Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Juliana Daniel Shonza (9 total)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza:-
Uandaaji wa Mashindano ya Kimataifa ya Mpira wa Miguu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) unataka Miji miwili iteuliwe kuendesha mashindano hayo:-
Je, Serikali imeteua mji upi wa pili mbali na Dar es Salaam kuendeshea Mashindano ya AFCON ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya mwaka 2019 yatakayofanyika Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu, naomba kwanza nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kwa kipekee kabisa nichukue nafasi hii kuweza kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani yake kubwa ambayo ameionesha kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kipekee kabisa nikushukuru wewe mwenyewe Naibu Spika pamoja na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango wenu na ushirikiano wote ambao mlikuwa mkinipa kipindi nikiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako pia naomba nichukue nafasi hii kuweza kuwapa pole wazazi, wanafunzi pamoja na Walimu wa Nduda iliyopo katika Mkoa wangu wa Songwe kwa kuondokewa na wanafunzi ambao walifariki baada ya kupigwa na radi wakiwa shuleni. Nawaombea Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uteuzi wa maeneo ya nchi yetu yatakayotumika kuendesha mashindano ya AFCON mwaka 2019 kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, utafanywa na Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya AFCON 2019 iliyotangazwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo siku ya Jumamosi tarehe 11/11/2017 Jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya mashindano haya ukiwemo uteuzi wa maeneo ya kuendeshea mashindano hayo, ni sehemu ya hadidu za rejea za Kamati hiyo ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Makamu wake ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ndugu Leodger Tenga na Mtendaji wake mkuu ni Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania, ndugu Henry Tandau.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kazi kubwa inayoikabili Kamati hii ni uboreshaji wa miundombinu kwa viwango vya Kimataifa, kazi ya uteuzi wa maeneo ya kuendeshea mashindano hayo itafanyika mapema iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Wilaya ya Lushoto itaanza tena kupokea matangazo ya Redio ya Taifa (TBC)?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kijiografia Wilaya ya Lushoto katika Mkoa wa Tanga ni kati ya Wilaya ambazo zinazozungukwa na milima, mazingira ambayo huzuia mawimbi ya TBC FM pamoja na TBC Taifa, ambayo hurushwa kutokea mitambo ya FM iliyoko katika eneo la Mnyuzi Wilayani Muheza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua changamoto hii, TBC imeamua sasa mtambo wa kurushia matangazo hayo ujengwe katika Wilaya ya Lushoto ili matangazo ya redio yaweze kufika kwa uhakika katika wilaya hii. Ili kufanikisha kazi hii, TBC imetenga shilingi milioni 50 toka bajeti yake ya ndani kwa ajili ya mnara utakaotumika kuweka mtambo wenye nguvu ya watt 500 na viunganishi vyake kwa ajili ya kupokea matangazo hayo. Mtambo huu utafungwa katika eneo la Kwemashai ambako kuna miundombinu ya kuwezesha zoezi hili kukamika kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Wananchi wa Wilaya ya Chunya wameanza kujenga uwanja wa michezo wa kisasa wa Wilaya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi huu ili ukamilike haraka?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 kifungu cha 5.1.8(b) (vi) inaelekeza wajibu wa mamlaka ya Serikali za Mitaa kushirikiana na wananchi katika kujenga, kulinda na kutunza miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja vya michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo wa Chunya unatekelezwa kwa kuzingatia sera ya michezo ikisimamiwa na Serikali kupitia Halmashauri ya Chunya kwa ushirikiano wa karibu na wananchi pamoja na wadau. Mradi huo unaotarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni nane umetumia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 100 zilizotolewa na Hamashauri ya Wilaya ya Chunya katika mwaka huu wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Seriakli kupitia Halmashauri ya Chunya imetenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuendelea na hatua mbalimbali za mradi wa ujenzi wa uwanja huo wa michezo.
MHE. PROSPER J. MBENA aliuliza:-
Kutokana na kuongezeka kwa matangazo ya biashara kwenye vyombo vya habari, upo uwezekano wa baadhi ya matangazo hayo kuwakera na kuleta hisia tofauti kwa baadhi ya watu na hasa watoto kutokana na maudhui mabaya ya baadhi ya matangazo haya.
(a) Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuunda chombo cha kusimamia maudhui ya matangazo ya kibiashara ili kuweka na kusimamia taratibu na kanuni za matangazo?
(b) Je, ni idara gani ya Serikali inahusika moja kwa moja na malalamiko ya wananchi dhidi ya kampuni na taasisi zinazotoa matangazo yenye athari kwa jamii?
