Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Leah Jeremiah Komanya (20 total)

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kutia moyo wananchi wa Wilaya Meatu. Mradi huu ni wa muda mrefu wa mwaka 2009, yapata sasa miaka sita, wananchi walitoa eneo hilo na kuacha kufanya shughuli zao pasipo malipo, matokeo yake bwawa hilo limekuwa likijaa na kusababisha uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa udongo. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie Wizara katika mpango mkakati wake wa mwaka 2016/2017, imepanga ni lini mradi huo utakamilika na uanze kutumika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, nimekuwa nikishuhudia miradi kama hii, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuchimba mabwawa, lakini yamekuwa hayakidhi mahitaji kama ilivyokusudiwa, kwa mfano mradi wa maji Mjini Mwanuhuzi, naomba Serikali iniambie je, inaniahidi nini kukamilisha mradi huo na kuusambaza katika Vijiji vya Jinamo, Paji, Mwanjolo, Koma na Itaba?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ameuliza ni lini bwawa la Mwanjolo litakamilika; katika bajeti yangu ambayo nitawasilisha hapa Bungeni muda siyo mrefu, tumeliwekea bwawa hili mpango wa kuweza kulikamilisha, kwa hiyo, tutaleta maelezo na kazi ambazo zitafanyika ili tulikamilishe bwawa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu mradi wa maji anaoelezea, lini tutakamilisha katika vijiji vingine; mambo yote haya tumeyaweka kwenye mpango, kwanza tunakamilisha miradi yote ambayo inaendelea iliyokuwa kwenye program ya maji awamu ya kwanza, halafu tunaingia awamu ya pili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge nia ya Serikali ni kwamba, miradi yote ambayo ipo tutaikamilisha na tutakwenda kuikagua kuhakikisha kwamba inafanywa jinsi inavyotakiwa. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Serikali katika kutatua upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo kame vijijini, imekuwa ikihamasisha kujenga miundombinu ya uvunaji wa maji kwa kutumia mapaa ya nyumba za Serikali, Asasi za Umma na nyumba za watu binafsi; na pia imekuwa ikitoa miongozi katika Halmashauri kutunga Sheria ndogo kwa ajili ya uvunaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimekuwa nikishuhudia uvunaji huu wa maji ya mvua katika paa, ukivunwa kwenye mabati yaliyopakwa rangi. Naomba niambiwe kama kuna matatizo yoyote yanayopatikana kutokana na maji yaliyovunwa toka kwenye mabati yaliyopakwa rangi.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Komanya, ameelezea vizuri kabisa kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba Halmashauri zinaweka Sheria ndogo ndogo na zinapitisha michoro kwenye ujenzi wa nyumba kuhakikisha kwamba kila nyumba inakuwa na kisima cha kuvuna maji kutoka kwenye mapaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi ni kuhusu yale mabati yenye rangi. Mheshimiwa Mbunge nakushukuru kwa swali lako zuri. Rangi ikipakwa, baada ya siku 90 process ile ya oxidation inaondoa kabisa kemikali katika rangi,
kwa hiyo, baada ya miezi mitatu hata ukivuna yale maji yanakuwa hayana madhara ya aina yoyote. Kwa hiyo, wala hakuna wasiwasi wowote.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hiyo elimu wale waopaka hizo rangi wanapewa kweli? Kama mvua ikinyesha kabla ya miezi mitatu!
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nielekeze Wakurugenzi kwamba wasimamie, kwasababu nchi yetu imegawanywa na katika mgawanyo huo, utawala uko katika Halmashauri na Halmashauri ina wataalam wote. Kwa hiyo, Wahandisi wote walio katika Halmashauri wasimamie suala hili la upakaji rangi kwenye mabati. Ni kweli upakaji rangi umekuwa unafanyika kwa jinsi mtu anavyopata hela yeye mwenyewe, lakini naomba kupitia Halmashauri, basi elimu itolewe kwamba rangi nayo ina sumu ila baada ya muda fulani ile sumu inaondoka. Kwa hiyo, elimu hii itolewe kwa wananchi pale ambapo wananchi wanataka kupaka rangi katika maeneo yao. Utaratatibu ndivyo ulivyo kwamba unapotaka kufanya ukarabati wa aina yoyote kwenye nyumba ni vyema uombe kibali ili uwe na usimamizi unaofaa.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii.
