Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Juliana Daniel Shonza (26 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha na mimi kuwa Mbunge ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mhe
shimiwa Mwenyekiti, vilevile niungane na Watanzania wote kuonyesha masikitiko makubwa sana kwa hiki ambacho kimetokea leo ndani ya Bunge letu. Nakumbuka huko nyuma nilishasema na kuwaambia Watanzania kwamba hawa wenzetu hawana ajenda yoyote ya kutaka kumkomboa Mtanzania wa leo, ajenda yao kubwa ni vurugu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge ambao tuko ndani ya Bunge hili tutakumbuka siku ya tarehe 20 Novemba, 2015 wakati Mheshimiwa Rais amekuja kufungua Bunge hili, wenzetu hawa walikuwa mstari wa mbele kupinga na hatimaye kutoka nje ya Bunge hili. Kwa kweli mimi jana tulipoanza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais nilishangaa kuona wao wanakuwa mstari wa mbele kuchangia na kukosoa hotuba hii adhimu ya Mheshimiwa Rais. Nashangaa ujasiri huo waliutoa wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hizi vurugu ambazo zimetokea humu ndani, ni imani yangu Watanzania wameona ukweli wa yale tunayoyazungumza kila siku kwamba hawa wenzetu hawana ajenda yoyote zaidi ya kutaka kuvuruga. Sisi kama Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, tunatambua kwamba Mheshimiwa wetu Rais ana kazi kubwa sana, ana ajenda nzuri ya kutaka kuwakomboa Watanzania lakini vilevile kuhakikisha kwamba Tanzania inaenda kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajikita kwenye mchango wangu napenda nitoe elimu ya uraia kidogo hata kama hawapo narusha jiwe gizani najua huko waliko litawakuta. Tunakumbuka kabisa kwamba baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na Chama cha Mapinduzi kuibuka kidedea kutokana na kuwa na Ilani ambayo kwanza inatekelezeka lakini wenzetu wale waliwaambia Watanzania kwamba Ilani yao inapatikana kwenye tovuti wakati Watanzania wa leo hawajui tovuti ni kitu gani na wengi wanaishi vijijini. Kutokana na kuwa na Ilani ambayo haieleweki Watanzania waliweza kukichagua Chama cha Mapinduzi hatimaye Rais wetu mpenzi, Dkt. John Pombe Magufuli kuweza kuibuka kidedea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo kumekuwa na upotoshaji mkubwa sana juu ya utendaji kazi wa Rais wetu Magufuli. Wenzetu hawa kama kawaida yao ya kukurupuka kama ambavyo leo wamekurupuka katika Bunge hili, wameendelea kupotosha umma na kusema kwamba Mheshimiwa Pombe Magufuli anatekeleza Ilani ya UKAWA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nisikitike sana kwa sababu sisi sote ni mashahidi wakati wakizindua kampeni zao pale Jangwani walitaja vipaumbele vyao ambavyo vilitajwa na mgombea wao wa Urais ambapo cha kwanza kilikuwa ni kumtoa Babu Seya ndani, kipaumbele kingine wakatuambia wao wakipata ridhaa ya kuweza kuongoza Taifa hili watajenga reli kiwango cha lami. Mimi niseme kwamba, kabla mgombea wao hajatangaza kwamba ana mpango wa kwenda kugombea Urais mwaka 2020, ni vema angejua kwamba reli hazijengwi kiwango cha lami. Vilevile wakasema kwamba wao wana mpango wa kuwatoa wafungwa wa Uamsho. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ndivyo vilikuwa vipaumbele vyao ambavyo waliwaambia Watanzania na ndio maana leo hata wanapokuja katika Bunge hili wanafanya fujo sishangai kwa sababu nawajua, ndiyo tabia zao na hawana ajenda yoyote na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Rais alijikita zaidi katika kubana matumizi, kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na maisha ya kiwango cha kati lakini vilevile kufungua Mahakama ya Mafisadi vitu ambavyo kwao wala hatukuvipata kuvisikia. Niwatoe hofu Watanzania kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Rais wetu John Pombe Magufuli, imejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba Tanzania inaenda kufikia uchumi wa kiwango cha kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite katika kuchangia hotuba hii adhimu ya Mheshimiwa Magufuli. Mimi natoka katika Mkoa wa Songwe na kama tunavyojua ni mkoa mpya ambao una changamoto nyingi za kiuchumi. Vilevile mimi kama mwakilishi wa wanawake wa Mkoa wa Songwe hapa Bungeni, nina ombi moja na napenda nijikite katika kuchangia kwenye masuala ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Songwe kabla hawajaugawa ulipokuwa katika Mkoa wa Mbeya tulikuwa na hospitali kubwa kabisa ya rufaa lakini vilevile kulikuwa na hospitali kubwa kabisa ya mkoa. Baada ya sisi kuwa Mkoa wa Songwe tumebaki kama yatima, Mkoa wetu hauna huduma za afya, hatuna hospitali ya rufaa wala ya mkoa. Akina mama wa mkoa ule wanapata shida sana linapokuja suala la uzazi. Nikitolea mfano kwenye Wilaya yangu ya Mbozi inakabiliwa na changamoto kubwa sana kwa sababu wodi ya akina mama ni ndogo haikidhi mahitaji na hospitali ile imekuwa ikihudumia akina mama wanaotoka katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wetu wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano wa Wilaya yetu ya Momba, pale Tunduma kuna hospitali moja tu. Hospitali ile ni ndogo, haikidhi mahitaji, haina madaktari wa kutosha, haina vifaa vya kujifungulia hata inapokuja suala la operation hawana theatre inabidi wasafirishwe kutoka Tunduma, Wilaya ya Momba kuja Wilaya ya Mbozi na ukizingatia pia hospitali liyopo Mbozi haina jengo la kuwatosha akina mama wale. Kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameeleza katika hotuba yake kwamba atahakikisha Watanzania wanakuwa na afya, atahakikisha akina mama wanapata sehemu bora za kujifungulia, napenda nichukue nafasi hii kuweza kumuomba Rais wetu John Pombe Magufuli aufikirie mkoa wangu mpya wa Songwe tuweze kupatiwa hospitali za kutosha. Katika hotuba yake ukurasa wa 22 amesema atahakikisha kila mkoa unakuwa na hospitali, kila kata inakuwa na zahanati, tunaomba sana Mheshimiwa Rais aweze kuufikiria mkoa wangu wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia pia katika hotuba yake ukurasa wa 24, Mheshimiwa Rais alitueleza kabisa kwamba ana mpango madhubuti wa kuhakikisha Watanzania tunatoka kuishi gizani na tunakuwa na umeme wa uhakika.
Niseme jambo moja kwamba Mkoa wangu wa Songwe tatizo la umeme limekuwa kubwa sana, umeme ukishakatika saa tano unakuja kuwaka kesho yake saa kumi na mbili alfajiri. Unaweza kuona mazingira hayo yalivyo magumu, akina mama wanaofanya kazi kwa kutegemea umeme hawawezi kufanya kazi zao. Vilevile hata vijana wanaokaa Mkoa wa Songwe ambao wanategemea umeme kufanya shughuli mbalimbali ili kuweza kujiingizia kipato hawapati nafasi ya kufanya shughuli hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru sana Serikali ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ni hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo alikuja kwenye Mkoa wangu wa Songwe. Naamini kabisa aliona changamoto ambazo zipo katika mkoa ule na ni ishara tosha kwamba sasa wananchi wa Songwe wataenda kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JULIANA DANIEL SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue nafasi hii kushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia, lakini vile vile nimpongeze Waziri wa Elimu pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja kujadili suala la Bodi ya Mikopo. Tatizo kubwa ambalo linawa-face wanafunzi wengi wa elimu ya juu ni suala la mikopo. Tumeshuhudia katika vyuo vingi kwamba wanafunzi wamekuwa wakifanya maandamano, wakipinga Sera ya Bodi ya Mikopo ambayo kwa kweli ni tatizo kubwa kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mfano, tutakumbuka miaka ya nyuma ukisikia migomo katika Vyuo Vikuu, ilikuwa ni migomo ambayo inapinga sera. Kuna mgomo ambao ulifanyika 1969 ulikuwa ni mgomo wa kupinga sera ya wanafunzi kwenda JKT, kuna mgomo mwingine ukafanyika miaka ya 90, ambao moja kwa moja ilikuwa ni kupinga, suala la cost sharing katika elimu ya juu. Nisikitike kwamba migomo ya sasa hivi imekuwa ni tofauti, wanafunzi wa sasa hawapingi masuala ya sera kama ambavyo ilikuwa zamani. Agenda yao kubwa ni Bodi ya Mikopo, suala la mikopo limekuwa ni jipu kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia chimbuko la matatizo ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu ni Sheria ambayo imeunda Bodi ya Mikopo. Kuna vigezo ambavyo vimeainishwa, ukisoma Sheria ya hiyo, kifungu cha 17, kimeainisha vigezo vya mwanafunzi kuweza kupata mikopo, kigezo cha kwanza awe ni Mtanzania. Sote tunatambua kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi ni Watanzania, kwa hiyo, bado hiki sioni kama ni kigezo cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kigezo kingine lazima awe ni mwanafunzi ambaye anaendelea na amefaulu katika mwaka husika, bado siyo kigezo. Kigezo kingine cha tatu, lazima awe ameandika barua, sidhani kama kuna mwanafunzi nchi hii ambaye atashindwa kuandika barua. Kigezo kingine ni lazima mwanafunzi huyo awe amedahiliwa katika Chuo ambacho kimesajiliwa na Serikali. Sote, tunashuhudia katika nchi ya Tanzania kwamba, kuna utitiri mkubwa sana wa vyuo. Kwa hiyo, suala la mwanafunzi kuweza kudahiliwa bado siyo kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa makini hivi vigezo ndivyo vinavyopelekea kuwa na migomo, wanafunzi wanalalamika, wale ambao wanastahili kupata mikopo hawapati na wale ambao hawastahili mara nyingi ndiyo tumekuwa tukishuhudia wakipata mikopo. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali, ni vyema ikaangalia hili suala kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna mkanganyiko mkubwa sana katika suala hili la Bodi ya Mikopo. Suala la kwanza, ni suala la kimtazamo, kwamba kama Bodi yenyewe haijajitambua, kwamba ule mkopo wanaotoa je, ni mkopo au ni hisani na ndiyo maana mpaka leo hii tunashuhudia kwamba hakuna vigezo ambavyo wameviweka, ambavyo mwanafunzi akipata mkopo, vinambana mwanafunzi huyo aweze kurejesha ili wanafunzi wengine waweze kwenda kutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkanganyiko wa pili, kwamba hata yule anayepewa mikopo, bado yeye mwenyewe hajajitambua, kwamba je, huu ni mkopo au ni hisani na tumeshuhudia Waheshimiwa Wabunge wengi ambao tupo katika Bunge hili tumesomeshwa na hizi kodi za Watanzania, lakini tuulizane ni nani ambaye ameweza kurudisha mkopo huo. Hata Mheshimiwa Waziri ameligusia asubuhi, lakini kusema kwamba Wabunge twende kulipa bado halitoshi, kusema kwamba atatoa majina kwenye magazeti bado haitoshi; lazima kama Wizara, kama Bodi ya Mikopo, mje na mkakati, mje na system ambayo itambana yule ambaye anapewa mikopo na Serikali ili basi aweze kurudisha kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia hata kwa wafanyakazi wanaofanya kazi Serikalini, wanasema kwamba hawajaambiwa wameanza kukatwa, wanashuhudia tu kwenye salary slip wamekatwa, hawajui mikopo hiyo watakatwa mwisho lini. Hii ni changamoto kubwa ya Bodi ya Mikopo na inaonesha kwamba Bodi kimsingi haijajipanga kwa suala hili la kuhakikisha kwamba, hizi fedha wanazozitoa ziweze kuwa revolving fund, ili mtu anapopata na wanafunzi wengine waweze kuja kuzipata. Ndiyo maana tunashuhudia migomo katika nchi yetu haiishi kwa sababu Bodi ya Mikopo haijajipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ya Bodi ya Mikopo, tumeshuhudia kwamba mikopo hiyo inatolewa Dar es Saalam. Nimeshindwa kuelewa , kwamba Bodi ya Mikopo ipo Dar es Salaam, mwanafunzi atoke Mbozi, Ileje, mimi nikienda Dar es Salaam, watajuaje kama kweli Shonza ana sifa ya kupata mikopo. Siyo rahisi kuweza kumtambua, kwa hiyo hii nayo ni changamoto kubwa sana ambayo kama Wizara ihakikishe kwamba inalifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuishauri Serikali pamoja na Wizara, Mama yangu Ndalichako tunatambua kwamba wewe ni mweledi, una uwezo mkubwa, lakini bado kuna upungufu mkubwa katika Wizara hii ya Elimu. Nishauri Serikali, kwanza sisi kama Wabunge lazima tukubaliane kwamba, mahali tulipofika mpaka sasa hivi ni ngumu kwa Serikali kuweza kutoa michango kwa asilimia mia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipofika ni ngumu na wala tusijidanganye, lazima Serikali ije na njia mbadala kuhakikisha kwamba hizi fedha ambazo zilikwishaanza kutolewa miaka mingi, kama zingekuwa revolving fund, leo hii tusingekuwa tunajadili bajeti ya mikopo humu ndani, kwa sababu fedha ambazo zimeshatolewa ni nyingi na zingekuwa zimeshazunguka na zingesaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kuishauri Serikali, la kwanza ni vyema wakahakikisha kwamba wanaanzisha mfumo wa kutoa scholarship, kwa wanafunzi wanaofanya vizuri, kwamba kigezo pekee cha kuweza kupata mkopo, iwe ni ufaulu. Mwanafunzi ambaye amekaa kule Mbozi, ajue kabisa kwamba ili nipate mkopo, lazima nipate division one. Tofauti na ilivyo sasa hivi, kwamba aliyepata division three anapata mkopo, aliyepata division one hapati mkopo. Hiyo ni changamoto kubwa sana, kwa hiyo, kama Wizara tuwe na utaratibu wa kuzawadia bidii, itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nataka kuishauri Serikali ihakikishe kwamba inatoa mikopo asilimia mia kwa zile taaluma ambazo ni taaluma za huduma, kwa mfano Walimu pamoja na Madaktari. Hii itasaidia pia zaidi kuweza kuleta motisha, katika kozi hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, niiombe pia Serikali, iangalie namna ya kuhakikisha kwamba Bodi ya Mikopo isihusike moja kwa moja katika kutoa mikopo hiyo. Ni vema mikopo ikatolewa katika Wilaya zetu, kwa sababu kule kwenye Wilaya kuna Taasisi za kifedha, leo hii Serikali imeingia taaluma ambayo naweza nikasema kwamba siyo ya kwake, ni taaluma ya kibenki. Taaluma ya kukopa na kukopeshana ni taaluma za kibenki siyo taaluma ya Serikali. Kwa hiyo Serika iache kufanya biashara, kwa kupitia Bodi ya Mikopo na kuna Taasisi ambazo zipo ambazo ni za kifedha, ziachiwe kazi hizo, hao ndio waratibu zoezi zima la kutoa mikopo, kwenye Wilaya zetu, kwa kuangalia kwamba ni nani anafaa ni nani ambaye hafai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, naamini kwamba itasaidia ili fedha hizo ziweze kuzunguka kama ambavyo tumeshuhudia nchi za wenzetu suala la mikopo mzazi anafanya jitihada kuhakikisha kwamba anamwepusha mtoto wake na mikopo, lakini Tanzania kwa sababu ni bure, ndiyo maana kila mtu ambaye ana uwezo, asiye na uwezo anaomba apate mkopo, kwa sababu ni bure. Naomba suala hili lifanyiwe kazi na likifanyiwa kazi masuala ya migomo yatakuwa yamekwisha katika nchi yetu, lakini wananchi wengi na wanaostahili watapata nafasi ya kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nizungumze kwamba, nimesikiliza kwa makini sana hotuba ya Kambi ya Upinzani. Wamezungumza kwamba, Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndiyo ambayo inawanyanyasa wanafunzi ambao ni wa UKAWA. Mimi niseme kwamba, hilo siyo kweli, mimi mwenyewe nilikuwa ni mwanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nilikuwa upande wa CHADEMA, nilishawahi kuongoza migomo na nikakamatwa nikaenda ndani siku mbili, lakini hakuna siku ambayo nilifukuzwa chuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi, hata Mama yangu ambaye amewasilisha hotuba hiyo tulikuwa naye pale Chuoni na alikuwa aki-support, hakuna siku ambayo mwanafunzi amerudishwa. Nami kama mwanzilishi wa CHASO katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mama yangu alikuwa akini-support vizuri sana na wala sikuwahi kufukuzwa. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tuwe wa kweli. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile suala la kusema kwamba Mheshimiwa Nape amezomewa Mwanza, naomba Waheshimiwa Wabunge, sote humu ndani ni waelewa na kwa sisi ambao ni waelewa wa haya mambo tunafahamu, kwamba haya mambo wanapanga nani asiyejua CHADEMA kwamba wanawapa viroba vijana waende kuwazomea viongozi wa Chama cha Mapinduzi, nani asiyejua? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Nape, wewe endelea na kazi yako, piga kazi Watanzania tuko nyuma yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa miongozo yote ambayo amekuwa akinipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Vilevile nichukue nafasi hii kuweza kuwashukuru akinamama wote na wanawake wote wa Mkoa wa Songwe kwa imani yao kubwa kwangu ambayo inaniwezesha katika kutekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nichukue nafasi hii kuweza kuwashukuru Wabunge wote ambao wameweza kuchangia na hoja yetu, nami niseme kwamba, michango yao yote imekuwa ni michango ambayo ina tija sana na tunaahidi kwamba, tutaichukua na kuweza kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu baadhi ya hoja ambazo zimeweza kuzungumzwa, kwanza nianze na kujibu hoja za Kamati. Hoja ya kwanza ambayo imeibuliwa na Kamati ni juu ya usajili wa magazeti kwamba uko chini ya kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti yetu ya mwaka 2018/2019, Wizara tumejipanga kuendelea kusajili magazeti yote nchini, lakini vilevile kwa sababu ni takwa la kisheria chini ya Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 tumepokea ushauri wa Kamati na Wizara tutaendelea kuhakikisha tunaendelea kusajili magazeti ambayo yapo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema pia tukubaliane na Waheshimiwa Wabunge katika jambo hili kwamba, katika suala zima la usajili wa haya magazeti Wizara imefanya kazi kubwa sana kwa sababu ukiangalia ndani ya muda mfupi katika kipindi cha mwaka mmoja magazeti ambayo yamesajiliwa ni magazeti 169 ukilinganisha na magazeti 400 ambayo yamesajiliwa tangu kuanzishwa kwa sheria hii mwaka 1976.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba, jitihada kubwa zinahitajika, lakini pamoja na hayo, Wizara imefanya kazi kubwa sana na tunaahidi kwamba usajili wa magazeti tutaendelea nao katika mwaka huu wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili pia ambayo imeweza kuibuliwa na Kamati ni kuhusiana na Serikali kufanyia kazi andiko la TBC kwamba wanahitaji shilingi bilioni 80 kwa ajili ya kuboresha usikivu wa TBC. Serikali imeendelea kusaidia shirika hili la TBC katika kuboresha usikivu katika nchi yetu ya Tanzania, hilo limejidhihirisha kwa sababu ukiangalia bajeti ya mwaka 2016/2017, fedha ambayo ilitengwa ilikuwa ni shilingi bilioni moja, lakini kwenye bajeti ya mwaka wa 2017/2018, bajeti hiyo ya kuboresha usikivu ilipanda na kuweza kufika shilingi bilioni tatu. Kwenye bajeti hii sasa ambayo tunaomba leo Waheshimiwa Wabunge muweze kuipitisha Shirika la TBC limetengewa shilingi bilioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kabisa kwamba kwa kuwa, Serikali katika fedha ambayo ilitenga mwaka uliopita shilingi bilioni tatu na fedha hiyo imeshatolewa yote, ni imani yetu kabisa kwamba, katika bajeti hii ambayo imetengwa ya shilingi bilioni tano kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019, Serikali tunaahidi kwamba hiyo fedha itatoka na kwa namna moja au nyingine itasaidia sana katika kuboresha tatizo la usikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii vilevile iliweza pia kuchangiwa na Mheshimiwa Abdallah Bulembo ambaye alisema kwamba fedha hii ambayo imetengwa ni ndogo sana. Niseme tu kwamba Mheshimiwa Mbunge naomba tukubaliane kwamba Serikali ina nia ya dhati kabisa katika kuboresha usikivu na kulisaidia Shirika la TBC. Wanasema kwamba safari ni hatua, kwa hiyo tumeanza kidogo kidogo na sasa hivi tunaendelea vizuri kuhakikisha kwamba tunamaliza kabisa tatizo la usikivu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imeibuliwa na Kamati ni kutoa ushauri kwamba Serikali iweze kutoa fedha kwa TBC Redio ili iweze kusikika nchi nzima. Waheshimiwa Wabunge katika mwaka wa fedha 2017/2018 Shirika la TBC limefanya kazi kubwa sana katika kuboresha usikivu hasa katika maeneo ambayo ni ya mipakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukienda maeneo ya kule Namanga, Tarime, Kankoko, Nachingwea, Mtwara TBC inasikika vizuri sana. Hiyo yote ni kazi ambayo imefanyika

