Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Najma Murtaza Giga (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kwanza. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika mwezi huu wa Ramadhani tukiwa wazima na kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kabisa kwa kuunga mkono hotuba ambayo imetolewa na Wizara hii ya Nishati na Madini. Kwa kweli Serikali kwa upande wa Wizara hii imejitahidi. Vyovyote tutakavyofanya na kusema hatuna budi kuishukuru Serikali kwa jitihada inazochukua katika suala la sekta hii ya nishati na madini hasa tukizingatia usimamizi imara uliopo katika Awamu hii ya Tano ya Serikali yetu chini ya uongozi makini kabisa wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia sina budi kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa namna ambavyo amepokea wito wa uungwana kabisa na busara kulipokea deni ambalo ZECO inadaiwa na TANESCO na kuahidi kulilipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile dawa ya deni ni kulipa, Mheshimiwa Rais amechukua hekima na busara kuweza kukubali na mpaka hivi sasa deni la shilingi bilioni 11.8 limeshalipwa ambapo shilingi bilioni 10 zimelipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na shilingi bilioni 1.8 zimelipwa kupitia ZECO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hatuna budi kuipongeza Serikali kupitia TANESCO, tusipoipongeza tutakuwa hatuna shukrani. Pamoja na upungufu yote ambayo TANESCO inayo lakini kazi inayofanywa lazima tuishukuru na kuithamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwenye kitabu humu miradi mbalimbali imeshatekelezwa ikiwemo Kinyerezi I na II ambazo zinaendelea lakini pia tuna REA, usambazaji wa umeme vijijini, kazi inafanywa kubwa kwa mazingira magumu. Tukipita sisi wengine tunaona juu ya milima kuna nguzo huko, tunashangaa zimetandazwaje, chini ya mabonde huko tunakuta nguzo tunashangaa zimetandazwaje, lazima tuwe wenye kushukuru na lazima tuwapongeze. Naamini kwamba Serikali kupitia TANESCO itatatua changamoto hatua kwa hatua ili tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utaelekea huko huko kwenye nishati ya umeme na hapa nitazungumzia mfumo uliopo baina ya Shirika la TANESCO na ZECO. Niseme wazi kwamba kutokana na mfumo uliokuwepo siku za nyuma na pengine huu uliopo sasa hivi, ndiyo umepelekea ZECO kuwa na deni kubwa kwa TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielezee yale ambayo yamepeleka mfumo huu kuonekana kama unaendelea kuipa deni ZECO. Kwanza ni tozo ya KVA. Hii nikizungumza wataalam wanaelewa, ni tozo ya watumiaji wakubwa wa umeme kwa mfano viwanda na kadhalika. ZECO tunachukua kilovoti 132 kwa bei ya shilingi 16,550 lakini watumiaji hawa wa kilovoti 33 ambao wanachukua kwa Tanzania Bara wanatozwa shilingi 13,200 kwa kilovott moja. Kwa hiyo, utaona difference iliyopo ya mfumo katika uendeshaji na kuipelekea ZECO kuweza kulimbikiza deni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wawekezaji ambao wana tamaa ya kuwekeza Zanzibar wanashindwa kuwekeza kwa ajili ya tozo hii, hivyo naomba sana Serikali ilizingatie. Kwa mfano, mwaka 2011 utaona pia mtiririko wa mabadiliko ya tozo unavyobadilika, naweza kutoa mfano mwaka 2011 ZECO iliongezewa tozo ya asilimia 81.1 wakati Tanzania Bara iliongezwa tozo ya asilimia 19.4 tu, ni difference kubwa sana. Kwa hiyo, naomba Serikali izingatie sana kupitia Shirika hili la Umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoa mfano pia mwaka 2013 TANESCO na ZECO walikubaliana kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwamba sasa umefika wakati hizi kilowatts per hour Zanzibar ipunguziwe kwa asilimia 31. Matokeo yake, TANESCO iliendelea kuingiza hiyo asilimia 31 hatimaye deni hili likatajwa mwisho wake kuwa ni shilingi bilioni 121.9 ambayo round figure ni shilingi bilioni 122 wakati ZECO wanaendelea kuhesabu kwamba wameshatolewa punguzo la asilimia 31 na kulikubali deni hilo kuwa ni shilingi bilioni 65.5. Kwa hiyo, tunaweza kuona difference hizo na naomba sana Mheshimiwa Waziri husika na timu yake waweze kuangalia kwa upande huu wa TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la ZECO kuwa end user, nikizungumza end user anakuwa kama mtumiaji wa kawaida wa Tanzania Bara. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu mtumiaji wa kawaida wa Tanzania Bara anapelekewa umeme kupitia miundombinu ya TANESCO lakini ZECO tunaletewa umeme kwa bei ambayo mtumiaji wa Tanzania Bara anapewa with operational costs za ZECO, miundombinu na gharama zote ni za ZECO. Kwa hiyo, tuangalie hali inavyokwenda tuone mfumo uko vipi, nia yangu ni kueleza mfumo huu tuweze kuusahihisha ili tuweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hili tunasema kwamba ZECO na TANESCO ni mashirika ya Serikali, moja kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano na lingine kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. ZECO yenyewe inakuwa na madeni ambayo inadai Taasisi za Serikali ikiwemo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Hussein Mwinyi, Wizara yake imeweza kupunguza shilingi milioni 400 deni ambalo tulikuwa tunawadai na sisi ndiyo tumeweza kurudisha TANESCO. Kwa hiyo, tuangalie haya mambo ili sisi tuweze kulipa deni na Serikali taasisi zake iweze kulipa. (Makofi)

Kwa hiyo, hilo ni moja ambalo nilipenda nizungumzie kwa upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna huduma nyingine za jamii ambazo zinaigusa jamii moja kwa moja. Kwa mfano, ZAWA ambayo inashughulika na masuala ya kusambaza maji Zanzibar, tunaidai zaidi ya shilingi bilioni 20. Tunashindwa kuwafungia umeme kwa sababu Watanzania wanaoishi Zanzibar watakosa maji. Kwa hiyo, inabidi shirika hili tuone mfumo gani ambao utaweza kuwa bora na mzuri ili tusije tukaingia kwenye migogoro ambayo mimi sipendi kuiita kero, nasema bado ni challenge, tuzirekebishe hizi challenge ili Watanzania wote wanaoishi Tanzania Bara na wale walioko Zanzibar ambao wote ni wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania waweze kunufaika na huduma hii bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili Shirika la ZECO linafanya kazi kubwa kuikusanyia mapato TANESCO. Mbali na hayo madeni ambayo yametokana na hizo sababu nilizozitaja, tunatumia umeme kuanzia shilingi milioni 400 hadi shilingi milioni 500 kwa mwezi na bahati nzuri kuanzia mwaka 2015 Desemba tunalipa current bill kwa maana kwamba ankara kamili ya kila mwezi. Kwa hiyo, ili kuweka sawa mambo haya, tuonekane na sisi ZECO kule kwamba tunaifanyia biashara TANESCO ambayo ni taasisi ya Jamhuri yetu ya Muungano Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano mwingine, tumeweza kuikusanyia shilingi bilioni 41.8 katika kipindi cha miezi tisa kuanzia 2016 hadi kufikia Machi, 2017. Kwa hiyo, sasa nachoshauri mbali na kuwekwa huyu Mtaalam Mwelekezi nitaomba ushauri wake ufuatwe ili twende sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni kwamba sisi ZECO basi angalau tupewe fursa ya kuwa agent wa TANESCO ili tuweze kulipwa na kuweza kugharamia operation cost ili tusiweze kuleta migogoro katika Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, pamoja na kuunga mkono hotuba hii naomba sana ushauri huu uweze kuzingatiwa ili tuweze kuimarisha Muungano wetu. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. NAJMA MURTAZA. GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa jinsi anavyokuwezesha Mheshimiwa Waziri (mwanamke mwenzetu) kufanya kazi zake kwa ujasiri na uweledi unaothibitisha kuwa wanawake tunaweza kabisa.