Matatizo ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mpwapwa yanafanana na matatizo ya Mamlaka ya maji ya Mji wa Mwanuhuzi. Mradi wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mwanuhuzi ulikamilishwa mwaka 2009 na ukakabidhiwa katika Mamlaka ya Maji Mwanuhuzi. Mradi huu ulilenga kusambaza maji katika vijiji Nane lakini ni vijiji Vitatu tu vilisambaziwa maji; na kusababisha qubic mita za ujazo wa maji, ambayo yanatumika ni moja ya tatu tu, na hivyo gharama ya uendeshaji katika Mamlaka ya maji kuwa juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishiriki katika Bajeti ya mwaka huu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, naomba uulize swali tafadhali.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri haikuwa na fedha kwa ajili ya upanuzi wa mradi huu, kwa sababu fedha iliyokuwepo ilikuwa ni kwa ajili ya Mkandarasi mshauri wa vijiji 10;
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kusambaza maji katika vijiji vilivyobaki vya Bulyanaga, Mwambegwa, Mwagwila, na Mwambiti ili wananchi waweze kunufaika na mradi huu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze yeye ni Mama anajua matatizo ya maji, kwa hiyo ufuatiliaji wake ni kwamba unamgusa moja kwa moja. Ametoa taarifa kwamba kuna mradi ulikamilika lakini umehudumia vijiji vichache. Mheshimiwa Leah Komanya, naomba sana ushirikiane na Halmashauri; kwa sababu mwaka huu tumetenga fedha kwa kila Halmashauri, kuhakikisha kwamba hayo maeneo ya vijiji yaliyokuwa yamekosa kupata maji basi muhakikishe kwamba nayo yanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kama kuna tatizo la utaalam, Mheshimiwa Komanya, naomba utakapokuwa umefika kule na mmepata shida ya wataalam basi tuwasiliane ili tuweze kushirikiana kuleta wataalam atuweze kufikisha huduma hiyo hapo. Suala la nyongeza ni kwamba hii Mwanuhuzi iko Mkowa wa Simiyu, na Mkoa wa Simiyu tuna mradi mkubwa ambao utachukua maji kutoka ziwa Victoria, usanifu sasa umekamilika; na wakati wowote tutakamilisha taratibu ili kuhakikisha kwamba Mkoa wote wa Simiyu sasa tatizo la maji tunaliondoa.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la usambazaji wa umeme lipo pia katika Wilaya ya Meatu. Wilaya ina vijiji 109 lakini ni vijiji 21 tu, sawa na asilimia 19 vilivyopatiwa umeme. Ni lini Serikali itavipatia umeme vijiji vilivyosalia?
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo aliyoyataja ni vijiji 21 tu vimepatiwa umeme, na ninadhani anazungumzia eneo la Meatu; na vijiji takribani 105 havijapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyosema kwamba ugawaji wa umeme unakwenda kwa awamu. Tumemaliza awamu ya pili ambayo imehusisha vijiji vingi sana, na awamu ya tatu inakwenda sasa kumalizia kwenye vijiji vyote vilivyobaki nchi nzima. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, vijiji 100 vilivyobaki, pamoja na maeneo ya vitongoji ambavyo pia hajayataja nimhakikishie kwamba yote yatapata umeme kunzia mwaka 2017, 2018 hadi 2019.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na majibu ya Naibu Waziri. Wilaya ya Busega, Itilima na Kituo cha Polisi cha Mwandoya kilichopo Jimbo la Kisesa katika Wilaya ya Meatu, Askari wa Jeshi la Polisi wanaishi katika mazingira magumu. Nikisema mazingira magumu namaanisha hata zile nyumba za wananchi ni za shida sana kupatikana kwa ajili ya kupanga. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri katika mikoa aliyopanga kutembelea yuko tayari kutembelea Mkoa wa Simiyu ili aweze kujionea namna Askari wa Jeshi la Polisi wanavyoishi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Wilaya ya Meatu ilianzishwa mwaka 1986 na majengo hayo yalijengwa mwaka 1999, yapata sasa ni miaka 17. Majengo hayo yameanza kuchakaa na kuoza, lakini kwa mujibu wa majibu ya Naibu Waziri, nimeona hata kwenye ule mgawo wa nyumba 4,136 majengo hayo hayamo. Je, Serikali sasa haioni haja ya kukamilisha majengo hayo na kuweza kuyanusuru?