Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Munira Mustafa Khatib (8 total)

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko mengi ya wananchi kutopata huduma nzuri katika hospitali za umma, vituo vya afya pamoja na zahanati:-
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kusimamia Madaktari na Wahudumu wa Afya ili kuweza kuwapatia wananchi huduma bora na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatib, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
kuhusu huduma zinazotolewa na vituo vya huduma za afya vya ngazi zote hapa nchini. Katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinazotolewa zina ubora unaotakiwa na zinawafikia wananchi…
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge upande wa Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba utulivu tafadhali, tumsikilize Naibu Waziri.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo malalamiko ya wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na vituo vya huduma za afya vya ngazi zote hapa nchini. Katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinazotolewa zina ubora unaotakiwa na zinawafikia wananchi, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeweka utaratibu wa kusimamia utoaji wa huduma hizo. Utaratibu huu ni pamoja ni:-
(1) Kuwepo kwa Mabaraza ya Taaluma yenye nguvu za kisheria ambayo husimamia wataalam katika taaluma husika. Kila taaluma ya afya, ikiwemo ya udaktari ina Baraza linalosimamia wanataaluma wake;
(2) Kuwepo kwa miongozo inayosimamia utoaji wa huduma za afya zenye ubora unaotakiwa; na
(3) Kuwepo kwa uongozi katika kila kituo cha kutolea huduma za afya ambao husimamia utoaji wa huduma katika kituo husika kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imebaini udhaifu wa utekelezaji wa utaratibu uliowekwa. Hii imedhihirishwa na ukweli kwamba hata katika vituo vyenye dawa za kutosha na watumishi wa kutosha pamoja na vitendea kazi vingine bado malalamiko yamekuwepo. Tofauti kati ya halmashauri zinazofanya vizuri na zile zinazofanya vibaya ni uongozi madhubuti katika ngazi mbalimbali za usimamizi. Kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara inaendelea kuboresha utekelezaji wa taratibu zote zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kuboresha usimamizi wa utoaji wa huduma bora za afya katika vituo vyote nchini.
MHE. SUBIRA K. MGALU (K.n.y. MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB) aliuliza:-
Kumekuwa na ongezeko kubwa la vijana wanaomaliza kidato cha nne kutokana na ongezeko la shule za kata nchini, vijana hawa wamekuwa wakizagaa mitaani bila kujua la kufanya na matokeo yake kujiingiza kwenye vitendo hatarishi kama dawa za kulevya, uvutaji wa bangi, wizi, udokozi na kadhalika.
Je, ni kwa nini Serikali isianzishe mpango maalum wa kuwapeleka Jeshi la Kujenga Taifa vijana wanaomaliza kidato cha nne nchini ili wakimaliza mafunzo waweze kujiajiri wenyewe pamoja na kuwa wazalendo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatib kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu uliopo hivi sasa, wa vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa ni ule wa vijana kujitolea ambao ni wenye elimu kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu na ule wa mujibu wa sheria ambao ni kwa vijana waliomaliza kidato cha sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango maalum anaoushauri Mheshimiwa Mbunge wa kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha nne kwa sasa hautawezekana kutokana na uwezo mdogo wa kifedha. Hivi sasa uwezo wa JKT kuchukua vijana wa kujitolea ni ni kati ya vijana 5,000 hadi vijana 7,000 kwa mwaka kutokana na bajeti inayotolewa. Hata hivyo, ushauri huu ni mzuri na Serikali itafanya maandalizi ya kambi nyingi zaidi na kutenga bajeti kubwa zaidi kwa ajili ya uendeshaji kadri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu.
MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha vituo maalum vya kulelea watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kuliko ilivyo sasa ambapo huchanganywa na watoto wenye matatizo mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustafa Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum, kwa niaba wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati wanayo mahitaji maalum ukilinganisha na watoto wengine. Matatizo yanayoambatana na kuzaliwa kabla ya wakati au uzito pungufu yaani chini ya kilo 2.5 yanachangia kwa asilimia ishirini na tano ya vifo vya watoto wachanga nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwamba Serikali wameshindwa