Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Shally Josepha Raymond (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, namshukuru Mungu kwa neema za kutujalia sote uhai. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Profesa Sospeter Mwijarubi Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Mheshimiwa Dkt. Merdad Matogolo Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kero yangu kubwa ni kuhusu gharama kubwa ya biogas kwa kuwa maeneo ya vijijini ni wafugaji hususan wanawake wa Kilimanjaro. Naomba iwepo namna ya kupunguza gharama ya kujenga na kuunganisha nishati na madini ya biogas majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, michango mikubwa watumiaji wanayotozwa kwa ajili ya EWURA hainiingii akilini na wala haipendezi kwa watumiaji wa maji na umeme wanavyotozwa na EWURA katika ankara tofauti, bahati mbaya EWURA yenyewe hairejeshi chochote kwa wananchi kama CSR, natumaini kuona wakitoa mchango wa kuwaelimisha wanawake kwenye ujasiriamali na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumiaji wengi wa umeme vijijini ni kwa ajili ya taa na baadhi luninga na kuchaji simu. Namwomba Mheshimiwa Waziri awaagize Mameneja wa Mikoa wateremshe tozo za vijijini ili familia nyingi zinufaike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tozo la umeme kwenye shule na vyuo; kumekuwepo na malalamiko makubwa sana kwa wamiliki wa wa maeneo tajwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kurekebisha tatizo hili, mfano, Kibosho School of Nursing, Chuo hiki kiko Moshi Vijijini katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo. naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa pongezi kwako na Waheshimiwa wote kwa kuchaguliwa kuingia kwenye Bunge la Kumi na Moja. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaliwa kuwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa nami nampongeza sana. Nimeisoma hotuba yake nzuri na nimekubaliana naye, lakini naomba ufafanuzi kwa mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezeshaji wananchi kiuchumi. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, ukurasa wa 14 na 15, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi imeelezwa vizuri sana, naomba kunukuu:-
“Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuwadhamini wajasiriamali wenye miradi inayokidhi vigezo kwenye taasisi za fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba ufafanuzi wa kina kwani Tanzania ni kubwa na wajasiriamali ni wengi sana na hivyo si rahisi kama maandiko yalivyokaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rahisi kusema kuliko kutenda, hivi Waziri Mkuu anavyosema Serikali itaendelea kuwadhamini wajasiriamali anaweza kuwaeleza Watanzania ni lini dhamana hiyo ilitolewa na ni akina nani walifaidika? Endapo anazungumzia mabilioni ya JK, naomba kutofautiana naye kabisa kwani fedha zile zimetoweka na mzunguko sasa umekwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia nzuri ya Serikali, naomba wananchi wapatiwe miradi zaidi ya fedha. Katika Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwawezesha wajasiriamali na wakulima wa Kilimanjaro mradi wa kopa ng’ombe ambao uliweza kuwapatia lishe bora, nyumba za kisasa, ada za watoto shuleni na hatimaye maisha bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aya ya 23 inasema, nanukuu:-
“Serikali imehamasisha uanzishaji na usajili wa vikundi vya kiuchumi kama vile Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na Benki za Jamii Vijijini (VICOBA).