Mheshimiwa Waziri hoja yangu inajikita moja kwa moja kwenye hotuba yako kwenye ukurasa wa 101 hadi 107 na ukurasa wa 109 hadi 110. Umekiri kabisa kuwa ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa hapa nchini, na mimi ninakiri pia kwa kauli yako hii. Matukio ya ukatili dhidi ya watoto yameongezeka kwa asilimia 28 kutoka mwaka 2016 hadi kufikia mwaka 2017, ninaamini kabisa elimu sahihi kuhusu vitendo hivi ikiwafikia Watanzania walio wengi na kuweza kutoa taarifa za matukio ya ukatili dhidi ya watoto, asilimia hii inaweza kuzidi hadi kufikia asilimia 60 au zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sichoki na wala siyachoka kutoa ushauri wa kuangalia adhabu mbadala kwa makatili wazoefu wanaoharibu maisha ya watoto wetu ambao ni Taifa letu la kesho.

Mheshimiwa Waziri inasikitisha sana kuona kuwa haki za binadamu zinapewa kipaumbele kwa hawa makatili wa watoto wetu na hasa wabakaji watoto wa kike na wanaolawiti watoto wakiume, mbali na kutumikia kifungo kwa miaka 30 makatili hawa sugu (ambao wanathibitika kuwa wazoefu katika kuwaharibu watoto wetu) wafikiriwe adhabu mbadala ya kuhasiwa uume wao ili iwe funzo kwa wengine na kuwaokoa watoto wetu kutokana na janga hili ambalo tukizidi kuwaonea huruma kwa kisingizio cha haki za binadamu tutaliangamiza Taifa la kesho kwani hili janga mwisho wa siku litakuwa janga la kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza wazi kwamba haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambavyo itasababisha kuingiliana kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma; kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru wa haki za watu bibafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali kuwa ibara hii ya Katiba ikionekana kuvunjwa kwa namna yoyote kwa mujibu wa ibara 30 mtu anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu. Hili suala la kufungua shauri katika mahakama zetu bado inaonekana siyo muafaka sana kwa maslahi ya watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakushukuru Mheshimiwa Waziri ukiwa kama mwanamama mwenzangu ulitafakari na kukaa na timu yako kutafakari zaidi suala la kuleta muswada wa sheria ya kuwahasi wabakaji sugu wa watoto wa kiume na wa kike, tukizingatia ibara hizo hapo juu za Katiba yetu zinaturuhusu kutunga sheria katika jambo la aina hii, tuache kabisa kisingizio cha kuvunja haki za binadamu wakati hawa wabakaji wanaendelea kuvunja haki za binadamu wadogo.

Naomba sana Wizara yako ijaribu kutafiti na kuona uwezekano wa kutungwa sheria hii ya adhabu ya kuhasi kwa kulinganisha na nchi nyingine ambazo tayari zina hukumu za aina hii. Mfano Mheshimiwa Mary Karooro Okurut, Waziri wa Jinsia Kazi na Maendeleo wa Uganda anaunga mkono suala hili la kuwahasi wabakaji hawa.

Mheshimwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa ni lazima nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ananiwezesha kila jambo. Hata hivyo, pia sina budi kuushukuru Umoja wa Wazazi Tanzania kwa imani yao juu yangu kwa kunikubalia na kuniwezesha kuwa Mbunge ninayewawakilisha kupitia Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile sina budi kukushukuru wewe pamoja na Wabunge wote kwa imani yenu juu yangu ya kunikubalia kuwa miongoni mwa Wenyeviti wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee kabisa lazima nizipeleke kwenye uongozi mpya wa Awamu hii ya Tano unaoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli dhamira yao njema imeshaanza kuonekana, kwa hiyo tuwaombee tu Mwenyezi Mungu azidi kuwaendeleza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia sina budi kabisa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Ummy pamoja na msaidizi wake, Naibu Mheshimiwa Kigwangalla kwa kazi nzuri waliyoanza nayo. Sina haja ya kuwalaumu kabisa, ni lazima niwapongeze. Changamoto ndiyo sehemu ya maisha na kazi yetu ni kuwashauri.
niongelee kwenye suala zima la ukatili wa kijinsia ambalo Mheshimiwa ameainisha humu katika kiambatanisho namba 10.
Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumza hapa kuhusiana na suala hilo kwa maoni tofauti, lakini naomba nielekeze moja kwa moja kwenye ushauri kwenye mambo sita tofauti ambayo ameainisha.
Suala la kwanza ni ukatili wa kingono. Hilo limezungumzwa, lakini nasema, pamoja na elimu ambayo itatolewa ambayo wamejipangia katika Wizara hii lakini ushirikiano wa karibu kabisa ni lazima kwa vitengo vya sheria. Mwanasheria Mkuu atanielewa nikisema zaidi kwamba ushahidi katika suala hili la hao wahalifu ni mgumu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, bila ushirikiano wa karibu na vitengo vya sheria na kuhakikisha kwamba tunapunguza masharti ya sheria za ushahidi ili tuwadhibiti hao wenye vitendo vinavyofanya mporomoko wa maadili katika nchi yetu na kusababisha idadi inayoripotiwa kwa mwaka 2015 kufika 6,722 ambapo naamini kabisa idadi hii ni ya wale walioripotiwa tu, lakini kuna wengine huku ambao hawakuripotiwa wapo wanaathirika na janga hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukaribu baina ya Wizara pamoja na Wizara nyingine, ukajenga mnyororo madhubuti, tutaweza. Naamini kabisa mkituletea hapa Wabunge tujaribu kurekebisha hizi sheria za ushahidi wa jambo hili, basi hawa watakamatwa na watadhibitiwa na hivi vitendo vitapungua, vinginevyo tutaongeza vitendo hivi jamani. Kwa sababu hata Mwenyezi Mungu kwenye kitabu chake kitukufu cha Qurani amesema tusikaribie zinaa, hakusema tusifanye, amesema, tusikaribie kwa maana, tusipokaribia hatutofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ikiwa tutawadhibiti hawa kwa ushahidi mwepesi wakapatikana, wataacha na wao watakoma na Taifa letu litanusurika na janga la huu ukatili wa ngono kwa akinamama na watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakuja suala la pili, utupaji wa watoto na wizi wa watoto, vitu viwili sambamba. Kuna watu wanahitaji watoto hawana, wanaiba. Kuna watu wanapata watoto wanatupa na wanakufa. Kwa hiyo, nashauri kwa Wizara hii hebu tujaribu, kama Wizara itakuwa ni vigumu labda kifedha, basi hebu tutoe uhamasishaji kwa wananchi waweze kujitolea kujenga vituo vya kulelea yatima ili wale akinamama ambao wanaona watoto wale hawawahitaji, wawapeleke wakalelewe kule na wale wezi waache kuiba wakachukue kule. Kwa hiyo, huo ni ushauri ambao pengine Serikali inaweza ikashindwa lakini wadau wengine watakubali. Kwa hiyo, naomba sana hilo tulifanye.
Mheshimiwa Spika, katika hilo hilo kuna suala la utoaji mimba. Hili naomba pia Wizara ilishughulikie, baadhi ya mimba zinazotolewa wanashirikiana na wakunga na manesi. Kwa hiyo, sasa hawa manesi wenye tabia hizi wadhibitiwe kwa sababu ni watu wachache wenye ujasiri wa kutoa mimba wenyewe, lazima wasaidiwe na wanaoelewa wanakuwa ni wakunga ama manesi. Kwa hiyo, sasa Wizara hii inabidi katika upande wake, katika sera zake na mambo yake, ihakikishe kwamba hao wanaofanya vitendo hivi wanadhibitiwa ipasavyo na kuadhibiwa ili kuondoa tatizo la utoaji mimba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiondokana na hayo nakuja kwenye mauaji ya vikongwe. Ni kweli inawezekana hawa vikongwe wanatuhumiwa, inawezekana ni kweli lakini kwa nini tuchukue sheria mkononi? Kwa nini, hakuna Serikali za vijiji? Hakuna uongozi wa vijiji? Kwa nini tusiende tukatoa taarifa kule. Kwa hiyo Wizara hii naomba sana kwa kushirikiana na vitengo vya sheria, narudia tena tudhibiti jambo hili kwa kuhakikisha tunatoa elimu tosha