Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maida Hamad Abdallah (14 total)

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria wale wote walioshiriki vitendo hivi, lakini pia kuna wengine ambao tayari sasa hivi wameshakamatwa, yaani watuhumiwa wameshakamatwa, je, Serikali itakubaliana nami kwamba baada ya kugundulika watu hawa waliofanya vitendo hivi kwa raia wa Zanzibar, Serikali iko tayari pamoja na hatua kali zitakazochukuliwa za kisheria, iko tayari kuwataka walipe fidia kwa wale wote waliowafanyiwa vitendo hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na uamuzi wa hatua gani za kuchukua baada ya kubainika na makosa ni maamuzi ya Mahakama. Kwa hiyo, pale ambapo Mahakama itaamua kulingana na sheria za nchi yetu basi nadhani ndivyo ambavyo inapaswa kutekelezwa. Siyo jukumu la Jeshi la Polisi kuamua hukumu gani ambayo watuhumiwa hawa wachukuliwe.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa wanavyojitahidi na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa kuhusiana na kadhia hii au suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza. Katika uhakiki unaondelea kuchukuliwa hadi tarehe aliyoitaja Mheshimiwa Waziri ni hasara kiasi gani Serikali imepata hadi kufikia tarehe hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; pamoja na mikakati ambayo Serikali imekuwa ikichukua kuhusiana na watumishi pamoja na maafisa waliohusika na swala hili. Serikali itambue kwamba kuna udhoroteshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokuwa inakwama pamoja na ukosefu wa madawa pamoja na ufinyu wa bajeti uliokuwa unajitokeza.
Je, Serikali inaweza kukubaliana na mimi kwamba pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa kwa watumishi kwamba iwepo adhabu ya kurudisha fedha ambazo walizipoteza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mara nyingi tumekuwa tukitoa takwimu mwezi hadi mwezi endapo watumishi hao hewa wasingeondolewa kwa mwezi husika wangeisababishia hasara kiasi gani? Niseme tu kwamba hadi sasa tumeshaondoa watumishi hewa 19,629 ambao endapo wangeendelea kubaki katika orodha ya malipo ya mshahara kwa mwezi husika mmoja wangeisababishia Serikali hasara ya shilingi 19,749,737,180, hiyo ni kama wangebaki kwa mwezi mmoja husika bila kuondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nitoe labda takwimu ya Halmashauri mojawapo. Ningeweza kutaja kwa ujumla wake maana yake tuliomba takwimu lakini sijapiga mahesabu kwa jumla kwa haraka. Nikianzia na Kinondoni tangu ambavyo wameondoa watumishi hewa waliondoa watumishi hewa 107 na kwa kiasi cha fedha ambacho walilipwa watumishi hao ni shilingi bilioni 1.279. Nikija kuchukua kwa Halmashauri ya Kishapu watumishi 73 wamelipwa shilingi milioni 543. Kwa hiyo, ambacho naweza kusema ni kwamba endapo wangeendelea kubaki kwa kweli ni gharama kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili ni mikakati gani ambayo Serikali inachukua kuhakikisha kwamba pamoja na watumishi hawa hewa kuondolewa basi wanarejesha fedha. Nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kama nilivyotoa takwimu kwa wale ambao tayari mashauri yao yamefikishwa mahakamani wametakiwa pia aidha kulipa faini lakini pamoja kurejesha fedha na endapo watashindwa kufanya vyote viwili basi watapata kifungo jela. Na kesi mbalimbali zimekuwa zikiendelea; tayari kesi 38 zilishamalizika mahakamani, tayari kuna majalada mengine ya uchunguzi 126 yanaendelea, lakini vilevile bado tunaendelea kuhakikisha kwamba tunakamilisha na wote walioshiriki basi wanafikishwa katika vyombo vya kisheria.