Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Leah Jeremiah Komanya (53 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu jioni hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kuchangia, naomba niwashukuru akinamama wa Mkoa wa Simiyu walioniwezesha kuingia katika Bunge hili. Pia, naomba niwashukuru wananchi wote wa Mkoa wa Simiyu waliokichagua Chama cha Mapinduzi nafasi ya Ubunge kwa asilimia mia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyofanya kazi ya kutumbua majipu. Wananchi wa Simiyu wana imani na Serikali na wanaiunga mkono. Hii imejidhihirisha katika ziara ya Waziri Mkuu aliyoifanya mapema mwezi wa Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo naomba niombe yafuatayo katika bajeti ya mwaka huu. Mkoa wa Simiyu ni mpya una changamoto nyingi na changamoto moja ni ukosefu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Wananchi wanalazimika kusafiri umbali wa kilomita zaidi ya 100 wakifuata huduma hiyo Mkoa wa Shinyanga ama Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali katika bajeti yake ya mwaka 2015/2016, ilitoa fedha kidogo kwa ajili ya uanzishaji wa jengo la mapokezi. Naomba katika bajeti hii pia Serikali itenge fedha za kutosha ziweze kujenga hospitali hiyo na iweze kukamilika na kuanza kutumika. Hospitali hii itasaidia kuondokana na tatizo la mama wajawazito wanapopata dharura za kujifungua kusafiri zaidi ya kilometa 100 na hali barabara zetu zikiwa na ubovu hasa katika kipindi cha mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuharakisha maendeleo katika uchumi wa viwanda pamoja na maandalizi mengine ni vyema Serikali ikaona haja sasa ya kuandaa mafundi mchundo wa kutosha ambao watahitajika kwa wingi katika viwanda vyetu. Mafundi hao wanaandaliwa na VETA zilizopo katika wilaya na mikoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa masikitiko yangu, Mkoa wa Simiyu hauna Chuo cha VETA hata kimoja katika wilaya ama mkoa kwa ujumla. Naomba Serikali kupitia bajeti hii iweze kuuona Mkoa wa Simiyu ili hata vijana wetu waweze kupata mafunzo ya ufundi stadi ambayo pia yatawasaidia kujiajiri wenyewe. Pia chuo hicho kitaweza kusaidia kutoa ushindani katika kazi ambazo sasa halmashauri zinapaswa kutenga 30% ya kazi za zabuni kwa ajili ya vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naiomba Serikali katika kufanya uchaguzi wa wanafunzi wanaoenda kidato cha tano kuwepo pia na uchaguzi wa wanafunzi watakaokwenda katika vyuo vya VETA. Hii itasaidia kuwepo na uhakika na wanafunzi katika vyuo vya VETA, pia itasaidia kuondoa ile dhana kwamba wanaoenda VETA ni wale waliofeli kuendelea na kidato cha tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie upande wa nishati ya umeme. Ni dhamira ya Serikali kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika unaokidhi mahitaji na wenye gharama nafuu ili kusukuma mapinduzi ya viwanda kwa kasi zaidi. Wilaya ya Meatu iko nyuma sana katika usambazaji wa umeme wa vijijini wa REA ukilinganisha na maeneo mengine. Wilaya ya Meatu ina vijiji 109 na Majimbo mawili, lakini ni asilimia 19 tu ya vijiji vilivyopata umeme. Niiombe Serikali yangu sikivu iangalie kwa jicho moja Wilaya ya Meatu iweze kusambaziwa umeme huo wa REA. Umeme huo utawasaidia wanafunzi wetu tunaowaandaa kuweza kujisomea vizuri na kuepukana na vibatari wanavyotumia. Umeme pia utawasaidia wananchi wetu waweze kununua mashine za kukamua alizeti na kuweza kujipatia kipato na kujikwamua kutoka katika umaskini tulionao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie kuhusu upatikanaji wa maji salama. Natambua Serikali katika Mpango huu wa Miaka Mitano imepanga kuleta maji kutoka Ziwa Viktoria kwa kupitia Wilaya ya Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu lakini maji haya yata-cover vijiji vilivyo ndani ya umbali wa kilomita 12. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Simiyu una changamoto ya upatikanaji wa maji. Kuna ukanda ambao unahitaji mabwawa kama vile ukanda wa Meatu. Tunaomba Serikali kwa maeneo ambayo hayatafikiwa na Mradi wa Maji toka Ziwa Victoria, ichimbe mabwawa zaidi katika Wilaya ya Meatu kuliko visima vya maji ambavyo vinakauka wakati wa kiangazi. Hata maji hayo yakipatikana huwa ni ya chumvi. Kanda zingine kama za Itilima, Kisesa, Bariadi, Busega, Maswa Serikali iendelee kuchimba visima virefu kwa ajili ya upatikanaji wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono sana hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda huu niliopewa naomba nijikite zaidi katika mazingira na nitajikita katika mazingira hususan katika Mkoa wa Simiyu. Ni dhahiri kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi zinaongeza uwezekano wa kaya kuendelea kuishi katika umasikini. Umasikini huu utaendelea kuongezeka kwa miaka ijayo, hususan kwa mwanamke ambaye ni mkuu wa kaya kama hatua mathubuti na endelevu za kukabiliana na athari za tabianchi hazitachukuliwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanamke wa Mkoa wa Simiyu amekuwa akikabiliana na njia mbalimbali katika kukabiliana na athari ya tabianchi. Mwanamke amekuwa akijishughulisha katika kilimo cha umwagiliaji ambacho ni kidogo na hakina tija. Nikiongelea Wilaya ya Busega, Kata za Kiloleni, Nyashimo, Kabita, Kalemela, kata hizi ziko kandokando ya Ziwa Victoria lakini mwanamke anatumia ndoo kumwagilia katika kilimo chake ambacho hakina tija. Niendelee kuiomba Serikali, itakapoanza kutekeleza mradi wa maji ya Ziwa Victoria, na ninaamini utekelezaji wa mradi huu uko chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, basi itenge maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili iweze kumsaidia mwanamke huyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiongelea Kata ya Gambasingu, Wilaya ya Itilima na Kata ya Mwashata, Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu, wanawake wanatumia ndoo kumwagilia maji kutoka Mto Simiyu ambapo kilimo hicho kinakuwa hakina tija. Niiombe basi Serikali kupitia hizi asilimia tano ama shilingi milioni 50 zikianza kutolewa kwa kila kijiji, zianze na Mkoa wa Simiyu ili wanawake waweze kukopesheka na kuweza kununua pampu ambazo zitawasaidia katika umwagiliaji na hivyo waweze kukabiliana na athari ya tabianchi, ikiwemo pia na Kata ya Mwamanimba iliyopo katika Jimbo la Meatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, njia nyingine wanazotumia wanawake kuweza kukabiliana na athari hizi ni kufanya biashara ndogo ndogo; lakini changamoto wanayoipata ni ukosefu wa mtaji pamoja na kujengewa uwezo. Halmashauri hutenga asilimia tano katika bajeti yake kwa ajili ya kuwawezesha wanawake, lakini fedha hizi zimekuwa hazitolewi, zinabaki kwenye makaratasi tu. Niombe basi kuwe na msukumo wa utekelezaji wa utoaji wa fedha hizi, hata kupitia vikao vya RCC iwe ajenda mojawapo ya kufuatilia utekelezaji wa asilimia tano kwa ajili ya akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine, wanawake…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante,
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia katika Bajeti ya Serikali na Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inaiyofanya ikiwemo ukusanyaji wa mapato. Serikali imekuwa ikikusanya mapato vizuri tumeona na mpaka sasa imeshafikia zaidi ya asilimia 100 ya ukusanyaji wa mapato yanayotokana na kodi. Changamoto ninayoiona ni ule upelekaji wa fedha katika Halmashauri mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu cha mkaguzi alichokisoma cha hesabu za mwaka 2014/2015 tumeona upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo katika Halmashauri tatu zilipelekwa zaidi kuliko fedha zilizoidhinishwa na Bunge. Halmashauri moja imepelekewa fedha za miradi ya maendeleo zaidi ya asilimia 56 nyingine kwa zaidi ya asilimia 59 na nyingine kwa zaidi ya asilimia 63. Ukiangalia maeneo mengine pia tunayo miradi inayopaswa kutekelezwa, tuna maboma ya zahanati ambayo hayajakamilika, tuna miradi ya maji ambayo haijakamilika. Hata ukiangalia fedha za mwaka huu kwa namna tulivyokusanya ukiangalia ofisi ya CAG ambayo ndiyo inayokagua na kudhibiti matumizi ya fedha ilipelekewa fedha kwa asilimia 52 za ruzuku ukilinganisha na idara nyingine zikiwemo na Wizara zimepelekewa fedha zaidi ya asilimia 100, nyingine asilimia 117, asilimia 125, asilimia 124, sijui ni kigezo gani kinachotumika kupeleka fedha. Naishauri Serikali izingatie uidhinishaji wetu wa Bunge tunavyoidhinisha isitumie fedha nje ya bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu kwa mwaka huu imeonekana kupunguziwa fungu lake na ukiangalia Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo tumetoka asilimia 26 na sasa tumeweka asilimia 40 ya fedha ya miradi ya maendeleo. Ofisi ya CAG inatakiwa iwezeshwe kikamilifu ili iweze kutekeleza majukumu yake. Kwa mwaka uliopita CAG alishindwa kukagua miradi ya maendeleo ya vijijini, aliishia ngazi ya Halmashauri, tukiangalia Halmashauri ni receiving station, miradi inafanyika katika ngazi ya chini. Fedha ya capital development grant ambayo ni fedha ya maendeleo asilimia 50 inapelekwa vijijini, endapo CAG atakuwa anaishia katika ngazi Halmashauri hakuna ambacho tutakuwa tunakifanya kuhusu matumizi mabaya ya fedha za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika subvote 1005 ambayo inahusiana na Serikali za mitaa safari za ndani, mwaka wa fedha uliopita ilitengewa shilingi bilioni 5.4 lakini mwaka huu imetengewa shilingi milioni 332 sawa na asilimia sita tu. Kwa hiyo, naomba ofisi hii iangaliwe vinginevyo fedha tunayopeleka itakuwa haifanyi mambo yaliyokusudiwa.
Napenda pia nichangie kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2015. Kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi za kilimo na mifugo kwa mwaka 2015 zilionekana kushuka ikilinganishwa na mwaka 2014. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite zaidi katika Mkoa wa Simiyu. Wananchi wa Mkoa wa Simiyu uchumi wao unategemea kilimo na ufugaji. Tukiangalia ufugaji, mifugo hiyo inatumika kuuzwa na kununua chakula kwa ajili ya familia, kuuzwa na kununua mahitaji kwa ajili ya familia na hata sasa nimeona wananchi wangu wa Mkoa wa Simiyu wakichangia mifugo kwa ajili ya ununuzi wa madawati kwa ajili ya wanafunzi wetu, naomba niwapongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifugo hii ina changamoto nyingi sana, athari ya mabadiliko ya tabia ya nchi yameathiri upatikanaji wa maji pamoja na malisho. Niiombe Serikali upande wa maji wakati wa utekelezaji wa ule mradi wa kutoa maji ziwa Victoria na kuyaleta Mkoa wa Simiyu, itoe pia kipaumbele cha upatikanaji maji kwa ajili ya mifugo, endapo maji yale yote yataingia katika treatment plant mifugo haitaweza kutumia yale maji kwa sababu yatakuwa na gharama kubwa. Naomba Serikali ikumbuke kutenga maji kwa ajili ya mifugo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu malisho, mifugo imeonekana kukonda na mengine kufa kwa ajili ya ukosefu wa malisho na hata ikienda kwenye minada bei imeonekana kuwa ya chini kwa sababu ya ule udhaifu. Niiombe Serikali iweze kupitia mipaka upya ya hifadhi ya Busega, Bariadi, Itilima na Meatu ili kuweza kupatikana eneo kwa ajili ya malisho kwa sababu jamii imekuwa ikiongezeka na mifugo imekuwa ikiongezeka pamoja na athari ya mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia katika vijiji vinavyounda WMA vilivyopo Wilaya ya Meatu Serikali iharakishe mchakato wa matumizi bora ya ardhi ndani ya hifadhi ili wafugaji waweze kupata sehemu ya kuchungia pamoja na kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiongelea kuhusu kilimo cha pamba, zao la pamba limeonekana likidolola mwaka hadi mwaka, wakulima wamekuwa wakilima pamba badala yake wamekuwa hawarudishi ile gharama wanayotumia katika kilimo. Serikali inao mpango mzuri wa kuweza kuleta viwanda vya nguo kwa ajili ya kuongeza thamani ya zao la pamba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata viwanda vilivyopo nikiongelea Kiwanda cha Mwatex 2001 Ltd. Kiwanda hicho baada ya kubinafsishwa kilianza kufanya kazi 2003 kilishindwa kuendelea kwa sababu ya changamoto mbalimbali. Naomba Serikali itatue hizo changamoto ambazo changamoto mojawapo ni upatikanaji wa nishati ya kutosha, upatikanaji wa maji, Kiwanda cha Mwatex kiko kanda ya ziwa ya umeme Mkoa wa Mwanza ambapo kuna ziwa Victoria, Serikali ifanye jitihada za haraka kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha. Changamoto nyingine iliyokikumba kiwanda hicho ilikuwa ni watumishi wasio na ujuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu. Niungane na Wabunge wenzangu kuwapongeza Wizara ya Maji ikiongozwa na Mheshimiwa Aweso, Injini Prisca Mahundi lakini shukrani za kipekee pia ziende kwa Watendaji wa Wizara ya Maji wakiongozwa na Injinia Sanga. Lakini niwashukuru sana kwa ushirikiano wao mkubwa walionipa wakati wa kutekeleza miradi ya maji katika Jimbo la Meatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri inayofanya, fedha nyingi sana zimekusanywa na zimepelekwa. Yapo mabadiliko makubwa ya fedha ukilinganisha na mwaka jana. Mfuko wa Maji wa Taifa umeendelea kukusanya vizuri fedha zake na kuzipeleka kama ilivyo katika Wizara ya Maji. Mwaka jana zilipelekwa kwa asilimia 97 lakini kwa mwaka huu toka mwezi wa tatu asilimia 94 zimeshapelekwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 160.8 zimepelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia upelekaji wa fedha katika Mfuko Mkuu wa Serikali umechangizwa haswa na tozo tuliyoipitisha mwaka jana. Kwa sababu mwaka jana ni asilimia 43 tu ya fedha za Mfuko Mkuu wa Serikali zilipelekwa Wizara ya Maji. Lakini mwaka huu mpaka Machi zimepelekwa asilimia 94 kama nilivyoeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba wananchi tuendelee kuunga tozo hii iliyowekwa katika mafuta, inatusaidia kupata maji. Nanyi ni mashahidi mnaona kila Mbunge anavyonyanyuka anapongeza katika Jimbo lake kwa fedha zilizopelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimejikita katika mapato yaliyotokana na ruzuku ya Serikali Kuu. Nijielekeze katika Jimbo la Meatu. Jimbo hili lina ukame mkubwa, lakini kazi kubwa sana imefanyika ndani ya mwaka mmoja. Ndani ya mwaka mmoja miradi imetelekezwa ya Shilingi bilioni tatu. RUWASA imetekelezwa miradi ya bilioni 1.5, huku Mamlaka ya Maji Mji wa Mwanuzi Shilingi bilioni 1.6 zilipelekwa kutekeleza miradi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Mwanuzi ambayo inatekelezwa na Mamlaka ya Maji, Vijiji vyote saba ndani ya Kata ya Mwanuzi Makao Makuu ya Wilaya ya Meatu zinaenda kupata maji kwa mara moja. Historia inaenda kuandikwa, haijawahi kutokea. Kata hiyo imekuwa na adha kubwa ya upatikanaji wa maji. Sisi wote ni mashahidi, ilifikia mahali tukaanza kuletewa maji kwa kutumia maboza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa RUWASA miradi iliyotekelezwa ni Mwabuzo Shilingi milioni 267; Malwilo Shilingi milioni 100; Isembanda Kabondo Shilingi milioni 586; Itongolyangamba Shilingi milioni 100 na Kata ya Mwamanimba fedha zilizotokana na mapambano ya UVIKO Shilingi milioni 452 zimepelekwa katika Kata ya Mwamanimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mwamanimba ilipewa kipaumbele kwa sababu ni kata iliyokuwa imeathirika na mabadiliko ya tabia nchi. Kama tutakumbuka, miaka ya nyuma shule moja pale iliwahi kuwa ya mwisho kitaifa, kwa sababu muda mwingi watoto walienda kufanya kazi zilizotakiwa kufanywa na mama zao, wakati huo mama zao walienda kutafuta maji zaidi ya umbali wa kilomita saba wakichukuwa masaa mengi kwa ajili ya ufuatiliaji wa maji. Kwa hiyo, kupatikana kwa mradi huu utakuwa ni ukombozi katika Kata ya Mwamanimba. Wanawake wenzangu watajikita sasa katika kufanya majukumu ya kujiongezea kipato katika maisha yao kwa sababu maji yatakuwa yamepatikana yaliyokuwa yanachukuwa muda mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya kwa kuidhinisha fedha mbalimbali katika miradi mbalimbali ya Jimbo la Meatu. Naomba nitofautiane na kauli iliyotolewa jana kwamba mradi wa Mwanuzi ulipokamilika tayari kumekuwa na mgao wa maji. Mheshimiwa Waziri ni shahidi, ule mradi una muda wa miezi miwili. Hata kwenda kuuzindua, ndio tunategemea kwenda kuuzindua na Mheshimiwa Waziri. Matumizi yake, hata 0.001 ya 100, bado hatujaanza kuyatumia. Tumekuwa tukiufuatilia ule mradi toka hatua ya usanifu mimi pamoja na viongozi wa kimkoa, viongozi wa kiwilaya. Tulifuatilia, kile chanzo kina maji mengi sana sana. Ilikuwa ni ndoto ya wana- mwanuzi zaidi ya miaka 20 kukipata kile chanzo kukitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya awamu ya sita chanzo kile kimeweza kutekelezwa. Kinachochangiza kuwe na mgao katika Mji wa Mwanuzi ni kukatikakatika kwa umeme. Naomba niweke kumbukumbu sahihi. Siyo kwa sababu chanzo hakina maji, ni kukatikakatika kwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme unapokuwepo wananchi wote wanapata maji kwa wakati mmoja na wenyewe ni mashahidi. Umeme unapokatika zaidi ya siku tatu, lazima tugawane kidogo kidogo ili tusimalize kabisa. Kwa hiyo, naomba niwatoe wasiwasi wananchi wenzangu wa Jimbo la Meatu, maji yapo ya kutosha. Nami kama Mbunge, kazi yangu sasa itakuwa ni kuiomba Serikali ikamilishe ujenzi wa kituo cha kupozea umeme katika Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kile kitakapokamilika zile dharura ndogo ndogo zinazosababishwa na kukosekana kwa kituo cha kupoozea umeme zitapunguza ile kasi ya kukatikakatika kwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite katika mradi wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Mradi huu umekuwa wa muda mrefu sana. Mwaka 2021 wakati nachingia nilimwomba Mheshimiwa Waziri kama hawa wafadhili wameshindwa kutuchangia fedha, basi Serikali ifanye kwa mapato yake yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri, aliichukua hoja yangu akaifanyia kazi kwa kukaa na yule mfadhili na alikubali kutoa fedha. Naye mara nyingi amekuwa akinishuhudia, sasa mradi utaanza kutekelezwa. Naomba sasa kazi ya utekelezaji wa mradi basi ianze kwa speed, kwa kuwa mradi huo ulifungwa mkataba mwezi Mei, 2019 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Benki ya KFW ya Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee namshukuru Rais, Mama yetu Mheshimiwa Samia, mfuko huu ulitafutiwa fedha na Ofisi ya Makamu wa Rais, yeye akiwa Makamu wa Rais. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa namna anavyopambana na athari ya mabadiliko ya tabianchi. Ndiyo maana alipambana kuhakikisha mradi huu tunaupata. Mradi huu ulikuwa unatekelezwa kwa phase ya kwanza toka Busega, Bariadi mpaka Itilima mpaka mwaka 2026.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi toka Bunge la Kumi na Moja nilikuwa nikiomba mradi huu utekelezwe hadi Wilaya ya Meatu ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi ili kuleta dhana nzima ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Namshukuru Mheshimiwa Rais, kwa sasa mradi huu Meatu inaenda kuingia katika awamu ya kwanza. Mheshimiwa Rais anaifahamu Wilaya ya Meatu ilivyo, alikuja zaidi ya mara tatu katika Wilaya ya Meatu. Mara ya kwanza alikuja kuomba kura, mara ya pili alikuja kushukuru na mara ya tatu alikuja kuzindua Bwawa wa Mwanjoro. Maeneo yote anayajua jinsi yalivyoathirika na ukame ndiyo maana ameridhia Wilaya ya Meatu iingie katika awamu ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wananchi wa Meatu tutaendelea kukuombea Mheshimiwa Rais, Mwenyezi Mungu akupe afya, Mwenyezi Mungu akupe nguvu uweze kuendelea kutekeleza majukumu yako. Nami nikiri kabisa katika awamu ya sita utekelezaji wa miradi ya maji umeongezeka kwa kasi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuomba ambayo niliyokuwa nayasemea. Naomba katika utekelezaji huu wa mradi wa mabadiliko ya tabianchi iwepo component ya maji ambayo hayajatibiwa ili yaweze kusaidia mifugo yetu, ili yaweze kusaidia kilimo cha umwagiliaji. Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Meatu ina athari kubwa. Kwa mwaka huu Jimbo la Meatu wananchi walilima hawakuotesha kwa sababu ya ukame mrefu. Mifugo ya wananchi ilikufa sana kwa sababu ya ukame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutapata maji yasiyotibiwa yatasaidia kupunguza gharama. Kwa mwaka huu upo uwezekano mkubwa hata mchicha tunaenda kuununuliwa Mwanza, upo uwezekano mkubwa hata nyanya tunaenda kuzinunulia Mwanza kwa ajili ya ukame mkubwa. Endapo mradi huu utatekelezwa kwa njia ya umwagiliaji, changamoto hizi ndogo ndogo tutaweza kukabiliana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kutoa maoni katika hoja iliyopo mbele yetu. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya za kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi mikubwa ya kimikakati. Naomba nimtie Mheshimiwa Rais moyo, tuko pamoja naye kazi anayoifanya inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mwigulu pamoja na Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na jukumu kubwa la kutafuta fedha lilipo katika majukumu ya Wizara ya Fedha. Kazi ya kutafuta fedha ni ngumu, kazi ya kuchangisha kodi ni ngumu. Naomba niwatie moyo, tuko pamoja na ninyi, na naomba Watanzania hususan wananchi wa Jimbo la Meatu tuielewe hii Wizara katika suala zima la ukusanyaji wa kodi, kwani fedha nyingi sana zinazoletwa katika Jimbo la Meatu zinatokana na kodi hizi tunazochangia wananchi. Zinatokana na fedha zinazotafutwa za mikopo ya masharti nafuu nje. Naomba tuiunge mkono Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja iliyopo mbele yetu. Niishukuru Serikali hivi karibuni Jimbo la Meatu tumeletewa milioni 857.7 kwa ajili ya upanuzi wa shule ya wasichana Nyalanja Sekondari ambapo yatajengwa mabweni manne, matundu 18 ya vyoo pamoja na madarasa 12. Shule hii ni high school, kwa hiyo kuwepo kwa high school pia kutachangiza watoto wale wa form one hadi form four kupenda kujifunza kwa sababu kutakuwa na wasichana wengi wanaotoka sehemu tofauti za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naishukuru Serikali wiki iliyopita imesaini mikataba saba ya ujenzi wa barabara za kimkakati ikiwemo barabara yetu ya Sibiti, Mwanuzi, Lalago Maswa kwa kiwango cha lami. Niombe Serikali yetu kusaini mikataba si maana yake fedha ziko mezani, maana yake Serikali iendelee kutafuta fedha. Fedha nyingi zinatakiwa kwa ajili ya hii miradi saba takribani trilioni tatu. Fedha hizi zinatokana na kodi zetu, fedha hizi zinatokana na tozo zetu tunazotozwa pamoja na mikopo ya masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru Serikali, mwishoni mwa mwezi Mei, Wizara ya Maji ilienda kusaini mradi wa kimkakati wa maji wa kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi. Kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hoja yake aliahidi, kwamba angeenda kusaini mkataba, ni kweli amesaini mkataba wa bilioni 440 kwa ajili ya kutoa maji Ziwa Victoria na kuyaleta katika Wilaya za Mkoa wa Simiyu. Naamini sasa maji haya yatafika katika Wilaya ya Meatu ambayo imeathiriwa kabisa na mabadliko ya tabianchi. Nimshukuru Mheshimiwa Aweso wakati, huo alitupatia milioni 500 kama nilivyoomba wakati nachangia Wizara ya Maji kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la kati ya Mwambajimu pamoja na Lukale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe wananchi wa Jimbo la Meatu, bwawa hili litajengwa kati ya Kijiji cha Lukale na Mwambajimu ambako watu wetu hawapati maji kutokana na chumvi. Kuna ziwa Eyasi pale ambalo lina chumvi kabisa; wananchi wanasafiri mpaka siku nne kuyapata maji kwa ajili ya kunywesha mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite sasa kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Nishukuru Serikali kwa program ya mikopo kwa wanafunzi wanaochaguliwa na Serikali kusoma kwenye vyuo vinavyotoa elimu katika fani za kipaumbele. Jambo hili ni zuri kwa watoto wanaotoka kwenye familia duni. Hii ni kwa sababu wengi walichaguliwa kwenda kwenye vyuo vya kati walishindwa kuhimili ada kwa ajili ya kulipa masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kuna fani ambazo zimeachwa. Kwa mfano katika Jimbo la Meatu wanafunzi wametoka Sekondari ya Kimali na Mwamalole, wengine wameenda chuo cha IFM kilichopo Bariadi, wengine wameenda vyuo vya maji. Lakini, wanafunzi hawa wamepata division nzuri, wamepata division two wamepelekwa katika hivi vyuo vya kati lakini havipo kwenye vyuo vya kipaumbele. Wanafunzi hawa wanatoka kwenye familia zenye maisha duni kwa hiyo ndoto yao inaweza ikakatishwa pale katikati kwa kukosa ile ada. Kwa macho tunaweza tukaiona ile ada ni ndogo lakini ipo jamii ambayo haiwezi kuilipa hiyo ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanafunzi walitamani waende A-level kwa sababu kule elimu ni bure hakuna ada angalau waliweza kubaingiza kwa kutafuta nauli wengine walikaa miaka miwili shuleni bila kurudi nyumbani ili waweze kuhitimu katika ile miaka miwili na hatimaye waende chuo kikuu ambako kuna mikopo. Kwa hiyo kwa kuwapeleka kwenye vile vyuo wanaweza kupoteza ndoto zao kwa ajili ya kukwamua zile familia zao. Niiombe Serikali iende zaidi, ipanue wigo, ione vyuo vya kati vingine kwa sababu kuna wengine wamepata division three wameenda form five wakatimiza ndoto zao, waliopata division two wanaenda chuo cha kati wanaweza wakapoteza ndoto zao pale katikati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la upatikanaji wa fedha za kigeni limekuwepo katika kipindi hiki cha hivi karibuni na Serikali imebainisha sababu za kuwepo changamoto hii lakini ninaunga maoni ya Kamati ya Bajeti yote. Imechambua, ikaona sekta kuu tatu ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la fedha za kigeni ikiwemo sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee mazao ya kimkakati ambayo mojawapo lipo zao la pamba na zao la alizeti ambayo ni mazao ya kimkakati katika Mkoa wetu wa Simiyu katika Wilaya yetu ya Meatu. Mwaka jana wananchi walifurahi baada ya kuona bei ya pamba imefikia hado 2000. Wananchi wengi walijitokeza na kulima pamba hiyo, lakini mwaka huu bei yake ni 1,000, inazidi kuwanyongonyesha na kuwakatisha tamaa wananchi wetu wa Mkoa wa Simiyu hususan katika Wilaya ya Meatu. Kwa hiyo wananchi wamekuwa wakitangatanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana waliona bei ya alizeti ilipanda wengine waliacha pamba wakaenda kwenye alizeti lakini tunaona bei ya alizeti imeshuka zaidi ya asilimia 50 kwa wakulima wetu. Kwa hiyo wananchi hawajui cha kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto nyingine, katika yale mazao tunayoyalima bado Tembo wanakuja kuyavuruga yale mashamba yao. Tuone namna gani tunaenda kuwasaidia wakulima hawa wa pamba na alizeti. Pamoja na mwaka jana Serikali ilipeleka tani 28 za mbegu katika Wilaya ya Meatu, lakini tani 8 tu ndizo na zilinunuliwa tani 20 zilirudishwa na ASA kwa sababu zilienda kwa kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo pia wananchi walipanda mbegu hazikuwa na tija nak ama mbegu zingekuwa zina tija pamoja na kuporomoka kwa bei zingeweza kuwasaidia zaidi. Huenda wenye viwanda wanashindwa kununua labda mbegu hazina tija, tuliangalie suala la tija katika mbegu za alizeti. Serikali iliagiza mafuta inawezekana zaidi ya upungufu uliokuwepo. Tukiangalia Serikali iliagiza mafuta ghafi ya michikichi kwa ajili ya kuja kuchakata na kwenda kuyauza nchini na mengine kuyauza nchi ya Malawi, Rwanda, Burundi na DRC. Niiombe Serikali ifatilie takwimu na kuangalia, je, yale mafuta yanayochakatwa kwa ajili ya kuuzwa katika nchi nilizozitaja yanauzwa kweli? ama yanazunguka ndani ya nchi na kuleta ongezeko kubwa la mafuta na kukosesha bei ya mafuta ya alizeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la Tembo. Suala la Tembo linavuruga mashamba yetu, ya wakulima wetu mpaka wanakosa vyakula. Nimshukuru Mheshimiwa Rais mwaka huu alituletea mahindi yenye bei nafuu. Nishukuru wepesi wa Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe pamoja na Naibu walitusikiliza Wabunge kwa urahisi na kuyaleta yale mahindi. Lakini bei ile ya mahindi bado ni ndogo ukilinganisha na gharama ya fidia ya ekari ya mahindi ambayo wananchi wanalipwa, na fedha hizi zinaletwa kwa kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imesema inaweka mbinu ya kukabiliana na tembo, imesema inaleta radio caller. Radio caller katika hifadhi ya makao ziliwekwa lakini hazikuwa na ufanisi kwa sababu ziliweza ku-detect ni wapi Tembo wapo kwa kuangalia kwenye mtandao lakini walikosa vifaa vya risasi, walikosa radio kwa hiyo yaliendelea kuwa kama ni mapambo tu ilhali radio caller moja inatumia fedha nyingi sana za kigeni. Serikali imesema wakulima wa kando kando ya hifadhi walime mazao ambayo si rafiki kwa tembo; lakini, hakuna mazao ambayo si rafiki ya tembo. Hata pamba inavurugwa na tembo, alizeti inavurugwa na tembo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena niiombe Serikali ile habari ya kusema kwamba wananchi wamejenga katika ushoroba, na mimi niwaulize. Je, Tembo zamani walikuwa wanakula matikiti yalipandwa na nani? wanakula viazi vilipandwa na nani? kwa hiyo Serikali ikubali mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya maisha hata kwa hawa tembo ianze kukabiliana nao badala ya kuanza kusemea ushoroba, ushoroba, ushoroba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. LEAH J. KOMANYA: …tumechoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kuweza kuchangia hotuba hii kwa maandishi pia naiunga mkono na kushauri yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuishukuru Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kutoa elimu bure kwa kuchangia madawati katika Wilaya zinazopakana na hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua na kuthamini uhifadhi wa wanyamapori na faida yake kwa Taifa ambapo unachangia 25% ya Pato la Taifa katika sekta ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapaswa iendelee kutoa elimu katika jamii inayoishi karibu na hifadhi na wananchi waone/wapate faida kutokana na hifadhi. Wawekezaji wamekuwa wakitoa michango ya maendeleo katika Pori la Akiba la Makao lakini mazingira yanaonesha wananchi hawaelewi mwekezaji anatoa kiasi gani cha fidia, ipo haja taarifa ya mapato na matumizi yasomwe katika vijiji vinavyounda Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ili wananchi wasiendelee kumchukia mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mgogoro wa wananchi na mwekezaji wa Mwiba Holding Company katika Pori la Makao na magazeti yamekuwa yakiandika habari mbalimbali kutoka pori hilo lililopo Wilaya ya Meatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huo ukiuangalia kwa nje kuna mgongano wa maslahi hivyo kuendelea kuiathiri Wilaya ya Meatu. Mimi nikiwa Mbunge Viti Maalum kutoka Mkoa wa Simiyu na ninayehudumia Halmashauri ya Wilaya ya Meatu nilifika kuongea na wananchi (viongozi) wa kijiji cha Makao mgogoro huo unazungumzika pia zipo sheria za nchi zinaweza kutumika.
Naiomba Serikali itoe tamko kuhusu mwekezaji Mwiba Holding Company ili wananchi wa Wilaya ya Meatu waweze kupata msimamo kuhusu mwekezaji katikati ya mwezi Aprili, 2016 wakati wa kikao cha wadau wa maendeleo ya Wilaya. Baraza la Madiwani lilishindwa kupokea ahadi ya mchango katika mfuko wa maendeleo kwa kuwa bado kuna mgogoro. Serikali itakapotoa suluhu itasaidia sasa kama Wilaya kuweza kushirikiana katika shughuli za maendeleo na pia kuweza kushirikiana katika shughuli za maendeleo na pia wananchi wakazi wa Wilaya ya Meatu walioajiriwa na Mwiba Holding Company waweze kujua hatma ya ajira zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara ya Maliasili na Utalii kuharakisha mchakato wa matumizi bora ya ardhi ndani ya hifadhi ili wananchi waweze kulima na kuchunga mifugo. Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 aliahidi wananchi akiwa Jimbo la Meatu kuwa tatizo hilo la malisho litapatiwa suluhisho.
Pia niishauri Serikali kutokana na ongezeko la mifugo na wananchi, athari ya mabadiliko ya tabia ya nchi maeneo mengi katika Mkoa wa Simiyu yamekuwa makame kwa kipindi kirefu hivyo Serikali iangalie upya mipaka ya hifadhi katika Wilaya ya Bariadi, Busega, Itilima na Meatu ili kupata suluhu ya migogoro ya wafugaji na hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kifuta machozi/fidia; kumekuwepo na tatizo la wanyama pori kuwaua wananchi mfano; mtoto Malangwa Kasenge mwenye umri wa miaka tisa wa Kijiji cha Mwaukoli, Wilayani Meatu aliuawa kwa kuliwa na fisi mnamo tarehe 03/05/2013 lakini hadi leo familia haijalipwa kifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo uharibifu wa mazao mashambani kutokana na tembo na nyati katika maeneo tofauti na wakati tofauti katika Wilaya ya Meatu na yamefanyiwa tathimini lakini hadi leo wananchi hawajalipwa fidia au kifuta machozi na sijaona katika bajeti ya Wizara ya Fedha imetengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathimini ilifanyika kwa kuzingatia Sheria Uhifadhi wa Wanyamapori Namba Tano ya mwaka 2009 (The Wildlife Conservation Act, No. 5 of 2009) na kanuni yake (The Wildlife Conservation rates of Consolation Payment). Hivyo naiomba Serikali ifanye fidia kwa wananchi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inapaswa irejeshe asilimia 25 ya uwindaji wa kitalii ya mapato katika Halmashauri, lakini marejesho haya yamekuwa ni ya kusuasua pia yamekuwa yakitofautiana mwaka hadi mwaka, naiomba Serikali yafuatayo:-
Kwanza Halmashauri ijue ni kiasi gani kinapatikana kutoka katika hifadhi inayoizunguka Wilaya ili kuweza kujua stahili zao na pili, Serikali irejeshe kikamilifu asilimia 25 ya uwindaji wa kitalii katika Halmashauri. Naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu usimamizi wa masuala ya hedhi mashuleni. Mashuleni hakuna wataalam wanaotoa elimu ya masuala ya hedhi wala elimu ya afya ya uzazi ili wanafunzi waweze kupata elimu ambayo itawasaidia kuweza kuepukana na mimba za utotoni kwa kuwa miili yao bado ni midogo kuhimili kubeba mzigo (mimba) ambazo huweza kuleta madhara yakiwemo upungufu wa damu, shinikizo la damu, ugonjwa wa fistula na hata vifo vitokanavyo na uzazi. Nashauri wataalam wa idara ya afya wanaoshughulika na masuala ya outreach services watoe elimu ya masuala ya afya mashuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mradi wa uimarishaji wa afya ya msingi kwa kuzingatia matokeo (result based financing); Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa ambayo mradi huu unatekelezwa kulingana na vigezo vya star rating na tayari kuna baadhi ya zahanati zimepatiwa kiasi cha shilingi 10,000,000 kwa ajili ya kutekeleza shughuli zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya upungufu wa watumishi, naomba Mkoa huu upewe kipaumbele mara ajira za afya zitakapotoka, pia wapo wahitimu ambao wapo tayari kuajiriwa Mkoa wa Simiyu kulingana na changamoto ya watumishi kuhama mara baada ya kuajiriwa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukushukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia mpango wa bajeti kwa mwaka 2017/2018. Kwanza, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa mpango mzuri aliotuletea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuchangia, naomba niunge mkono mpango huu ila naomba nishauri katika maeneo yafuatayo na Mheshimiwa Waziri aweze kuzingatia ushauri wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchangia kuhusu madeni ya ndani na nitajikita zaidi katika madeni ya Halmashauri. Halmashauri zetu zinakabiliwa na madeni makubwa ambayo yanaleta ugumu katika utendaji wa kazi. Napenda ku-declare interest nilikuwa mtumishi katika Serikali za Mitaa pia ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Madeni haya yamegawanyika katika sehemu mbalimbali naomba niyataje, madeni ya wazabuni, ya watumishi na ya mradi kwa mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zinapata ugumu katika ulipaji wa madeni haya kutokana na baadhi ya Halmashauri vyanzo vyao vya mapato ni vidogo. Kwa hiyo, kutegemea Halmashauri ziweze kulipa madeni haya mambo mengi yatakwama kwa sababu wazabuni wamekopa mikopo, watumishi wanahitaji malipo yao na miradi kwa miradi inadaiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni haya nayazungumzia kwa sababu nina hoja za msingi, yamesababishwa na upelekaji kidogo wa fedha ambapo Serikali ilikuwa inatekeleza majukumu mengine muhimu ya kitaifa. Sababu nyingine ni Halmashauri zilitekeleza maagizo mbalimbali mengine ya Serikali ambayo ni muhimu na tumeona matokeo yake ikiwepo ujenzi wa maabara. Kwa hiyo, Halmashauri zimeachwa na madeni makubwa. Mheshimiwa Waziri naomba katika mpango wako uweke mpango pia wa kuzisaidia Halmashauri kulipa madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili naunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuhamisha ukusanyaji wa kodi ya majengo kukusanywa na TRA. Ninazo sababu za msingi. Kwanza, baadhi ya Halmashauri zilikuwa hazina takwimu za majengo yanayopaswa kukusanywa kodi ya majengo, hazikuwa na makadirio yanayoeleweka ya kukusanya mapato hayo zilikuwa zikikadiria mapato kidogo. Hata yale mapato kidogo yaliyokuwa yakikadiriwa ukusanyaji wake ulikuwa ni hafifu sana. Hivyo tu niishauri Serikali mfumo wa Taifa wa kukusanya mapato ya Serikali za Mitaa uzifikie Halmashauri kwa wakati na fedha hizo zikipatikana basi zirejeshwe haraka Halmashauri ili waweze kutekeleza shughuli zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali kwa namna inavyokusanya mapato kikamilifu na imekuwa ikivuka malengo. Hata hivyo, ukusanyaji huu wa mapato kikamilifu hauwezi kupunguza umaskini walionao wananchi wetu. Serikali inapaswa iwekeze kikamilifu katika sekta zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja zikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niongelee upande wa kilimo cha pamba. Sekta ya pamba bado inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinapelekea wakulima kuanza kujiondoa kuzalisha zao hilo. Baadhi ya changamoto ni ukosekanaji na uhafifu wa pembejeo wanazopewa wakulima. Wakulima wamekuwa wakipewa pembejeo hafifu kwa mfano mwaka jana dawa za kuua wadudu hazikufanikiwa, ziliwafanya wale wadudu wasinzie. Kwa mwaka huu dawa ziko kidogo, ziko kama kopo 500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iweke mpango wa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wingi kwa sababu wananchi wamepata pia mwamko wa kulima kutokana na bei ya pamba iliyotolewa mwaka jana ambayo Mheshimiwa Rais aliisimamia na wakulima wakapata angalau bei iliyoweza kuwanufaisha kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni kukabiliwa na tatizo la mbegu. Ipo mbegu ya UK91 ambayo imeingia sokoni kwa muda mrefu na kupoteza ubora wake. Mbegu hii imekuwa ikipandwa na wakulima wakati mwingine imekuwa haioti na kusababisha umaskini kwa wakulima wetu. Nashauri Serikali iweke mpango kwa mwaka 2017/2018 wa kuidhinisha mbegu mpya ya pamba ili iweze kuinua uchumi wa wananchi hasa Kanda ya Magharibi, zao la pamba linategemewa katika uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuongelea afya. Wakati tukichangia bajeti ya mwaka 2016/2017, yalitoka matamko ya Serikali kwamba Serikali inajipanga kufanya tathmini ya ujenzi wa zahanati na vituo vya afya. Kwa hiyo, natumaini safari hii mpango mzuri utakuwepo na bajeti ya kutosha itawekwa ili kuweza kukamilisha ujenzi wa zahanati na vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna ufadhili ambao unatolewa kwa kitengo cha afya kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli ambazo siyo za construction. Tumeona wafadhili wakitoa fedha za result based financing. Naomba vigezo vinavyotumika vipitiwe upya kwa sababu ili hospitali ya wilaya au kituo cha afya kiweze kufuzu kupata fedha hizi inatakiwa zifikie nyota tano. Vituo hivi vya afya au zahanati zinawezaje kufuzu kupata hizo nyota tano ili ziweze kupata fedha hizo kwa sababu ukiangalia changamoto nyingi zinasababishwa na Serikali. Kwa hiyo, inakuwa viko nje ya uwezo wa Halmashauri. Naomba yafanyike upya mapitio ya vigezo hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo, machache naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ili na mimi niweze kuchangia taarifa hizi za Kamati mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Naomba nianze kuchangia moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016, Sehemu ya Nne fasili ya (16) inasema Kamati yetu ya LAAC itafanya kazi kwa kutumia taarifa zilizokaguliwa na Mkaguzi wa Nje. Kamati ilikumbana na changamoto nyingi wakati wa utekelezaji wa majukumu haya ikiwemo Ofisi ya CAG kukosa fedha kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukichangia bajeti ya mwaka 2016/2017 tuliongelea sana suala hili. Pamoja na bajeti iliyopitishwa upelekaji wa fedha umekuwa ni wa shida. Tunafahamu kwamba kazi za CAG zinafanyika kwa msimu kwa hiyo, kufikia ile Julai, 2016, CAG alikuwa hajapelekewa fedha za kutosha kumuwezesha kutekeleza majukumu yake ili Kamati iweze kutumia taarifa zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hiyo ilipelekea Halmashauri ya Korogwe ambayo walikuwa wametumia fedha kwa ajili ya kujiandaa kuja kukaguliwa na Kamati mfano usafiri, posho za kujikimu, stationery tuliwarudisha kwa sababu hoja zao zilikuwa hazijafanyiwa verification. Hivyo, nashauri Wizara ya Fedha ipeleke fedha kulingana na plan of action ya Ofisi ya CAG. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kipengele cha mishahara isiyolipwa. Serikali ilianza utaratibu wa kulipa mishahara ya watumishi wa Halmashauri moja kwa moja kupitia akaunti zao. Changamoto iliyopo, Mkurugenzi wa Halmashauri anatoa zuio la mishahara kulipwa kwa Meneja wa Benki. Mishahara inapozuiliwa Meneja wa Benki anairudisha moja kwa moja Hazina Kuu, Hazina Kuu inakiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Meneja wa Benki. Changamoto inayotokea ni kwamba kunakuwa na gap kati ya Meneja wa Benki na Mkurugenzi na Mkurugenzi na Wizara ya Fedha. Meneja wa Benki hana document ya kuweza kumrudishia Mkurugenzi kuonyesha mishahara iliyozuiliwa kwa sababu hawezi kuirudisha kwenye akaunti ya Halmashauri. Hazina hawawezi kutoa risiti tena kwa Mkurugenzi itakuwa ni double accounting ya revenue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Wizara ya Fedha haijatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ni nini wafanye ili kuweza ku-reconcile mishahara ambayo haijalipwa. Wasipofanya hivyo kutatokea loophole kwa watumishi wa benki wasio waaminifu, wakiona hakuna ufuatiliaji wa karibu mishahara mingine inaweza ikalipwa tu kwa watumishi wasiostahili.
Naishauri Wizara ya Fedha ifanye mawasiliano na Wakurugenzi Watendaji. Kwa mfano, Jiji la Tanga lilikuwa lina hoja ya mishahara isiyolipwa ya shilingi milioni 168.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie katika kipengele cha mfumo wa kihasibu wa EPICOR. Halmashauri nyingi zilikuwa zina hoja…
Mheshimiwa Mwenyekiti,…
Ninyi mbona mnanichanganya bwana.
Haya sawa. Mheshimiwa Naibu Spika,…
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunilinda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri nyingi zilikuwa zina hoja ya matumizi mabaya ya mfumo wa EPICOR. Tunavyofahamu Serikali ilitumia fedha nyingi kwa ajili ya kupeleka mfumo huu kwa lengo la kudhibiti matumizi mabaya na kudhibiti mapato. Changamoto iliyopo kuna baadhi ya package bado hazijaingizwa katika mfumo wa EPICOR, kwa mfano asset management. Hii inapelekea Halmashauri nyingi kutoa taarifa au kukamilisha kazi zao nje ya mfumo kwa sababu mfumo haupo wakati Serikali ilitumia fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la mfumo huu pia ilikuwa ni ku-control matumizi mabaya ya vifungu. Tukiangalia kuna hoja nyingi za wrong accounting coding. Hii inapelekea hata taarifa zinazotolewa kwenye Halmashauri katika vikao mbalimbali kuwa siyo zenyewe kwa sababu zinafanywa nje ya mfumo. Nashauri Serikali ifanye ufuatiliaji kuhusu matatizo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu matumizi ya fedha nje ya bajeti katika fedha za miradi. Kwanza, napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa maagizo anayotoa kwa ajili ya Halmashauri. Mheshimiwa Rais ana lengo zuri lakini changamoto inakuja maagizo yanapotolewa zipo Halmashauri nyingine zina uwezo wa kutumia wadau waliopo katika Manispaa au Majiji kazi hiyo ikafanyika. Halmashauri nyingine hazina uwezo wa kupata wadau hao inawalazimu watumie fedha kwa kutozingatia bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunapitia taarifa Halmashauri nyingi zilionekana miradi mingi haijatekelezwa kwa mfano miradi ya maji, miradi ya …
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fedha hizo zimetumika katika maabara. Je, Serikali inafahamu ni miradi kiasi gani iliyoathirika na ina mkakati gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia hoja ya Wizara ya TAMISEMI pamoja na Utumishi; Utawala Bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya. Wananchi wa Mkoa wa Simiyu wanamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kazi zote anazozifanya za kupambana na wote wasio na nia nzuri na nchi. Hii yote imejidhihirisha
katika ziara yake aliyoifanya mapema mwezi wa Kwanza katika Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuzindulia Kiwanda cha Chaki kilichopo Maswa Mkoani Simiyu. Katika uzinduzi wake, alitujengea mazingira ya kuona namna ya kuweza kupanua kiwanda hicho na tayari sasa hivi kiwanda hicho kitapanuliwa kwa kushirikiana na Halmashauri pamoja na TIB. Naomba niwajulishe tu kwamba chaki za Maswa ni nzuri; na vijana wako hapa Dodoma kwe ye maonesho wanazo hizo chaki. Kwa hiyo, nawaombeni Waheshimiwa Wabunge mfike mzione ili muweze kununua katika Halmashauri zenu na kukuza uchumi wa vijana wa Maswa. Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuzindulia barabara ya lami ya kutoka Lamadi mpaka Bariadi yenye kilometa 71, kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mwigumbi mpaka Maswa yenye kilometa 52. Mheshimiwa Rais alipokuwa Mkoani Simiyu aliahidi sasa utekelezaji wa ujenzi wa lami wa barabara ya Maswa mpaka Bariadi yenye kilometa 50 uanze. Hivi sasa ninavyoongea, mchakato wa kumpata Mkandarasi unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri upande wa Serikali. Nimeshuhudia miradi mingi mikub wa wakati ikitekelezwa, wakandarasi wamekuwa wakija na vijana kufanya kazi ambazo zingeweza kufanywa na vijana ambao wanatoka pale pale. Wakandarasi wengine
wameweza kuthubutu kuja hata mpaka na unga kwenye eneo analoweza kufanyia kazi. Naomba Serikali isaidiane na wakandarasi, kuwatumia vijana wa eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi ule utatekelezwa katika Wilaya ya Bariadi, Itilima na Maswa, wachukue vijana wa kutoka pale kwa sababu nina imani wanazo nguvu na ni waadilifu. Pia wanunue bidhaa zinazotokea katika maeneo yale. Kuna samaki wazuri wanapatikana katika soko la Bariadi ambao wanavuliwa katika Ziwa Victoria Wilaya ya Busega; kuna nafaka nzuri inatoka Wilaya ya Itilima; na mchele mzuri unaotokea katika Wilaya ya Maswa. Nawakaribisheni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kwa kusema, Mheshimiwa Rais wakati anafanya kampeni zake mwaka 2015, alipokuwa Wilayani Meatu aliawaahidi wananchi kwamba atawawezesha kujenga nyumba bora kwa kupunguza bei ya vifaa vya ujenzi. Hapa ninapoongea, mfuko
mmoja wa saruji Wilayani Meatu ulikuwa unauzwa shilingi 20,000/=, lakini kwa sasa hivi unauzwa shilingi 16,000/=; lakini bei hiyo bado iko juu ukilinganisha na wilaya za jirani. Hii inatokana na kwamba simenti inapokuja, ni mpaka ifike Shinyanga halafu ianze kurudi tena kuja Wilaya ya Meatu. Changamoto ya kutatua mzunguko wa usafiri huu ni ukamilishaji wa ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu daraja hilo linatekelezwa na TANROAD, Singida, lakini vikao vya Mfuko wa Barabara vya Mkoa wa Simiyu toka mwezi wa Tisa tumekuwa tukiahidiwa kwamba, vifaa viko China vinatengenezwa, leo yapata miezi saba, vifaa vile havijaletwa. Tunaomba basi ujenzi huu uharakishwe, vifaa hivyo viletwe ili daraja hilo liweze kufungua milango ya biashara kwa Mkoa wa Simiyu, hususan Wilaya ya Meatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo itakapoanza kazi, itasaidia wananchi. Mwananchi anapoondoka Meatu kwa kupitia Shinyanga, anatumia sh. 95,000/= kwa sababu inabidi aende Shinyanga, alale Shinyanga kesho yake asafiri. Kwa kutumia daraja la Mto Sibiti pale, atatumia sh. 45,000/= kufika Dar es Salaam. Kwa hiyo, ataokoa sh. 50,000/= pamoja na siku moja ambayo angeweza kutumia katika shughuli nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie upande wa maji. Katika hotuba ya Waziri wa TAMISEMI amesema kwamba Serikali imeunda vyombo vya utumiaji maji COWSO, vipatavyo 1,800 kwa ajili ya usimamizi na uendelezaji wa vituo vya maji, ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu. Mimi nikiwa Mjumbe wa Kamati ya LAAC, tumekuwa tukitembelea miradi hiyo, tumeona changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa hiyo miradi iliyokabidhiwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati zile hazijajengewa uwezo namna ya uendeshaji wa miradi hiyo. Kamati hizo hazijui hata namna ya utunzaji wa fedha, namna ya kupokea mapato, hazina hata 'O' and 'M' Accounts (Operation and Maintenance Account), kiasi kwamba tatizo likitokea
wanapaswa wachukue fedha ili mradi uendelee. Matokeo wamekuwa wakichangishana fedha kienyeji na kusababisha hata ile gharama kwa ndoo kuwa kubwa. Tunaomba vyombo vile viwezeshwe ili viweze kuendesha miradi hiyo ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie mchango wangu kwa 5% ya wanawake na vijana. Ni kweli Halmashauri zimekuwa zikitenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha akinamama na vijana, lakini Halmashauri zimekuwa zikiishia kutenga tu bila kutoa michango ile kwa akinamama. Kwa
kuwa michango hiyo haiko kisheria, ni waraka tu unaotumika, wakati tukiwa mbioni kuandaa sheria, nashauri ili utekelezaji ufanyike vizuri, basi ajenda hii ya mchango iwe ya kudumu kwenye vikao vya RCC ili Mkuu wa Mkoa na Kikao chake aanze yeye kwanza kufuatilia badala ya kusubiri Kamati ya LAAC ndiyo ije kwanza ionekane kwamba ule mchango ndiyo kwanza wameuona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii jioni ya leo na mimi niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa namna wanavyojituma. Muda mwingi nimekuwa nikifuatilia na kuwaona wako field. Kwa maana hiyo, wamekuwa wakifuatilia kuangalia namna miradi ya maji inavyotekelezwa na kuona changamoto zinavyojitokeza katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na Mheshimiwa Chenge Mbunge wa Bariadi kuhusu kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Bariadi, nami niongeze mambo mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Bariadi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu. Hivyo, ongezeko la watu limekuwa likiongezeka kila siku. Mji umekuwa ukipanuka kila siku na mradi huu umekuwa ni wa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba basi wakati wanakamilisha utekelezaji, waweze kufanya tathmini tena, waweze kuona ongezeko la watu na ongezeko la makaazi ya watu lilivyoongezeka ili waweze kuendelea kuupanua mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, naomba niungane na Mheshimiwa Chenge kuhusu Serikali katika utekelezaji, iweze kukumbuka yale makubaliano kwamba wakati wa utekelezaji wa huo mradi maji yatatengwa kwa ajili ya mifugo na kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini soko la Bariadi lina mahitaji makubwa, lina mahitaji ya mboga za majani, matunda na kadhalika. Angalau wanawake waweze kujipatia sehemu ya kuuza, kwa kulima mboga mboga na mazao mengine ambayo watapata soko lao katika Mji wa Bariadi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie upande wa programu ndogo ya maji na usafi wa mazingira. Programu hii imekuwa mkombozi kwa wananchi waishio vijijini. Programu hii ilianza mwaka 2006 hadi 2016, sasa yapata miaka kumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa Mtendaji nimeshuhudia kwa namna gani imeweza kusaidia upatikanaji wa maji vijijini. Nitoe masikitiko yangu; ukiangalia Kifungu 4001 - Maji Vijijini; Kifungu kidogo cha 3280 ambayo ni Maji na Usafi wa Mazingira, mwaka wa fedha wa 2016/ 2017 zilitengwa shilingi bilioni 310.7, lakini mwaka huu wa fedha wa 2017/2018 zimepungua hadi shilingi bilioni 158.5, zimepungua kwa zaidi ya asilimia 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba fungu hili liongezewe fedha. Kwa kuwa bajeti kuu imeongezeka basi na kifungu hiki kiongezewe fedha. Kwa sababu ukiangalia sehemu kubwa ya nchi ni vijijini. Kwa mfano, nikiongelea mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria kwa Mkoa wa Simiyu, kutoka Busega na maeneo yake. Mradi huu tu uta-cover vijiji 253. Ukiangalia vijiji ambavyo havitafikiwa na mradi viko zaidi ya asilimia 50.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nikiangalia Jimbo la Maswa Magharibi, Jimbo zima hakuna kijiji kitakachofikiwa na mradi huu. Kwa hiyo, bado ipo changamoto ya uhitaji wa mradi wa maji vijijini, uongezewe bajeti. Kwa mfano, kuna Vijiji vya Kinamgulu, Mwabayanda, Ilamata na Mwandu. Vijiji hivi vipatiwe hata visima virefu kwa sababu kule mradi hautapitia hata kijiji kimoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niungane na Wabunge wengine kwamba sasa shilingi 100 ziweze kukatwa katika bei ya petroli na diesel. Ziongezwe shilingi 50/= kwa sababu hii itaongeza bajeti ya maji vijijini. Nashauri asilimia 70 ielekee vijijini kwa sababu huko kuna changamoto ya upatikanaji wa vyanzo vya maji. Nashauri pia awepo Wakala wa kusimamia fedha hizi zitakapopatikana ili ziweze kuratibiwa kikamilifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kuhusu Bwawa la Mwanjolo lililopo Wilaya ya Meatu, Jimbo la Meatu. Mwaka 2016 mwezi wa Tano Mheshimiwa Waziri mwenyewe aliniahidi kwamba litafanyiwa tathmini ili liweze kukamilishwa, lakini hakuna utekelezaji ulioendelea. Bwawa hili lilianzishwa 2009, wananchi walitoa eneo wenyewe lakini sasa hivi limeanza kuwa kero kwao, limesababisha mmomonyoko wa udongo, wananchi waliacha kufanya shughuli zao kwa ajili ya mradi huo, lakini utekelezaji hakuna. Naomba sasa utekelezaji wake ukamilike. (Makofi)

