Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Pauline Philipo Gekul (2 total)

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni Serikali imetoa Waraka katika Halmashauri zetu kuhusu elimu bure na Waraka wenyewe ni wa tarehe 6 Januari, 2016.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waraka huu umezua sintofahamu katika sehemu ya chakula cha wanafunzi katika shule zetu. Mfano, Waraka huu unasema kwamba wanafunzi wanaosoma day wazazi walipe chakula, lakini wanafunzi wanaosoma shule za bweni ambao wazazi wao wana uwezo hata wameweza kuwafikisha katika shule hizo, hawatakiwi kulipa hata chakula, Serikali itapeleka chakula.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali inasemaje katika hali hii ambayo imezua mtafaruku kwa wazazi kuona kwamba wamebaguliwa wale ambao hawana uwezo na Serikali imewaongezea uwezo wale ambao kidogo wana uwezo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philip Gekul, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini kama ifuatavyo:-
Ni kweli kwamba ipo mikanganyiko imejitokeza sana hasa baada ya kuwa tumeanza kutekeleza mfumo wa elimu bure. Hata hivyo, nataka niwajulishe Watanzania wote maeneo ambayo Serikali imejikita, kuwa ni ya bure.
Moja, kwa upande wa sekondari, tulikuwa na ada ya shilingi 20,000/= kwa mwaka kwa shule za kutwa, eneo hilo sasa hawatalipa. Eneo la sekondari za bweni, wazazi walikuwa wanalipa shilingi 70,000/= kwa mwaka eneo hilo halilipiwi, ni bure. Eneo la tatu, kwa shule za msingi na sekondari mitihani yote ya darasa la nne na kidato cha pili, iliyokuwa inafanywa kwa wanafunzi kuchangia, eneo hilo sasa wanafunzi hawatachangia. Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mitihani hiyo ya kidato cha pili na darasa la nne, watafanya bure.
Mheshimiwa Spika, eneo la lingine kwa shule za sekondari za bweni ambazo wanakula chakula tunaendelea na utaratibu wa kuwalipia, kuwagharamia. Sasa mkanganyiko unaojitokeza kwa uelewa wangu, Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote, ni pale ambako zipo shule za kutwa, ambazo kisera shule za kutwa, ni za mtoto anatoka nyumbani anaenda shuleni, anasoma anarudi kula nyumbani. Hizi sasa ndiyo ambazo zimeleta mkanganyiko hasa kwa wazazi ambao walikuwa wamejiwekea mpango wao, wao wenyewe ili kuweza kuwafanya vijana wetu waweze kupata lishe shuleni.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili nikiri kwamba pamoja na mkanganyiko ikiwemo na hili, Wizara sasa inaandaa utaratibu mzuri wa maelezo mazuri ya namna tutakavyotekeleza kwenye eneo hili halafu tutatoa taarifa, kwa sababu ndiyo tumeanza kutekeleza mwezi Januari, hizi changamoto zimeanza kujitokeza, yako maeneo mengine wanaendelea kuchangisha. Kwa hiyo, tunataka tutoe Waraka ambao sasa utaweka wazi kila kitu na Waheshimiwa Wabunge, tutawaletea nakala ili mtusaidie katika kuratibu jambo hili. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imekuwa ikitoa kauli na matamko mbalimbali kwa wakulima wa mbaazi kote nchini kwamba Serikali inafanya mazungumzo na Serikali ya India ili wakulima hawa wapatiwe soko. Hata hivyo hadi sasa mazungumzo hayo hayajakamilika na wakulima wamebaki na mazao yao.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nifahamu, kwa nini Serikali isione ni busara kuwatangazia wakulima wa mbaazi kote nchini kwamba wameshindwa kuwapatia soko na wasiende kulima katika msimu huu wa kilimo ambao unakwenda kuanza sasa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hata juzi wakati tunapeana maelekezo ya msingi jambo hili la matatizo ya masoko ya mazao yetu lilijitokeza, mbaazi ikiwemo. Ninachoweza kusema hatuwezi kuwaambia wakulima msimu huu wasijiandae kulima kwa sababu suala la masoko, awali zao la mbaazi tulikuwa na soko la uhakika la nchi ya India na ndio wanunuzi wakuu wa zao hili. Huku kwetu sisi mikoa yote inayolima imeendelea kulima kila mwaka na tumeendelea kufanya biashara na nchi ya India bila tatizo lolote lile.

Mheshimiwa Spika, lakini pia hata hivi karibuni Waziri Mkuu wa India alipokuja nchini, aliweza kusisitiza pia tulime mbaazi nyingi na wao pia wanalima na sisi tumelima. Sasa tulipofikia hatua ya kuuza kwa bahati mbaya au nzuri kwao nchi ya India imeweza kuzalisha mbaazi kwa asilimia 30 zaidi na kwa maana hiyo wana mbaazi ziada na kwa hiyo, walisitisha utaratibu wa kununua mbaazi kutoka nchi za nje kuingiza kwao mpaka hapo akiba yao watakapoifikiria vinginevyo. Kwa kufanya hilo wametuathiri kwa sababu soko pekee la mbaazi kwetu sisi ilikuwa ni nchi ya India.

Mheshimiwa Spika, sasa nini jukumu la Serikali kwa sasa; tunaendelea kutafuta masoko na ndiyo sababu tumewasihi wakulima wa mbaazi nchini kote, na ni mikoa mingi inayolima sana mbaazi, tumeendelea kuwasihi kwamba waendelee kutusubiri kwa sababu Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo inashughulikia mbaazi pia sasa inaendelea kutafuta masoko, likiwemo na lile zao la tumbaku ambalo nimelieleza muda mfupi uliopita.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jitihada hizi zitakapofikia hatua nzuri, tutauza. Kwa sasa hatuwezi kuwaambia kwamba tutauza kwa sababu bado negotiations zinaendelea na mataifa ambayo yatataka kununua zao hili la mbaazi ikiwemo na India yenyewe kwa sababu ya ile commitment ambayo ilikuwa imeshatolewa kati yetu na wao; na ndiyo utaratibu wa kawaida kwa nchi ambazo tunafanya nao biashara za mazao. Pale ambapo kunatokea tatizo lazima na sisi tupate taarifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii ni taarifa kwa wakulima wote wa mbaazi kwamba kwa sasa wawe watulivu, tunaendelea na utaratibu huu wakati wowote tutawapa taarifa. Ni kweli tunajua wanaathirika sana lakini ni muhimu pia taarifa hii kuwa nayo na uvumilivu ni muhimu pia kuwa nao.