Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Shally Josepha Raymond (28 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Mkaguzi Mkuu huwa anakagua mashirika mengine, lakini ningependa kujua au kwa niaba ya wengine pia, yeye huwa anakaguliwa na nani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mkaguzi Mkuu naamini yeye pia hujikagua mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii.
Kwa kuwa, ndizi ni kati ya zao ambalo linatumika sana nchini lakini kipimo chake kimekuwa na tatizo na wakulima wa ndizi wanapunjika sana zikiwemo ndizi kama mishale, minyenyele, mlelembo, toke, kitarasa na mtwishe. Mheshimiwa Waziri anatueleza nini kuhusu soko la bidhaa kama hiyo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ndizi zimenilea, lakini msema kweli ni mpenzi wa Mungu, sijui international standard za kupima ndizi, nitakwenda kuwa task watu wa TBS na watu wa vipimo kusudi tuweze ku-establish kipimo standard cha ndizi. Lakini kitakachoamua bei nzuri kwa mkulima ni soko la ndizi, watu wa (TAHA) Tanzania Horticulture, chini ya ndugu Jacquline wanatafuta soko la ndizi nje ya nchi, na tumeshapata soko ambalo tunahitaji kuuza nje ya nchi tani 50 kwa wiki. Kwa hiyo tunawasiliana na mama Raymond kusudi tuweze kumuunganisha na Jacquline tuone kama Kilimanjaro mnaweza kulima kusudi kupeleka nje ya nchi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa kuna mtazamo kwamba kila kundi kufungua benki ndiyo jibu la huduma ya benki, siyo jema; na kwa kuwa hapa tulipofikia, huko nyuma tulikuwa na Benki ya Posta ambayo iko kila mahali na watumiaji wa benki ni hao hao wananchi wa eneo lile; je, ni kwa nini sasa Serikali isiipe uzito Benki ya Posta ikasambaa kote?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika benki ambazo zinakuja juu sasa ni Benki yetu ya Posta. Tumeiwezesha vizuri, Menejimenti yake imekaa vizuri sasa, imezindua huduma nyingi ambazo hata benki nyingine kubwa za kibiashara zimeshindwa kuanzisha huduma hizo. Kwa hiyo, ni imani yangu kubwa Benki ya Posta ndani ya muda mfupi ujao itarejesha hadhi yake ndani ya nchi yetu ya Tanzania.
Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kuiunga mkono Benki yetu ya Posta, tufungue akaunti kule, tuiwezeshe sisi kama shareholders muhimu ili Benki ya Posta iweze sasa kurejea. Tuko vizuri na inakimbia Mheshimiwa Shally, itafungua matawi yake sehemu zote nchini.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa
kuwa katika swali la msingi linazungumzia pombe za kienyeji na pombe za
kienyeji katika Taifa letu ni nyingi ikiwemo mbege, kimpumu, ulanzi na pombe
nyinginezo. Ni lini sasa hawa watu wa viwango vya kuandika kilevi kilichoko
kwenye pombe ikiwemo TBS wataingia katika maeneo husika ili kuweza kujua
kwamba ni kiwango gani cha ulevi kinachoruhusiwa katika pombe za kienyeji?
NAIBUWAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna pombe mbalimbali. Kuna mbege, kuna
ulanzi na nyinginezo, bahati mbaya pombe hizi hazijawekwa katika viwango
stahiki na ndiyo maana maeneo mengine utakuta kuna kesi mbalimbali
zimejitokeza. Baadhi ya watu saa nyingine wamekunywa pombe, pombe ile
imewadhuru na matukio haya tumeona kwamba yametokea maeneo
mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwa sababu sasa hivi tuna Wizara
ambayo inafanya kazi vizuri zaidi na hususan suala zima la viwanda na naamini
wenzetu sasa wa TBS watachukua jukumu lao katika maeneo mbalimbali
kuhakikisha ni jinsi gani tunafanya kurekebisha utaratibu mzuri hasa katika hivi
vikundi vidogovidogo vinavyojihusisha na pombe za kienyeji, lengo kubwa ni
kumlinda Mtanzania anywe kitu kinachoridhisha maisha yake lakini na afya yake
ya msingi vilevile.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya hatua husika za mradi huu, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri ametueleza kuhusu awamu ya kwanza inayotarajiwa kukamilika Disemba, 2019. Je, huo ndiyo wakati ambapo mabomba ya Same yatafungua maji hayo na kuona maji yakitiririka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Same haiko vizuri kifedha kuwasaidia watu wa Same ambao mpaka sasa hawana maji safi na salama zikiwepo Kata za Njoro, Same Mjini, Makanya na Hedaru. Je, Serikali iko tayari sasa kuwapatia fedha za kuchimba visima virefu ili watu hao wapate maji safi na salama wakati wakisubiri kukamilika kwa mradi huo mwaka 2019?