Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Shally Josepha Raymond (6 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Ushirika hususani wa mazao hauna maendeleo mazuri na umekuwa ukisuasua kwa sababu mbalimbali.
(a) Je, ni vigezo gani vinatumika kupima na kutathmini maendeleo ya ushirika?
(b) Je, ni hatua zipi zinachukuliwa na Serikali kuboresha mazingira ya ushirika kukua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupima na kutathmini maendeleo ya ushirika nchini, Serikali inatumia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya Vyama vya Ushirika vinavyoandikishwa na idadi ya wanachama kwenye vyama hivyo; idadi ya wananchi wanaopata huduma za kijamii na kiuchumi kupitia Vyama vya Ushirika nchini; uzalishaji na mauzo kupitia Vyama vya Ushirika; mitaji ya Vyama vya Ushirika na Vyama vya Ushirika vinavyouza mazao yaliyoongezwa thamani.
Pia uwekezaji wa Vyama vya Ushirika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii mfano, huduma za kifedha, shule na majengo ya vitega uchumi; ajira kupitia Vyama vya Ushirika pamoja na thamani na idadi ya mikopo inayotolewa kwa wananchama wake katika kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vingine ni pamoja na kupima ufanisi wa uendeshaji wa shughuli za Vyama vya Ushirika kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Vyama vya Ushirika ikiwemo kupitia Ukaguzi wa mara kwa mara wa nje (external audit) kila mwaka.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha mazingira ya ukuaji wa sekta ya ushirika nchini. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini kwa lengo la kuijengea uwezo wa kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Maafisa Ushirika katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya na kuendeleza kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu watendaji wa Serikali, Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika kwa kushindwa kusimamia sheria katika kutekelza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine zinazochukuliwa ni pamoja na kutoa elimu na kuendelea kuboresha mifumo ya masoko hususan wa Stakabadhi Ghalani; kuendelea kuviwezesha Vyama vya Ushirika kuzitambua kwa kuzihakiki mali zao na kuweka mikakati ya kuziendeleza mali hizo kwa manufaa ya wanachama; kuimarisha usimamizi na ukaguzi katika Vyama vya Ushirika kuzitambua kwa kuzihakiki mali zao na kuweka miakkati ya kuziendeleza mali hizo kwa manufaa ya wanachama; kuimarisha usimamizi na ukaguzi katika Vyama vya Ushirika.
Pia kuwajengea uwezo wanachama; kusimamia upatikanaji wa viongozi waadilifu na wawajibikaji wanaozingatia madili na misingi ya ushirika na pia kushirikisha Wizara za Kisekta na wadau mbalimbali katika kuhamasisha na kuendele za ushirika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Kuna miundombinu ya kusambaza maji safi na salama iliyokamilika lakini inatoa huduma chini ya kiwango cha ujenzi wake (below design and built capacity).
(a) Je, ni miradi mingapi ya maji safi na salama inayotoa huduma chini ya uwezo wa usanifu na ujenzi wake kutokana na vyanzo kupungua au kukauka maji?
(b) Je, ni hatua zipi zinachukuliwa kuepusha miradi mingine kukumbwa na matatizo kama hayo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, miradi iliyosanifiwa na kujengwa inaweza kutoa huduma ya maji chini ya kiwango kutokana an sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu iliyojengwa, ongezeko la matumizi, uharibifu wa miundombinu, kupungua au kukauka kwa vyanzo vya maji kunakoweza kusababishwa na uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa takwimu hivi sasa jumla ya miradi 114 nchini kote imebainika kutoa huduma ya maji chini ya kiwango tofauti na ilivyosanifiwa.
Mheshimiwa Spika, ili kuepusha miradi mingine kukumbwa na matatizo kama hayo, Wizara imeandaa na inatekeleza mkakati wa kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji wa mwaka 2014 na mpango wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka 2013 ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinakuwa endelevu.
Mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kutoa elimu kwa wananchi ambao wananchi wanahamasishwa kutokufanya shughuli za kibinadamu katika umbali usiopungua mita 60 kutoka kwenye mito na vijito na mita 500 kutoka kwenye bwawa na kuondoa watu wote wanaofanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji na maeneo oevu kwa maeneo hayo kupandwa miti rafiki kwa ajili ya kurejesha uoto wa asili.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Halmashauri zina wataalam wa kusimamia na kutekeleza mipango yao na zina uwezo kisheria kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo, elimu, afya, maji kilimo na ardhi pasipo kuingiliwa. Viongozi na Watendaji wa Serikali ngazi za Mkoa na Wilaya huambiwa watawajibishwa kufikia malengo mathalani, katika ujenzi wa maabara, madarasa na kutengeneza madawati:-
Je, mipaka ipi ni ya kinadharia (theoretical) na ipi inatekeleza (practical) kiutendaji na uwajibikaji kati ya viongozi wa Serikali Kuu na Halmashauri za Majiji, Miji na Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Joseph Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugatuzi wa madaraka ya kisiasa, fedha na utawala kutoka Serikali Kuu kwenda kwa wananchi kupitia Serikali za Mitaa umetokana na mahitaji ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 145 na 146. Madhumuni ya ugatuzi ni kuwapa wananchi kupitia Mabaraza yao ya Madiwani, uwezo wa kufanya maamuzi kulingana na mahitaji yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali za Mitaa zimeundwa kwa mujibu wa Sheria Na.7 (Mamlaka za Wilaya) na Sheria Na.8 (Mamlaka za Miji)kwa malengo ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi pamoja na kusimamia ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sheria kuweka utaratibu wa Serikali za Mitaa kujiamulia mambo yake kupitia vikao rasmi, hazijapewa uwezo wa kukataa maelekezo ya Serikali Kuu. Kwa mujibu wa Sera ya Maboresho ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1998, Serikali Kuu ina majukumu ya kutunga sera, kutoa miongozo ya namna bora ya kutekeleza sera, kuandaa mikakati ya kitaifa, kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa sera kwa kuzipatia Serikali za Mitaa rasilimali watu, rasilimali fedha na baadhi ya vitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuweka viwango vya utekelezaji, kufuatilia utekelezaji ili kujiridhisha kuwa miongozo na viwango vinazingatiwa na kuchukua hatua dhidi ya utekelezaji usioridhisha inapobidi hasa inapobainika matumizi yasiyo sahihi ya fedha ikiwemo viwango duni vya miradi visivyolingana na thamani ya fedha iliyotumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali Kuu huwakilishwa na viongozi wa Mikoa na Wilaya katika kusimamia utekelezaji wa sera na miongozo, Viongozi Wakuu wa Serikali ngazi ya Mikoa na Wilaya hutekeleza majukumu yao ya kisheria ya kuziwezesha Serikali za Mitaa kutimiza majukumu yao kikamilifu ikiwemo kutekeleza maagizo halali na ushauri wa viongozi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikibainika kiongozi wa Mkoa au Wilaya ameshindwa kutimiza wajibu wake na hivyo kusababisha Mamlaka ya Serikali za Mtaa zisitimize vizuri majukumu yao, Mamlaka ya uteuzi huchukua hatua za kiutawala. Napenda kusisitiza kwamba Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi zikirejewa vizuri hakuna mgogoro wowote wa kimipaka wala kiutendaji utakaodhihiri.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Kuna ongezeko la bidhaa bandia na zisizo na viwango zinazoingizwa nchini, miongoni mwa bidhaa hizo ni pembejeo za kilimo, madawa ya mifugo, dawa za binadamu, vyakula, vinjwaji, vifaa vya nyumbani na kadhalika.
(a) Je, ni hasara gani imepatikana kwa mwaka mmoja uliopita kutokana na bidhaa hizo kuingizwa nchini na kutumiwa na wananchi?
(b) Je, ni hatua gani zinachukuliwa kukomesha bidhaa hizo kuingia nchini hasa maeneo ya vijijini ambako uelewa wa watumiaji ni mdogo na maafisa wadhibiti ni wachache?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Ushindani (FCC) na kwa kushirikiana na wamiliki wa nembo za biashara, inaendelea kudhibiti bidhaa bandia zisiingie nchini ili kuhakikisha ushindani wa haki katika biashara. Katika kipindi cha Januari hadi Disemba, 2016 Tume ya Ushindani ilikamata bidhaa bandia zenye thamani ya shilingi bilioni 18.67. Bidhaa hizo zilikamatwa kwenye kaguzi za bandarini, vitengo vya makontena (ICDs) na katika masoko.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi Machi, 2017, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Taasisi nyingine waliteketeza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya shilingi bilioni 2.4. Bidhaa hizo ni pamoja na nguo, nyama na sausage, vilainishi vya injini, battery za magari na za solar 1,430.
