ushauri wako nakuahidi tunauchukua, ni mfumo mzuri na Waziri wa Ujenzi yupo, Wizara ipo, itatumia mfumo huo na Wizara ya Fedha ipo, itaangalia mwenendo wa mapato yetu, nao ndio wanaoweza kuangalia mfumo huo tunaweza kupata kwa kiasi gani; na kama tunakopeshwa gharama yake ni kiasi gani? Kwa maana hiyo, tutakubali mfumo huo pale ambako tunaweza kupata mkopo huo wenye gharama nafuu ili tuweze kutekeleza miradi yetu.
Mheshimiwa Spika, nataka nimwakikishie Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba ile miradi yetu tuliyoipendekeza kuitekeleza kwenye bajeti hii, hata kama hatutakusanya kwa kiwango cha kutosha, mapato ambayo tunayo, tutatumia mfumo ambao Mheshimiwa Njeza ametupendekezea hapa kwa sasa, ahsante. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, urasimishaji wa makazi yaliyojengwa holela kwenye miji mingi katika nchi yetu ni zoezi ambalo lina gharama kubwa lakini mwisho wake yale makazi hayawi na ubora unaotakiwa hata kufikika na hata kwenye anuani za makazi yana shida kwa sababu barabara na huduma nyingine haziko vizuri:-
Mheshimiwa Spika, ni nini mpango wa Serikali wa kupima maeneo katika maeneo ya Miji, Manispaa pamoja na Majiji na yale maeneo ya pembezoni ili kuhakikisha sasa tunaipanga miji yetu vizuri na huduma zinawafikia wananchi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia suala la upimaji wa ardhi kwenye maeneo yetu ikiwemo na maeneo ya miji ambayo yeye ameeleza. Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango huu ni endelevu ndani ya Wizara yetu ya Ardhi, kuhakikisha kwamba tunapima maeneo yote ya ardhi nchini na kwenye vipimo hivi tunabainisha huduma zote zinazotakiwa kutumika kwenye ardhi hiyo; kwanza makazi, maeneo ya taasisi, maeneo ya huduma za jamii kama vituo vya mabasi na masoko na kila kitu. Huo ndiyo mkakati ambao sasa unaendelea chini ya Wizara ya Ardhi.
Mheshimiwa Spika, sasa nini kinafanyika baada ya kuwa tumekamilisha kupima, tunakabidhi kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ambapo wao ndiyo wanaitunza ile ardhi na kuitumia na kuitoa kwa Watanzania ambao wako kwenye maeneo hayo. Pia hata kwenye mamlaka yenyewe inaweza kuwa inapanga sasa mipango yake. Kwa mfano, pale Moshi Mjini, baada ya kuwa tumeupima ule mji na kupanga matumizi yake, tunawakabishi Manispaa ya Moshi ili waanze kupanga sasa, hapa panatakiwa masoko, hapa vituo vya mabasi, maeneo mengine makazi na kila kitu. Kwa hiyo, mkakati huu ni endelevu na siyo tu kwa maeneo ya miji, tunakwenda sasa mpaka vijijini.
Mheshimiwa Spika, tunataka Watanzania sasa wapate maeneo yaliyopimwa, yanayotambulika rasmi ili pia tuweze kuwapa hati. Ile hati inawasaidia pia kama mtaji wa kukopea kwenye mabenki na taasisi nyingine za fedha. Kwa hiyo, malengo yetu ni endelevu na ni mapana kidogo kwa sababu tunataka kila Mtanzania anufaike na ardhi iliyoko nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naitaka sasa Wizara ya Ardhi kuendelea kukamilisha zoezi hili ili Watanzania wanufaike na ardhi waliyonayo kwenye maeneo yao. Kwa kufanya hivyo, itawezesha pia hata wawekezaji kujua wanapofika wanaambiwa eneo la uwekezaji lile pale, litakuwa limeshapangwa tayari. Kwa hiyo, mnakamilisha kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo pia kuna Afisa wetu wa Ardhi. Hhii sera ni endelevu na itakuwa na msaada mkubwa kwa Watanzania, ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwa na ongezeko la wanyama wakali hasa tembo ambao wamekuwa wakivamia maeneo ambayo yako mbezoni mwa Hifadhi za Taifa, lakini pia na mapori tengefu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu wanyama hawa kwa nyakati tofauti wamekuwa wakiathiri shughuli za kijamii, kiuchumi lakini pia wakati mwingine kusababisha hata vifo.
Mheshimiwa Waziri Mkuu suala la ulinzi wa mali na usalama wa raia ni jukumu la Serikali. Je, ni kwa kiasi gani Serikali itawahakikishia wananchi hawa walioko pembezoni mwa hifadhi hizi usalama wao ili wasiendelee kupata athari zinazosababishwa na wanyama hao? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nimeona nilijibu hili swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge kutoka Lushoto kwa sababu pia nimefanya ziara maeneo mengi na nimekuwa nikilalamikiwa na Watanzania wanaoishi kwenye maeneo yaliyo kando kando na maeneo ya hifadhi kwa maslahi ya Taifa.
Nikubaliane naye kwamba Serikali inao wajibu wa kulinda mali lakini pia usalama wa raia ndani ya nchi. Pia nikiri kwamba tuna ongezeko kubwa la wanyamapori hasa baada ya kuwa tumeimarisha ulinzi kwa maana ya uvamizi, uwindaji haramu, kwa hiyo wanyama wengi wameongezeka na tembo nao pia wameongezeka sana.
Mheshimiwa Spika, huu mjadala huu nimeusikia sana pia hapa Waheshimiwa Wabunge wakichangia wakati wa bajeti ya Maliasili na Mheshimiwa Waziri amejitahidi kueleza namna Serikali inavyojitahidi kudhibiti wanyamapori wanaoingia kwenye maeneo ya makazi ya watu, lakini mashamba na kusababisha pia upotevu, uharibifu wa mali pia hata vifo kwa baadhi ya Watanzania ambao wako karibu sana na maeneo haya ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, ziko jitihada za Serikali zinafanyika sasa za kuhakikisha kwamba tunapunguza au kuondoa kabisa madhara haya kwa yale maeneo yaliyo pembezoni ikiwemo kwenye Jimbo la Mlalo anakotoka Mheshimiwa Shangazi ambalo linakaribiana sana na Mbuga ya Mkomazi.
Mheshimiwa Spika, na ziko Wilaya kadhaa, nimeenda Liwale, Mkoani Lindi, nimefanya ziara Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi na hata Lindi Vijijini pia. Nimefanya ziara Mkoani Ruvuma maeneo ya Tunduru Jimboni kwa Mheshimwia Mpakate. Nimefanya ziara pia Meatu, Bariadi maeneo ambayo yamekaribiana sana na Mbuga wa Serengeti pia hata Wilaya ya Serengeti kote huko nimepita na moja kati ya vilio vya Watanzania ni ongezeko la Tembo ambao pia wanakuja hapa. Na kwenye mjadala hapa nilimsikia hata Mheshimiwa Mulugo akirejea misahafu na biblia juu ya jambo hili. (Makofi)
Sasa jitihada ambazo tumezifanya ni kwanza tumeongeza idadi ya askari wa wanyamapori na askari hawa tunawapeleka kwenye maeneo yote yaliyo karibu na makazi ya watu kwenye mbuga hizi ambazo ziko karibu na watu.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumeimarisha na tunaendelea kujenga amary ya hivyo vituo ambavyo vinatunza silaha ambazo zitasaidia pia angalau kuwaondoa hawa tembo warudi kwenye maeneo yao. Na sasa hivi Wizara inaendelea kuratibu ujenzi wa vituo vile 32 kando kando ya maeneo yote haya. Hata nilipokuwa Mkoani Lindi, eneo la Rondo zamani ilikuwa ni Kituo cha Maliasili ambao walikuwa wanasaidia sana kupunguza idadi ya wanyama hatari wanaoingia kwenye makazi ya watu kwa Wilaya za Lindi Vijijini, lakini pia Kilwa maeneo ya Kilanjelanje na maeneo mengine. Kwa hiyo tunarudisha vile vituo uhai wake ili tupeleke hawa askari ambao tunawapeleka kwenye maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanyama tembo pamoja na ongezeko lake Serikali haikusudii kuvuna, lakini kusudio hasa na ndio kazi kubwa tuliyonayo ni kuzuia wanyamapori kuingia kwenye makazi. Tembo yuko kwenye kundi la top five ya wanyama ambao wenyewe kazi yetu ni kuhifadhi kama sehemu ya nyara za Taifa. Tembo wenyewe, tuna simba, tuna twiga, chui na faru hawa wako kwenye top five ambao Serikali kwa namna yoyote ile itaendelea kuwahifadhi waendelee kuwa ni tunu ya Taifa letu. (Makofi)
Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wote wanaoishi kwenye maeneo ya pembezoni mwa mbuga ambao wameendelea kupata tatizo la tembo kwamba mkakati wa Serikali wa kuongeza askari wengi watakaokaa kwenye maeneo hayo na wakafanya kazi hiyo na tumewakabidhi TAWA wasimamie kwa kina wahakikishe kwamba madhara haya hayajitokezi tena.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutaendelea kufanya tathmini kadri tunavyoendelea ili kupunguza athari hiyo na Mheshimiwa Shangazi eneo lile mimi nimefanya ziara Wilayani Same kwa Mheshimiwa Kilango, lakini pia nilikuja mpaka mpakani mwa vijiji vyako nimeona hiyo na nimepata malalamiko hayo. Kwa hiyo, tutaendelea kudhibiti maeneo yale ya vijiji vyako vile ambavyo tembo wanaingia kwako kutoka Mkomanzi ili wananchi waweze kuishi kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niliona nilijibu hili nifafanue niwahakikishie Watanzania kwamba Serikali inaimarisha mifumo ya kuzuia madhara haya kwa kuhakikisha tunaongeza askari wanaoweza kusaidia kuwazuia tembo wasiingie kwenye makazi ya watu. Tathmini itatuonesha zaidi nini tufanye baada ya zoezi la awali tunalotekeleza sasa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu, na nitambue dhamira ya Serikali katika kuhakikisha kuna usalama wa hali ya juu kwa wananchi wanaosafiri kwenye maziwa makuu kama Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika. (Makofi)
Vilevile wananchi wamekushuhudia Mheshimiwa Waziri Mkuu namna unavyosimamia ujenzi wa meli kwenye Ziwa Victoria, lakini kwa bahati mbaya katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa wananchi wamekuwa kwa muda mrefu wanatumia usafiri wa jadi kama mitumbwi na maboti, na maziwa haya yana mawimbi makali sana na eneo hili ni nyeti sana kwa kukuza diplomasia ya kiuchumi na biashara kati ya nchi jirani na Malawi na kwa Ziwa Tanganyika, meli MV-Liemba inasemekana ililetwa na wakoloni mwaka 1905.
Sasa je, nini mkakati wa Serikali kisera na kisheria kuhakikisha kwamba wananchi wanaosafiri kwenye Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa wanapewa usafiri ambao ni mzuri ambao utalinda usalama wao, lakini kuuza biashara kati ya Tanzania, DRC, Burundi, Congo na nchi jirani ya Malawi? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kamonga, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, najua swali lilikuwa refu, lakini anataka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba tunapeleka usafiri kwenye maeneo haya ya maziwa haya matatu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ili kuwawezesha Watanzania wanaoishi hapo kutumia fursa zilizopo za kibiashara katika kuongeza uchumi wao.
Mheshimiwa Spika, ziko jitihada zinaendelea za kuhakikisha kwamba maeneo haya ya maziwa hata bahari kuu tunaimarisha usafiri ambao utawezesha pia Watanzania na ndugu zetu walioko majirani kufanya biashara zao na kujiongezea kipato kwa kusafirisha biashara pia na uvuvi kwenye maeneo haya.
Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi, jitihada ziko zinaendelea za ujenzi wa meli Ziwa Victoria na hivi karibuni mwanzoni mwa mwaka huu Mheshimiwa Rais alikuwa Mkoani Mwanza kushuhudia kutia sahini wa ujenzi wa meli za Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Pia Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi imeshafanya kazi kubwa ya kukarabati meli na vivuko kwenye maeneo yote matatu hayo, Victoria, Tanganyika pamoja na Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri nimefanya ziara maeneo yote haya. Mbali ya ujenzi wa meli ambazo zinaendelea kujengwa na kukarabatiwa Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa pia tunaimarisha na bandari zake. Ziwa Victoria tumeimarisha bandari mkoani Mara na bandari zake zote mpaka Bunda, Kisorya, lakini pia Mwanza, Geita na Kagera, na kule Mkoani Kigoma mimi pia nimetembelea Kibirizi, nimeenda pia Kabunga ambako tulishajenga bandari na haikutumika kwa muda mrefu, lakini nimeenda Kabwe, Kasanga kule Rukwa kuona bandari hizi, na bandari kubwa tunaijenga pale Karemie Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi hizi ni jitihada kubwa.
Mheshimiwa Spika, hat akule Ziwa Nyasa, bandari ya Itungi imeimarishwa sana na mimi pia nimeenda kuzindua na meli, kwanza kukagua ujenzi wake, lakini nimezindua na meli kule Wilayani Mbambabay. (Makofi)
Kwa hiyo, jitihada zote hizi malengo yetu ni kufikia azma ambayo Mheshimiwa Mbunge hapa ameieleza ya kuimarisha usafirishaji na kuwawezesha Watanzania kutumia fursa hiyo kufanya biashara na nchi jirani. Na tunaendelea pia kushirikiana na nchi jirani nao kama wana meli tunaziruhusu kuingia. Kwa hiyo, tunataka tutengeneze network ambayo itaendelea kupanua wigo wa kufanya biashara na kuingiliana kwenye maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jitihada hizi zitaendelea na tutakapoanza kuimarisha ujenzi wa meli hizo tutafanya biashara. Lakini bahari kuu pia nako miongoni mwa zabuni zilizotangazwa ni ujenzi wa meli yenye uwezo wa tani kuanzia 3,000 mpaka 3,500 ambayo itakuwa inasafirisha abiria, mizigo na shughuli za kibiashara kati ya Zanzibar na Bara, lakini tunataka twende mpaka Comoro. Ujenzi huu utakapokamilika kutakuwa na usafiri wa ndani tutapita mpaka Mafia pia. Malengo ni kuimarisha fursa za Watanzania kufanya biashara kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwahakikishie Watanzania kwamba tutaendelea kuimarisha njia za usafirishaji kwenye maziwa, lakini pia na nchi kavu ili kutoa fursa kwa Watanzania wanaotaka kufanya biashara, wanaotaka kufanya utalii kwa nchi jirani waweze kwenda, lakini nchi jirani kuja kuingia nchini. Kwa hili tunaendelea kulifanyia kazi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu sera ya Serikali ya kuwa na shule ya sekondari kila kata imefanyika vizuri na imekuwa na mafanikio, na nia yake ni kuhakikisha watoto wote ambao wanastahili kwenda sekondari wanakwenda, lakini kupunguza umbali ambao Watoto/wanafunzi walikuwa wanatembea na wakawa wanapata tabu kidogo, lakini zaidi kupunguza pia gharama ya nauli kwa wazazi ambao walikuwa na watoto wale wa sekondari. Sasa mafanikio hayo yamepelekea kwamba watoto wale wanaofaulu form four sasa wanapangiwa shule mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, sasa kumekuwa na wimbi kubwa la kupangiwa shule za mbali mtoto anatoka Mtwara kwa mfano anapangiwa Kagera, anatoka Kilimanjaro anapangiwa Kigoma, sasa ile gharama ya nauli ile imekuwa kidogo inakuwa nzito kwa wazazi, lakini pia usalama wa wale watoto. Najua zamani kulikuwa kuna utaratibu wa kuwasafirisha kwa treni kabla ya kipindi ambacho nimesoma mimi.
Sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu, swali langu ni nini mkakati wa Serikali, aidha kwa kuwapangia shule za karibu au kutafuta namna nzuri zaidi ya kuwasafirisha wanafunzi hawa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tarimo, Mbunge wa Manispaa ya Moshi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza mkakati wa ujenzi wa shule za sekondari kila kata nchini kuanzia mwaka 2006 kwa lengo la kuwezesha watoto wanaotoka kwenye kata hiyo wasome eneo lililo karibu ili kupunguza gharama pia usumbufu. Zoezi hili limeendelea vizuri na leo hii angalau kila Wilaya au Halmashauri tumefikia ujenzi wa zaidi ya asilimia 95 wa shule za kata kwenye maeneo yake na kazi hiyo inaendelea kwa malengo yale yale ya kupunguza gharama za wazazi kuwasomesha Watoto, lakini hao watoto wenyewe kuwapunguzia usumbufu wa kutembea umbali mrefu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua Serikali ina mkakati gani wa mpango wetu wa kuwasomesha watoto shule za mbali.
Sasa kwenye sekondari huku tuna kidato cha kwanza mpaka cha nne, lakini kuna kidato cha tano mpaka cha sita. Wanaosoma mbali ambao tunaweza kuwatoa Dodoma kuwapeleka Kagera, Lindi na maeneo mengine ni wa kidato cha tano na sita. Sisi tuliona Serikali kwamba ni muhimu pia Watanzania hawa wakatambua pia jiografia ya nchi yao, lakini pia tukaimarisha uzalendo, pia waweze kujua jiografia ya maeneo mengine na waweze kuingiliana na makabila mengine. Kwa sababu Tanzania ya leo hatuna suala la udini, ukabila wala rangi kwa sababu Watanzania tunaingiliana tulitaka tulidumishe hilo, na kwenye elimu ya sekondari tunalifanya sana kwenye kidato cha tano na sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa suala la usumbufu kwa kuwa Serikali imesema kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne wanasoma bure, tunaamini mzazi tunampa nafasi ya kujiandaa kwa mtoto wake kwenda kidato cha tano popote atakapopangiwa nchini ili kumuimarisha vizuri kitaaluma na aweze kuendelea vizuri kwa kufahamu jiografia ya nchi yake na namna nyingine yoyote ambayo tunaweza kujifunza kwa utaratibu huo. Na huko atakakokwenda tunajitahidi pia kupunguza gharama zake, shule yoyote ya kidato cha tano na cha sita ni zile shule ambazo zinagharamiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali halafu kiasi kidogo wananchi wanachangia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumeendelea kumpungia mzigo wa kuchangia elimu kwa mtoto wa kidato cha tano na cha sita. Kwenye sekondari kidato cha tano wanalipa shilingi 70,000 lakini gharama zake ni kubwa na Serikali inapeleka chakula na huduma nyingine. Kwa hiyo, haya yote yanalenga kukuza ule utamaduni ambao tuliujenga kutoka Serikali ya Awamu ya Kwanza ambayo ilikuwa imeimarisha sana watanzania kuondoa watu kukaa eneo moja na kujigawa kuwa ndio wako sehemu moja ili kila mmoja aweze kufahamu maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri, lakini tunaendelea kuangalia namna bora ya kuwapunguzia mzigo wazazi kwenye upatikanaji wa elimu na tutakuwa tunafanya maboresho kadri tunavyoendelea, kama ambavyo Wizara ya Elimu sasa inaendesha mjadala wa mtaala haya yote yatakuwa yanaingia kwenye mtaala na kuona namna bora ya kuendesha elimu na namna nzuri ya kuwapunguzia gharama wazazi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii leo kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu maswali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi nyingi duniani zimeanza kuachana na mpango mzima wa kutumia pembejeo, viatilifu, madawa makali ya viwandani kwa kilimo na zinajikita zaidi katika kilimo hai.
Mheshimiwa Waziri Mkuu nchi yetu bado inakuwa soko la mbolea, viatilifu, dawa za viwandani ambazo si nzuri kwa afya na ubora wa ardhi yetu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna viatilifu 24 ambavyo vimeshapigwa marufuku duania kwamba vinasababisha kansa na kuharibu uzazi, lakini bado vinaendelea kutumika Tanzania yetu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi kama Ufaransa tayari ina Wizara nzima inashughulikia kilimo hai na Uganda jirani yetu ana sera; je, Serikali haioni sasa kwamba ni muda muafaka wa kuanzisha walau idara maalum ya kushughulikia kilimo hai na kunusuru afya za wananchi wake na kuboresha ardhi yetu na vilevile kupanua soko la bidhaa za kilimo hai ambazo ina bei kubwa duniani na hasa kwa vile Tanzania tuna nchi ya kutosha na friendly kwa ajili ya shughuli hizo za kilimo hai na kuwapa msukumo vinara wa kilimo hai? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Mshua, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua mpango wa Serikali wa kuanzisha idara maalum inayojikita na utafiti au kilimo hai. Ni kweli kwamba Serikali imeendelea kuhamasisha wakulima kwenda na kilimo hai. Kilimo hai hakihitaji mbolea za kemikali na tumeona mafanikio makubwa kwa wakulima ambao wanalima kilimo hai kwenye mazao kadhaa. Wiki mbili, tatu zilizopita nilikuwa mkoani Kagera ambako tulikuwa tunahamasisha kilimo cha kahawa na tulikuta wakulima wa makindi mawili wale ambao wanalima kilimo kinachohitaji pembejeo zilizotoka kwenye viwanda, lakini wako ambao wanalima kahawa wanatumia pembejeo ambazo zinatokana na mimea yetu ya asili ambayo bado tunaendelea nayo kama vile samadi, mboji na vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumeanza mpango wa kuimarisha kilimo hiki pale ambako tumeunda taasisi tunaita TPRI iko pale Arusha ambayo inapima viatilifu vyote vinavyoingia nchini kwa ubora wake kulingana na ardhi tuliyonayo ndani ya nchi. Kwa sababu matumizi ya mbolea yanategemea na ardhi tuliyonayo na hasa zile mbolea za kemikali ili kuzuia uharibifu wa ardhi tuliyonayo.
