Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Pauline Philipo Gekul (70 total)

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu kumekuwa na migogoro katika nchi yetu baina ya wananchi na hifadhi, lakini tatizo hili limekuwa haliishi kwa Wizara hizi mbili ya Ardhi na Maliasili kukaa pamoja na kumaliza matatizo haya.

Nahitaji kufahamu kutoka kwa Serikali ni lini Wizara hizi mbili watakaa pamoja kumaliza migogoro ya Wananchi katika Vijiji ambavyo vinapakana na hifadhi mfano, Wananchi wangu wa Wilaya ya Babati na hifadhi ya Tarangire.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul, Mbunge wa Babati na Mjumbe wa Kamati ya Ardhi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba iko migogoro inayosababishwa na mipaka kati ya Vijiji na Hifadhi za Misitu, Hifadhi za Wanyama na migogoro hiyo tunaijua na ni kweli kwamba hata katika maeneo anayotoka Mheshimiwa Mbunge ya Tarangire na sehemu nyingine tuliiona hiyo. Sasa tumekubaliana ndani ya Serikali katika awamu hii ni kuhakikisha kwamba aina hii ya migogoro yote tunaiondoa, na ndiyo maana nimeandika barua kuwapeni Waheshimiwa Wabunge nafikiri mtapewa leo. Nimeomba kila Mbunge aniambie aina ya migogoro iliyopo katika maeneo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua kama Serikali tuna utaratibu wetu wa kupata taarifa lakini nilitaka nipate taarifa za pande mbili. Iko migogoro kati ya vijiji na vijiji, iko migogoro kati ya mipaka ya vijiji na vijiji na Wilaya, iko migogoro kati ya vijiji na Hifadhi za Misitu na wanyamapori na mengine, kwa maana hiyo tukipata hizo taarifa na zile tulizoagiza Mikoani sisi kama Serikali tutakaa pamoja.

Najua hapa tunahusika, Waziri mwenzangu wa Maliasili anahusika, Waziri wa TAMISEMI anahusika tutakaa pamoja na tutaunda timu na sisi tutakwenda pamoja kuhakikisha kwamba tunaondoa migogoro hii kwa manufaa ya Wananchi wetu.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kuniona niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa katika Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja ulio mbele yetu, miundombinu si kipaumbele.
Kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Magufuli wakati akiomba kura aliahidi ujenzi wa barabara za lami nchini kote ikiwemo Jimbo langu la Babati Mjini ambako aliahidi ujenzi wa kilometa 20 za lami. Naomba nifahamu, ni lini ahadi hii itatekelezwa kwa wananchi wa Babati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi zote ambazo zimetolewa kwanza na Chama Tawala kupitia Ilani yake ya mwaka 2015 - 2020 Serikali hii ina wajibu wa kuzitekeleza. na tutaitekeleza
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo anayoiongelea namuomba awasiliane na TANROADS mkoa ili kuangalia vipaumbele vya sasa vilivyopo katika mkoa ule. Kama barabara hiyo ni moja kati ya vipaumbele vya mkoa, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaitekeleza katika kipindi hiki kama ambavyo iliahidiwa katika kipindi cha kampeni
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Pamoja na mikakati ya Serikali kujenga barabara za lami, lakini kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa katika maeneo yetu wakati anaomba kura, ya ujenzi wa barabara za lami. Katika Bunge hili tuliomba tupatiwe time frame kwamba ni muda gani hizi ahadi zinatekelezwa. Nataka kufahamu ni lini Mheshimiwa Waziri atatuletea ratiba ya ujenzi wa barabara hizo za lami kwa ahadi ya Rais ili tufuatilie kwa karibu ikiwemo Jimbo langu la Babati Mjini kilomita ishirini za lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini, kifupi time frame ya ujenzi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, imeainishwa ndani ya miaka mitano 2015-2020. Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha ndani ya kipindi hiki zile ahadi ambazo tumeahidi kwa kadri ilani yetu ilivyojielekeza, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo, ili mwisho wa siku tuone kwamba ilani yetu imetekelezwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maendeleo ya kutosha na siyo Babati peke yake, isipokuwa kwa Tanzania nzima kwa mujibu wa Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri unafahamu kwamba gawio la Halmashauri za Mfuko wa Barabara ni ndogo sana zinazoenda kwenye Halmashauri zetu, tatizo la barabara siyo la Nzega tu lipo kwa nchi nzima baada ya mvua kunyesha sana mwaka huu barabara nyingi zimeharibika na madaraja. Napenda kufahamu Mheshimiwa Waziri kama upo tayari kuzungumza na Wizara ya Ujenzi ili gawio la Halmashauri ya fedha za Mfuko wa Barabara ziongezeke badala ya hivi sasa Halmashauri zimeshindwa kutengeneza barabara hizo zikiwemo za Babati Mjini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba gawio ambalo Halmashauri zinapata kama fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara zetu hazina uwezo wa kuhimili mambo ya dharura. Kwa maana hiyo, kweli ipo haja ya kutafuta nguvu ya ziada katika kuhakikisha kwamba kwa dharura za mvua hasa zilivyokuwa nyingi kwa mwaka huu, basi tunapata fedha ili tuweze kukarabati hizo barabara lakini pia kutokuathiri miradi yake ya kawaida iliyokuwa imepanga na Halmashauri katika maombi yao ya fedha za kibajeti. Kwa kufanya hivyo ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge Wizara ya Ujenzi mara nyingi imekuwa ikitengewa fedha kwa ajili ya dharura hiyo ambayo kusema kweli inaweza isitoshe, lakini pale kunapokuwa kuna dharura kubwa tunachukua hatua na wanatoa fedha na tunaweza kutengeneza barabara hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama dharura hiyo itakuwa ni kubwa kama ninavyoisema basi Serikali haitasita kufanya hivyo.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Haya mashamba ya NAFCO hata kwa Babati yapo, yaka-transform kwenda RIVACU. Hivi karibuni mwaka jana, Waziri wa Ardhi alitaka Ofisi ya DC katika Wilaya ya Babati, shamba la RIVACU - Dareda lirudishwe kwa wananchi ambalo wanalihitaji kwa kilimo. Lakini hadi leo jambo hilo halifanyiki ilihali wananchi hao wamekuwa wakihangaika sana. Naomba nifahamu kupitia kwa Waziri wa Kilimo, je, uko tayari sasa kushirikiana na Waziri wa Ardhi, kuhakikisha mashamba ya RIVACU Babati yanarudi kwa wakulima wa Babati?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya ardhi katika Mkoa wa Manyara yamekuwa yakipigiwa kelele sana na Waheshimiwa Wabunge akiwepo Mama Mary Nagu upande wa Hanang na Mheshimiwa Jitu Soni.
Kwa hiyo, kwa jambo hili alilolisema schoolmate wangu, Mheshimiwa Gekul, Serikali tunafanya kazi kwa pamoja, na ndugu zangu wa Manyara ni majirani zangu, nitazungukia kuona maeneo hayo kama ratiba itaweza kwenda sambamba tutaweza kupata fursa hata ya kuwa na wenzentu wa Ardhi ili tuweze kuamua kama Serikali tukiwa wote tuko na taarifa sahihi ambalo zinahusu eneo hilo ili tuweze kuwa na jawabu la kudumu la maeneo hayo. Kwa hiyo, kwa sababu si mbali sana Manyara, tutapangilia utaratibu tuweze kufika katika maeneo hayo, na mimi sioni taabu kwenda kuwasalamia watani zangu japo tu sitaenda na nyama ya punda.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imetangaza kwamba nchi yetu sasa masomo ya sayansi ni lazima kwa wanafunzi wetu; lakini hakuna maandalizi ambayo yamefanyika mpaka sasa, hatuna walimu hao kabisa. Nitolee mfano katika Jimbo langu la Babati Mjini, walimu wa mathematics katika shule kumi za sekondari, ni shule moja tu ndiyo ina mwalimu wa hesabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu, Serikali haioni kwamba inawachanganya wananchi wa Tanzania katika kutoa kauli zao wakati hawajajiandaa kukabiliana na tatizo hilo? Ni lini wanaajiri walimu hao wa sayansi? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme kwamba wanafunzi kusoma sayansi kama somo la lazima halijaanza, lakini Serikali iko katika maandalizi. Hatua muhimu ambayo imefanyika ni kuhakikisha kwamba kila shule inakuwa na maabara ambapo hizi maabara tunashukuru kwamba zimejengwa kwa ushirikiano na wananchi hatua inayofuata, sasa hivi Serikali ipo katika utaratibu wa kuhakikisha kwamba maabara zote za sayansi zilizojengwa kwenye shule za sekondari zinakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali wa kwamba masomo ya sayansi yatakuwa ni ya lazima, unaendana sambamba na Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ambapo elimu inakuwa ya msingi kwamba wanafunzi wanasoma kuanzia msingi mpaka sekondari. Kwa hiyo, Serikali bado ipo katika maandalizi ya kuhakikisha kwamba inatengeneza mazingira mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mafunzo kwa Walimu ni kwamba sasa hivi kuna vyuo 10 ambavyo tumeviangalia na tunaviimarisha maabara zake ili ziweze kutoa mafunzo zaidi kwa masomo ya sayansi. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa pamoja na mishahara ya watumishi hawa wa sekta ya afya, Serikali ilikuwa ikitoa motisha mbalimbali ikiwemo on call allowance kwa wauguzi wetu; lakini hadi hivi tunavyoongea Serikali haipeleki pesa hizi kwa wakati; na nitoe mfano kwa Hospitali yangu ya Mrara katika Jimbo la Babati Mjini, tangu mwezi wa pili wauguzi wale katika hospitali ile tangu mwezi wa pili hawajalipwa fedha hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu, ni kwa nini Serikali haipeleki fedha hizi kwa wakati kama ilivyoahidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa katika bajeti iliyopita OC katika Halmashauri zetu na katika hospitali zetu zilipunguzwa kwa zaidi ya asilimia 60; nitoe mfano wa hospitali yangu ya Mrara, ilikuwa inapokea OC ya shilingi milioni 154 lakini ikapunguzwa hadi shilingi milioni 46 kwa mwaka na hizi fedha sasa zilipe likizo za watumishi, maji na umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifahamu kauli ya Serikali, ni kwa nini fedha hizi zimepunguzwa ilhali mambo haya sasa yamekwama? Mfano sisi, zaidi ya shilingi milioni 10 hospitali inadaiwa, imeshindwa kulipa BAWASA bili ya maji. Serikali iko tayari kufikiria kuhusu uamuzi huu wa kupunguza OC katika hospitali zetu za Wilaya ili waweze kuziendesha hospitali hizi? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Pauline Gekul, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Eeh, unisamehe Mheshimiwa Pauline Gekul, ni Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, ulitokea Viti Maalum, uniwie radhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la kwanza kwamba ni kwa nini Serikali haipeleki kwa wakati posho mbalimbali hususan ya on call allowance, nimejaribu kufanya ziara katika maeneo mbalimbali, ni kweli posho hii imekuwa ikichelewa, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba itaendelea kutolewa kwa wakati kwa kadri hali ya uchumi itakavyoendelea kuimarika kwa sababu fedha hizo tayari zilishapangwa katika bajeti, kwa hiyo, zitatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na OC kupunguzwa, haijapunguzwa kwenye OC za Hospitali ya Mrara peke yake, ukiangalia nchi nzima fedha za matumizi mengineyo zilipunguzwa na wote tunajua kabisa, tulikuwa na malengo ya aina gani kama nchi, asilimia zaidi ya 40 imepelekwa katika miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba watumishi waendelee kuvuta subira, tutakapoenda katika mid year review, siwezi kulisemea hili kwa Wizara ya Fedha, tunajua kabisa kila mwaka mwezi Januari au Februari huwa kuna mid term year review. Kwa hiyo, hilo niwaachie wao, naamini itakapofika wakati huo, wataona ni maeneo gani yanayoweza kufanyiwa maboresho ili kuweza kuendana na wakati. Nakushukuru.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na tatizo la soko la chai kuna tatizo kubwa sasa linaendelea katika Mkoa wangu wa Manyara kuhusu soko la mbaazi. Wafanyabiashara wamekataa kununua mbaazi kabisa katika Wilaya ya Babati na katika Wilaya zote za Mkoa wa Manyara na wakulima wamebaki na mbaazi zao kwa sababu India mwaka huu ambao walikuwa wanunuzi wakubwa wao wamelima, Uganda wamelima na Kenya wamelima.