katika mwaka huu wa fedha na bajeti ambayo ilitengwa katika mwaka huu ambao unaenda kumalizika, bajeti ya 2017/2018, maboresho hayo yamefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 TBC ilikuwa inasikika katika Wilaya 81 tu, sasa hivi tumefikia Wilaya 100 ambazo TBC inasikika vizuri. Kwa hiyo, niseme kwamba, ushauri tumeupokea lakini kama ambavyo nimezungumza awali kwamba fedha inaendelea kutengwa na sasa hivi bajeti ya maendeleo ya TBC imepanda kufikia bilioni tano tunaamini kwamba tatizo hili litaenda kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumziwa na Wabunge wengi ni kuhusiana na suala zima la Wasanii pamoja na BASATA, kwamba BASATA inafungia nyimbo pale ambapo nyimbo zinakuwa tayari zimekwishapigwa, halafu BASATA inakuja kufungia nyimbo hizo baadaye. Hoja hii imejadiliwa na Mheshimiwa Tauhida na pia Mheshimiwa Amina Mollel ameizungumzia vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Filamu kwa maana ya Bodi ya Filamu, Sheria ya Bodi ya Filamu pamoja na kanuni zake inataka wasanii wote ambao wanatengeneza filamu kabla hawajapeleka filamu zao sokoni wahakikishe kwamba filamu hizo zimepita Bodi ya Filamu kuweza kuhakikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwa Bodi ya Filamu hata kanuni ambazo tunazo katika chombo ambacho kinasimamia sanaa kwa maana ya BASATA, tuna kanuni ambazo zinawataka wasanii wote kabla hawajapeleka nyimbo zao kuanza kurushwa katika vyombo mbalimbali vya habari, wahakikishe kwamba nyimbo hizo wanazipeleka BASATA ili ziweze kupitiwa na kama zina marekebisho ziweze kufanyiwa marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo tunayo katika nchi yetu lakini kwa wasanii ni utii bila shuruti. Wasanii wengi hawapeleki kazi zao, nyimbo zao BASATA wala hawapeleki filamu zao. Hii ndiyo sasa imekuwa changamoto inapelekea BASATA wanakuja kushtukia tayari kazi imeshaingia sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii pamoja na changamoto mbalimbali ambazo tulikuwa nazo BASATA, lakini Serikali haina ugomvi wowote na wasanii. Ugomvi ambao Serikali inao na wasanii ni juu ya mmomonyoko wa maadili. Nichukue nafasi hii kusema kwamba Serikali na Wizara hatutaacha kulisimamia niwaombe wasanii wote kuhakikisha kwamba kazi zao kabla hawajazipeleka sokoni wanazipitisha katika vyombo hivi ambavyo nimeweza kuvitaja ili kazi hizo ziweze kuhakikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo limezungumziwa pia na Kaka yangu ‘Profesa J’ Mheshimiwa Joseph Haule amesema BASATA imekuwa haina mahusiano ya karibu na wasanii badala yake sasa BASATA imekuwa kama chombo cha kuwachukulia hatua na adhabu wasanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, BASATA imekuwa ni chombo ambacho kipo karibu sana na wasanii. Katika kudhihirisha hilo kuanzia mwaka 2010 BASATA imeandaa makongamano na matamasha mbalimbali ambayo wasanii wengi wamekuwa wakishirikishwa. Mpaka sasa wasanii zaidi ya 30,000 wameweza kushiriki makongamano hayo ambayo kwa namna moja au nyingine yamewasaidia wao kama wasanii pia kuweza kupata elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mwaka huu wa fedha BASATA imeweza kukutana na wasanii zaidi ya 2,000 na kuweza kujadili changamoto zao mbalimbali. Tatizo linalojitokeza ni kwamba baadhi ya wasanii ni kutokushiriki pale ambapo hivi vikao vinaitishwa na hivyo wanakuwa hawajui kwamba BASATA ina msimamo gani na mambo gani ambayo wao kama wasanii wanapaswa kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kuna hoja nyingine pia imeibuliwa hoja ya uhakiki wa video. Waheshimiwa Wabunge suala la uhakiki wa video ni suala ya Bodi ya Filamu kama ambavyo nimezungumza awali kwamba Bodi ya Filamu imekuwa ikifanya kazi nzuri sana kuhakikisha kwamba inaendelea kuhakiki kazi zote za sanaa. Mpaka sasa hivi tunavyozungumza katika mwaka huu wa fedha zaidi ya filamu 689 za Kitanzania na 155 filamu ambazo zinatoka nje zimehakikiwa. Kwa hiyo niendelee tu kusisitiza kwa wasanii kuhakikisha kwamba wanapeleka kazi zao ili ziweze kuhakikiwa na kuepusha matatizo ambayo yanaweza kuwapata hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumziwa ni kuhusiana na vazi la Taifa. Hii ni hoja ambayo imeibua mjadala mkubwa, Mheshimiwa Lucy Owenya ameweza kuchangia pia kwa maandishi na kudai kwamba ni lini sasa mchakato wa vazi la Taifa utaweza kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wa Vazi la Taifa ni mchakato ambao tayari ulikwishaanza tangu Serikali ya Awamu ya Nne ikiwa madarakani. Changamoto kubwa ambayo ilitokea katika mchakato huo ni ulipofika katika Baraza la Mawaziri na kama tunavyojua kwamba nchi yetu ni nchi ambayo ina makabila zaidi ya 120, hivyo inakuwa ni vigumu sana kuweza kujua kwamba ni vazi gani ambalo Watanzania tunaweza kulitumia kama vazi letu la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni vigumu kuweza kuamua kwamba ni vazi gani ambalo linafaa kuweza kuwa Vazi la Taifa, hivyo maamuzi ambayo yalifikiwa ni kwamba ni vema kwamba vazi la Taifa likatokana miongoni mwa mavazi ya jamii husika. Mpaka sasa hivi mchakato huo umeachwa kwa Watanzania wenyewe ili waweze kuamua kwamba ni vazi gani ambalo litawafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara tumeendelea pia kutoa taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari, lakini vilevile kwa kutumia tovuti yetu ya Wizara ili kuwapa nafasi sasa Watanzania waweze kujadili namna gani ambavyo wanadhani kwamba vazi gani ambalo litafaa kuwa ni Vazi la Taifa, lakini mpaka sasa hivi ni mchakato huo umeachwa kwa jamii yenyewe kwamba vazi litokane na jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imezungumziwa ni suala la usikivu wa TBC ambapo Mheshimiwa Ramo Makani Mbunge wa Tunduru Kaskazini amezungumzia tatizo la usikivu wa TBC eneo la Tunduru. Napenda tu kuchukua nafasi hii kuweza kumhakikishia Mheshimiwa Ramo Makani kwamba katika Wilaya ya Tunduru tayari mtambo wa TBC umekwishafungwa na sasa hivi maboresho yanaendelea kufanyika. Tunaamini kabisa kwamba maboresho hayo ifikapo mwezi wa Tano maboresho hayo yatakuwa yamekwishakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna tatizo pia la usikivu wa TBC katika Wilaya ya Lushoto ambapo Mheshimiwa Shaabani Shekilindi pia ameweza kuzungumza. Niseme kwamba katika Wilaya ya Lushoto wote tunafahamu kwamba kuna changamoto ya milima ambayo kwa namna moja au nyingine imekuwa ikiathiri mawimbi ya TBC FM pamoja na TBC Taifa. Mpaka sasa hivi ninavyoongea tayari tumeshapata eneo ambalo litatumika kufunga huo mtambo na tunaamini kabisa kufikia mwezi Mei, tatizo la usikivu wa TBC katika Wilaya ya Lushoto litakuwa limeshakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Machano Othman Said pia amezungumzia tatizo la usikivu Zanzibar. Nichukue nafasi hii kuweza kumhakikishia tu Mheshimiwa Machano kwamba katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019, tayari Zanzibar imewekwa kwenye kipaumbele katika kuonesha kwamba tunaboresha usikivu wa TBC na siyo tu kwa Zanzibar peke yake, kuna mikoa mitano ambayo ni Mkoa wa Songwe, Mkoa wa Simiyu, Katavi pamoja na Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine pia ambayo imeibuliwa na Mheshimiwa Rhoda Kunchela ambaye amesema kwamba Serikali iweke ofisi za usajili kila mkoa kwa ajili ya wasanii kuweza kununua sticker za TRA. Ni kweli Mheshimiwa Rhoda kwamba mpaka sasa hivi sticker za TRA zinapatikana katika Mkoa mmoja tu ambao ni Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tayari jitihada za makusudi zimeanza kufanyika na mpaka sasa hivi ninavyoongea Kamati ya Urasimishaji imekwishakaa na sasa hivi tunaandaa utaratibu mzuri kabisa ili kwamba sticker hizo hata wasanii ambao wanapatikana mikoani waweze kuzipata kwa njia ya kununua hizo sticker kwa njia ya mtandao. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba hili litakapokamilika itakuwa ni njia mojawapo ya kutatua tatizo la usumbufu wa kuwatoa wasanii kutoka mikoani kuja kununua sticker hizo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imejadiliwa ni hoja ambayo ameizungumza Mheshimiwa Peter Lijualikali ambaye amesema kwamba kama Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kukarabati viwanja vyake ni vema viwanja hivyo vikarejeshwa Halmashauri. Mpaka sasa hivi Chama cha Mapinduzi hakijashindwa kukarabati viwanja vyake na nasema hilo nikiwa na ushahidi na uhakika kwa sababu hata ukiangalia katika Mkoa wa Singida kiwanja ambacho kinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi Kiwanja cha Namfua kimeshakarabatiwa na kipo kwenye ubora wa kisasa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Uwanja wa Sokoine Mkoa wa Mbeya ambao nao upo kwenye ukarabati. Vilevile kuna uwanja mwingine ambao pia Mheshimiwa Mbunge ameweza kuuzungumzia Uwanja wa Samora Iringa. Kwa hiyo, siyo Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kukarabati viwanja vyake, nasi ndani ya Chama cha Mapinduzi kuna msisitizo kuhakikisha kwamba chama kinakarabati viwanja vyake, lakini ni vema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu; na kwa kuzingatia pia kuwa asilimia 75 ya Watanzania wanaishi vijijini na wanategemea kilimo ili kuweza kukidhi mahitaji yao ya kila siku. Suala la pembejeo limebaki kuwa changamoto kubwa kwa wakulima wa Tanzania, hususan wakulima wa kahawa na mahindi Mkoani Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, vocha za mbolea huwafikia wakulima kwa kuchelewa sana na hata hivyo, huwa hazikidhi mahitaji. Hii inatokana na kwamba Mawakala wengi hawana sifa za kuwa Mawakala. Hivyo, hutaka makusudi kuchelewesha vocha za mbolea kwa wakulima ili baadaye baada ya msimu kupita, hupeleka vocha kwa wakulima na kwa kuwa msimu huwa umepita, hulazimika kupokea fedha kidogo toka kwa mawakala ili waweze kusaini kuwa wamepokea vocha kumbe sivyo. Hali hii hurudisha nyuma kilimo nchini na kuwakatisha tamaa wakulima wetu. Nashauri yafuatayo ili kuleta kilimo chenye tija:-
(a) Mfumo wa upatikanaji Mawakala wa Vocha za Mbolea, upitiwe upya ili kuondoa Mawakala ambao hawana sifa, wanaopata nafasi hizo kwa kujuana tu. Hili liende sambamba na kupitia upya mfumo wa ugawaji pembejeo ili ziweze kuwafikia walengwa tofauti na ilivyo sasa ambapo vocha za mbolea huwafikia wasio walengwa na walengwa wenyewe hawanufaiki na mfumo uliopo sasa.
(b) Nashauri Serikali ipitie upya hili suala la bei ya mazao ya wakulima wetu. Ni vyema Serikali ikafungua mipaka ili wakulima waweze kuuza mazao yao nchi jirani. Kutokana na kwamba uzalishaji ni mkubwa lakini soko siyo la kuridhisha, maana Serikali hushindwa kununua mazao yote toka kwa wakulima. Ni vyema Serikali ikafungua mipaka ili soko liamue bei ili kuongeza motisha ya uzalishaji kwa wakulima wetu.
(c) Nashauri Serikali ipunguze tozo katika zao la kahawa, ambapo kuna tozo zaidi ya 36, hivyo wakulima hawanufaiki na kilimo chao. Ni vyema Serikali ikapunguza hizo tozo zisizo za lazima kama walivyofanya kwenye zao la korosho.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka 53 iliyopita (1962) ambapo ilikuwa ni mwaka mmoja tu baada ya Uhuru, Mwalimu Nyerere aliwaambia Watanganyika kuwa we must run while they walk, kwamba kama Taifa ni lazima tukimbie wakati wao wanatembea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaelekea katika mfumo wa viwanda ili kuwezesha Watanzania kuweza kuwa na uchumi wa kati, ni vyema kama Taifa tukajitathmini upya. Hatuwezi kufikia uchumi wa viwanda kama tutaacha nyuma sekta shirikishi, mfano sekta za miundombinu na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa viwanda vinategemea uwepo wa miundombinu kama barabara na reli ili kuweza kusafirisha malighafi kutoka shambani kwenda viwandani, vilevile kusafirisha bidhaa toka viwandani hadi sokoni, hivyo ni vyema kama Serikali ikazitupia jicho pia sekta wezeshi hizi ili kuwezesha viwanda vyetu kuwa na malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema pia kama Taifa tuondoe kauli mbaya kuwa tunazalisha tusichokitumia na tunatumia tusichokizalisha. Tuungane kwa pamoja kumpa nguvu Mheshimiwa Rais katika kujenga uchumi unaozingatia mahitaji ya nchi na soko kwa ujumla, nchi ya viwanda vitakavyoongeza thamani ya mavuno kwa mkulima. Kujenga Taifa ambalo mkulima wa kahawa atanufaika kuliko mnunuzi wa kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa Mkoa wa Songwe ni mkoa mpya hivyo kukabiliwa sana na changamoto ya kiuchumi, naishauri Serikali tunapoelekea uchumi wa viwanda ni vyema Serikali isiiache nyuma mikoa mipya kama ya Songwe, Njombe na Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kusikitisha, Mkoa wa Songwe hauna kiwanda chochote kikubwa ilhali Mkoa wa Songwe ni maarufu kwa kuzalisha mahindi na kahawa. Hivyo naiomba Serikali itujengee kiwanda kikubwa cha kukoboa mahindi ili kuweza kuzalisha unga ambao utauzwa ndani na nje ya nchi, sambamba na kiwanda cha kahawa ili kuwezesha wananchi wa Mkoa wa Songwe kunufaika pia na mpango huu madhubuti wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hii nyeti kwa uchumi wa nchi yetu. Kwa kuzingatia unyeti wa Wizara hii naomba kuchangia yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni Makumbusho ya Taifa, kumekuwa na tatizo la muda mrefu kwa watumishi wa Makumbusho ya Taifa kutopandishwa vyeo. Hali hii inakatisha moyo sana kwa wafanyakazi wengi kuhamia taasisi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya waajiriwa wapya wanapogundua Makumbusho hawatoi vipaumbele kwa wafanyakazi wake wanaamua kuacha kazi. Shirika la Makumbusho ya Taifa ni muhimu katika kuhifadhi mambo yanayoshamiriwa na jamii na ambayo yanapotea kwa kasi sana, lakini Wizara haiipi kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imetegemea zaidi kwa wanyamapori na tangu Waziri na Katibu Mkuu wateuliwe hakuna aliyefika Makumbusho. Nyumba haitoshi Makumbusho ya Posta kumbi mbili zimefungwa, ukumbi wa baiolojia na wa mila na desturi umefungwa kwa zaidi ya mwaka sasa.
Naomba suala hili lifanyiwe kazi na Makumbusho ya Taifa ipewe kipaumbele katika bajeti hii ili kuyapa uhai. Vilevile kuongeza motisha kwa wafanyakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kimondo Wilayani Mbozi. Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe kuna kimondo ambacho kilianguka, kimekuwa kikitembelewa na Watanzania kutoka pande zote za nchi yetu na vilevile wasanii kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali iangalie namna nzuri ya kuboresha mazingira ya kile kimondo. Mazingira yale yakiboreshwa na vilevile kimondo kile kikipewa kipaumbele na Wizara katika kutangazwa kitaweza kujulikana Kimataifa na hivyo Taifa litaweza kujiingiza kipato huku wakazi wa Mbozi wakinufaika kiuchumi na kijamii na uwepo wa kivutio hicho katika Wilaya yao na Mkoa wa Songwe kiujumla.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema na uzima kuweza kufika siku ya leo. Kipekee kabisa, nitumie fursa hii kumshukuru Waziri wangu, Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe, kwa miongozo mikubwa ambayo amekuwa akinipatia katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nitumie fursa hii kuishukuru kwa dhati Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa michango yake mizuri ambayo imekuwa ikitoa kwa Wizara yangu. Vilevile nishukuru pia michango yote ambayo imeweza kutolewa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimepewa muda mchache, nitaomba nijielekeze katika masuala machache, hususan nikianza na hoja ambazo zimeibuliwa na Kamati. Kuna hoja ambayo imetolewa na Kamati ya namna gani sisi kama Wizara tutaboresha suala zima la Chaneli yetu ya Utalii ambayo tumeianzisha mwaka jana.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba sisi kama Wizara tunayo mipango mizuri kabisa ya kuhakikisha kwamba tunaboresha Chaneli yetu hii ya Utalii. Kwa sababu ndiyo tunaanza mwaka wa fedha wa 2019/2020 tumejipanga kushirikiana na wadau wetu kuhakikisha kwamba Chaneli hii ya Utalii inafanyiwa maboresho makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na Wajumbe wa Kamati kwamba tunayo mipango mizuri sana ya kuhakikisha kwamba Chaneli hii ya Utalii kwanza inaboreshwa lakini vilevile itakuwa ni chaneli ambayo inaweza kusikika kimataifa. Kwa sababu lengo ni kuhakikisha chaneli hii siyo kwamba inasikika tu ndani ya nchi lakini pia iweze kusikika kimataifa.

Mheshimiwa Spika, mipango ambayo tunayo mpaka sasa hivi tayari Chaneli hii ya Utalii imekwishaanza kuoneshwa kwenye chaneli mbalimbali za kimataifa ikiwepo kwenye chaneli ya DSTV, Zuku na kwenye chaneli zote ambazo zinatumia mfumo wa satellite. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwa kufanya hivyo itakuwa ni njia mojawapo ya kuweza kusaidia Chaneli yetu ya Utali iweze kutazamwa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, Chaneli yetu hii ya Utalii kwa sababu ni chaneli ambayo iko ndani ya nchi lakini tunajua kwamba kimataifa huko tunazo chaneli nyingi sana ambazo zimebobea katika masuala haya ya utalii, mpango wetu wa kwanza ni kuhakikisha kwamba tunashirikiana na makampuni mbalimbali ya kimataifa ambayo yamebobea kwenye masuala haya ya utalii kuhakikisha na sisi kama nchi Chaneli yetu ya Utalii inaweza kutazamwa kimataifa. Kwa hiyo, huo mpango tunao na tunaamini kabisa kwamba muda mfupi na ndani ya mwaka wa fedha huu ambao tunauanza wa 2019/2020, mazungumzo hayo yatakuwa tayari yameshakamilika na Chaneli yetu ya Utalii itaanza kuonekana katika hizo chaneli za kimataifa ikiwemo Chaneli ya National Geographic.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine ya Kamati ambayo imezungumza kuhusu kuboreshwa Shirika letu la Magazeti (TSN). Nikiri kwamba kumekuwa na changamoto ya muda mrefu hususan katika suala zima la mapato, kwamba mapato mengi hususani suala zima la matangazo katika magazeti haya ya Serikali yamekuwa yakishuka. Changamoto hii ilitokana na kwamba kumekuepo na ukuaji mkubwa sana wa kasi ya teknolojia ambayo kwa namna moja ama nyingine iliathiri upatikanaji wa matangazo katika magazeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba sisi kama Wizara tumeliona hilo na kunapokuwa na changamoto yoyote ile lazima tuangalie namna gani ambavyo tutaitumia hiyo changamoto kama fursa. Sisi kama Wizara kwa kushirikiana na TSN tumekuja na mpango wa kuhakikisha kwamba tunaweza kukabiliana na hiyo changamoto, kwa sababu suala la ukuaji wa teknolojia, pamoja na kwamba inaweza kuwa changamoto kwa namna moja lakini vilevile ni fursa ambayo naamini hata sisi tukiitumia inaweza kusaidia sana katika kuboresha haya Magazeti ya TSN.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tuna mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba na sisi tunaanzisha chaneli yetu wenyewe ya kimtandao. Televisheni hiyo tayari imekwishaanzishwa ambayo inaitwa Daily News Digitals. Tunashukuru kwa sababu televisheni yetu hiyo ya mtandao inafanya kazi nzuri sana. Ndani ya muda mfupi mafanikio ni makubwa sana kwani watazamaji wameongezeka lakini vilevile imesaidia sana kuweza kuongeza mapato katika Taasisi yetu hii ya TSN.

Mheshimiwa Spika, iko hoja pia ya Kamati ambayo imezungumzwa kuhusu Serikali iangalie namna gani ya kuweza kuongeza fedha katika Chuo chetu cha TaSUBa kwa sababu kumekuwa pia kuna changamoto kwamba chuo kipo kwenye ukingo wa ufukwe wa bahari na mara kwa mara kunatokea mawimbi ambayo yanaathiri miundombinu ya chuo kile. Niseme kwamba ushauri ambao umetolewa na Kamati tumeupokea lakini kwa sababu ni suala la kushauriana na Wizara ya Fedha na uzuri wenzetu wa Wizara ya Fedha wako humu ndani, sisi kama Wizara tunaendelea na mashauriano kuhakikisha kwamba chuo chetu hiki ambacho kimsingi kimetunukiwa kuwa chuo cha ubora uliotukuka katika Afrika Mashariki kwa maana ya center of excellence, kuhakikisha kwamba Serikali inatenga pesa lakini kila mwaka pesa zinatolewa. Hilo likifanyika tutaweza kumaliza changamoto mbalimbali ikiwemo hilo suala la kuweka fensi ili kuweza kuzuia bahari isiweze kuharibu miundombinu ya chuo vilevile kuhakikisha tunajenga na kuboresha madarasa pamoja na kumbi mbalimbali ambazo zipo kwenye hicho chuo.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine ambayo pia imetolewa kuhusiana na Kampuni ya Beijing Construction Engineering, kwamba inakwenda kumaliza muda wake mwezi Agosti 2019, itasababisha Uwanja wetu wa Taifa utakosa mdhamini wa kuweza kuukarabati. Nikiri kwamba ni kweli, sisi kama Wizara tunatambua kwamba tuliingia mkataba na Jamhuri ya Watu wa China kupitia hiyo Kampuni ya Beijing Construction Engineering na unakwenda kumalizika Agosti, 2019.