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu la msingi limezungumzia mradi wa Same-Mwanga-Korogwe kwamba ifikapo mwaka 2019 utakuwa umekamilika kwa maana kwamba maji tayari yatakuwa yamefika Mwanga na yatakuwa yamefika Same, yatafunguliwa wananchi wanaanza kupata maji na miradi hiyo inaendelea vizuri na fedha zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili kuhusu Same, katika bajeti hii tuliyonayo kwa sasa na ninyi Waheshimiwa Wabunge mliipitisha, tulihakikisha kila Halmashauri tumeipatia fedha ili Waheshimiwa Wabunge na Madiwani katika Halmashauri zao wapange miradi kutokana na hiyo fedha ambayo tumeituma kwenye Halmashauri. Kwa bahati nzuri Halmashauri ya Same ilipewa Sh. 663,847,000 kwa ajili ya miradi ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba Halmashauri hizi sasa zinao uwezo, zitekeleze miradi kutokana na fedha hii kwa kuchimba visima au maji ya mtiririko kutokana na hali ya mazingira ya Halmashauri husika ili kuhakikisha wananchi wanapata maji. Mwaka huu wa fedha unaokuja tutaendelea kutenga fedha kwenye Halmashauri ili wao wenyewe waweze kutekeleza miradi ya kuwapelekea maji wananchi wao.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Waziri ametueleza kwamba shida kwenye kuwekeza hisa iko kwenye elimu kwa umma; na kwa kuwa ametutajia kwamba wanaonufaika na lile dirisha dogo zaidi ni makampuni. Nilikuwa naomba kuuliza kwa kuwa wengi wa wajasiriamali ni wadogo wadogo wakiwepo wale wamama wa Kilimanjaro na mpaka sasa elimu ya hisa inatoka tu labda kutokea Benki ya CRDB kupitia matawi yake, ni lini sasa mabenki mengine yaliyotajwa pamoja na TOL, TCC, NMB watatoa elimu ya hisa kupitia matawi yao yaliyo huko mikoani?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sikusikia vizuri jina la Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza swali.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza haya mashirika na taasisi ambazo nimezitaja, linalonufaika na dirisha dogo, mashirika haya, hisa zao zile wao ndio wanapopata faida wanawagawia wanahisa wao. Kwa hiyo, wananchi wadogo wadogo wananufaika kupitia hizo taasisi ambazo zinanufaika na hilo dirisha dogo. Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa swali dogo la pili nitumie nafasi hii kuyashauri mashirika yote yanayohusika na benki hizi kuongeza elimu katika matawi mbalimbali ili wananchi waweze kupata elimu na kunufaika na hilo dirisha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika,
ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hadhi ya Hifadhi ya
Ngorongoro inafanana kabisa na hadhi ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, mlima ambao ni mrefu sana, mlima ambao unaingiza kipato kikubwa kwenye utalii, mlima ambao ni wa pekee wenye theluji katika nchi za tropic.
Je, Serikali sasa ina mpango gani kuhakikisha
kwamba wanaozunguka mlima ule wanaweza kuwekwa katika hali ambayo wataendelea kuutunza ili ile theluji isije ikayeyuka yote na ule mlima ukabakia katika ubora wake?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kwa maana ya sifa za uhifadhi, lakini pia faida za kiuchumi zile za Ngorongoro zinafanana kwa karibu sana na za hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Sasa kuhusu swali lake nini Serikali itafanya ili kuweza kuboresha zaidi shughuli za uhifadhi kwa faida za kiuchumi Kitaifa lakini pia kwa faida ya jamii inayoishi kwenye maeneo haya ya Hifadhi ya Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba kwanza Serikali inatambua umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi na kwa kweli tunatoa wito kwa wananchi wanaoishi katika eneo hili la Mlima Kilimanjaro waweze kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kwamba uhifadhi unaimarishwa katika eneo la Kilimanjaro. Mheshimiwa Spika, jitihada za Serikali ni kuendelea kusimamia sheria iliyopo lakini pia tunakaribisha maoni kutoka kwa wananchi wanaoishi kwenye eneo hilo hata wengine waweze kutusaidia ili kuweza kupata maoni ya
wananchi yatakayotuwezesha kuboresha zaidi shughuli za uhifadhi katika eneo la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. Ni takribani miaka kumi sasa toka hili swali linaulizwa. Nakumbuka lile Bunge la Tisa niliuliza hili swali
mwaka 2007 na Bunge la Kumi aliuliza Mheshimiwa Maida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu la Serikali siku zote ni kwamba muswada unaandaliwa. Ni lini sasa muswada huo utaletwa hapa Bungeni ili uweze kupitishwa kama sheria?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mbunge najua una imani na mimi. Sasa upele umepata mkunaji, safari hii unaletwa chini ya uongozi wangu.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa kuwa Serikali kwa kutambua wanawake inakuwa vigumu kupata mikopo kwenye mabenki, imekuwa ikitoa hela na wakati mwingine pia ikipeleka kwenye mabenki, lakini wanawake wanakopeshwa kupitia kwenye vikundi vyao zikiwemo mabilioni ya JK.
Swali langu nauliza, wanawake wa vijijini hawakunufaika na hizo hela, sasa Serikali inafanyaje kuhakikisha kwa kuwa zile hela ni za mzunguko na bado tuna amini zipo, zitawafikiaje wale wanawake wa vijijini?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi wote ni wajumbe katika zile Halmashauri zetu na mikopo inapopitishwa inapitia katika vikao vya Baraza la Madiwani.
