Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwantum Dau Haji (4 total)

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nakushukuru kwa siku hii ya leo adhimu kwa kunijalia kunipa nafasi hii katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa leo hii ni siku yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili, nishukuru viongozi wangu wote walioniwezesha kufika hapa pamoja na Mwenyezi Mungu; nimshukuru Rais wangu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa ushindi alioshinda wa kishindo siku ya tarehe 20 Machi, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwashukuru na wadau wangu walioniwezesha wa Mkoa wa Kusini Unguja, kuniamini na kunithamini wakanipa kura zao ili niwe Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Unguja. Nasema sitawaangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia suala la Wizara hii ya Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa. Kwanza niseme, alisimama mwenzangu hapa akazungumzia kwamba Jeshi limepindua Zanzibar. Jeshi halijapindua Zanzibar! Nataka kuuhakikishia ukumbi huu kwamba Serikali ya Mapinduzi tarehe 20…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, Mwantumu, hiyo kauli ilifutwa asubuhi. Kwa hiyo, tuendelee. (Makofi)
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuendelea kuchangia, kuna ndugu zetu wa polisi ambao ni trafiki na pamoja…
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Usinishuhulishe!
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa jitihada zao wanazozifanya katika Serikali ya Muungano huu wa Tanzania ninawapongeza kwa dhati. Hufanya kazi zao kubwa sana, kuimarisha Muungano ndiyo maana tumekuwa na utulivu, amani na uhuru wa nchi yetu. Nawaomba wazidi kulinda Muungano, wasirudi nyuma na wala wasitetereke. Waulinde, wausimamie na wautetee kwa maslahi ya nchi yetu na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuendelea katika huduma za jamii, mfano afya, ujenzi na utalii kuwa karibu na wananchi kutoa mafunzo ya ulinzi ili wananchi wazidi kufaidika na kujijengea kwenye harakati za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Kusini Unguja tuna ulinzi wa uhakika kwenye Jeshi la Ulinzi na wanatusaidia vikubwa kutulinda na wala hatuna tatizo tunakwenda nao vizuri, tunashirikiana nao vizuri na ndiyo tumejivunia mpaka leo hii tumefikia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nichangie kuhusu suala la ujenzi wa Kituo cha Mkoa cha Polisi Jumbi; kuna Kituo cha Mkoa wa Kusini Unguja kilikuwa kinafanya kazi pale Fuoni lakini Kituo kile kilihamishiwa Mkoa wa Kusini, Wilaya Kati pale Jumbi. Naomba Mheshimiwa Waziri, kwa udhati wako wa moyo, kwa imani yako, utusaidie kituo kile kiwe na jengo imara, lenye mvuto na pale lilipo ni njiani basi paonekane kwamba pana jengo la Kituo cha Polisi; na watu wote wanaopita pale wajue kwamba hili ni jengo la polisi la Mkoa wa Kusini Unguja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa jitihada na busara zake jinsi anavyoliendesha Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MWANTUMU D. HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru Serikali yangu chini ya Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufulikwa jinsi anavyoisimamia Serikali yake, nasema ahsante. Pia nimshukuru Waziri, Mheshimiwa Ummy na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kusimamia vyema Wizara yao kikamilifu, nawapongeza sana, Mwenyezi Mungu awasaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusu huduma ya afya ya uzazi na watoto. Vifo vitokanavyo na uzazi bado vinaendelea japokuwa vimepungua lakini wajawazito wengine hawana elimu kutokana na umbali kutoka wanakoishi mpaka kwenye vituo vya afya. Kwa hiyo, naishauri Serikali wapatiwe huduma elekezi, japo wauguzi wa vituo mbalimbali wasogee vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini wajawazito wengi wanapata operesheni, kwa nini iwe hivi? Watoto wengi sasa wanaozaliwa afya zao zinakuwa si nzuri. Aidha, wamekuwa wadogo sana au wamelegea. Mzazi anahangaika mpaka anachoka. Huduma wodini madaktari wanajitahidi sana, lakini wodi ndogo hazina ukarabati, vitanda vidogo, inafikia hatua kitanda kimoja wazazi watatu au wawili, hivi na magonjwa kila mtu na yake ukizingatia maambukizi ni