Pia nichangie kuhusu Mamlaka ya Maji Mjini Mwanhuzi. Tunategemea maji kutoka Ziwa Victoria, lakini Wilaya ya Meatu itakuwa awamu ya pili. Ukiangalia bwawa lile, limejaa matope, nina wasiwasi kama maji yatafika hata mwezi wa Kumi. Mji mdogo wa Mwandoya, chanzo kilichopo cha Igobe kimezidiwa. Nashauri basi uwepo mpango wa dharura ili kuweza kuinusuru Wilaya ya Meatu, Mji mdogo wa Mwandoya pamoja na maji mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maji haya pia yanaweza yakapatikana kutoka Mto Sem ambayo itasaidia kupitiwa Kijiji cha Mwagila, Sem, Isengwa, Manyahina na Busia, Busia ambako tenki lipo pale lakini wananchi wa pale hawapati maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie pia kuhusu dhana ya mradi wa vijiji kumi. Katika WSDP 1 dhana ya mradi wa vijiji kumi niliona kila kijiji kilikuwa kikitafuta chanzo cha maji. Nashauri katika WSDP 2 kama ni vijiji viwili au vitatu kinaweza kikapatikana chanzo kimoja, mtindo huo utumike ili kuweza kuokoa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC; wakati wa ufuatiliaji miradi RWSSP katika ile component ya sanitation utekelezaji wake haufanyiki vizuri, kwa sababu unapofanyika mradi wa maji lazima kijengwe choo. Ukiangalia mradi wa maji wenye mabilioni umekamilika, lakini kipengele cha usafi na mazingira kujenga choo, yaani hela kidogo tu miradi hiyo haijatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii asubuhi ya leo na mimi niweze kuchangia katika Wizara ya Elimu.