ya kuelekeza wananchi wetu vijijini ili waende wakatoe taarifa wanapoona kwamba kuna wazee wanahatarisha jamii yetu, basi waende wakashughulikiwe kisheria kuliko kuchukua hatua au sheria mkononi ya kwenda kuwaua wazee wetu, inawezekana wengine si kweli. Kwa hiyo, naomba sana hilo nalo tulifuatilie kwa uzuri wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija suala la nne, mashambulio ya kudhuru na lugha za matusi. Hii zamani ilikuwa haipo kabisa jamani. Utamaduni wetu sasa unaporomoka, ni tatizo kubwa. Naomba sana niwashauri Wabunge wenzangu humu ndani, tuanze sisi na lugha nzuri. Sioni sababu ya kutoa lugha ya matusi wakati tunaambiwa maneno mazuri humtoa nyoka pangoni. Kwa hiyo, sasa wale wanaotusikia nje au wakihadithiwa nje kwamba Wabunge ndani wanazungumza lugha mbovu, tutakuwa hatuna mfano mzuri kwa wananchi wetu. Haya matendo yanazidi, idadi yake ni kubwa mno hapa tunaambiwa 14,561 mashambulio ya kudhuru pamoja na lugha za matusi. Kwa hiyo, naomba sana sisi Wabunge tuwe mfano ili image yetu iwe reflected nje, watu waweze kuwa na adabu nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la tano ni utelekezaji wa familia. Naunga mkono kweli elimu ni ndogo, pengine vijana wetu wengi hawajui nini maana ya familia, lakini bado narudi tena pamoja na kutoa elimu kuna akinababa wengine wazima zaidi ya miaka 40, anatelekeza familia yake anakwenda kutafuta mwanamke mwingine. Hili ni baya sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri kabisa hii Wizara inayohusiana na jinsia jamani Mheshimiwa Ummy, hawa akinababa wenye tabia hizi na wana uwezo wao wengine wanafanya kazi na wana uwezo tuwadhibiti, tukiwajua wakatwe baadhi ya mshahara wao ama vipato vyao viende kwenye familia zile.
Mheshimiwa Spika, pia sisi akinamama nao wake wa pili, nyumba za pili, tusiwe na roho mbovu, tusidhibiti kila kitu. Tuwaachie akinababa wawashughulikie na akinamama wenzetu wengine na familia zao. Hili ni jambo zuri sana, naomba jamani kwa heshima kubwa sana hili tulifikirie na tulizingatie, litaondosha kabisa tatizo hili jamani.
SPIKA: Mheshimiwa Najma, sijakusikia vizuri. (Kicheko)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, nasema kwamba kuna tabia ya akinababa hawa ambao ni watu wazima zaidi ya miaka 40, wanaacha familia zao za kwanza, yaani nyumba ya kwanza wanatafuta nyumba nyingine, ile wanaitelekeza. Kwa hiyo, hili ni jambo baya. Hawa wadhibitiwe na kama wanafanya kazi wana uwezo basi kile kinachopatikana wagawiwe familia ya kwanza.
Pia na akinamama hawa wa nyumba za pili, tuwe na huruma kwa akinamama wenzetu wa nyumba za kwanza. Nafikiri hili limeeleweka vizuri na naamini kabisa utelekezaji huu utapungua, tukifanya hivyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, namalizia kuhusu mimba za wanafunzi. Mimba za wanafunzi zinaweza kuleta madhara kwa wasichana wetu na kuwayumbisha kimaisha jamani! Hapa tunaambiwa idadi ya ripoti ni 412 lakini naamini ziko nyingine ambazo hazijaripotiwa. Kwa hiyo, hili suala nalo tulidhibiti vizuri kwa kushirikiana tena na vitengo vya sheria. Ikiwa ni mtu mzima amempa mimba mwanafunzi, basi huyu asiachiwe, adhabu iwe kali. Vilevile ikiwa ni mwanafunzi na mwanafunzi waadhibiwe wote wawili ikiwezekana, kwa sababu wengine wakome. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yangu kwa kweli yalikuwa ni hayo. Nakushukuru sana kwa muda huu. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Najma….