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kwamba niko tayari kutembelea Wilaya ya Busega? Jibu, niko tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba, katika mradi wa nyumba 4,136, Wilaya ya Busega na Itilima haimo. Ukweli ni kwamba, katika Mkoa Mpya wa Simiyu katika mradi wa nyumba 4,136 tunatarajia kujenga nyumba 150. Sasa nadhani sasa hivi kwa concern ambayo ameonesha Mheshimiwa Mbunge, tujaribu kuangalia sasa katika mgawo wa nyumba 150, tuhakikishe kwamba, zinakwenda katika Wilaya ya Busega na Itilima ili kukabiliana na changamoto kubwa ya makazi ambayo Mheshimiwa Mbunge amelizungumza na sisi tunalifahamu.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa makazi haya ya watu wenye ulemavu yako ndani ya Halmashauri, je, Serikali sasa haioni haja Halmashauri ikatenga bajeti ndogo ili iweze kusaidia upatikanaji wa chakula ili wananchi hao wawe na uhakika wa kupata chakula badala ya kusubiri msaada kutoka kwa mwananchi mmoja mmoja? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na jitihada za Serikali za kupambana na mauaji haya. Je, sasa naomba Serikali inihakikishie ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha watu hawa wanahudumiwa na vitendo hivi vinakoma ili wananchi hawa waweze kuungana na ndugu zao na jamii ili waweze kushirikiana katika shughuli mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Halmashauri, ni kweli, kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu labda nifafanue kwanza; jukumu la kwanza la kumlinda mtu mwenye ulemavu linaanzia kwenye familia baadaye taasisi, Serikali kwa upande wa Halmashauri ni sehemu ya mwisho kwenye makazi kwa sababu msisitizo uko katika kuishi katika hali ya kuchangamana na wengine na kweli Halmashauri zinaagizwa kuhakikisha kwamba zinatenga bajeti kwa ajili ya kutoa misaada maalum hasa ya makazi na chakula kwa wale wanaohitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo ambalo liko wazi kisheria, na tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitoa maagizo hayo na kwa kutumia fursa hii niwakumbushe wote wanaohusika na Wabunge pia kwa sababu ni Wajumbe katika Mabaraza ya Madiwani ambayo yanahusika kupanga bajeti ya Halmashauri mbalimbali kuhakikisha kwamba wanasimamia bajeti katika Halmashauri zao ili kuhakikisha kwa mba watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele katika masuala mbalimbali si tu ya makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jitihada maalum, niseme tayari kumekuwa kuna jitihada mbalimbali na hata juzi tu nafikiri, siku ya Ijumaa kwa wale wanaosikiliza habari walisikia kuhusu hukumu nyingine ambayo ilitolewa na Mahakama Kuu - Kagera kwa watu waliofanya tukio mwaka 2008, majina yao siyakumbuki, lakini hizo hukumu zimetolewa na nafikiri katika mwaka huu kumekuwa kuna hukumu zaidi ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba makosa ya mauaji kwa sababu yana adhabu kubwa, kifo ushahidi wake inabidi uwe watertight kwa maana hiyo huwezi pia wakati mwingine ukaharakisha kutoa hukumu kwa sababu wengine wanasema kwa lugha ya kingereza justice rushed is justice buried na kuna changamoto zingine pia katika kesi hizi. Kuna baadhi ya watu hasa ukizingatia baadhi ya matukio yamekuwa yanafanywa na watu wa karibu katika familia, kumekuwa kuna ugumu wa kupata ushahidi kwa haraka, lakini niseme tu jitihada zinaendelea na zipo ambazo zimefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa yote kama nilivyosema, suluhisho la kudumu ni katika kubadilisha tabia na ndio maana siku zilizopita chache katika wiki ya vijana Serikali ilianzisha mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba elimu inatolewa ili tatizo hili liishe na nina imani hili tatizo litakwisha ndani ya muda mfupi.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, zana alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri zinatumiwa zaidi na wanaume na zinarahisisha zaidi kazi kwa
wanaume, hususan, kwenye kaya zenye uwezo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa zana ambazo zitamrahisishia mwanamke kulima mwenye kipato duni kama ninavyomwona mwanamke aishiye Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imekusudia kutoa ajira zaidi. Kwa kupitia malighafi za mazao, si tu ajira zitatoka katika viwanda bali pia katika mazao ambayo yatauzwa na wakulima. Je, Serikali
