Contributions by Hon. Rose Cyprian Tweve (18 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuchangia, naomba kwanza kuanza kwa kutoa shukurani. Moja kwa Mwenyezi Mungu; pili, kwa wazazi wangu; baba yangu na mama yangu, kwa kunilea, kunisomesha na zaidi ya yote kwa kunipa ujasiri mpaka nimeweza kufika hapa leo. Baba na mama nawashukuruni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nachukua fursa hii kuwashukuru akinamama wote wa Mkoa wa Iringa kwa kunidhamini, kwa kuniamini niwe mwakilishi wao. Kweli mmenipa heshima kubwa sana. Naomba mwendelee kuniombea Mwenyezi Mungu anipe nguvu, hekima na busara ili tuweze kushirikiana vyema tuisaidie Iringa yetu iweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, pia nitoe pongezi zangu kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa na ngumu anayoifanya kwa kujitoa muhanga, awe kimbilio, awe macho ya maskini na wanyonge. Mheshimiwa Rais, nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa niaba ya wanawake wote wa Mkoa wa Iringa, namshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kumchagua Mama yetu Samia, kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii inadhihirisha anatutambua sisi wanawake, anatambua mchango wetu kwa nchi hii na anataka tuendelee kushiriki kikamilifu katika maamuzi yatakayohusu Serikali ya nchi yetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais tunakushukuru sana. Mama Samia hongera sana; najua utatuwakilisha vyema na sisi wanawake wa Tanzania tupo nyuma yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja, niunge mkono hoja iliyoletwa mbele yetu na Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji. Natambua kuwa Serikali yetu inajipanga kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda ili tuweze kupambana na hili tatizo sugu la ajira na umaskini hasa kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kuwa asilimia 75 ya Watanzania, wanategemea aidha kilimo, uvuvi na ufugaji. Sasa wakati Mpango wa Maendeleo umeletwa hapa kujadiliwa, wengi tulishauri kuwa corner stone ya huu uchumi wa viwanda, viwe vikubwa au vidogo lazima vitumie raw materials ambazo zitakuwa zinazalishwa na hawa wakulima wadogo wadogo ambao wanatoka vijjini. Lengo lilikuwa, kusaidia kupata soko na ku-add value ya hizi hizi raw materials ambazo zitakuwa zinazalishwa na hawa wakulima wadogo wadogo. Kwa kufanya hivyo, tutasaidia kuinua uchumi wa wakulima na kuisaidia Tanzania iweze kufika kwenye huu uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi kama Malaysia na India, zilikuwa nchi maskini. For example Malaysia was one of the poorest country kuliko hata Tanzania, lakini wenzetu wameweza kupiga hatua na sekta ambayo imeweza kuwafikisha hapo ni Sekta ya Kilimo. Waliwatengenezea mazingira mazuri wakulima hawa wadogo na wafugaji wadogo wadogo. One of the things they did ni kutengeneza hizi collection centers; zikawa ni kiunganaishi kati ya wafugaji, wakulima na viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi collection centres zinasaidia huyu mfugaji au mkulima anapoamka asubuhi wazo lake kubwa ni kuzalisha na siyo soko la mazao yake; lakini hapa Tanzania bado kidogo tuko nyuma. Kwa mfano, mifugo; Tanzania is one of the leading countries kwenye mifugo, lakini bado tuna-import maziwa kutoka nchi nyingine. What is problem here? Hatuna viunganishi, hatuna collection centers ambazo zitawaunganisha hawa wafugaji na viwanda vilivyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano kidogo tu. Pale Mkoani kwangu Iringa tuna kiwanda kikubwa cha Asasi, kina-process products nyingi zinazotokana na maziwa; mengine tunatumia hapa kwenye restaurant yetu ya Bunge, naomba mwendelee kutuunga mkono. Kiwanda hiki kinaweza ku-process lita 100,000 kwa siku, lakini mpaka leo hii kinapokea maziwa lita 15,000; na hizi zitoke Mikoa mitatu; pale Iringa, Njombe na Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha zaidi, pale Iringa kuna wafugaji ambao maziwa yanaozea ndani. Tatizo hapa ni nini? Ni kile ambacho nimesema kwamba hatuna viunganishi, hatuna collection centers ambazo zitawaunganisha hawa wafugaji na hiki kiwanda kilichoko pale. Kwa hiyo, Waziri Mheshimiwa Mwigulu nakuomba, umefanya kazi kubwa kwenye Mkoa wangu wa Iringa, naomba ufike pale tuwe kiunganishi, tuwatengenezee hizi collection centers kwenye Wilaya yangu ya Mufindi, Wilaya ya Iringa Mjini, Iringa Vijijini na Kilolo. This will be a win-win situation. Tutakuwa tume-create soko kwa wale wafugaji wadogo wadogo na pia tutam-assure raw material huyu mwekezaji ambaye amefungua kiwanda pale Mkoa wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho ningependa kushauri, tu-invest kwenye elimu. Wakati TAMISEMI wanawasilisha bajeti yao, ilionesha kuwa kuna hawa Maafisa Ugani, less than fourteen thousand, kuna thirteen thousand five hundred and thirty two. Hii ni namba ndogo and this can be easily solved.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna watoto wengi ambao wamemaliza Shule za Kata, tuwape incentives. Hizi ruzuku tunazotoa kwenye pembejeo, tuhakikishe tunawekeza kwenye elimu. Hawa Maafisa Ugani ndiyo watakaokuja kuwa Walimu wa kuwafundisha huyu bibi na babu kwa sababu lengo ni kuhakikisha hii asilimia 75 inaendana na huu uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Waziri wa fedha kwa kutambua unyeti wa Sekta hii ya Kilimo akaahidi kutoa nyongeza ili iweze kutusaidia kufikia malengo ya uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nihitimishe kwa kusema yafuatayo:-
Tanzania ya viwanda inawezekana, Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana; uzuri Sekta hii imepewa Waziri Mheshimiwa Mwigulu aliye makini, ambaye yuko competent, ambaye atatufikisha pale tunapotaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia kwenye Wizara hii nyeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja niunge mkono hoja iliyoletwa mbele yetu leo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Sote tunatambua Tanzania kuna uhaba mkubwa wa Walimu hususani kwenye masoma ya Mathematics na English. Tanzania hatuna Chuo cha Ualimu kinachoandaa Walimu wa English watakaofundisha shule za msingi. Maana yake kuna 100% lack of trained English Medium Primary School Teachers.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Teachers Colleges za Primary Schools zinafundisha kwa Kiswahili. Sasa changamoto inakuja kwamba, pamoja na kuwa Wizara ya Elimu inatambua mapungufu hayo hakuna coordination na Wizara zingine kama Wizara ya Kazi.
Wizara ya Kazi ina charge $500 kutoa class B work permit regardless wewe ni Mwalimu au ni Injinia wa Dangote Cement au Barrick Gold Mine. Kinachosikitisha zaidi, Wizara ya Mambo ya Ndani yaani Uhamiaji wao wanatoza $2000 fee ya resident permit kwa hawa Walimu ambao tunawahitaji sana. Hii fee imeongezwa kutoka $600 iliyokuwa wanatozwa mwanzo mpaka $2,000 kwa sasa na hii fee ya $2,000 ni kwa miaka miwili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli Taifa letu linataka kusaidia watoto wetu, napenda nishauri yafuatayo:-
(i) Hizi fee zifutwe ili kuvutia kupata Walimu bora watakaoweza kufundisha vijana wetu; na
(ii) Tuwape support ya kutosha hawa ndugu zetu wenye private schools wakati Serikali yetu inaendelea kuboresha hizi government schools kwa sababu utafiti unaonyesha private schools ndizo zinatoa elimu bora zaidi kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, naomba maslahi ya Walimu wetu yaboreshwe ili kuwapa motisha ya wao kuendelea kuwasaidia vijana wetu. Pia tuhakikishe shule za msingi wanapewa madawati ya kutosha hususani Mkoa wangu wa Iringa watoto wetu bado wanakaa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hoja iliyoletwa mbele yetu siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri sana. Vilevile nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Wizara hii. Hii inadhihirisha kuwa Wizara imepata Waziri pamoja na Naibu Waziri walio makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niende moja kwa moja, niunge mkono hoja iliyoletwa mbele yetu. Natambua kuwa Serikali yetu imefanya mambo mengi na inaendelea kuhakikisha kuwa utamaduni, sanaa na michezo inapewa kipaumblele hasa kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya msingi ningependa kuishauri Serikali. Kwanza tuhakikishe kwamba sanaa na michezo inapewa kipaumbele toka shule za msingi. Lazima tuhakikishe vijana wetu wanapewa vifaa vya michezo na sanaa. Shule nyingi hazina viwanja vizuri vya michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuhakikishe tunawekeza kupata walimu wazuri wa kuwafundisha hawa vijana wetu. Lazima sisi kama Taifa tuhakikishe tuna academy kuibua vipaji vya vijana wetu katika michezo mbalimbali kama vile basketball, volleyball, mbio na sanaa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo tutajihakikishia Taifa letu litakuwa na uhakika wa kuwa na vijana ambao wataweza kushindana na mataifa yaliyoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu iliyoletwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Mheshimiwa Spika, tatizo la maji limekuwa ni changamoto kubwa kwa Taifa letu hususan, Mkoa wangu wa Iringa.