(c) Je, ni hatua gani zinachukuliwa dhidi ya kampuni hizo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, Mbunge wa Morogoro Kusini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari ina vyombo vya kusimamia maudhui ya vyombo vya habari nchini, yakiwemo maudhui katika matangazo. Vyombo hivyo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inayoundwa chini ya kifungu cha Sheria Na. 4 cha Mamlaka ya Mawasiliano Na. 12 ya mwaka 2003, ambayo ina Kamati ya Maudhui iliyoundwa chini ya kifungu cha 26 cha sheria hiyo na marekebisho yake katika kifungu cha 173 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroni na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010. Kamati hii ndiyo inayosimamia maudhui ya matangazo ya kielektroniki (redio, television na mitandao ya kijamii).
Mheshimiwa Naibu Spika, chombo cha pili ni Bodi ya Filamu Tanzania ambayo vilevile inasimamia maudhui katika picha jongevu zinazorushwa katika majumba ya sinema, hadharani vilevile katika michezo ya kuigiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara ya Habari Maelezo ni chombo cha tatu ambacho kimehuishwa chini ya kifungu cha Sheria Na. 4 na Sheria Na. 5 vya Sheria ya Huduma ya Habari Namba 12 ya mwaka 2016 kinachosimamia maudhui katika machapisho mbalimbali yakiwemo magazeti, majarida pamoja na vipeperushi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali inapobainika bila kutia shaka kuwa kampuni, asasi au taasisi imechapisha ama kutoa tangazo lenye athari kwa jamii. Hatua hizo ni pamoja na kupewa onyo, kufungiwa kutoa huduma kwa kipindi kitakachotajwa au kufungiwa kabisa kutokujihusisha na utangazaji au uchapishaji wa habari pamoja na matangazo. Serikali inaendelea kuhimiza jamii nzima kuendelea kuzingatia sheria na taratibu zilizopo katika kusambaza habari mbalimbali kwa jamii.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Tunatambua kuwa michezo duniani kote imekuwa chanzo cha mapato na kuinua uchumi wa Taifa husika, lakini nchini Tanzania michezo hususan soka imebaki kuwa burudani tu.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuinua Soka la Tanzania?
(b) Je, kuna mahusiano gani kati ya Serikali na TFF
katika kuimarisha soka la Tanzania kuanzia ngazi ya Wilaya?
(c) Je, Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) linapata fedha za ruzuku kiasi gani toka FIFA na Wadhamini kama TBL na Serengeti Breweries?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuhakikisha kuwa michezo ikiwepo soka inaimarika nchini, imeendelea kuendesha mashindano mbalimbali ya michezo mashuleni kitaifa ikiwepo UMISETA pamoja na UMITASHUMTA ili kuibua vipaji mapema na imeteua shule 56, mbili kwa kila mkoa hadi tatu kwa kila mkoa ili ziwe shule za michezo kwa ajili ya kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo ikiwepo mchezo wa soka.
Aidha, Serikali kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, imeendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na mafunzo ya muda mrefu kwa wakufunzi wa michezo mbalimbali ukiwepo mchezo wa mpira wa miguu.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, TFF, vyama vya michezo pamoja na mashirikisho mengine ya michezo vimesajiliwa na kufanya kazi chini ya Sheria ya Baraza la Michezo (BMT) Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 1971. Aidha, TFF inaendelea na uboreshaji wa viwanja vya soka nchini, mfano ni viwanja vya Kaitaba na Nyamagana mkoani Mwanza. Vilevile TFF inatoa msaada wa kiufundi katika viwanja mbalimbali ili kuhakikisha kwamba viwanja vinakuwa katika ubora unaotakiwa. Wizara yangu inaunga mkono programu mbalimbai za TFF katika kukuza mchezo wa mpira wa miguu wilayani na mikoani zikiwemo programu mpya kabisa za grass root pamoja na programu ya live your goals kwa wanawake ambazo zilizinduliwa Mkoani Kigoma Februari, 2018. BMT nayo inaendelea kusimamia utekelezaji wa Katiba, Kanuni na Sheria zinazosimamia michezo mbalimbali nchini.