Naomba nipate kauli ya Serikali juu ya wakulima hao wa mbaazi katika Mkoa wa Manyara ambao wameshindwa kuuza mbaazi zao kwa sababu wafanyabiashara wamegoma kabisa kununua mbaazi hizo.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba bei ya mbaazi imetetereka katika miezi ya hivi karibuni na si jimboni kwake tu lakini Tanzania nzima. Soko la mbaazi limetikisika siyo nchini kwetu lakini ni duniani kote, wanunuzi wakubwa ambao wamekuwa wakinunua mbaazi yetu katika siku za hivi karibuni hawajaendelea na utaratibu ule wa kununua kwa bei ile kwa hiyo imepelekea mtikisiko utokee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalifahamu hili, inajaribu kulifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kupata wanunuzi mbadala. Nikubali tu kwamba ni kweli kabisa mbaazi imeshuka bei kwa baadhi ya maeneo kama Lindi na Mtwara imeshuka mpaka hata kufikia shilingi 500 kwa kilo ambayo ni tofauti kabisa na ilivyokuwa huko nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili tunalifahamu na tunalifanyia kazi na nimuahidi tu kwamba pale Serikali itakapopata suluhu tutamtaarifu kwa niaba ya wananchi wake wa Babati.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa miongoni mwa sababu ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezitaja, ambazo zinasababisha uharibifu wa barabara, magari na wakandarasi wasio waaminifu, sababu kubwa mwaka huu iliyosababisha barabara zetu kuharibika ni mvua za masika ambazo hazikutegemewa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa kauli humu ndani katika Bunge la Bajeti kwamba TANROADS watoe fedha katika Halmashauri zetu kwa sababu ni dharura, wasaidie Halmashauri kujenga hizo barabara. Naomba nifahamu hii kauli ya Serikali imetekelezwa kwa kiwango gani, hususan katika Mkoa wangu wa Manyara na Jimbo la Babati Mjini maana hizo barabara hazijatengenezwa kabisa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwa uelewa wangu kauli ambazo tulikuwa tunazitoa kati ya mwezi wa nne na mwezi wa sita kuhusu kuwataka Regional Managers wote wa TANROADS kuhakikisha wanarudisha mawasiliano katika barabara zilizokatika yalitekelezwa. Kwa kuwa anahitaji takwimu, naomba anipe muda nichunguze katika eneo lake kama kulitokea tatizo lolote, ili tuweze kulirekebisha.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa watoto wenye mtindio wa ubongo wamekuwa wakipata matatizo mbalimbali sawasawa na wale watoto wenye ulemavu wa ngozi, hususan suala la haki ya kupata elimu. Naomba nifahamu Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watoto hawa ili wapate haki ya kupata elimu kwa kuanzisha madarasa maalum au shule maalum walau kwa kila Wilaya ili watoto hawa wapate haki hiyo ya elimu ikiwemo Wilaya yangu ya Babati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kusema kwamba wale watoto wenye learning difficulties nachelea kutumia jina mtindio wa ubongo sio wote wanaohitaji kwenda kwenye madarasa maalum. Tutofautishe normal learning difficulties na usonji yaani autism wako wengine ambao wanaweza wakaanzishwa katika shule za kawaida kabisa na wakafunguka, actually kuna taarifa za watu ambao walionekana kama wana learning difficulties wakasoma katika elimu shirikishi na wakafaulu mitihani ya darasa la saba na wako wengine depending on the level wanaweza wakaishi kwa kusoma na kufanya kazi katika mazingira mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo msisitizo upo katika elimu shirikishi isipokuwa kwa wale ambao kutokana na hali yao basi kuna madarasa maalum ninafahamu kuna shule maalum ambazo zimeanzishwa kwa ajili hiyo na Serikali inafanya jitihada za kutosha ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kwa sababu tunaamini hali ya ulemavu ni sehemu tu ya mjumuiko wa binadamu kwa hiyo kila mwanadamu ana haki ya kupata fursa sawa na kila binadamu ana namna fulani ya kipaji chake ambacho hakipaswi tu kupuuzwa kwa ajili ya hali ya ulemavu.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba niongezee majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na eneo hili la wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi mpaka sasa hivi Serikali tayari kwa kushirikiana na Halmashauri kumeshakuwa na shule nyingi za watu wenye ulemavu lakini lazima nikiri kwamba kumekuwa na mapungufu katika shule nyingi nilizozitembelea, shule hizo zimekuwa hazipati rasilimali za kutosha pamoja na kuzipitia mara kwa mara, hata pia katika masula ya kibajeti. Lakini Wizara baada ya kutembea tumeshaona hayo mapungufu na sasa hivi mikakati tuliyonayo ni kwanza ni kuziboresha shule zenyewe ikiwemo kuziwekea miundombinu ikiwemo fensi pamoja na majengo, kwa sababu shule nyingi wanazokaa wanafunzi hawa wenye ulemavu ni zile za zamani kabisa. (Makofi)
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
8
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tayari Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya elimu tayari kuna vifaa maalum ambavyo vimeagizwa kwa ajili ya kusaidia hao wanafunzi wenye ulemavu. Lengo ni kuona kwamba wanafunzi hawa wasitengwe wala kubaguliwa lakini wakati huo huo wapewe haki zao za msingi za kusoma kadri inavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu hayo lakini niseme tu kwamba haitatosha kuwa na shule nyingi za watu wenye ulemavu kama hazitapewa huduma inayostahili, ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa sababu ambazo Madaktari Wakuu au Waganga Wakuu wamekuwa wakitoa kwa suala zima la ukosefu wa dawa katika hospitali zetu ni kwamba, kundi hili la msamaha la wazee, akinamama wajawazito na watoto ni wengi na wanaugua mara kwa mara. Naomba nifahamu, Serikali mmefanya utafiti kwa kiasi gani ili kuona kwamba hili kundi halilemei makundi mengine na kusababisha ukosefu wa dawa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kundi la wazee linapewa kipaumbele cha kipekee kwenye Serikali ya Awamu ya Tano, ndiyo maana kuna portfolio maalum ambayo iko chini ya Waziri wa Afya inayosimamia mambo yanayohusu maslahi ya wazee. Kwa msingi huo, huduma hizi za afya kwa wazee zimepewa kipaumbele na Waziri na ndiyo maana alipoteuliwa tu, alitangaza kwamba wazee wapewe dirisha lao maalum, lakini pia wazee wapate haki ya kutibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakoelekea, tumezielekeza Halmashauri zote nchini ziwakatie Bima ya Afya, aina ya CHF (Mfuko wa Afya ya Jamii), wazee wote waliopo kwenye Halmashauri zao ili wazee hawa badala ya kusema tu wanatibiwa bure, watibiwe kwa kutumia kadi zao za CHF.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama kuna maamuzi mabaya yalishawahi kufanyika ni maamuzi tuliyoyafanya katika Bunge la bajeti hii iliyopita ya 2016/2017 kwa kuondoa au kufuta vyanzo vikubwa ambavyo vinazipatia Halmashauri mapato na kuvipeleka Serikali Kuu.
Mfano kodi ya majengo ambayo mpaka sasa TRA wameshindwa kukusanya, kodi ya ardhi inapelekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina lakini mpaka sasa hazijarudishwa, Halmashauri hazina fedha. Swali, Mheshimiwa Waziri ni kwa nini msifikirie upya uamuzi huu na kurudisha vyanzo hivi kwenye Halmashauri zetu kwa sababu hata Serikali Kuu mkikusanya hamzirudishi kwa wakati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri juzi hapa kwenye Bunge hili kwamba Halmashauri zetu nyingi hazina set za upimaji viwanja, hakuna vile vifaa na katika majibu yake amesema kwamba ataangalia utaratibu wa kurudisha fedha hizi. Ni kwa nini sasa hizi pesa zisitumike kununua vifaa vya upimaji katika Halmashauri zetu ilhali amekiri mwenyewe kwamba hakuna vifaa hivyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ambalo ameanza na maelezo anasema kwamba kama kuna maamuzi mabaya yamefanyika ni Bunge la bajeti lililopita. Mimi niseme tu maamuzi ya Bunge yaliyopitishwa na yeye ni mhusika kwa sababu ni mmoja wa Wabunge waliopitisha.
Maana yake ni kwamba Bunge linapoamua Wizara inatekeleza yale ambayo yanakuwa yameamuliwa kwa sababu yanakuwa na manufaa kwa Taifa. Kwa hiyo, sisi tunatekeleza kile ambacho Bunge hili liliona kinafaa kuzingatiwa kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya Taifa hili kwa ujumla wake. Kwa hiyo, hayo ni maamuzi ya Bunge na tunayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili amezungumzia suala la gharama za vifaa na nilisema hapa wazi ni kweli na tulitaja mpaka na gharama zake kwamba ni kubwa. Katika utaratibu mzima wa kuziwezesha Halmashauri zetu, Wizara kama Wizara kwa sasa na juzi nilisema hapa kwamba tayari tumeshatangaza zabuni ya kununua vifaa vitakavyokwenda katika ofisi zetu za kanda na zitafanya kazi katika Halmashauri zile. Wizara kuwa na vifaa katika kanda haizuii Halmashauri zenyewe kuweka mpango wake wa kununua vifaa kwa ajili ya kufanya kazi. Wizara inasaidia kuhakikisha kwamba kazi zile zinafanyika katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu suala hili linaonekana ni tatizo na ni changamoto kubwa, ndiyo maana nimesema kwa utaratibu wa sasa Wizara yangu pamoja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunaangalia namna bora ya kuhakikisha kwamba idara hii haishindwi kufanya kazi zake katika Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati Wizara inaangalia namna bora ya kufanya, basi pia ni jukumu la Halmashauri zetu kuona ni namna gani tutaliwezesha zoezi hilo ili tuweze kufanya kazi za upimaji na kazi za ardhi kwa ujumla ziweze kufanyika vizuri.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wakulima wa Tanzania wanaelekea sasa kwenye msimu mwingine wa kilimo ikiwa mazao yao bado wanayo manyumbani hawajauza. Tuliona wakulima wa nyanya, mbaazi, mahindi na mazao mengine, na Serikali ilitoa kauli katika Bunge hili kwamba wanatafuta masoko nje ya nchi nilijibiwa na Naibu Waziri wa Kilimo. Naomba nifahamu mchakato huo umefikia hatua gani maana wakulima mpaka sasa wana mazao yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, majibu ya Waziri ni kwamba, wanaanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata mazao ili mazao haya yapate soko na mtawezesha sekta binafsi na Serikali haitoi moja kwa moja fedha kwa ajili ya viwanda hivyo watu binafsi waanzishe. Wakulima wa Tanzania wasubiri kwa muda gani mpaka hivyo viwanda vianzishwe ili mazao yao yapate soko?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nianze na hili ambalo ni rahisi. Wananchi wasubiri kwa muda gani kuanzisha hivyo viwanda?
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunajenga viwanda. Lengo la kujenga viwanda ni kuongeza thamani na kupunguza uharibifu wa mazao (post-harvest loss). Jambo la kufanya Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote na Watanzania nendeni SIDO, na nimekuwa nikilisema, kusudi waweze kutambua na Naibu Waziri wa Ajira alizungumza hapa, kuna kitu kinaitwa ODOP (One District One Product) inalenga kuangalia katika eneo lenu tatizo ni nini, fursa ni ipi.
Mheshimiwa Spika, sasa watakuongoza wale na watakuvuta mpaka uje ufikie kwangu tuweze kupatia suluhisho lakini mimi nina imani na Watanzania wakielekezwa, wakiongozwa wanauwezo wa kuwekeza. Kwa hiyo suluhisho ni tutaanza lini, tumeshaanza sasa hivi tunajenga viwanda. (Makofi)
Tatizo lake Mheshimiwa Mbunge nenda kamuone Meneja wa SIDO kama ukiwa na wepesi njoo unione mimi nitaweza kukupatia suluhisho.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; tatizo la nyanya na tatizo la mbaazi. Tanzania kama Taifa tumepata tatizo kubwa la bei ya mbaazi na ndiyo maana wananchi unao wazungumzia wameweka mbaazi zao. Mwaka jana kilo ya mbaazi ilikwenda mpaka shilingi 2,000 lakini bei ya soko la mbaazi imeshuka mpaka shilingi 500 tatizo tunalijua.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, tunawasiliana na Serikali ya India ili tuwe na makubaliano ya moja kwa moja kuuza mazao hayo ya mbaazi kwa kushirikiana na Serikali ya India. Tanzania tulikuwa tunauza tani laki moja ya mbaazi, Mheshimiwa Mo ametupa order ya tani milioni mbili nina uhakika tutafanikiwa kuwapa majibu Watanzania.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Miongoni mwa matatizo ambayo tunayapata katika Wilaya ya Babati kwa Hospitali ya Mrara ni ranking ya hospitali hiyo ambapo mpaka sasa inaitwa Kituo cha Afya wakati hospitali hiyo imekuwa ikihudumia watu wa Kondoa na watu wa Babati Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi tumekuwa tukipendekeza kwamba hospitali hii tuipandishe rank iwe Hospitali Teule ya Wilaya, lakini Serikali imekuwa haitupi ushirikiano. Je, sasa wako tayari kutusaidia ili hospitali hiyo ipate dawa na vifaa tiba kuhudumia watu wote hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Gekul kwamba Serikali lazima inatoa kipaumbele na ndiyo maana naye anakumbuka juzi juzi tulikuwa pamoja jimboni kwake tukikagua miradi mbalimbali katika Mkoa wa Manyara. Nimeweza kubaini changamoto mbalimbali kimkoa, kiujumla wake kwamba kuna mambo mengi ya kuweka kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama jambo hili lililetwa kama request Serikalini, lakini bado halijafanyiwa kazi, sasa ni jukumu letu kukumbushana tuone jinsi gani tutafanya ili pale ambapo pamepungua tusukume kwa sababu mwisho wa siku tunataka wananchi wapate huduma.
Kwa hiyo, ni commitment ya Serikali kwamba tutaangalia ni kitu gani kilichokuwa kinakwamisha mwanzo, jambo gani (gap) ambalo inabidi tuliweke vizuri ili tuboreshe eneo na mwisho wa siku wananchi wapate huduma ya afya, kwani ni commitment ya Serikali kuwahudumia wananchi wake.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, juzi Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake walijibu kuhusu suala hili la makundi maalum (akina mama wajawazito, watoto na wazee), walisema kwamba sasa wameiagiza Halmashauri zetu waorodheshe wazee ili wapatiwe kadi za bima ya afya. Naomba nifahamu kama Serikali ipo serious huo mwongozo umeshatolewa na TAMISEMI katika Halmashauri zetu ili Madiwani wapange fedha hizo za kuwalipia wazee bima ya afya katika bajeti inayofuata?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza mwongozo ulikwishatoka na Halmashauri tayari zimeanza kutekeleza mpango huo wa kuwakatia CHF wazee wote waliopo katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaomba Wabunge wote washiriki kwenye vikao vya bajeti vya mwaka huu ili wasimamie suala hili, kwa sababu utekelezaji wake upo kwenye Halmashauri. Pesa za kuwakatia kadi za CHF wazee wa nchi yetu waliotumikia ujana wao kuletea maendeleo Taifa letu zipo kwenye own source, kwenye vyanzo vya ndani vya Halmashauri ambavyo sisi kama Wabunge ni Madiwani tushiriki kwenye vikao hivyo, tuweze kuwakatia kadi za CHF wazee wetu.
