Primary Questions from Hon. Najma Murtaza Giga (20 total)
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD (K.n.y. MHE. NAJMA MURTAZA GIGA) aliuliza:-
Licha ya kuwa na sheria kali kuhusu udhalilishaji wa wanawake na watoto, bado watoto wadogo wa kike na wa kiume chini ya miaka 10 wameendelea kudhalilishwa, baadhi ya watu wanaowafanyia udhalilishaji ni baba wazazi wa watoto hao:-
(a) Je, Serikali haioni haja ya kuweka adhabu tofauti kwa wazazi wanaobainika kuwaharibu kwa kuwabaka watoto wao wenyewe;
(b) Je, Serikali haioni haja ya kuongeza adhabu kwa kuwahasi wanaume wanaopatikana na tabia hii chafu na ya kikatili, licha ya kuwafunga kifungo cha miaka 30?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009, imeelekeza adhabu kali kwa yeyote atakayebainika kutenda kosa la kumdhalilisha mtoto au kumbaka mtoto ikiwemo kifungo cha miaka 30. Hata hivyo, imekuwa vigumu kuwatia hatiani wakosaji hasa wa ndani ya familia kwa kukosekana kwa ushahidi. Wengi wao wanaogopa kutoa ushahidi kutokana na hofu ya kupoteza moja ya wanafamilia kutokana na adhabu ya kifungo cha maisha. Aidha, kutokana na mtazamo hasi wa jamii, familia nyingi huhofia kudhalilika au kunyanyapaliwa baada ya kubainika mkosaji.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatunga sheria kwa kuzingatia Katiba ya nchi na Mikataba ya Haki za Binadamu, hivyo haitakuwa busara kuwahasi wanaume wanaopatikana na makosa ya aina hii kwa kuwa kumhasi binadamu siyo tu ni ukatili bali pia ni kinyume cha haki za msingi za binadamu.
Serikali pia inaandaa Mpango wa Taifa wa kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Mpango huu utachangia kutoa elimu kwa familia na jamii na kuhakikisha kuwa sheria zinatumika inavyotakiwa ili wahusika wa matukio haya wapewe adhabu wanayostahili na kuwalinda watakaotoa ushahidi wa matukio ya vitendo vya ukatili vinavyofanywa dhidi ya watoto na wanawake. (Makofi)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Ulevi wa kupita kiasi hasa wa pombe za kienyeji umekuwa na athari kubwa za
kiafya na kiakili kwa Watanzania wenye tabia ya ulevi wa kukithiri:-
Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na tatizo hilo hasa ikizingatiwa kuwa Sheria
ya Vileo ya mwaka 1969 ni ya zamani sana kiasi kwamba inawezekana kabisa
haikidhi mabadiliko ya hali halisi ya vileo kwa wakati huu.
NAIBUWAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli. Sasa hivi kuna tabia kwenye baadhi ya Mikoa,
utakuta watoto wadogo asubuhi au wakati wa weekend wananyweshwa pombe. Jambo hili kwanza kimsingi ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu kwanza
na haki za watoto ambapo mtoto mdogo anatakiwa kuendelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuchukue huu ushauri kwa
sababu sheria hii ni ya muda mrefu sana na kutokana na maoni ya wadau
mbalimbali tutaangalia jinsi gani tutafanya turekebishe, lengo kubwa ni
kuhakikisha kwamba Taifa letu linakuwa Taifa imara kwa sababu lazima tuwalee
hawa watoto kwa kizazi kijacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuchukue ushauri.
Itakapoonekana pale ina haja, basi wadau mbalimbali wataleta maoni yao na
sisi Wabunge ni miongoni mwa wadau wa kutengeneza hizo sheria. Kwa hiyo, hili
nadhani tutalifanyia kazi vema tuweze kulifanikisha.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. NAJMA MURTAZA GIGA) aliuliza:-
Matumizi ya SHISHA yamegundulika kuwa ni miongoni mwa aina ya uvutaji wa sigara ambao wauzaji wengine huchanganya na aina mbalimbali za dawa za kulevya na vileo vikali na kusababisha vijana wadogo kuathiriwa kwa kiasi kikubwa.