Mheshimiwa Naibu Spika, shida hii ya maji inamgusa mwanamke moja kwa moja. Wanawake wamekuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji badala ya kujitafutia maendeleo yao ya kiuchumi. Tatizo hili la maji si tatizo mjini tu, bali vijijini nao wamesahaulika kwa muda mrefu. Ili nchi yetu iweze kufikia malengo ya Tanzania ya uchumi wa kati lazima tuhakikishe hii nguvu kazi (wanawake) ambao ndio wazalishaji wakubwa tunawaondolea adha hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, naomba tuongeze tozo ya sh.50 kwa lita, ili tuwe na chanzo chenye uhakika. Kama hii haitawezekana, basi tupunguze kwenye other sources kama Road Funds na REA. Nina imani kubwa na Serikali na Wizara kuwa watapokea ushauri wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Naomba niende moja kwa moja, niunge mkono hoja ambayo imeletwa leo hapa mbele yetu na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri Lukuvi na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya kuongoza na kusimamia wizara hii nyeti. Matunda ya kazi yao kweli yanaonekana, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, personally naomba nimshukuru Mheshimiwa Lukuvi kwa kuwa mfano wa kuigwa hasa kwangu mimi nikiwa kijana kiongozi. Amedhihirisha ni jinsi gani tunatakiwa kuwajibika pale tunapopewa majukumu yetu, ahsante sana Mheshimiwa Lukuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Ardhi ya kuhakikisha Watanzania wanapata hati zao na kutatua hii migogoro inayojitokeza katika maeneo mbalimbali, napenda kushauri suala la elimu ya ardhi litiliwe mkazo. Watanzania lazima watambue haki na thamani ya ardhi yao. Hili limekuwa ni tatizo kubwa linaendelea kujitokeza hususan kwenye Mkoa wangu wa Iringa. Kumekuwa na wajanja wachache ambao wanafika kwenye maeneo ya vijijini na kuwashauri hawa wanavijiji kuwauzia haya maeneo, moja kwa bei ya chini na pili wengine wamediriki kuwashawishi hadi kuuza maeneo yao yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea hawa wanavijiji wanakosa hata maeneo ya kuzalisha mazao ambayo yanaweza kuwasaidia wao kuendelea kupambana na kukidhi mahitaji ya familia zao. Kwa hiyo, hili suala la elimu Mheshimiwa Lukuvi naomba tulipe kipaumbele sana. Hii elimu isitoelewe tu kwa wale wanakijiji lakini hata hawa wawekezaji wanaokuja kununua haya maeneo kule vijijini waambiwe kuwa wanapopewa yale maeneo wahakikishe hawa wananchi wanaachiwa eneo ambalo wataendelea kuzalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nakazania hii elimu? Tumesema tunataka Tanzania sasa iwe nchi ya viwanda na wote tulikubaliana kuwa hawa wakulima wadogo wadogo, hii asilimia 75 ambao wako kijijini wanaotegemea kilimo ndiyo wangetumia hiki kilimo kuzalisha raw materials ambazo zitapelekwa kwenye hivi viwanda. Kama haya maeneo yote yatakuwa yamebebwa na hawa watu chache, tutakapoanzisha hivi viwanda watakaonufaika ni wale ambao watakuwa na maeneo makubwa ya kuzalisha hizi raw materials na hii dhana nzima ya kuwasaidia hawa wakulima wadogo wadogo waweze kufikia ule uchumi wa kati itakuwa ni vigumu kufikiwa. Kwa hiyo, naendelea kusisitiza lazima suala la elimu lipewe kipamumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la hati miliki hasa hizi za kimila limechangiwa kikubwa sana na Wabunge hapa ndani na mimi ningependa niongezee. Naomba hizi hati miliki za kimila zipewe uzito na ziwe zinatambuliwa kisheria. Hata nchi za wenzetu zilizoendelea, mtu anayemiliki ardhi anapewa heshima kubwa na hiyo heshima inatokana na kuwa ile hati yake popote anapokwenda, hata kwenye hizi financial institutions anaweza kukopesheka lakini hapa nyumbani kwetu bado ni changamoto kubwa sana hususan kwa wanawake. Sisi ni asilimia kubwa hapa nchini, population yetu ni zaidi ya asilimia 51 lakini ni asilimia 19 tu…
MWENYEKITI: Ahsante, kwa heri, dakika tano zako zimekwisha mlikubaliana kugawana dakika na mwenzako Mheshimiwa Juliana Shonza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa muda huu mfupi niliopewa nitakuwa na jambo moja tu la kulielezea, nalo ni hali halisi ya balozi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na takribani wiki mbili zimepita tulipata fursa ya kutembelea Balozi mbalimbali ikiwemo Sweden, South Africa na Maputo. Mimi binafsi nilipata kutembelea Ubalozi wa Maputo, kwa hiyo, saa hizi nitaelezea hali halisi ambayo tumeiona kwenye Ubalozi wetu na mradi ambao unaendelea pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mchango mkubwa ambao Taifa letu liliutoa kwa nchi ya Msumbiji, Serikali hiyo ilitupa jengo la Ubalozi, nyumba ya Balozi na uwanja ambao uko mkabala na jengo hili la ghorofa tisa. Mwaka 2012 Serikali iliamua kufanya matengenezo ya Ubalozi huu kwa sababu hili jengo limeanza kutumika toka mwaka 1975. Sasa kwa kuwa mradi huu ulikuwa viable tukapitisha kuwa jengo hili lifanyiwe ukarabati. Mradi huu umechukua muda mrefu sana, sasa hivi ni takriban miaka mitano na imeisababishia Serikali hasara kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi tunatumia dola za Kimarekani 240,000 kila mwaka kuhakikisha tunalipia nyumba ya Balozi na watumishi kwa ajili ya kuendesha shughuli za Ubalozi nchini Msumbiji. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, you know this is not reflecting well on our part. Haiwezekani tukawa tumepewa jengo, tumepewa kiwanja, tumepewa nyumba ya Balozi na sisi tunaendelea kupoteza pesa hizi kila mwaka kulipia pango.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, wewe umekuwa ni mwanadiplomasia mzuri, nakuomba, hizi pesa ambazo zinaombwa kuhakikisha tunamaliza jengo hili zipelekwe kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tuko Msumbiji tuliweza kuonana na Mkandarasi akasema anadai dola za Kimarekani 888,000. Akipewa pesa hizi, ataweza kukamilisha jengo hili within two months. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kulinda heshima ambayo nchi ya Msumbiji ilitupa Tanzania, tuhakikishe tunaendeleza hata kile kiwanja ambacho kiko pale. Kama Serikali inashindwa kujenga kiwanja hiki, basi iwashirikishe Shirika la Nyumba waweze kwenda ku-develop lile eneo kwa sababu demand ya real estate Mjini Maputo ni kubwa sana. Tukimaliza ghorofa hili tuna uwezo wa kuiingizia Serikali shilingi milioni 600 kwa mwaka ambayo itatusaidia sisi ku-service ule Ubalozi wetu na kusaidia balozi mbalimbali ambazo zinazunguka Kusini mwa Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo haya, namwomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe ule Ubalozi wa Msumbiji unatengenezwa kwa wakati, image yetu pale haionekani vizuri. Nina uhakika miezi miwili ijayo tutaweza kufungua Ubalozi huu ili uweze kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia siku ya leo. Kwa kuwa hoja iliyoletwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2016/2017 inagusa maslahi mapana ya wananchi wa Mkoa wa Iringa hususani wanawake ambao wameniwezesha kufika hapa leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa Wabunge wanaowakilisha wananchi wa Mkoa wa Iringa. Sasa ndani ya huu Mkoa wa Iringa tunahifadhi kubwa ya Msitu wa Taifa wa Sao hill. Kwa muda huu niliopewa nina jambo moja kubwa ambalo nitalizungumzia, ni suala zima la TFS na utaratibu mzima wa utoaji wa hivi vibali vya kuvuna msitu wa Sao hill. Hili limekuwa ni tatizo kubwa sana. System nzima ya utoaji wa hivi vibali haieleweki. Vibali hivi vimekuwa vinawanufaisha wachache. Watanzania ambao ni wazawa, wavunaji wadogo wadogo, kundi la akinamama, vijana na walemavu hawapewi kipaumbele. Hawa wazawa ndiyo waliolima msitu huu, hawa ndiyo wameweza kuutunza huu msitu mpaka umefikia hapo ulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka Serikali inatoa cubic meter 600,000 kwa Watanzania waweze kuvuna msitu huu. Hapa ndipo nina tatizo napo na ndipo panaposikitisha. Watanzania hawa ambao ni wazawa hawanufaiki na huu mgao, ni wawekezaji ambao wanapewa kipaumbele kuweza kunufaika na huu msitu. Nitatoa mfano mmoja, tuna hawa Wawekezaji ambao wamepewa kuendesha Kiwanda cha Mgololo, wanajiita RAI-Group. Hawa ndio wamekuwa beneficiary wakubwa wa huu mgao wa vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii 600,000 inayotolewa na Serikali RAI-Group wanapewa cubic meter 250,000 na kinachosikitisha zaidi, hawa RAI-Group wanalipa nusu ya bei ambayo wanatakiwa kulipia vibali hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibali kimoja, Mtanzania, Mwanairinga, Mwanamufindi analipa sh. 28,000/=, RAI-Group wanalipa sh. 14,000/= tu. Sasa ukipiga mahesabu kutoka kwenye hizo cubic meter 250,000 wanazopewa, ukizidisha mara hiyo Sh. 14,000/= maana yake wanalipa bilioni 3.5 kwa mwaka. Sasa wangeweza kulipa hiyo Sh. 28,000/= ambayo Mtanzania wa kawaida analipa, Serikali ingeingiza bilioni saba kwa mwaka. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri anipe maelezo, ni vigezo gani wanatumia kuwapunguzia bei hawa RAI-Group na ni vigezo gani wanafanya hawa Watanzania waendelee kulipa hii Sh. 28,000/=? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nipewe maelezo ni kwa sababu gani hawa RAI-Group wanapewa kipaumbele? Wanapewa hizi cubic meter 250,000 wakati hawa Watanzania wa kawaida Wanairinga hawawezi kunufaika na msitu huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa nipewe ufafanuzi wa ukusanyaji wa kodi kutoka kwa hawa wawekezaji wa hiki Kiwanda cha Mgololo. Cha kusikitisha zaidi hawa RAI-Group wanapasua haya magogo, wanatengeneza hizi raw materials wanapeleka Kenya, wanaenda ku-process makaratasi ndipo waturudishie sisi hapa kununua wakati haya makaratasi yangekuwa processed hapa Tanzania, tungetengeneza ajira kwa vijana wetu. Kwa hiyo, naomba majibu yanayonitosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa RAI-Group walishakuwa na Kiwanda Malawi, wamefukuzwa wamekuja hapa, sasa sisi tunawa-protect, moja tuwape vibali vingi, mbili bei ya chini, hii kweli inahuzunisha, inatukatisha tamaa sisi Wanairinga, inatukatisha tamaa sisi Wanamufindi, naomba tulifanyie kazi hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, hawa RAI-Group wapande misitu yao na kama bado wataendelea kupanda msitu huu wa sao hill basi walipe bei moja sawa na Watanzania. Hata kama wakilipa bei hiyo moja lazima hivi vibali vipunguzwe, viende kwenye makundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua asilimia kubwa ya wanawake na vijana sasa hivi wako kwenye hivi vikundi vya ujasiriamali. Tatizo la hivi vikundi ni maskini, havina pesa, hakuna miradi endelevu ambayo ingeweza kuwasaidia wao kuendelea kupambana na hizi changamoto zao za kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri angewawezesha hawa vijana, angewawezesha hawa akinamama katika Wilaya zote, Iringa Mjini, Iringa Vijijini, Kilolo na Mufindi waweze kutumia hivi vibali angekuwa; moja, amewainua kiuchumi; pili, hivi ndivyo vitakavyokuwa vikundi darasa vya kuwashawishi watu wengine waendelee kupanda miti kwa sababu watakuwa wameona matunda na benefits ambazo zinatokana na upandaji na upasuaji wa miti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa RAI-Group tunawapa vibali vikubwa. Hawajihusishi na mambo yoyote ya kijamii, barabara mbovu, madawati watoto wanakaa chini, kuna manufaa gani ya kuendelea kuwashikilia watu hawa wakati pale Mufindi tuna wavunaji wazuri wana viwanda, wamekuwa msaada mkubwa kuchangia madawati, kuchangia hospitali, hebu tuwape kipaumbele watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri please, doesn’t get me wrong. Najua ndiyo umepata kuongoza Wizara hii, so prove to me kuwa unakasirishwa na jambo hili, tuwapiganie Watanzania wetu waweze ku-enjoy matunda ya nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, after all Mheshimiwa Waziri tunasema tunataka Tanzania iende katika uchumi wa kati, Wizara hii ina nafasi kubwa ya kuwainua hawa wananchi, tuwawezeshe, tuwape kipaumbele hii ita-trickle down sasa tukiendelea kuwashikilia hawa RAI-Group tunawapa vibali cubic meter 250,000, hawa wengine hawanufaiki tutafikaje huko, lazima tuwaonjeshe matunda ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti sasa kwa kumalizia namwomba Mheshimiwa Waziri, najua yeye ni msikivu, he is competent. Naomba tufike Mufindi, hawa wavunaji wanajua matatizo ya hivi vibali, wanajua solution ya kuweza kutatua hili tatizo…
MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia tena siku ya leo. Naomba nianze kwa kutoa pongezi zangu za dhati kwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mpango na Naibu Waziri Mheshimiwa dada yangu Ashatu, kwa kuandaa na kuwasilisha bajeti hii elekezi kwa mwaka wa fedha 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ni ya kuungwa mkono kwa sababu kwa mara ya kwanza kabisa kama Waziri wa Fedha alivyosema asilimia 40 ya hii shilingi trilioni 29.53 inategemewa kujielekeza katika miradi ya maendeleo. Kama kweli bajeti hii itakwenda kama ilivyopangwa na kama kweli mipango na malengo tuliyoyaweka yatakwenda kama yalivyopangwa, basi Serikali hii ya Awamu ya Tano ina nafasi kubwa ya kubadilisha maisha ya Watanzania na kuwajengea tena imani ambapo tunatambua karibu watu milioni 10 wanaishi katika hali ya umaskini hususani wanawake, watoto na vijana wetu. Kwa hiyo, namuunga mkono sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niongelee suala la TRA, mimi binafsi naunga mkono TRA waende kwenye hizi Halmashauri zetu na kukusanya mapato haya. Naziomba Halmashauri za Mkoa wangu wa Iringa watoe ushirikiano wa kutosha na nina sababu zangu za msingi.
Moja, tunatambua kabisa Halmashauri zetu hazina watumishi na wataalam wa kutosha wa kuweza kukusanya mapato haya kwa wakati na kwa kiasi kinachotakiwa.
Pili, kama ripoti ya CAG inavyoonesha, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa na ufisadi ambao unaendelea kwenye hizi Halmashauri zetu na tunajua miradi mikubwa ya maendeleo kama vile zahanati na maji inategemea sana kodi ambazo zinatoka ndani ya hii Halmashauri yetu. Kwa hiyo, kwa hili mimi namuunga mkono Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ombi, Serikali ihakikishe inapeleka hizi pesa kwenye hizi Halmashauri kwa wakati na kwa bajeti ambayo itakuwa imependekezwa na Kamati ya Bajeti kutoka kwenye hizi Halmashauri husika. Vilevile ningeomba hii Ofisi ya CAG ipewe pesa ya kutosha, kwa sababu hii ndiyo macho na masikio ya Serikali yetu, ndiyo itakayoweza kuhakikisha pesa hizi zilizotengwa zinakwenda kufanya yale malengo ambayo yamekusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme machache. Najua nia na lengo la Waziri ni zuri. Naomba nishauri machache ili tuweze kuiboresha hii bajeti yetu kwa sababu na mimi lengo na nia yangu ni kuhakikisha Watanzania wanaishi vizuri. Kwenye ukurasa wa 39 wa hotuba Waziri alikiri kabisa kuwa huduma za afya na maji bado ni changamoto na akaenda mbali zaidi akasema upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama bado ni changamoto hususani majumbani na viwandani. Naomba nimkumbushe alisahau eneo moja nyeti la hospitali kwani hospitali zetu nyingi bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tukubaliane na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti, wao wameshauri tuongeze tozo ya Sh. 50 kwa kila lita ambayo itatusadia sisi kupata shilingi bilioni 250 na wakaenda mbali zaidi kusema shilingi bilioni 230 itakwenda kwenye miradi ya maji na shilingi bilioni 30 itakwenda kuboresha zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waziri wa Afya hapa anasoma hotuba yake alieleza kabisa kuwa hali ya zahanati bado ni mbaya na vifo vya akinamama na watoto bado vinaendelea. Mwaka 2010 watu 454 walikuwa wanapoteza maisha wakati wa kujifungua, sasa hivi 2015 ni watu 398 bado wanaendelea kupoteza maisha. Sasa hili ni jambo la kusikitisha si jambo la kujivunia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wakati nachangia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii nilisema yafuatayo:-
Mkoa wa Iringa kuna hifadhi kubwa ya msitu wa Sao Hill. Serikali inapoteza takribani shilingi bilioni sita kwa mwaka na hii ni kuanzia mwaka 2007 na Mheshimiwa Cosato alilisemea hili pia. Kwa taarifa nilizopata jana, hawa wawekezaji wa RAI Group sasa hivi wanafanya lobbying Dar es Salaam kuhakikisha wanaendelea kulipa hiyo Sh.14,000 kwa cubic metre. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ahakikishe hao watu wa RAI group wanalipa fair share sawa na Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna zahanati ziko katika hali mbaya, Wilaya yangu ya Kilolo hawana hata Hospitali ya Wilaya na wanahitaji shilingi bilioni 2.2 ili kuweza kukamilisha hospitali hii na nimesema tutapata shilingi bilioni sita kwa mwaka kutoka kwa hawa wawekezaji wa RAI group waweze kuchangia pato la Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wameweka imani kubwa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano, wananchi wa Iringa wana matumaini makubwa sana kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano. Sasa kama tutaendelea kuwabeba hawa wawekezaji na kuwatwisha mzigo Watanzania wanyonge, wauza mitumba, waendesha bodaboda, tukawaacha hawa RAI Group waendelee kuvuna matunda ya nchi hii kweli itatusikitisha. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha afuatilie kuhakikisha hawa RAI Group wanalipa fair share. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. (Makofi)
Awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Dada yangu Ummy na Mheshimiwa Kigwangalla, mmekuwa mabalozi wazuri, kweli hilo jina linawafaa. Ni matarajio yangu Watanzania hasa wanawake na watoto wanatambua na wanajivunia mchango mkubwa ambao mnautoa kwenye Wizara yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niende moja kwa moja kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 55 anasema: “Maendeleo endelevu ya Taifa lolote yanategemea uwekezaji katika makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 idadi ya watoto ni asilimia 51.6 ya Watanzania wote.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ambazo zimepiga hatua, zilifanya jitihada za makusudi kuhakikisha zinawekeza kwenye hii rasilimali watu. Kwa hiyo, kwa hotuba hii Mheshimiwa Waziri naungana na wewe kabisa kuwa ni jukumu letu kama Taifa kuhakikisha kuwa tunawatengenezea mazingira mazuri hii asilimia 51.6, kwa sababu tunasema tunataka Tanzania iweze kufika uchumi wa kati na hii ndiyo nguvu kazi ambayo itatusaidia kuweza kufika hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na utafiti ambao umefanywa na World Health Organization wakishirikiana na World Bank wanasema, Taifa kama tunataka kuhakikisha tunawekeza kwenye watoto umri ambao unafaa ni kuanzia mwaka sifuri mpaka miaka miwili. Sasa Mheshimiwa Waziri nikupongeze kwa kuleta takwimu hizi, imetupa picha kamili kuwa sasa ni zaidi ya nusu ya Watanzania ni watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ningependa turudi nyuma kwa kutumia huu utafiti na ushauri ambao umetolewa na World Health Organisation. Turudi nyuma sasa tujue katika hii asilimia 51.2 ni watoto wangapi wako kwenye umri wa mwaka sifuri mpaka miaka miwili, kwa sababu hii ni critical age ndiyo maana wamesema kama Taifa tunatakiwa kuanza kuwekeza hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunasema ni critical? Kama hotuba yako ambavyo inaonesha mortality rate ya watoto wa mwaka sifuri mpaka miwili ni kubwa sana, tunapoteza watoto 21 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa.