Kwanza, naunga mkono hotuba ya Wizara ya Elimu na pili naomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa namna wanavyojituma kuhakikisha elimu ya Tanzania inainuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie dakika zangu nyingi nijikite katika mpango wa kuinua ubora wa elimu (Equip Tanzania). Nitatoa ushauri pamoja na ushauri wangu naomba Serikali nayo itanieleza imejipangaje kutatua yale ambayo mimi nitayaongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ni wa miaka minne unaotekelezwa na Serikali ili kuweza kuboresha elimu katika maeneo yaliyokuwa nyuma kielimu. Mpango huu upo katika mikoa saba na Simiyu ni mkoa mmojawapo uliopo katika mpango huu. Naupongeza sana mpango huu kwani umeweza kuinua kiwango cha ufaulu katika Mkoa wa Simiyu kwa kiwango cha asilimia 30.7. kabla ya mpango huu ufaulu katika Mkoa wa Simiyu ulikuwa ni asilimia 36.7 na Mkoa ulikuwa wa 24 kitaifa. Matokeo ya mwaka 2016 kiwango cha ufaulu kimeongezeka mpaka asilimia 67.4 na mkoa umekuwa wa 14 kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Simiyu akisaidiana na Afisa Elimu wa Mkoa kwa namna wanavyoisimamia elimu na kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi na wazazi wa Mkoa wa Simiyu. Pamoja na ufaulu huu bado kuna changamoto zilijitokeza ambapo watoto wa kike waliripotiwa kupata mimba na mimi ni mmojawapo niliyeshuhudia mwanafunzi amepata ujauzito akashindwa kuendelea na masomo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la mradi huu pia ni kuinua ubora wa elimu inayotolewa hasa kwa mtoto wa kike. Mtoto wa kike katika mpango huu umemtaka amalize elimu ya msingi aendelee na elimu ya sekondari. Nikiangalia mtoto wa kike anazo changamoto nyingi sana ambazo zinaweza zikamsababisha asiweze kufaulu na kuendelea na sekondari ama akatishwe masomo yake na asiendelee na sekondari na kumaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niweze kufahamu pamoja na ushauri wangu, je, Serikali imejipangaje kutokomeza yafuatayo katika mpango huu? Serikali imejipangaje kutokomeza mimba na ndoa za utotoni kwa kutoa elimu ya uzazi kwa wanafunzi? Nikiangalia katika shule zetu wataalam wa elimu ya uzazi ni wachache na sehemu zingine hawapo kabisa. Katika ajira hizi zinazotolewa za Serikali sijafahamu wakunga na manesi wataajiriwa wangapi. Naomba hilo pia liangaliwe wakati wa ajira. Tunao watumishi wa idara ya afya wanaofanya outreach service.
Nashauri pia waweze kufanya kazi hili kwa kwenda kutoa elimu katika shule za msingi na za sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna unyanyasaji wa kijinsia na udhalilishaji wa kingono. Serikali imejipangaje katika mpango huu kutokomeza hayo? Matukio yamekuwa yakiripotiwa kila siku. Juzi tarehe 9, Mkoa wa Mara mtoto wa miaka minne amebakwa, nasikia uchungu sana. Kwa mazingira haya bado itakuwa ni vigumu kwa mtoto wa kike kumaliza shule ya msingi na kuendelea na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna tatizo la ukeketaji watoto wa kike. Pia napenda kupata majibu ya Serikali imejipangaje kulishughulikia tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna tatizo ukeketaji wa watoto wa kike napenda kupata majibu, pia kuna tatizo la kutokuwa na usawa wa kijinsia katika elimu. Kwa mfano, shule ya Sekondari ya Itinje iliyopo Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu ilikuwa ya kwanza Kiwilaya, ya tatu Kimkoa, lakini shule hii ina tatizo la kutokuwa na matundu ya choo. Je, Serikali inaisaidiaje? Watoto wana hamasa ya kusoma lakini wana mazingira ambayo yanawakwamisha. Ninashauri, katika ule mpango wa RWSSP katika kile kipengele cha sanitation matenki ya maji yajengwe zaidi shuleni, ambapo matenki hayo yakijengwa lazima pia matundu ya choo yatajengwa. Kwa hiyo, ninaomba matundu hayo yakijengwa yapewe kipaumbele matundu ya watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya adhabu yanayoweza kudhuru mwili au akili ya mtoto, tumeona juzi kuna mahali imeripotiwa watoto wamefungiwa kwenye safe mpaka wamefariki, Serikali ina mpango gani wa kumlinda mtoto katika adhabu zenye kudhuru mwili na akili shuleni, viboko visivyo na mpangilio na kufungiwa kwenye vyumba ambavyo havina hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango, umejikita vipi katika kusaidia watoto walio katika mazingira hatari zaidi. Kwa mfano, watoto waliotelekezwa, watoto yatima, watoto walio katika umaskini wa kupindukia. Je, mpango umejikita vipi kupata mlo mmoja kwa watoto wakati wa mchana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ambao wamepitwa na muda kutokana na kwamba wakati ule kabla ya elimu bure walikuwa wanashindwa kwenda shule kwa ajili ya michango na kadhalika. Je, Serikali imejipangaje katika elimu ya MEMKWA na elimu zingine ili kuweza kuwanusuru kuwatoa katika wimbi lile la ujinga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu pia katika kila shule waliambiwa kuandaa business plan ili waweze kupata angalau milioni 1.5 kwa ajili ya elimu ya kujitegemea, tayari shule zimeshaweza kupatiwa mchango huu. Naomba kujua, je, katika lile darasa la mtihani la saba, hii elimu ya kujitegemea kuna watoto wa kike ambao watapata changamoto ya kutokwenda shule wakiingia katika siku zao za hedhi na katika darasa la saba naamini bado watoto ni wadogo lakini kuna one third ambao tayari wameshaingia kwenye hedhi. Je, katika elimu ya kijitegemea mpango ule umejikitaje hata kununua taulo kwa ajili ya watoto hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Shule ya Sekondari ya Wasichana Weruweru toka form one hadi form four kwa kupitia elimu ya kujitegemea, tulikuwa tukipatiwa mataulo shuleni, sikujua gharama ya mataulo toka ninaanza mpaka namaliza. Kwa maana hiyo hata hili linawezekana maana yake katika mipango hii watoto wanaweza wakafanya miradi hata ya ufiatuaji matofali, kulima na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie pia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Awali ya yote naomba niunge mkono hoja hii. Pia napenda niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyojitahidi kufanya utafiti kuhusiana na zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii imekuwa ikifanya utafiti wa aina mbalimbali hatimaye ulitoa mbegu aina ya manyoya kwenda kwenye mbegu ambayo haina manyoya. Pamoja na changamoto zilizopo katika mbegu hiyo, Serikali imejitahidi kutoa elimu kwa wakulima na hatimaye wakulima wameweza kufanya kama inavyotakiwa na hapa tunaona ongezeko la pamba mbegu kutoka tani 122,000 mpaka 150,000. Kwa hiyo, kuna kuwa na ongezeko la tani 28,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba zao hili ni zao la uchumi katika Mikoa yetu ya Magharibi. Ni zao ambalo linategemewa lakini limeonekana haliwezi kumnufaisha mkulima kama inavyotakiwa. Pamoja na elimu inayotolewa hii mbegu ambayo imetolewa manyoya ambayo ni UK 91 imekaa muda mrefu sokoni na kupoteza ubora wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michango yangu iliyopita niliweza kuchangia kuhusu udhaifu wa mbegu hii, mbegu hii imekuwa ina matunda machache sana ukilinganisha na wakati ilivyokuwa inaanza. Kwa sasa inakuwa ina matunda kumi tu kwenye shina hadi ishirini kwenye shina moja, kwa hiyo inasababisha uvunaji wa kilo 300 katika heka. Kwa hiyo, pale bado hatujamsaidia vizuri mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali baada ya kusikia michango yetu iliyopita sasa imeweza kuja na mbegu mbya aina ya UK M08. Sisi Wabunge tunaotoka Mkoa wa Simiyu tunaelewa kwamba mbegu hii imefanyiwa majaribio katika Kata ya Mwabusalu na kuanzia inavyoota majani yanavyotoka mbegu hii imekuwa ikiweka matunda kuanzia chini mpaka juu na mpaka sasa takribani kuna wastani wa matunda 50 mpaka 100 katika shina moja na hivyo kutegemea katika msimu huu kilo zitaongezeka kwa heka moja kutoka kilo 300 mpaka 1000 au 1200. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshangaa Mbunge mwenzangu wa Mkoa wa Simiyu ambaye bado anaongelea mbegu ya manyoya; Simiyu hatupo huko. Huyo haudhurii vikao vya RCC, hajui Simiyu tunaendaje, kwa hiyo asiturudishe nyuma kwenye mbegu za manyoya, sisi tupo na mbegu ya UK M08.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kabla pamba hii haijaanza kuvunwa katika Kata ya Mwabusalu aende akaingalie kwa namna ilivyostawi ili walete sasa mbegu ya kutosha katika Mkoa wa Simiyu, hatutegemei tena kutumia mbegu ya UK 91. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo lingine la pembejeo; wakulima wa pamba walizoea dawa ya pembejeo ya mafuta, lakini nimefuatilia na kuona kwamba dawa hii imekataliwa kwa sababu ina sumu nyingi na kuletwa aina nyingine ya dawa ya maji aina ya bametrim. Dawa hii bado haiui wadudu vizuri, tunaomba pia utafiti uendelee kufanyika ili dawa hii iweze kuwaua wadudu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao hili pia linakaribiwa pia na kupungua kwa mbolea katika ardhi, tunaomba wakulima wahamasishwe kwa hiyari waweze kuweka samadi, tunao ng’ombe wengi hivyo waweke samadi ambayo itaweza kuiboresha ile rutuba ambayo muda mrefu mbolea yake imeonekana kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto zingine; mzunguko dhaifu wa usambazaji wa pembejeo. Taasisi zenye msaada dhaifu kiufundi na kifedha kama Mfuko wa Uendelezaji Zao la Pamba (CDTF) pamoja na Bodi ya Pamba zimekuwa hazina msaada wa karibu kwa wakulima. Mkulima anakatwa Sh.15/= kwa kilo kwa ajili ya kuongeza uboreshaji wa zao hilo lakini matokeo pembejeo zimekuwa haziletwi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aziangalie hizi taasisi, ziimarishwe au zifanyiwe kama kule kwenye Bodi za Korosho kulivyofanywa ili na sisi wananchi wa Simiyu wakulima wa pamba tunahitaji tija katika zao letu la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichangie tozo katika sekta ya mifugo; naipongeza Serikali kwa namna inavyoendelea kufuta tozo katika sekta hii ya mifugo. Kabla sijachangia naomba niweke kumbukumbu sahihi, siyo kweli kwamba mfugaji anapopeleka ng’ombe wake mnadani anatozwa ushuru wowote, mfugaji huyo ambaye kwa jina lingine anajulikana kama muuzaji. Serikali ilifuta ushuru wa aina yoyote kwa mfugaji anaepeleka mfugo wake mnadani toka mwaka 2003. Baadhi ya ushuru kama wa Halmashauri ulifidiwa na Serikali kuu kwa ile general purpose. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, Mheshimiwa Mbunge naposema kwamba wananchi wa Simiyu wale wafugaji wanatozwa ushuru anapotosha. Ushuru unaotozwa ni kwa mnunuzi; kuna ushuru wa Halmashauri na ushuru wa kusafirisha mifugo nje ya Wilaya. Nashukuru Serikali imeazimia kuufuta ushuru huo nami naiunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiunga mkono kwa sababu ushuru huu haukuwa na tija yoyote kwa Halmashauri au Serikali Kuu. Serikali iangalie vyanzo vya Serikali Kuu vinavyotozwa kule chini kwa kutumia ERV na stakabadhi yoyote inayotoka Serikali Kuu, fedha nyingi haiingii katika Mfuko wa Serikali, inaingia katika mifuko ya watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unataka kushuhudia hilo, tafuta wiki moja yoyote uangalie makusanyo ya ushuru yaliyotokana na mifugo kwa wiki katika Halmashauri moja ulinganishe na zile permit zilizokusanywa na Serikali Kuu kwa idadi ya ng’ombe. Obviously, ng’ombe waliokusanywa na halmasahuri wako juu kuliko waliokusanywa na Serikali Kuu, kwa hiyo fedha nyingi inaingia katika mifuko ya watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna huu mnada wa upili, Mnada wa Mhunze, mnada huu ni secondary market. Wafanyabiashara wengi wa mifugo…
…naomba itozwe ile tozo ya Sh.2,500/= kwa sababu Sh.5,000/=…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa namna inavyoendelea kufuta kodi, tozo, ushuru na ada ambazo zinaleta kero kwa wananchi hususan wafanyabiashara kama vile tozo ya afya ya kusafirisha mifugo nje ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifute tozo ya kusafirisha mifugo nje ya Mkoa katika Minada ya Upili, kwa mfano, Mnada wa Mhunze, Wilaya ya Kishapu, Serikali Kuu hukusanya tozo zote, ushuru Sh.5,000/= kwa ng’ombe na tozo ya kusafirisha ng’ombe nje ya Mkoa Sh.2,500/= jumla Sh.7,500/
=, zote huchukuliwa na Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu haipati kiasi chochote cha fedha. Naomba permit ya Sh.2,500/= iondolewe ili kumpunguzia mzigo mfanyabiashara wa mifugo ile Sh.5,000/= inatosha kabisa Mkoa kugawana na Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii jioni ya leo na mimi niweze kutoa mchango wangu katika mpango wa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza naomba kwa kuongelea utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kulipa madeni ya wakandarasi wa miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu. Wakandarasi wamelipwa shilingi milioni 672 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji. Nina amini watakapokamilisha wataenda kumtua ndoo mwanamke na vijiji vya Lubiga, Itinje, Mwandoya, Igobe, Mwanuzi, Mkoma, Mwamalole na Bukundi vitanufaika na miradi hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nipende pia kuongelea fedha za miradi ya maendeleo. Kumekuwa na upungufu wa kutokuletwa au kuchelewa kwa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hili ni tatizo katika takribani Halmashauri zote za nchi nzima. Miradi imekuwa ikitekelezwa nusu nusu au kwa kusuasua au kutekelezwa kwa kipindi kirefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekuwa wakitekeleza hatua yao ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hata hivyo Serikali imekuwa ama inaleta fedha kidogo za CDG ama kutokuleta kabisa fedha za CDG ama kutokuleta kabisa fedha za CDG na kusababisa miradi mingi kuwa viporo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mpaka sasa ipo miradi viporo ya miaka 10, tisa na nane. Halmashauri ya Wilaya peke yake kwa kipindi cha kuishia Juni, 2017 walikuwa na miradi ya viporo ya shilingi bilioni tano na walitenga shilingi milioni mia tano zikiwa ni fedha za CDG na mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza. Kwa hiyo, nimshauri Mheshimiwa Waziri aweze kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi iliyo viporo. Kama Halmashauri ya Wilaya ya Meatu peke yake tu inadai shilingi bilioni tano, na kwa mwaka mmoja tu imepanga milioni 500; kwa hiyo itachua miaka 10 kukamilisha miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Meatu ilikuwa na tatizo la uvamizi wa wanyama pori katika makazi ya wananchi pamoja na mashamba ya wananchi na kusababisha vifo ama mavuno yao kuliwa na wanyamapori. Hata hivyo sioni jitihada yoyote inayofanywa na Serikali ya kuwafidia wananchi ambao mazao yao yalikuwa tayari kuvunwa lakini yakaliwa na wanyama poli. Naiomba Wizara pia iweke mpango wa kulipa fidia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alisema Mkuu wa Wilaya ambaye ataleta tatizo la njaa latika Wilaya yake ataonekana kwamba hatoshi; lakini sisi Wilaya ya Meatu wananchi wamejitahadi lakini wanyamapori wamekula mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu ukamilishaji wa Daraja la Mto Sibiti. Ni muda mrefu sasa wananchi wamekuwa na kiu ya kuona daraja hilo sasa limekamilika. Hata hivyo tangu Septemba, 2016 katika kikao cha ushauri wa Mkoa tulihaidiwa kwamba vyuma vya kufunga daraja hilo vinatengenezwa China, lakini mpaka leo ni mwaka wa zaidi vifaa hivyo havijafungwa na tulihaidiwa kwamba masika hii tutapita. Mimi binafsi nimekuwa mpitaji wa hiyo sioni dalili yoyote ya kukamilika kwa daraja hilo. Binafsi ninaona mradi unaenda pole pole. Kukamilika kwa daraja hilo kutainua uchumi wa Mkoa wa Simiyu hususani katika Wilaya ya Meatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hata vifaa vya ujenzi vimekuwa vikipanda bei kutokana na mzunguko kwamba vipite Shinyanga ndipo vije Mkoani Simiyu, lakini kukamilika kwa daraja hili kutakuwa ni mkombozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu elimu ya bila malipo. Tunaishukuru Serikali kwa kuleta mpango wa elimu ya bila malipo. Hata hivyo mpango huu umesababisha ongezeko la udahili kwa wanafunzi na kusababisha upungufu wa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Meatu kuna changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu mpaka kwenda kusoma na kusababisha mahudhurio kuwa hafifu. Kwa mfano shule ya sekondari Mwamaloe form one walianza wanafunzi 78, lakini waliohitimu ni wanafunzi ni 23. Moja ya sababu iliyosababisha ni umbali mrefu. Kwa hiyo, wanafunzi waliacha shule kwa ajili ya umbali mrefu. Kwa maana hiyo ninaomba shule ya bweni ya Wasichana ya Nyalanja ijengewe uwezo ikiwa ni kuongezewa mabweni pamoja...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika hoja zilizoletwa na Kamati hizi mbili. Napenda nizipongeze kwa taarifa nzuri za Kamati zote hizi mbili. Kwa kuanza naomba nijikite katika taarifa ya hesabu za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ilijikita kufanya mahojiano na Halmashauri pamoja na kutembelea miradi ya maendeleo. Katika kufanya mahojiano na Halmashauri, hoja nyingi zilizojitokeza ni Halmashauri kutokujibu hoja za ukaguzi hususani katika hoja za miaka ya nyuma. Halmashauri zinafanya uzembe na mazingira yanaonesha kwamba hawataki kujibu hoja hizo kwa sababu siyo sehemu ya ku- form opinion. Nitoe ushauri kwa Serikali kuchukua hatua ya ziada ili hoja hizo ziweze kupatiwa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkaguzi wa Hesabu aliendelea kuibua hoja za ukaguzi ambazo nyingi zilisababishwa na upungufu uliopo katika kutumia mfumo wa kihasibu wa EPICAR. Kama Serikali haitachukua hatua ya ziada kuweza kutatua tatizo katika mfumo wa hesabu (EPICAR version 9.05) hoja nyingi zitaendelea kuibuliwa kutokana na mapungufu yaliyopo katika mfumo wa kihasibu wa EPICAR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu ulianza Julai 2012 leo ni miaka sita mfumo hauna asset modal ambayo inasababisha madeni kutokuripotiwa katika hesabu za mwisho ama Mkurugenzi kuamua kufunga hesabu kwa namna anavyotaka zionekane mwenyewe. Haina ubishi kwamba Mkurugenzi inamlazimu aichukue trial balance afanye export akafanye kwenye excel. Kwa hiyo, hii moja kwa moja anaweza akafanya udanganyifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu unatumia cash basis na tunajua Halmashauri zinatakiwa zifungwe hesabu kwa matakwa ya IPSAS na full adoption ya IPSAS kwa Tanzania katika Halmashauri ilikuwa ni mwaka 2013 lakini mpaka sasa hivi mfumo huu hauna accrual basis. Halmashauri zimeendelea kuandika LPO nje ya mfumo kwa sababu mfumo hau-support accrual basis.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama una-support cash basis ni changamoto kwa Halmashauri kununua vifaa kwa kutumia cash. Ni dhahiri kwamba siyo muda wote Halmashauri itakuwa na fedha taslimu. Kwa hiyo, inazilazimu Halmashauri ziandike LPO nje ya mfumo na hivyo kujikuta madeni mengine hayatolewi ripoti katika hesabu za mwisho. Kwa hiyo, ile hoja ya kulipa madeni ambayo hayakuwa kwenye hesabu za Halmashauri, hoja hii itaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ilifanya ziara katika Mkoa wa Tanga na mikoa mingine, naomba nijikite katika hoja kubwa ambayo ilijitokeza katika miradi, hoja ya upungufu katika miradi ya maji. Tunao mradi wa RWSSP ambao unatekeleza miradi ya maji vijijini. Changamoto mojawapo iliyopo kwanza katika RWSSP kuna component ya sanitation lakini component hiyo imekuwa haifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kukagua miradi ya Tanga ya maji, sikuwahi kuona mahali popote kwamba kuna miradi ya usafi wa mazingira. Tulienda Iringa kukagua miradi, miradi mingine ya maji imekamilika lakini ile component ya sanitation fedha zake amepewa Mkandarasi lakini miradi haijatekelezwa. Kwa hiyo, Serikali pia iangalie kipengele cha sanitation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi iliyokamilika ina jukumu…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Leah Komanya...

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba niongelee mwenendo wa maduhuli katika Halmashauri zetu. Ni dhahiri kwamba Halmashauri za Wilaya, ufanisi katika ukusanyaji wa mapato umekuwa wa kusuasua, Halmashauri katika mikakati yake ya kukusanya mapato imekuwa ikionesha lakini changamoto wanayoipata ni kutokuwa na sheria ndogo na sababu ya kutokuwa na sheria ndogo wamekuwa wakisema kwamba sheria zinacheleweshwa kusainiwa TAMISEMI. Hivyo nitoe wito TAMISEMI iwaishe kusaini sheria ndogo ili ufanisi wa mapato uongezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifuta baadhi vyanzo vya mapato ambazo vilikuwa kero katika bajeti ya mwaka 2017/2018 na ninaamini Halmashauri pamoja na Serikali Kuu zilifanya mapitio katika bajeti zao. Lakini cha kusikitisha Halmashauri zinaendelea kutoza mapato kwa vyanzo vilivyofutwa. Kwa mfano Halmashauri hiyo hiyo ina ushuru wa pamba imepunguza asilimia mbili, kwa hiyo inatoza asilimia tatu, lakini Halmashauri hiyo hiyo inaendelea kutoza chanzo kilichofutwa kwa mfano kusafirisha mifugo ndani ya Wilaya. Ukimuuliza mkurugenzi kwa nini anafanya double standard anasema hana mwongozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Mkurugenzi asitumie kigezo alichotumia kuteremsha ushuru wa pamba akatumia hicho hicho kigezo kutoza ushuru wa kusafirisha mifugo. Hapa tunawaonea wananchi wetu na tunawaweka katika matabaka. Kwa hiyo ninaomba Wizara husika ilete miongozo ili halmashauri ziweze kurekebisha sheria ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango wangu katika Bajeti Kuu. Kwanza naomba kuunga mkono hoja hii ya bajeti ya Serikali kwa kuwa inakwenda kujibu matatizo ya wananchi wetu. Niipongeze Serikali kwa namna inavyoanza kutekeleza miradi ya vielelezo ambayo itakwenda kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Reli hii kwa Mikoa ya Magharibi inakwenda kuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi kwa kushusha gharama ya usafirishaji na gharama ya maisha. Reli hii inakwenda kusaidia kushusha bei ya saruji kwa kupunguza gharama ya usafirishaji, kwa sababu Mikoa ya Magharibi haina kiwanda cha saruji na saruji hii imekuwa ikisafirishwa kwa mfuko Sh.5,000/= kwa hiyo na kuongeza bei ya saruji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, bei ya saruji baadhi ya Wilaya ni Sh.16,000/= wakati wilaya nyingine ni Sh.12,000/= hadi Sh.13,000/=. Inakwenda kushusha bei ya gharama ya kusafirisha ng’ombe kutoka Mikoa ya Magharibi na kuleta mikoa mingine. Inakwenda kupunguza gharama ya usafirishaji wa marobota ya pamba kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa na kupeleka bandarini Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha nje. Reli hii inakwenda kusaidia kupokea mizigo kutoka nchi ya Rwanda ambayo itapita reli ya kati na kuongeza kodi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niipongeze Serikali kwa kuleta marekebisho kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ili kupunguza ushuru wa mazao unaotozwa na Halmashauri za Wilaya kutoka kiwango cha asilimia tano hadi tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali kwa msimu mfululizo katika Awamu hii ya Tano, bei ya pamba mwaka jana ilitoka Sh.600/= mpaka Sh.1,000/=, mwaka huu bei ya pamba kwa kilo ni Sh.1,200/=, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwajali wakulima wa pamba. Kwa kupunguza ushuru huu pia kwa bei ya mwaka huu tunakwenda kuongeza Sh.24/= kwa kila kilo, lakini bado upo wigo mwingine, Serikali inaweza ikaangalia ni wapi pia iweze kupunguza tozo ili iweze kumwongezea mkulima bei ya pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Uendelezaji Zao la Pamba. Mkulima amekuwa akichangia Sh.15/= na mnunuzi amekuwa akichangia Sh.15/=, sawa na Sh.30/= kwa ajili ya uendelezaji wa zao la pamba. Fedha hizi kwangu mimi naziona ni nyingi, kwa mfano 2015/2016 tani 149,000 zilikusanywa, mfuko huu uliwekewa Sh.4,483,350,000/=. Naishauri Serikali ifuatilie matumizi ya fedha hizi ili iweze kulinganisha, je, matumizi ya hizi bilioni nne yanamsaidia mkulima wa pamba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hakuna tija mnunuzi apunguziwe Sh.10/= na mkulima apunguziwe Sh.10/=, wachangie shilingi tano tano, naamini itakwenda kusaidia katika kuendeleza zao la pamba katika mambo ya utafiti. Ukizingatia Serikali imekuja na mbegu mpya ambayo inaongeza uzalishaji, kwa hiyo kilo za pamba zinakwenda kuongezeka na fedha zinakwenda kuwa nyingi sana, kwa hiyo Sh.10/= pekee inatosha kuendeleza zao la pamba katika shughuli za utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia kuna tatizo katika ucheleweshaji wa usambazaji wa mbegu na dawa na wakati mwingine hayatoshelezi. Nashauri Mabaraza ya Madiwani yapewe mamlaka ya kuweza kuuhoji huu mfuko ili utekelezaji uweze kuharakishwa. Kwa kufanya hivyo, naomba mfuko huu kama kuna viongozi wa kisiasa wasiwe viongozi katika Mfuko wa CDTF ili kuepuka mgongano wa maslahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee athari zitakazopatwa na Halmashauri kuhusu kupunguza ushuru huu. Halmashauri za Mkoa wa Simiyu zaidi ya asilimia 60 ya bajeti yake ya mapato zinategemea ushuru wa pamba. Naishauri Serikali ifanye kama ilivyofanya 2003, baadhi ya vyanzo vya mapato vilivyokuwa kero kwa wananchi vilifutwa, Serikali ilifanya mapitio kuangalia athari ya bajeti na baadaye Halmashauri hizo zilifidiwa. Naomba Serikali iweze kufidia Halmashauri zitakazoathirika kwa kushuka tozo ile kwa asilimia mbili kwa sababu zitashindwa kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/2017, umeendelea kutekeleza maeneo ya kipaumbele kwa kufungamanisha maendeleo ya uchumi na watu. Serikali imeendelea kusomesha kwa wingi kwenye fani za ujuzi maalum ambao pia ni adimu ili kuendana na mahitaji katika viwanda tarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa wana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipatia muda ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Mambo ya Ndani. Awali ya yote, naomba nimpongeze na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya, Mheshimiwa Rais amekuwa akiguswa na matukio yanayohusishwa na wananchi kuuawa kutokana na ajali na matukio mbalimbali na Mheshimiwa Rais amekuwa akichukua hatua mara moja bila kusita. Naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri toka ateuliwe, akishirikiana na wasaidizi wake pamoja na Naibu Waziri wameweza kusimamia vizuri Wizara ya Mambo ya Ndani na kuweza kudhibiti matukio makubwa ambayo yalikuwa ni tishio kwa usalama wa raia yakiwemo uvamizi mkubwa katika mabenki yetu ambao ulikuwa ukigharimu maisha ya raia pamoja na askari wetu.

Mheshimiwa Spika, mauaji ya watu wenye albino, mauaji ya watu wenye albino yameweza kudhibitiwa, tumekuwa hatusikii yakiripotiwa. Naomba niwapongeze sana. Naomba pia nipongeze kwa upande wa mauaji ya vikongwe; sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa, jambo hili lilikuwa kero na lilitutia aibu wananchi tunaotoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa, lakini nipongeze Jeshi hili limeweza kudhibiti mauaji ya wazee wetu vikongwe. Vile vile ajali za mabasi zimekwisha ama zimepungua, matukio yamekuwa hayaripotiwi. Naomba waendelee hivyo hivyo walivyoanza kwa kuendelea kutoa elimu kwa madereva pamoja na raia.

Mheshimiwa Spika, Askari hao wanafanya kazi nzuri sana lakini wana changamoto katika mazingira ya kufanyia kazi pamoja na vitendea kazi ofisini. Ukifika vituo vya polisi hata karatasi za kuandikia maelezo ya mtuhumiwa wanapata shida, inalazimu wakati mwingine kuomba waletewe na hii pia itaweza kusababisha wasitende haki kwa sababu hata vitendea kazi havipo.

Mheshimiwa Spika, nyumba wanazoishi ni shida, naomba waongezewe bajeti ya kutosha ili askari waweze kujengewa nyumba bora, waweze kutoka uraiani. Vile vile nishukuru kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kukamilisha maboma katika Wilaya ya Meatu ambayo yalikuwa ya mwaka toka 1999. Maboma haya nimekuwa nikiyaongelea toka nilipoingia Bungeni na swali langu la pili lilikuwa kukamilisha maboma hayo. Nawashukuru kwa sasa wametenga bajeti kwa ajili ya kukamilisha maboma.

Mheshimiwa Spika, pia niongelee upande wa dawati la jinsia. Dawati la jinsia lipo kwenye level ya wilayani katika kituo cha Polisi, lakini ukatili mkubwa unafanyika katika ngazi ya chini. Naomba waboreshe waone namna gani wanaweza wakafanya ili kuweza ku- accommodate yale matukio kwa wakati yanayotokea katika ngazi za chini, kwa sababu matukio mengi ya ukatili yanafanyika katika ngazi ya nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti ajali za bodaboda, pia naomba elimu itolewe kwa raia pamoja na waendesha bodaboda hususan katika uvaaji wa helmet, nashauri ili waweze kuvutia uvaaji wa helmet…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. LEAH J. KOMANYA: Usafi uzingatiwe.

Mheshimiwa nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipatia nafasi jioni ya leo nami niweze kutoa mchango wangu. Awali ya yote, napenda kuwapongeza na kuwashukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanazozifanya, wamekuwa wakinipa ushirikiano ninapowafuata. Moja ya ushirikiano walionipa ni tarehe 16 Mei, katika swali langu waliponijibu kwamba sasa Wizara itaanza kutoa takwimu kwa kila halmashauri ili ziweze kujua ni kiasi gani cha fedha za uwindaji ama upigaji picha wa kitalii kimepatikana katika eneo husika la uhifadhi ili halmashauri ziweze kufuatilia fedha yao ambayo ni asilimia 25. Halmashauri zimekuwa zikipewa asilimia 25 ya uwindaji wa kitalii bila ya kujua msingi wa tozo ya hiyo asilimia 25. Naamini kuanzia tarehe 1 Julai, walivyoahidi tutaanza kuziona takwimu hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema bado pale pana changamoto, fedha hizi tumekuwa tukifuatilia Wizarani unaambiwa hazipo kisheria kwa maana hiyo tunapewa kama hisani. Kama ni hisani basi ni muda muafaka sasa sheria hiyo iletwe ili sisi tuweze kuipitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni ya huo mgawanyo wa asilimia 25, sababu asilimia 60 inatakiwa iende katika vijiji, asilimia 40 ibaki katika Idara ya Wanyamapori ili iendeleze mambo ya uhifadhi. Changamoto iliyopo zile asilimia 60 hazipelekwi na halmashauri kwa sababu zinaingia katika mfuko wa amana na kufanya matumizi mengine. Nashauri sasa kwa kuwa vijiji vina akaunti, fedha hiyo ipelekwe moja kwa moja katika vijiji ili na wenyewe wawe na ule mwamko wa kuhifadhi maliasili na kupambana na ujangili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini wananchi walioko kandokando ya hifadhi wanafanya kazi hiyo kwa sababu nikiangalia katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ambapo mchango wangu wa leo utajikita huko katika hifadhi ya wanyamapori, kumekuwa na uvamizi mkubwa wa wanyamapori wakubwa na wakali ambao wanavamia makazi ya wananchi na kuleta taharuki katika maisha ya wananchi na wakati mwingine kusababisha vifo. Kumekuwa pia na uharibifu wa mali, mashamba na mazao ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu wamekuwa na juhudi mbalimbali za kukabialiana na wanyama hao. Makundi makubwa ya tembo yamekuwa yakiingia hasa nyakati za usiku, tembo wanne mpaka sitini, hali hii inakuwa ni ngumu mpaka wanapeana zamu za usiku kwenda kulinda. Wametumia mbinu mbalimbali ikiwemo kutumia mavuvuzela. Waheshimiwa Wabunge tumenunua mavuvuzela, mwanzo yalikuwa yanafanya kazi lakini baadaye hayafanyi kazi ikawa kama vile tembo wale tunawapigia muziki. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2016/2017, heka 135 ziliharibiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, katika miezi hii mitano ya mwaka huu hekari 200 zimefanyiwa uharibifu. Kwa hiyo, wananchi wameingia katika tatizo la njaa. Naheshimu maamuzi ya Mheshimiwa Rais kwamba hakutakuwepo na chakula cha bure kwamba wananchi wafanye kazi. Hilo nalikubali na naliunga mkono na naona wanachi wamelima, mazao ni mengi lakini changamoto iliyopo wananchi wa vijiji vile mazao yao yaliliwa na tembo. Kwa hiyo, Serikali inapofanya uamuzi sasa iangalie maeneo mengine mahsusi ambapo wananchi hawakujitakia wenyewe isipokuwa ni tembo ndiyo walisababisha. Viongozi wamekuwa waoga kufanya maamuzi ili kuyaleta juu kuelezea hali halisi ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema mbele yako leo hali si nzuri katika maeneo yale. Naomba vijiji vile viangaliwe kwa upande mwingine siyo kuogopa tamko la Mheshimiwa Rais. Viongozi wengine wanaogopa matamko ya Rais na kuyatasfiri visivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa halmashauri wa kukabiliana na changamoto dhidi ya wanyamapori waharibifu ni kubwa sana. Kwanza eneo la hifadhi ni kubwa. Ukiangalia Halmashauri ya Wilaya ina kilomita za mraba 8,835, eneo la hifadhi ni karibia nusu kwa sababu lina kilomita za mraba 3,900 sawa na asilimia 44.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili kubwa la hifadhi kuna mwingiliano mkubwa wa matumizi ya rasilimali zilizopo kati ya wanyamapori na wananchi. Rasilimali hizo ikiwa ni matumizi ya maji pamoja na malisho. Nakubaliana na hotuba ya Kamati kwamba katika vijiji vinavyopakana na hifadhi pachimbwe visima au mabwawa ili wananchi hao wapate maji, wasiende kuchangia na wanyamapori katika mito iliyopo kandokando. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo nyingine ni malisho. Pamoja na agizo lililopo nashauri kwa upande wa pili basi katika buffer zone tuangalie hata mita 500 tuwape hawa wananchi. Naamini ndiyo watakuwa walinzi wa ujangili na wako tayari kuweka mipaka. Tukiangalia Tanzanite ukuta umejengwa ili kuhifadhi Tanzanite yetu, hata sisi tuko tayari kuhifadhi wanyamapori, tunaweza tukaweka hata mipaka ambayo haina gharama kubwa ili mradi wananchi waweze kujipatia malisho kwa ajili ya mifugo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la uhifadhi la kilomita hizo za mraba, asilimia 70 linajulikana kwamba ni eneo la wanyama wanaohama yaani migratory belt. Asilimia 70 ya hawa wanyamapori wanakaa nje ya maeneo yale maalumu ya hifadhi. Hii ni changamoto kubwa sana kwa halmashauri yetu, ukiangalia asilimia 70 ya hao wanyama tena wanakaa nje ya yale maeneo yao, maana yake wanakaa vijijini. Changamoto iliyopo ni uhaba wa watumishi, tuna watumishi watatu tu, naomba idara iongezewe watumishi. Pia tuna changamoto za vitendea kazi kama silaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwiba Holding Company kwa kununua silaha tatu, Mzinga Corporation. Naomba sasa mchakato wa kumilikishwa zile silaha uharakishwe kwa kuanzia na kwa OCD wa Wilaya ya Meatu maana toka apelekewe mwezi wa pili hajaanzisha mchakato huo na mchakato ni mrefu. Kupitia Bunge hili naomba mchakato huo upelekwe haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la Operesheni Tokomeza silaha saba zilichukuliwa mpaka leo hazijarudishwa. Naomba Wizara warudishieni sasa hao watumishi hizo silaha. Mmeyaona hayo makundi makubwa ya tembo pamoja na wanyamapori wakali wakiwemo na viboko ili wale watumishi waweze kupambanana nao. Ainza za silaha zile nina orodha pamoja na namba zake. Naomba sasa zile silaha zilizochukuliwa wakati wa zoezi la Tokomeza ziweze kurejeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri…