ina mkakati gani wa kuhakikisha inatoa mbegu ambazo zitaleta tija katika kilimo cha mtama na alizeti katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, jitihada mbalimbali ambazo Serikali inachukua kuboresha kilimo za kugawa na kuleta zana za kilimo zinawasaidia wakulima wote wakiwemo na wanawake. Tunaamini kwamba tukiweza kuwa na zana za kilimo za kisasa, wanufaika wa kwanza watakuwa ni wanawake kwa sababu wao hasa ndio kwa kiasi kikubwa
wanajihusisha na kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile Wizara kupitia Mfuko wa Pembejeo imeweka utaratibu wa kuweza kukopesha zana za kilimo kwa bei nafuu na wanawake kwa kupitia vyama vya ushirika lakini vikundi mbalimbali ni wanufaika wakubwa wa huduma hii. Vilevile Wizara kwa kupitia Benki
ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo kwa ajili ya pembejeo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge aweze kuwasiliana na sisi ili kuwaunganisha akinamama wakulima
wa Simiyu ili waweze kupata huduma hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kugawa mbegu za mtama na alizeti, katika mwaka wa fedha unaokwisha na hasa baada ya changamoto ya mvua kutokuwa nzuri, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iligawa zaidi ya mbegu milioni 14 za mtama. Vilevile tumegawa mbegu za alizeti kwa wakulima mbalimbali nchini wakiwepo na wakulima wa Mkoa wa Simiyu.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye mikakati mizuri. Naomba nitumie muda wangu kuuliza swali moja tu la nyongeza. Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mwanuzi Wilayani Meatu inasuasua kwa kuwa chanzo chake cha bwawa kimejaa matope na kuathirika na mabadiliko ya tabianchi sambamba na chanzo cha New Sola Zanzui kilichopo Wilaya ya Maswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira imefanikiwa kupata sh. 230,000,000,000 ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa maji Ziwa Victoria na kuyaleta Mkoa wa Simiyu na usanifu bado unaendelea. Je, Serikali haioni haja katika usanifu huo ikajumuisha kupeleka bomba kuu katika Makao Makuu yote ya Mkoa wa Simiyu ikiwemo Wilaya ya Meatu na Maswa kwa awamu ya kwanza kwa sababu Wilaya hizi zimeathirika kiasi kikubwa na ukame na ziko katika phase two na fedha ya phase two haijapatikana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kuuliza swali na kwa umakini anaouonesha katika kufuatilia shida za maji za wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe habari njema kwamba baada ya kupatikana sh. 250,000,000,000 siyo 230,000,000,000 za awamu ya kwanza sasa tunaanza utaratibu wa kupata fedha nyingine zaidi za awamu ya pili ambazo zitapeleka maji sasa katika maeneo yote aliyoyataja pamoja na mkoa mzima na mikoa mingine ambayo inakabiliwa na ukame mkubwa unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, Serikali inatamka rasmi kwamba, inatambua changamoto ya maji na ina mipango ya kuyapeleka kwa wananchi wote wanaokabiliwa na ukame katika eneo hilo kwa kupitia mradi huu. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara imeanza kutekeleza ujenzi wa Bwawa la Mwanjolo, lakini mapungufu yaliyopo katika mkataba huo ni mabirika ya kunyweshea mifugo; je, Serikali haioni haja ya kuongeza mabirika ya kutosha ukizingatia Ukanda huo una ng’ombe wengi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sisi tunatambua ya kwamba mifugo ni maisha yetu na ufugaji ndiyo maisha yetu. Nataka nimhakikishie kwamba wao kupitia Halmashauri waibue miradi hii na sisi katika Serikali tutahakikisha kwamba tunawaunga mkono ili kusudi jambo hili linalohusu malisho na maji kwa ajili ya mifugo tatizo hili liweze kuisha.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi nzuri za Serikali, takwimu zinaonyesha kuwa, asilimia 60 ya wagonjwa wanaohudumiwa Hospitali ya Ocean Road wanatoka Kanda ya Ziwa, lakini katika huduma zinazotolewa kwa sasa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando zipo changamoto kubwa ikiwemo uhaba wa fedha wakati wa ku-service ile mashine. Hospitali yenyewe haijitoshelezi na kusababisha huduma hiyo kusitishwa wakisubiri fedha na kuendelea kuleta usumbufu kwa wagonjwa katika Hospitali ya Ocean Road. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka ruzuku ya kutosha katika kitengo cha saratani kilichopo Bugando?