Pia umekiri kabisa kuwa udumavu ni tatizo kubwa sana kwa Taifa letu, tumekuwa na watoto ambao uelewa wao unakuwa ni mdogo sana. Tunajua kabisa tatizo la udumavu linafanya mtoto ashindwe kufikiri, kutunza kumbukumbu na hata kufanya maamuzi inawawia vigumu sana.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tuna kazi kubwa kama taifa kuhakikisha tunalinda hawa watoto wetu ili tuweze kufikia malengo hayo ya uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo kwa Serikali yatakuwa kama yafuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema hii age ya mwaka sifuri mpaka miwili ni critical na tunataka tuwe na watoto ambao wataweza ku-grasp hizi concept, sasa hivi kumekuwa na frustration. Mtoto anakwenda shuleni, mwalimu ameandaliwa na tumetengeneza miundombinu mizuri lakini watoto hawa bado wanashindwa ku-grasp hizi concept zinazofundishwa shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali na kama wizara naomba tupitie hizi sheria, tuzilete hapa ili tuweze kufanya mabadiliko na tunaweza tukaanza kidogo tu, hizi maternity leaves tunazipuuzia, tunasema zipo vizuri, hazipo vizuri, ukiangalia nchi ambazo zimeendelea kwa mfano, Scandnavian countries wanatoa kipaumbele kikubwa sana kwa wamama wajawazito, si ndiyo. Wengine wanapewa hadi siku 480 sisi hapa bado ni siku 120, siku hizi hazitoshi kwa sababu tunatakiwa kumlinda huyu mama ili aweze kumlea mtoto wake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze juhudi za Serikali za kuhakikisha tunatoa elimu kwa mama mjamzito juu ya lishe ya motto, lakini hii haitoshi tunatakiwa kwenda mbali zaidi. Tumesema kuna viwanda…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja nitaleta mapendekezo yangu kwa maandishi. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Watendaji wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya kwa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii, bajeti ambayo huwa inapangwa na kuidhinishwa inatolewa kidogo, hata hiyo kidogo haipelekwi kwa wakati. Ucheleweshwaji huu unaathiri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Fungu 38 lilipokea asilimia 41 tu ya fedha ambazo zilitengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze kazi nzuri inayofanywa na SUMA JKT. Naomba Serikali kuboresha maslahi ya walinzi wa SUMA JKT Guard. Pesa inayolipwa kwa walinzi hawa haiendani kabisa na living cost za sasa. Taifa tunaendelea kuwa na amani na usalama kwa sababu Jeshi letu linafanya kazi kubwa usiku na mchana, lakini hali ya kimaisha/living conditions zao ni mbaya sana. Nyumba za kuishi bado haziridhishi. Kama Taifa tuna wajibu wa kuhakikisha wana makazi bora (Makambi) na siyo waachiwe kuishi mitaani ambapo tumejionea baadhi yao wamekuwa wakijihusisha kwenye vitendo visivyopendeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kuwa tax exemption kwenye yale maduka ilifutwa, basi Mheshimiwa Waziri atueleze Jeshi wameongezewa allowances kwa ajili ya manunuzi ya mahitaji muhimu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kumekuwa na ukusanyaji kwenye ukusanyaji wa madeni kwa wale waliokopa matrekta, ushauri wangu kwa Serikali tutumie list of shame bila kujali nafasi ya watu hata kama ni viongozi wa juu. Nadhani hii itashawishi watu kulipa madeni yao kwa kupitia magazeti na televisheni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kabla sijaanza naomba ninukuu maneno ya busara kabisa ya baba wetu wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye kitabu chake cha Freedom and Socialism.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 32 anasema; for too long we in Africa and Tanzania as part of Africa we have slept and allowed the rest of the world to walk around and over us. Kwa tafsiri isiyo rasmi anasema; sisi Bara la Afrika na Tanzania tukiwa sehemu ya Afrika tumelala kwa kipindi kirefu wakati wenzetu wakitembea na wengine wakitembea hadi kwenye migongo yetu. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Iringa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu wanchi hii ambaye hajalala na anaendelea kutuamsha Watanzania wote kuhakikisha hatupotezi rasilimali za Taifa hili. I know some people are still in denial, lakini kwa yaliyotokea juzi I am sure a lot of people are catching up. Najua tutafika, Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo naomba nichukue fursa hii nikupongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, baba yangu Mheshimiwa Mpango na dada yangu Mheshimiwa Ashatu kwa kutoa bajeti ambayo imetatua changamoto nyingi zilizokuwa zinawasumbua Watanzania. Nikupongeze kwakutoa tozo la kwenye mazao. Hii imewasaidia sanaespecially wanawake ambao ndiyo nguvukazi kubwa wanaojishirikisha na shughuli za kilimo. Kwa hilo nawapongezeni sana.
Vilevile nikupongeze kwa kuongeza hii tozo ya shilingi 40, lakini nakusihi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ili wananchi wasisikie uchungu wa tozo hii, tunaomba zitakapokusanywa tuhakikishe tunaenda kutatua zile kero ambazo zimekuwa zikiwasumbua muda mrefu especially issue ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wangu wa Iringa bado tuna changamotokubwa ya maji. Maeneo ya kilolo kule Ilula bado ni changamoto kubwa, Mufindi, Mafinga bado ni changamoto kubwa, pale mjini kidogo wamejitahidi na Iringa Vijijini bado tuna changamoto ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kuna jambo lingine ambalo ningependa niliongelee. Kwa mujibu wa Sheria ya Finance Bill ya 2016, tulitaka hawa operators wote wa simu walete hisa zao sokoni maana ya Dar es Salaam Stock Exchange. Lengo lilikuwa ni kuongeza transparency ili tujue ni nini kinaendelea kwenye haya makampuni.