Mheshimiwa Mwenyekiti, nauga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa maoni yangu katika mpango wa bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kuipongeza Wizara ya Fedha kwa namna ilivyotuletea mpango na kwa jinsi ilivyojikita zaidi kufuta tozo au kodi zilizokuwa kero kwa wananchi, naipongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuanza mchango wangu, naipongeza Serikali kwa namna ilivyoanza kulifufua zao la pamba kiasi kwamba sasa kumeanza kuwepo matumaini kwa wakulima wa pamba katika Mkoa wa Simiyu na Kanda ya Ziwa kwa ujumla. Naipongeza Serikali kwa kufuta mchango uliokuwa ukitozwa, Sh.30 kwa kila kilo kwa ajili ya kuendeleza zao la pamba. Mchango huu haukuwa na tija kwa sababu Mfuko huu ambao unajulikana kama CDTF haukuwa na tija yoyote, haukuweza kumsaidia mkulima na badala yake uliendelea kuleta pembejeo hafifu na uzalishaji uliendelea kupungua. Kwa mfano, takwimu za msimu 2015/2016, zilikuwa tani 149,000 na kupungua zaidi katika msimu wa 2016/2017 ambapo zilivunwa tani 121,000. Kwa hiyo, hakukua na tija yoyote kuwepo kwa mfuko huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kazi zilizokuwa zinafanywa na Mfuko huu zitafanywa na Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na Maafisa Kilimo walioko katika halmashauri zetu. Kwa sababu muda wote ule kulikuwa na mgongano wa maslahi, mkulima alikuwa anamfahamu tu Bodi ya Pamba pamoja na Mfuko ule kwa sababu ndo uliokuwa unapelekea pembejeo ya mbegu na dawa kiasi kwamba Afisa Kilimo hakupewa nguvu yoyote au hakuthaminika kwa mkulima kuweza kulisimamia zao hilo kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina shauri sasa Serikali kupitia halmashauri iwawezeshe Maafisa Kilimo kikamilifu kwa sababu kila Kata kuna Afisa Kilimo. Iwawezeshe usafiri na iwawezeshe kwa namna yoyote ili waweze kulisimamia lile zao badala ya Bodi ya Pamba ambayo ina mtu mmoja tu katika Wilaya ndiyo aliyekuwa anasimamia zao hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali kwa kufufua ushirika na kwa msimu huu imeanza kununua pamba kupitia vyama vya ushirika. Nafahamu mwanzo ni mgumu, sisi Wabunge tuko nyuma yenu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jitihada zote anazozifanya kulisimamia hili zao. Mheshimiwa Waziri Mkuu mimi niko nyuma yako nitaendelea kukupa ushirikiano ambao ninaweza kukupa ili kuweza kufikia malengo ambayo Serikali inatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini sasa zao hili linaenda kuwa mikononi mwa Serikali, Serikali itakuwa na uwezo wa kuweza kulitolea maamuzi yoyote tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Naamini sasa vile vyama vinaibuka na kutoza hela kwenye ushuru huo sasa vinaenda kujifuta vyenyewe kupitia ushirika. Halmashauri za Wilaya zinaenda kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kutoza ushuru wa pamba. Nachoshauri vile vitabu vinavyotumika Wakurugenzi waone kwamba ni nyaraka muhimu kwa sababu zinaenda kutumika kukokotoa kupata takwimu sahihi badala ya ule mgongano uliokuwepo baina ya Halmashauri na Bodi ya Pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tatizo lililopo hatuna Maafisa Ushirika wa kutosha. Halmashauri zetu zina Afisa Ushirika mmoja mmoja wengine wanaenda kustaafu mwezi wa sita. Kwa kipindi hiki cha mpito Maafisa Ushirika ni wa umuhimu kwa ajili ya kufufua ushirika, kwa sababu mara tu baada ya msimu ukaguzi unatakiwa ufanyike mara moja ili vyama vya ushirika vijiendeshe kwa faida. Bila Maafisa Ushika tunaenda kurudi nyuma, mapato yanayotokana na ushirika kwa vyama vya ushirika hayatajulikana badala yake tutaendelea kutengeneza hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hiki ni muhimu sasa kuwezesha kuwepo kwa COASCO kwa ajili ya ukaguzi ili baadaye tusirudi kule tulikotoka. Kwa mfano, Wilaya ya Meatu ina AMCOS 80, ina vituo vya kununulia pamba 200, lakini Afisa Ushirika aliyepo ni mmoja. Je, ni nani anaenda kukagua mapato na matumizi ya vyama vya ushirika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali kwa kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani katika taulo zinazotumiwa na akina mama na wasichana wakati wa hedhi,. Kufuta tozo hiyo inaenda kumpunguzia mwanamke mzigo kwa kiasi fulani. Naishauri Serikali bado ina nafasi kubwa ya kumsaidia mwanamke kupunguziwa bei ya taulo hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nikiangalia pedi nyingi zinatoka nje, sisi Tanzania tunatumika kama wasambazaji, pamba inayozalishwa asilimia 30 tu ndio inayotumika nchini asilimia 70 inaenda nje. Hii inamaanisha kwamba hatuna viwanda vya kutosha vinavyoweza pia kutengeneza pedi. Hata pedi tunazotengeneza nchini pamba inayotumika inaenda nje kwanza ndipo inarudi Tanzania kwa ajili ya kutengeneza. Kwa hiyo, Serikali inalo jukumu kubwa la kuhakikisha sasa tunakuwa na viwanda vya kutosha ili sasa asilimia kubwa ya pamba iweze kutumika nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali katika ukurasa wa 85 umesema kwamba unaongeza uzalishaji wa mbegu bora za pamba aina ya UKM09 tani 40,000. Pia, inaenda kutenga maeneo kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu hiyo; kutoa elimu kwa ajili ya wakulima; na kutoa vitendea kazi na kuhamasisha wakulima. Ukiangalia mikoa iliyotajwa Simiyu haijatajwa kama inaenda kuwezeshwa na hapo hapo Serikali imepanga shilingi bilioni 6.1 kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo. Ukiangalia Mkoa wa Simiyu pia asilimia 60 ya pamba inayozalishwa nchini inatoka Mkoa wa Simiyu. Kwa hiyo, naiomba Serikali Mkoa wa Simiyu na wenyewe uwemo katika kuwezeshwa kwa namna Serikali ilivyojipanga kuwezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Simiyu unacho kituo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu. Namshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuniwezesha kusimama hapa jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kuipokea hoja hii ya bajeti ya Wizara ya Maji na naiunga mkono na natoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa namna wanavyojituma katika shughuli za maji. Nitoe shukrani zangu za dhati kwa jinsi walivyounusuru Mradi wa Maji wa Bwawa la Mwanjoro kutoka Wilayani Meatu kwa sababu bwawa hili lilikuwa limetelekezwa toka mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, nikijielekeza upande wa hotuba, naomba kuongea kuhusu huduma ya maji vijijini. Katika kitabu cha hotuba ukurasa wa saba, Wizara imesema kwamba imejenga vituo vya kuchotea maji 123,000 na vituo 85,000 ndiyo vinavyofanya kazi tu. Kwa hiyo, ukiangalia pale ni vituo 38,000 ambavyo havifanyi kazi ambapo ni sawa na asilimia 30. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukienda zaidi Wizara imeona changamoto inayosababisha vituo visitoe maji ni usimamizi pamoja na uendeshaji wa miradi hii unaosababishwa na uendeshaji kwa kutumia dizeli. Naiomba Wizara iende zaidi kuangalia changamoto inayosababisha vituo visifanye kazi ikiwa ni pamoja na usanifu mbovu, usimamizi mbovu na utafiti mbaya. Kama Wizara itazichukua hizo sababu nyingine tatu kama changamoto, itaweza kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa sababu tumeona usanifu umekuwa ukifanyika chini ya viwango, utafiti mwingi wa maji unafanyika wakati water table iko juu na kusababisha maji kupatikana wakati wa masika tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichangie kuhusu mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria na kuyaleta katika Makao Makuu ya Wilaya ya Busega ambayo ni Nyashimo, Bariadi pamoja na Itilima. Utekelezaji wa mradi huu imekuwa ni muda mrefu sasa. Toka Septemba, 2016 Waziri wa Mazingira alitujulisha kwamba fedha tayari zimeshaletwa lakini mpaka leo usanifu unafanyika. Naomba usanifu uishe haraka ili mradi utekelezwe kwa sababu maji yanahitajika kwa ajili ya hiyo miji mipya ya kiutawala iweze kujengeka. Nyashimo ni Makao Makuu ya Wilaya ya Busega, Bariadi ni Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu na Itilima na Makao Makuu ya Wilaya ya Itilima yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maji haya pia ni muhimu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na fedha hizi zililetwa kwa ajili ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa namna unavyochelewa kutekelezwa maana ya makusudio ya kuletwa hii fedha itakuwa haipo.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee Mradi wa Maji wa Kitaifa wa Wilaya ya Maswa. Katika kitabu cha bajeti wamesema kwamba utekelezaji wa ujenzi wa mtambo na kuchujia na kutibu maji unaendelea kukamilika na kwamba mradi utakamilika Mei, 2018 ambao ni mwezi huu. Ukiangalia muda wa mkandarasi wa kufanya kazi umekwisha lakini kazi haijakamilika. Mtambo huu utatumika kuchuja, kusafisha na kutibu maji lakini ukiangalia bwawa lile halina maji, limejaa tope. Kwa hiyo, hapa mimi naishauri Serikali itenge fedha kwa ajili ya kutoa tope hilo ili kuweza kuongeza kina cha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee mradi wa skimu ya umwagiliaji iliyopo Wilaya Meatu ambapo mimi ni Mjumbe wa Baraza la Madiwani pia ni mjumbe wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji. Ipo skimu ya umwagiliaji Kijiji cha Magwila na ilianza kutekelezwa 2012/2013 na ungekamilika 2013/2014 lakini mpaka leo mradi huu haujakamilika. Fedha iliyotumika ni shilingi 1,165,000,000 na kazi iliyofanyika ni kujenga chujio, kujenga mfereji wa kati wa mita 1,000 kati ya mita 7,000 pamoja na sehemu 12 za kusambazia maji. Shilingi bilioni 1 ikawa imetumika na imekwisha lakini mradi huo mpaka leo haujakamilika kwa ajili ya kunufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, mimi nataka Mheshimiwa Waziri aieleze jamii ya Meatu kwa nini mradi huu haujakamilika? Kwa sababu fedha ilikuwa ya Mfuko wa Maendeleo ya Benki ya Afrika na usimamizi ulikuwa unafanywa na DASIP Kanda ya Mwanza. Halmashauri ya Wilaya haikuhusika na chochote katika usimamizi wa kiufundi. Mshauri wa mradi ilikuwa ni kampuni kutoka Jijini Nairobi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kujua ni lini mradi huu utatekelezwa? Naishauri Serikali ikamilishe sehemu iliyobaki ya mita 6,000 ya mfereji wa kati pamoja na kujenga mfereji mkuu ili sasa ule mradi uweze kufanya kazi. Pia naomba mradi huu ufuatiliwe ili kuona kama thamani ya fedha ipo. Maana mradi huu ungekamilika ungeweza kusaidia kaya 123 za kijiji hicho kati ya kaya 650 na ungeweza kusaidia upatikanaji wa mbogamboga na mazao mengine kwa Wilaya nzima ya Meatu.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipatia nafasi hii, nikianza na kuunga mkono kwa asilimia mia moja hoja iliyoletwa mbele yetu na Wizara ya Maji. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kazi nzuri anazozifanya katika Wizara hii, Mheshimiwa Waziri nampongeza amekuwa akitembelea mazingira yetu na kuona hali halisi ya upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kufanya masahihisho katika ukurasa wa 56 wa hotuba. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri imesema kwamba, nishukuru kwanza kwa Serikali kutoa shilingi bilioni 1.7 ili kukamilisha Bwawa la Mwanjolo, lakini nataka kusema kwamba maelezo yalitolewa katika kitabu kwamba tayari wananchi wa Mwanjolo, Jinamo, Mbushi Wilayani Meatu wanapata huduma ya maji wananchi 13, 859 siyo sahihi. Kilichopo hapa ni mabirika ya maji kwa ajili ya mifugo, ndiyo wanaokunywa maji. Usambazaji wa maji katika vijiji vilivyotajwa hapa haujafanyika. Ninachoomba fedha kwa ajili ya kufanya usanifu kwa ili kusambaza maji kwa wananchi katika vijiji tajwa hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali na kuishukuru kwa kusaini mkataba wa shilingi bilioni 330 kwa kutoa maji Ziwa Victoria kwa ajili ya Mkoa wa Simiyu na kuyapeleka Nyashimo, Bariadi pamoja na Itilima ambao utekelezaji wake utakamilika mwaka 2022. Nataka nitoe maoni yangu machache; toka mwaka 2016, Wabunge wa Mkoa wa Simiyu tumekuwa tukiomba mradi huu yajengwe mabomba mawili, lakini fununu niliyoisikia kwamba linajengwa bomba moja. Kama litajengwa bomba moja dhana nzima ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi haitakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zilitafutwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa lengo kuu la kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi katika Mkoa wa Simiyu ambao umekumbwa na ukame wa muda mrefu, endapo kama litajengwa bomba moja wananchi hawataweza kumudu maji haya kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Lengo kuu lilikuwa ni kukabiliana kwa kilimo cha umwagiliaji, kama litajengwa bomba moja maji haya yakitibiwa gharama yake itakuwa juu wananchi hawataweza kuyanunua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri mawazo ya Wabunge yasikilizwe kuwe na mabomba mawili ambayo litakuwa na maji ghafi ambayo hayajatibiwa ambayo hayatakuwa na gharama kubwa ili wananchi waweze kuyamudu kwa ajili ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa kuwa mradi huu unatekelezwa kwa awamu mbili na Wilaya ya Meatu na Maswa ni Wilaya zilizo na ukame mkubwa...

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu. Awali ya yote napenda kupongeza Wizara ya Fedha kwa kazi wanazofanya ikiwemo za upelekaji fedha katika Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika kitabu cha hotuba ukurasa wa 32 Wizara imetoa mafunzo kwa Maafisa Ugani na Ununuzi 75 kwa ajili ya mafunzo ya kutumia mfumo wa malipo wa Serikali EPICOR. Hata hivyo, mafunzo haya hayatakuwa na tija kama Serikali haitarekebisha upungufu uliomo katika mfumo wa EPICOR, kwa sababu mfumo huu unatumia cash basis. Kwa hiyo LPO sasa hivi zinaandaliwa kwa kutumia cash tu, asilimia kubwa ya LPO zinatumiwa nje ya mfumo, kwa hiyo dhana zima ya internal control au udhibiti wa ndani haipo.

Mheshimiwa Spika, upungufu mwingine pia upo ikiwemo asset management bado hazijawekwa humo, naishauri sasa Wizara ione namna inavyoweza kutekeleza kuweza kuingiza package ambazo zinazopungua katika mfumo mzima wa EPICOR.

Mheshimiwa Spika, nishauri pia Wizara ijitahidi kuweka mfumo ambao utaweza ku-link mifumo mbalimbali kama PLANREP ili sasa taarifa mbalimbali ziweze kutoka katika mfumo wa EPICOR badala ya taarifa nyingine kutengenezwa nje ya mfumo ama taarifa baadhi za ufungaji wa hesabu zikafanyikia nje ya mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia niipongeze Wizara kwa namna inavyopeleka fedha za elimu bila malipo, inapeleka vizuri, nimeangalia katika kitabu cha CAG hoja iliyopo ni ndogo tu shilingi bilioni moja haikupelekwa na upungufu huu ulitokana na Wizara yenyewe kule ya Elimu ambako kulikuwa kuna utofauti wa takwimu. Kwa hiyo, naipongeza kabisa kwa namna inavyopeleka fedha za elimu bila malipo. Niipongeze pia Wizara kwa kupeleka fedha za ujenzi wa vituo vya afya au kuboresha vituo vya afya. Vituo vyetu sasa hivi vilivyoboreshwa vina hadhi nzuri kiasi kwamba wananchi sasa hivi wana mvuto wa kwenda hospitali za Serikali.

Mheshimiwa Spika, nipongeze pia kwa namna inavyopeleka halmashauri ruzuku za matumizi ya kawaida. Kumekuwa hakuna na matatizo ya upelekaji wa ruzuku za kawaida, lakini tukumbuke kwamba ruzuku hizi zilipunguzwa kutoka asilimia 100 mpaka 40. Ukiangalia pale pale mahitaji ya halmashauri yako pale pale, stahiki za watumishi ziko pale pale, mtumishi anatakiwa aende likizo, mtumishi anatakiwa agharamiwe masomo.

Mheshimiwa Spika, kwa kupunguza hiyo asilimia kutoka 100 mpaka 40 kumekuwa na changamoto kubwa sana inayozikumba halmashauri katika upungufu wa fedha. Pamoja na hayo halmashauri zilitegemea sasa wangetumia fedha za mapato ili kuweza ku-accommodate shughuli za idara zinazopata ruzuku.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ilizozikumba halmashauri ni mapato mengine kuchukuliwa na Serikali Kuu na mapato mengine kupunguzwa. Kwa mfano, Mkoa wa Simiyu ushuru wa pamba ulipunguzwa kutoka asilimia tano hadi tatu kwa ajili ya standardize bei ya pamba. Halmashauri za Mkoa wa Simiyu zaidi ya asilimia 60, bajeti yake inatumia ushuru wa pamba.

Mheshimiwa Spika, changamoto zimeendelea kuzikumba halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zake. Ukiangalia kazi ziko pale pale, Waheshimiwa Madiwani wako pale kwa mujibu wa Sheria, wanahitaji kulipwa, wanahitaji kufanya ziara, lakini saa hizi Madiwani hao wamekuwa wakikopwa fedha kwa muda mrefu zaidi hata ya miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hao hao Madiwani tunategemea wakasimamie miradi ya maendeleo. Ukiangalia sasa hivi Serikali imejikita kutumia force account hilo ni jambo jema. Hapo hapo ukiangalia force account hiyo Wahandisi wengi wemeenda TARURA. Kwa hiyo, Madiwani ambao ni Wenyeviti wa WDC wanapaswa kusimamia ile miradi. Changamoto ukiangalia wenyewe kwanza hawana fedha wamekopwa, halafu wanaenda kusimamia force account ambayo kwa kiasi kikubwa ina-involve cash, pale Serikali ifanye tathmini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba Wizara ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha wafanye review kwa sheria ambazo tumezipitisha. Kwa mfano wa kupunguza rukuzu ya matumizi ya kawaida kutoka asilimia 100 hadi asilimia 40, kuondoa vyanzo vya mapato, wafanye review waangalie ni athari gani zilizopo katika halmashauri. Ikiwezekana sasa halmashauri hizi ziweze kupewa fidia, kama ilivyofanyika 2013 baada ya kupunguza vyanzo vilivyokuwa kero kwa wananchi, halmashauri zilipatiwa fidia mpaka leo hiyo fidia inaletwa. (Makofi)

Mheshimia Spika, naomba pia niongelee kuhusu upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo, nikijikita katika ruzuku ya uendelezaji wa mitaji za Serikali za Mitaa LGCDG au inavyojulikana kwa CDG. Ni miaka mitatu sasa hivi fedha hiyo imekuwa haipelekwi, fedha hiyo ni ya Wafadhili lakini sio asilimia 100. Kuna sehemu ambayo ni fedha ya mapato ya ndani ambayo inajulikana, kama Local kuna foreign na Local. Hata hivyo, ukiangalia hata zile fedha za local hakuna fedha iliyopelekwa katika miradi ya CDG. Kama wafadhili hawaleti je, Serikali ambayo inakusanya kwa nini haipeleki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali sasa ione namna inavyoweza kuinusuru miradi hii iliyotekelezwa kwa fedha ya CDG kwa sababu kila mwaka tunaopanga wananchi lazima waibue miradi na kuianzisha kwa ule mfumo wa C-matching. Kwa hiyo, miaka mitatu tumekuwa tukilimbikiza magofu, magofu, magofu kiasi kwamba tunawapelekea wananchi wanakuwa hawana imani sasa na Serikali waanza kupoteza imani kwa Serikali. Wananchi sasa hivi wametokea kuiamini sana Serikali ya Awamu Tano, sasa tusiwakatishe tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya TAMISEMI ilifanya kikao iliwaita Waheshimiwa Wenyeviti na Wakurugenzi kwamba, waainishe miradi inayoweza kutekelezwa ambayo inaweza kumalizwa na fedha ya CDG ili sasa iletwe, lakini mpaka ninavyoongea sasa hivi fedha haijaletwa. Tukumbuke halmashauri zingine ziliitisha Mabaraza Maalum, wakatumia fedha ili kuweza kupitisha miradi ambayo sasa inaweza ikatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri tuone namna tunavyoweza kui-rescue hii miradi, mingine ina miaka 10, mingine ina miaka mitano na kama Mfadhili haleti fedha kwa nini tunaendelea kubajeti? Nashauri kama mfadhili hajaonesha nia ya kuleta basi kwenye hicho kifungu tuweke token figure ili mfadhili atakapoleta tufanye supplementary budget, kuliko kuendeleza kulimbikiza magofu, watoto wetu hawana madarasa, zahanati zetu hazijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu jioni hii ya leo, nikimshukuru Mungu kwa kuniweka niweze kutoa maoni. Awali ya yote, napenda nipongeze Wizara kwa kutuletea mpango mzuri ambao umeambana na utekelezaji wa shughuli za maendeleo uliotekelezwa kwa vipindi vilivyoainishwa katika kitabu cha mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango utajielekeza kwa kupongeza Serikali kwa kazi ilizozifanya kwa kuwa tumeletewa utekelezaji wa miradi ya maendeleo pia na kutoa ushauri katika Mapendekezo ya Mpango kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais na kumshukuru kwa ziara aliyoifanya Mkoani Simiyu mapema mwezi Septemba ambapo alifungua Hospitali ya Mkoa ya Rufaa. Kufunguliwa kwa Hospitali ya Mkoa katika Mkoa wa Simiyu kutaenda kuwapunguzia wananchi kutembea umbali kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyango ambapo kulikuwa kuna umbali wa kilometa 140. Kwa kufanya hivyo pia tutaweza kunusuru vifo ambavyo vilitokana na kusafirishwa kwa mgonjwa na kufariki kabla ya kupatiwa hata huduma wakati wa kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais akiwa Mkoani Simiyu alizindua vituo vya afya, maabara pamoja na wodi 39 na aliweka jiwe la msingi katika Daraja la Mto Sibiti na utekelezaji wa daraja hilo uko kwa asilimia 79.8. Daraja hilo litakapokamilika litakuwa lina manufaa kiuchumi katika Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine ya jirani kwa sababu itasaidia bei ya vifaa vya ujenzi kupungua. Kwa mfano, cement katika Mkoa wetu inauzwa kwa Sh.18,500 kutokana na gharama kubwa ya usafirishaji. Cement mpaka ikafike mkoa huo inazungukia Mkoa wa Shinyanga ndiyo irudi kuingia katika Mkoa wa Simiyu. Kwa hiyo, kuna manufaa ya kiuchumi kuwepo kwa Daraja la Sibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi walikuwa wakisafiri kwenda Dar es Salaam kwa muda wa siku mbili. Walisafiri mpaka Shinyanga na kulala Shinyanga na kuanza safari ya kwenda Dar es Salaam. Kwa hiyo, kuwepo kwa daraja hilo kutasaidia wananchi kusafiri kwa muda mfupi na kuokoa fedha zao ambazo wangezitumia katika usafiri wa siku mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijikita katika mpango, naomba nishukuru Serikali kwa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge. Wakati Kambi Rasmi ya Upinzani ikiwasilisha hotuba yake ilisema kwamba Standard Gauge haitakuwa na manufaa kwa sababu muda mwingi itasafirisha abiria, siyo kweli, yapo manufaa ya kiuchumi kwa kutumia reli hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Standard Gauge ina manufaa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na Magharibi. Tukumbuke kwamba Kanda ya Ziwa pamoja na Mikoa ya Magharibi haina viwanda vya cement. Kuwepo kwa Standard Gauge kutasaidia kuokoa gharama ya usafirishaji wa saruji. Kwa mfano, saruji kutoka Pwani pamoja na Mbeya kwa malori ingesafirishwa kwa gharama kubwa lakini kuwepo kwa Standard Gauge tutaweza kuokoa Sh.5,000, kwahiyo bei ya saruji pamoja na vifaa vingine vya ujenzi itapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Ziwa inazalisha pamba ya kutosha, marobota yanasafirishwa Dar es Salaam kwa kutumia magari. Kuwepo kwa reli hiyo marobota ya pamba yatasafirishwa kutoka Kanda ya Ziwa kwa gharama ndogo. Wafugaji watasafirisha ng’ombe zao kwenda Dar es Salaam na mikoa mingine kwa kutumia reli hiyo, kwa hiyo, tutaokoa gharama za usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia itatumika kupeleka na kutoa mizigo katika nchi jirani ya Rwanda. Kwa hiyo, wanaobeza kwamba Standard Gauge haina manufaa ya kiuchumi, manufaa ya kiuchumi yapo. Nashauri sasa katika mpango waweke fedha ya kutosha kwa ajili ya usanifu wa mazingira ambapo mradi huo utapitia ikiwemo pia ulipaji wa fidia. Serikali ifanye juhudi ya kumpata mwekezaji kwa ajili ya kujenga kipande cha Isaka-Rusumo. Kanda ya Ziwa inategemea bandari ya nchi kavu iliyopo Isaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia niishukuru Serikali ndani ya miaka mitatu imeweza kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mpaka shilingi bilioni 269. Hii hatua ni kubwa sana, imeweza kusaidia upatikanaji wa dawa ambao siyo chini ya asilimia 80. Wauzaji wa dawa binafasi wanalalamika biashara yao imekuwa mbaya, hii ni kwa sababu kuna dawa za kutosha katika hospitali zetu. Serikali imewasaidia wananchi kuwapunguzia gharama za kununua dawa katika hospitali na pharmacy za watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mazuri yanayofanywa na Wizara ya Afya kuna changamoto katika kutoa huduma kwa wazee. Wazee wetu wanapewa huduma kwa kupewa vitambulisho lakini ikumbukwe kwamba vitambulisho hivyo vinatolewa ndani ya Wilaya. Wazee wetu wanapopata rufaa vitambulisho vile havikubaliwi. Nashauri kuwepo na mpango wa kuweka fedha kwa ajili ya kuwakatia bima ya afya sambamba na kupatiwa dawa muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee wetu hawa wanaugua magonjwa ya moyo, sukari ikiwemo saratani, ni dhahiri kwamba magonjwa haya mengine hayatibiwi katika hospitali za Wilaya. Kwa hiyo, wazee wanayo changamoto ya kutokuwa na fedha ya kutosha kwa ajili ya kwenda kutibiwa nje kwa sababu vibali vile havikubaliki. Kwa hiyo, nashauri kuwepo na bima ya afya kwani itasaidia kuwepo na mzunguko wa fedha katika Hospitali za Wilaya. Wazee wetu wanatibiwa bure na Serikali kwa sasa hivi haifanyi marejesho ya fedha walizotibiwa wazee. Nashauri wazee hawa wapatiwe bima ya afya ambayo itazisaidia hospitali zetu kuwepo na mzunguko wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja mkono, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango katika hoja za Wizara hizi mbili. Kwanza nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunipa kibali chake na kuniwezesha kusimama mbele kuweza kutoa mchango. Pia nipongeze kazi nzuri inayofanywa na Mawaziri wote wawili na wasaidizi wao kazi zao ni nzuri tunaziona kwa vitendo, maneno wanayoyatoa hapa katika Bunge ndivyo kazi inavyofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kuongelea idadi kubwa ya Wakuu wa Idara wanaokaimu kwa muda mrefu bila kuthibitishwa katika nafasi hizi. Kumekuwa na idadi kubwa sana ambayo ikiongezeka siku hadi siku ya Wakuu wa Idara katika Halmashauri zetu wanaokaimu kwa kipindi kirefu bila kuthibitishwa. Nakubaliana na kwamba zoezi la uchunguzi ni muhimu sana ili kuweza kupata wakuu wa idara. Zoezi hili limekuwa likichukua muda mrefu sana. Ningependa kutoa ombi katika idara inayohusika kuwepo na muda maalum hata kama mtumishi ana mambo mengi anatakiwa kuchunguzwa kuwepo na muda maalum kwamba itachukua miezi mingapi kuchunguzwa kama hana matatizo mengi itachukua kipindi gani, kuwe na time frame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani Kamati ya LAAC tumetembelea halmashauri nyingi kwa mfano, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Wakuu wa Idara wanaokaimu sita, Bukombe sita, Mbogwe sita, Ngara wanne kwa kigezo kwamba wanasubiri kufanyiwa vetting. Hii inapunguza ufanisi kwa wakuu wa idara kwa sababu wanaona hawana uhakika na kesho yao. Mara nyingi imekuwa ikitokea anakaimu mpaka mwaka mzima mwisho wa siku analetwa mkuu wa idara mwingine kutoka sehemu nyingine. Hii inavunja moyo sana kwa sababu upande wa Serikali bajeti ya mishahara ya wakuu wa idara ipo kwa kila halmashauri, kinachochelewesha ni suala la vetting, naomba kuwe na timeframe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kuna upungufu mkubwa sana wa wahandisi wa majengo katika wilaya zetu kwa sababu wahandisi wengi wameenda TARURA. Kwa hiyo kazi za majengo zimekuwa zikifanywa na ma-local fundi bila kuwepo na ufuatiliaji wa wahandisi wa halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru na kupongeza kazi nzuri sana inayofanywa na mradi wa TASAF pamoja na MKURABITA. TASAF inafanya kazi nzuri sana na wananchi wetu wanapata fedha, wasio na uwezo na wengi imewasiadia pia kuanza kujiongezea biashara ndogondogo. Naomba nishauri, fedha hizi zimekuwa zikiletwa halmashauri na kuingia katika kapu kuu la halmashauri, hivyo kupelekea fedha nyingine kutumika kwa matumizi yasiyotarajiwa na kuchelewesha utekelezaji wa shughuli za TASAF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa lengo la Serikali la kudhibiti akaunti nyingi, lakini naomba kwa fedha hizi za wafadhili zingepewa special account kwa sababu mwisho wa siku utekelezaji wa miradi unachelewa na baadaye wanapata hoja za ukaguzi. Hofu yangu ni kuweza kuleta shida kwa wafadhili wetu. Katika Wizara hii hii kuna mradi pia wa MKURABITA, zote ziko chini ya Wizara ya Utumishi. Hata hivyo, MKURABITA wenyewe wamekuwa wakisubiri tu fedha kutoka kapu kuu la Mfuko Mkuu wa Hazina wakati TASAF wanaandika maandiko na kuweza kupata ufadhili. Mwanzo MKURABITA walikuwa wanaandika maandiko na kupata ufadhili, sasa sielewi tatizo limekuwa lipo upande gani. Nashauri pia katika Wizara ya Utumishi katika OPRAS zao kiwe kigezo pia cha kuangalia kwa nini hawa wameshindwa kutafuta namna ya kujipatia fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu pia naomba nichangie vigezo vinavyotumika katika kupata fedha za EP4R katika halmashauri zetu. Kigezo kikuu kimekuwa kikitumika ili halmashauri zipate fedha kwa ajili ya kujenga madarasa, maabara na shughuli zingine, ni Mwalimu kuhudumia darasa lenye wanafunzi 40 hadi 50. Kigezo hiki katika halmashauri zetu ni changamoto kubwa sana kwa kuwa Halmashauri zinatofautiana mazingira. Nashauri vigezo hivi vingekuwa categorized kwa halmashauri kwa mfano manispaa na majiji zikawa na vigezo vyake na halmashauri za wilaya zikawa na vigezo vyake. Bila kufanya hivyo fedha nyingi zitakwenda sana kwenye Halmashauri za Majiji na Manispaa kwa sababu wenyewe wanakidhi vigezo vya Mwalimu kuhudumia wanafunzi 40 hadi 55. Katika halmashauri za wilaya kigezo hiki ni kigumu. Ombi langu kwa Serikali ziwapelekee Walimu wa kutosha hizi halmashauri ama ziwahamishe kule walikojaa na kuletwa ambako kuna upungufu wa Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama halmashauri zitapewa zile asilimia 10 za msawazisho wa ikama fedha hii haitoshi kwa sababu, kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu asilimia 10 inayoletwa inaweza ikafanya msawazisho kwa Walimu 10 ikawahamisha, lakini na hiyo siyo solution…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nianze kwa kuipongeza Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi naona juhudi za Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake, kwa kuendelea kuongoza vizuri Wizara ya Elimu. Nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi Wakaguzi wa shule, yaani wadhibiti elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuamua kuwajengea Ofisi katika Wilaya 100 ambazo zitawasaidia kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Nashukuru katika Wilaya 50 zinazoanza, Wilaya ya Meatu imo na tayari Wilaya hizo 50 zimeanza kuletewa fedha za kujengea Ofisi zao. Naamini muda wowote pia Wilaya ya Meatu nayo itaingiziwa fedha tayari kwa kuanza kujenga Ofisi ya Wadhibiti ubora wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa hatua ya makusudi iliyochukua kuweza kunusuru maboma yaliyokuwa yameanzishwa na wananchi ili nguvu za wananchi zisipotee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa makusudi ya hatua ilichukuwa ya kuweza kunusuru maboma yaliyokuwa yameanzishwa na wananchi ili nguvu za wananchi zisipotee, binafsi nishukuru kwa Mkoa wa Simiyu tumeletewa Sh.1,337,500,000 kwa ajili ya kukamilisha madarasa ya sekondari 107. Naishukuru sana Serikali kwa hiyo nguvu za wananchi hazitapotea bure. Hata hivyo, binafsi nikupongeze wewe binafsi huwezi kujisemea kwa kazi nzuri unazozifanya Jimboni kwako kwa fedha zako binafsi kwa kuanzisha maboma na hatimaye leo umepewa maboma 54 yakiwa kwa Halmashauri ya Bariadi DC na Bariadi TC hiyo ni juhudi yako ndiyo maana umeletewa mengi. (Makofi)

Pamoja na hayo Serikali inatoa fedha nyingi sana kwa ajili ya elimu ikiwepo elimu bila malipo. Kwa makusudi Serikali imeamua kuifanya elimu ya sekondari kuwa elimu ya lazima. Pamoja na fedha nyingi zinazotolewa na zinatumika kama zilivyokusudiwa nilikuwa nina wazo moja la kuweza kuboresha ili fedha zitumike kama zilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo changamoto kubwa katika sheria. Sheria ya kuhakikisha mwanafunzi akianza sekondari ya kumbakisha mpaka anamaliza, zipo sheria ambazo zinasema mtoto haruhusiwi kupata ujauzito au kuoa au kuolewa lakini sheria ya kumbakiza shuleni haipo. Naomba Wizara ione iweze kuleta sheria ili tuweze kuipitisha ili Walimu wasiwe na matatizo, wale wanafunzi wanaokatisha masomo waweze kuchukuliwa hatua na hatimaye warejee mashuleni.

Mheshimiwa mwenyekiti, lakini Mkoa wetu wa Simiyu unayo changamoto kubwa tatizo la mimba kwa wanafunzi bado ni kubwa kwa mwaka 2017 tulikuwa tunamimba 196, mwaka 2018 mimba 187 lakini kwa makusudi wananchi wameanza kujenga hosteli kwa ajili ya watoto wa kike. Ombi langu kwa Serikali ni ku-support nguvu za wananchi ili mabweni yale yaweze kukamilika na yanufaishe watoto wao. Manufaa si tu kwa ajili ya kupunguza mimba za wanafunzi, bali pia itawaweka pamoja wanafunzi wawe na mawazo pamoja wawapo shuleni na kuondokana na mawazo ya mtaani, lakini pia itaongeza ufaulu hususan kwa watoto wa kike kwa kuwa maeneo yetu yanafahamika hamna maeneo ya kuishi inabidi wakae kwenye majumba ya ndugu na jamaa na unavyojua tabia zetu sisi ukikaa mahali lazima ufanye kazi huwezi kukaa tu kwa ajili ya kusoma, lazima ufanye kazi katika familia unayokaa lakini hii pia inapunguza pia kiwango cha ufaulu kwa watoto wa kike. Pia mabweni haya yatapunguza ule utoro kwa wanafunzi, wanafunzi wamekuwa wakiacha masomo kwa sababu ya kutembea umbali mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jamii yetu pia ni wafugaji, kwa hiyo kuwepo na mabweni kutawasaidia wanafunzi wale wabaki mashuleni. Binafsi niipongeze Wilaya ya Meatu kwa juhudi zake binafsi kwa kuanzisha shule maalum ya makao kwa ajili ya watoto wa wafugaji ili waweze kubakia pale. Niiombe Serikali iweze kuwasaidia juhudi waliyofikia. Wamekamilisha madarasa manne, wamejenga maabara mawili yanahitaji kukamilishwa, wamejenga bwalo moja linatakiwa kukamilisha. Namwomba Waziri mgawo utakaopatikana waione pia Shule ya Sekondari Makao ambayo iko katika Kata ya Mwangudo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka nianze Ubunge wangu hapa niliikuta shule ya High School ya Nyalanja ina madarasa sita ambayo hayafanyi kazi kwa kuwa hawana bweni. Shule ile ni ya bweni upande wa High School na O-level ni shule ya kutwa. Naomba basi ili kuwepo na thamani ya fedha yale madarasa sita yapatiwe bweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa mara nyingi namfuata Waziri pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, naomba basi katika bajeti hii waisaidie High School ya Nyalanja ipate bweni tuweze kupata mchepuo mwingine ambao pia utawaleta watoto wa kutoka mikoa mingine. Sambamba na hilo pia inawasaidia wanafunzi wa shule ya kutwa wa O-level kuweza na wenyewe kuvutiwa kupata matamanio na wenyewe waweze kufika kama wenzao walivyofikia.