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninalo swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hamasa pia mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya kuhamasisha uendelezaji wa zao hili, lakini bado hadi sasa kipo kiwanda kimoja tu kinachopokea mazao haya ambapo kipo Kisiwani Pemba. Je, Serikali inawaambia nini wananchi katika uendelezwaji wa viwanda hasa katika mkakati huu wa uendelezaji wa viwanda nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba kwa sasa bado kuna changamoto kubwa ya kuwa na viwanda vya usindikaji kwa ajili ya mazao ya mdalasini na mchaichai na kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, kwa sasa tuna kiwanda kimoja kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuongeza thamani katika mazao haya, ni lazima tuchukue hatua za makusudi kuhakikisha kwamba kunakuwa na viwanda vya kutosha. Kwa sasa sambamba na kutafuta fursa za kujenga viwanda, Serikali bado inatilia mkazo zaidi kuongeza uzalishaji kwa sababu uzalishaji uliopo wa sasa ni mdogo sana kuweza kuvutia uwekezaji kwenye viwanda. Kwa hiyo, rai yetu kwa Waheshimiwa Wabunge wanaotoka maeneo yale yanayolima mchaichai na mdalasini waendelee kuhamasisha wakulima walime zaidi ili tuweze kuwa na uzalishaji wa kutosha wa kuweza kuvutia viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba mdalasini na mchaichai ni mazao ambayo wengi wetu hatujui faida zake, lakini ukweli wa mambo ni kwamba ukiacha faida ya mazao haya kwa burudani kama kinywaji lakini vilevile inatibu magonjwa mengi. Hata hivyo, nilivyokuwa nasilikiza swali lile Namba 21 la Mheshimiwa Khatib Said Haji hata zile changamoto alizoelezea kwa ufahamu wangu ni kwamba hata mdalasini na mchaichai navyo husaidia kuondoa changamoto hizo.
MHE. MAIDA H. ABDALLAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa miradi mingi ya maendeleo ngazi ya Halmashauri imekuwa ikisuasua na ikikwama kutokana na ucheleweshwaji wa fedha kutoka Hazina. Je, Serikali inatoa kauli gani katika ukamilishwaji wa miradi ya maendeleo iliyopitishwa na bajeti ya Serikali mwaka 2015/2016 na 2016/ 2017?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kusuasua kwa miradi; huku kunategemea na eneo na mradi na Halmashauri husika. Ziko Halmashauri ambazo tumekuwa tukizifuatilia na kuwashauri kuhusu matumizi ya fedha kwa wakati. Wakati mwingine wanakuwa na fedha kwenye akaunti lakini wakati mwingine watekelezaji kule kwenye mradi wanakuwa hawajui kama fedha zimekuja. Kwa hiyo matatizo mengine ni ya kimawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusisitiza, Halmashauri mara zinapopata fedha kutoka Serikali Kuu, zijipange kwa haraka na kwa wakati kutumia fedha hizo kwa ajili ya wananchi, wasiziache kwenye akaunti. Pale ambapo kuna ucheleweshaji wa aina yoyote wafanye mawasiliano haraka na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kusudi tuweze kufuatilia kwa wenzetu tuweze kusuluhisha suala hilo mara moja.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Hata hivyo ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mheshimiwa Waziri kujibu swali hili na kunihakikishia/kukiri kwamba yapo baadhi ya maeneo Kisiwani Pemba ambayo yanapata shida ya mawasiliano, hata hivyo ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo la mawasiliano Kisiwani Pemba katika maeneo ya Makangale, Kipange, Tumbe Kiungoni, Mtambwe, Gando na maeneo mengine yaliyopo Kaskazini na Kusini Pemba na kupelekea wananchi wa mikoa hiyo kupata usumbufu wa mawasiliano hasa katika kipindi cha dharura…
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali kupitia Wizara hii inawaambia nini tena wananchi kuhusu kutatua changamoto hii ambayo imekuwa ikiwaletea shida muda mrefu na wakati mwingine wananchi hulazima kupanda kwenye miti mirefu kutafuta mawasiliano? (Makofi)