kuweka sehemu yao ila imeonekana kuwa ni msaada kuwafanya waweze kupona na kukua katika uhalisia na mazingira bora kama watapewa huduma na wazazi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ilianzisha huduma ya matunzo ya mtoto mchanga aliyezaliwa kabla ya wakati kwa kumbeba kifuani ngozi-kwa-ngozi yaani Kangaroo method na huduma hii ilianzishwa katika hospitali zote za mikoa na baadhi ya hospitali za wilaya na hivi sasa tuna vituo vipatavyo sabini vinavyota huduma hii muhimu hapa nchini. Wizara inaendelea na kazi hii ya kuanzisha vituo hivi kwa kasi zaidi na tunategemea kuanzisha vituo vingine zaidi katika hospitali za wilaya nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017, kwa ufadhili wa fedha za RMNCH Trust Fund, Wizara imenunua vifaa mbalimbali ili kurahisisha uanzishaji wa huduma hii. Vifaa hivyo ni pamoja na vitanda maalum vya kutolea huduma hii, vikombe vidogo vya kulishia watoto hawa ambao mara nyingi hushindwa kunyonya ipasavyo, vipima joto maalum (low reading thermometers), mizani ya kupima uzito na watoto wachanga na mablanketi.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufuta tozo na gharama za vifaa vya kujifungulia na upasuaji kama ilivyofuta za matibabu ya wazee na wagonjwa wa kisukari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Malaam kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Afya ya mwaka 2007 inaeleza kuwa huduma za kina mama wajawazito katika vituo vya ngazi zote zinapaswa kutolewa bila malipo. Serikali haijawahi kuweka tozo na gharama za vifaa vya kujifungulia na wala vya upasuaji. Huduma hizo zinatolewa katika ngazi zote katika vituo vya umma vya kutolea huduma kwa gharama za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha sera hii inatekelezwa kwa vitendo, Wizara inahakikisha akina mama wanakuwa na vifaa muhimu vya kujifungulia, ambapo vifuko maalum vyenye vifaa vya kujifungulia (delivery packs) kwa wanawake 500,000 vitasambazwa nchi nzima kulingana na uhitaji. Kwa wastani nchini Tanzania jumla ya akina mama 1,900,000 wanajifungua kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa tusaidiane kusimamia utekelezaji wa sera tulizokubaliana katika maeneo yetu kwa kuhakikisha huduma hizi za akina mama zinapatikana kwa gharama za Serikali ili azma ya Serikali ya kuhakikisha akina mama wajawazito wanapata huduma nzuri na lengo la kupunguza vifo vya Mama na watoto hapa nchini lifikiwe. (Makofi)
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU aliuza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuratibu na kuwatambua wasichana wanaokatiza masomo kwa sababu ya ujauzito na wale walionyimwa fursa ya kuendelea na masomo na kuwaandalia mpango maalum wa kujiendeleza kimasomo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inao utaratibu wa kuwatambua wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali. Takwimu hutolewa kupitia kijitabu kinachojulikana kwa jina la National Basic Education Statistics in Tanzania (BEST). Kijitabu hicho hutoa takwimu za kielimu ikiwa ni pamoja na idadi ya wanafunzi, walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima hutoa fursa za kielimu kwa makundi tofauti ya walengwa wakiwemo waliokosa nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari kwa sababu mbalimbali kama ujauzito, utoro na utovu wa nidhamu. Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima huendesha Mpango wa Elimu ya Sekondari kwa ujifunzaji huria katika vituo vilivyopo katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Katika mwaka 2017, walengwa 10,420 wamesajiliwa kati yao 7,074 ni wanawake na 4,346 ni wanaume. Aidha, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima huandaa na kuendesha Programu ya Elimu Mbadala kwa Vijana na Watu Wazima kulingana na mahitaji yao ambapo hutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kama vile ujasiriamali, stadi za maisha, ufundi wa awali na Programu za Kisomo cha Kujiendeleza kwa Watu Wazima ili waweze kuendesha maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wanaoacha shule za msingi, hupata fursa ya kuendelea na masomo kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA). Pia Serikali ina mpango wa kuimarisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) ili viweze kuongeza wigo wa kudahili wanafunzi kwa nyanja mbalimbali za mafunzo na hivyo kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi wanaoacha masomo kwenye mfumo rasmi wa elimu.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI (K.n.y. MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB) aliuliza:-