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja wala sina haja ya kupinga.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niende direct to the point na naingia kwenye ukurasa wa 101 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu haki na maendeleo ya mtoto. Ninashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri amekiri mwenyewe kwamba ukatili dhidi ya watoto bado ni tatizo kubwa hapa nchini na asilimia 28 ambayo imeoneshwa kuongezeka katika wanaoripoti kuanzia mwaka 2016/2017 mimi ninasema bado hiyo itakuwa ni kidogo ikiwa Watanzania wengi watalielewa hili suala. Kwa hiyo, tunaweza tukafika hata kwenye asilimia 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi tena kwenye ombi langu, namwomba Mheshimiwa Waziri kigezo cha kusema kwamba hawa wabakaji sugu, nikisema wabakaji sugu wa watoto wa kike na wa kiume sikusudii mtu mwingine yoyote, sikusudii mbakaji wa mume kwa mke, hilo ni lao. Nakusudia watoto wadogo wa kike na wa kiume. Naomba sana tuache hii ya kufikiria kwamba tunapowaamulia au kuwatungia sheria hawa wabakaji sugu kuhasiwa, ni kosa au ni haki za kibinadamu, naomba nije kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ninukuu; “Haki na uhuru wa binadamu ambapo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba hii havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.”

Pili, inasema: “Ifahamike kwamba masharti yaliyomo katika sehemu hii ya Katiba yanayofafanua misingi ya haki, uhuru na wajibu wa binadamu, hayaharamishi sheria yoyote iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote halali kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo kwa ajili ya:- (a) kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutumia ibara hiyo, ninaomba nikushawishi na ninaomba nishawishi Bunge, mwisho wa siku tusipolivalia njuga jambo hili litakuwa ni janga la kitaifa. Ninasema hivi nawaambieni mfano, mwisho wa siku hatima yake, kiongozi ambaye yupo mbele yetu sasa hivi ni mwanaume, atakuja kiongozi ambaye ana ndoa ya jinsia moja, hilo ndiyo mwisho wa siku. Kwa hiyo, naomba tusifanye masihara wala tusione hili jambo ni la utani. Taifa letu la kesho linakwenda kuangamia. Taifa letu lenye utamaduni bora Tanzania linakwenda kutoweka ikiwa tutakuwa hatupo makini katika suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema, Mheshimiwa Waziri kaa na Wizara husika tuangalie namna bora ya kutengeneza sheria ya kuwahasi wabakaji sugu wa watoto wetu wa kike na wa kiume ili tuweze kuondokana na janga hili sugu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo yangu ya leo.
Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 5) wa Mwaka 2017
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na natumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwanza lakini kuwatakia Waheshimiwa Wabunge wote heri zote za mwaka mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache tu ya kuchangia katika Muswada huu wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 5 wa mwaka 2017. Sheria hizi ukitazama zimeletwa kwa uchache kwa maana ni kidogo lakini zina impact kubwa na maslahi mapana sana katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa sheria hii ya Ufilisi ni sehemu ndogo tu lakini lengo lake nalo pia ni zuri katika kufanya utekelezaji uwe mwepesi katika Sheria ya Ufilisi kwa kuweka tafsiri ya neno hili la official receiver. Kwa hiyo hili halina mjadala mkubwa na naamini wote mtakubalina na mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Sheria ya Bajeti hii inadhamiria kuweka hali sawa katika Bunge letu baina ya kanuni zetu na sheria. Kwa hiyo hili nalo nafikiri ni jambo zuri na naamini wote tutakubaliana, kwamba kupokea Mpango wa Bajeti wa Serikali katika kipindi cha Oktoba na Novemba itakuwa ni vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naishukuru Serikali kwa kuona kwamba kuna umuhimu wa kuweka exception