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuongozana na wataalamu wake kwenda Pemba kutafuta maeneo na vijiji mbalimbali kuweka minara ili kuwatatulia matatizo wananchi wa Pemba? (Makofi
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nimeeleza kwamba kuna uwezekano pamoja na Kata nyingi nilizozitaja kwamba zina mawasiliano, kuna sehemu nyingine baadhi ya vijiji havina mawasiliano kutokana na jiografia ya Pemba ikiwemo Matangale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge aniorodheshee majina ya vijiji vyote ambavyo mpaka sasa hivi havipati mawasiliano ili tuwatume watu wetu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote watembelee sehemu ile ili kuweza kuleta mawasiliano kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lengo la Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ya nchi yetu wananchi wanawasiliana. Napenda nichukue nafasi hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba mpaka sasa hivi kwa takwimu tulizonazo kutoka Mfuko wa Mawasiliano wa Wote Watanzania asilimia 94 wanawasiliana. Kwa hiyo, asilimia sita iliyobakia inawezekana ni baadhi ya vijiji ambavyo amezungumza Mheshimiwa Mbunge; na ninamkaribisha Ofisini aje atuletee majina ya vijiji ambavyo hawawasiliani ili tuweze kutatua changamoto hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kwa ruhusa yako, mimi niko tayari kuongozana naye mpaka Pemba ili tuweze kwenda kuangalia hizo sehemu ambazo zina changamoto. Ahsante. (Makofi)
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Je, Serikali inaweza kutuambia ni kwa nini wazee kama baba na mama wa Mbunge hawakuwekwa miongoni mwa wategemezi katika bima ya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taratibu wa Sheria ya Bima ya Afya, inatambua yule mwenye kadi, mwenza wake na watoto wake, wategemezi wengine; baba, mama, walezi, wale wako nje ya utaratibu huo. Kwa hiyo, niendelee kuwasisitiza Waheshimiwa Wabunge kwamba changamoto hii na sisi tumeiona, tunaendelea kuitafakari kuangalia jinsi bora zaidi ya kuweza kulifanyia kazi ili hawa nao waweze kunufaika.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa kama alivyokwishasema Mheshimiwa Waziri kwamba mapato ya Halmashauri ndiyo vyanzo vikuu vinavyoendeleza maendeleo katika Halmashauri. Kwa kuwa makusanyo yanayotokana na mapato na kodi ya ardhi na majengo urejeshaji wake kutoka katika mamlaka husika umekuwa ukisuasua huku Halmashauri zikiwa zimejipangia majukumu mbalimbali na hivyo utekelezaji wake kuchelewa. Je, Serikali haioni kwamba mtindo huu unaathiri utekelezaji wa haraka wa vipaumbele ilivyojipangia Halmashauri? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ndani ya Halmashauri zetu kwa mujibu wa sheria wametakiwa kutekeleza agizo la kuwawezesha wanawake na vijana kwa kutenga asilimia 10 ili ziwaendeleze kiuchumi. Kwa kuwa changamoto hii imekuwa ikiathiri sana agizo hili, je, Serikali sasa ipo tayari kuleta waraka Bungeni wa mapendekezo ya kwamba mapato yanatokana na kodi za ardhi na majengo baada ya makusanyo zibaki kwenye Halmashauri husika? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kodi za ardhi na majengo zinakusanywa kwa sehemu, kwa mfano, kodi ya ardhi inakusanywa na kupelekwa Wizara ya Ardhi na baadaye kupelekwa Hazina na hupaswa kurejeshwa kwenye Halmashauri zetu asilimia 30. Urejeshaji huu haujawa mzuri kwa muda sasa, lakini katika bajeti ya mwaka huu tunaokwenda nao katika makusanyo yaliyopelekwa karibu shilingi bilioni 29 angalau kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kimerejeshwa, kwa hiyo, utaona tunafanya hivyo.