mengi. Kwa hiyo, naishauri Serikali ifanye juhudi zake ili ipanue wodi au ukarabati kwenye hospitali zetu zilizokuwa zimechakaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na vilevile nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika zangu ndogo kwa hiyo siwezi kusema mlolongo mkubwa. Naipongeza hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa hotuba hii ambayo ni nzuri, aliyoipanga na haina mjadala, isipokuwa kuna mambo tu madogo madogo yaweze kuwekwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha Polisi Daraja ‘B’ Mkokotoni Unguja kina asilimia 60 na haya ninayozungumza yamo katika hotuba hii. Kituo hiki kina asilimia 60 Mkokotoni tayari kimeshakuwa kimefanikisha, lakini kuna vituo humu nchini ambavyo havina hadhi na havina mashiko. Tukizingatia katika Mkoa wangu wa Kusini Unguja kituo hiki cha Paje ambaye hapa kidogo mwenye hili Jimbo alilizungumzia lakini hakulitoa sahihi sana. Kituo kile hakina hadhi na ukipita pale utahisi kama hiki siyo kituo cha Polisi, kama wenyewe watakuwa hawapo pale nje basi huwezi hudhani kwamba hiki ni kituo cha Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo pia hiki kilikuwa kimo ndani ya mgao kwamba kitengenezwe na kiwe kituo cha hadhi cha Wilaya ya Kusini, naomba kama hili suala kweli lipo basi hiki kituo kiweze kutengenezwa kwa sababu ukanda mzima ule ni ukanda wa watalii na watalii wote waliopo kile kituo hiki ndicho kinachohusika kuanzia Jambiani hadi Michamvi. Naomba kituo hiki kitengenezwe kuwa kituo cha hadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MWATUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya. Nishukuru ukumbi huu leo wote tuliopo hapa pia tupo wazima wa afya mpaka hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba kuchangia Hotuba hii ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nachangia kuhusu JKT hasa kwa vijana na kule kwetu Zanzibar. Kule Zanzibar kuna vijana wetu ambao wanakwenda JKT na wanakuwa wazuri tu wakirudi kule wameiva, lakini wakifika kule wanakuwa hawana ajira rasmi za kujiajiri, wanahangaika isipokuwa ajira zao ziwe mikononi mwao. Vijana hawa wanakuwa wanatupigia kelele sana sisi wazazi au kama hivi sasa mimi ni Mheshimiwa, lakini huko nyuma nakumbuka sisi Wabunge waliopita walikuwa wanapata hizi ajira kama kwa mtoto wake au mtoto wa ndugu yake lakini ajira walikuwa wanapata kwa mtu mmoja mmoja, kwa hiyo zoezi hili limeondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba hili zoezi lirudi tena sisi Wabunge tuwe mfano wa kupata kwa kila mtoto kama mmoja mmoja au katika jamii tulizonazo wapate ajira hizi za Jeshi ili na wao wajiajiri na wajisikie. Na wanakuwa na hamu sana ya kwenda Jeshini, lakini ajira kama tunavyozungumza ni ngumu. Hili lirudi na lizingatiwe sana ili wale vijana wawe na imani na Nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwapongeze Jeshi kwa kazi zao wanazozifanya na hasa jana tu, wakati mimi nakuja huku Bungeni nipo maeneo ya Mlandizi, ilitokea ajali mbaya kati ya basi la Tanga na coaster inayotokea Morogoro, walisaidia roho za binadamu pale… (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. MWATUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo siikubali kwa sababu mimi sikusema kwamba huyo Mbunge ndiye anayetoa hiyo ajira hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umesikia, mimi naomba kwamba sisi Wabunge hivi sasa tunaomba kwamba zikitokea hizi ajira za Jeshi basi kama kuna uwezekano tuzipate ili tuwasaidie wale vijana na wale watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na hotuba yangu hii…majimboni, hata ikiwa majimboni ikiwa kwa jamii lakini tunaomba kwamba tupatiwe na sisi hizi ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi jana limeokoa roho za binadamu pale Mlandizi kati ya basi la Tanga na basi la coaster linalotokea Morogoro, ana-overtake basi la Tanga kwa bahati yule amejitahidi kulivusha lakini hakufanikiwa likaenda uso kwa uso dereva katoka miguu hana. Kwa hiyo, pale watu walishindwa kumtoa kila mmoja na imani yake basi walitokea vijana wetu hawa wa Jeshi na wakaenda pale wakaokoa roho zile wakawakwamua na palepale ikatokea gari wakapelekwa hospitali. Mimi ninawashukuru sana na ninawapongeza sana kwa kitendo kile walichokifanya jana.