Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Maida Hamad Abdallah (11 total)

MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH) aliuliza:-
Baadhi ya miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri imekuwa ikisuasua kutokana na uchache wa fedha pamoja na kuingia mikataba na wakandarasi wasiokuwa na uwezo wa kutosha na kusababisha miradi hiyo kutokamilika kwa wakati:-
Je, Serikali imejipanga vipi kumaliza tatizo la maji kwa wananchi wa vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Programu ya Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Serikali ilipanga kutekeleza miradi ya maji 1,870 katika Halmashauri mbalimbali nchini. Miradi iliyotekelezwa na kukamilika ni 1,110 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, Halmashauri zilitengewa shilingi bilioni 129.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji. Hadi sasa fedha zilizopelekwa kwenye Halmashauri ni shilingi bilioni 97.6 sawa na asilimia 75.5 ya fedha zilizotengwa.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya upelekaji wa fedha za miradi ya maji katika Halmashauri, imechangiwa kwanza na kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato kwa mwaka na pili baadhi ya wahisani kuchelewa kutoa fedha walizoahidi. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 290 ambazo zitatumika kulipa madeni ya wakandarasi na kukamilisha miradi viporo.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuimarisha makusanyo ya fedha ili fedha zilizotengwa ziende katika utekelezaji wa miradi iliyopangwa.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu suala la watumishi hewa limekuwa likiathiri sana uchumi wa Taifa na kwa kuwa waliohusika wengi wao ni maafisa na watumishi wa Serikali.
Je, Serikali inasema nini juu ya wale waliohusika kurudisha nyuma maendeleo ya nchi kwa njia hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 25/10/2016 Serikali imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wa umma 1,663 kutoka katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao walibainika kusababisha uwepo kwa watumishi hewa kwa mchanganuo ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wizara ni watumishi wa umma 16, kwa upande wa Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali ni watumishi wa umma tisa, kwa Sekretarieti za Mikoa ni watumishi wa umma wa sita, Mamlaka za Serikali za Mitaa watumishi wa umma 1,632 inayofanya jumla ya watumishi 1,663.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hii inajumuisha kuwasilishwa kwa masuala yanayohusu baadhi ya watumishi hawa katika vyombo vya ulinzi na usalama ambapo kufikia tarehe 25/10/2016 jumla ya watumishi wa umma 638 wamefunguliwa mashitaka polisi, watumishi 50 wanafanyiwa uchunguzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na watumishi wa umma 975 mashtaka yao yamefikishwa kwenye mamlaka zao za kinidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hatua hizi Serikali inaendesha ukaguzi wa mara kwa mara kwa mfumo wa taarifa za kiutumishi au Human Capital Management Information System na maafisa wanaobainika kuhusika au kusababisha kuwepo kwa watumishi hewa katika taasisi au mamlaka zao wanachukuliwa hatua za kinidhamu kama vile kuwafungia dhamana na uwezo wa kuingia na kufanya kazi katika mfumo huo na hatua nyingine za kinidhamu. Nakushukuru.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR (K.n.y. MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH) aliuliza:-