Kwa hiyo, mimi naomba pale ambapo tunapitisha vikundi vyetu viweze kupewa mikopo ni lazima tuzingatie pia tunao akina mama wanaotoka katika maeneo ya Vijiji ili na wao waweze kufikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la mabenki, benki wana masharti yao ambayo yanatakiwa yatimizwe, kwa hiyo tujaribu kuwaelimisha wakina mama ili waweze kukidhi vigezo vinavyotakiwa na mabenki na sisi wenyewe tuwe mstari wa mbele katika kuangalia ni vikundi vipi ambavyo vimekidhi vigezo hivyo na tuawasidie katika hatua za kuweza kupata mikopo either kutoka katika benki au kutoka katika Halmashauri kupitia ule Mfuko wa Wanawake na Vijana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ili wananchi waupende ushirika ni pamoja na kuona kuwa mali zao ziko salama na wananufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza Serikali, kwa Vyama vya Ushirika ambavyo mali zake zimetapanywa yakiwemo mashamba, viwanja, nyumba, hususani KNCU, Serikali inasaidiaje ili kurejesha mali hizo ili wananchi wanufaike? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inasaidiaje mikataba mibovu iliyoingiwa na Vyama vya Ushirika na wale ambao wamechukua mali za vyama hivyo iletwe ili irekebishwe wananchi hao waweze kuona sasa ushirika wao unaendelea vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba baadhi ya mali za Vyama vya Ushirika zimetapanywa na hazitumiki kwa utaratibu unaotakiwa na ndiyo maana Wizara yangu kwa kushirikiana na Maafisa Ushirika nchini kote kwa sasa wanafanya tathmini kuhusiana na mali zote za Vyama vya Ushirika ili kujua ni zipi ambazo hazitumiki, zipi ambazo zimeingia mikononi mwa watu binafsi kinyume na taratibu, kwa lengo la kuhakikisha kwamba zile ambazo zimechukuliwa kinyemela ziweze kurudi, lakini vilevile ili mali hizo za ushirika ikiwa pamoja na ardhi ziweze kutumika katika mazingira ambayo yanaleta tija zaidi na kwa manufaa ya ushirika na wana ushirika wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali la pili kwamba tunafanyaje kurejesha mali ambazo zilichukuliwa kinyume na taratibu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tokeo Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, tumechukua hatua kadhaa za kuhakikisha kwamba uovu uliokuwa ukifanyika katika Vyama vya Ushirika hautokei tena. Kwa hiyo, wale wote ambao wamehusika katika kufanya ubadhirifu na upotevu wa mali za ushirika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata viongozi wa Vyama vya Ushirika ambao nao wanakuwa ni sehemu ya ubadhirifu huo tumeendelea kuwachukulia hatua. Ni hivi karibuni tu tumevunja Bodi za Vyama vya Ushirika zaidi ya 200 Mtwara na Lindi. Vilevile mmesikia yaliyotokea Nyanza, jitihada zinaendelea kurudisha mali za Ushirika wa Nyanza. Pia tunajitahidi kuendelea kusaidia vyama vingine ambavyo siku za nyuma kimsingi taratibu zilikiukwa na mali zao kwenda nje kwa watu binafsi bila kufuata utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maswali haya na jitihada za Serikali, naomba niendelee kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wahamasishe wanaushirika wawaeleze kwamba ushirika ni wa kwao, Serikali yenyewe inasaidia. Kwa hiyo, inatakiwa wenyewe wawajibike kuhakikisha kwamba mali za ushirika zinalindwa na pale kasoro zinavyotokea basi watoe taarifa kwa Serikali ili tuweze kuchukua hatua.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika jibu lake la msingi amekiri kwamba kuna miradi 114 ambayo imekuwa haiendelei au imeharibika kabisa na katika miradi hiyo 114 mmojawapo ninaoufahamu mimi ni ule wa Kili Water kule Mkoani Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, ni lini sasa Serikali itahakikisha imeukarabati mradi huo ili kuondoa adha ya Wanawake wa Tambarare ya Rombo kubeba ndoo za maji Alfajiri na mapema walio katika Kata ya kule Ngoyoni, Mamsera chini pamoja na wale ambao wako kule pembeni ya Ziwa Chala?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tambarare yote ya Mkoa wa Kilimanjaro imekumbwa na adha hii ikiweko Wilaya ya Mwanga, Same Mjini mpaka kule Hedaru. Ni lini sasa Serikali itakamilisha ule mradi wa maji wa Ziwa la Nyumba ya Mungu ambao utapeleka maji kupitia Mwanga, Same, Hedaru mpaka Mombo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali kumpongeza sana Mbunge kwa maana kwamba anafuatilia kuona namna gani miradi hii inawea kuathiri matumizi ya wananchi kwa maana kwamba maji yamekuwa yanapungua kwa namna hali ya hewa inavyobadilika. Kwa hiyo ni jambo ambalo ni la msingi lakini pia ni lazima tuchukue hatua. Hatua mojawapo ni lazima sisi sote tuhakikishe kwamba tunalinda vyanzo vya maji lakini pia tupande miti ambayo ni rafiki lakini pia tuvune maji ya mvua kwasababu rasilimali za maji zinapungua mwaka hadi mwaka kama hatuchukui hatua yoyote ya kukabiliana na tatizo hilo. (Makofi)
Sasa kuhusu mradi ambao unasema ni lini utakarabatiwa, Mkoa wa Kilimanjaro Serikali kwa mwaka huu wa 2017/2018 tumetengea shilingi bilioni 8.95 kwa ajili ya kumaliza miradi inayoendelea lakini pia kukarabati miradi ambayo ipo haifanyi kazi katika kiwango kwahiyo watumie fddha zile katika kuangalia vipaumbele na kuona kama wanaweza kukarabati kwa mwaka huu wa fedha vinginevyo wapange katika mwaka wa fedha unaofuata.