Mheshimiwa mwenyekiti, lakini niseme changamoto moja ambayo niliiona wakati wa ziara tukikagua LAAC, ni gharama kubwa ya kuweka umeme katika shule. Shule inaomba kuwekewa umeme inapohitaji kuweka transformer TANESCO inaiagiza shule ilipie, wakati huo shule haina uwezo wa kulipia gharama hizo kubwa kama milioni 12. Naamini kwamba transformer ile ikienda itasaidia pia kijiji kwa sababu katika yale maeneo kuna taasisi nyingine za Serikali pamoja na kijiji kwa hiyo haitafanya kazi tu kwa ajili ya Sekondari. Niiombe sasa Serikali itoe zile fedha zenyewe badala ya kuiagiza shule itoe zile fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya CCM kwa kutumia zaidi ya bilioni mia mbili kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti ambalo litaunganisha Mkoa wa Simiyu na Singida na kunufaisha kiuchumi na kijamii wananchi wa Mkoa wa Simiyu hususan Wilaya ya Meatu. Naomba kusaidiwa yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, kujenga kwa kiwango cha lami kilomita 25, ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati wa uzinduzi wa daraja. Pili, Daraja la Mto Sibiti halitakuwa na tija wakati mvua kubwa itakaponyesha mfululizo kama makorongo ya Itembe na Chombe yaliyopo barabara ya kutoka Sibiti hadi Mji wa Mwanhunzi hayatajengewa madaraja ya juu. Naomba makorongo hayo yajengewe daraja ili kuwepo na thamani ya pesa kwa daraja hilo kupitika kwa uhakika na magari ya aina zote.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kutoa maoni yangu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kuniwezesha katika kuchangia mapendekezo ya Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutokukubaliana/kukataa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani yaliyoko ukurasa wa sita kwamba Serikali imezifilisi Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzinyang’anya vyanzo vya mapato na kuzifanya ombaomba kwa Serikali kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikubaliani kwa sababu mapato ya Halmashauri zaidi ya asilimia 95 yalikuwa yanatumika katika matumizi ya kawaida. Nikiri kwamba pamoja na Serikali kuchukua vyanzo hivyo, Serikali hii imerithi madeni mengi ambayo ni malimbikizo ya mshahara na matumizi mbalimbali ya watumishi kutoka katika Halmashauri hizi. Serikali imerithi madeni ya wazabuni wa Halmashauri ambapo Halmashauri zilikuwa zinakusanya na kutumia fedha kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kuchukua baadhi ya vyanzo hivi, kwa sababu mambo mengi mazuri yameweza kufanyika. Mwanzo asilimia hizo nyingi zilikuwa zinatumika kwa wachache, lakini sasa hivi fedha hizi zinatumika kwa wananchi wengi ambao pia ni sehemu ya Halmashauri. Watumishi ni sehemu ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba mishahara ilikuwa inalipwa mpaka tarehe 5 ya mwezi unaofuata lakini sasa hivi mishahara inalipwa mapema sana, siyo zaidi ya tarehe 25. Vilevile zaidi ya shilingi bilioni 20 zinapelekwa kwa ajili ya elimu bure, hakuna watoto wanaorudishwa majumbani. Pia mikopo ya elimu inatolewa kwa wakati, inatolewa miezi miwili kabla na ongezeko la wanafunzi wanaolipwa limeongezeka kutoka 100,000 mpaka 128,000. Hatuoni migomo kwa wanafunzi wa vyuoni. Wametulia, wanasoma bila maandamano yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri madeni ya watumishi na ya wazabuni yamelipwa kwa kiasi kikubwa. Fedha za miradi ya maendeleo zimepelekwa kuimarisha miundombinu kwa wananchi wetu. Kwa mara ya kwanza nimeona Mkoa wa Simiyu Vituo vya Afya vinatoa huduma ya upasuaji, mpaka Zahanati na Vituo vya Afya dawa zimejaa. Hayo yote ni sehemu ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mapendekezo katika Mpango, kwamba Serikali iweke mpango mahsusi sasa wa kuhakikisha madeni ya watumishi yaliyohakikiwa yote yanalipwa; na maboma ya maabara na majengo mengine yakamilishwe ili kuwepo kwa thamani ya fedha ili maabara hizo pia zitumike kwa kadri ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri pia maboma ya madarasa ya sekondari, Serikali inakamilisha, lakini sasa Serikali iweke mpango mahsusi wa kuajiri wahandisi wa kutosha wa ujenzi. Kwa sababu wahandisi wengi wameenda TARURA na wahandisi wa majengo katika Halmashauri hawapo. Fedha nyingi za miradi ambazo zimekuwa zikipelekwa zinatumika na mafundi ambao ni local ambapo inasababisha miradi mingine haitekelezwi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie upande wa miradi ya maji. Nakiri kwamba Serikali inapeleka sana fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji kiasi kwamba mimi nashindwa sasa kusema fedha ziongezwe au zisiongezwe kwa sababu fedha kwanza zinazopelekwa hazijaleta tija. Miradi mingi imekamilika lakini haitoi maji. Fedha nyingi zinapelekwa, miradi haitoi maji, mingine inatoa maji siku tu ya uzinduzi. Kwa hiyo, Serikali pamoja na kuwa tumezipa mamlaka za maji vijijini tuhakikishe upungufu uliokuwepo sasa unafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizokuwepo ni usanifu mbovu, usimamizi mbovu na utafiti mbovu. Haiwezekani Wilaya ya Muleba yenye vyanzo vya uhakika vya maji, lakini miradi yake inakamilika halafu haitoi maji. Kwa hiyo, hapo nakiri kulikuwa na usanifu mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa pia na upungufu wa wahandisi wa maji. Serikali iweke Mpango madhubuti wa kuhakikisha inaajiri wahandisi wa maji wa kutosha. Vile vile utafiti pia ulikuwa mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya nchi hii yanatofautiana. Kuna maeneo ambayo water table iko juu, mengine water table iko chini. Kwa mfano, Mkoa wa Simiyu kuna maeneo ambayo water table iko chini sana, lakini inapelekewa miradi ya visima virefu. Kuna maeneo mengine hata ukichimba maji hata Lukale maji yale hata kwenye maabara ya maji hayakubaliki kwa sababu ni chumvi. Naiomba Serikali iweke mpango kwa kufanya utafiti mzuri na kupeleka miradi kulingana na maeneo. Kwa mfano, Wilaya ya Meatu kuwepo mpango wa kupeleka mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu, naiomba Serikali iweze kuusaidia Mji wa Mwanuzi ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Meatu. Kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji. Bwawa lile limejaa matope kiasi kwamba hata maji yale hayawezi kutibiwa, hayawezi kupampiwa katika matenki, ni matope matupu. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Maji afike Wilaya ya Meatu akashauriane na wahandisi na wataalam waone namna gani wanavyoweza kuunusuru Mji wa Mwanuzi, kwa sababu hatuna chanzo kingine cha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipewa mradi wa visima nane, lakini vimefeli kwa sababu water table iko chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo, naunga mkono hoja na ninakushukuru sana. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali niweze kuchangia katika hoja hizi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa kipindi chote nilichokuwa Bungeni katika awamu hii nimeweza kuhudumu Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Mengi nimejifunza, mengi nimeyaona kumekuwa na mabadiliko katika halmashauri zetu katika utendaji kazi. Kumekuwa pia na mabadiliko katika usimamizi wa miradi, miradi imeongezeka tofauti na tulivyokuwa tunaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Halmashauri katika kujinasua katika ukusanyaji wa mapato pia kumekuwepo na miradi ya kimkakati. Niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kuziwezesha Halmashauri zetu kupata miradi mikubwa ya kimkakati kwa mfano soko la Job Ndugai hapa Dodoma, stendi ya basi, soko la Morogoro na miradi mingine iliyopo katika mikoa mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwepo kwa miradi ya mikakati kutatengeneza sasa mazingira ya kuwezesha ukusanyaji mzuri wa kodi kwa ajili ya Halmashauri. Kubwa pale niombe kuwepo na mikakati mizuri ya uendeshaji ili kuwe na tija katika ukusanyaji wa mapato na tija katika kutoa huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia ripoti yetu kumekuwa na tatizo kubwa upande wa mafao ya watumishi, tofauti na tulivyokuwa tunaanza Kamati hakukuwa na matatizo ya michango ya watumishi katika mifuko yao ya mafao lakini kwa sasa kasi inakuwa kubwa sana ya mafao ya watumishi kutokupelekwa katika mifuko yao hususan kwa watumishi wa Halmashauri wanaolipwa na mapato ya ndani. Naomba hili kama Mwenyekiti wa Kamati alivyosoma jambo hili likemewe kabisa kwa sababu michango ni midogo lakini riba inaenda kuongezeka kwa kasi kubwa mpaka inazielemea Halmashauri kuweza kulipa mafao hayo na kusababisha watumishi wanaostaafu kupata shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nichangie upande wa Halmashauri kutokukusanya kikamilifu mapato yao. Katika taarifa zetu Halmashauri nyingi zimeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kutokana na sababu mbalimbali za kimiundombinu na hali ya hewa. Moja ya sababu zilizotajwa ni uduni wa mtandao wa mawasiliano (internet) kwa kutumia zile mashine zetu za kukusanyia mapato. Sisi kama Kamati Halmashauri nyingi zilizofika katika Kamati zilionekana mapato hayakuweza kuwasilishwa Halmashauri wakati wa ukaguzi wa CAG, lakini baadaye yalionekana lakini pia yalisababisha kushuka kwa asilimia ya ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto zilizo katika mashine hizi, sababu hii haimuondoi Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa kufuata sheria na kanuni za fedha za Serikali za Mitaa. Kwa sababu misimu ya ukusanyaji wa mapato inajulikana, unajua ni msimu gani upo juu lakini Mweka Hazina amekaa tu ofisini eti anasubiri mtandao usome. Kuna vigezo vingi vya kuangalia, anaweza kuangalia kwenye taarifa ya mapato na matumizi, anaona haipandi lakini umekuwa kama ni mwanya wa fedha hizi kutumika kwa matumizi mengine kabla hazijafikishwa Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kupitia TAMISEMI imeweza kutoa mashine za kukusanyia mapato 7,227 ambazo zimewekewa udhibiti zaidi na mashine hizi zinaonekana pia hazitakidhi mahitaji ya Halmashauri zilizopo. Ushauri wangu napenda kutokana naupungufu uliopo katika mashine zilizopo sasa hivi, Serikali ifanye utaratibu wa kuzitoa katika mzunguko zile mashine kwa sababu zifuatazo:-

Kwanza hazijulikani ziliponunuliwa, hakukuwa na mzabuni mmoja kwa hiyo udhibiti wa hizi mashine haukuwepo. Kuendelea kuwepo katika mzunguko zinaendelea kukusanya fedha ambazo haziingii katika mapato ya Halmashauri.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupitia mashine hizi mpya zilizoletwa zitasababisha sasa kuwe nacontrol ya mnunuzi Halmashauri fulani atajulikana POS yake iko Halmashauri fulani. Kwa hiyo, ushauri mkubwa ziondolewe katika mzunguko.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wenzangu walivyochangia nataka kuchangia kuhusu madai ya watumishi wa Halmashauri zetu za Serikali. Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali za kulipa madeni ya watumishi lakini kumekuwepo na malimbikizo makubwa ya madeni ya watumishi katika halmashauri zetu. Kwa mfano, Halmashauri ya Chamwino kwa madai ya watumishi ni shilingi bilioni 1.3; Sumbawanga bilioni 1.3; na Halmashauri ya Meatu bilioni 1.5. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa Serikali inafanya uhakiki, ushauri wangu ambao nataka kuutoa, kama kuna watumishi ambao hawastahili kulipwa basi taarifa zirudishwe ili Halmashauri ziweze kupunguza katika madeni yaliyopo katika hesabu zao. Pia, Serikali iwe na mkakati wa makusudi wa kulipa madeni ya watumishi. Ushauri mwingine madeni mengine yanasababishwa na mishahara kwa ajili ya ule mfumo wa Lawsonuidhinishaji wake ni mdogo, kwa hiyo inasababisha kutengeneza malimbikizo ya mishahara ambayo hayastahili yangeweza kulipwa katika mishahara kusiwepo na usumbufu wa watumishi kudai madeni yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni yanayotokana na watumishi kukaimu kwa muda mrefu yamekuwa ni mengi hususan kwa watumishi wasio na barua za kutoka TAMISEMI ndio wanatengeneza madeni hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nashukuru kwa mazuri yanayofanywa. Nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri inayofanya na Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri kama timu ya pamoja wamekuwa wakifanya maamuzi yenye tija katika mazao ya chakula na kibiashara. Wilaya ya Meatu imechaguliwa kuwa Wilaya itakayozalisha mbegu mama ya pamba na tayari kazi hiyo inafanyika katika Kata ya Mwabusalu.

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 5/2/2019 Baraza la Madiwani lilikataa taarifa ya Bodi ya Pamba kuwa Wilaya nzima kuwa ya kilimo cha mkataba tena Bodi ilichelewa kuwaandaa wakulima na pamba iikuwa imechanganya na magugu ya msimu uliopita.

Mheshimiwa Spika, ushauri, kwa msimu huu 2019/2020, pamba haifai kuwa mbegu mama isipokuwa ya Kata ya Mwabusali. Kuruhusu wanunuzi wanaotaka kununua pamba Wilaya ya Meatu ili kuwepo na ushindani wa bei na mkulima anufaike. Katika msimu ujao wanunuzi watakaotakiwa kununua pamba mbegu watapatiwa kwa taratibu za uzabuni, taratibu za Serikali ili kuondoa mazingira ya rushwa.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali itengeneze mazingira ya kuwa na bei nzuri ili isitofautiane na bei ya pamba katika wilaya jirani ambayo itawafanya wakulima wasitoroshe pamba wilaya jirani, hivyo kuikosesha halmashauri ushuru wa pamba na kuwavutia wakulima katika kulima kilimo bora. Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wakulima wa pamba Meatu kuwa wanalima pamba mbegu mama.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika hoja ya TAMISEMI. Nianze moja kwa moja kwa kuiomba Serikali itenge fedha kwa ajili kujenga daraja la Mwamanongu ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati akiomba kura mwaka 2015 kama Mgombea Mwenza. Alitoa ahadi hiyo akiwa katika Kata ya Mwabuzo kwamba daraja la Mto Mwamanongu lijengwe, lenye urefu wa mita 120 ambalo linaweza likagharimu shilingi billion 1.5. Sisi kama halmashauri tayari tumeliweka katika mpango wa mwaka huu katika fedha za maendeleo. Naomba katika miradi iliyowekwa katika miradi ya maendeleo lipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, niungane na maoni ya Kamati ya TAMISEMI kwamba Serikali isimamie na kuhakikisha halmalshauri nchini zinatenga na kutoa fedha katika Mfuko wa Barabara. Kabla ya TARURA Julai, 2017, halmashauri zilitenga fedha kwa ajili ya miradi kwa ajili ya kuanzisha barabara mpya na fedha hizo zilitengwa katika miradi ya maendeleo. Kwa halmashuari niliyopo fedha hizi zaidi zilitengwa kwenye fedha ya CBG. Kazi ya halmashauri ilikuwa ni kuanzisha barabara mpya, baadaye zilikuwa zikichukuliwa wakati huo zilikuwa ni Mfuko wa Barabara (Road Fund).

Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kuanzisha TARURA, halmashauri imejitoa katika kuanzisha barabara mpya, kwa hiyo TARURA haina barabara za kuzirithi kutoka halmashauri. Niishauri Serikali katika asilimia 40 ya mapato ya ndani, Kamati ya TAMISEMI kila inapoidhinisha bajeti ya halmashauri, ihakikishe kiasi fulani kimetengwa kwa ajili ya kuanzisha barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga pia mkono kuhusu fedha za TARURA, Serikali iendelee kuziongoeza. Sisi Halmashauri ya Meatu mtandao wa barabara ni kilomita 1,041, lakini tumetengewa shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kilomita 253 na Makalvati 11, sawasawa na asilimia 24. Fedha hii haitoshi kabisa kwa ajili ya mtandao mzima. Kwa hiyo unakuta barabara nyingi zaidi ya miaka 10 hazijafanyiwa ukarabati, ikiwepo barabara ya Mwambegwa - Sapa, barabara ya Itaba - Mbushi mpaka barabara hizo zimeota miti mikubwa kwa sababu hazifanyiwi ukarabati. Halikadhalika zaidi ya miaka 15 barabara ya Mwamanoni mpaka Mwanzugi haifanyiwi ukarabati kiasi kwamba maji yameosha maboksi kalvati na wananchi wanapitia pembeni na wengine wameng’oa nondo katika makalvati haya.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwepo na utaratibu wa kuzipatia zamu za kufanyiwa ukarabati ili wananchi pia waweze kufaidika na kuweza kupita bila tatizo lolote. Lakini katika utangazaji wa kazi za barabara za TARURA naomba at least asilimia 50 ya barabara ziwe zinatangazwa mapema kuliko hivi sasa zinasubiri kutangazwa wakati zinaanza. Inakuwa ni masika, fedha yenyewe ni kidogo zinashindwa kutekeleza na wananchi wanaendelea kupata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo nina wasiwasi na mkandarai tuliyepewa katika Jimbo la Meatu. Nina wasiwasi na uwezo wake, mara ya kwanza alikuwa anasingizia mvua lakini sasahivi mvua hakuna na hakuna chochote kinachoendelea kwa ajili ya barabara ya Mwanuzi - Mwabuzo, barabara ya Mwambegwa – Mwamanigwa. Niiombe Serikali wakati wa utoaji tenda ufanyike katika level ya wilaya ili waweze kumu-own yule mkandarasi tofauti na sasa kazi zinatolewa katika ngazi ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuwa mchangiaji wa kwanza katika siku hii ya leo. Moja kwa moja nikiunga mkono hotuba ya bajeti kuu ya Serikali iliyowasilishwa, nikikubaliana na mapunguzo ya tozo yaliyofanyika na mabadiliko ya kanuni mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani katika taulo zinazotumiwa na wanawake. Ninaunga mkono kwa sababu, kupungua kwa kodi hii wote tuliona hakukuwa na mabadiliko yoyote katika bei na Serikali ilieleza kwamba, kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani, lakini gharama ya uzalishaji iliendelea kuwa juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, gharama ya uzalishaji imeendelea kuwa juu kwa sababu, pamba nyingi tunayozalisha, asilimia 70 ya pamba tunayozalisha Tanzania inaenda nje na asilimia 30 tu ndiyo inayobaki kutumiwa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata wale wanaozalisha nchini, ile pamba inakwenda kutengenezwa kwanza kule nje ya nchi na kurudi Tanzania ili iweze kuzalisha pedi, kwa hiyo, moja kwa moja gharama za uzalishaji inakuwa iko juu. Kwa hiyo, ninaunga mkono kufutwa kwa kodi ya ongezeko la thamani katika taulo za kike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya makampuni kutoka asilimia 30 hadi 25 kwa wawekezaji wapya wa kuzalisha taulo za kike. Ninaunga mkono kwa sababu gani, kutawezesha kuvutia wawekezaji, kutaongeza ajira, kutaongeza mapato na hata asilimia kubwa ya pamba yetu tunayozalisha itatumika nchini, pamba yetu itakayotumika nchini, gharama ya uzalishaji itakuwa chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema, Mkoa wa Simiyu mapema mwaka 2017, tulipitisha mpango wa uwekezaji katika mkoa. Moja ya uwekezaji ilikuwa nikuwekeza kiwanda cha kuzalisha vifaatiba, vikiwemo drip za maji, pamoja na taulo za kike.

Mheshimiwa Naibu Spika,kwa nini Mkoa wa Simiyu, ni kwa sababu tunauhakika wa maji ya kutoka Ziwa Victoria, tuna uhakika wa pamba, kwa sababu asilimia 60 ya pamba inayozalishwa Tanzania inatokea Mkoa wa Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwepo kwa kiwanda katika Mkoa wa Simiyu, pamba itazalishwa kwa gharama ndogo kwa sababu pamba hiyo inatokea mkoa huohuo, na nina uhakika kiwanda kitakapotengenezwa kitamudu soko la nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili pia limekuwa likiungwa mkono na Makamu wa Rais, kwamba Simiyu sasa tuanzishe kiwanda cha uzalishaji wa taulo za kike. Ninavyooingea, Mfuko wa Wafanyakazi umeonesha nia ya kujenga kiwanda katika Mkoa wa Simiyu, Mfuko wa Bima ya Afya umeonesha nia ya kuwekeza kiwanda. Ninachoomba ni commitment ya Serikali; kwamba watakapokuja kujibu watupe uhakika ni lini sasa kiwanda hicho kitajengwa ili tuweze kumpnguzia mzigo mwanamke katika bei itokanayo na ununuzi wa taulo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kwa kuunga mkono Serikali; moja ya kipaumbele katika kuandaa mpango ilikuwa imezingatia umuhimu wa kumaliza miradi inayoendelea ili kupata matarajio tarajiwa. Vilevile naunga mapendekezo ya kurekebisha Kanuni ya 23 ya Kanuni za Sheria za Bajeti ya Mwaka 2015 ambayo inampa mamlaka Mlipaji Mkuu wa Serikali kuongeza muda wa kukamilisha miradi hiyo. Mwanzo fedha ilikuwa ikibaki mwisho wa mwaka anapewa miezi mitatu tu ili fedha hizo zimalizwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono si tu kwa ajili ya kuwepo fedha za kulipa walipaji ambao wanadai hati za madai, lakini hii pia itasaidia katika halmashauri za mitaa kupunguza matumizi mabaya yaliyokuwa yalifanyika kwa fedha iliyobaki. Fedha nyingi sana zimekuwa zikibaki katika Halmashauri. Kwa mfano, fedha iliyopokelewa 2017/ 2018 katika halmashauri 176, bilioni 783 iliyotumika ni milioni 521 tu; kwa hiyo asilimia 33 ilibaki mwisho wa mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri nyingi zimekuwa zikifukuzana kumaliza fedha mwisho wa mwaka na si kukamilisha miradi kwa ubora. Kwa kumuongezea muda Mlipaji wa Serikali fedha hizi zitatumika kama zilivyotarajiwa. Naomba kukiri kwamba Waheshimiwa Madiwani walikuwa wakihoji kuhusu matumizi ya fedha wanaambiwa wakubaliane kwa sababu tusipokubali fedha zitarudi Serikalini; na pale kulikuwa kuna mianya ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Nikiri kwamba Serikali imeona kuongeza muda kwa sababu fedha nyingi zinaletwa mwisho wa mwaka. Kwa kuwa tunatekeleza cash budget naomba basi kuwe na time frame ya mwisho wa fedha ziletwe angalau mwanzoni mwa mwezi wa sita ili fedha nyingi zisiendelee kubaki maana yake badala yake miradi inatekelezwa kwa ubovu, ubovu, ubovu, ubovu kwa sababu ya kukimbizana kumaliza fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichangie kuhusu mapato yanayokusanywa na halmashauri zetu nikiweza kulinganisha na mchanganuo wa matumizi namna jinsi ulivyo ili sasa tuone wapi tunatakiwa tufanye ili ule mgawanyiko uweze kuleta manufaa kama yalivyokusudiwa. Mapato ya halmashauri ambayo ni asilimia 100 mgawanyiko wake bado unaleta uzito katika utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, asilimia 40 inakwenda kwenye miradi ya maendeleo, asilimia 10 inakwenda kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ile asilimia 50 inayobaki matumizi yake mengine, fedha zake ni mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), wengine mamlakaa ya maji, kuna likizo na matibabu ya Watumishi, kuna uendeshaji wa Ofisi ya Mkurugenzi. Nasema hivyo kwa sababu gani? natafuta pale kuhusu Mheshimiwa Diwani fungu lake pale liko wapi? kwa kuwa fedha nyingi ziko allocated kwa matumizi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hatutaona haja ya kuwasaidia Waheshimiwa Madiwani waletewe angalau posho ile ya madaraka ya mwezi walipwe na Serikali Kuu utekelezaji wa fedha za miradi ya maendeleo hautafanyika, asilimia 10 ya wanawake haitapelekwa, kwa sababu ni vigumu sana utetee asilimia 10 ipelekwe halafu fedha za miradi ya maendeleo ikafanyike wakati wewe Mheshimiwa Diwani maslahi yako hayajalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja nikisema sasa Wizara ya Fedha an TAMISEMI wakae wapiti ile asilimia 10 mgawanyiko wa matumizi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushuru kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuchangia katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa. Vile vile namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kuchangia, naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kunipa nafasi ya kugombea katika Jimbo la Meatu. Kubwa pia, nawashukuru wananchi wa Jimbo la Meatu kwa kunichagua kuwa mwakilishi wao, nami nawaahidi sitawaangusha na ninamwomba Mwenyezi Mungu anisaidie. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Hebu subiri kidogo Mheshimiwa. Subiri subiri, nimezima microphones zote, kwa sababu sielewi kelele inatoka wapi. Hebu hamia kwenye mic ya jirani halafu ujaribu kuisimamisha. Zima kwanza hapo ulipotoka.

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita katika moja ya maeneo makuu matano ya kipaumbele ambayo ni kuchochea maendeleo ya watu. Eneo hili linajumuisha utekelezaji wa miradi ambayo inajikita katika kuboresha maisha ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mpango wa pili kumekuwepo na mafanikio makubwa katika Sekta ya Afya. Tumeona miundombinu katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali zikijengwa, vilevile na upatikanaji wa dawa, ongezeko la watumishi pamoja na vitendea kazi. Hata hivyo, sekta hii bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Kwa hiyo, naomba katika Mpango huu wa Tatu changamoto hizi zitatuliwe ili tuweze kufikia malengo ya mpango huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ikamilishe sasa maboma ya Zahanati na Vituo vya Afya ili yaweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa. Vile vile kukamilishwa kwa maboma haya kuende sambamba na upatikanaji wa vitendea kazi, watumishi wa kutosha na dawa za kutosha. Ni ukweli usiopingika kwamba Zahanati zetu nyingi hazina watumishi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ziara zangu, nimeshuhudia, baada ya mtumishi kustaafu Zahanati inafungwa. Mojawapo ni Zahanati ya Mwabalebi. Pia katika Zahanati ya Mwabagalu kuna watumishi wawili ambao mmoja amekwenda maternity, mmoja ni mgonjwa, Zahanati imefungwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweke mkazo katika kuajiri wataalamu wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Serikali itoe fedha za kutosha ambazo zitapaswa kutolewa katika chombo chetu cha MSD ili kiweze kusambaza dawa za kutosha nchini. Ni ukweli usiopingika, katika Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa Serikali imeongeza Bajeti kubwa ya madawa kutoka shilingi bilioni 29 mpaka shilingi milioni 250. Madawa katika hospitali zetu yaliongezeka mpaka upatikanaji wa dawa muhimu ulifikia asilimia 80 mpaka 90. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ninavyoongea, ukienda kwenye hospitali zetu, hakuna dawa. Wananchi wanaandikiwa dawa na kuhitajika kwenda kununua dawa katika maduka ya dawa. Naiomba Serikali niweke mkazo katika mauzo ya dawa. Tutategemea bajeti zitaongezwa, lakini Serikali ikiacha tu kutoa fedha, hospitali zile zinakosa dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano tu. Robo tatu zilizopita za basket fund haikuweza kuletwa katika hospitali zetu. Kwa hiyo, ilisababisha ukosefu wa dawa katika hospitali zetu. Kwa hiyo, Serikali ikiweka mkazo katika mauzo ya dawa, itasaidia kuwa na mzunguko, kutakuwa na revolving. Hata hivyo, wataalam wetu wamekuwa na kisingizio kwamba madawa haya yanamalizwa na wagonjwa ambao wako kwenye makundi ya msamaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naishauri Serikali, ijue ni asilimia ngapi itakwenda kwenye makundi ya msamaha, ni asilimia ngapi itakuwa ni ya mzunguko na hiyo isimamiwe. Hata kama Serikali ikichelewa kupeleka fedha za ruzuku, hospitali hizo kuwe na mzunguko wa kutosha na madawa yaweze kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sekta ya Elimu kumekua na mafanikio makubwa. Tumeona ongezeko la wanafunzi kutokana na Elimu Bila Malipo na miundombinu mingi imejengwa. Hata hivyo, sekta hii bado ina changamoto nyingi katika miundombinu ya kujifunzia na ya kufundishia. Kwa hiyo, kwanza naiomba Serikali itoe fedha iweze kukamilisha maboma ya maabara katika Shule zetu za Sekondari, itoe fedha za kutosha kukamilisha maboma ya vyumba vya madarasa pamoja na nyumba za watumishi. Pia udahili wa wanafunzi uendane na ongezeko la vyumba vya madarasa pamoja na nyumba za watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri za vijijini, nimeshuhudia kuwepo kwa tatizo kubwa la walimu wengi kuhama. Hivyo Serikali inapaswa ifuatilie kujua ni nini kinachosababisha walimu hawa wanahama kwa wingi? Kwa mfano, katika Halmshauri ninayotoka ya Meatu, katika robo moja walihama walimu 60.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili linachangiwa na ukosefu wa nyumba za walimu. Kwa mfano, katika jimbo langu, Shule ya Mabambasi miaka mitatu iliyopita ilikuwa ya mwisho kitaifa. Ukifika pale, walimu wote sita wanaishi katika nyumba moja; na shule hiyo ni kilomita 30 mpaka Makao Makuu ya Wilaya. Kwa hiyo, familia zao inabidi ziishi Wilayani na wenyewe mwisho wa wiki inabidi waende kwenye familia zao. Kwa hiyo, kunakuwa na gharama kubwa za nenda rudi nenda rudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shule moja ya Mwanyagula yenyewe ina nyumba moja ambayo sasa inavuja na yule mwalimu amehamia Wilayani. Kwa hiyo, ukifika pale, hakuna mwalimu anayeishi shuleni, inabidi walimu wasafiri kila siku kilomita 20 kwenda na kurudi na hivyo kunakuwa na gharama kubwa ya kimaisha. Naomba Serikali iwekeze zaidi katika miundombinu ya nyumba za watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tatizo la miundombinu ya barabara inachangia walimu kuhama kutokana na gharama kubwa ya usafiri, huduma ya maji nayo ni tatizo na umeme nao ni tatizo. Endepo Serikali itasawazisha haya, ninaamini walimu wengi hawatapenda kuomba uhamisho kwenda kwenye maeneo ambayo yana huduma kama ambazo nimezitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sekta ya Maji, Serikali katika mpango wake imeeleza kwamba kwa ujumla miradi yote iliyotekelezwa imewezesha wananchi zaidi ya milioni 25 kupata huduma za maji, hivyo kupata wastani wa upatikanaji wa maji vijijini asilimia 70 na mjini asilimia 84 hadi mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoiona Serikali, haipo serious na changamoto na upungufu wa maji. Katika takwimu hizo walizozitoa, ukiangalia wanananchi wanaopata milioni 25, na Watanzania tuko takribani milioni 50, kwa hiyo, ni dhahiri kwamba asilimia 50 tu ya wananchi ndio wanaopata maji. Kwa hiyo, takwimu hizi za asilimia 70 kwa 84 haziakisi uhalisia wa upatikanaji wa maji katika maeneo yetu. Ni vyema sasa Serikali ikatafuta nini chimbuko kubwa la ukosefu wa maji ili ije na suluhu, iweke mkakati maalum wa upatikanaji wa maji hadi tutakapokuwa tunamaliza Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu. Pia nimshukuru na kumpongeza Waziri wa Maji, ndugu yangu Mheshimiwa Aweso kwa hotuba nzuri na ushirikiano anaonipatia ninapompelekea hoja zinazohusu maji za Jimbo la Meatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya na kwa kuweka mkazo mkubwa katika upatikanaji wa maji hususan katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji. Mheshimiwa Rais wakati akilihutubia Bunge alisisitiza zaidi katika uchimbwaji wa mabwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana kabisa na ninaunga mkono. Ni ukweli usiopingika katika Wilaya ya Meatu yenye majimbo mawili kuna uhaba wa vyanzo vya maji. Niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikitutengea fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji lakini miradi hiyo inashindikana kutokana na ama kukosekana kwa chanzo cha maji ama maji yanayopatikana yana chumvi nyingi sana kiasi kwamba maji yale hayafai kwa matumizi ya binadamu na hata katika maabara zetu za maji yamekuwa hayakubaliki. Solution kubwa kwa Wilaya ya Meatu ni uchimbwaji wa mabwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi na Waziri ni shahidi katika Mradi wa Mji wa Mwanhuzi tumeletewa mradi wa visima kwa ajili ya kuongezea Bwawa la Mwanhuzi lakini chanzo cha maji kimekosekana imebidi tukachimbe bwawa ndani ya mto wa mchanga. Serikali imeleta fedha mpaka leo navyoongea zipo na utekelezaji wake ulitakiwa ukamilike Julai, 2021 lakini inashindikana. Zile fedha zipo toka mwezi Februari, 2021 kwa sababu utekelezaji wake umekwamisha na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Meatu la awamu iliyopita kwa kauli moja tulikubaliana Meatu tuletewe miradi ya mabwawa ili kukabiliana na tatizo la chanzo cha maji katika Wilaya ya Meatu yenye majimbo mawili. Serikali imekuwa ikileta fedha nyingi ili kutekeleza miradi hiyo lakini fedha hizo hazikidhi mahitaji, thamani ya fedha haipo kwa sababu imekuwa haitekelezi kwa mujibu wananchi tunavyotakiwa kutekelezewa changamoto zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee mradi mmoja wa Bwawa la Mwanjolo ambao ulitekelezwa katika awamu iliyopita na uligharibu shilingi bilioni1.8 na Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia akiwa Makamu Rais alikuja kuuzindua. Leo hii navyosema tunaambiwa kwamba haliwezi kujengwa tenki la maji lolote kwa sababu yale maji hayatoshi lakini mradi huu ulitekelezwa na watu wa Wizara ya Maji kuanzia usanifu mpaka ujengaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niliwahi kutembelea wakati wa ujengaji wa mradi ule kwa macho yangu mimi ambaye siyo mtaalam niliona yale maji hayatakidhi au hayatatosheleza kusambazwa katika vijiji vinne tu vinavyoizunguka ile kata. Nimshauri Mheshimiwa Waziri afike Wilaya ya Meatu alione lile bwawa la maji. Sisi Wilaya ya Meatu tumekuwa tukionewa miradi mingi imekuwa ikiletwa inagharimu fedha nyingi lakini hainufaishi wananchi kama ilivyokusudiwa. Inauma sana bilioni 1.8 imepotea tu lakini wananchi hawajaweza kupata maji kama ilivyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuishauri Serikali iendelee kutekeleza miradi itakayowezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa haraka ili iweze kusaidia maeneo yenye uhaba mkubwa zaidi wa maji. Miradi hii nilipendekeza vyanzo vyake iwe ni maziwa yaliyopo katika nchi yetu pamoja na mito ambayo haikauki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ikubali kutumia fedha nyingi ambapo itakuwa ni mwarobaini wa kutatua matatizo ya maji hususan kwenye maeneo ambayo yanakabiliwa na uhaba wa maji. Kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Simiyu tunao mradi wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Toka naanza Ubunge wangu 2015 mradi huu umekuwa ukizungumziwa lakini mpaka leo hakuna dalili yoyote ya kuoneshwa ni lini mradi huu utakamilika ambao unatekelezwa kwa awamu mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati akijibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum wa Simiyu tarehe 30 Aprili, 2021 alisema mradi huu utakamilika ndani ya miaka minne. Hata hivyo, mradi huu ukiungalia kwenye utekelezaji wa kazi za Serikali katika awamu iliyopita haumo, kwenye mpango wa miaka mitano haumo, lakini hata kwenye mpango wa mwaka mmoja haumo. Je, mradi unaenda kutekelezwaje ndani ya miaka minne wakati hata kwenye mipango ya Serikali haujapewa kipaumbele? Mradi huu ni mkubwa utagharimu shilingi bilioni 370. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Waziri ya mwaka jana aliahidi ungeanza kutekelezwa Julai, 2020 lakini tumekuwa tukipigwa danadana. Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuwa akijibu swali lile juzi alisema utaanza kutekelezwa Agosti, 2021. Leo hii ukiangalia ni mwezi Mei, 2021 lakini hata hatua za kumpata mkandarasi wa ujenzi hazijaanzwa na wakati huu Serikali inahuisha kupitia usanifu uliofanywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge wa Simiyu ndio mradi uliotusababisha tukapewa kura, tuliji-commit kwa ajili ya mradi wa mradi wa Ziwa Victoria lakini sasa hivi sioni dalili zozote. Naomba Serikali itumie fedha za ndani ni shilingi bilioni 370 katika Awamu ya Kwanza, tunategemea fedha za nje lakini ninyi ni mashahidi fedha za nje zimekuwa zinasuasua na sasa hivi Watanzania tunajivunia kutumia fedha za mapato ya ndani. Naomba mradi wa maji ya Ziwa Victoria uanze kutengewa fedha za kutosha katika mapato ya ndani ndiyo itakuwa suluhu ya utekelezaji wa mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu. Lakini naomba nianze kwa kuunga hoja bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, lakini niishukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti lililogharimu shillingi bilioni 34.5. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja hilo liko kwenye barabara inayotoka Kolandoto – Lalago, Mwanuzi – Sibiti, Matala mpaka Junction ya Karatu. Barabara hii ni barabara ambayo jana Mheshimiwa Flatei alitaka kuirukia sarakasi, Mheshimiwa Mbunge alikuwa na haki kwa sababu barabara hii ni ahadi ya muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini, nikushukuru na niishukuru Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuendeleza daraja hili la Sibiti na barabara unganishi yenye km 25 kwa ujenzi wa lami.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika,taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Leah Komanya kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Flatei.