Hata hivyo, wakati wa hotuba yangu ya bajeti nilisema tunajaribu kuangalia na kupitia sheria hizi ili tuweze ku-harmonize ili fedha ambazo zinakusanywa zirejeshwe kwa utaratibu mzuri zaidi. Kwa hiyo, nachotaka kuahidi tu ni kwamba kwa kodi hizi zote mbili, ya ardhi na majengo, Waziri wa Fedha atakaposoma Sheria ya Fedha kwa mwaka 2017/2018 kutakuwa kuna mabadiliko ambayo yatazingatia maoni mengi ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati nawasilisha bajeti yangu lakini katika mazungumzo mbalimbali kupitia maswali ya Wahemishiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na asilimia kumi ambayo inatolewa kama mikopo kwa vijana na akina mama, tutajaribu kuangalia kama tunaweza tukaanzisha sheria mahsusi kwa ajili ya jambo hili kwa sababu kwa sasa lilikuwa limewekwa kisera tu lakini hakukuwa na sheria inayo- enforce. Hata hivyo na lenyewe tumeliweka katika utaratibu endapo tutapata fursa ya kuleta mabadiliko ya sheria mbalimbali basi tutaliweka na maandalizi yake sisi kama Wizara tayari tumekwishayafanya.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa, niipongeze Serikali kwa juhudi zake katika kuwaendeleza wananchi kiuchumi na niwapongeze pia kwa kutoa shilingi bilioni 22 kwa ajili ya kuendeleza SACCOS hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Serikali lakini pia ninayo maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri lakini niseme kwamba pamoja na Serikali kuingia mikataba na benki na kufikia uamuzi wa kusaini kwa ajili ya kuwaendeleza wakulima hawa kwa kuwapatia mikopo lakini bado benki za Zanzibar zimekuwa zikisuasua kuhusiana na suala la mikopo hiyo. Je, Serikali iko tayari kuzisimamia benki hizi ili kuweza kufikia utekelezaji ili wananchi hawa waweze kupata mikopo hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nataka kusisitiza tu Serikali kwamba SACCOS zetu mara nyingi hazina elimu za kuendeleza biashara zao kimitaji na kimasoko. Kwa hiyo, naiomba Serikali kufika Zanzibar kuwapa elimu wananchi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali la kwanza, ni kweli Benki ya Kilimo (TADB) ilikwishaingia makubaliano na benki nilizoziainisha pale awali ikiwemo Benki ya Watu ya Zanzibar. Kwa hiyo, rai yangu ni kuziomba taasisi za fedha kwa upande wa Tanzania Visiwani kwa maana ya Zanzibar kuichangamkia fursa hii ili wakulima wengi zaidi wa Zanzibar waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na benki hii kwa sababu ipo kwa ajili yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi tu niseme kwamba kwa upande wa Zanzibar tunaendelea pia na hatua za kuviwezesha vikundi hivi. Hivi sasa tayari vikundi kwa maana ya SACCOS 231 zimeshafikiwa na tayari zaidi ya shilingi bilioni 24 ziko katika mzunguko kwa ajili ya ukopeshaji. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuziomba na kuzitaka benki za Zanzibar kuchangamkia fursa hii ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili kuhusu elimu, katika Programu hii ya MIVARF, kabla ya kuanza utoaji wa fedha na uwezeshaji iko package ambayo inahusisha masuala ya mafunzo hasa nidhamu ya matumizi ya fedha na utunzaji wa fedha. Kwa hiyo, ombi kuhusu suala la elimu ni kwamba ni sehemu ya mradi huu na imekuwa ikifanyika na ninavyozungumza hivi sasa tayari vikundi 57 vya uzalishaji mali kule Zanzibar wameshapewa elimu ya kutosha juu ya matumizi bora ya fedha na namna ya kukopa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu niongeze majibu ya ziada kwenye swali zuri sana la Mheshimiwa Maida na hasa faida ambazo wanaweza wakazipata wenzetu wa upande wa pili wa Muungano yaani kule Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichokifanya mpaka sasa ni kuhakikisha kwamba Mradi huu wa MIVARF unakuwa ni
