Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maida Hamad Abdallah (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais na Baraza la Mawaziri. Sekta ya Kilimo inayojumuisha uzalishaji wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na mazao ya misitu ndiyo tegemeo la maisha ya Watanzania walio wengi.
Hata hivyo, ukuaji wa sekta hii siyo wa kuridhisha sana kutokana na matumizi ya teknolojia isiyoendana na wakati na pia tunategemea majaliwa ya Mwenyezi Mungu katika hali ya hewa. Hata hivyo, tunashukuru hali ya hewa haijawa mbaya sana, kwa zaidi ya miaka kumi tunapata mvua za kutosha na chakula kinapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu kwa kipindi hiki imedhamiria kuwekeza zaidi katika uchumi huu wa viwanda, uchumi wa viwanda utategemea sana kilimo chetu kwa namna tutakavyojipanga vizuri na mikakati endelevu ya kilimo kwa mazao yetu yenye ubora unaostahili. Kwa kipindi kirefu Mkoani Lindi tumekuwa na mbegu za mazao ya mahindi, muhogo, mpunga, korosho, ufuta, zisizo na ubora. Wakulima wetu wanajitahidi sana kulima mazao haya lakini mavuno yake hayaleti tija kutokana na mbegu isiyo bora lakini na namna ya kilimo cha jembe la mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji sasa Serikali ya Awamu ya Tano kuleta mapinduzi ya kilimo na kuondokana na kilimo cha jembe la mkono, kuwa na mbegu bora na kuwa na kilimo endelevu kwa kutumia pia skimu zetu na mabanio. Tunahitaji Maafisa wa Kilimo watusaidie kutoa elimu ya kilimo bora cha kisasa cha mazao ya biashara, kilimo ni biashara lazima sasa tuondoke tulipo tusonge mbele.
Wakulima wetu wanahitaji kupewa elimu, kupata mbegu bora na pembejeo za kilimo kwa wakati, Serikali ni vema ikajipanga kujua mahitaji ili vijana wetu na wanawake waweze kupata ajira na kuweza kukuza vipato vyao kupitia kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Lindi Manispaa tunalo banio limejengwa kwa pesa nyingi sana lakini bado halijawanufaisha wakazi wa Kata ya Ng‟ape, sasa lina zaidi ya miaka mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu korosho; korosho ndiyo zao la biashara katika Mkoa wa Lindi, kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa fedha wakati wa mauzo ya korosho, Vyama vya Ushirika vinawakandamiza sana wakulima hata kama bei elekezi inatolewa. Tunaiomba sana Serikali kutusaidia kusimamia Vyama vya Ushirika, wakulima wetu wamekuwa maskini kwa kipindi kirefu na hawana msaada wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yangu ina dhamira njema ya mfumo wa stakabadhi ghalani, lakini kwa namna unavyoendeshwa wakulima wanapata kero ya kutopata fedha zao kwa wakati na wapo watu wanatajirika kwa mfumo huu hasa wanaoendesha Vyama vya Ushirika na wakulima wanaendelea kuwa maskini na kukatishwa tamaa na Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sekta ya Uvuvi; Mkoa wa Lindi wakazi walio wengi ni wavuvi, maeneo ya Kilwa, Lindi Vijijini na Lindi Manispaa uvuvi uliopo hauna tija. Changamoto kubwa ni pamoja na:-
(i) Kutokuwa na zana bora za uvuvi;
(ii) Kutokuwa na elimu ya uvuvi;
(iii) Kutokuwa na boti zenye engine wakaweza kwenda masafa marefu kwa ajili ya kuvua; na
(iv) Masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri ni kwamba, tunaiomba Serikali kutusaidia Mkoa wa Lindi, vijana wetu wakaandaliwa katika vikundi na wakawezeshwa kufanya shughuli za uvuvi ili kuleta ajira kwa vijana na kuleta ustawi wa wananchi wa Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa kazi nzuri anazofanya na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili na mimi nichangie machache katika bajeti hizi za Wizara mbili. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia jioni hii ya leo kusimama katika Bunge hili na kuchangia bajeti iliyoko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kuhusu ufinyu wa bajeti. Takribani Wizara zote katika bajeti hii zimekabiliwa na ufinyu mkubwa wa bajeti. Kwa hiyo, ni vyema Serikali katika vyanzo vyake vya mapato vilivyopo na vile ambavyo inaendelea kuvibuni siku hadi siku ndani ya bajeti hii iweze kufikiria Wizara tofauti tofauti, hizi tunazozijadili na kuwaongezea ili ziwe na bajeti za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua majukumu waliyonayo Wizara hizi lakini pia nataka nijikite katika Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na ile Tume ya Ajira. Tume hizi zimekuwa zikifanya kazi kwa nguvu zote kwa maslahi ya wananchi na viongozi wa umma walioko katika nchi hii. Tume hizi zimekuwa zikikabiliwa na ufinyu wa bajeti mkubwa na zaidi majengo au ofisi wanazofanyia kazi ni za kupangisha