Kuhusu swali lake la pili, mradi wa Nyumba ya Mungu kupeleka maji Mwanga mpaka Same, sasa hivi mkandari huko mwanzo alikuwa anusua sua lakini sasa hivi anakwenda kwa kasi na nina uhakika kwamba mradi ule utakuja kukamilika lakini pia tumeanza na awamu nyingine ya kupeleka maji kule Same nayo Mkandarasi yupo site na kazi inakwenda vizuri. Serikali inafuatilia kwa nguvu zote ili miradi hii iweze kukamilika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa uhusiano wa benki na mtu wa kawaida ambaye hafanyi biashara, ni kuweka hela yake ili apate faida na pia kwa usalama; na sasa hivi tunashuhudia kwamba hata mitandao ya simu mtu unaweza ukawekeza hela yako. Ni lini sasa benki hizi zitakaa chini na kuona kwamba kuna umuhimu wa kuongeza faida (interest rate) kwa wale wanaoweka hela zao kwenye savings account?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikisema tangu mwaka 1991 nchi yetu iliingia katika soko huru katika masuala ya kifedha nchini na interests zinazopangwa na mabenki yetu katika savings accont huwa zinawekwa kulingana na uhalisia wa soko. Ina maana faida inapatikana kwa mabenki na kwa wananchi. Kwa kumbukumbu ambazo tunazo Wizara ya Fedha na Mipango, interest hii imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe angalizo kwa mabenki yetu kuangalia kwamba wana balance interest wanayotoza waone interest wanayowapa wananchi kwa kuweka pesa hizi katika akaunti zao hasa savings account.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina uhakika katika hili mabenki yetu yanafanya kazi vizuri kuhakikisha wao wanapata na wateja wao ambao ni wananchi wanapata vizuri kwa kuwa tupo katika soko huria na wanapambana kuweza kupata wateja kuweka pesa katika benki zao.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Swali langu linahusu umbali wa wananchi hawa na benki zao. Kwa kuwa benki hizo zina nia nzuri ya kuwakopesha, lakini tatizo ni wananchi wanakoishi ni mbali na zile benki, kwa sababu benki nyingi zimefunguliwa mijini na nyingi zinafanya kibiashara zaidi.
Ni lini sasa Serikali itawasiliana na hizi benki zifungue matawi yao kule vijijini zikiwemo kule Mamba Miamba kule Same na kwingineko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tunashukuru sana kwa concern yake ya kuona kwamba wananchi wengi wanahitaji huduma hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kama Serikali hatua ambazo zinaanza kuchukuliwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba mabenki haya ya biashara yanakwenda kutafuta wateja maeneo ya pembezoni ili sasa watu wengi zaidi wapate fursa ya kuweza kupata huduma hizi za kifedha.
Kwa hiyo, naamini kabisa katika mipango ile ya Serikali ambayo mojawapo kubwa lililofanyika mwaka 2015 ni kuhakikisha kwamba fedha ambayo ilikuwa ni ya Mashirika ya Umma ambayo mabenki mengi walikuwa wanaitegemea, ilirudi Benki Kuu sasa ili mabenki waende kuwatafuta wateja wengi zaidi. Kwa kufanya hivyo pia itasaidia sana mabenki haya kwenda katika maeneo ya pembezoni ili kuwahudumia wananchi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalichukua hilo na kazi inaendelea kufanyika, kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata huduma hii ya kifedha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya tambarare ya Kilimanjaro yana shida ya maji safi na salama. Ni lini sasa Serikali itatumia Lake Chala ili kuyapatia maeneo ya tambarare maji vikiwemo vijiji vya Mahida, Malawa, Ngoyoni, Ngareni, Holili na kwingineko?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari na inatekeleza miradi mingi ya maji na mipango kemkem ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutoa maji kutoka Lake Chala, naomba tushirikiane na Halmashauri yako ambayo hilo bwawa liko katika hiyo Halmashauri ili tuone jinsi gani tunaweza tukafanya utafiti na kuweka fedha kuhakikisha vijiji vinavyozunguka sehemu hiyo vinapata maji.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali la nyongeza. Serikali iko moja nayo ni Serikali Kuu na hao wote waliotamkwa wanatekeleza kutokana na maagizo ya Serikali Kuu. Je, inakuwaje pale ambapo hela hazipelekwi za kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali inafuatilia vipi kuepusha migongano hiyo kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo fedha za kutekeleza mradi fulani hazijapelekwa zote mawasiliano yanafahamika kati ya waliopokea na waliopeleka. Kwa hiyo hayo yanakuwa ni maelezo sahihi wakati wa tathmini kwamba hatukuweza kutekeleza vizuri mradi huu au hatukukamilisha kwa sababu fedha imekuja nusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hiyo ni mawasiliano ya ndani ya Serikali na mara nyingi imefanyika; lakini kitu kimoja kizuri kwa upande wa Serikali za Mitaa ni kwamba wanapopewa wakati mwingine fedha imezidi au imechelewa kuja imekuja mwishoni mwa mwaka wa fedha wenzetu wanaruhusiwa kubaki na fedha ile halafu mwezi wa Saba wanakaa kwenye vikao vyao rasmi wanazipitisha kwa ajili ya matumizi yaliyovuka mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili kwamba tunafuatiliaje mgogoro; Serikali ina macho usiku na mchana. Kule kule ziliko Serikali za Mitaa wapo waangalizi wa Serikali ambao wanakusanya taarifa kila siku asubuhi na mchana kwa masaa yote. Kwa hiyo kama kuna harufu yoyote ya mgogoro Serikali Kuu huwa inapata taarifa hizo mara moja. Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hali ya kusuasua kwa huu mradi wa Mande, Tela kunafanana kabisa na miradi mingine iliyo katika maeneo ya tambarare ya Mkoa wa Kilimanjaro, ukiweko ule mradi wa Mwanga mpaka kule Hedaru mpaka Mombo. Ni lini sasa Serikali itatupa muda muafaka wa kukamilika kwa miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Tunapozungumzia suala la maji, maji hayana mbadala, si kama wali, ukikosa wali eti utakula ugali. Kwa hiyo kuna haja kubwa sana ya kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi kama Wizara ya Maji katika kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa wakati lazima kuwe na ufuatiliaji na usimamizi wa karibu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji tumejipanga katika kufuatilia na kusimamia miradi hii kwa wakati ili wananchi waweze kupata maji kwa muda muafaka uliopangwa. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa uwezo wa Halmashauri unatofautiana na Halmashauri nyingine ni duni kabisa hazina kipato zikiwepo Halmashauri za Hai, Siha, Rombo na kwingineko; je, Serikali ina mpango gani sasa wa kufanya top up ili nia yao njema ya kuwezesha wanawake na vijana ifanane Tanzania nzima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la mama ni zuri, Halmashauri zingine pato lake ni dogo lakini kutokana na wazo hilo zuri ndiyo maana Serikali ina mifuko mingine ya ku-top up. Kuna Mfuko kutoka katika empowerment programu yetu ambayo inasaidia na tuna fedha nyingi sana hapa, takribani kuna Mifuko 17.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni wazo zuri lakini Serikali imeshachukua initiative tayari, Mifuko hiyo ipo, isipokuwa jamii yetu wakati mwingine hawana taarifa sahihi kuhusu mifuko hiyo. Ndiyo maana sasa wakati programu hii inaendeshwa hapa Dodoma takribani mwezi mmoja uliopita uwezeshaji huo umeshatolewa na tumewaelekeza sasa Maafisa wetu wa Maendeleo ya Jamii waweze kushuka katika grassroot ili kuweza kuwaelimisha wananchi ni wapi watapata hizi fedha na uwezeshaji ili kujiinua kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wazo zuri na Serikali hivi sasa inaendelea ku-top up isipokuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wafanye kazi yao sasa kuhakikisha jamii sasa inapata uelewa wa kutosha juu ya mifuko hii ili waweze kupata uwezeshaji wa kutosha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante; nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya ufafanuzi. Kwa kuwa tumeshuhudia kwenye luninga wakiteketeza vifaa hivi na wanaoingiza kupata hasara, Je, ni hatua gani zaidi zinazochukuliwa kwa wale wanaoingiza ili kukomesha hali hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vifaa bandia havitoki tu nje ya nchi, vingine vinatengenezwa humu humu nchini. Mimi naomba kujua ni hatua gani zinazochukuliwa na Serikali ili kukomesha kabisa vifaa hivyo, vikiwemo viatilishi, pembejeo za kilimo, vipodozi vya kina mama, na hata vingine ambavyo si rahisi kutamka hapa hadharani? Naomba kujua. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI):
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza nakiri na amekubali jibu kwamba kweli vile vifaa vinateketezwa na yeye mwenyewe ameona; lakini ni hatua gani zinachukuliwa sasa kwa wale ambao wameshikwa na hizo bidhaa bandia.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba, tunazo sheria nchini, yule anayeshi kwa na vifaa bandia ni kwamba anapata stahili kulingana na sheria. Wakati mwingine wanatozwa faini na pengine inaweza hata zaidi ya hiyo akapewa adhabu stahiki.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili amesema kwamba hivi vifaa bandia sio kwamba vinatoka nje ya nchi tu, kuna vingine vinatengenezwa humu ndani. Kwa mfano, kama vipodozi wapo watu wanachanganya vipodozi na wamewaathiri sana wale ambao wanatumia.
Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kufunga viwanda vile ambavyo havijasajiliwa na mara nyingi hivi vitu ambavyo vinafanywa ambavyo havipo katika viwango vinafanywa na viwanda bubu. Kwa hiyo, Serikali inafanya ukaguzi, kama tulivyojibu katika swali la msingi ili kuhakikisha kwamba hawa wote wanaofanya hivyo wanakamatwa na wanapewa adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria na viwanda vinavyojihusisha na hivyo tayari vinafungwa ili kuhakikisha kwamba suala hilo haliendelei. Vilevile pia nimeongea na Mheshimiwa Waziri akasema kwamba wanatarajia kuleta sheria itakayotoa adhabu kali zaidi hasa kwa hawa watu ambao wanatengeneza vitu bandia.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika majibu ya msingi, Naibu Waziri ametueleza kwamba takwimu za mwaka 2014 miaka minne nyuma zinaonesha kuwa vijana 65,614 hawakupata ajira. Naamini kabisa baada ya miaka hiyo idadi hiyo imeendelea kuongezeka. Swali la kwanza; je, ni nini hasa kinawachofanya wahitimu washindwe kuajiriwa au kujiajiri?
Mheshimiwa Spika, swali l a pili, ni hatua zipi mahususi zinazochukuliwa na Serikali kuwawezesha au kuwajengea wahitimu hao mazingira wezeshi ya kuajiriwa au kujiajiri. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameulizia kuhusu ni kwa nini sasa watu hawa wanashindwa kupata fursa ya kuajiriwa au kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, jibu lake ni kwamba katika nchi yoyote duniani suala la ajira limekuwa ni suala ambalo limekuja na changamoto nyingi sana, kutokana na kwamba nafasi za ajira zinazozalishwa na idadi ya watu ambao wana uwezo wa kufanya kazi vinakosa uwiano. Kwa hiyo, kama Taifa tunaendelea kuwa na mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunakuja na mipango madhubuti ya kufanya nguvu kazi yetu hii kubwa iweze kupata nafasi ya kuajirika.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa tafiti ya mwaka 2014 ambayo wanaiita Integrated Labour Force Survey inasema takribani watu wa kuanzia miaka 15 na kuendelea ambayo ndiyo working age population, ambao wana uwezo wa kufanya kazi kila mwaka wanaojitokeza ni wengi zaidi kuliko nafasi za ajira.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika kujibu swali lake la pili, niseme tu kwamba kama Serikali tumeona kabisa suala la kwanza la kuweza kukabiliana na changamoto hii hasa kwa wahitimu wa vyuo vikuu, tumekuja na utaratibu wa kwanza wa kuzindua mpango maalum wa mafunzo ya uanagenzi na mafunzo ya vitendo ambao Mheshimiwa Waziri Mkuu alizindua mwaka jana ambao unamfanya mhitimu yeyote wa Chuo Kikuu....