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapato ya TFF; kwanza TFF ina udhamini wa miaka minne (2015-2018) kutoka FIFA kwenye programu ya FIFA Forward ambayo hutoa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1.25 kwa mwaka ambapo kati ya hizo dola za Kimarekani 750,000 hutumika kwa ajili miradi ya maendeleo na dola za Kimarekani 500,000 hutumika kwa ajili ya gharama za kuendeshea ofisi, timu za Taifa pamoja na ligi. Fedha hizi za maendeleo hazikuwahi kutolewa na FIFA tangu mwaka 2015, hivyo, TFF wanatarajia kupokea kiasi fedha cha dola za Kimarekani milioni tatu kwa ajili ya kutekeleza miradi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TFF iliingia mkataba na Kampuni ya Bia ya TBL mwaka 2013-2017 kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni 10 kwa ajili ya Timu ya Taifa ambap kwa sasa mkataba huo umeshamalizika. Hivyo, TFF imeingia mkataba wa ufadhili na Kampuni ya Bia ya Serengeti wa miaka mitatu (2017-2019) wenye thamani ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya timu ya Taifa ya wanaume na shilingi milioni 450 kwa ajili ya ligi kuu ya wanawake nchini.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI (K.n.y. MHE. NURU A. BAFADHILI) aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na maadili pamoja na silka na desturi za Kitanzania kama walivyo wazazi wao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Awadhi Bafadhili, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusisitiza kuwa wazazi na familia kwa ujumla ndiyo walezi wa kwanza wenye jukumu la makuzi ya mtoto kuanzia hatua za awali. Wazazi hufuatiwa na vyombo vya elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari hadi elimu ya juu. Jukumu la kusimamia malezi na makuzi ya watoto na vijana ni pamoja na kuelimisha kwa maneno na vitendo kuhusu utambuzi wa mambo mema na mambo mabaya, mambo yanayofaha na mambo yasiyofaha yanayostahili na yasiyostahili yakiwemo masuala ya mavazi, kauli, staha, mwenendo pamoja na muonekano kwa vijana.
Mheshimiwa Spika, hatua ya awali ya malezi ya makuzi ikishapita ndipo wajibu mkubwa wa Serikali unajitokeza katika ukuaji wa vijana kupitia sera, kanuni, sheria, taratibu pamoja na miongozo na kwa kutumia majukwaa mbalimbali ya elimu na nasaha kama vile semina, warsha, makongamano, mikutano, maonesho pamoja na matamasha.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayolikabili Taifa letu leo ni athari ya utamaduni wa nje kwa maadili, mila na desturi zetu kupitia muingiliano mkubwa wa watu wa dunia kwa njia ya utalii, biashara na kadhalika, vilevile kupitia maendeleo ya kasi ya TEHAMA. Pamoja na juhudi za Serikali kudhibiti wimbi la utamadunisho hasi nchini kwa kutumia sheria, kanuni na vilevile kuboresha mitaala yetu toka shule ya msingi hadi elimu ya juu ili izingatie elimu ya uraia, utaifa, uzalendo, mchango wa wazazi na wananchi kwa ujumla katika kufanikisha jitihada za Serikali hauna mbadala. (Makofi)
MHE. JOSEPH L. HAULE (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya muda mrefu katika kuimarisha ushiriki wenye tija kwa Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako naomba uniruhusu nitumie nafasi hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri kuipongeza timu yetu ya vijana ya Serengeti Boys kwa kuweza kufuzu kuingia mashindano ya nusu fainali katika mashindano ya CECAFA ambayo yanafanyika nchini Burundi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na timu zetu za michezo kuonesha kuwa matokeo yasiyoridhisha katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa, dalili za Tanzania kurejesha sifa yake ya zamani ya umahiri katika michezo zimeanza kuonekana baada ya mwanariadha wetu nyota Alphonce Simbu kushika nafasi ya tano katika mashindano ya mbio ndefu za Olympic Brazil mwaka 2016. Simbu na wanariadha wengine wa Tanzania waliendeleza rekodi hiyo ya ushindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Januari 2017, Simbu alinyakua medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Kimataifa ya mbio ndefu ya Mumbai – India; Aprili 2017 Cecilia Ginou Kapanga aliipatia Tanzania medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Beijing International Marathon nchini China; lakini vilevile tarehe 23 Aprili, 2017 Magdalena Chrispin Shauri alishika nafasi ya tano kati ya wanariadha 25,000 kwenye mashindano ya Hamburg Marathon nchini Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Aprili, 2017 Emmanuel Ginouka Gisamoda alikuwa mshindi wa kwanza na kuipatia Tanzania medali ya dhahabu kwenye mashindano ya Shanghai International Half Marathon. Lakini vilevile mwezi Aprili, 2017 Simbu alishika nafasi ya tatu kwenye mashindano makubwa ya London Marathon.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumeona mafanikio yaliyojitokeza kwenye mchezo wa mpira wa miguu ambapo timu ya Taifa vijana Serengeti Boys ilifuzu kucheza fainali za michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 nchini Gabon na kufuta historia hasi tuliyokuwa nayo ya timu zetu kushindwa kufika ngazi hiyo kwa miaka yote 37.