Mheshimiwa Spika, lakini nitumie fursa hii kuwatoa hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi kama Wizara tupo kwenye mazungumzo na kampuni hii ili kuhakikisha tunauhuisha mkataba huu. Niseme kwamba mazungumzo yetu yamefika pazuri na tunaamini kwamba tutakapofikia mwafaka mkataba ule utaweza kuhusihwa ili kuhakikisha kwamba kampuni hii inaendelea kuhudumia Uwanja wetu wa Taifa katika masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya umeme, maji pamoja na miundombinu mingine.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye hoja mbalimbali ambazo zimeibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Kuna hoja ambayo imeibuliwa na Kamati, Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mheshimiwa Shangazi pamoja na Mheshimiwa Juma Nkamia kuhusiana na suala zima la kuboresha mitambo ya TBC. Ni kweli kwamba siku za nyuma tulikuwa tuna tatizo kubwa sana la uchakavu wa mitambo ya TBC. Nikiri kwamba Serikali ya Awamu ya Tano tangia ilipoingia madarakani tumeona bajeti ya uboreshaji wa Shirika letu la TBC ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Ukianza bajeti ambayo ilitolewa mwaka 2016/2017 ilikuwa Sh.1,000,000,000; mwaka 2017/2018 ikapanda ikawa Sh.3,000,000,000; na sasa hivi 2019/ 2020 imefika Sh.5,000,000,000. Sasa tunavyoingia kujadili bajeti ya mwaka 2019/2020, bajeti kwa ajili ya kuboresha masuala yote yanayohusiana na TBC imefika Sh.5,000,000,000. Kwa hiyo, Serikali ina nia ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba tunaboresha mitambo. Hata ukienda kwenye ofisi ambazo ziko pale Mikocheni, Dar es Salaam imefungwa mitambo mipya kabisa ambayo inafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, lengo la haya yote ni kuhakikisha kwamba Shirika letu la TBC kwa sababu kazi yake ni kuhabarisha umma, Watanzania waweze kupata habari ambazo ni za ukweli na za uhakika, tunataka shirika hili lifanye kazi yake kwa umakini ili Watanzania waweze kuhabarishwa. Yapo mambo mengi mazuri ambayo yametekelezwa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya mambo mazuri sana, ndiyo maana mimi nikisikia humu Bungeni Wabunge wanakuja na hoja kwamba kwa nini TBC inaonesha Live ziara za Mheshimiwa Rais, hilo suala mimi linanipa shida sana kwa sababu kwanza kile ni chombo cha umma lakini vilevile Mheshimiwa Rais anafanya kazi ya Watanzania, hafanyi kazi ya Chama cha Mapinduzi na anapokuwa kwenye ziara anagusa matatizo ya Watanzania wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tutakuwa ni mashahidi namna gani ambavyo kwenye ziara za Mheshimiwa Rais huko mikoani ukipita sehemu zote unakuta Watanzania wametulia wanafuatilia kazi ambazo Mheshimiwa Rais anazifanya; iwe ni baa, saluni au mabenki kwa sababu Watanzania wanaona namna gani ambavyo Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri. Kwa hiyo, mimi niseme kwamba hatuwezi kuacha kuonesha ziara za Mheshimiwa Rais kwa sababu ni mambo ambayo yanahusu maendeleo na yanawagusa Watanzania na Watanzania ni vitu ambavyo wanapenda kuviona. Sasa kusema kwamba kwa nini tunamuonesha ni hoja haina nguvu wala mashiko. Kwa sababu Mkurugenzi wa TBC yuko humu ndani, mimi nimwambie kwamba aendelee kufanya kazi kuhakikisha kwamba Watanzania wanajua namna gani ambavyo Serikali yao inatekeleza Ilani pamoja na ahadi ambazo ziliahidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine ambayo imeibuliwa na Mheshimiwa Amina Mollel, amezungumza kuhusiana na maslahi duni ya wafanyakazi wa TBC. Niseme kwamba kwa kipindi kirefu sana sisi kama Wizara tumekuwa tukijitahidi kuhakikisha kwamba maslahi ya watumishi wa TBC yanaboreshwa na tumechukua hatua mbalimbali. Mojawapo ni kuhakikisha kwamba tunapeleka ombi kwa Msajili Mkuu wa Hazina ili basi aweze kuboresha mishahara ya watumishi wa TBC. Tunaamini kwamba katika mwaka huu wa fedha 2019/2020, maslahi hayo ya watumishi likiwemo suala la kupandishwa mishahara yatazingatiwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, malizia Mheshimiwa Naibu Waziri, tayari muda.

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi kumekuwa kuna changamoto kubwa sana ya malimbikizo ya madeni kwa watumishi wa TBC. Niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu mpaka sasa hivi imekwisha kutoa Sh.3,200,000,000 kwa ajili ya kumaliza madeni yote ya watumishi wa TBC. Kwa hiyo, Serikali ipo makini inafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kabla sijaanza kutoa mchango wangu napenda nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mama yetu kipenzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kutupia jicho kwenye Idara ya Maendeleo ya Jamii, kwa kumteua Naibu Waziri ambaye kimsingi atawajibika moja kwa moja kwenye kusimamia Idara hii ya Maendeleo ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hayo kwasababu, ni Afisa Maendeleo wa Jamii kwa hiyo nisingekuwa Mbunge leo hii Juliana Shonza ningekuwa Afisa Maendeleo ya Jamii kwa hiyo, ninajua changamoto mbalimbali ambazo zinaikumba Idara hii. Ukiangalia chanzo cha kuanzishwa Idara ya Maendeleo ya Jamii, ni zile changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza kipindi kile miaka 1750 kipindi ambacho kulitokea na mapinduzi ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapinduzi hayo ya viwanda yalipelekea changamoto mbalimbali kwenye jamii ikiwepo, ukosefu wa ajira, watoto wa mitaani, lakini vile vile, migomo pamoja na maandamano ndipo walipoamua wakaona kwamba sasa kuna umuhimu wa kuja na sekta au Idara ambayo moja kwa moja ita-deal na masuala ya jamii kwa maana ile mifumo mizima ya jamii ambayo inaletwa na mabadiliko mbalimbali kwenye jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema haya yote kwasababu, leo hii kwenye halmashauri zetu tunao maafisa maendeleo ya jamii lakini katika namna ya kushangaza na kusikitisha sana, maafisa maendeleo hawa hawafanyi majukumu yao ya kimsingi, ile dhana halisi ambayo ilipelekea kuanzishwa kwa Idara hii ya Maendeleo ya Jamii imeachwa na hatimaye sasa hivi, maafisa hawa wamegeuka kuwa maafisa mikopo. Kitu ambacho sio jukumu lao la kimsingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu kwamba kwenye jamii yetu sasa hivi changamoto ziko nyingi. Kuna masuala ya ubakaji kwa watoto, ulawiti na hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kesi nyingi sana ambazo zipo huko kwenye jamii zetu, nyingi zinaishia kule kule kwenye jamii, hazisikiki na haki inakuwa haitendeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Iringa Mheshimiwa Rose Tweve kuna siku alisimama hapa akazungumza kwa hisia sana kwamba kuna mtoto ambaye amebakwa na mzazi wake na mwisho wa siku akaambukizwa na UKIMWI, lakini kesi hiyo haijaenda popote, mzazi huyo yuko mtaani, anaendelea kudunda wakati mtoto huyu tayari future yake imeshaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu changamoto kama hizi ziko nyingi. Unaweza kujiuliza kwamba kesi kama hizi ziko ngapi kwenye jamii yetu? Hata hivyo, sisi kama Serikali ni nani ambaye tumemweka kule chini ambaye moja kwa moja anawajibika kwenye kushughulikia hizi kero na changamoto na mifumo hii ya kijamii ambayo inaleta athari kwenye jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia suala zima la mmomonyoko wa maadili, suala zima la miradi mikubwa ya maendeleo ambayo Serikali imekuwa inapeleka fedha nyingi sana kule chini kwenye jamii yetu; lakini mwisho wa siku miradi ile imekuwa haiendelei, inakufa. Ukiangaliza chanzo ni nini? Ni kwa sababu jamii ile haijashirikishwa ipasavyo kuweza kuji-engage kwenye ule mradi ili waweze kuona kwamba nao ni sehemu ya ule mradi na kwamba Serikali imewaletea ule mradi siyo kwamba ni mradi wa Serikali peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo ni la msingi sana, nami nikaona kwa sababu sasa hivi tumepata Naibu Waziri wa kusimamia suala hili, ni vyema niweze kutoa maombi yangu kwamba jambo la msingi la kufanya kwa sasa hivi, cha kwanza kama akiona inafaa, Serikali iweze kuangalia ili tupitie upya ule mfumo wa upatikanaji wa Maafisa Maendeleo ya Jamii na majukumu yao. Warudi wakafanye kazi yao ya msingi kule kwenye jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, Serikali imekuja na Mpango mzuri sana na imetuahidi kwamba ikiwezekana ndani ya Bunge hili wataleta Muswada wa Bima ya Afya kwa wote. Muswada huo ni mzuri kwa sababu upo kwenye Ilani ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ila swali la msingi la kujiuliza ni je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba mradi huo unaweza kutekelezwa ipasavyo na ukaleta tija kama ambavyo Serikali imekusudia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu suala la Bima la Afya kwa wote siyo suala la Serikali peke yake, maana yake ni Serikali pamoja na wananchi wote kwa pamoja tuna jukumu la kuchangia na kushiriki kikamilifu kuhakikisha kwamba mradi huu, mkakati wa Serikali na sera hiyo inaweza kutekelezwa ipasavyo na kuweza kuleta matunda ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi ni kwamba tumejiandaa vipi? Kwa sababu hili ni suala la elimu. Tutoke kwenye ule mfumo wa kuanzisha miradi au mikakati au sera halafu tunawapa taarifa wananchi. Tuingie kwenye mfumo wa kuwaelimisha wananchi wafahamu umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu, tunaishi kwenye jamii ambayo ina misingi mbalimbali. Tunatofautiana masuala ya mila na desturi; na mapokeo juu ya mambo mbalimbali ya kijamii. Kwa mantiki hiyo, ni lazima tupate watu ambao wataenda kule chini kuelimisha jamii waone umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko dini ambazo mpaka sasa hivi wao hawaamini kabisa kuhusiana na suala la tiba za kisasa. Zipo jamii zetu ambazo zinaamini katika ugonjwa wowote, ni mtu amelogwa. Hizi ni changamoto zilizopo kwenye jamii yetu. Pia ziko jamii ambazo zinaamini sana kwenye mitishamba kuliko kwenda hospitali. Kwa hiyo, ukiangalia mabadiliko haya na suala zima la mfumo kwenye jamii; ili Serikali iweze kutekeleza azma yake hiyo ambayo ni njema sana kwa Watanzania, ni lazima tuwatumie Maafisa Maendeleo ya Jamii waende kule chini wakaelimishe jamii waweze kuona umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijikite kwenye kutoa ushauri wangu kwa Serikali. Kwanza napenda kuishauri Serikali ipitie upya mfumo mzima wa Maafisa Maendeleo ya Jamii, warudi wakafanye kazi zao za kimsingi. Tunafahamu kwamba kule chini wako Maafisa Ushirika ambao kimsingi ndio ambao wanasajili VIKOBA pamoja na SACCOS. Naamini hawa wanaweza wakatumiwa vizuri na wakaleta maendeleo, wakafanya kazi ya kusajili vile vikundi vya vijana, akina mama pamoja na watu wenye ulemavu ili hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii wabaki kwenye jukumu lao la msingi la kushughulika na matatizo ambayo yapo kwenye jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa pili kwa Serikali, kwa sababu tunatambua kwamba imekuwepo changamoto pia ya muda mrefu kwamba Maafisa Maendeleo ya Jamii tulionao sasa hivi hawatoshi; nikisemea tu kwenye Mkoa wangu wa Songwe tunazo wilaya nne, lakini tuna Maafisa Maendeleo ya Jamii wawili tu. Sasa huko chini kwenye vijiji na Kata bado hatuna Maafisa Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe tu ushauri kwa Serikali kwamba katika kipindi hiki ni vyema wakaangalia namna gani ya kuweza kuajiri Maafisa Maendeleo ya Jamii kama ambavyo Serikali imefanya na imefanikiwa kuajiri Watendaji wa Vijiji. Kwenye kila Kijiji Tanzania kumekuwa kuna Watendaji wa Vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini hata kwa hili la Maafisa Maendeleo ya Jamii haliwezi kushindikana kwa sababu ni Idara ambayo ni nyeti sana; na kama tukiipa kipaumbele kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha kuipa kipaumbele Idara hii, naamini hizi changamoto za kijamii za kimfumo zitapungua ikiwezekana, kumalizika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine, nataka kuishauri Serikali kwamba wanasema jambo lolote ili liweze kufanikiwa, ni lazima liandaliwe. Kwa hiyo, vile vile kwa sababu tunakwenda kwenye Bima ya Afya kwa wote, waangalie sasa namna gani ambavyo watawaita hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii baada ya kwamba wameshaajiriwa na kupatikana kwa kutosha ambao ndio tunategemea kwamba waende kule chini wakaelimishe jamii, ni vyema Serikali sasa ikaangalia na wao pia waweze kuelimishwa, waandaliwe ili vile vile waweze kutafsiri ile Sera ya Serikali kulingana na tofauti za kijamii ambazo tunazo, kulingana na mila na desturi na tamaduni zote ambazo zipo kwenye jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala la vitendea kazi. Hii imekuwa ni changamoto kubwa sana kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii. Wengi wako maofisini, hawafanyi kazi yoyote ya kwenda kule chini kwenye jamii kwa sababu tu inawezekana hawana vitendea kazi, lakini kwa sababu walikuwa bado hawajajua kwamba wao wanasimamia kwenye majukumu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri pia Serikali yangu ya Awamu ya Sita kwamba ni vyema, kama ambavyo imefanya vizuri kwenye Maafisa Kilimo, sasa hivi kila Afisa Kilimo amepewa usafiri, vile vile wale Waratibu Kata wa Elimu wamepewa usafiri. Naamini hata kwa hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii wakipewa vitendea kazi, wanaweza wakafanya kazi nzuri zaidi na hata miradi ya Serikali itapiga hatua mbele kwa sababu hawa ndiyo wa kwenda kuelimisha jamii na kuhakikisha kwamba Serikali inaweza kufikia yale malengo ya milenia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nashukuru kwa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishukuru kwa kupata nafasi ya kuweza kutoa maoni yangu katika bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nataka nianze kwa kumpongeza sana Waziri wa Fedha kwa bajeti yake hii ambayo ameiwakilisha, bajeti ambayo kimsingi ni ya kimkakati na imejikita kweli kweli kwenye kutatua changamoto za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana mama yetu mpendwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa bajeti hii nzuri, ambayo moja kwa moja inaonyesha nini ambacho amekusudia kuwatendea Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe kusema kwamba, hii ni bajeti ya wananchi; na ziko sababu nyingi sana ambazo zinaonesha na kuthibitisha kwamba bajeti hii ni bajeti ya wananchi wa Tanzania. Ikizingatiwa kwamba, ndiyo bajeti yake ya kwanza tangu alipoingia madarakani, lakini ndani ya muda mfupi huo amefanikiwa kwa asilimia 100 kuonesha nini ambacho amepanga kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. Vilevile ameonesha vipaumbele vyake vizito alivyonavyo katika kufikia maono hayo. Ni wazi kwamba Rais wetu Samia Suluhu Hassan, amebeba maono makubwa sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kana kwamba haitoshi, ukifuatilia hii bajeti imegusa makundi mbalimbali katika jamii yetu. Sisi sote ni mashahidi, tumekuwa tukizungumza humu Bungeni changamoto kubwa ya watumishi. Kilio kikubwa cha watumishi ilikuwa ni kupandishwa madaraja. Kupitia kwenye bajeti hii, mama yetu ameweza kutenga zaidi ya bilioni 449, kwa ajili ya kupandisha madaraja watumishi. Jambo hilo lina tija kubwa sana. Kwa sababu, kwanza litasaidia sana kuweza kuongeza motisha kwa watumishi wetu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi, tunafahamu, ilikuwepo tozo ya asilimia sita ya ongezeko la thamani. Tozo ile ilikuwa inasababisha deni lilikuwa haliishi; unalipa lakini bado deni linaendelea kuongezeka. Watumishi wamefurahi sana kwa kuondokewa kwa tozo hiyo, kwa sababu sasa ni wazi moja kwa moja, itasaidia kuweza kukuza uchumi wa watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu changamoto ambazo zipo kwenye barabara zetu, na barabara nyingi ambazo zinachangamoto kubwa ni zile barabara za vijijini. Lakini kupitia bajeti hii fedha zimetengwa za Kimarekani milioni 300 kwa ajili ya kwenda kusaidia barabara za vijijini, na hizo fedha zinatoka kwenye mkopo wa Benki ya Dunia. Vilevile, dola za kimarekani milioni 50, kwa ajili ya kwenda kuhudumia barabara zetu za vijijini (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kilichonifurahisha zaidi ni kwa sababu huu mkopo moja kwa moja utapelekwa kwenye yale maeneo ambayo yana tija kubwa ya uzalishaji, na hicho ndicho kilichokuwa kilio cha Bunge hili, kwamba sehemu nyingi ambazo zinatumika kwa ajili ya uzalishaji barabara zake zilikuwa zina changamoto kubwa sana. Mimi kama Mbunge wa wanawake wa Mkoa wa Songwe nimefurahi sana kwa sababu sote tunafahamu wazalishaji wakubwa ni wanawake. Kwa hiyo moja kwa moja fedha hizi zitasaidia sana kuweza kukuza uchumi wa wananchi, hususani uchumi wa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ipo tozo ambayo imewekwa kutoka kwenye mafuta. Mimi nasema Bunge lililopita Waheshimiwa Wabunge wote humu Bungeni tulikuwa tukisimama tunaiomba Serikali. Kwamba Serikali tunaomba iongeze tozo kwenye mafuta ili kwenda kushughulikia changamoto zetu. Na leo tumeshuhudia Serikali imesikia kilio hicho na tozo hiyo imeongezeka, kwa lengo ambalo ni jema la kwenda kukarabati barabara zetu za kule vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wanawake tunajua namna ambavyo tulikuwa tunapata shida sana inapokuja suala la hizi barabara. Wanawake wengi walikuwa wanajifungulia barabarani, wanajifungulia njiani kutokana na ubovu wa hizi barabara. Sisi wanawake tunamshukuru sana Rais wetu kwa sababu sasa suala la wanawake kujifungulia barabarani linafikia kikomo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi ambayo nikianza kuyaeleza ni mambo mazuri ambayo yapo kwenye bajeti yetu. Lakini ni wazi kwamba, ili mambo hayo yote yaweze kutekelezwa itakuwa si sawa kwamba mzigo huu wote ukaachiwa Serikali. Ni lazima wananchi tuweze kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba haya mambo mazur, ambayo Rais wetu ameyakusudia kwa Watanzania yanapatiwa ufumbuzi. Na namna pekee ya kuwashirikisha wananchi ni kupitia kodi. Mwalimu Nyerere alisema wakati wa Azimio la Arusha; naomba ninukuu kwamba:-