Mheshimiwa Spika, shirika pia lilifanya ukaguzi wa mabati na kutekeleza mabati 84,000 ambayo hayakukidhi viwango. Aidha, takriban lita 94,869 za vilainishi vya injini, na katoni 200 za bendera za Taifa zilirudishwa nchi zilikotoka. Vilevile aina 11 za pombe kali katoni 123,942 zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki vilizuiliwa kuingia sokoni na kurudishwa katika nchi zilikotoka.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Ushindani na TBS zinafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine katika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kudhibiti bidhaa zinazopitia katika mipaka na nchi jirani, kufuatilia ubora wa bidhaa hafifu na bandia na kuziondoa katika soko. Ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi hizi, Serikali inongeza ajira za watumishi, kufungua vituo vya ukaguzi wa bidhaa katika mipaka yote na kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama vile luninga, redio na magazeti na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalma kuzuia magendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote tushirikiane kupambana na bidhaa bandia na zisizokidhi viwango. Adui namba moja wa viwanda ni bidhaa bandia na zile zisizokidhi viwango.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
(a) Je, Serikali inazo takwimu za kuaminika za vijana waliohitimu vyuo mbalimbali ambao hawajaweza kujiajiri au kuajiriwa;
(b) Je, ni taaluma zipi zina fursa nyingi za zipi zina fursa chache za kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu?
(c) Je, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ni ajira ngapi zilipatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Joseph Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali ina takwimu sahihi na za kuaminika za vijana waliohitimu vyuo mbalimbali, lakini hawajaweza kujiajiri au kuajiriwa ambazo hutumika katika kupanga na kutathmini utekelezaji wa programu zinazohusiana na masuala ya ajira. Takwimu hizo huptikana kupitia tafiti za nguvu kazi na tafiti za hali ya ajira na mapato zinazofanywa na ofisi ya Taifa ya Takwimu, pamoja na zinazofanywa na Taasisi za Elimu, kama vile Tracer Studies. Kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi nchini, vijana 65,614 ambao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali hawakuwa wamejiajiri wala kuajiriwa mwaka 2014.
(b) Mheshimiwa Spika, taaluma zenye fursa nyingi za kuajirika ni pamoja na fani za afya ya binadamu zikiwemo utabibu, uuguzi, ufundi sanifu wa maabara, ualimu na ufundi. Aidha, taaluma zenye fursa chache za ajira ni pamoja na masomo ya utawala, biashara na rasilimali watu. Napenda kuchukua fursa hii kuwashauri wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kwa kuwa yana fursa nyingi zaidi za ajira hususani wakati huu ambao Taifa linaelekea kuwa nchi ya viwanda.
(c) Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2015 hadi 2017/2018, jumla ya ajira mpya 1,336,957 zilipatikana kama ifuatavyo:-
Kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali ajira 593,986, sekta binafsi ajira 571,073 na Serikalini ajira 171,898. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Kuna miradi ya umwagiliaji iliyogharimu fedha nyingi kuijenga lakini inatumika chini ya uwezo na usanifu (below designed capacity) kwa sababu mbalimbali.
a) Je, ni Halmashauri ngapi zina fursa ya kilimo cha umwagiliaji na zimewekeza kwa kiwango cha kutosha kwenye miundombinu ya umwagiliaji?
b) Je, kuna mpango wowote unaotekelezwa wa kuwapata wataalam wa umwagiliaji katika muda mfupi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zote nchini zina fursa ya kilimo cha umwagiliaji na Halmashauri hizo zimeweka katika mipango yake ya maendeleo miradi inayofaa kuendelezwa kuwa kufuata vipaumbele. Skimu za umwagiliaji zimejengwa katika Halmashauri mbalimbali nchini, lakini kutokana na kukosekana kwa fedha baadhi ya skimu hizo ujenzi wake haukukamilika. Kwa sasa Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japani (JICA) imefanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Taifa ulioandaliwa mwaka 2002. Mapitio hayo yataainisha maeneo yote yanayofaa kwa umwagiliaji katika kila Halmashauri na mikoa yote nchini. Mapitio hayo yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata kibali cha kuajiri wataalam wa kutosha katika fani ya umwagiliaji. Pamoja na hayo, Halmashauri ambazo hazina wataalam wa umwagiliaji zinashauriwa kuajiri wataalam wa fani hizo.