Baadhi ya Kampuni binafsi zimekuwa zikiwafanyisha kazi Watumishi wao zaidi ya muda wa saa za kazi, kutowapa chakula na kuwalipa kima kidogo cha mshahara:-

Je, Serikali ina kauli gani kuhusu suala hilo linalowakandamiza Wafanyakazi hao ambao wengi wao ni vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inasimamia ipasavyo mahusiano ya kikazi sehemu zote za kazi ikiwa ni pamoja na kampuni binafsi. Kupitia Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004, Serikali inasimamia viwango stahiki vya kazi ikiwa ni pamoja na masaa ya kazi, likizo mshahara na kazi staha kwa wafanyakazi wa sekta zote.

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa Mwajiri kutii matakwa ya sheria kwa kumlipa mfanyakazi wake mshahara na maslahi stahiki. Hivyo, mwajiri anayekiuka matakwa ya sheria hii anastahili adhabu.

Aidha, katika kuimarisha uwajibikaji upande wa waajiri, mwaka 2016, Bunge letu Tukufu lilifanya marekebisho katika Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya Mwaka 2004 na kuimarisha mfumo wa kaguzi za kazi mahali pa kazi kwa kuruhusu kutoa adhabu za papo kwa papo (compounding of offences) kwa waajiri wanaokiuka matakwa ya sheria, ikiwa ni pamoja na kutowalipa wafanyakazi malipo ya ziada kwa saa za ziada walizofanya kazi na kulipa mshahara chini ya kiwango cha chini cha mshahara.

Mheshimiwa Spika, Ofisi yangu itaendelea kusimamia sheria na kuimarisha mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi na kufanya kaguzi za kazi sehemu za kazi ili waajiri watimize wajibu wao kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB aliuliza:-

Vyama vya Wafanyakazi nchini licha kuwa na uwezo wa kujitegemea bado vinaendelea kutoza ada kubwa ya Uanachama, mathalan, Chama cha Walimu (CWT) kinatoza asilimia mbili.

Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kulinda maslahi ya Watumishi kwa kuleta Sheria ya kupunguza makato hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napeda kueleza kwamba, Serikali imeweka utaratibu chini ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba sita (6) ya mwaka 2004 unatoa uhuru na haki kwa Chama cha Wafanyakazi na Chama cha Waajiri, kuamua na kufanya mambo yao wanayotaka kwa maslahi yao ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu Katiba zao. Kifungu cha 11 cha sheria hiyo, kimeeleza bayana kuhusiana na haki hizo.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha na kuboresha maslahi ya Wanachama, Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wanao uhuru na haki ya kufanya mabadiliko katika Katiba zao ambazo zinasimamia uendeshaji wa shughuli za chama chao. Hivyo, suala la kupunguza makato ya Watumishi kwa Vyama vya Wafanyakazi lipo chini ya mamlaka ya Chama cha Wafanyakazi husika na Wanchama wenyewe kupitia vikao vya kikatiba kwa kufanya mabadiliko katika Katiba ya chama chao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kusimamia viwango vya michango ya wanachama ni kukiuka Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 87 na 189 juu ya uhuru wa kujumuika na majadiliano ya pamoja ambayo Serikali yetu imeridhia na kuzingatia katika Katiba ya nchi na Sheria mbalimbali za Kazi nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu juu ya haki na wajibu, uhuru wa kujumuika na mambo muhimu yahusuyo Wanachama na Katiba zao.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU aliuliza:-

Kumekuwa na biashara haramu za mitandao maarufu kama pyramid schemes. Biashara ambazo zimeshamiri sana miji ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti biashara hizo ambazo zimekuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Taifa?

(b) Je, ni kampuni ngapi za aina hiyo ambazo zimeingia nchini na kupata kibali cha kuendesha biashara za aina hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura Na. 16 kifungu cha 171A, 171B na 171C, biashara ya pyramid schemes au upatu, ni haramu na huendeshwa kinyume na sheria na taratibu za nchi. Ili kudhibiti biashara hiyo, Serikali huchukua hatua dhidi ya wahusika kama ilivyofanya kwa taasisi ya DECI. Aidha, Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu ubaya na madhara ya biashara ya upatu. Mathalani tarehe 14 Juni, 2017 Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ilitoa taarifa kwa umma kuhusu madhara ya biashara ya upatu na kuwahimiza wananchi kutoa taarifa kwenye vyombo vinavyohusika pindi wanapopata taarifa ya baadhi ya watu au taasisi kujihusisha na biashara ya upatu.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya upatu siyo biashara halali, hivyo hakuna mtu au taasisi yenye leseni ya kufanya biashara hiyo. Kampuni au watu binafsi wanaojihusisha na biashara hiyo wanavunja sheria na wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.