Kwa hiyo, tunaendelea na mkakati huo na kuwawezesha na kuwahamasisha wakulima kulima kilimo hai na tunawashauri ni aina gani ya mbolea inahitaji kutumia kilimo hicho na tunaweza kuona pia faida kwamba ukilima kilimo hai cha kahawa unapata bei kubwa zaidi kuliko kilimo kinachotumia mbolea za kemikali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumeendelea kuhamasisha hilo na taasisi yetu ya TPRI inaendelea kutoa mafunzo, lakini tunaanzisha kitengo maalum, kurugenzi maalum ndani ya Wizara ya Kilimo kusimamia hamasa ya kilimo hai kwenye mazao kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote na wananchi ambao wanashughulika na kilimo kwamba wale wanaotaka kulima kilimo hai hii ni fursa sasa na tunaendelea kuwaambia aina gani ya mbolea inayotokana na mazao mbalimbali tukiozesha na kuweza kutumia mbolea hizo wakapata bei nzuri.
Nimepata nafasi ya kwenda Busokelo kwenye zao la Kokoa nako pia kuna wakulima wanalima kilimo hai na wanapata bei nzuri tu. Tumeenda pia hata kwenye chai tumeona watu wanalima kilimo hai wanapata bei nzuri tu. Kwa hiyo, kilimo hai kina tija zaidi kuliko kulima mazao yanayohitaji hizi mbolea za kemikali.
Kwa hiyo, hamasa hiyo inaendelea na tutaendelea kuwafikia wakulima na Wizara sasa imeimarisha kupeleka Maafisa Ugani mpaka Wilayani na moja ya jukumu lao ni kuhamasisha wakulima kulima kilimo hai lakini kuwaonyesha ni aina gani ya viatilifu ambavyo vinaweza kuwasaidia wao kukuza zao lao kwa kilimo hai, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tunatambua kwamba vijana ambao wanakuwa wamemaliza kidato cha sita na wengine wanawajibika kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa ili kuweza kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha lakini cha zaidi utayari wa kulitumikia Taifa.
Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Juni kuna wito umetolewa na JKT kuwaita vijana waliomaliza kidato cha sita kujiunga na JKT, lakini umeambatana na orodha ya mahitaji mengi sana ambayo wanatakiwa waende nayo. Tunatambua kwamba ni muhimu sana vijana hawa kujiunga na JKT na hapo zamani ilikuwa ikitolewa na vijana wanaenda kuripoti kambini vifaa vyote vinatolewa kule kambini.
Sasa nilitaka tu kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni kwa nini sasa Serikali isione kwamba ni muhimu kuwajengea uwezo hawa vijana ili tuweze kuwaacha wale vijana ambao wanatoka kwenye kaya maskini iweze kutoa vifaa hivi kama ilivyokuwa ikitoa hapo zamani? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa wito kwa vijana wetu kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa malengo ambayo Mbunge ameeleza kujenga uzalendo, kumjengea uwezo wa kujiamini ili pia kushiriki katika ulinzi wa Taifa lake na tunapofanya hili tunawapeleka kwenye makambi yetu.
Mheshimiwa Spika, Mbunge akitaka kujua kwa nini sasa tunapowaita tunaambatisha na orodha ndefu ya vifaa vinavyotakiwa jeshini. Serikali tumejipanga na tumeandaa utaratibu wa kuwahudumia hawa na vifaa vilivyo muhimu vya shughuli ile ya kijeshi kama bukta, viatu pamoja na sare yenyewe zile ambazo zinatumika kwenye shughuli yenyewe ya mazoezi na uimara na ukakamavu.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali tumetoa nafasi ya watu kuja na vifaa ambavyo tunaweza kuvitumia viko vifaa ambavyo tumewaambia kwamba ukija kwenye eneo hili unatakiwa kuja na moja, mbili, tatu, nne ili uweze kuishi kwenye maeneo haya. Lakini vile vifaa muhimu vyote vinapatikana kwenye eneo lile la ulinzi.
Kwa hiyo, tofauti ya vifaa vile vinavyoagizwa na vile ambavyo vipo ni kwamba vilivyopo ni muhimu kwa mazoezi lakini kuna vile ambavyo vina-support wakati wote kijana huyu akiwa jeshini navyo pia anaweza kujitafutia ndio tunaorodheshea kwamba wanapokuja Makutupora uje na hiki na hiki kulingana na mazingira hayo.
Mheshimiwa Spika, hata sisi tulipokuwa jeshi wakati ule tuliagizwa na tulienda navyo na tulipata vifaa vingine jeshini. Kwa hiyo, ni utaratibu wa kawaida kuagiza vifaa muhimu vya jeshi ambavyo vinapatikana pale pale jeshini, lakini vile ambavyo ni muhimu kwa kuishi kwenye eneo lile basi tunakuagiza uweze kuja navyo ili uweze kuvitumia.
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kutoa majibu hayo. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza nikupongeze sana kwa wasilisho zuri ambalo kwa kweli limekuja wakati muafaka katika kusimamia tasnia nzima ya Sekta ya Elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametaja wadau muhimu katika ushirika huu, lakini hadi hivi ninavyozungumza hakuna chombo maalum kinachoisimamia Sekta Binafsi ya Elimu, hivyo kuwa na sauti ya pamoja pale inapotimiza majukumu yake ya kutoa elimu. Tutakumbuka kwamba shule za Serikali zipo chini ya TAMISEMI na zinapokea miongozo yote kutoka TAMISEMI, lakini Shule za Sekta Binafsi na Vyuo vya Sekta Binafsi na vya Kidini hawa hawana chombo ambacho kinawaunganisha kwa pamoja. Sasa nataka tu kufahamu kwamba ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba sekta hii nayo inakuwa na chombo ambacho inaweza ikakisimamia? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sera yetu ya Elimu imetoa nafasi kutekelezwa kupitia Sekta ya Umma ambayo ni ya Serikali, lakini pia Sekta Binafsi na ndio kwa sababu leo Taasisi za Kidini zimeanzisha shule za msingi, sekondari hata vyuo, mtu mmoja mmoja ameweza kuanzisha shule ya msingi, sekondari na vyuo na wote hawa wako kwenye utekelezaji wa Sera ya Elimu kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, sasa suala la chombo kwa Sera ya Elimu inavyotekeleza, Wizara ya Elimu ndio msimamizi wa sera na yeye ndio anayeshughulikia na udhibiti ubora wa elimu hapa nchini wakati usimamizi wa shughuli za kila siku kwa shule za msingi na sekondari inafanywa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hiyo matatizo yote na shughuli zote za Elimu ya msingi na sekondari zinasimamiwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Wanapofanya hivi pamoja na Sekta ya Elimu ambayo inatambua Sekta Binafsi ambayo inafanya kazi ya kutoa elimu nchini inaingia kwenye utaratibu huo huo. Watatekeleza sera ya nchi, lakini pia watakaguliwa kwa mifumo iliyopo nchini, lakini utendaji wa kila siku utaendelea kufuatiliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa sababu shule zote za msingi na sekondari za sekta binafsi ziko kwenye Halmashauri husika na msimamizi ni Mkurugenzi wa Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mkurugenzi na Idara yake ya Elimu wataendelea kufuatilia mwenendo wa utoaji elimu nchini kupitia Idara ya Elimu watakwenda kwenye shule za sekta ya umma za Serikali watakwenda na kwenye shule za sekta binafsi ili kuona kuwa mwenendo wa utoaji wa elimu unakuwa mmoja na ndio kwa sababu wanafuata ratiba ya Serikali hata Sekta Binafsi, wanafanya mitihani ya Serikali chini ya Baraza la Mitihani pia ni pamoja na Sekta Binafsi.
Mheshimiwa Spika, hii sasa inaweza wakajua sasa sekta binafsi kwamba wanawajibika kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika. Suala la kuwa na chombo maalum cha sekta binafsi kwa kuwa tumesema shule za msingi, sekondari zote zinawajibika kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa hicho ndio Chombo chao ambacho inatakiwa kuripoti matatizo yao, mafanikio yao na kama kuna changamoto nyingine zozote zile wataripoti kwa Wakurugenzi wa Halmashauri. Shule hizo za Binafsi zinakaguliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia chombo cha Wizara ya Elimu cha Udhibiti Ubora tulichokipeleka kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, hii inafanya uendeshaji wa elimu kwa ujumla wake kuwa hauna matatizo na tumewaruhusu pia Sekta Binafsi kuanzisha umoja wao, watajadili mafanikio yao, watajadili mapungufu yao na watapeleka kwenye ngazi husika za Serikali pale ambapo wanaona kuna umuhimu wa kushirikiana na Serikali. Kwenye maboresho ya Sera hii ambayo leo tunaisoma hapa na kwamba tumeshakamilisha, tunasubiri kuzindua. Sekta Binafsi wameshirikishwa kikamilifu na waliitwa wote hapa Dodoma wamezungumza kwa pamoja, wamekubaliana, wamerudi wakiwa wameridhika na naamini wako Waheshimiwa Wabunge hapa nao wamejikita kwenye utoaji wa elimu na wao pia wanajua kwamba walishirikishwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie wadau wote wa utoaji elimu kwa Umma kwamba Sera yetu inalenga kufanya maboresho makubwa. Dhamira ya Rais wetu katika kuanzisha mchakato huu, lakini michango ya Waheshimiwa Wabunge imepelekea kukamilika kwa Sera hii na Wadau wa Sekta Binafsi ambao wamechangia, yote inapelekea kwenda kuimarisha Sera hii na iweze kutekelezeka. Kwa hiyo wajibu wetu sasa ni kuipokea na kuanza maandalizi ya kutekeleza Sera hii. Hayo ndio majibu ya msingi. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza nikupongeze sana kwa Serikali kukamilisha mchakato huu na leo kutuletea rasmi kwamba nchi yetu inakwenda kutekeleza Sera na Mtaala Mpya, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu katika maelezo yako umeeleza kwamba Mtaala huu unakwenda kujikita katika Elimu ya Ujuzi. Hata hivyo, tuna upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia katika level zote primary, secondary na Elimu ya kati kwa maana ya vyuo vya kati.
Je, Serikali inajipanga vipi kwenda kuhakikisha kwamba tunapata Makarakana na vifaa vya kufundishia vya kutosha ili kuweza kutekeleza mtaala huu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tumeeleza kwamba elimu sasa isiwe ya kitaaluma pekee bali iingize masuala ya ujuzi kwa lengo la wanaomaliza elimu ya msingi hii ambayo imeenda mpaka kwenye sekondari ngazi ya chini, wanapomaliza wawe wana ujuzi ambao wanaweza wakaanza pia kuingia kwenye ujasiriamali moja kwa moja. Sasa Serikali imejipangje kupata vifaa vya kufundishia, tumeeleza kwenye Sera na kwa kuwa Sera itatekelezeka mwaka 2027, bado Serikali itaendelea kutafuta uwezo wa kuanza kununua vifaa na kupeleka kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, sisi sasa tumeanza ujenzi wa VETA, Vyuo vya Ufundi, lakini pia tuna Vyuo vya Wananchi (FDCs) ambavyo pia vyenyewe vinatoa elimu ya ujuzi. Kwa hiyo kwa kipindi hiki cha mpito tunaanza kuimarisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Vyuo vyetu vya VETA ambavyo wanajenga kila Wilaya kwa lengo la kuanza kutoa ujuzi huku tukijipanga kutafuta vifaa na kupeleka kwenye shule zetu za sekondari. Kama Sera inavyosema mafunzo ya mali na ufundi tutaanza na kidato cha kwanza. Kwa hiyo tuta-concentrate, tutaongeza nguvu katika kutoa vifaa na hasa katika kuongeza bajeti na tutaleta maombi yetu hapa kwenu Waheshimiwa Wabunge, naomba mridhie bajeti zetu ili tuweze kununua vifaa tupeleke sekondari na tutafanya hivyo awamu kwa awamu ili tufikie malengo ambayo tunayakusudia. Hii ndio namna ambayo tunakusudia kuitekeleza ili tuweze kufikia mafanikio, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba hatimaye imehuishwa Sera ya Elimu ambayo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 lakini mpaka inahuishwa tena haikuwahi kutekelezwa kwa sababu ilikosa nguvu ya sheria. Sasa kwa mahuisho haya yaliyofanyika sasa hivi, je, Serikali imejipanga lini kuleta Sheria ya Elimu mpya Bungeni ili kuyapa nguvu haya mahuisho ambayo yamefanyika?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli hata Sera ya mwanzo tulipokuwa tunatekeleza tulikuwa na Sheria inasaidia, inaongoza utekelezaji wake, lakini kutokana na mabadiliko haya tumegusa maeneo yanayohitaji mabadiliko ya kisheria pia ili Sera hii iweze kutekelezeka; na kwa kuwa tunaelekea kwenda kuizindua na Wizara ya Elimu inaendelea na mchakato wa kusimamia maboresho ya Sera hii mpaka kuzinduliwa na utekelezaji wake, tutaendelea kubaini maeneo muhimu ya kubadilisha Sheria ili tuweze kutunga Kanuni ili ziweze kuwezesha urahisi wa utekelezaji wa Sera hii. Kwa hiyo Wizara ya Elimu imejipanga, inaendelea na mchakato na nimetoa wito hapa na nimeeleza kwamba, bado tunaendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali, kushirikisha wadau wote. Kwa hiyo hii hatua tunayoendelea nayo ya kila hatua itakuwa inabaini kadiri ya mahitaji ya mabadiliko ya sheria na kutengenezea kanuni za usimamizi wa utekelezaji wa sera hiyo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Waziri Mkuu swali la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri mmefanya kazi kubwa sana kupunguza miaka kutoka 11 sasa na kuwa 10 kwa maana ya miaka sita na miaka ile minne ya lazima, lakini kuna mzigo mkubwa sana wa masomo mengi kwa watoto wa shule za awali. Je, kuna utaratibu gani ambao Serikali imeuona wa kupunguza idadi ya masomo lakini quality ikabaki palepale? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge wa Mbeya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu ilipokuwa inatekeleza Sera hii ambayo tunaimalizia muda wake iliaandaa masomo kulingana na uhitaji. Sasa mabadiliko ya sera hii nayo yataangalia mzigo huo na kwa kuwa wadau walishapata nafasi ya kuchangia tunaamini hili nalo walishalisema na Wizara ya Elimu imechukua maoni yote yaliyotolewa na wadau katika kuhakikisha kuwa mzigo huu unapungua na utaratibu ambao upo kwa madarasa ya awali yanayomwandaa mwanafunzi kuingia darasa la kwanza wale masomo yao ni kusoma, kuhesabu na kuandika.
Mheshimiwa Spika, walikuwa wanaandaliwa hivyo kwa kipindi chote cha mwaka mmoja au miwili kulingana na umri wa mtoto. Wanamwandaa kujua kuandika, kusoma na kuhesabu ili aingie darasa la kwanza akiwa anajua kuhesabu, kuandika na kusoma na anapoingia kwa darasa la kwanza, la pili anaanza sasa kuingia masomo ya shule za msingi. Hapa sasa sera na michango ya wadau watakuwa wameshapitia hayo na ushauri upo Wizara ya Elimu, kuona ni masomo yapi yafundishwe kutoka darasa la kwanza mpaka la sita na pia yataangalia uzito na umuhimu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa sasa tunawaandaa kwa ajili ya kuingia kwenye mafunzo ya sekondari, lazima watafanya mapitio tena ya masomo haya ili kutoa idadi ya masomo ambayo yataweza kubebwa na kijana huyu wa umri huu ambaye anasoma mpaka darasa la sita ili kumfanya awe na uelewa mpana na wa haraka zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi inavyojitahidi kuboresha elimu nchini, hongereni sana. Nina swali dogo tu, Serikali sasa mtuambie mna mkakati gani wa kuweza kutosheleza walimu wenye weledi kufundisha masomo haya ya amali ukichukulia tuna upungufu wa walimu nchini?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly Ntate, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri kwamba tunao upungufu wa Walimu kwenye shule zetu kwa ngazi mbalimbali na hii inatokana na kuwepo kwa Walimu wanaostaafu, wanaotangulia mbele za haki na wagonjwa ambapo tunajua yapo mapengo ya ufundishaji hasa kwenye eneo hili la elimu ya amali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali kwenye mpango huu ni kuhakikisha kwanza, tunaendelea kupokea vibali vya ajira kama ambavyo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyotoa vibali vya kuajiri walimu, miongoni mwa Walimu ambao tunawaajiri hasa tunaangalia zaidi kwenye eneo hili la elimu ya amali ili kuwezesha utekelezwaji mzuri wa Sera hii mpya inayogusa kwenye maeneo ya amali ili kuwezesha ufundishaji na wanafunzi waweze kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati wetu ni kuongeza ajira kwenye sekta ya elimu ili kuwa na walimu wa kutosha, ahsante. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniruhusu kuuliza swali moja. Tumekuwa na tatizo sugu la upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi katika Shule za Sekondari na huu wimbo umekuwa wa muda mrefu sana: Je, ni nini sasa mkakati wa kudumu wa Serikali, kuondoa upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi katika shule za Sekondari?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Baba Askofu, Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vilevile tunao upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kwenye Shule zetu za Sekondari. Tunapoelekea kutekeleza Sera hii mpya ya Elimu, eneo hili tumeliangalia. Tumeanza kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi kutoka Shule za Msingi na kuelekea Sekondari na kuhakikisha kuwa tunapata wafaulu ambao pia na wao tunawapeleka kwenye Vyuo vya Ualimu ili kupata taaluma ya ufundishaji wa masomo ya sayansi tuweze kupata walimu ambao watakuja kufundisha tena elimu hii kuanzia ngazi zote za msingi na sekondari ili tuweze kuongeza idadi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa, mkakati uliopo ni ule ambao nimeueleza awali kwamba kupitia vibali tunavyopata kutoka kwa Ofisi ya Rais, tunatoa nafasi zaidi ya ajira za walimu wa masomo ya sayansi. Kwa mfano, ajira ya mwisho ya walimu 4,000, nafasi 2,500 zilikuwa za walimu wa masomo ya sayansi na nafasi 1,500 zilikuwa za walimu wa masomo ya Arts. Kwa hiyo, hii ilikuwa inatoa mwanya kwa mwalimu yeyote aliyehitimu mafunzo ya ualimu wa masomo ya sayansi kupata ajira ili kuongeza nguvu ya ufundishaji kule kwenye shule zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati huu utaendelea na utakuwa endelevu. Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa pamoja na Wizara ya Elimu wanaendelea kusimamia hili kwa karibu ili kuondoa upungufu mkubwa uliopo kwenye masomo ya sayansi, ahsante sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu, elimu, hasa kwa upande wa mtaala mpya kwa maana ya amali, ni jambo mtambuka. Baada ya utekelezaji wa mtaala, wanafunzi watakaohitimu watahitaji kuwezeshwa kwenye sekta nyingine, kwenye maeneo kama TAMISEMI, kilimo, afya na maeneo mengine hasa ya ufundi: Ni kwa vipi Serikali inajiandaa kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya watoto watakaohitimu upande huo wa amali?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sekiboko, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili, kwanza nataka kutoa uelewa kwamba tunapotekeleza Sera yetu mpya ya Mitaala, hatuendi moja kwa moja na madarasa yote, tunaanza na makundi machache. Wanaoanza kufundishwa mwaka huu wa 2024 kama tulivyosema tunaanza mwezi Januari, ni darasa la awali, darasa la kwanza na darasa la tatu. Kwa sababu kwenye Elimu ya Msingi tuna makundi matatu; tuna awali, halafu darasa la kwanza na la pili; kundi la tatu, ni darasa la tatu na darasa la sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wanaoanza kufundishwa mtaala mpya ni awali, darasa la kwanza na darasa la tatu. Tunaanza nao mwaka huu. Hiyo ni kwa Shule za Msingi. Kwa upande wa Sekondari, tunaanza na Kidato cha Kwanza. Pia kwa Sekondari, tunajua tuna elimu jumla na kuna zile shule za ufundi. Kwa hiyo, tumechagua Shule za Ufundi, siyo zote, chache ambazo tayari zina miundombinu na walimu wa kuanzia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu huu, utawezesha sasa Serikali kujipanga kupitia Bajeti yetu kuweza kumudu kuongeza pia hata idada ya walimu, kununua vifaa ili kufanya utekelezaji huu wa sera kuwa endelevu. Mwaka huu tunapoanza na awali na darasa la kwanza, darasa la pili hawahudhurii, wanaanza darasa la tatu, tunamfanya kijana wa awali anapohitimu, anapokwenda darasa la kwanza, anaendelezwa. Darasa la pili hapati, lakini anaanzia darasa la tatu, huyu wa darasa la kwanza anakuwa darasa la pili. Kwa hiyo, utakuta awali mpaka darasa la pili itakuwa endelevu kuanzia mwakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila mwaka tutakuwa tunaenda hivyo. Yule wa darasa la tatu anaenda la nne, la tano, mpaka la sita, mwisho wa Elimu ya Msingi. Utakuta sasa tunaweza ku-cover maeneo yote, kila mwanafunzi anapata elimu hiyo vizuri. Wizara ya Elimu sasa itajitahidi, itapangilia mtihani kulingana na muda waliosoma masomo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunawezaje kuimarisha eneo hili? Ni pale ambapo bajeti sasa tutakuwa tunaiimarisha, kwanza kuongeza miundombinu ya majengo ya kusomea, vifaa vinavyohitajika, na walimu wenye uwezo wa fani hizo. Kwa hiyo, kila mwaka tutakuwa tunaongeza uwezo wetu. Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba tunaweza kufanikiwa hayo ili sera hii mpya iweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mpango wa Serikali uliopo. (Makofi)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; moja kati ya jambo litakalosaidia sana utekelezaji wa Sera hii ya Elimu na kuendeleza maendeleo ya elimu yetu, ni maelekezo na uamuzi wa Serikali wa Elimu Msingi Bila Malipo. Hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya shule kuwa na utitiri mkubwa wa michango kiasi cha kupelekea kuondoa ile dhana ya Elimu Msingi Bila Malipo. Ni nini kauli ya Serikali juu ya jambo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, msimamo wa Serikali umebaki vilevile kwamba michango holela hairuhusiwi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposema michango holela, tunajua tuna michango inayokubalika kwenye jamii. Hizi shule zetu za msingi na sekondari ni shule za jamii, ziko kwenye meneo hayo. Tumeunda Kamati ya Shule kwa Shule za Msingi lakini tuna Bodi ya Shule kwa Sekondari. Wajumbe wa Bodi hizi ni wale walioko kwenye maeneo yale kwa lengo la kuwa wanapaswa kusimamia maendeleo ya shule, kushauri mwenendo wa shule na pia kupata changamoto zinazotokana na mwenendo wa kila siku, nao washiriki katika usimamizi wa uendeshaji au uendelezaji wa shule hiyo na taaluma yake kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, Kamati ya Shule inajua inawajibika kwenye ile shule kufuatilia maendeleo yake na pia mahitaji yake. Inaweza kutokea kwa mfano, choo cha shilingi milioni mbili kimebomoka. Siyo lazima kusubiri Serikali ije kujenga choo. Jamii inaweza ikaweka mpango mkakati wa kujenga choo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, michango holela na michango inayokubalika, hapa iko ya aina mbili. Michango inayokubalika ni hiyo ya maendeleo; ya choo kimebomoka, Kamati ya Shule inakutana, wanasema kuna choo kimebomoka tunataka kijengwe kwa haraka watoto wetu waanze kukitumia kesho. Badala ya kusubiri kuandika barua, bajeti ipangwe mpaka TAMISEMI, wanaweza kukubaliana kwamba bwana, tuchangie hapa shilingi mia tano, mia tano, mchango ambao unaenda kwenye choo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, michango hii pamoja na maamuzi hayo tumeidhibiti kidogo. Pamoja na maamuzi yenu ninyi Kamati ya Shule na Kijiji kwa ajili ya jambo la maendeleo, bado mwenye idhini ya kuanza kuchangisha ni Mkuu wa Wilaya. Tumeiweka hiyo kuondoa pia watu kukaa pamoja kutengeneza michango ambayo pia haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, msimamo wa Serikali umebaki pale pale kwamba hatuhitaji michango holela. Michango holela ni ile ambayo wakati wote ninapokuwa ziara huwa natoa mifano. Mtu mmoja tu anakurupuka anasema, kesho kila mmoja awe na shilingi mia mbili mia mbili, hazina maelekezo, hazina maelezo. Michango kama hii ndiyo ile holela ambayo haikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeagiza pia kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kusimamia kutokuwepo kwa michango holela inayokwaza wazazi katika kuendesha shughuli au usimamizi wa mtoto kupata taaluma. Hiyo ndiyo maana ya michango holela na michango rasmi ambayo pia nayo tumeidhibiti na msimamo wetu umebaki pale pale kwamba michango holela haikubaliki. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napongeza uthubutu wa Serikali kubadilisha mitaala kwa lengo la kuboresha elimu, lakini tutambue pia kwamba katika shule, muda ni wa msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoongea leo, kuna changamoto kubwa ya vitabu havijawafikia walengwa. Printing ya vitabu lakini pia vitabu kwenye shule wametumiwa softcopy, sasa vijijini watazitumiaje? Pia elimu haijafika. Naomba kujua mkakati wa Serikali, wakiangalia umuhimu wa muda, kwa sababu leo ni mwezi umetimia, shule zimefunguliwa. Ni upi mkakati wa haraka wa kuhakikisha vitabu vinafika na elimu inafika kwa wakati ili watoto waweze kupata elimu hiyo kwa wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali na kupokea ushauri kutoka kwa Mheshimiwa Anatropia. Kwanza nimhakikishie kuwa tumeendelea kuzalisha vitabu kulingana na mahitaji ya mtaala tulionao. Wakati huu tunapoanza kufundisha kwa Sera mpya ya Elimu kwenye mitaala mipya, kwenye mipango yetu ya bajeti, ndiyo tumesema tumeanza awamu kwa awamu. Hatukuanza full string, yaani hatukuanza madarasa yote. Tumeanza na awali, darasa la kwanza, darasa la tatu, na kidato cha kwanza kwa sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumeanza hivyo ili kujipa uwezo wa kupata vifaa, miundombinu ikiwemo na vitabu vya kujifunzia na kufundishia. Mkakati huu kama nilivyosema mwanzo kwamba tunaendelea kuongeza uwezo wa Serikali kibajeti kila mwaka ili kusheheneza maeneo haya, kumfanya mwanafunzi aweze kuipata ile elimu na aendelee nayo hata kule mwisho anapopimwa, apimwe akiwa ana uelewa na mahali pa kupata vitabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wizara ya Elimu imeweka mpango wa kuimarisha elimu ya TEHAMA ambayo pia itasaidia wanafunzi kupata taaluma hiyo kupitia mitandao yetu na kumwezesha kuwa na uwanda mpana wa kupata elimu kwa vitabu ambavyo tunapeleka, na hata kwenye mitandao ili iweze kumsaidia kuelewa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mpango wetu wa Serikali.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada kubwa ambayo Serikali inafanya ya kuhakikisha kwamba Nchi yetu inakuwa na sukari ya kutosha wakati wote, lakini katika siku za hivi karibuni kumekuwa na taharuki na upungufu wa sukari kiasi cha wananchi kuwa na malalamiko. Vilevile, ikizingatiwa kwamba katika kipindi hiki cha karibuni tunategemea kuwa na mfungo wa Ramadhan na Kwaresma, kwa hiyo wananchi wanakuwa na hofu juu ya suala hilo.