Mheshimiwa Mwenyekiti, somo kubwa tunalojifunza ni umuhimu wa mazoezi toka umri mdogo hivyo mkakati wa Serikali wa muda mrefu ni kama ifuatavyo:-
(i) Kuimarisha michezo shuleni ili kuibua na kulea vipaji vinavyojitokeza. Hivyo basi, shule 56 za sekondari zilizoteuliwa mwaka 2013 na mwaka 2014 na Serikali kila mkoa kuwa shule za michezo hazina budi kuimarishwa kwa vifaa, ufundishaji na miundombinu ili ziweze kutekeleza wajibu wake.
(ii) Katika kuimarisha uongozi katika vyama vya mashirikisho ya michezo mbalimbali nchini kwa kuvisimamia kwa karibu ili vizingatie katiba na sheria za michezo.
(iii) Kuimarisha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA ambayo ndiyo kisima kikubwa cha kuwapata wanamichezo wa michezo yote nchini. Ahsante. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Tanzania inayo makabila yapatayo 124 yanaongea lugha tofauti na yanazo mila tofauti ambazo wamekuwa wakiziheshimu tangu enzi za mababu:-
(a) Je, ni lini Serikali itaandika lugha za makabila hayo ili yasiweze kupotea kwenye uso wa dunia?
(b) Je, ni lini Serikali itaandika historia kwa kila kabila nchini ili vijana wanaokua waweze kujua tamaduni za makabila yao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ni msimamizi na mratibu wa shughuli mbalimbali za utamaduni nchini. Aidha, kwa mujibu wa Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997, jamii ndiyo mmiliki wa utamaduni, hivyo wajibu wa kufanya tafiti, kuorodhesha na kuandika historia za kila jamii ni wetu sote.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande wake inaendelea na utaratibu wa kukusanya tafiti za lugha za jamii mbalimbali zinazofanywa na wadau wanaojishughulisha na ustawi wa lugha nchini na inaandaa kanzidata ili lugha hizo zisipotee kwenye uso wa dunia. Hadi sasa lugha za jamii 38 zimeshakusanywa na kufanyiwa tafiti na zimehifadhiwa kwa njia ya kamusi. Ikumbukwe kuwa lugha ni sehemu ya utamaduni wa Taifa lolote lile.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali na wadau mbalimbali wameandika na wataendelea kuandika historia za jamii, mila na desturi zake. Kwa sasa, karibu kila jamii imekwishaandika historia ya mila na desturi zake. Wizara inaendelea na utaratibu wa kukusanya maeneo ya kihistoria ya jamii mbalimbali hapa nchini na kuyahifadhi kwa njia ya TEHAMA. Vitabu vya historia na maandiko hayo yanapatikana katika Ofisi za Idara ya Nyaraka za Taifa, maktaba pamoja na maduka mbalimbali ya vitabu nchini.
MHE. MARTHA M. MLATA (K.n.y. MHE. AISHAROSE N. MATEMBE) aliuliza:-
Sanaa ya Maigizo na muziki ni miongoni mwa Sekta zinazochangia asilimia kubwa ya vijana kujiajiri lakini kuna Vyuo vichache nchini vinavyotoa elimu hiyo ya sanaa ya muziki na maigizo ambavyo ni Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku masharti yake yakiwa ni changamoto kwa vijana wa mikoani:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha matawi ya Vyuo hivyo kwenye Kanda ama Mikoa ili kuongeza fursa zaidi kwa vijana?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mafunzo ya Elimu ya Sanaa ya Maigizo na Muziki au kwa ujumla Sanaa, yanatolewa kwa ngazi ya Shahada na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam kwa upande wa Serikali na Chuo Kikuu cha Tumaini Arusha kwa upande sekta binafsi. Aidha, mafunzo kwa ngazi ya Stashahada na Cheti kwa Vyuo vya Serikali hutolewa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yenye matawi takribani nchi nzima. Vipo vilevile vyuo binafsi ambavyo hutoa mafunzo ngazi ya Stashahada pamoja na Cheti.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa vijana na wadau wengine wanaotaka kubobea kwenye sanaa wajiunge na vyuo hivi ambavyo vimetawanyika nchi nzima. Aidha, nawapongeza wadau wote walioanzisha vyuo hivyo ili kuunga mkono jitihada za Serikali.