katika ule mwaka ambao tutafanya uchaguzi na kuweza kupokea mpango huu sasa katika mkutano wa pili wa Bunge. kwa hiyo, nalo hilo limekaa vizuri halina tatizo lolote na naamini wote tutakubaliana hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye suala la ardhi, yaani masharti kuhusu kutumia ardhi kwa ajili ya kupata mkopo. Hapa lazima niseme kidogo zaidi. Kwanza naiunga mkono na kuipongeza sana Serikali kwa kuweza kuona kwamba umuhimu wa kuendeleza ardhi yetu ya Tanzania. Hili ni jambo muhimu sana, tusilione kwa udogo tukaitizama kwa urahisi lakini inaonekana muda mrefu Serikali yetu inapata hasara, watu wanakopa kwa kutumia ardhi iliyopo Tanzania ambayo haijaendelezwa na wanaweza kuendeleza maeneo mengine ambayo yapo nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuwepo au kuletwa kwa marekebisho ya sheria hii, yatasaidia ardhi ya Tanzania kuweza kuendelezwa. Haiwezekani leo mtu anakopa kwa kutumia rasilimali ya ardhi ya Tanzania na kuendeleza sehemu nyingine ambayo si ya Tanzania. Kwa hiyo, sheria hii naamini Watanzania wote wazalendo wa nchi hii wataunga mkono na kukubaliana na marekebisho haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye sehemu ya mwisho ambayo ni Sheria ya Utumishi wa Umma, kuongeza umri wa wastaafu hasa tukienda kwenye kada ya maprofesa na madaktari bingwa. Kuhusiana na hili Serikali pia imeleta hoja nzito na hoja za msingi. Ni kweli kabisa kada hii ni muhimu sana kwa Taifa letu na hao watu bado tunawahitaji kwa uchache wao kwa maslahi ya Taifa letu, hii haina mjadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa tunakubali kurekebisha sheria hii kwa maslahi mapana ya Taifa letu lazima Serikali ione namna mbadala wa ku-fill gap, hiyo ndiyo itakuwa solution ya kudumu. Tutaenda na sheria hii tutarekebisha leo, tutaweza kuitumia na naamini itatufikisha pazuri ili kuondoa gharama kubwa ambayo tumeitumia siku zote katika Serikali yetu katika kuongeza mikataba ya watu hawa ambao tunawahitaji katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida zipo pande mbili, kwamba kuna wengine ambao wanaongezewa muda wanajiweza bado wapo na afya nzuri na bado wataleta maendeleo katika Taifa letu. Pia tutawakwepa wale ambao wanasomeshwa na Taifa hili halafu wanafika umri wa miaka 55 wanasema wanataka kustaafu kwa hiyari anakwenda kutafuta mpango mwingine wa binafsi na anaacha maslahi mapana ya Taifa letu yanakwenda pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mambo hayo mawili yamesaidia kuonesha hoja ya msingi ya Serikali na kwa kweli naunga mkono suala hili, lakini narudi pale pale tena, Taifa letu bado lina uchache wa kada hizi, kwa hiyo naomba tupange tu mpango endelevu wa kuona kwamba tunaondoa urasimu kwanza katika kuhakikisha hawa wasomi wetu wanafikia level hizi ambazo tumezikusudia za Maprofesa na Madaktari Bingwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu pia kwa upande mmoja urasimu ndio unaosababisha, mtu anaandika paper miaka mitatu mizima hasogezwi popote au hajibiwi lolote. Kwa hiyo hii inarudisha nyuma kuongeza hizi kada za Mprofesa au Lectures wa vyuo vyetu. Kwa hiyo, naomba hilo suala la urasimu liangaliwe sana na Serikali ili tuweze kuwasogeza mbele hawa wasomi wetu ambao wanatakiwa wafike katika kada hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba gharama ya kusomesha Madaktari bingwa nje ya nchi ni kubwa sana lakini bado nasisitiza kuna umuhimu mkubwa sana wa Serikali yetu kupanga fungu maalum la kuweza angalau basi tusiwafikie wenzetu wa nchi nyingine za jirani ambao wanaweza kupeleka wasomi wetu kwenda kutafuta hii fani ya udaktari bingwa nje ya nchi, basi angalau na sisi tuweze kufanya japo kidogo tuanze taratibu ili kuona kwamba gap hili linaweza kuondoka miaka ya mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini nimeeleweka kwa machache haya, naomba na wengine waweze kuchangia. Ahsante sana.