T A A R I F A

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Leah, barabara hiyo haipiti kule inapita Singida kuja Haydom kwenda Mbulu kwenda Karatu, kwa hiyo siyo hiyo anayosema.

NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Leah Komanya unaipokea taarifa hiyo?

MHE. LEAH J. KONANYA: Naipokea taarifa ni hiyo hiyo niliifupisha kwa ajili ya kuokoa muda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha daraja la Mto Sibiti na barabara unganishi. Barabara hii ya km 25 ni muhimu sana, nimuombe Mheshimiwa Waziri aje kuiona kutokana na changamoto ya eneo lililopo, eneo hilo ni mbuga kali sana na ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe umechukua miaka mingi sana mpaka kukamilisha, nimuombe aje aone ili ajue ni wakati gani aanze kujenga barabara hiyo kwa sababu sasa imeanza kuliwa na mvua ambayo inaweza ikapelekea hasara nyingine kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuishukuru Serikali kwa kuanza kuonyesha nia kuijenga hii barabara niliyoitaja angalau kwa kutenga bilioni 5, angalau imeonyesha nia ni zaidi ya miaka 25 hii barabara imekuwa ikiwekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, angalau sasa shilingi bilioni 5 zimetengwa. Mimi kama Mbunge niliomba kipaumbele kipelekwe katika ujenzi wa madaraja katika mito iliyo karibu na daraja la Sibiti ambayo ni Mto Itembe, Mto Chobe, Mto Nkoma na Mto Liusa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kujengwa kwa madaraja katika Mito hii kutaleta tija katika daraja la Mto Sibiti kwa sababu daraja hili limekuwa mara nyingi likitumika tu wakati wa kiangazi wakati limechukua shilingi bilioni 34. Na matumizi ya barabara hii ni makubwa kutokana na magari ya mizigo yanayotoka Musoma, Mwanza, Simiyu kuelekea Iguguno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali imeonyesha pia katika kipande cha kutoka Mkalama mpaka Iguguno ambayo ni barabara ya kutoka Bariadi, Kisesa, Mwandoya, Mwanuzi, Sibiti mpaka Iguguno kwamba wako kwenye hatua ya kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wanafanya hiyo niiombe TANROADS Singida, kipande cha kutoka Mkalama hadi Nduguti, Gumanga hali ni mbaya sana, hakuna changarawe inayoweka ya kutosha na kufanya magari haya kudidimia. Ninaungana na Mbunge wa Wilaya ya Mkalama ambaye alichangia jana, magari yamekuwa yakizama kutokana na barabara hazijatengenezwa vizuri kwa kiwango cha changarawe na ili hali fedha hizi zinatoka kwenye mfuko wa TANROADS ambao sisi tunaamini TANROADS ina fedha za kutosha kuliko mfuko wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ombi katika jimbo langu, nitoe ombi la kuipandisha hadhi barabara ya Mwanuzi- Mwabuzo. Barabara hii inatengenezwa na TARURA na kwenye kikao cha barabara cha Mkoa niliomba nikakubaliwa, lakini tuliambiwa tusubiri Serikali iidhinishe upandishaji wa hadhi. Barabara ni muhimu ambayo itaunganisha mpaka Wilaya ya Igunga ni muhimu kiuchumi kwa sababu wafanyabiashara wa Wilaya ya Meatu, Maswa, Singida wote sasa wanaelekea Igunga kwa ajili ya kupata bidhaa hiyo, hivyo na kuchochea uchumi katika Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla. (Makofi)

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ngasa.

T A A R I F A

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mchingiaji kwamba wafanyabiashara wanaotoka Meatu, Shinyanga na Simiyu pamoja na Singida, imefikia hatua wamelipa soko la Igunga jina Kariakoo ya Igunga na kila Jumatano wanakuja pale kufanya mnada na kununua bidhaa. Kwa hiyo, kama anavyoomba Mheshimiwa taarifa kuhusu barabara yake, naomba nimpe taarifa ili aweze kupewa kipaumbele na Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge narudia tena, mmesikia taarifa aliyoitoa Mheshimiwa Massay? Mmeisikia Wabunge? Maana saa nyingine tunaongea sana kwa hiyo hatusikilizi. Taarifa inayoweza kutolewa ni kama ile, sijui kama tunaelewana vizuri! Tutumie muda wetu vizuri, wabunge wengi wanataka kuchangia hapa mbele sawa jamani, nadhani hilo limeeleweka. Mheshimiwa Leah Komanya malizia mchango wako.

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuiomba Serikali kwa kuonyesha nia sasa ya kujenga daraja la Mto Simiyu upande wa Mwanza ambalo linaunganisha Mkoa wa Simiyu kwa upande wa Wilaya ya Busega. Barabara hii ni muhimu pia kwa magari yanayoteka Rwanda, Mwanza na mikoa mingine kuelekea Nairobi. Lakini kumekuwa hakuna mahali pa kupishana lakini niipongeze Serikali, imeonyesha nia kwa kutafuta fedha kwa kupitia Benki ya Dunia. (Makofi)

Mheshimwa Naibu Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kutoa maoni yangu. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ili niweze kutoa maoni yangu katika Kamati ya Maliasili. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla kwa kazi nzuri wanazozifanya. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wamekuwa wakitoa ushirikiano wa kutosha kwetu sisi Wabunge mara tunapofikwa na matatizo. Niendelee kuwaomba waendelee hivyo hivyo kutusaidia sisi Wabunge wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kuishukuru Serikali kwa kuipatia Wilaya ya Meatu shilingi milioni 51 kwa ajili ya kulipa fidia na kifuta machozi. Fedha hii imelipwa kwa wananchi 272 kati ya wananchi 520, lakini malipo haya yamefanyika kwa walioathirika kwa kipindi cha nyuma kwa mwaka 2017/2018 na 2018/2019, hivyo kuendelea kuwepo kwa madeni kwa wananchi walioathirika kwa 2019/2021. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwango hivi vimekuwa ni vya muda mrefu. Naomba kanuni ile ya mwaka 2011 ifanyiwe marekebisho ili viwango hivi viendane na hali halisi kwa kuwa haviridhishi wala haviakisi thamani ya uharibifu unaofanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, mimi nilipenda Serikali ijikite zaidi katika kuzuia uharibifu ambao unasababisha vifo na pia kuiingizia Serikali gharama kubwa. Tunavyoelekea, Serikali inaweza ikashindwa kumudu kulipa fidia na kifuta machozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa mikakati ambayo imekuwa ikiiweka. Imekuwa ikiandaa vijana kwa kuwapa mafunzo ya namna ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ambao pia wanasababisha vifo kwa wananchi, lakini mafunzo haya yamekuwa yakidumu kwa muda kidogo na baadaye yanashindwa kwa sababu wale tembo wamekuwa wakizoea zile mbinu na kuleta uthubutu kufanya uharibifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niungane na Kamati ya Maliasili kwa maoni yake kwamba ni vyema kuimarisha utendaji wa TAWA ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, ikiwemo masuala ya kibajeti. Naamini TAWA inao watumishi wa kutosha. Katika Pori la Akiba la Maswa hadi Januari 21, kulikuwa na watumishi 87. Watumishi hawa wanatosha; wakiwezeshwa kikamilifu wataweza kufanya doria zao kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe maoni yangu, TAWA wajikite zaidi katika ile miezi ambapo sasa wananchi wameanza kuivisha mazao yao kwa kuweka doria zaidi ili tuweze kuokoa yale mazao yasifanyiwe uharibifu, lakini hata kuzuia vifo. Katika Wilaya ya Meatu miaka miwili iliyopita wananchi 16 waliuawa na wananchi tisa waliuawa na tembo, lakini kama tukiweza kukabiliana vifo vitapungua na Serikali itapunguza gharama inayotokana na kulipa gharama za uharibifu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mwananchi anayependa kufanyiwa uharibifu ili alipwe fidia. Hakuna ndugu anayependa ndugu yake auawe ili eti alipwe shilingi milioni moja kwa ajili ya kufuta machozi. Tuwekeze zaidi katika kuzuia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbinu nyingine nilitaka Serikali katika kukabiliana na wanyamapori wakali iwezekeze zaidi katika kutumia teknolojia kwa baadhi ya tembo, kuwawekea vifaa maalum vya kielektroniki kwa lengo la kufuatilia mienendo yao. Kazi hii imefanyika katika Pori la Akiba la Maswa katika Ranch ya Wanyamapori ya Makao; tembo 18 waliwekewa radio call. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili limeshindwa kuleta ufanisi kwa sababu, kwanza access ilitolewa kwa maafisa wanne akiwemo DGO wa Meatu na walifanikiwa kuwaona wale tembo wakitoka kwenye maeneo kuingia katika maeneo ya wananchi, lakini changamoto kubwa hata wakiwaona, hawana magari, hawana silaha. Ni kwa namna gani wataweza kwenda kukabiliana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, maeneo manne yaliweza kubainika ambapo tembo wanaweza kutoka. Eneo la N’hanga lililopo Jimbo la Kisesa, Mwanyaina sehemu ya Landani, Sabha na Witamia.

Ombi langu kwa Serikali, kijengwe kituo Mwamongo katika Jimbo la Meatu kwa Askari wa Wanyamapori, kijengwe Kituo cha Askari katika eneo la Landani Mwanyaina katika Jimbo la Meatu. Tukifanya hivyo tutarahishia kuweza kuwarudisha wanapoonekana katika zile call walizowekewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru mwekezaji Mwiba, kupitia Frederick Conservation, walifadhili ule uwekezaji wa kuweka radio call. Nami naamini wako tayari kuendelea kuleta ufadhili huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwawezesha TAWA naishauri Serikali ikubaliane na ile kanuni waliyoomba ibadilishwe katika kikao chao walichokifanya cha ujirani mwema TAWA na Maafisa Wanyamapori Meatu kwamba, asilimia 40 ya fedha inayotoka kwenye asilimia 25 ya uwindaji ipelekwe TAWA ili kuongeza nguvu zaidi. Kwa maana hiyo, wakiwa huko watanunua vifaa, watakuwa na magari kuliko urasimu unaofanywa na ofisi ya Mkurugenzi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii niweze kutoa maoni yangu katika mpango ujao. Lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu, kipenzi chetu, kwa kazi nzuri anazozifanya, kwa dhamira yake ya dhati ya kuifungua Tanzania kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nishukuru kwa shilingi trilioni 1.3 ambayo kwa Jimbo la Meatu kwa trilioni 1.3 tumepata bilioni 2.6 ikiwepo miradi ya elimu, afya na maji. Lakini ukiongeza na fedha zingine ndani ya miezi mitatu, miradi ya barabara Jimbo la Meatu katika miezi mitatu tuna bilioni sita. Na kama watendaji wetu watakuwa na dhamira ya dhati ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, dhamira ya dhati kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Meatu, ndani ya muda mfupi Jimbo la Meatu linakwenda kubadilika kwa muda mfupi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika mpango wetu, nianze kwa kuunga mkono hoja ya Serikali, lakini niunge mkono hoja maoni ya Kamati ya Bajeti ambayo ni Mjumbe na nimpongeze Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Daniel Sillo, kwa namna anavyotusimamia katika Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali inatarajia kuongeza makusanyo kwa asilimia 7.4 ikilinganishwa na mwaka 2021/2022. Kazi kubwa iliyopo mbele ya Serikali ni namna gani hizi asilimia saba tunaweza kuzifikia. Na Serikali imeweka msisitizo kuhakikisha kwamba mapato yote katika Wizara na taasisi za Umma yanaendelea kukusanywa kupitia mfumo wa GEPG, lakini katika utekelezaji wa mpango huu unaoendelea, Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 20 amesema kwamba kuna uvujaji mkubwa wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali kwa Serikali za Mitaa na ulegevu wa matumizi ya EFD. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ninapenda niiambie Serikali, pamoja na kuzisema Halmashauri za Serikali za Mitaa, bado kuna taasisi 72 za Serikali ambazo hazijaanza kutumia mfumo wa EFD. Matokeo yake taarifa zake, takwimu zake haziwezi kusomwa katika mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali itoe mkazo na msisitizo kuhakikisha kwamba taasisi zote za Serikali zinajiunga na mifumo iliyoidhinishwa na Serikali kwa kuwa Serikali imetumia fedha nyingi kutengeneza mifumo hiyo. Hata kama tukisema taasisi hizo zipewe mitaji na Serikali, lakini pia kunakuwa na udhibiti katika makusanyo ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imeendelea kupokea fedha za mikopo ili kutekeleza miradi ya maendeleo. Naunga mkono hoja ya Kamati kwamba miradi yote inayotekelezwa kwa muda mrefu itumie mikopo ya muda mrefu ambayo ina masharti nafuu ambayo inaiva ndani ya miaka 10 Ili iweze kuleta faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali pia katika miradi ya aina hii, inayotekelezwa kwa muda mrefu ambayo inahitaji fedha nyingi itekelezwe kwa uchache. Inavyotekelezwa kwa uchache inatoa fursa ya kuweza kukamilishwa kwa wakati na kuanza kuleta faida ili iweze kusaidia kuchangia kurejesha mkopo na kuweza kusaidia deni letu liendelee kuwa himilivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, ipo miradi mingi iliyotekelezwa kwa kutumia mikopo, kwa mfano; daraja jipya la Selander alimaarufu kama Tanzanite Bridge. Miradi ya aina hii na mingine inayoonesha fursa ya kuweza kukusanya ushuru, naunga mkono hoja ya Kamati kwamba Daraja la Tanzanite litakapokamilika liweze kutumika kutozwa fedha kwa sababu kuna njia mbadala ambayo mwananchi ambaye ataona hawezi kutoa ushuru atatumia njia nyingine, kwa sababu taarifa tuliyoipokea ni kwamba magari mengi yanapita takriban kwa wastani magari 5,000 yanapita kwa siku katika barabara ile ya zamani. Kwa hiyo endapo kama asilimia kidogo au 25 au 30 itatumia Tanzanite Bridge kwa kutumia tozo, Serikali inaweza ikaingiza fedha ambayo itasaidia pia kuongeza katika kurejesha mikopo yetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipatia nafasi niweze kutoa maoni yangu katika mapendekezo ya mpango wetu wa mwaka mmoja. Moja kwa moja naunga mkono mapendekezo ya mpango pia naunga mkono maoni ya Kamati yangu ya Bajeti ambayo na mimi ni mmoja wa wanakamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimshukuru Mheshimiwa Rais, niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutupatia tani 30 za mahindi Wilaya ya Meatu kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa chakula. Wilaya ya Meatu tuna upungufu wa tani 19,000 hii imesababishwa na ukame uliokuwepo wananchi hawakuweza kulima kwa kiasi kikubwa na waliolima mazao hayakuweza kuota na yaliyoota wengine hawakuweza hata kupalilia. Hivyo tuna upungufu mkubwa wa chakula na tunaomba Serikali iendelee kusaidia Wilaya ya Meatu pamoja na jirani zetu Mkoa wa Singida ambao wanatusaidia mahindi kwa kuleta mahindi yale yamekwisha katika Mkoa wao, Serikali iongeze speed ya kusaidia Wilaya ya Meatu. (Makofi)

Mhshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa mipango yake mizuri na kwa kazi yake nzuri hasa katika matumizi ya zile Trilioni 1.3. kazi kubwa imefanyika. Pamoja na kazi kubwa iliyofanywa ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa pia kazi kubwa imefanywa katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Miundombinu ya barabara imetengenezwa vizuri kwa ajili ya kuwawezesha watalii wetu ili ku-facilitate kazi za utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa, uwekezaji mkubwa umefanywa katika ununuzi wa mitambo ya kutengenezea barabara pamoja na ununuzi wa magari makubwa katika Wizara ya Maliasili Idara ya TANAPA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu na ushauri wangu, Wizara hii sitegemei uendeshaji wa mitambo hii utegemee asilimia 100 kutoka ruzuku ya Serikali. Mitambo hii iliyopelekwa ni mipya kwa sasa ina sifuri katika suala zima la uchakavu, niliomba mitambo hii ijiendeshe yenyewe kwa kufanya miradi mbalimbali si ya TANAPA peke yake lakini hata taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili ikiwemo TAWA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu niltaka sasa kuwena mpango Pamoja na mpiango mingine ya TANAPA na Maliasili kuwe na mitambo ya kuchimba malambo katika hifadhi zetu katika mapori ya akiba ili kuodoa suala la binadamu na wanyamapori kuchangia miundombinu iliyotengenezwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani katika Wilaya ya Meatu bwawa letu la Meatu tembo wapatao 15 zaidi ya mwezi mmoja waliweka kambi katika bwawa letu ambalo ni kilomita tatu kuja Mjini Mwanuhuzi. Kwa hiyo, kuwapunguzia wananchi huduma kulikuwa kuna uhaba mkubwa wa maji katika Mji wa Mwanuhuzi kutokana na tembo hao ambao 15 waliweka kambi lakini zaidi ya 15 walikuwa wanakuja na kuondoka. Kwa hiyo Serikali ijikite kuchimba malambo katika hifadhi ili wale Wanyama waendelee kubakia kule kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Wizara hiyo kupewa fedha ya uwekezaji huo nilitaka sasa fedha zile zitakazopangwa ziwekwe katika kuwekeza miradi mingine, katika Maliasili na Utalii kufikiria kuanzisha miradi itakayo ingiza mapato ujenzi wa mahoteli, tuna upungufu wa hoteli katika Mbuga zetu kutokana na uwingi wa watalii wanaokuja kutokana na Mama yetu kuutangaza utalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Halamga ya kufungua malango. Tuombe katika Wilaya ya Meatu tufunguliwe lango la kuingia katika Hifadhi ya Serengeti kwa sababu Wilaya ya Meatu Serengeti imo kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono maoni ya Kamati katika kipengele cha kilimo cha umwagiliaji na ujenzi wa mabwawa. Wizara ya Kilimo ina hekta Milioni 29 ambayo inaweza ikafanywa umwagiliaji lakini ni asilimia Mbili tu ambayo iko chini ya umwagiliaji ambayo ni hekta Laki Nane. Tukiangalia katika hekta Laki Nane hizo naamini kabisa kuna miundombinu ambayo ilishakufa kuna miradi ambayo ilitekelezwa lakini haijakamilika. Kwa Mfano miradi iliyotekelezwa na DASP katika miaka ya 2014 miradi ile haikukamilika lakini ilitumia Mabilioni ya Shilingi kwa mfano kutokana na fedha za Benki ya Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe miradi hiyo ya DASP iliyoanzishwa ya umwagiliaji ili iweze kukamilishwa iingizwe katika ile idadi kukabiliana na uhaba wa maji katika nchi yetu. Mfano Wilaya ya Meatu mradi ulitekelezwa kiasi kwa Bilioni 1.2 ambo ungeweza kuhudumia hekta 150 sawa na kaya 129 ambapo tungepunguza kabisa uhaba wa chakula, kwa sababu tulitegemea kulimwa mazao ya bustani, mahindi, mpunga na mambo mengine lakini pia wananchi wangeweza kujipatia kipato kwa kuuza ziada. Kwa hiyo, niombe miradi ya DASP ikamilishwe ambayo haijakamilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, pamoja na hayo nilitaka kuomba Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo ziweze kushirikiana kwa sababu kitengo cha umwagiliaji kiko katika Wizara ya Kilimo. Wizara ya kilimo haiwezi kufanya peke yake ikaweza kutekeleza miradi ya umwagiliaji. Kwa mfano, Wizara ya Kilimo inaweza ikachangia fedha zake katika miradi ya kutoa maji katika maziwa makuu kwa mfano ule mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya athari ya Tabianchi unaotekelezwa katika Mkoa wa Simiyu kuna component ya umwagiliaji, katika fedha za ufadhili zinahitaji pia nchi yetu ichangie, basi zile fedha ambazo ziko katika Wizara ya Kilimo ziletwe katika mradi huo ili tuweze kutekeleza ule mradi mkubwa wa kukabiliana na athari ya mabadiliko ya Tabianchi hii katika Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuisaidie Meatu, Meatu ina uhaba mkubwa sana wa mvua kwa ajili ya binadamu na hata kilimo. Mimi ninashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Mama Samia kwa kazi nzuri inayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha huu tunaoutekeleza fedha nyingi sana zimeletwa katika majimbo yetu na mimi katika Jimbo la Meatu tumeshapokea wastani wa shilingi bilioni 10 katika miradi mbalimbali, elimu, afya, maji, barabara na miradi mingine mbalimbali ikiwemo mifugo pamoja na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu wake mkubwa kwa Wabunge wenzake. Ni kipindi kirefu nimekuwa nikifuatilia kutekelezwa kwa ahadi aliyoitoa Mheshimiwa Samia Suluhu wakati akiomba kura, akiwa mgombea mwenza mwaka 2015, Meatu, aliahidi kujengwa kwa daraja la Mto Semu katika Kijiji cha Mwamanongu, lakini muda mfupi tu alipoingia nilivyomueleza jambo hili nishukuru tayari juzi tumeshapokea shilingi bilioni 43 kwa ajili ya kufanya usanifu wa daraja hilo, lakini nimshukuru pia Engineer Seif kwa ushirikiano wake mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niombe tu tusiishie katika usanifu kila tunapouliza maswali tuambiwe usanifu unaendelea. Kwa kuwa sisi Wilaya ya Meatu katika Mfuko wa TARURA tumetenga shilingi bilioni 2.7 katika miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo la Mto Semu katika Kijiji cha Mwamanongu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niiombe Serikali mwaka jana mwezi wa tisa iliniahidi kupanua shule ya Sekondari Nghoboko. Naomba wafanye utekelezaji huo kwa sababu, tulijipanga toka mwaka 2008 kupandisha hadhi shule ya Sekondari Nghoboko kuwa ya kidato cha tano na sita kwa sababu, tayari madarasa manne tumekamilisha, ofisi tatu, bwalo linahitaji kupauliwa, tunaomba bweni pamoja na maktaba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu leo kwa kiwango kikubwa nitajikita katika mapato. Tumeona Mheshimiwa Waziri amesema kutakuwa na ongezeko la asilimia 17.1 katika mapato ya Halmashauri ni jambo jema, lakini katika mapato ya Halmashauri yamekuwa na changamoto nyingi katika ukusanyaji wake ikiwemo mapato mengi ya Halmashauri yanakusanywa nje ya mfumo rasmi wa Halmashauri kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianza ikatoa property tax ambayo ilipaswa ikusanywe na Serikali za Mitaa. Tumeona wameondoa parking fees, wametoa tozo za maji ambazo zote zilipaswa kukusanywa na Serikali za Mitaa na sasa kwa asilimia kubwa ushuru wa huduma unakusanywa na TRA. Mapato haya yalitakiwa yalindwe yakusanywe na Serikali za Mitaa kwa sababu zina mahitaji mengi na ni makubwa. Tumekuwa tunaziongezea mapato, lakini mapato yake yamekuwa yakipungua kila mwaka kwa kadri tunavyokwenda. Naomba hili suala liangaliwe kwa kina, Halmashauri zetu zinakuwa hazistawi katika mapato wakati kazi zake ni nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika taarifa iliyopita ya Julai/Disemba kwa mwaka wa fedha uliopita ushuru wa huduma ulionekana kuongoza kuwa chanzo chake kikubwa kwa sababu asilimia 19 ilikuwa imekusanywa ya mapato yote, lakini chanzo hiki kika changamoto nyingi. Mwanzo kazi za kandarasi zilikuwa zikilipwa Halmashauri, ushuru wa huduma ulikuwa ukibakia Halmashauri, lakini certificates sasa zinalipwa Hazina za miradi ya maji, miradi ya barabara, kwa hiyo, ushuru wa huduma umeendelea kukusanywa na TRA.

Niombe namna Serikali inavyoweza kurudisha katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuweza kuzirudishia Halmashauri ziweze kujitegemea kwa mapato kwa sababu Halmashauri zimeendelea kutegemea Serikali kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna miradi mikubwa pia kimkakati ambayo haikusanywi vizuri. Kwa mfano tulivyofanya ziara Kamati ya Bajeti, SGR hawajaanza kukusanya ushuru wa huduma, basi miradi kama hiyo ikibaki hata Serikali Kuu ikakusanywa irudishwe katika Serikali Kuu iweze kuzisaidia Halmashauri kwa sababu, tunaona watendaji wetu wa kata hawana ofisi, baada ya mradi ule wa undelezaji mtaji kusitishwa, kwa hiyo, yamebakia maboma. Warudishiwe basi zile fedha watendaji wetu wapate ofisi, wapate hata vitendea kazi kama pikipiki, waweze kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato kama ushuru wa mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha pili kulichoonekana ni kikubwa ni ushuru wa mazao, lakini ushuru huu umekuwa na changamoto nyingi katika ukusanyaji wake. Nishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuamua kuwapatia pikipiki Maafisa Ugani waweze kusimamia uzalishaji wa mazao, lakini wameenda zaidi wakawawezesha kwa posho, jambo ambalo litasaidia uzalishaji wa mazao ambayo yanachangia kupata ushuru wa mazao tofauti na mwanzo mafaili yalikuwa yakibaki pale kwa Wakurugenzi mpaka msimu unakwisha hawajawaona wakulima wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niombe na sisi TAMISEMI tuige jambo lililofanywa na Wizara ya Kilimo kwa kuwawezesha watendaji wetu wa kata. Watendaji wa Kata ndiyo asilimia kubwa wanasimamia ukusanyaji wa ushuru wa mazao, lakini hawana pikipiki, hawalipwi posho, tumepewa shilingi 100,000; lakini shilingi 100,000 hii wakati mwingine inapita miezi miwili haijalipwa. Basi tuone namna inavyoweza kulipwa na Serikali kuu kwa sababu wenyewe hawawezi kumshinikiza Mkurugenzi kwa sababu ni mwajiri wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia ushuru huu wa mazao kumekuwa na uvujaji wa mapato kwa sababu katika hoja za ukaguzi tumeona fedha zimetumika zikiwa mbichi na moja ya sababu inayochangia kwa kuwa hawalipwi fedha za ukusanyaji wakati mwingine wanajilipa kabla zile fedha hazijafika Halmashauri. Kwa hiyo, tukiwawezesha mianya hii ya uvujaji haitakuwepo kwa sababu fedha inayotumiwa kabla haijafika Halmashauri haiwezi kutambulika katika vitabu vya Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namba tatu katika ukubwa wa mapato ya Halmashauri ni uchangiaji wa huduma ya afya, tumeona wananchi wamekuwa na mwitikio, lakini wananchi wamekuwa wakishindwa kuchangia kikamilifu, tukisimamia vizuri uchangiaji mapato yatakuwa zaidi kuliko mlivyoyategemea 13%. Yapo matatizo kwa sababu kuna upotevu mkubwa wa madawa, lakini Serikali tumekuwa tukiangalia tu upotevu wa dawa lakini pia kuna fedha ambazo hazilipwi na bima ya afya kwa sababu ya ujazwaji mbaya wa fomu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka miwili mfululizo Halmashauri zimepoteza bilioni mbili kwa ujazaji mbaya wa fomu za bima ya afya. Niiombe Serikali iwasaidie weledi katika ujazaji wa fomu watumishi wetu ili yale mapato yasiendelee kupotea, yale mapato yakiendelea kuwepo yatasaidia kuwa-revolving katika Halmashauri zetu wananchi wakienda hawatakosa dawa, wataendelea kujiunga na bima ya afya tutaisaidia Serikali siku ambapo itashindwa kupeleka fedha sisi tayari tutakuwa na fedha za revolving ambazo zitasaidia kuendeleza upatikanaji wa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika service levy pia kuna mapato mengi ambayo hayakusanywi kutokana na kwamba tu ofisi za makampuni haziko Halmashauri ambapo wametekeleza miradi hiyo. Lakini pia kuna halmashauri zinakusanya ushuru huo bila kujua ni faida kiasi gani kilipatikana katika yale makampuni ni kwa sababu hazina access ya kupata turnover ya ile kampuni husika. Niiombe Serikali kupitia TRA na mwenyekiti wa mapato wa mkoa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwosha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Haya malizia sekunde mbili.

MHE. LEAH K. KOMANYA: Azisaidie Halmashauri kupata takwimu cha kiasi ambacho Halmashauri zinatakiwa kutozwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yetu. Nianze kwa kuipongeza Wizara kwa hotuba yao nzuri na kwa kazi nzuri wanazozifanya pamoja na ushirikiano wanaotupatia sisi Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu kuishukuru Serikali kwa namna inavyotekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Katika mwaka huu wa fedha ajira 44,000 zinaendelea kutekelezwa, na tayari ajira 11,000 zimeshatolewa lakini pia watumishi 92, 619 watapandisha vyeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa nashauri kipaumbele kiangaliwe kwenye halmashauri zenye upungufu mkubwa wa watumishi ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ambayo upungufu wake upo juu sana kwa asilimia ikilinganishwa na upungufu wa kitaifa.

Mheshimiwa Spika, katika miaka mitano Halmashauri ya Meatu imekumbwa na uhaba mkubwa wa watumishi kwa sababu watumishi wengi wamekuwa wakihama. Ndani ya miaka mitano walimu 232 walihama huku halmashauri tukipokea walimu 39 tu. Vilevile waliokoma utumishi ikiwemo kustaafu ni walimu 156. Shule za Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Meatu tuna upungufu wa walimu 930 sawa na upungufu wa asilimia 47 huku sekondari tukiwa na upungufu wa walimu 199 sawa na asilimia 42. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nishukuru kwa tangazo la Wizara ya Afya lililotolewa na Professor Abel Makubi kwamba angalau watumishi waweze kudumu kwa miaka mitatu kabla hawajaanza kuomba kwenda katika halmashauri nyingine kwa kuwa sisi halmashauri za pembezoni tumekuwa tukiathirika kabisa; na watumishi wanaporipoti na kuomba uhamisho. Kwa hiyo sisi halmashauri tunakuwa daraja la kupitia watumishi katika kupata ajira.

Mheshimiwa Spika, katika upande wa afya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu tuna upungufu wa watumishi 675 sawa na upungufu wa asilimia 68. Hospitali ya Wilaya ya Meatu peke yake tuna upungufu wa watumishi 201 sawa na upungufu wa asilimia 64 huku zahanati zaidi ya nane zikiwa na mtumishi mmoja mmoja. Mtumishi akihama, akistaafu au akijifungua ile zahanati inafungwa.

Mheshimiwa Spika, tuiangalie kwa jicho la huruma Wilaya ya Meatu ambapo kama nilivyotaja zahanati nane zina mtumishi mmoja mmoja. Hospitali ya Wilaya ya Meatu zaidi ya miaka sita hatuna mtalaamu wa mionzi, (X-RAY) kiasi kwamba inawalazimu wananchi kusafiri kwenda Shinyanga, Mwanza, na Bariadi. Hii inasababisha wananchi hao wanapata gharama na wengine kupata ajali wanapoelekea kwenda kupata kipimo cha X-RAY.

Mheshimiwa Spika, pia Wilaya ya Meatu hatuna Mhandisi wa Vifaa Tiba na hivyo kuisababisha halmashauri kuingia gharama kubwa kwa kuwaleta watalaamu kutengeneza vifaa hivyo. Mathalani kiliharibika kifaa cha kutoa dawa ya uzingizi, kiligharimu shilingi milioni nne kumleta fundi kuja kukitengeneza kifaa hicho. Kwa hiyo kama halmashauri tunaingia gharama kubwa na kutokutekeleza majukumu ya kutibu kwa sababu ya kukosa watalaamu hao. Kwenye ajira nimeona wahandisi wapo naomba Halmashauri ya Meatu tupatiwe mtaalamu mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali katika mfumo wake mpya wa taarifa za utumishi na mishahara. Mifumo hii inatengenezwa na Watanzania wenzetu na wazalendo wenzetu. Mfumo huu ukitumiwa vizuri utasaidia kupunguza tatizo la watumishi hewa kwa sababu mtumishi akistaafu ataondolewa moja kwa moja na mfumo.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Waziri kuna changamoto ya mawasiliano kati ya Wizara ya Utumishi na Wizara ya Fedha. Mfumo wa Lawson unaonesha wage bill ipo chini lakini fedha inayotolewa hazina ipo juu ukilinganisha na wage bill. Kwa mfano; katika ripoti ya CAG iliyopita Halmashauri ya Wilaya ya Uyui ilipelekewa zaidi ya shilingi milioni 309 katika mishahara kutoka hazina zaidi ya Lawson, Kaliua milioni 209.9, Urambo milioni 149. Ni ukweli usiopingika, sababu ya msingi inayosababishwa hivi ni kufuta majina ya watumishi waliokoma utumishi ambapo tunachelewa kupeleka taarifa hazina. Udhaifu huu usipodhibitiwa utaibua upya mishahara hewa Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mwaka 2016 Serikali ilipoanzisha zoezi la kutafuta watumishi hewa kuna watumishi waliokuwa wamepata barua za kupandishwa madaraja ya mishahara yao na asilimia ndogo waliweza kubadilishiwa; lakini kundi kubwa lilisitishwa kusubiri zoezi la kusafisha watumishi. Kundi hili lilikaa hadi mwaka 2017 na wengine mwaka 2018 ambapo walipewa barua mpya zikafutwa zile za zamani; kwa hiyo wamechelewa miaka miwili wakilinganishwa na wale wenzao waliopandishwa mwaka 2016. Waliopandishwa mwaka 2016 walipandishwa tena mwaka 2021 ilhali lile kundi la pili limeendelea kubaki hivyo hivyo na kusababisha manung’uniko kutoka kwa watumishi kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali sasa, kwamba, kwakuwa hawa watumishi hawakuwa na makosa isipokuwa lilikuwa ni zoezi zuri; watakapokuja kupandishwa wale wa 2021 wawachukue na wale wengine lile kundi lingine ili waweze kuwa-balance, maana yake athari yake itakuwa pia katika kiwango cha mshahara ambacho wanatakiwa kustaafu nacho.