“kila mtu anataka mendeleo, lakini si kila mtu anaelewa na kukubali mahitaji ya msingi, kwa ajili ya maendeleo”. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya msingi kwa ajili ya maendeleo ni pamoja na kuwa na Serikali nzuri, kufanya kazi kwa bidii, wananchi kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yao pamoja na Serikali kusimama kidete katika ukusanyaji wa kodi. Ni wazi kwamba Serikali isiyokusanya kodi ni Serikali ambayo ni mfu. Ni Serikali ambayo ni mfu kwa sababu daima haiwezi kuwapelekea maendeleo wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia kwenye bajeti hii, kwamba Serikali imeleta kodi aina mbalimbali. Sasa mimi nataka nizungumzie kodi ya Property Tax kwa sababu, ni kodi ambayo ilikuwepo miaka mingi, si kitu ambacho ni kipya. Hata hivyo changamoto yake ilikuwa ni kwamba, kodi hiyo wananchi tulikuwa hatulipi nikiwemo mimi mwenyewe Juliana Shonza, sijawahi kulipa kodi ya majengo. Hii ni kutokana na usumbufu ambao mtu ukifikiria, utoke, uende ukapange foleni TRA, ilikuwa ni usumbufu mkubwa sana. Sasa Serikali imekuja na ubunifu wa kukusanya kodi, na imetumia akili kwamba sasa kodi hii itakusanywa kwa akili kuliko kutumia nguvu na mabavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie changamoto chache ambazo zipo kwenye hii kodi. Niishauri Serikali, kwamba tunatambua wazo ni jema na ubunifu ambao umefanyika ni mzuri. Ni lazima sasa Serikali iweze kusimamia, ili basi, katika utekelezaji wa agizo hili la Serikali kusije kukaibuka sintofahamu na changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ya majengo ya awali inasema kabisa kwamba suala la kulipa kodi ya majengo ni suala la mwenye nyumba si suala la mpangaji. Kwa hiyo kwenye agizo hili nataka nimuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, atakaposimama hapa kuja ku-windup bajeti yake atuambie Serikali imejipangaje, ina mkakati gani wa kuondoa sintofahamu kati ya mwenye nyumba pamoja na mpangaji? Kwa sababu ni kweli mmiliki wa nyumba ni mwenye nyumba, lakini kwa kuwa kodi inakatwa kwenye LUKU maana yake atakayekuwa anakatwa ni mpangaji na si mwenye nyumba. Kwa hiyo nilikuwa naomba Serikali ilete utaratibu mzuri ambao imejipanga kuhusiana na kodi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunafahamu katika sheria ya kodi wazee wa miaka 60 walikuwa exempted kwenye kulipa kodi hii. Sasa sijajua, kwenye sheria hii haijazungumza kwa sababu sheria hii imesema kwamba agizo hili kwenye bajeti, kwamba ni nyumba yoyote ambayo ina umeme. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-windup atuambie kuhusu kwa wale wazee ambao wana miaka 60 na kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kuna zile nyumba ambazo inakuwa ni nyumba moja lakini kila mtu anakuwa na LUKU yake, utaratibu utakuwa vipi? Kama haitoshi kuna yale maeneo ambayo yalikuwa nje ya wigo wa kodi; kuna maeneo ambayo kodi hii ilikuwa haiwagusi, je, Serikali imejipangaje kuweza kuhakikisha kwamba kodi hiyo wakati wa kuanza kuikusanya haitaleta mgongano? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema kwamba, bajeti hii ni nzuri sana. Ni kwa sababu ni takwa tu la kisheria kwamba ijailiwe, lakini ilipaswa ilipomalizwa kusomwa pale Wabunge wote tuipitishe iweze kupita kwa kishindo kwa sababu imebeba mambo mazuri sana. Rais wetu ni sawa na mama ambaye ameandaa chakula kazi yetu imebaki ni kuweza kula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tuiunge mkono bajeti hii kwa sababu, imekusudia kuweza kutatua changamoto mbalimbali kwa wananchi. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa kupata nafasi ili niweze kutoa mchango wangu. Kwanza nianze kwa kupongeza Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. Vilevile kipekee kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba anawapatia maendeleo Watanzania. Nimpongeze sana kwa kampeni yake ambayo ameianza ya kuwapanga wamachinga ili waweze kupata maeneo bora kwa ajili ya kuweza kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Spika, nikupongeze pia wewe mwenyewe binafsi pamoja na Bunge lako. Wewe na Bunge lako mmekuwa mstari wa mbele sana katika kuhakikisha kwamba mnasimamia masuala ya usawa wa kijinsia ndani ya Bunge. Bunge lako linazo Kamati mbalimbali na katika hizo Kamati pamoja na Wabunge mbalimbali hakuna Kamati hata moja ambayo Mbunge wa Viti Maalum anazuiliwa kuingia ndani ya Bunge hili. Wabunge wa Viti Maalum wanaingia mpaka kwenye Kamati ya Bajeti, lakini katika hali ya kusikitisha iko shida kubwa sana katika halmashauri zetu Wabunge wa Viti Maalum tunakatazwa kuingia kwenye Kamati ya Fedha. Kamati ambayo ndiyo inapanga mipango yote ya maendeleo ya halmashauri zetu, Kamati ambayo ndiyo inayopanga hata zile asilimia 10, kwa maana nne kwa ajili ya akinamama, nne kwa ajili ya vijana, lakini asilimia mbili kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, hali hiyo inasikitisha sana na sisi kama Wabunge na nakumbuka kwa sababu mimi ni Mbunge wa kipindi cha pili sasa, tumekuwa tukizungumza sana hata Bunge lililopita tuliongea, lakini mpaka sasa hivi hakuna ambalo limefanyika.

Mheshimiwa Spika, kazi nzuri na kazi kubwa ya Mbunge ni kusimamia maslahi ya watu anaowaongoza. Kwa hiyo na sisi Wabunge wa Viti Maalum tumeaminiwa na wanawake wa mikoa yetu. Mimi Shonza ni Mbunge wa kipindi cha pili, nimeaminiwa na wanawake wa Mkoa wangu wa Songwe ili niwasimamie maslahi yao na namna ya kusimamia maslahi yao ni Bungeni na kule kwenye halmashauri zetu, ambapo huko ukiingia Mbunge wa Viti Maalum wanasema kwamba sheria inakataza Mbunge wa Viti Maalum kuweza kuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha. Sasa matokeo yake fedha hizo ambazo zinatolewa ni nyingi lakini fedha hizo zimekuwa hazirejeshwi. Aliongea hapa juzi Mheshimiwa Festo kwa uchungu mkubwa sana, fedha zinazotolewa ni nyingi lakini shida ipo kwenye marejesho, kwa sababu sisi ambao ndiyo viongozi ambao tunakaa na hao watu tunajua changamoto zao…

SPIKA: Mheshimiwa Shonza, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Leah Komanya.

T A A R I F A

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa hata kwenye kukabidhi fedha hizi katika mkoa mmoja sehemu moja anakabidhi Mkuu wa Mkoa sehemu moja anakabidhi Mbunge, kwa hiyo kunakuwa na double standard lakini makundi yale ya jamii hayashirikishwi katika ule mwongozo uliopewa, kazi hii tungeachiwa Wabunge kwa sababu tunawajua wananchi ili vijiji vyote viweze kutendewa inavyotakiwa.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Niseme kwamba nakubaliana kabisa na taarifa ambayo amenipa na maelezo ambayo umeyatoa.