Je, kwa nini Serikali hadi sasa inaendelea kuruhusu matumizi ya SHISHA kwenye baadhi ya migahawa na hoteli kubwa ambayo inatumiwa na watu wa rika zote?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Najma Giga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali mara baada ya kuona kuwa matumizi ya shisha yanaleta athari kubwa kwa afya za binadamu, kutokana na utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya, Serikali ina mpango mkakati wa kutengeneza utaratibu wa kudhibiti na kutungia sheria kupiga marufuku utumiaji, uuzwaji na usafirishwaji wa shisha nchini Tanzania ili kuweza kuokoa afya za Watanzania walio wengi ambao ni nguvu kazi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tukiwa tunasubiri kutungwa kwa sheria na kanuni, Mheshimiwa Waziri Mkuu alishaelekeza kupiga marufuku matumizi ya shisha na utekelezaji ulishaanza kutekelezwa mikoani ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kilimanjaro na mikoa mingine.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa Serikali zetu zote mbili zimekuwa kwenye jitihada za kukabiliana na kero za Muungano:-
(a) Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Zanzibar kuhusu ushiriki wa Wizara zisizo za Muungano na Zanzibar kwenye Taasisi za Kimataifa zinazotambua utaifa wa wananchi katika uwakilishi wake?
(b) Je, Serikali inapata ugumu gani kuwafahamisha wananchi kwa uwazi kabisa kila kero za Muungano zinazopatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kweli kwamba Wazanzibari kwa muda mrefu wamekuwa na kero ya kutoshirikishwa katika medani za Kimataifa. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mabadiliko yake, masuala ya mambo ya nje yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikishirikishwa kwa kiasi kikubwa katika taasisi za Kimataifa zinazotambua utaifa wa Tanzania kwenye Wizara zisizo za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa katika mikutano ya Kimataifa na taasisi za Kimataifa, kama vile Mikutano ya mabadiliko ya Tabianchi, Mikutano ya Shirika la Kazi Duniani, Mikutano ya Kamisheni ya Hali ya Wanawake, Mikutano ya Shirika la Kazi Duniani, Mkutano kuhusu utekelezaji wa lengo Namba 14 la Maendeleo Endelevu linalohusu Uhifadhi na Matumizi Endelevu ya Bahari na Rasilimali zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Viongozi wa Mashirika ya Kimataifa waliofanya ziara hapa nchini kwa mwaka 2017, walitembelea pia Zanzibar na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambao ni Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Mkurugenzi wa FAO, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali haijawahi kupata ugumu wala kugugumizi katika kuwafahamisha wananchi kwa uwazi kuhusu changamoto zilizopatiwa ufumbuzi na hata zile ambazo ziko katika hatua mbalimbali ya kutafutiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe nikiwa Waziri mwenye dhamana ya Muungano, nimefanya jitihada kubwa za kuwafahamisha wananchi kwa uwazi kabisa kuhusu jitihada za Serikali katika kutatua changamoto za Muungano kupitia vyombo vya habari mfano television, redio na magazeti, makongamano, hotuba za viongozi wakati wa maadhimisho ya Muungano na hata kupitia Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Masuala ya kunajisi na ubakaji kwa watoto pamoja na mapenzi ya jinsia moja yamekithiri nchini na kuongezeka siku hadi siku:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya utafiti wa kina na kuona athari zinazoendelea kuikumba jamii katika suala zima la usagaji (lesbianism)?
(b) Je, ni lini Serikali itaanza kuandaa sheria ya kuwaadhibu wanawake wanaoharibu vijana wa kiume chini ya umri wa miaka 18 na wale wenye kuwafunza na kuwaharibu watoto wetu wa kike katika masuala ya usagaji (lesbianism)?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 inakataza vitendo vilivyo kinyume na maadili ikiwemo mapenzi ya jinsia moja. Hadi sasa Serikali haina takwimu za hali ya usagaji na ushoga nchini. Hivyo, Serikali inaona umuhimu wa kufanya utafiti wa kina kuhusu masuala ya mapenzi ya jinsia moja ikiwepo usagaji ili kubaini ukubwa na athari za suala hilo.
(b) Mheshimiwa Spika, pindi utafiti utakapofanyika, Serikali itaangalia uwezekano wa kuzifanyia marekebisho na kuboresha sheria zilizopo ili kubaini na suala hilo?
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali inatambua kuwa sheria pekee haitoshi kutatua tatizo hili, hivyo inaendelea kutoa elimu kuhusu malezi chanya yanayozingatia maadali ya Kitanzania?