Serikali pia imesimamia uanzishwaji wa Taasisi mwamvuli ya kusimamia VICOBA inayoitwa VICOBA FETA. Takwimu zilizotolewa Februari, 2016 na Taasisi hiyo zinaonesha kuwa, kuna vikundi 100,000 vya VICOBA vyenye wanachama milioni 2.2 na mtaji wa shilingi trilioni 1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya wanachama wa VICOBA ni wanawake”. Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na taarifa njema alizotupa Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu ushirika wa SACCOS na VICOBA, naomba atufafanulie ni jinsi gani wanawake hao watapatiwa mafunzo ya ushirika. Mpaka ninavyozungumza, jukumu kubwa limekuwa kwa Wabunge. Naomba nichukue nafasi hii nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atufafanulie jinsi ya kuwapatia mafunzo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ule ukurasa wa 16, aya ya 24, hotuba imeonesha wazi hali ya Vyama vya Ushirika, SACCOS zinazokidhi vigezo vya usajili nchini imepungua kutoka 5,559 mwaka 2013 hadi 3,856 mwaka 2015. Huu ni upungufu wa asilimia 30.6 sawasawa na 31%. Huu ni upungufu mkubwa na tatizo ni kwamba, Serikali haitoi kipaumbele kwa ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba kufafanua, Novemba 2006, Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Magufuli alitangaza Baraza la Mawaziri na ndipo umma wa Tanzania ulipozisikia Wizara zilizopo. Wengi mpaka sasa wanajiuliza hivi Wizara ya Ushirika iko wapi? Endapo ni idara, je, iko kwenye Wizara gani? Pendekezo ni kwamba, ipelekwe kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwenye Awamu ya Nne, Wizara hiyo ilikuwa kwenye Kilimo na ilijulikana kama Wizara ya Kilimo na Ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii; na jina langu ni Shally Josepha Raymond, lakini kwa vile baba yangu alikuwa anaitwa Joseph, mkiita hivyo naitika na nakubali pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu sana kwamba ametuweka wote hapa tuweze kuzungumzia mambo ya maendeleo ya nchi yetu. Kipekee naomba shukrani hizi ziwafikie wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao ndio walionipigia kura nikaingia hapa kupitia Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia Wizara ambayo ni nzito na Wizara ambayo kwa kweli Ilani ya CCM inazungumza wazi kwamba sasa twende kwenye uchumi wa viwanda kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Iko kwenye ilani! Mwasilishaji wa hotuba hii, Waziri wetu yuko makini na ni mzungumzaji mzuri, ameongea kwa makini, wataalam wameandaa hotuba vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla yangu amezungumza Mwenyekiti wa Kamati hii, na mimi niseme kwamba naungana naye na yote aliyosema, lakini na mimi nataka nihoji kupitia kwako Mwenyekiti, Kamati ilipokaa ilikuwa na nia nzuri na imetuambia, ila kuna mambo magumu nimeyaona kwenye taarifa ya Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna shida ya uwasilishwaji wa fedha za maendeleo. Hadi kufikia mwezi huu wa tatu walikuwa wamepewa shilingi bilioni moja tu. Sasa shilingi bilioni 1.6 kwa viwanda vya Tanzania nzima, itafanya nini? Nirudi pia kwa Waziri wangu, yeye leo hapa amekuja na kitabu chake hiki, anatuomba hapa tumpitishie shilingi bilioni 81.8, Tanzania nzima! Hivi kweli fedha hiyo ndiyo italeta mabadiliko ya viwanda? Haifiki hata trilioni moja! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipitia hiki kitabu cha Mpango wa Maendeleo, nikidhani kwamba labda hiyo ndiyo Wizara iliyopewa fedha nyingi kutokana na mabadiliko tunayotarajia, lakini nikakuta hapana, kuna Wizara ambazo zimepewa mpaka shilingi trilioni tatu. Sasa hii Wizara ya Viwanda na Biashara inashindikana nini kuipa hata shilingi trilioni mbili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuwaombea fedha ili hii mipango mizuri iliyoainishwa kwenye kitabu hiki iweze kutekelezeka. Niseme wazi kuna jambo ambalo linanikera. Wakati sisi huku tunawaombea fedha au tunaona kwamba fedha hii haitoshi, Mawaziri wetu wanatuambia hiyo hiyo, tutaenda kigumu kigumu! Hii siyo kazi ya mtu! Ni kazi ya nchi hii, sisi tumeona, na ninyi mnatakiwa mwone! Fedha hii haitoshi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miaka ya 1980, SIDO ilikuwa inafanya vizuri sana nchini. SIDO zikuwepo katika Mikoa yote na sasa hivi SIDO zimebaki mfumfu tu, haziko vizuri. Sasa najua tunapoongelea viwanda, kuna viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Mimi kwa ajili ya ajira ya vijana wetu, naomba nibaki kwenye viwanda vya kati au vidogo kiasi ili nianzie hapo SIDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mkoa una eneo la SIDO limetengwa na wapo sasa watu wanafanya shughuli kule ndani ya SIDO, lakini Serikali kiasi imetoa mkono wake. Mimi nilikuwa naomba maeneo haya ya SIDO na viwanda hivi vilivyokuwa vimeanzishwa kwenye SIDO, sasa vifanyiwe kazi maalum ya kivifufua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shughulil za viwanda, wengi tunazungumzia tu mashine, lakini nguvu kubwa ya kiwanda ni rasilimali watu, na sisi watu tunao. Tunao vijana wetu ambao wanatafuta ajira. Ndiyo maana unakuta hata zile nchi zinazoendelea, zinatafuta nchi ambayo ina labor, yaani cheap labor inakwenda kufanya huko viwanda vyao. Sisi iko hapa hapa, tunataka kufanya viwanda hapa. Kwa hiyo, tuna hao vijana watakaopata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumbukumbu zangu sahihi kabisa, kila kitu kilikuwa kinapatikana SIDO, vijiko vizuri vya SIDO, makufuli mazuri ya SIDO, vitasa vizuri vya SIDO, makarai, mabeseni, leo imekuwaje? Kwa nini hatuvipati vitu hivyo? Eti tunaagiza, tunataka vitu imported, vitusaidie nini? Matokeo yake ndio hata vitu vingine tunaishia kwenye mitumba, wenzetu wamechoka wametupa, sisi tunaletewa huku, hapana!