Mheshimiwa Spika, changamoto imekuwa kubwa kwa sababu fedha hizi kama ambavyo nimesema, huwa hazirejeshwi, kwa sababu hakuna intervention ya Wabunge kwenye kusimamia hizi fedha. Nitatoa mfano mmoja. Kwenye Jimbo la Tunduma ambalo anatoka Mheshimiwa David Silinde, Mheshimiwa Naibu Waziri, amekuwa akizisimamia hizi fedha na tumeona juzi alitoa fedha nyingi sana; alitoa bodaboda, akatoa bajaji akatoa na zaidi ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya kusaidia makundi ambayo yapo kwenye Mkoa wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto kwenye Halmashauri nyingine na Majimbo mengine Wabunge hawashirikishwi. Nami kama Mbunge wa Viti Maalum, nilipigiwa simu na nikaambiwa kumbe ni kweli hizi fedha huwa zipo. Kwa sababu wengine wanaona kama ni historia, ni kitu ambacho hakipo, kumbe ni fedha ambazo zipo na Serikali inafanya kazi kubwa sana kutoa hizi fedha, lakini changamoto ni kwamba intervention ya Wabunge hakuna. Kwa hiyo, tumeona kwamba maeneo ambayo yamepata fedha hizi na kuna intervention ya Mbunge, mafanikio ni makubwa sana. Nampongeza Mheshimiwa David Silinde kwa sababu ni Waziri hawezi kusema, lakini mimi kama Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wake, ninampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni kwamba hizi fedha haziendi kwa wahusika, yaani unakuta kuna watu wanapata fedha lakini hawana vigezo vya kupata hiyo mikopo. Pia kuna maeneo mengine Wilaya moja ina vijiji 100, lakini kwenye kuzigawa hizi fedha utashangaa mgao ni shilingi milioni 100. Shilingi milioni 50 yote inakwenda kwenye Kijiji kimoja, kwenye kikundi kimoja. Kwa hiyo, bado unakuta kuna double standard kwenye kugawa hizi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema, kwa kweli wakati umefika, sisi kama Wabunge tukae, tujadili. Hili suala naomba lifike mwisho ili sisi Wabunge, wakiwepo Wabunge wa Viti Maalum wanawake, Wabunge wanaowakilisha Vijana na wa Majimbo, sisi ndio tuwe wasimamizi wa huu mfuko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijikite kwenye kutoa ushauri kwa Serikali. Kwa kuwa Wabunge kwa miaka mingi tumekuwa tukilalamika juu ya suala la Wabunge kutokuingia kwenye Kamati ya Fedha, naomba sasa, kwa sababu Mawaziri wapo hapa na wanatusikia, ni wakati muafaka sasa hili suala lifike mwisho, mtoe miongozo. Kama ni suala la kikanuni, basi hizo kanuni ziletwe humu ndani ya Bunge zibadilishwe; na tukishabadilisha humu ndani ya Bunge, hiyo miongozo ichukuliwe ipelekwe kule kwenye Halmashauri zetu ili tuweze kuondoa hii changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili; kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa sana kwamba sisi Wabunge Viti Maalum hatuna Mfuko wa Jimbo, Wabunge wa Viti Maalum vile vile hatuna miradi yoyote ambayo tunasimamia kwenye Halmashauri zetu; ukiwa Mbunge wa Viti Maalum, huwezi ukasema hata uende kukagua hospitali, haiwezekani. Utaulizwa, umekuja kukagua kama nani? Kwa hiyo, hatuna kazi specific ambayo Wabunge Viti Maalum tunapewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nitoe ushauri kwa Serikali, ninaamini kwamba Serikali inatusikia; naomba Serikali, ikiwezekana hii asilimia nne kwa ajili ya akina mama isimamiwe na Wabunge wa Viti Maalum. Kwa sababu ilivyo sasa hivi, asilimia nne kwenye hicho kikao, tena ikiwezekana iwe ni Mfuko wa Jimbo, kama ambavyo Wabunge wa Majimbo wana Mfuko ya Jimbo, nasi asilimia nne hii iwe ndiyo Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya Wanawake. Kwa sababu sisi ndio tunajua changamoto za wanawake, tunajua makundi gani ambayo yanapaswa kupatiwa mikopo na tunajua makundi gani ambayo hayana sifa. Kwenye hiyo Kamati, Mwenyekiti wake awe ni Mbunge wa Wanawake ili aweze kuisimamia vizuri hiyo asilimia nne. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe unafahamu, kwenye chaguzi zetu huwezi kuwa Mbunge wa Wanawake kama siku ya uchaguzi hujajipanga vizuri kwenda kuwaeleza wanawake utawasaidiaje waweze kupata mikopo ya asilimia nne? Kwa hiyo, huwa tunaongea tunawaambiwa wanawake, lakini kimsingi hatuna instrument ya kuweza kuwasaidia waweze kupata hii mikopo. Malalamiko yamekuwa mengi, kikundi kina sifa zote, kinaomba mikopo zaidi ya miaka mitano, miaka kumi, hakipati, lakini vikundi vingine ambavyo havina sifa vinapata mkopo. Hii ndiyo sababu ambayo inapelekea hata marejesho yake yanakuwa ya kusuasua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho kwa Serikali; naomba, kwa sababu tumeshuhudia sasa hivi Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan ameanzisha kampeni nzuri sana ya kuwapanga Machinga ili waweze kupata maeneo mazuri, wafanye wafanye biashara zao kwa amani ili hizi fedha ambazo zinakopeshwa kwa Machinga ziweze kurejeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri, kwa sababu Halmashauri inatenga 10%, naomba Serikali iangalie uwezekano wa ku- top up angalau 3% kwenye ile 10% ambayo inatengwa na Halmashauri ili hiyo 3% iende ikaboreshe miundombinu kule kwa wafanyabiashara kwenye kujenga masoko, kujenga viwanda, ili Serikali inapotoa fedha kuweza kuwakopesha, basi hawa vijana, akina mama na watu ambao wana makundi maalum, waweze kuwa na sehemu ya kuzifanyika hizi kazi. Nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuweza kukushukuru kwa kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Afya. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kasi kubwa anayoenda nayo ya kuhakikisha kwamba anatumbua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niseme kwamba inashangaza kuona waliokuwa wakipiga kelele kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni dhaifu sasa wamegeuka wanasema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni ya kibabe, wamegeuka wanasema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina utawala wa kiimla. Nashindwa kuelewa ni kipi ambacho hawa wenzetu wanataka tuwasaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka kwamba siku zote wamekuwa wakipiga kelele na bahati nzuri Hansard za Bunge hili zipo wamekuwa wakisema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kabisa kukusanya mapato. Tumeshuhudia baada ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kasi yake ya kuendelea kutumbua majipu, TRA kwa mwezi Aprili wameweza kukusanya mapato ya shilingi trilioni 1.035. Hii yote ni matokeo ya kasi kubwa na uwezo mkubwa wa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli lakini wenzetu hawa wamegeuka wanasema kwamba Serikali hii ni ya kibabe inatumbu majipu hovyo, hali hii inasikitisha. Kwa sisi kama wanasiasa vijana tunashindwa kujua nini hasa ambacho tutajifunza kutoka kwa hawa wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijielekeze kuzungumzia Wizara ya Afya. Kwa kuzingatia kwamba mwaka 2015 ilikuwa ni ukomo wa kuweza kufikia Malengo ya Milenia ambapo Lengo Kuu la Tano ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunapunguza vifo vya akina mama kufikia asilimia 75. Mpaka sasa hivi takwimu zinaonyesha kwamba vifo vya akina mama kila mwaka ni zaidi ya 15,000. Hali hii inatisha sana, inatisha kwa sababu akina mama wetu kule vijijini wanapata shida sana inapofika suala la huduma za kiafya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha kwa kina mama ukija kwenye vifo vya watoto, takwimu zinaonyesha kwamba ni zaidi ya watoto 40,000 kila mwaka wanafariki ndani ya saa 24. Takwimu hizi sisi kama Taifa hatupaswi kabisa kuweza kuzifumbia macho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile takwimu zinaonyesha kwamba akina mama 250,000 kila mwaka wanapata vilema vya uzazi, hali hii inasikitisha sana.
Mimi niombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ambayo ni sikivu iweze kuwahurumia kina mama hawa mfano mama zangu wa kule Songwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niishukuru sana Serikali kwa sababu imeweza kutupatia mkoa. Mkoa wetu wa Songwe, ni mpya lakini kama unavyojua changamoto ni kubwa kwa hii mikoa mipya. Mkoa wa Songwe hatuna kabisa Hospitali ya Mkoa, hiki ni kilio chetu, mimi nikiwa kama mwakilishi wa akina mama wote wa Mkoa Songwe naomba utusaidie katika jambo hili. Nashukuru kwa sababu Waziri wa Wizara hii ni mwanamke mwenzetu, Wanawake wa Mkoa wa Songwe wanapata shida sana, tunaomba na sisi muweze kutufukiria muweze kutujengea Hospitali ya Mkoa ili basi akina mama wale waweze kupata tiba kiurahisi. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, vilevile katika Wilaya ya Momba ambayo ni Wilaya mpya, cha kushangaza mpaka leo hii hatuna kabisa Hospitali ya Wilaya. Unaweza ukaona akina mama wa Wilaya ya Momba wanapata shida kiasi gani? Wilaya ile hakuna Hospitali ya Wilaya na sera katika Wizara ya Afya inasema kwamba ni kuhakikisha kwamba kila Halmashauri kunakuwa na Hospitali ya Wilaya. Halmashauri ile ya Momba mpaka leo hii hakuna kabisa Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kituo cha Afya pale Tunduma lakini ni kidogo, hakiwezi kutosheleza kuweza kuhudumia Wilaya nzima. Ni kituo ambacho kwa sasa hivi kinatumika kama Hospitali ya Wilaya ya Momba lakini kina changamoto nyingi. Naomba Waziri aweze kukiangalia Kituo kile cha Afya cha pale Tunduma. Kituo kile hakina madaktari wa kutosha, hakina x-ray za kutosha, ukiangalia hata sehemu ambako mama zetu wanaenda kujifungulia kwa kweli hali pale inasikitisha. Inafika mahali mama mjamzito anayeenda kujifungua katika kituo kile lakini hakuna sehemu ambayo mama huyo anaweza akaendelea kujisubirishia wakati anasubiri kwenda theater. Naomba sana Serikali iweze kukiangalia kile kituo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi navyoongea kuna vitanda vinne tu vya akina mama kujifungulia. Hicho ni kituo cha afya ambacho kinatumika kama hospitali ya wilaya lakini chagamoto zake ni kubwa mno. Mpaka sasa hivi kuna vitanda vitano tu ambavyo vinatumika kwa akina mama kupumzika baada ya kuwa wameshamaliza kujifungua. Kama unavyojua mama akishamaliza kujifungua inatakiwa akae chini ya uangalizi wa daktari si chini ya saa 24 lakini kwa sababu ya uhaba wa vitanda wanawake wale wanalazimika kutolewa ndani ya saa mbili, tatu kurudi nyumbani. Naomba sana suala hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kuweza kukumbusha ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni. Alipita pale Momba na kwa bahati nzuri pale Momba tuna majengo yako pale Chipaka. Majengo yale yalikuwa ni ya wakandarasi yameachwa pale, ni makubwa mno yanafaa kabisa kuweza kutumika kama hospitali ya Wilaya. Jambo zuri ni kwamba Mheshimiwa Rais alituahidi kwamba majengo yale ataweza kuyakabidhi kwa Serikali ili yaweze kutumika kama Hospitali ya Wilaya. Nimesimama mahali hapa kwa niaba ya wanawake wote wa Mkoa wa Songwe kuweza kumkumbusha Mheshimiwa Rais akumbuke ahadi yake aweze kuwapatia akina mama wale majengo yale ili basi Wilaya ya Momba tuweze kuwa na Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nizungumzie kidogo Idara ya Maendeleo ya Jamii. Idara hii ni muhimu sana kwa Taifa letu na ni mtambuka. Huwezi kwenda vijijini kwenda kutoa elimu ya ujasiriamali kwa akina mama kama hujatumia idara hii. Nionyeshe masikitiko yangu makubwa kwamba idara ile imesahaulika sana, wale Maafisa Maendeleo wamekaa pale kwenye Halmashauri hawana kazi, hawapelekewi pesa za OC ambazo zitawasaidia kushuka kule kijijini kuhakikisha kwamba wanatoa elimu ya ujasiriamali kwa akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawaomba Mawaziri wetu na nashukuru sana kwa sababu tuna Mawaziri ambao ni sikivu, dada yangu Ummy naomba sana wakati mwingine utakapokuwa ukitembelea hospitali unavyoenda unakutana na ma-DMO uchukue nafasi uweze kuonana pia na Maafisa Maendeleo ili waweze kukupa changamoto zao. Wamekaa pale Halmashauri hawana kazi, wanalia sana, kilio chao wanaomba ukisikie na mimi nina imani kabisa kwamba Serikali hii ni sikivu, itaweza kwenda kuwasikiliza na siku moja changamoto hizi zitafika mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ni huduma ya afya katika Wilaya ya Mbozi. Wilaya ya Mbozi ndiyo makao makuu ya Mkoa wetu wa Songwe. Ukifika pale ile wodi ya kujifungulia kwanza ni ndogo mno, wanalala kitanda kimoja akina mama wawili, watatu, inafika mahali mpaka wengine wanajifungulia chini. Naomba Serikali na naomba Mheshimiwa Waziri aweze kutuangalia katika wodi ile ya akina mama pale Mbozi kwa kuiongeza ukubwa ili basi wa akina mama wale waweze kujifungua mahali ambako ni salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naamini kwamba maombi haya yamezingatiwa na kilio cha akina mama wa Mkoa wa Songwe kitafika mwisho, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nishukuru kwa kupata nafasi hii. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ardhi pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya katika Wizara hii. Vilevile tuwashukuru sana kwa sababu wameweza kutupatia taarifa zote ambazo zinahusu Wizara hii ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua Mkoa wetu wa Songwe ni mpya na changamoto kubwa ni kwamba maeneo mengi hayajapimwa na wananchi wake wanamiliki ardhi kwa hati za kienyeji. Suala hili kwa Mkoa wa Songwe imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kama tunavyojua sasa hivi Wilaya yetu ya Mbozi imeweza kuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe ambapo wananchi wengi wanamiminika kwenda mahali pale kwa ajili ya kupata ardhi. Hata hivyo, ardhi wanauziana kienyejienyeji kwa sababu hakuna mpango wowote wa kuweza kurasmisha ardhi ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi kuomba Wizara ya Ardhi kwa kutambua kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya wahakikishe kwanza wanakomboa ile ardhi ambayo inamilikiwa na wananchi lakini ukienda kuangalia katika mpango wa Mkoa unakuta sehemu zingine zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Kwa hiyo, naomba Wizara hii iweze kuliangalia hili suala ili waweze kukomboa yale maeneo ambayo yanamilikiwa na wananchi lakini kiuhalisia yametengwa kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Wananchi wale wa Wilaya ya Mbozi walipwe fidia waweze kuyaachia maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, kama tunavyojua katika Wilaya yetu ya Momba, katika Mji wa Tunduma, mji ule unakua kwa kasi kubwa sana lakini mpaka sasa hivi mipango miji ya Mji wa Tunduma kwa kweli haieleweki. Mji ule ni mji wa wafanyabiashara, population iliyopo pale ni kubwa sana na nyumba zimejengwa kiholela holela na pale ndiyo taswira ya Tanzania kwa nchi hizi za Kusini. Mtu anapokuwa anatoka Zambia akifika pale, ile ndiyo picha halisi ya Tanzania, mtu anapotoka South Africa akifika pale ile ndiyo picha halisi ya Tanzania lakini mazingira ya pale Tunduma kwa kweli hayaridhishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuomba Wizara ya Ardhi, nimuombe sana Mheshimiwa Lukuvi aweze kuangalia eneo lile la Tunduma. Tumeshuhudia katika nchi zingine kwa mfano China, wenzetu waliweza kubadilisha miji yao wakajenga maghorofa, wananchi wakapata nyumba ambazo ni makazi mazuri. Kwa hiyo, naiomba Wizara hii iweze kutupia jicho katika Mji ule wa Tunduma ili basi yale maeneo yote ambayo ni squatter yaweze kuondolewa. Yakishaondolewa waje na mpango wa kutujengea majengo ya ghorofa ili basi wananchi wa pale waweze kuishi katika makazi salama. Naamini hili kwako Mheshimiwa Lukuvi linawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo tukijenga majengo ya ghorofa katika eneo lile, moja kwa moja Serikali itakuwa imepata ardhi ya wazi ambayo najua kabisa itatumika kwa ajili ya matumizi mengine ya Serikali. Kwa mfano, katika mji ule suala la miundombinu ya barabara haieleweki, barabara kuu ni moja tu kwa sababu nyumba zimejengwa kiholela. Kwa hiyo, naomba Wizara hii iweze kutupia jicho pale Tunduma, wahakikishe eneo lile linapimwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JULIANA D. SHOZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kuishukuru Serikali kwa kukubali ombi la kupandisha hadhi Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na hatimaye kuwa na hadhi ya Hospitali ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri machache. Hospitali hii inapandishwa hadhi ikiwa na changamoto nyingi. Idadi ya Manesi na Madaktari ni ndogo mno ukilinganisha na mahitaji yaliyopo, ukizingatia kuwa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi inahudumia Wilaya ya Momba, pia kutokana na kwamba Wilaya ya Momba mpaka sasa hakuna Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hiyo ya kuwepo kwa uhaba wa Madaktari inapelekea Madaktari kufanya kazi kwa muda wa ziada huku ulipwaji wa on call allowance wakicheleweshewa kupatiwa hivyo kupunguza ufanisi. Naomba Serikali katika ajira mpya zinazotarajiwa kutolewa, basi na Hospitali ya Wilaya ya Mbozi iliyopandishwa hadhi iongezewe Madaktari, kwani mpaka sasa kuna MD watano tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, changamoto ya dawa bado ni kubwa pamoja na jitihada za Serikali ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 fedha za dawa zilizokuwa zimetengewa ni Sh. 143,937,133/= na zilizopelekwa mpaka Aprili, 2017 ni sh. 165,144,778/=. Hivyo Serikali ilivuka malengo, tunaishukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya dawa katika mwaka huu 2017/2018 ambapo tayari hospitali hii imepandishwa hadhi ni Sh. 173,938,158/=. Ongezeko hili ni dogo ukizingatia kuwa tayari hospitali hii imepandishwa hadhi na kuwa ya Mkoa. Hivyo, naomba bajeti ya dawa iongezwe pia MSD wahakikishe wanaleta dawa kulingana na bajeti ya fedha waliyopewa ili kupunguza tatizo la uhaba wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Hospitali ya Wilaya ya Mbozi imepewa hadhi ya Mkoa, lakini katika Bajeti ya mwaka huu sijaona mahali popote kuhusu mchakato wa ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Songwe. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha Bajeti yake, aniambie ni lini mchakato wa ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Songwe utakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu kuwa ni lini Wilaya ya Momba ambayo iko mpakani mwa Tanzania na Zambia itapatiwa Hospitali ya Wilaya, ukizingatia kuwa Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni yake Mjini Tunduma, 2015 aliahidi kutupatia majengo yaliyoachwa na Wakandarasi kuwa Hospitali ya Wilaya? Ni lini ahadi hiyo itatekelezwa ili wanawake na wananchi wa Wilaya ya Momba wapate haki yao ya kupata huduma hiyo muhimu ya kiafya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naomba kufahamu, ni lini Serikali itafikiria kuwa wagonjwa wa kisukari nao wapatiwe kadi bure kama ilivyo katika wagonjwa wa UKIMWI? Pia Serikali ijitahidi dawa za wagonjwa wa kisukari ziwe zinapatikana kwa wingi katika hospitali zetu ili kuwapunguzia mizigo wagonjwa wa kisukari kwa kununua katika maduka binafsi ambapo zinauzwa ghali.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote na mimi nishukuru kwa kuweza kupata nafasi hii. Vilevile nichukue nafasi hii kuweza kuzungumzia hii hali ambayo inaendelea humu Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwanza kwa kukutoa hofu kwa sababu kwa sisi ambao tunasoma Biblia, ukifuatilia kitabu kile cha Mathayo utakuta kuna historia ya Mfalme Herode, tabia ya Mfalme Herode inafanana kabisa na tabia wanayoifanya viongozi wa CHADEMA ndani ya Bunge lako Tukufu. Mfalme Herode alikuwa na tabia ya wivu. Kilichomsababisha Mfalme Herode akatangaza kwamba watoto wote wa kiume wauwawe ni wivu aliokuwa nao kwa sababu alipoiona ile nyota ya mashariki akaona kabisa kwamba nyota hii ni ishara Mfalme anakwenda kuzaliwa kwa hiyo ataenda kuchukua nafasi yake. Naomba nikutoe hofu kwamba nyota yako ndani ya Bunge hili imeng‟ara sana na ndiyo inayowatisha Wapinzani kiasi kwamba wanabaki wanahangaikahangaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tukumbuke na nichukue nafasi hii kuweza kuwakumbusha Wapinzani kwamba pamoja na mbinu zote ambazo Herode alizifanya kumuangamiza Yesu mpaka leo hii Yesu ndiyo Mfalme wa dunia, ukitaja Wafalme wa Dunia wako wawili, ni Yesu pamoja na Mtume Muhammad, hakuna cha Herode wala cha nini. Kwa hiyo, watoke ndani ya Bunge au wasitoke bado Naibu Spika utabaki kuwa Naibu Spika na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tunakutakia kila la kheri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa historia inaonesha kwamba Herode alianza kufa kabla ya Yesu pamoja na mbinu zake zote, kwa hiyo ni wazi kwamba sasa hivi CHADEMA kinaenda kufa na kinaenda kutoka miongoni mwa vyama Tanzania kwa sababu mambo wanayoyafanya katika Bunge hili siyo mambo waliyotumwa na wananchi wa Majimbo yao. Kwa hiyo, naomba nikutoe hofu, wewe ni kiongozi makini na sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuko pamoja na wewe kama ambavyo jina lako ni Dkt. Tulia tunaokuomba utulie. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba moja kwa moja nianze kwa kuunga mkono hoja ya bajeti ya Wizara ya Fedha. Nichukue nafasi hii kuipongeza Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa sababu imefanya kazi kubwa sana. Niiombe Serikali iweze kuzingatia maoni ya Kamati ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Ghasia kwa sababu maoni waliyoyatoa ni mazuri na yakifanyiwa kazi yataleta tija na kuongeza mwamko katika Serikali hii ya Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia moja kwa moja Wizara ya Afya ambayo imetengewa kiasi cha fedha cha shilingi trilioni 1.99, vipaumbele vyake vikiwa ni kununua dawa, vifaa tiba pamoja na kulipia deni la MSD. Tunatambua kwamba ni jambo zuri kulipa deni la MSD na najua zahanati zangu kule Mkoani Songwe sasa zitaenda kuwa na uhakika wa dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kwamba zahanati zetu nchini zina hali mbaya hususani zahanati ambazo zipo katika Mkoa wangu wa Songwe. Zahanati zangu zina hali mbaya sana na Sera ya Wizara ya Afya inasema kwamba kutakuwa na zahanati kwa kila kijiji na kutakuwa na kituo cha afya kwa kila kata lakini mpaka leo hii ambapo tumesimama kujadili bajeti hii ni wazi kwamba hatujafikia hata nusu ya malengo ambayo tulikuwa tumejiwekea. Mfano, nikienda katika Mkoa wangu wa Songwe katika Wilaya ya Ileje ina zahanati 23 tu zote zinakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji, wanatumia maji ambayo siyo safi na salama, matatizo ya umeme pamoja na ukosefu wa watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Tarafa ya Bulambya katika Zahanati ya Chabu pamoja na Izuba, zinatumia maji machafu yanayotoka katika Mto Songwe na ukiangalia maji yale yalishapimwa yakaonekana kwamba yana vijidudu asilimia 18, kwa hiyo hayafai kwa matumzi ya binadamu. Kama hiyo haitoshi, nikienda katika Wilaya yangu ya Mbozi ina zahanati 99, zahanati ambazo zinafanya kazi mpaka sasa hivi ni 62 tu na zote matatizo yake yanafanana. Hakuna umeme, maji, wahudumu na waganga wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, katika zahanati ambayo ipo katika kijiji cha Wasa mpaka leo hii ina Mganga mmoja tu. Ukienda katika Zahanati ya Ipunga ina Mganga mmoja tu kiasi kwamba siku Mganga akipata shida zahanati zile zinafungwa. Unaweza kuona kwamba tunaweka rehani maisha ya mama mjamzito na watoto. Kwa hali hii, inaashiria kwamba bado afya ya mama mjamzito na mtoto iko hatarini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, katika Wilaya ya Mbozi kuna Kata ya Itaka, kuna mfadhili alishatoa vifaa vya maabara vikiwepo vifaa vya kupimia CD4 lakini kwa sababu mpaka leo hii hakuna umeme, vile vifaa vimebaki kama mapambo. Ndiyo maana sisi kama Wabunge wanawake tunahitaji commitment ya moja kwa moja ya Serikali yetu katika kuzihudumia zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukienda Wilaya ya Momba mpaka sasa hivi ina zahanati 27 tu na vituo vya afya vitatu. Hili jambo nimekuwa nikilipigia kelele katika Bunge hili kwamba Wilaya ya Momba hata Hospitali ya Wilaya hakuna, hivyo vituo ambavyo viko 27 bado havitoshi na ukizingatia havina mahitaji muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba commitment ya Serikali katika kuhakikisha kwamba inaweka mkono wake na siyo kuziachia tu Halmashauri zetu. Tunataka commitment ya moja kwa moja ya Serikali katika kuzihudumia zahanati zetu. Sote tunatambua vifo vya akina mama na watoto vinatokea kule chini katika zahanati lakini siyo katika Hospitali za Mikoa au Wilaya. Hivyo, kama tumejipanga kuhakikisha kwamba tunakomesha vifo vya watoto na akina mama, niishauri Serikali isiziangalie tu Hospitali za Wilaya na Mikoa, tutupie jicho chini katika zahanati zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwa umakini sana bajeti ya Serikali Kuu. Bajeti hiyo haijatenga bajeti ya moja kwa moja kuzihudumia zahanati zetu. Ndiyo maana ukisoma kuna kiwango cha fedha ambacho kimetengwa katika bajeti ya TAMISEMI shilingi bilioni 32, hizo ni fedha ambazo zinatoka katika own source kwa maana ni fedha ambazo zimetengwa na Halmashauri zetu na fedha hizi siyo za uhakika, kwa sababu ni fedha ambazo inategemeana na makusanyo ambayo Halmashauri zetu zitakuwa zimekusanya. Nimesoma hiyo bajeti ya TAMISEMI kuna Kituo cha Afya cha Tunduma ambapo kuna ukarabati ya wodi ya wazazi, kujenga sehemu ya kujisubirishia akina mama wajawazito pamoja na jengo la upasuaji na chumba cha kujifungulia katika Zahanati ya Katete na Chiwezi, zote zimetengewa kiasi cha shilingi milioni 128 lakini ukiangalia source ni kwenye local governments, UNICEF na vyanzo vya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo hivi siyo vyanzo vya kuaminika. Ndiyo maana sisi kama Wabunge wanawake tunaotoka katika mikoa ambayo ina shida ya huduma za kiafya, tunaomba commitment ya Serikali kwamba sasa iweze kuzingatia ushauri ambao umetolewa na Kamati ya Bajeti. Ushauri ule ni mzuri kwamba iongezwe Sh.50 kwenye kila lita ya mafuta ya petrol na diesel ili kwa mwaka tuweze kukusanya shilingi bilioni 250 ambapo shilingi bilioni 220 zikatumike katika kuhakikisha kwamba tunasambaza maji katika mikoa yetu na shilingi bilioni 30 zipelekwe kumalizia zahanati zetu na kuzifanyia ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika Kamati yangu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama nikiwa Mjumbe wa Kamati hiyo. Nianze moja kwa moja kuzungumzia namna ambavyo bajeti inaathiri utendaji katika Wizara hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Taarifa ya Kamati imejieleza, kwa muda mrefu sana Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imekuwa ikishindwa kutekeleza majukumu yake kulingana na bajeti ambayo imekuwa ikitengwa, haifiki kwa wakati na hata ile ambayo ni ndogo ambayo imekuwa ikitengwa kwa ajili ya Kamati hiyo imekuwa haitoshelezi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo ripoti imesema ukienda kuangalia Balozi zetu zina hali mbaya. Balozi zetu katika nchi za nje kwa kweli zimechakaa, fedha za matengenezo hakuna. Kama haitoshi, inafika mahali kama Kamati tunaona kwamba sasa lile lengo la kuwa na hizi Balozi nje haina maana. Kwa sababu lengo mojawapo la kuwa na Balozi katika nchi za nje ni kuhakikisha kwamba tunakuza diplomasia ya kiuchumi, lakini ukiangalia uhalisia huo kwa sasa haupo, Balozi zetu zinashindwa kufanya kazi kutokana na kwamba fedha za maendeleo zimekuwa hazipelekwi. Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watumishi ambao wanafanya kazi katika Balozi hizo wamekuwa ni watu wa kupewa mishahara, lakini wanashindwa kutekeleza yale majukumu yao ya kimsingi kutokana na kwamba fedha zimekuwa haziendi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri juu ya hilo kwamba ni vema sasa kama Wizara, ikaangalia utaratibu hizi fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya Wizara hiyo zikaenda moja kwa moja kwenye Balozi kama ambavyo fedha za maendeleo zimekuwa zikienda katika Halmashauri zetu. Kwa kufanya hivyo naamini kwamba itarahisisha utendaji kazi wa hizo Balozi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, hata shughuli za Kamati katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 kwa kiasi fulani Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama tumeshindwa kutekeleza majukumu yetu kama ambavyo tunapaswa kutekeleza, hususan kwa suala la mambo ya nje. Sisi kama Wajumbe wa hii Kamati tunavyozungumzia kwenda kutekeleza majukumu yetu, mojawapo ni kwenda kutembelea hizi Balozi kuangalia kama zinatekeleza majukumu yao ya kukuza diplomasia ya kiuchumi. Ni wazi kwamba kama Kamati haijawezeshwa kutekeleza jukumu hilo, sasa inafika mahali sisi Wajumbe tunakuja kuchangia hapa Bungeni kwa vitu ambavyo tumeletewa ripoti ya kwenye makaratasi, kitu ambacho sio kizuri. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kushauri katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2017/2018 nashauri kwamba Wizara iweze kuangalia utaratibu mpya kwamba fedha ambazo zinatengwa ziende kama zilivyopangwa na siyo kama ambavyo imetokea katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Wizara imetengewa bilioni nane lakini imeenda bilioni tatu. Haijafika hata nusu yay ale malengo ambayo, kama Wizara ilikuwa imejiwekea. Vilevile hata vyama vya kibunge; kuna vyama kwa mfano PAP, ilikuja kwenye Kamati yetu lakini wakasema sisi hatuna kitu cha kuwasilisha kwa sababu hatujaenda popote. Ninaomba sana suala hili la bajeti liweze kuzingatiwa. Kwa kufanya hivyo tutaongeza ufanisi katika Bunge kama muhimili. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba pia nizungumzie suala lingine kama Kamati tuliweza kutembelea magereza mbalimbali. Tumetembelea Gereza la Songwe, gereza ambalo linajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na wamekuwa wakifanya hivyo na kuweza kulisha magereza mengine. Tatizo kubwa ni kwamba wamekuwa hawalipwi fedha zao kwa wakati na hiyo inasababisha kuwavunja moyo na inawaondolea ile hali ya kuendelea kuzalisha zaidi. Nashauri Wizara iangalie katika bajeti ijayo basi waweze kuzingatia yale madeni ambayo gereza linakuwa linaidai Serikali yaweze kwenda kulipwa kwa wakati kama ilivyo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala la polisi. Siku zote polisi wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, lakini niipongeze Serikali kwa sababu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kutoa mapendekezo yangu kuhusu Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji. Ni ukweli usiopingika kuwa suala la maji bado ni changamoto hususan kwa Watanzania waishio vijijini. Hivyo ni lazima kama Serikali kuja na mipango kabambe inayotekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha kwamba Bajeti ya Maji ambayo imekuwa ikitengwa haitoshelezi kulingana na mahitaji halisi ya Watanzania lakini tatizo kubwa ni kuwa fedha hiyo huwa haitolewi yote kama inayoidhinishwa na kupitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kupitia Wizara ihakikishe kuwa fedha inatolewa kama iliyoidhinishwa na hii kwa sababu maji ni uhai na kwamba bila maji hakuna maisha. Ni vyema Serikali ikabuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo ni vyanzo vya ndani na ambavyo ni vya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo naungana na maombi na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wengi juu kuongeza tozo ya sh.50/= na kuwa sh.100/= kwenye kila lita moja ya mafuta ya diesel na petrol ili kuwezesha miradi mbalimbali ya maji kuweza kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuonesha kuwa Serikali iko committed katika kumaliza tatizo la maji hususan vijijini ambako ndiko hasa changamoto ya maji iko kubwa, nashauri katika hayo makusanyo yatakayopatikana baada ya kuongeza tozo ya sh.50/= ni vyema asilimia 70 ya fedha hiyo ikaenda vijijini na asilimia 30 ikaenda mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri kuwa ile sera ya uvunaji maji ni vyema Serikali sasa ikalitilia mkazo na kuhakikisha kwamba kila Halmashauri inatoa maelekezo ya kuhakikisha wananchi wetu wanapojenga nyumba wakumbuke kuweka system ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niombe itakapoongezwa tozo ya sh.50/= Wizara iangalie pia Mkoa wa Songwe ambao ni mpya na unakabiliwa na upungufu wa maji hususan kwa vijijini. Wanawake wanapata shida sana, mfano Wilaya ya Mbozi, Kata ya Vwawa na Mlowo, shida ya maji ni kubwa mno. Mheshimiwa Waziri wa Maji alituahidi kutuletea mradi mkubwa wa maji lakini mpaka sasa hatujui mpango huo umefikia wapi. Pia, naomba watukumbuke kutuletea mradi wa maji katika Mji Mdogo wa Tunduma, lakini pia Wilaya ya Ileje na Wilaya ya Songwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii ya TAMISEMI. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanafanya kwenye Taifa letu. Niseme kwamba walikuja kwenye Mkoa wangu wa Songwe na hakika wameacha alama ambayo
haiwezi kufutika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, moja kwa moja naomba nielekeza mchango wangu katika kuchangia masuala ya elimu. Nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais wake Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuweza
kusimamia vizuri Sheria ya Haki ya Mtoto ya mwaka 2009 inayohusu haki ya mtoto kupata elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake yamekuwa ni makubwa kwa sababu tumeshuhudia kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi idadi ya wanafunzi ambao wameandikishwa darasa la kwanza mpaka kidato cha nne imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Ukisoma hotuba
ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amesema kwamba katika mwaka huu 2017 zaidi ya wanafunzi 300,000 wamedahiliwa ukilinganisha na idadi ya wanafunzi ambayo walidahiliwa kwa mwaka jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba haya ni mafanikio makubwa sana kwa Serikali hii kwa sababu unaweza kujiuliza kwamba endapo hawa watoto wasingepata hiyo haki yao ya msingi ya kupata elimu bure wangekuwa wapi. Sera hii imesaidia sana kwani vilevile imepunguza matabaka katika jamii yetu kwamba kwa sasa hivi mzazi ambaye hana uwezo na mwenye uwezo watoto wao wanakuwa na haki ya kupata elimu, lakini vilevile imepunguza mimba za utotoni hususani kwa mabinti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi huwa nashangaa sana napoona Mbunge katika Bunge hili anasimama na kuponda Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba imeshindwa kusimamia elimu bure. Hilo jambo si kweli na uzuri ukiangalia hao watu ambao kila siku wamekuwa ni watu wa kuponda wao wenyewe mpaka leo hii wameshindwa kujenga jengo moja la makao makuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la kusitisha sana, kama umeshindwa kujenga Ofisi ya Makao Makuu utaweza kutoa elimu bure? Ni kitu ambacho hakiwezekani. Kwa hiyo, niseme kwamba Wabunge tujifunze kusimamia ukweli na tujifunze kusifia pale ambapo Serikali inafanya vizuri. Vilevile tujifunze kushukuru hata kwa kidogo ambacho Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ikifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi mimi kama Mbunge nilitegemea mtu anapokuja kuponda Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuona hata kwenye zile Halmashauri ambazo wao wanaziongoza wangefanya vizuri, lakini matokeo yake sioni jipya lolote kwenye hizo Halmashauri. Hata ukiangalia kwenye suala la madawati, wamesubiri mpaka Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefikiria namna gani ya kuweza kuhakikisha kwamba wanafunzi wa nchi hii wanapata madawati. Ni vema Watanzania wakaelewa kwamba hizi ni porojo tu ambazo
tumeshazizoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya naomba nielekeze mchango wangu kwa masuala mbalimbali ya elimu na wote tunafahamu kwamba kinachosababisha mwanafunzi akafeli ni mazingira magumu ya mwalimu na wala sio mazingira magumu ya mwanafunzi.
Nasema hivyo kwa sababu kama mwalimu akirekebishiwa mazingira yake na akipewa motisha ya kutosha mwanafunzi hata kama anatoka kwenye mazingira magumu lakini akikutana na mwalimu ambaye ameandaliwa vizuri ni rahisi sana kwa mwanafunzi huyo kufanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo limejidhihirisha hata katika hotuba hii ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ukurasa wa 31 ambapo amezunguzia motisha kwa Walimu Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata. Hotuba hii imesema kwamba katika mwaka wa fedha 2016 kuanzia Julai mpaka Machi, 2017, Serikali imeanza kupeleka fedha kwa ajili ya kutoa motisha kwa Walimu Wakuu wa Shule. Mpaka sasa
Serikali imepeleka shilingi bilioni 25.7 kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi lakini imepeleka shilingi bilioni 7.20 kwa ajili ya walimu wa sekondari lakini imepeleka shilingi bilioni 7.79 kwa ajili ya Waratibu wa Elimu Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba huu ni mwanzo mzuri wa kuhakikisha kwamba tunaboresha viwango vyetu vya elimu. Hata hivyo, kwa utaratibu huo, ni kwamba sasa kila Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari anapata kiasi cha shilingi 250,000 kwa kila mwezi lakini vilevile Mratibu pia anapata shikingi 250,000 na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi anapata motisha ya shilingi 200,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mafanikio makubwa, lakini nataka kushauri machache. Nimejaribu kusoma sana hiyo hotuba ya TAMISEMI lakini sijaona mahali ambapo Serikali imezungumzia kuwapa motisha wale walimu ambao ni wa hali ya chini, walimu ambao ni wa kawaida.
Sote tunafahamu kwamba unapozungumzia Idara ya Mwalimu Mkuu, Mwalimu Mkuu ni taasisi. Unapozungumzia Mwalimu Mkuu, unazungumzia mwalimu wa taaluma, mwalimu wa nidhamu, mwalimu wa michezo pamoja na mambo mengine. Serikali kupeleka fedha hizi moja kwa moja kwa Mwalimu Mkuu peke yake, mimi kama Mbunge limenipa shida kidogo. Ni vema Serikali ikaangalia namna nzuri
ambayo inaweza kuhakikisha kwamba hata wale walimu wengine wa masomo ya kawaida wanapata hii motisha ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunatambua kwamba Walimu Wakuu hawa ndiyo ambao hata semina mbalimbali ambazo huwa zinafanyika zinawalenga wao moja kwa moja.
Waratibu wa shule, semina hizi zinawalenga moja kwa moja.Hata ukija kwenye masuala ya nyumba za walimu, wanufaika wa kwanza ni hao Walimu Wakuu wa Shule, lakini wale walimu ambao wanafundisha masomo ya kawaida, walimu ambao kimsingi wao ndiyo wanabeba jukumu kubwa la kuhakikisha wanaboresha mifumo ya elimu, ndiyo wanaohangaika na wanafunzi asubuhi mpaka jioni, naona kama Serikali imewasahau kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ushauri wangu kwa Serikali kwamba iweze kuangalia suala hili.
Afadhali hii fedha ikapelekwa katika shughuli za uendeshaji wa ofisi. Kwa kupeleka fedha hiyo kwenye uendeshaji walimu wote wataweza kunufaika. Vilevile tunatambua kwamba walimu wana changamoto ambazo zinafanana, fedha hii ikipelekwa katika shughuli za ofisi naamini kwamba walimu wote pamoja na Walimu Wakuu wataweza kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ulikuwa ni huo, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Simbachawene atakapokuja kutoa maelezo aniambie ni kitu gani ambacho wao wamekitumia
katika kuona kwamba motisha hii ipelekwe kwa Walimu Wakuu wa shule peke yao.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami kuweza kuchangia Wizara hii ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. (Makofi)