kwa bei ya juu. Vitendea kazi vya kutosha hawana na ukiangalia bajeti yao ilivyo na ukiangalia mahitaji ya fedha ambazo zinatakiwa kulipwa kwa ajili ya ofisi wanazofanyia kazi basi utashangaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunatembelea ofisi hizi, kuna Mheshimiwa mmoja wakati wanatoa changamoto zao alijitolea kuchangia kompyuta pamoja na vifaa vyake. Hii ni aibu jamani, sisi tunakwenda kule kuwapa ushauri na mambo mengine lakini pia sisi sio watu wa kuchangia vifaa vya ofisi hizi wakati ofisi hizi ni muhimu sana katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa ikifanya kazi kwa nguvu zote, lakini pia cha kusikitisha bajeti yake yote ikiwemo mishahara ya watumishi ni ufadhili kutoka nje, inasikitisha sana. Ni vema Serikali ikajitahidi na ikajikita katika suala la kuongeza bajeti katika ofisi hizi. Mara nyingi tumekuwa tukiwalaumu, tukiwakosoa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwamba hawatekelezi majukumu yao lakini kumbe hawana bajeti, hawana ofisi ya kufanyia kazi, wana-share ndani ya ofisi, wanakaa nje, hawana sehemu nzuri za kufanyia kazi, hawana vifaa vya kutosha lakini pia yote haya yanatokana na ufinyu wa bajeti unaozikumba ofisi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niende moja kwa moja katika mikoa na Halmashauri husika. Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wamechangia na kusema kwamba asilimia 30 ya kodi ya majengo ndani ya Halmashauri hazirejeshwi. Wanajitahidi kukusanya kodi hizi lakini pia mrejesho unakuwa hauwafikii. Serikali imewapangia makusanyo kupitia vyanzo vyao vya mapato asilimia 30 kwa mujibu wa bajeti na Halmashauri zimekuwa zikijitahidi sana kukusanya lakini leo kutokana na kuwa hawana mrejesho katika makusanyo kama haya au kodi hizi kwa hiyo imefikia hatua hawawezi kutumia au hawawezi kufaidika na fedha hizi. Pia Halmashauri zetu zina upungufu wa Maafisa Ugani, zina upungufu wa wataalam wa kilimo na hakuna watafiti wa kilimo. Kwa hiyo, ni vyema tukazipa uhuru Halmashauri hizi ili ziweze kujitegemea na kile wanachokikusanya pia tusiwabane sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuweka mfumo sahihi wa matumizi ya electronic kwa kusambaza vifaa vya electronic katika Halmashauri zote ili kuhakikisha kwamba mapato ndani ya Halmashauri hayawezi kuvuja. Yote yanatokana na kuwa hakuna mashine za electronic na ndiyo maana tukaona mapato yanapotea siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la wastaafu. Mara nyingi wastaafu wamekuwa wakiilalamikia Serikali kwamba wanapata usumbufu mkubwa katika kufuatilia haki zao. Baadhi ya changamoto wanazozieleza wastaafu moja ni kutokana na kuwa waajiri hawatekelezi wajibu wao kwa wale wafanyakazi ambao wamejiunga na Mifuko ya Hifadhi jamii ambapo wanakuwa hawafikishi fedha zile mpaka inafikia mfanyakazi anafikia kustaaafu. Pia kuna tatizo la kuchelewa kufikisha nyaraka Hazina. Yote haya inawasababishia wastaafu kuchelewa kupata haki zao na kuja kupata usumbufu baada ya kustaafu. Niiombe sana Serikali kuwafikiria kwanza wastaafu hawa au wastaafu watarajiwa na kuwaomba hizi ofisi kwamba itakapofikia mtu karibu na kustaafu ndani ya miezi mitatu kabla basi nyaraka ziweze kufikishwa mapema kunakohusika ili wastaafu hawa itakapofikia kustaafu waweze kufaidika na wasipate usumbufu. (Makofi)
Kuhusiana na suala la MKURABITA, niipongeze sana Serikali kwa jitihada zake za kufanikisha na suala hili. Pia nitoe pongezi kwamba imeenea katika maeneo mengi Tanzania Bara na kule Zanzibar, wengi wameweza kupimiwa maeneo yao na kupata hati miliki za kimila. Pia niombe sana Serikali kupitia hati hizi za kimila kwa vile tumefungua Benki ya Kilimo wananchi waruhusiwe kuzitumia kama dhamana pale wanapohitaji mikopo kwa ajili ya kuendeleza kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye TASAF, mfuko huu ni muhimu sana katika Taifa letu lakini cha kusikitisha pamoja na kazi kubwa inayofanywa lakini pia jamii ni pamoja na wananchi waliotuzunguka katika Majimbo yetu. Sisi Wabunge mara nyingi hatujui nini mfuko unafanya wala kushirikishwa maendeleo yanayopatikana na hata tukihoji basi inakuwa ni kazi ngumu kupata majibu. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali iwashirikishe Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wawe wa Viti Maalum au wa Majimbo katika maeneo wanayotoka kushirikishwa kwa miradi yote na kwa namna yoyote au hata katika Kamati za TASAF zinazopanga utaratibu mzima kuhusiana na masuala yale ya kijamii na uwezeshaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, nakushukuru sana.