Mheshimiwa Spika, kwanza tumekuja na framework hiyo ambayo hivi sasa tutaanza kuwachukua wahitimu wa vyuo vikuu kwa kwenda kuwa-attach katika mashirika mbalimbali, kampuni mbalimbali, waende kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu, hilo ni eneo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, tumekuja na utaratibu wa kubadilisha mindset kwa mujibu wa sera ya ajira inasema ajira ni shughuli yoyote halali inayompatia mtu kipato. Kwa hiyo, tunawatoa sasa wale wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu kutoka kwenye kufikiria kuajiriwa moja kwa moja ofisini na kubadilisha mtazamo kwenda kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji na biashara.
Mheshimiwa Spika, Serikali tumeandaa mazingira wezeshi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili vijana hao waweze kupata fursa na kupata mitaji na maeneo ya kufanyia shughuli zao. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru tena. Nianze kwa kumshukuru sana Naibu Waziri aliyepata muda wa kuitembelea barabara hiyo na Mheshimiwa Anne Kilango mnamo tarehe 8 Agosti. Mheshimiwa Anne Kilango anatuma salamu na anasema ahsante sana na nadhani aliiona kazi kubwa hiyo. Pamoja na shukurani hizo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maji ni adui mkubwa sana wa barabara ya lami na baada ya mvua kila wakati vile vipande vya lami vilivyojengwa katika eneo husika zikiwemo zile kilomita tatu Kihurio, kilomita tano kisiwani, kilomita tano Ndungu zinaendelea kumomonyoka kila wakati. Je, Serikali haioni sasa kuna kila sababu ya kufanya haraka kuunganisha vipande hivyo ili lami ile iliyowahi isifagiliwe kabisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wote wa Kilimanjaro ilionekana wazi kwamba katika vikao vya RCC Same iko nyuma sana kwenye miundombinu ya barabara na barabara iliyotajwa hapa ni barabara muhimu ambayo pia ina Mbuga za Wanyama. Je, ni lini sasa, baada ya upembuzi yakinifu Serikali iko tayari kupeleka hela hiyo mapema ili zoezi hili lifanyike kwa sababu hii ni ahadi ya Waheshimiwa wagombea Marais toka Awamu ya Nne na Awamu ya Tano? Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa jinsi ambavyo anafanya kazi zake kutetea Mkoa wa Kilimanjaro na wananchi wake kwa ujumla. Swali lake la kwanza ni kweli kwamba mvua au maji ni adui mkubwa sana wa barabara zetu na hasa zile za lami na hata zile ambazo si za lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyoeleza katika majibu ya swali la awali, kwamba baada ya usanifu wa kina kukamilika na kujua gharama tutatangaza tena tutampata mkandarasi, tukishampata mkandarasi hatua za haraka za kutafuta pesa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hiyo zitaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, sisi tunasubiri taarifa za kitaalam, zitakapokuwa tayari na kujua gharama hatutachukua muda mrefu kama Serikali kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami na tutaendelea kuilinda hiyo barabara kwa pesa tulioitenga kwenye bajeti ya mwaka huu. Ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na niseme wazi nimeyaelewa sana majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na majibu hayo mazuri na ufafanuzi huo, wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro wamehamasika sana kwenye SACCOS na sio vikundi vya ambao wameshapata maradhi tayari, bali ni vikundi vya akinamama ambao wanafundishana mambo mengi ikiwemo ujasiriamali, scheme za elimu pamoja hiyo kujiunga na NHIF. Ni muda mrefu sasa toka mwaka jana wameandikiwa barua kusitisha zoezi hilo, lakini kwao imekuwa ni usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri haoni kwamba itakuwa sasa ni usumbufu wale akinamama kurudi kuanza upya, badala ya kuweka muendelezo kwamba walikuwepo kwenye NHIF na waendelee?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sina maelezezo kamili kuhusiana na hivi vikundi vya Mkoa wa Kilimanjaro ambavyo Mheshimiwa Mbunge anaviongelea, mimi nimuombe sana Mama Shally Raymond baada ya Kipindi cha Maswali na Majibu tuonane anipe maelezo na mimi nimtume Meneja wangu wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro aende akavitembelee na kuvikagua vikundi, kwa sababu tunapozungumzia vikundi vya washirika na vikundi hivi vya SACCOS ni vikundi ambavyo na sisi tumekuwa tunavihamasisha vijiunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichotaka tuweze kupata maelezo kidogo tuweze kubaini changamoto zilizopo na tuweze kuchukua hatua kwa haraka zaidi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Serikali na ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Moshi Vijijini ina skimu ya umwagiliaji inayoitwa Lower Moshi Irrigation ambayo ilifadhiliwa na Japan, lakini skimu hiyo sasa iko taabani kwa sababu ya upungufu wa maji na miundombinu mibovu na imesababisha kupungua sana kwa zao la mpunga. Ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kutuchimbia visima au mabwawa ili kuongeza maji ili skimu hiyo iweze kuwa endelevu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ni wengi sana wanategemea mpunga kutoka eneo hilo la Lower Moshi, ni lini sasa Serikali itafanya jambo la dharura kutupelekea wataalam hao ili hali irudi kama ilivyokuwa siku za awali? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala ya maji. Lakini pia hata masuala ya umwagiliaji na hasa kwa eneo la Lower Moshi. Lakini katika hoja zake mbili naomba kumjibu kwamba ni kweli tunayo taarifa kwamba Lower Moshi Irrigation ilijengwa miaka ya nyuma na Serikali ya Japan na ilifanya kazi kubwa sana kule Moshi ya kuzalisha mazao ya mpunga. Lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi ni kweli maji yamepungua na ndiyo maana huu mpango kabambe ambao tunaukamilisha tutahakikisha ama tunachimba visima na bahati nzuri Kilimanjaro kule chini ya ardhi maji ni mengi au tunajenga mabwawa ili kuvuna maji ili wananchi wale. Lakini pia miundombinu ya Lower Moshi pia kidogo imechakaa, tutahakikisha pia tunaiboresha ili wakulima wale waendelee kufaidi matunda ya kilimo.