Awali ya yote nichukue nafasi hii kuweza kumpongeza Waziri wa Wizara hii, kwa kweli anafanya kazi nzuri na kazi yake siyo ya kubeza hata kidogo anastahili pongezi pamoja na Naibu Waziri wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nijikite sasa katika kuelezea Idara ya Maendeleo ya Jamii. Naomba nielezee kwanza historia, Idara hii ya Maendeleo ya Jamii ni zao la kihistoria la mapinduzi ya viwanda yaliyofanyika katika karne ya 19 katika Bara la Ulaya. Walipojenga viwanda yalijitokeza matatizo mengi ya kijamii hivyo wakaanzisha masomo ambayo yatazalisha wataalam ambao watashughulika na masuala ya mabadiliko katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu nchi za Afrika ikiwemo Tanzania haikufanya makosa kuchukua funzo hili na hatimae kujenga na kuanzisha Vyuo Vikuu vya Maendeleo ya Jamii, pamoja na vyuo vya kati ambavyo moja kwa moja vita-deal na mabadiliko ya kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 87 ameelezea kabisa kwamba vyuo hivyo vitaendelea na udahili wa wanafunzi watakaojishughulisha na masuala ya maendeleo ya jamii, ni vema tukaangalia kwamba tunapoendelea kudahili wanafunzi katika vyuo vya maendeleo ya jamii tuangalie na wale ambao kwa sasa hivi wapo maofisini, hawa Maafisa wa Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mantiki hiyo, ni wazi kwamba kwa sasa hivi ambapo nchi yetu inapiga hatua kuelekea kwenye uchumi wa viwanda hakuna namna yoyote ambayo tunaweza tukaiacha nyuma Idara hii ya Maendeleo ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha sana idara hii kwa kifupi imesahaulika. Mwaka jana wakati nachangia Wizara ya Afya, nilizungumzia Idara ya Maendeleo ya Jamii, lakini ni wazi kwamba sijaona mabadiliko yoyote ambayo yamefanyika. Leo hii ukitembea katika Halmashauri zetu nyingi, siyo katika Mkoa wa Songwe tu nchi nzima Idara hizi za Maendeleo ya Jamii ziko hoi. Watumishi wa idara hii ya maendeleo ya jamii hawapelekewi fedha za oc, wala hakuna vitendeakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Halmashauri nyingine unakuta idara ya maendeleo imewekwa nyuma ya Halmashauri, nyingine ziko nje kabisa ya Halmashauri kuonesha kwamba siyo part ya Halmashauri zetu. Suala hili linasikitisha sana. Hali hiyo imepelekea sasa hata fedha ambazo zinapelekwa fedha za miradi, miradi mingi katika Halmashauri zetu inakufa haizai matunda, haioneshi mafanikio kwa sababu tumeiacha nyuma idara ya maendeleo ya jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitolea mfano katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Mbozi, kuna miradi mizuri sana ambayo imeanzishwa na Serikali, lakini kwa sababu wananchi hawajashirikishwa, watu wa idara ya maendeleo ya jamii hawajashirikishwa, inapelekea wananchi sasa hawana ile sense of ownership, wanaona kwamba ile miradi siyo ya kwao, wanaona miradi ile ni ya Serikali, kumbe tatizo hawajaelimishwa kuona kwamba ile miradi ina faida hivyo wanapaswa kuitunza, hii yote ni sababu Idara ya Maendeleo ya Jamii imesahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi utaratibu uliowekwa na Serikali wa kutenga asilimia tano ya vijana pamoja na asilimia tano ya wanawake, lengo lilikuwa ni zuri lakini ukiangalia katika Halmashauri idara inayohusika moja kwa moja kufuatilia pesa hizi ni idara ya maendeleo ya jamii lakini hawashirikishwi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda leo hii katika Halmashauri zetu hususan Halmashauri ambazo zipo katika Mkoa wangu wa Songwe, wanawake hawana kabisa uelewa wa asilimia tano ambayo inatengwa na Halmashauri. Ukienda kwenye makaratasi unaona kabisa kwamba fedha zinatengwa lakini impact kwenye jamii haionekani, swali ukijiuliza ni kwa sababu Idara hii ya Maendeleo ya Jamii ambayo ndiyo inategemewa kwenda kutoa mafunzo kwa vijana pamoja na wanawake wajue namna gani ya kuweza kuzitumia hizo fedha za Halmashauri, wajue namna gani ya kuweza kuzifuatilia fedha hizo ili ziweze kutumika kama ilivyopangwa. Kwa sababu idara hii haishirikishwi, unaona kabisa kwamba fedha hizo hazijulikani zinaenda wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Wabunge wa Viti Maalum siyo Wajumbe wa Kamati ya Fedha, kwa hiyo unaweza ukaona ni namna gani ambavyo hizi asilimia tano za wanawake na asilimia tano za vijana zinapotea katika mazingira ambayo ni ya kutatanisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la bima ya afya. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumzia kwamba bado mwamko ni mdogo sana wananchi kuweza kujiunga na hii mifuko ya hifadhi ya hifadhi ya jamii, mifuko ambayo ingeweza kuwasaidia pia wanawake ambao wako vijijini, ambao kimsingi wao ndiyo wana matatizo makubwa sana ya kiafya, wanapata matatizo makubwa sana wanapoenda kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaojiunga na hii mifuko ukiangalia idadi ni ndogo kwa sababu wanachi bado hawajaelimishwa, elimu bado haijawafikia kwa hiyo hawaelewi umuhimu wa kujiunga na hii mifuko ya bima ya afya. Hii yote ni kwa sababu tumepuuza Idara hii ya Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukiangalia hata katika jamii zetu, masuala ya unyanyasaji wa kijinsia ya wanawake na watoto yamekua kwa kasi kubwa sana. Dada yangu hapa ameongea kwa uchungu, ni masuala ambayo hata katika Mkoa wangu wa Songwe yapo kwa kiasi kikubwa, watoto wadogo wanaozeshwa, hivi ninavyosema nina mtoto ambaye namsomesha sekondari kwa sababu tu mzazi wake alikwishakupokea ng’ombe 60 ili amuozeshe huyo mtoto. Masuala kama haya tunapaswa kama Taifa kuyapinga… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pia kwa kunipa nafasi niweze kuchangia machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua nafasi hii kuwapongeza Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya, lakini vilevile nawapongeza kwa dhati Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada kubwa ambazo imezifanya katika kukuza diplomasia ya kiuchumi na hatimaye kufanikisha kufungua Balozi sita ambazo ni Balozi mahususi kwa ajili ya kukuza biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja; nimeshangazwa sana na uchangiaji wa baadhi ya Wabunge humu ndani. Walipinga ndani ya Bunge hili wakisema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi Rais wake ni dhaifu. Leo hii tumempata Rais ambaye ni mchapakazi, tumempata Rais ambaye anasimamia maslahi ya umma, maslahi ya Watanzania masikini, wamegeuka na kusema kwamba anafanya maamuzi ambayo ni ya hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwanza nichukue nafasi kuweza kuwakumbusha, wanasema ukiwa mwongo usiwe msahaulifu. Ni wewe mwenyewe kaka yangu Mheshimiwa Lissu ulisimama na kusema kwamba CCM imempa fomu ya kugombea Urais fisadi Lowassa, lakini ni wewe mwenyewe ambaye ulizunguka kumnadi Lowassa katika nchi hii. Sasa naomba niulize swali, je, kuna maamuzi ya hovyo kama hayo kusema mtu ni fisadi na baadaye mzunguke kuanza kumnadi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Lema alisema kwamba ni heshima kwa Mungu kumzomea na kumpiga mawe mtu kama Lowassa, lakini wewe ndio ulizunguka nchi nzima kumnadi. Jamani mnapoongea maneno, msiwe wepesi kusahau. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niseme jambo moja, hawa watu wameshazoea sana kila kitu kinachofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi wamekuwa wakikipinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kitu ambacho Serikali hii inafanya wao wamekuwa ni wapondaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijashangaa kuona hawa wenzetu wawili wanaponda jitihada za Mheshimiwa Rais Magufuli, kwa sababu hawa kila kitu kinachofanywa wao wamekuwa ni wapondaji; wamejipa vyeo vya kuwa mtoto wa kambo kwamba kila kitu lazima wao walalamike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inahitaji Rais kama Magufuli. Hata kama, hatuwezi kuona kwamba tunakuza diplomasia ya kiuchumi wakati tunaendelea kuibiwa. Kwa hiyo, huu utaratibu wa kuendelea kutetea wezi, tumeshauzoea, ninyi wenzetu kazi yenu kutetea wezi na ndiyo maana mko tayari kwamba Taifa hili liendelee kuibiwa dhahabu eti kwa sababu tu tunakuza diplomasia ya kiuchumi. Hilo jambo haliwezi kukubalika na tunaomba tumpe nafasi kama Rais aweze kutimiza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwamba mngekuja kushauri, lakini ninyi mmekuwa watu wa kulalamika. Kwa hiyo, napenda kusema kwamba Mheshimiwa Rais aendelee kuchapa kazi, huu ni wakati wetu wa sisi kuchapa kazi na hawa wenzetu waliojipa vyeo vya watoto wa kambo tuwaache waendelee kulalamika, hapa kazi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa niweze kuzungumzia suala la uhaba wa Maafisa katika Balozi zetu. Balozi zetu zinakabiliwa na uhaba mkubwa sana wa Maafisa… (Kicheko/Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Mpango. Vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Mpango kwa hotuba nzuri ambayo ameiwasilisha hususani kwa kuweza kugusia vipengele muhimu, kuainisha vipengele ambavyo ni vya kipaumbele kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimevutiwa sana na kipengele cha kuainisha kwamba moja ya vipengele vya msingi ni Mchuchuma pamoja na Liganga. Hii itakuwa ni mkombozi lakini nimwombe sana Mheshimiwa Mpango aweze kuangalia anavyoenda kushughulikia hivi vipengele vya msingi aangalie sana kwa yale maeneo ambayo yanazalisha makaa ya mawe (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia kwa Mkoa wangu wa Songwe, katika Wilaya ya Ileje kuna makaa ya mawe, vilevile ukienda kwenye Wilaya ya Mbozi Magamba kuna makaa ya mawe. Nichukue nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Mpango aviunganishe pamoja haya maeneo katika mpango huu mkubwa wa mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuweza kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa Taifa letu. Sote ni mashahidi tumeshuhudia namna ambavyo Rais anapambana kuhakikisha kwamba anasimamia rasilimali za Mtanzania likiwepo suala la madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashangaa sana watu ambao wanaibuka katika Bunge hili kuponda jitihada kubwa ambazo Mheshimiwa Rais anazifanya. Jana nimemsikiliza kwa umakini sana Mheshimiwa Msigwa, ameuliza kwamba eti Mheshimiwa Pombe Magufuli alikuwa wapi miaka yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kama ambavyo Watanzania huko nje sasa hivi wameungana na Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba wanamtia moyo katika vita hii kubwa ambayo ameianzisha, nilijua kabisa kwamba hata humu ndani Bungeni tutaungana wote kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunamtia moyo Mheshimiwa Rais, lakini wenzetu wanauliza kwamba alikuwa wapi. Sasa kwa sababu yeye ameamua kufukua makaburi na mimi naomba nimsaidie kufukua makaburi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya huko nyuma, ukifuatilia historia ya nchi hii, wakati Mwalimu Nyerere akiwa Rais, Mzee wangu Ndugu Mtei alikuwa ni Waziri wa Fedha na hilo wenzangu wanalijua vizuri sana na tutakumbuka kwamba ni Ndugu Mtei huyu ambaye alimshawishi Mwalimu Nyerere kwamba akubaliane na masharti magumu ambayo walitupa mabeberu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sharti mojawapo ikiwa ni kwamba kuweza kushusha thamani ya fedha yetu, lakini Mheshimiwa Nyerere alikataa na alipokataa tunaona kabisa Mzee wangu Mtei alijiuzulu na akahama nchi akaenda kufanya kazi World Bank kwa wale wale mabeberu ambao alikuwa anawatetea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo siyo jambo jipya kushuhudia hawa wenzetu wakiendelea kutetea mabeberu ndani ya Bunge hili, kwa sababu hata Muasisi wao ni kitu ambacho alishakianzisha tangia huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi wanavyouliza kwamba Mheshimiwa Magufuli alikuwa wapi? Wakati Mwinyi akiwa Rais Mheshimiwa Lowassa pamoja na Mheshimiwa Sumaye walikuwa ni Mawaziri, kweli siyo kweli? Sasa na kipindi hicho Magufuli hakuwa Waziri. Sasa unapouliza Mheshimiwa Magufuli alikuwa wapi, naomba waanze kuwauliza ambao wanao huko Mheshimiwa Lowassa pamoja na Mheshimiwa Sumaye walikuwa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, Mheshimiwa Mkapa akiwa Rais wa nchi hii Sumaye alipanda cheo akawa Waziri Mkuu kwa maana ndiye Kiongozi wa shughuli zote za Serikali ikiwemo suala la mikataba ya madini. Sasa leo hii wanauliza kwamba eti Magufuli alikuwa wapi, kaka yangu Msigwa amenisikitisha sana. Hata kwenye Serikali ya Jakaya Mtendaji Mkuu wa Serikali Mkuu wa Serikali alikuwa ni Mheshimiwa Lowassa na mikataba yote ambayo ilikuwa ikisainiwa katika Bunge hili yeye alikuwa anahusika na sote tunafahamu alishirikiana na Karamagi kwenda nje wakaenda wakasaini mkataba ambao leo hii umeliingiza Taifa letu katika matatizo makubwa. Sasa mtu anapohoji kwamba eti Magufuli alikuwa wapi, naomba kabisa kwamba aanze kumuuliza Mheshimiwa Lowassa pamoja na Mheshimiwa Sumaye walikuwa wapi? Kwa sababu wao kipindi hicho ndio walikuwa Watendaji Wakuu wa shughuli zote za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja, inapokuja vita kama hii ni vizuri kama Taifa tukaungana wote kwa pamoja kumsemea na kumshauri Rais wetu. Kaka yangu Mheshimiwa Lissu unapoanza kutaja watu kwamba Mheshimiwa Jakaya alihusika kusaini, unasahau kabisa kwamba Jakaya akiwa Waziri wa Maji Sumaye alikuwa Waziri Mkuu. Sasa nashangaa jana umemtaja Jakaya lakini Sumaye vipi ulimsahau? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inaonesha kabisa kwamba hawa watu ni watu ambao wanafanya vitu kwa double standard, ni watu ambao hawajielewi na sasa hivi Magufuli amewashika pabaya, walizoea kufanya siasa za matukio, siasa za matukio sasa hivi hamna. Walizoea mtoke humu Bungeni wakafanye maandamano, sasa hivi wananchi wanakipenda sana Chama cha Mapinduzi na ndio maana wanavyoona Rais anafanya kazi nzuri wanageuka wanasema Rais hatekelezi Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie masuala ya madini yapo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ukisoma ukurasa wa 28 imezungumzia kwamba Serikali hii itaenda kusimamia kuhakikisha kwamba suala la madini linawanufaisha Watanzania wote wakiwepo Watanzania ambao ni maskini. Sasa mtu anapokuja kusema kwamba haipo kwenye ilani anajitahidi baada kuona kwamba Serikali yetu inafanya kazi nzuri sasa hivi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anafanya kazi nzuri, anageuka kuanza kumtenga Rais pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo rahisi kumtenga Rais wetu na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kazi anayoifanya anafanya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kumtenga Rais na Ilani ya Chama cha Mapinduzi haiwezekani ni kama kumtenga Lowasa na ufisadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nizungumzie jambo moja. Kuna suala ambalo limejadiliwa katika bajeti yetu kuhusiana na road license, wasijaribu kupotosha umma, Serikali imefuta na kuondoa kabisa tozo ya road license. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo limepunguza mzigo mkubwa sana, mzigo ambao ulikuwa ni lazima mwananchi aweze kwenda kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi hiyo tozo ambayo imeongezeka, tumshauri Waziri Mpango ahakikishe kwamba hiyo tozo Sh.40/= moja kwa moja anaipeleka katika kutatua changamoto za Mtanzania. Kwa sababu Mtanzania wa sasa anachoangalia je, hiyo Sh.40/= inaenda kufanya kazi gani? Shida hapa siyo tozo kuongezeka, shida ni kwamba hiyo tozo inayoongezeka inakwenda kufanya kazi gani? Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Mpango hiyo Sh.40 ambayo imeongezeka basi iende moja kwa moja kutatua matatizo ya Watanzania ikiwepo matatizo ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango katika Mkoa wangu wa Songwe akinamama wanapata shida kubwa sana ya maji na ni jambo ambalo nimekuwa nikilisema katika Bunge hili. Kwa hiyo, naomba sana namna pekee ya kuweza kuwapunguzia Watanzania machungu ni kuhakikisha kwamba tunatatua kero za Watanzania. Tunaomba sana hiyo pesa iende moja kwa moja kutatua kero za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kesema hayo, nashukuru na naunga mkono hoja.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nami nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu katika Bunge hili la Kumbi na Mbili, naomba niruhusu nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia wote uzima na afya njema na vile vile kwa kuniwezesha mimi mtoto wake kuweza kurejea katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee, nataka niwashukuru sana wanawake wenzangu wa Mkoa wa Songwe kwa imani yao kubwa walionionyesha, vilevile kwa kura za heshima walizonipatia na hatimaye nimeweza kurudi tena katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, sasa naomba nianze kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiitazama Hotuba ya Mheshimiwa Rais, nami nimepata muda wa kuipitia na kuisoma; ni hotuba nzito na imebeba matumaini ya Watanzania. Ni hotuba ambayo ina taswira mbili; taswira ya kwanza, ni hotuba ambayo inaeleza namna gani Serikali ya Awamu ya Tano imeshatekeleza masuala mbalimbali na kutatua changamoto mbalimbali za Watanzania. Pia ni hotuba ambayo imeeleza kwa kina sana namna gani ambavyo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amejipanga katika kipindi hiki cha pili kuhakikisha kwamba zile changamoto ambazo zilibaki kwenye awamu ya kwanza, zinaweza kumalizika katika awamu yake hii ya pili. Hotuba hii ni nzito na imebeba matumaini ya Watanzania. Ni hotuba inayotoa dira na taswira ya Tanzania tunayoitaka na namna gani ambavyo tutafikia Tanzania hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hotuba ile ni maelekezo rasmi kwa viongozi wote wa Serikali pamoja na taasisi zake, namna gani ambavyo wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ile hotuba ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa. Yapo masuala mengi sana ambapo ukifuatilia ndani ya ile hotuba yameweza kuelekezwa kwa kina zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijadili suala moja la afya kwa sababu tunatambua katika nchi yoyote, msingi wowote wa maendeleo ni afya ya watu wake. Hakuna namna ambavyo Tanzania inaweza ikapata maendeleo kama watu wake hawana afya ambayo ni stable. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika hotuba hii Mheshimiwa Rais ameeleza namna gani ambavyo miaka mitano ameshuhulikia changamoto za afya kwa Watanzania. Kwa kuwa mimi ni mwanamke, natambua namna gani ambavyo sisi wanawake tulikuwa tunapata changamoto wakati wa kujifungua lakini ndani ya miaka mitano changamoto hizo zimeweza kufanyiwa kazi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ameelekeza namna gani ambavyo kwa hii miaka mitano, kwa kupitia Sera ya Afya ambayo inasema kwamba kutakuwa na Kituo cha Afya katika kila Kata, kutakuwa na Zahanati kwenye kila Kijiji, Hospitali za Wilaya kila Wilaya, Hospitali za Mkoa kila mkoa; na hilo tumeliona limetekelezeka kwa kishindo kweli kweli. Nimesimama hapa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo amefanya katika miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma hotuba vizuri, ameeleza namna gani ambavyo ameweza kujenga Zahanati 1,198, siyo kazi ndogo. Pia amejenga Vituo vya Afya vipatavyo 900, siyo kazi ndogo. Vilevile amejenga Hospitali za Wilaya 90, amejenga Hospitali za Mikoa 10 na Hospitali za Kanda tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake ni nini? Nachotaka kuongea hususani kwenye afya ya msingi, kwa sababu tunatambua asilimia kubwa ya Watanzania huwa wanaanzia kwanza kule chini kwenye afya za msingi, kwa maana ya vituo vyetu vya afya, ukiangalia Vituo vya Afya ambavyo vimejengwa, hoja siyo kwamba vimejengwa vituo 478, hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ni kwamba vituo hivi ambavyo vimejengwa, ukiangalia maeneo mbalimbali ya nchi yetu, vimekuwa na hadhi sawa na Hospitali ya Wilaya. Ukiangalia facilities zote zinazopatikana kwenye hivi Vituo vya Afya, havitofautiani sana na Hospitali zetu za Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kwamba ni wakati muafaka sasa kuviita hivi Vituo vya Afya siyo sawa, tutakuwa hatumtendei haki Mheshimiwa Rais. Hivi vinapaswa viitwe Vituo vya Rufaa vya Kata. Kwa sababu ndivyo ambavyo vinachukua wananchi kutoka kule chini kwenye Zahanati wanakuja kutibiwa kwenye hivi Vituo vya Kata. Nataka nitoe ushauri kwa Serikali, kwa sababu tumeona kwamba vituo hivi vimejengwa vizuri, nasi pale kwetu kwenye Jimbo la Tunduma, tunacho Kituo cha Afya kimoja ambacho kimejengwa vizuri kiasi kwamba ukifika pale unashindwa kuelewa kwamba hiki ni Kituo cha Afya au ni Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vichache ambavyo nadhani kama vikifanyika kwenye hivi Vituo vyetu vya Afya vitasaidia sana kuvipa hadhi sawa na Hospitali ya Wilaya. Nataka nitoe ushauri kwa Wizara ya Afya na pia ushauri kwa Serikali kwamba ni wakati muafaka sasa waangalie, kama kuna uwezekano kwenye hivi Vituo vyetu vya Afya, yaongezewe majengo mawili, kwa maana ya jengo la jumla la wanawake na jengo la jumla la wanaume. Kwa sababu ni Vituo vya Afya viko pale lakini vinahudumia mama pamoja na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Serikali ikitenga fedha tukapata hayo majengo mawili pale, moja kwa moja tutakuwa tumevipa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya. Nasema hivyo kwa sababu, kwa kufanya hivyo, itasaidia sana kuweza kupunguza msongamano kwenye hospitali zetu zile za Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo pia nataka nilizungumzie ni suala la maji. Kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ameeleza vizuri sana namna gani ambavyo Serikali imeweka pesa za kutosha zaidi ya shilingi trilioni 2.2 ndani ya miaka mitano, zimepelekwa kwenda kutatua changamoto ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amesema kwamba imejengwa miradi zaidi ya 1,422 katika nchi nzima ya Tanzania. Hata hivyo, ni ukweli ulio wazi kwamba jitihada za Serikali ziko wazi na tumeona namna gani ambavyo Wizara ya Maji imekuwa ikifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba inatatua changamoto za maji, lakini bado changamoto ya maji ni kubwa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amesema na hotuba ya Mheshimiwa Rais ni maelekezo; nataka nishauri kwamba pamoja na mambo yote ambayo tutaongea ndani ya hili Bunge, lakini bado changamoto itabaki pale pale kwa sababu Mfuko wa Maji chanzo chake bado hakitoshi. Ukiangalia miradi ya maji ni mingi lakini yote inategemea Mfuko mmoja wa Maji ambao fedha zake ni ndogo. Hili suala ndani ya Bunge lako Tukufu tumekuwa tukilizungumza hata kipindi kilichopita kwamba pamoja na jitihada ambazo zitakazofanyika lakini kuna umuhimu na haja kuhakikisha kwamba Serikali inaongeza fedha kwenye Mfuko wa Maji ili kuweza kutatua tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Maji. Kwa kuanza napenda nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anafanya katika Taifa letu, katika kuhakikisha kwamba Watanzania tunapata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Mheshimiwa Aweso anafanya kazi kubwa sana. Sisi kama Wabunge tutaongea masuala mengi humu Bungeni, lakini yote ni katika kushauri, haiondoi ukweli kwamba Wizara ya Maji ipo vizuri na inafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sote tunafahamu kwamba kwa miaka mingi tangu nchi yetu ipate uhuru, miradi mingi sana ya maji imeshapelekwa kwenye maeneo yetu. Kama haitoshi ni fedha nyingi sana ambazo zimepelekwa kwenye miradi ya maji na miongoni mwa Wizara ambazo zimeshapelekwa fedha nyingi ni Wizara hii ya Maji, lakini bado kilio ni kikubwa sana, unapokuja suala la maji kilio ni kikubwa sana huko kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha zaidi kwa sababu vilio hivi vinatoka kwenye maeneo yale yale ambayo tayari Serikali imeshapeleka miradi mikubwa ya maji. Ukiangalia chanzo cha haya yote ni kwa sababu hakuna usimamizi wa kutosha kule chini kwenye mikoa yetu, wilaya zetu na kata zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019, Bunge lako Tukufu lilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Maji na mojawapo ya kipengele ambacho kilikuwa ni muhimu sana kwenye hiyo sheria ni kuzipa mamlaka zile jumuiya za maji ziweze kuajiri lakini vile vile kufukuza wataalam wa maji endapo watakuwa hawajafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jema, lakini ni lazima kwamba Serikali iweze kutia mkono wake. Serikali pamoja na kwamba ina dhamira kubwa na nzuri ambayo inayo lakini watambue kwamba bado ina kazi ya kufanya ili kuweza kufikia malengo ambayo tumejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwamba Sera ya Maji ya mwaka 2002 imesema wazi kwamba jukumu la maji si la Serikali peke yake, wananchi wanajukumu kubwa la kuchangia huduma za maji. Lakini vile vile hizo fedha ambazo zinapatikana kwenye hiyo miradi ya maji lazima ziende kwenye uendeshaji, kwenye upanuzi, lakini vile vile ziende kwenye ukarabati wa miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tafsiri hiyo, ili sasa sheria pamoja na sera ziweze kufanya kazi, hatupaswi kuachia jumuiya za maji peke yake ndiyo ziajiri wataalam wa maji. Nasema hivi kwa sababu tumeshuhudia maeneo mengi ambapo kuna Jumuiya za maji, wataalam wengi ambao wanaajiriwa kwenye hayo maeneo ni wale ambao wengi wao hawana uzoefu wa kutosha. Lakini wengi wao hawana ujuzi wa kutosha. Kwa hiyo unakuta kwamba miradi ile pamoja na kwamba Serikali imeweka pesa nyingi, lakini ile miradi inakuwa haina sustainability, ndani ya muda mfupi tunaona miradi imekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ile dhana kamili ya kuweka Sera ya Maji ili basi wananchi waweze kuona matunda ya fedha zao ambazo wanachangia kwenye miradi, inakuwa haipo. Pia sote tunafahamu kwamba, ili miradi ya maji iweze kuleta tija ni lazima kuwepo na usimamizi mzuri wa miradi ya maji. Kwa hiyo tutaongea mambo mengi sana hapa Bungeni, lakini kama hakuna usimamizi mzuri itakuwa ni sawa na kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kutokana na hayo nataka nishauri masuala machache na kwa sababu najua Mheshimiwa Waziri wa Maji ni kijana ambaye ni msikivu, naamini atafanyia kazi ushauri wa Wabunge. Ushauri wangu wa kwanza; ni vema sasa Serikali ikachukua hili suala la hizi jumuiya kuweza kuajiri wataalam wa maji liwe ni suala la Serikali. Kwa maana ya kwamba Serikali iwatafute hawa ambao ni wataalam, iwaajiri, lakini vile vile iwalipe, kwa sababu jumuiya nyingi zimeshashindwa kuwalipa na inapelekea miradi kusuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo zuri ni kwamba Wizara hii inayo Chuo cha Maji na kile chuo kimekuwa kinazalisha wataalam karibu kila mwaka na wale wataalam wapo tu mtaani hawana kazi. Kwa nini sasa Wizara isifikirie kwamba wawaajiri hawa watalaam angalau kwenye kila kata ili basi kila kata kuwe na usimamizi mzuri wa miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Rais wetu wa Awamu ya Sita alizungumza alipokuja hapa Bungeni, alisema kwamba Serikali yake imejipanga kuweka usimamizi mkubwa wa fedha za Serikali ambazo zinatoka Serikalini kwenda kule chini kwenye miradi. Hata hivyo, swali la msingi la kujiuliza ni kwamba, hizo fedha zinapoenda kule chini je, ni nani ambaye ni mtumishi wa Serikali anayewajibika moja kwa moja? Kwa sababu hawa ambao walikuwa wanaajiriwa na hizi jumuiya hawawajibiki kwa mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawawajibiki kwa Serikali na kuna baadhi ya maeneo tumeshuhudia kabisa kwamba wamekusanya pesa na wakakimbia nazo kwa sababu hakuna sehemu wanapowajibika. Kwa hiyo nataka niombe, pamoja na kwamba Serikali italifanyia kazi hili suala, lakini kuna ulazima mkubwa sana wa Serikali watakapoajiri hawa wataalam kila kata waangalie sasa namna gani ambavyo watatekeleza ile sera ambayo tunasema kwamba ni muhimu hawa wataalam waweze kupatiwa mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapatiwe mafunzo namna gani ya kuweza kusimamia miradi ya maji, kwa sababu good governance ndiyo kitu pekee ambacho kinatakiwa ili miradi ya maji iweze kuleta tija. Kwa hiyo mafunzo ni suala ambalo ni la msingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, linguine, tunatambua kwamba wanahitaji pia kupata uzoefu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa naambiwa hapa kengele ya pili imegonga.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Aah! Mara hii imeshagonga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja niweze kumalizia. Pia katika Mkoa wetu wa Songwe, naomba sana Serikali iweze kutusaidia, mkoa ule ni mpya lakini mpaka sasa hivi hatuna mradi wa kimkakati ambao tayari umeshafanyika katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mradi ambao unaweza kuhudumia Miji ya Tunduma, ikahudumia Mji wa Vwava pamoja na Mji wa Mloo kwa kutoa maji Ileje, kwa hiyo napenda kumwomba sana Mheshimiwa Waziri, aweze kuliangalia vizuri suala hili la Mkoa wetu wa Songwe ili uweze kuwa na mradi mmoja wa kimkakati kuliko kuwa na miradi mingi ambayo haina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nami nishukuru kwa kupata nafasi niweze kutoa mchango wangu. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana, nasi kama Wabunge tupo pamoja nao kuhakikisha kwamba tunatekeleza azma ya Mheshimiwa Rais katika kumaliza changamoto ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru kipekee sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ameendelea kuhakikisha kwamba Watanzania anawatua ndoo kichwani hususan wanawake wa Tanzania. Yapo mambo mengi yameelezwa ikiwepo miradi mbalimbali ambayo Mheshimiwa Rais ameendelea kuitekeleza ikiwa ni pamoja na mradi wa miji 28. Vile vile wanawake wa Mkoa wa Songwe wamenituma nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea mradi wa zaidi ya Shilingi bilioni 4.9 katika Wilaya ya Ileje. Ni imani yetu kwamba mradi huu utakapokamilika, utasaidia sana kutatua changamoto ya maji hasa katika Kata ya Itumba pamoja na Isongole ambazo zilikuwa na changamoto kubwa sana ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu tayari hizi fedha zipo kwenye bajeti, wananchi wa Ileje wana imani kubwa sana naye. Tunategemea kwamba fedha ambazo zimebaki, kwa sababu mpaka sasa hivi tumeshapata kama Shilingi bilioni moja, tuna imani kwamba hizo fedha zitaletwa kwa wakati ili kuweza kuwapunguzia adha ya maji wananchi ya Jimbo la Ileje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba nijikite kwenye kueleza hali ya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Songwe. Katika Mkoa wetu wa Songwe, Mkoa ambao ni mpya tuna changamoto kubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu ameshafika siyo mara moja, siyo mara mbili kwenye Mkoa wetu wa Songwe. Kwa hiyo, ninavyozungumza changamoto hizi, Mheshimiwa Waziri anazifahamu. Zipo ambazo amezifanyia kazi nasi tunamshukuru sana na tunampongeza. Hata hivyo bado changamoto ya maji kwenye Mkoa wetu wa Songwe ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye takwimu, zinasema kwamba upatikanaji wa maji kwa vijijini ndani ya Mkoa wa Songwe ni asilimia 73 lakini kiuhalisia ukienda kule site hizo asilimia 73 hazionekani, zinaonekana tu kwenye makaratasi kama ambavyo Kamati imesema kwamba kuna shida kwenye hizi takwimu za maji, uhalisia wake hau-reflect hali halisi ya upatikanaji wa maji katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati akielezea bajeti yake. Ameeleza mambo mengi na ya msingi sana, lakini upo mradi wa miji 28 ambao Mheshimiwa Waziri ameutaja, lakini kwenye Mkoa wetu wa Songwe tunayo miji mikubwa mitatu; kwa maana ya Mji wa Mloo, Mji wa Vuawa pamoja na Mji wa Tunduma. Miji hii ina changamoto kubwa sana ya maji na Mheshimiwa Waziri analifahamu hilo, ameshakuja kama ambavyo nimesema awali. Unapozungumzia suala la maji, moja kwa moja unamgusa mwanamke. Wanawake wenzangu wa Mkoa wa Songwe wa Miji hii mitatu wanapata shida sana ya maji. Kwa hiyo, mimi kama Mbunge wa wanawake Mkoa wa Songwe ni jukumu langu kuweza kuwasemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha, nikawa nina shauku sana kuweza kusikia, huenda mji mmoja kati ya hii mitatu itasikika kwenye hii miji 28. Kwa kweli sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe nionyeshe masikitiko yetu makubwa kwa sababu hata mji mmoja haujaingizwa katika hii miji 28. Wabunge wenzangu wamesimama wameishukuru Serikali kwa sababu wamepata angalau mji mmoja au miji miwili, lakini Mkoa wa Songwe ambako changamoto ya maji ni kubwa; kuna Mji wa Tunduma una wakazi zaidi ya 200,000 lakini hakuna maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi kama Wabunge wa Mkoa wa Songwe tulitegemea kabisa kwamba angalau na sisi tutapata mji mmoja. Hii ndiyo maana imekuwa ni changamoto hata kwenye masuala ya ajira. Wabunge imefika mahali tukashauri kwamba ikiwezekana hizi ajira basi zitolewe kule kwenye ngazi za Majimbo yetu ili kuwe na mgawanyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesoma hii bajeti, Mikoa yote ambayo inazunguka Mkoa wa Songwe, kwa maana ya Mkoa wa Mbeya, wamepata miji miwili; Iringa miji miwili; Mkoa mpya wa Njombe ambao ni mpya kama Mkoa wa Songwe wamepata miji miwili; Katavi mji mmoja; lakini Songwe hata mji mmoja hatujapata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nioneshe masikitiko yangu makubwa na niseme kwamba Mheshimiwa Aweso tunatambua sana kazi kubwa unayoifanya lakini kwa hili sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe tumesikitika mpaka tukahisi labda inawezekana Mheshimiwa Aweso ulidhani kwamba Songwe labda ipo Zambia. Sisi hatupo Zambia Mheshimiwa Aweso, tupo Tanzania hii hii. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri wangu kwa Serikali. Kwa sababu tumeshakosa kwenye hii miji 28, na changamoto katika miji hii ni kubwa sana, tunao mradi wetu mkubwa sana wa kutoa maji Ileje kuyapeleka Tunduma pamoja na Mji wa Vuawa; mradi huu ni mkubwa sana na kwa bahati mbaya sana Marais wote kuanzia Mkapa, amekuja Rais Kikwete, Rais Magufuli wameendelea kuahidi mradi huu lakini mpaka sasa haujatekelezwa; kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa sababu sasa hivi ameshatutafutia mfadhili, Mjerumani kwa ajili ya kuja kukamilisha mradi huu wa maji kutoa maji Ileje kuyasambaza Mji wa Tunduma pamoja na Mji wa Vuawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanawake tuna imani kubwa sana na Rais wetu, na kwa sababu mfadhili wa kufadhili huu mradi ameshapatikana, naomba sasa Wizara iweze kusimamia jambo hili likamilike. Kwa sababu kumekuwa kuna kusuasua sana, imechukua muda mrefu. Ukifuatilia, mara wakwambie sijui upembuzi, mara sijui nini, yaani story zimekuwa nyingi.