Swali langu la pili, tafiti zinaonesha kuwa maji yaliyoachwa kwenye gari lililopo kwenye jua na yakakaa kwa muda mrefu katika vyombo vya plastiki inaonyesha inapopata joto kuna chemical zinatoka kwenye plastiki aina ya dioxin ambazo zinaonyesha kuna uwezekano wa kupata saratani hususani saratani ya matiti. Je, Wizara ina mikakati gani ya kutoa elimu kwa wananchi?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza kuhusu ruzuku kuongezwa kwa ajili ya kituo cha tiba ya saratani kilichopo Kanda ya Ziwa kwa maana ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando ndiyo kwanza kimeanza kufanya kazi, kwa hiyo, tunatarajia uwepo wa changamoto mbalimbali ambazo zitajitokeza mpaka pale ambapo kita-stabilize. Kwa hivyo, ninaomba niichukue hii kama changamoto na tutatazama changamoto hii inasababishwa na nini ili wakati wa mchakato wa bajeti inayokuja, tuone ni kwa kiasi gani tunahitaji kuongeza ruzuku kwenye kituo hiki ili kiweze kutoa huduma bora zaidi katika mwaka wa fedha unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili ambalo linahusu plastics ambazo zinatumika kuwekea maji ambayo yakikaa kwenye jua kwa muda mrefu inasemekana yanaweza yakasababisha saratani, hili ni jambo ambalo limekuwa likisemwa kwenye mitandao mara nyingi lakini halina ukweli wowote ule na naomba niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote kwamba Serikali iko makini na haiwezi kuruhusu kitu chochote kile ambacho kinauzwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na kikawa na madhara kikaingia kwenye soko, kwa sababu tunafanya uchunguzi pia tunafanya udhibiti wa bidhaa zote ambazo zinaenda kutumika kwa wananchi kupitia taasisi yetu ya Tanzania Foods and Drugs Authority (TFDA) - (Mamlaka ya Chakula na Dawa) ambapo mambo yote haya yakisemwa ama yakizungumzwa kwenye jamii huwa tunayafanyia utafiti wa kimaabara na hatimaye kuthibitisha kama yana ukweli ama hayana ukweli ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili analolisema Mheshimiwa Komanya tulikwishalifanyia kazi na tukabaini ni uzushi na halina ukweli wowote ule na kwa hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuwatia wasiwasi wananchi.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Jeshi la Polisi pamoja na wadau mbalimbali kuhusu kutoa elimu kuacha imani potofu na mila dhidi ya ukatili unaofanywa kwa watu wenye ualbino.
Je, ni lini Serikali itaanzisha database ili kuwepo na takwimu kwa jinsia na umri ambazo zitasaidia kuhakiki mauaji na ukatili ambao haukuripotiwa? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Leah kwa kulileta swali hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali tunazo taarifa za masuala ya sensa ya watu aliowaongelea, ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, kwa sababu tuna taratibu za kupata taarifa kufuatana na mfumo wa Kiserikali. Kwa ajili ya mambo ya kiusalama huwa hatupendi kuziweka wazi kwamba huyu yuko wapi na anafanya nini, lakini tunachofanya ni kuimarisha ulinzi kwa ajili ya kuwahakikishia usalama wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitangazie tu Bunge lako Tukufu kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hakukuwepo na tukio lolote lililojitokeza linalohusisha kitendo cha kikatili kwa ndugu zetu wenye ulemavu. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kupambana na vitendo vyote vya kikatili likiwemo jambo hili alilolisemea Mheshimiwa Mbunge. Kanzidata hiyo ipo na ilishazinduliwa tayari kama nilivyotangulia kusema. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Simiyu mapema Januari, 2017 baada ya kuona maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa, kwanza hakuridhishwa na bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 38 ya kujenga Hospitali ya Mkoa. Hivyo, akasema hospitali hiyo ijengwe kwa shilingi bilioni 10 na kwamba akatoa ahadi zitolewe shilingi bilioni 10 ili mwaka 2019 aje kuzindua hospitali hiyo. Mpaka sasa ni jengo la OPD tu ndilo lililokamilika na 2017 mpaka leo hakuna fedha yoyote iliyoletwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba commitment ya Serikali kuhusiana na ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, swali langu dogo la pili; tunayo Hospitali Teule ya Somanda, hospitali hiyo ina changamoto. Madaktari wanaohitajika ni 22, waliopo ni wanane, lakini hao wanane hawana examination room, hamna Mganga wa Usingizi wala hakuna casuality room.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha hospitali hiyo teule ya mkoa ili wananchi wa Mkoa wa Simiyu wasihangaike kwenda Mkoani Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa maswali mawili ya Mheshimiwa Leah Komanya; na nimpongeze kwa kufuatilia afya na maendeleo ya wananchi wa Simiyu.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba, Mheshimiwa Rais mwishoni mwa mwaka 2017 alikabidhi hospitali zote za rufaa za mikoa ambazo zilikuwa zinasimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuja katika Wizara ya Afya. Na sisi ndani ya Wizara ya Afya tumeshajipanga kuhakikisha kwamba hospitali hizi tunazihudumia na kuzisimamia kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kama nilivyosema katika jibu langu la awali.