Je, ni lini kauli ya Serikali ili wananchi waweze kuondokana na hofu hiyo? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Mbunge wa Mbamba Bay, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tuna upungufu wa sukari nchini na upungufu huu umetokana na kuwepo kwa mvua nyingi ambazo maeneo yetu ya mashamba ya miwa inayozalisha sukari maji yamejaa kiasi cha kwamba, wale wa miliki wa mashamba haya hawawezi kutoa miwa kutoka mashambani kupeleka viwandani na kule viwanda vimebaki havina sukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa upungufu huu umeishafanyiwa kazi na Wizara ya Kilimo na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania mmepata kumsikia Mheshimiwa Waziri wa Kilimo akitoa maelezo hapa ya nini Serikali inafanya ili kukabiliana na upungufu huu ili Watanzania na wananchi kwa ujumla waweze kutumia bidhaa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja Wizara imetoa vibali kwa Wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wazalishaji wa sukari wenyewe. Kuingiza sukari nchini zaidi ya tani laki moja na zoezi hilo linaendelea na taarifa ambazo ninazo kutoka Wizara ya Kilimo tayari tumeanza kupata sukari kutoka nje. Hii itaendelea kupunguza makali ya kukosekana kwa sukari nchini ili Watanzania waweze kutumia bidhaa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeendelea kukaa na viwanda kuona namna bora ya kupata bidhaa hii pale ambako mvua zinapungua ili waendelee kuzalisha, upungufu huu siyo wa muda mrefu na kipindi hiki tunaamini tutafika mpaka kipindi cha Ramadhan. Kwa hiyo ndugu zetu Waislam watafunga Ramadhan na Serikali itawahakikishia kwamba sukari itakuwepo nchini, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa letu linapitia katika changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi sasa hivi, jambo ambalo linakuwa linazorotesha sana shughuli za kimaendeleo katika nchi yetu. Wananchi walio wengi wamekosa imani na Watendaji wa Wizara ya Ardhi. Je, hatuoni sasa kama ni muda muafaka wa kuweza kupitia mifumo ya utendaji katika Wizara hii ili kuweza kuepukana na changamoto hii? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salim Omar, Mbunge wa Gando Zanzibar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninakiri kwamba tuna migogoro mingi ya ardhi nchini na migogoro hii inatokana na mahitaji makubwa sasa ya matumizi ya ardhi hiyo, iko migogoro ya wakulima na maeneo yaliyohifadhiwa, iko migogoro ya wafugaji na maeneo yaliyohifadhiwa, lakini tuna migogoro hiyo iliyosababisha na utoaji wa hati mbili mbili kwa kiwanja kimoja na mipaka. Sasa nini Serikali inafanya? Kwa sasa hivi tunaendelea na maboresho ya Sera yetu ya ardhi nchini. Tunaamini Sera hii ikikamilika kuandaliwa ikipitishwa hapa kwetu Bungeni itasaidia sana kupunguza matatizo ya ardhi, kwa sababu kwenye Sera tutaainisha maeneo yale ambayo tumepata uzoefu wa migogoro yake kwa wakati huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kukabiliana na changamoto hii wakati huu tunaendelea kuiandaa sera, Serikali imeendelea kufanya maboresho ya utoaji vibali vya ardhi kwa wakulima na wale wanaotaka kujenga miundombinu mbalimbali. Mifumo hii tunaendelea kuihimarisha mifumo ya ki-electronic ili ipunguze kitendo cha kutumia makaratasi pekee katika utoaji wa vibali vya matumizi ya ardhi. Tunajua pia kwamba kuna Watumishi wachache kwenye Halmashauri zetu na Wizara ya Ardhi wanaokiuka taratibu na sheria tulizonazo kwenye ardhi na utoaji vibali kwa watumiaji wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine hulazimika kutoa Hati Mbili kwenye kiwanja kimoja hapo lazima mgogoro utakuwepo, ikiwemo na kuimarisha sheria tulizonazo maeneo yale yenye migogoro. Kwa hiyo Serikali kazi kubwa tunayoifanya sasa ni kutoa elimu na elimu hii tunashirikisha wananchi waweze kujua Sheria zetu za Ardhi na matumizi yake lakini pale ambako tunaona tunahitaji kufanya maboresho, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya wanaendelea kwenye maeneo yao kusikiliza kero mbalimbali kwa wananchi ili kutatua migogoro ya ardhi pale ambako kero hiyo inawasilishwa kwa Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kutoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kote nchini kuendesha vikao vinavyokusanya wananchi wenye changamoto na kusikiliza changamoto zao ikiwemo na ardhi, ili kutatua changamoto hizi na wananchi waweze kufanya shughuli zao kikamilifu. Tunaahidi kwamba migogoro hii tutaipunguza kwa kiasi kikubwa, kwa sababu sera ambayo inaandaliwa na utekelezaji wa kufuata sheria na usikilizaji wa kero kwa wananchi utasaidia na hasa matumizi ya ki-electronic ambayo tunaendelea sasa kuyaboresha ndiyo ambayo yataendelea kupunguza kero za ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kwamba sasa hivi tumesogeza huduma za ardhi mpaka kwenye ngazi ya Mikoa. Mikoa yote tumepeleka Makamishna wa Ardhi ambao watasaidiana, watashirikiana na Mkuu Mkoa kutatua matatizo na Halmashauri zilizoko ndani ya Mkoa, lakini mpango wa baadaye pia ni kushusha Mamlaka za Ardhi ambazo zitakwenda kutatua matatizo hayo hasa kwenye maeneo ya Majiji na Manispaa ambayo kuna idadi kubwa ya watu na mahitaji makubwa ya viwanja ili huduma hii iweze kupatikana huko huko kwa ukaribu zaidi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maendeleo makubwa ya kiteknolojia duniani, watoto wetu wamekuwa wakiingia kwenye mitandao na wakitumia vifaa vya ki-electronic kwa ajili ya kujifunza masuala ya TEHAMA na masuala mengine ya kujipa maarifa katika masomo yao. Tunafahamu wanapoingia katika mitandao wanakutana na mambo mengi ambayo yanaweza kupelekea mmomonyoko wa maadili na udhalilishaji wa watoto mitandaoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2014 Umoja wa Mataifa ulielekeza dunia kuweka mikakati madhubuti ya kuwalinda watoto dhidi ya ukatilii wa mitandao. Nchi nyingi zime-adopt, zimeweka sera madhubuti na sheria madhubuti za ulinzi wa watoto mitandaoni. Sasa nchi yetu imekuwa ikiendesha kampeni zisizo rasmi za ulinzi wa watoto mitandaoni, naomba kufahamu Serikali imejipangaje kuhakikisha inatengeneza mazingira bora ya kisera na ya kisheria kuhakikisha kwamba online child protection inapewa nguvu. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Hanje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, dunia sasa hivi inaendea kwenye maendeleo makubwa ya matumizi ya mifumo yetu mbalimbali ki-electronic. Pia dunia imeanza kuelimisha umma wake kutumia mifumo hii ya ki-electronic kwa urahisi zaidi, sasa mifumo hii imekuja ikiwa na faida lakini pia kuna changamoto zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizopo ni miongoni mwa hayo uliyoyaeleza kwamba jamii baadhi yetu tunatumia vibaya matumizi ya TEHAMA, matumizi ya Mifumo hii ya ki-electronic vibaya kwa kukashfu, kutumia mitandao kudhalilisha watu wakiwemo watoto na wanawake, lakini pia hata juzi tulipokuwa tunapitisha Muswada wetu hapa wa Vyama vya Siasa tulilizungumza hili na tumeliwekea mbano kidogo wale ambao watatumia vibaya mitandao kwa ajili ya kudhalilisha kwenye eneo la siasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huu ni mkakati ambao Serikali pia tumekubaliana na tumesaini mikataba ya kimataifa kukabiliana na unyanyasaji, vitendo vya kikatili kwa watoto na wanawake. Sisi kama Serikali tumeweka utaratibu wetu kupitia Wizara yetu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ili kukabiliana na wale wote wanaotumia vibaya mifumo hii kwa kudhalilisha watoto, wanawake na makundi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu ambao tumeufanya huku tukiwa tunapeleka pia kwenye Mtaala wetu wa elimu kufundisha kutoka Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo mbalimbali mpaka elimu ya juu, elimu hii ya matumizi ya ki-electronic tumeweka pia na Sheria zinazowabana hawa wote wanaotumia vibaya mitandao hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali inaendelea kuwahakikishia Watanzania kwamba, tutaendelea kuimarisha kudhibiti wale wote ambao wanatumia vibaya mitandao hii na tutachukua hatua kali dhidi ya wale wote ambao watatumia vibaya matumizi haya ya TEHEMA kwa kudhalilisha na kukatili wengine wa aina yeyote ile kwao ili itoe mafundisho kwa wengine ambao wanaweza kuungana nao kwenye matumizi mabaya haya. Kwa hiyo, nitaendelea kuwahakikishia ya kwamba matumizi ya TEHAMA tutaendelea kuhamasisha yake lakini hamasa hii ni kwa matumizi sahihi na siyo vingine. ahsante sana. (Makofi)
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi kwa kupata nafasi kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Natambua kwamba mwaka 2006 Bunge hili lilipitisha Sheria ya Benki ya Tanzania, ambayo chini ya kifungu cha 27(1)(b) inaipa Mamlaka Benki hii ku-design fedha kwa kuweka nembo na material mbalimbali. Pia natambua mwaka 2021 nchi hii imepata Rais wake wa kwanza Mwanamke anaefanya kazi nzuri na anatambulika katika Bara la Afrika na Duniani kama Rais madhubuti na wa mfano. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, natambua pia kwamba Bunge la Marekani sasa lipo katika utaratibu kupitisha sheria ambayo itawezesha Harriet Tabman, mwanamama, mwanaharakati aliyefanya kazi kubwa kwenye vita dhidi ya utumwa, kuwekwa kwenye dola ishirini kama kumbukumbu. Natambua kwamba katika Bara letu la Afrika nchi kama Nigeria, Malawi na Tunisia zimekwishafanya hatua hizi na zimetambuliwa na Benki ya Dunia na IMF kama hii hatua katika uelekeo unaofaa. Je, Serikali haioni sasa kwamba kuna haja ya kuweka kumbukumbu ya kudumu kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka picha yake katika fedha za nchi hii? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi, Mbunge Vijana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameonesha kutambua kazi nzuri, mchango unaotolewa na Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuona kama je, Serikali inaweza kuona umuhimu wa kutumia picha yake kwenye fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekekaji wa picha za viongozi mbalimbali ni maamuzi ambayo huko nyuma tulitoa kwa lengo la kukumbuka mchango wa Viongozi hawa kwenye Taifa hili, hasa picha ambazo zinatumika sasa za Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere lakini pia na Mheshimiwa Sheikh Abeid Aman Karume Rais wa kwanza wa Zanzibar ili kutambua tu mchango wao walioutoa katika Taifa hili na kwa hiyo picha zao zilitumika kama sehemu ya kumbukumbu zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunazo aina ya fedha noti na hizi sarafu ambazo pia tunatumia kuweka alama za wanyama wetu. Hii ilikuwa ni kuenzi tunu ya Taifa lakini pia kuuboresha hamasa kwenye Utalii. Sasa maamuzi ya kuweka picha kwenye noti mara nyingi yanafanywa na maamuzi ya kiongozi mwenyewe kwa kushauriana na Benki Kuu. Sasa kwa kuwa umelileta hili na sisi tunatambua kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mchango mkubwa kwenye Taifa hili, niseme tu tunapokea ushauri wako na litaingia Serikali litajadiliwa, pale ambako watafanya maamuzi kwa kushauriana na Benki Kuu taarifa zitatolewa rasmi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi uliyonipa na mimi kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu kuhamahama kutoka eneo moja kwenda lingine kwa sababu mbalimbali. Moja ikiwa kutafuta malisho na maji kwa wafugaji lakini pia wakulima kutafuta maeneo ya kilimo na pia kutafuta maisha kwa ujumla. Wanakohamia kunakuwa hakuna huduma muhimu za kijamii. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuongeza maeneo ya utawala kama kusajili Vijiji na Kata mpya ili kupeleka huduma za msingi katika maeneo hayo ambayo watu wamehamia? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gwau, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhamahama kwa wananchi, kutafuta maeneo ya kuendesha shughuli za kijamii kwenye maeneo mengi, ndiyo hasa wananchi sasa hivi tumeona wakisambaa maeneo mbalimbali, lakini Mheshimiwa Mbunge anahitaji kujua kama je, Serikali haioni umuhimu kuanzisha maeneo mapya ya utawala?