Sisi wananchi wa Tunduma tumechoka kusubiria huu mradi. Tunataka kuona utekelezaji wake kama ambavyo Mheshimiwa Rais ametafuta fedha, ametafuta mfadhili, na mfadhili amepatikana. Mheshimiwa Aweso na sisi tuna imani kubwa sana na wewe kwamba mradi huu utaanza kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba mtukamilishie huu mradi na tunaamini kwamba ndiyo mradi pekee mkubwa kwenye Mkoa wetu wa Songwe ambao kwa kiasi kikubwa sana utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye Mji wa Tunduma pamoja na Mji wa Vwawa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba pia nijikite kwenye kuzungumzia hoja yangu ya pili. Nimesikiliza sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nilikuwa nataka sana kusikiliza kuhusiana na suala la upotevu wa maji ambao bado ni changamoto kubwa sana kwenye nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya upotevu wa maji...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, kengele imegonga hapa.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, changamoto ya upotevu wa maji ni kubwa sana. Nilikuwa na takwimu za kuweza kuzitaja, lakini kwa sababu muda umekwisha, naomba sasa Wizara, inafanya kazi kubwa sana kwenye kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji, naomba nguvu hiyo hiyo pia ielekezwe kwenye kuhakikisha kwamba tunadhibiti upotevu mkubwa wa maji. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi, lakini kutokana na changamoto ya muda naomba kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa ajira kila mwaka. Nasema hivi kwa sababu katika kipindi kama hiki ambacho wote tunafahamu kwamba uchumi wa dunia umeyumba lakini uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika. Vile vile tumeshuhudia kwamba baadhi ya nchi hata suala la kulipa mishahara kwa watumishi wake imekuwa ni changamoto, lakini kwetu sisi kama Watanzania siyo tu kwamba Mheshimiwa Rais ana uwezo wa kulipa mishahara kwa wakati, lakini vile vile ana nguvu ya kuweza kutoa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili siyo jambo dogo, ni jambo ambalo tunapaswa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu. Sote tunafahamu, Mheshimiwa Rais ametoa hizi ajira 21,200. Ni vyema tukafahamu kwamba mahitaji kati ya mkoa mmoja na mkoa mwingine yanatofautiana. Kwa hiyo tukipeleka kwenye mlengo wa kuzigawa hizi ajira kwa kuangalia tu kwamba kuzigawa hizi ajira kimikoa bila kuangalia kwamba mahitaji yanatofautiana, ni wazi kwamba kuna baadhi ya mikoa tutakuwa hatujaitendea haki hususan mikoa mipya kama ilivyo Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kwamba Mkoa wa Songwe ni mkoa mpya. Tangu kuanzishwa kwake sasa hivi una takribani miaka saba, lakini katika hiyo miaka saba, ni miaka mitano sote tunafahamu kwamba Serikali haikutangaza ajira. Ajira zimetangazwa ndani ya hii miaka miwili ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. Katika Mkoa wetu wa Songwe, ndani ya muda mfupi hii miaka miwili sasa hivi tumeshuhudia kwamba Hospitali yetu ya Mkoa imekamilika japo haihusiani na TAMISEMI na iko tayari kuanza kazi.

Mheshimiwa Spika, tunayo Hospitali yetu ya Wilaya ya Songwe. Wilaya ya Songwe kwa muda mrefu ilikuwa haina Hospitali ya Wilaya. Hivi ninavyoongea hospitali hiyo imekamilika na ipo tayari kuanza kazi. Tunayo Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma ambayo ina hadhi sawa na Hospitali ya Wilaya. Hivi ninavyoongea Hospitali ile imekamilika na ipo tayari kuanza kazi.