Mheshimiwa Spika, mwongozo ulikwishatoka na kuna baadhi ya Halmashauri zimeanza kutekeleza mfano mzuri ni Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa rafiki yangu Mheshimiwa Allan Kiula, wao wanatekeleza na wazee wengi wamefaidika na mpango huu.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa TANESCO wameondoa service charge na hawa ndiyo wanatusaidia kusukuma maji katika vyanzo vyetu lakini wenzetu wa Wizara ya Maji kwenye bili zetu za maji bado kuna service charge. Je, ni lini hii service charge itaondolewa kwa wananchi wetu kwa sababu kwa kweli ni gharama kubwa pamoja na bili hizi ambazo zimepanda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Gekul kuhusu ni lini tutaondoa service charge kwenye bili za maji. Mpango huo tumeuanza na kwa sasa Mkoa wa Iringa meter reading haisomwi tena na watendaji, meter reading hakuna kwa sababu tumeweka mita za LUKU. Ukitaka maji unakwenda kulipia kwa kutumia mfumo uliopo, unapata maji kama jinsi ambavyo unanunua umeme. Kwa kufanya hivyo, sasa hivi Mkoa wa Iringa bado muda kidogo hakutakuwa na service charge. Kwa hiyo, tukifanya hivyo nchi nzima service charges zitaondolewa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti tarehe 12 Januari, 2017 nilifika kwenye Gereza la Babati nikakuta watuhumiwa wa kesi ya mauaji na dawa za kulevya wamekaa zaidi ya miaka minne na sheria haijaweka time frame, hizo siku 60 ni kwa makosa ya kawaida. Mheshimiwa Waziri tuambie ni lini mtafanya marekebsho ya sheria ili hata kwa makosa haya ya mauaji na dawa za kulevya watu wasikae magerezani au mahabusu kwa muda mrefu kama ilivyo sasa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya makosa na hata makosa mengine yanawafanya Watanzania wengi walioko magerezani kukaa huko kwa muda mrefu. Lakini swali hili lilikuwa linauliza tunachukua hatua zipi? Naomba kumuelezea Mheshimiwa Mbunge hatua ambazo Serikali imezichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, sasa hivi tunaangalia njia za kuboresha mifumo yetu ya adhabu mbadala ambayo mnafikiri wote Waheshimiwa Wabunge mnajua mmepitisha sheria nyie wenyewe hapa ya Parole, kuna suala la community service na vilevile kuna kitu kinaitwa extra mural penal employment, lakini vilevile ipo haja na hili ni suala pia linawahusu Waheshimiwa Wabunge tukiwaletea bajeti hapa kuongeza vikao vya Mahakama Kuu ambayo Mahakama Kuu ndiyo pekee inakaa kufanya sessions kwa ajili ya murder cases na wafungwa wengi kwa kweli, mahabusu wengi tunawakuta magerezani wa murder cases kwa kweli vikao vya mahakama ni vichache, inabidi tuongeze hiyo frequency.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile tatu, kuna tatizo sasa siyo tu kwa wale wanao-face murder cases hata kwa watuhumiwa wengine kwamba kuna tatizo la ucheleweshaji wa hukumu za mahakama na mwenendo wa mashitaka ambao unawafanya watuhumiwa waweze kwenda mahakamani au wafungwa au mahabusu kwenda mahakamani kudai haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe wito sasa hivi kwa mahakama ku-adhere, kuheshimu au kufuata, kutekeleza waraka namba moja wa mwaka jana wa Jaji Mkuu unaotaka mashauri yote na mwenendo wake unapokwisha ichukue siku 21 tu kila kitu kiweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la mrundikano wa kesi mahakamani na watu kukaa ndani tumelifanyia kazi kubwa mno na tukiangalia record ya nchi hii miaka mitatu iliyopita tulikuwa na mrundikano wa kesi zaidi ya asilimia 60 za zamani, lakini leo mrundikano wa kesi umebakia ni asilimia 5.8 hivi na ambao ni kesi hizo za jinai kama alizoziongelea Mheshimiwa Gekul.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika,
ninakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa gharama kubwa ambazo Hifadhi ya Ngorongoro inatumia ni pamoja na kumtunza faru Fausta ambaye chakula chake kwa mwezi ni shilingi milioni zaidi ya 64. Naomba kufahamu, Serikali ina mpango gani juu ya faru huyu Fausta ambaye analigharimu Taifa au hifadhi ile kwa fedha nyingi sana kwa mwezi na
hata kwa mwaka?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli yuko faru Fausta pale
Ngorongoro na amewekwa kwenye cage kwa sababu amekuwa mzee sana na amekuwa ananyemelewa na magonjwa aina mbalimbali na lengo ni kuhakikisha kwamba maisha yake yanaendelea utafiti na takwimu ambazo zinakusanywa kwa ajili ya faru huyu zinaendelea, kwa sababu wanyama hawa ni wachache sana nchini hivi sasa na kila takwimu ambayo tunakusanya na kuilinganisha na maisha halisi ya wale ambao wako kwenye pori ni muhimu kwa
maisha ya wale wengine ambao wanaishi humo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kufanya kazi hii kuna gharama, lakini hizi ndiyo gharama halisi za uhifadhi. Namuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kutuamini kwamba tunafanya jambo hili kwa nia njema na kwamba takwimu zinazopatikana zinathamani halisi kwa ajili ya
uhifadhi wa wanyama hawa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Hapo mwanzo Mfuko huu wa Bima ya Afya ulikuwa unatoa mikopo mbalimbali katika vituo vyetu vya afya, hospitali, kwa ajili ya ku-support matibabu kwa wateja wao, lakini tangu mwaka jana utaratibu huu wa kutoa mikopo katika hospitali zetu umekuwa sasa na urasimu kwa kupitia Hazina na tangu mwaka jana mwezi wa Tatu mikopo mingi imekwama Hazina. Naomba nifahamu, Serikali ina mpango gani
kurudisha utaratibu huu wa Mfuko wa Bima ya Afya katika Wizara husika ili hospitali zetu zipate mikopo ikiwemo Hospitali ya Mrara, Babati ambayo tumeomba mkopo tangu mwaka jana na hatujajibiwa? Naomba ufafanuzi.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Utaratibu wa mikopo ni kwamba ni lazima taasisi za Serikali zinapokopa ziwe zimepata kibali cha kutoka kwa Msajili wa Hazina (Treasury Registrar) na huo ni utaratibu wa
kawaida wa ndani ya Serikali. Kama ilikuwa ikifanyika hivyo huko nyuma maana yake taratibu zilikuwa haziko sawa lakini kwa mujibu wa circular ambayo ilitolewa na Msajili wa Hazina miezi takribani 24 iliyopita, utaratibu uliwekwa kwamba taasisi yoyote ile ya Serikali haitaruhusiwa kuchukua mkopo ama kutoa mkopo kwenye taasisi nyingine bila kuwa kuna kibali cha mwenye mali kwa maana ya Treasury Registrar ambaye anazishikilia mali zote za mashirika ya umma, kwa hiyo ni utaratibu wa kawaida wa kisheria ambao ni lazima ufuatwe.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti
nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa michakato hii inachukua muda mrefu sana ambayo inaanzia kwenye ngazi za vijiji mpaka juu kama Naibu Waziri alivyosema.
Je, endapo michakato hii katika ngazi za chini
itakamilika mapema, nini kauli ya Serikali Kuu ili na wao waharakishe na wananachi hawa wapate haki zao?
Swali la pili, kwa kuwa tunapokaribia wakati wa
Uchaguzi Mkuu, Serikali imekuwa na hali ya kugawa kata zetu na vijiji ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kwa karibu. Naomba nifahamu Serikali ina mpango gani
kuanza mchakato huo mapema kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuondoa usumbufu na maandalizi pia ya muhimu kwa wananchi hawa ambao maeneo yao ni makubwa na Kata zao ni kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti kwanza katia
sehemu ya kwanza ni kwamba mchakato umekamilika na
Makao Makuu ya Halmashauri imeshathibitishwa ndiyo ile
ambayo imetajwa pale isipokuwa Mheshimiwa Mbunge
alikuwa na utata katika hayo Makao Makuu mapya, kwa
hiyo mchakato huo ulishakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la kugawa
wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi nadhani hii sasa ni
mamlaka zetu katika Ward Council zetu, vikao vyetu vile vya
kisheria kama nilivyovisema, ambapo inaonesha baadaye
jambo hili litaenda katika Tume ya Uchaguzi kupita Ofisi ya
Waziri Mkuu.
Kwa hiyo, hakuna shaka naamini kwamba kila mtu
katika maeneo yake anabaini changamoto zinazokabili eneo
hilo na tutafaya maandalizi ya awali ilimradi kuepusha
ukakasi kwamba maeneo yanagawiwa muda mfupi kabla
ya uchaguzi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni TBA walikabidhiwa maeneo ambayo yalikuwa ya National Housing ambayo
yalikuwa katika Halmashauri zetu ili waweze kufanya ujenzi mbalimbali. Lakini kwa bahati mbaya maeneo haya ambayo TBA wamekabidhiwa yaliyokuwa tayari yanatumika na Halmashauri zetu, mfano ni eneo la National Housing lililoko pale Mji wa Babati ambalo linatumika na vijana wetu wa Machinga. Ombi hilo tulishapeleka Waziri ya Ardhi, lakini sasa maeneo yale yamekabidhiwa TBA ambayo iko Wizara ya Ujenzi.
Naomba nifahamu Serikali au Wizara ya Ujenzi iko tayari na TBA kupokesa maombi yetu tena ili eneo hilo la
National Housing libaki kwa vijana wetu wa Machinga wasisumbuliwe kama ambavyo kauli ya Rais imesema?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iko tayari
kupokea hayo maombi kama ambavyo umesema na tutayaangalia kwa maslahi mapana ya nchi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara katika Jimbo la Babati Mjini na akabaini kero za maji. Kwa hiyo, haya nitakayoyauliza anayafahamu vema na atanipa majibu.
Swali la kwanza, kwa kuwa mradi wa maji wa kijiji cha Malangi umechukua muda mrefu sana na kwa kuwa mradi huu ulitelekezwa na mkandarasi wa awali, na kwa kuwa mradi huu sasa thamani yake siyo shilingi milioni 400 ni shilingi milioni 600.
Je, Serikali iko tayari kutupatia fedha hizo shilingi milioni 600 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji Malangi ili wananchi hao wapate maji kwa muda mrefu ambao walikuwa wameyakosa?
Swali la pili, kwa kuwa mradi wa maji wa kijiji cha Nakwa wenye thamani ya shilingi milioni 801 umekuwa na changamoto nyingi, mabomba yapo juu hayajawekwa chini, yamekuwa yakipasuka wakati huu ambapo mradi unafanyiwa majaribio, na kwa kuwa vijana ambao pia walichimba mitaro kwa ajili ya kulaza yale mabomba hawajalipwa na mkandarasi ambaye anafanya kazi hiyo. Ilikuwa vijana hao walipwe shilingi 4,000 kwa kila mita wamelipwa shilingi 700.
Je, Naibu Waziri Wizara yako iko tayari kuunda timu ya wataalam kwenda kukagua mradi wa kijiji cha Nakwa ambao umekuwa ukisumbua wananchi hawa kwa mradi huo kuchakachuliwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli nilitembelea Babati na hizi changamoto tukiwa pamoja na Mheshimiwa Mbunge tuliziona na tulizijadili na kutoa maekelezo. Nikuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa utaratibu tuliouweka kwamba kila Halmashauri inapata bajeti. Kwa hiyo, hii fedha kwenye mradi wa Malangi tutahakikisha sasa unasimamiwa vizuri na pale nilitoa maelekezo kwamba Waheshimiwa Wabunge mnapoona inasua sua kwenye Halmashauri kama Mamlaka ya Maji ya Mkoa ambayo ipo chini ya Wizara ya Maji basi ni lazima tushirikiane katika utaalam ili kuhakikisha kwamba miradi inatekelezwa katika viwango vinavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumetenga fedha katika mwaka wa fedha unaokuja. Ile bakaa ya upungufu iliyobaki itaongezwa kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kijiji cha Nakwa, Mheshimiwa Mbunge mwenyewe ni shahidi unakumbuka kwanza tulitengeneza utaratibu kwamba kama mradi wa maji uliotekelezwa na Halmashauri uko karibu na Mamlaka ya Maji ya Mkoa, wakati wanapotekeleza ule mradi inabidi washirikiane ili kuhakikisha kwamba vile viwango vinavyotakiwa katika mradi viweze kufikiwa na hasa kwa kuwa mara nyingi miradi kama hiyo kwa sababu mamlaka za maji zina maji mengi, kumekuwa na tabia ya Wakurugenzi wanaomba mradi huo uunganishwe kwenye Mamlaka ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala hili pale tuliagiza kwamba Mkurugenzi wa Maji wa Babati sasa ashirikiane na Halmashauri ili kuweza kuhakikisha kwamba huu mradi ambao haukutengenezwa vile inavyotakiwa basi uhakikishe kwamba kwanza wanautekeleza katika viwango vinavyotakiwa. Pia nakubaliana na wewe kwamba Serikali italiangalia hili ili kuhakikisha wale walioharibu hatua stahiki zinachukuliwa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nina swali moja la nyongeza. Najua kwenye Wizara Mheshimiwa Waziri hana muda mrefu sana, lakini Mahakama ya Mkoa wa Manyara iliyojengwa pale Babati Mjini, Mtaa wa Negamsi ni Mahakama ya Mwanzo, ya Wilaya, mpaka ya Mkoa, kuna baadhi ya wananchi hawajalipwa fidia zao, mpaka leo wameachia eneo hilo kwa Mahakama. Ni miaka 14 sasa tangu 2004. Pamoja na ugeni wake katika Wizara, je, yuko tayari kufuatilia kwa karibu ili wananchi wale, ndugu zake, wajomba zake wapate fidia zao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana kabisa na maoni aliyoyatoa na nitafuatilia kuona fidia ya hao watu ambao walitoa ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hizo, linafanyiwa kazi haraka. Nitalifuatilia kwa karibu na najua watu wengine wanaweza kuwa wanashangaa ukaribu huo umetoka wapi? Ni kwa sababu katika mishipa yangu pia nina damu ya Kibarbaigi.(Kicheko)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Mpango wa Afya ya Msingi (MMAM) muda wake ilikuwa uishe mwaka huu 2017 lakini fedha hizo haziji kwa muda mrefu, takribani kama miaka mitatu nyuma fedha haziji. Ni kwa nini mpango huu wa MMAM ambao ulikuwa unasaidia kujenga zahanati zetu umekwama na anawaambiaje Watanzania kwa sababu maboma/zahanati nyingi bado hazikajamilishwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa sio suala la maboma ya afya peke yake hata maboma ya nyumba za Walimu halikadhalika madarasa. Kipindi fulani hapa takribani miaka mitatu, minne fedha hizi zilikuwa haziendi. Ndiyo maana nimesema kupitia Mfuko ule wa LDGD ambapo kwa sasa mwaka huu kwa mara ya kwanza, namshukuru Mheshimiwa Waziri wangu alilisimamia kwa karibu sana, ndiyo maana hivi sasa Wabunge kama tumepitia katika Kamati zetu za Fedha katika Halmashauri zetu tunaona kuna fedha nyingi zimekuja ambazo zimesaidia kwa kiwango kimoja au kingine kuweza kuhakikisha maboma mengi sana yameweza kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia hili kwani nilipopita maeneo mbalimbali nilikuwa nikipata taarifa mbalimbali kutoka kwa Wakurugenzi jinsi gani fedha hizi sasa wameweza kuzielekeza katika kuhakikisha zile nguvu za wananchi ambazo wamezitoa hazipotei kwa kukamilisha viporo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, naomba tushirikiane kwa pamoja. Lengo kubwa ni kutekeleza mpango wa D-by-D kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, tufanye hili kwa ajili ya mustakabali mzuri kwa kuunganisha nguvu za wananchi katika kuhakikisha Taifa hili linaenda mbele.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka tu kumfahamisha Mheshimiwa Gekul kwamba tayari tumeshaanza kuufanyia mapitio Mpango wa Afya ya Msingi (MMAM). Kwa hiyo, tunategemea kabla ya mwisho wa mwaka tutakuwa tumetoa mpango wa pili ambao utatueleza kama, je, ni lazima tuwe na zahanati kila kijiji wakati sasa hivi barabara zinapitika? Je, ni lazima tuwe na kituo cha afya kila kata? Kwa hiyo, hayo maeneo yote tutayaangalia kwa upana wake. Lengo letu ni kuhakikisha tunasogeza huduma bora kwa wananchi. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwanza ni vizuri Serikali ikakiri kwamba imeshindwa katika Sera hii ya Elimu Bure na nitatoa mfano. Fedha wanazopeleka katika shule zetu asilimia 35 ni fedha kwa ajili ya utawala na chini ya utawala kuna mambo matano yafuatayo: Kuna stationery, maji, walinzi, umeme na dharura. Nitoe mfano katika sekondari moja ya Babati, sekondari ya Bagara – wanapeleka milioni moja na laki saba asilimia 35 ni 302, 4716.55. Katika 324,000 mlinzi analipwa 150,000, maji 200,000 acha stationery, acha dharura, kwa hali ya kawaida walinzi wameshaondoka katika shule zetu. Maji yamekatwa katika shule zetu za msingi na sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini hawataki kueleza ukweli kwamba wameshindwa kutekeleza sera hii kwa sababu shule zetu zimeachwa sasa na hakuna maji. Naomba majibu ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa wamefanya uchambuzi huu tangu Februari, 2017 mpaka sasa hawajarekebisha haya, ni kwa nini sasa wasiruhusu wazazi wachangie maji na walinzi katika shule zao kwa sababu sasa ukitaka kuchangia tu wanasema Serikali inapeleka fedha wakati Serikali haipeleki. Watoe mwongozo tuchangie kuliko watoto wetu wakose maji na walinzi waache shule zetu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Serikali haijashindwa! Narudia tena kusema, Serikali haijashindwa! Kwa nini nasema Serikali haijashindwa? Nimeshatembelea mikoa mingi sasa hivi, nimeshatembelea shule nyingi sasa hivi, kimsingi wanashukuru sana kwamba sasa kuna utaratibu wa wazi wa kupeleka fedha hizo kwenye shule. Wao wenyewe wanapanga, isipokuwa, lazima nikiri bado yapo matatizo machache yanayohitaji kurekebishwa. Tatizo mojawapo lilikuwa ni kutokuwa na ubora wa takwimu. Kuna baadhi ya shule zilikuwa hazijaweza kuleta takwimu zilizo sahihi na hapo ndipo tulipoweza kubaini hata wanafunzi hewa na hivyo tukaweza hata ku-save baadhi ya fedha takriban shilingi milioni 720 zilizokuwa zinaenda zikiwa hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Rais na sisi kupitia Wizara hizi mbili tumekuwa tukisema kila wakati kwamba, wazazi wasijitoe katika kuendelea kusaidia elimu nchini. Pale panapoonekana kuna mahitaji ya msingi zipo taratibu zimeshatolewa mwongozo, Kamati za Shule kushirikiana na wazazi kuweza kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nadhani nimejibu yote kwa ujumla. Kwa hiyo, ninachomwomba tu Mheshimiwa kule kwenye jimbo lake aendelee kuhakikisha anashirikiana na Kamati za Shule lakini pia na uongozi kuona kwamba elimu hii tunaishughulikia wote kwa pamoja na hili sio suala la kusema nani afanye, nani asifanye! Mzazi anao wajibu wa kwanza katika kuhakikisha mwanafunzi wake anasoma vizuri. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri, katika Bunge la Bajeti lililopita, tulipitisha au tulirekebisha Sheria ya Serikali za Mitaa kuhusu ushuru wa mazao; chini ya tani moja wakulima hawa wasitozwe, hasa mazao ya chakula, mfano mahindi na mazao mengine. Lakini Wakurugenzi na Mawakala katika halmashauri zetu wameendelea kuwatoza wananchi ambao wana magunia matano, matatu ya mahindi, mfano Geti la Galapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati – na hilo Geti la Galapo unalifahamu mtani wangu.