Kuhusu suala la wataalam kama ambavyo nimejibu katika suala la Mheshimiwa Mbunge aliyeuliza suala la wataalamu Mheshimiwa Shally Raymond tunalifanyia kazi na tumeelekeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji itaajiri wataalam wa umwagiliaji kwa ajili ya kutengeneza scheme za umwagiliaji. Lakini baada ya kutengeneza kwa sababu utekelezaji wake utafanywa na Halmashauri tumeelekeza pia Halmashauri nao iajiri wataalamu wa umwagiliaji ili wakati wanapojenga wawe wanatoa taarifa jinsi miundombinu inavyobadilika ili tuweze kwenda vizuri.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye majibu ya msingi Naibu Waziri amesema kwamba tatizo ni pia uelewa mdogo wa wananchi kuhusu kutunza mazingira. Kwa kuwa sasa Mlima Kilimanjaro ile theluji inaendelea kuyeyuka na mazingira yamekuwa kame muda wote lakini wanawake na vijana wa Kilimanjaro wapo tayari kuungana na Wizara hiyo katika kuboresha mazingira hayo. Ni lini sasa hii Wizara ya Mazingira itawezesha wanawake na vijana wale kiuchumi ili wapate miche waweze kuotesha miti kwenye mashamba yao kuzunguka mipaka na pia kwenye barabara inayoelekea Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la shemeji yangu Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba katika Mlima Kilimanjaro kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo maeneo mengi yameathirika ni pamoja na theluji ambayo imekuwa ikipamba ule mlima kule juu unakuwa ni kivutio katika masuala ya utalii. Pia tumeendelea kusisitiza kupitia Halmashauri za Hai, Rombo, Moshi Vijijini pamoja na Moshi Mjini kuhakikisha kwamba wanapanda na kuhifadhi miti. Hawa akina mama ambao amesema mimi nipo tayari kabisa kuja kwa hao akina mama japo hakuwasema ni wengi kiasi gani ili na mimi pengine niambatane na akina baba wengi kidogo kuja kuonana na hao akina mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Shally, baada ya Bunge hili, naye ni shahidi nilipokuwa Kilimanjaro nilimpa taarifa na kukupigia simu kwamba aje tushughulike na mazingira. Aliweza kuja na akanipa msaada ambao kwa kweli mpaka leo bado naukumbuka. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE.SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mkoani Kilimanjaro, Wilaya ya Same, Kata ya Makanya yanapatikana madini ya gypsum, madini hayo Tanzania nzima yanapatikana Manyoni, Pindilo na Makanya kwenyewe. Hata hivyo, miundombinu ya hapa ni mibaya sana na wachimbaji hao ni wachimbaji wakiwemo akinamama na akinababa. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wachimbaji hao wakati tunapoelekea kwenye Sera ya Viwanda na Biashara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kama Serikali tunazidi kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo tunawawezesha kimiundombinu, kimitaji na kuwasaidia kiteknolojia ili waweze kuchimba na waweze kujipatia kipato chao. Ni kweli kabisa hayo madini ya gypsum ni madini ambayo ni muhimu na yahahitajika katika soko la dunia na baadhi ya nchi za jirani wanahitaji madini hayo na kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali pamoja na kupitisha sheria ile ya mwaka jana ya Marekebisho ya Sheria ya Madini tumetaka kwamba madini yote ya gypsum tuweze kuwasaidia wachimbaji waweze kuchimba na kuya-process ili kusudi wapeleke kwenye soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi pamoja na Wizara nyingine tunasaidiana kupeleka miundombinu kwa maana ya maji, umeme, barabara kwa wachimbaji wadogo dogo ili waweze kuchimba vizuri na kwa gharama ndogo ili waweze kupata faida. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Baba wa Taifa alisambaza mitamba bora katika maeneo yote ambayo yanafanya zero grazing. Kwa kuwa ni muda mrefu sasa na cross breeding imeshafifisha mazao yale ni lini sasa Serikali itaweza kuboresha na kutawanya mitamba bora, vifaranga bora vya kienyeji na vifaranga bora vya samaki katika maeneo ya wafugaji kama Kilimanjaro ambapo kuna wanawake wengi sana ambao ni wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Raymond, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza swali ni zuri sana juu ya Serikali kuhakikisha kwamba tunasambaza mitamba bora kwa wafugaji hasa akina mama wa Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa zima. Progamu hii Serikali tunayo kupitia mashamba yetu ya mifugo yaliyosamba nchi nzima tunafanya kazi hii. Kwa mfano tu ni kwamba hivi karibuni kupitia dirisha letu la sekta binafsi tumewawezesha Ushirika wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa Mkoani Tanga yaani TBCU, wamekopeshwa pesa na Benki yetu ya Kilimo ili waweze kununua mitamba bora 300 ambapo kufikia tarehe 30 ya mwezi huu mitamba ile itaenda kusambazwa kwa wafugaji wote wa Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tuko tayari kuhakikisha kwamba na wafugaji wengine kote nchini wanapata fursa hii. Shime wafugaji wote wa ng’ombe wa maziwa, kuku hata wale wa samaki wajiunge katika vikundi ili waweze kutumia fursa hii inayopatikana kupitia dirisha letu la ukopeshaji la Benki ya Kilimo.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii. Wauguzi wanaofanya kazi katika Wodi za Wagonjwa wa Akili, wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi sana kwa sababu wagonjwa hao mara nyingi wako hyper:-