Mafuta na gesi ni rasilimali zinazotegemewa kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa letu:-
Je, ni aina ngapi za gesi zilizogundulika na faida iliyopatikana tangu ugunduzi huo ulivyotokea?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, lililoulizwa na Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, Mbunge wa Chakechake, Pemba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lilianza utafiti wa masuala ya mafuta na gesi asilia nchini mwaka 1950 ikihusisha utafiti katika maeneo ya baharini ya kina kirefu, maziwa na nchi kavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi asilia iliyogunduliwa katika maeneo ya bahari ya kina kirefu ni futi za ujazo trilioni 47.08 na katika nchi kavu ni futi za ujazo trilioni 10.17, hivyo kuwa na jumla ya futi za ujazo trilioni 57.25 ya gesi asilia nchini. Gesi asilia iliyogunduliwa ni ya aina moja ya sweet gas, yaani gesi ya kiwango cha juu sana ambayo ina kiwango cha chini sana cha sulfur.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida kubwa iliyopatikana kutokana na ugunduzi wa matumizi ya gesi asilia nchini ni uzalishaji wa umeme wa bei nafuu kwa matumizi ya gesi asilia ikilinganishwa na mafuta. Uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia umeongezeka kutoka unit 2,714.25 kwa mwaka 2014 hadi kufikia unit 4,119 mwaka 2016. Hii ni sawa na asilimia 54.66 ya ongezeko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya umeme imeshuka kutoka wastani wa sh. 188.56 kwa unit mwaka 2014 hadi wastani wa sh. 125.85 kwa unit kwa mwaka 2016, sawa na punguzo la asilimia 33.26. Mbali na punguzo kubwa la umeme, gharama za maombi ya service charge ziliondolewa tangu tarehe mosi Aprili, mwaka 2016, lengo likiwa ni kupunguza gharama za umeme kwa wateja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Helium One imefanya ugunduzi wa gesi ya helium katika maeneo ya Ziwa Rukwa katika bonde la ufa. Kiasi kilichogundulika kinakadiriwa kufikia futi za ujazo bilioni 54. Gesi ya helium hutumika katika matumizi ya mashine za MRI Scanners na vinu vya nuclear katika matumizi ya baluni kwa matumizi ya ndege, hasa kuruka na ndege hewani.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-
Mazao ya mdalasini na mchaichai yanategemewa sana kama viungo na pia hutumika kutibu afya zetu ndani na nje ya nchi na mazao haya yanastahamili sana ukame na hayategemei mbolea lakini wakulima wengi hawana uelewa wowote kuhusiana na mazao haya; kwa upande wa mchaichai bei shambani ni Sh.250,000/= kwa tani moja na bei ya kiwandani ni Sh.400,000/= kwa kila tani moja:-
Je, Serikali ipo tayari kutoa elimu kwa wakulima ili kuweza kufahamu faida ya mazao hayo ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naaomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao ya mdalasini na mchaichai ni miongoni mwa mazao ya bustani yanayozalishwa kwa wingi na wakulima wadogo hususan katika Mikoa ya Tanga, Morogoro na Kigoma. Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mazao hayo na faida ya kitabibu na kiburudisho, kumechochea ongezeko la bei na hivyo kupelekea hamasa kwa wakulima kuzalisha zaidi. Hivyo, uzalishaji wa mazao haya umeongezeka kutoka tani 10 za mchaichai mwaka 2010 hadi tani 15 mwaka 2014 na tani 600 za mdalasini hadi 15,000 kwa kipindi hicho hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ongezeko hilo la mavuno, uzalishaji wa mazao haya hapa nchini unakabiliwa na changamoto mbalimbali hususan mwamko hafifu wa wakulima katika baadhi ya maeneo hivyo kufanya uzalishaji wake kuwa siyo wa kibishara kutokana na kutokuzingatia kanuni bora za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuongeza hamasa na elimu ya uzalishaji wa mazao ya viungo ikiwemo mchaichai na mdalasini Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wengine iliandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani wa miaka 10 (2011-2021). Pia, Serikali imeandaa mwongozo wa uzalishaji wa mazao yakiwemo ya viungo kulingana na kanda za kiikolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, taasisi zisizo za kiserikali na sekta binafsi, Serikali imeendelea kutoa hamasa kuhusu mazao ya bustani ikiwemo mchaichai na mdalasini katika ngazi za Kata, Vijiji kupitia huduma za ugani na maonesho ya nane nane. Hivyo basi, Serikali itaendelea kutoa hamasa na elimu kuhusu kanuni bora za kilimo kwa wakulima ili kuongeza kiwango cha uzalishaji na kuweza kupata mazao bora kulingana na uhitaji wa soko.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-
Baadhi ya maeneo katika Kisiwa cha Pemba yamekuwa na tatizo la kukosa mawasiliano ya simu kwa mitandao ya Tigo, Airtel na Zantel hali ambayo imekuwa ikisabbisha usumbufu.
Je, Serikali inatoa kauli gani kwa vile tatizo hili ni la muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu la Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na watoa huduma za mawasiliano kuhakikisha kuwa huduma bora za mawasilino nchini zinawafikia wananchi wote kwa kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali za kiufundi na kiutendaji. Kwa mujibu wa takwimu za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Kisiwani Pemba kuna jumla ya minara saba ya Airtel, minara tisa ya Tigo, minara tisa ya Vodacom, minara 24 ya Halotel na minara 47 ya Zantel.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, minara hiyo imejengwa katika Kata zifuatazo: Kata za Kisiwa Panza, Muambe, Kangani, Stahabu, Kengeja, Jombwe, Kendwa, Mtambile, Ng’ombeni, Uweleni, Mtangani, Chambani, Ukutini, Ngwachani, Chumbageni, Mizingani, Kilindi, Pujini, Mvumoni, Kibokoni, Mgogoni, Kichungwani, Wara, Tibirinzi, Mkoroshoni, Ndagoni, Michungwani, Ngw’ambwa, Ziwani, Ole, Kiuyu Minungwini, Mtambwe Kusini, Piki, Mtambwe Kaskazini, Pandani, Limbani, Jadida, Utaani, Selem, Finya, Wingwi, Kinyasini, Junguni, Gando, Chimba, Kojani, Chwale, Konde, Makangale, Tumbe Magharibi, Kiuyu Mbuyuni na Kata ya Majenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu hizi, tunaamini kuwa Kisiwa cha Pemba kinapata huduma nzuri ya mawasiliano kutoka kwa watoa huduma. Hata hivyo, kulingana na jiografia ya Pemba, baadhi ya maeneo yanaweza kupata shida ya kupata huduma kwa uhakika na mfuko utawasiliana na watoa huduma wakiwemo Zantel, Airtel, Tigo, Halotel na Vodacom ili kuona ni jinsi gani maeneo yote yenye changamoto hizi yanapata huduma nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, namwomba Mheshimiwa Mbunge kama ana majina ya vijiji hivyo vyenye shida ya mawasiliano, anikabidhi ili tuvifanyie kazi mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutupatia taarifa hizi na pia naomba nimhakikishie kwamba Wizara yangu itaendelea kufanyia kazi changamoto za Mawasiliano katika maeneo mbalimbali ikiwemo Pemba.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaamua kurudisha fedha zilizokusanywa na Halmashauri kupitia vyanzo vyake vya ndani ili ziweze kutekeleza majukumu yake na mikakati iliyopangwa kwa ufanisi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinakusanya mapato kupitia vyanzo vyake vya ndani kwa mujibu wa Sheria na Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kifungu cha 6, 7, 8 na 9. Ukusanyaji wa mapato hayo unasimamiwa na Sheria Ndogo zinazofafanua sheria mbalimbali za kodi zinazopaswa kukusanywa na mamlaka hizo.
Mheshimiwa Spika, mapato ya ndani yanayokusanywa na Halmashauri hutumika kwa shughuli za maendeleo na uendeshaji wa Halmashauri kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na Halmashauri zenyewe kwa kuainishwa katika mipango na bajeti zao za kila mwaka. Jukumu la Serikali Kuu ni kuidhinisha mapato na matumizi ya fedha hizo, kusimamia na kudhibiti matumizi ili kuhakikisha yanazingatia sheria na taratibu za fedha zilizowekwa na kuhakikisha zinatumika kwa madhumuni ya kuwaletea maendeleo wananchi katika maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kukusanya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwasilisha Serikali Kuu na kisha kuzirejesha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa haupo.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-