Nini kauli ya Serikali kuhusu ukaidi huu wa Wakurugenzi na Mawakala kuendelea kuwatoza wakulima wetu hata magunia matatu ya mahindi wanalipa ushuru huo wa mazao, nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, sheria inabaki kuwa sheria na tunawataka wasimamizi wa sheria hii kule kwenye halmashauri zetu ambao ni Wakurugenzi wetu Watendaji wa Halmashauri zote kuhakikisha sheria hii inasimamiwa, mazao yetu yote ya biashara pamoja na ya chakula chini ya tani moja hayatakiwi kutozwa ushuru wowote, na hii ni sheria naomba itekelezwe. Na kama kuna jambo specific ambalo limetokea niwaombe sana wananchi wetu tuwasiliane. Namba zetu ziko hewani, ofisi zetu ziko wazi, tuwasiliane ili kuhakikisha sheria hii inatekelezwa kama ilivyopitishwa na Bunge letu Tukufu.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wavuvi wa Ziwa la Babati wamekuwa wakipata taabu sana kwa Ziwa Babati kufungwa miezi sita kwa mwaka ilhali wavuvi hawa wanategemea uvuvi katika kuendesha maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kufika Ziwa Babati na kushauriana na watalaam wa Halmashauri ya Mji wa Babati ili kupata mbegu ya samaki ambayo itatumika kwa mwaka mzima badala ya kama ilivyo sasa ambapo wavuvi hao huvua kwa miezi sita tu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kama niko tayari kwenda Babati kwenda kuongea na Halmashauri kuhusiana na hili, mimi sina shida na niko tayari hasa tukiandamana na yeye mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kufungwa mara kwa mara kwa Ziwa Babati ni utaratibu wa kawaida katika small water bodies yaani maji madogo. Kama usipodhibiti ni rahisi uvuvi ukafanyika na ukamaliza kabisa bioanuwai iliyopo ya samaki. Kwa hiyo, ni uataratibu wa kawaida. Hata ukisikia Bwawa la Nyumba ya Mungu limefungwa, ni kawaida. Kwa hiyo, Serikali inafanya hivyo ili kuwasaidia wananchi wako wa Babati. Lengo siyo baya, lakini tunatambua kwamba tusipodhibiti baada ya muda hakutakuwa hata na samaki mmoja katika Ziwa Babati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini akitaka twende, tutaenda.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri ulituahidi kwamba unaajiri walimu wa hesabu katika shule zetu, lakini ajira iliyotoka mwezi wa nne kwa upande wa walimu ni walimu wa biology na chemistry, ulituletea katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi nimesema katika Bunge hili kwamba, katika shule zangu kumi za Babati Mjini za sekondari hakuna shule yenye mwalimu wa hesabu. Sasa naomba nifahamu ni kwa nini msituambie kwamba walimu wa hesabu ninyi hamna na hamna mpango wa kutuletea badala ya kutuahidi kila siku kwamba mtatuletea walimu? Watoto wetu hawasomi hesabu. Naomba kauli ya Serikali. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Bahati nzuri ninayo orodha ya nafasi 3,081 za walimu wa hesabu na sayansi ambao tumewapangia vituo katika mwezi Aprili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Babati Mjini naweza kuangalia kwa haraka haraka, lakini nitoe tu mfano kwa Tarime DC, tumepeleka walimu wa hesabu, Musoma DC tumepeleka walimu wa hesabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tutaliangalia na kama katika Manispaa yake hajapata kabisa, tutaweza kulifanyia kazi ili naye aweze kupata walimu hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kumtoa hofu Mheshimiwa Gekul kwamba tulitoa kibali cha walimu wa sayansi na hesabu 4,129 na hizi ni kwa ajira za mwaka 2015. Tayari ukiangalia tumepata tu Walimu 3,081, bado kuna nafasi zaidi ya 1,000 na zaidi katika kibali hicho ambacho tumekitoa, bado hawajajitokeza. Tunashirikiana na Wizara ya Elimu pamoja na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) tuweze kupokea maombi hayo, tumeanza kuyachambua. Watakaopatikana naamini ikitokea na walimu wa hesabu wako katika kundi hilo, basi kwa hakika kabla ya mwaka wa fedha na wewe utakuwa umepata walimu hao wa hesabu.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mkoa wa Manyara kwa ujumla wake unazalisha sana zao la mbaazi hususan katika Jimbo langu kata ya Singe, kata nzima na mnapita barabarani pale kama mnaenda Arusha ni mbaazi na imestawi. Hata hivyo, kwa kuwa hakuna viwanda vinavyochakata zao hili na Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri na kwa kuwa bei hii imekuwa ikishuka kila mwaka, wananchi wetu wamekuwa wakipata hasara.
Je, Serikali haioni kwamba ni vizuri wakanunua zao hili wao kama wanavyofanya kwa zao la mahindi kwa NFRA ili wao watafute soko badala ya wananchi wetu kuendelea kupata hasara maana hata viwanda havijaanza sasa kutekeleza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kwa sasa bado hatuna viwanda vya kuchakata siyo zao la mbaazi tu lakini mazao mengi yakiwepo mazao mengine ya jamii ya mikunde kama njegele, dengu, choroko na lentili na hiyo inaleta changamoto katika upatikanaji wa soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sasa Serikali haina mpango wa kununua zao hilo kutoka kwa wakulima, lakini tunachofanya ni kujaribu kwenda kule kwenye soko lenyewe India na ndiyo maana tayari tumeshaingia mkataba wa awali ili wananchi wetu waweze kuuza kwa uhakika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la India kwa sasa hata kama tukifanikiwa kupata tatizo litakuwa ni sisi kuweza kuzalisha kiwango ambacho wanahitaji. India kimsingi wana mahitaji makubwa na ndiyo maana tunafikiri njia sahihi na njia ambayo itawakomboa wakulima ni kutafuta hilo soko pamoja na kwamba kama tulivyosema tutaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niseme kwamba changamoto nyingine iliyopo katika uuzaji wa mbaazi na mazao mengine ni mfumo wetu wa soko. Nimshauri Mheshimia Mbunge pamoja na Wabunge wengine wahamasishe wakulima waanzishe vyama vya ushirika kwa sababu ni mfumo ambao utawasaidia kuuza kwa pamoja na kwa urahisi zaidi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi nimuulize mtani wangu swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha amesema kwamba Serikali inapeleka fedha katika Halmashauri zetu na fedha wanazopeleka kwa upande wa OC ni fedha za mitihani tu. Mfano, Halmashauri yangu ya Mji wa Babati wamepeleka 265,605,000 za mitihani tu, hakuna fedha za OC. Je, nini kauli za Serikali kuendelea kudumaza Halmashauri zetu, Wakurugenzi wanashindwa kuendesha ofisi na ni lini wanapeleka pesa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze pia kwa kumpongeza kwa kukiri kuwa tunapeleka fedha kwenye Halmashauri. Kwa sababu swali hili linahitaji takwimu nitamletea takwimu sahihi katika Halmashauri yake tumepeleka kiasi gani kama OC katika utekelezaji wa bajeti. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vyombo hivi vya usafiri bodaboda na bajaji vimekuwa vikisababisha ajali nyingi na wananchi wengi wanapoteza maisha, lakini kwa hali ilivyo sasa wamiliki wanakatia bima ndogo ambayo haim-cover yule anayeendesha na yule abiria wake. Je, Serikali haioni umuhimu wa kukaa na wamiliki wa bodaboda wakatie bima kubwa (comprehensive) ili kuwalinda wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake ilikuwa ni kwamba Serikali haioni umuhimu wa kukaa ili kutengeneza mfumo mzuri ambao utasaidia na hawa ambao ni abiria lakini vilevile na hawa ambao wanaendesha vyombo hivi kuwa katika hali ya usalama. Limeletwa wazo na sisi kama Serikali tunalichukua kuona utaratibu mzuri ambao utasaidia katika kuondoa adha hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kuongezea si tu katika bima tutakwenda mbali zaidi kuwataka pia na hawa waajiri ambao wanawaajiri hawa vijana wajiunge na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa maana ya WCF ili inapotokea tatizo lolote la muendesha bodaboda huyu basi na yeye awe katika sehemu nzuri ya kuweza kupata utaratibu ambao umewekwa na WCF kwa maana ya kuweza kumshughulikia katika matatizo ambayo yanatokana na magonjwa au ulemavu kutokana na shughuli ambayo wanaifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Gekul kwamba suala hili tunalichukua lakini tutakwenda mbali zaidi kusisitiza kwamba na hawa wanakuwa katika utaratibu huo mzuri.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiahidi mara nyingi sana kulipa fidia wananchi ambao maeneo yao yanapitiwa na umeme wa KV400. Miongoni mwa maeneo hayo ni Mkoa wa Manyara na katika Jimbo langu la Babati Mjini, wameahidi zaidi ya mara tatu na ahadi ya mwisho ni tarehe 17 Disemba, kwamba, mngewalipa. Hata hivyo, mpaka sasa Mheshimiwa Naibu Waziri mmekuwa mkisema kwamba, Wizara ya Fedha haiwapi pesa na Waziri wa Fedha yuko hapa. Naomba awatangazie wananchi wa Jimbo langu la Babati Mjini kwamba, ni lini wanawalipa fidia hiyo kwa sababu, wamechoka kusubiri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Pauline Gekul kwa swali lake zuri, lakini naomba niseme haijapata kutokea Wizara yetu ya Nishati ikasema Wizara ya Fedha haijatupa pesa, kwa sababu Serikali inafanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo ilijitokeza ni kwamba tulipata jedwali la thamani ya fidia. Wizara yetu ya Fedha kazi yake yeye hata inapoleta pesa ni kuangalia malipo yanafanyika kwa walengwa na kwa viwango sahihi. Kwa hiyo kulikuwa na changamoto ndogo ndogo tu za kumalizia kwa ajili ya kuthibitisha uhalali, kiwango na walipwaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwambie Mheshimiwa Mbunge mradi huu wa KV400 msongo huu ni muhimu ambao unaunganisha na nchi ya jirani ya Kenya kwa kusafirisha umeme kwa maeneo mbalimbali. Kwa hiyo nimthibitishie kwamba fidia ya wananchi wa maeneo hayo italipwa muda si mrefu, ndani ya mwaka huu wa fedha na maandalizi yanaendelea vizuri. Ahsante sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kulitendea haki swali langu maana yake ni swali la muda mrefu miaka mitatu, lakini hizo fedha tumeshazipokea na tumezisahau.
Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa NFRA walipewa eneo la kujenga godown au kiwanda katika Halmashauri ya Mji wa Babati kwa ajili ya kuchakata mahindi yetu kuongezea thamani, pamoja na kuwapa kiwanja hicho au eneo hilo zaidi ya heka sita mpaka leo mwaka wa tatu NFRA hawajafika kujenga godown kiwanda hicho. Naomba nifahamu ni lini NFRA watafika katika Halmashauri ya Mji wa Babati kujenga kiwanda hicho?
Swali la pili, kwa kuwa wananchi wetu wengi katika Mkoa wa Manyara na katika Halmashauri ya Mji wa Babati msimu huu wa kilimo cha mahindi hawajapata pembejeo za kilimo, hawajapata mbegu na mbolea, wamelazimika kupanda mahindi ya mwaka jana waliyovuna mashambani, mbegu hawajapatiwa. Mbegu zilizopo zinauzwa kwa bei ya juu kilo mbili shilingi 12,000.
Naomba nipate kauli ya Serikali ni kwanini hampunguzi bei ya mbegu za mahindi ili wananchi wetu waweze kupanda mbegu hizo badala ya kuwaachia sasa wanapanda mahindi ya mwaka jana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote pia na mimi naomba nimpongeze kwa dhati kabisa Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo kama alivyosema amekuwa akifuatilia jambo hili tangu miaka mitatu iliyopita. Vilevile naomba nichukue fursa hii kuwapongeza wananchi wote wa Jimbo la Babati Mjini kwa jinsi ambavyo wanafuatilia na kuzingatia umuhimu wa kilimo na vilevile kuweza kutoa ardhi kwa ajili ya kujenga mradi huu wa maghala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo ninaomba nitamke hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba mradi huu tayari umeshakamilika na ninamuagiza Mtendaji Mkuu wa NFRA kuanza kazi mara moja ifikapo mwisho wa mwezi wa tatu. Huu mradi unagharimu milioni 8000. Kwa hiyo, Mtendaji Mkuu wa NFRA hili ni agizo, mwezi wa tatu mwishoni mradi huu uanze kazi mara moja kwa ajili ya kuongeza thamani ili wananchi hawa wa Babati waweze kupata ajira na thamani ya mazao yao pia iweze kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge ameuliza suala zima la mbegu. Katika suala zima la mbegu, sisi kama Serikali mbegu huwa zinakusanywa na makampuni binafsi na ndiyo maana unakuta bei inakuwa ni kubwa, lakini kupitia Wakala wetu wa Taifa wa Mbegu tumeanzisha mpango mahsusi wa kuhakikisha kwamba tutakuwa tunazalisha mbegu ambayo inaitwa hybrid kwa ajili ya kuboresha ili iweze kuwa na bei pungufu.
Vilevile tunashirikiana na makampuni binafsi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata mbegu bora na kwa bei nafuu.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa madaraka ya Wakuu wa Mikoa ambayo ipo kisheria si kushusha vyeo walimu ambao wamekuwa wakifundisha watoto wetu katika mazingira magumu. Hata hivyo hili limekuwa likijitokeza sasa baadhi ya Wakuu wa Mikoa akiwemo Mkuu wangu wa Mkoa wa Manyara kuwashusha vyeo walimu kwa kisingizo cha kwamba eti wamefelisha wakati watoto wanafeli kwa sababu ya mazingira magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu nini tamko la Serikali juu ya Wakuu hao wa Mikoa akiwemo wa Mkoa wa Manyara ambaye ameshusha Simanjiro, Kiteto na Babati Vijijini na anaendelea na ziara kuendelea kuwashusha walimu vyeo, nini kauli ya Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo inaeleweka ni kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio wasimamizi wakuu wa shughuli zote za Serikali katika Wilaya na Mikoa yao. Kwa hiyo, kama inatokea masuala yanayohusu uzembe au utoro wanayo mamlaka ya kutoa maelekezo kwa mamlaka za nidhamu ambazo ni TSC. Mamlaka ya nidhamu TSC inaanzia katika eneo la shule, shuleni pale Mwalimu Mkuu mwenyewe ni mwakilishi wa TSC. Kwa hiyo, kama yeye mwenye ndio anakuwa anaongoza katika kuonyesha uzembe labda na utoro, hiyo lazima hatua ziweze kuchukuliwa. Lakini mambo mengine ambayo pengine yanaonesha kwamba labda kuna mambo ambayo yamevuka mpaka, tutayafanyia uchunguzi maalumu, ahsante sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika Babati ukaona hospitali yetu ya Mrara na tukakueleza kwamba tunapata wagonjwa kutoka Kondoa ambalo ndiyo swali la msingi siku ya leo. RCC tulishakaa kwamba hospitali yetu ipandishwe hadhi kutoka kituo cha afya kwenda hospitali ya Wilaya naomba nifahamu Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini pendekezo letu hilo la RCC mtalifanyia kazi maana hospitali ya Mrara ina hali mbaya na wagonjwa ni wengi tunashindwa kuwahudumia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimefika na Mheshimiwa Mbunge tuliambatana pamoja siku ile tukitembea. Ni kweli wanachangamoto kubwa sana ni kwa vile utaratibu wa upandishaji wa vituo uko kwa mujibu wa sheria na utaratibu ambao ninyi mmeshakamilisha jambo hilo lote na hivi sasa liko Wizara ya Afya katika final stages, nadhani Wizara ya Afya itakapokamilisha hilo jambo mtapata mrejesho, kwa sababu dhamira ya Serikali ni kuwahudumia wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kama mambo yote katika Mkoa yamekamilika naamini Wizara ya Afya ita- finalizes hilo jambo lengo kubwa ni kuwasaidia wananchi wa Babati waweze kupata huduma vizuri. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Katika Jimbo la Babati Mjini, vijiji vya Himiti, Chemchem na Imbilili havina mawasiliano na hili nililiandikia kwa Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii akanijibu kwamba, anafanya maongezi na watu wa Halotel mwezi wa Tatu mwaka huu minara ya Halotel ingeweza kusimikwa katika vijiji hivyo, lakini hadi sasa hakuna kazi yoyote inayoendelea. Naomba nipate kauli ya Serikali, ni lini mazungumzo yao na watu wa Halotel yatakamilika ili wananchi wa Jimbo la Babati Mjini katika vijiji nilivyovitaja vipate mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mazungumzo yanaendelea na eneo ambalo tuna tatizo nalo ni eneo la kodi ya vifaa ambavyo vinatakiwa vitumike katika kukamilisha haya mawasiliano. Namwomba tu maadam bajeti wameipitisha jana na kuna baadhi ya kodi tumeziondoa, nina uhakika mazungumzo haya yatakamilika karibuni na yakishakamilika tutakuja kumwambia watu wa Halotel watakamilisha lini.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nina swali moja la nyongeza. Najua kwenye Wizara Mheshimiwa Waziri hana muda mrefu sana, lakini Mahakama ya Mkoa wa Manyara iliyojengwa pale Babati Mjini, Mtaa wa Negamsi ni Mahakama ya Mwanzo, ya Wilaya, mpaka ya Mkoa, kuna baadhi ya wananchi hawajalipwa fidia zao, mpaka leo wameachia eneo hilo kwa Mahakama. Ni miaka 14 sasa tangu 2004. Pamoja na ugeni wake katika Wizara, je, yuko tayari kufuatilia kwa karibu ili wananchi wale, ndugu zake, wajomba zake wapate fidia zao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana kabisa na maoni aliyoyatoa na nitafuatilia kuona fidia ya hao watu ambao walitoa ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hizo, linafanyiwa kazi haraka. Nitalifuatilia kwa karibu na najua watu wengine wanaweza kuwa wanashangaa ukaribu huo umetoka wapi? Ni kwa sababu katika mishipa yangu pia nina damu ya Kibarbaigi. (Kicheko)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Jimbo la Babati Mjini pamoja na kwamba ni Halmashauri ya Mji kuna baadhi ya maeneo bado hayana maji. Tulipeleka maombi katika ofisi ya Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya kuchimbiwa visima katika Mtaa wa Wa’wambwa, Kijiji cha Singu na cha Hala, maombi hayo yameishafika kwa Wakala wa Uchimbaji Visima. Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya maombi yetu haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa wakala wetu wa kuchimba visima unapeleka maombi kwao moja kwa moja hatuwaingilii, wanakujibu, mkiingia mikataba sisi kazi yetu ni kuchukua sehemu ya hela yako uliyotengewa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji, wakishachimba tunawalipa ili shughuli ziendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri wa taasisi yetu hii, ina- survey yenyewe, inachimba yenyewe, haikupata maji haidai ndiyo uzuri wake. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwamba tujaribu kutumia taasisi yetu na sisi tunaendelea kuiimarisha kwa kuiongezea mitambo ili iweze kutusaidia katika hili suala la matatizo ya maji vijijini. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Udhalilishwaji wa watoto ni pamoja na watoto wa kike kutopata mahali pa kujisitiri katika shule zetu za msingi na sekondari. Serikali ilishatoa kauli kwamba shule zetu ziwe na vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa mashuleni lakini vyumba hivyo mpaka sasa havijakamilika. Ni kwa nini Serikali imeshindwa kusimamia kauli yake yenyewe wakati watoto wa kike wamekuwa wakidhalilika katika mazingira yao ya masomo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba watoto wa kike ambao wako shule wanahitaji sehemu ya kujisitiri wakati wakiwa katika siku zao. Niseme tu kwamba hili tumeshaanza kulifanyia kazi kwa kushirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Elimu. Katika vyoo ambavyo sasa hivi tumeanza kuvijenga kwenye baadhi ya shule tumeshaweka utaratibu huo wa kuwa na vyumba na vyoo maalum kwa ajili ya watoto wa kike.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri mapema mwaka huu alifanya ziara katika Halmashauri yetu ya Mji wa Babati nasi tukakueleza juu ya ahadi ya Mheshimiwa Rais kuhusu ujenzi wa barabara za lami kilometa 20 alizoahidi wakati wa kampeni. Wananchi wa Babati wanauliza ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilometa 20 za lami katika Mji wao wa Babati utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli nilipata fursa ya kutembelea Babati, lakini pia katika ziara yangu sikumbuki kama Mheshimiwa Gekul alisema hilo. Hata hivyo, kwa sababu ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na ahadi zake ni mkataba baina yake yeye na wapiga kura na mkataba huu ni ndani ya miaka mitano, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yale yote ambayo yameahidiwa na Mheshimiwa Rais yanaratibiwa na ndani ya miaka mitano yataweza kutekelezwa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri kwa muda mrefu wafanyakazi wamekuwa hawapandishwi madaraja yao kwa kigezo cha uhakiki wa vyeti feki, jambo ambalo linakwenda kuathiri pensheni zao. Naomba nipate kauli ya Serikali kwa nini hawamalizi zoezi hili ili wafanyakazi hususan Walimu waweze kupandishwa madaraja na pensheni zao zisiende kuathirika baadaye?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri swali hili ni jipya wala halihusiani na swali la msingi ambalo nimelijibu. Hili ni suala la kiutumishi na naamini Waziri wa Utumishi wakati alipowasilisha bajeti yake hapa alilisema hili suala vizuri kabisa nini kimefanyika, uhakiki ulishakamilika, zipo kasoro zilizoonekana ndio maana wanamalizia uhakiki huu na ni imani yangu watakamilisha muda sio mrefu, lakini siamini kwamba imekuwa ikizuia watumishi kupanda madaraja yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema Mheshimiwa Waziri wa Utumishi atalitolea ufafanuzi mzuri na alishalisemea, kwa hiyo nimwombe kwa kauli ya Serikali sitoweza kuitoa hapa kwa sababu swali hili ni jipya.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni kweli majibu hayo aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri ni ya kweli kabisa kwa hatua ambazo zinaendelea katika Halmashauri, lakini huyu Mkandarasi Maswi kimsingi amekuwa akitusumbua sasa muda mrefu kweli amekuwa akitoa sababu mbalimbali kwamba sijui ni masika hawezi kutafuta haya maji. Sasa naomba kwa sababu ilikuwa ni commitment ya Waziri wa Maji alifika katika Kata hii na katika kijiji hiki, je, Wizara hii pamoja na Wizara ya Maji wanaweza wakatupa ushirikiano DDCA wakatusaidia, kwa sababu wao wanafahamu ni wapi maji yanapatikana badala ya huyu Maswi akaendelea kutusumbua na wananchi wale wakapata maji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nakubaliana na Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba huyu Mkandarasi wa awali anayechimba maji katika Kijiji cha Imbilili kwa kweli amekuwa akitusumbua sana, lakini hayo tutayafanyia kazi kwenye Baraza letu kama alivyoshauri. Naomba nifahamu Wizara iko tayari sasa kuangalia bili tunazolipa za maji katika Mji wetu wa Babati kwa sababu wananchi wetu wakilalamika sana, pamoja na upungufu wa maji lakini wanatozwa bili kubwa sana za maji. Je, Wizara hii na Wizara ya Maji mko tayari ku-review bili ambazo wananchi wa Babati wanalipa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kitaalam ni kweli kwamba huwezi kufanya utafiti mpya wa maji chini ya ardhi hasa kama unataka kuchimba visima wakati huu wa masika. Kwa hiyo, kama Mkandarasi ameomba muda kidogo apewe ambapo yupo asilimia 25 kwa sasa hivi, kama anapewa muda wa mwezi wa Tano anaweza akachukua muda wa mwezi mmoja kumalizia visima vile ambavyo alikuwa anachimba kwenye vile vijiji na ikiwezekana mwezi wa Sita au mwezi wa Saba akamaliza kazi ya kuchimba visima. Nashauri kitaalam apewe muda wa mwezi wa Tano na Sita ili kusudi aweze kukamilisha kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Spika, kama Mkandarasi huyu Maswi ataondolewa sasa hivi halafu wakaanza mchakato mpya wa kumpata kazi mtu mwingine wanaweza wakachukua miezi sita kukamilisha kumpata Mkandarasi ambayo itakuwa ni siyo faida sana kwa wananchi. Kwa hiyo, nashauri avumiliwe kidogo kwa kipindi hiki cha miezi miwili ama mitatu ili aweze kukamilisha kazi yake. Wizarani tutasukuma ili kusudi aweze kufanya kazi yake kitaalam zaidi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ningependa kuisifu sana Mamlaka ya Maji Mjini Babati, kama ambavyo imesifiwa pale ambapo Waziri Mkuu alienda mwaka juzi waliisifu wao wenyewe BUWASA kwamba inafanya kazi nzuri na hata Mheshimiwa Diwani Sumaye ambaye anatoka kwenye Kata ile ya Sigino ambako hakuna maji kabisa, mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kwamba bwana kwa kweli tunashukuru wenzetu wa Mjini Babati wanapata maji vizuri, tatizo hapo ni bili.