Naomba kupitia kwako, Wizara hii isimamie SIDO, vijana wetu wapate ajira na ndiyo hiyo sasa tuanze kuona tunafufua viwanda kwa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vikubwa ambavyo vilikuwa nchini na bado baadhi vipo. Wakati huo nitoe mfano wa Kiwanda cha Kuzalisha Sukari (TPC), kiwanda cha kuzalisha sukari. Ajira yake ni watu 5,000, lakini haikuishia tu ajira, kiwanda hicho kilikuwa pia kina training school. Wale vijana wanakuwa trained pale, wanakuwa na shule ya kuwafundisha, wanaweza kuchonga vyuma, wanaweza kukarabati vyuma hivyo, wanaweza kuvitumia. (Makofi)
Sasa nilikuwa naomba kila mwekezaji anayekuja akaweka kiwanda, awe pia na nafasi ya ku-train vijana wetu ili wawe ni watu ambao wana ujuzi katika jambo lile linalofanyika. Hili linaweza kufanyika pia kwenye viwanda vya sementi, bia labda na viwanda vingine. Pia kwenye hicho kiwanda cha TPC ningependa pia wafufue ile training school.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi nyumbani. Naelewa kwamba charity starts at home. Mimi nitokako ni Kilimanjaro, viwanda vyetu vyote vimekufa, sasa hivi tunacho hicho kiwanda kimoja cha TPC na labda kile cha Bonite ambacho ni private na kiwanda kingine ambacho kipo ni kiwanda kidogo tu cha kutengeneza bia. Tena ni bia ya Serengeti maana ile Kibo imeshakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anapita katika kampeni zake za kuomba kura za Urais, alisema haitachukua muda mrefu viwanda vyote vitafufuliwa. Kwa haraka haraka naomba nivitaje tu; najua haviwezi kufufuliwa mwaka huu au mwaka ujao, lakini ianze sasa basi process ya kifufua. Tuna Kilimanjaro Machine Tools, tuna Kiwanda kile cha Magunia na hiki ni kiwanda muhimu kwa sababu pale Kilimanjaro ni wakulima wa kahawa na hii kahawa haiwekwi kwenye gunia lingine labda kama la sulfate, hapana, unyevu utabakia. kwenye kahawa. Gunia moja tu linalofaa kuweka kahawa ni lile la jute. Kwa hiyo, bado kuna soko la magunia hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wangu ajue kwamba sasa kuna kazi kufufua kile Kiwanda cha Magunia. Haiishii hapo, pia kuna Kiwanda cha Ngozi. Kwenye kiwanda cha ngozi, kuna private sector ambayo kuna muhindi, ni Shaha Industries, anatengeneza vifaa vya ngozi ila umeme unakuwa ni shida na pia kodi zimemuwia ngumu amefunga, aweze pia kuzungumza naye ili kiwanda hicho kifunguliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tuna shauku kubwa, tuna hamu ya kuona kwamba tunapiga hatua. Naomba nimtakie kila la heri na ninaunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kipekee namshukuru Mungu na nakiri kwamba Mungu ni mwema kila wakati ndiyo maana tuko hapa wote kama ilivyompendeza yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme wazi kwamba nitazungumzia maeneo matatu tu na nitajikita katika hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Nashukuru kwamba kitabu hiki ni kizuri, kimeeleweka na sasa basi nataka kuzungumzia machache ili niendelee kuboresha maeneo aliyotuletea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na ule ukurasa wa 38 pale alipozungumzia Mfuko wa Afya ya Jamii (Community Health Fund). Mfuko huu ulianzishwa siku nyingi na ulianza pia wakati inaanza NHIF lakini hauko katika mfumo rasmi kama NHIF ambao uko kwa watu ambao wana ajira na wanapata mishahara yao kila leo. Kwa hiyo, NHIF utakatwa kwenye mshahara lakini hii CHF ni ya hiari. Inapokuwa hiari leo ukiwa nacho utatoa kesho huna hutoi. Bahati nzuri sana Serikali inajazilia mkitoa kumi Serikali inajazia kumi, mijini au manispaa inaitwa tele kwa tele huku kwingine inaitwa kujazilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia nzuri ya Serikali mfuko huu umedumaa. Pamoja na takwimu tulizopewa hapa kwamba wanachama wameongezeka lakini kwa Tanzania nzima figure ni kidogo. Sasa nini kifanyike? Serikali ina nia nzuri kuwa na wananchi wenye afya nzuri kwa sababu Taifa lenye wananchi wenye afya nzuri ni Taifa zuri. Watu wanafanya kazi, watu hawaumwiumwi, hakuna wengi waliolazwa hospitalini na pale anapopata rufaa anakwenda kutibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shida ya CHF unakatwa au unakuwa na hiyo kadi unatibiwa katika eneo linalokuzunguka, pale pale katika kata labda sanasana wilaya, huwezi kwenda mbali. Inapokuja rufaa ile kadi haitumiki wakati NHIF unaweza ukatibiwa Tanzania nzima. Ombi langu la msisitizo Serikali ione sasa kuna kila sababu kuuongezea mfuko huo ili mtu akishakuwa na ile kadi ya CHF atibiwe kutoka wilayani mpaka mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wetu hawajiwezi sana, mara nyingine kama mtu hana watoto basi inakuwa uwezo wake ni mdogo. Naomba hili lifikiriwe kwa mapana, Serikali haiwezi kupungukiwa kwa kiasi hicho. Siku za nyuma watu hawa walikuwa wanatibiwa bure leo imekuja lazima tuchangie na sasa tuko kwenye wakati wa mpito Serikali inataka iwe na ule mfuko wa jinsi ya kutibu kwa ujumla, naomba sana hili jambo lisimamiwe na liwezekane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema kilio changu cha CHF, kwa sababu naumia sana kwani wanawake wa Kilimanjaro wengi wangependa kujiunga lakini wamejiunga wachache kutokana labda na hali duni, wakati mwingine mazao hayatoshi au kipato ni kidogo na ninaamini hata huko kwa Wabunge wengine hali ni hiyo. Niseme wazi Wabunge tulio hapa ni wadau wakubwa wa mfuko huo kwa ajili ya watu wetu na hasa wale Wabunge wa Viti Maalum tunaweza kutumiwa kutoa hiyo elimu na siku zote tuungane kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naomba sasa nizungumzie jambo lingine ambalo ni ajira kwa vijana. Jambo hili limezungumzwa kwa muda mrefu, ajira kwa vijana, mimi najiuliza vijana wa wapi? Najiuliza mwenyewe vijana wa Tanzania walio wapi? Ni kina nani hao?
Wana ujuzi gani? Je, hii ajira mnayomfikiria anaitaka? Sasa leo ilivyokuja TAMISEMI nikajua hapa hapa jungu kuu, kwa sababu hakuna zaidi ya TAMISEMI. Halmashauri zetu ndizo zenye watu wote na vijana wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ufanyike utaratibu rasmi wa kutambua vijana ambao hawana ajira. Vijana hawa wakishatambuliwa tuwajue wako eneo fulani kama ni kata, kama ni wilaya wako vijana wangapi na wanataka ajira za aina gani? Suala hili linaweza likaonekana gumu lakini tuna vijana wetu wengi wanafanya research zao lakini hazifanyiwi kazi. Kuna vijana wengi ambao wako kwenye shule au kwenye vyuo lakini nao pia hawatumiki. Naomba sasa halmashauri ziwajue vijana ambao hawana kazi na watambulike rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano kidogo tu. Hivi tulivyo hapa kuna vijana wanaandikishwa kwenda JKT unakuta wilaya nyingine wamepeleka maombi vijana 5,000 na wanatakiwa vijana 200 tu. Je, wale 4,800 wanakwenda wapi? Tuwatumie sasa wale vijana tuwajue hawa ndiyo kundi linalohitaji ajira na tuwaelekeze namna ambavyo watasaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ambayo hayatumiki mfululizo, mojawapo ni eneo la Nane Nane unakuta nyumba zipo, watu ambao wanakuweko pale au mashirika wakishatumia ile wiki ya Nane Nane nyumba zile zinafungwa sana sana zinakuwa ni maeneo matupu. Kwa nini sasa vijana kama wale tukishirikiana na hawa wadau ambao wana majengo huko Nane Nane, tusiwatumie kama majeshi yetu, kama ni wale wakulima, vijana wale wakafundishwa pale kwa muda hata wa mwaka mzima mpaka tena itakapofika Nane Nane na baadaye Serikali ikasaidia kuwapa kianzio? Mtu kusimama na kuweza kujitegemea au kusimama mwenyewe ni kitu kigumu. Ndiyo maana unakuta hata mstaafu anapofika wakati wa kustaafu anaomba kuongezewa muda kwa sababu hajasimama sembuse vijana wetu hawa wadogo? Naomba Serikali na sisi wenyewe tuwasaidie vijana hao wasimame wapate ajira na waweze kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo nataka kulizungumzia ni hili eneo la biashara ndogo ndogo. Ni kweli tamko limetolewa kila mahali watambue maeneo ya kufanyia biashara na yapimwe. Hili ni jambo zuri na ningeomba kabisa hata hizo Halmashauri hivi sasa zilinganishwe au zipimwe kwa kigezo hicho kwamba ni Halmashauri gani zimeweza kutambua maeneo hayo au Halmashauri ngapi zimeweza kuweka hayo maeneo katika hali nzuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niseme jambo moja. Kuna zile biashara ndogo ndogo zaidi, biashara za babalishe, mamalishe, nataka niufahamishe umma huu kwamba sasa hivi watu wengi wanapenda kula kwa mama lishe kwa sababu chakula ni kitamu, kinapikwa kidogo na kilichoungwa vizuri na nazi na kila kitu. Mtu anapiga kona tu anachota anakula kwa mama lishe. Shida ya maeneo haya yamekaa hovyo hovyo, takataka zinatupwa hovyo, mitaro inaziba, huwezi kumchukulia mtu hatua matokeo yake ni kipindupindu na magonjwa ambayo hatukuwa tumetarajia. Hii yote ni kwa sababu wale ni watu ambao wanatembea na jiko na vitu vyake vya kulia, dakika yuko hapa, dakika yuko pale, wanahamahama. Athari nyingine Serikali inaingia gharama kubwa sana kusafisha miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika ule ukurasa wa 37, Mheshimiwa Waziri ameongelea shughuli za usimamizi wa usafi kwamba sasa baada ya tamko la Rais tufanye miji yetu safi kila mwisho wa mwezi kila mtu akafanye usafi, itadumu kwa muda gani? Is this sustainable? Inatakiwa sasa tujue kwamba watu wote wanatakiwa waweke maeneo yao safi hususani hao akina mamalishe na babalishe. Mwarubaini wake ni nini? Ni Halmashauri zetu kutenga maeneo sasa ya kina mamalishe wawaambie hapa ndiyo mtakapokuwa mnafanyia biashara zenu na msionekane kwingine. Siyo tu kwa akina mamalishe ni pamoja pia na wale vijana wetu ambao wanaitwa matching guys.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninamshukuru Mungu kwa kuwezesha kujadili mada za kuiletea nchi yetu ya Tanzania maendeleo.
Pili, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri, Injinia Edwin Ngonyani na Injinia Joseph Nyamhanga, Katibu Mkuu Ujenzi, Dkt. Leonard Chamuriho, Katibu Mkuu Uchukuzi, Profesa Faustine Kamuzora, Katibu Mkuu Mawasiliano, Injinia Dkt. Maria Sasabo, Naibu Katibu Mkuu Mawasiliano na watendaji wote wa Wizara husika na bodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kuhusu mawasilianio ya simu. Utakubaliana na mimi kwamba simu za mkononi zimeshamiri kila kona ya nchi hii, lakini kila leo gharama za simu zinapanda.
Swali, hivi Mtanzania wa kawaida anafaidikaje na wawekezaji hao wa mitandao mbalimbali wakiwemo Airtel, Vodacom, Tigo, Zantel, Halotel na wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atoe mwongozo kwa makampuni hayo yatoe elimu ya ujasiriamali kwa wanawake kama mgao wa CSR. Niko tayari kuungana nao kule Kilimanjaro ili elimu hiyo iwafikie wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi naungana na wenzangu kuendelea kumpongeza Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache lakini sitaweza kumaliza ila nianze tu na yale ambayo ni muhimu zaidi. Kwenye ukurasa wa 43 kwenye kile kifungu cha 58 kazi mojawapo au shughuli aliyotuambia ni pamoja na programu ya Taifa ya kurasimisha na kuzuia ujenzi holela mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sizungumzii hayo anayokwenda kufanya nazungumzia miji ilivyo sasa hivi. Ni kweli miji yetu ilikuwa imepangwa hasa ili miji ya awali kwamba kuna maeneo ya residential, industrial areas, miji na kadhalika. Kilio changu ni hali tuliyofikia sasa, eneo kama Oysterbay ni residential area lakini sasa unakuta Oysterbay kumekuwa ndiyo kwenye pubs, vilabu, ndiyo kwenye kelele usiku na mchana, Oysterbay. Leo Mwalimu angefufuka angesema nini? Sasa sijui jinsi gani yeye Waziri ambaye anashughulikia makazi analizungumzia hili na anafanya nini ili Halmashauri zisiruhusu kujenga hivyo? Sasa hivi Oysterbay hakukaliki, ni fujo tupu. Namuomba Waziri huyu mhusika aweze kuona ni jinsi gani sasa watu watalala usiku na kuamka mapema wakafanye kazi zao. Oysterbay na kwingineko kumeharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu huu Mji wa Dodoma, ni mji mtarajiwa kuwa Mji Mkuu au Jiji la Taifa, lakini kuko hovyo, Dodoma haijakaa namna hiyo na Dodoma ndiyo yenyewe yenye Capital Development. Iweje watu wa Nigeria walivyokuja huku, walichukua zile ramani zetu wakati wakitaka kuhamisha Lagos kwenda Abuja, wameweza kutekeleza, mji ule umehama na ni kuzuri tu. Si kweli kwamba hawa Mawaziri wetu hawajasafiri, kabla hujatua nchi yoyote ndege ikianza kutua unaona miji ilivyopangika, kwa nini wanakwenda tu wanang‟azang‟aza macho hawatuletei huo ujumbe. Sasa hivi Lagos imeshahamia Abuja na kumepangika, kwa nini siyo Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kuzungumza ni makazi ya watu wa kawaida. Ni miaka mingapi sasa, hamsini na ya uhuru bado watu wanaishi kwenye tembe, zile nyumba ambazo tukiwa tunakuja Dodoma tunaziona, bado watu wanaishi kwenye makuti, bado watu wanaishi kwenye nyumba ambazo hata huwezi kujua kama bado tuko Tanzania. Mabati yameshushwa bei watu wajenge nyumba nzuri, haiwezekani, Waziri mhusika anasemaje, anatoa semina lini kwa watu walio vijijini wajue maana ya kuishi katika nyumba bora? Tunataka kuona anatoa semina, watu waishi kwenye nyumba zenye mabati, zenye kuta nzuri na wasaidike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda ni mfupi sana na nakosa amani kabisa kwa vile hakika ni mambo mazuri ningetaka kuongea lakini nizungumzie mkoa wangu. Mkoa wa Kilimajaro sasa hivi hatuna tena mahali pa kuishi vihamba vimegawiwa limebakia eneo la makaburi tu. Naomba huyu Waziri wetu kila inapowezekana tuonyeshwe eneo jipya ili vijana wetu wahamie huko sasa wakaweke makazi mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuhusu Dodoma, tulikuja lile Bunge la Tisa tukakuta viwanja vimepangwa ukutani tukajichagulia viwanja, tumepelekwa Itega, mpaka leo kule Itega hawajapeleka maendeleo. Mimi ni mmojawapo ambaye nimeathirika, nilinunua kiwanja shilingi milioni nne lakini nakwendaje kujenga Itega, hakuna juhudi zozote za kuwezesha watu kujenga makazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumzie National Housing. Ni Shirika ambalo limefungua watu macho na hata hapa Dodoma wakaone ghorofa za Medeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwamba, ametuweka tena hapa kuzungumzia maendeleo ya nchi yetu, hii ni fursa ya pekee kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeze sana Waziri wetu wa Fedha na Mipango. Bajeti hii ni nzuri na imeweka mazingira ambayo yataweza kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani, lakini kuna maeneo ambayo yanatakiwa tuyaangalie kwa undani zaidi, nitaongelea kwa hawa wawekezaji wetu wa ndani ambao ni wakulima, wavuvi, wafugaji na wachimbaji wadogo wadogo, kwa sababu hao ndiyo walio karibu zaidi na wale wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu lazima iweke mazingira rafiki kwa watu hawa kuweza kufanya shughuli zao, hawa wakifanya biashara zao vizuri au wakifanya mafanikio katika biashara zao watawezesha wale wananchi wa kawaida ambao wanatumia bidhaa zao wapate chochote ili waweze kukitumia na hivyo basi kwa kutumia vile ambavyo hawa wanazalisha kodi itapatikana na itachangia katika bajeti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ina maeneo mawili, kuna ukusanyaji wa mapato na matumizi ya mapato. Ni muhimu kabisa wote tulio hapa na walio nje waone jinsi gani makusanyo yanafanyika na yanafanikiwa. Mara nyingi makusanyo yakishakuwa kidogo hata matumizi hayapatikani kabisa. Bajeti ya mwaka uliopita, mwaka 2015/2016 tuliona jinsi gani makusanyo yalisuasua na haya yalipelekea matumizi kutokufanyika kwa wakati. Suala hili la wakati ni suala ambalo linafanya mambo yote yanakuwa hayatekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kabisa ambavyo watu wamekuja kupewa hela miezi miwili kabla au wanapewa hela kipindi ambacho hawawezi kuzitumia tena. Hii inawapelekea wale watu kutumia vibaya kwa ubadhirifu au inaleta mambo mengine ambayo siyo mazuri. Naomba kuanzia sasa tusimamie makusanyo na hapa nipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, tumeona makusanyo ambavyo ni mazuri, tunaambiwa kwa mwezi ni trilioni moja na zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuyasimamie makusanyo hayo na yaende sasa na jinsi bajeti ilivyopangiliwa, makusanyo yaende kama yalivyopangiliwa kwenye matumizi. Wale ambao wanapewa kutumia wasimamiwe, kwa sababu kama hujampa huna cha kumsimamia na wewe sasa huwezi kumuuliza chochote, unamuulizaje na hukumpatia? Naomba hilo liwe angalizo na wote tushirikiane kuona inaendaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia hapa ni kuhusu vijana na wanawake, nikisema vijana ile dhana kwamba kijana ni mtoto wa kiume tu hapana hata mabinti zetu ni vijana, vijana ni ‗ke‘ na ‗me‘ sasa inapokuja kwamba wanafanya shughuli zao mathalani wengi wa vijana wetu wanafanya mambo ya saluni za kike na kiume, lakini pia wana ujasiriamali wa lishe, kuna hawa ambao wanapika na kuna wengine ambao wanatengeneza vitu ambavyo vimekaushwa, kama ndizi za kukausha, popcorn na vitu vingine, yote hiyo ni vitu vya ujasiriamali mdogomdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wanatakiwa wawezeshwe kwenye vifungashio ili wafanye vitu vyao kwa usafi. Nani atakayewawezesha? Ni Serikali iweke mazingira rafiki ya wale ambao wanawapatia vifungashio hivyo vipatikane kwa wingi na kwa urahisi. SIDO ndiyo mahali ambapo vifungashio hivyo vingetoka kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona maeneo ambayo SIDO imetamkwa kwamba itasaidika au itafunguliwa zaidi. Nimeona Mkoa wa Mbeya, nimeona Mkoa wa Pwani lakini sikusikia Kilimanjaro ikitajwa, naomba kwa vile ile SIDO ya Kilimanjaro iko vizuri na vitu hivi vinafanyika, Mheshimiwa Waziri wetu wa Viwanda na Biashara aweke jicho lake kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mengi ya kutaka tushirikiane lakini sasa muda siyo rafiki kwangu; naomba nirudi kwenye jambo moja ambalo naona nisipolisema leo nitaweza nikakosa usingizi, kuhusu Serikali kulipa madeni yake ya ndani. Tulizungumza hapa na wakatueleza ambavyo taasisi zake zinadaiwa na mojawapo ikiwa ni taasisi ya maji inayoitwa MUWSA kule katika Mkoa wa Kilimanjaro. Mamlaka ya maji ile imefinywa sana, wametoa maji katika Chuo cha Polisi (CCP) na maeneo mengine ya Serikali kama Magereza lakini maji yale hayalipiwi. Itamkwe wazi kama Serikali inaona taasisi hizo zitumie maji bure ijulikane!
Mheshimiwa Naibu Spika, napata uchungu, inabidi sasa maji yapandishwe bei na anayeumia kwenye maji zaidi ni mwanamke, mwanamke yule atasaidiwaje! Inawezekanaje taasisi za Serikali zitumie maji bure na zile mamlaka zinajilipa mishahara zenyewe hazitegemei Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena naomba Serikali ilipe madeni yake mapema iwezekenavyo, taasisi zile zifufuke ziweze kununua vitendea kazi kama magari. Tumeambiwa kwamba, kuanzia sasa madeni ya taasisi yatalipwa centrally, naomba Hazina ilipe haya madeni mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu hizi milioni 50 za kila Kijiji. Nauliza, inapozungumziwa hapa kama ndiyo kwanza imeanza inakuwaje? Tulikuwa na hela za uwezeshaji kwa wanawake kuanzia enzi za Mwalimu Nyerere, zikaja mabilioni ya Kikwete, lakini zikishatolewa hivyo hakuna ufatiliaji, nendeni kule kwenye zile benki, achene kuziachia benki zinateseka na pesa ambazo zinawekwa kwenye suspense. Naomba Serikali ikadai kupitia Wizara ya Fedha, hatuanzi kwenye clean plate.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo najua kwamba zile zikipatikana na hizi milioni 50 zitakuwa zimekuwa nyingi tutakuwa tumefungua wigo wa kuwawezesha wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru nisingependa kengele ya pili inigongee. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba kumpongeza sana Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe na Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Ramo Makani, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na watendaji wote wa Wizara, Wakuu wa Mashirika na Taasisi zote zinazohusiana na Wizara hii. Baada ya pongezi hizo, naomba sasa kueleza yangu machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ni kati ya hifadhi chache zinazoingizia nchi yetu Tanzania pato kubwa sana la fedha za kigeni. Mlima huu unayo theluji kileleni ambayo inapungua siku hadi siku. Haya ni matokeo ya tabia nchi, lakini ukame unachangia sana. Hakuna mashaka kabisa kuwa ukame unaweza kupunguzwa kwa kuotesha miti maeneo yanayozunguka mlima. Jambo hili linawezekana kabisa endapo wanakijiji watapatiwa miche.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali ni lini Serikali itaagiza miche kwa wanavijiji hawa ili waoteshe kwa nguvu zote? Nitapenda kupata majibu wakati Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mgao wa asilimia 25 wa mapato ya mlima kwa Halmashauri zinazozunguka mlima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.