Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Pauline Philipo Gekul (4 total)

MHE. KUNTI Y. MAJALA (K.n.y. MHE. PAULINE P. GEKUL) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la ulipaji wa ushuru wa huduma ambao ni asilimia 0.3 unaotozwa kutoka mitandao ya simu ambao kwa sasa Halmashauri zimeshindwa kukusanya ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline P. Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wa ushuru wa huduma za mawasiliano ambao ni asilimia 0.3 limekuwa ni tatizo kwa pande zote mbili yaani Halmashauri ambazo ndiyo zinakusanya kwa upande mmoja na kampuni za mawasiliano ambazo anakabiliwa na ugumu wa kuzilipa kwa upande mwingine.
Mheshimiwa Spika, suala hili limejadiliwa na wadau kwa kuongozwa na Wizara yenye dhamana na Mawasiliano na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMESEMI), hivi sasa inafanyia marekebisho Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290 ili kuwezesha kukusanya ushuru wa huduma wa mawasiliano pamoja na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, hatua hii litasaidia sana kupatia ufumbuzi tatizo lililoelezwa na Mheshimiwa Mbunge kwa mapato kukusanywa sehemu moja na Halmashauri zote kupata mapato stahiki. Rasimu ya Sheria hiyo ikikamilika inatarajiwa kujadiliwa katika kikao cha wadau hivi karibuni
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali imekuwa hairudishi katika Halmashauri zetu 30% ya mauzo ya viwanja?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara yangu haikuwahi kuwa na utaratibu wa kurudisha asilimia 30 za mauzo ya viwanja kwa Halmashauri, kwa sababu mauzo ya viwanja hufanywa na Halmashauri husika wanapokuwa na mradi wa viwanja katika maeneo yao na Wizara hupokea ada ambazo zinahitajika kisheria katika uandaaji wa hati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 30 ya fedha ambazo zilikuwa zinarejeshwa Halmashauri ni kodi ya ardhi ambapo katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara ilipeleka mgao wa Sh. 3,541,212,774.01 kwa Halmashauri zote nchini na Halmashauri ya Babati ilipokea jumla ya Sh. 24,138,421.39.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Wizara imekuwa inakumbwa na changamoto kadhaa katika kurejesha asilimia 30 ya fedha za makusanyo. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:-
(i) Halmashauri nyingi kutotuma taarifa za makusanyo kwa wakati ili kuiwezesha Wizara kufanya ulinganisho wa kiasi kilichopokelewa na kile kilichokusanywa.
(ii) Baadhi ya Halmashauri kutumia fedha za makusanyo kabla ya kuziwasilisha kwenye akaunti ya makusanyo ya maduhuli inayosimamiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
(iii) Wizara kupatiwa mgao mdogo wa fedha unavyopokelewa Wizarani kutoka Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imeondoa utaratibu wa marejesho ya retention ya asilimia 30 ya makusanyo ya fedha zote zinazoingia katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaangalia namna bora ya kuweka utaratibu wa utoaji wa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa sekta ya ardhi katika Halmashauri zetu.
MHE. PAULINE P. GEKUL Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya miradi ya maji ya visima kumi katika vijiji inayofadhiliwa na Benki ya Dunia?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philipo Gekul, Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika ilifanya tathmini ya awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji mwaka 2015 ambapo katika Halmashauri ya Mji wa Babati, Serikali ilipanga kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Mutuka, Chemchem, Kiongozi, Malangi, Managhat, Halla, Himti, Haraa, Nakwa na Imbilili. Ujenzi umekamilika katika vijiji vinne vya Mutuka, Himti, Chemchem na Managhat ambapo wananchi wanapata huduma za maji. Ujenzi wa miradi mingine katika vijiji sita unaendelea na umefikia hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itahakikisha inazifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika kutekeleza awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Baadhi ya changamoto hizo ni kuchelewesha manunuzi ya miradi, upungufu wa wataalam wa maji, kukosa wataalam wabobezi wa taaluma za kifedha pamoja na baadhi ya maeneo yaliyokusudiwa kuchimba visima kukosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Halmashauri zote zinaendelea kupewa mafunzo ili kujenga uwezo wa kusimamia miradi, kusajili na kuunda vyombo na kuimarisha usimamizi wa mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za miradi ya maji vijijini ili kuwa na takwimu sahihi.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Serikali iliwahi kuliahidi katika Bunge hili kuwa inafanya mapitio ya Sera ya Elimu Bure na kwamba ingeleta Bungeni mambo yanayohitaji kuboreshwa:-
Je, ni lini mapitio hayo yatakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wangu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Phillip Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliamua kuondoa malipo ya ada kwa elimu msingi inayojumuisha elimu ya awali pamoja na darasa la kwanza hadi kidato nne kama utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Ibara ya 3.1.5 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 Ibara ya 52(a). Lengo la Sera hii ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata fursa hiyo bila kikwazo chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa maamuzi hayo ya Serikali kwa ustawi wa wananchi na Serikali kwa ujumla mwezi wa Februari mwaka 2017 Wizara ilifanya ufuatiliaji kuhusu utekelezaji wa Sera hii ili kubainisha mafanikio na changamoto kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itatumia matokeo na mapendekezo ya ufuatiliaji uliofanyika kutatua changamoto zilizojitokeza ili kuhakikisha lengo la Serikali la kutoa fursa kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule linafikiwa.