Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Mariamu Nassoro Kisangi (1 total)

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, mvua zimenyesha pasipo kueleweka, zimekwenda kuua mazao mengi sana katika maeneo mbalimbali, hali ambayo inaonesha kabisa kuna viashiria vya njaa huo mbele tunapokwenda. Je, Serikali yetu imejipanga vipi katika kukabiliana na janga kubwa la njaa ambalo linaweza kuja baadaye kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kisangi, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kupitia swali hili kwanza naomba nitoe pole kwa wananchi wote ambao wamekumbwa na matatizo makubwa ya mafuriko. Mafuriko haya yameleta madhara makubwa ya vifo, uharibifu wa mali, lakini pia mashamba yetu yote yamesombwa na maji. Nilisema hapa nilipokuwa nahitimisha hoja yangu wiki iliyopita kwa kuwatahadharisha Watanzania baada ya kuwa tumepata taarifa kutoka chombo chetu cha hali ya hewa kwamba mvua hizi bado zinaendelea. Natoa pole kwa watu wa Kilosa, natoa pole kwa watu wa Moshi Vijijini na Rombo ambako pia ndugu zetu wengi wamepoteza maisha na madhara hayo ambayo nimeyataja.
Mheshimiwa Spika, Serikali imejipanga kuwahudumia Watanzania wote wanaopata madhara na mpango huu upo kwenye Ofisi yangu kupitia Kitengo cha Maafa. Tunaendelea kufanya tathmini na tathmini hii inafanywa kwanza na Halmashauri zote zote za Wilaya ambazo ndiyo zimeunda Kamati ya Maafa kwenye maeneo yao. Wakishafanya tathmini, Mkoa unafanya mapitio na mahitaji yao halafu wanatuletea ofisini kwetu; nasi tunapeleka misaada kadiri walivyoomba kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tuna hifadhi ya chakula, yaani tunacho chakula cha kutosha cha kupeleka kwenye maeneo hayo na tayari tumeshaanza kupeleka chakula kwenye maeneo yote yaliyopata maafa. Tumejiimarisha tena kwa ajili ya maafa haya yanapoweza kutokea hapo baadaye na kutumia msimu huu wa kilimo kwa maeneo ambayo hayajapata madhara.
Nataka nitoe wito kwamba tulime sana, tupate chakula kingi tuweze kutunisha hifadhi yetu ya chakula ili pia tunapopata tatizo la mahitaji ya chakula, basi chakula hicho tuweze kukipeleka maeneo yote yenye maafa.
Mheshimiwa Spika, pia kitengo hiki sasa tunakiboresha, tunaanza mazungumzo ndani ya Serikali kuifanya kuwa agency ambayo itakuwa inaratibu shughuli zote za maafa popote nchini, ambapo tutakuwa tunatengea fedha ziweze kutafuta maturubai au vibanda vya kujihifadhi kwa muda mfupi lakini pia kununua vyakula, madawa na mahitaji mengine ili yanapotokea tu maafa kama haya, basi kitengo chetu kiende mara moja.
Kwa sasa tumejiimarisha vizuri, maeneo yote yenye maafa tumeshayapitia na wataalam wetu wapo huko kwenye maafa ili kunusuru maisha ya Watanzania wenzetu ambao sasa wamepata mahangaiko kutokana na mvua nyingi ambazo zimenyesha.
Mheshimiwa Spika, pia tahadhari kwa wale wote ambao wako kwenye mabonde, narudia tena, nataka niwasihi Watanzania wote ambao wako kwenye maeneo hatarishi wapishe maeneo hayo, watafute maeneo mazuri. Viongozi wa Serikali za Vijiji, Kata na Wilaya wawasaidie Watanzania hao kuwapeleka maeneo sahihi ili waweze kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza itakapotokeza mvua nyingi kunyesha tena ambazo zinaendelea kwa sasa.