Mheshimiwa Spika, ili kusudi ianzishwe bili, EWURA kabla hawajaidhinisha huwa wanafanya kitu kinaitwa mkutano wa wadau, wanajadili, wakishakubaliana wadau ndiyo bili ile inaidhinishwa. Kwa hiyo, nashauri Halmashauri kama inaona kwamba bili ni kubwa basi wawasiliane na EWURA kwa barua rasmi ili kusudi suala hilo liweze kutatuliwa. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la by-pass la Mji wa Arusha linafanana kabisa na tatizo la by-pass Mji wa Babati ambako kuna by-pass ya Arusha – Singida na Arusha - Dodoma. Wananchi takribani miaka saba wanasubiri fidia hawajawahi kulipwa na hawajui ni lini watalipwa juu ya by-pass hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri, Babati ni karibu, yuko tayari kuambatana nami ili akawajibu wananchi hao ni lini wanalipwa fidia zao za by-pass hizi mbili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi kabisa niko tayari.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, maeneo mengi nguzo zimeshapelekwa katika vijiji hususani Mkoa wangu wa Manyara, kinachokosekana ni zile conductor na nyaya kwa ajili ya kuunganisha zile nguzo na umeme uwake na Mkandarasi wetu wa Mkoa wa Manyara ameagiza hizo conductors na nyaya muda mrefu viwandani na hili halijafanyika huenda hili tatizo lipo maeneo mengine. Naomba nifahamu ni lini sasa hizo conductors na nyaya zitatoka ili umeme uwake kwenye maeneo na vijiji vyetu ambavyo nguzo zimeshafikishwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba nitambue jitihada kubwa ambazo zimefanywa na Wizara hii, wamelipa shilingi milioni 102 kwa fidia ya wananchi wa Haraa kwa ajili ya umeme huu wa REA, Naibu Waziri anafahamu tulilishughulikia kwa karibu sana. Nitambue jitihada za KV400 ambazo zimefanyika na hivi navyoongea katika Mkoa wangu wa Manyara pale TANESCO Babati …
Mheshiwa Spika, ahsante. Jitihada hizi zinaendelea isipokuwa Mheshiwa Naibu Waziri kuna tatizo moja limejitokeza la variation kati ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati kwa baadhi ya wananchi ambao wanadai fidia hii ya KV400. Naomba nifahamu, hili tatizo la variation na reconciliation kujua hawa wanastahili kiasi gani linamalizwa lini kabla hawajaondoka Babati waweze kupata fedha hizo? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Pauline Gekul, Mbunge Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kwa niaba ya Serikali tunapokea shukrani za Mheshimiwa Pauline kutokana na jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika katika miradi hii ya REA. Amekiri na kutambua kwamba nguzo zimefika katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala la vifaa vya conductors na nyaya, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge ni kweli hivi vifaa kwa mfano conductors wanaagiza nje ya nchi, lakini kwa kuliona tatizo la ucheleweshaji ndiyo maana baadhi ya vifaa katika mradi huu tulitoa maelekezo viwanda vyetu vya ndani vizalishe na wakandarasi waagize. Kwa hiyo, suala hili la vifaa hususani nyaya, viwanda vinavyohusika ni ni East African Cable pamoja na Kilimanjaro Cable, jambo ambalo limejitokeza wakandarasi wengi wanapenda kuagiza kwa mtu mmoja.
Mheshimiwa Spika, tumetoa rai kwamba kwa kuwa Serikali ilivyotoa maagizo ya kuviwezesha viwanda vya ndani kusambaza vifaa vya utekelezaji wa miradi hii, wakandarasi wote waone namna gani ya ku-order hivi vifaa wasirundike order kwa mtu mmoja. Kwa hiyo, naomba nilichukue hili tuende tukashulighulikie kwa kuwa nguzo zimefika maeneo mengi, basi vifaa vilivyosalia vifike ili kazi ikamilike na wananchi wapate huduma ambayo imekusudiwa.
Mheshimmiwa Spika, swali lake la pili nami nimshukuru kwa kufuatilia malipo ya fidia kwa wananchi wake na maeneo mbalimbali hususani katika mradi huu wa ujenzi wa njia ya umeme KV400 unaotoka Singida mpaka Namanga. Katika Wilaya yake kama alivyosema Serikali imeanza kulipa fidia, niishukuru sana Wizara ya Fedha kwa kutekeleza ahadi hiyo lakini amesema kuna variation. Naomba baada ya kikao hiki tukutane naye Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kushughulikia suala ambalo amelisema. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali yangu ya nyongeza naomba tu nimsahihishe Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tuna Kata ya Nangara na siyo Mangara lakini pia tuna Kata ya Bagara siyo Bagala, kwa hiyo nafikiri uta-capture hayo msahihisho. Naomba niulize maswali haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa mara ya kwanza niko disappointed kwa mara ya kwanza, hii ni essay siyo majibu na umenikumbusha wakti nipo Chuo Kikuu nilikuwa nikikosa jibu naandika the whole topic kama ni democracy and election naandika…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea…
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri haya uliyoandika ya Ziwa Jipe umeanzia Kenya, ukaja Ziwa Manyara kwanza lipo Mto wa Mbu hili andiko la Ziwa Manyara wala halihusiani na Babati na hakuna ulichojibu naomba sasa nikushauri; ni kwa nini usiongee na watu wa TANAPA watoe fedha, wasafishe Ziwa Babati kwa sababu sisi tuliomba mtupatie fedha wewe hapa hujasema unatupa fedha.
Sisi tunawalindia viboko wao, wanaua watu wetu, hakuna fidia basi nenda TANAPA wakupe fedha tusafishe Ziwa Babati otherwise msituachie Halmashauri sisi hatuna vyanzo hata ushauri huo naamini unaupokea. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea ushauri. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri bado anaona kwamba uchumi unakua wakati masoko ya wananchi ya mazao yao hayapo, hakuna annual increment kwa wafanyakazi, hakuna mazingira mazuri ya wafanyabiashara wetu kufanya biashara jambo ambalo limesababisha stress kwa wananchi na tumeshuhudia matukio ya watoto kuchomwa moto kwa upotevu wa Sh.2,000 na mwanafunzi kuuawa kwa sababu ya Sh.75,000…
Kwa nini bado anaona uchumi unakua wakati stress hizi zimesababisha matukio makubwa katika Taifa letu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini naamini uchumi wa Taifa unakua ni kwa sababu ya takwimu na hali halisi ya uchumi wetu ulivyo.
Napenda kuliambia Bunge lako tukufu na uniruhusu nisome kipengele hiki kwenye mkutano uliokwisha mwezi uliopita wa Wakuu wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) yalisemwa haya yafuatayo kuhusu uchumi wa Taifa letu, naomba kusoma, mkutano uliombwa ku-note that the majority of member states underperformed in achieving the agreed microeconomic indicators only three member states of SADC have attained that and all these three countries is Botswana, Lesotho and Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa Taifa letu unakua, watu wa nje wanaona kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Watanzania wanayaona na tupo imara tutaendelea kusimamia uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kumekuwa na kauli ya Serikali kwamba kila Halmashauri wapande miti 1,500,000 kwa ajili ya kuhifadhi mazingira yetu. Nafahamu Wizara hii, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Mazingira wanahusika na hawa wana mbegu za miti mbalimbali. Kwa nini msione umuhimu wa kutoa miti katika Halmashauri zetu hiyo 1,500,000 ili tuipande na kuhifadhi mazingira kwa sababu mkitegemea Halmashauri watoe fedha, wanunue hiyo miti Halmashauri zetu hazina fedha, kwa nini msitupe hiyo miti 1,500,000 tupande?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pauline Gekul, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa ni sera ya Serikali kuhakikisha kwamba Halmashauri zote nchini zinapanda miti angalau kila Halmashauri 1,500,000 lakini kumekuwa na upungufu wa miche ya kupanda. Hivi sasa kama Serikali tumechukua hatua kwa kutumia Wakala wetu wa Misitu kuhakikisha kwamba wanashirikiana na Halmashauri kwanza kwa kuwapatia mengi lakini katika maeneo mengi kuwapa miche ile ambayo tayari tumeshaiotesha ili kusudi zile Halmashauri ziende kufanya kazi ile ya kupanda katika maeneo mbalimbali. Siyo tu suala la kupanda lakini baada ya kupanda pia Halmashauri zihakikishe kwamba zinailinda ile miti na kuhakikisha kwamba kweli inakua sio tu inapandwa halafu inaachwa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza nimuambie tu Mheshimiwa Waziri hatuna kata ya singena tuna kata ya Singe. Lakini pia swali langu la msingi niliuliza vijiji vitatu ikiwemo Kijiji cha Chemchem Kata ya Mutuka ambayo pia haina mawasiliano.
Mheshimiwa Waziri swali la kwanza kama Halotel wameshindwa kwa nini sasa Wizara yako isifuatilie Kampuni nyingine weather Airtel au Vodacom waje waweke minara hiyo kwasababu mazungumzo haya ya Halotel ni tangu mwaka jana na hakuna kazi inayofanyika na hivi vijiji havina mawasiliano. Kwa nini usifuatilie hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Serikali miaka iliyopita mwaka juzi na mwaka jana wali-centralize makusanyo yanayotokana na makampuni haya ya simu ya service levy mwanzo halmashauri zilikuwa zinalipwa moja kwa moja tulikuwa tunakusanya Halmashauri lakini Serikali ilivyo-centralize makusanyo hayo walisema watatuletea kwenye Halmashauri zetu hadi hivi ninavyoongea Halmashauri zetu hawapati service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba ni lini Serikali watarudisha makusanyo hayo kwenye Halmashauri zetu maana wao ndio wanakusanya sasa halmashauri hatukusanyi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimemuelekeza Mheshimiwa Gekul kwamba tumeunda timu ya wataalam kuchunguza minara yote ya simu wala sio ya kampuni moja wapo ya Halotel au Tigo au Vodacom kuangalia uhakika wa mawasiliano kwa maeneo husika ambako imewekwa minara hiyo. Kwa hiyo, hii timu itakapotuletea taarifa tutaweza kujua tufanye vitu gani kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata mawasiliano ya kutosha. Namshauri Mheshimiwa Mbunge awe mvumilivu hiyo timu itatuletea majibu ambako tutaweza kupata mahala pa kuanzia kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala lake la pili kuhusu service levy haya masuala bado kwanza yanaanzia kwenye Halmashauri zetu ambapo sisi Wabunge ni Madiwani huwa mapato yakipatikana huwa yanapelekwa accordingly kutokana na mapatano kati ya halmashauri zetu na makampuni ya simu.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Naomba nifahamu huu Mradi wa Maji ambao ameutenga muda mrefu katika Wizara ya Maji wa Mji wa Mtwara na Mji wa Babati na uko kwenye ukurasa wa 71 kwenye Kitabu cha Mheshimiwa Waziri cha Hotuba; huu mradi wa bilioni sita; umekuwa hautekelezwi kwa muda mrefu sasa, kila mwaka anaweka kwenye bajeti lakini hizi fedha hatuzipati za Euro milioni 18.9. Naomba nifahamu ni lini fedha hizi zitapatikana ili Mji wa Babati na Mji wa Mtwara wapatiwe maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza fedha ipo, lakini kulikuwa na matatizo ndani ya Wizara yangu na wenyewe ni mashahidi naendelea kuyatatua yale matatizo. Fedha ipo tuliajiri Mhandisi Mshauri akafanya mchezo tumemwondoa, sasa hivi tumeweka Mhandisi Mshauri mwingine. Fedha hizo ni sawa na fedha za mradi wa Mgango Kyabakari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge huo Mradi wa Babati pamoja na Mradi wa Mtwara ambao unatumia fedha hiyo hiyo nahakikisha mwaka ujao wa fedha kazi ya kujenga miundombinu ya maji inaanza.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, haya matatizo ya ardhi yanasaidiwa na Mabaraza yetu ya Kata na Wilaya kufanya kazi, lakini tuna tatizo kubwa kwa Wenyeviti wetu wa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kuhudumia Wilaya zaidi ya mbili au tatu na wakati mwingine Wenyeviti hao mikataba yao imekuwa ikiisha lakini haiwi renewed kwa wakati. Kwa mfano, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Babati ambaye anahudumia Mbulu, Hanang na maeneo mengine mkataba wake umeisha muda mrefu na wananchi wanapata shida. Naomba nifahamu, ni lini mkataba wa Mwenyekiti huyu na Wenyeviti wengine mta-renew ili wananchi wapate haki zao kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, itakuwa si vizuri sana tukaliongea suala hili in blanket maana kuna kesi na kesi si kwamba Tanzania nzima mikataba haijakuwa renewed. Ingekuwa vizuri baada ya kumaliza kipindi hiki tukajua exactly ni nini ambacho kimetokea kwa kesi yake ambayo ameisema na ingekuwa ni vizuri na mimi nikalijua ili tujue namna nzuri ya kuweza kulitatua ili wananchi hao waendelee kuhudumiwa kama ipasavyo.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika jimbo letu la Babati Mjini tuna A – level moja (Babati Day) lakini Serikali walitupa mwongozo kwamba tutafute A – level nyingine na sisi halmashauri yetu tukapendekeza Sekondari ya Kwaangw’, Kata ya Maisaka. Mheshimiwa Naibu Waziri anapafahamu sana hapo maana anapita, tukawekeza nguvu zetu zote pale, sasa halmashauri haina vyanzo vya kutosha na A – level hiyo inatakiwa ianze mapema. Mheshimiwa Naibu Waziri Serikali sasa iko tayari kutuongezea nguvu ili hiyo sekondari ya A – level ianze mapema?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Wizara yetu ambayo Wabunge wametupitishia kwa ajili ya mwaka unaokuja tumetenga shilingi bilioni 168 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika taasisi mbalimbali za elimu kwa ngazi mbalimbali; kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu. Kwa hiyo, Wizara ina fedha za kusaidia ujenzi wa miundombinu. Tunachotaka kutoka kwenu Waheshimiwa Wabunge na mkiwa sehemu ya Mabaraza la Madiwani leteni maombi nasi tukijiridhisha kwamba kuna mahitaji hatutasita kuwasaidia. Kwa hiyo, nimshauri Mheshimiwa Gekul kwamba sisi tuko tayari kupokea maombi yenu lakini leteni kwa taratibu zilizowekwa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni vizuri Serikali kwa hili la mishahara na stahili za watumishi wakawa tu wakweli. Mfano zoezi la uhakiki limeathiri madaraja kutokupandishwa na watumishi wengine wakastaafu wakati Serikali inaendelea na uhakiki jambo ambalo limeathiri pensheni zao. Naomba nifahamu Mheshimiwa Naibu Waziri, hawa walioathirika na zoezi hili wakastaafu na pensheni zao zimeathirika Serikali inawafikiriaje ili walipwe stahiki zao kwa sababu wao hawakupenda hilo zoezi lifanyike na wao wameathirika sasa? Naomba nifahamu Serikali inasema nini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Gekul, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika zoezi kama hili ambalo lilifanyika mwisho wa siku lazima kutakuwepo changamoto mbalimbali ambazo zimejitokeza. Niseme tu, Serikali ambacho inaweza kukifanya ni ku-deal kwa case by case. Inapotokea mazingira kama hayo, Ofisi ya Utumishi iko wazi kwa ajili ya kujadiliana na kuona namna bora ya kuwasaidia watumishi hawa wameathirika na mpango wa Serikali wa uhakiki wa vyeti. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba bado nafasi ipo kwa wote ambao wamepitia katika mazingira hayo kufanya majadiliano na Serikali na kuona namna nzuri ya kuweza kurekebisha changamoto hiyo.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri alibahatika kufanya ziara katika Jimbo letu la Babati Mjini, nasi tukamuonesha jinsi gani tumeathirika baada ya vyanzo vyetu vya Halmashauri kuchukuliwa na Serikali Kuu. Hivi karibuni mliwaita Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri na Maafisa Mipango mkasema kwamba mtatupatia fedha na gawio letu lilikuwa shilingi milioni 900 kwa ajili ya kukamilisha vituo hivi na miradi mingine. Naomba nifahamu, fedha hizo shilingi milioni 900 zinafika lini Babati maana Vituo vya Singe, Mutuka na Sigino tumeshapaua, tunasubiri hela za finishing?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuliwaita Wenyeviti na Wakurugenzi ili waainishe vipaumbele katika maeneo ambayo yataenda kuanza kutumika pindi pesa itakapokuwa imepelekwa kule kwao na wakaainisha. Ofisi ya Rais, TAMISEMI zoezi lile tulishalikamilisha na tulishakabidhi Hazina. Ni matarajio yetu kwamba Hazina wakishakuwa na pesa ya kutosha kutoa, tutaweza kupeleka ili zikafanye kazi ambazo zilikusudiwa. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya chama changu kwa kuunganisha jimbo letu na miradi barabara ya lami. Tumeunganishwa na Arusha Dodoma na Singida lakini tuna kilomita 10 za lami ambazo zinaendelea na taa za barabarani zinawekwa. Kwa hiyo, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, huu mchakato wa kumpata Mhandishi Mshauri umechukua zaidi ya miaka mine. Naomba nifahamu Wizara yako ipo tayari kuwasiliana na African Development Bank ili huu mchakato ufike mwisho na wale wananchi wapate fidia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hizi barabara za lami zilivyopita mita 7.5 ziliongezeka tangu 2007 kwa mujibu wa Sheria ya Barabara lakini wananchi hao hawajafidiwa na wameshindwa kujenga nyumba zao. Naomba nifahamu kwa nini Serikali isipitie kanuni hii ya fidia muone wananchi hawa ambao wapo kwenye road reserve walipwe at least wale ambao wamejenga nyumba zao kwa sababu sasa wanashindwa hata kuzikarabati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda uniruhusu nitumie muda mfupi huu nimkaribishe sana Mheshimiwa Gekul upande huu. Nimpongeze sana kwa sababu anapigania kweli maendeleo ya Mji wa Babati. Nami namuahidi kwamba tutaendelea kushirikiana kama tunavyoshirikiana na Waheshimiwa Wabunge wote ili kuhakikisha kwamba maendeleo yanawafikia wananchi wetu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza ametoa ushauri, kwa hiyo, nikubali kuwa ushauri wake tutauchukua na tutaufanyia kazi. Kikubwa ni kwamba tunaendelea kushirikiana na wafadhili kwa sababu wamekuwa na imani na Serikali yetu na nimuahidi kwamba AfDB tutaendelea kuwasiliana nao ili kuhakikisha kwamba yale yote yanayohitajika kuweza kutekeleza mradi huu tunaweza kutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu fidia ya wananchi ambao walipisha eneo la mradi, nakubaliana naye kwamba tutaendelea kulitazama. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote tunaendelea kulipa kwa kasi na maeneo yote ambayo miradi inapita tutaendelea kufanya malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme kwamba jambo hili nimelichukuwa, nitaendelea kuzungumza na wenzetu ili tuweze kuhakikisha kwamba wale wanaostahili fidia wanalipwa kulingana na taratibu ambazo zipo. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Babati kwamba tutaliangalia suala lao kwamba wamepisha eneo la mradi na wanastahili kulipwa kama sheria inavyotaka.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuunipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza. Sisi Babati tuna ziwa ambalo lina viboko na wavuvi wanapokwenda kufanya kazi zao wamekuwa wakiuawa na viboko hao, lakini hakuna fidia. Tulipohoji pia, hata kwa Wataalam wa Halmashauri wanadai kwamba, wavuvi wanakuwa wamefuata viboko hivyo, hawastahili fidia. Naomba nifahamu Wizara inatusaidiaje ili kujua kwamba, wavuvi wa Babati na wananchi wale wanastahili fidia au la?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gekul, Mbunge wa Babati, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yapo matukio ya wananchi wa Babati kushambuliwa wao wenyewe na viboko, lakini pia mashamba yao kuharibiwa na mamba. Kimsingi wananchi wale wanastahili kupata fidia iwapo shambulio hilo litatokea nje ya eneo la makazi ya viboko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu ya sheria viboko hawa wanapokuwa katika eneo lao makazi
wanapomshambulia mtu inakuwa ni mtu ndiye aliyekwenda kuwavamia katika eneo lao. Nimhakikishie Mheshimiwa Gekul, iwapo kuna wananchi ambao malalamiko yao yapo na walishambuliwa nje ya eneo ambalo ni makazi ya viboko, Wizara yetu itachukuwa hatua ikiwa ni pamoja na kuagiza pia watu wa TAWIRI kufanya utafiti na kuona idadi ya mamba hao kama wanaleta tishio ili waweze kuvunwa.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada nzuri za Serikali kuwapatia wananchi maji, kuna mradi mmoja wa KfW wa tangu mwaka 2008 ambao ulikuwa uhudumie Mikoa saba ya Manyara, Babati, Mtwara, Kigoma, Lindi na maeneo mengine. Mikoa mingine mitano ilishapatiwa huduma ya maji bado Babati na Mtwara na tulikuwa tumepangiwa shilingi bilioni 20 na kila mkoa shilingi bilioni 10. Mpaka sasa mradi huu haujasainiwa na wenzetu wa Ujerumani pamoja na Serikali ya Tanzania. Naomba nifahamu ni lini mradi huu sasa utasainiwa kwa sababu tunahitaji hizo shilingi bilioni 10 zitusaidie kuondoa tatizo la maji Babati na Mtwara ambako kumesalia.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Babati na mimi nilishafika Babati pamoja na huu mradi mkubwa lakini zipo jitihada pale za utekelezaji wa mradi wa maji. Nataka nimhakikishie, kama tulivyoahidi tutatekeleza lakini tutalifanya hili jambo kwa haraka ili wananchi wake wa Babati waweze kupata maji safi na salama. Ahsante sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Mimi nina mambo mawili, la kwanza ni ombi, la pili ni swali.

Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza naipongeza Serikali. Hivi ninavyoongea leo, tangu siku ya Ijumaa na leo asubuhi Jumatatu watu wa KV 400 wako Babati eneo la Singu wakilipa wananchi fidia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ombi langu kwa Serikali, kwa kuwa kuna sintofahamu kati ya wananchi na Mwekezaji katika shamba la Singu, wananchi walikuwepo tangu miaka ya 1970, mwekezaji amepewa hati mwaka 2011 na wananchi wanalipwa asilimia 34 leo ya ardhi. Hebu niiombe Wizara ya Ardhi, ilitazame hili jambo upya, waone kati ya wananchi na mwekezaji, ni nani mvamizi, ili haki itendeke wale wananchi walipwe asilimia 100 ya ardhi.

Swali sasa kwa Wizara ya Nishati. Mheshimiwa Naibu Waziri, siyo wananchi wote wanaolipwa, leo wanalipwa tu Sigino pale, lakini mtaa wa Sawe, Maisaka Kati, Kijiji cha Kiongozi na Malangi, wao cheki zao hazijaandaliwa mpaka sasa. Naomba nifahamu, ni lini Wizara ya Fedha na Mipango nao watamaliza kukamilisha cheki hizi ili na hao wananchi waweze kulipwa? Maana mazao yao yameshafyekwa na mradi unaendelea. Ni lini cheki zao zitafika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo umesema, swali la kwanza ni ombi; lakini kabla sijaendelea, naomba nitoe pole kwa wakazi wa Mkoa wa Manyara, kufuatia kifo cha Meneja wa TANESCO wa Mkoa huo wa Manyara, pamoja na Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Mbulu ambao walifariki siku za hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, napenda nijibu hili swali la pili, ambalo Mheshimiwa Pauline Gekul ameuliza Mitaa ya Sawe, Mwaisaka Kati, Kiongozi, lini watalipwa fidia zao? Kwa kuwa Wizara ya Fedha ilifanya uhakiki na kukabainika baadhi ya changamoto na ikapelekea sasa kupeleka watathmini wengine ambao walifanya mapitio; hivi ninavyosema, jedwali jipya ambalo linawasilishwa kwa Ofisi ya Mtathimini Mkuu wa Serikali, limeshafika Dodoma na Mtathimini Mkuu wa Serikali yuko katika hatua za mwisho za kusaini na kisha malipo yataandaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake wa hili suala mara kwa mara, pamoja na wananchi wake. Nimwahidi tu kwamba, hili suala kwa kweli kwa kuwa amesema na yeye na sisi tumepokea pongezi, malipo yameanza kwa wakazi wa maeneo hayo ya Sawe, Mwaisaka Kati, Kiongozi, kwamba malipo yatafanyika siyo muda mrefu kuanzia sasa kama ambavyo jibu letu la msingi limesema. Ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Pamoja na Halmashauri zetu kufanya vizuri, kuna baadhi ya vyanzo hawafanyi vizuri. Mfano, chanzo cha Kodi ya Ardhi, mwanzoni walikuwa wakikusanya wanapata retention ya 30 percent lakini sasa hawapati retention hiyo ambayo ilikuwa inawasaidia kujaza gari mafuta waweze kufuatilia wale ambao hawalipi Kodi ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu: Je, Serikali iko tayari kuangalia upya chanzo hili ili kisaidie kukusanya kodi hii ya ardhi kwa asilimia 100?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Gekul kwa kazi nzuri anayoifanya kule Babati kuwasemea watu wa Babati, lakini pili, naomba nilipokee suala hili kama sehemu ya changamoto, tuwasiliane na Halmashauri ya Babati Mjini, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI tuone changamoto zilizopo tuweze kuziimarisha.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali na niishukuru kwa moyo wa dhati kwa kutusaidia kutujengea jengo kubwa la NFRA pale Babati kwa ajili ya kununua mahindi na kuyachakata. Bahati mbaya mwaka huu tangu Januari mvua hazinyeshi Kanda ya Kaskazini na hali si nzuri, hatuna maharage wala mahindi. Naomba nifahamu Serikali imejipanga vipi kwa ajili ya kukabiliana na hali hii ambayo wananchi wanakwenda kukabiliana nayo ya ukosefu wa mahindi na maharage ili wananchi wetu wapate mazao hayo kwa bei rahisi na wasiingie katika baa la njaa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mheshimiwa Gekul anataka kujua kwamba Serikali tumejipanga vipi katika kukabiliana na tishio la upungufu wa chakula nchini kutokana na ukame uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwanza tumetenga shilingi bilioni 15 kupitia Wakala wetu wa Taifa (NFRA) kwa kuendelea kununua mahindi kwa ajili ya kuyahifadhi kwa ajili ya kuja kuyasambaza au kupeleka sehemu ambazo zitakuwa na mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sasa hivi tumeshawaelekeza wataalam wetu wamesambaa nchi nzima kufanya tathmini ya kina kujua athari iliyoletwa na mabadiliko ya tabianchi hususan huu ukame ili kujua athari iko kiasi gani ili tuweze kuongeza mikakati mingine. Pia tumetenga zaidi ya shilingi bilioni tisa kupitia Bodi yetu ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuendelea kununua mahindi na mazao mengine kukabiliana na hali hiyo.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru umenipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru sana Wizara ya Mambo ya Ndani kutupatia fedha kujenga nyumba sita za askari pale Babati Mjini, kwenye Mtaa wa Bagala Ziwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la RPC katika Mkoa wetu wa Manyara liko Mtaa wa Komoto. Tangu mwaka 2006 liko kwenye lenta, miaka 13 sasa Wizara hamjatuletea fedha. Mmeweza kutuletea shilingi milioni 150 kazi inaendelea, ni lini sasa mtatuletea fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo la RPC pale Babati Mjini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pauline Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi kabisa kwamba jengo hilo linahitaji kukamilika. Tunayo majengo kadhaa nchi nzima ambayo yanahitaji kukamilishwa, siyo tu kwa Jeshi la Polisi, kwa upande wa Jimbo lake la Babati, nadhani atakubaliana nami hata jengo la Uhamiaji nalo linahitaji kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si dhamira ya Serikali kuona majengo haya yanafikia robo ama nusu kukamilika. Dhamira ya Serikali ni kuona majengo haya ambayo yametumia fedha nyingi na yana umuhimu mkubwa kwa ajili ya vyombo vyetu yakamilike haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo inatukabili ni fedha kwamba bajeti haitoshi kukamilisha majengo yote kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, pale ambapo hali ya kibajeti itakaa vizuri tutakamilisha majengo yote mawili ikiwemo la Polisi na Uhamiaji katika Jimbo lake pamoja na majengo mengine ambayo yanasubiri kukamilishwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kiasi ambazo zitaendelea kutatua changamoto hiyo. Kadri miaka inavyokwenda na hasa tukitilia maanani uchumi wa nchi yetu unakwenda vizuri sasa kutokana na kazi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, naamini kabisa miaka ya mbele tutakuwa na fedha za kutosha kuweza kukamilisha majengo yote ambayo hayajakamilika.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri Mradi wa Maji wa Kata ya Sigino, Mheshimiwa Waziri alifika mwaka jana akaahidi kwamba wataalam wake watafika ndani ya siku 10 ili ule mradi uanze.