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mapya ya utawala yanaanzishwa kwa vigezo. Moja, idadi ya watu; pili, uwezo wa mapato wa maeneo hayo ili kuweza kuendesha mamlaka husika; tatu, uwepo wa huduma za jamii; vile vile, uwezo wa Serikali wa kujenga makao makuu ya mamlaka hiyo mpya iliyoko eneo hilo. Mara kadhaa tumepata maswali haya maeneo mengi. Binafsi nilipofanya ziara kwa wananchi, yapo maeneo wameomba kugawanywa ili wapate mamlaka mpya ya halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini msimamo wa Serikali? Ni kwamba tukiwa tunaendelea kupata takwimu mbalimbali za maeneo haya na kuona umuhimu wa kugawa maeneo haya kuwa na utawala mpya, kwa miaka mitano iliyopita Serikali ilitoa mamlaka mpya kwa maeneo mapya ya vijiji, kata, wilaya, halmashauri na hata majimbo kwa upande wetu Wabunge na mikoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya bado tunaendelea kuratibu kwa kupeleka miundombinu wezeshi ya utoaji huduma ya wananchi wa eneo hilo kama makao makuu yake. Sasa hivi, tunaendelea na ujenzi wa ofisi, nyumba za kuishi watumishi wa viongozi kwenye maeneo haya na Serikali imeshaweka msimamo wake kwamba tunaendelea na kuimarisha meneo haya. Hatuwezi kuanzisha maeneo mapya huku tukiwa hatujakamilisha kuandaa mazingira mazuri ya maeneo ambayo tayari yametolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pindi itakapokamilika, ujenzi wa miundombinu wezeshi kwenye maeneo haya ili viongozi wa maeneo haya waweze kutoa huduma na wananchi wapate huduma kwenye maeneo hayo, sasa tangazo la Serikali litatoka. Halmashauri, mikoa, wilaya na maeneo mengine yanahitaji kuwa na mamlaka mpya zitaanza mchakato wa kuomba mamlaka hizo kwa kufuata taratibu zilizowekwa hasa zile ambazo zinajumuisha vikao vya wadau wenyewe kuanzia huko huko walipo, wakubaliane kugawana na pia kama kuna jambo lolote ambalo litahusisha mgawanyo huo, basi maamuzi ya vikao hivyo utakuja na baadaye muhtasari utakuja Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais atakapoona sasa tumekamilisha ujenzi wa miundombinu, anaweza kutoa kibali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili kutoa mamlaka nyingine mpya. Huo ndiyo utaratibu wa Serikali tulionao kwa sasa. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pia kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kwa kipindi kirefu kuondoa tozo mbalimbali hasa zaidi kwenye mazao ya biashara kama vile pamba, kahawa, korosho pamoja na mazao mengine. Nia ya kuondoa tozo hizi ilikuwa ni kumletea nafuu mnunuzi ambaye naye anakwenda kumpelekea nafuu mkulima ili aweze kupata faida nzuri kwenye mazao yake ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo siku za karibuni kumeonekana kama tozo zilikuwa zinajirudia na kusababisha kuanguka kwa bei ya mazao ya kilimo, ikiwemo ya Korosho. Ni nini, kauli ya Serikali kuhusu kufanya marejeo ya tozo mbalimbali ambazo zinaathiri bei ya Korosho? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba haya mazao yetu yote na hasa yale mazao yanayolimwa kwa ushirika kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, ni mazao ambayo miaka mingi huko nyuma kumekuwa na ongezeko la tozo mbalimbali na ikasababisha hata kuanguka kwa bei na pia kero kwa wakulima kwa kupata kipato kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulifanya mapitio kwenye mazao yote yenye bodi na yanayouzwa kwa mifumo ya ushirika na kugundua kwamba tuna makato mengi. Mazao mengine yana makato mpaka 30 au 20. Tulifanya hizo jitihada kupunguza makato hayo na kufikia kiwango cha mwisho makato sita na kuleta unafuu mkubwa kwa wanunuzi na pia kuwapa kipato cha kutosha wakulima. Hiyo inaendelea hata sasa, mazao aliyoyataja pamoja na kakao kule Kyela, sasa hivi bei imepanda juu sana baada ya kuwa tumesimamia kuondoa tozo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali bado inaendelea na imeshatoa maagizo kwa bodi zote za mazao kufanya mapitio ya mara kwa mara ya tozo na pia mwenendo wa soko la mazao yenyewe. Lengo hapa, tunataka Serikali tuone kuwa mkulima anayelima zao hili, ambaye anatumia muda wake mwingi kulima zao hili, ananufaika kwa kupata bei nzuri. Sasa, bei nzuri ni pale ambapo tunapunguza gharama kwa wanunuzi ili gharama hiyo iweze kuhamia kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato huu unaendelea na hasa usimamizi wa Vyama hivi vya Ushirika vya Msingi ambako ndiyo kunaanza kuwekwa kwa tozo, pia vyama vyake vikuu ambako nao ndio wanatoa vibali vya tozo kuhakikisha kwamba tozo hizi haziendelei. Tumeweka ukomo wa tozo muhimu kwenye zao husika kulingana na mazingira waliyonayo ili kuweza kuleta unafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie kuwa Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote ambao mnatoka kwenye maeneo yanayolima mazao yenye bodi na kuuzwa kwa ushirika kwamba, Serikali itaendelea kusimamia kwa ukaribu, kuhakikisha kwamba wakulima wananufaika na mazao haya kwa kuwatafutia masoko, lakini baada ya kuwa tumeuza tozo mbalimbali zisiingie bila kuwa na utaratibu. Bodi nazo tumesisitiza kufanya ufuatiliaji wa kuhakikisha kwamba hakuna tozo nyingi kwenye eneo hili ili makundi haya mawili; wanunuzi na wakulima waweze kunufaika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Sote tunatambua jitihada kubwa inayofanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa katika eneo la kuhakikisha kwamba miundombinu hasa ya barabara inaimarishwa mijini na vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi hiki tumekuwa na wakati mgumu wa mvua hasa katika baadhi ya mikoa, mfano Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Pwani Kaskazini, hali ambayo imekuwa ikisababisha kwa hali ya juu sana uharibifu wa miundombinu hii ambayo tumeijenga na kutumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka na wa dharura wa kibajeti ilimradi kuhakikisha kwamba tunanusuru hali ya mawasiliano kwa maana ya barabara ambayo sasa imekuwa ni mbaya sana; katika maeneo ya vijijini na mjini, ili wananchi waendelee kutoa huduma na kusafirisha na kusafiri kama ilivyokuwa kawaida na kama ilivyo azma ya Serikali ya CCM? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Butondo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa maelezo yake, anataka kujua mpango wa Serikali wa kibajeti wa kuwezesha kurudisha miundombinu iliyoharibiwa kutokana na mvua nyingi. Kwanza nikiri kwamba mvua ni nyingi na mvua inaendelea kunyesha kote nchini. Tumeendelea kushuhudia maafa mbalimbali ikiwemo na miundombinu zetu barabara, madaraja na makalavati yanabomoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo tu kwa barabara pia hata maisha ya watu. Kuna maeneo imesababisha mafuriko; nyumba, mali mbalimbali zimepotea, hata maisha ya Watanzania wengine hawapo, wametutangulia mbele ya haki kutokana na kusombwa na maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niungane na Waheshimiwa Wabunge kuwapa pole wale wote waliofikwa na maafa hayo. Wale ambao wametutangulia mbele za haki, Mwenyezi Mungu aweke roho zao mahali pema Peponi, Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali umeelezwa vizuri sana hapa. Kulikuwa na maswali kadhaa kwa Waziri wa Ujenzi ambaye aliulizwa swali la namna Serikali inavyoweza kukabiliana na jambo hili. Mtakumbuka pia Waheshimiwa Wabunge kwamba hata Mheshimiwa Spika alitoa nafasi nyingi kwa Wabunge kuuliza kwenye eneo hili na kuitaka Serikali itoe maelezo ya nini Serikali tumekifanya mpaka sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, maafa hayo na kuharibika kwa miundombinu ya barabara na makalavati, tumezipa jukumu zile taasisi zetu mbili; TANROADS pamoja na TARURA inayosimamia barabara zilizoko wilayani na vijijini, kuhakikisha wakati wote wanafuatilia mwenendo wa mvua zinazoendelea kunyesha nchini na kama kuna eneo limeharibiwa, kulirudisha kwa haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila taasisi kupitia Wizara zake; TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi, kibajeti zimejiweka vizuri na hata Mheshimiwa Waziri alipokuja hapa Waheshimiwa Wabunge waliouliza swali hili, kila mmoja aliambiwa fedha iliyopelekwa kwenye eneo lake. Kwingine tumeleta shilingi milioni 500, shilingi milioni 300. Kwa hiyo, Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa, tunarudisha miundombuinu ili huduma za wananchi kwenye maeneo hayo ziendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua hatutarudisha kwa viwango vya awali, lakini muhimu ni kuwafanya watu waendelee kupita na kutumia miundombinu hiyo vizuri. Pia, tukiwa tunaendelea kuona mvua zinanyesha, nitoe tahadhari kwa Watanzania hasa walio kwenye maeneo hatarishi, kuondoka kwenye maeneo hayo hatarishi na kukaa kwenye maeneo ambayo yapo kwenye miinuko ili tuweze kupunguza maafa haya hasa pale ambapo maji yanazidi kiasi na kufika kwenye nyumba zilizo kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwahakikishia Watanzania kwamba Serikali tupo macho kupitia Taasisi zetu za TARURA na TANROADS pale ambako kuna uharibifu tunaanza na halmashauri yenyewe ambako TARURA ipo. Pia, kwenye TANROADS, Ofisi zipo kwenye mikoa, jukumu lao sasa ni kupita maeneo yote na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, kila mvua zinaponyesha kuona kama je, miundombinu yote imebaki salama au kuna tatizo limejitokeza, na kuhakikisha kwamba tunarudisha huduma hiyo kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo mpango wetu ndani ya Serikali, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri Mkuu, TMA imekuwa ikijitahidi sana kutoa taarifa sahihi kuhusu uwepo wa mvua kubwa nchini kwetu na Serikali ina vyombo vyake vingi vya kujua kwamba mvua inanyesha kubwa sehemu gani. Sasa, badala ya kuacha utashi wa mzazi aseme nimpeleke mtoto wangu shule au nisimpeleke, kwa nini zile mamlaka zetu kule chini zisiwe zinatoa taarifa kwamba leo Mtwara kuna mvua kubwa, watoto wote wasiende shuleni ili kuepusha maafa ambayo yanatokea na yanawakumba watoto wetu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema kwamba, Serikali yetu imefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye mfumo wa utoaji taarifa ya hali ya hewa kila siku hapa nchini. Taarifa hizi ambazo zinatokana na mitambo na wataalam walioko kwenye sekta zinatakiwa zizingatiwe pia na mamlaka zote mpaka kule vijiji. Kwa hiyo ni jukumu la mamlaka zetu ambazo pia ni Kamati za Maafa kutoa taarifa za hali ya hewa ili kuepusha maafa hayo kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa maelekezo hapa kwa halmashauri zote nchini na mikoa kwa kupitia wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, wahakikishe kuwa wanajenga utamaduni wa kutoa mawasiliano wakati wote pindi wanapopata taarifa za hali ya hewa. Kama taarifa ya hali ya hewa hiyo inaweza kuwa mbaya kwenye eneo hilo, basi ni wajibu wa Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bado narudia tena kuwasihi na kuwataka Wakuu wa Mikoa kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa hasa kipindi hiki ambacho kinaonesha kwamba mvua zitaendelea kuwa kubwa mpaka mwezi Mei, waweze kujua, je, kwenye mkoa wao hali ya hewa ikoje na waweze kutumia njia hiyo kuweza kutoa taarifa kwa wananchi wao kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, naendelea kusisitiza viongozi wetu walioko mikoani kuhakikisha kwamba wanatoa taarifa hizi mara kwa mara na ndio wajibu wao ili kuweza kuokoa hali hii ambayo watu wengine walikuwa hawapati taarifa huku mamlaka zetu za Serikali zikiwa ziko pale.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nalichukua hili kwa ajili ya kuendelea kuliimarisha zaidi kwenye kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kuwa nyingi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Waheshimiwa Mawaziri ambao walitutembelea wakati tulipopata maafa.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa aliyotoa Mheshimiwa Waziri Mkuu, hakutaja katika taarifa Mkoa mzima wa Morogoro ambao pia ulikumbwa na mafuriko, ikiwemo Wilaya ya Mvomero, Morogoro DC ambayo mimi natoka na Ulanga. Kwa mfano kwenye jimbo langu zaidi ya nyumba 300 na kitu zimevunjika na mashamba. Sasa swali, ni je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na mafuriko haya ambayo yanatokea kila mwaka hasa katika Mkoa wa Morogoro, katika suala la kuchimba mabwawa ili kuweza kupunguza kasi ya mito ambayo iko mingi katika Mkoa wa Morogoro na kuendelea kuleta maafa kwa wananchi wetu na Serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na majanga haya? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Kalogeris, Mbunge wa Morogoro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nakiri kwamba tumesahau kuiweka Ulanga, lakini Ulanga pamoja na Malinyi ni miongoni mwa Wilaya ambazo zimeathirika. Kote huko Kamati zetu za Maafa za Wilaya na Mkoa pamoja na hawa Waheshimiwa Mawaziri Nane na Makatibu Wakuu wote wamepita kule na wameona hiyo hali. Pia nimepata nafasi, nimepita maeneo hayo kutoka kule Mlimba, nimekuja Ifakara Mjini. Nilipokuwa naenda Malinyi nilipitia Ulanga kuona hali hiyo. Hakika hali siyo shwari sana kwa sababu eneo lote limejaa maji; na bado nikapita juu ya Mto Rufiji mpaka Rufiji kwenye kuona hali hiyo na ujaaji wa maji. Ni kweli kwamba maeneo hayo yamepata athari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba bonde hili tunalitumia vizuri na hasa kwa kuelekeza maji kwenye maeneo yanayoweza kuleta manufaa kwa wananchi. Tayari Wizara zetu mbili, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeshaandaa mpango wa kuchimba mabwawa, yatakayoweza kukusanya maji haya kwa matumizi mbalimbali ikiwemo moja, umwagiliaji na mbili, kutakuwa na uvuvi mdogo mdogo kwa maeneo hayo yenye mabwawa pamoja na kunyweshea mifugo yetu. Tayari wataalamu wako Ifakara kuona maeneo sahihi ya kuchimba mabwawa hayo ili kuchepusha maji kutoka kwenye ule Mfereji Mkubwa wa Rufiji na kupeleka kwenye mabwawa hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati huu pia unaendelea mpaka uelekeo wa Mto Wami, ambako huko nako pia kupitia mfereji ule tunachimba Bwawa kubwa sana la Kidunda kwa ajili ya matumizi ya maji ambayo yataingia Jijini Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaendelea na mpango huu mpaka Bonde la Mto Rufiji, Maeneo ya Rufiji yenyewe nako pia tumeshatenga fedha kwa ajili ya kuchimba mabwawa ili tuelekeze maji yetu katika maeneo hayo, tuyahifadhi halafu tutakuwa tunayatumia kulingana na mahitaji kwenye maeneo yote matatu ya kilimo, mifugo pamoja na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna hii hii tutaendelea na mabonde yote. Bonde la Mto Ruvuma tutafanya kazi hiyo; kule eneo la Nyasa tutafanya jambo hilo na Wizara zetu zimeendelea kuongezewa bajeti na wataendelea na kazi hiyo kadiri tunavyopata fedha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na napenda pia kutumia nafasi hii kupongeza jitihada za Serikali katika masuala mazima ya hali ya hewa. Kwa kweli taarifa zinazotolewa zimekuwa na usahihi wa hali ya juu na zinatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nchi yetu pamoja na ushiriki wa uhifadhi na mazingira, lakini pia Mheshimiwa Rais wetu amekuwa mshiriki wa Mikutano ya Kimataifa ya Mazingira. Mara zote ameyasihi mataifa makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa yana mchango mkubwa katika mabadiliko ya tabianchi, kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia nchi hizi ambazo zinaendelea ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama sehemu ya ushawishi wake, mataifa makubwa kupitia Umoja wa Mataifa walikubaliana kuanzisha Mfuko wa Fidia unaitwa Loss and Damage Fund, kwa ajili ya kuzisaidia nchi zinazoendelea pale ambapo zinakuwa zimepata athari kama hizi zinazoendelea za mafuriko kama matokeo ya tabianchi. Je, Serikali iko tayari kuunda kikosi kazi ambacho kitahusisha wataalam kutoka vyuo vya elimu ya juu, sekta binafsi na NGOs na wataalamu kutoka Serikalini ili kuona kwa namna gani sisi tunapata fedha hizo ili ziweze kutusaidia kukabiliana na athari ambazo zimetokana na mabadiliko haya ya tabianchi?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chumi, Mbunge wa Mufindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu imekuwa inashiriki mikutano mingi na pia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki mikutano mingi, pia Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye ndiye mwenye ofisi yenye dhamana ya mazingira ameshiriki mikutano hii. Serikali tumeihakikishia dunia kwamba na sisi tuko kwenye mchakato na mpango unaoweza kudhibiti uharibifu wa mazingira hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kuunda chombo, tayari Wizara ya Mazingira ndani ya Ofisi ya Makamu wa Rais inayo timu ambayo inafanya kazi wakati wote pamoja na Idara ya Mazingira kuhakikisha kuwa inakuwa na mipango ya sasa endelevu ambayo itawezesha Serikali yetu kutambua na kubaini maeneo ambayo yanahitaji kuimarishwa kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira. Pia tathmini na tafiti mbalimbali zimekuwa zinafanyika ili ziweze kutuongoza Serikali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mpango huu unaoendelea ndani ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira ni endelevu kwa sababu tunahitaji kuelimisha umma na tunaona ghasia za mabadiliko ya tabianchi zinazojitokeza kwenye maeneo yao. Lengo hapa ni kupitia tafiti hizo zinazofanywa na kikosi kazi hicho ambacho tayari kimeshaundwa, tutaona mahitaji zaidi ili tuongeze vikosi kazi kulingana na mahitaji yenyewe. Lengo ni kufikia hatua nzuri ili Taifa letu tuwe kwanye nafasi ya kuhifadhi mazingira na kuepusha majanga yanayoweza kujitokeza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ni kweli kwamba Taifa limekutwa na janga la mafuriko na mikoa mbalimbali imeathirika na mafuriko haya ambayo yanaendelea.
Mheshimiwa Spika, pale kwenye Jimbo la Kibiti tuna kaya takriban 6,150 zimeathirika, idadi ya watu takriban 31,900, lakini sambamba na hilo ekari zilizokuwa zimesambaratishwa na mafuriko haya ni takriban ekari 71,366. Tukizingatia kwamba wananchi hawa wanategemea sana kilimo; je, nini mkakati wa Serikali mara baada ya hali hii ya mvua kuwa imepungua, kuweza kuwasaidia wananchi hawa wa Jimbo la Kibiti pamoja na Rufiji kuweza kupata mbegu ili kuendelea na masuala ya kilimo? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nampa pole, miongoni mwa wilaya ambazo zimepata athari kubwa ni Wilaya ya Kibiti, eneo la delta. Kwa bahati nzuri eneo lile nalifahamu, nimeishi pale, nimefanya kazi pale na athari hii tumeitembelea na tunazo taarifa ofisini kwetu. Kwa hiyo, pole sana Mheshimiwa Mpembenwe na wananchi wote ambao wamepata athari kwenye eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na Taifa zikiendelea kuratibu utoaji misaada kwenye maeneo yote ikiwemo Kibiti bado pia tumeweka mpango imara wa kuhakikisha kwamba baada ya utulivu wa hali ya hewa sekta zetu zote ambazo zinaguswa na maafa yale; miundombinu, Wizara ya Kilimo, mashamba na maeneo ya mifugo, sekta ya afya kama kulitokea mlipuko wa magongwa baada ya uwepo wa maji mengi yaliyopita katika maeneo mbalimbali. Wizara hizi zina mpango kazi kupitia Kamati ya Kitaifa ya Maafa.
Mheshimiwa Spika, moja kati ya jukumu ambalo sasa lipo kwa Wizara ya Kilimo kwa wakulima wale ni kwamba tumeshaandaa mbegu. Tulitoa taarifa kwa Mheshimiwa Rais kiwango cha tani ambazo tumeamua tuzipeleke kwenye eneo lile. Rufiji tumeona mazingira hayo wakulima walikuwa wanalima mazao gani, tumeandaa mbegu za kutosha kwa ajili ya kuwawezesha kuanza kulima tena. Kwa kuwa eneo lile ni chepechepe, tunaamini bado wanaweza wakalima mazao ya muda mfupi na yakaiva. Tumeamua kupeleka mpunga ili waweze kurudisha mashamba ya mpunga kwenye maeneo hayo chepechepe, mazao kama mahindi na mazao mengine ambayo ni ya muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utaratibu wote umeandaliwa na timu yetu iko pale Kibiti, Rufiji na maeneo mengine ambayo yamepata athari, wanaendelea kuratibu na kufuatilia mwenendo huo. Mwisho, kila hatua inayofikiwa wale watakuwa wanatupa taarifa. Kwa hiyo, tutaendelea kuwasiliana na Mheshimiwa Mbunge na yeye atakuwa anatupa mrejesho wa huduma zinazoendelea kutolewa pale ili tushirikiane na wananchi wale waweze kurudi kwenye hali yao ya kawaida. Huo ndiyo Mpango kazi wa Serikali. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika nchi yetu kumekuwa na sheria, sera, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali kwa watumishi wa Serikali na taasisi zake kuzingatia muda wa kuingia kazini na muda wa kutoka kazini, lakini kumekuwa na changamoto kwenye baadhi ya watumishi wa kada moja kutofautiana muda wa kutoka kazini, kwa mfano, walimu wa shule za msingi mijini wanatoka kazini saa 8.30 mchana lakini wale wa vijijini wanatoka mpaka saa 10.30 alasiri.
Je, Serikali haioni haja ya kupitia upya utaratibu huu ili kuweka sawa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha leo kuwa na uhai, uzima na hatimaye leo asubuhi hii tunaanza programu zetu kwa kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nchi yetu inayo sheria ya kazi ambayo inaainisha pia muda wa kuingia kazini na muda wa kutoka kazini na kwa mujibu wa sheria zetu muda wa kazi Kiserikali ni saa zisizopungua nane, kuanzia saa 1.30 asubuhi mpaka saa 9.30 alasiri.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amezungumzia utofauti wa muda wa kutoka kwa walimu wa shule za msingi wa mijini na vijijini, kwa bahati nzuri na mimi pia ni mwalimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kinachopelekea utofauti wa muda wa kutoka ni mazingira ya maeneo hayo ya miji na vijijini. Maeneo ya mijini mara nyingi ofisi za elimu na kwa kupata kibali kutoka TAMISEMI wanafunzi wakiingia asubuhi na walimu wakiingia asubuhi mchana hawapati muda wa kwenda kupumzika na kwa hiyo, wanaunganisha mpaka saa 8.30 mchana, lakini vijijini muda wa mchana wanapata nafasi ya kurudi nyumbani kwenda kula.
Kwa hiyo, ule muda wa kula ndio unaokuja kulipiwa pale mbele na kufanya muda wa kutoka uonekane kuwa ni mrefu zaidi, lakini saa za kazi ni zile zile. Kwa hiyo, huu ni mpango kazi uliowekwa kulingana na mazingira yaliyopo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwa nini huku mijini wanaamua kuunganisha moja kwa moja? Kwanza kuna shida ya usafiri, huwezi kuruhusu mwanafunzi mchana arudi nyumbani, aende shule utaona mazingira kama Jiji la Dar es Salaam mazingira yale mwanafunzi kutoka nyumbani kwenda shuleni peke yake shida, ukimruhusu mchana saa moja arudi nyumbani, halafu arudi tena saa saba bado ni shida vilevile, kwa hiyo wanaamua kuunganisha moja kwa moja na ndio sababu wanaonekana wanaingia saa 1.30 asubuhi na kutoka saa 8.30 mchana.
Mheshimiwa Spika, lakini vijijini kwa sababu hakuna tatizo la usafiri na shule za msingi ziko vijijini, kwa hiyo, ni kiasi cha kutembea kwenda nyumbani anapumzika, anakula, anarudi shule na ule muda alioutumia kwa kula unasogezwa mbele na kwa hiyo, muda wa kuondoka shuleni unaongezeka na kwa hiyo, hata walimu nao wanatoka muda huo huo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni mpango kazi ambao pia umeridhiwa na TAMISEMI, kwa hiyo tuchukue hiyo tuipeleke TAMISEMI waone kama kuna umuhimu wa hata vijijini kuunganisha muda bila kuruhusu wanafunzi wetu kupata chakula, hiyo pia inaweza kuamriwa na Wizara kulingana na mahitaji na mazingira yalivyo, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa ya kujenga madarasa kwenye shule zote za msingi na sekondari na wakati mwingine imejenga shule iliyokamilika, kutokana na kufanya kazi hii tumeongeza wanafunzi wengi na kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi tumeongeza upungufu wa walimu.
