Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Khadija Hassan Aboud (7 total)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, baada ya ushahidi kutolewa na mhukumiwa kupata adhabu, je, kuna mikakati gani au mipango gani inayochukuliwa kuwasaidia hawa watoto hasa wa jinsia ya kiume ili kuwaepusha na unyanyapaa pia kuathirika kisaikolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali namba mbili; naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ni hatua gani zinachukuliwa kuharakisha kesi hizi za udhalilishaji wa watoto ili kuepusha kukosekana au kupotoshwa kwa makusudi ushahidi na vielelezo muhimu na pia kwa sababu mtoto huyu anakuwa mdogo kupoteza kumbukumbu zake yeye mwenyewe binafsi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali la kwanza kwamba baada ya ushahidi kukamilika na hatua za kisheria kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na Mahakama dhidi ya mtuhumiwa, nini kinafanyika kwa mtoto aliyeathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtoto aliyeathirika na familia yake kwa ujumla kwa utaratibu wa kitaalam uliopo kwa sasa huchukuliwa na kurudi kwenye familia yake, pia huunganishwa na wataalam wa kutoa ushauri nasaha katika vituo vyetu mbalimbali vya kutolea huduma za afya. Anaweza akaunganishwa na Wataalam wa Ustawi wa Jamii ili aweze kurudi kuwa katika hali yake ya kawaida, lakini pia ataunganishwa na Wataalam wa Saikolojia na Wanasihi aweze kujengewa confidence ya kuweza kurudi sawa kama alivyokuwa zamani kabla hajafanyiwa vitendo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwamba ni nini Serikali inafanya. Serikali ina mikakati mingi ikiwemo hiyo kwanza kuwa na Sera ya Kuwalinda Watoto ya mwaka 2008, pili Sheria na tatu kuwa na utaratibu mahsusi wa kuweza kutoa ulinzi kwa watoto. Kwa maana hiyo, sasa hivi tunakwenda kukazia kwa kutunga sheria nyingine ya kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, nataka kuongeza kwenye sehemu ya pili ya swali la Mheshimiwa Khadija Aboud kwamba, mikakati ya Serikali ni ipi katika kuhakikisha kesi hizi za udhalilishaji dhidi ya watoto zinaharakishwa. Tumeanza majadiliano na wenzetu wa Mahakama kwamba sasa Mahakama iwe na vipindi maalum ambavyo Mahakama itakuwa inasikiliza kesi tu za udhalilishaji dhidi ya watoto na wanawake.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na mawazo kwamba tutengeneze Mahakama Maalum za Watoto, lakini tumeona hapana, tunaweza tu tukawa katika kipindi fulani cha mwaka Mahakama inakaa na kusikiliza kesi za udhalilishaji wa watoto, maana yake tutaweza kuhakikisha wabakaji na walawiti wa watoto wote wanachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nawapongeza Wizara kwa juhudi zao za kuwasaidia wakulima wetu. Pamoja na majibu yaliyojitosheleza suala langu, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wamehamasika sana kulima kilimo cha pamba, nauliza Serikali ni kwa nini haioni umuhimu wa kuanzisha soko huria la uzalishaji wa mbegu bora ili kumrahisishia na kumpa unafuu mkulima wa pamba na kuachia kampuni moja tu ya Quton ambayo inazalisha mbegu hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na majibu ya Serikali, pamba imehamasika sana na kwa wastani tani 600,000 itazalishwa na itakuwa sokoni. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha pamba yote iliyozalishwa inanunuliwa ili kuwaondolea usumbufu wakulima wa pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba nichukue fursa hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Khadija Aboud kwa maswali yake mawili ya nyongeza na vilevile kuwa makini katika kufuatilia kilimo ambacho ni mojawapo ya zao la mikakati kilimo cha zao la pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake ya msingi (a)na (b) swali la (a) amezungumzia kuhusu Kampuni ya Quton ambayo ndio imekuwa iki-dominate katika kufanya biashara hii ya pamba.
Naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli Kampuni hii ya Quton ilikuwa imeshinda tender, lakini katika kushinda tender yenyewe ilikuwa inafanya tu ...ginnery na kwa maana ya kwamba ilikuwa inafanya mbegu zile za kunyonyoa tu halafu inapeleka kwa ginners. Sasa baada ya Serikali kuona mapungufu hayo ikawa imefuta ile tender na ikaamua kuweka soko huria kwa ginners ili wao waweze kuwa wanafanya biashara moja kwa moja na wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wakulima wote wa zao la pamba ambalo ni zao la kimkakati kwamba kuanzia sasa hivi zao la pamba litakuwa linafanyika katika soko huria bila kujali kwamba ni nani anafanya hiyo biashara. (Makofi)
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nina swali dogo kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha katika Halmashauri zote hawa mawakala wa maji, pre-paid meter ili kuepusha wananchi kubambikiziwa bili na kuepusha wananchi au taasisi kutokulipa bili za maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Wizara ya Maji ni katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na mpango wa kisasa kuwa na pre-paid meter. Mpaka sasa Mheshimiwa Waziri ameshaziagiza mamlaka hizo zifungwe na mpaka sasa zipo mamlaka saba ambazo zimeshaanza kutekeleza mradi huo. Kwa zile mamlaka ambazo bado hazijatekeleza lazima watekeleze katika kuhakikisha tunaondoa tatizo hilo.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kutia moyo lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kuna minara imejengwa katika Kata ya Mapanda, Kijiji cha Mapanda na Kata ya Ikweha Kijiji cha Ikweha, lakini mpaka nauliza swali hili hakuna mawasiliano na Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa ameonana na Mheshimiwa Waziri wa Mawasiliano. Je, ni lini watapata mawasiliano katika kata hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili yuko tayari kwenda katika Kata ya Mapanda, Ikweha, Mpangatazara, Ihanu kujionea mwenyewe matatizo ya mawasiliano yanayowapata wananchi wa maeneo hayo? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khadija, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba kuna baadhi ya minara ambayo imewekwa lakini haijaanza kutoa mawasiliano kutokana na sababu mbalimbali. Sababu ya kwanza inaweza ikawa kutokuwepo umeme eneo hilo na wakategemea kutumia solar ambapo kama kunatokea hali ya mawingu, basi zile solar haziwezei kupeleka umeme wa kutosha kwenye minara na hivyo kusababisha wananchi kutokuwa na mawasiliano. Sababu nyingine ni za kijiografia. Hivyo, nawaelekeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote watembelee eneo alilolitaja Mbunge kuhakikisha kwamba wanatambua chanzo cha sababu ya minara hiyo kuwepo lakini haitoi mawasiliano. Nami nitafutilia kuhakikisha kwamba minara yote ambayo imewekwa na haina mawasiliano basi inaanza kupeleka mawaliano kwa wananchi kwa kuwa ndiyo lengo kuu la Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, niko tayari baada ya Bunge hili na nimeshaahidi hata Wabunge wengine kwamba nitafanya ziara ya miezi miwili na timu yangu ya watu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha tunatambua maeneo yote ambayo hayana mawasiliano tuweze kuyapatia mawasiliano. (Makofi)
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu haya ya Serikali, pia nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kusaidia mashirika haya ya Kiserikali na kuyawekea utaratibu mzuri. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Taasisi Zisizo za Kiserikali, Ofisi za Mrajisi wa Mashirika hayo kati ya Zanzibar na Tanzania Bara wana ushirikiano mzuri na ushirikiano wa pamoja, lakini kuna changamoto moja. Taasisi zisizo za Kiserikali zinapotaka kufungua upande mmoja wa Muungano aidha Bara au Zanzibar taasisi hizo zinalipishwa sawasawa na taasisi za kigeni zinapotaka kufungua Mashirika ya Kiserikali hapa Zanzibar.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto hiyo ili mashirika yetu ya kiserikali ya Zanzibar na Bara yasiwe yanalipishwa sawasawa na taasisi ambazo zinatoka nje ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Taasisi Zisizo za Kiserikali zimekuwa zikitoa mchango mkubwa sana katika kuinua mchango wa nchi na uchumi wa wananchi, zimekuwa zikisaidia sana kutatua baadhi ya changamoto mbalimbali za kusaidia jamii na huduma mbalimbali za kijamii. Je, Serikali inatambua vipi mchango huo wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika,
kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu sana wa utendaji wa Wizara yetu ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na hususan masuala haya ya NGOs. Niseme tu kwamba kwa mujibu wa sheria tuliyokuwa nayo sasa hivi ambayo inasimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni sheria ambayo si ya Muungano, kwa maana kwamba Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Serikali Tanzania Bara ni tofauti na yule ambaye yuko kule Zanzibar. Hata hivyo, tunatambua kwamba kuna NGOs nyingi hapa nchini ambazo zinafanya kazi Tanzania Bara na vilevile Tanzania Visiwani.