Pili, tulitaka kuwapa fursa Watanzania ili waweze kushiriki moja kwa moja katika kumiliki uchumi wa nchi yao, haya ndiyo yalikuwa matarajio yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Vodacom walikwenda sokoni ili kutekeleza takwa hili la kisheria. Nikiuliza hapa Wabunge wangapi wamenunua hisa hizi they will be very few. Sasa kama muitikio huu umekuwa mdogo kwa Waheshimiwa Wabunge, imagine kwa mwananchi wa kawaida kule kijijini ambaye hajapewa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kama ifuatavyo; wakati haya makampuni mengine yanajipanga kwenda sokoni sasa sisi ingebidi tuhakikishe tunatoa elimu kwa wananchi. Elimu ya kutosha na tusiwaachie makampuni ya simu peke yao. Sisi kama Serikali tuna taasisi nyingi ambazo ziko jirani na hawa wananchi zitaweza kutoa elimu juu ya umuhimu wa kumiliki hisa hizi. Sasa kwa sababu muitikio umekuwa mdogo basi tupunguze kutoka kwenye hii asilimia 25 tuanze asilimia10 mpaka15 then baade hali ikikaa vizuri tutarudi back to asilimia 25. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tushirikishe hata wenzetu kuna hawa East African Community,SADCna baadae hata iende dunia nzima kama wenzetu wa TBL na TCC walivyofanya. Nina uhakika hili jambo linawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa MWenyekiti, nina jambo lingine ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri utakapokuja kumalizia hapa ulipatie kidogo ufafanuzi. Wenzetu wa Kenya, Serikali ya Kenya imefanya non tax barrier kwa wasambazaji na wasindikaji wa gesi ambayo inatumika nyumbani. Sasa hivi hawa wasambazaji kutoka Tanzania hawaruhusiwi kupeleka gesi hii nchini Kenya. Hii ni kinyume kabisa na matakwa ya East African Community. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi kama Wakenya wataendelea na msimamo huu na sisi tuzuie bidhaa zao kuingia nchini Tanzania. Ni nani haelewi ni kiasi gani Wakenya wame-benefit kutoka kwenye nchi hii? Leo Blue Band tunazotumia nyingi zinatoka Kenya, tukija kwenye maziwa, robo tatu ya maziwa ambayo yanaingia Tanzania yanatoka Kenya, madawa, sabuni zinatoka Kenya. Hii sio sahihi, natambua ushindani wa kiuchumi lazima uwepo na mimi hapa nilishauri lazima tu-send statement uwezo wa kuzalisha maziwa nchi hii tunao! Tuna ng’ombe wa kutosha, tuna viwanda vizuri vya kisasa. Iringa pale tuna kiwanda kikubwa cha Asas, nilisema last time kina uwezo wa ku-process lita laki moja kwa siku. Na pale Iringa kuna wananchi ambao maziwa yanaozea ndani. Nimekuwa naongea, tuwatengenezee miundombinu, collecton centres tuwape hawa wakusanye maziwa yaende kwa yule mwenye kiwanda pale. Tu-send statement kwa hawa Wakenya kuwa tuna uwezo wa kuendesha viwanda vya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na tukiikubali hii habari ya gesi moja tutapoteza ajira, pili tutapoteza mapato. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba hili jambo tulitolee ufafanuzi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naendelea kukupongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, nawatakia heri katika utekelezaji wa bajeti hii. Nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu siku ya leo. Awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Ni matumaini yangu Watanzania wanatambua mchango mkubwa ambao wanautoa kwenye Wizara yao na kwa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, nina jambo moja tu ambalo nitapenda kuliongelea siku ya leo ambayo ni issue ya hawa ndugu zetu wa TIRA (Tanzania Insurance Regulatory Authority). Mwaka 2009 Bunge lako lilipitisha Sheria Ndogo, Sheria ya Bima Na. 10 na lengo lilikuwa ni kutatua changamoto kwa wananchi, hasa pale wanapopata ajali, kama mtu amepoteza maisha, basi ndugu zao waweze kupata fidia na kama kuna upotevu wa mali, basi waweze kupata stahiki zao.
Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Waziri alivyokiri kwenye hotuba yake ukurasa wa 60 kumekuwa na upungufu mkubwa kwenye chombo hiki ambacho kilipewa mamlaka ya kusimamia na kuratibu taratibu zote zinazohusu bima nchini. Kwenye ukurasa wa 60 Mheshimiwa Waziri anasema, Wizara imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi hasa ya ucheleweshaji wa fidia pale wanapopatwa na majanga. Hiki kimekuwa ni kilio kwa nchi nzima hasa wananchi wangu wa Mkoa wa Iringa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, chombo hiki kimekuwa na upungufu mkubwa, kwanza hakijulikani na hao wachache wanaokijua chombo hiki, notion iliyopo inakuwa ina-benefit sana makampuni ya Insurance badala ya wananchi wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, chombo hiki kiliundwa kuhakikisha kinaratibu shughuli zote za bima, lakini suala hili niliuliza ilikuwa tarehe 3 Aprili, nikataka kujua takwimu ni ajali ngapi zimetokea na watu wangapi walikuwa wamelipwa stahiki zao? Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo hapa kuanzia 2016 - 2018 ni majeruhi na vifo ilikuwa ni zaidi ya 14,000. Mpaka tarehe hiyo 3 Aprili, Mheshimiwa Waziri alipokuwa anatolea hapa ufafanuzi ni watu 1,500 tu ndio ambao walikuwa wamelipwa stahiki hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hiki chombo kifanyiwe mapitio, kumekuwa na upungufu mkubwa sana. Kuna hata hili suala ambalo wameweka la Msuluhishi wa Bima. Chombo hiki hakitambuliki na ofisi yao ipo moja tu Dar es Salaam. Sasa kwa hali halisi Mheshimiwa Waziri mtu atoke sijui Makete, Njombe, Iringa aende kwa huyu Msuluhishi wa Bima inakuwa ni kazi kubwa. Kwanza umbali na pili ni gharama.
Mheshimiwa Spika, juu ya hilo, kuna upungufu, huyu Msuluhishi wa Bima anataka kuonana na mdai mwenyewe, hawaruhusu Mwanasheria au Mwakilishi yeyote kukutana na chombo hiki. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwa sababu hawa TIRA wako chini ya Wizara yake, hebu tuangalie tena kwa namna ya utendaji wao kazi. Moja, watoke maofisini waweze kuwafikia wananchi.
Mheshimiwa Spika, elimu ya Bima bado ipo nyuma kwa wananchi wetu, wengi wanajua tu ni Bima pale ajali inapotokea. Kuna wananchi wengi mkoani kwetu Iringa pale wanajishughulisha na shughuli nyingi za kilimo, mashamba yanaungua pale lakini hawajui bidhaa ambazo zinapatikana kwenye hizi huduma za bima ili pale wanapopata majanga waweze kupata stahiki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba kwanza tupitie sheria, kama kuna upungufu wowote ziletwe hapa zipitiwe ili tuweze kufanya mabadiliko tuwasaidie Watanzania. Pia TIRA wapewe pesa za kutosha. Najua sasa hivi wameanzisha Website yao, nawapongeza kwa hilo, at least inafanya kazi, watu wanaweza ku-check wamelipwa premium zao wanaweza kufanya follow-up kujua kama zimelipwa na hayo makampuni. Kwa hiyo, wapewe pesa za kutosha, watoke maofisini wasiishie Dar es Salaam, waweze kufika sehemu mbalimbali hata zile za vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hizi dakika chache zilizobaki, naomba pia niwasemee Walimu. Kumekuwa na manunung’uniko makubwa juu ya kulipa malimbikizo yao. Tunajua wana mchango mkubwa sana kutuandaa na na kutulinda. Wengine tumefika hapa Bungeni ni mchango wa Walimu.
Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa ufafanuzi mzuri asubuhi, tunaomba kuendelea ku-keep update kuhakikisha tunalipa hizi stahiki zao kwa wakati, wanafanya kazi kubwa kuhakikisha wanajenga Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi ili niweze kutoa maoni yangu kwenye Wizara hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwenye Wizara hii. Wizara ya Viwanda na Biashara ndiyo yenye jukumu la kusimamia Sera ya Viwanda na Biashara nchini na Wizara nyingine ndiyo watekelezaji. Kwa hali ya kawaida, Wizara ya Kilimo ndiyo tulitegemea ichangie sana au zaidi kwenye maendeleo ya viwanda hapa nchini. So far Wizara ya Viwanda haina direct link na Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Taifa tunategemea kuingiza mafuta ya kula kutoka nje. Sasa Wizara ya Viwanda inge-link na Wizara ya Kilimo tungehakikisha tunakuwa na mbegu bora na kuweza kuzalisha mafuta ya kula hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2018 tulizindua mradi wa ASDP II na mradi huu una pesa nyingi sana. Tungekuwa na link na Wizara ya Kilimo ingetusaidia sisi kama nchi kuweka mkakati mzuri wa kuzalisha products zetu badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati umefika sasa kuhakikisha tunatengeneza soko la ndani. Lazima taasisi za kiserikali wapewe tamko rasmi kuhakikisha vitu vyote ambavyo vinatumiwa na hizi taasisi za kiserikali watumie bidhaa ambazo zimezalishwa hapa nchini. Tanzania ya Viwanda inawezekana kwani lazima tujipange vizuri na sector zote nchini lazima zishirikiane.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwatakie kheri Mheshimiwa Waziri na watendaji wote katika utekelezaji wa bajeti yao. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mawazo yangu kwa Wizara muhimu sana, Wizara ya Elimu. Awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa mchango mkubwa ambao mnautoa kwenye Wizara yenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa tumekuwa na matamanio sasa ya muda kuhakikisha nchi yetu inafikia uchumi wa kati. Ni imani yangu na ya Watanzania wengi kuwa Wizara ya Elimu ni kiungo kikubwa ambacho kitatusaidia sisi kuweza kufikia malengo hayo ya uchumi wa kati na ambayo yataendeshwa kwa viwanda na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Wizara ya Elimu ndiyo iliyopewa jukumu la kuandaa Sera ya Elimu nchini, mitaala ambayo ita-reflect pale ambapo sisi Watanzania tunataka kufikia na kuandaa walimu ambao tunategemea watakuwa na hizi skills na knowledge ambapo wata-transfer kwa hawa watoto wetu ambao tunategemea waje waweze kuendesha hivi viwanda ambavyo tayari vimeanzishwa kwenye mikoa yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake kesho angetueleza Wizara ya Elimu, Sera ya Elimu hapa nchini ni nini? Je, sera na mitaala ambayo tumeiandaa inaweza kuwasaidia hawa vijana kutimiza malengo yao? Let’s say watoto ambao wata- graduate miaka mitano ijayo anaweza akatumia hizi skills na utaalam ambao amepata shuleni kufanya kazi kwenye viwanda hivi? Je, huu ujuzi alioupata anaweza akatumia fursa zilizopo akaanzisha biashara, akajikita kwenye kilimo chenye tija, akawa mfugaji badala ya sasa ambao asilimia kubwa ya vijana wanategemea kuajiriwa Serikalini? Hilo ni jambo la msingi sana Mheshimiwa Waziri, napenda ulitolee maelekezo ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili, nilitaka tujue sasa kama Wizara tumejiandaa vipi kuhakikisha hawa walimu ambao nimesema ndiyo nguzo muhimu wameandaliwa kuhakikisha wana utaalam wa kutosha kuweza kuwafikisha hawa watoto hapo ambapo tunataka wafikie. I stand to be corrected, nakumbuka kwenye hotuba ya bejeti ya mwaka 2018/2019 ilionesha kabisa tuna upungufu wa walimu hasa shule za msingi, nakumbuka idadi ilikuwa zaidi ya 85,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kuwa mwaka huu tumeweza kuajiri hao walimu 4,500 lakini ni wachache, hawawezi kukidhi shida ambayo tunayo sasa hivi na walimu wapo. Nakumbuka Waziri wa TAMISEMI alivyotangaza ajira hizi, zaidi ya walimu 90,000 walituma application kupata nafasi hizi za kazi.
Kwa hiyo, tushirikiane na Wizara ya TAMISEMI tuhakikishe tunaajiri walimu wa kutosha. Hali ya walimu kwenye maeneo yetu hasa Mkoa wa Iringa bado ni changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili walimu wetu wawe na ufanisi wa kufundisha lazima workload yao iwe ndogo, uwiano kati ya walimu na wanafunzi lazima uwe mzuri. Nitatoa mfano, kwa walimu wa shule ya awali inakadiriwa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 189, in average tunatakiwa tuwe na mwalimu mmoja kwa watoto 25. Kwa hiyo, tumeanza kuajiri ni jambo jema lakini tusiishie hapo, tuna jukumu la kuhakikisha tunaajiri walimu wa kutosha ili wawe na uwezo wa kufundisha hawa watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii workload waliyokuwa nayo tumeona inavunja morale. Hata hawa ambao sasa hivi wanakwenda kufundisha, wakifika kule kwa workload iliyopo ni vigumu wao kufanya followup, kuhakikisha hawa watoto wame-grasp hizi concept ambazo wanawafundisha darasani. Kwa hiyo, tunajikuta tuna walimu nusu, nadhani watu wa Hakielimu walionesha last year, less than 40% walimu wako motivated kufundisha darasani. Sasa tutapaleka hao walimu wako pale lakini kumbe zaidi ya nusu hawana morale ya kufundisha watoto wetu. Kwa hiyo, tunatakiwa tufanye jitihada za makusudi kuhakikisha jambo hili tunaliweka vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali utakuwa kama ufuatavyo. Kama nilivyosema walimu ni kiungo kikubwa sana sasa tuhakikishe in-service training tukishirikiana na Wizara ya TAMISEMI tunawaendeleza hawa walimu wetu. Kama Wizara mmekuwa mnatoa miongozo mbalimbali, tunabadilisha mitaala, je, hawa walimu wako trained kuhakikisha wanaenda na hiyo miongozo na mitaala mipya ambayo mmeileta? Kwa hiyo, tuhakikishe in-service training inakuwepo kwa walimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile issue ya IT (Information Technology), ni lazima kama nchi tuanze hii conversation, hatuwezi kukwepa. Wenzetu wa Rwanda sasa hivi wameshaanza, Kenya wameshaanza haya majadiliano, najua ni gharama na itakuwa ni kazi kubwa lakini lazima tuanze. Hivi viwanda tunavyoanzisha lazima tuwe na vijana ambao wako multiskilled. Tutaanzisha viwanda tutaishia kuchukua expert’s kutoka nchi za nje kuja kufanya kazi kwenye viwanda vyetu. Inasikitisha mtoto anakuja kuona desktop au tablet anapofika labda chuo, lazima hawa watoto wawe exposed kwenye hizi sayansi na teknolojia mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama nilivyosema, issue ni kubwa, we have to start somewhere at least tuwe na conversation. Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha atueleze tuone inakuwaje. Uzuri sasa hivi tuna umeme mpaka vijijini, kwa hiyo, tuna access ya kuweka hata computer moja moja kwenye shule ili watoto wawe exposed kwenye hizi new technology. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mheshimiwa Waziri ana uwezo (competent) wa kututoa hapa tulipo kwa kutengeneza sera na mitaala yetu mizuri ili tuweze kufika pale ambapo tunataka kufika kwenye uchumi wa kati. Tuhakikishe tunaajiri walimu wa kutosha, tuwawezeshe, tuna uwezo wa kufika huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimtakie kheri Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara katika utekelezaji wa bajeti hii. Nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru na kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa namna ambavyo ameandaa na kuwasilisha huu mpango hapa Bungeni, ili na sisi tuweze kutoa mapendekezo yetu.
Mheshimiwa Spika, nitajikita kwenye vipaumbele vitano ambavyo Mheshimiwa Waziri alivielekeza hapa Bungeni kuwa ambavyo, ndivyo vitakavyotusaidia kuhakikisha sisi kama Watanzania tutakuwa na uchumi endelevu na shindani na tutoke sasa kwenye hii asilimia sita tuweze kufika kwenye asilimia nane. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na nita-zero in kwenye kile kipaumbele namba tano ambacho umehakikisha kama Taifa tutahakikisha tunaendeleza hii rasilimali watu. Na issue hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha umeeleza kuwa unataka kufanya maboresho kwenye sekta ya elimu. Mheshimiwa Waziri maboresho peke yake hayawezi kutusaidia sisi kufikia yale malengo yetu, we need total transformation kwenye sekta ya elimu, tunahitaji mapinduzi makubwa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika nchi zilizobarikiwa Tanzania is one of them. Tuna natural resources za kutosha, tuna ardhi ya kutosha na hii rasilimali watu ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha anaiongelea ndipo hapa kwenye changamoto. Tuna vijana ambao zaidi ya asilimia 65 wangetumika kama nguvukazi ya kuja kuboresha uchumi wetu. Hapa ndipo tunapotaka kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata nchi za wenzetu ambazo zimepiga hatua, let say China, wao tayari wapo juu, lakini na wao wameamua kufanya total transformation kwenye mfumo wao wa elimu kuhakikisha vyuo hivi vikuu wamebadilisha vyuo vikuu 600, ili vije kuwa vyuo vya kati; vyuo vya ufundi kuhakikisha wanazalisha vijana ambao wana skills za kuajiriwa kwenye viwanda vyao na pia thinking. Wana critical thinking ya kuhakikisha wanatumia mazingira ya kujianzishia biashara na kufanya shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, twende Singapore. Wao kuanzia mwaka 1997 mpaka 2012…
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge nawaombeni sana, hata ninyi wenyewe mkikaa mnaona masikio yenu jinsi yanavyokataa hizi kelele ambazo mnapiga. Na hizi five minutes ambazo kila Mbunge anaongea hapa ni very critical ni vizuri ukasikiliza argument ya mtu anasema nini. Mkitaka kuongea mnakwenda canteen pale mnapiga na kahawa kidogo, mnapiga story zenu zote mnamaliza. Tupeane nafasi tusikilize watu wanaongea kitu gani, kuna hoja muhimu sana zinazoongelewa humu ndani.
Endelea Mheshimiwa Rose Tweve!
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nilikuwa natoa mfano wa Singapore wenzetu kwa miaka 15 walihakikisha wanabadilisha mfumo wao wa elimu wakajikita focus yao ikawa kwenye skill development na kuhakikisha watoto na vijana wao mashuleni wana uwezo wa kufikiri, critical thinking. Sasa sisi hapa Tanzania it is opposite, tuna human resources, tuna ardhi, tuna natural resources, lakini mfumo wetu wa elimu, tume-focus sasa kwenye vyuo vikuu kuzalisha degree ambapo mmekuja kutueleza hapa hazina tija hata kwenye soko letu la ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndipo hapa ningeomba kama Taifa tufanye total transformation. Mdogo wangu pale Viti Maalum kutoka Mwanza alisema tuwe na agenda za kitaifa; hii ndio iwe agenda yetu sasa kuhakikisha hawa vijana wetu wanaweza kuwa na uwezo wa kufikiri na kuwa na skills za kuweza kuajiriwa. Tuhakikishe hivi vyuo vya kati ndio vinapewa msukumo na vyuo vya ufundi. Sasa hivi funding zote zinakwenda kwenye elimu ya juu, hii ndio iwe think tank yetu, moja tutakuwa na vijana ambao wanajitambua, tutaongeza wigo wa walilipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi as of today number ya walipa kodi ni 3,985,493 out of 60 million people. Hata tukisema tutoe hao wazee na vijana bado tungekuwa na milioni 23 ya Watanzania ambao wangekuja kuongeza pato la Taifa. Hata tuweke mazingira mazuri kiasi gani kwa hawa watu less than four million hatuwezi kufikia malengo yetu ya kuhakikisha tunakuwa na uchumi endelevu na shirikishi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nakuomba tuhakikishe sasa hata hivi viwanda tunavyoajiri tukiweka msukumo huku kwenye mfumo wetu wa elimu hata hawa investors wanaokuja watakuwa attracted kuja Tanzania kwasababu watakuwa na guarantee na vijana ambao wapo much skilled. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hizi nchi zinazokwenda ku- invest China kama Marekani wanakwenda kule sio kwasababu kuna cheap labor, wanakwenda kule kwasababu wana vijana ambao wako much skilled. Anaweza akafanya na akawa mchango kuhakikisha wanaendeleza viwanda vilivyopo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hapa ndipo tunapotakiwa kuanza. This is a piece of the puzzle ambayo ina-miss kwenye mfumo wetu wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nimtakie heri Mheshimiwa Waziri katika utekelezaji wa majukumu yake natuhakikishe tunaanza hapo. Nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Elimu ambayo ni muhimu sana. Awali ya yote namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa namna ambavyo amewasilisha bajeti yake hapa ili sasa sisi Wabunge tuweze kutoa mchango wetu na maoni yetu.