Mheshimiwa Spika, hii inaonyesha kwamba namna gani ambavyo Mkoa wangu wa Songwe una uhitaji mkubwa sana wa watumishi wa afya ukilinganisha na mikoa mingine. Hili siyo jambo la upendeleo ni suala la uhitaji. Ukiangalia hata kwenye takwimu. Hivi tunaposema Mkoa wangu wa Songwe mahitaji rasmi ya watumishi wa afya ni 3,481 lakini waliopo mpaka sasa hivi ni watumishi 1,191. Gap iliyopo ni watumishi 2,385. Hata nusu hatujafikia. Hili ni janga na ninavyomfahamu Mheshimiwa Waziri ni mtu ambaye ni rahimu sana. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kwenye hizi ajira atakavyokuwa akizigawa autupie jicho Mkoa wangu wa Songwe, uhitaji ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado kwenye vituo vyetu vya afya, bado kwenye zahanati zetu tumepata zahanati nyingi, vituo vya afya vingi lakini uhitaji ni mkubwa sana na zipo kada ambazo zina uhitaji mkubwa. Nikianza na kada ya Wauguzi, ambayo ni kada ya muhimu sana. Kwenye Mkoa mzima wa Songwe takwimu zinaonyesha kwamba mahitaji ni Wauguzi 1,284, lakini waliopo ni wauguzi 434 tu. Gap iliyopo ni wauguzi 890, bado hatujafika hata nusu. Sasa ndiyo maana hata ukienda kule kwenye vituo vyetu vya afya, changamoto ni kubwa sana. Kwenye zahanati changamoto ni kubwa sana. Unafika kwenye kituo cha afya au kwenye zahanati unakuta hakuna Muuguzi wala Daktari.

Mheshimiwa Spika, hili ni janga na sisi kama Wabunge wa Mkoa wa Songwe tuna kila sababu ya kuomba kwamba Serikali iangalie kwa kina Mkoa wetu wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, tuna suala la Madaktari; mahitaji maalum ni madaktari 67, lakini hivi ninavyoongea tuna Madaktari 29 tu. Tuna gap na uhitaji wa Madaktari 38. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri kwenye mgawanyo wa hizi ajira aweze kuutupia jicho Mkoa wa Songwe kwa sababu mahitaji ni makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, vile vile tuna mahitaji makubwa sana ya watumishi katika sekta ya Wakunga na hawa ni watu ambao ni wa muhimu sana. Serikali ya Awamu ya Sita imejikita kuhakikisha kwamba la kwanza tunapunguza vifo vya mama na mtoto. Ni wazi kwamba hatuwezi kupunguza vifo vya mama na mtoto kama hatujahakikisha kwamba kule kwenye zahanati zetu kwenye vituo vya afya, kwenye hospitali za wilaya, kuna kuwa na Wakunga wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tunapokuwa tunahamasisha akinamama kwamba wanapojihisi kwamba ni wajawazito waende kwenda kuripoti clinic. Wakifika kule basi wawakute Wakunga au wawakute hawa wahudumu. Nilikuwa naomba sana Serikali iweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, pia nikija kwenye upande wa elimu. Mkoa wetu wa Songwe ni mpya na tunaishukuru sana Serikali ya Mama Samia kwa sababu ametupatia Shule ya Mkoa ya Sekondari kwa ajili ya wanawake, mabinti wasichana. Tunamshukuru sana lakini sisi Mkoa wetu wa Songwe tuna upungufu mkubwa sana wa Walimu wa masomo ya Sayansi. Tunatamani kwamba tuzalishe Madaktari wengi, tunatamani kwamba miongoni mwa Madaktari bingwa nchini Tanzania watoke ndani ya Mkoa wa Songwe, lakini kwa sababu tuna upungufu mkubwa sana ya hawa Walimu wa masomo ya sayansi, haitawezekana!

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kwamba 440 hatuna Walimu wa masomo ya sayansi ndani ya Mkoa wa Songwe. Tunaomba sana kwenye huu mgao, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa akifanya basi ni vyema akautupia jicho Mkoa wetu wa Songwe. Wabunge wengi wamezungumza sana kuhusiana na zile ajira za Walimu na kutoa ushauri kwamba ni wakati muafaka sasa Serikali ikawaangalia wale Walimu ambao wamejitolea kwenye halmashauri zetu na napenda kusisitiza hilo na kuungana na maoni ya Wabunge wengine ambao wameongea kwamba ikiwezekana hizi ajira zikatolewe kule kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu kule kwenye Halmashauri ndiko ambako hawa Walimu wapo kule wanajitolea maana yake Halmashauri ndio zinawajua kwamba fulani anafaa, fulani hafai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika vile vigezo ambavyo Mheshimiwa Waziri juzi nilikuwa namsikiliza wakati akivitaja, kigezo cha kujitolea pale hakikuwepo. Ukienda Wizara ya Kazi na Ajira wamekuwa wakitoa program za Walimu kuweza kujitolea ili waweze kupata uzoefu waweze ku- compete kwenye soko la ajira. Sasa kama kwenye vile vigezo vya kutoa hizi ajira kwa nafasi ya ualimu tusipoweka kile kigezo cha watu wanaojitolea tukawapa vipaumbele itakuwa ni disaster kubwa sana. Kwanza tutakuwa tunawavunja moyo nasi tunafahamu kwamba katika shule zetu Mikoa yote Tanzania upungufu wa Walimu ni mkubwa. Kwa hiyo, hawa walimu ambao wanaenda kule kwenye shule zetu wanajitolea wanasaidia sana kuweza ku-cover lile gap la upungufu wa walimu. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri muweze kuangalia na kuwatupia jicho wale Walimu ambao wapo kwenye Halmashauri zetu wanajitolea bure ili pia kuweza kuwahamasisha na wengine katika miaka mingine waone umuhimu wa kusema ukijitolea unakuwa kwenye possibility kubwa ya kuweza kupata ajira.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji Pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi kubwa ambayo wanafanya hasa katika upelekaji wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni siku chache tu zimepita tangu Mheshimiwa Waziri aje kwenye Mkoa wetu wa Songwe na amekuja pale Mlowo ametupatia mradi mkubwa wa shilingi milioni 601. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya wananchi wenzangu wa kata ya Mlowo kukushukuru sana. Lakini pia tunafahamu kwamba kwenye Mkoa wetu wa Songwe tunao mradi mkubwa sana wa maji wa kutoa maji kwenye Mto Momba kuyasambaza kwenye Miji ya Tunduma, Vwawa Pamoja na na mji wa Mlowo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimuombe Mheshimiwa Waziri, kwamba kwneye bajeti ya mwaka jana alutuahidi kwamba mradi huo ungeanza mwaka huu, lakini mpaka sasa hivi mradi huo haujaanza. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri mradi huo uweze kuanza. Sote tunafahamu kwamba azma kubwa ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejionesha kwa namna ambavyo anavyotafuta fedha na kuzipeleka kwenye miradi mikubwa ya maji. Miongoni mwa Wizara ambazo Mheshimiwa Rais amepleka fedha nyingi ni Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo lazima azma hiyo njema ambayo anayo iendane sambamba na kuondoa vikwazo vyote ambavyo vinaweza vikachelewesha azma ambayo anayo Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nasema hivyo kwa sababu miongoni mwa matatizo makubwa ambayo tunayo kwneye Wizara ya Maji, na niseme kwamba ni jambo ambalo bado halijapewa umuhimu na Wizara, ni suala la upotevu mkubwa wa maji; hii ni changamoto. Hata ukiangalia, kwenye Ripoti ya EWURA ambayo imetolewa ya mwaka 2021 imeonesha namna gani ambavyo mamalaka mbalimbali za maji hapa nchini zina kiwango kikubwa sana cha upotevu wa maji. Hali hiyo inasababisha kwamba wananchi wanakosa maji lakini vilevile Serikali inapoteza mapato mengi kutokana na tatizo hilo la kutokudhibiti hali ya upotevu wa maji katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika hiyo ripoti ya EWURA, na sisi tunafahamu kwamba kiwango cha kimataifa cha upotevu wa maji ambacho kinakubalika duniani kote ni asilimia 20, lakini mamlaka nyingi za maji hapa Tanzania zimevuka hicho kiwango cha asilimi 20. Nikianza, mamlaka namba moja ambayo inaongoza kwa upotevu mkubwa wa maji ni Mamlaka ya Mbozi kwenye Mkoa wa Songwe, Mkoa ambao mimi natoka. Ile ripoti imezungumza kwamba kwenye Mji wa Vwawa Pamoja na Mji wa Mlowo ndiko kwenye changamoto kunbwa sana ya upotevu wa maji. Ukiangalia kwenye hii miji mikubwa ndiko ambako shida ya maji ni kubwa sana. Hata huo mradi ambao tunauomba wa kuoa maji Momba ni kuja ku–cover hili gap la changamoto ya maji katika huu Miji ya Tunduma, Vwawa Pamoja na Mji wa Mlowo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu mojawapo kubwa ni uchakavu wa mabomba; na ninaamini kwamba hiyo changamoto haipo tu kwenye mkoa wa Songwe ni nchi yote kuna uchakavu mkubwa sana wa miundombinu. Lakini ukiacha kwenye Halmashauri hiyo ya Mbozi kuna Mkoa wa Arusha, wao upotevu wa maji ni asilimia 51, Dar es salaam 39, Lindi 37, Mwanza 36, Moshi peke yao ndio wako kwenye 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa ni kwamba ni lazima sasa Serikali kwa maana ya Mheshimiwa Waziri uje na mkakati Madhubuti wa kumaliza tatizo la upotevu wa maji katika nchi yetu ya Tanzania. Mheshimiwa Waziri umesikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge wote wameonesha namna gani ambavyo kwanza tunakuamini na tuajua kwamba wewe ni jembe kweli kweli. Kama Mheshimiwa Waziri umeweza kudhibiti mabomba ambayo yanapaa usiku na sasa hivi yanatoa maji mimi naamini Mheshimiwa Waziri huwezi kushindwa kukabiliana na tatizo la upotevu wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe ushauri wangu katika maeneo machache. Ushauri wangu wa kwanza, niombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa hii ni bajeti mpya jambo la kwanza ambalo nataka nishauri Mheshimiwa Waziri kuwe na ajenda maalumu ya kudhibiti suala la upotevu wa maji. Niombe Wizara ibebe jambo hili kama ajenda ili fedha za Serikali zisipotee, lakini vile vile wananchi wapate maji kwa wakati, na ile azma ambayo Mheshimiwa Rais anayo ya kumtua ndoo mwanamke kichwani iweze kutekelezwa. Lakini jambo la pili, nataka niishauri Wizara ifanye utafiti wa kina nchi nzima ili kuweza kubaini maeneo yote ambayo yana uchakavu wa mabomba ya maji. Mimi naamini wakishafanya utafiti, kwa sababu tayari tunayo taarifa EWURA, itasaidia sana kuweza kujua ukubwa wa tatizo uko vipi ili Wizara iweze kujipanga kuweza kukabiliana na hiyo changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la tatu, niishauri Wizara itenge bajeti maalumu kwa ajili ya kukarabati miundombinu yote nchini Tanzania. Katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri umetaja miradi mikubwa mbalimbali ambayo mmeifanya na ambayo mnakwenda kuifanya kwenye mwaka huu wa fedha. Miradi hiyo tukiendelea kutenga, tukijenga miradi mikubwa ya maji kama hatutengi bajeti kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya maji bado tatizo la maji litabaki pale pale. Kwa hiyo niombe tuanze kutenga bajeti ili tuweze kuzisaidia zile mamlaka ambazo zinashughulika na matatizo ya maji katika mikoa yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo jingine, nadhani ni wakati muafaka sasa tuhame kwenye mfumo wa kutumia bili za maji. Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukishauri sana kwa miaka mingi, kwamba tuanzishe luku za maji. Kwani changamoto ya kuwa na luku za maji ni nini? Kama kwenye umeme tumefanikiwa kwa nini kwenye maji tushindwe? leo hii kuna changamoto kubwa sana wananchi wanalalamika kwanza wanabambikiziwa bili za maji. Leo hii kuna taasisi zina madeni kubwa ya maji. Mwarobaini wa haya yote ni sisi kuwa na luku za maji kama ambavyo tuna luku za kwenye umeme tuwe na luku za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini hili likifanikiwa, tutaondoa tatizo kubwa la ukosefu wa maji na changamoto kubwa ya fedha za Serikali kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu, watumishi wake huko mikoani wana imani kubwa sana naye. Kwenye Mkoa wangu wa Songwe mara zote nikiongea na watumishi, kwa maana ya Mameneja, wale wa Mikoa, Mameneja wa Wilaya, mara zote wananiambia kwamba, Mheshimiwa Shonza tunaomba pamoja na yote, msiache kumpongeza Mheshimiwa Waziri wetu, msiache kumshauri kwa sababu, jamaa anafanya kazi kubwa sana, ndio kauli yao siku zote. Kwa hiyo, hii inaonesha watumishi wa Mheshimiwa Waziri kule chini wana imani kubwa sana naye. Nimwombe Waziri jambo moja, wanazo changamoto kubwa ikiwemo changamoto ya ukosefu wa magari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unakuta mabomba yamepasuka sehemu, kuna changamoto sehemu, lakini wanashindwa kufika kwa sababu hakuna magari. Hivi juzi kuna mtumishi mmoja wa Wizara amefariki kwa sababu ya kukosa usafiri. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri alichukue hili katika bajeti yake ya mwaka huu anunue magari, kama ambavyo wamefanya kwenye elimu, kama ambavyo wenzetu wa TARURA wamefanya na kwenye afya, naamini hata kwenye Wizara ya Maji anaweza kuwapatia vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwa sababu tunajua kwamba, Waziri ni mtu wa kazi, nimwombe tu, tumekuwa tukimwona mara kwa mara akishughulika na wakandarasi na mameneja ambao hawafanyi kazi yao ipasavyo; nimwombe Mheshimiwa Waziri aweke target kwamba, kigezo mojawapo cha mtu kuwa promoted kwenye kazi yake ni kudhibiti tatizo la upotevu wa maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii na mimi niweze kuchangia Muswada huu wa Huduma za Habari. Awali ya yote, nichukue nafasi hii kupongeza Serikali hususan Waziri wa tasnia hii ya Habari kwa kutuletea muswada huu ambao ni muhimu kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nipongeze kwa dhati kabisa Kamati ya Huduma za Jamii chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Serukamba, kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana na sisi kama Wabunge tunaunga mkono mapendekezo yao yote ambayo wameyatoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijazungumza jambo lolote, naomba kwanza tuweze kuwekana sawa kwa baadhi ya vipengele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani akiwasilisha hotuba yake hapa ndani, katika ukurasa wa tisa alisema kwamba sheria hii inakwenda kubana mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni upotoshaji, nami nimeshangaa sana kama kaka yangu Sugu anaweza akaingia katika Bunge hili akaongea upotoshaji wa namna hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda naomba niende…
Naomba niendelee kabla ya kujielekeza kwenye vifungu. Naomba mtulie, mtapata muda wenu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika muswada huu, ukurasa wa tisa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Naomba nilindie muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika Muswada huu ukurasa wa tano, umeelezea neno media. Jinsi ambavyo limeelezewa hapa, neno media ime-define moja kwa moja kwamba ni vyombo vyote vya habari vikiwemo na vyombo vya mitandao ya kijamii; lakini muswada huu hatuzungumzii media. Muswada huu unazungumzia print media na ndiyo maana ukisoma…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia muswada huu ume-define neno media kama ambavyo duniani kote umekuwa defined. Unapozungumzia neno media duniani unamaanisha vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii. Muswada huu umejielekeza katika kuelezea neno print media na ukisoma ukurasa huo huo wa tano wa muswada huu, neno print media limeelezewa kwamba ni journal, magazeti pamoja na machapisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nimwambie kaka yangu Sugu kwamba unapozungumzia print media, unazungumzia machapisho, kaka yangu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utofauti mkubwa sana kati ya media na print media. Kwa hiyo, naomba sana usitake kupotosha umma wa Watanzania. Kwa bahati mbaya sana imekuwa ikizoeleka kwamba Bunge hili limekuwa likitumika kupotosha. Napenda kuwambia Watanzania kwamba watu hawa ni watu wa kuwapuuza kwa sababu kila kitu ambacho kimekuwa kikiletwa na Serikali hii, wao wamekuwa wakisema kwamba ni kitu kibaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa kuelezea kwamba nimeshangaa sana ambacho kaka yangu Mheshimiwa Zitto amekizungumza. Kaka yangu Mheshimiwa Zitto siku zote nimekuwa nikikuheshimu kwa taaluma yako na kwa weledi wako, lakini kwa hiki ambacho umekizungumuzia leo kusema kwamba hii taaluma ya habari isiwe na accreditation, kwa kweli ni maajabu. Tunachokijadili hapa ni kuipa hadhi taaluma hii ya habari ili iweze kuheshimika kama ambavyo taaluma nyingine za udaktari na sheria zinavyoheshimika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi tukasema kwamba kwa sababu mimi nina wito wa kuwa mwalimu na sijasomea ualimu ukanikuta ninafundisha, haiwezekani! Leo hii naweza nikamtolea mfano kaka yangu Mheshimiwa Kubenea, hata form four hajamaliza, tumkute pale Chuo Kikuu, itakuwa ni ajabu sana endepo tutamkuta kaka yangu Mheshimiwa Kubenea anafundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eti kwa sababu tu ana passion ya kufundisha. Hiki kitu hakiwezekani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana muswada huu unakuja kuhakikisha kwamba taaluma hii inaheshimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Mbunge amezungumzia taarifa ya habari ya MV Bukoba ilitolewa na machinga…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nimeshangaa sana. Kuna tofauti kubwa sana kati ya habari na taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile iliyotolewa ilikuwa ni taarifa, siyo habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ni taaluma. Kama ambavyo taaluma nyingine zinavyoheshimka, ndiyo maana Serikali ya Chama cha Mapinduzi iliona kwamba muswada huu umechukua muda mrefu sana, lakini sasa tumeamua kuweza kuupitisha ili maslahi ya Watanzania yaweze kuzingatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa sana pia Mwenyekiti wa Chama cha CHADEMA, baba yangu Mheshimiwa Mbowe amekuja hapa Bungeni leo hii anaacha kujadili masuala ya muswada anaanza kusema kwamba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi eti tumeongwa shilingi milioni 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni ajabu sana. Kama Mwenyekiti wa chama kikuu cha Upinzani tunachokitegemea katika Taifa hili, anaingia Bunge badala ya kujadili masuala ya msingi, anaanza kujadili shilingi milioni 10, kwa nini hajazungumzia mabilioni ambayo alipewa na Mheshimiwa Lowassa akampokea CHADEMA? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea kwamba angeingia katika Bunge hili atuambie, ikiwa yeye ndio alikuwa akizunguka akisema kwamba Mheshimiwa Lowassa ni fisadi, lakini alipopewa mabilioni, kitabu kikabadilika akaanza kumsifia kwamba Mheshimiwa Lowassa ni msafi.
Hayo ndiyo tulitegemea kwamba aje ayaongee katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niwakumbushe wenzangu wa Upinzani; wakumbuke kwamba muswada huu, Chama cha Mapinduzi hakijakurupuka…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha ameelezea historia ya muswada huu; muwe mnasoma ndugu zetu wa Upinzani, siyo mnakuja hapa mnapinga bila kuwa na hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu wa habari umeanza tangu mwaka 1993 na ndiyo maana hata ulipoletwa katika Bunge lililopita mwaka 2015, ninyi leo ambao mmesimama kupinga, mlisimama mkaupinga hata mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sishangai kwamba walipinga muswada huu mwaka 2015, wakasema kwamba tusubiri Serikali ya Awamu ya Tano ije ijadili muswada huu, ndiyo maana nasema hatuna namna, lazima muswada huu uweze kupita, kwa sababu hiki tunachokijadili leo ni makubaliano yaliyofanyika mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, muswada huu ni mzuri na wadau wameshirikishwa, wametoa maoni yao. Kwa hiyo, muswada huu kama Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuna haki ya kuunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nitangaze rasmi kuunga mkono muswada huu kwa nguvu zote na nielezee kwamba tasnia hii ya habari ni mojawapo ya tasnia muhimu sana katika Taifa letu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya tasnia hii ya habari ni kutoa habari kwa jamii, kuelimisha pamoja na kuburudisha. Kwa miaka mingi sana tasnia hii imepoteza mwelekeo, imepoteza dira, watu wamekuwa wakijifanyia mambo wanayoyataka kwa sababu kulikuwa hakuna sheria ambayo tulitegemea ingetoa mwongozo katika vyombo hivi vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa sheria hiyo kwa muda mrefu imepelekea kuwepo kwa wanahabari na wamiliki wa vyombo vya habari ambao wengine ni wanasiasa, tunao humu Bungeni, ambao wamekuwa wakitumia vyombo hivi kwa ajili ya malengo yao binafsi na ndiyo maana unashangaa vyombo vya habari leo vinamsifia fulani kama ni fisadi, kesho vinamsafisha, kwa sababu vyombo vimetumika kwa maslahi yao kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kukosekana kwa sheria hii, imepelekea kwamba vyombo hivi kutumika kwa ajili ya kutimiza malengo ya watu fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, vyombo hivi vya habari vimekuwa vikitumika vibaya na wanasiasa kwa ajili ya kuchafuana kitu ambacho sheria hii ni mwarobaini wa vitu kama hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa sheria hii… Naomba mtulie!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono sheria hii. Sitashangaa nitakapoona leo Waheshimiwa Wabunge wa CHADEMA wanaipinga halafu kesho wakaikubali kwa sababu ndiyo kawaida yao wamekuwa hawajielewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja!