Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Neema William Mgaya (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi tena ya kuweza kurudi ndani ya Bunge hili Tukufu. Lakini vilevile niwashukuru wapiga kura wangu akina mama wa Mkoa wa Njombe kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwakilishi wao, ahsanteni sana akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa taa ya ulimwengu. Hivi sasa Mataifa mbalimbali yamekuwa yakimzungumzia kwa utendaji wake wa kazi mzuri. Gazeti la New York Times nchini Marekani limemzungumzia na kumwelezea vizuri katika suala zima la uadilifu na utekelezaji wa sera aliokuwanao tangu alipokuwa Waziri kwa kipindi cha miaka 20. Pongezi sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna gazeti lingine nchini Uingereza linaitwa London Times, limeelezea jinsi wananchi wanavyomshauri Malkia Elizabeth kuwa siku ya yake ya kuzaliwa iwe siku ya usafi nchini Uingereza. Hii yote ni kwa sababu ya utendaji mzuri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ndiyo maana watu sasa hivi wanatamani ku-copy mambo yake. Hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la elimu. Naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuweza kutukeleza ahadi yake katika suala zima la elimu, kwa maana ya kwamba ada kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne imefutwa. Ni kweli sasa hivi wanafunzi wa shule ya msingi hadi kidato cha nne hawalipi ada tena. Vilevile ahadi yake ya kutoa vitabu kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha nne pia imetekelezeka. Hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali na kuijulisha kwamba dhana hii ya kufutwa kwa ada bado haijaeleweka kwa wananchi. Hivyo basi, naishauri Serikali ishuke chini kwa wananchi ili iwaeleweshe vizuri dhana nzima ya elimu bure, kwa maana ya ufutwaji wa ada kutokea shule ya msingi mpaka kidato cha nne, lakini vilevile na Serikali kuchangia vitabu kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la huduma ya afya. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipoendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais wangu kwa sababu hivi sasa tumeona ameweza kutatua kero mbalimbali katika Wizara ya Afya kwa muda mfupi sana aliokuwa madarakani. Kero kubwa ya CT-Scan katika hospitali ya Muhimbili imetekelezeka. Wananchi wanapata kipimo hiki cha CT-Scan ndani ya Hospitali ya Muhimbili ukilinganisha na zamani walikuwa wanaenda kupima kipimo hiki nje ya hospitali kwa gharama kubwa. Hongera sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeona uanzishwaji wa maduka ya madawa ya MSD ndani ya hospitali ya Muhimbili na kule Mwanza. Hivi sasa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam ambao wanakwenda kupata matibabu pale Muhimbili na wananchi wa Jiji la Mwanza wanapata dawa kwa bei nafuu. Hongera sana Mheshimiwa Rais kwa kutekeleza hilo ndani ya muda mfupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeanza kuona mabadiliko ya wafanyakazi katika hospitali, lakini vilevile na vituo vya afya. Hii inapelekea zile ziara za kushtukiza katika hospitali hizi na vituo vya afya.
Rai yangu kwa Serikali, naomba sasa Serikali ishuke, iende kwenye mikoa mingine ili iweze kutatua kero ambazo zinawakabili wananchi wa mikoa mingine katika hospitali. Mfano kule kwetu Njombe, hospitali yetu ya Njombe sasa hivi imekuwa ni chakavu sana; haina dawa za kutosha, haina wahudumu wa kutosha wala hospitali hii haina vipimo, ukizingatia kwamba hospitali hii ya Njombe sasa hivi tunaitegemea kama hospitali ya Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Halmashauri ya Njombe Mji wanatibiwa pale, wananchi wa Halmashauri ya Wanging‟ombe wote wanatibiwa pale. Namwomba Waziri, Dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, tukitoka kwenye Bunge hapa mje kuona jinsi ilivyochakaa, dawa hakuna, hatuna Madaktari wa kutosha na vipimo hakuna. Nawaomba mje kuangalia changamoto hii ili muweze kututatulia, kwa sababu sisi mkoa wetu wa Njombe ni mkoa mpya, tunahitaji kupata, hospitali ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumwomba Mheshimiwa Simbachawene kwamba katika mkoa wetu wa Njombe, tuna Wilaya mpya ya Wanging‟ombe, Wilaya hii haina hospitali ya Serikali. Wananchi wa Wanging‟ombe…
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo ameanza kutekeleza, vilevile niwapongeze Mawaziri wetu wote wa Wizara zote. Kazi mnazozifanya tunaziona, tunazidi kuwatia nguvu ili muendelee kufanya kazi zaidi. Nimpongeze pia Waziri Mkuu kwa usimamizi mzuri na kazi nzuri anayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijikite moja kwa moja kuzungumzia maendeleo ya Mkoa wa Njombe. Kwa kuwa hotuba tunayoijadili sasa hivi ni ya TAMISEMI, Mkoa wa Njombe ni Mkoa mpya na katika Mkoa huu mpya wa Njombe kuna Wilaya mpya ya Wanging‟ombe. Wilaya hii ya Wanging„ombe tuna uhaba wa hospitali hatuna hospitali ya Serikali tuna hospitali moja tu ya Ilembula ambayo ni ya binafisi, ya Kanisa hivyo basi wananchi wa Wilaya ya Wanging‟ombe wanatumia gharama kubwa sana katika matibabu. Naiomba Wizara hii ya TAMISEMI ione umuhimu wa kujenga hospitali ya Serikali ili kuweza kuwasaidia Wabena wenzangu wa kule Wanging‟ombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati zetu katika Wilaya Wanging‟ombe hazina wahudumu wa kutosha, madaktari ni pungufu kabisa hakuna madaktari, utakuta nesi anafanya kazi ya daktari naomba pia Wizara hii ya TAMISEMI iangalie umuhumu wa kuongeza wauguzi kwa maana ya madaktari katika zahanati zetu za Wilaya ya Wanging‟ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumzia suala hili la afya nataka niguse Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe. Halmashauri ya Mji wa Njombe ambayo ni Jimbo la Lupembe, pia kuna changamoto ya hospitali, hospitali hatuna kule katika ile Halmashauri. Kuna zahanati mbili tu, vituo vya afya viwili na vituo vya afya hivyo viwili havina huduma ya upasuaji. Naiomba Wizara iangalie umuhimu wa kuendelea kuboresha na kujenga zahanati zingine ndani ya Halmashauri ya Mji katika Jimbo la Lupembe. Najua wao wakiongeza zahanati nyingi basi Wizara Afya Mheshimiwa Waziri wa Afya Dada yangu Ummy Mwalimu ataleta dawa za kutosha na kuweza kuwahudumia Wabena wetu kule wa Lupembe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto pia hii ya afya ipo pia katika Halmashauri ya Makete, hospitali ni chakavu tunaomba hospitali ile ikarabatiwe, vilevile na waaguzi ni wachache katika hospitali ile ya Makete. Tunaomba sasa tuongezewe wauguzi ili wananchi wa kule Makete waweze kupata huduma vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende sasa Halmashauri ya Mji ya Njombe Mjini. Pale kuna Hospitali ya Kibena, hospitali ile ya Kibena sasa hivi inatumika kama hospitali ya Mkoa kwa sababu Wilaya zote zinategemea hospitali ile. Ninaiomba Serikali sasa ikarabati kwa haraka ile hospitali, iongeze wahudumu kwa sababu tuna changamoto bado za madaktari na baadhi ya manesi. Kwa kuwa hospitali ile inahudumia watu wengi sana tunaomba waongezeke madakitari pamoja na manesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia miundombinu ya maji katika hospitali ile ya Kibena ni chakavu, umeme ni shida, naomba Serikali iangalie kwa karibu kwa sababu hospitali ile sasa hivi ndiyo inatumika kama Hospitali ya Mkoa ukizingatia kwamba Mkoa wetu wa Njombe ni mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wanatoka umbali mrefu sana karibia kilometa 147, wale akina mama wanaotoka Lupembe kwenda kufuata huduma ya upasuaji. Ni vema basi tukaona sasa na madaktari wa upasuaji waongezeka wawe wengi ili akina mama wale wanapokwenda wasikae kwa muda mrefu pale hospitali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niende kwenye suala la elimu; tunaishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu na kuweza kutoa elimu bure kuanzia chekechea mpaka elimu ya sekondari. (Mkofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kulipongeza Bunge kwa kutambua umuhimu wa elimu na kuweza kuchangia shilingi bilioni sita iende kununua madawati. Ina maana kila Jimbo litapata madawati 600; tunatambua umuhimu wa elimu na ndiyo maana tumeweza kufanya hivyo, nipongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kule kwetu katika hizi Halmashauri zote nilizozitaja kwa maana ya Wanging‟ombe bado tuna tatizo la wafanyakazi katika shule, pia shule zilizokuwepo majengo yake ni chakavu sana yanatakiwa kukarabatiwa, miundombinu ya vyoo ni mibovu inatakiwa kukarabatiwa. Kwa mfano kule Wanging‟ombe kuna shule moja inaitwa shule ya msingi ya Mjenga ina walimu wawili tu. Kwa hiyo, bado uhaba wa walimu katika shule za msingi na sekondari bado ni changamoto kubwa sana katika Halmashauri ya Wanging‟ombe, vilevile ukienda kwenye Halmashuri ya Ludewa changamoto hii ipo katika shule 108 ni shule nne tu, ambazo zina walimu wa uhakika, lakini shule 104 zote hazina walimu wa kutosha katika Halmashauri ya Ludewa. Tunaomba pia Serikali iangalie na iweze kutatua tatizo hili. Tatizo hili vilevile liko Halmashauri ya Mji kule Jimbo la Lupembe pia kuna changamoto hiyo shule haziko za kutosha na zilizopo zipo katika hali mbaya, zinahitaji kukarabatiwa, hali kadhalika katika Wilaya ya Makete na Wilaya ya Njombe kwa ujumla. Natumaini Mawaziri wetu wa TAMISEMI watazichukua changamoto hizi kwa haraka zaidi ili kuweza kutatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie barabara ambazo ziko katika Halmashauri zote za Mkoa wa Njombe. Zile barabara za Halmshauri, nilikuwa naiomba sasa Serikali iweze kutenga pesa nyingi ili ziweze kukarabatiwa katika kiwango kizuri ili ikifika msimu h wa mvua zile barabara zisiwe zinaharibika kwa urahisi. Kwa sababu Mkoa wetu wa Njombe ni Mkoa wenye neema kama jina langu, tunalima sana kule kwa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Njombe wanashindwa kutoa yale mazao kutoka ndani kule vijijini kwa kutumia zile barabara za Halmashauri ili kukutana na zile barabara za TANROADS. Naomba Serikali izingatie hilo na iweze kutoa pesa ya kutosha katika suala zima la barabara za Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wazungumzaji wengi waliopita wamezungumzia suala la asilimia kumi. Labda tu niwambie Wabunge wenzangu na wale waliokuwa kwenye Halmashauri Madiwani wenzetu ni kwamba asilimia kumi ni lazima iende kwa wanawake na vijana kwa sababu hiyo asilimia kumi inatokana na mapato ya Halmashauri, ina maana kama hiyo asilimia kumi haijaenda kwa wanawake na vijana hiyo Halmashauri haijakusanya mapato yoyote? Hili ni jipu, Mheshimiwa Waziri hili ni jipu lazima mliangaliye kama Halmashauri inaweza kukusanya mapato lazima ile ten percent ambayo asilimia tano inaenda kwa vijana na asilimia Tano inaenda kwa wanawake lazima zipelekwe ili ziweze kusaidia akina mama pamoja na vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, nipo, nashukuru kwa kunipa nafasi naomba nami sasa nianze kuchangia Hotuba ya Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano. Nianze kwa kusema kwamba Mkoa wetu wa Njombe ni mkoa mpya, sitoacha kusema hivyo, kwa sababu tunahitaji maendeleo ili mkoa uweze kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kati ya barabara ambazo zimeshafanyiwa usanifu ndani ya Mkoa wa Njombe ni pamoja na barabara ya Njombe - Makete inayopita Mbunga ya Kitulo kwenda kutokezea Isonja, Mkoa wa Mbeya. Barabara hii iliwekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi namba moja, lakini vilevile barabara hii iliwekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2005 mpaka mwaka 2010 iliwekwa tena upya. Hiyo haitoshi, barabara hii Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati anakuja kuomba kura za Urais kule Makete na Wilaya ya Wanging‟ombe alisema kwamba barabara hii ndiyo ya kwanza ambayo itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali itekeleze ahadi ya Mheshimiwa Rais, barabara hii ina umuhimu mkubwa sana kwa sababu, barabara hii kama itatengenezwa kwenye kiwango cha lami itainua uchumi wa Taifa, katika zao la Pareto, lakini vilevile katika masuala ya utalii. Sisi kule Makete kuna Mbuga ya Kitulo kwa sababu barabara hii imepita kwenye mbuga ya Kitulo, sasa hivi watalii wanashindwa kwenda kwa wingi kwenye ile mbuga ya Kitulo kwa sababu barabara ile haipitiki. Hasa kipindi cha mvua ndiyo haipitiki kabisa. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kujenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kule katika barabara ile pia kuna mazao ambayo yanasafirishwa ya mbao, viazi mnavyokula Dar es Salaam vinatoka Makete. Barabara hii ina umuhimu mkubwa, naiomba Serikali iweze kujenga barabara hii. Vilevile ndani ya Mkoa wa Njombe bado kuna barabara nyingine ambayo imefanyiwa usanifu, barabara ya Njombe-Mdandu-Iyayi ambayo nayo inakwenda kukutana na Mkoa wa Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara hii wakazi wa Wanging‟ombe wanaolima mazao ya alizeti pamoja na mbao wanashindwa kusafirisha kwa urahisi kupeleka Mbeya, lakini vilevile wanashindwa kusafirisha kwa urahisi kuja Njombe ili kwenda mikoa mingine kama Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna barabara nyingine ambayo imefanyiwa usanifu, barabara ya Njombe - Ludewa, Manda – Itoni. Barabara hii ni muhimu kwa sababu kule Ludewa kuna makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma. Naiomba pia Serikali ikamilishe barabara hii kwa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara yote ili kuweza kusafirisha makaa ya mawe kwa urahisi.
Mheshimwia Spika, pia tuna barabara ya kibena - Lupembe-Madete ambayo inaunganisha Mkoa wa Morogoro, tunaomba pia barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami. Nakumbuka asubuhi Mheshimiwa Hongoli aliuliza swali na Mheshimiwa Waziri alisema kwamba, barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami mwaka 2016 - 2017. Ukienda kwenye hotuba ukurasa wa 37 inasema kwamba Lupembe-Madete Kilometa 125 taratibu za kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu zinaendelea. Nimwambie tu Mheshimiwa Waziri, stage hii ilishapita, nilitegemea sasa hivi watatuambia kwamba labda tender inatangazwa kwa ajili ya kujenga barabara hii.
Mheshimiwa Spika, nina ombi moja kwa Serikali kuhusiana na Jimbo la Lupembe. Lupembe kuna barabara ambayo inatoka Lupembe-Lukalawa, inapita Ikonda kutokea Makambako. Barabara hii ni business road, kuna wakulima wanasafirisha sana mbao, maharage, pamoja na chai. Naomba sasa barabara hii itoke katika ngazi ya Halmashauri ipelekwe iwe barabara ya TANROAD, ili iweze kujengwa kwenye kiwango cha lami kwa uharaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoke kwenye barabara niende kwenye kiwanja cha ndege. Mkoa wetu wa Njombe kiwanja chetu cha ndege cha Njombe kina hali mbaya sana. Kwa nini naomba kiwanja hiki? Ruvuma hakuna kiwanja cha uhakika cha ndege, lakini kama tutakarabati kiwanja kile cha ndege cha Njombe na kuweka kwenye kiwango cha lami ina maana ndege nyingi sana zitakuja. Kwa hiyo, Mkoa jirani wa Ruvuma watafaidika na kiwanja kile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, istoshe kule Njombe tunalima zao la maua haya, tunalima maua mazuri sana, kuna roses nyingi sana kule, tunashindwa kusafirisha kufikisha Dar es Salaam zikiwa fresh kwa sababu hatuna kiwanja cha ndege cha uhakika, hakuna ndege zinazokuja mkoani pale. Hivyo inasababisha kulega lega kwa kilimo hiki cha maua. Naiomba sasa Serikali ione umuhimu wa kiwanja hiki, wakarabati katika kiwango cha lami ili na sisi tuweze kusafirisha maua kwa wingi kuja Dar es Salaam na kwenda nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika nimalizie kwa kuipongeza Serikali kwa mradi wa DART, mabasi yaendayo haraka. Naipongeza Serikali kwa kuweza kutengeneza mradi mkubwa kama huu ambao umegharamia takribani bilioni 322. Hata hivyo, katika mradi huu bado kuna upungufu mwingi sana, kitu cha kwanza nilichokuwa naiomba Serikali ihakikishe kwanza lile suala la hisa. Suala la hisa halijakaa vizuri kwenye mradi huu, Serikali irudi iende ikaangalie kwa umakini jinsi gani ya utaratibu wa hisa. Vilevile nashangaa kwa nini mradi huu hauanzi? Mradi umetumia gharama kubwa sana, bilioni 322, uanze kufanya kazi ili wananchi waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna vituo ambavyo havijakamilika katika mradi huu, kituo cha Kimara pale mwisho, kuna kituo cha Ubungo Terminal, kituo cha Morocco, kituo kule Posta ya zamani. Vituo hivi viko wazi, ni hatari kama mradi utaanza ina maana watu watakuwa wanaingia kwenye mabasi bure. Naiomba Serikali sasa iangalie umuhimu wa kukamilisha vituo hivi na Serikali iwape fedha huu mradi uweze kukamilika ili uweze kutumika.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Vilevile namshukuru Mungu kwa kuweza kunipa afya bora na kuweza kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu kuchangia hotuba hii ya bajeti kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumzia suala la afya, nasikitika kusema kwamba sijaona mkakati mahsusi wa kujenga zahanati pamoja na vituo vya afya. Tuko katika mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapunguza vifo vya akinamama wajawazito. Najiuliza tunawezaje kupambana na vita hii ilhali hatuna facilities za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Katika bajeti hii nimeona Hospitali za Mikoa ndiyo ziko chini ya Wizara lakini kiuhalisia watu wengi wapo kwenye Kata na kwenye Halmashauri zetu. Watu waliokuwa kwenye Kata, kwenye vijiji vyetu macho yao yanakuwa yanatazama zahanati zao na vituo vyao vya afya ambavyo viko kwenye Kata na kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua Kanuni ya 106 inasema kwamba Mbunge hataruhusiwa kupendekeza mabadiliko yoyote katika makadirio na mapato ya bajeti ya Serikali, lakini naiomba Serikali kwa bajeti inayokuja iweze kuliangalia vizuri suala la zahanati na vituo vya afya viwekwe katika Serikali Kuu ili tuweze kuviboresha na kuvijenga kwa ufanisi mkubwa ili kuweza kutatua tatizo lile la vifo vya akinamama wajawazito ambapo wengi wao wako kwenye Kata huko kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niishauri Serikali, ni vyema kuweka pesa nyingi katika Mfuko wa Maji kwa sababu tatizo la maji ni kubwa sana Tanzania na anayeteseka katika matatizo ya maji ni sisi wanawake. Akinamama wa mkoani kwangu kule, akinamama wa Kata za Saja, Kijombe, Wanging‟ombe, Mkongobaki, Nkomang‟ombe, Ludewa Mjini, Ludewa Vijijini pamoja na Njombe Mjini kuna shida sana ya maji kwa muda wa miaka mingi. Ni vyema Serikali itambue umuhimu mkubwa wa kuweka pesa nyingi katika Mfuko wa Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba nizungumzie suala la utalii. Wenzetu wa Kenya wametoa kodi katika suala la utalii lakini sisi Watanzania tumeamua kuweka kodi katika suala la utalii. Kiuhalisia sisi Tanzania mshindani wetu mkubwa katika suala la utalii ni Mkenya. Wenzetu Wakenya wana ndege ya moja kwa moja kutoka Europe na America kwenda Kenya na mtalii anapotumia ndege hiyo anapata ahueni ya pesa katika tiketi karibu asilimia 45 ya air ticket. Hiyo ni advantage kwa wenzetu wa Kenya kwa sababu watalii wengi watakuwa wanataka kwenda Kenya kwa ajili ya ku-save hizo costs za air ticket na mambo mengine. Kabla hatujaweka asilimia 18 bado utalii wetu wa Tanzania ulikuwa wa gharama kubwa ukilinganisha na wa Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mtalii kabla hajaamua kuja vocation huwa analipa in advance, mwaka mmoja kabla au miaka miwili kabla. Kwa kuweka kodi hii kutatokea usumbufu kwa wale watalii ambao tayari walishalipa hela zao kuja kutalii kwa mwaka huu wa fedha 2015/2016 na ikiwezekana 2017. Kwa mkanganyiko huo, kuna uwezekano mkubwa wa watalii wengi kuahirisha na kutaka pesa zao warudishiwe kwa sababu wanaona kwamba mimi nilishajipanga bajeti yangu ya vocation ni kiasi hiki na sasa hivi naambiwa kwamba niongeze asilimia 18 ya pesa ambayo ilikuwa haiko kwenye bajeti yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara iangalie suala hili la utalii katika masuala mazima ya ushindani wa utalii baina yetu sisi na watu wa Kenya, huenda tukasababisha watalii wengi waache kuja Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ile wanaita msafara wa nyumbu wanaokuwa wanazunguka Kenya na Tanzania, migration ya wanyama. Nina wasiwasi wanaweza watalii hawa wakawa wanasubiri wanyama wakifika Kenya ndio waende badala ya kuja kuangalia kwetu Tanzania wakati sisi tuna advantage kubwa wakati wanyama wanasafiri miezi ya saba ndiyo kipindi ambacho nchi nyingi za Ulaya wanakuwa wako kwenye holiday na wanatumia muda huo kuja kutalii Tanzania. Naomba Serikali iangalie ili tusiweze kupoteza mapato katika suala la utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika bajeti zilizopita imeonesha kabisa kwamba utalii unachangia asilimia 25 ya mapato ya Tanzania. Kwa nini leo tuisumbue sekta hii na twende katika kushusha mapato hayo? Naomba Serikali iangalie kwa umakini kwa sababu asilimia 25 ya kuchangia kwenye mapato ni asilimia kubwa sana, tuiangalie kwa umuhimu wa kipekee ikiwezekana hii kodi tuitoe ili tusiweze kukosa watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie suala la kiinua mgongo. Najua Serikali ina dhamira njema ya kuongeza mapato katika bajeti yetu, lakini nashangaa katika category ya watu tisa akiwemo Makamu wa Rais, Prime Minister, Chief Justice, High Court Judges, Maspika, Supreme Court Judges, Regional Commissioners na hawa Wakuu wa Wilaya, kwa nini wame-single out Mbunge tu ndiyo akatwe kodi ya kiinua mgongo ilhali katika hilo group hao watu wote nao wanatakiwa waingizwe kwenye kukatwa makato haya. Kama kweli Serikali ina nia ya dhati na hawa watu wengine wote wakatwe au labda kama kuna kitu kimejificha tunaomba Wabunge tukijue hicho kitu ni kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge tuna mzigo mkubwa, Wabunge tunahudumia watu wengi huko vijijini kwa hela hiyo hiyo, Wabunge tunapeleka watu hospitalini, tunahudumia misiba, harusi, wagonjwa, kwa kipindi hiki cha Ramadhani Wabunge ndiyo hao hao ambao wanasaidia kule watu wengine ambao hawajiwezi katika masuala mazima ya kuhakikisha kwamba wanafuturu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iwaangalie Wabunge kwa jicho la huruma na hatuna nia mbaya kwamba hatutaki kuchangia mapato kwa sababu katika mishahara yetu tunakatwa kodi. Naomba sasa watuangalie na sisi ili tujue ni jinsi gani ya kurudi humu ndani na tuendelee kuwahudumia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.