Mheshimiwa Spika, nitajikita zaidi kwenye Bodi ya Mikopo. Nachukua fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo iliona ni muhimu kuhakikisha mtoto yeyote wa Kitanzania ambaye atakuwa hana uwezo wa kulipia elimu ya juu, basi Serikali ikatengeneza mkakati maalum wa kutengeneza funds ambapo tulipata chombo cha Bodi ya Mikopo ili kuratibu hili zoezi la utoaji mikopo kwa vijana wetu wa Kitanzania. Hili lilikuwa ni jambo jema na lengo lilikuwa na nia njema, lakini namna ya utoaji wa hii mikopo ndipo kwenye changamoto. Hapa ndipo tulipo-create crisis. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mikopo hii namna ambavyo inatolewa haikuzingatia nini kama Taifa tunahitaji hasa kwa sasa hivi? Pia haijafanya utafiti. Mheshimiwa Mpina hapa amesema asubuhi, hivi wenzetu wa Wizara ya Elimu mnafanya utafiti kuona sokoni ni nini kinahitajika? Mheshimiwa Waziri wa Elimu, asubuhi umekuja hapa umetueleza kuwa tumeongeza sasa Bodi ya Mikopo kutoka 4.6 billion sasa hivi zitakwenda kwenye five billion. Ni jambo jema, lakini zinakwenda kufanya nini? Zinakwenda kusaidia vijana wa aina gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Bodi ya Mikopo walikuja kutupa mtiririko wa namna ya hizi fedha zimetumika so far. Kwenye kada ya sayansi ya jamii na sanaa, maana yake Bachelor of Art, 64.9 percent; Uhandisi 5.3 percent; Afya 4.7%; Sayansi ya kilimo, inaendelea kushuka 1.8, Uhandisi wa Mafuta na Gesi ndiyo kabisa, 0.10 na mengineyo.
Mheshimiwa Spika, hapa ndipo tulipo-create crisis. Kama mikopo hii yote; 64 percent ya hii mikopo inakwenda ku-fund vijana ambao wana degree ambazo ziko mitaani, sasa hivi soko liko saturated. Nikawa najiuliza, hivi Wizara ya Elimu hatujaliona hili? Sasa hivi na hizo five billion tunaenda bado ku-create hawa vijana wa Bachelor of Arts ambao bado tunaenda ku-create degrees ambazo hazihitajiki kwenye soko la elimu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimezidi kujiuliza, what’s wrong na vyuo vyetu vya kati? Vyuo vya ufundi, ndio doers, hawa ndio wanaoingia kule field. Tulishauri hapa Mheshimiwa Waziri, nchi za wenzetu ambazo zinaendelea sasa hivi China inakua kwa asilimia 10, lakini bado wameona umuhimu wa kuhakikisha wanarudi kwenye vyuo vya kati. Kwa sababu mmesema kigezo kikubwa ni mtoto kutokuwa na uwezo wa kujilipia.
Je, hivi vyuo vya kati hakuna watoto wa masikini wanaohitaji hii mikopo? Hawa ndio doers Mheshimiwa Waziri. Ukienda Kituo cha Afya, tuna daktari mmoja, lakini wale wasaidizi karibia watu 30 wote ni wa elimu ya kati. Who is funding these people? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, engineer pale anatengeneza daraja, tunahitaji ma-engineer wangapi? Ni engineer mmoja na watu wenye ujuzi wa kati. Who is funding these people? Nina uhakika tungekwenda huko, I am not arguing what, tupunguze kiasi. Kama tutapeleka at least three billion, at least hizi two billion zije huku ziwasaidie watoto wa uchumi wa kati kuendeleza uchumi wa kati. Moja, hawa watoto wataweza kulipa hii mikopo kwa sababu, hizo taaluma zao ndizo zinahitajika huku. Pili, wataweza hata kuongeza pato la Taifa kwa sababu, wataweza kulipia mikopo na kujikimu na shughuli zao za kilasiku na kutunza familia zao. Kwa hiyo, focus yetu… (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa ambao mlikuwa mnachangia hapa, mnaona Mbunge mzoefu anavyokwenda? Yeye amechagua Bodi ya Mikopo na anavyoiona Bodi ya Mikopo na analysis yake. Dakika saba siyo nyingi, huwezi kuongea vitu vitano. Endelea Mheshimiwa Rose. (Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Bado narudi kwenye umuhimu wa hivi vyuo vya kati. Tulikuwa na CBE, Mipango, Chuo cha Tengeru; sasa hivi kaka yangu amesema hata Chuo cha Mwanza, kile cha Uvuvi, sasa hivi watu wote wanakwenda kwenye degree. Why are we expect na hivi vyeti wakati tunahitaji hivi vyuo vya kati?
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, hii Bodi ya Mikopo ije na sura na mikakati ambayo Watanzania tunaitaka. We can not be doing the same thing over and over and expect different results. Kama hawa watoto wa art ndio wamejaa kule na mwakani tena Bachelor of Art zimejaa mtaani, manung’uniko lazima yataendelea na tuna-create bomu ambalo kuja kulizima itakuwa ni kazi sana Mheshimwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ushauri wangu kwa Serikali utakuwa kama ifuatavyo: Moja, kama tume-create special window kwa ajili ya kilimo, why not education? Sasa hivi tutakapokuja hapa iwe ni Bodi ya Mikopo not Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Tuzi-involve na sekta nyingine kama banks ili nao waje wawe na michango katika kuendeleza elimu yetu nchini.
Mheshimiwa Spika, la mwisho,…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Natamani nikuongeze muda, lakini…
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, hili ni la mwisho.
NAIBU SPIKA: Bahati mbaya.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, tulikuwa na new formula ya capitation kwenye kutoa ruzuku shuleni. Mheshimiwa Dada Grace amesema pale asubuhi, hali ni mbaya, tulishajulishwa ianze kutumika, imekwama wapi Mheshimiwa Waziri? Ni kwenu Wizarani au Wizara ya Fedha? Hii ndiyo ilikuwa more practical inajibu zile shule ambazo ziko mbali na shule ambazo zina uhitaji maalum ili waweze kupata pesa zaidi.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Rose Tweve. Anastahili makofi makubwa zaidi ya hayo. (Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nakushukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu kwa namna ambavyo amewasilisha bajeti hii hapa Bungeni ili nasi sasa tuweze kutoa mapendekezo na maoni yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nachukua fursa hii kumpongeza Rais wetu, mama yetu Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan kwa namna ambavyo amesisimama imara kuendelea kuliongoza na kulisimamia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo zilifanikiwa kupiga hatua kubwa ya kupanda kiuchumi ingawa tulipitia changamoto kubwa sana kidunia, lakini tuliweza kufika uchumi wa kati. Sasa ni jambo jema na hii haina guarantee kuwa tutaendelea kuwepo hapo, tunaweza kushuka au kupanda zaidi. Ni matamanio yangu na Watanzania wengine kuwa tutaweza kupiga hatua kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunawekeza ili uchumi wowote uweze kupiga hatua, lazima tuwekeze na eneo kubwa ambalo ningependa kuweka msisitizo ni kuhakikisha tunawekeza kwenye rasilimali watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais yetu Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiongea hapa tarehe 8 mwezi wa Sita alisisitiza sana umuhimu wa kuhakikisha tunaendelea kuwekeza kwenye rasilimali watu na akaenda mbali zaidi kuisihi sekta binafsi kuhakikisha wanaendelea kuchangia ile 4% ya gross pay kuendelea kuboresha na kukuza ujuzi hasa wa vijana wetu. Hii hiko kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2006 Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Mafunzo ya Elimu ya Ufundi Stadi kuhakikisha hawa wenzetu sekta binafsi waendelee kuchangia vipaji vya vijana wetu hapa nchini. Hapa ndipo ambapo kidogo pana changamoto. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha twende sasa na mahitaji na mabadiliko ambayo nchi hii inataka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii kile Kifungu cha 15 kinasema two third ya yale makusanyo yaende Serikali Kuu na one third ilikuwa inaelekeza kuwa iende kuboresha miundombinu tu ya hivi vyuo vya ufundi na siyo kufadhili elimu yetu. Hapa ndipo ambapo pamekuja na changamoto. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hii pesa ambayo inakusanywa ililenga kuhakikisha inaendeleza ufundi na ujuzi wa vijana wetu. Tuje na mapendekezo kama ambavyo amefanya marekebisho ya sheria na tozo mbalimbali, it is a high time tupitie sheria hii, tulete hapa tufanye mabadiliko ili tuendane na uhitaji na kuendelea kukuza uchumi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, as of today tuna vijana zaidi ya 357 ambao wako vyuo na kama 201,000 ni vijana wa elimu ya vyuo vikuu na vijana 157,000 wako kwenye vyuo vya ufundi, sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha ulipokuja kuwasilisha bajeti hapa, tumeonyesha kabisa nia njema ya kuhakikisha kupeleka fund kwenye vyuo vikuu. Tulipopitisha bajeti iliyopita tumeongeza kutoka shilingi bilioni 464 mpaka shilingi bilioni 500 ambayo itaenda kwenye vyuo vikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa na sheria hii ilivyo hapa sasa hivi, ambayo hiyo two third bado inakwenda Serikali Kuu, nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha tulete mabadiliko ya sheria hapa ili tutengeneze mfuko maalum kwa sababu Tanzania ya Viwanda sasa hivi inahitaji vijana ambao watakuwa na ujuzi na ubunifu ili tuweze kupiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili sasa kwa sababu hawa wenzetu wa vyuo vikuu wana mfuko huu wa bodi ambao unawasaidia. Hawa vijana wafundi nao tuwatengenezee mfuko wa mikopo wa vyuo vya ufundi kwa sababu kianzio kipo. Kutoka kwenye hii ongezeko ambalo wenzetu wanalilipa, tuanzishe huu mkopo ili hawa vijana waweze kuutumia. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, wenzetu Rwanda wamepiga hatua kubwa sana. Vyuo vyao vya Ufundi wamevi-brand. Mtoto anapotoka pale, kama anajifunza ufundi, anatoka na cherehani; kama anataka kwenda makenika anakuwa na tool box yake ambayo tayari itamwezesha yeye kuanza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kama wenzetu wameweza kufanikiwa, nina uhakika tukiwekeza huko sisi Tanzania tutakuwa na uwezo wa kupiga hatua kubwa sana. Siyo tu kukua kwa asilimia sita au saba, tunaweza tukaenda hata double digit kama tukiweka nguvu kuhakikisha hawa vijana wetu wa Kitanzania wanaendelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa ninukuu maneno ya mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipokuwa anahitimisha hotuba yake ambayo aliifanya hapa Dodoma ile tarehe 8 mwezi wa sita. Aliongea kwa kusisitiza sana kuwa kwa heshima zote anaomba sisi kama Watanzania tumuunge mkono na tumsaidie. Kwa bajeti hii ambayo umeileta Mheshimiwa Waziri wa Fedha inaonyesha nia njema ya Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan kutaka Watanzania tufikie yale malengo ambayo tumejiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania twende tukamuunge mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunalifikisha Taifa letu pale tunapotakiwa lifike.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu na ninaomba anisimamie katika mchango wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwa imara na mwanamke ambaye hajatikisika kuhakikisha anaendelea kuliongoza Taifa hili. Vilevile nikupongeze Mheshimiwa Mwigulu, kaka yangu na Mheshimiwa Mkumbo kwa namna ambavyo mnaendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ndiyo tunakwenda kuhitimisha Bajeti Kuu na kwa bahati nzuri kwa utaratibu mzuri ambao tumejiwekea ni kuwa, hata kama bajeti za kisekta tumeshazipitisha, mchakato huu unapata kutuongoza pale tunapoona kuna mapungufu na maboresho tunaweza kwenda kushauri kuhakikisha sasa bajeti yetu inakuwa na tija kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha bajeti yake hapa aliongea kwa masikitiko makubwa sana, aliongea kwa uchungu mkubwa sana na aligusa mioyo na mimi alinigusa sana pale ambapo alionekana akisema tunapoteza Watanzania wengi kwa vitu ambavyo tunaweza kuvi-control, vipo ndani ya uwezo wetu. Nami naungana na wewe Mheshimiwa Waziri, na mimi nasikitishwa sana, pale kama taifa tunakuwa na uwezo wa kuzuia vifo vya Watanzania na hatufanyi hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunapoteza zaidi ya Watanzania 1,500 ndani ya miaka mitano tumepoteza Watanzania zaidi ya 6,000 hadi 7,000. Naomba nitumie fursa hii kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo iliona jambo hili na walisikitishwa na jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009 mpaka 2015 walichukua juhudi za maksudi wakatenga milioni zaidi ya 48 za Kimarekani, pesa za walipa kodi, pesa za watu maskini wakajenga kiwanda pale Kibaha, Kiwanda cha Viuadudu kuhakikisha tutazalisha dawa na kuzipeleka kwenye maeneo yetu kuhakikisha tunatokomeza malaria nchini. Kiwanda hiki ni cha kipekee, tuna viwanda kama hivi vitatu tu duniani, Japan, Tanzania na Cuba, kiwanda hiki kinatumia bio technology ambayo bidhaa hii haina madhara kwa binadamu, haina madhara kwa wanyama, haina madhara kwa mimea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema nasikitishwa na NIMR walitoa hati kuwa dawa inayozalishwa pale Kibaha ni salama na safi kwa matumizi ya binadamu. Kitu cha kushangaza kwa taarifa iliyokuja hapa wiki iliyopita, toka mwaka 2017 mpaka 2024 tumenunua lita laki moja na tisini tu ndani ya miaka sita! Uwezo wa kiwanda hiki ni kuzalisha lita milioni sita, wakati tunajiwekea mikakati tulisema ndani ya miaka mitano maana yake lita milioni 30 tungezalisha pale na kutokomeza malaria kwenye Taifa hili. Tungeokoa maisha ya watoto, tungeokoa maisha ya akinamama na nguvu kazi ambayo ingekuja kufanya kazi kupandisha Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naungana na wewe, hatuna sababu ya kuona Watanzania wakiendelea kuteketea, tume-invest zaidi ya dola bilioni 48, this ball is in your hands Mheshimiwa Waziri. Kama ambavyo umekasirishwa na vifo vinavyotokana na ajali ndivyo hivyo tukahakikishe kupambana kuhakikisha tunaokoa maisha ya Watanzania yanayopotea kwa sababu tu hatujatekeleza majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee kwa unyenyekevu mkubwa sana. Kila mwaka tunatumia zaidi ya shilingi bilioni 100 kwenye kununua net, kufanya makongamano na kufanya semina. Sasa najiuliza kwa nini pesa hizi... (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Rose, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Chumi. Mheshimiwa Chumi, tafadhali.
TAARIFA
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa dada yangu Mheshimiwa Rose, napenda pia kumuongezea taarifa kwamba dawa zinazotengenezwa na kiwanda kile moja wapo wa wateja wakubwa ni Nchi ya Angola. Kwa hiyo, pamoja na sisi dawa ile pia ingeweza kutuongezea kuwa chanzo cha mapato ya fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Angola wameamini dawa hiyo na mimi nilishiriki wakati wa uzinduzi wa kile kiwanda, alikuja Makamu wa Rais wa Cuba. Kwa hiyo kama Angola wameamini kwa nini sisi kama Taifa tunashindwa kuamini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimuongezee taarifa Mheshimiwa Dada Rose. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Rose Tweve, unapokea taarifa?
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa ya Mheshimiwa kaka yangu Chumi na yeye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunatokomeza malaria kwenye Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu. Nilikuwa nahoji na ninajiuliza na nimejaribu kuuliza watu wengi; if we are spending shilingi bilioni 100 kwenye semina, ununuzi wa net na kufanya makongamano, kwa nini nguvu hiyo hiyo tusitumie kwenda kununua dawa ya viuadudu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnakuja hapa mnatuambia ndani ya miaka mitano hadi sita tumenunua tu lita 200,000 na nchi zingine wanakuja kununua dawa kwenye kutokomeza malaria kwenye nchi yao. Mheshimiwa Waziri, ndiyo maana nimesema mazungumzo tuliyonayo hapa bado tuna room. Naiomba Serikali twende tukakae Kamati ya Bajeti, Wizara ya Afya na TAMISEMI; twende kuokoa maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Bajeti ya Afya, wametaja malaria mara 57 lakini hakuna kifungu kinachosema tutaenda kununua dawa na kwenda kutokomeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza hivi kwa nini tunatumia hata neno “mapambano dhidi ya malaria,” tunapambana na nini Mheshimiwa Waziri? Kiwanda kipo pale ni kununua dawa na kunyunyizia, hayo mapambano tuyapeleke huko kwingine tukapambane na magonjwa ambayo yanashindwa kutibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili tutafanya historia. Mheshimiwa Waziri utaleta historia kwa nchi hii kuwa ndani ya miaka mitano ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tumeweza kutokomeza malaria kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, as long as...
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuwa kwenye Bunge hili, asubuhi, mchana na jioni nitaimba malaria kuhakikisha tuna...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Rose...
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ooh, thank you. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Stella, samahani muda umeisha. (Makofi/Kicheko)
TAARIFA
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na kwamba muda umeisha nilipenda kumpongeza kiongozi wa mbio za mwenge kwa kuungana na haya maneno aliyoongea Mheshimiwa Rose sasa hivi, kwamba Serikali za mitaa halmashauri zote zinapaswa kwenda kununua dawa zile ikiwemo Halmashauri yangu ya Nyasa. (Makofi)
MWENYEKITI: Kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za Bunge sawa sawa Mheshimiwa Rose Tweve unapokea taarifa ya Mheshimiwa Mbunge?
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Pia naomba unilindie muda wangu nina point za kumalizia.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Rose, muda wako umeisha, ahsante sana.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja.
MWENYEKITI: Naomba hitimisha, ninakupa dakika moja.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini nisipopata majibu ya kuridhisha, Mheshimiwa Kaka nyangu Dkt. Mwigulu anajua how much I am proud of him, nitashika shilingi kuhakikisha Tanzania sasa inakuwa malaria free country. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)