kielelezo kizuri cha Muungano wetu katika nchi yetu. Kwa sababu inaonekana upande wa pili wa wenzetu bado mikopo hii hawajaifahamu vizuri na bado hawajanufaika nayo, naomba niliahidi Bunge lako Tukufu, tutafanya ushirikiano na mawasiliano ya karibu na Waziri mwenye dhamana ya Vijana na Uwezeshaji kule Zanzibar ajue uwepo wa mikopo hii ili aweze kutusaidia kusimamia na kuhakikisha kwamba wenzetu wa upande wa pili wa Zanzibar na wao wanafaidika na wanajua uwepo wa mikopo hii kupitia benki yao ambayo itawahudumia kupitia Mpango wa MIVARF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kuweza kuendelea kuwahudumia wananchi wake wawapo kazini na wale ambao wamestaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba kuna mabadiliko ya utaratibu wa uchangiaji kutoka miaka 10 hadi
15 lakini bado baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiendelea kuchangia miaka 20 na kuendelea lakini wazazi wao hawajatambuliwa kuwa wafaidika wa mfuko huo na ukiangalia wamechangia fedha nyingi na muda wanaopata matatizo ni mdogo. Vilevile kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hawana watoto, mume wala mke. Je, Serikali inaweka utaratibu gani wa kisheria kuweza kuwatambua Waheshimiwa Wabunge katika kufaidika na Mfuko huo watakapokuwa wamestaafu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Maida, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, amegusia kuhusiana na Wabunge ambao wamekua wanachangia Mfuko huu na kwa nini Serikali isifanye mabadiliko ya sheria. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge ndiyo tunatunga sheria na hii sheria ambayo inahusu mafao yetu ni sisi wenyewe tunahusika. Pili, ni sisi wenyewe Wabunge ambao tunatengeneza Kanuni zetu za Uendeshaji wa Bunge letu. Kwa hiyo, hili suala wala siyo suala la Serikali ni la Bunge lenyewe kukaa na kuamua kupitia Kanuni zao na Tume ya Utumishi wa Bunge kuweka utaratibu wa mafao na haki stahiki katika masuala ya bima ya afya kwa Waheshimiwa Wabunge.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeza sana Serikali kwa kuweza kuweka mkakati madhubuti…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali.

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa mapambano dhidi ya malaria nchini Tanzania yalianza toka mwaka 1890; na wengi tunafahamu kwamba suala la malaria linatokana na mbu; kwa vile tunacho kiwanda kinachozalisha dawa ya viuadudu ambayo inamaliza kabisa mazalia ya mbu: Je, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kuzitaka Halmashauri kutenga bajeti katika bajeti zao ili kuweza kununua dawa hizi kila Halmashauri iweze kudhibiti malaria kupitia kila Halmashauri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wenzetu toka nje ya nchi wanakithamini sana na kuona umuhimu wa kiwanda hiki na dawa hii inayozalishwa Tanzania: Je, Serikali kupitia Wizara hii inatoa elimu gani kwa wananchi kuhusiana na suala la dawa zinazozalishwa na kiwanda hiki kilichoko Kibaha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maida kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni namna gani tutakitumia kiwanda ambacho kiko Kibaha kuweza kushirikiana nacho kumaliza tatizo la malaria? Hili tunalichukua. Vile vile ndani ya swali la kwanza ameuliza Halmashauri itafanyaje? Tutaenda kushirikiana na TAMISEMI na hasa kwa sababu kuna tozo ambazo zimekuwa zikitozwa kule Halmashauri zinazotokana na masuala ya afya, fedha hizo zinaweza zikatumika asilimia fulani, vile vile kusaidia kugharamia eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili linaonekana linahusu elimu. Nafikiri kwenye strategic ya mwaka 2021 – 2025 kwa kweli tutakwenda kuwekeza kwenye eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelishauri. Tunachukua ushauri wake na tutaenda kuufanyia kazi kwa nguvu zote kabisa.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo linalowaathiri wananchi wa Nanguji na Kiwani linafanana kabisa na tatizo linalowaathiri wakazi wa Kijiji cha Kojani. Na kwa kuwa, wananchi wa Kijiji cha Kojani wamekuwa wakilalamika muda mrefu kuhusiana na suala la maji ya bahari kuwaathiri katika makazi yao ya kudumu. Je, Serikali ina mpango gani au inaweza kuweka mkakati gani ili kuweka ukuta, pamoja na alama, lakini ili kunusuru makazi ya wananchi wa Kijiji cha Kojani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kojani ni ndani ya jimbo lang na Kojani ni sehemu yangu nitashawishi Serikali na kuandika miradi tofauti kwa ajili ya kuhami kisiwa hicho cha Kojani. (Makofi)