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwakatia Wauguzi hao bima ya maisha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, matibabu ya afya ya akili ni taaluma na wataalam wetu hawa wamepata mafunzo mazuri tu ya jinsi gani ya kuweza kuwatibu wagonjwa hawa wenye matatizo ya afya ya akili katika hatua zile za awali ambazo sisi mara nyingi katika lugha ya kitaalaam tunaita acute phase, lakini vilevile katika hatua ya mwendelezo wa yale matibabu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimthibitishie tu kwamba wataalam wetu wako vizuri na ndiyo maana hujawahi kusikia kwamba kuna muuguzi wala daktari amefariki au amepata kipigo kikubwa kutokana na kuhudumia wagonjwa hawa wa afya ya akili. Kwa hiyo, kwa sasa hatuna evidence ya kutosha ya kusema kwamba sasa watu wote ambao wanatoa huduma za afya kwa wagonjwa wa akili tuweze kuwakatia bima ya maisha.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nimeyapokea.

Swali la kwanza; kwa kuwa Benki ya Kilimo mpaka sasa haijaweza kuwa katika Mikoa yote na hizo benki nyingine alizozizungumzia kama NMB na alitaja benki mbili zote hizo ni Commercial na zinahitaji wewe unayekwenda kukopa lazima uwe na dhamana na wanawake wengi hawana nyumba wala hawana dhamana ambazo zinatambulika kibenki: Je, Serikali iko tayari ku-guarantee mikopo hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Tatizo katika kilimo ni pamoja na mbegu bora na mara nyingi unakuta kwamba mbegu hizo ni ghari na pia siyo rahisi kumfikia mkulima. Ni lini sasa mbegu hizo zitagaiwa kwa wanawake hao kupitia katika Kata zao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Shally Rymond anataka kujua kwamba kwa sababu benki ya Maendeleo ya Kilimo haipo kila Mkoa na kwamba hizi benki nyingine ni za kibiashara, anataka kujua mikakati ya Serikali kama iko tayari kudhamini mikopo hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali tupo tayari na tulishaanza na ndiyo maana kama alivyosema Benki ya Maendeleo ya Kilimo haipo kila Mkoa, ni kwa sababu hii ni Benki ya Maendeleo, ni benki ya kimkakati na lengo lake ni kuwasaidia wakulima kupitia madirisha mbalimbali ya Taasisi za Fedha. Moja, tulichokifanya, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tumedhamini mikopo yote ambayo inayotolewa na Benki ya NMB ili kwenda kwenye Sekta ya Kilimo hususan pamoja na akina mama.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba ni lini Serikali itatengeneza mazingira ya mbegu hizi zikapatikana katika ngazi za Kata ili wanawake wazipate kiurahisi?

Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba Serikali siku zote kwamba tuko tayari. Mbegu hizi kupitia Shirika letu la Mbegu (ASA) na Taasisi nyingine binafsi na mawakala mbalimbali, tumeweka mazingira mazuri kwamba mbegu hizi zinapatikana Tanzania kote, siyo kwa kwenye Kata tu, mpaka ngazi za vijiji kwa kuzingatia mahitaji. Kama kuna mahitaji maalum katika eneo unalotoka, baada ya Bunge hili tuone ili tuwaelekeze wenzetu wa ASA ili waweze kupeleka mbegu haraka iwezekanavyo ziwafikie wakulima.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa njema ni vyema zikawa na sauti, leo asubuhi kuanzia saa 12.00 TBC haikuwa na sauti kabisa na hakuna namba yoyote iliyokuwa inaonesha pale tupige kwa dharura wale ambao tuna ving’amuzi vya Azam TV.

Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini na wakati walipokuja kurudi kutupatia sauti saa 1:10 asubuhi hawaku- apologize?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hata mimi mwenyewe nimeona hiyo hitilafu ikitokea leo, lakini siyo leo tu imekuwa ikitokea mara kwa mara kwa sababu TBC, television yenu ya Taifa sasa hivi ipo katika programu ya mageuzi makubwa sana kiteknolojia ndiyo maana muonekano wa TBC sasa hivi ni bora kupita miaka iliyopita nyuma na naomba ndani ya mwezi mmoja mtaona hata background, nyuma ukiangalia TBC haitatofautiana sana na CNN. Kwa hiyo, kaa mkao wa kuangalia Television ya Taifa.