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Sheria ya Makosa ya Kujamiiana kwenye suala la ubakaji (SOSPA) ya mwaka 1998 na marekebisho yaliyofanywa mwaka 2017 yote yana lengo la kukomesha vitendo vya ubakaji wa watoto chini ya miaka 18 na wanafunzi (kifungo miaka 30) na watoto chini ya miaka 10 (kifungo cha maisha):-
(a) Je, tokea kupitishwa kwa sheria hii (SOSPA) na marekebisho yake, ubakaji umepungua au kukoma hapa nchini?
(b) Je, kama bado changamoto ipo Serikali ina mpango mkakati gani mpya katika kupambana kutokomeza ubakaji Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Giga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Makosa ya Kujamiana (SOSPA) ya mwaka 1998 na marekebisho yaliyofanyika 2002 imeingiza vifungu vya makosa ya kujamiana kwenye Kanuni za Adhabu ili kukomesha vitendo vya ubakaji kwa watoto ambapo yeyote akipatikana na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka thelathini jela au kifngo cha maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na adhabu hii ambayo ni kubwa ambayo ingeweza kufanya watu waogope kujihusisha na vitendo vya ubakaji lakini vitendo vya ubakaji kwa watoto nchini vimeendelea kuongezeka. Kwa mujibu wa Takwimu ya Hali ya Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani, matukio ya ubakaji yameongeza kutoka matukio 394 Desemba 2015 hadi kufikia matukio 2,984 Desemba 2017. Hii ni kutokana na jitihada kubwa ambayo Serikali imefanya na wadau ambalimbali ya kuhamasisha jamii kutoa taarifa ya masuala ya ubakaji pindi yanapotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetekeleza afua mbalimbali katika kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 10, 988 katika ngazi za Halmashauri, Kata na Vijiji; kuanzisha vikundi vya malezi 1,184 na kuwezesha huduma ya simu kwa watoto ambapo wanaweza kupiga simu namba 116 ili watoto na jamii waweze kutoa taarifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hii, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto 2017/ 2018 - 2021/2022 ambapo kupitia mpango huu Serikali inatekeleza afua mbalimbali za kutoa elimu bure, kuandaa na kutoa elimu juu ya malezi chanya kupitia vitini vya malezi na makuzi na kuandaa mkakati wa mawasiliano wa kuelimisha wananchi kuachana na mila potofu.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA (K.n.y. MHE. NAJMA MURTAZA GIGA) aliuliza:-
Utaratibu wa kuweka pamoja watuhumiwa wenye makosa tofauti kama vile, wizi wa kuku, mazao, mauaji, ujambazi sugu na ubakaji ni utaratibu wa kawaida katika magereza na mahabusu zetu hapa nchini, hali kadhalika kwa wafungwa wenye rika tofauti:-
(a) Je, Serikali haioni kuwaweka pamoja wafungwa na watuhumiwa hao ni hali hatarishi kwa mustakabali wa maisha yao ya baadae?
(b) Je, Serikali haioni inapoteza nguvu kazi ya vijana wetu kwa kuwachanganya pamoja na wale wabakaji hususan vijana wa kuanzia umri wa miaka 18 hadi 30?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapokea na kuwahifadhi magerezani wahalifu wa aina zote wanaoletwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi. Sanjari na jukumu hilo, Kanuni za Uendeshaji wa Magereza za mwaka 1967 (The Prisons Management Regulations) zinaelekeza kuwa uhifadhi wa wahalifu magerezani utafanyika kwa kuzingatia utenganisho kwa vigezo vya jinsia, umri, kosa na kifungo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa katika baadhi ya magereza yetu nchini hususani magereza yenye mahabusu, suala la kuwatenganisha wahalifu kwa kuzingatia vigezo vya umri, kosa na kifungo limekuwa halizingatiwi kutokana na sababu ya msongamano wa mahabusu na uhaba wa mabweni na hivyo kupelekea mahabusu kuchanganywa na wafungwa. Hata hivyo, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeshachukua hatua mbalimbali ikiwemo kujenga magereza katika Wilaya zisizokuwa na magereza, kufanya upanuzi na kujenga mabweni kwenye magereza na kutoa elimu kwa wahalifu juu ya madhara hasi ya vitendo ya uhalifu katika jamii na kutojihusisha na vitendo hivyo katika maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda ilieleweke kwamba kitendo cha wahalifu wa aina mbalimbali kuwemo magerezani au kuchanganywa hakuhalalishi wao kuendelea na vitendo vyao vya uhalifu kwani zipo Sheria, Kanuni na Taratibu za Magereza ambazo zinakataza na zinatoa adhabu kwa mhalifu endapo atabainika kufanya vitendo hivyo akiwa gerezani. Mathalani Kanuni ya makosa Gerezani ya Mwaka 1967 (The Prison Offences Regulations).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni hii imeainisha makosa mbalimbali ambayo mhalifu hapaswi kuyafanya akiwa gerezani sanjari na hatua za kuchukua na adhabu endapo itabainika ametenda kinyume. Hivyo msingi wa kanuni hii ni kuwataka wahalifu watambue kuwa wanapaswa wajirekebishe kwa kuachana na tabia ya kufanya vitendo vya kihalifu na pia Serikali inathamini na kulinda nguvu kazi yao.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA Aliuliza:-
(a) Je, Serikali inasemaje kuhusiana na ongezeko la vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa watoto nchini?
