Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri (1 total)

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi. Swali langu, je, kwa tafiti ambazo zimefanywa nchi nyingi sana, ikiwemo kwa nafasi kubwa nchi za Kiarabu, sigara ina madhara makubwa, mara dufu kuliko hii Shisha na kila siku tunasema ajira, ajira. Biashara ya Shisha ilikuwa inaajiri vijana wengi sana na kweli wamepata matatizo tangu hili zuio.
Swali langu kwa Serikali; je, mlifanya utafiti wa kutosha wa kuona kwamba hii Shisha ina madhara makubwa kuliko sigara? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mariam kwa kutaka kujua kuhusu utafiti wa jambo hili. Nimhakikishie tu kwamba jambo hili lilifanyiwa utafiti na Wizara ya Afya na hivi vitu ambavyo vina vilevi, ubaya wake ni kwamba vijana wetu hawavitumii peke yake, wanachanganya na vitu vingine, kwa hiyo, wanaongeza makali zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira, nimhakikishie Mheshimiwa Mariam kwamba vijana bado wana fursa nyingi sana na nitolee mfano wa kwake yeye mwenyewe, ni mmoja wa vijana wanaofanya vizuri sana kwenye kilimo na yeye ni shahidi na amefanikiwa sana; ni mmoja wa Waheshimiwa Wabunge vijana waliofanikiwa sana kwenye kilimo. Kwa maana hiyo, vijana wengine wanaweza wakaiga mfano ule, wakalima mazao ya biashara. Mheshimiwa Mariam analima ufuta, wao nawakaribisha walime alizeti ama mazao mengine yanayostawi katika mikoa yao ili waweze kufanya biashara iliyo halali isidhuru maisha ya watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira ya kudumu, ndiyo maana Mheshimiwa Rais ana mpango wa muda mrefu wa kukuza uchumi kwa kuhakikisha kwamba fedha zote zinatumika vizuri ili kuweza kutengeneza uchumi wa viwanda, uchumi unaojitegemea, uchumi unaotengeneza ajira nyingi ambazo zitakuwa zinaingiza kipato halali kwa vijana na afya za Watanzania.