Mheshimiwa Spika, niendelee kusema tu kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais ni commitment, nasi ndani ya Wizara tutaendelea kuisimamia kuhakikisha kwamba fedha hizo zinapatikana kwa malengo ambayo yamekusudiwa, baada ya kufanya tathmini ya kina kuangalia mahitaji halisi ya Hospitali hii ya Simiyu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, swali lake la pili lilikuwa ni kuhusiana na watumishi. Katika mwaka wa fedha uliopita, Serikali iliajiri watumishi 3,152 ambao tuliwagawa katika mikoa mbalimbali. Tunatambua bado tuna changamoto kubwa sana ya watumishi na tunatarajia kwamba Serikali itatoa kibali hivi karibuni na Mkoa wa Simiyu utazingatiwa katika mahitaji yake.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali kwamba asilimia 40 ifanye kazi ya uhifadhi. Vile vile kwa mujibu wa waraka asilimia 60 inatakiwa iende katika vijiji vinavyopakana na hifadhi ambavyo ni Mwambegwa, Mwanyaina, Mwagwila, Semu, Nyanza, Matale na vingine vingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2016/2017 vijiji vile havikupelekewa hela na asilimia 40 haikufanya kazi ya uhifadhi na hivyo kuipelekea Idara ya Wanyamapori kushindwa kununua silaha kwa ajili ya kukabiliana na wanyamapori. Je, Serikali haioni sasa ipo haja ya zile fedha zikapelekwa moja kwa moja katika vijiji na asilimia 40 ikapelekwa katika Pori la Akiba kuliko kupelekwa Akaunti ya Amana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, asilimia 44 ya kilometa za mraba ya Wilaya ya Meatu ni hifadhi. Halmashauri imepata ugumu katika kukabiliana na ujangili, uhifadhi wa maliasili na uvamizi wa wanyamapori kwa sababu ina changamoto ya vitendea kazi. Je, Serikali iko tayari kuipatia gari Wilaya ya Meatu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Leah kwa jinsi ambavyo amekuwa akifanya kazi na kufuatilia masuala mbalimbali yanayohusu Jimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali asilimia 60 zinazobaki kule kwenye Halmashauri kwamba ziende kwenye vijiji kama alivyosema, ni wajibu kila Halmashauri zinazopata mgao huu ile asilimia 60 inatakiwa iende katika vile vijiji vinavyozunguka hifadhi, kwa sababu zinatakiwa zitumike katika kuleta maendeleo ya vijiji vile vinavyohusika. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuziomba Halmashauri zote nchini kutekeleza hilo agizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu maombi ya gari, naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto katika lile eneo na Wizara yangu inazo taarifa za kutosha. Tutalifanyia kazi maadam amelileta, tutaona pale hali itakaporuhusu kifedha tutawapelekea gari lile ambalo litawasaidia katika shughuli hizo. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa daraja la Sanjo katika Mto Simiyu na kilometa 4 za lami Mjini Mwanhuzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Komanya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi za Viongozi Wakuu zipo nyingi na kuna baadhi ya maeneo ambapo ahadi zinaendelea kutekelezwa na maeneo mengine tunaendelea na utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunatekeleza. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano tutahakikisha sehemu kubwa ambazo viongozi wameahidi tunaendelea kutekeleza. Kikubwa tu ni kwamba kila wakati tunaendelea kufanya uratibu ili kuhakikisha hizi ahadi zinatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira. Maeneo haya nina interest ya kuyatembelea, nitatembea pia niweze kuona hili daraja alilolitaja pamoja na mipango mizima ya kuhakikisha kwamba ahadi zinatekelezwa, lakini kikubwa tunaboresha miundombinu ya barabara maeneo yote.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inapeleka fedha Halmashauri kulingana na makusanyo lakini kumekuwepo na malimbikizo ya madeni yanayotokana na stahiki za watumishi kama gharama za mazishi, matibabu yasiyo ya Bima za Afya, gharama za kufungasha mizigo kwa wastaafu, masomo na likizo. Je, ni lini Serikali italipa madeni ya mwaka 2016/2017 yaliyohakikiwa na kuwasilishwa Januari, 2018? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali ilipunguza ruzuku ya matumizi ya kawaida kutoka asilimia 100 kwenda asilimia 40, mafungu niliyoyataja yanaonekana kuelemewa. Je, Serikali haioni ipo haja ya kufanya mapitio katika mafungu niliyoyataja na kuweza kuyaongezea bajeti? Mheshimiwa Spika, ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Komanya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza la kulipa madeni ambayo yameshahakikiwa, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu imekuwa ikilipa madeni yote ambayo yamehakikiwa kwa ajili ya watumishi wetu. Kama ambavyo nimekuwa nikiliarifu Bunge lako Tukufu ni mwezi Aprili tu Serikali yetu ililipa zaidi ya shilingi bilioni 43 kwa ajili ya madai mbalimbali ya watumishi wetu katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuongezewa kwa bajeti katika mafungu aliyoyataja Mheshimiwa Leah Komanya, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba katika mafungu ambayo tunayapa kipaumbele kuyapatia fedha za ruzuku ni Mafungu ya Utawala ambayo ndiyo yanashughulikia haya matatizo aliyoyasema kama gharama za mazishi na gharama za uhamisho. Kwa mfano, kwa mwaka huu 2017/2018 tuliomaliza tulikuwa na bajeti ya Sh.27,447,000,000. Kati ya hizi shilingi bilioni 27, Serikali yetu ilipeleka shilingi bilioni 22 kulingana na mahitaji yaliyoletwa kutoka kwenye Halmashauri zetu ambayo ni zaidi ya asilimia 90 ya bajeti ambayo ilikuwa imepangwa. Hili lilikuwa ni Fungu la Utawala ambalo ndilo linaloshughulika na madai mbalimbali aliyoyataja Mheshimiwa Leah Komanya.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo tunatoa kipaumbele kupeleka fedha za ruzuku ni katika Fungu la Elimu ambapo Serikali yetu imekuwa ikiajiri Walimu na tunahakikisha Walimu wetu wanalipwa pesa zao kabla hawajafika kwenye vituo vyao vya kazi au wanapofika tu kwenye vituo vyao vya kazi. Kwa mfano, kwa mwaka 2017/ 2018 tulipanga kupeleka shilingi bilioni 116 na tukapeleka zaidi ya shilingi bilioni 111 kulingana na mahitaji yaliyoletwa kutoka kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tunajua umuhimu wa mafungu haya na tunayapa kipaumbele katika kuyapelekea fedha za ruzuku.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mazingira ya Mkoa wa Simiyu yanafanana na mazingira ya Mikoa ya Kati kwa zao la alizeti lakini wakulima wa Simiyu wamekuwa wakilima zao hili kwa kubahatisha mbegu za alizeti zisizo na tija ukilinganisha na Mikoa ya Kati. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuleta mbegu zenye tija ikiwemo na kutoa elimu kwa wakulima wa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa majibu yangu ya swali la msingi nilizungumzia mikakati iliyopo kwa Shirika letu la ASA, TOSKI na TARI. Mbegu zipo na nawaelekeza watu wa ASA wapeleke mbegu kule kwa Mheshimiwa Mbunge ili mbegu hizi zipatikane kwa gharama nafuu kwa hii mbegu aina ya Record. Pia kuna makampuni binafsi ambayo yamethibitishwa na Taasisi yetu ya Kudhibiti Ubora ya TOSCI yanauza mbegu kihalali nayo nayaomba yapeleke mbegu katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge ili wananchi wapate mbegu kwa urahisi zaidi.
MHE. LEAH. J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona kupitia mradi wa uwekezaji katika sekta ya kilimo (DASP) Serikali ilitumia shilingi bilioni 1.1 fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika kutekeleza mradi wa umwagiliaji katika kijiji cha Mwagwila Wilayani Meatu, lakini mradi huo ulitelekezwa.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari tutaongozana naye.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kutokana na mwamko uliopo wa wananchi kujiunga na vikundi vya ujasiriamali pamoja na VICOBA lakini wananchi wamekabiliwa na kutokuwa na uwezo wa uzalishaji. Tatizo hili linachangiwa na kutokuwepo na Maafisa Biashara wa kutosha katika Halmashauri zetu na kuwajengea uwezo wananchi. Halmashauri zote nchini zina Afisa Biashara mmoja au wawili au hakuna kabisa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaajiri Maafisa Biashara wa kutosha? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema katika mazingira ya sasa kuna vikundi vingi vya uzalishaji mali, kuna VICOBA na shughuli nyingi za kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Kalemani na timu yake kueneza umeme vijijini na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Profesa Mbarawa na timu yake kujenga barabara na sisi kupitia TARURA kujenga barabara za vijijini, fursa nyingi sana zinajitokeza. Kwa hiyo, kuna kazi kubwa sana iliyoko mbele yetu ambayo tunahitaji kuifanya kupitia kada hizi za Afisa Biashara, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Wachumi. Serikali itahakikisha kwamba wanapatikana wa kutosha ili kusudi wananchi wahudumiwe vizuri. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu inapaswa kunufaika na miradi ya maendeleo inayotokana na ujirani mwema, Outreach Department kutokana na Serengeti National Park na Ngorongoro Conservation; lakini ni zaidi ya miaka kumi haujawahi kutekelezwa mradi wowote.