Miradi ya MIVARF ina malengo mapana ya kuwaendeleza wakulima wa vijiji kibiashara na kimtaji; na hatua za awali kama vile ujenzi wa barabara za vijijini umekamilika lakini pia masoko ya kuongeza thamani yapo katika hatua za kukamilika:-

Je, ni lini hatua za mwisho za kuwawezesha wananchi kimtaji zitaanza rasmi kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha inaunga mkono juhudi za wananchi kushiriki katika uchumi wa kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa mitaji na kuwapatia mafunzo stahiki. Mpango wa Kuwawezesha Wananchi Kimtaji umezingatia hatua zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa MIVARF, imevijengea uwezo wa kiutawala na kiutendaji Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya uzalishaji Tanzania Bara na Visiwani ili viweze kuratibu na kusimamia kwa ufanisi matumizi ya mitaji yatakayopatikana kupitia mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 3 Novemba, 2017, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Benki ya Maendelea ya Kilimo Tanzania (TADB) walisaini makubaliano ya uendeshaji wa Mfuko wa Dhamana. Kwa kupitia makubaliano hayo, Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 22 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ili kuanza utekelezaji kwa kushirikisha benki za biashara kufikisha huduma ya mikopo kwa makundi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania walishatangaza utaratibu wa namna benki mbalimbali za biashara zinavyoweza kushiriki katika Mfuko wa Udhamini ambapo Benki za CRDB, NMB, TPB na PBZ zilionesha nia. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilishakutana na benki zote zilizoonesha nia ya kushiriki katika Mfuko wa Dhamana na kufafanua jinsi Mfuko wa Udhamini unavyofanya kazi. Benki za NMB na TPB wameshakubaliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kushiriki katika utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hatua ya mwisho ya kuwawezesha wananchi kimtaji imeshafikiwa baina ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na Benki za NMB na TPB kama ilivyoelezwa hapo juu, napenda kutoa wito kwa Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya uwezeshaji Zanzibar kuwasiliana na Benki za NMB na TPB kwa upande wa Zanzibar ili kupata utaratibu wa kukopa fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-

Sheria ya NHIF inamtambua Mtumishi wa Umma ambaye amechangia kwa miaka 10 pale anapostaafu kuwa atahudumiwa na Mfuko yeye na mwenza wake hadi mwisho wa maisha yao:-

Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu kama huo kwa Viongozi wa Umma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wastaafu ni moja ya makundi ya wanachama ambayo yametajwa katika Sheria ya Mfuko. Kundi hili linapata huduma bila ya kuendelea kuchangia hadi mwisho wa maisha kwa sababu fedha za kugharamia kundi hili zinatokana na mapato yatokanayo na uwekezaji wa michango ya wanachama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa utaratibu wa fao la wastaafu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unalenga mwanachama ambaye ni Mtumishi wa Umma, amechangia katika Mfuko huu kwa kipindi kisichopungua miaka kumi katika utumishi wake. Hata hivyo, idadi ya wastaafu imeendelea kuongezeka na gharama za madai kuzidi kuwa kubwa kwa kuwa magonjwa ya kundi hili ni yale yenye gharama kubwa. Mfuko umefanya tathmini ya kugharamia kundi hili na kupendekeza kubadili kigezo cha muda wa kuchangia kabla ya kustaafu kutoka miaka 10 hadi miaka 15 ambapo mabadiliko yameanza kutumika kuanzia tarehe 1 Septemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa matibabu kwa Viongozi wa Umma waliostaafu unatekelezwa kwa kufuata miongozo ya utumishi wa umma iliyopo. Kwa upande wa Waheshimiwa Wabunge huduma za matibabu kwa mujibu wa Sheria ya Uendeshaji Bunge (The National Assembly (Administration) Act) ya mwaka 2008 ambapo kupitia Kanuni zake, Mheshimiwa Mbunge hupata huduma za matibabu kwa kipindi chake cha Ubunge. Aidha, Mfuko umekamilisha utaratibu unaowapa fursa wananchi mbalimbali kujiunga na Bima ya Afya kupitia mpango wa Vifurushi unaomwezesha mwananchi kujiunga kulingana na aina ya huduma na uwezo wa kuchangia.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH Aliuliza: -

Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kupambana na ugonjwa wa Malaria, bado ugonjwa huo unaendelea kuwaathiri wananchi wakiwemo watoto: -

Je, Serikali inaweza kutuambia hatua zilizofikiwa za kutokomeza ugonjwa huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitekeleza afua na kazi mbalimbali za kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini na kufanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria kutoka zaidi ya asilimia 40 mwanzoni mwa miaka ya 2000 mpaka asilimia 7.5 mwaka 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara inatekeleza Mpango Mkakati wa Malaria (National Malaria Strategic Plan 2021 – 2025) ambao umeweka malengo ya kupunguza kiwango cha Malaria kutoka asilimia 7.5 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025. Lengo mahususi ni kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria ifikapo 2030.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-

Vipo baadhi ya Vijiji vilivyoorodheshwa kwa ajili ya kufikiwa na miradi ya TASAF III Awamu ya Kwanza upande wa Zanzibar lakini bado havijafikiwa na mradi unaelekea mwisho:-

Je, Serikali inasemaje juu ya maeneo ambayo hayajafikiwa na Mradi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) naomba kujibu swali la Mhe. Maida Hammad Abdalla Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mradi wa TASAF haujafika mwisho na TASAF itafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba kaya zinazotambuliwa na kuandikishwa kwenye mpango ni zile kaya maskini sana.

Mheshimiwa Spika, kipindi cha pili cha utekelezaji wa Mradi wa TASAF kimeanza baada ya uzinduzi uliofanyika tarehe 17 Februari, 2020. Zoezi la utambuzi na uandikishaji wa kaya za walengwa katika Vijiji/Mitaa/Shehia 5,590 ambazo hazikufikiwa na mpango wakati wa kipindi cha kwanza kimeanza tarehe 19 Aprili mpaka tarehe 6 Mei, 2021 kwa mzunguko wa kwanza.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar jumla ya Shehia 304 tayari zinanufaika na mpango wa TASAF. Hata hivyo, jumla ya Shehia 157 ambazo hazikuwa kwenye mpango zimeshaandikishwa na ifikapo mwezi Julai, 2021 Shehia hizo zitaanza kunufaika na Mpango wa TASAF.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuwasisitiza viongozi katika Vijiji/Mitaa na Shehia zote kutoruhusu vitendo vya upendeleo na kuingiza kaya ambazo hazina vigezo kwenye Mpango. Maeneo ambayo yatabainika kuwa na kaya zisizo na vigezo, viongozi watachukuliwa hatua za kinidhamu kwani watakuwa wamehusika kufanya udanganyifu na kuingiza wasiohusika kwenye Mpango. Naomba kuwasilisha.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza: -

Je, lini Serikali italipa madeni ya fedha za kusafirishia mizigo kwa Askari Wastaafu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi limeshafanya uhakiki wa madeni ya kusafirisha mizigo ya askari polisi wastaafu 624. Uhakiki huo unaonesha kuwa jumla ya fedha zinazohitajika kwa ajili ya kusafirisha mizigo ya askari polisi wastaafu ni shilingi 806,067,788.02. Madai hayo yatalipwa baada ya Wizara ya Fedha kukamilisha taratibu za kuhamishia fedha hizo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kukamilika. Ninakushukuru sana. (Makofi)