Mheshimiwa Spika, ziko halmashauri na majiji ambayo yanakusanya fedha nyingi, lakini nao wanasubiri mgao wa ajira hususan kama ya walimu waweze kupata sawa na halmashauri zingine ambazo hazina mapato.
Je, Serikali haioni kama ni busara na ni vyema kwamba halmashauri na majiji ambayo yana uwezo wa kuajiri walimu waweze kuajiri ili inavyokuja ule mgao wa kitaifa hawa wengine ambao hawana tuwe tumewapunguzia mzigo huo na kufanya hivyo ni kwamba maeneo yale tayari tutakuwa tumeondoa tatizo la walimu? Ahsante sana.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imesimamia mifumo ya ajira na ajira zote za kudumu ziko chini ya Serikali Kuu ikiwemo na sekta ya elimu kwa walimu. Nikiri kwamba tunao upungufu wa walimu kwenye shule zetu za msingi hata sekondari na upungufu huu unatokana na vipindi vya ajira, lakini hapa katikati kabla ya ajira kunakuwa na vifo kunakuwa na kustaafu lakini pia hata mpango usiokuwa mzuri wa kwenye halmashauri zenyewe kwa sababu walimu wengi wanaonekana wanajaa sana mijini kuliko vijijini, nitalisema baadae.
Mheshimiwa Spika, kwa nini ajira zote zimepelekwa Serikali Kuu? Lengo ni kuwa na mfumo mmoja wa kuajiri na kupata kanzidata yaani takwimu ya idadi ya waliopo kazini wanaoajiriwa, lakini pia kuweza kusambaza kwa usawa kwenye halmashauri zote ili kusiwe na halmashauri moja kuwa na mlundikano mkubwa kwa sababu tu wana uwezo wa wao kuajiri. Kwa hiyo, Serikali Kuu inasimamia kusambaza walimu nchini kote kulingana na mahitaji, kulingana na fani walizosomea, kwa mfano, masomo ya sayansi na masomo ya sanaa hiyo. Kwa hiyo, mahitaji yanakwenda nchini kote.
Mheshimiwa Spika, tunajua ziko halmashauri zenye uwezo, lakini kuna halmashauri ambazo hazina uwezo. Tukiruhusu halmashauri zenye uwezo ziajiri kuna hatari ya halmashauri ambazo zinapata pato chini ya uwezo wake hakutakuwa na walimu hakutakuwa na wafanyakazi na kwa hiyo, hakutakuwa na usawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali hatuwezi kuruhusu hili na ndio sababu ajira zote tumeweka za Serikali Kuu yenyewe inaajiri walimu 4,000 tunawagawa nchi nzima kulingana na idadi, uwiano wa masomo kwa maana ya fani, lakini na mahitaji ya hizo halmashauri. Tutaendelea kufanya hivi inatusaidia pia Serikali katika kulipa stahiki zao pamoja na mafao yao ya mwisho wa kustaafu, lakini pia inatusaidia kuwa na takwimu.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, sasa nitoe agizo kwa Maafisa Elimu na Wakurugenzi wa Halmashauri kufanya mapitio ya ikama zao. Hapa ndipo tatizo lilipo kwamba halmashauri inaruhusu eneo fulani kuwa na walimu wengi halafu kule vijijini hakuna walimu na kusababisha kuwa na upungufu mkubwa wa walimu, kumbe kama wangekuwa wamewasambaza vizuri ingekuwa na walimu wanaotosha kwenye fani zao. Kwa hiyo, wapitie ikama yao ili wajaribu kuona mlundikano wa walimu kwenye maeneo ya miji na barabarani ili wawapeleke pia na vijijini kuwe na utoshelevu halafu ile kanzidata isaidie pia katika kufanya kila shule kuwa na idadi nzuri ya walimu, hizi ndio sababu ambazo zinapelekea Serikali Kuu kuajiri centrally, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL E. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi hii ya kuuliza swali kwa Waziri kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, hapa nchini Serikali imekuwa ikitoa 10% ya mikopo kwa walemavu, wanawake, lakini pia vijana ambao wako chini ya miaka 35, lakini kuna kundi hili ambalo linazidi miaka 35 ambalo ndio mhimili mkubwa wa familia na ndio walipa ada wakubwa kwa watoto na ndio wanaotibisha familia, lakini pia ndio kundi ambalo linalinda uchumi wa familia.
Sasa ni nini mkakati mkubwa wa Serikali wa kuweza kulikumbuka kundi hili katika masuala ya mikopo? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imetenga fungu maalum la mapato ya ndani katika kila halmashauri kutoa fursa za kuendeleza ujasiriamali kwa kutoa mikopo midogo midogo na ya kati kwa makundi ya wanawake 4%, walemavu 2% na vijana 4%. Sasa kundi hili la zaidi ya miaka 35 sio kwamba tumelisahau bali tunazo fursa nyingine za kupata mitaji kupitia mifuko mbalimbali, lakini pia kwenda kwenye taasisi za fedha kama vile mabenki na ile mifuko ambayo imepata vibali maalumu vya kukopesha.
Mheshimiwa Spika, haya makundi tunayoyazungumza kutokana na tathmini za ndani za Serikali ziko changamoto zinazokabili makundi haya ya vijana, lakini pia walemavu na wanawake. Mpango wetu ni kuhakikisha kwamba makundi haya nayo yanakuwa na eneo ambalo wanaweza kwenda kupata mikopo hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kuwapa faraja Watanzania kwamba Serikali imeendelea kuzungumza na benki kwa maana ya taasisi za fedha kufungua madirisha ya kutoa mikopo ya viwango mbalimbali kulingana na mahitaji ya mteja mwenyewe na huku ndiko ambako pia tunaruhusu hili kundi la watu kutoka miaka 35 na kuendelea ili kuweza kupata mikopo na kwa hiyo, kadiri Serikali itakapokuwa na uwezo itaendelea kufungua milango na kuanzisha mifuko mingine ili kutoa fursa kwa makundi mengi zaidi kupata mikopo kama mitaji kwa ajili ya shughuli zao za ujasiriamali.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kupata nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, michezo ya kubashiri imekuwa ikichangia Pato la Taifa, lakini mapato ya michezo hii yamekuwa hayanufaishi moja kwa moja sekta ya michezo kutokana na michezo hii kusimamiwa na Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, Serikali haioni haja ya kuihamisha michezo hii kutoka kwenye Wizara ya Fedha kuipeleka kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upo ukweli kwamba tunayo michezo ya kubahatisha na kubashiri michezo ambayo inaratibiwa na Bodi ya Bahati Nasibu na makampuni haya yanayoendesha ubashiri wa michezo wanalipa kodi na kwa mujibu wa sheria zetu nchini kodi zote huwa zinapewa mamlaka inayokusanya kodi ambayo huwa ni TRA.
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Mbunge anataka kusema kwa nini kibali hiki kisipewe Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuweza kuendeleza michezo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli hii Bodi ya Michezo ya Kubahatisha iko Wizara ya Fedha na anayekusanya mapato ni TRA kama ambavyo kodi zingine zinavyokusanywa na TRA, lakini baada ya kukusanya fedha hii Baraza la Michezo lililoko ndani ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo linapata mgao wa 5% ya makusanyo ya fedha kutoka kwenye michezo hii ya kubahatisha na kwa hiyo suala la uendelezaji wa michezo linabaki pale pale, kwa sababu hiyo 5% ndiyo inayotakiwa kukusanywa na hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lengo la kuipa TRA kukusanya mapato ni katika kudhibiti mianya ya fedha katika kuweka uelewa wa taasisi husika ya ukusanyaji kodi ambao pia ni TRA na mamlaka ambayo imepewa na kwa hiyo sasa tuna uhakika kila ikikusanya tukishapata takwimu 5% tunapeleka kwenye mfuko wa kuendeleza michezo ulioko chini ya Baraza la Michezo kwa ajili ya shughuli za michezo na ndiyo utaratibu ambao kwa sasa unaendelea.
Mheshimiwa Spika, pia kama wadau wa michezo wataona kuna haja ya kuishauri Serikali, sisi tunapokea ushauri na kupitia vikao vyetu tutabadilisha kanuni na sheria zetu ili tuelekeze huko kama umuhimu upo kwa ajili ya kuendeleza michezo kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Wakuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutokana na nchi yetu uchumi kuboreka na kuendelea kukua na hali ya amani iliyopo katika Taifa letu, kumekuwa na ongezeko kubwa sana la wafanyabiashara wa ndani ya nchi, lakini vilevile wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje kitendo ambacho kimekuwa kikipanua na kuendelea kuweka wigo mpana zaidi kwenye ufanyaji wa biashara.
Mheshimiwa Spika, lakini kumekuwa kuna tatizo kwamba baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji ambao wanakuja kufanya biashara hapa Tanzania wamekuwa wakifungua biashara au wakifungua viwanda, lakini wamekuwa wanakwenda kwenye ngazi ya chini kabisa kule vijijini kitu ambacho kinasababisha wale Watanzania ambao ni wafanyabiashara au watanzania wananchi wa kawaida kushindwa kufaidika na biashara hizi katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kujua, je ni lini Serikali italeta sera nzuri ili kuweza kumnufaisha Mtanzania huyu walau baadhi ya wafanyabiashara wafikie kwenye level fulani waishie huko kwenye uzalishaji na huku kwenye usambazaji na kufungua maduka mengine mpaka ngazi za chini kazi hizi zifanywe na Watanzania kama ilivyo kwenye baadhi ya nchi za wenzetu? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Mayenga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nitambue mchango wa wafanyabiashara wadogo ambao wananchangia sana kwenye pato letu la Taifa kutokana na shughuli zao za kibiashara, wanalipa kodi na tunaendelea kutunisha mfuko wetu. Pia nchi yetu inayo sera ya mahusiano ya kidiplomasia na nchi marafiki ambao pia wamefungua milango kuingia nchini kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo biashara.
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu pia inazo sheria na kanuni ambazo zinaongoza wageni hawa kufanya shughuli mbalimbali hapa nchini ikiwemo biashara, lakini kwa vibali maalumu ambavyo pia vinazingatia aina ya biashara ili kuruhusu Watanzania kufanya biashara nyingi huku ndani.
Mheshimiwa Spika, kutokana na mwingiliano wa wengine kuacha biashara ya ngazi yao kulingana na vibali vyao na kufanya biashara ambazo Watanzania wangeweza kufanya, Serikali tumeimarisha ufuatiliaji wa vibali hivi ambavyo tumevitoa kwa hawa wageni ambao wanafanya biashara ili kuzuia kuingia kufanya biashara ambazo ni fursa kwa Watanzania ili waweze kujipatia mapato yao.
Kwa hiyo, taasisi ambayo inatoa vibali vya kazi inazingatia sana vibali wanavyovitoa ili kuzuia mianya ya wageni kuja kufanya biashara za wananchi wa Tanzania ikiwemo biashara ndogo ndogo.
Mheshimiwa Spika, hili ndilo ambalo Serikali yetu imeweka mazingira ya wafanyabiashara wadogo kufanya biashara zao kwenye maeneo maalumu kama vile hapa Dodoma eneo la Machinga Complex, lakini maeneo mengine yote tulitoa kibali cha halmashauri kuandaa maeneo ya wafanyabiashara wadogo ili isaidie hata ukaguzi na ufuatiliaji tunaoufanya wa kukuta wageni ambao hawakupata vibali vya kufanya biashara hiyo, wanafanya biashara hiyo na huwa tunaendelea kuzuia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania na wafanyabiashara kwamba sera tunayo ya kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao kwenye ngazi za chini bila kuingiliwa na watu wa mataifa ya nje na ufuatiliaji huu unabaini haya yote na tunaendelea kuusimamia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa miongozo aliyoitoa kwa ajili ya kuimarisha biashara ndogo nchini na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wetu kufanya biashara kwa uhuru mkubwa kwa ajili ya kupata kipato chao, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mkuu, kutokuzingatia kwa sheria za barabarani na uzembe wa madereva wa bodaboda inatajwa kuwa ni sababu inayosababisha vifo vingi kwa Watanzania wengi hususan vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.
Je, Serikali ina jitihada gani za makusudi kuhakikisha kwamba vijana wote waliojisajili katika vijiwe wanapata mafunzo sahihi ya usalama barabarani?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba tunao wajasiriamali ambao wanaendesha bodaboda ambao wanasaidia sana katika kuchangia pato la Taifa pale ambapo wanafanya biashara zao, lakini pia wanasaidia sana Watanzania kupata usafiri wa haraka wa maeneo mafupi mafupi. Wafanyabiashara hawa wameratibiwa kwenye maeneo mbalimbali, lakini pia wengine wako kwenye vijiwe.
Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya ili kuondoa au kupunguza sehemu kubwa ya ajali na kuwafanya wafanye shughuli zao kwa usalama?
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi na Usalama Barabarani wanaendelea kutoa elimu kwenye makundi haya ya bodaboda kwenye makundi ambayo yameratibiwa na yamesajiliwa na kwa miongozo ambayo imetolewa LATRA sasa wamepewa mamlaka ya kusajili vikundi vyote vya vijana wa bodaboda ili kuwezesha kuwafikia na kuwapa elimu ya usalama barabarani, lakini pia kuwasaidia katika kufanya biashara zao kwa usalama zaidi.
Mheshimiwa Spika, pia uko mpango unaoratibiwa na kila halmashauri kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuwaanzishia SACCOS na ushirika wao mdogo kwa ajili ya kuendesha biashara zao kwa usalama zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea kuratibu kundi hili la madereva bodaboda kwa lengo la kupeleka elimu zaidi, lakini pia kuwaanzishia ushirika mdogo mdogo ambao utaweza kuwasaidia kuchangia fedha na kuwaonesha maeneo ya kupta mitaji na kupanua wigo wa shughuli zao za kibiashara na za usafirishaji.
Mheshimiwa Spika, pia nitoe wito kwa madereva wetu wa bodaboda popote walipo, ni vema sasa wakaamua kukaa maeneo ambayo yako rasmi na yameainishwa na halmashauri ili iwe rahisi sasa kwa taasisi yetu ya LATRA kuwafikia na na kuendesha elimu pamoja na kuwapa fursa mbalimbali za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kuwahakikishia Watanzania kwamba, eneo hili ambalo limeonekana kuwa na ajali nyingi linaendelea kuratibiwa vizuri kama ambavyo nimesema na Wizara ya Mambo ya Ndani, Kitengo cha Usalama Barabarani kwa lengo la kuwafanya waweze kufanya shughuli zao kwa usalama mkubwa zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwa na kubadilika badilika kwa wakusanyaji wa kodi ya ardhi ndani nchi yetu kwa maana ya Serikali, kuna wakati kodi ya ardhi imekuwa ikikusanywa na TAMISEMI na kuna wakati kodi ya ardhi imekuwa ikikusanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wakati mwingine kodi hii imekuwa ikikusanywa na TRA.
Mheshimiwa Spika, kubadilika badilika huku kwa wakusanyaji wa kodi kumesababisha kukosa ufanisi kwenye makusanyo ya kodi ndani ya nchi yetu, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali inatoa kauli gani kuhusu jambo hili? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kwagilwa, Mbunge wa Handeni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria tuliyonayo sasa ukusanyaji wa kodi ya ardhi unafanywa na Wizara ya Ardhi yenyewe, Wizara ambayo imepewa mamlaka na Wizara ambayo inafanya kazi ya upimaji wa ardhi, kutoa vibali na inatunza kumbukumbu. Tuliona ni vema na Waheshimiwa Wabunge pia mmechangia pia katika kutunga sheria hii kwamba Wizara ya Ardhi yenyewe ikusanye na sasa tunaona mafanikio ya Wizara hii kukusanya kodi na uelewa wa Watanzania katika kulipa kodi unakuwa mkubwa na kwa hiyo, ukusanyaji unakuwa mzuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, suala la ukusanyaji wa halmashauri na TRA, miaka minne iliyopita hapa tulikutana na Waheshimiwa Wabunge mlitoa ushauri kwa Serikali. haikuwa ni kwa kodi ya ardhi, yalikuwa ni yale malipo ya tozo za nyumba (umiliki wa nyumba) ambayo pia na yenyewe tuliona kuwa ili kupata kodi ya nyumba za ngazi mbalimbali tukabidhi mamlaka iliyoko kule kule ambayo ni halmashauri na TRA iko kule kule kwenye wilaya. Kwa hiyo, hawa wakishirikiana pamoja ni rahisi kuzifikia nyumba zao kuliko Wizara ambayo imeishia tu Wizarani na haina tawi kubwa kule kwenye halmashauri. Hiyo ndiyo ambayo tulikuwa tumeipatia halmashauri na TRA. Hata hivyo, suala la kodi ya ardhi bado liko chini ya Wizara ya Ardhi na tunaona mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika, mimi nataka nimpongeze Waziri wa Ardhi kwa kuendelea kufanya maboresho kwenye eneo hili la makusanyo ambako sasa watu wanalipa kielektroniki. Sasa tunaona Watanzania wanapata bili zao kupitia simu zao za mkononi na wanalipa kupitia simu zao za mkononi. Kwa hiyo, makusanyo ya kulipa kodi yanakuwa makubwa kuliko sasa kuliko huko awali ambako tulikuwa tunatumia makaratasi zaidi katika kulipa kodi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania na kuwahamasisha Watanzania kulipa kodi, kodi ndiyo msingi wa maendeleo yetu. Tutakapoendelea kulipa kodi ni rahisi sana kwa Wizara kuratibu mipango mbalimbali ya maboresho ya uratibu wa ardhi kama ambavyo sasa tuna Mradi wa Upimaji wa Matumizi Bora ya Ardhi kwenye vijiji ili kila mmoja aweze kutambua eneo lake na anapotaka kulipa kodi ajue kwamba analipa kodi kwa eneo alilopewa na akiwa na hati yake kamili. Iwe ni hati inayotolewa na Wizara yenyewe au hati ya kimila, zote hizi ni sehemu ya vibali vinavyokuruhusu wewe umiliki ardhi na kukutaka sasa ulipe kodi kwa maendeleo ya Taifa letu, ahsante. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na maelezo ambayo umeyatoa ambayo yanaonesha msimamo wa Serikali lakini Ibara ya 15 (1) ya Katiba inatoa uhuru na inasema: “Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru”. Katika maelezo yako umesema kutaandaliwa kambi maalumu ya kuwaweka watu wenye ualbino. Sasa huoni kwamba kuwaweka katika makambi ni kuwanyima haki yao ya kuwa huru?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera yetu ya Serikali ni kuanza kuwalinda hawa wote wenye ulemavu wa aina yoyote ile ili pia na wao waweze kushiriki kwenye maendeleo ya Taifa letu wakiwa salama. Tunaendelea kutafuta njia mbalimbali ambazo zinaweza kuwafanya hawa kuwa salama zaidi, huku tukiimarisha ulinzi wao kwenye vyombo vyote vya ulinzi na usalama, hapa malengo yetu ni kutoa uhakika wa maisha yao wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia hizi mbalimbali tunazozitafuta wakati mwingine tunafikiria kwamba tukiwaweka pamoja wanakuwa salama zaidi, tukiwaweka pamoja tuna tatizo la kisaikolojia la kujiona wao ni walemavu. Tumeanza kufanya marekebisho ya vijana wote wenye ulemavu kote nchini kwamba, badala ya kuwapeleka kwenye shule maalumu ya watoto wenye ulemavu wa aina hiyo, tunajaribu sasa kuwachanganya kwenye shule za msingi na sekondari pamoja ili na wao washiriki pamoja kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, michezo wakiwa darasani na kila mmoja kwa ulemavu wake na sasa tumeanza kuona na tunaanza kupata mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunapoelekea kujaribu hili na kuona mafanikio haya pia Serikali imekwishaanza kutoa ruzuku kwa maana kunaongeza kwenye bajeti ya Wizara ya TAMISEMI kwenye kila Halmashauri. Tumewapelekea fedha katika kila Halmashauri ili fedha hii iende kwa wanafunzi walioko shuleni wenye uhitaji maalumu. Kwa mfano, tukiwa na mwanafunzi mwenye uono hafifu, fedha ile itatumika kununua fimbo lakini pia ule mtambo braille ya kuandikia na sasa hivi tuna kompyuta. Kwa hiyo, kila Halmashauri inawajibika kununua fimbo na braille kwa ajili ya vijana wetu ambao wana uono hafifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wenye ualbino tunanunua lotion (mafuta ya kupaka ngozi) na kununua kofia zinazosaidia kuzuia mionzi ya jua. Hili linaendelea kutekelezwa. Vilevile, kwa wale ambao wana tatizo la viungo (hawawezi kutembea) Halmashauri inawajibika kununua baiskeli kupitia fedha ile ili mtoto aweze kutembea, kushiriki na wenzake. Hata kwenye michezo tunaona pia kuna baiskeli za walemavu wanacheza michezo kama basketball na baseball. Kwa hiyo, tunaendelea kufanya haya tukijaribu kuona ni njia ipi itaweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aendelee kutupatia nafasi Serikali tuendelee kufanya tafiti na tathmini ni njia ipi nzuri zaidi inayoweza kuifanya jamii ya wenye ulemavu kushiriki kikamilifu pamoja na jamii husika kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika nchi yetu matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, wanawake na watu wengine wa makundi mengine umekithiri sana. Watu wanafanya na adhabu zinatolewa, lakini matukio hayo yamekuwa yakiendelea, sasa hivi hali imekuwa mbaya, watu wanalawiti mpaka wanyama. Nataka kujua Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuleta muswada Bungeni ili aidha, tuongeze adhabu, ama tubadili adhabu ili zitolewe adhabu zitakazokidhi haja ili matukio hayo yaweze kukoma kwani yamekuwa yakiathiri watoto wetu, wanawake wenzetu na watu wengine? Nakushukuru.