(b) Je, kwa nini Serikali haifanyi tafiti kujua sababu za kesi nyingi kushindwa kuwatia hatiani wabakaji na kuja na mpango mpya wa kudhibiti vitendo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum yote mawili kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wa Serikali kuwalinda wananchi wakiwemo watoto dhidi ya makosa ya ubakaji na udhalilishaji. Ili kupambana na vitendo hivi Serikali imekuwa ikichukua hatua kali ikiwemo kifungo cha miaka 30 jela kwa wanaojihusisha au kusaidia kufanyika kwa vitendo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tafiti nyingi zimefanywa na asasi mbalimbali za Serikali na zisizokuwa za Kiserikali na zimebaini kwamba kuna sababu mbalimbali ambazo zinasababisha. Sababu hizi zikiwemo sababu za muhali lakini pia kuna sababu za kumalizana nje ya Mahakam ana wahanga kuchelewa kuripoti vituo vya polisi. Kwa kipindi cha mwaka 2020 jumla ya washtakiwa 1,183 walihukumiwa vifungo jela.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako tukufu naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kutoyafumbia macho matukio ya udhaliliishaji na ubakaji ikiwemo kutoa taarifa kwa vyombo vya dola vinavyohusika. Ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na Sera na Mitaala shirikishi ili kuwa na msingi wa aina moja kuanzia elimu ya maandalizi, elimu msingi na sekondari kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuongeza ufaulu zaidi kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba kuchukua fursa hii kuwatakia heri wanafunzi wetu wote wa kidato cha sita walioanza mitihani yao siku ya jana ambayo itaendelea mpaka tarehe 25. Tuna watahiniwa wa kidato cha sita 81,343 katika vituo 808 kote nchini. Sambamba na hao vilevile tuna watahiniwa 6,973 wa vyuo vya ualimu ambao nao vilevile wanafanya mitihani yao katika vyuo 75 nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana vizuri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala mbalimbali ikiwemo suala la elimu hususan katika utekelezaji wa mitaala na kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Sera na Mitaala shirikishi baina ya pande mbili za Muungano, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) hushirikiana na Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ) katika masuala mbalimbali yahusuyo utekelezaji wa mitaala. Ushirikiano huu hutoa fursa mbalimbali ikiwemo mijadala kuhusu utekelezaji wa mitaala na jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zitokanazo na ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya mapitio ya Sera ya Elimu ili kuweka uwiano wa miaka kwa Elimu ya Msingi baina ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara. Hivyo, nitoe rai kwa Watanzania wote kutumia nafasi hii ili kutoa maoni yao kuhusu mfumo huo. Ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: aliuliza: -
Kumekuwa na kawaida kwa baadhi ya Taasisi za Serikali kutotumia huduma za Shirika la Bima la Zanzibar kwa kisingizio kuwa shirika hilo siyo la Umma.
(a) Je, Serikali inalitambua shirika hilo kama la Serikali au shirika binafsi?
(b) Kama ni shirika la Serikali, nini wito wa Serikali kwa watendaji ambao wamekuwa wakikataa kutumia huduma hiyo kwa kisingizio cha kuwa siyo shirika la Serikali?
NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Bima la Zanzibar yaani Zanzibar Insurance Corporation limesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima Namba 10 ya mwaka 2009 na lina leseni hai yenye usajili Na.00000704 inayoruhusu Shirika hilo kufanya biashara ya bima za kawaida yaani Non-Life Insurance. Shirika hilo linamilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa asilimia 100. Hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua kuwa shirika hilo ni mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sio Shirika binafsi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Shirika la Bima la Zanzibar ni mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wito wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa watendaji ambao wamekuwa wakikataa kutumia huduma zake kuendelea kulitumia shirika hilo kwa ajili ya kupata huduma za bima kama ambavyo wanalitumia Shirika la Bima la Taifa hasa ukizingatia kuwa biashara ya bima nchini ni biashara Huru na Huria inayosimamiwa na Sheria ya Bima Namba 10 ya mwaka 2009 pamoja na Kanuni zake. Ahsante. (Makofi)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha somo maalum la maadili kuanzia shule za msingi sambamba na somo la afya kwa mtoto ili kukabiliana na mabadiliko ya maumbile ya hisia za mwili pindi mtoto anapoanza kukua ikiwa ni njia ya kukabiliana na tatizo la watoto kuanza kushiriki mapenzi mapema?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatambua umuhimu wa kufundisha maadili kwa mtoto ili kukabiliana na mabadiliko ya maumbile ya hisia za mwili kama njia ya kukabiliana na tatizo la watoto kuanza kushiriki mapenzi mapema.
Mheshimiwa Naibu Spika, mitaala ya elimu inayotumika kwa sasa imetilia msisitizo kuhusu masuala ya maadili katika ngazi zote za elimu. Katika ngazi ya elimu ya msingi kuna Somo la Uraia na Maadili ambalo ni somo la lazima kwa wanafunzi wote kuanzia darasa la tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, suala la mabadiliko ya maumbile ya mtoto hufundishwa katika Somo la Sayansi na Teknolojia, Stadi za Kazi, na Uraia na Maadili. Katika ngazi ya sekondari masuala ya maadili hufundishwa katika Somo la Civics Kidato cha kwanza mpaka cha nne na katika Somo la General Studies Kidato cha tano na cha sita. Masomo haya ni ya lazima kwa wanafunzi wote wa sekondari. Aidha, masuala ya afya hufundishwa katika Somo la Biologia ambalo pia ni somo la lazima kwa wanafunzi wote wa Kidato cha kwanza mpaka cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na zoezi la kuboresha mitaala kwa ngazi za elimu ya awali, msingi na sekondari. Zoezi hilo linahusisha kupokea maoni ya wadau ambayo yatazingatiwa katika maboresho ili kuhakikisha mitaala yetu inakidhi mahitaji na inawajengea wanafunzi maadili ya Kitanzania. Ahsante sana.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha masomo ya ziada ya kazi za mikono kama vile useremala, upishi, ushonaji, kilimo na ujenzi katika shule za msingi na sekondari ili kupunguza changamoto ya ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufundisha masomo ya kazi za mikono kama vile Useremala, Upishi, Ushonaji, Kilimo na Ujenzi ili kuwajengea wanafunzi stadi mbalimbali za maisha zitakazowasaidia kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutilia mkazo masomo ya ziada ya kazi za mikono katika ngazi mbalimbali za elimu. Kwa mfano, katika ngazi ya Elimu ya Msingi, Stadi za Useremala, Upishi, Ushonaji, Kilimo na Ujenzi hufundishwa katika somo la Stadi za Kazi kuanzia Darasa la Tano. Pia, masomo ya ziada ya kazi za mikono yamekuwa yakifundishwa kama masuala mtambuka kupitia vilabu vya masomo. Katika ngazi ya sekondari, stadi na maarifa haya hufundishwa katika somo la Home Economics pamoja na masomo ya ufundi yakiwemo ya useremala na ujenzi. Vilevile, somo la Kilimo hufundishwa ngazi ya sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na mapitio ya mitaala ya elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa lengo la kuboresha elimu na mafunzo yatolewayo ili yaweze kutoa stadi mbalimbali na kukidhi mahitaji ya jamii kwa maendeleo ya Taifa letu. Hivyo, nawaomba wadau mbalimbali wa elimu kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato huu kwa kutoa maoni na ushauri utakaosaidia kuboresha elimu yetu. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -
Je, nini Sababu ya kukosekana uwiano wa jinsia ya kike kwenye nafasi za uteuzi na ajira nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI NA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kunakuwepo na uwiano sawa wa kijinsia kwenye nafasi za uteuzi na ajira nchini kwa kuweka mazingatio ya usawa wa kijinsia katika nyaraka zinazosimamia Utumishi wa Umma, ikiwemo Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 inayotaka kila mamlaka ya ajira kuhakikisha uwiano wa kijinsia katika uteuzi na ajira zote. Pia Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2019, Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2009 pamoja na Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2021.