Je, ni lini sasa Halmashauri ya Meatu italetewa miradi ya maendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba taasisi zetu zote zinazohusika na masuala ya uhifadhi zinao mpango madhubuti kabisa wa kuhakikisha kwamba zinachangia katika miradi mbalimbali ya vijiji vile vinavyozunguka katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya ya Meatu nina uhakika kabisa kwamba imetengewa kiasi cha fedha ambazo zitatekeleza miradi mbalimbali ya vile vijiji vinavyozunguka katika maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa tukifanya hivyo, kwa mfano, takribani kuanzia mwaka 2004 mpaka 2016 jumla ya shilingi bilioni 17.2 zimetumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya vijiji vinavyozunguka hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nina uhakika na Wilaya ya Meatu ni mojawapo ambayo imefaidika na itaendelea kufaidika. Na mimi naomba tuwasiliane baadae ili tuone kwamba imetengewa kiasi gani katika mwaka unaofuata.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa fedha za mafunzo zimekuwa zikibaki kila mwaka kutokana na wawezeshaji kutoka Vyuo vikuu Vya Tanzania; fedha hizo zimekuwa zikibaki kwa sababu wakati wa kutekeleza, wawezeshaji kutoka Vyuo Vikuu wamekuwa na programu nyingine katika vyuo vyao. Je, Serikali haioni ipo haja ya kutengeneza TOT wa Mkoa ili hata kama mradi utakapokwisha wanafunzi waendelee kupewa mafunzo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya mimba katika Mkoa wa Simiyu bado ni kubwa. Kwa mwaka 2017 wanafunzi 37 wa Shule za Msingi walipata ujauzito; 2018 wanafunzi 38; halikadhalika katika Sekondari kwa mwaka 2017 wanafunzi 159 walipata ujauzito; na mwaka 2018 wanafunzi 153.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchungu huo mkubwa wananchi waliamua kuanzisha ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Mwanjoro: Je, Serikali ipo tayari kuunga nguvu za wananchi waliofikisha jengo usawa wa boma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Leah Komanya kwa kuendelea kutaka watoto wa kike wapate elimu nzuri na juhudi hizi za kuunga mkono Serikali ambazo imeziweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anasema kuna fedha zinabaki kwenye programu hii. Ni kweli katika mazingira mbalimbali fedha inaweza kubaki, lakini maelekezo ya Serikali ni kwamba fedha ikibaki, wahusika wanapewa taarifa kwenye Wizara na inapangiwa majukumu mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo Mheshimiwa Mbunge aliyotoa ni mazuri, tuyapokee; kuandaa TOT ili programu itakapoisha wawezeshwe watu wa eneo husika kwani itapunguza gharama, wenyewe kwa wenyewe watafundishana kwa lugha zao za nyumbani, hii kazi itaenda vizuri. Kwa hiyo, tunapokea wazo hili, tunalifanyia kazi. Ni wazo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, anazungumza habari ya mimba na kuunga mkono juhudi za kujenga mabweni. Utakumbuka tangu juzi mpaka jana kumekuwa na mjadala katika Bunge hili Tukufu la kumalizia maboma ya madarasa lakini pia na mabweni na Vituo vya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba kazi hii inatekelezwa na Serikali inaunga mkono juhudi za wananchi, tunafanya mpango, tukipata fedha tutaweka nguvu katika maeneo hayo. Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo imepewa miradi mingi ya kuwezesha watoto wa kike wasome, kujenga madarasa, matundu ya vyoo na mabweni. Jambo hili tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika programu ijayo, fedha ikipatikana tutatoka hapa kuunga mkono nguvu za wananchi katika kumalizia mabweni ambayo wananchi wamechangia wenyewe.