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kwamba matukio kadhaa ya unyanyasaji wa kijinsia yapo na Serikali inachukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaokutwa wakitenda matukio haya ya unyanyasaji wa kijinsia. Matendo haya na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kwa sasa si Serikali pekee bali pia hata jamii inatakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea na kuchukua hatua kwa kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, kwa sababu matukio ya unyanyasaji wa kijinsia mengi yanatokana na ulevi wa vilevi holela ambavyo vinatumika vinavyoweza kumpotezea mtu uwezo wa kufikiri na kutafakari matendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, malezi ya watoto wetu kutoka ngazi ya chini na makuzi yao na namna ambavyo wazazi tunawajibika kulea watoto hawa. Pia, tunazo zile imani kwenye jamii zetu, watu wanaamini labda ukitenda tendo fulani unapata mafao, unapata utajiri, haya yanasukuma watu kufanya matendo ya unyanyasaji wa kijinsia. Pia kuna zile mila kandamizi za baadhi ya makabila. Haya niliyoyataja machache yanachangia sana kwenye utendaji wa matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua Mheshimiwa Mbunge, ameshauri kuchukua hatua kali zaidi kwa kuweka sheria kali na ikiwezekana sheria iletwe hapa ifanyiwe mapitio kwa ajili ya kuongeza ukali zaidi. Kwa kuwa, nimekiri kwamba tatizo lipo kwenye jamii kwa baadhi ya maeneo na hatua kali zinachukuliwa, inawezekana pia yanajirudia kwa sababu ya baadhi ya maeneo ambayo pia yana sheria, sheria zake bado si kali sana kwa sababu jambo hili ni mtambuka na linagusa Wizara nyingi na kila Wizara inaweka sheria yake katika kukinga jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napokea ushauri wa kufanya mapitio wa sheria hizi, malengo yetu ni kuhakikisha kwamba jamii inabaki kuwa salama na wale wote wanaotenda matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia wanaendelea kuchukuliwa hatua kali zaidi na tunatamani tuone jambo hili likikoma kwenye jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiase jamii yetu kuzingatia mila, desturi na tamaduni zetu ili tusiingie kwenye matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia kwa sababu kila mmoja ana haki ya kuishi, kupunguza ulevi holela ambao unaweza kusababishia watu wakalewa halafu wakatenda vitu visivyo, kwa sababu ukishalewa akili inakuwa siyo ile ya kawaida na hizi imani ambazo ziko kwenye baadhi ya makabila, mila potofu na malezi kwa mfululizo wake kama ambavyo nimesema awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nakiri kwamba, jambo hili tutaendelea kulifanyia mapitio na pale ambapo panahitaji mabadiliko ya sheria, kanuni, tutaleta Bungeni kwa ajili ya kufanya marekebisho zaidi ili tuweze kujipanga zaidi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa Serikali imekuwa inajitahidi sana kujenga vituo vya kutolea huduma ya afya kama hospitali za wilaya lakini kuna wilaya zingine ambazo zina majimbo zaidi ya moja, zingine zina majimbo mawili, zingine majimbo matatu, kwa sababu hiyo kunakuwa na matatizo ya upatikanaji wa huduma ya hospitali ya wilaya kutokana na umbali na jiografia za wilaya hizo. Je, Serikali haioni kwamba ifanye mkakati wa kujenga hospitali za ziada kwenye wilaya ambazo zina majimbo zaidi ya moja? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imefanya maboresho makubwa sana kwenye sekta ya afya kwa kujenga maeneo ya ngazi tofauti ya utoaji huduma za afya. Tumeanza na zahanati kila vijiji na kazi hiyo inaendelea kwenye halmashauri zetu kwenye vijiji pia tunajenga vituo vya afya kimkakati kwenye maeneo yetu ya halmashauri kama maeneo ya rufaa ya zile zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajenga hospitali za wilaya lakini kwenye hili kwa kweli nataka nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye katika kipindi chake cha uongozi aliona kuna umuhimu wa kujenga hospitali za halmashauri kwenye wilaya tukijua kwamba ziko wilaya zina halmashauri zaidi ya moja, kwa hiyo kila halmashauri inapata hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Mbunge anataka kujua hizi wilaya zenye halmashauri zaidi moja Serikali ina mpango gani? Tumeanza ujenzi wa hospitali za halmashauri, tumeanza awamu ya kwanza kwa zaidi ya halmashauri arobaini na kitu, tunaendelea na ujenzi wa hospitali kwenye halmashauri. Sasa tuna wilaya zina halmashauri moja, lakini ina majimbo zaidi ya moja na jiografia ya maeneo haya, unakuta maeneo ya jimbo yako kwenye halmashauri moja, lakini yako mbali na Makao Makuu ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalizungumza hili kwa sababu najua pia mazingira ya Jimbo la Mheshimiwa Mbunge anayeuliza pale Same, nimefanya ziara nimepita Same Magharibi ambako ni Makao Makuu ya Wilaya, lakini Same Mashariki mbali zaidi ya kilometa 100 ambako ndiyo jimbo lingine lipo na huko ndiyo kuna idadi kubwa ya wananchi, pia kuna uzalishaji mkubwa sana na wengine wako milimani. Ni ngumu kupata huduma za wilaya pale Makao Makuu ya Wilaya ambako tuna hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka hili liliingia kwenye mjadala tulipopeleka mgao wa kujenga hospitali ya halmashauri, lakini bado imejengwa tena Makao Makuu ya Wilaya. Sasa hili linawafanya wananchi walioko kule mbali kutopata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa halmashauri, kwa kuwa nia njema ya Serikali hii ni kusogeza huduma kwa wananchi na wananchi wa Same Mashariki wako mbali sana na Makao Makuu ya Wilaya na huduma ziko Makao Makuu ya Wilaya, nashauri Halmashauri ya Wilaya kupitia Ofisi ya RAS, Mkoa wa Kilimanjaro watuandikie sasa Serikali, waeleze mazingira hayo ili kwenye mgao unaofuata tuifikirie Same Mashariki kupata hospitali yenye hadhi ya wilaya huko huko Same Mashariki ili wananchi wale wasipate usumbufu tena wa kuja Same Magharibi ambako ndiko Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini litaweza kutatua tatizo hili kwenye halmashauri kama hiyo ya kwako na halmashauri nyingine ambazo zina mazingira haya. Tukiwa tunaelekea awamu ya pili watuandikie waeleze sababu na wataalamu watakwenda kuangalia sababu hizo, pale ambako sababu zinakidhi, Serikali iko tayari kuendelea kusogeza huduma kwa wananchi kama ambavyo imeelezwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kumekuwepo na ongezeko kubwa la leseni za utafiti na hasa katika maeneo ya madini hapa nchini. Leseni hizi zimekuwa zikitolewa kwa wageni wa nje, lakini leseni hizi kwa sehemu kubwa zimekuwa zikihodhi maeneo makubwa ambayo wachimbaji wadogo wamekuwa wakifanyia shughuli zao za kuendeleza maisha yao na shughuli za uchimbaji kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini mpango wa Serikali wa kudhibiti utaratibu huu wa kuhodhi maeneo makubwa na hivyo kufanya kuwanyima nafasi ama fursa hawa wachimbaji wadogo ambao wanajishughulisha na uchimbaji wa madini hapa nchini? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwenye Sekta ya Madini sasa fursa zimeanza kuonekana na Watanzania wanapenda kuingia kwenye fursa hizi ili kujipatia kipato. Tumeona matamanio ya makundi mbalimbali kutaka kuchimba, Watanzania wenyewe kwa makundi mbalimbali wakiwepo vijana, wachimbaji wadogo, pia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, nao wanatamani kuwekeza. Tunayo makundi ambayo yanaendelea kufanya tafiti na Wizara yenyewe imeimarisha kitengo cha utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita hapa wakati wa hoja ya Waziri Mkuu, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Mavunde kwenye mchango wake kwenye hoja ya Waziri Mkuu alilieleza vizuri hili akieleza nia ya Serikali na mpango wa Serikali wa kuimarisha kupata maeneo mengi kwa wajasiriamali wadogo au wachimbaji wadogo. Yako maeneo makubwa yametwaliwa na wanaofanya utafiti kwa muda mrefu na hakuna kazi inafanywa, hakuna matokeo lakini wengine hawajalipia gharama za kumiliki na kufanya kazi hiyo. Mheshimiwa Waziri ameshatoa maelekezo kwenye ofisi za mikoa kufanya mapitio ya leseni zote za utafiti na maeneo makubwa yaliyogawiwa kwenye maeneo hayo ambayo mpaka leo hakuna kazi yoyote inayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kwamba, maeneo hayo yaliyokaliwa kwa muda mrefu tunataka tuyatwae yote, halafu tuyagawe kwa wachimbaji wadogo ili kupanua wigo wa vijana wetu kupata nafasi na fursa ya uchimbaji ili waweze kupata nafasi hiyo. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kufanya mapitio baada ya agizo la Wizara kwa watu wa Mikoa. Niwaagize sasa Makamishna, Meneja wa Mikoa wa Madini wakamilishe kazi hiyo haraka sana. Tutambue maeneo makubwa yanayofikiriwa ambayo yanafanya kazi, ambayo tumetoa leseni lakini hayajalipiwa ili tufute leseni hizo na tuanze kufanya mgao upya kwa wenye uhitaji wakiwemo wachimbaji wadogo ili nao wapate nafasi ya kuchimba kwenye maeneo hayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na wadau ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na majanga kama vile moto, hasa katika majengo ya umma pamoja na majanga ya asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na mrejesho usioridhisha wa matumizi ya michango hiyo na hivyo kusababisha kutokamilika kwa miundombinu iliyokusudiwa kurejeshwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha michango hiyo inasimamiwa ili kutokatisha tamaa wadau pamoja na Serikali ambao wamekuwa na nia njema ya kuhakikisha majengo hayo hasa ya umma yanarejea katika hali ya asili ili shughuli za umma ziendelee? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, majanga ya moto na maafa ya aina yoyote yale ambayo pia wadau au Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kuwawezesha waathirika, yote haya tunaweka kwenye kundi moja linashughulikiwa na Kamati za Maafa. Serikali imeweka utaratibu wa Kamati za Maafa kwa ajili ya kushughulikia majanga hayo kwenye ngazi ya vijiji, kata, wilaya pia mkoa na ile Kamati ya Taifa ya Maafa ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Huku chini wale wakuu wa maeneo yale ndiyo Wakuu wa Kamati zile za Maafa.
Mheshimiwa Naibu Spika, panapotokea majanga kama moto umesema Mheshimiwa Mbunge, tumeona baadhi ya masoko yanaungua, majengo ya utoaji huduma wa umma yanaungua. Majanga haya yanaanza kuratibiwa na ngazi husika tukio linapoanza. Kama kunakuwa na michango ya aina yoyote ile kuwezesha miundombinu kurudi kwenye hali yake inaratibiwa na ngazi husika. Baada ya michango hiyo ambayo imechangiwa na wadau, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa kama ngazi ya wilaya, Mkuu wa Wilaya anapaswa kuwajulisha wadau wake waliochangia pia kazi iliyofanywa kurejesha miundombinu hiyo na vilevile katika ngazi ya mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ndiyo inaratibu maafa kitaifa, jukumu lake ni kuona kama mwenendo wa utoaji huduma unaendelea na wakuu wa maeneo hayo wanatoa mrejesho kwa jamii iliyochangia ili kuwajengea imani wakati mwingine likitokea jambo kama hilo waweze kujitokeza kutoa mchango kwa jamii hiyo. Nitoe mfano, soko lililokuwa limeungua Kilimanjaro, Serikali ilichangia pia wadau walichangia kwa hiyo ni jukumu la Mkuu wa Wilaya wa Moshi Manispaa kutoa mrejesho wa michango waliyoipokea ili kuwatia imani wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa Kusini kule Lindi, shule ya sekondari iliungua pale na nilisimama jukwaani kuhamasisha watu kuchangia, lakini michango ile haikwenda Ofisi ya Waziri Mkuu, ilibaki Ofisi ya Mkoa ambaye ndiye mratibu. Kwa hiyo Mkuu wa Mkoa wa Lindi anawajibika kutoa taarifa kwa wananchi wa Manispaa ya Lindi, kwanza kuwaonesha kazi iliyokusudiwa na kiwango cha fedha kilichotumika na tathmini itafanywa na wadau. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kuwapa imani wachangiaji ili waendelee kuchangia. Kwa hiyo utaratibu wetu uko wazi, kila ngazi inapaswa kutoa taarifa. Hata haya mafuriko ambayo leo yamejitokeza Mkoani Morogoro katika maeneo ya Kilombero ambako jana nilienda, kule Mkoani Pwani (Rufiji na Kibiti), michango mingi sana imeenda, lakini inaratibiwa na Kamati ya Maafa ya Mkoa. Kamati ya Taifa inakwenda kuona kama shughuli za utoaji huduma zinaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jukumu la kutoa mrejesho ni ngazi ya mkoa na ngazi ya wilaya ambao ndiyo wako pale na wadau. Wanapaswa pia kutoa taarifa kama mrejesho wa hatua ambazo zimechukuliwa katika kurejesha hali kama ilivyokuwa. Kwa hiyo utaratibu huo uzingatiwe na natoa wito sasa kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wote nchini, Wakuu ya Wilaya ambao ndiyo Wakuu wa Kamati za Maafa kwenye maeneo hayo, kutekeleza wajibu wao wa kutoa mrejesho wa michango iliyochangwa na jamii ili jamii iweze kuhamasika kutoa michango zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mkoani Manyara eneo la Hanang nako pia mrejesho utolewe ili wadau waliochangia kutoka maeneo yote wapate imani kwamba michango iliyotolewa imeenda kutumika kama ilivyokusudiwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunakushukuru sana kwa kutembelea Kilombero, tunaomba utusaidie. Swali langu ni kuwa nchi yetu ina utajiri mkubwa sana wa mabonde mengi makubwa ambayo yanaweza kuendelea kutumika kwa kukuza kilimo, kuhifadhia maji na kadhalika. Mfano Bonde la Rufiji, Kilombero, Mbarali na mengine. Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mabonde haya yamekuwa ni changamoto kubwa sana kwa wananchi. Je Serikali ina mkakati gani wa kina wa kuyaendeleza mabonde haya ili tuendelee kunufaika nayo zaidi? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asenga, Mbunge wa Ifakara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mabonde mengi nchini na mabonde yote tumeyapangia mkakati wa kuyaendeleza ili yaweze kuleta manufaa kwa jamii inayoishi karibu na maeneo haya ya mabonde. Tumeunda Mamlaka za Mabonde, hata Bonde la Kilombero lina Mamlaka ya Bonde Kilombero, tuna Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji, Ruvuma na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka hizi zinasimamia na kuratibu mikakati ya kufanya maboresho ambayo Wizara yoyote ile ya kisekta ikitaka kutumia bonde hilo, basi ile Mamlaka ilishaweka mpango mkakati ambao Wizara hiyo inaweza kuingia. Inaweza kuwa Wizara ya Kilimo, wanayo fursa ya kuendeleza bonde hili kwa kilimo cha umwagiliaji, Wizara ya Maji wanaweza kulitumia bonde hilo na Mamlaka ile kwenda kuchimba mabwawa ya kupatia maji. Watu wa mifugo nao wanaweza kutumia bonde lile kwa kujenga mabwawa kwa ajili ya kunyweshea mifugo na kadhalika na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mpango wa Serikali upo, mzuri tu wa kuboresha mabonde haya na kuleta manufaa kwa jamii. Kwa mfano, tunalo Bonde hapa la Mto unaotoka Kondoa unapita Chemba kwenda mpaka Bahi ambao unatiririsha maji. Tumeamua kujenga, kutumia Bonde lile kupata manufaa ya kuleta maji Dodoma Mjini. Tunajenga Bwawa la Farkwa, kubwa sana ambalo litapokea maji na kuyaleta hapa mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutaendelea kuyatumia mabonde hayo kwa maslahi ya wananchi, tutaendelea kubuni njia mbalimbali za kutumia mabonde haya ili yaweze kuwanufaisha wananchi wake. Kwa hiyo mpango wa Serikali upo na tunaendelea kutumia mabonde haya vizuri ili tuweze kunufaisha jamii. Hata kule Kilombero jana nilikuwa kwenye semina ya wadau wa kilimo, kulikuwa na kongamano la kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya taarifa ambayo ililetwa mbele yangu pale kama Mgeni Rasmi, ni uendelezaji wa maboresho ya miradi ya umwagiliaji, Bonde la Kilombero ambako tayari mabwawa kadhaa yameshaandaliwa. Yataanza kuchimbwa wakati wowote ule kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wa Kilombero na wengine kwenda kulima kwa kutegemea kilimo cha umwagiliaji kupitia bonde hilo. Hiyo ndiyo mipango iliyopo kwenye mabonde yetu yote hayo. Ahsante sana.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na matukio ambayo yanaashiria uvunjifu wa haki za binadamu. Matukio haya ni pamoja na mauaji, utekaji lakini pia utekaji na uuaji wa watoto. Matukio haya yamekuwa na sura tofauti tofauti ikiwepo wivu wa kimapenzi, lakini pia ushirikina na matukio mengine ya kutekwa na kupotea kwa watu yanahusishwa na vyombo vya dola.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua mkakati wa Serikali, moja kuzuia matendo haya, lakini kuondoa taharuki ambayo inajitokeza kwenye jamii. Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuanza na ufafanuzi huo ili Watanzania waweze kujua. Nataka nieleze tu kwamba tunapoilinda nchi ni wajibu wetu Watanzania wote kwa kushirikiana na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Spika, tunavyo vyombo vya ulinzi na usalama nchini vyenye jukumu la kupokea taarifa mbalimbali zinazoonesha uvunjifu wa amani popote pale kadri taarifa zinavyokuja pale kwenye meza za vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Jukumu lao hawa wakishapokea taarifa ni kuhakikisha kwanza wanafanya uchunguzi na uchunguzi utakapobaini waliotenda makosa wanachukuliwa hatua kwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Spika, Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kujikita kusimamia misingi ya amani katika nchi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi. Pia tumeendelea kujikita kwenye misingi yetu ya amani na ulinzi kwa gharama yoyote ile kuhakikisha kwamba mipaka yetu, raia wetu lakini na mali zao zinabaki kuwa salama na hiyo ndiyo inayoleta amani katika nchi. Kwa hiyo, niwahakikishie Watanzania kwamba suala la ulinzi na usalama bado lipo mikononi mwetu pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunasaidia vyombo vya ulinzi kwa kutoa taarifa zozote zile ambazo zinaleta tishio la amani katika nchi ili kuvisaidia vyombo vyetu viweze kuchukua tahadhari na hatua stahiki ili kuwabaini wale wote ambao wanasababisha kutokuwepo kwa amani kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, pia nitoe wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na wajibu wao wa kuhakikisha kwamba kila taarifa inayopatikana lazima ifanyiwe uchunguzi, lakini pia na kubaini wale wote ambao wanahusika kama wanapatikana wachukuliwe hatua mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nashukuru sana kwa maelezo yako ya msingi ya awali ili kuondoa upotoshaji ambao unaweza kuwa unaendelea na kufanya vyombo vyetu vishindwe kufanya kazi yake halafu tukawavunja moyo hawa watu ambao wanafanya kazi masaa 24 kwa ajili ya ulinzi ambao leo unatufanya hapa tubaki salama.
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu, swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu inaamini katika uongozi wa kisheria na utawala bora ili kujenga umoja, mshikamano na upendo baina ya wananchi na Serikali yao, lakini kumekuwa kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya wateuliwa wa Mheshimiwa Rais, Wakuu wa Mikoa na baadhi ya Wakuu wa Wilaya kwa kutumia nguvu na mamlaka yao vibaya kukamata viongozi na wananchi na kuwatupa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kujua kwanza jambo hili moja, limetengeneza chuki kubwa baina ya wananchi na Serikali yao, lakini pili, linafifisha jitihada kubwa za Mheshimiwa Rais za kuhubiri 4R. Linatengeneza chuki kubwa, mwisho wa siku hili jambo linakuwa halileti mantiki. Nataka kujua kauli ya Serikali ni ipi katika kukemea jambo hili ambalo linatengeneza chuki kubwa baina ya Watanzania na Serikali yao. Je, ni ipi kauli ya Serikali kwa hawa watawala ambao wanatumia mamlaka yao vibaya kutesa na kuwanyanyasa wananchi?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali hili analoliuliza Mheshimiwa Mbunge ni lile ambalo jana Mheshimiwa Kunambi, Mbunge wa Ifakara eneo la Mlimba aliliuliza jana na Mheshimiwa Spika, alitupa kazi Serikali kulifanyia kazi. Tutakapokamilisha tutatoa majibu kwa Mheshimiwa Mbunge na naamini kwa majibu hayo pia tutamjibu na Mheshimiwa Fiyao.
Mheshimiwa Spika, kwa utangulizi ni kwamba ni kweli baadhi ya watawala kwenye maeneo yao wanazo sheria ambazo zinawaruhusu kuhakikisha kwamba hali ya utulivu na ulinzi wa usalama kwenye maeneo yao inaimarika na kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba baadhi ya wateuliwa.
Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie wale waliotamkwa jana, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ambao pia ipo sheria wanaitumia. Jana ulisimama ukafafanua vizuri na nataka kuungana na wewe kuuhakikishia umma wa Tanzania kwamba sheria ile inayomruhusu Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya kumkamata mwananchi au yeyote yule kumweka ndani haikulenga kama ambavyo baadhi wanaitumia. Lengo ni katika kuhakikisha kwamba mazingira hayo kusitokee uvunjifu wa amani mkubwa na kwa hiyo anaweza akatumia sheria hiyo kumhifadhi mahali ili hali itulie na baadaye aweze kutoka na kuendelea na majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, anaweza kuwa tishio lipo kwa Mkuu wa Wilaya mwenyewe au Mkuu wa Mkoa mwenyewe anaweza kutumia nafasi hiyo ili kulinda, inaweza kuwa jambo hilo ni hatari kwa wananchi anaweza kuitumia nafasi hiyo kulinda usalama wa raia wale lakini pia hata huyo huyo mwananchi ambaye analeta hiyo hoja kulinda usalama wake, basi sheria inaweza kutumika kwa yeye kumwondoa eneo lile na kumhifadhi mahali.
Mheshimiwa Spika, jambo hili limeshazungumzwa mara kadhaa hapa Bungeni, jambo hili tumeshatoa ufafanuzi mara kadhaa hapa Bungeni na tulitaka tuchukue hatua. Nataka nikuhakikishie kwamba wiki mbili, tatu zilizopita Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wote waliitwa hapa Mkoani Dodoma kwa semina katika maeneo mbalimbali. Eneo hili la sheria hii limezungumzwa sana na wameelimishwa sana na tunaamini sasa watakuwa wanaelewa namna ya kuitumia sheria ile bila kuleta madhara, bila kuleta chuki miongoni mwao na wananchi na bila kuleta mtafaruku katika jamii ili waweze kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, hata kama anatumia sheria hii mashariti yake ni kwa masaa 24 ambayo baada ya masaa 24 anatakiwa kutoa taarifa ya kwa nini yule aliyepo ndani kawekwa na kuwezesha chombo husika kuchukua hatua. Kama hana jambo lolote anatakiwa baada ya masaa 24 yule aliyeingizwa polisi anatakiwa aondoke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jana tumefuatilia kule Kilombero tumeona wale watuhumiwa wote wameshapelekwa Mahakamani. Kwa hiyo jambo lile hatuwezi kulizungumza tena kwa sababu tayari hatua zimeshachukuliwa na sasa hivi wapo Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, jambo hili tutaendelea pia kuelimisha wateule wote wenye sheria hizi ili waweze kuzitumia kwa weledi, lakini kwa uaminifu na uadilifu kuzingatia sheria na taratibu za nchi ili pia kuleta amani katika jamii bila kuleta msuguano, migongano isiyokuwa muhimu ili kuwezesha kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo maelezo ya msingi kwa awali. Tutakavyopata taarifa zilizokamili ya tukio hili lilikuwaje ili tuweze kuhusisha swali la Mheshimiwa, hoja ya Mheshimiwa Kunambi na Mheshimiwa Stella Fiyao, wote Waheshimiwa Wabunge tutawapa taarifa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata fursa hii kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kumekuwa na changamoto ya watoto wenye ulemavu kutokupata huduma za kunyooshwa na kurekebishwa viungo katika maeneo mbalimbali nchini. Sasa hii inapelekea ongezeko kubwa la watoto wenye ulemavu na ongezeko la watu wenye ulemavu. Je, ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha wanaweka vituo katika kila mkoa ili mtoto pale anapozaliwa aweze kupata huduma hii? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kadija Taya, maarufu Keysha, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, masuala ya afya hapa nchini kwa sasa yameimarishwa sana na uwekezaji mkubwa umefanywa. Kwa mujibu wa tafiti zetu ndani ya Wizara ya Afya imeelezwa kwamba hatua mbalimbali za mama mjamzito kabla hajajifungua zinaweza kubaini aina ya ulemavu wa mtoto alionao na uwezekano wa kupunguza ulemavu kwa zaidi ya 80% inawezekana. Kwa maana hiyo kwa uwekezaji ambao sasa Serikali umeufanya kutoka ngazi ya zahanati, vituo vya afya lakini hospitali za wilaya, hospitali za mkoa, kanda na kitaifa; siyo tu kuamua hospitali moja katika mkoa ndiyo iwe inashughulika na kutoa huduma kwa walemavu, ni vituo vyote vinavyotolea huduma vinatakiwa kupata vifaa na vifaa vimeshapatikana na sasa kila eneo huduma hii inaweza kutolewa ya kupunguza uwezekano wa mtoto kuwa na ulemavu kama nilivyosema ulemavu huu unaweza kuepushwa kwa zaidi ya 80%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo huduma hizi zinapatikana sasa kuanzia vituo vya afya mpaka huko juu kwa kutoa wito kwa wamama wajawazito kuhudhuria kliniki ambayo itasaidia kupata elimu, lakini na uchunguzi wa mara kwa mara mpaka anapojifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtoto anapobainika amezaliwa ana ulemavu bado wataalam wetu wa afya kupitia vituo vyote vya utoaji huduma wanaweza kulifanyia kazi hilo kutoka umri mdogo wa mtoto mpaka umri ambao ulemavu huu unaweza ukapunguzwa kwa zaidi ya 80%. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili halihitaji ku-specialize hospitali moja kwenye eneo, kwenye mkoa ni kila eneo la utoaji huduma kuanzia zahanati na kuendelea. Pale ambapo mama anahudhuria kliniki tunaweza kubaini na tunaweza tukaanza kazi ya kuokoa ulemavu huo kwa zaidi ya 80%. Hayo ndiyo majibu ya Serikali. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Uchumi wa dunia sasa unabadilika na unajielekeza kwenye digital economy, kwa maana ya uchumi wa kidigitali. Katika hili vijana wengi wa Kitanzania wamekuja na ubunifu wa aina mbalimbali. Wapo waliobuni mifumo ya kufanya kazi mbalimbali, wapo hata waliotengeneza umeme. Changamoto kubwa ya vijana wetu inakuwa ni mtaji wa kukuza ubunifu wao kuwa bidhaa.
Mheshimiwa Spika, sasa zipo nchi mbalimbali zimeanzisha mifuko ya ubunifu (innovation funds) ikiwemo Kenya na Ethiopia. Je, nchi yangu ipo tayari sasa kuanzisha Mfuko huu kwa ajili ya kuwasaidia vijana wa Kitanzania wenye ubunifu kupata mitaji ili kuendeleza ubunifu wao?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric Shigongo, Mwandishi wa Magaziti pendwa, Mbunge wa Buchosa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake linahitaji kujua, kwamba Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Mfuko ambao utawasaidia wabunifu ndani ya nchi kuendelea na majukumu yao. Ametoa mifano kutoka katika nchi nyingine. Nataka nimhakikishie kwamba Serikali ilikwishaanza mkakati huu muda mrefu wa kuhakikisha kwamba kwanza tunawatambua wabunifu kwa kuanzisha maonesho mbalimbali ya wabunifu mbalimbali kuwaleta pamoja kuja kuonesha kazi. Hili linasimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo kwa miaka sita sasa inakuwa na maonesho kila mwaka ya kuwaleta wabunifu pamoja ili kuonesha kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeshaanzisha Mifuko inayoweza kusaidia wabunifu hawa kufanya kazi yao kwa uhakika zaidi. Moja, Tume ya Ubunifu (COSTECH). Tume ile inayo pia Mifuko miwili; Mfuko wa kwanza ni wa utafiti wa wabunifu. Watafiti wote wanaobuni kazi zao Mfuko ule una fursa nao ya kwenda kupata msukumo wa kuendelea na utafiti wao. Sasa upo ule Mfuko wa jumla wa wabunifu ambao pia baada ya kuwa umebuni kazi yako unataka kuiendeleza, ukienda pale COSTECH unakuta kuna dirisha linaweza kutoa mitaji ya kuendeleza ubunifu ulioubuni.
Mheshimiwa Spika, hatujaishia hapo, pia Wizara ya Elimu yenyewe inao Mfuko ambao unawawezesha wabunifu kufanya kazi zao. Miaka yote hii inaposimamia maonesho ya ubunifu Wizara ya Elimu inachangia sana ubunifu huu kukua. Vijana wengi sasa waliopo shuleni kwenye shule zetu za msingi, sekondari wameweza kunufaika na Mfuko huu kwa ajili ya kuandaa ubunifu wao na kwenda kuuonesha kwenye jamii.
Mheshimiwa Spika, Wizara kadhaa ikiwemo na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Wasanii wabunifu wanao Mfuko wao, Mfuko wa Ubunifu wa Sanaa na Utamaduni ambao pia upo kwenye Wizara hiyo na Mifuko mingine ambayo inaweza kuwezesha wabunifu hawa kupata mitaji ya kuendeleza ubunifu wao, hiyo ipo.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali imefungua milango ya kwenda kuzungumza na private sector, taasisi za fedha ili ziweke dirisha na dirisha tayari lipo, lipo CRDB, NMB, AZANIA, NBC na Benki nyingine. Kama Mwanga hapa Dodoma nayo pia imefungua dirisha linalowaruhusu wabunifu kwenda kupata mtaji na kubuni kazi zao.
Mheshimiwa Spika, sasa Mifuko hii niseme tu kwamba tumepata wazo zuri na ushauri mzuri na Mheshimiwa Eric Shigongo tutahakikisha kwamba kwanza inabidi tuutangaze na kujua namna hatua ya kupata mitaji hiyo ili itoe fursa ya wabunifu wote sasa kwenda kupata mitaji hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kushauri haya nataka nikuhakikishie kwamba tutalifanyia kazi kwa sababu sasa Serikali imeweka msisitizo wa ubunifu kwa Watanzania na tumeona mafaniko yake makubwa. Nataka ubunifu huu uendelee na utengeneze kazi waingie kwenye masoko na iwasaidie wabunifu kupata masoko ya kazi yao. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SALIM A. HASHAM: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa kuwa nchi yetu imejipambanua sana kwenye uwekezaji na wawekezaji wengi wamekuwa wakiingia kwa ajili ya uwekezaji, lakini kumekuwa na hali duni katika maeneo ya barabara pamoja na huduma za afya. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inaboresha huduma hizo ili kuwezesha uwekezaji zaidi katika nchi yetu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salim, Mbunge wa Ulanga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ninapoelekea kujibu swali hili kwanza nataka nimpongeze Mheshimiwa Salim yeye ni mwekezaji mkubwa hapa nchini. Amewekeza kwenye madini, lakini pia na viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwenye mazao ya kilimo. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la uwekezaji nchini limepata msukumo mkubwa baada ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuonesha dhamira ya dhati nchini ya kupanua wigo wa uwekezaji kwa kuwashawishi Watanzania kuwekeza, lakini pia na mataifa ya nje kuwekeza nchini. Alipokuwa anatoa msukumo huu tayari Serikali ilishakuwa na mwelekeo mzuri. Kwanza kisiasa, siasa yetu inaruhusu uwekezaji hapa nchini; mbili, tuliimarisha Sera ya Uwekezaji ambapo tumetoa fursa kwa Watanzania na mataifa ya nje kuingia nchini kuja kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeweka sheria na kanuni nzuri tu ambazo zinaruhusu uwekezaji na kumletea faida mwekezaji, yeye mwenyewe ni shahidi kwa sababu yeye ni mwekezaji. Kwenye eneo hili Serikali ilishapunguza hata gharama ya uwekezaji kwa Watanzania kutoka dola 100,000 mpaka dola 50,000, ambayo tayari una uwezo wa kuwekeza na wale wa nje tuliwapunguzia kutoka dola 200,000 mpaka dola 100,000. Hii inaruhusu wawekezaji wengi kuingia nchini. Tunataka tuone uzalishaji unakuwa mkubwa ndani ya nchi ili tupeleke bidhaa zetu nje.
Mheshimiwa Spika, pia, tunapotoa wito wa uwekezaji Serikali imejiimarisha katika kutoa huduma muhimu kwa wawekezaji. Moja, nishati ya umeme ya kuendesha viwanda, sasa hivi tuna umeme mwingi wa kutosha na bado Bwawa la Mwalimu Nyerere linaendelea kufunguliwa milango ya kuzalisha umeme. Sasa hivi tupo mlango wa tatu na kila mlango unatoa megawati 235; na tunaendelea mpaka milango yote tisa. Hii nchi tutakuwa tupo mbali sana, tutakuwa na umeme mwingi wa kutosha na unaopatikana kwa uhakika, hilo hatuna mashaka nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la usafirishaji, ili mwekezaji aweze kusafiri yeye mwenyewe na bidhaa zake Watanzania wote mnajua tuna network yetu nzuri tu ya barabara nchini. Kila Mkoa unafikika kwa barabara ya lami na kule vijijini tunaimarisha barabara za vumbi. Pia, kwenye maji tuna meli, tumeshajenga Ziwa Victoria na Ziwa Nyasa. Wote mnajua kwamba Ziwa Nyasa, sasa meli inakwenda mpaka Malawi, Ziwa Tanganyika tunajenga meli na bandari tumeziimarisha.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la huduma ya afya kama alivyosema, mwenyewe na Watanzania wanajua kwamba tuna zahanati ambazo zimeimarika na tunaendelea kujenga zahanati, vituo vya afya Hospitali za Wilaya na Halmashauri mpaka ngazi ya Kitaifa. Kwa hiyo, mwekezaji akija nchini hatuna mashaka na huduma zinazoweza kumwezesha yeye kuishi ndani ya nchi lakini pia kupata huduma pale anapopata tatizo yeye na wafanyakazi wake kwa sababu Serikali imejiimarisha kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa niendelee kutoa wito kwa wawekezaji wote wa ndani kwa Watanzania na walioko nje ya Tanzania kuja Tanzania, kuja kuwekeza kwa sababu tuna rasilimali za kutosha ambazo pia na sisi wenyewe tunazitumia hapa ndani na zinafaa pia kuja kuwekeza ili tuweze kuzalisha bidhaa nyingi na tuzipeleke nje ya nchi tuweze kupata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Salim, kwamba uwekezaji wake hatapata hasara na wawekezaji wengine wote hawatapata hasara. Serikali ipo pamoja na wao pale wanapopata tatizo wasisite kutuona ili tuweze kutatua tatizo la uwekezaji hapa nchini. Ahsante sana
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa swali ili niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu sote kwamba vijana ni kundi muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi wa nchi yetu. Hivi karibuni kumeibuka wimbi kubwa la vijana kulewa sana wakati wa kazi wakati wa mchana na hii ni kutokana na uingizwaji wa vilevi vikali sana kutoka nje ya nchi, lakini vilevi ambavyo vinapatikana kila mahali kiasi kwamba kijana anaweza kwenda gengeni akamiminiwa kakinywaji kidogo baada ya hapo analewa kabisa na kushindwa kuendelea na kazi. Je, Serikali ina kauli gani juu ya udhibiti wa vileo hivi vikali ambavyo vinaathiri uchumi wa vijana na vinaathiri ujenzi wa uchumi wa nchi yetu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inao utaratibu unaowezesha kutambua uzalishaji, uuzaji lakini pia kudhibiti bidhaa ya vileo inayoingia hapa nchini. Vileo hivi vinaendelea kusambaa kwa wateja kwa utaratibu uliowekwa wa wanaopata vibali vya biashara na kuendesha biashara za vileo. Serikali yetu inaendelea kutoa elimu kwa jamii yetu, ile ya kuelekeza au kuonesha madhara ya ulevi uliopitiliza, ikiwemo na hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, kwamba vijana wengi wanalewa wanakosa uwezo wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kwenye hili siachi kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amefanya kazi kubwa ya kuhamasisha vijana kujiunga pamoja na kutengeneza makundi yanayoweza kufanya shughuli za ujasiriamali. Vipo vikundi vya ujasiriamali vya mtu mmoja mmoja pamoja na vya pamoja wanaofanya biashara kwa siku zima na vinawapatia mapato. Utaratibu huu umesaidia sana vijana wetu kupata pato linaloendesha yeye na jamii yake.
Mheshimiwa Spika, tumeona hapa Dodoma Machinga Complex vijana wa kawaida wapo pale wanafanya biashara zao. Tumeona kila Wilaya waendesha bodaboda, bajaji, wafanyabiashara za kawaida na machinga. Hii yote ni jitihada za Mheshimiwa Rais katika kuhamasisha kwamba wanakaa pamoja na kutafuta shughuli ya ujasiriamali. Sasa hivi tunaendelea kuwahamasisha nchini kwa vijana wote kuingia kwenye shughuli ambazo zinawazalishia mali kuliko kuingia kwenye makundi ambayo hayana tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ni nini kinafanyika; ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii hii kuhakikisha kwamba wanaingia zaidi kwenye shughuli za uzalishaji mali huku pia tukiimarisha sheria kwa wazalishaji wanaoingiza bidhaa za vilevi ndani ya nchi, wauzaji na watumiaji, hasa kwenye maeneo yale ya wanaokiuka sheria maana tunazo sheria zetu. Kwa hiyo wale wanaokiuka sheria huwa tunawachukulia hatua. Hii inasaidia kupunguza kuingiza kwa pombe ambayo ni kali kupitiliza kiasi. Malengo yetu ni kwamba kila aina ya kileo kinachoingia nchini kinakidhi mahitaji ya afya ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jamii itusaidie kutambua uingizaji na utengenezaji wa bidhaa usiokuwa rasmi ambao haujapata vibali. Hawa ndio wanaotengeneza bidhaa hiyo ambayo ni kali kupita kiasi bila kutambuliwa na wale wote ambao wana leseni wanatengeneza bidhaa ambayo nayo imepimwa na inakidhi mahitaji ya afya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe wito kwa taasisi zote zinazofanya shughuli za vijana kuendelea kuwaelimisha vijana hawa maadili mema na pia kuendelea kutoa elimu stadi za maisha kwa vijana hawa. Muhimu zaidi kutoa elimu ya ujasiriamali kwa lengo la kuwaonesha kwamba njia nzuri sahihi ni hii ambayo utakuwa unajishughulisha, unapata pato kuliko njia hii ya kuendelea kula viroba ambavyo baadaye vitamlaza siku zima; hana mtaji hawezi kupata mafao, hawezi kupata kujikimu kwenye familia. Huu ndio mpango mkakati ambao Serikali tunao, wa kuhakikisha kwamba vijana wetu tunawapa fursa za kushiriki kwenye ujasiriamali ili waachane na shughuli nyingine waendelee kwenye ujasiriamali. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kufuatia uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Elimu uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika shule za sekondari na shule za msingi na shule mpya nyingi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga nyumba za walimu kuziba upungufu au ombwe la nyumba za walimu katika shule zote za sekondari na msingi nchini? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Maige, Mbunge wa Tabora, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye Sekta ya Elimu. Tumejenga miundombinu mbalimbali kwenye Kurugenzi ya Msingi, lakini pia miundombinu mbalimbali kwenye Kurugenzi ya Sekondari. Tunaendelea kubaini mahitaji ili tuweze kujenga miundombinu mingine ikiwemo na nyumba za walimu.