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa utekelezaji wa TASAF III, Awamu ya Kwanza wapo wafaidika 1,000 na zaidi wanaotoka katika Shehia 78 za Pemba ambao walikuwa katika utaratibu wa malipo na majina yao yaliachwa. Je, Serikali inasema nini kuhusu kulipwa fedha zao wafaidika hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wananchi hawa maskini waliingia katika mikopo mbalimbali kwa kutegemea kwamba fedha wanazoendelea kuzipata zinawasaidia katika kujikimu kimaisha. Je, Serikali inaweza kututhibitishia kwamba ni bajeti ipi itawalipa fedha hizi kwa sababu mradi wa TASAF III, Awamu ya Kwanza umeisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maida, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mwaka jana mwezi Juni ulifanyika uhakiki wa kaya zote ambazo zinapokea fedha za TASAF. Kaya zile ambazo hazikutokea kwenye uhakiki ziliondolewa kwenye mpango mpaka pale watakapokuja tena kuhakikiwa ili malipo yao yaweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa kesi hii ya Pemba kwenye Shehia 78 kuna walengwa 1,200 ambao hawakujitokeza kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki na malipo yao yalisitishwa. Hata hivyo, ilipofika uhakiki wa awamu ya pili uliofanyika mwezi Desemba, 2020 walengwa 300 walijitokeza na walengwa 900 bado hawajajitokeza kufanyiwa uhakiki.

Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pale tu walengwa hawa watakapojitokeza kufanyiwa uhakiki basi malipo yao yatarejeshwa na wataendelea kupokea fedha hizi za TASAF.

Mheshimiwa Spika, swali lake la nyongeza la pili ameuliza ni nini Serikali inafanya, kama nilivyojibu kwenye swali lake la nyongeza la kwanza ni pale tu hawa 900 watajitokeza kufanywa uhakiki basi malipo yao yatarejeshwa na wataendelea kuwepo kwenye mpango.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muda mrefu sasa wastaafu hawa tokea waliostaafu kipindi cha miaka ya 2020 hadi 2021. Ni bajeti gani ambayo imepanga fedha hizo kupewa wastaafu hawa. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kama nilivyosema, wastaafu jumla walikuwa 624, ili kulipa madeni haya lazima kufanaya uhakiki. Kama nilivyosema, tumeshahahikiki tayari wastaafu 579 ambao ndiyo jumla ya fedha hizo ambazo zimepangwa katika mwaka wa fedha kulipwa, ambazo ni shilingi 806,067,788.02. Hao wengine waliobakia nao tunaendelea na uhakiki ili kujiridhisha kwamba tunalipa stahiki zao bila kumpunja mstaafu yeyote katika Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali inahakikisha itatenga hizi fedha ili kuwalipa baada ya uhakiki huu kukamilika. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MAIDA H. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri ya Serikali inayoongozwa na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali ipo tayari kuongeza bajeti ya JKT ili kuwezesha vijana wengi zaidi kuchukuliwa kujiunga na JKT? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali haioni kwamba mpango huu utawezesha vijana walio wengi kujifunza katika fani tofauti kwa masuala ya ulinzi karibu na jeshi na maeneo mengine? Pia, kuongeza ajira ikiwa ni njia mojawapo ya kukuza uchumi wa Taifa letu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maida, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la bajeti kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, sasa tumeunda timu maalum ya tathmini ili kuangalia uwezo wa makambi haya katika kuchukua vijana wengi zaidi na hili litakwenda sambamba na kuangalia uwezekano wa bajeti kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli kwamba mpango wa kuongeza nafasi za vijana kujiunga na jeshi ni mpango ambao unaweza kuleta matokeo makubwa sana kwenye kuwajengea uwezo hawa vijana, lakini kama nilivyosema, acha tumalize hii tathmini itakayotupa mwelekeo mzuri wa namna ambavyo tutachukua idadi kubwa zaidi ya vijana na hapo Serikali itazingatia vilevile ongezeko la bajeti na kadhalika. (Makofi)