Naomba nifahamu hawa watalaam watafika ili wananchi wale wapate maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya tukutane basi baada ya Bunge ili tuweze kukutana na wataalam wetu na kuweza kuwaagiza haraka wafanye kazi. Ahsante sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, swali la kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri, ukweli ni kwamba halmashauri nyingi hasa za Mijini wamesha exhaust karibia vyanzo vyote vya mapato. Sasa nilifikiri kwamba Serikali ingetusaidia kuweka mpango wa haraka kwa ajili ya nyumba za walimu.

Ni lini Serikali itaweka kwenye bajeti kuu fedha za ujenzi wa nyumba za walimu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili nishukuru kwanza Serikali ilitupatia fedha milioni 152 kwa ajili ya kukamilisha bweni la Sekondari ya Nakwa katika Halmashauri ya Mji wa Babati lakini ujenzi umefika katika upauzi bado finishing, niombe serikali itupatie fedha kwa sababu tatizo la vyanzo vya mapato kuwa vichache kati Halmashauri ya Kalenga ina fafana pia Halmashauri ya Mji wa Babati.

Ni lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya finishing ya bweni la Sekondari ya Nakwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli tungependa kuona nyumba za walimu katika maeneo ya jirani ili walimu wetu wasiweze kupata shida wnapotoa huduma na kuhudia vijana wetu katika maeneo mbalimbali na hasa Vijijini. Vilevile tungependa pia kuwa na mabweni ya kutosha kwa watoto wa kike ili kuwapunguzia majanga ya kupata mimba na wakati mwingine mazingira magumu kuplekea kufanya vibaya katika mitihani yao.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tuko kwenye bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha ya kukamilisha nyumba zaidi ya 364 katika maeneo mbalimbali, pia kumalizia mabweni na kumbi mbalimbali. Ningependa niseme tu kwa mfano fedha hizi ambazo zinazungumzwa hapa ambazo tungeweza mkopo ambayo wenzetu humu ndani wametuhujumu kwa kufanya hizi fedha zisiweze kuchelewa zingeweza kunufaisha vijana, watanzania wazalendo wenzetu zaidi ya milioni sita, tungeweza kujenga matundu ya vyoo kwenye mashule ya Sekondari, 1000, tungejenga matundu ya vyoo 2000 katika maeneo mbalimbali, kutengeneza kumbi za mikutano, mabwalo na hosteli mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naomba tu niseme katika jambo hili ni jambo la mkakati la pamoja Serikali, Waheshimiwa Wabunge na wadau mbalimbali tushirikiane tunapoona kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato wenzetu wanapokula kitumbua wasitie mchanga ili fesha ije katika eneo hili na watanzania wapate huduma kama ambavyo imetupasa kufanya, ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza, Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikiuliza mara nyingi katika Bunge hili vijiji vya Imbilili, Imiti na Chemchem kwamba havina mawasiliano na nimekuwa nikipatiwa majibu ya Serikali kwamba dawa ya tatizo hili ni kuongezea nguvu minara ya Voda na Airtel, lakini kazi hii haifanyiki naomba nifahamu ni lini sasa kazi hii itafanyika ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata mawasiliano.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, nampongeza sana Mbunge kwa sababu tumeongea mara nyingi sana kuhusu changamoto za jimbo lake Mheshimiwa Mbunge na sisi tumejipanga. Kama nilivyozungumza juzi kwamba katika mradi huu wa Awamu ya IV ya kupunguza changamoto ya mawasiliano tunazo kata mia tano 21 na vijiji 1222 ambavyo viko kwenye mpango. Nimuombe tu Mheshimiwa Gekul kwa sababu kile kijitabu ninacho hapo baadaye tuwasiliane ili tupitie kwa pamoja uweze kuona namna tulivyojipanga kutatua changamoto za mawasiliano katika eneo la kwako na tutaendelea kufanya hivyo mpaka wananchi waweze kuwasiliana vizuri katika maeneo yao ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu kwamba zao la mbaazi lilipata soko hivi karibuni kidogo ilipanda kutoka shilingi 150/= ya mwaka jana mpaka shilingi 900/=, lakini imeanza ku-drop. Tatizo kubwa ni kwamba msimu wetu unapokuwa unaanza, wale ambao wanatupa soko kama India, Pakistan, na nchi nyingine wao kule msimu ukianza huku kwetu zao hilo linakuwa haliuziki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu sasa mkakati wa Serikali kusaidia wananchi wetu ili waendane na msimu wa nchi ambazo wanatumia zao hili kwa sababu hatuna soko la ndani sisi wenyewe.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba inapofika baada ya Oktoba bei ya mbaazi huanza kushuka na sababu moja, unakuta kwamba quarter yetu inakuwa imekaribia kwisha wakati nchi nyingine zimeanza kuzalisha. Kwa hiyo, kama Wizara ya Kilimo, tunachokifanya cha kwanza ni kujaribu kuwahamasisha wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitumie nafasi hii kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara na hasa wanaonunua mazao ya mbaazi. Katika kipindi cha Septemba na Agosti, kipindi hiki bei ya mbaazi na demand yake inakuwa ni kubwa. Niwashauri kwamba, ni kipindi cha kutoa stock na kuuza kabla ya production ya upande mwingine haijaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sisi kama Wizara tunafanya jitihada kuongea na masoko kama ya India ili kuongeza quarter na volume ambayo tunahitaji. Yapo mazao ambayo mpaka sasa hatuko tayari kuyaingiza katika mfumo wa Stakabadhi Ghalani likiwemo mbaazi ili kuruhusu free trade iweze kuchukua nafasi yake na kwa sababu kuna sensitivity ya bigger consumer wa dunia vilevile ndio wazalishaji wakubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapunguza bureaucracy kuruhusu watu waendelee kufanya hii biashara. Pia Wizara tunaendelea kufanya jitihada kuongeza quarter ya ku-export mbaazi, lakini nasisitiza mwezi wa Nane na wa Tisa tunapata bei nzuri, wakulima na wafabiashara wanaouza mbaazi hakikisheni mnauza mbaazi hizo wakati ambapo bei imefika juu. Ilifika mpaka shilingi 900/= na kuna maeneo ilifika mpaka shilingi 1,000/=. Mkiendelea ku-hold stock, Oktoba na Novemba tunaelekea duniani ambao wanazalisha na wenyewe wanakuwa wameingiza sokoni. Kwa hiyo, competition inakuwa kubwa na bei inaanguka.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Waziri nikushukuru pia kwa majibu ya Serikali ambayo ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza Mheshimiwa Waziri, Serikali haioni kwamba sasa badala ya barabara hii inayotoka Babati mjini hizi kilomita 20 kuendelea kuwekewa fedha za maintenance, ni vizuri wakatenga fedha za kuweka lami hizo kilomita 20 hadi lango la Tarangire ili watalii wanapofika Babati wasafiri vizuri mpaka hapo Hifadhini kuliko ambavyo sasa ni rough road.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Swali la pili miongoni mwa vitu ambavyo vinachochea utalii wetu ni pamoja na miundombinu mizuri barabara pamoja na viwanja vya ndege uwanja wetu wa Mkoa wa Manyara ambao uko pale Magugu sasa haujawahi kutengewa fedha na watalii wamekuwa wakilazimika sasa watue Arusha na watembee umbali mrefu.

Je, Serikali iko tayari kututengea fedha haraka iwezekanavyo kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Manyara ili watalii waweze kufika mapema hifadhini Tarangire?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI MAWASILIANO NA UCHUKUZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu barabara hii ya Babati kwenda Tarangire kwenye lango niseme iko kwenye mipango na sasa kama kinachofanyika ni kuhakikisha kwamba inakuwa vizuri ndiyo maana Bunge lako imetutengea fedha kwa ajili ya kufanya maboresho makubwa ili kuondoa usumbufu kabisa ili wananchi wakati tunafanya harakati za ujenzi watalii waweze kupita bila shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege kwanza niipongeze Serikali ya mkoa, kupata eneo hili la Mbuyu wa Mjerumani kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege na nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla ni kwamba Wizara yangu kupitia TIA inaendelea na usanifu ili sasa tuweze kujua namna uwanja utakavyokuwa na gharama zake na hatimaye tuweze kujenga uwanja huu wa ndege. Ahsante sana.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Waziri Gereza la Babati linadaiwa na BAWASA shilingi milioni 182 bili za maji hawajawahi kulipa, maana yake wafungwa wanavyokuwa wengi na matumizi ya maji yanakuwa mengi, muda mrefu watu wa BAWASA wamedai sana hiyo bili milioni 182.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu ni lini Serikali italipa deni hili la Gereza la Babati kwa BAWASA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima nikiri kwamba taarifa za hilo deni ndiyo nazipokea hapa, kwa hiyo ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kujibu maswali tutafuatilia tuweze kujua ni kwa nini deni hilo halijalipwa na ili tuweza kuangalia utaratibu wa kuweza kulipa pale ambapo tutakuwa tumepata kasma ya ulipaji wa madeni kama tunavyofanya katika magereza mengine nchini.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza nikushukuru kwa kutupatia zile 150,000,000 ambazo zimetusaidia kujenga majengo ya polisi katika eneo la Bagara Ziwani na nyumba zinakamilika.

Mheshimiwa Spika, sasa eneo hilo halijawahi kufidiwa, wananchi hawajawahi kufidiwa tangu 2004, polisi wanajenga majengo yao, wananchi hawajalipwa fidia tangu 2004. Nini kauli ya Serikali juu ya wananchi hawa ambao wametoa eneo kwa polisi lakini hawajapatiwa fidia mpaka leo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tunachukua pongezi kama Serikali kutokana na kazi ambayo inaendelea nchi nzima maeneo mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za askari polisi.

Mheshimiwa Spika, la pili nimpongeze yeye binafsi kwa kufuatilia kwa karibu hii kadhia ya wananchi wake kutolipwa fidia. Hata hivyo, naomba nimhakikishie kwamba jambo hilo nimelichukua na tutalifanyia kazi na baadaye tutarudi kwake kuweza kumpatia majibu ya hatua ambazo zimefikiwa na changamoto gani kama zipo na nini mikakati ya Serikali katika kukabiliana na changamoto hizo ili hatimaye wananchi hawa waweze kupata fidia stahiki.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Ninavyofahamu mimi, service levy haichajiwi kwa mfanyabiashara mmoja ambaye amefungua duka lake na amelipa leseni na kodi ya mapato, lakini wafanyabiashara wadogowadogo kwenye baadhi ya Halmashauri wanachajiwa service levy, nini kauli ya Serikali juu ya hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pauline Gekul, Mbunge wa Babati Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli, ulipaji wa kodi ni kwa mujibu wa sheria na taratibu na sheria zipo na wasimamizi wanatakiwa kufuata taratibu hizo. Sasa Mheshimiwa Mbunge kama kuna maeneo ambayo watu wanachanganya analipa service levy ambayo imeelekezwa na bado anatozwa kodi nyingine, nafikiri tupate maelekezo yake na taarifa muhimu tuweze kulifanyia kazi.

Hata hivyo, kodi italipwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na sheria ipo, tunaomba hao wote wanaosimamia jambo hili watende haki na wasikilize watu na kutoa elimu ya umma. Ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri yana ukakasi barua aliyoiandikia TANROADS Mkoa wa Manyara alimwandikia meneja kwamba kwa kuwa wananchi hawa wamekaa zaidi ya miaka mitano wakipisha eneo hilo wale wanaodhani wameathirika na wanahitaji fidia wapeleke majina yao ili wazingatiwe katika fidia, leo ananiambia fidia hii imesitishwa, imesitishwa lini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa jambo hili limegusa nusu nzima ya wananchi wa Jimbo la Babati Mjini maana yake ni mchepuo wa Singida, Dodoma na Arusha, lile jimbo lote. Naomba busara yake kwa nini yeye au Mheshimiwa Waziri wasiwatembelee wananchi wa Jimbo la Babati Mjini ili jambo hili liishe kwa amani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, njia iliyokuwa imependekezwa kwa kuwa imesitishwa, lakini kama alivyosema Mbunge, Sheria ya Utoaji Ardhi, Sura ya 118(19)(1) kimeelezea taratibu za namna ya ku-deal na suala kama hili pale ambapo wale uliokuwa umewasimamishia ama umewasababishia usumbufu unatakiwa ufanye. Kwa hiyo taratibu hizo zimeainishwa kwenye hiyo sheria na zitafuatwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Wizara kutembelea tuko tayari kwenda kuangalia, lakini pia nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba nia ya Serikali siyo kutoa usumbufu kwa wananchi, nia ya Serikali kimsingi ni kuwapelekea maendeleo, kuwatengenezea miundombinu bora. Ndiyo maana baada ya kuona tutavunja nyumba nyingi, lakini pia kwa mji ulivyopanuka, barabara iliyokuwa imependekezwa ni kama inaenda sambamba na barabara iliyopo, kwa hiyo tunaona tufanye jambo kubwa zaidi kuliko hili ambalo lipo. Kwa hiyo, nia si kuwasumbua na kama watu watakuwa na haki kwa kutumia hii sheria haki yao watapewa. Ahsante. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais na Serikali kutupatia fedha hizi zaidi ya bilioni 17 kwa ajili ya ujenzi huu naamini utakamilika. Nina swali moja tu, Mji wa Babati ni Makao Makuu ya Mkoa tuna uhitaji mkubwa wa ujenzi wa soko kuu. Je, Serikali iko tayari kututengea fedha kwa ajili ya soko kuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Mji wa Babati ni mji ambao unakua haraka, lakini una uhitaji mkubwa wa soko. Mheshimiwa Mbunge Gekul amefuatilia mara nyingi sana Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuona namna ambavyo wananchi wa Babati Mjini wanapata Soko Kuu. Ninaomba nimhakikishie tu kwamba tulishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wetu wa Miji na Halmashauri kuweka vipaumbele katika ujenzi wa masoko, lakini pia kuandika maandiko maalum kwa ajili ya maombi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa masoko hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI nimwelekeze Mkurugenzi wa Hamalshauri ya Mji wa Babati waandike andiko la mahitaji ya soko hilo na kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuingizwa kwenye miradi ya kimkakati ili itafutiwe fedha kwa ajili ya ujenzi. Ahsante. (Makofi)