Mheshimiwa Spika, nataka nieleze mkakati wa Serikali unaenda kwa awamu, tulianza na ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na matundu ya vyoo kuruhusu wanafunzi kwenda shuleni. Kwa upande wa sekondari tumeendelea kujenga maabara ili waweze kusoma masomo ya sayansi, tumejenga majengo ya utawala ili walimu wapate nafasi ya kukaa na kusimamia shughuli za masomo na sasa tunaingia kwenye phase ya ujenzi wa nyumba za walimu ili walimu waweze kuishi maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wote mnatambua bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI mliyopitisha kipindi kilichopita, sasa tunaingia kwenye awamu ya ujenzi wa nyumba za walimu. Kwa hiyo, huo ndiyo mkakati ambao Serikali unao wa ujenzi wa nyumba za walimu kupitia bajeti hii. Migawo itakapoanza, Waheshimiwa Wabunge mtashuhudia kwenye maeneo yenu na tunaomba msaidie kusimamia fedha hizo, kusimamia ujenzi, ili walimu waweze kupata nyumba za kuishi kwenye maeneo hayo. Huo ndiyo mkakati wa Serikali kwa sasa. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wanawake wengi wamekuwa wakijihusisha na biashara za mazao ya kilimo kandokando ya barabara kuu hapa nchini. Je, ni upi mkakati wa Serikali sasa kuhakikisha kwamba wanawake hawa wanatengenezewa mazingira bora ikiwa ni kujengewa mabanda ili waweze kufanya biashara zao katika hali nzuri zaidi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Malleko Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeshuhudia akinamama sasa hivi wamekuwa na mwamko mzuri tu wa kufanya shughuli za ujasiriamali na kufanya biashara kando kando ya barabara zetu. Unapokwenda Dar es Salaam tunawakuta hapo Gairo, lakini pale mbele kidogo Dumila hata Mikese unakuta wamejipanga wanafanya biashara zao na barabara zote nchini utakuta akinamama wengi na vijana wengine wa kiume wakifanya biashara zao. Zipo baadhi ya halmashauri zimekuwa na maono na zimeendelea kusimamia wajasiriamali hawa kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya biashara zao kwa kuwajengea vibanda vya kibiashara kama pale Dumila palivyo, lakini na eneo la Mikese kwa Halmashauri ya Morogoro Vijijini. Mheshimiwa Taletale ameshiriki pia kuwajengea vibanda wafanyabiashara, wananchi wake eneo la Mikese, Mbunge wa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utaratibu huu ni utaratibu ambao unawahamasisha hawa wafanyabiashara kufanya biashara zao vizuri, lakini pia wanakingwa na mvua na jua wanapofika kwenye msimu huo wakiwa wanaendelea kufanya biashara zao, lakini hata bidhaa inayouzwa inabaki kuwa salama na inafaa kwa kuendelea kuliwa pale ambapo inakaa kwenye kivuli na mahali sahihi pa kutunzwa.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua mipango ya Serikali, nitoe maelekezo kwa halmashauri zote nchini zihakikishe zinaendelea kutambua wajasariamali wanawake na vijana wanaouza biashara zao kandokando ya barabara kwa ajili ya wasafiri wanaosafiri ili watengenezewe mazingira mazuri ya kufanya biashara hiyo kwa kuwajengea vibanda vinavyowakinga na jua na mvua, lakini vinavyokinga pia bidhaa zile kwa jua na mvua ili bado mlaji apate bidhaa iliyo safi na salama ambayo bado ina mng’aro unaovutia kununuliwa. Hili litasaidia sana wajasiriamali hawa kupata kipato chao kwa uhakika na kufanya biashara kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunalichukua hili na kama ambavyo nimeiagiza Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia halmashauri zote wasimamie jambo hili ili wajasiriamali hawa wafanye biashara kwenye maeneo haya na wapate manufaa ya biashara zao. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Daktari Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa na kuzidi. Hivi karibuni ulifanya ziara Mkoani Mbeya na ulitembelea halmashauri zetu ikiwemo Busekelo, tunakushukuru sana. Lakini mojawapo ya changamoto ulizokutana nazo kwa wananchi wote kwa ujumla ni kwamba, katika nchi yetu kumekuwepo na tatizo la kutolewa kwa hati za ardhi za kimila ambazo hazithaminiwi na taasisi za kifedha za kibenki, hususan wanapokwenda kukopa na wamekuwa wakizungushwa mara njoo leo mara njoo kesho na hatimaye wanakata tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa wananchi wanaoishi vijijini wameendelea kuwa maskini kwa sababu hawapati mikopo kupitia hati za kimila za ardhi na tatizo hili limetokana na sheria Na. 5 ya mwaka 1999 ambayo ndio inayotoa hati hizi. Je, ni mkakati gani wa Serikali ili kuwarahisishia wananchi hawa wa vijijini waweze kupata hati kama wanavyopata mijini na ziweze kuthaminiwa na benki kwa kubadilisha sheria hii Na. 5 ya mwaka 1999? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye anaendelea kutupa afya na kutekeleza majukumu yetu kama hivi leo tumekutana hapa pamoja, tunaamini Mwenyezi Mungu ataendelea kutujalia kutupa neema zake.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakibete Mbunge wa Busekelo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria zetu za ndani ya nchi, hati zetu zote, zile zinazotolewa na Wizara yenyewe, zile zinazotolewa kama hati za kimila zote hizi ni hati zinazotambulika kisheria. Hati zote hizi ikiwemo na hati za kimila zinayo fursa ya mwenye hati hiyo kupata mikopo kwenye taasisi zote za kifedha. Inaweza kuwa yako maeneo ambayo ziko taasisi ambazo hazikubali tu kwa sababu ya matakwa yao au mpango kazi wao lakini kwa mujibu wa sheria hati ya kimila ambayo yenyewe pia inatolewa kwa vipindi kama vile vya hati inayotolewa na Wizara yenyewe, miaka 33, miaka 66, hata miaka 90, zote hizi zinatambulika kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nitoe wito kwa taasisi zote za kifedha ambazo zimeridhiwa na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya kazi yake nchini kwa mujibu wa sheria za nchi, waendelee kutumia na kutoa fursa kwa wale wenye hati za kimila au hata hizi hati ambazo zinatolewa na Wizara ya Ardhi kuwa ni hati halali zinatambulika na zinatoa fursa kwa mtanzania au kwa mmliki wa ardhi nchini kupata stahiki yake ya mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii tunaendelea chini ya Wizara ya Ardhi kufanya kazi ya upimaji wa ardhi yetu kwenye ngazi za vijiji tunapima mashamba, tunapima maeneo ya makazi, tunapima maeneo ya taasisi na maeneo yote yanayotolewa hati na Wizara imeshaanza na inaendelea inapita kila halmashauri kuendelea na kazi ya upimaji wa ardhi kwa maana ya kupanga matumizi bora ya ardhi kwenye ngazi za vijiji na hati hizo zinatolewa. Kwa hiyo, hati hizi watanzania waendelee kuziona kama ni hati kamili na inatambulika kisheria na inatoa fursa ya mikopo kama ambavyo nimeeleza awali.
Mheshimiwa Spika, naomba kueleza hayo, ahsante. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu imepata nafasi adhimu ya kuandaa michuano ya AFCON mwaka 2027. Ukifatilia maandalizi ya michuano hii kwenye mataifa mengine ilivyofanyika kama Ivory Coast inafanyika katika upana mkubwa na inagharimu mambo mengi sana. Sasa Serikali kuna maandalizi ambayo yanatakiwa yafanyike ya ujenzi wa viwanja vya kuchezea, ujenzi wa viwanja vya mazoezi, transport facilities kwa maana ya mabasi pia emergency hospitals. Serikali haioni haja ya fedha zinazotokana na magawio, fedha zinazotokana na CSR kwa asilimia kadhaa na fedha ambazo zinatokana na betting kwa asilimia kadhaa, ikaelekeza kama ni mfuko maalum kwa ajili ya maandalizi ya AFCON kwa kipindi cha miaka mitatu kama mkakati wa makusudi wa Serikali kujiandaa na tukio hili kubwa ambalo linakwenda kuheshimisha nchi yetu? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sanga Mbunge wa Makete kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza niseme nilitegemea kupata swali hili kutoka kwake, kwa sababu ndio Mwenyekiti wetu wa michezo hapa Bungeni na ni mwanamichezo halisi.
Mheshimiwa Spika, katika kujibu swali hili nataka nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu amewezesha Taifa hili kutambulika sasa katika michezo kwa kiwango cha juu ambako tunaiona michezo imeshamiri na Watanzania wanashiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo pia na michezo ya kukimbia na mpira na mpaka imetufikisha kuwa na ligi bora Afrika na kuwa kwenye nafasi ya tano. Tunaona ligi ya Zanzibar nayo imeshamiri, tumeshapata bingwa, tumeona pia ligi ya Bara tumeshapata bingwa pia tumeona bingwa wa muungano ameshachukua kombe na yeye. Kwa hiyo, tunaona michezo namna inavyoshamiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia Taifa letu kuungana na nchi za Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON mwaka 2027. Hii ni heshima kubwa na muono wa mbali kwa sababu michezo kama hii inapofika mahali ni nchi inapewa heshima ziko fursa nyingi zinatumika na hakika Taifa lazima lijipange vizuri ili kuweza kumudu kupokea wageni, kuhimili mashindano ndani ya nchi na mpaka kukamilika kwakwe na ikiwezekana basi Taifa wenyeji tuwe mabingwa ikiwemo Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameshauri Serikali tutumie mapato kadhaa CSR zetu katika kuimarisha ujenzi wa viwanja. Leo hii tumeshaweka mikataba ya kujenga uwanja Jijini Arusha. Tunaendelea na ujenzi tutaweza kuanza wakati wowote hapa Dodoma lakini tunakarabati viwanja kadhaa, ikiwemo Uwanja wa Benjamini Mkapa, Uwanja wa Uhuru kule Mwanza Kirumba, Uwanja wa Majimaji Mkoani Ruvuma na upande wa Zanzibar Uwanja wetu wa Amani utatumika pia kwa ajili ya michezo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nauchukua ushauri huu na Wizara iko hapa wiki mbili zilizopita tulikutana tukaweka mpango wa kuunda kamati kuanzia sasa ili kuanza maandalizi. Nitoe wito kwa watanzania heshima ambayo nchi hii tumeipata ambayo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia michezo hii kuchezwa hapa Tanzania, sisi tutakuwa tumepata fursa na kwa hiyo kila mmoja ajiandae katika kuhakikisha kwa pamoja tunaiandaa timu yetu kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kila mmoja anajiandaa kupokea ugeni mkubwa wa timu mbalimbali kutoka duniani kote; tatu, tufungue fursa za kibiashara kwa sababu hawa watakapokuja watalala, watakula, watakunywa na watapata huduma mbalimbali ikiwemo na usafiri hapa nchini. Kwa hiyo, fursa hii na ushauri ambao tumeupata hapa utatusaidia pia katika kuboresha. Kwa hiyo, niahidi kwamba ushauri tumeupokea na tutaufanyia kazi, ahsante sana. (Makofi)
JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni lini Serikali itaboresha Sheria ya Uhamiaji ili kuwezesha urahisi kwa wawekezaji wa kimkakati kusudi waweze kupata uraia wa uhamiaji kutokana na heshima ya uwekezaji wao kwenye Taifa letu, kama ambavyo wanafanya mataifa mengine? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mahawanga, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali yetu inayo mifumo pia inayo sheria za uhamiaji nchini kama nchi nyingine zote duniani. Sheria zetu hizi zinaruhusu pia watu kutoka nje kuja nchini kwa vibali maalum na kufanya shughuli mbalimbali. Wako ambao wanakuja kwa lengo la utalii, wako ambao wanakuja kikazi, wako ambao wanakuja kwa uwekezaji. Serikali yetu imeweka sheria lakini imefungua milango ya wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali. Ni kweli kwamba wawekezaji hawa tumewaweka kwenye madaraja wakiwemo wale wawekezaji wenye miradi ya kimkakati ambayo ni miradi ya gharama kubwa na ni ya muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge, anahitaji kujua kama Serikali ina mpango upi wa hawa wawekezaji wa miradi ya mikakati na ya muda mrefu na gharama kubwa, kuwa na wao wapate hadhi ya Taifa hili. Serikali yetu pamoja na sheria zetu tulizonazo tumeweka eneo ambalo mwananchi yoyote kutoka nje anahitaji kuishi nchini anafuata sheria za nchi yetu na zipo sheria na zinaruhusu na hii pia inatoa fursa hata kwa wawekezaji wakubwa. Moja kati ya sheria zetu awe ameshaishi nchini kwa miaka 10 na uwekezaji huu mkubwa kimkakati hauwezi kuwa mwaka mmoja, miwili, mitatu, minne.
Mheshimiwa Spika, hawa wa miaka 10 ni wale ambao wameishi hapa kwa muda mrefu na wanahitaji uraia lakini kwa wawekezaji kupitia Wizara ya Mipango na Uwekezaji na chombo chetu cha Taasisi ya Uwekezaji Nchini (TIC) tunapojiridhisha kwamba huyu ni mwekezaji wa mradi wa gharama kubwa na ni wa muda mrefu unahitaji usimamizi wa karibu hawa nao tumewafungulia dirisha lao la kuona umuhimu wa wao kuwa sehemu yetu. Lakini tunachofanya ni kumpa fursa mbalimbali za kikodi, kufanya biashara katika mazingira rahisi pia kumpa ushirikiano katika uendeshaji wa biashara hiyo na atakapoishi hapa zaidi ya miaka kumi anapata nafasi ya kupata kuomba uraia na anafikiriwa ili mradi tu atakapopata uraia lazima akubali kuendelea kuwa Mtanzania. Pia awe ni miongoni wanaochangia uchumi, kwa kuwa umekuwa na mradi mkubwa na wa gharama kubwa huyu atakuwa mmoja kati ya wanaochangia uchumi wetu, lakini pia azungumze lugha yetu ya Kiswahili na lugha ikiwa ya kiingereza na haya yote yanapokuwa yanafikishwa uhamiaji hakuna shida kwa sababu pia anasimamiwa na Taasisi ya Uwekezaji hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, tunapojiridhisha kwamba huyu ni mwekezaji wa mradi mkubwa, gharama kubwa na ni wa muda mrefu unahitaji usimamizi wa karibu, hawa nao tumewafungulia dirisha lao la kuona umuhimu wa wao pia kuwa sehemu yetu. Tunachofanya ni kumpa zile fursa mbalimbali za kikodi kufanya biashara katika mazingira rahisi lakini pia kumpa ushirikiano katika uendeshaji wa biashara hiyo na atakapoishi hapa zaidi ya miaka kumi anapata nafasi ya kuomba uraia na anafikiriwa ili mradi tu atakapopata uraia lazima akubali kuendelea kuwa Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini awe ni miongoni mwa watu wanaochangia Uchumi, kwa kuwa na mradi mkubwa na wa gharama kubwa huyu lazima atakuwa ni mtu mmoja kati ya wanaochangia uchumi wetu. Pia azungumze Lugha yetu ya Kiswahili au na Lugha nyingine ya Kingereza na haya yote haya yanapokuwa yanafikishwa uhamiaji, hakuna shida kwa sababu pia anasimamiwa na Taasisi ya Uwekezaji hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, basi nitoe wito kwa wawekezaji ambao wako tayari kuja kuwekeza nchini kwamba, Serikali yetu imefungua milango, lakini pia imetoa fursa kwa Wawekezaji wakubwa miradi ya kimkakati wanapata nafasi lakini pia zile fursa za kupata punguzo kwenye maeneo kadhaa ikiwemo na masharti ya kikodi yanapungua. Pia kupata ardhi, ule urasimu nao umepungua na hii ndiyo kwa sababu sasa tunashuhudia sasa wawekezaji wengi wanaingia hapa nchini. Kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha na kuboresha sheria zetu kama ambavyo imeshauriwa na Mheshimiwa Mbunge. Pia, tutaendelea kufungua milango ya uwekezaji wote kutoka nje na kwa kuangalia kuwa hawa wanaowekeza wana uzalendo lakini pia ni salama kwa usalama wa Taifa letu, ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kusimamia majukumu au shughuli za Serikali. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwenye nchi nyingi duniani kumekuwa na sera lakini sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ambayo inatoa nafasi kwa wahitimu wa vyuo mbalimbali kujitolea kufanya kazi Serikalini na kupewa posho kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye nchi yetu tunayo Taasisi ya Wakala wa Ajira wa Serikali (TaESA) ambayo inapeleka wahitimu wachache kwenye maeneo mbalimbali ya kazi na kule wanapewa posho kidogo, lakini walio wengi wanajiombea wenyewe, kwa baadhi waajiri wanawalipa lakini wengine hawalipwi kabisa. Je, Serikali haioni ni muhimu wa kuwa na sera, sheria, kanuni na miongozo kama hii ili wale wote ambao wanajitolea (wahitimu) waweze kulipwa posho? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba Jijini Dar es salaam, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye michakato ya ajira ambayo pia inasimamiwa na Wizara ya Kazi iliyoko Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunatambua kuwa tunayo makundi yanayopata ajira rasmi na wale ambao hawajapata ajira lakini wanatamani na wanapenda kujitolea. Kitendo cha kujitolea kinamsaidia sana mwajiriwa, kwanza kuimarisha uelewa wa sekta anayojiajiri, ambayo pia anakwenda kujitolea lakini pia anapata uzoefu mkubwa sana na waajiri wanatusaidia kubainisha watu wenye weledi, uaminifu, uadilifu katika utumishi wa ajira hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kazi na Ajira iliyoko Ofisi ya Waziri Mkuu nayo inafanya kazi kwa karibu na Baraza la Ajira (LESCO), LESCO iko kwenye Wizara yetu. Baraza hili lina ratibu pia ajira za kujitolea kupitia Sheria zetu za Kazi na Ajira. Tunafanya kazi pamoja na chombo ulichokitaja Mheshimiwa cha TaESA ambacho chenyewe ni chombo ambacho kinaratibu hawa wote wanaokwenda kwenye ajira za kujitolea na wakisubiri fursa za kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafasi hizo kama nilivyosema, wanapata nafasi ile ya kuwa wanapata uzoefu wa ajira zao, wawe wanatambuliwa kwenye chombo kile na kinasimamia maslahi yao. Kinahamasisha waajiri wale ambao wamewapokea wanaokwenda kujitolea kupata motisha wanapotekeleza majukumu yao, ile inasaidia sana kwa sababu hata mwajiri huyu iwe ni sekta ya umma au sekta binafsi anapohitaji waajiriwa, kuajiri watu ambao wanataka kufanya kazi kwenye taasisi yake anaanza na wale ambao wanajitolea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sheria zetu zinaruhusu watu kujitolea kupitia chombo chao cha TaESA akiamua kujiunga na chombo kile anasimamiwa kwa maslahi yake na motisha kwa kujenga mawasiliano kati ya TaESA pamoja na mwajiri. Kwa hiyo, kuwepo usimamizi natambua kwamba wako wengine hawaja kitambua hiki na wanajitolea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia swali hili ni vyema sasa wale wote ambao wanajitolea kwenye sekta mbalimbali wakajua kwamba tunacho chombo kinaitwa TaESA ambacho wao wakijitambulisha na kujisajili watasimamiwa wao wanaojitolea pamoja na kile chombo kinafanya mazungumzo, kinamtambua pia mwajiri na kumhamasisha mwajiri kuona kuwa hawa wanapofanya kazi wanahitaji huduma zao kama vile chakula, mavazi na huduma nyingine muhimu kama afya. Kwa hiyo, mwajiri lazima atenge kidogo motisha kwa ajili ya kuwafanya hawa waweze kufanya kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, chombo tunacho na baraza tunalo na Wizara ya Kazi na Ajira ipo, iko Ofisi ya Waziri Mkuu. Jukumu lake moja ni kusimamia na kuhamasisha pia hawa ambao wamesoma kwenye ngazi fulani au wana ujuzi wa aina fulani pale ambapo wanasubiri ajira wanaweza kujitolea kwenye eneo ambalo ajira yake anaweza kuitumia vizuri na vyombo hivi vinafanya kazi ya kuungana na hawa waajiri kwa kuona motisha zao wakati wote wanapokuwa kazini, ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni dhahiri wote tunajua uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali yetu hasa katika Bandari ya Dar es Salaam tukitegemea kwamba mizigo mingi inapita kwenye central corridor kuelekea katika nchi jirani hasa Burundi, Rwanda na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na check points za polisi zaidi ya 44, Mizani, TRA zaidi ya tatu lakini pia kuna mizani zaidi ya nane kwenye lane ya central corridor kutokea Bandari ya Dar es Salaam mpaka kuelekea Rusumo. Serikali kuweza kupunguza trans time na kuwasaidia wasafirishaji wasisafirishe mizigo kwa gharama hatimaye wakashindwa wakaona ni mzigo mkubwa. Ilianza kujenga one-stop inspection centers, tunacho cha Vigwaza pale Pwani lakini tuna kingine Dumila pale Morogoro. Kulikuwa na ujenzi ilibidi ufanyike Manyoni – Singida na ujenzi mwingine ilibidi ufanyike Nyakanazi – Biharamulo.
Mheshimiwa Spika, lakini baadhi ya vituo bado havijajengwa na ujenzi wake uliishia njiani umesimama. Sasa ili kuweka azma nzuri ya Serikali ni lazima vitu hivi vimalizike ili viweze kutusaidia kwenye kusafirisha hiyo mizigo na hatimaye uwekezaji tuliofanya kwenye Bandari ulipe kwa watu kupitisha mizigo katika Bandari yetu ya Dar es Salaam. Sasa ni nini kauli ya Serikali kwenye kumalizia ujenzi wa hivi vituo ili hatimaye Bandari yetu iweze kufanya kazi katika malengo ambayo Serikali inayatarajia? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Chiwelesa, Mbunge wa Biharamulo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja, uko mpango wa kuimarisha ukaguzi, lakini mbili mapato kupitia mizigo inayoingia ndani ya nchi kupitia Bandari ya Dar es Salaam na kwenda nje ya nchi yetu na inapita pia ndani ya nchi lakini pia kwenda kwenye mipaka yetu. Mkakati ambao Serikali umefanya ni kujenga vituo vya ukaguzi kwa malengo yote mawili, usalama lakini pia kupata mapato na vituo hivi vimejengwa kimkakati.
Mheshimiwa Spika, tunapopeleka magari Nchi za Burundi, Kongo na Rwanda za ukanda huu maana yake lazima tuimarishe vituo kwenye barabara kuu inayotoka Dar es Salaam inapita Dodoma - Singida na kwenda Mkoa wa Kagera kule Ngara kupitia Biharamulo, lakini pia hatujajenga kwenye barabara hii tu hata maeneo yote yanayoingia na kutoka kwenye mipaka yetu nchini kama vile Horohoro – Holili – Mtukula na huku Tunduma tunaimarisha, kujenga na kazi ya ujenzi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tuna vituo vingi vina mahitaji haya yote na ni lazima tujenge vituo kwa ajili ya ukaguzi kwa usalama lakini pia kwa ajili ya mapato. Kazi ya ujenzi inaendelea na ujenzi huu unaendelea kadiri tunavyopata fedha za kujenga vituo hivi. Kwetu kama Serikali ni muhimu sana kwa usalama wa nchi lakini ni muhimu sana katika kukusanya mapato ipasavyo ili tuweze kutunisha mfuko wetu kwa ajili ya ujenzi wa miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango mkakati upo wa Ujenzi wa Vituo hivi vyote vya ukaguzi kwenye maeneo haya. Pia, sasa tumeamua tunapojenga katikati ya nchi tunajenga kwa umbali ambao hauwezi kuleta usumbufu kwa wasafirishaji kwa kukaguliwa kila mahali wanapopita bali watakuwa wanakaguliwa kwenye vituo hivyo maalumu kama vile Vigwaza, Dodoma labda Manyoni kama ulivyosema Manyoni na huko Nyakanazi – Biharamulo na hata kule mpakani Ngara.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kufanya haya kwa kuhamasisha mataifa ya nje kutumia Bandari yetu ya Dar es salaam na bado tunao mpango wa kuimarisha Bandari za Mtwara na Tanga na sasa Serikali inao mpango wa kujenga Bandari Bagamoyo na kule tutaimarisha hiyo corridor yote, kuhakikisha kwamba usalama wa nchi tunapoingiza nchi nyingi kuja kuchukua mizigo hapa unaimarika. Pia, upatikanaji wa mapato pia na wenyewe tunauimarisha. Kwa hiyo, mipango hii yote ipo ndani ya Serikali, nashukuru sana. (Makofi)