Mheshimiwa Spika, changamoto ambayo ameeleza Mheshimiwa Mbunge tunakiri kwamba tunayo, lakini sisi kama Serikali tulishaanza kuchukua hatua, Msajili wa Mashirika Yasiyo Serikali Tanzania Bara pamoja na kule Zanzibar wamekuwa wakifanya vikao. Kikao cha kwanza walikifanya mwezi Septemba na Disemba mwaka jana wamekaa tena na kuweza kuweka utaratibu mzuri ambapo Taasisi ama NGOs ambazo zinafanya kazi Tanzania Bara zinaweza zikapata unafuu wa kuweza kufanya kazi Zanzibar na zile za Zanzibar zinaweza zikafanya kazi Tanzania Bara wakati marekebisho ya sheria yakiendelea ili kuweza kuweka utaratibu mzuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili ameuliza kuhusiana na mchango wa NGOs. Tulipofanya marekebisho ya Sheria ile ya NGO’s, lengo na mahususi lilikuwa ni hilo, kwa sababu kwanza kulikuwa kuna mkanganyiko mkubwa sana wa usajili wa NGOs, kulikuwa kuna NGOs ambazo zilikuwa zinasajiliwa chini ya Msajili wa NGOs na kulikuwa kuna NGOs ambazo zilikuwa zinasajiliwa BRELA, kulikuwa kuna NGOs ambazo zilikuwa zinasajiliwa kwa Msajili wa Societies. Usimamizi na mchango ilikuwa ni mgumu sana kuuratibu, lakini kwa utaratibu huu mpya sasa hivi ambao umeuhisha usajili wa NGOs, sasa hivi tutaweza kujua mchango wa NGOs zote takribani 10,000 ndani ya nchi na sisi kama Serikali tutakuwa tunautambua na kuuthamini mchango huo katika taarifa zetu mbalimbali za Serikali.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Watanzania tuna shauku kubwa;

Je, ni lini reli yetu ya kisasa ya mwendokasi itaanza kutoa huduma kwa wananchi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Reli hii ya mwendokasi (SGR) kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro, kilometa 300 itaanza kutoa huduma mwezi wa saba. Hivi sasa mwezi huu wa sita tunategemea kupokea mabehewa yenye ghorofa na hatimaye mwezi wa saba tutapokea kichwa. Na kwa kuwa tayari miundombinu yote testing na kila kitu kimeshafanyika katika njia hii ipo tayari kwa ajili ya kuanza mara baada ya mabehewa haya yatakayoingia mwezi huu wa sita na vichwa vitakavyoingia mwezi wa saba.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza naipongeza Serikali katika kuhamasisha kilimo na huduma za ugani suala langu Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imenunua pikipiki kwa ajili ya Maafisa Ugani, lakini bado pikipiki hayo hayajagawiwa ili kuepusha uchakavu, ni lini Serikali itayagawa pikipiki hizo kwa walengwa ili yakafanya kazi kwa wakulima? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Hassan Aboud kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli bajeti ya Wizara ya Kilimo na hasa katika eneo la huduma za ugani, imeongezeka kutoka shilingi milioni 600 mpaka shilingi bilioni 15 kwa ndani ya miaka miwili kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya na ndani ya bajeti hiyo pia na sisi tulinunua vifaa kwa maana ya pikipiki, kwa ajili ya kuwapatia Maafisa Ugani.

Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba zilikuwepo na taratibu za ndani za kuzifuata ambazo zimekamilika na kuanzia jana zoezi la usambazaji pikipiki limeanza, jana Mkoa wa Dodoma wamechukuwa pikipiki 264, leo Singida watachukuwa 161 na kesho kutwa Tabora na maeneo mengine wataendelea kuzichukuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nikuondoe hofu pikipiki zile ndani ya muda mrefu zitaondoka eneo hilo ili ziweze kuwafikia Maafisa Ugani.