Mheshimiwa Spika, hatua hizi zimeiwezesha Serikali kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufikia uwiano sawa wa kijinsia katika nafasi za Uteuzi na ajira nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua kuwa suala hili ni kipaumbele cha Dunia kupitia ajenda 2020/2030 kuhusu Maendeleo Endelevu, Lengo Na. 5 Usawa wa Kijinsia, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameazimia kuhakikisha uwepo wa uwiano sawa wa kijinsia katika nafasi mbalimbali za uteuzi katika kipindi chake cha uongozi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, hivyo, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iko katika hatua za mwisho za kutoa Mwongozo wa Ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma. Mwongozo huu unatoa maelekezo kwa mamlaka za ajira katika utumishi wa umma kote nchini kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanakuwa na fursa sawa kuanzia katika mchakato wa ajira, upandishaji madaraja, uteuzi, mafunzo, ubadilishanaji pamoja na urithishaji madaraka. Lengo likiwa ni kuondoa vikwazo kwa kujenga uwezo wa ushindani kwa jinsia zote ili kupata sifa stahiki za kushika madaraka na fursa mbalimbali.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali isiagize kuwe na madereva na kondakta wa jinsia zote kwenye mabasi ya shule ili kudhibiti vitendo vya ubakaji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Waraka wa Elimu Na. 1 wa Mwaka 2023 imetoa maelekezo kwa wamiliki wote wa shule zinazotoa huduma ya usafiri kwa wanafunzi kuhakikisha kuwa wanakuwa na mhudumu wa kike na wa kiume katika kila basi au gari linalosafirisha wanafunzi kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Waraka huo, Wizara ilikutana na wadau wa elimu kujadiliana namna bora ya kutekeleza Waraka tajwa na tulikubaliana kwamba deadline ya kutekelezwa imefutwa. Hivyo, wadau wote wanatakiwa kujitahidi kutekeleza Waraka huo na kabla ya kupanga deadline nyingine tutapanga kikao na wadau wote kujadiliana namna ya utekelezaji. Kwa sasa tunahimiza kwamba, mabasi yote ya wanafunzi yawe na watumishi au wahudumu wa jinsia zote. Ninakushukuru sana.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itarudisha masomo ya kazi za mikono kama useremala, mapishi, kushona, kilimo, ujenzi kwa shule za Msingi na Sekondari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha taratibu za kufanya mapitio na kuboresha mitaala ya ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu. Katika maboresho hayo, fani za ufundi zaidi ya 55 zikiwemo useremala, mapishi, kushona, kilimo na ujenzi zimejumuishwa katika mitaala mipya. Hivyo, wanafunzi watapata fursa ya kujifunza kazi za mikono kupitia chaguzi za mikondo ya masomo kwa kadri ya amali watakazozipenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo haya katika ngazi ya Sekondari yatatolewa kwa kutumia mtaala wa VETA na yatatahiniwa na NACTVET kwa lengo la kuwezesha wahitimu kupata vyeti vitakavyotambulika katika soko la ajira,. Nakushukuru.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -
Je, kuna mikakati gani kuhakikisha changamoto za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi hazileti madhara nchini na lini zitapatiwa ufumbuzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimetengeneza utaratibu wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za Muungano. Serikali za (SMT) na (SMZ) zimeunda Kamati ya pamoja ya (SMT) na (SMZ) ambayo huundwa na Wajumbe wa pande zote mbili za Muungano. Katika Kamati hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza changamoto nyingi za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwa Kamati ya Pamoja ya (SMT) na (SMZ) za Kushughulikia hizi kero za Muungano za mwaka 2006, hoja 25 zimepatiwa na kujadiliwa kwa lengo la kulipatia ufumbuzi. Kati ya hoja hizo, hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja ya changamoto za Muungano. Hoja zilizobakia zipo katika hatua mbalimbali za kuzipatia ufumbuzi na kwa kuwa Serikali zetu zote mbili za SMT na SMZ zina nia thabiti na dhahiri ya dhati ya kuhakikisha mambo yote yanayoletwa na changamoto katika utekelezaji wa masuala ya Muungano yanapatiwa ufumbuzi ni matumaini yangu ya kwamba hoja hizo zitapatiwa ufumbuzi hivi karibuni. Ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -
Je, kwa nini Tamaduni za kigeni zimetawala sanaa zetu kuliko utamaduni wetu wakati BASATA ipo kuhimiza na kukuza utamaduni wetu?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kuu zinazosababisha tamaduni za kigeni kutawala kwenye sanaa zetu ni utandawazi pamoja na ukuaji wa teknolojia. Sababu hizi zimesababisha dunia kuwa kijiji hali inayotoa fursa kwa wasanii kupitia majukwaa ya kidigitali kuona mambo mbalimbali yanayofanyika duniani na kuyaiga na hivyo, kuathiri sanaa ya kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linafanya kazi ya kufufua, kukuza na kuendeleza sanaa zenye asili ya Kitanzania kupitia program mbalimbali mfano: Sanaa Mtaa kwa Mtaa na BASATA Vibes ili kutoa elimu kwa wasanii kuhusu umuhimu wa kuzienzi tamaduni zetu kupitia kazi za sanaa, kushirikiana na wadau wa sanaa kuandaa matamasha mbalimbali yanayolenga kutangaza utamaduni wetu. Hata hivyo, BASATA inaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wadau wa sanaa wanaokiuka kanuni za maadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, BASATA kwa kushirikiana na Kamati Maalum imetengeneza Kivunge cha Mtozi (Producers Kit) chenye vionjo zaidi ya 400 vya midundo ya makabila ya Kitanzania kitakachowezesha wasanii wa muziki kutumia midundo na vionjo vyenye asili ya Tanzania.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali isiweke kwenye mpango wa maendeleo wa kila mwaka kipaumbele cha kudhibiti vitendo vya udhalilishaji watoto nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imejumuisha masuala yote ya ukatili na udhalilishaji wa watoto katika Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ambapo tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa kwanza inaonesha jumla ya shilingi bilioni 30.5 zimetumika katika utekelezaji wa afua za kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na huku Serikali ikiwa imetumia shilingi bilioni 25 na wadau wa maendeleo wametumia shilingi bilioni 5.5 za fedha hizo. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha za utekelezaji wa Mpango Kazi wa Pili wa MTAKUWWA ikiwa ni jitihada za kuendelea kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hapa nchini, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja ya kuleta Muswada wa Sheria utakaotoa adhabu ya Kifo kwa wabakaji wa watoto walio chini ya miaka tisa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu cha 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 imeainisha adhabu ya makosa ya kubaka kuwa ni kifungo kisichopungua miaka 30, viboko na Mahakama inaweza kutoa amri ya kumlipa fidia muathirika wa tukio. Aidha, Kifungu 131(3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kimeainisha kuwa ikiwa muathiriki wa tukio ni mtoto mwenye umri chini ya miaka 10 adhabu pekee iliyokuwepo ni kifungo cha maisha jela.
Mheshimiwa Naibu Spika, adhabu ya kifungo cha maisha kwa mujibu wa sheria zetu ni muda wote wa uhai wa mkosaji ambayo ni adhabu ya pili kwa ukubwa ukiachilia adhabu ya kifo inayotolewa kwa makosa ya uhaini na kuua kwa kukusudia. Hata hivyo, Serikali inalichukua suala la Mheshimiwa Mbunge, kama sehemu ya maeneo ya kufanyiwa kazi na kuona kama ipo haja ya kuongeza adhabu kwa wanaobaka watoto chini ya miaka 10 au tuendelee na adhabu iliyopo ya kifungo cha maisha jela, nakushukuru. (Makofi
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali isiweke kwenye mitaala somo la uraia na uzalendo ili kizazi kijacho kiwe na uelewa wa haki na wajibu wa raia nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kutoa elimu ya uraia na uzalendo kwa kizazi cha sasa na kijacho, ilifanya maboresho ya Mitaala ya Elimu mwaka 2023, ambapo katika maboresho hayo, tayari maudhui kuhusu elimu ya uraia na uzalendo yameingizwa katika mitaala hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia somo jipya la Historia ya Tanzania na Maadili, litakalofundishwa kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Sita, somo la Historia na Maadili litabeba maudhui yanayolenga kumjenga Mtanzania kuwa mzalendo na mwajibikaji anayefahamu historia, desturi, mila na maadili ya nchi yake, nakushukuru.