Mheshimiwa Spika, zoezi hili lilisababisha pia wengine waliostaafu wasiweze kurekebishiwa mishahara yao. Kuna wengine walirekebishiwa mishahara yao lakini hawakuweza kulipwa mapunjo yao na hivyo kusababisha mafao yao kupigiwa hesabu kwa mishahara ya zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niiombe Serikali yetu Sikivu, Wizara ya Fedha itoe mapunjo ya mishahara kwa waliostaafu. Tunafahamu sasa hivi hawana faili kwa Mkurugenzi na pia hawana faili popote; ni wao wenyewe kutafuta wabunge wao ili waweze kuwasaidia. Serikali iangalie kwa pamoja na iwalipe mapunjo yao ili yawekwe katika mafao na hivyo stahiki ya mafao yao wanayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hoja ya maji. Lakini kabla ya kutoa mchago wangu, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia bajeti, naomba nitoe shukrani za pekee kwa Serikali yetu ya chama cha mapinduzi chini ya Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi zilizoletwa katika Jimbo la Meatu kwa ajili ya kutekeleza miradi. Naomba niseme kwamba chini ya uongozi wa Mama Samia amwekwenda kuandika historia katika Jimbo la Meatu kwa miradi ambayo haikutekelezwa na haikuwahi kufikiriwa kwamba itatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, nishukuru, tumepata mgao wa shilingi milioni 348.5 kwa ajili ya kujenga shule mpya ya msingi Mwanuzi “B” katika Jimbo la Meatu, nakushukuru Mheshimiwa Angela Kairuki. Lakini nashukuru pia jana tumepokea shilingi milioni 229 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa VETA ya Wilaya ya Meatu. Nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Naibu wake. Vijana wanaenda kufurahi, vijana wanaenda kutimiza ndoto zao. Niwaombe tu masomo yatakayopelekwa yaendane na fursa zinazopatikana katika Wilaya ya Meatu. Nishukuru kwa mawaziri wote kwa ushirikiano wao wanaonipa mimi wakati natekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Spika, sasa nijielekeze katika hoja. Niishukuru Serikali mwaka juzi tulipata fedha kwa ajili ya mradi wa dharura wa kuongeza maji katika Mji wa Mwanuzi, mradi wa kutoa maji Mwagwira, kwa kuongeza maji pale mjini Mwanuzi hali ni nzuri tunaendelea vizuri tofauti na miaka mitatu ilivyokuwa wananchi walikuwa wakitumia Bwawa la Mwanainya, kwa hiyo walikuwa wanatumia matope matupu. Lakini mradi huu kulingana na ukame unaoendelea bado baadaye utaanza kuonesha changamoto. Solution kubwa ni kupata mradi wa maji ya kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, 2016 Ofisi ya Makamu wa Rais iliibua mradi wa maji wa kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi chini ya Waziri January Makamba, lakini leo ni miaka saba bado mradi huo haujaweza kutekelezwa; na badala yake Serikali imekuwa ikitupiga danadana kila mwaka, na hata maana halisi ya kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi inaondoka.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri alisema kwamba mfadhiri yuko tayari kutoa fedha lakini, mpaka leo hakuna dalili yoyote; kwa sababu mwaka jana walisema anatafuta mkandarasi wa ujenzi lakini mpaka leo ni zaidi ya mwaka mmoja yule mkandarasi hajatafutwa. Mimi niliomba, kama mfadhiri ameshindwa basi akabidhi mradi huu Serikalini ili utekelezwe na fedha za Serikali kwa sababu Mheshimiwa Rais ameongeza fedha katika mfuko wa maji kupitia shilingi 100 ya kila lita ya mafuta.

Mheshimiwa Spika, mpaka leo hakuna dalili yoyote. Inawezekana kuna masharti magumu; naomba Waziri unapohitimisha uliweke wazi sisi wananchi tuelewe. Mwaka jana pia ulisema kwamba mradi huu katika awamu ya kwanza utatekelezwa mpaka Wilaya ya Meatu, bomba litafika, lakini nimezipata taarifa mradi huu wa awamu ya kwanza ya Meatu haitakuwemo.

Mheshimiwa Spika, mimi mwaka jana nilienda kifua mbele nikaitisha mkutano mkubwa, nikawaambia wananchi Meatu inaingia katika awamu ya kwanza. Leo hii Mheshimiwa Waziri tukimaliza bajeti twende ukawajibu wewe kwa nini mradi haufiki katika awamu ya kwanza. Wewe mwenyewe umekiri kuna hali ya ukame mkubwa katika Jimbo la Meatu lakini tumekuwa tukipata fedha za kusuasua katika bajeti. Kwa mfano, mwaka jana kati ya bilioni 3.1 jimbo la meatu limepata mradi mmoja wa makao shilingi milioni 600 sawa na asilimia mbili. Mwaka huu katika bilioni 5.7 tulikuwa tumepangiwa bilioni 1.4 sawa na asilimia 20 lakini nimepambana ndani ya wiki angalau tumepata asilimia 50 katika bajeti hii tunayoendelea kuitekeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutawezesha kutekeleza mradi Mbushi Kata ya Burashi, Mwangudo, Mwakipopo, Mwanjoro.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na maombi yafuatayo kwa Mheshimiwa Waziri. Tunaomba gari jipya la maji. Jiografia ya Meatu unaijua. Lakini ninaleta kwako, ninaomba uniruhusu nilete maombi maalum kuweza ku-rescue hali ya maji katika Jimbo la Meatu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri mwenyewe anaijua, na tumekuwa tukipata asilimia ndogo ya bajeti. Kwa hiyo naomba nilete maombi maalumu kwa ajili ya kulisaidia Jimbo la Meatu. Lakini ninaomba sasa katika eneo la Lukale Kata ya Bukundi ambako kuna Lake Eyasi eneo lile ni la chumvi maji yale yakipelekwa kwenye sample huwa hayakubaliwi kwa ajili ya matumizi ya binadamu

Mheshimiwa Spika, niombe; katika bajeti ya Serikali Kuu naomba bwawa moja kwa ajili ya Kijiji cha Muhabagimu ambacho kitasaidia Likale na vijiji vya jirani ili wananchi waondokane na adha ya maji ya chumvi ambayo hayaruhusiwi kwa matumizi ya binadamu. Lilijengwa bwawa la Mwanjoro limepasuka kabla ya kutumia, naomba likwarabatiwe na Wizara kwa sababu mkoa na wilaya hawalitambui, lilijengwa na Wizara. Naomba Wizara waje walikarabati ili liweze kusambaza maji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukame katika Jimbo la Meatu nilitaka kutoa ushauri ufuatao;

Mheshimiwa Spika, tunapotekeleza miradi ya barabara, kwa kuwa Serikali ni moja, niombe kila baada ya kilomita kumi moramu ya kujenda barabara itoke kandokando ya barabara ili tuweze kuruhusu ile mifereji iingie katika yale mashimo yaliyojengwa. Maji yale yatasaidia mifugo, na kwa baadaye yataweza kusaidia kuchimba kisima kirefu baada ya muda mrefu ili tutafute solution ya kukabiliana na ukame ulipo katika Jimbo la Meatu. Kwa mfano kutoka Mwanuzi kwenda Mwabuzo tuchimbe pale Mwangikuru ambako hawana chanzo chochote cha maji.

Mheshimiwa Spika, niombe pia katika Bwawa la Mwanyaina basi awatume wataalau wake wakajaribu ku-test kama watapata maji kiweze kuchimbwa kisima kirefu kwa pembeni kusaidia upungufu wa maji. Niombe, kupitia mitambo iliyoletwa, kama alivyosema, kwamba inakuja Meatu, lakini gharama ya uendeshaji wa mitambo hii mikubwa ni asilimia 100 ni sawa na bei ya mkandarasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mitambo hii ni ya Serikali halafu ni mipya kwa nini bei isiwe nusu? Badala ya kujenga visima vinne tutajenga vinane. Na kwa kuwa meneja wa visima ni nchi nzima ni pool, fedha zote zinaingia mle badala yake msisubiri mitambo ichakae muanze kununua mitambo michache michachemichache ili inapoharibika ile ya zamani iwepo mingine ya kuweza ku-replace kutokana na mfuko huu wa revolving.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi jioni hii ili niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yetu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na watendaji wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa namna anavyofikika kirahisi pamoja na Naibu wake, lakini naomba nitoe case study ndogo kwa Mheshimiwa Waziri Ummy pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki kupitia Fedha za Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO–19. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walipatiwa fedha bilioni 69.1 kwa ajili ya kununua magari ambulance na magari ya kusambazia dawa, chanzo lakini walipoona bei ya supplier ni kubwa waliamua kufanya mazungumzo na UNICEF. Kwa hiyo, wakaweza kununua magari haya moja kwa moja kwa mzalishaji. Bei waliyopewa na mzabuni ilikuwa milioni 144.3 kwa ajili ya basic ambulance na gari la chanjo milioni 163, lakini badala yake walinunua ambulance kwa milioni 99 na la chanjo wakanunua milioni 162. Kwa hiyo waliokoa fedha taslimu bilioni 13.2 na hivyo wakaongeza magari kutoka 503 hadi 663. Kukawa na ongezeko la magari 160 na magari hayo 160 yana uwezo wa kusambazwa katika halmashauri zote zilizopo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hapa tunalo la kujifunza, tuendelee kuangalia Sheria zetu za Manunuzi, tuiruhusu Serikali au taasisi kunapokuwa na manunuzi makubwa wanunue moja kwa moja kwa mzalishaji. Tutaokoa fedha nyingi ambazo zitafanya kazi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hivyo hivyo naomba nijielekeze…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, hilo analolizungumza Mheshimiwa Mbunge ni sahihi kabisa na lilifanyika chini ya GPSA na Wizara ya Afya wakaamua kumuacha GPSA na kuenda kununua hayo magari na kuokoa zaidi ya bilioni kumi na kitu ambazo zimetajwa. Kwa hiyo ule msimamo wa Mheshimiwa Rais ni kweli GPSA lazima waondoke kwa sababu walitaka kuiangamiza Wizara ya Afya kwenye ununuzi wa magari. Ahsante sana na hongera kwa mchangiaji. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ummy haya ndio nataka uandike kwenye taarifa yako uyaseme. Haya Mheshimiwa Leah.

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, naunga mkono hoja kabisa kabisa yapo manunuzi makubwa yanafanywa tunaendelea kupoteza fedha kwa kupitia watu wa kati badala ya kwenda moja kwa moja kwa mzalishaji. Suala hili pia lipo upande wa manunuzi wa madawa, tuiruhusu MSD kunapokuwa na manunuzi makubwa waende moja kwa moja kwa mzalishaji na haya yafanywe, sheria iletwe hapa tuweze kufanya mabadiliko ya sheria. Niombe sheria upande wa madawa isilingane na vifaa vingine kutokana na umuhimu uliopo kwa dawa za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kabisa MSD ina changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na sisi Kamati ya Bajeti mwaka jana tulipendekeza unapoanza mwaka wa fedha wakopeshwe bilioni 150 na Benki Kuu ili wanunue madawa. Hospitali zinapohitaji dawa MSD wakutwe wanazo, sio hospitali zinapohitaji dawa ndio MSD waende wakanunue. Suala hili halijatekelezwa lakini naunga mkono maombi yao ya kuomba bilioni 592 kuweza kufanya maboresho MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba hizo fedha zina mgawanyo, uwekezaji, ujenzi wa maghala pamoja na usambazaji wa madawa kwenye item ya madawa, naomba kutoa ushauri mnapoenda kufanya maboresho, lakini maboresho haya bila kuziba mianya ya uvujaji wa dawa, bado katika jambo hili watakuwa hawajafanya kitu chochote. Niwaombe katika fedha walizoomba wameweke kipengele cha udhibiti cha TEHAMA, kuwepo na mfumo katika upokeaji na utoaji wa dawa hadi kwa mgonjwa ili tuweze kujifunga wapi dawa zinapotelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano kwa Hospitali yetu ya Taifa ya Benjamin William Mkapa, inayo mfumo mzuri wa utoaji wa dawa. Naomba na hospitali za mkoa nazo basi zijifunze kupitia Benjamini Mkapa na hapo tunaweza tukajua wapi dawa zinavuja, wapi dawa zilipotelea, lakini pia wataalam wetu wa hospitali hawana weledi wa kutosha katika matumizi ya mfumo na hii inapelekea fomu nyingi kuweza kukataliwa Bima ya Afya. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi jioni ya leo nami nitoe mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yangu. Lakini leo nitajikita kushukuru kwa yale tuliyofanyiwa katika Jimbo la Meatu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna anavyofanya kazi na kwa namna alivyoiendeleza miradi iliyoanzishwa Awamu ya Tano na sasa mingi amekwenda kuikamilisha, likiwepo Daraja la Tanzanite, anaendeleza ujenzi wa Daraja la Magufuli la Kigongo – Busisi ambapo kazi inaendelea na mwaka huu tunaokwenda kuuanza ametenga bilioni 15 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri na Watendaji wote kwa kazi nzuri wanazofanya. Mheshimiwa Waziri hana maneno mengi lakini ana utekelezaji mkubwa nae nimshukuru. Miradi ambayo mimi binafsi niliongea na Mawaziri watangulizi wake ilikuwa haijaanzishwa lakini yeye ameianzisha na inaendelea, nakushukuru sana Mheshimiwa Profesa na Naibu Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia Meneja wetu wa TANROADS Mkoa wa Simiyu kwa kazi nzuri anazofanya za kiwango kwa barabara nzuri zinazojengwa, zinanyanyuliwa juu kiasi kwamba hakuna sasa kukatikakatika kwa barabara wakati wa mvua, lakini pia kwa usimamizi wa fedha mpaka unaona thamani ya pesa inakuwepo.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru katika mpango huu ahadi ya kujenga barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Mto Sibiti – Lalago – Maswa ni ahadi ya muda mrefu, ilikuwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, na sasa Serikali imekwenda kufunga mkataba unaotarajiwa kusainiwa kabla ya mwisho wa mwezi wa Juni kwa mfumo wa EPC+F, lakini imetengwa bilioni 5.5 kwa ajili ya kuanzisha ujenzi huu. Mimi nashukuru kwa sababu hata hiyo bilioni tano itafanya kazi za awali ikiwemo kulipa malipo ya awali.

Mheshimiwa Spika, niendelee kushukuru, tarehe 14 mwezi huu wa Mei, Mheshimiwa Waziri akiwa Itigi wamefunga mkataba wa kilometa 25 katika maingilio ya Daraja la Sibiti kwa shilingi bilioni 21.77. Mimi nashukuru sana, ilikuwa ni kilio cha muda mrefu cha watu wa Jimbo la Meatu, Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kwa sababu ni watumiaji wakubwa wa barabara hii wanapokuja Dodoma. Nikuombe tu utakapofunga mikataba ijayo katika hii barabara niliyoitaja mwanzo basi uje ufungie katika maeneo husika ya urefu ule ikiwemo Meatu na wananchi wafurahi kuona, lakini sisi tunafurahi kwa sababu mkataba umeshafungwa na ujenzi utaanza wakati wowote.

Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa ajili ya daraja la Itembe tumetengewa bilioni 8.4 na Mkandarasi ameshalipwa advance payment ya bilioni 1.2, lakini sasa hivi tayari ana certificate ya kwanza, ninaombe tu malipo ya awali yalichelewa na mkataba huu ni wa mwaka mmoja leo tumebakiza miaka mitano tu lakini bado iko chini. Niombe Serikali iongeze kasi ya ulipaji. Pia madaraja yaliyobaki ya Lyusa, Chobe na Nkoma, naomba na yenyewe pia yawekwe kwenye mpango wa kuyajenga.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru tuliomba lami kilometa mbili pale Mjini Mwanuzi, mmetupatia bilioni moja kwa ajili ya kujenga kilometa 1.25. Barabara hii inakwenda kuwasaidia akina mama kufanya biashara zao usiku na mchana kwa sababu pia inaweza kuwekewa mataa, lakini inakwenda kupunguza mavumbi yaliyokuwa yanachafua maduka ya watu, yalikuwa yanasababisha ajali wakati wa misafara.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru daraja la Paji ambalo lilikuwa ni kilio cha muda mrefu, milioni 389 lilishatekelezwa. Watu wa Meatu hatukutarajia kama daraja la chini litaweza kujengwa, lakini Serikali imetoa milioni 90 kwa ajili ya kufanya usanifu, mimi nashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ninakuomba tuna barabara yetu ya TARURA ya kilometa 45 inayotoka Mwanuzi kwenda Mwabuzo, tunaomba ipandishwe hadhi imekidhi vigezo, barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Meatu, Wilaya ya Maswa na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla. Wataalam kutoka ofisi yako walikuja kuiangalia iweze kuunganishwa na Wilaya ya Igunga, basi naomba uridhie upandishe zile kilometa 45. Nikuombe Meneja wa TANROADS Shinyanga na TANROADS Tabora na wenyewe basi tuungane pale, kwa sababu wafanyabiashara wengi wa Meatu wanaelekea kule Igunga na kusisimua biashara na uchumi wa pale Igunga.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru Serikali kwa jitihada inazofanya daraja la Mwamanongu ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Samia ya 2015 akiomba kura akiwa mgombea mwenza aliahidi kujenga daraja. Daraja lile lina mita 120 ni daraja la TARURA, uhakiki umeshafanyika litagharimu bilioni saba. Naomba sasa upande wa TARURA na wenyewe walitekeleze kwa sababu sikupata muda wa kuongea kwenye Wizara ya TAMISEMI. Naomba sasa na lenyewe litekelezwe, liko katika hii barabara kilometa 45.

Mheshimiwa Spika, nimalizie sasa kwa kuwaambia wananchi na kuwashukuru Serikali kwa kupewa fedha za bottleneck kutoka katika Mfuko wa Fedha wa Dunia, shilingi milioni 400, ambapo tunakwenda kujenga Daraja la Mang’wina kwenda London na Mwajidalala.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii niweze kutoa maoni yangu kwa hoja iliyopo mbele yetu. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Fedha lakini pamoja na maoni ya Kamati ya Bajeti ambayo ni mmoja wa Wajumbe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazofanya ikiwepo kurejesha nyongeza ya mshahara wa watumishi annual increment hii ni faraja kubwa kwa watumishi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake na wataalam wote waliopo chini ya Wizara ya Fedha, kwa kweli kazi nzuri wanafanya katika kutekeleza majukumu yao lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuendelea kulipa madai ya watumishi na watumishi wanafurahi. Nimewauliza wakasema hawana changamoto zilizopo ni ndogo ndogo lakini kubwa kurudisha on call allowance, kwa sabbau tunatambua kwamba watumishi wetu ni wachache. Mtumishi mmoja wa afya anafanya kazi ya watumishi ambayo ingefanywa na watumishi watatu, hivyo kurudisha on call allowance ni faraja sana kwa watumishi wetu. Lakini nikupongeze kwa namna mnavyolipa madai ya wakandarasi, madai ya watumishi, kwa hiyo, hata uchumi wa Nchi unaendelea kuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kushukuru kwa Mheshimiwa Waziri katika majukumu ya Wizara ya fedha niongelee jukumu moja ambalo amelifanya vizuri na sisi wote tunaona kuhusu kuratibu upatikanaji wa fedha kutoka taasisi za fedha za kikanda na za kimataifa kwa ajili ya kutekeleza bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika katika miaka ya nyuma upelekaji wa fedha hususan fedha za maendeleo katika halmashauri za Serikali za mitaa ulikuwa chini kabisa. Hadi kumaliza mwaka ni asilimia 30 au 20 ya miradi ya maendeleo ndio iliyokuwa imepelekwa lakini sasa tumeona wote ni mashahidi na zaidi ya asilimia 90 na wengine kuvuka malengo na wengine kuletewa fedha ambazo hazikuwa kwenye mfumo wa bajeti ya halmashauri za wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru wengi tunaona wananchi wanaona miradi inatekelezwa katika halmashauri zetu kila kata ukienda, kila kata watumishi wako bize kutekeleza miradi ya maendeleo. Huu ni ushahidi tosha kabisa katika Wizara ya Fedha kwa awamu hii upelekaji wa fedha katika ngazi za chini unaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mapato mengi yanatumika pia yanatumika pia mapato ya ndani. Nishukuru tunatumia fedha zetu wenyewe kupeleka kutokana na tozo mbalimbali lakini niipongeza TRA kwa mwezi Desemba ilivunja rekodi ya makusanyo ambayo ilikusanya trilioni 2.7 ambayo haijawahi kutokea. Niombe tuendelee kuwatia moyo watumishi wa TRA pamoja na Kamishna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee na niipongeze Serikali kwa kutumia mifumo yetu wenyewe iliyotengenezwa na wataalamu wetu. Kiupekee nimpongeze Mkurugenzi wa Mifumo wa TAMISEMI, nimpongeze Mkurugenzi wa Mifumo wa Hazina lakini niombe sasa, niishauri Serikali tuendelee kuwajengea uwezo, tuendelee kuwapa motisha ili waweze kufanya kazi vizuri, kwa sabbau wameokoa fedha nyingi za kigeni ambazo tulikua tunatumia kulipa mifumo iliyotengenezwa nje lakini mifumo hiyo inatengenezwa na wataalamu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sikuchangia TAMISEMI, naomba niongelee maboresho katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kwa kuboresha Mfumo wa LGRCIS na kuupa jina la Tausi. Ni ukweli usiopingika katika mfumo uliokuwepo wa POS mapato ghafi mengi yalikuwa yanapotea kabla ya kufikishwa benki. Fedha nyingi zilikua zinakusanywa na kutumia kabla ya kufika benki na hivyo kupunguza mapato ya halmashauri husika. Lakini sasa kwa kutumia Mfumo wa Tausi niipongeze TAMISEMI kutakuwa na udhibiti wa mapato ghafi kwa kutumia matumizi ya zuio la kiwango katika ukusanyaji ambayo ni float management. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ushauri wangu kwa kutumia mfumo huu wa float management, nina uhakika sasa ule wasiwasi uliokuwepo wa halmashauri kumpa wakala chanzo kwa kuhofu kwamba atakusanya mapato mengi yasifike halmashauri na yeye akanufaika. Sasa tatizo hili linaenda kutatuliwa na float management kwa kuwa wakala yule atatoa kwanza fedha ambazo alitakiwa kulipa aikusanye, ikiisha anapewa nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika niiombe Serikali, niwaombe watumishi wetu waongeze umakini katika kutumia mfumo huu kwa sababu kwa kutumia float management sasa halmashauri inaweza ikafanya tathmini ya chanzo kimoja baada ya kingine. Niwaombe wakala anapofikia kile kiwango ambacho alitakiwa kulipa mwisho wa mwaka, basi tusifanye udanganyifu wa kukusanya mapato nje ya mfumo, tumuache akusanye mpaka mwisho wa mwaka na itatupa dira ya kiwango kwa kila chanzo kinachotakiwa kukusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii itasaidia sasa kuondokana na tatizo lile la underestimate na niombe sasa niombe Serikali kwa kutumia mfumo huu basi ipo haja sasa baadaye watumishi wetu wajitoe katika kukusanya mapato ya halmashauri, tuwaachie mawakala kama mfumo huu utatumika ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu. Nianze kwa kuunga hoja bajeti ya Wizara ya Ujenzi na nikiipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri zilizofanywa. Ni ukweli usiopingika katika majimbo yetu barabara nyingi sana zimefunguliwa na nyingine zinaendelea kufunguliwa kupitia Mfuko wa TARURA katika fedha za tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiupekee nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuidhinisha kazi hii ifanyike kwa sababu tungeweza kutegemea tu bajeti ile asilimia 30 kutoka Mfuko Mkuu wa Barabara kazi hii kubwa isingeweza kufunguka. Kufunguka kwa barabara hizi kunasadia kupungua kwa gharama ya usafiri katika maeneo yetu ambayo walikuwa wanatumia fedha nyingi kufika katika sehemu za huduma za jamii kwa sababu ya kutokuwa na barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kufunguka kwa barabara hizi kunaenda kuongeza mtandao mkubwa katika barabara za TARURA, kunaenda kuhitaji fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati na kuziendeleza hizi barabara na huku tukiangalia fedha za ukarabati wa barabara za TARURA ni asilimia 30 ya Mfuko wa Barabara; huku ni asilimia 20 tu ya mtandao katika mtandao wote ukitekelezwa. Mathalani katika Jimbo la Meatu, Wilaya ya Meatu katika mtandao wote ni asilimia 20 tu ndio inatekelezwa kwa kila mwaka kutokana na ile asilimia 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni wakati muafaka, tunajua yapo maombi mengi kutoka katika Halmashauri mbalimbali ambazo wanaomba barabara zao zipandishwe hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS. Mimi naomba sasa Wizara ya Ujenzi ipitie maombi haya iweze kuzipandisha hadhi ili tuupunguzie mzigo mkubwa ilionao TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanafanya hayo wasiisahau Wilaya ya Meatu, barabara ya kutoka Mwanhuzi – Mwamanongu mpaka Mwabuzo ni kilometa 40 ambayo tumeiombea kuipandisha hadhi kutokana na umuhimu wa barabara hii ambayo inaunganisha Meatu na Wilaya ya Igunga. Ni barabara muhimu kiuchumi ambayo wakati wa masika imekuwa ikijifunga na wananchi kushindwa kupita hiyo barabara na wananchi kushindwa kufika Igunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu umuhimu wa hiyo barabara kutokana na uchumi wa Meatu ambao unategemea pamba. Magari ya pamba yamekuwa yakikwama kutokana na ubovu wa barabara hiyo. Barabara hii inahitaji fedha nyingi kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niiombe Wizara ya Ujenzi watuunganishie sasa barabara kutoka Mwabuzo kwenda Igunga kwa sababu barabara ya TANROADS inayotoka Kabondo mpaka Mwabuzo imeshia hapo halafu ikakosa mwelekeo. Watumishi kutoka Wizara ya Ujenzi walifika wakaikagua ile barabara na waliona wingi wa magari yanayopita kutoka Igunga mpaka Mwabuzo. Niombe sasa watufungulie ile barabara ili wananchi waweze kupita mwaka wote mzima wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulipitisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa na katika mpango huo kwa mara ya kwanza barabara ya Kolandoto – Lalago – Nghoboko – Mwanuzi mpaka Sibiti iliingizwa katika mpango wa maendeleo na sisi Wanasimiyu tulifurahi. Isitoshe katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango barabara hiyo iliingizwa katika kutekelezwa baada ya miaka takribani 20 kuwepo tu katika ilani ya uchaguzi bila kuingizwa katika mpango wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ilipoingizwa kiasi cha shilingi milioni 5,000 kilitengwa kwa ajili ya barabara hiyo na walianza kwa kutengeneza daraja la Mto Itende, lakini ni mwaka mzima kuanzia Julai mpaka leo ninapoongelea ni mchakato wa manunuzi unafanyika. Mimi najiuliza kama ni kipande hicho tu kidogo mwaka mzima tunafanya mchakato wa manunuzi, je, tutakapopokea yale mafedha tunayoyategemea kutoka wahisani tutafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niiombe Wizara iangalie hii changamoto kwa nini miradi mingi changamoto iliyopo ni mchakato wa manunuzi? Mara tender imerudiwa, mara mchakato mwaka mzima na kuendelea. Hii inakwamisha utekelezaji wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile barabara kuna Daralja la Sibiti ambalo liligharimu takribani shilingi bilioni 34.4 kujengwa. Barabara hiyo imechukua muda mrefu na imetekelezwa, lakini imekosa tija kwa sababu zifuatazo; kwanza kuna kilometa 25 ambazo ilinyanyuliwa mbuga, magari mengi kwa sasa hivi hata kiangazi hayapiti kwa sababu changarawe ile inapasua madaraja, kwa hiyo, inawalazimu kuzungukia Shinyanga. Mwaka jana ilitengwa fedha, lakini mwaka huu sijaona hata nini kinaenda kufanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe hizo kilometa 25 za maingilio ya Daraja la Sibiti zitengenezwe kwa kiwango cha lami kwa sababu magari makubwa yanayoleta mizigo inabidi yazunguke kwa sababu inachana matairi, lakini sababu ya pili, daraja lile lilitengenezwa kwa gharama kubwa, lakini sasa hivi linaanza kumalizwa na mvua, kwa hiyo, itaigharimu tena Serikali kuanza kulinyanyua tena ili liweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami. Daraja hili linakosa manufaa kwa ajili ya ile mito iliyopo upande wa Meatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ni kubwa. Mito hiyo imekuwa ikipoteza maisha ya wananchi, mito hiyo imekuwa ikizifunga kata zilizopo ng’ambo ya pili kuja Wilayani, lakini wananchi wamekuwa wakipoteza mali zao kutokana na mito ile inapojaa maji, wanafunzi wamekuwa wakishindwa kwenda shuleni kwa sababu ya mito ile kujaa maji. Niiombe sasa Serikali kama imekusudia kutekeleza ifanye basi ili lile daraja liweze kupata thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kushukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu, lakini nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali niweze kusimama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwani siku ya jana sisi wananchi wa Jimbo la Meatu na wananchi wa Wilaya ya Meatu kwa ujumla, ilikuwa ni faraja kubwa kwetu sana kutokana na ule utiaji saini wa miradi 28 ya maji. Lakini Mheshimiwa Waziri aliendelea kusisitiza kwamba mradi ule wa kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabianchi ya kutoa maji Ziwa Victoria utatekelezwa mpaka Wilaya ya Meatu, Jimbo la Meatu. Kutekelezwa kwa mradi huu kutaokoa fedha nyingi inayotumika kufanya utafiti na maji yasipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nijielekeze katika hoja iliyopo mbele yetu na niishukuru Wizara ya Fedha na niunge mkono hoja. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa mwaka huu katika kutekeleza majukumu ya Wizara ya Fedha kazi kubwa sana mmeifanya. Kazi kubwa mmeifanya ya kupeleka fedha katika Halmashauri zetu, nadhani mwaka huu mmeweka historia katika upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo. Tumezoea kuona miradi ya maendeleo ikipelekewa fedha kwa asilimia 36 mpaka 40 kwa mwaka mzima, lakini kwa mwaka huu hadi mwezi Aprili, 2022 miradi mingi imepelekewa fedha kwa asilimia 80 na kuendelea. Mimi nishukuru sana na niipongeze sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha hizi zilizopelekwa nyingi tunategemea Serikali ya Chama cha Mapinduzi itatekeleza miradi hii ili kuwe na manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu leo utajikita katika Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali hususani katika katika level ya Halmashauri. Fedha nyingi zinapelekwa, lakini sasa ni wakati muafaka Mkaguzi wa Ndani akawezeshwa kwa ufasaha ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Kwa mfano, Halmashauri ya Meatu yenye Majimbo mawili mpaka sasa hivi imepelekewa shilingi bilioni tisa za kutekeleza miradi ya maendeleo upande wa Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiongelea katika Jimbo la Meatu nasema shilingi 10,500,000,000 kwa sababu fedha zingine tunazipata katika Wakala wa Barabara na Wakala wa Maji. Lakini ukiangalia sasa Mkaguzi wa Ndani kuna upungufu mkubwa wa wakaguzi wa ndani katika Halmashauri yetu ukilinganisha na fedha nyingi sana zinazopelekwa katika miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mimi nishauri kuanzia sasa ipo haja Wakaguzi wa Ndani wakaanza kutekeleza majukumu yao kuanzia fedha zinavyopelekwa, wasisubiri miradi ipelekwe ndio waone changamoto ziweze kuibuliwa. Changamoto nyingi zinajitokeza katika utekelezaji wa miradi ambazo zingeweza kuzuiliwa na Mkaguzi wa Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao uhaba mkubwa wa watumishi tunaomba waongezwe, kuna changamoto ya vitendea kazi ikiwemo mafuta hata magari. Magari yao yamepelekwa miaka mingi sana na yalikuwa yakitumiwa na utawala. Mimi niombe Serikali iangalie, ipeleke magari kutokana na utekelezaji ulivyo wa kasi wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto ya fedha, fedha nyingi wanategemea wapewe na Mkurugenzi ambaye wanakwenda kumkagua. Hapo zamani walikuwa zilizokuwa zinapelekwa katika Fungu la General Purpose, lakini ile General Purpose Halmashauri zingine kwa sasa hivi hazipelekewi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mkaguzi wa Ndani kuendelea kuwaomba Wakuu wa Idara/Mkurugenzi ambaye anakwenda kumkagua kwa hiyo anaweza apate sio kwa wakati ambao unatakiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini mimi niombe Wakaguzi wapelekewe miongozo ya matumizi ya fedha inayopelekwa ili waweze kunusuru miradi ambayo inakwenda kutekelezwa kinyume na ilivyopangiwa. Nitolee mfano, Jimbo la Meatu lilipelekewa fedha za kutekeleza/kukamilisha maboma, lakini user department ambaye ni Mkuu wa Idara ya Afya alibadili matumizi. Tunayo maboma kumi ya zahanati, lakini alikwenda kuanzisha boma jipya, akaacha kukamilisha yale yaliyokuwepo ambayo ndio ilikuwa base ya kuombea zile fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi milioni 35 zilikwenda kuanzisha na mpaka nilipokuwa mimi natembelea lilikuwa usawa wa kifua changu. Lakini mwaka huu wamepelekewa fedha nyingine za kukamilisha maboma mwezi Machi, Mkurugenzi alikuwa kwenye bajeti, yeye kwa kushirikiana na Afisa Mipango wamebadilisha fedha zile, badala ya kwenda kukamilisha maboma yale kumi wamekwenda kufanya miradi mingine wanayojua wenyewe. Lakini tukimuwezesha Internal Auditor ataweza kulizuia hili ndani ya CMT kabla halijapelekwa katika Kamati ya Fedha na Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niunge mkono hoja ya Kamati kwamba kuna haja ya kufanya mabadiliko ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma ili kuleta tija kwenye Kkitengo cha Ukaguzi wa Ndani. Tunaona Kamati za Ukaguzi zinashindwa kufanya vikao vyao kutokana na ukosefu wa fedha, lakini muundo wake kama ulivyoelezwa bado hauleti tija katika kusimamia fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu wanaweza wakaa akidi ikawaruhusu kufanya wakiwa watumishi wa Halmashauri, lakini mimi niliwahi kuhudumu Halmashauri moja Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi alikuwa Afisa Maendeleo ya Jamii. Hili liangaliwe, Wenyeviti wawe na weledi, wawe na uelewa wa uhasibu ili kuweza kuleta tija katika usimamizi wa majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya majadiliano taarifa hii inawasilishwa kwa Afisa Masuuli wa Wilaya au wa Serikali ambaye ndiye mhusika aliyekaguliwa, kwa hiyo, yeye ni hiari yake aifanyie kazi ile taarifa au asiifanyie. Na hoja nyingi zimekuwa zikibaki mpaka zinakutwa na mkaguzi wa nje. Mimi niiombe Serikali ichukue maoni ya Kamati ya Bajeti ili sasa Mkaguzi wa Ndani awajibike moja kwa moja kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa Komanya.

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, lakini niombe taarifa ya internal auditor iwe ajenda ya kudumu katika Kamati ya Ushauri ya Mkoa ili hoja ziwe zinafanyiwa kazi. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, ninaipongeza Serikali kwa kuja na bajeti nzuri, nimshukuru Mheshimiwa Rais wetu mama yetu Samia kwa kuweza kuruhusu kuanzisha dirisha maalum kupitia TASAF itakayosaidia watoto wanaotokea familia maskini. Watoto wengi wanaotoka katika familia maskini wamekuwa wakifaulu vizuri sana na kupangiwa mbali na kushindwa kumudu gharama. Kwa hiyo, kupitia mpango huu kutawasaidia hawa vijana wetu waweze kutimiza ndoto zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee na mchango wangu katika hoja yetu hii katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika eneo la mazingira ya biashara ndogo ndogo na sekta binafsi, ameelekeza kwamba wataitoa asilimia tano iende ikatengeneze miundombinu pamoja na masoko kwa ajili ya wamachinga. Naomba Serikali iahirishe kwanza hili jambo kwa sababu mazingira katika maeneo yetu yanatofautiana. Hivyo ikafanye tathmini pamoja na kuangalia fursa zilizopo katika maeneo yetu ili waone kama tunauhitaji wa kujengewa yale masoko na miundombinu ya Wamachinga vinginevyo miundombinu hii itakwenda kukaa bila kuleta tija yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema kwamba toka tupitishe sheria yetu mwaka 2018 Wakurugenzi wamekuwa wakichangia kwa kasi asilimia 10 katika makundi yaliyotajwa katika sheria hii na kuleta tija, katika kuinua wananchi wetu vijana wetu na wakina mama kiuchumi, tutakapowaondolea asilimia tano tutaendelea kuwadidimiza. Pamoja na Serikali ilitoa maelekezo kwamba mifuko yote ya uwezeshaji kiuchumi iweze kuunganishwa Pamoja, iweze kuhudumia vijana, lakini mpaka leo katika Wilaya ya Meatu hatujawahi kupata mfuko wowote kwenye hiyo mifuko ya uwezeshaji kiuchumi. Kwa hiyo, tutakapopunguza hii asilimia tano tutaendelea kuwapunguzia uwezo wa kujijenga kiuchumi vijana wetu na wakina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, mazingira ya Meatu hayaruhusu kuwa na miundombinu ya kimachinga kwa sababu ya vikundi vinavyojishughulisha na shughuli tofauti ambazo hazihitaji miundombinu hii. Shughuli hizi ni kilimo cha vitunguu, kilimo cha ufugaji ng’ombe, ambao soko lao ni kupeleka minadani tayari soko lipo, kwa ajili ya ile mifugo na mingine inasafirishwa kwenda Dar es Salaam tena inaleta matokeo kwa haraka. Kama asilimia tano itatumika kujenga miundombinu wa wamachinga pale, sioni mwananchi anayetoka Mwasengera kilomita 120 kuja pale makao Makuu ya Wilaya atanufaikaje na hiyo miundombinu. Kwa hiyo, miundombinu hii itakaa idle bila kuleta tija yoyote kwa vijana wetu, labda nimuombe tu Mheshimiwa Waziri aongeze ifikie hata asilimia tano ziwe 15 ili ziweze kunufaisha na kuziba zile pengo la mifuko ya kiuwezeshaji kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika maoni ya Kamati ya Bajeti iliongelea kwamba kilimo ni moja ya sekta ambazo ni nguzo kuu ya maendeleo ya viwanda kwa sababu ndio malighafi zinazopatikana. Mimi naunga mkono maoni ya Kamati kwa sababu zifuatazo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali iwekeze zaidi katika mazao ambayo inayaona ni malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu. Kwa mfano, Kamati ilitembelea Kiwanda cha Nguo cha NIDA kiwanda kile kilionekana kinaupungufu mkubwa wa malighafi ambayo ni pamba, pia Serikali inataka kufufua viwanda vingi vya ginnery kikiwemo kiwanda cha solar, hata viwanda vilivyopo havina malighafi ya kutosha kwa sababu msimu wao unakwenda miezi mitatu tu ile pamba inakuwa imekwisha. Zao hili pamoja na mazuri yaliyofanywa na Serikali mimi nimshukuru Rais kwa miaka miwili mfululizo, bei ya pamba imepanda juu maradufu kuliko miaka ya nyuma ilivyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kusamehe madeni ya pembejeo kwa ajili ya wakulima wa pamba. Nimshukuru kwa sababu, zao hili limekuwa na changamoto nyingi sana kuanzia pembejeo ya kuua wadudu pamoja na mbegu. Pamoja na ukame ulioikumba nchi yetu ikiwemo Wilaya ya Meatu wakulima walipanda mbegu ya pamba lakini hazikuweza kuota kutokana na ukosefu wa mvua, walipotaka kurudishia mbegu zingine walikosa kwa sababu hakukuwa na mbegu zilizokaribu kwa ajili ya kupanda mbegu nyingine. Hii ni kutokana na kiwanda cha kuzalisha mbegu kiko Mkoa wa Katavi, lakini pamoja na kuwa Serikali imeweka ruzuku kwa ajili ya pembejeo bado kuna gharama kubwa ya kusafirisha mbegu hizo kuzitoa Katavi mpaka kuzileta Simiyu. Ninaiomba Serikali ifanye inavyoweza ili wananchi wasiwe na changamoto ya ukosefu wa pembejeo ya mbegu kwa ajili ya viwanda tunavyovifufua pamoja na viwanda vya nyuzi na viwanda vya ushonaji nguo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa nyingine iko kwenye dawa za kuua vidudu. Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais alipokuja Mkoa wa Simiyu alitoa maelekezo wataalam wetu wajikite kutengeneza dawa ambayo itauwa vidudu, lakini mpaka leo Mheshimiwa Samia akiwa Rais bado wakulima wa pamba wanaletewa dawa za kuua wadudu ambazo haziui wadudu, zinafifisha tu. Ukimwagia wadudu ndio wanashamiri, ukimwagia ndio matunda yanaanguka chini, lakini sasa ni afadhali ambao hawakumwagilia angalau wameweza kuvuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali yetu inapoongea kwamba, uzalishaji wa pamba unaenda kuongezeka mara dufu msimu huu, sikubaliani nao, kuweza kulichukua lile kijumlajumla, waangalie maeneo ambayo zao litaongezeka mara dufu, lakini waangalie maeneo ambayo yana changamoto ili waweze ku-deal na changamoto zilizojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kushukuru pia pamoja na upungufu uliopo katika AMCOS zetu na kwamba, utaratibu wa ununuzi maeneo mengine unataka kubadilishwa, lakini AMCOS imefanya kazi kubwa. Mkulima miaka yote amekuwa akipunjwa kilo yake ya pamba, lakini toka AMCOS zianze wakulima hawalii kuhusu kupunjwa mizani kwenye zao la pamba. Hata kama watabadili utaratibu, lakini waendelee kulinda mkulima asiendelee kupunjwa katika mizani ya pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maoni yangu katika hoja zilizopo mbele. Nitoe pongezi kwa mapendekezo mazuri yaliyoletwa na Mawaziri wetu wote wawili. Sina wasiwasi juu ya utendaji wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Samia kwa kazi nzuri anazozifanya hususan katika utekelezaji wa miradi mikubwa na mingine ya vielelezo. Kwanza ni utekelezaji wa mradi wa umeme wa Mwalimu Julius Nyerere ambao hadi Juni, 2023 ulikuwa umefikia asilimia 91 na malipo yake hadi Julai yalikuwa asilimia 84.3. Kutekelezwa kwa mradi huu kunatuletea uhakika wa kupata umeme na tukiwa na uhakika wa kupata umeme, mambo mengi yataenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunahitaji uhakika wa umeme? Hata mapendekezo yaliyoletwa na Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji katika kuanzisha viwanda ambavyo vitafanya mchakato wa awali vinahitaji uhakika wa umeme. Tunahitaji uhakika wa umeme ili kupunguza gharama ya uzalishaji katika viwanda vyetu ili zile bidhaa ziweze kushindana na bidhaa zinazotoka nje ili kuweza kuwavutia wananchi wetu wanunue bidhaa zinazozalishwa nchini zikiwa na gharama ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanalazimika kununua vitu vya nje kwa sababu vitu vile vinazalishwa kwa gharama ndogo, lakini changamoto mojawapo inayosababisha kuwa na gharama kubwa ya uzalishaji ni kutokuwa na uhakika wa umeme. Kwa hiyo, mimi naunga mkono Mpango huu na ninawatakia kila la heri katika utekelezaji au kutuletea mpango ujao ukiwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango, katika mapendekezo aliyoyatoa katika kuchochea na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi ya jamii vijijini yaliyopo katika ukurasa wa 21 na moja ya hatua atakazozichukua ni kuweka mazingira maalum katika kuvutia ujenzi wa viwanda vidogo vijijini kwa lengo la kufanya ongezeko la awali la thamani katika sekta za kimkakati kwa lengo la kuongeza ajira na kubakisha thamani vijini. Maeneo ya kimkakati mojawapo ni kilimo, madini, uvuvi pamoja na mifugo. Nilikuwa nataka nitoe mapendekezo yangu au maoni yangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani kwa upande wa kilimo, mazao yanayotegemewa kufanyiwa mchakato wa awali, mojawapo ni zao la alizeti. Ni ukweli usiopingika, mwaka huu zao hili bei yake iliporomoka vibaya sana na hivyo kukatisha tamaa wakulima kulilima tena. Natambua thamani ya mafuta ya alizeti, yanahitajika katika nchi za wenzetu. Kwa hiyo, maoni yangu, baada ya kufanya mchakato wa awali, basi tutengeneze mazingira ya kuwepo wengine wengi ambao watafanya final processing. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwa na wengi, bado kutakuwa na wachache watakaoweza kuhodhi malighafi hii. Mathalani, katika mwaka huu, wananchi wa Wilaya ya Meatu walichukua alizeti na kupeleka kwenye kiwanda ambacho siwezi kukitaja. Walinunua debe kwa shilingi 6,000/= na walipofika kule walikutana na bei ya shilingi 4,000/=, kwa hiyo, elfu mbili ziliwakata wananchi wetu na yule aliyekuwa anapelekewa alizeti ile anai-process na kuipeleka moja kwa moja nje, ambapo inatuletea fedha za kigeni. Sasa naye anaposema kwamba soko la alizeti limeshuka, nakuwa sielewi. Kwa hiyo, Serikali inavyoweka hii mipango, iwahakikishie wananchi wetu masoko ambapo hakutakuwa na ukiritimba wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja zilizoletwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika maelekezo ya maandalizi ya mpango wa bajeti wa 2024/2025 ni kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabia nchi. Naomba kuwepo na mpango kabambe wa kutekeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuendelea kufanya uhifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2022 kama tutakumbuka, katika kongamano la nishati safi ya kupikia, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo ya taasisi kuanza kutumia nishati safi. Mheshimiwa Waziri wa Mazingira, alitoa tamko kwamba matumizi ya kuni mwisho Januari, 2024. Wakati anatoa yale matamko, tayari sisi huku Bungeni tulikuwa tumeshapitisha bajeti, kwa hiyo, ilikuwa ni ngumu kufanya utekelezaji au itakuwa ni vigumu by Januari, 2024 kwamba matumizi ya nishati ya kuni yawe mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi naomba Serikali iwe na mpango kabambe. Kama ni kukopa fedha katika mfuko wa hazina ikope, kwa sababu taasisi hizo zinatakiwa zipate hii nishati safi na wakati huo huo bado zitaendelea kufanya matumizi kwa nishati iliyokuwa inatumika awali. Kwa hiyo, tukichukua kwa pamoja zile fedha tukajenga ule mfumo, na zile taasisi zinahitaji kupika kila siku, itakuwa ni ngumu kutekeleza mpango huu. Kwa hiyo, naiomba Serikali ije na mpango kabambe katika mapendekezo kuhusu suala zima la nishati safi ya kupikia katika taasisi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu maoni ya Kamati yaliyopo katika ukurasa wa 50 kuhusu Wizara, Idara, Mamlaka na Taasisi za Umma kutoshirikiana wakati wa kupanga na kutekeleza miradi. Hali hii imesababisha baadhi ya taasisi kutekeleza miradi katika ngazi ya Serikali za Mitaa huku utaratibu na usimamizi wa ufanyikaji ukitoka Serikali Kuu moja kwa moja na hivyo miradi hiyo kukosa uangalizi ama kutekelezwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika, tunapoteza fedha nyingi kutokana na huu mpango wa kutozihusisha Serikali za Mitaa. Kama utakumbuka, jana niliongelea mfano, mojawapo wa utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji ambapo watekelezaji walitoka moja kwa moja DASIP bila kuishirikisha halmashauri, tukapoteza shilingi bilioni 1.2, wananchi hawana kitu. Ukienda pale kwenye ule mradi utafikiri ni uwanja wa mpira, hakuna kinachoendelea pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji nayo ilitekeleza Bwawa la Mwanjolwa kwa shilingi bilioni 1.8, limebomoka na sasa wananchi wanahangaika na maporomoko ya maji na mradi ule haujawahi kunufaisha hata siku moja. Sasa basi, kama Meatu ni shilingi bilioni tatu, ukiingiza na uhamilishaji wa mifugo 1,000 ambao ulifanywa moja kwa moja kwa Wizara, leo hii ukienda Meatu huwezi kuona ng’ombe mmoja aliye bora aliyetokana na uhamilishaji, lakini fedha nyingi za Serikali zilipotea. Kama Meatu ni shilingi bilioni tatu: Je, nchi nzima itakuwa ni shilingi ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ione namna inavyopoteza fedha kwa kutozishirikisha halmashauri na viongozi waliopo katika level ya mkoa pamoja na halmashauri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Ninaunga mkono hoja ya Bajeti ya Wizara ya Maji ambayo imesheheni miradi ya kimkakati ya maji kila kona ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza moja kwa moja katika miradi 247 ya maji safi na usafi wa mazingira katika Mamlaka ya Mji wa Mwanuzi ambapo shilingi milioni 867.8 zimetengwa. Niliomba hii kwenye item ya ujenzi wa mabwawa ya majitaka na uboreshaji wa huduma ya maji katika Mji wa Mwanuzi, katika zile component mbili tupewe kipaumbele cha ujenzi wa ma-tank katika mji huu. Kwa sababu, tunavyo vyanzo viwili vya maji ya kutosha, lakini hatuna ma-tank ya kupokelea maji, ili yaweze kusogezwa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye uendelezaji wa rasilimali za maji, hususan ujenzi na ukarabati wa mabwawa ya ukubwa wa kati na madogo, ili kuweza kukabiliana na maeneo yenye adha ya uhaba wa maji kutokana na ukame, mojawapo likiwa ni Jimbo la Meatu. Naipongeza Serikali kwa kutekeleza miradi 14 iliyokamilika nchi nzima, miradi mingine 26 inaendelea, lakini miradi 92 imepangwa katika bajeti tunayoiongea sasa hivi, ikiwemo Jimbo la Meatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaomba kura za marudio ya Uchaguzi wa Udiwani, wananchi waliomba kile chanzo mlichojenga cha Lukale kitanuliwe, ili kiweze kupokea maji ya kutosha na niliwaahidi maombi haya nitayaleta. Nakushukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu Wizara ya Maji ombi hili mmelipokea na mmetutengea shilingi 1,117,000,000 za kutengeneza bwawa hili. Oneni namna mtakavyolijenga, ili muweze kusaidia pia, Kijiji cha Mwabagimu kwa sababu, eneo lile lina chumvi kutokana na Lake Eyasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, nimeangalia katika ukurasa wa 70, hongera kwa hatua hiyo na pia, hongera kwa kazi zilizoanzwa. Matamanio ya mradi huu ilikuwa ni kukabiliana na athari ya mabadiliko ya tabia-nchi ikiwepo upatikanaji wa maji ya umwagiliaji, maji kwa mifugo na maji kwa ajili ya binadamu ambapo kazi mlizoziainisha zimelenga katika majisafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia ujenzi wa kituo cha kusukuma majighafi na ulazo wa bomba ambalo ni la kilomita 75 kutoka kituo cha kusukuma majighafi hadi kituo cha kusafisha maji inaonesha kwamba, component ya maji ya mifugo, component ya maji ya umwagiliaji haimo. Naomba basi hizi Wizara tatu, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo mfanye kazi kwa coordination, kwa kushirikiana, na wa Wizara ya Maji, mkitekeleza tutapata maji ya binadamu, maji mkitekeleza tunapata mifugo na umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Kilimo katika fedha za ECF mmeweka usanifu wa maji na mnashirikiana. Kutokana na maelezo ya Waziri mtashirikiana, ili muweze kuweka bomba la maji ambayo hayajatibiwa, ili yawafikie wananchi kwa gharama ndogo waweze kumwagilia pamoja na mifugo iweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie mwisho. Wizara imeandaa mwongozo na matumizi ya mitambo 25 ya uchimbaji wa visima na seti tano za mabwawa. Mmeweka mwongozo wa utaratibu wa muda wa ufanyaji kazi, muda wa matengenezo, kinga na matengenezo makubwa ya mitambo. Nataka kuuliza, je, gharama za uendeshaji wa hiyo mitambo kwa kila RUWASA mmeziainisha? Je, kuna mfuko unaozunguka au mtategemea asilimia 100 ya bajeti ya Serikali Kuu? Wakati mwingine tumekuwa tukifeli katika bajeti, maana yake ni tutafeli katika kuendesha ile mitambo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba kushauri muweke mfuko wa kuzunguka (Revolving Fund), ili wakati Serikali inapochelewa ninyi muendeleze mitambo. Je, mmetenga katika bajeti fedha za mafuta kuongeza hizo RUWASA? Kwa sababu, naona fedha zinaenda kununua mabomba na kusambaza, je, ruzuku ya mafuta tutapa kutoka Serikali Kuu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Jimbo la Meatu katika vile visima vitano vya kila jimbo liangaliwe kwa mtazamo wa malambo madogo kwa sababu, kwa miaka mitatu mfululizo miradi mikubwa imeshindwa kutekelezwa, muda wote tunatafuta vyanzo. Naomba muweke mtazamo wa kutengeneza malambo madogo madogo. Nakushukuru. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu. Vilevile nitoe pongezi kwa Waheshimiwa Mawaziri wote wawili (Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango na Uwekezaji) kwa kutuletea mapendekezo mazuri na mwongozo mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa moyo wake wa dhati kwa kuamua kuendeleza miradi iliyokuwa imeachwa na mtangulizi wake, mpaka sasa tija inaonekana na miradi inaendelea kuonekana. Kwa mfano ujenzi wa Daraja la juu la Kigongo – Busisi, ambalo utekelezaji wake umefikia 93%, daraja hili gharama zake zote kwa 100% zinagharamiwa na fedha za mapato ya ndani. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa dhati ya moyo wake kwa maamuzi haya makubwa kwa kuhakikisha daraja hili linakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa daraja hili italeta tija na kuchochea uchumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Pia nami nishauri katika mpango huu ili hili daraja liweze kuleta tija zaidi, tujenge upya barabara ya kutoka Kisesa – Daraja la Simiyu – Bunda mpaka Mara Border Ili kuweza kufungua mipaka kwa ajili ya ufanyaji biashara katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maamuzi yake ya dhati ya kuwa na mikakati ya kukuza sekta ya uvuvi ili kuanza kunufaika na rasilimali zilizopo katika bahari kuu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa bluu. Huu ni ujenzi wa bandari ya uvuvi pamoja na ununuzi wa meli ya uvuvi. Utekelezaji wa ujenzi wa bandari ya uvuvi umefikia 70%, ili ni jambo jema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika, sekta ya uvuvi nchini ilikuwa bado haijaweza kunufaisha Taifa pamoja na kuwa na rasilimali za maziwa makuu, ukanda mrefu wa pwani, pamoja na bahari kuu. Kwa mfano, nchi ya Kenya yenye ukanda wa pwani wa kilometa 600 ilikuwa inachangia Pato la Taifa kwa 0.6%, lakini nchi yetu ya Tanzania yenye ukanda wa pwani kilometa 1,424 inachangia 0.03%. Mchango huu ni chini ya malengo ya mpango ambapo ilitakiwa kuchangia 1.9% ifikapo mwaka 2025/2026. Hivyo basi, naungana na ushauri wa Kamati kwamba ujenzi wa bandari ya uvuvi uende sambamba na kuweka mazingira ya biashara nyingine zinazoendana na bandari ya uvuvi, kwa mfano maeneo ya kuchagulia samaki (sorting). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ilikuwa inafanyika nje ya nchi kwa kuwa Tanzania hatukuwa na bandari ya uvuvi wala miundombinu hii haikuwepo. Kwa hiyo, meli za nchi za nje zilizokuwa zinafanya uvuvi katika bahari kuu uchambuzi ulikuwa unaenda kufanyika nje ya nchi, kwa mfano nchi ya Shelisheli na hii ilikuwa inaikosesha nchi, ama kutokuwa na takwimu za uhakika kwa mfano, kwenye tozo ya loyalty. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukuwa na takwimu za uhakika kwenye ushuru wa loyalty, lakini pia samaki ambao walikuwa wanavuliwa nje ya mkataba, nje ya makubaliano, mapato yake yalikuwa hayafahamiki. Kwa hiyo, kama tutakuwa na miundombinu katika bandari yetu inayojengwa tutaweza kuokoa mapato yetu yaliyokuwa yanapotea kutokana na uvuvi na kufahamu loyalty ambayo tunatakiwa tuipate katika uvuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuwe na sehemu za kuhifadhia na kuchakata samaki. Serikali iharakishe ununuzi wa meli na siyo kwamba isubirie ujenzi utakapokamilika ndipo inunue meli. TAFICO inayo nafasi ya kununua meli nyingi zaidi kwa kutumia ubia kwa sababu mazingira ya uwekezaji tayari yatakuwa yametengenezwa, yatakuwa yamevutia na hii itasaidia kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa na bahari kuu, maziwa makuu na mito mingi, nchi yetu bado haiko katika nchi tano ambazo zinafanya uvuvi wa kutumia vizimba. Bado haiongozi, iko nyuma, tunashindwa hata na nchi ya Kenya yenye ziwa peke yake, inatushinda katika uvuvi wa kutumia vizimba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba pamoja na juhudi zinazofanywa na Wizara ya Mifugo ya kuwezesha watu wetu kufanya ufugaji wa vizimba basi wasimamie kuwe na tija zaidi kwa sababu hata nchini bado tuna upungufu mkubwa wa zao la samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuwa mchangiaji wa kwanza. Napenda niunge mkono hoja ya Mabadiliko ya Sheria mbalimbali, nimwombe tu Waziri baada ya mabadiliko kupita alete waraka haraka mahali husika ili sasa mabadiliko hayo yaanze kutumika mapema.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuchangia na mchango wangu utajikita katika kutenga asilimia 10 inayotokana na mapato ya halmashauri. Nishukuru Serikali sasa kwa kuliona hili maana limekuwa na muda mrefu, halmashauri zimekuwa hazitekelezi kwa sababu mara ya kwanza kulikuwa na mwongozo. Naishukuru Serikali pia kwa kufanya mabadiliko yale ya 50/50 kwenda kwa asilimia 40/40/20 kwa sababu ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, fedha hizi mwongozo huu ulitolewa kwa ajili ya kusaidia makundi ambayo yalikuwa yameachwa nyuma kimaendeleo. Makundi haya yalikuwa ni Wanawake, Vijana, wakiwemo na Walemavu. Kwa hiyo, tukitoka 50 / 50 kwenda four, four, two, maana yake ni nini? Tutachukua na wale wanaume walemavu ambao walikuwa wasihesabike katika kundi la vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaamini pia kundi la walemavu na wenyewe wako nyuma sana katika maendeleo wanatakiwa wasaidiwe ili waweze kusonga mbele. Kama fedha hizi halmashauri itazitoa na kuzisimamia vizuri zitaweza kusaidia makundi hayo katika kujikwamua kiuchumi, maana yake nini? Halmashauri itaendelea kutenga kila mwaka katika bajeti yake asilimia10, kwa wakati huo huo kutakuwa na marejesho ya vikundi maana yake fedha hiyo itakuwa na mzunguko.

Mheshimiwa Spika, hapo tatizo liko wapi? Fedha hii awali ilikuwa ina akaunti yake ilikuwa kwa wanawake na vijana, lakini Serikali iliamua kupunguza akaunti zake kutoka thelathini na kitu mpaka sita. Kwa hiyo fedha hizi zilijikuta zinaingia kwenye Akaunti ya Amana. Tunavyoelewa akaunti ya amana ina fedha za kila aina, zikiingia mle zinatumika kwa matumizi mengine. Naishauri Serikali kama tumedhamiria kuyasaidia makundi haya naomba basi ifunguliwe akaunti maalum kwa ajili ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Walemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali pia kwa kutenga riba ndogo ya asilimia mbili ambayo itaenda kushawishi wakopaji. Fedha hizi baada ya kurudisha kumekuwa na tatizo, Maafisa Maendeleo ya Jamii wamekuwa wakizitumia kwa matumizi mengine badala ya kufanyika kama fedha ya mzunguko yaani revolving fund. Hivyo nashauri katika fasili ya nne Waziri mwenye dhamana anapoweka kanuni aangalie matumizi ya fedha hizi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa pia na tatizo katika kubadilisha matumizi ya fedha. Halmashauri kila mwaka zimekuwa zikifanya bajeti kabla ya kupitishwa na TAMISEMI lazima watenge asilimia 10 ya wanawake na Vijana na walemavu, lakini sasa utakuta halmashauri imekusanya asilimia 100 mapato yake, imetumia kwa asilimia 100 ndani yake kuna kifungu cha mchango wa asilimia 10, lakini ukiangalia hakuna fedha yoyote iliyotolewa kama mchango wa asilimia 10, maana yake nini? Halmashauri ilifanya matumizi aidha kwa kupokea maagizo mbalimbali ya Serikali ama ilipoona baadhi ya vifungu vilizidiwa ikabadili yale matumizi ya asilimia 10. Nashauri kwenye kanuni fedha zile zisifanyiwe mabadiliko ya matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya halmashauri zimekuwa hazitambui michango ile kama madeni baada ya mwaka kufunga zinaposhindwa kuyalipa. Niombe sasa taratibu za kihasibu zinaruhusu kuyaingiza kama madeni ili yatambulike mwisho wa mwaka na baadaye zile vikundi viweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo lingine sisi Wabunge na Madiwani kwenye vikao vyetu tumekuwa tukijitahidi kuwaomba Wakurungenzi watoe hizi fedha, bajeti ipo lakini wanatoa sababu kuna matumizi mbalimbali. Nishauri katika taratibu Waziri mwenye dhamana akasimu Madaraka kwa Katibu Tawala wa Mkoa ili aweze kuwafuatilia Wakurugenzi ambao hawataweza kutekeleza utoaji wa hizo fedha ili waweze kuchukuliwa hatua. Maana yake kutenga ni kitu kingine na kutoa fedha ni kitu kingine.

Mheshimiwa Spika, huo ndio ulikuwa mchango wangu, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
The Finance Bill, 2022
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Waziri wa Fedha kwa kuleta Muswada na kupokea maoni ya Kamati na kuweza kuyafanyia kazi, kwa hatua hii nampongeza sana.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kushukuru Serikali kwa kutofanya marekebisho ya kubadili mgawanyo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, wewe mwenye ni shahidi kwa namna Wabunge wengi walivyokuwa wakiunga kwamba asilimia 10 isifanyiwe mgawanyo hii inaonekana ni kwa kiasi gani fedha hii inawasaidia wananchi wetu, ni kiasi gani bado kuna uhitaji mkubwa wa vikundi kuweza kupata hii asilimia 10.

Mheshimiwa Spika, hapa nilitaka kushauri sasa ni wakati muafaka, ni fursa kwa mabenki yetu kuliona hili jambo la uhitaji wa mikopo kwa vikundi vyetu katika Halmashauri. Kwa kuwa sasa, kama kikundi kinaweza kukopa Coaster ya Shilingi Milioni 100 itashindwaje kukopeshwa na mabenki yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa changamoto ni mabenki yetu yaone uwezekano wa kupunguza masharti ikiwepo na vigezo pamoja na dhamana ya mkopo, ikiwezekana basi Wakurugenzi waweze kuwadhamini vikundi kama hivyo ili viweze ku-graduate viende kwenye mabenki viachie vikundi vidogovidogo vingine vinavyoweza kuchipikia, kwa sababu kila mwanachi, kila kijana anayo haki ya kuweza kupata mkopo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie Sheria ya Mifumo ya Malipo, Sura 437 na lengo la marekebisho ni kuweka usawa kwenye utozaji wa tozo hii kwenye miamala inayofanana. Ninaipongeza Serikali kwa kuchukua hatua hii kwa sababu mwaka jana tozo hizi ziliwekwa kwenye makampuni ya simu ambayo yaliwasababisha wananchi wengine kuhama na kwenda kwenye taasisi nyingine zinazofanya miamala kama hiyo. Kwa hiyo, iliathiri mapato ya makampuni ya simu, pia kodi ya pato kutoka katika makampuni haya. Kwa kufanya hivi, italeta usawa na Serikali ione iendelee kuangalia kodi za aina hii ziwezwe kutozwa kwa aina hii.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nishukuru kwa kuweka ukomo wa tozo ya shilingi 4,000 kutoka shilingi 10,000, hii itawapunguzia ugumu wananchi wetu kwa sababu wengi wanaotumia miamala hii ni wenye biashara ndogo ndogo, lakini wenye kipato kidogo kidogo, lakini mitaji yao ilikuwa inaliwa kutokana na gharama kubwa iliyokuwa imewekwa. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kusikiliza jambo hili na lengo la Serikali pia ni kupanua wigo wa watu wengi kuweza kuchangia katika tozo hizi.

Mheshimiwa Spika, nikiri tozo za mwaka jana zimeweza kufanya makubwa katika Jimbo la Meatu tumejenga Kituo cha Afya Iramba Ndogo tumekamilisha madarasa katika Shule za Sekondari Bukundi, Mwamanongu na Ng’hoboko. Kwa hiyo, niwaombe wananchi kwa kuwa kiwango kimeteremshwa, naamini wengi watarudi kuweza kutumia huduma hizi ambazo wengi waliacha au kutumia mbadala wake.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee kuhusu Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41; Serikali imepunguza kiwango kwenye zawadi ya ushidi game task on winnings kutoka asilimia 15 hadi asilimia 10. Niishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa usikivu wake kwa sababu tozo hii imeanza kupungua kutoka mwaka jana na hili lilikuwa ni ombi la Gamming Board, wakati inaanza 2015 ombi lake lilikuwa ni kutoza kwa asilimia 10, lakini Serikali iliweka asilimia 20 kwa wakati huo ilikuwa sawa na VAT.

Mheshimiwa Spika, kwa wakati huo, kodi hii ilikuwa ni kubwa, kwa hiyo ilileta mdololo katika kupatikana kwa mapato ya Serikali lakini ilileta mdololo katika mchezo mzima, kwa sababu Watanzania wengi walikuwa wanaenda kucheza michezo ya nje ambayo hawatozi kodi yoyote, kwa hiyo waliacha kucheza katika michezo ya ndani.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri, niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuendelea kupata, tunaona tulivyopunguza kutoka asilimia 20 mwaka jana hadi 15, kulikuwa na ongezeko la kodi ya bilioni 4.2 na hiyo ilikuwa ripoti hadi Aprili mwaka jana, lakini sasa na hivi tunavyoendelea, Serikali itaendelea kupata zaidi kutokana na kupungua kwa tozo hii. Hili ni jambo pia la kujifunza kwa namna tunapoona kuna wigo mkubwa Serikali iendelee kupunguza tozo ili wananchi wengi waendelee ku-comply vizuri bila changamoto yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze Serikali kwa kuchukua hatua ya kuondoa hatua ya kutoza kodi ya awali kwenye kodi ya mapato ya shilingi 20 kwa kila lita ya mafuta pamoja na sababu zilizoelezwa na Serikali, lakini wauzaji wengi wa rejareja hawana mitaji, wanategemea kukopeshwa ndiyo waweze kulipa. Kwa hiyo tukiweka hii kodi wangeweza kuyumba katika biashara hii. Hii pia inasaidia kwa jicho la pili kwa sababu kila kulipo na vituo vya mafuta, mkoa una malengo yake ya kukusanya. Kwa hiyo, tukipeleka kwenye pull tutakosa jicho la pili la kuangalia kama kodi imeweza kulipa. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuchukua hatua hii.

Mheshimiwa Spika, niongelee marekebisho kwenye Sheria ya Ardhi, Sura 113, nishukuru kwa hatua zilizochukuliwa, lengo likiwa kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari, lakini nataka niseme pamoja na marekebisho hayo yaliyofanywa, kodi nyingi zimelala kwenye hati ambazo zimeshikiliwa kwenye Ofisi za Makamishna zilizoko mikoani hata tukipunguza hii riba hakutakuwa na ufanisi kama Wizara haijachukua hatua ya kuwaambia maafisa kuziachia hati, hati za viwanja walizozishikilia katika maofisi. Ufike wakati kwa jinsi dunia inavyokwenda ya kidigitali, Wizara nayo sasa itumie mitandao kuwajulisha wananchi wanaomiliki viwanja sasa muda umefika wa kulipia. Kinachofanyika ni kusubiri kuletewa karatasi ama unapohitaji kuhusu kiwanja chako ukikenda pale ofisini ndiyo unaambiwa una deni.

Mheshimiwa Spika, nishukuru sana na niunge mkono hoja. (Makofi)